• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Saudia kuruhusu mahujaji milioni 1

Saudia kuruhusu mahujaji milioni 1

NA AFP

RIYADH, SAUDI ARABIA

SAUDI Arabia jana Jumamosi ilisema itaruhusu mahujaji milioni moja wa Kiislamu kutoka ndani na nje ya nchi hiyo, kushiriki Hija mwaka huu 2022.

Hii ni idadi kubwa ikizingatiwa kuwa miaka miwili iliyopita janga la Covid -19 lilifanya utawala wa nchi hiyo kupunguza kiwango cha mahujaji walioshiriki desturi hiyo ya kidini katika mji mtakatifu wa Mecca.

“Wizara ya Hija imeruhusu mahujaji milioni moja, kutoka nje na nchini, kushiriki Hija ya mwaka huu,” taarifa kutoka wizara hiyo ikasema.

Hija ni mojawapo ya nguzo tano za Kiislamu zinazodumu kwa siku tano, na kila Mwislamu aliye na uwezo anahitajika kwenda Mecca angalau mara moja maishani mwake kuitimiza.

Mwaka 2019 takriban Waislamu 2.5 milioni walifika kwa Hija nchini Saudi Arabia.

Hata hivyo, baada ya mkurupuko wa Covid-19 kutokea baadaye, serikali ya Saudia iliruhusu mahujaji 1,000 pekee mnamo 2020.

Mwaka jana, idadi hiyo iliongezwa hadi kufikia mahujaji 60, 000; ambao walitakiwa kuwa tu wale ambao wamepokea dozi zote mbili za chanjo ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, vinavyosababisha Covid-19.

Wale ambao wataruhusiwa kuhudhuria Hija mwaka huu mnamo Julai, ni watu walio chini ya miaka 65 na ambao wamepata awamu zote za chanjo, ilisema taarifa ya Saudia.

Wanaotoka nje ya nchi watahitajika kuwa na cheti cha PCR kinachoonyesha wamepimwa na kubainika kuwa hawana virusi vya corona.

Sharti wawe wamepimwa saa 72 kabla ya kusafiri Saudi Arabia.

Kando na desturi ya kidini, Hija ilikuwa ikiletea Saudia takriban Sh1.2 trilioni kila mwaka kama mapato.

“Serikali inataka kulinda usalama wa mahujaji hata inavyojizatiti kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya watu wanashiriki haji, “ taarifa hiyo ilieleza.

Haji inajumuisha msururu wa shughuli za kidini zinazodumu kwa zaidi ya siku tano katika Mji Mtakatifu wa Mecca na maeneo ya karibu magharibi mwa Saudi Arabia.

Watawala wa Saudi Arabia huona fahari kuu kwa nchini hiyo kuwa mwenyeji wa haji kwa sababu nchi humo ndiko kuna maeneo matakatifu.

Kabla ya kutokea kwa mlipuko wa Covid-19, mahujaji wa Kiislamu walikuwa wakiileta Saudi Arabia karibu dola bilioni 12 (Sh1.2 trilioni ) kila mwaka.

Marufuku ya kutosafiri Mecca kwa haji iliyowekwa katika miaka ya 2020 na 2021 iliwavunja moyo Waislamu kutoka mataifa mengine.

Kufikia sasa Saudi Arabia imeandikisha visa 751,000 vya maambukizi na vifo 9,055 kutoka na Covid-19. Hii ni kulingana na data kutoka Wizara ya Afya nchini humo.

  • Tags

You can share this post!

WALIOBOBEA: Parpai aliangusha mbabe, akawa waziri miezi 7 tu

Chelsea waaibisha Southampton kwa kichapo cha 6-0 katika...

T L