Lori la polisi lagonga nyumba za mtaa wa mabanda

Na STEVE NJUGUNA

LORI la polisi Jumamosi lilikosa mwelekeo na kugonga nyumba za watu katika mtaa wa mabanda wa Maina, viungani mwa mji wa Nyahururu, Kaunti ya Laikipia.

Kwa mujibu wa Naibu Chifu Purity Mumbi, dereva wa lori hilo lililokuwa kwenye barabara ya Nyahururu-Maralal alipoteza udhibiti wake kisha likagonga nyumba hizo za mbao na kusababisha uharibifu mkubwa.

Hata hivyo, wananchi walifika katika eneo la tukio hilo baada ya ajali hiyo ya saa mbili usiku na kumwondoa mtoto mwenye umri wa miaka 10 ambaye alikuwa amefunikwa kwenye vifusi.

Mtoto huyo mvulana alivunjika mguu na akapelekwa hospitalini.

Rais aongoza Wakenya kuomboleza seneta aliyefariki kwa ajali

Na Mary Wangari

VIONGOZI na wanasiasa mbalimbali wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na naibu wake, Dkt William Ruto jana waliungana na Wakenya kumwomboleza Seneta Mteule, Victor Prengei, aliyefariki katika ajali ya barabarani.

Kupitia kwa taarifa kwa vyombo vya habari, Rais Uhuru alimtaja marehemu kuwa kiongozi shupavu aliyejitahidi kuboresha maisha ya vijana na jamii za wachache nchini.

“Inahuzunisha sana kuwa kifo kimetupoka kiongozi hodari na mchanga aliyejitahidi kuimarisha maslahi ya vijana na jamii za wachache,” taarifa ikasema.

Seneta huyo wa Chama cha Jubilee aliaga dunia baada ya kuhusika kwenye ajali Jumatatu, saa tatu na robo usiku, kwenye barabara ya Kabarak-Nakuru.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyoonwa na Taifa Leo, gari la Bw Prengei lilipoteza mwelekeo katika eneo la Kioto, kabla ya kuyumbayumba na kugonga ukuta.

Seneta huyo aliyekuwa amejeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Moi Memorial ambapo alikata roho alipokuwa akitibiwa.

Marehemu alikuwa miongoni mwa maseneta sita waliofikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu katika chama cha Jubilee mapema mwaka huu.Kupitia rambirambi zake, Naibu Rais alimtaja marehemu kama kiongozi aliyejitolea mhanga kutetea haki za walio wachache.

“Taifa letu limempoteza mwanamme muungwana. Seneta Victor Prengei alikuwa mpole na mtumishi wa umma aliyejitolea kuendeleza maslahi ya walio wachache,” alisema.

Huku akifariji familia na jamaa wa marehemu, Kiongozi wa ODM Raila Odinga alimwomboleza Seneta Prengei akisema “kifo chake cha ghafla ni pigo kuu kwa jamii ya Ogiek na bunge.”

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alituma rambirambi zake akisema jamii ya Ogiek, Seneti na taifa kwa jumla limempoteza kiongozi aliyewakilisha matumaini makubwa.

Akielezea kushtshwa na habari hizo, Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula alisema Bw Prengei alikuwa muundasheria aliyekuwa na uhusiano mwema na wenzake katika seneti huku akitoa wito kuhusu kuimarisha usalama barabarani.

Kwa upande wake, Seneta Mteule Millicent Omanga alimwomboleza marehemu akisema kuwa juhudi zake zitakumbukwa milele.Seneta wa Nakuru Susan Kihika alimtaja marehemu kama rafiki na “mwakilishi wa vijana mwenye unyenyekevu aliyewakilisha wanajamii walio wachache katika Seneti.”

“Kaka yangu.Hii inaumiza sana. Maisha ni nini hasa? Upo hapa leo kesho umeenda. Mwenyezi Mungu aingilie kati…,” aliomboleza Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot..

Majonzi 18 wakifa ajalini

Na WAANDISHI WETU

WATU 18 walifariki Jumamosi katika ajali za barabarani maeneo mbalimbali nchini, huku idadi ya visa hivyo ikiendelea kupanda baada ya serikali kufungua nchi wiki moja iliyopita.

Katika eneo la pwani, watu watano wa familia moja Jumamosi asubuhi walifariki katika ajali ya barabarani katika eneo la Taru kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Watano hao walikuwa wakienda kwa mazishi.

Polisi walisema kuwa watu wengine wanne walinusurika katika ajali hiyo iliyotokea saa kumi na moja na dakika 10 za alfajiri.

Watu hao walikuwa wakisafiri kutoka Mombasa kwenda Kisumu gari lao lilipogonga trela iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi kwenda Mombasa.

Kamanda wa polisi wa trafiki eneo la Pwani, Bw Peter Maina alisema watu hao walifariki papo hapo. Manusura ambao wako katika hali mbaya wanatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kinango.

Bw Maina alisema visa vya ajali ya barabarani vimekithiri eneo hilo na kwamba maafisa wake watatumia vifaa vya kudhibiti kasi ya magari kama njia ya kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za trafiki.

Katika Kaunti ya Kakamega, watu watano walifariki papo hapo baada ya lori moja kugongana na pikipiki mbili katika eneo la Emukangu katika barabara ya Ekero-Buyangu.

Akithibitisha ajali hiyo, kamanda wa trafiki eneo la Butere, Bw George Owori alisema miili ya waliofariki ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Butere.

Wakati huo huo, watu watatu walifariki Jumamosi katika ajali tofauti za barabarani katika barabara ya Kenol-Murang’a.

Bodaboda wawili walifariki walipogongwa na magari ambayo baadaye yalitoweka. Mmoja aligongwa nje ya kituo cha polisi cha Maragua, Kaunti ya Murang’a.

Maafa mengi yalitokea katika daraja la Sabasaba karibu na kituo cha usambazaji maji, eneo ambalo linachukuliwa kuwa lenye mikosi ya ajali. Mwendesha bodaboda aligongwa na gari na kurushwa ndani ya mto.

Afisa mkuu wa polisi wa Murang’a Kusini, Anthony Keter alisema ajali hizo zinachunguzwa ili kubaini kiini chake.

Watu wengine wanne Jumamosi walifariki katika Kaunti ya Nyeri baada ya magari mawili kugongana eneo la Solio katika barabara kuu ya Nyeri-Nyahururu.

Watu wengine wawili walikimbizwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya katika ajali hiyo iliyohusisha gari la aina ya Nissan na jingine aina ya probox.

Akithibitisha ajali hiyo, Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Kieni Magharibi, Ahmed Ali alisema ajali hiyo ilitokana na kupasuka kwa gurudumu moja la mojawapo ya magari hayo.

Mnamo Alhamisi, watu watano walifariki katika ajali ya barabarani eneo la Shangia katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Eneo hilo liko kilomita chache kutoka mahala ambapo ajali ya Jumamosi ilitokea Taru.

Taarifa za Anthony Kitimo, Shabaan Makokha, Mwangi Muiruri na Steve Njuguna

Watatu wafariki lori na matatu zikigongana mjini

Na WACHIRA MWANGI

WATU watatu walifariki jana kwenye ajali iliyotokea katika Barabara ya Makupa, Kaunti ya Mombasa.

Kamanda wa Trafiki katika ukanda wa Pwani, Bw Peter Maina, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, iliyohusisha matatu na lori.

Kulingana na walioshuhudia, matatu hiyo ilipoteza mwelekeo na kugongana na lori hilo lililokuwa likielekea Mombasa.

Matatu hiyo ambayo inamilikiwa na Kampuni ya Matco Sacco iliondoka jijini Mombasa asubuhi ikielekea Kitui wakati ajali hiyo ilipofanyika.

Dereva wa lori hilo, Bw Daniel Omondi, alisema alibahatika sana kunusurika ajali hiyo pamoja na kondakta wake.

“Matatu hiyo ilikuwa ikisafiria upande wangu. Nusura nitumbukie baharini kwani nilikuwa nikijaribu kuepuka kugongana nayo. Hata hivyo, iliingia upande wangu ndipo ajali ikatokea,” akasema Bw Omondi aliyeongeza kuwa alikuwa amesafiri usiku kucha kutoka Nairobi.

Miili ya waliofariki ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Coast General.

18 wafariki kwenye ajali mbili tofauti Kisumu, Kilifi

CHARLES LWANGA na ALDRIN OCHIENG

WATU 18 walifariki Jumatano kwenye ajali mbili tofauti za magari katika kaunti za Kilifi na Kisumu.

Kwenye ajali ya Kilifi, watu 14 walifariki papo hapo na mmoja akipelekwa hospitalini, baada ya basi la Muhsin kugongana ana kwa ana na matatu eneo la Kwa Shume, barabara kuu ya Mombasa kuelekea Malindi.

Kamishna wa Kaunti ya Kilifi, Kutswa Olaka, aliyeongoza polisi na maafisa wa Msalaba Mwekundu kuokoa majeruhi, alisema madereva wote wawili walifariki dunia papo hapo.

“Ajali hii imehusisha basi ya Muhsin linalosimamiwa na Garissa Sacco, ambalo lilikuwa likisafiri kutoka Mombasa kuelekea Garissa na matatu ya Sabaki Travellers Shuttle iliyokuwa inatoka Malindi kuelekea Mombasa,” akasema. Bw Olaka.

