LEONARD ONYANGO: Siasa zimesaidia wafisadi kuendelea kuponda raha

Na LEONARD ONYANGO

MARA baada ya kutangaza kushirikiana na kinara wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 2018, almaarufu handisheki, Rais Uhuru Kenyatta alianzisha operesheni kali dhidi ya wafisadi.

Kila siku Wakenya walishuhudia ‘sinema’ katika runinga maafisa wa idara mbalimbali za mashirika ya serikali wakinaswa na polisi na baadaye kufikishwa kortini chini ya ulinzi mkali.

Baadhi ya wanasiasa na maafisa wakuu serikalini walienda kukamatwa na msururu wa magari ya kifahari.Gangaganga hizo za serikali ziliacha Wakenya na matumaini kwamba mamilioni ya fedha zao zinazoibwa kila siku kupitia ufisadi zingenusurika na badala yake zitumiwe katika miradi ya maendeleo inayofaidi wote.

Japo Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inasema kuwa imefanikiwa kurejesha zaidi ya Sh20 bilioni kutoka kwa wafisadi tangu 2018, vita dhidi ya ufisadi humu nchini vilimefeli kwa kiwango kikubwa.

Kwa mfano, kati ya 2018 na 2019, EACC inadai ilifanikiwa kubaini mali ya Sh27 bilioni iliyopatikana kwa njia ya wizi wa fedha za umma; lakini tume hiyo ilifanikiwa kurejesha Sh4.5 bilioni pekee.

Kulingana na ripoti ya Hali ya Uchumi ya 2021 iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) na kuzinduliwa wiki iliyopita, EACC imemkabidhi Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) zaidi ya faili 500 zinazohusiana na ufisadi tangu 2018.

Lakini hakuna mshukiwa hata mmoja wa ngazi ya juu serikalini ay mwanasiasa ambaye ametupwa gerezani.

Lawama

Badala yake, Rais Kenyatta amekuwa akirushia Idara ya Mahakama lawama kwa kujikokota kusikiliza na kuwahukumu washukiwa.

Kwa upande mwingine, Idara ya Mahakama pia inalaumu DPP kwa kuwasilisha kesi dhaifu bila ushahidi wa kutosha hivyo kuomba kusikilizwa kwazo kuahirishwe mara kwa mara.

Ukweli ni kwamba siasa ndicho kizingiti kikuu ambacho kimezuia Rais Kenyatta kukabiliana na ufisadi ambao wakati mmoja alidai kuwa unasababisha Wakenya kupoteza Sh2 bilioni kwa siku.

Vita dhidi ya ufisadi viliingizwa siasa hivyo imekuwa vigumu kuwanasa wanasiasa pamoja na maafisa wa ngazi za juu serikalini wanaoiba fedha za umma.

Kwa mfano, Gavana wa Kirinyaga Bi Anne Wauguru ambaye alifika Alhamisi mbele ya EACC kujibu maswali kuhusiana na madai ya ufisadi, alidai kuwa aliandamwa kwa sababu alitangaza mpango wa kutaka kugura chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta.

Bi Waiguru amekuwa amekuwa akihojiwa na EACC kwa miaka mingi lakini hajawahi kufunguliwa mashtaka kortini.Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua ambaye amekuwa akihojiwa mara kwa mara na EACC, anadai kuwa analengwa kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto.

Dkt Ruto pia amenukuliwa mara kadhaa akidai kuwa wanandani wake wanasingiziwa mashtaka ya ufisadi kama njia mojawapo ya kutatiza safari yake ya kutaka kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Ni wazi kwamba Rais Kenyatta amelemewa na vita dhidi ya ufisadi na hana budi kusalimu amri.

Waiguru alia kuhangaishwa tena na EACC

Na WANDERI KAMAU

GAVANA Anne Waiguru wa Kiringaga amedai kuwa ameanza kuhangaishwa na washindani wake kisiasa baada ya kusema anatathmini mwelekeo wa kisiasa atakaofuata, uchaguzi mkuu wa 2022 unapoendelea kukaribia.

Hapo jana, Bi Waiguru alisema ameagizwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufika katika afisi zake, kwa madai ya “matumizi mabaya” ya Sh52 milioni.Kulingana na Bi Waiguru, matumizi ya fedha hizo yaliidhinishwa na Bunge la Kaunti ili kulipa deni ambalo kaunti hiyo imekuwa nalo tangu mwaka 2010.

Alisema deni hilo lilitokana na ugavi wa ardhi ulioendeshwa katika eneo la makazi la South Ngariama, lenye zaidi ya ekari 7,000.

“Ni kinaya kwa EACC kuniagiza nifike katika afisi zake ilhali inafahamu hili ni deni ambalo serikali ya Kaunti imekuwa nalo kwa muda mrefu,” akajitetea gavana huyo kwenye taarifa.Bi Waiguru alihusisha maagizo hayo na “vitisho vya kisiasa” ambavyo amekuwa akipokea tangu Mchakato wa Kubadilisha Katiba (BBI) ulipoanza.

“Harakati za kuipigia debe BBI zilipoanza, nilisema nitatangaza msimamo wangu baada ya muda. EACC ilivamia afisi zangu. Majuzi, nilisema ninatathmini mwelekeo wa kisiasa nitakaofuata, sasa nimepewa maagizo hayo. Je, hii ni sadfa ama ni vitisho ambavyo vimekuwa vikiendeshwa dhidi yangu?” akashangaa.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema kuna uwezekano patashika hizo zinatokana na mwelekeo wa siasa za 2022 katika eneo hilo.

Ingawa Bi Waiguru ametangaza atatetea kiti chake cha ugavana, amekuwa akionekana kuwa miongoni mwa viongozi walio na nafasi kubwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kama msemaji wa Mlima Kenya.

Baadhi ya viongozi ambao wametangaza nia ya kuwania ugavana katika kaunti hiyo ni Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho, Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirichi, kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua kati ya wengine.

Kwa muda sasa, Bi Waiguru amekuwa akimlaumu Dkt Kibicho kwa kutumia ushawishi wake kuingilia utendalazi wa serikali ya kaunti.Hata hivyo, Dkt Kibicho amekuwa akijitenga na madai hayo, akisisitiza yeye ni mtumishi wa serikali na hana azma yoyote ya kujitosa kwenye siasa.

Wito EACC ichunguze maafisa wa elimu

Na MAUREEN ONGALA

CHAMA cha Walimu wa Sekondari (KUPPET) kimeomba Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ianzishe uchunguzi dhidi ya maafisa wawili wa elimu Kaunti ya Kilifi.

Walimu hao wanataka uchunguzi uanzishwe dhidi ya mkurugenzi wa elimu anayeondoka, Bi Eunice Khaemba na aifsa wa kutathmini ubora wa elimu, Bw Isaac Wasai wakiwahusisha na sakata za ufisadi.

Akizungumza katika kikao cha wanahabari afisini mwao mjini Kilifi, mwenyekiti wa KUPPET tawi la kaunti hiyo, Bw Caleb Mogere alidai kuwa wawili hao walihusika katika njama za kuhangaisha baadhi ya shule zilizotaka kusajiliwa, na pia kutatiza juhudi za bodi za usimamizi wa shule nyingine kuboresha miundomsingi.

“Kuna miradi mingi katika shule mbalimbali ambayo imekwama kwa sababu wamekataa kuidhinisha na tunashuku kuna ufisadi katika suala hilo zima,” akasema.

Malalamishi yao yanahusu pia kukwama kwa juhudi za kugeuza shule za kutwa ziwe za mabweni ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopokea elimu.

Hata hivyo, Bi Khaemba alikanusha madai hayo akasema masuala yanayotajwa hayatekelezwi na afisi yake kibinafsi wala afisa wa ubora wa elimu.

