Niko salama, asema Cherargei

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Seneta wa Nandi Samson Cherargei ameongea kufuatia ripoti zilizosambaa kwamba amehusika katika ajali ya barabarani katika barabara ya Eldoret kwenda Kapsabet usiku wa kuamkia Jumamosi.

Seneta Cherargei alisema yuko “hai na salama” na kuwataka Wakenya kuzingatia masharti ya serikali ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

“Niko hai na buheri wa afya. Mungu awabariki nyote. Nawa mikono na make nyumbani. Nawatakia Sabato nzuri,” akasema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Ilisemekana kuwa Bw Cherargei alihusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Mulango, eneo bunge la Kapseret. Alikuwa ndani ya gari lake aina ya Prado.

Alipata majeraha madogo na kuhudumiwa katika Hospitali ya Kibinafsi ya St Luke, Eldoret, kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Siku ya Ijumaa Bw Cherargei alikuwa miongoni mwa viongozi walioandamana na Naibu Rais William Ruto kuhudhuria hafla moja ya kitamaduni eneobunge la Chesumei, kaunti ya Nandi.

Seneta Cherargei ahusika katika ajali ya barabarani

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Nandi Samson Cherargei anapokea matibabu katika hospitali ya kibinafsi ya St Luke, Eldoret baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani Jumamosi asubuhi.

Duru zinasema kuwa ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Eldoret kwenda Kapsabet katika eneo la Kapseret.

Bw Cheragei aliripotiwa kupata majeraha madogo kufuatia ajali hiyo.

Picha za gari aina ya Prado, linaloaminiwa kuwa lake Seneta Cherargei, lililobondeka zilisambaa kwenye mitandao dakika chache baada ya ajali hiyo.

Bw Cherargei ni miongoni mwa viongozi wa jamii ya Wakalenjin walioandamana na Naibu Rais William Ruto katika mkutano wa kisiri katika eneo bunge la Chesumei nyumbani kwa mzee mmoja wa ukoo wa Talai, uliosemekana na kumtakia “heri njema” katika azma yake (Ruto) ya kuingia Ikulu 2022.

Katika mkutano huo wa faragha Dkt Ruto aliripotiwa kukutana na zaidi ya viongozi 50 wa jamii ya Nandi, wakiwemo wazee na viongozi wa kidini.

Wakenya mitandaoni wamemtakia Bw Cherargei afueni ya haraka.

Cherargei aachiliwa kwa dhamana

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kaunti ya Nandi Samson Cherargei aliachiliwa huru Jumanne alasiri kwa dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu baada ya kufikishwa katika mahakama ya Nairobi kwa kosa la kuchocea chuki.

Hata hivyo, Seneta huyo alikanusha mashtaka hayo.

Japo Bw Cherargei hakuwa na pesa taslimu wakati huo, mahakama ilimwepusha na aibu ya kulala korokoroni baada ya kumruhusu kutoa majina ya watu wawili ambao wangemsimamia.

Hata hivyo, seneta huyo ametakiwa kuwasilisha pesa hizo Sh300,000 kufikia saa sita adhuhuri Jumatano bila kuchelewa.

“Nimezingatia kuwa mtuhumiwa ameshtakiwa wakati ambapo benki nyingi zimefungwa. Kwa hivyo, naamuru kwamba awasilishe pesa hizo kesho (leo Jumatano) kufikia saa sita,” Hakimu Mkuu Francis Andayi alisema katika uamuzi wake.

Cherargei alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la kuchochea chuki ya kikabila kinyume cha Sheria kuhusu Uwiano na Utangamano wa Kitaifa.

“Hii Kenya siasa sio skwota, na wakicheza tutakanyagana… Hii Kenya mpaka wajue hawajui ama tufunge hii Kenya,” Bw Cheragei anadaiwa kusema maneno haya katika mkutano mmoja wa kisiasa katika kaunti ya Uasin Gishu.

Mahakama iliambiwa kuwa matamshi hayo ambayo seneta Cherargei anadaiwa kuyatoa mnamo Agosti 2019 katika hafla ya kuchanga fedha za kisaidia klabu ya soka ya Kilibwoni, yalilenga kuchochea jamii ya Kalenjin dhidi ya jamii zingine zinazoishi eneo hilo.

