• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
USIKU WA CHEO: Wito Waislamu waimarishe ibada wapate fadhila za Lailatul Qadr

USIKU WA CHEO: Wito Waislamu waimarishe ibada wapate fadhila za Lailatul Qadr

Na MISHI GONGO

KUMI la mwisho la mwezi wa Ramadhan ni wakati muhimu kwa waumini wa Kiisilamu ambao hukithirisha ibada zao kwa matumaini ya kupata usiku wa cheo wa “Laylat al-Qadr” au pia “Lailatul Qadr”.

Miongoni mwa ibada hizo huhusisha kukesha misikitini kwa swala na dua kwa wingi.

Kulingana na Qur’an Lailatul Qadr ni usiku bora kuliko miaka 1,000.

Iwapo muumini ataupata usiku huu, basi husamehewa madhambi yake.

Kwa sasa ibada hazifanyiki misikiti kufuatia marufuku yaliyowekwa na serikali kama mmojawapo wa mikakati ya kuzuia maambukizi ya Covid-19.

Sheikh Athman Mohammed kutoka Kaunti ya Kwale alisema kufuatia hali hiyo, amelazimika kutekeleza ibada zake nyumbani japo hakuna utulivu kama wa msikitini.

“Utulivu wa ibada uko chini nyumbani ikilinganishwa na msikitini  kwa sababu hapa kuna watoto ambao labda wanacheza, na unajipata ukiulizwa maswali kadha wa kadha ambayo yanatoa umakinifu wako katika maombi,” akasema Sheikh huyo.

Aliwashauri waumini kukithirisha maombi zaidi nyakati za usiku ambapo hakuna vishawishi vingi.

“Wakati huu watu hufanya ibada usiku na mchana kama njia ya kutaka msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini ibada zinapungua mchana kufuatia vishawishi mbalimbali,” akasema.

Katibu Mwandalizi wa Baraza la Waislamu na Wahubiri wa Kenya, Sheikh Mohamed Khalifa aliendelea kuwahimiza waumini kuzingatia utaratibu na sheria zilizowekwa na Wizara ya Afya kujilinda na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Alisema ni wakati mgumu kwa Wakenya na dunia nzima kwa jumla na hivyo ni muhimu kwa waumini kuomba janga la corona liishe mara moja.

“Ibada ya mwezi huu wa Ramadhan imetatizika pakubwa, lakini tunawaomba waumini wazidishe ibada nyumbani kwao,” akaeleza.

You can share this post!

Mikakati ipo kulainisha sekta ya utalii baada ya kunywea

DORTMUND MOTO: Schalke 04 yapata kichapo...

adminleo