“Sina habari kuhusu shule zozote ambazo zimenyimwa usajili baada ya kutimiza mahitaji yanayotakikana. Ni muhimu itambulike kuwa usajili hufanywa na bodi wala si mtu binafsi,” akasema.

Uozo wa kimaadili miongoni wa wabunge waanikwa

Na CHARLES WASONGA

HUKU Spika wa Bunge Justin Muturi akiahidi kuwa madai ya ufisadi yaliyoelekezewa wabunge fulani na kampuni moja ya kutengeneza mvinyo yatachunguzwa imebainika kuwa wabunge hutumia kamati zao kama majukwaa ya kujitajirisha kinyume cha sheria.

Bw Muturi amethibitisha kupokea barua kutoka kwa mwenyekiti wa kampuni ya London Distiller Kenya Ltd (LDK) Mohan Galot, akilalamika kuwa wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji walihongwa na kampuni ya nyumba ya Erdermann Property Ltd ili wapendekeze kufungwa kwake.

Kampuni hiyo inayomiliki mtaa wa makazi ya Great Wall Garden iliyoko Athi River ilidai kuwa LDK imekuwa ikiachilia maji taka katika mto Athi na hivyo kuhatarisha maisha ya wakazi. Madai hayo yalichunguzwa na Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira na Mali Asili ambayo ilipendekeza kampuni ya LDK ifungwe ikiwa haitasita kuachilia maji taka katika mto Athi.

Katika barua yake kwa Muturi Bw Galot anasema hivi: “Wabunge wanachama wa kamati hiyo walipokea nyumba bila malipo au kwa bei nafuu kupitia jamaa zao au kampuni ambazo wao ni wakurugenzi ili wapendekeze kufungwa kwa LDK. Tunaomba afisi yake iwachukulie hatua wanachama wa kamati hii.”

“Malalamishi yaliwasilishwa na karani wa bunge alimwandikia mlalamishi akithibitisha kupokea barua yake. Suala hilo linachunguzwa,” Bw Muturi akasema.

Lakini mwenyekiti wa Kamati hiyo Moitalel Ole Kenta alipuuzilia mbali madai hayo akisema hayana msingi wala ukweli wowote.

“Tunataka yule aliyetoa madai hayo ya kiajabu kuyafafanua na kutoa ushahidi mbele ya asasi huru ya uchunguzi.” Akasema Bw Ole Kenta ambaye ni Mbunge wa Narok Kaskazini.

Bw Ole Lenta ameutaka usimamizi wa kampuni hiyo ya kutengeneza mvinyo kufika mbele ya Spika Muturi na ushahidi unaonyesha kuwa wanachama wa kamati yake walipokea hongo.

“LDK lazima ifike mbele ya kamati na kutaja majina ya wabunge inaodai kuwa walipewa nyumba. Hatujawahi kuhongwa na tutaendelea kufanya kazi yetu. Ripoti ya Kamati ya Mazingira lazima itekelezwe,” akasema mbunge wa Narok Kaskazini.

Alimshutumu Bw Galot kwa kujaribu kuwanyamazisha wanakamati.

“Kwake yeye maisha ya Wakenya wanaoathiriwa na uharibifu wa mazingira si muhimu. Kampuni hii ilifaa kufungwa miezi sita iliyopita kama tungetekeleza mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Mazingira. Tulisikiza vilio vya wafanyikazi na tukaipa LDK muda wa kutekeleza mapendekezo ya wabunge,” akasema Bw Ole Kenta.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Geoffrey Osotsi alisema wanachama wamekuwa wavumilivu na watatekeleza usawa kwa pande zote husika katika mzozo huo.

Mapendekezo ya Kamati ya mazingita yaliidhinishwa na Bunge mwaka 2018 kutokana na kesi iliyowasilishwa na Erdemann Ltd na wanunuzi 3,000 wa nyumba, waliolitaka Bunge lichunguze athari za shughuli za LDK kwa mazingira.

Madai ya ufisadi dhidi ya wanachama wa kamati ya bunge kuhusu utekelezaji ni mojawapo tu ya msusuru wa madai kama hayo ambayo yameshusha hadhi ya bunge.

Wabunge wamekuwa wakikashifiwa kwa kupokea mamilioni ya fedha ili kuwakinga maafisa wa umma wanaofika mbele ya kamati zao kuchunguzwa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za ufisadi na uhalifu wa kifedha.

Wabunge wanachama wa kamati ambazo huchunguza ripoti za Mkaguzi wa Hesabu zinazofichua visa mbalimbali vya matumizi mabaya ya fedha za umma katika asasi za serikali na serikali za kaunti wameshutumiwa kupokea hongo ili kuwalinda maafisa husika au kuandika ripoti inayowaondolea lawama.

Vile vile, kumekuwa na madai ya wabunge kuhongwa ili kutupilia mbali ripoti ya kamati za bunge zinazopendekeza maafisa fulani wakuu serikali kuchukuliwe hatua za kisheria.

Kwa mfano, mnamo 2018, Kamati ya Bunge kuhusu Hadhi na Mamlaka ya Bunge chini ya uenyekiti wa Spika Muturi ilipendekeza kuita Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ichunguze madai kuwa wabunge walihongwa kwa hadi Sh20,000 ili watupilie mbali ripoti kuhusu sakata ya uagizaji sukari yenye sumu.

Kiongozi wa wachache bunge John Mbadi aliungama kuwa madai hayo yana mashiko akisitikisha kuwa yanashusha hadhi ya bunge kama asasi ya kulinda masilahi ya raia.

“Uvumi kwamba wabunge wamekuwa wakihongwa una mashiko. Kwa mfano, kuhusu sakata ya sukari, ilidaiwa kuwa shahidi mmoja aliwahongwa wanachama wa kamati husika kwa Sh300,000 kila mmoja. Tunaambiwa kuwa afisa mwingine aliwapa baadhi ya wabunge Sh500,000 kila mmoja ili wamtetee,” akasema Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

Wakati wa sakata hiyo Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alidai kuwa Mbunge Mwakilishi wa Wajir Fatuma Gedi alijaribu kumhonga kwa Sh10,000 ndani ya ukumbi wa bunge ili kumshawishi aangushe ripoti hiyo ya sakata ya uagiza sukari.

Ripoti hiyo ilipendekeza kwamba aliyekuwa Waziri wa Biashara Adan Mohamed na aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuruhusu kuingizwa nchini kwa sukari yenye sumu na bila kulipiwa ushuru inayohitajika.

Mbunge Mwakilishi wa Kiambu Gathoni Wa Muchomba alitoa madai ya kiajabu kwamba baada ya wabunge wa kike walikuwa wakipokezwa hongo zao msalani.

EACC yaelezea hofu ya fedha za serikali kuporwa uchaguzi ukinukia

Na WALTER MENYA

ASASI za kuchunguza ufisadi zimeelezea hofu kuhusu kutokea kwa visa vya wizi na ubadhirifu wa pesa za umma kupitia ununuzi wa bidhaa kinyume cha sheria wakati huu uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

Magavana 22 wanaohudumu muhula wao wa pili watakuwa wakiondoka afisini, huku katika ngazi ya kitaifa utawala mpya utaingia mamlakani kwani Rais Uhuru Kenyatta atakuwa akiondoka baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho.

Kando na hayo, maafisa kadha wa umma, wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini watakuwa wakijiuzulu kufikia Desemba mwaka huu kuwania nyadhifa za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao unaoratibiwa kufanyika Agosti 9, 2022.

Kwa sababu hii, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imesema inafuatilia kwa makini matumizi ya fedha za umma serikalini katika mwaka huu wa kifedha na mwaka ujao wa 2022/2023.