Walioshuhudia walisema basi la Muhsin lilipoteza mwelekeo baada ya kupasuka gurudumu na kugongana na matatu hiyo.

Msimamizi wa hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi, Dkt Joab Gayo, alisema aliona miili 14 ambayo ilipelekwa katika chumba cha maiti.

“Tulipokea watu 18 wakiwa wamejeruhiwa. Kati yao sita waliokuwa katika hali mahututi wamepelekwa hospitali Mombasa kwa matibabu maalum,” akasema.

Dkt Gayo alisema watu wengine waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo walipelekwa katika hospitali za kibinafsi kama vile Tawfiq na Star mjini Malindi.

Dereva wa basi la Simba Coach, ambaye alikuwa safarini wakati wa mkasa huo, alimlaumu mkandarasi anayepanua barabara kuu ya Malindi- Mombasa kwa kuchukua muda mrefu.

“Inawezekana mabonde na mashimo kwenye barabara hii inayoendelea kupanuliwa yamechangia kupasuka kwa gurudumu. Tunaomba serikali imhimize akamilishe kazi hii ambayo imechukua muda mrefu,” akasema dereva huyo.

Kamishna wa Kaunti ya Kisumu, Samuel Anampiu kwa upande wake alisema lori la kubeba miwa liliacha njia likiwa kwenye kivuko kwenye barabara ya juu ya Kachok eneo la Nyamasaria na kuanguka umbali wa mita 20.

“Dereva wa trela hilo la kubeba miwa alikufa papo hapo. Watu wawili aliokuwa nao walikufa walipokuwa wakikimbizwa hospitalini,” alisema Bw Anampiu.

Magari mawili yaliyokuwa yakioshwa chini ya barabara hiyo ya daraja yaliharibiwa.

Hata hivyo, hayakuwa na watu wakati wa ajali hiyo.

Trela hilo lilikuwa likisafirisha miwa kutoka eneo la Awasi.

Kulingana na Bernard Otieno, ambaye alishuhudia ajali hiyo, trela lilikuwa likipanda kwa kasi mno. Vijana ambao huosha magari chini ya mwinuko huo wa barabara walikimbilia usalama wao.

Miili ya waliokufa ilipelekwa katika chumba cha maiti ch hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga.

Matatu iliyoua abiria 9 ilikiuka kanuni za kudhibiti Covid-19

JOSEPH OPENDA na HILLARY KIMUYU

MATATU iliyohusika katika ajali iliyowaua watu tisa Ijumaa eneo la Gilgil ilikuwa imekiuka masharti ya kuzuia Covid-19, polisi wameelezea.

Taifa Leo imebaini kuwa, matatu hiyo ya shirika la Mololine Shuttle iliyogongana moja kwa moja na trela katika eneo la Soysambu, Gilgil, kwenye Barabara Kuu ya Nakuru-Nairobi, ilikuwa imejaza abiria katika viti vyote, kinyume na masharti ya Wizara ya Afya kuhusu kudumisha umbali wa kutangamana.

Kamanda wa Polisi eneo la Gilgil Jonh Onditi alisema, matatu hiyo ilikuwa ikisafirisha abiria 14 Nairobi kabla ya kugongana na trela nyingine.

Watu wasiopungua tisa walithibitishwa kufariki huku wengine watano wakilazwa katika hospitali mbalimbali wakiwa na majeraha tofauti tofauti.

Bw Onditi alisema trela hiyo iliyokuwa ikielekea upande wa Nakuru ilikuwa ikijaribu kupita gari lingine ilipogongana na matatu iliyokuwa ikitoka upande mwingine mwendo wa saa kumi na moja alfajiri.

“Kulingana na mkuu wa polisi, watu wanane walifariki papo hapo huku mmoja akipata majeraha na kutangazwa kufariki alipowasili katika Hospitali ya Misheni ya St Joseph,” alisema Bw Onditi.

Afisa wa hospitali hiyo aliyekuwa kwenye zamu Bw Dominic Mutua alisema walipokea wahasiriwa watano kutoka eneo la ajali hiyo lakini mmoja akaaga dunia.

Alisema wagonjwa wawili walikuwa na majeraha mabaya na wakahamishwa katika Hospitali ya Nakuru ya Level Five huku wawili waliosalia wakitibiwa na hali yao kudhibitiwa.

Manusura mmoja wa ajali hiyo, Bi Mercy Wacuka alisema familia yao iliondoka nyumbani mjini Njoro saa nane alfajiri na walikuwa wakielekea Nairobi kuwatembelea wazazi wake.

Walipofika Nakuru, waliabiri matatu hiyo iliyoondoka kituoni saa kumi alfajiri.

“Nilikuwa nimeketi nyuma ya dereva pamoja na mume wangu na mtoto wetu wa miaka mitano. Wakati wa ajali hiyo, nilikuwa nimelala kabla ya kuamshwa na mayowe kutoka kwa abiria wengine waliojeruhiwa,” alisema Bi Wacuka.

Yeye pamoja na mtoto wake walinusurika kifo lakini mume wake hakuwa na bahati.

Kwingineko, maelfu ya waendeshaji magari na abiria Ijumaa walikwama katika msongamano mbaya wa trafiki katika Barabara Kuu ya Thika Super Highway.

Mkuu wa Trafiki jijini Nairobi Joshua Omukata alisema msongamano huo ulisababishwa na ajali ambapo trela ya kuchanganya simiti ilibingiria katika Barabara ya Wangari Maathai, karibu na Kituo cha Petroli cha Shell.

“Trela ya kuchanganya simiti ilianguka kwenye barabara ya Wangari Maathai mapema Ijumaa asubuhi na kufunga kabisa barabara kuu kabla ya kusababisha msongamano wa trafiki. Kreni mbili zilishindwa kuondoa trela hiyo ambapo ya tatu iliitwa,” alisema tatu Bw Omukata.

Bwanyenye wa Zimbabwe ashangaza alivyopanga maziko yake kabla ya mauti

MASHIRIKA NA WANGU KANURI

BWANYENYE mtajika nchini Zimbabwe Genius Kadungure almaarufu Ginimbi ameshangaza wengi baada ya kuibuka kuwa alikuwa amenunua jeneza wiki moja kabla ya ajali iliyoyakatisha maisha yake kufanyika.

Isitoshe, dadake marehemu, Juliet Kadungure amefichua kuwa kakake alikuwa amepanga jinsi mazishi yake yatakavyoendeshwa mwezi mmoja kabla ya kufa kwake huku akiwa na orodha kamili ya watakaohudhuria, wageni waheshimiwa na mavazi yatakayovaliwa na kila mtu atakayehudhuria.

Kulingana na ombi la Ginimbi, kila mtu atakayehudhuria kwenye mazishi yake sharti avalie mavazi meupe. Mavazi hayo yamenasibishwa na jinsi Ginimbi alivyovalia alipokuwa kwenye sherehe zake.

Vile vile, Juliet aliongeza kwa kusema kuwa kulingana na utaratibu ambao marehemu Ginimbi alikuwa amewacha, marafiki zake ambao wanaishi barani Afrika sharti wawepo kwenye mazishi na kama watachelewa basi mazishi yaahirishwe.

Alizidisha kwa kusema kuwa marehemu alitaka asizikwe kwa haraka. Hali kadhalika, marehemu Ginimbi alitaka jumba lake kifahari lifanywe hoteli ama jumba la makumbusho atakapoaga.

Imeripotiwa kuwa Ginimbi alikuwa akiliendesha gari lake aina ya Rolls Royce Wraith kwa kasi alipogongana na gari aina ya Honda Fit.

Gari lake Ginimbi liliondoka barabarani na kugonga mti ambapo liliteketea kadiri ya kufahamika huku likimuua pamoja na waabiri wenzake ambao ni Mimie Moana, rafikiye wa kike wa Moana Elisha na rafikiye Ginimbi, Limumba Karim. Watatu hao waliteketea kadiri ya kujulikana huku mwili wa Ginimbi ukiwa na majeraha ya moto.

Ginimbi alikuwa akitoka katika sherehe ya kuzaliwa kwa Michelle Amuli almaarufu Mimie Moana katika klabu mojawapo mjini Harare ya Dreams.

Saa chache kabla ya mwendazake kuondoka nyumbani kwake na kuelekea katika klabu hiyo ya Dreams, aliwarekodia video wafuasi wake akiwafahamisha kule atakakokuwa kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram.

“Ni wakati wa kutoka. Tunaenda klabu ya Dreams baada ya dakika chache zijazo ambako kutakuwa na sherehe. Tutakuwa tukisherehekea siku ya kuzaliwa kwake Moana na tutazifungua mvinyo kadhaa. Tuonane huko,” alisema.

Mwendazake Genius Kadungure alikuwa amevutiwa sana na biashara ya petroli na gesi na hadi kifo chake alikuwa mwanabiashara tajika mwenye kampuni ya uuzaji wa gesi nchini na hata nchi jirani.

Alifahamika na wengi kwa vile alivyoishi na alivyokuwa na magari ya kifahari aina nyingi ambayo ni Bentley Continental, Ferrari, Rolls Royce Ghost, Lamborghini Aventador S Roadster, Rolls Royce Wraith, Range Rovers, Mercedes Benz S Class na BMW.

