• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
Waqo akaidi tena mwaliko wa PIC

Waqo akaidi tena mwaliko wa PIC

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Halakhe Waqo Ijuma alikaidi mwaliko kwa kutofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) inayochunguza sakata ya ununuzi wa vifaa vya Covid-19 na Shirika la Kusambaza Dawa na Vifaatiba (Kemsa).

Hii ndiyo ilikuwa mara ya pili kwa Waqo ambaye ni mwanachama wa Bodi ya Vyuo Vikuu kufeli kufika mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, kujibu maswali kuhusu uhusiano wake na sakata hiyo ya kiasi cha Sh7.8 bilioni.

Bw Waqo alihusishwa na kampuni ya Aszure Commercial Services ambayo ilipwa Sh347 milioni na Kemsa kwa kuwasilisha bidhaa za Covid-19 baada ya kupewa zabuni kinyume cha sheria.

Jina la Afisa huyo Mkuu Mtendaji wa EACC ilitajwa na mkurugenzi mmoja wa kampuni hiyo alipokuwa akijibu maswali mbele ya kamati hiyo kuhusiana na sakata hiyo.

Mkurugenzi huyo, kwa jina Bw Zubeda Nyamlondo, aliwaambia wanachama wa PIC kwamba Bw Waqo alitia saini stakabadhi kama mdhamini wa Aszure Commercial Services, ilipoomba mkopo kutoka kwa benki ya First Community Bank.

Bw Nassir na wabunge wanachama wa PIC wanataka kupewa majibu kuhusu ni jinsi kampuni hiyo ilivyopewa zabuni ya kuwasilisha barakoa kwa Kemsa ilhali haijasajiliwa kuuza vifaa vya kimatibabu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) Abdulswamad Nassir akihutubia wanahabari katika majengo ya bunge, Ijumaa, Machi 12, 2021. Hii ni baada ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Halakhe Waqo kutofika mbele ya kamati yake kujibu maswali baada ya kuhusishwa kwake (Waqo) na sakata ya Sh7.8 bilioni katika Kemsa. Picha/ Charles Wasonga

Aszure Commercial Services imesajiliwa kama kampuni ya kuuza fanicha za afisi na vifaa vinginevyo vya nyumbani wala sio bidhaa za kimatibabu.

Akiongea na wanahabari Ijumaa katika majengo ya bunge baada ya kupata habari kwamba Bw Waqo hangefika mbele yao, Bw Nassir alisema kamati hiyo haitatoa mwaliko mwingine kwake bali itatoa agizo kwamba afike kwa lazima.

“Hatutakubali arifa zake anazawasilisha kwa njia ya simu kwamba hatafika. Hii ni mara ya pili kwa Bw Waqo kususia mwaliko wa kumtaka afanye hivyo. Kinachosalia sasa ni kwa Kamati hii kutoa amri kwamba afike kwa lazima,” mbunge huyo wa Mvita akawaambia wanahabari.

You can share this post!

Chepkirui, Cherotich wang’ara mbio za mita 5,000...

Newcastle United na Aston Villa waridhika na sare katika...