Kwenye mahojiano na Taifa Jumapili, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw Twalib Mbarak, alisema wameanza kupokea ripoti kuhusu ubadhirifu wa pesa za umma na “tutachukua hatua hivi karibuni.”

“Katika miaka ya nyuma, tumegundua kuwa makosa mengi hufanyika katika miaka miwili ya mwisho kuelekea uchaguzi mkuu, kuhusiana na usimamizi wa fedha za umma. Tunajua kuwa wanasiasa wengi sasa wanasaka fedha za kufadhili kampeni zao. Katika ngazi ya kaunti, maafisa wengi wanajaribu kuiba kwa kukiuka sheria za ununuzi bidhaa za umma kwa lengo la kufadhili ndoto zao za kisiasa,” Bw Mbarak akaeleza.

Afisa huyo anasema kwamba uchanganuzi wao umeonyesha kuwa ndani ya miaka miwili kuelekea Uchaguzi Mkuu, huwa kuna shughuli nyingi za ununuzi bidhaa na huduma na matumizi ya fedha hupanda.

Kando na hayo, huwa kuna msukumo mkubwa wa ulipaji wa malimbikizi ya madeni ya miaka mitatu iliyopita “kwa sababu ni kwa njia hiyo ambapo watu hujifaidi.”

“Tunashirikiana na maafisa wanaoshikilia vyeo vya juu katika utumishi wa umma. Kwa mfano, utapata kuwa mwanasiasa au waziri anamsukuma afisa fulani kuvunja sheria za ununuzi. Kwa hivyo, tunawaonya maafisa kama hao kwamba wakikubali kutekeleza uvunjaji sheria katika ununuzi, basi tutawaandama huku wale waliowasaidia watakuwa huru wakifurahia matunda ya uovu huo. Kwa hivyo, ili wawe salama tunawaomba wawe makini wasishawishiwe kuvunja sheria,” akasema Bw Mbarak.

Miaka miwili kabla ya chaguzi mbili zilizopita (2013 na 2017) kulikuwa na visa vya kupotea kwa fedha za umma kupitia matumizi yasiyozingatia sheria.

Kulingana na Bw Mbarak sakata kama hizi hutokea kwa sababu maafisa fulani wa umma hutaka kutumia mianya ya ulegevu wa asasi za kufuatilia matumizi ya fedha za umma, kama vile bunge, kutokana na shughuli za kampeni za kuwania nyadhifa za kisiasa.

Afisa huyo mkuu mtendaji wa EACC pia alitetea hatua ya tume hiyo kutamatisha uchunguzi kuhusu sakata ya ukodishaji wa ndege ya kifahari iliyotumiwa na Naibu Rais William Ruto katika ziara rasmi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Boga na Mwashetani washtakiwe kwa wizi wa mahindi – EACC

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wakuu katika Wizara ya Kilimo wakiongozwa na Katibu Hamadi Boga na Mbunge wa Lungalunga Khatib Mwashetani wanakabiliwa na hatari ya kushtakiwa kwa sakata ya uagizaji wa mahindi ya thamani ya Sh1.8 bilioni mnamo 2017.

Katika ripoti iliwasilishwa bungeni Jumanne, Novemba 10, 2020, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inapendekeza kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji awafunguliwe mashtaka kwa makosa mbalimbali ya ufisadi.

EACC inasema kuwa uchunguzi wake umebaini kuwa Bw Mwashetani ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Blackstone ambayo ililipwa Sh792.5 milioni licha ya kwamba kampuni hiyo haikuwa imepewa zabuni.

“Uchunguzi pia ulionyesha kuwa kampuni ya Blackstone Investment haikuwa imealikwa kuwasilisha ombi la zabuni. Lakini ilipewa kandarasi ya kuwasilisha mahindi kinyume na Sheria ya Ununizi na Uuzaji wa Bidhaa za Umma (PPDA),” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak kwenye ripote ya pili ya utendakazi wake kati ya miezi ya Aprili 1, 2020 na Juni 2020.

“Uchunguzi pia ulibaini kuwa mbunge huyo ana uhusiano na kampuni ya Blackstone Investment Ltd na alifaidi kutokana na fedha zilizolipwa kampuni hiyo,” ripoti hiyo inaongeza.

Profesa Boga na maafisa wengine wa wizara ya kilimo walipatikana na hatia kutoa Sh1.8 bilioni kutoka kwa akaunti za Hazina ya Shirika la Uhifadhi wa Kimkakati wa Chakula (SFR) katika Benki Kuu kwa ajili ya kuingiza mahindi nchini Kenya mnamo 2018.

EACC iligundua kuwa maafisa hao walitoa pesa hizo bila idhibi ya Bodi ya SFR, hatua ambayo ni kinyume na Kanuni za Sheria ya Usimamizi wa Pesa za Umma (PFM Act).

Pesa hizo zilitolewa mwaka jana Wizara ya Kilimo na kulipwa kampuni ya kibinafsi kama malimbikizi deni kwa mahindi yaliyonunuliwa katika mwaka wa kifedha wa 2016-2017.

Ununuzi huo ulifanyika wakati ambapo Willy Bett ndiye alikuwa Waziri wa Kilimo lakini malipo yalitolewa wakati ambapo Bw Mwangi Kiunjuri ndiye alikuwa Waziri.

Bw Kiunjuri ni miongoni mwa maafisa wakuu wa Wizara ya Kilimo waliohojiwa na wapelelezi wa EACC kuhusiana na sakata hiyo.

Waziri huyo wa zamani pia alihojiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (PAC) iliyochunguza sakata hiyo. Hata hivyo, ripoti ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ugunja haikupendekeza kushtakiwa kwa Kiunjuri.

ONYANGO: EACC iadhibu wanasiasa wanaopuuza maagizo

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wanaonekana kupuuzilia mbali agizo la Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) la kuwataka kukoma kuchapisha majina au picha zao kwenye bidhaa za misaada wanazonunua kwa kutumia fedha za umma.

Inaonekana wanasiasa wamechukulia onyo hilo la EACC kuwa sawa na kelele za chura ambazo haziwezi kumzuia ng’ombe kunywa maji.

Juni 2020 EACC ilitoa onyo kwa magavana, wabunge na MCAs dhidi ya kubandika picha au majina yao kwenye misaada wanayotoa kwa wananchi wakati huu wa janga la corona.

Tume hiyo ilisema kuwa wanasiasa wanaotaka kuchapisha majina au kubandika picha zao kwenye misaada, basi hawana budi kutumia fedha zao za kibinafsi.

Onyo hilo lilitolewa ya viongozi, haswa magavana na wabunge, kubandika picha zao kwenye misaada iliyonunuliwa kwa fedha za umma.

Kwa mfano, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alishutumiwa vikali kwa kubandika picha yake kwenye chupa za sanitaiza iliyokuwa imetolewa kama msaada na kiwanda cha sukari cha Kibos.

Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Nairobi Esther Passaris, pia alikosolewa na Wakenya kwa kuweka picha yake kwenye sodo za bure kutoka kwa serikali kuu.

Lakini licha ya onyo la EACC, wanasiasa wanaendelea kusambaza misaada ya sanitaiza, barakoa, sabuni na vyakula iliyo na picha zao. Labda wanasiasa hao wanachukulia EACC kuwa sawa na jibwa lenye mazoea ya kubweka tu bila kung’ata.

Ili kuzima tabia hii, EACC inafaa kuanzisha uchunguzi dhidi ya wanasiasa wote ambao wamekuwa wakiweka picha na majina yao kwenye misaada na wanaopatikana na hatia waadhibiwe.