Marehemu Ginimbi atazikwa Novemba 14, 2020 katika shamba lake kama alivyotaka.

Simanzi vijana watano marafiki wakiangamia ajalini

Na Mwangi Muiruri

HALI ya majonzi imetanda katika kijiji cha Kagurumo, Muthithi Kaunti ya Murang’a, baada ya vijana watano marafiki kufariki pamoja kwenye ajali ya pikipiki.

Wakazi wa kijiji hicho wasema bado wamo kwenye hali ya mshtuko kufuatia tukio hilo la Oktoba 25, ambapo mabarobaro hao waliokuwa wamealikwa na mwenzao kusherehekea hatua yake ya kupata pikipiki kufanyia kazi ya bodaboda waliangamia.

Waliofariki kwenye ajali hiyo walitambuliwa kama Samuel Chege, 25, Moses Kamande, 21, James Wanyoike, 25, Duncan Muchiri, 33, na mtu mwingine ambaye hakutambuliwa.

Inadaiwa kuwa siku hiyo, Bw Chege alienda katika kituo cha kibiashara cha Kamucii, na kufanikiwa kupata pikipiki, ambapo angeajiriwa na mwenyewe kama kibarua, kwa kuwabeba watu na kumlipa baadaye.

Kutokana na furaha aliyokuwa nayo, aliwaalika wenzake ‘kuifanyia majaribio’ pikipiki hiyo na kusherehekea mafanikio hayo.Kama sehemu ya ‘sherehe’ hizo, walipanda pikipiki kuelekea katika kituo hicho cha kibiashara.

Hii ni licha ya kanuni za serikali kuhitaji pikipiki kuwabeba watu wawili pekee; dereva na abiria wake.Inadaiwa watano hao walifariki mwendo wa saa sita usiku, pikipiki hiyo ilipogongana na lori katika eneo la Makenji.Cha kusikitisha ni kuwa wakati wa ajali hiyo, wote walikuwa walevi.

 

ONYANGO: Ajali za barabarani zitaangamiza maelfu ya raia hadi lini?

KUONGEZEKA kwa ajali za barabarani nchini licha ya kuwepo kwa marufuku ya kusafiri usiku na uuzaji wa pombe, kunafaa kushtua serikali.

Katika hotuba yake ya Septemba 28, Rais Uhuru Kenyatta aliwaambia Wakenya kuwa vikwazo vilivyowekwa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona – kama vile kafyu, kutojaza abiria kwenye matatu na marufuku ya kuuza pombe –vilisaidia pakubwa kupunguza visa vya uhalifu na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa Rais Kenyatta, visa vya uhalifu vilipungua kwa asilimia 21 kati ya Machi na Septemba. Ajali za barabarani zilipungua kwa asilimia 10 ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka jana.

Lakini takwimu kuhusu vifo vilivyotokana na ajali za barabarani zilizotolewa hivi karibuni na idara ya polisi, zinatoa taswira tofauti.Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa ajali za barabarani zimeongezeka kwa asilimia 1.3 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.Watu 2,689 walifariki katika ajali za barabarani kati ya Januari 1 na Septemba 30, mwaka huu.

Watu 2,655 waliangamia katika kipindi sawa na hicho mwaka uliopita.Takwimu hizo zinaonyesha kuwa pikipiki zilisababisha vifo vya watu 1,075 kati ya Januari na Septemba 30, mwaka huu.

Watu 971 waliangamia kwa kukanyagwa na magari au pikipiki mwaka huu. Kenya ilipoteza madereva 233. Watumiaji wa baiskeli 68 pia walipoteza maisha yao barabarani katika kipindi cha miezi tisa iliyopita.

Kwa ufupi, ajali za barabarani zimeua watu wengi zaidi humu nchini kuliko virusi vya corona kati ya Machi na Oktoba.Wengi tulitarajia kuwa mwaka huu ungekuwa na idadi ndogo zaidi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani. Hii ni kwa sababu kwa miezi saba sasa pamekuwapo kafyu wala magari hayaruhusiwi kusafiri usiku.

Hiyo inamaanisha kuwa ajali hizi zinatokea kati ya alfajiri na jioni. Kwa muda wa miezi sita baa zilikuwa zimefungwa. Uwezekano wa madereva kuendesha magari wakiwa walevi uko chini.

Aidha, magari yamekuwa yakibeba asilimia 60 ya abiria ili watu wasikaribiane katika juhudi za kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Hivyo basi, hatuwezi kusema kuwa ajali hizo zinasababishwa na hatua ya matatu kubeba abiria kupita kiasi.Serikali haina budi ila kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kiini cha ajali hizi mbaya za barabarani nchini humu.

Wawili wajeruhiwa baada ya V8 kugonga nguzo za barabarani

Na SAMMY WAWERU

WATU wawili Jumanne wamenusurika kifo baada ya gari walimokuwa kupoteza mwelekeo na kugonga chuma katika barabara kuu ya Thika Superhighway.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Carwash, kati ya mtaa wa Githurai na Kasarani.

Kulingana na walioshuhudia, gari hilo aina ya V8 lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi.

“Lilikuwa kwa mwendo wa kasi sana, na tuligutushwa na kishindo cha kugonga chuma kilichoko kandokando mwa barabara ya kasi, hadi kikajipinda,” mhudumu mmoja wa bodaboda akaambia Taifa Leo.

Alisema baada ya kugonga chuma, lilielekea katika upande – leni – ya kasi ya juu.

“Ni bahati tu magari yaliyokuwa nyuma yake, yalikuwa mbali,” akasema.

Akithibitisha tukio hilo, mmoja wa maafisa wa trafiki wanaohudumu eneo hilo Fridah Makena, alisema hakukuwa na majeraha.

“Lilikuwa na watu wawili na hakuna aliyejeruhiwa. Hata hivyo, tunaonya watumizi wa Thika Road wawajibike sababu kuendesha gari kwa mwendo wa kasi ni hatari,” akasema.

Visa vingi vya ajali Thika Road vinahusishwa na utepetevu miongoni mwa madereva, uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi na ubadilishaji wa leni kiholela, hasa katika barabara ya kasi.

Eneo la Carwash, limetajwa kuwa hatari kutokana na ajali za mara kwa mara.

“Eneo hili kila wiki halikosi ajali. Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini (KeNHA), itathmini eneo hili,” akapendekeza mmoja wa wenyeji.

Kulingana na mkazi huyo, maafa na majeruhi yameshuhudiwa eneo hilo, licha ya maafisa wa KeNHA kuonekana kupiga doria kila siku.

Mmoja afariki katika ajali Limuru

Na MARY WANGARI

MTU mmoja amefariki Jumatano abiria wengine kadhaa wakiuguza majeraha mabaya kufuatia ajali iliyohusisha matatu na lori la mchanga katika eneo la Mutarakwa, Limuru, Kaunti ya Kiambu, mnamo Jumatano.

Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa tatu asubuhi dereva wa matatu hiyo iliyokuwa ikielekea eneo la Ndeiya kutoka Limuru aliposhindwa kuidhibiti, kulingana na Kamanda wa Polisi katika Kituo cha Polisi cha Tigoni, Bw Joseph Ireri aliyezungumza na Taifa Leo.

Afisa huyo ameeleza kuwa matatu hiyo ilipoteza mwendo na kugongana na lori la kusafirishia mchanga kwenye barabara kati ya Mai Mahiu – Nairobi.

Aidha, alieleza kuwa majeruhi katika ajali hiyo walipelekwa katika Hospitali ya Limuru Nursing Home almaarufu ‘Kwa Patel.

“Dereva alishindwa kudhibiti gari hilo; tumepoteza mtu mmoja na majeruhi wamepelekwa katika kituo cha afya cha Limuru Nursing Home kwa matibabu,” amesema Bw Ireri.

Afisa huyo aliwahimiza madereva kuwa waangalifu na kuhakikisha magari yao hayana hitilafu yoyote wanaposafirisha abiria, akiongeza kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini cha ajali hiyo.

Kisa hicho kimejiri huku ajali katika barabara hiyo inayounganisha eneo la Mutarakwa na Thogoto, Kikuyu, zikizidi kuongezeka kwa kasi eneo hilo na kuibua wasiwasi miongoni mwa wakazi.

Waendeshaji magari wameelekezewa kidole cha lawama kwa kukosa uangalifu kwenye barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Mmoja apata majeraha baada ya kuhusika katika ajali Thika Road

Na SAMMY WAWERU

WATU watano walinusurika kifo katika ajali iliyotokea Jumatano jioni katika barabara ya Thika Superhighway.

Ajali hiyo iliyotokea eneo la Clayworks, kati ya Roysambu na Githurai, ilihusisha magari mawili ya kibinafsi.

Akithibitisha mkasa huo, afisa mmoja wa trafiki anayehudumu Thika Road alisema mtu mmoja alipata majeraha.

“Gari moja lilikuwa na watu wawili na lingine watatu, mmoja miongoni mwao alipata majeraha na amepelekwa hospitalini,” afisa huyo akasema.

Aidha, ajali hiyo ilifanyika katika leni ya kasi, na kulingana na afisa huyo wa trafiki uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini.

Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa manusura na aliyekuwa katika gari lililokuwa mbele, alimokuwa liligongwa kutoka nyuma. “Liliendeshwa kwa mwendo wa kasi, na ni kwa neema ya Mungu tumenusurika kifo,” alieleza.

Ajali hiyo imetokea majuma kadhaa baada ya nyingine kufanyika mita kadhaa kutoka eneo la tukio la Jumatano.

Mnamo Juni 13, 2020, watu watatu waliponea kifo kwa tundu la sindano baada ya lori la kusafirisha kokoto na vifaa vya ujenzi, walimokuwa, kupoteza mwelekeo likiwa katika leni ya kasi, likang’oa vyuma vya kando ya barabara na kuanguka katika mtaro wa majitaka ulio kati ya leni ya kasi na ya nje inayotumika kuchukua na kushusha abiria.

Visa vya ajali Thika Superhighway vinaendelea kuongezeka, uendeshaji wa magari kwa kasi na ubadilishaji leni bila uangalifu vikitajwa kama visababishi vikuu.

Pia, eneo kati ya Roysambu na Githurai, limeanza kumulikwa kutokana na ajali za mara kwa mara.

Watatu wanusurika baada ya lori kuanguka Thika Superhighway

Na SAMMY WAWERU

WATU watatu Jumamosi wamenusurika kifo baada ya lori la kusafirisha kokoto na vifaa vya ujenzi kuanguka eneo la Carwash katika barabara kuu ya Thika Superhighway.

Watatu hao ni dereva na wasaidizi wake wawili.

Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo iliyofanyika eneo la Carwash, kati ya mtaa wa Rosyambu na Githurai, lori hilo lenye nambari za usajili KCH 364T, lilikuwa katika mwendo wa kasi.

“Inaonekana breki zilikataa kufanya kazi, likapoteza mwelekeo wa barabara,” mmoja wa wahudumu wa bodaboda Carwash akaambia Taifa Leo.

Aidha, lori hilo lililokuwa limebeba kokoto lilikuwa katika barabara ya kasi. Liling’oa vyuma vya kando ya barabara na kuanguka katika mtaro wa majitaka ulio kati ya barabara ya kasi na ya nje inayotumika kuchukua na kushusha abiria, ikiwa ni pamoja na magari kutoka Thika Superhighway na kuingia.

Vilevile, tangi la mafuta, gurudumu la kulia la mbele na kioo cha mbele, vyote vilitoka.

“Alichokifanya cha busara dereva huyo ni kujaribu kuliondoa katika barabara ya kasi. La sivyo ingekuwa hasara ya maafa na majeraha mabaya, ikizingatiwa kuwa barabara hii magari huenda kwa mwendo wa kasi,” akasema dereva mmoja wa basi linalohudumu katika barabara hiyo.

Maafisa wa Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini, ndiyo KeNHA, waliofika wamewataka watumizi wa barabara hiyo wawe waangalifu, wakihimiza madereva kupunguza kasi.

Mei 2020 kulikuwa na ajali nyingine iliyohusisha lori la mizigo mitaa chache kutoka katika tukio la Jumamosi.

Ni mwezi huo huo ambapo mwanamuziki wa nyimbo za Benga za jamii ya Agikuyu Jimmy Walter maarufu kama Jimmy Wayuni aliangamia katika ajali eneo la Kahawa Sukari, karibu na Chuo Kikuu cha Kenyatta, KU..

Visa vya ajali Thika Superhighway vinaendelea kuongezeka, uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi na kubadilisha leni bila uangalifu ukitajwa kama kiini kikuu cha mikasa ya ajali.

Wawili wanusuruka kifo katika ajali Thika Superhighway

Na SAMMY WAWERU

WATU wawili Jumamosi wamenusurika kifo baada ya lori walimokuwa kuhusika katika ajali mbaya katika barabara ya Thika Superhighway eneo la Carwash, Githurai.

Wawili hao ni dereva wa lori la masafa marefu na kondakta wake.

Kulingana na dereva, lori hilo lenye nambari za usajili KBU 591R lilipoteza mwelekeo baada ya usukani wake kujiloki likiwa kwenye kasi.

“Ni kwa neema ya Mungu tumenusurika na halikuhusisha gari jingine,” akasema.

Usukani wa lori kujiloki na kutajwa kama tukio hatari barabarani linaloweza kusababisha maafa, kichwa cha lori hilo lililokuwa katika leni ya kasi, kilijipinda upande wa kulia na kung’oa vyuma kadhaa vya reli.

Lori hilo lililokuwa likielekea Nairobi hata hivyo halikuwa na mizigo.

Akithibitisha kisa hicho, afisa Antony Guchu wa kitengo tamba cha trafiki Thika Road, amehimiza madereva kuwa waangalifu na kuhakikisha magari yao yanakaguliwa iwapo yana hitilafu yoyote kabla kuingia barabarani.

“Kuendesha gari kwa mwendo wa kasi kunaua, mbali na kujihatarishia maisha yako mwenyewe kama dereva pia unahatarishia maisha ya watumizi wengine wa barabarani,” Bw Guchu akaonya.

Afisa huyo pia alihimiza madereva kuwa waangalifu hasa wanapobadilisha leni, ubadilishaji leni kiholela Thika Super Highway na uendeshaji gari kwa mwendo wa kasi ukilaumiwa kuwa kiini kikuu cha ajali nyingi.

Ajali hiyo imetokea siku kadhaa baada ya mwanamuziki Jimmy Walter Githinji maarufu kama ‘Jimmy Wayuni’ (Wa nyimbo za Benga kwa lugha ya Agikuyu) kupoteza maisha baada ya gari lake kuhusika katika ajali mbaya Thika Road, karibu na Chuo Kikuu cha Kenyatta, KU.

Ajali hiyo ya mnamo Jumanne usiku, inadaiwa gari la Wayuni liligongana na lori la kusafirisha mizigo, katika leni ya kasi.

Watatu wafariki, wanane wajeruhiwa kwenye ajali eneo la Kyumbi

Na BENSON MATHEKA

WATU watatu wamefariki na wengine wanane kulazwa hospitalini baada ya magari mawili kuhusika kwenye ajali eneo la Kyumbi, Kaunti ya Machakos.

Walioshuhudia wamesema kwamba ajali hiyo ilihusisha matatu aina ya Nissan na basi moja iliyokuwa ikisafirisha wafanyakazi wa kampuni moja ya ujenzi kutoka Konza City.

“Ajali ilitokea matatu aina ya Nissan ilipogongana na basi lililokuwa likibeba wafanyakazi wa kampuni moja ya ujenzi kutoka Konza City,” amesema Kioko Kalii, mkazi aliyeshuhudia ajali hiyo.

Mkuu wa kitengo cha huduma za dharura Kaunti ya Machakos David Mwongela amesema kwamba majeruhi wamepelekwa hospitali ya Machakos Level Five na ambulensi za serikali ya kaunti.

“Watu wanane waliopata majeraha mabaya wamewahiwa hospitali ya Machakos Level Five na wanaendea kupata matibabu. Nissan iligongona na basi lililokuwa likibeba wafanyakazi kutoka Konza City,” amesema Bw Mwongela.

Maiti za waliokufa zinahifadhiwa katika mochari ya hospitali hiyo.

Bw Mwongela amewataka madereva kuwa waangalifu barabarani

Sita wafa katika ajali

Na SAMUEL BAYA

WATU sita walifariki Jumamosi katika ajali iliyotokea kwenye barabara kuu ya Nakuru-Kericho.

Kulingana na maafisa wa polisi pamoja na wahudumu wa hospitali ya Kericho, watu watano walifariki papo hapo huku mmoja akiaga dunia alipokuwa akitibiwa katika hospitali kuu ya mjini Kericho.

Kulingana na msimamizi wa polisi eneo la Londiani, Bw Musa Kongoli, ajali hiyo ilitokea baada ya trela lililokuwa likitoka Nakuru kupoteza mwelekeo na kugonga magari mengine.

“Ajali hiyo ilihusisha trela ambalo lilikuwa likiekelea upande wa Kericho kutoka Nakuru. Dereva wa trela alipoteza udhibiti alipofika eneo hilo na kugonga magari mengine matano ambayo yalikuwa ni pamoja na matatu mbili. Watu watano, wanaume watatu na wanawake wawili walifariki papo hapo,” akaeleza Bw Kongoli.

Wa sita alifariki akipokea matibabu.

Aliambia wanahabari kwamba walioaga dunia walikuwa katika matatu iliyokuwa ikielekea Nakuru kutokea Kericho. Dereva wa trela alipata majeraha na anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo kuu ya Kericho.

Watu 5 waangamia kwenye ajali

NA MWANDISHI WETU

Watu watano waliangamia kwenye ajali hapo Jumamosi katika barabara kuu ya Nakuru kuelekea Kericho.

Ajali hiyo iliyohusisha lori na magari mengine matano ilitokea katika kaunti ya Kericho.

Musa Kongoli, OCPD wa Londiani, alisema kuwa dereva wa lori hilo alikuwa akielekea Kericho akitoka Nakuru alikpopoteza mwelekeo na akagongana na matatu iliyokuwa ikielekea Nakuru ikitoka Kericho.

Magari mengine manne yalihusika katika ajali hiyo iliyosababisha kifo cha wanawake wawili na wanaume watatu.

