• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:10 PM
Ukraine: Mkataba wasifiwa na US, EU

Ukraine: Mkataba wasifiwa na US, EU

NA AFP

INSTANBUL, UTURUKI

AMERIKA (US) na mataifa ya Uropa (EU) yamesifu kutiwa saini kwa mkataba unaoruhusu Ukraine kusafirisha nje nafaka kupitia bandari zake zilizoko katika bahari ya Black Sea, hatua hiyo ikisababisha kushuka kwa bei ya ngano.

Maafisa wa Amerika walisema mkataba huo uliotiwa saini na Urusi na Ukraine Ijumaa nchini Uturuki, “uliandaliwa vizuri” ili kuwezesha mataifa ya ulimwengu kufuatilia utekelezaji wake.

Muungano wa Ulaya (EU) ulihimiza utekelezaji wa haraka wa mkataba huo huku Waziri wa Kigeni wa Uingereza, Liz Truss akisema nchi hiyo itafuatilia kwa makini kuhakikisha Urusi inafanikisha utekelezaji wa mkataba huo.

Mkataba huo ulitiwa saini jijini Instanbul, Uturuki katika hafla iliyoshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan.

“Leo, kuna nguzo katika bahari ya Black Sea… nguzo ya matumaini, nguzo ya uwezekano, nguzo ya afueni,” Guterres akasema dakika chache kabla ya kutiwa saini kwa mkataba huo.

Kwa upande wake, Rais Erdogan – aliyeongoza shughuli ya upatanisho na aliye na uhusiano mzuri na Urusi na Ukraine – alielezea matumaini kuwa mkataba huo utafufua matumaini ya kukomeshwa kwa vita kati ya nchi hizo mbili.

Bei ya ngano katika masoko ya kimataifa ilishuka bei hadi viwango vilivyokuwa kabla ya Urusi kuvamia Ukraine Februari 24, dakika chache baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu aliwaambia wanahabari, baada ya kuhudhuria hafla ya kutiwa saini kwa mkataba huo, kwamba alitaraji utaanza kutekelezwa “siku chache zijazo”.

Aliongeza kuwa Amerika na Ubelgiji zimeihakikishia nchi yake kuwa zitaondoa vikwazo vyote zilizoiwekea Urusi dhidi ya kusafirishwa nje kwa nafaka na mazao mengine ya shambani.

Urusi ilizuia Ukraine kusafirisha nafaka kupitia bandari zake katika bahari ya Black Sea, ilipoivamia Februari 24, 2022.

Hatua hiyo ilisababisha uhaba wa nafaka katika mataifa mengi ya ulimwenguni ambayo huagiza mazao hayo kutoka Ukraine.

  • Tags

You can share this post!

Edna Talava alenga makuu katika uigizaji

Furaha huku kiwanda cha Mumias kikianza kusaga miwa baada...

T L