Kubandika picha kwenye miradi au bidhaa zilizonunuliwa kwa kutumia fedha za umma ni ufisadi wa kiwango cha juu na matumizi mabaya ya afisi.

Wanasiasa pia wamekiuka agizo la serikali la kuwataka kutotoa misaada moja kwa moja kwa wananchi ili kuzuia mikusanyiko ya watu ambayo inaweza kusababisha kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Vilevile, Shirika la Kudhibiti Ubora wa Bidhaa (Kebs) linafaa kuchunguza ubora wa sanitaiza, sabuni au barakoa ambazo zimekuwa zikisambazwa na wanasiasa.

Waziri Msaidizi wa Biashara Lawrence Karanja hivi karibuni alilalamikia kuhusu ongezeko la bidhaa feki kama vile sanitaiza, barakoa na sabuni, ambazo zimefurika nchini.

Kuna uwezekano hizi ndizo zimekuwa zikinunuliwa na wanasiasa na kusambazwa kwa wapigakura wao ili kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Juhudi za kuzima ufisadi zachacha mali ikitwaliwa

JOSEPH WANGUI Na CHARLES WASONGA

VITA dhidi ya ufisadi vinaonekana kuzaa matunda nchini baada ya Mahakama kukubaliana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na kutoa adhabu kali kwa wanaohusika na uovu huu.

Mwezi mmoja baada ya mahakama kuhukumu Mbunge wa Sirisia John Waluke na Grace Wakhungu, kifungo cha miaka 67 gerezani kwa kuilaghai Bodi ya Kitaifa na Mazao (NCPB) Sh340 milioni, wiki hii iliamuru kutwaliwa kwa mali ya watu wanaoshukiwa kufaidi kutokana na Sh791 milioni za shirika la NYS mnamo 2015.

Mahakama Kuu iliamuru kutwaliwa kwa nyumba na magari ya kifahari ya washirika sita wa kibiashara wa mshukiwa mkuu katika sakata hiyo, Bi Josephine Kabura.

Hii ni kufuatia ombi lililowasilishwa na Shirika la Kutwaa Mali ya Wizi (ARA) mbele ya Jaji Mumbi Ngugi.

Miongoni mwa washukiwa hao ni; Anthony Gethi Sh3.1 milioni, mamake, Charity Gethi na dadake Jedidah Wangari Wangui.

Wengine wanaoshukiwa kufaidi kutokana na Sh791 milioni za NYS ni Sam Mwadime Sh40 milioni, John Kago (Sh273 milioni), John Ndung’u, Jame Gachoka na James Kisingo.

Shirika hilo limepatiwa idhini ya kutwaa mali hiyo. Na jana EACC ilipata idhini ya mahakama kufunga akaunti nne za benki za Mkurugenzi wa Rasilimali katika Hazina Kuu ya Kitaifa, Charles Muia Mutiso, anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Bw Mutiso anadaiwa kufuja fedha za umma kati ya Aprili 2015 na Aprili 2020.Akaunti zake za benki ya Absa, Kenya Commercial Bank (KCB) na Cooperative zina jumla ya Sh36.7 milioni.

Katika benki ya Absa, Bw Mutiso ana akaunti mbili; moja ina Sh23.4 milioni na nyingine Sh5.8 milioni.Katika benki ya Cooperative amehifadhi Sh1.9 milioni na KCB kuna Sh5.5 milioni.

“Mali aliyo nayo Bw Mutiso inaonekana kuwa nyingi kuliko mapato yake. Hata hivyo, atapewa fursa ya kujitetea huku uchunguzi ukiendelea kwa mujibu wa sheria,” ikasema taarifa ya EACC.

Tume ya kupambana na ufisadi pia inachunguza gari la Bw Mutiso na vipande vyake vitano vya ardhi vilivyoko katika Kaunti za Nairobi na Machakos.

Jaji Mumbi Ngugi aliagiza akaunti hizo zifungwe kwa kipindi cha miezi sita kuwezesha EACC kukamilisha uchunguzi wake kabla ya kuanza mchakato wa kutaifisha mali hiyo iwapo atapatikana na hatia.Hiyo inamaanisha kwamba Bw Mutiso hataweza kutoa au kuweka fedha kwenye akaunti zilizofungwa hadi Januari mwaka ujao.

Kadhalika, hataweza kuuza gari lake au vipande vyake vya ardhi vinavyochunguzwa.Kulingana na EACC, Bw Mutiso mara nyingi amekuwa akiweka fedha kwenye akaunti zake za benki kupitia ATM.

“Kwa mfano, mwezi wa Juni 2015, aliweka Sh2 milioni kwenye akaunti zake katika benki ya Absa ndani ya siku chache,” ikasema taarifa ya EACC.

Bw Mutiso alikuwa akipata mshahara wa Sh144,675.60 kila mwezi. Kati ya Aprili 1, 2015 na Aprili 30, 2020 alipokea mshahara wa jumla ya Sh7,148,991.25.

Kulingana na EACC, Mutiso alijiunga na Hazina Kuu ya Kitaifa na kuwa Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali mnamo Julai 16, 2014.

Kabla ya kujiunga na Hazina Kuu ya Kitaifa, Bw Mutiso alikuwa mwanauchumi katika Wizara ya Fedha ambapo alihudumu tangu Julai 31, 2002.

Joho awindwa na EACC

MOHAMED AHMED na FARHIYA HUSSEIN

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inachunguza madai ya ufujaji wa pesa katika Serikali ya Kaunti ya Mombasa inayoongozwa na Gavana Hassan Joho.

Mkuu wa EACC jijini Mombasa, Bw Mutembei Nyaga jana alithibitisha kupokea ripoti kutoka kwa madiwani wa kaunti hiyo kuhusu utawala wa Bw Joho, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Nyaga alisema EACC itaamua hatua Za kuchukua baada ya kuchunguza madai yaliyowasilishwa, ambayo yanahusu utumiaji mbaya wa takribani Sh30 bilioni zilizokuwa kwa bajeti ya kaunti tangu 2017.

Haya yamefichuka siku chache baada ya kubainika kuwa Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed, pia anaandamwa na makachero wa EACC kuhusu kashfa ya ufisadi katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) iliyotokea mnamo 2015.

“Tulipokea barua hiyo juzi na bado tunaangalia madai hayo kutoka kwa madiwani,” akasema Bw Nyaga.

Katika barua yao kwa EACC, madiwani wanadai kumekuwa na ubaridhifu wa fedha katika utekelezaji wa bajeti za kaunti kuanzia 2017.

Wakiongozwa na Diwani wa Wadi ya Mjambere, Bw Fahad Kassim pamoja na mwenzake wa Frere-Town Charles Kitula, waliitaka EACC kuhakikisha usimamizi wa kaunti unapeana ripoti zake za fedha bungeni ipasavyo.

‘Tulimpa gavana muda atueleze jinsi pesa zilitumiwa. Tuliomba pia Idara ya Fedha kupitia kwa mwenyekiti wake itupatie angalau sababu ya kuridhisha kuhusu jinsi pesa zilitumiwa lakini hatujawahi kujibiwa hadi sasa. Tunasema tumechoka, wacha EACC ishughulikie hilo suala,’ akasema Bw Kitula.

Bw Kassim alidai kaunti hiyo ilikuwa inapanga kutumia Sh64 milioni kuweka maua katika kaunti na Sh3.4 milioni nyingine kuchimba visima akisema pesa hizo ni nyingi kwa miradi hiyo.

Kando na kupeleka kesi kwa EACC, walitishia kuwasilisha hoja ya kumng’oa Bw Joho mamlakani wakisema, pesa hutengewa maendeleo kwenye bajeti lakini hakuna miradi inaonekana mashinani.