“Inahuzunisha sana kupoteza watu watano kwa ajali hii. Walioumia walikuwa kwenye matatu. Dereva wa lori alipata majeraha na akakimbizwa hospitalini,” alisema Bw Kongoli.

Alisema kuwa wengine kumi na wawili wanatibiwa hospitalini.

Tafsiri: Faustine Ngila

YASIKITISHA: Badala ya mwangaza nyaya za stima zasababisha maafa mtaa wa mabanda wa Bangladesh

Na WINNIE ATIENO

NYAYA za stima zinaning’inia vibaya katika nyumba za wakazi wa mtaa wa mabanda wa Bangladesh, Mombasa na watoto wanazichezea pasi kujua hatari wanayoikodolea macho.

Hata hivyo, wakazi hao kwenye mahojiano wanasema wametoa wito kwa kampuni ya kusambaza umeme ya Kenya Power kushughulikia swala hilo, lakini miezi miwili baadaye “hakuna ilichofanya.”

Maafa yalibisha hodi Jumamosi ambapo watoto wawili walifariki baada ya kushika nyaya hizo hatari za umeme na mara baada ya mkasa huo kampuni hiyo ilifika na kuzirekebisha.

Wakazi wanaendelea kughadhabishwa na mkasa huo ambao uliwaacha wengine wawili wakiwa hali mahututi na hivyo kulazwa katika hospitali kuu ya Pwani.

Aidha wakazi wamenyooshea kidole cha lawama kampuni hiyo kwa kuchelewa kurekebisha nyaya hizo wakisema watoto wao wangalikuwa hai zingalirekebishwa mapema.

Mzazi kwa jina Simon Kabale amesema alimpoteza mwanawe Fridah Khavai aliyekuwa na umri wa miaka 10 na mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi ya St Peter huko Bangladesh baada ya kupigwa shoki na nyaya hizo.

“Nilipigiwa simu kwamba kulikuwa na ajali iliyowahusisha watoto katika eneo langu, nikawahi katika hospitali ya mmiliki binafsi huko Mikindani ambako nilitafuta mwanangu, lakini nikapata alikuwa ashaaga dunia. Nimesononeshwa na kisa hicho,” akasema baba huyo wa watoto watatu.

Akiongea na Taifa Leo huko Bangladesh, Bw Kabale alisema mwanawe ni miongoni mwa watoto waliohusika kwenye ajali ya nyaya za stima walipokuwa wakicheza.

Rafikiye marehemu alinusurika alipokuwa akijaribu kumwokoa kutoka kwenye nyaya hizo.

Kulingana na babake manusura, Bw Newton Magandi mwanawe Nixon Charo alikuwa anajaribu kumsaidia Fridah ambaye alikuwa ameshikwa na nyaya hizo.

“Lakini hakuweza naye akashikwa na nyaya hizo lakini akanusurika na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali kuu ya Pwani,” akasema Bw Magandi.

Bw Kabale anasema amepoteza mtoto mtiifu, shujaa na mwenye bidii.

“Ninataka haki itendeke; hatuwezi kuzika watoto wetu sababu ya utepetevu wa kampuni ya umeme. Tangu Disemba tumekuwa tukiwalilia waje kurekebisha nyaya hizi lakini kilio cha mnyonge hakikusikika,” aliongeza.

Bi Monica Achieng na Bw Michael Onyango ambao mwana wao Dolan Onyango alipatikana ameuawa kwenye ajali nyingine ya nyanya za umeme siku hiyo ya Jumamosi na kuzikwa kesho yake Jumapili anailaumu kampuni hiyo ya huduma za umeme.

Bw Onyango anasema mwana wao wa kwanza alijaribu kumwokoa nduguye lakini akashindwa.

“Alimpiga kwa kutumia mbao lakini alikuwa ameshafariki. Mtoto wangu alikuwa akicheza akashika socket na akarushwa na umeme,” akaeleza Bw Onyango.

Haya ni majanga ambayo wakazi wamekuwa wakikumbana nayo kila kuchao.

Lakini mkurugenzi wa kampuni ya Kenya Power tawi la Mombasa Bw Hicks Waswa anasema ajali hiyo ilitokea kufuatia mmomonyoko wa udongo (earth movements) uliosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha.

“Sehemu ya mkasa ni bondeni ambapo ilitikishwa kufuatia mvua kubwa. Mlingoti wa nyaya za kusambaza umeme uliondoka sehemu yake na watoto walikjuwa wakichezea waya wakakumbana na mauti. Inasikitisha,” akasema Bw Waswa.

Amewasihi wakazi kuwa makini na wakome kushika nyaya hizo.

Wiki hiyo hiyo mtoto mchanga aliaga dunia huko Bombolulu baada ya ajali ya nyaya za stima (electrution).

Afisa mkuu wa Nyali Bw David Masaba alisema mtoto huyo aliaga dunia baada ya kufikishwa katika kituo cha afya eneo la Ziwa la Ngombe.

Nyaya za umeme zikiwa zimegusa matawi na majani ya miti katika Tom Mboya Street, Nairobi Januari 10, 2020, hivyo kuwa hatari kwa wapita-njia, abiria, utingo na madereva. Hitilafu ya nguvu za umeme huwa mara kwa mara katika majumba kadhaa yaliyoko kando ya barabara hiyo. Picha/ Paul Waweru

KAFYU: Wanne wanusurika kifo

NA SAMMY WAWERU

Watu wanne walinusurika kifo Jumatatu jioni baada ya gari walimokuwa kuhusika katika ajali mbaya katika barabara kuu ya Thika.

Ajali hiyo iliyofanyika eneo la Carwash, kilomita moja kutoka Kasarani, ilihusisha magari matatu, dakika chache kabla ya kafyu kuanza kutekelezwa.

Kulingana na manusura wa gari ndogo la kibinafsi na lililoathirika pakubwa, lori la kusafirisha changarawe, liliendeshwa kwa mwendo wa kasi likibadilisha leni bila uangalifu.

Dereva wa lori hilo alidaiwa kutoroka baada ya kusababisha mkasa, na kurejea maafisa wa trafiki walipowasili.

“Nilianza kushuku lori hili kuanzia Roysambu, kutokana na lilivyoendeshwa bila uangalifu wa magari yaliyo nyuma na mbele,” alilalamika dereva wa gari aina pick-up, ambalo pia lilihusika.

Dereva wa gari ndogo alidai alikuwa katika leni ya kutoka barabara ya kasi, na gari lake lilisukumwa hadi leni ya kasi zaidi. “Tulikuwa tunaelekea Juja, ni Mungu aliyetuokoa,” alisema, akiongezwa kwamba alihisi maumivu kwenye bega la mkono wa kulia.

Madereva wametakiwa kuwa waangalifu wakiwa barabarani, hasa wakati huu taifa limegubikwa na janga la Covid – 19.

“Hatutaruhusu utepetevu wa aina yoyote ile barabarani. Hebu tazama athari za msongamano zilizojiri kufuatia tukio hili, watu wakijaribu kufika makwao kabla ya kafyu kuanza kutekelezwa,” alionya afisa mmoja wa trafiki kutoka kituo cha polisi cha Kasarani, Nairobi.

Mkasa huo ulitatiza shughuli za uchukuzi kwa saa kadhaa, gari lililoharibika kupita kiasi likifutwa dakika chache kabla ya saa mbili za jioni.

Visa vya ajali kushuhudiwa kati ya mtaa wa Githurai na Kasarani, Thika Super Highway si vigeni. Uendeshaji magari kwa mwendo wa kasi na kubadilisha leni bila uangalifu unatajwa kama kiini kikuu cha ajali katika barabara hiyo ya kasi.

Taahira aponea baada ya ambulansi aliyoendesha kugongana na lori

JEREMIAH KIPLAGAT na STANLEY KIMUGE

MGONJWA wa akili Jumanne alijeruhiwa vibaya alipoamua kuendesha ambulansi kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret, iliyogongana na lori la kusafirisha mafuta eneo la Marura kwenye barabara ya Eldoret-Iten.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye ni mkazi wa Kapseret, alikuwa amepelekwa katika hospitali hiyo kwa matibabu.

Lakini aliwashangaza wengi alipochomoka kutoka hospitali hiyo na kuingia kwa ambulansi tukio ambalo nusura limsababishie mauti.

Polisi walimwandama, baada ya kupashwa habari kuhusu kisa hicho na wakampata amejeruhiwa baada ya ajali hiyo kutokea katika eneo la Marura, katika barabara ya Eldoret-Iten.

Mgonjwa huyo alipata majeraha mabaya kichwani lakini dereva wa lori hilo alipata majeraha madogo. Alikwepa kugonga matatu mbili za abiria 14 kabla ya kugonga lori hilo la mafuta.

Afisa Mkuu Mtendaji katika hospitali hiyo, Bw Wilson Aruasa alisema mwanamume huyo alikuwa akihudumiwa na mhudumu mmoja wa afya alipochomoka na kuangia ndani ya ambulansi na kuiendesha kwa kasi.

Ilisadifu kuwa ambulansi hiyo ambayo ni mali ya kituo cha afya cha Kaptendon, Kapseret, Uasin Gishu, ilikuwa na ufunguo.

