• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 3:17 PM
Walanguzi 3 wa dawa za kulevya wakamatwa

Walanguzi 3 wa dawa za kulevya wakamatwa

NA TITUS OMINDE

WASHUKIWA watatu wa ulanguzi wa dawa za kulevya walikamatwa Jumapili na maafisa wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Turbo.

Washukiwa hao walikamatwa wakiwa na misokoto 375 za bangi kwenye kingo za mto Sosiani, eneo la Maangula maarufu kwa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi Kaunti Ndogo ya Turbo Edward Masibo alisema washukiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika huku wakitarajia kukamata walanguzi zaidi.

“Tumeimarisha operesheni zetu dhidi ya dawa za kulevya na pombe haramu, tunawahakikishia wananchi kwamba operesheni hiyo itaimarishwa” alisema Bw Masibo.

Afisa huyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwa polisi kuhusu washukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya katika kaunti ndogo ya Turbo.

Bw Masibo alitoa hakikisho kuwa watakaotoa taarifa, watalindwa na taarifa hiyo kuwekwa kama siri ili kuwalinda dhidi ya kuvamiwa na wahuni.

Wakati huo huo, katika Kaunti Ndogo ya Soy watu 58 wametiwa mbaroni katika operesheni sawia inayoendelea dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya.

Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo Bw Henry Zuma anasema zaidi ya lita 1, 000 za chang’aa, lita 60 za busaa na lita 4, 590 za kangara zilinaswa na kuharibiwa na maafisa wa polisi mwishoni mwa juma.

“Nataka kuwasihi wananchi wetu hasa katika mitaa ya Kamukunji, Vumilia na Jabali waachane na biashara ya pombe haramu na biashara ya dawa za kulevya, hakuna atakayesazwa katika operesheni hii inayoendelea,” alionya Bw Zuma.

Tayari baadhi ya watu 58 waliokamatwa kati ya Aprili 13 na Mei 6 kuhusiana na ulanguzi wa dawa za kulevya wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Wananchi kuwa na usemi mkuu katika biashara ya pombe

Kampuni ya maji yashtakiwa kwa kuhatarisha afya

T L