“Kwa miaka mitatu hakujakuwa na uwasilishaji wa ripoti kuhusu matumizi ya fedha bungeni kama inavyotakikana kisheria,” akasema Bw Kassim kwenye mahojiano.

Aidha, viongozi hao wameitaka afisi ya fedha za kaunti kuhakikisha kuwa ripoti za fedha zinatumwa bungeni na kupelekwa katika afisi za serikali kuu kama inavyotakikana.

Viongozi hao wamedai hilo halitekelezwi ipasavyo kwa sababu ya njama za kuficha matumizi ya fedha za umma.

Uwasilishaji ripoti hizo ni hitaji la kisheria ambalo linapaswa kutekelezwa na kila kaunti nchini; jambo ambalo wawakilishi wa Mombasa wanadai halijakuwa likitekelezwa.

“Mambo yanafanywa tofauti hapa na ndio sababu hatuna imani na kamati ya fedha ambayo ndio imekuwa ikichangia kuwepo kwa shida hizi zote,” akasema Bw Kassim.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kaunti, Bw Mohammed Hatimy amepinga madai ya madiwani hao akisema hayana msingi. A

lisema ripoti hizo ambazo madiwani hao wanataka zimekuwa zikipelekwa katika afisi za wakuu wa fedha jijini Nairobi kama inavyotakikana.

“Serikali kuu inapata ripoti za kaunti kupitia kwetu, na bunge limekuwa likiwasilisha ripoti hizo ndio maana hakujakuwa na shida yoyote na afisi za serikali kuu zinazoangalia masuala ya fedha,” akasema Bw Hatimy.

Alieleza kuwa, pesa za kaunti zimekuwa zikitumiwa vyema kwa miradi ya maendeleo na kulipa mishahara ya wafanyakazi.

‘Kuna miradi katika kaunti, ilhali wanadai hakuna chochote kimefanywa. Pesa hutumiwa pia kulipa wafanyakazi mishahara yao miongoni mwa mahitaji mengine,’ akasema.

Junet hatarini kunyakwa na EACC kwa ufisadi

BRIAN WASUNA na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed, yumo hatarini kunyakwa na makachero wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa kuhusishwa na sakata ya ufisadi wa Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS).

Imefichuka kuwa, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Noordin Haji tayari ameidhinisha kesi ziendelezwe dhidi ya washukiwa wapya wa sakata ya kwanza ya NYS.

Uchunguzi wa EACC umeonyesha kuwa, mbunge huyo ambaye ni mwandani wa karibu wa Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, anashukiwa alinufaika kwa fedha zilizofujwa.

Sakata hiyo iliyohusisha ufujaji wa Sh1.9 bilioni ulitikisa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta katika awamu yake ya kwanza ya uongozi.

Katika mwaka wa 2015, Bw Mohamed alihusishwa na kampuni mbili zilizosambaza bidhaa za Sh129 milioni kupitia kwa zabuni za NYS ambazo zilitiliwa shaka.

Hata hivyo, wapelelezi wameamua kutilia maanani zabuni ambayo ilipeanwa kwa kampuni ya Zeigham Enterprises, ambapo Bw Mohamed ni mmoja wa wakurugenzi.

Zeigham Enterprises ilipewa kandarasi ya kuuzia NYS vifaa mbalimbali vilivyogharimu Sh21.8 milioni.

Uchunguzi umesema, baada ya Zeigham kupokea fedha hizo, kiasi fulani kilitumwa kwa akaunti ya benki ya Waziri Msaidizi wa Michezo Hassan Noor Hassan, na mkewe, Bi Meymuna Sheikh Nuh ambaye ni dadake Bw Mohamed.

Wakati huo, Bw Hassan alikuwa akifanya kazi katika Wizara ya Ugatuzi iliyokuwa ikisimamiwa na Bi Anne Waiguru, na ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya zabuni iliyochagua kampuni ya Zeigham.

Makachero wa EACC wamethibitisha kulikuwa na doa katika utoaji wa zabuni hiyo, kwani watu wengine wanaohusishwa na kampuni hiyo ni jamaa za Bw Mohamed.

Kakake mbunge huyo, Bw Hussein Mohamed Haji, pia ni mkurugenzi wa Zeigham Enterprises.

Mahakama yatetea uamuzi wa kumtoza faini ya Sh2m aliyeitisha hongo ya Sh15m

Na BENSON MATHEKA

MAHAKAMA imetetea uamuzi wa kumtoza aliyekuwa meneja wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), Robert Maina Ngumi faini ya Sh2 milioni kwa kuitisha hongo ya Sh15 milioni miaka sita iliyopita.

Uamuzi huo ulizua hisia kali miongoni mwa Wakenya wakishangaa jinsi mtu aliyeshtakiwa kwa madai ya kuitisha hongo ya Sh15 milioni alitozwa faini nafuu sana.

Hata hivyo, kwenye taarifa Alhamisi, idara ya mahakama imefafanua kuwa Bw Ngumi alikamatwa na wapelelezi wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kabla ya kupokea pesa alizokuwa akidai kama hongo.

“Siku aliyokamatwa, aliwekewa mtego na maafisa wa EACC. Pesa halisi alizopokea zilikuwa dola za Amerika 1,100 sawa na Sh110,000 za Kenya. Noti zingine zilikuwa feki, kwa hivyo kesi ilikuwa kuhusu Sh110,000,” imesema taarifa ya mahakama.

Mnamo Jumatano, Mahakama ya kusikiliza kesi za ufisadi ilimhukumu Bw Ngumi kufungwa jela miezi 18 akishindwa kulipa faini hiyo.

EACC pia imethibitisha kuwa Ngumi alikamatwa kabla ya kupokea pesa zote alizoitisha kama hongo ili aweze kupunguzia kampuni moja kodi iliyotakiwa.

“Pesa alizookea Bw Ngumi zilikuwa zimewekwa alama na EACC na ndizo alizopatikana nazo alipokamatwa. Hakupokea pesa zozote,” EACC ilisema kwenye taarifa.

UFISADI: Waandamanaji Kisumu watisha kufunga ofisi za EACC

Na BRENDA AWUOR

BAADHI ya wakazi wa Kaunti ya Kisumu wametisha kufunga ofisi za Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wakiilaumu kwa kuchelewesha pamoja na kushindwa kusukuma na kushtaki visa kadhaa vya tuhuma za ufisadi chini ya uchunguzi katika kaunti.

Aidha, wanasema inakawia na hata kukosa kubainisha majina kamili ya washukiwa wanaochangia kuzorota kwa sekta ya afya na mazingira Kisumu.

Wakazi kutoka Manyatta, Obunga, Kajulu, Bandani, Mamboleo, Nyamasaria, Ahero, Seme pamoja na maeneo mengine ya Kisumu, wakiongozwa na mwakilishi wao Bw Bonface Akach, wameonyesha ghadhabu zao wakitaka kujua sababu zinazochangia kuzorota kwa sekta ya afya na mazingira.

Wakiandamana mbele ya ofisi za EACC, Kisumu, wamesikika wakiwaita maafisa wa EACC watoke ofisini ili wawaelezee hali ya visa na ripoti kuhusu tuhuma za ufisadi ambazo wao kama tume wamekuwa wakizifanyia uchunguzi na kubaini majina ya washukiwa kwa kueleza iwapo wamefunguliwa mashtaka kortini au la.

Wametishia kufunga ofisi za EACC iwapo maafisa hawatajibu maswali hayo.

“Tume inapaswa kuelezea hali ya kesi walizofanyia uchunguzi, wabaini majina kamili ya washukiwa kwa kuelezea iwapo walifunguliwa mashtaka au la; vinginevyo tutafunga ofisi,’’ amesema Bw Akach.