“Dereva hakuwa amezima ambulansi hiyo. Mwanamume huyo aliingia ndani ya gari na kuchomoka nalo,” Dkt Aruasa akaambia Taifa Leo.

Afisa huyo alisema mwanamume huo aliwahi kupewa matibabu katika hospitali hiyo hapo awali ambapo alidhihirisha sifa zinazofanana na wagonjwa wenye akili punguani.

Dkt Aruasa alisema dereva wa ambulansi hiyo alikuwa ameiegesha karibu na kitengo cha shughuli za dharura na alikuwa akimsaidia muuguzi kumpeleka mgonjwa mwingine katika chumba cha dharura.“Huyu ni mtu anaugua ugonjwa wa kiakili.

Dereva ameagizwa aandikishe taarifa kwa sasa hiki ni kisa cha kushughulikiwa na polisi,” akaongeza Dkt Aruasa.

Eneo la kuingilia katika kitengo cha kushughulikia ajali na dharura nyinginezo ni wazi na halina lango. Kitengo hicho kiko karibu na barabara ya Nandi inayounganisha hospitali ya MTRH na eneo la katikati mwa mji wa Eldoret.Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) kaunti ndogo ya Turbo Eliud Maiyo alisema mgonjwa huyo anapokea matibabu.

“Alitwaa udhibiti wa ambulansi hiyo dakika chache baada ya mgonjwa mwingine kuondolewa na akaliendesha kwa kasi mno. Alipata majeraha na akakimbizwa hospitalini ambako anapewa matibabu ya dharura,” Bw Maiyo akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Bw Ambrose Lagat, aliyeshuhudia kisa hicho, alituambia kwamba mwanamume huyo alikuwa akiliendesha ambulansi kwa kasi na katika safu ya barabara isiyokubalika.

Ndio maana wenye magari walikwepa barabara kukwepa kugongana na ambulansi hiyo.

“Tulishangaa kuwa ambulansi hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa kasi na haikupiga king’ora kuonya magari mengine yaipishe. Iligonga vioo ya pembeni vya matatu mbili kabla ya kugongana na lori la mafuta upande wa kulia,” akasema.

Baada ya mgangano huo, lori la mafuta lilianguka barabarani na kuiziba, na kusababisha msongamano wa magari katika barabara yenye shughuli nyingi.

Polisi walikuwa na wakati mgumu kudhibiti umati wa watu waliofika eneo hilo la ajali. Maafisa hao waliwazuia kufyonza mafuta kutoka kwa lori hilo.

NMG yamwomboleza mhariri wa The East African

Na AGGREY MUTAMBO

KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) kwa mara nyingine inaomboleza kifo cha mwanahabari katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Mhariri wa gazeti la The East African Bi Christine Omulando aliyekuwa na umri wa miaka 46, alifariki kufuatia ajali iliyotokea katika  mzunguko wa Khoja, jijini Nairobi hapo Machi 16.

Kulingana na ripoti ya polisi, mwanahabari huyo pamoja na wapita njia wengine waliligongwa na matatu iliyokosa udhibiti na kutoka barabarani kabla ya basi ndogo kumkanyaga.

“Bi Omulando alifariki papo hapo baada ya kugongwa na basi ndogo,” ilisema ripoti.

Mwili wake ulipelekwa kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti jijini na wapita njia waliohusika wakakimbizwa katika hospitali kuu ya Kenyatta.

Mwanahabari huyo aliripotiwa kupotea Jumatano baada ya familia na marafiki kushindwa kumfikia kwa njia ya simu.

Asubuhi hiyo, alikuwa amefika kazini kisha baadaye akaondoka kwenda kula maankuli.

Hiki ni kisa cha pili, huku wanahabari wa NMG bado wakimwomboleza aliyekuwa mhariri wa video katika runinga ya NTV Raphael Nzioki.

Polisi walisema kuwa marehemu aligongwa kimaksudi na gari kwenye njia panda katika mtaa wa Kenyatta Avenue na Kimathi Street.

Madereva waliohusika katika visa vyote hivyo viwili tayari wamekamatwa.

Familia yalilia haki ya mtoto wao aliyegongwa na gari

Na SAMMY WAWERU

JUMAPILI Machi 8, 2020, mtoto Njeri alirauka alfajiri na mapema ili kujiandaa kuhudhuria ibada ya kanisa, misa ya watoto katika kanisa la PEFA Progressive eneobunge la Ruiru.

Asubuhi hiyo, mamake anasema alitangamana na watoto wenzake kwenye ploti na kama ilivyo kawaida wakacheza kabla kuelekea kanisani.

Walipoagana, mamake mtoto huyo wa darasa la pili, gredi ya pili chini ya mfumo wa kisasa wa elimu, uamilifu, ndio CBC, alikuwa katika harakati za kufua nguo.

Mwendo wa sita hivi za mchana, alipigiwa simu akiarifiwa kuwa mwanawe amehusika katika ajali na kwamba amepelekwa katika Hospitali ya St John iliyoko Githurai.

“Tulipofika pamoja na babake tulipata mwili ukiingizwa katika gari la polisi ili kupelekwa mochari,” mama huyo aliyezidiwa na huzuni akaambia Taifa Leo.

Alisema alifariki wakati akipelekwa hospitalini.

Inasemekana siku ya tukio, Njeri, 8, pamoja na watoto wenza walikuwa wakitoka kanisani.

“Walivuka barabara kwa kundi, na ndiye alikuwa wa nyuma, wakati gari lililoonekana kuendeshwa kasi lilipompiga dafrau,” akaeleza mmoja wa wakazi aliyeshuhudia.

Gari la kibinafsi lililosababisha maafa ya mtoto huyo lenye nambari ya usajili KCW 923X lilikuwa likiendeshwa na mama.

Inasemekana alikuwa akipeleka mwanawe hospitalini.

Kati ya eneo la ajali, kuna matuta mawili, pembezoni likiwa ni kanisa la PEFA na ambalo kila Jumapili hufurika washirika. Isitoshe, mita kama hamsini hivi kuelekea Githurai barabara hiyo imejipinda.

“Kandokando mwa barabara kuna ploti za kupangisha, magari hayaendeshwi kwa kasi na lazima dereva awe makini kwa kuwa ni eneo lenye idadi kubwa ya watu,” akasema mhudumu mmoja wa tuktuk.

Gari lililosababisha maafa ya mtoto Njeri lilipelekwa katika kituo cha polisi cha Kahawa Wendani, ambacho kina kitengo cha trafiki na kufikia sasa familia ya marehemu inalilia haki ikidai hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

Inasemekana mama aliyesababisha kifo cha mtoto wao aliachiliwa huru, ingawa gari limezuiliwa kituoni.

Afisa mmoja wa polisi na aliyeomba tusichapishe jina lake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na waandishi wa habari, alisema hatua ya kwanza ni gari kuzuiliwa kituoni ili kufanyiwa uchunguzi kubaini ikiwa inaruhusiwa kuwa barabarani.

“Uchunguzi umeanzishwa kujua iwapo imeafiki sheria za trafiki, ikiwamo kuwa na bima na ukaguzi wa kina (inspection),” akasema.

Pia alisema dereva atachunguzwa ikiwa amehitimu mafunzo ya udereva na kuwa na leseni ili kufunguliwa mashtaka.

Misongamano inavyotatiza huduma za dharura jijini

Na BENSON MATHEKA

JUHUDI za kupunguza misongamano ya magari katikati mwa jiji la Nairobi huwa haziwafurahishi watu wengi hasa wenye magari ya uchukuzi na wanaofanya kazi katikati mwa jiji.

Lakini kwa kampuni na mashirika yanayotoa huduma za dharura jijini kama vile madereva wa ambulensi, zima moto, polisi na kampuni za ulinzi ni baraka kubwa kwao.

Madereva wa ambulansi wanaohudumu jijini wanasema kuwa huwa wanaguswa moyo wanapowaona wagonjwa wanaobebwa katika ambulansi wakipelekwa kupata matibabu maalum wakisononeka katika msongamano wa magari barabarani.

“Ni jambo la kuudhi mno,” asema Bwana Eric Munywoki, anayeendesha ambulansi ya shirika moja jijini.


Bw Eric Oduor, dereva wa ambulensi asema ni mlima kufikisha mgonjwa hospitalini kwa sababu ya msongamano. Picha/ Benson Matheka

Munywoki asema kuwa kwa miaka minane ambayo amekuwa akihudumu jijini ameshuhudia watu wakipoteza maisha yao katika hali ambayo kama sio msongamano wa magari barabarani wangepona.

Anatoa mfano wa wakati ajali inapotokea na wanaitwa ili kuwapeleka wanaonusurika hosptalini.

“Wakati mwingine tunachukua muda mrefu kufika kwenye tukio ili kuwaokoa majeruhi tukipambana kwenye misongamano,” asema na kuongeza kuwa kuna nyakati anapotiririkwa na machozi mgonjwa anapokata roho akiwa amekwama barabarani na matabibu wakimhudumia kwa vifaa haba ndani ya ambulansi.

Dereva huyu anawalaumu madereva jijini kwa kutowapisha watoaji huduma za dharura hata kama ving’ora vinalia.

“Sielewi nia ya waendeshaji magari katika jiji hili. Hawana nidhamu, huwa wanapuuza ving’ora vya magari maalum kama ambulensi na wazima moto,” asema.