Cherargei aibua ubabe wa kisiasa kati ya Ruto na Moi

BARNABAS BII na WYCLIFFE KIPSANG

MATAMSHI ya Seneta wa Nandi Samson Cherargei ya kuwaonya wanaompiga vita Naibu Rais Dkt William Ruto yamezua upinzani mkali kati ya vyama vya Jubilee na KANU vinavyopigania umaarufu wa kisiasa katika eneo la eneo la Bonde la Ufa.

Akiwa katika hafla ya mazishi Kaunti ya Nandi, Bw Cherargei aliwaonya wanaompinga Dkt Ruto kuwa watachukuliwa hatua kali ambazo hakufichua na kuwataka wabadili nia na kumuunga mkono.

“Wale watu wanaendelea kumpiga vita Naibu Rais tunawaona. Ukimpinga Naibu Rais, unapigana nasi. Usifikiri kwamba hana wafuasi,” akasema Bw Cherargei.

Seneta huyo wiki jana alikamatwa na makachero kutoka Idara ya Upelelezi(DCI) lakini akawaachiliwa kwa dhamana ya polisi baada ya kuzuiliwa kwa saa kadhaa katika kituo cha polisi cha Central mjini Kisumu.

Viongozi wa Kanu sasa wanasema wapigakura hawafai kulazimishwa kumuunga Dkt Ruto wakidai ishara ziko wazi kuwa Jubilee haishabikiwi tena eneo hilo.

“Ishara ziko wazi kwamba umaarufu wa Jubilee unaendelea kudidimia huku wapigakura wengi wakikumbatia chama cha Kanu. Tumeanza kurindima ngoma yetu hadi mashinani ili chama kiwe dhabiti,” akasema Mshirikishi wa Kanu katika eneo la Bonde la Ufa, Bw Paul Kibet.

Naibu Rais na Mwenyekiti wa Kanu, Seneta Gideon Moi, wamekuwa na uhasama mkali wa kisiasa huku Bw Moi akiwapokea wanasiasa kutoka Jubilee ambao wamekuwa wakilalamikia udikteta wa viongozi wanaompigia upato ili aingie Ikulu mwaka wa 2022.

Viongozi wengine ambao pia hawamshabikii Dkt Ruto wamepata hifadhi katika Chama cha Mashinani(CCM) kinachoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet, Bw Isaac Ruto.

Kama njia ya kutafuta uungwaji mkono, Bw Moi wiki jana aliwakaribisha viongozi wengi maadui wa Dkt Ruto nyumbani kwake Kabarak ambapo inakisiwa siasa za 2022 zilijadiliwa kwa mapana na marefu.

Waliohudhuria mkutano huo ni Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos, Mbunge wa Moiben Sila Tiren, mbunge maalum wa ODM Wilson Sossion, Mbunge wa Tiaty William Kamket na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat. Mawaziri wa zamani Zakayo Cheruiyot, Musa Sirma, Frankline Bett, aliyekuwa Gavana wa Bomet Isack Ruto na mwanasiasa wa Uasin Gishu Zedikiah Bundotich(Buzeki) pia walikuwepo kwenye mkutano huo.

Bw Tolgos ambaye haelewani na Seneta wa kaunti hiyo Kipchumba Murkomen, mwandani wa Dkt Ruto, amewahi kunukuliwa akilalamikia namna wafuasi wa Naibu Rais wanavyowatisha viongozi wasiomuunga mkono.

Ingawa Bw Tolgos anashikilia kwamba bado yupo Jubilee na anawaheshimu Dkt Ruto na Rais Uhuru Kenyatta, amekuwa akimiminia sifa Bw Moi kama kiongozi shupavu ambaye anawaheshimu viongozi wengine.

“Nimependa sana jinsi Bw Moi amekuwa akiendesha siasa zake. Hamdunishi au kumchokoza kiongozi yeyote. Ana heshima kwa viongozi wengine kama tu mimi,” akasema Bw Tolgos akizungumza na Taifa Leo majuzi.

Bw Moi pia amekuwa akikutana na wazee wa jamii ya Kalenjin kama njia ya kuhakikisha anapata uungwaji mkono na kumpiga kumbo Dkt Ruto kwenye vita vya ubabe wa kisiasa katika Bonde la Ufa.