Waandamanaji wakiimba nyimbo za kiharakati, wameitisha naibu mkuu wa EACC eneo la Magharibi Bw Aura Chibole, kuyajibu maswali yao la sivyo wangechukua hatua ya kufunga ofisa zao.

Bw Chibole aliyasikia maombi yao ambapo ametoka ofisini na kuyasikia malalamishi yao, lakini akawashawishi waandae orodha ya maswala ambayo walitaka majibu.

Kiongozi mmojawapo wa Kituo cha Maswala ya Kijamii na Haki cha Kondele Bw Boniface Agutu azungumza na Naibu Mkuu wa EACC kanda ya Magharibi Bw Aura Chibole (kushoto) mjini Kisumu Machi 4, 2020. Picha/ Ondari Ogega

“Ni jambo zuri nyie kututembelea ofisini mwetu ila ningependa kuona orodha ya maswala yote na hasa kesi mnazotaka niangazie ofisini mwangu,’’ amesema Bw Chibole.

Bw Akach aidha, ametofautiana naye huku akisema kwamba EACC ina kesi zote kwenye faili, hivyo basi ni jukumu la Bw Chibole kupitia na kunakili kesi hizo upya.

Wakazi hao wameipa EACC muda wa siku saba kuwapa majibu yote ya maswali yao na iwapo haitatimiza ahadi, basi Jumatano wiki ijayo watafunga ofisi zote kwa sababu itakuwa ni wazi kwamba “tume imeshindwa kufanya kazi.”

“Tumewapa muda wa siku saba ambapo msipotupa majibu, tutafunga ofisi zenu,’’ ametisha Bw Akach.

Wakazi hawa wanatarajiwa kutembelea ofisi za NEMA pamoja na ofisi ya Gavana wa kaunti ya Kisumu Alhamisi asubuhi kutafuta suluhisho la malalamisho yao.

Maimamu wataka tume mpya ibuniwe kusaidia EACC

Na TITUS OMINDE

BARAZA la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK) ukanda wa North Rift linataka serikali kuunda tume mpya ya kusaidia Tume ya Kukabili Ufisadi (EACC) ambayo baraza hilo linadia imelemewa kutekeleza majukumu yake.

Mwenyekiti wa CIPK Sheikh Abubakar Bin alisema kuna haja ya kubuniwa kwa tume mbadala ili kuboresha utendakazi wa EACC.

Sheikh Bin alisema EACC imeshindwa kupiga msasa Wakenya wasiokuwa na maadili kabla ya kuruhusiwa kugombea nyadhifa mbalimbali katika afisi za umma.

Alitolea mfano kuidhinishwa kwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ambaye kwa mujibu wao ameshindwa ecckuonyesha uadilifu wa uongozi.

Akihutubu mjini Eldoret, Sheikh Bin alisema kesi ya sasa ya ufisadi inayomkabili gavana huyo ni dalili dhahiri za kutofaulu kwa EACC katika jukumu lao la kuwachunguza wanasiasa kabla ya kuwaidhinisha kugombea viti husika.

Alipendekeza viongozi wa dini wapewe jukumu la kutoa vyeti vya maadili kwa Wakenya wanaopania kugombea nyadhifa serikalini.

“Viongozi wa dini wanapaswa kupewa jukumu la kuchunguza viongozi wanaokusudia kuteuliwa katika ofisi za umma,” alisema Bin

Kiongozi huyo wa CIPK alijuta kwamba kwa sababu za ukosefu wa uwazi na uadilifu wa viongozi wengi nchini kumechangia ufisadi na ukosefu wa maadili unaozidi kuwa kero kila uchao.

Akirejelea tabia ya gavana Sonko alipokuwa akikamatwa na maafisa wa polisi eneo la Voi wiki iliyopita, alisema tabia hiyo inaashiria ukosefu wa maadili.

“Mfano ambao gavana Sonko alionyesha wakati alipokamatwa na maafisa wakuu wa polisi huko Voi ulionyesha wazi kuwa yeye si kiongozi mwenye maadili. EACC na DCI lazima wawajibikie tabia hiyo potovu,” alisema Sheikh Bin.

Wito EACC ipige msasa ugavi ardhi

Na ANTHONY KITIMO

WAKAZI wa Kwale wameitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kuchukua hatua ya haraka na kuchunguza ugawaji wa ardhi kwa watu mashuhuri kando ya barabara ya pembeni ya Dongo Kundu na kuwaacha wakazi bila makao.

Mamia ya wakazi wamelalamika kuwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), imevuruga orodha ya watu ambao walipaswa kulipwa fidia na kuwapa watu kutoka sehemu nyingine ploti kando ya barabara hiyo ambayo itaunganisha kaunti za Mombasa na Kwale.

“Tunataka asasi husika kuchunguza jinsi maafisa wa serikali na wafanyabiashara walipata ploti katika ardhi yetu huku sisi wenyeji tukiambulia patupu,” alisema Tsuma Madafu.

Aliongeza: “Tuna orodha yenye majina ya watu waliofaidika na ploti hizo ilhali mpango wa kutulipa fidia haujakamilishwa”.

Mkazi mwingine, Ali Mwadeje alisema wao kama wakazi wa Tsuza wamejawa na wasiwasi kutokana na hali kwamba NLC haijawalipa ridhaa na idadi kubwa ya wenyeji kuachwa nje katika mpango wa ugavi wa ploti.

“Wakati wale walioathiriwa na awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu, kulikuwa na shughuli nyingi ya uhamasisho. Lakini katika awamu ya pili na tatu wakazi hawapewi habari zozote kuhusu mipango ya ulipaji fidia. Na tunashangaa kugundua kuwa wavuvi na waendeshaji boti katika ufuo wa Mkupe hawajajuimishwa kwenye orodha,” alisema Bw Mwadeje.

Wakazi sasa wanatishia kumzuia mwanakandarasi kuendelea na mradi huo ikiwa malalamishi yao hayatashughulikiwa kwa njia ya kuridhisha.

“Tumeona matingatinga na mitambo mingine katika eneo la mradi lakini kuna masuala kadhaa ambayo hayajashughulikiwa. Hii ndio maana tumeapa kuzuia utekelezaji wa mradi huu hadi malalamishi yetu yatakaposhughulikiwa,” akasema Masoud Mohammed, mkazi wa eneo la Gandi.

“Tunaunga mkono mradi huu lakini hatufai kuchezewa shere,” akaongeza.

Awamu ya pili ya mradi huo inajumuisha ujenzi wa barabara ya safu mbili ya umbali wa kilomita 8.96, ambao unatarajiwa kuanza mwezi huu.

Kutakuwa na makutano ya barabara katika barabara kuu ya Likoni-Lunga Lunga na madaraja mawili yatajengwa, moja katika eneo la Mwache- la urefu wa mita 680 na lingine katika eneo la Mteza, la urefu wa kilomita mbili.

Mradi huo, utakaogharimu Sh25 bilioni, umeidhinishwa na afisi ya Mwanasheria Mkuu na tayara kampuni ya Fujita Corporation kutoka Japan itaweka vifaa vyake katika eneo la mradi. Wakati huo huo, ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi wa barabara ya pembeni ya Dongo Kundu kwa gharama ya Sh30 bilioni na ujenzi wa eneo la kiuchumi unakabiliwa na changamoto za ulipaji ridhaa kwa watakaopokonywa ardhi.

Maafisa wa EACC wafanya msako nyumbani kwa Gavana Waititu

Na MWANDISHI WETU

MAAFISA wa Tume ya Maadili na Kupambana dhidi ya Ufisadi (EACC) wamefanya msako Alhamisi katika nyumba ya Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu, iliyoko mtaani Kileleshwa, Nairobi.

