• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Viboko wahangaisha wakazi na wavuvi Naivasha wakivamia maboma   

Viboko wahangaisha wakazi na wavuvi Naivasha wakivamia maboma  

NA RICHARD MAOSI

HATARI inawakodolea macho wavuvi na wakazi kutoka maeneo yanayopakana na Ziwa Naivasha, viboko wakitishia maisha yao.

Kulingana na wenyeji, wanyama hao wanavamia makazi na maboma, jambo linalozidisha hofu.

“Mara nyingi wao hunyatia makazi ya watu usiku kung’ata, kuua na kuharibu mazao changa shambani,” anasimulia afisa wa Usalama katika mkahawa mmoja eneo la South Lake ambaye tumebana jina.

Anasema sehemu kubwa ya Ziwa Naivasha haijazungushiwa uzio au waya wa umeme, hii ikimaanisha hakuna kizuizi cha kudhibiti safari za viboko ndani na nje ya ziwa hususan inapokuja katika makazi ya watu.

Ikumbukwe viboko hushinda majini kwa takriban masaa 12 kila siku, na ifikapo usiku huingia nchi kavu kusaka chakula, na kumshambulia yeyote ambaye watakumbana naye.

Viboko wamegeuka kuwa kero kwa wavuvi na wakazi Ziwa Naivasha, wakisababisha maafa. PICHA|RICHARD MAOSI

Anasema tangu serikali iweke ulinzi wa Coast Guards katika Ziwa Naivasha visa vya wavuvi kushambuliwa na viboko vimepungua.

“Kwa sababu kazi yao kubwa imekuwa ni kushika doria ziwani, kuhakikisha shughuli za kuendesha uvuvi haramu usiku zimekoma.”

Kati ya mwaka wa 2020 hadi 2021, zaidi ya visa 20 vya binadamu kuvamiwa, kujeruhiwa na kuuawa kwa viboko viliripotiwa.

Naibu kamishna wa Kaunti ndogo ya Naivasha, Mutua Kisilu mwaka uliopita alikiri kuwa hatua ya serikali kutumia huduma za Coast Guards kwa asilimia kubwa zilisaidia kupunguza visa vya viboko kuvamia wakazi.

Aidha, alisema mikakati kabambe imewekwa ili kusaidia wavuvi kupokea Zana za kuwahakikishia Usalama wao majini.

Waathiriwa

Mei 2021, George Mwaura alienda kuvua samaki katika Ziwa Naivasha na aliandamana na rafiki yake.

Kwa sababu ya hali ngumu ya uchumi hawangemudu kujinunulia boti, hivyo basi walilazimika kupiga mbizi majini na neti zao wakisaka samaki, ingawa walifahamu ni jambo hatari.

Lakini kiboko aliwavamia wakiwa majini na kumuua rafiki yake, Mwaura aKIponea chupuchupu kwa sababu alikuwa na ujuzi wa kuogelea.

Anasema wakazi wa eneo la South Gate na Karagita ndio mara nyingi hujikuta pabaya, ikiwa ni baada ya viboko kutengeza njia za mkato kutoka Ziwa Naivasha ili kuyafikia makazi.

Kiboko kando ya Ziwa Naivasha. PICHA|RICHARD MAOSI

 

  • Tags

You can share this post!

Alfred Keter: Tuonyeshwe vituo vya petroli vya Kenya Kwanza...

Gachagua amkashifu vikali Waziri Kuria

T L