Makala

Biden aruhusu Ukraine kutumia mabomu ya Amerika kuvamia Urusi

Na MASHIRIKA November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Amerika Joe Biden ameruhusu Ukraine kutumia silaha zilizotengenezewa Amerika (U.S) kutekeleza mashambulizi ndani ya Urusi.

Haya ni kwa mujibu wa maafisa wawili wa U.S ambao wanafahamu uamuzi huo ambao umegeuza mkondo wa matakwa ya sera ya Washington kuhusu mzozo kati ya Ukraine na Urusi.

Bila kufichua zaidi kwa sababu za kiusalama, duru zinasema kuwa Ukraine inapanga kuzindua mashambulizi ya kwanza ya mbali siku zijazo.

Hatua hii inajiri miezi miwili kabla ya Rais mteule Donald Trump kuingia Ikulu ya White House Januari 20, 2025.

Pia imejiri baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kurai U.S iruhusu jeshi la Ukraine kutumia silaha za U.S kuvamia wanajeshi wa Urusi katika sehemu zilizo mbali na mipaka ya nchi hiyo.

Mabadiliko haya yamesukumwa na hatua ya Urusi kutumia vikosi vya jeshi la Korea Kaskazini kupiga jeki vikosi vyake vya kijeshi.

Afisa wa Amerika mwenye ufahamu kuhusu tukio hili anasema uamuzi wa Urusi umeibua wasiwasi Washington na Kyiv.

Rais Zelensky alisema maboma hayo ‘yatajiongelea.’

“Leo (Jumapili), wengi katika vyombo vya habari wanasema tumepokea ruhusu ya kuchukua hatua inayofaa,” alisema. “Lakini mashambulizi hayatekelezwi kwa maneno. Mambo kama haya hayatangazwi.”

White House na Wizara ya Mashauri ya Kigeni U.S zilidinda kutoa maoni kuhusu taarifa hii.

Vile vile hakujakuwa na jibu la moja kwa moja kutoka Kremlin, ambayo imeonya kuondolewa kwa kizingiti dhidi ya kutumia silaha za U.S kutaonekana kuwa hali ya kuibua ongezeko la wasiwasi sababu ya vita vya hali ya juu.

Vladimir Dzhabarov, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Urusi, alisema iwapo U.S itaruhusu Ukraine kurusha mabomu ndani ya Urusi, itasababisha vita baina ya nchi nyingi, pengine kuanzisha ‘vita vya tatu vya dunia.’

“Magharibi imeamua uzidishaji huu wa kivita ambao unaweza kufanya nchi ya Ukraine kuwa na maangamizi makubwa kufikia asubuhi,” akasema Andrei Klishas, afisa wa ngazi ya juu katika Bunge kuu la Urusi kupitia mtandao wa mawasiliano ya Telegram.

Mashambulizi ya kwanza ya masafa marefu ya Ukraine yanaweza kufanikishwa kutumia roketi za ATACMS (Army Tactical Missile System) ambazo zina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 306, duru zinasema.

Huku baadhi ya maafisa wa U.S wakionyesha wasiwasi iwapo mashambulizi ya mbali yatabadilisha mkondo mzima wa kivita, uamuzi huu utasaidia Ukraine wakati ambao majeshi ya Urusi yanapata ufanisi na pengine kuweka Kyiv katika hali nzuri ya mashauriano endapo majadiliano ya kusitisha vita yatafanyika.

Haijabainika iwapo Bw Trump atabadilisha uamuzi wa Bw Biden atakaposhika hatamu za uongozi.

Kwa muda mrefu, Rais huyu mteule amekuwa akipinga kiwango cha ufadhili unaotolewa na U.S kwa Ukraine na ameapa kumaliza vita upesi bila kueleza kwa njia gani.