Cherargei amtaka Gavana Sang ajiuzulu kwa ‘kupoteza’ Sh2.3b

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Nandi Samson Cherargei sasa anamtaka Gavana wa kaunti hiyo Stephen Sang’ kujiuzulu la sivyo atimuliwe afisini na wananchi kwa kile anachodai ni kupotea kwa takriban Sh2.3 bilioni pesa za umma.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano, Seneta Cherargei pia alimtaka Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai George Kinoti kumchunguza Bw Sang kwa lengo la kupendekeza kushtakiwa kwake kwa kutoweka kwa pesa hizo.

“Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko imeibua maswali kuhusu kupotea kwa jumla ya Sh2.3 bilioni tangu Gavana Sang’ alipoingia mamlakani mnamo 2017. Pesa hizi zimepotea katika idara sita za utawala wa Sang,” akasema Bw Cherargei.

Seneta huyo alidai kuwa hatua ya Bw Sang’ ya kuwasimamisha kazi maafisa 16 wa serikali yake, wakiwemo mawaziri watatu ni hatua ya kujiondolea lawama ilhali yeye ndiye chanzo cha uovu huo katika serikali yake.

“Gavana Sang’ asitudanganye kwa kuwasimamisha maafisa 16 kutoka na kutoweka kwa vifaa vya thamani ya Sh234 milioni vilivyonunuliwa na Idara ya Elimu ya Chekechea kwa ajili ya ujenzi wa shule za chekechea katika kaunti ya Nandi. Takriban Sh2.3 bilioni zimepotea chini ya usimamizi wa Sang’ tangu alipoangia afisini na anafaa kuwajibikia uovu huo.

“Kwa hivyo, kama mtetezi wa ugatuzi katika kaunti ya Nandi nataka DCI, DPP na EACC kumchunguza Bw Sang’ kwa lengo la kumshtaki kwa kosa hilo. Kabla ya hapo nataka ajiuzulu mara moja la sivyo sisi kama wakazi wa Nandi tutamwandama na kumkamata,” seneta huyo aliyeonekana mwenye hamaki akasema.

Na bila kutoa ithibati, Seneta Cherargei alidai kuwa mwaka 2018 Gavana Sang’ alitumia Sh2.4 milioni kukodi helikopta aliyotumia kwenda kujivinjari katika Mbuga ya Kitaifa ya Maasai Mara.

“Hizi Sh2.4 milioni ambazo Gavana Sang’ alitumia kwa starehe zake zinaweza kufadhili ujenzi wa zaidi ya madarasa matano kwa gharama ya Sh500,000 kwa kila darasa. Hatuwezi kuvumilia ubadhirifu wa pesa kiwango hiki,” akasema Bw Cherargei, akiongeza kuwa matumizi ya pesa hizo yaligunduliwa na katika ripoti ya Bw Ouko ya miaka ya kifedha ya 2017/2018 na 2018/2019.

TAHARIRI: Vita dhidi ya ufisadi havilengi kabila lolote

NA MHARIRI

Madai yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Bnde la Ufa kwamba vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelea humu nchini vinalenga watu kutoka jamii fulani yanafaa kushutumiwa vikali.

Madai hayo ambayo yalitolewa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei (pichani) kwamba maafisa wanaosimamia mashirika na taasisi mbalimbali kutoka Bonde la Ufa wanalengwa katika vita hivyo yanatishia kurejesha nyuma hatua ambazo Kenya imepiga katika kuangamiza zimwi la ufisadi.

Kulingana na Bw Cherargei, vita hivyo vinalenga kusambaratisha azma ya Naibu wa Rais William Ruto kuingia Ikulu 2022.

Lakini Naibu wa Rais amekuwa akikariri kuwa wanaolengwa ni wafisadi na wala si watumishi wa umma wasio na hatia.

Je, Seneta Cherargei anazungumza kwa niaba ya nani, ikiwa hata Bw Ruto hakubaliani na madai yake?

Tumekuwa tukiona watu kutoka maeneo mbalimbali wakikamatwa tangu kuanza kwa vita vya ufisadi humu nchini. Hivyo madai kwamba vita hivyo vinalenga watu wa jamii moja si ya kweli.