Maoni yake yanaungwa na aliyekuwa naibu mkurugenzi wa huduma za zima moto katika baraza la jiji Bw Peter Ngugi anayesema kuwa huduma za wazima moto huvurugwa kabisa na misongomano ya magari.

“Si ajabu kuwaona madereva wametulia tuli huku ving’ora vya magari ya wazima moto vikichana hewa,” asema Ngugi.

Kutokana na kukwama kwao katika misongamano, aeleza Ngugi, wakazi hulaumu idara za kutoa huduma hizi muhimu kwa kuzembea.

“Ieleweke bayana kuwa hakuna wakati idara yetu hukawia tunapopata habari kuwa moto umetokea katika eneo fulani.

Tatizo kubwa ni barabara zetu ambazo zimejaa magari na kutatiza huduma zetu,” asema.

Kutokana na hali hii, hasara kubwa hutokea mali ya mamilioni ya pesa inapoteketea zima moto likiwa limekwama katika msongamano barabarani.

Ngugi anapendekeza kuwa barabara muhimu za jiji zitengewe watoaji huduma za dharura ili wapate fursa ya kutekeleza kazi yao bila kutatizika.

“Sisemi magari yaondolewe kabisa. Ninachopendekeza ni kwamba baadhi ya magari yakatazwe kutumia barabara muhimu ili kurahisisha kazi yetu, ”asema.

Anaunga mkono pendekezo la awali ambapo serikali ilinuia kutenga laini maalum kwa msafara wa Rais, makamu wake na Waziri mkuu.

“Kwa maoni yangu laini iliyokusudiwa kutengewa viongozi hawa inafaa kutengewa magari ya wanaotoa huduma za dharura ili kuboresha huduma jijini, ” asema.

Kulingana na watoaji wa huduma mizunguko iliyo katika barabara kuu inapaswa kuondolewa ili kurahisha usafiri jijini.

Wanasema mingi ya misongamano hutokea kwenye mizunguko hii.

Bw Munywoki aliwaondolea lawama maafisa wa polisi wanaoelekeza magari jijini akisema kuwa huwa wanafanya kazi nzuri .

“Ukweli ni kwamba jiji hili lina magari mengi na mpangilio mbaya wa barabara. Nawashukuru maafisa wa polisi ambao licha ya ongezeko la magari kwenye barabara hizi huwa wanafaulu kuelekeza magari na kupunguza misongamano,” asema.

Hata hivyo anasema baadhi yao huwa hawatilii maanani ving’ora vya magari yao na huendelea kuzuia magari.

“Kuna wanaopuuza ving’ora vya ambulensi na wazima moto na hii haifai. Wanapaswa kufungulia magari ili watoaji wa huduma wafanye kazi na kuokoa mali na maisha,” asema.

Lakini afisa mmoja wa trafiki tuliyeongea naye katika barabara ya uhuru jijini kwa sharti kuwa hatutataja jina lake alisema huenda watu wakawalaumu kwa kutojali magari yanayotoa huduma za dharura jijini kwa kuwa hawaelewi ugumu wa kazi yao.

“Hii ni kazi gumu mno.Watu wanaweza kudhani hatujali wazima moto na magari mengine kama ambulensi kwa sababu hawaielewi,” alisema na kuongeza kuwa kazi yao ni kuongoza na kuelekeza magari tu na sio kujenga barabara.

“Serikali inapaswa kuchukua hatua ili kutafuta suluhisho ya kudumu la msongamano jijini,” asema na kuongeza hilo ni jukumu la serikali ya kaunti na wizara husika katika serikali kuu.

Wengi wa wanaotoa huduma hizo wanasema hatua madhubuti zapaswa kuchukuliwa ili kuondoa kabisa magari katikati mwa jiji na kupunguza kwa kiwango kikubwa magari kwenye barabara muhimu jijini.

“Huwa tunatatizika tunapofanya kazi yetu ya kuhudumia wakazi wa jiji,” asema Bw Vincent Kea, mfanyakazi wa kampuni moja ya ulinzi anayehudumu katikati mwa jiji.

Bw Vincent Oduor Kea, dereva wa kampuni ya ulinzi alalamika misongamano hutatiza kazi yao. Picha/ Benson Matheka

Kea aeleza kuwa wafanya kazi wa kampuni za ulinzi hupata wakati mgumu wanapotakiwa kuhudumia mteja wao linapotokea jambo la dharura.

“Ni kama kupasua mwamba kupata maji kujaribu kupenya msongamano wa magari katika barabara za Nairobi ukielekea kumuokoa mteja anapotoa kilio cha dharura,” asema Kea ambaye amefanya kazi hii kwa miaka 12.

Anasema huwa ni vigumu kuwaauni wateja wao hasa walio katikati mwa jiji kwa kuwa wanachelewa wakijaribu kupita katika misongamano ya magari.

“Mara nyingi huwa tunachelewa katika misongamano ya magari tunapoarifiwa kuwa mteja anahitaji huduma zetu,” asema.

Tuju apata ajali akiwa safarini kuhudhuria mazishi ya Moi

Na SIMON CIURI

KATIBU Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju amepelekwa hospitalini Kijabe baada ya kupata ajali akiwa safarini kuelekea Kabarak ahudhurie mazishi ya Rais Mstaafu Daniel Moi.

Hii ni baada ya gari alimokuwa kugongwa na matatu iliyokuwa inahepa gari jingine eneo la Magina katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.

Kamishna wa Kiambu Wilson Wanyaga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema Tuju alitarajiwa kupelekwa Nairobi kwa matibabu zaidi.

Bw Tuju aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Prado amepata majeraha kifuani na sehemu ya tumbo huku dereva wake Austin Oindo akipata jeraha katika mkono wake.

Wawili hao hata hivyo, imeelezwa, wanaendelea vyema.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju. Picha/ Maktaba

Gari la Toyota Allion nambari za usajili KCS 235w lilikuwa linatokea upande wa Naivasha na lilipofika eneo la tukio lilipunguza mwendo kuruhusu gari lililokuwa mbele yake kupinda kuingia katika barabara nyingine upande wa kulia ukiwa unaelekea Nairobi.

Gari hilo – Allion – limegongwa na matatu nambari za usajili KCH 051J ambayo ilipoteza mwelekeo na kuingia upande lililotokea gari la Tuju na hivyo kuligonga dafrau.

Anusurika kifo baada ya gari lake kugongana na tingatinga

Na SAMMY WAWERU

MWANAMUME mmoja Jumanne alinusurika kifo gari lake lilipogongana na tingatinga eneo la Progressive, katika barabara inayounganisha mtaa wa Mwihoko na Githurai.

Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, tingatinga lilikuwa limegonga magari mawili zaidi kabla kufikia gari hilo la kibinafsi.

Inasemekana mwendesha tingatinga na aliyeonekana kuzidiwa na makali ya pombe, alikuwa ameonywa na wafanyakazi wenza dhidi ya kuingia barabarani akiwa katika hali aliyokuwa.

“Tumejua hali yake si kamilifu baada ya kugonga gari aina ya Nissan na kujifanya hakuna kilichotokea. Isitoshe, ameendelea na safari, akaangusha tuktuk kabla kufikia kwa hili la kibinafsi,” akaelezea mhudumu wa bodaboda.

Vyuma vya tingatinga na vinavyotumika kuchimba udongo, vililenga upande wa dereva wa gari la kibinafsi, ambapo mlango pia uliharibiwa vibaya.

Licha ya kutakiwa afidie hasara aliyosababisha kwa magari husika, mwendesha tingatinga hakuonekana kujutia chochote. “Ninachosubiri ni askari waje wanikamate,” alieleza kwa ujeri.

Ilichukua juhudi za maafisa wa trafiki wanaohudumu eneo la Githurai, kuingilia kati kisa hicho, na kumtia nguvuni. “Ni hatia kwa dereva yeyote kuendesha gari akiwa mlevi, ninasihi madereva wawe waadilifu,” akashauri afisa wa trafiki aliyejitambua kama Bw Kairu.

Kwa mujibu wa sheria za trafiki, faini ya kuendesha gari ukiwa mlevi haipaswi kuzidi Sh100, 000 au utumikie kifungo cha miaka miwili gerezani, au adhabu zote mbili.

Mwaka waanza kwa mbwembwe lakini pia majonzi

Na WAANDISHI WETU

WAKENYA wengi walisahau hali ngumu ya maisha waliyopitia 2019 kuukaribisha mwaka mpya wa 2020 kwa mbwembwe za kila aina wakilipua fataki na kuomba Mungu awalinde na kuwapa afueni mwaka 2020.

Hata hivyo, kwa baadhi ya familia, mwaka ulianza kwa huzuni na kilio baada ya wapendwa wao kuangamia kwenye ajali za barabarani na mikasa mingine.

Watu 10 walifariki kwenye ajali zilizotokea maeneo tofauti nchini siku ya kwanza ya mwaka 2020.

Katika miji mikubwa nchini, Wakenya walifurika katika maeneo ya burudani na ibada kukaribisha mwaka mpya kwa furaha.

Viongozi wa kisiasa na kidini walitoa wito wa umoja, uwiano, kuvumiliana na amani mwaka huu wa kwanza katika mwongo wa pili wa karne ya 21.