Maafisa hao waliofika kwa makumi, waliingia katika makazi hayo ya Bellcrest Gardens, kando mwa barabara ya Githunguri, dakika chache tu baada ya saa kumi na moja alfajiri na kuanza kupekua wakitafuta faili na stakabadhi.

Upelelezi wa EACC ulidai kuwepo kwa ufisadi katika kaunti yake ambayo inapakana na ile ya Nairobi ambalo ni jiji kuu la Kenya.

Aidha, walikuwa wanatafuta stakabadhi muhimu zinazohusiana na kandarasi ambazo zilitolewa na utawala wa Bw Waititu.

Gavana huyo amemulikwa na EACC kuhusiana na madai ya ufisadi kugubika mipango kadha ya serikali ya kaunti ikiwa ni pamoja na ule wa Kaa Sober ulionuia urekebishaji mienendo na kuzima uraibu wa pombe miongoni mwa waathirika.

Vyanzo kadhaa vimeambia Taifa Leo kwamba maafisa wengine 15 wa serikali ya kaunti hiyo wamemulikwa katika uchunguzi unaoendelea.

Tutakuletea habari kwa kina.

 

Wakenya wachunguze vyama kabla ya kuwekeza fedha – EACC

NA CECIL ODONGO

MAAFISA wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi(EACC), wamewataka Wakenya kuchunguza kwa makini kabla ya kujiunga na Vyama vya Akiba na Mikopo, ili kuzuia kulaghaiwa fedha zao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Twalib Mbarak, alisema tatizo kubwa linalozonga vyama vingi vya ushirika ni uongozi usiofaa na ufisadi unaotekelezwa na wakuu wa vyama hivyo. Alisema wakuu hao wanaviunda ili kujiendeleza kwa pesa za wanachama.

“Inasikitisha Wakenya waliokuwa wamejawa na matumaini ya kufikia makubwa maishani kwa kuwekeza fedha zao katika vyama vya ushirika wanatapeliwa na kusalia bila chochote,” alisema Bw Mbarak.

Aliongeza, “Hata hivyo wanafaa kujilaumu wenyewe kwa kukimbilia utajiri wa haraka bila kuchunguza kwa makini jinsi vyama hivyo vinavyoendeshwa.”

Afisa huyo alikuwa akizungumza wakati wa kutiwa saini kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya EACC na vyama vya akiba na mikopo jijini Nairobi. Makubaliano hayo yatahakikisha kwamba EACC inahusika pakubwa kudhibiti masuala yanayoendelea ndani ya vyama hivyo. Bw Mbarak pia aliwataka wanachama wa vyama husika kuchukua tahadhari kabla ya kuwadhamini wanachama wenzao kuchukua mikopo baada ya kubainika wengi hutoroka kisha kuwaachia wadhamini mzigo mzito wa kulipa fedha zilizokopwa.

Ingawa hivyo, aliuhakikishia uongozi wa vyama vya akiba na mikopo kuwa watashirikiana nao kuwaandama wanaohepa kulipa mikopo yao.

Mwenyekiti wa EACC, Askofu Mstaafu Eliud Wabukala, naye alisifu mafanikio ambayo vyama vya ushirika vimesaidia wananchi wengi ila akaonya kwamba matukio ya ufisadi huenda yakayeyusha nia ya wengi kuwekeza kwa vyama hivyo.

“Binafsi vyama hivi vimenisaidia sana kufanya masuala mengi ya kibinafsi. Hata hivyo kama tume, ushirikiano huu utatuwezesha kuingilia kati na kurejesha uaminifu, nidhamu na maadili katika vyama vyetu,” akasema Bw Wabukala.

Kutiwa saini kwa makubaliano haya ya kudhibiti shughuli za vyama vya ushirika kunajiri baada ya wanachama wa Ekeza Sacco inayosimamiwa na Mhubiri mwanasiasa David Kariuki Gakuyo, kupoteza fedha zao baada ya kubainika walilaghaiwa.

UFISADI: Afisa mteule EACC afichua alinolewa katika FBI na CIA, Amerika

Na CHARLES WASONGA

AFISA MPYA aliyeteuliwa kwa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak ameahidi kurejesha imani ya Wakenya katika utendakazi wa tume hiyo endapo bunge litaidhinisha uteuzi wake.

Ijumaa, Bw Mbarak aliwaacha wabunge vinywa wazi alipofichua kuwa amewahi kupokea mafunzo katika Mashiriki ya Ujasusi Nchini Amerika, FBI na CIA, na kupata ujuzi ambao umemwezesha kuimarisha utendakazi wake katika asasi zote ambazo amewahi kuhudumia.

Pia, alielezea kwa kina tajriba yake kama afisa wa jeshi, afisa wa ujasusi katika jeshi, Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS), iliyokuwa Tume ya Kupambana na Ufisadi Nchini (KACC) na wadhifa wake wa sasa katika KenGen.

Aliwaambia wabunge kwamba, atachapa kazi kwa mujibu wa sheria na bila mapendeleo na kuahidi kujiuzulu ikiwa mtu yeyote atadhubutu kushawishi kazi yake kwa njia yoyote, haswa kisiasa.

Bw Mbarak, ambaye ni afisa wa usalama na maadili katika kampuni ya uzalishaji umeme, KenGen, jana aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kwamba, atapambana na ufisadi katika serikali kuu na zile za kaunti kwa kuwalenga washukiwa wote bila kujali nyadhifa zao.

“Dhana kwamba kuna watu au afisi fulani yenye ushawishi ambayo huingilia utendakazi wa EACC haitakuwepo chini ya uongozi wangu. Na endapo kutatokea ushawishi kutoka afisi yoyote ambao utaingilia utendakazi wangu kwa njia moja ama nyingine, nitaamua kujiondoa na kwenda nyumbani kwangu Kilifi,” akasema alipopigwa msasa na kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo.

“Sitakubali amri kutoka popote… Nitawahudumia Wakenya wote kwa usawa,” Bw Mbarak akaeleza.

Afisa huyo wa zamani wa ujasusi katika jeshi la Kenya alisema atachunguza upya faili za kesi zinazowahusu washukiwa wanaoshikilia vyeo vya juu, ambazo zimekwama katika EACC kwa muda mrefu kuhakikisha zinashughulikiwa kwa haraka.

“Najua kuna faili ambazo zimedumu katika tume hii kwa zaidi ya miaka saba. Hizi ndizo nitashughulikia kwa haraka endapo kamati hii itaidhinisha uteuzi wangu,” Bw Mbarak akasema.

“Na nitahakisha hilo kwa kutekeleza mabadiliko katika afisi kuu. Nitahakikisha kila afisa anafanya kazi aliyohitimu kufanya… na hili litawezakana tu kupitia upigaji msasa upya,” Bw Mbarak alieleza.

Aliwaomba wabunge kuzifanyia marekebisho sheria za EACC haswa sheria inayohusu kutwaliwa kwa mali zote zilizopatikana kwa njia ya ufisadi.

“Kwa sababu nitakuwa nikiwajibikia bunge katika utendakazi wangu, naomba kamati hii kuhakikisha kuwa EACC imepewa meno kisheria kuweza kutwa mali ya washukiwa wote wa ufisadi. Kwa sasa kuna udhaifu fulani wa kisheria ambao unahujumu uwezo wa tume hii kutwaa mali ya wezi wa rasilimali za kitaifa,” akasema.

Bw Mbarak aliwasisimua wabunge alipoelezea tajriba yake kama afisa wa jeshi, afisa wa ujasusi katika jeshi, Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS), iliyokuwa Tume ya Kupambana na Ufisad Nchini (KACC) na wadhifa wake wa sasa katika KenGen.

