• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
SACHANGWAN: Barabara ya mauti yaboreshwa

SACHANGWAN: Barabara ya mauti yaboreshwa

Na PETER MBURU

KWA miaka mingi sasa, maeneo ya Kibunja, Sachangwan, Salgaa, Migaa na Sobea kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret yamefahamika kwa sifa mbaya, kama ambapo ajali mbaya za barabarani hutokea mwaka baada ya mwingine, na kupoteza maisha ua watu wengi.

Kwa kusikia jina la maeneo hayo tu, Wakenya wengi huingiwa na woga, haswa ikiwa wanatarajia kutumia barabara hiyo kwa usafiri.

Hata hivyo, huenda hofu hii ikazikwa kwenye kaburi la sahau, kufuatia hatua ya serikali kujenga barabara ya mipito miwili katika barabara hiyo, ili kupunguza visa vya ajali.

Kazi hiyo iliyoanza mnamo Juni mwaka uliopita inahusisha upanuzi wa barabara hiyo eneo la urefu wa kilomita 22, baada ya serikali kutenga Sh500milioni kwa kazi hiyo.

Tayari kazi inaendelea na sehemu ya barabara yenyewe imejengwa ukuta kati, ili kuzuia magari yanayosafiri kuelekea pande tofauti kugongana kwa vyovyote vile.

Ni hatua ambayo imechangamkiwa na wakazi wa maeneo hayo, ambao kwa mara ya kwanza Desemba 2018 walishuhudia msimu wa sherehe za krismasi usiokuwa na mikasa ya ajali.

“Hatukushuhudia ajali yoyote msimu wa Desemba mwaka uliopita, tulikuwa tumejiandaa na timu za idara tofauti zikiwa barabarani kwani miaka ya mbeleni msimu huo huwa wa giza, lakini kwa bahati nzuri tulitoboa bila mkasa,” Naibu Mshirikishi wa Serikali eneo la Sachangwan Peter Mutiso alieleza Taifa Leo.

Shughuli za ujenzi wa barabara ya mipito miwili zinaendelea katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret, maeneo ya Salgaa-Sachangwan ili kupunguza visa vya ajali. Picha PETER MBURU.

Kwa wakazi, ujenzi wa barabara hiyo ni ukombozi wa aina fulani, haswa wakikumbuka namna siku za mbeleni wamekuwa wakilazimika kuamka usiku kwenda kusaidia watu wanaoumia kwenye ajali.

Hata hivyo, wakazi wana mahitaji yao ambayo wangeitaka serikali kusikiza inapojenga barabara hiyo, ili ujenzi usiwe kikwazo kwao tena.

“Tunataka hii barabara ijengwe ili iwe salama, lakini wanaojenga pia wajali maslahi yetu kwa kutuachia nafasi za kuingia vijijini na katika vituo vya kibiashara ili tuweze kuletewa bidhaa na kuendeleza biashara zetu,” Bw Paul Tesot ambaye ni mfanyabiashara eneo hilo akasema.

Wakazi aidha wanawataka wanakandarasi wanaojenga kuzingatia ukweli kuwa wakazi ni wakulima na wazazi, na kuwa wana mifugo wanaovuka barabara kwenda malishoni na watoto wanaovuka wakienda na kutoka shuleni.

Waliitaka serikali kuwa ikifanya vikao vya kuhamasisha umma inapotaka kutekeleza mradi wa aina hiyo, ili wakazi waeleze matakwa na matarajio yao yazingatiwe.

Baadhi ya viini vya ajali ambavyo wakazi wamebaini ni hali ya madereva kuendesha magari bila kujali na kwa kasi sana, haswa wale wa malori.

“Malori zinakimbia sana, kutoka hapo kwa GSU zinaweka free gear hadi Salgaa. Tulitambua kuwa wanalipwa kulingana na haraka yao kuwasilisha mizigo wanayosafirisha, hali ambayo inawafanya kuendesha magari kwa kasi sana,” akasema mkazi mmoja.

Sasa, wakazi wanapendekeza kuwa barabara hiyo inapojengwa, kuwe na njia ya kando ambapo gari likiona kuwa linaelekea kufanya ajali linaweza kutorokea, badala ya kurudi ndani ya barabara na kusababisha mkasa mkubwa.

Wakazi aidha bado wanasubiri kujengewa kituo cha afya cha kuwasaidia wanaoumia katika ajali ama kuwapa ushauri wa kisaikolojia wanaoathiriwa na mikasa hiyo, ambacho waliahidiwa na Rais Mustaafu Mwai Kibaki, alipohudhuria ibada ya mazishi ya waliokufa kwenye mkasa wa moto uliosababishwa na lori la mafuta lililopata ajali hao mnamo 2009.

“wakati Rais Kibaki alikuja hapa Sachangwa baada ya mkasa, aliamrisha kujengwe kifaa cha ‘trauma center’ hapa na tukadhani tutafaidika. Lakini tangu wakati huo hatujajengewa, baadaye pesa zilizotengwa zilipelekwa kusaidia mahali pengine na tunahisi uchungu sana,” Bi Rachael Ruto, kiongozi wa eneo hilo akasema.

Kituo hicho kilijengwa katika hospitali ya Nakuru Level Five, japo hakijawahi kukamilika kwani kilikwama miaka kadha iliyopita, baada ya Sh70 milioni kutumika. Jumba lisilokamilika liko katika hospitali hiyo ambapo kituo hicho kilihamishiwa.

You can share this post!

Menengai Cream Homeboyz inavyokuza vipaji vya raga

Mwanamke mwenye fikra chafu hatarini kusukumwa jela

adminleo