• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 4:28 PM
Vyombo vya habari kupeperusha matokeo ya kura

Vyombo vya habari kupeperusha matokeo ya kura

NA DAVID MWERE

KAMATI YA BUNGE kuhusu Haki na Sheria imewahakikishia wanahabari kuwa hawatazuiwa kupeperusha mbashara matokeo ya uchaguzi wa Agost 9 jinsi ilivyonakiliwa kwenye Mswada tata wa Uchaguzi 2022.

Kwenye mkutano na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Marjan Hussein, wanachama wa JLAC walisema hawana budi ila kutupilia mbali vifungu tata katika mswada huo.

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya alitia saini mswada huo na kuuwasilisha bungeni wiki iliyopita.

Mswada huo unalenga kuyafanyia marekebisho sheria ya vyama vya siasa na kuondoa kifungu kinachoruhusu matokeo ya uchaguzi kupeperushwa moja kwa moja jinsi yanavyotangazwa katika kituo cha kupiga kura.

“Matokeo ambayo yatakuwa yakipeperushwa yatafahamisha umma kuhusu takwimu za kila mwaniaji wala hayasisitizi kuwa lazima yatangazwe na IEBC,” inasema sheria ya sasa.

Kuondolewa kwa kifungu hicho cha sheria kutakuwa na maana kwamba runinga za hapa nchini na za mataifa ya nje, zitategemea takwimu zinazotolewa na IEBC.

Hata hivyo, Naibu Mwenyekiti wa JLAC Tom Kajwang’ (Ruaraka) alisema kuwa kamati hiyo bado haijaandaa kikao na IEBC kuhusu mswada huu.

Hata hivyo, alikariri kuwa iwapo itakuwa na maelezo ambayo kamati haikuidhinisha basi italazimu IEBC iwajibu kuhusu suala hilo.

“IEBC ilitoa pendekezo na sisi kama kamati tuliwashauri kuhusu sheria za kufuata.

Mswada huo utapitia kamati hii ili upigwe msasa na iwapo kutakuwa na maelezo ambayo hatukuidhinisha, IEBC itawajibikia hilo,” akasema Bw Kajwang’.

Aidha, mswada huo unasema IEBC itakuwa na mtandao maalum wa kupokea na kuchapisha matokeo na vyombo vya habari vitakuwa vikipata takwimu kuhusu uchaguzi huo kutoka kwa mtandao huo.

Mswada huo pia unalenga kuharamisha hatua ya Mwenyekiti wa IEBC kutangaza matokeo ya urais kabla ya hesabu za kura kutoka maeneobunge yote kuwasilishwa hata kama tume hiyo itakuwa imeridhishwa kuwa kura hizo hazitabadilisha matokeo ya mwisho.

Pia IEBC haitakuwa ikitangaza matokeo kwa mtindo maalum ambapo wao huanza na aliyevuta mkia hadi mshindi jinsi ilivyo kwa sasa.

Mbali na hayo, mswada huo unaamrisha kesi zinazopinga ushindi wa gavana zisikilizwe na ziamuliwe na mahakama kuu bila kuenda katika mahakama ya rufaa na hata ile ya juu.

Vivyo hivyo, inasisitiza kuwa kesi za kupinga uchaguzi wa madiwani zisikilizwe na kuamuliwa katika hatua ya mwisho na mahakama za hakimu.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yalemewa kukabili majangili Kerio

Video ya ‘njama’ ya shahidi dhidi ya Ruto ICC kuchezwa

T L