Kulingana na ripoti mbalimbali ambazo zimewahi kutolewa, nchi hii hupoteza zaidi ya nusu ya fedha za bajeti yake kwa wafisadi.

Mathalan, aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), Philip Kinisu alifichua kuwa Kenya hupoteza Sh608 bilioni katika ufisadi.

Kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi kunamaanisha kuwa wanasiasa hao wanataka fedha hizo ziendelee kuishia katika mifuko ya watu wachache huku mlipa-ushuru akiendelea kuteseka kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Kulingana na takwimu za EACC, zaidi ya faili 180 za washukiwa waliochunguzwa katika mwaka wa matumizi ya fedha wa 2017/18 uliokamilika Juni 30, mwaka huu, tayari zimepelekwa katika afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa EACC ilipokea malalamishi zaidi ya 400 na 150 kati yazo zimefanyiwa uchunguzi na wahusika kuchukuliwa hatua.

Je, washukiwa hao wote wanatoka katika jamii moja? Wanasiasa wanafaa kuweka kando masiahi yao ya kibinafsi na badala yake kuunga mkono juhudi za serikali kukabiliana na jinamizi la ufisadi.

Amri ya kubomoa jengo la gavana yakoroga seneta

Na DENNIS LUBANGA

SENETA wa Kaunti ya Nandi, Bw Kiprotich Cherargei, ametishia kushtaki Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) baada ya kuagiza kubomolewa kwa afisi ya gavana kwa msingi kuwa jengo hilo si salama.

Bw Cherargei aliikashifu NCA kwa kutaka jengo hilo libomolewe ilhali mamlaka hiyo ndiyo iliidhinisha ujenzi wake.

“Nilidhani kuwa katika uhandisi, kila awamu ya ujenzi huidhinishwa na mhandisi pamoja na mwanakandarasi. Katika hali hii ni NCA iliyoidhinisha ujenzi wa jengo hilo na sasa inataka libomolewe. Nitawashtaki kama watachukua hatua hiyo ya ubomoaji,” akasema Bw Cherargei.

Kwenye ripoti ya mapema iliyoandikwa Machi 23, 2018, NCA ilitilia shaka uthabiti na usalama wa muundo uliotumiwa kwa ujenzi huo.

Ripoti hiyo inasema usanifu ujenzi wa awali wa jengo hilo ulibadilishwa wakati ujenzi ukiendelea ili kuongeza orofa zaidi, na hivyo basi msingi wa jengo uko hatarini kuwa hafifu.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumapili, seneta huyo alimkashifu pia Gavana Stephen Sang, kwa kukubaliana na msimamo wa NCA.

“Hili jengo lilitumia zaidi ya Sh150 milioni za mlipa ushuru. Ubomoaji wake utatumia karibu Sh20 milioni au zaidi,” akasema.

Alidai uamuzi wa NCA umechochewa kisiasa ili kunufaisha watu ambao watapewa kandarasi ya ujenzi upya, akasisitiza uamuzi kama huo lazima ufanywe kwa kushirikisha maoni ya wananchi.

Aliomba utawala wa Bw Sang ujishughulishe na ujenzi wa nyumba ya gavana badala ya kujiingiza kwa mipango ya kubomoa afisi yake.

“Tuko katika awamu ya mwisho ya kupeana fedha za kaunti ambazo zilitengwa katika mwaka wa kifedha uliopita kwa hivyo inafaa tujihadhari kuhusu jinsi tunavyotumia pesa za kaunti. Sitakubali jengo hilo libomolewe. Linahitaji tu kuimarishwa zaidi,” akasema.

Waziri wa miundomsingi katika kaunti, Bw Hillary Koech, alisema serikali ya kaunti iliwaalika maafisa wa NCA kuthibitisha uthabiti wa jengo hilo wakati lilipopata nyufa.

Kaunti ilikuwa imetumia Sh124 milioni kwa ujenzi wake, na Sh10 milioni zingine zimepangiwa kutumiwa kulikamilisha.

Bw Cherargei alikanusha madai kuwa pingamizi lake linatokana na sababu za kibinafsi dhidi ya gavana akasema hana nia ya kuwania ugavana bali anataka utumizi bora wa pesa za umma.