• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Vilemba na nywele za rasta: Mbinu mpya ya walanguzi kusafirisha bangi   

Vilemba na nywele za rasta: Mbinu mpya ya walanguzi kusafirisha bangi  

NA RICHARD MAOSI

WALANGUZI wa dawa za kulevya na mihadarati wameibuka na mtindo mpya wa kusafirisha bidhaa hizo haramu, sasa ikifichuka kwamba wanatumia vilemba na nywele za rasta.

Hii ndiyo mbinu mpya ambayo wanatumia ili kuepuka wazee wa nyumba kumi, machifu na polisi kutambua bidhaa wanazosafirisha.

Kwa ustadi mkubwa sana wanaficha misokoto ya bangi ndani ya vilemba au kuvalia kofia nzito kiasi kwamba sio rahisi kuwashuku.

Mitaa ambayo biashara hii imenoga katika Kaunti ya Uasin Gishu ni pamoja na Kasarani, Panama, Kisumu Ndogo, Kambi Nguruwe na Yamumbi.

Baadhi ya bangi ambazo zimenaswa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Langas, Kaunti ya Uasin Gishu. PICHA|RICHARD MAOSI.

Jijini Nakuru mitaa ya Flamingo, Kaptembwa, Bondeni, Freearea, Murogi na Lakeview pia haijabaki nyuma.

Katika mtaa wa Kona Mbaya, Nakuru walanguzi wa mihadarati wamekuwa wakikabiliana na wazee wa nyumba kumi.

Kulingana na mzee wa nyumba kumi ambaye hakutaka kujulikana, anasema baadhi ya vijana wanashirikiana na maafisa wa polisi.

Hata hivyo, anawashutumu vijana kwa kujificha ndani ya mavazi ya kidini, ikizingatiwa kuwa ni kinyume na maadili mema ya kijamii.

Taifa Leo Dijitali pia imetambua kwamba vilevile wanatumia vibanda kandokando mwa barabara kama maficho yao.

“Hapa wanajifanya eti ni wauzaji wa nguo za mitumba, kumbe wanauza bangi, kutafuna mogoka au kuuza changaa,” anasema.

Mama Alice Moraa almaarufu kama mama Kade kutoka eneo la Kona Mbaya, anasema yeye ni muuzaji wa matunda na mboga ila nyakati za usiku vijana hutumia kibanda chake kuuza na kuvuta bangi.

Mama Kade anaomba polisi kuimarisha doria katika maeneo ya Kasarani, Panama na Kisumu Ndogo ili kukabili vijana ambao wamejiingiza kwenye ulanguzi wa dawa za kulevya na mihadarati.

“Wanauza mihadarati hata kwa watoto wa shule hasa wakati huu wa likizo ndefu ambayo huambatana na sherehe nyingi za mwisho wa mwaka,” akasema.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mwadime ataka mgao wa mbuga kabla ya Desemba

Mashabiki wa Karen Nyamu mitandaoni wafurahia kumuona...

T L