• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ronaldo aachwa nje ya kikosi cha kwanza cha Juventus tetesi za kuhamia PSG zikishika kasi

Ronaldo aachwa nje ya kikosi cha kwanza cha Juventus tetesi za kuhamia PSG zikishika kasi

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo aliachwa nje ya kikosi cha kwanza cha Juventus kilichoteuliwa na kocha Massimiliano Allegri kuvaana na Udinese katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) iliyokamilika kwa sare ya 2-2 mnamo Jumapili.

Huku tetesi kuhusu uwezekano wa Ronaldo kujiengua kambini mwa Juventus na kutua Paris Saint-Germain (PSG) zikishika kasi, magazeti mengi nchini Italia yameshikilia kwamba Ronaldo aliomba vinara wa benchi ya kiufundi ya Juventus kutompanga katika kikosi cha kwanza.

Ingawa hivyo, mkurugenzi wa soka kambini mwa Juventus, Pavel Nedved amefutilia mbali madai hayo na kusisitiza kwamba maamuzi hayo ya kutoteuliwa kwa Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa taji la Ballon d’Or, ni zao la maafikiano kati ya wasimamizi wote wa Juventus.

“Ronaldo hakuomba kuachwa nje ya kikosi ili afanikishe mipango ya kuondoka Juventus. Atasalia kuwa mchezaji wetu na dalili zote zinaashiria kwamba atatia saini mkataba mpya ambao tutampokeza hivi karibuni,” akasema Nedved katika mahojiano yake na kituo cha habari cha DAZN.

Ronaldo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, anahusishwa na PSG iwapo mpango wa Kylian Mbappe kuhamia Real utafaulu.

Kuingia kwake kambini mwa PSG kutashuhudia miamba hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) wakijivunia huduma za mafowadi bora zaidi duniani ikizingatiwa kwamba tayari wana Lionel Messi na Neymar Jr.

Ronaldo, 36, aliletwa uwanjani katika kipindi cha pili kujaza nafasi ya Alvaro Morata kunako dakika ya 60. Fowadi huyo raia wa Ureno alidhani alikuwa amefungia Juventus bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili ila goli hilo likafutiliwa mbali baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba Ronaldo alikuwa ameotea.

Allegri aliyerejeshewa mikoba ya ukocha kambini mwa Juventus mwishoni mwa msimu uliopita wa 2020-21 baada ya Andrea Pirlo kutimuliwa, aliteua Morata kuongoza safu ya mbele ya kikosi chake kwa kushirikiana na Paulo Dybala na Juan Cuadrado waliofunga mabao ya waajiri wao.

Bao la kwanza la Udinese lilipachikwa wavuni na Roberto Pereyra kupitia penalti baada ya kipa Wojciech Szczesny kumchezea vibaya Tolgay Arslan. Goli la pili lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Everton na Watford, Gerard Deulofeu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Lukaku aongoza Chelsea kuzamisha Arsenal katika gozi kali...

Raila asaka njia mpya ya Canaan