Watoto 16 walizaliwa katika hospitali ya Pumwani jijini Nairobi ilipotimu saa sita Jumanne usiku.

Katika kaunti ya Nakuru, wakazi walikaribisha mwaka kwa kuhudhuria tamasha mbili katika uwanja wa ASK mjini Nakuru, mkutano wa ibada katika uwanja wa michezo wa Afraha na katika hoteli ya Rift Valley Sports club ambako walitumbuizwa na wasanii mbali mbali.

Hata hivyo, katika kijiji cha Kihoto, eneo la Kabazi kaunti ya Nakuru, mafuriko ya hivi majuzi yaliwakosesha wakazi raha ya mwaka mpya.

Wakazi hao walisema ingawa wanashukuru Mungu kwa kuwavukisha mwaka salama, hawana cha kujivunia kwa sababu mimea yao ilisombwa na mafuriko.

Katika eneo la Pwani, wakazi, wageni na watalii mbalimbali walikaribisha mwaka kwa mtindo wa aina yake, wakijivinjari ndani ya bahari na maeneo ya burudani.

Mashua zilizojaa wakazi na watalii zilionekana zikizunguka baharini huko Lamu na nyingine kusimama katikati ya bahari zikiwa zimepambwa kwa mataa ya rangi tofauti na kuleta mvuto wa aina yake.

Mamia ya wakazi walijumuika katika bustani ya Kibarani kualika mwaka mpya. Hafla hiyo iliandaliwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho ambaye aliwahimiza wakazi kuishi kwa amani.

Katika kisa cha huzuni, watu watano walifariki Jumatano katika ajali iliyotokea kwenye barabara ya Eldama Ravine kwenda Eldoret, kaunti ya Baringo. Ilisemekana watu hao walikuwa wakitoka sherehe ya kukaribisha mwaka ajali ilipotokea.

 

Na BENSON MATHEKA, SAMUEL BAYA, VITALIS KIMUTAI, ERIC MATARA, KALUME KAZUNGU, na DIANA MUTHEU

Wasafiri waumia mabasi ya Modern Coast yakizimwa

MISHI GONGO na PIUS MAUNDU

MAMLAKA ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA), Alhamisi ilikiri kupokea malalamishi kuhusu mabasi ya kampuni ya Modern Coast kabla ajali kufanyika na kusababisha vifo vya watu watano.

Kwenye taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa NTSA Bw George Njao alisema shirika hilo limekuwa likifuatilia mabasi hayo kwa karibu, kufuatia ripoti za wananchi kuhusu matukio kadhaa ya kunusurika kogangana na mabasi mengine awali.

Haijajulikana wazi kwa nini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi ajali ikatokea jana alfajiri ikihusu mabasi mawili ya kampuni hiyo yaliyogongana na kusababisha vifo vya watu watano huku wengine 62 wakijeruhiwa.

“Kwa siku kadhaa sasa, shirika hili limekuwa likifuatilia kwa makini huduma za kampuni ya Modern Coast Limited baada ya ripoti kuhusu ajali kadhaa ambazo watu walinusurika kifo,” akasema, akitangaza kwamba mabasi hayo yamepigwa marufuku kwa muda.

Wasimamizi wa Modern Coast walisema watakutana na NTSA leo kutafuta mwafaka kuhusu marufuku hiyo ambayo imewaacha wasafiri wengi bila namna huku wakiahidi kurudishia wateja wao nauli ambazo walikuwa washalipa.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kiongwani, barabara kuu ya Mombasa-Nairobi, eneo ambalo limetajwa kuwa hatari mwaka huu, baada ya ajali zaidi ya 10 kutokea ndani ya wiki tatu zilizopita.

Abiria 50 walipata majeraha madogo huku 17 wakijeruhiwa vibaya. Majeruhi walipelekwa katika hospitali za Kaunti ya Machakos na Makueni.

“Basi moja lilikuwa linaelekea Malaba jingine likielekea Nairobi. Basi lililokuwa likitoka Mombasa lilitoka katika barabara yake na kugongana na lile lililokuwa likitoka Malaba,” alieleza kamanda wa polisi kaunti ya Makueni Ole Napeiyan.

Waliofariki walijumuisha dereva wa mabasi hayo na mtoto wa miaka miwili. Miili ya wendazao ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya Machakos.

Mamia ya abiria walitatizika katika vituo vya mabasi vya kampuni hiyo vilivyo miji tofauti ya nchi.

Mjini Mombasa, abiria ambao walifaa kusafiri jana asubuhi walibaki wameduwaa wasijue la kufanya, wakisubiri maelekezo kutoka kwa usimamizi wa shirika hilo.

Kituo hicho kililindwa na maafisa wanne wa polisi kuhakikisha kuwa hakuna basi linalosafiri kama walivyoelekezwa na NTSA.

Abiria mmoja, Bi Miriam Maingi ambaye alipaswa kusafiri na gari la saa mbili, alieleza hali ya kukerwa kufuatia usimamizi wa Modern Coast kutowapa taarifa kuhusiana na tatizo hilo.

“Nimefika hapa saa moja, niko na watoto, kila tunapowauliza kuhusu usafiri wetu hawatujibu wanatuambia tusubiri. Sasa hivi ni saa nne na hatujaambiwa kitu,” akasema.

Mwengine ambaye alidai alikuwa anasafiri kwenda kwa matibabu katika hospitali kuu ya Kenyatta.

“Sina uwezo wa ndege, treni zimejaa, nisiposafiri leo nitapoteza nafasi yangu ya kupokea matibabu,” akasema.

Gorge Otieno, alisema kusimamishwa kwa huduma za shirika hilo,kumewaathiri pakubwa hasa wafanyi biashara ambao wanatumia mabasi hayo kusafirisha mizigo.

“Niko na bidhaa ambazo zinafaa kufika Nairobi leo jioni,nishalipa ada husika lakini hadi sasa sijapatiwa usafiri,” akaeleza.

Anwar Juma alisema wanatarajia shirika hilo litatatua tatizo hilo kwa haraka na wataangalia maslahi ya abiria wao.

“Wakishindwa kutatua, watutafutie njia mbadala ya usafiri,” akasema.

Anusurika kifo katika ajali ya Ijumaa Thika Superhighway

Na SAMMY WAWERU

MTU mmoja alinusurika kifo Ijumaa baada ya gari lake kupoteza mwelekeo na kugonga reli katika barabara ya Thika Superhighway.

Ajali hiyo iliyotokea eneo la Clayworks, kilomita moja hivi kutoka mtaa wa Githurai, ilihusisha gari la mmiliki binafsi na lililoendeshwa na mwanamke.

Lilikuwa katika leni ya kasi kutoka jijini Nairobi.

Kulingana na walioshuhudia, huenda gurudumu lilipasuka na gari likapoteza mwelekeo ambapo liligonga nguzo za kando ya barabara na kung’oa vyuma.

Vyuma vinne viling’olewa na nguzo hiyo kukatika.

“Inaonekana lilikuwa kwa mwendo wa kasi, kiasi cha kung’oa vyuma hivyo na kujaribu kuvuka barabara ya kuelekea jijini Nairobi,” mmoja wa walioshuhudia akaambia Taifa Leo.

Maafisa wa Mamlaka ya Barabara Kuu Nchini (KeNHA) walifika ili kutathmini kilichosababisha ajali hiyo.

Mwanamke huyo aliyenusurika, hakuweza kuzungumza kwa wakati huo.

Sehemu ya mbele ya gari ilionekana kuharibika kupita kiasi, ingawa kioo cha kuzuia upepo hakikuvunjika.

“Kilichomuokoa ni kujifunga mkanda. Iwapo hangetekeleza hilo, kasi aliyokuwa ingemsababishia madhara,” akasema dereva mmoja wa matatu.

Afisa wa idara ya trafiki na aliyebana jina lake aliambia mtandao huu kwamba uchunguzi umeanzishwa.

“Tunahimiza madereva na watumizi wa barabara wawe waangalifu. Kasi ni hatari, na huua,” akaonya.

Mapema Novemba 2019 ajali nyingine ilitokea eneo la Githurai.

Ilihusisha magari manne; basi, gari aina ya probox, pickup na gari la binafsi.

Thika Superhighway si geni kwa visa vya ajali, vingi vikihusishwa na uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi, baadhi ya madereva wakiingia barabarani wakiwa walevi na ubadilishaji wa leni pasi uangalifu.

Endapo gurudumu la gari limepasuka ukiwa kwa mwendo wa kasi, unashauriwa kushikilia usukani na kulidhibiti, ukisalia katika leni ulioko. Usikanyage breki mara moja, kwani huenda likabingiria.

Washa mataa ya dharura ili kufahamisha walio nyuma yako. Litaanza kupunguza mwendo, na huo ndio wakati unashauriwa kukanyaga breki, hususan kasi ikiwa chini ya kilomita 50 kwa saa.

Toa vifaa vya dharura na kuviweka mita chache nyuma ya gari. Ili kuondoa msongamano barabarani, tafuta gari likuvute kwa unyororo au mekanike akurekebishie.

Maafisa wa KeNHA na trafiki hata hivyo huwa barabarani kwa ajili ya kuangazia masuala ya aina hiyo.