• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Ukapera hauathiri kazi yangu, asema Mbunge

Ukapera hauathiri kazi yangu, asema Mbunge

Na MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Igembe Kusini John Paul Mwirigi amejitetea dhidi ya madai kuwa ametelekeza majukumu yake ili ajishughulishe na kutafuta mke.

Bw Mwirigi, 25, ambaye bado ni kapera alikuwa mwepesi wa kufafanua kuwa utendakazi wake hauathiriwi kwa vyovyote vile na hali kwamba angali mseja.

Akiongea Ijumaa katika mkutano katika Chuo Anuwai cha Maua, mbunge huyo aliwataka wakazi hao wampe muda akiahidi kutengeneza barabara zote ambazo ziko chini yake.

“Nipeni muda kidogo tu, sijasahau majukumu yangu ya kuhakikisha kuwa barabara mbovu zimekarabatiwa ikiwemo hii ya Maua kwenda Kimongoro,” Bw Mwirigi akasema.

Akaongeza, “Najua wachache wenu mnanung’unika mkidhani kwamba nimetelekeza majukumu yangu kwa sababu sina mke. Naomba muda tu… hata nikioa kazi ya ujenzi wa barabara haitatekelezwa na mke wangu. Kazi hiyo itasalia yangu kama mbunge wa eneo hilo,”

Bw Mwirigi alisema hayo katika Chuo Anuwai cha Maua kwenye hafla ya usambazaji hundi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya chekechea na karakana katika chuo hicho. Hafla hiyo iliongozwa na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi.

Baadhi ya wakazi waliohudhuria shughuli hiyo walimkabili mbunge huyo wakilalamikia hali mbaya ya barabara kadhaa katika eneo bunge hilo, hasa ile ya Maua-Kimongoro, ambayo walisema ina mashimo mengi.

Baadhi ya vijana wamejitolea kuziba mashimo katika barabara hiyo kwa hiari.

yake, haswa katika eneo Red Canteen hadi soko lenye shughuli nyingi la Kamongoro.

Wakazi walalamika kuwa mwanakandarasi aliyepewa zabuni ya kukarabati barabara hiyo amekuwa akijivuta katika kazi hiyo ambayo ilianza mapema mwaka wa 2017.

“Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa ukarabati wa barabara hii itafanywa kwa haraka ili itumika na watu wetu,” Bw Mwirigi akasema.

Mbunge huyo mwenye umri mdogo zaidi aliwashangaza wengi alipowabwaga wagombeaji wa vyama vikubwa kama Jubilee na DP katika uchaguzi mkuu uliopita licha ya kwamba hakuendesha kampeni zake kwa fedha nyingi.

You can share this post!

Afisi yangu ipewe mamlaka zaidi – Ruto

Sahau urais wenye mamlaka makuu, Kuria aambia Ruto

adminleo