Bw Mbarak alisema ufanisi huu ulichangiwa pakubwa na mamake mzazi ambaye alijinyima anasa za dunia ili kufadhili masomo yake.

Alipandwa na hisia na kudondokwa machozi alipokuwa akielezea mchango wa mamake maishani mwake.

Wakenya 13 waomba kazi ya kusimamia EACC

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA 13 wameorodheshwa kwa mahojiano kujaza wadhifa wa mkurugenzi mkuu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Mahojiano hayo yanatarajiwa kufanyika Novemba 27. Naibu Mkurugenzi Mkuu wa EACC Bw Michael Mubea ni miongoni mwao.

Mahojiano hayo yamepangwa baada ya muda wa kuhudumu wa Halakhe Waqo kukamilika. Bw Waqo amehudumu kwa miaka sita na hana nafasi ya kutuma maombi kuzingatiwa tena kwa nafasi hiyo.

Wengine watakaohojiwa ni Bi Sarah Kilemi, mwanachama wa bodi ya Huduma ya Polisi Murshid Mohamed, Bw James Warui, Bw Vincent Omari, Bw Jillo Kasse, Bw Chege Thenya, Bw Reuben Chirchir, Bw Cyrus Oguna, Bw Abdi Mohamud, Bw Twalib Mbarak, Bw Joel Mabonga na Bi Lucy Wanja.

Bw Waqo aliingia afisini Januari 2013 baada ya EACC kubadilishwa kutoka Tume ya Kitaifa ya Kupambana na Ufisadi (KACC).

Majina ya watakaoorodheshwa yatatumwa bungeni kujadiliwa.

KURUNZI YA PWANI: EACC yachunguza ubaguzi katika ugavi wa basari Kibarani

NA SAMUEL BAYA

Tume ya kupambana na ufisadi (EACC) eneo la Pwani imeanzisha uchunguzi kuhusu ugawaji duni wa basari katika kamati ya basari ya wadi ya Kibarani, Kaunti ya Kilifi.

Kamati hiyo imekumbwa na madai ya ubaguzi katika ugawaji wa basari na tayari hazina ya basari katika kaunti ya Kilifi ilikuwa imeisimamisha kazi kamati hiyo mwezi uliopita.

Kumekuwa na madai kutoka kwa wakazi kuwa bodi hiyo iko na upendeleo katika kugawa fedha za masomo.

Ingawa lengo la basari ni kuwasaidia wanafunzi werevu kutoka jamii maskini kuendelea na masomo, kamati hiyo imelaumiwa kwa kuwanufaisha washirika wa karibu wa wanakamati.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo afisini mwake, mwenyekiti wa hazina hiyo Bw Mulewa Katana alisema waliarifiwa na EACC kwamba tume ilikuwa ikichunguza kamati hiyo hivyo ilikuwa ni makosa kuivunja. Na Samuel Baya

“Ni kweli tulikuwa tumesimamisha bodi hiyo baada ya lalama nyingi kutoka kwa wananchi. Wakazi wengi walikuwa wakilalama kuhusu jinsi wasimamizi wa kamati hiyo wamekuwa wakijitengea fedha nyingi kwa washirika wao na jamii zao.

Baada ya sisi kama hazina kuisimamisha kamati hiyo, mmoja wao aliamua kulipeleka suala hilo kwa tume ya kukabiliana na ufisadi. Tume hiyo baadaye ilituandikia barua kutuarifu kwamba wanafanya uchunguzi,” akasema Bw Mulewa.

Alisema kupitia kwa ushauri wa EACC hazina hiyo ilibatili uamuzi wake ili kutoa fursa kwa tume hiyo kuendelea na uchunguzi wake.

Bw Mulewa alisema hayo huku katibu wa kaunti hiyo Bw Arnold Mkare akiwaonya maafisa wasimamizi wa wadi kwamba watachukuliwa hatua kali endapo itabainika wanahusika na ubadhirifu wa fedha hizo za basari.

“Fedha za basari ni za umma na wala sio pesa za mtu binafsi. Tumepata habari kwamba kuna baadhi ya wasimamizi wa wadi wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya kamati za basari za wadi kufanya ufisadi na upendeleo. Hili ni onyo kwamba hatutavumilia tena, ” akaonya Bw Mkare.

Hazina hiyo ya basari hutenga kiasi cha Sh350 millioni kila mwaka ili kugharamia masomo kwa wanafunzi ambao hawana uwezo wa kulipa karo.

Katika wadi 35 za kaunti hiyo, kila wadi hupokea kiasi cha Sh10 millioni kila mwaka kwa ajili ya kuwapa karo wanafunzi.

Tahadhari ya ufujaji na ugawaji mbaya wa fedha hizo ulianza mwezi uliopita pale mwakilishi wa wadi hiyo Bw John Mwamutsi alipomuandikia barua hazina hiyo baada ya madai kuibuka.

Katika barua hiyo ya Oktoba 26, Bw Mwamutsi aliandika akiomba kamati hiyo isimamishwe haraka na uchunguzi uanzishwe.

“Kumeibuka madai mabaya sana ya usambzaji wa fedha za kamati ya basari ya Kibarani. Tafadhali kama hazina, tunaomba muisimamishwe kamati hiyo na kuruhusu uchunguzi ufanyike,” ikasema barau hiyo ambayo Taifa Leo ilifanikiwa kupata nakala yake.

Naye Bw Mulewa katika barua yake ya Oktoba 27 alitangaza kusimamishwa kwa kamati hiyo hadi pale uchunguzi ufanyike na kupata tatizo ambalo linakumba kamati hiyo.

“Kupitia narua ambayo tulipata kutoka kwa mwakilishi wa wadi ya Kibarani ninakufahamisha kwamba kamati yako imesimamishwa kuendelea na shughuli zozote hadi uchunguzi kamili utakapofanyika.

Kwa sasa ninamruhusu mwakilsihi wa wadiu kuanzisha juhudi za kuweka kamati ya muda ili kuhakikisha kwamba kumebuniwa kamati ya muda ndani ya wiki mbili zijazo,” akasema Bw Mulewa.

Hata hivyo mnamo Oktoba 29, hazina hiyo ilipata barua kutoka kwa tume ya kupambana na ufisadi ikiitaka hazina hiyo iachane na mpango wa kusimamisha kamati hiyo.

‘Tume ya kupambana na ufisadi inachunguza utumiaji mbaya wa fedha za umma katika kamati ya basari ya Kibarani kama jambo hilo lilivyoripotiwa kwetu.

Tayari jambo hili lilikuwa limewasilishwa kwako awali kulingana na barua ambayo tuko nayo. Tuko na habari kwamba mwenyekiti wa sasa wa kamati hiyo alirekodi taarifa na afisi yetu na uchuguzi unaendelea.

Haukufaa kuivunja kamati hiyo kwa sababu uchunguzi unaendelea,” ikasema sehemu ya barua hiyo ya EACC.

Naye Bw Mulewa katika barua ya Oktoba 31, aliandikia tume hiyo ya EACC akigeuza barua ya awali ya kuivunja kamati hiyo.

“Tumeona yale ambayo mulisema katika barua yenu na yote tumeyasikia na kwa sababu hiyo hazina ya fedha za basari ya Kilifi imebatilisha uamuzi wa kuivunja kamati hiyo ya Kibarani ili kuruhusu uchunguzi uendelee,” ikasema sehemu ya barua hiyo.

Tangu ianzishwe, hazina hiyo imesaidia jumla ya wanafunzi 220,416 kuendelea na masomo yao. Idadi kubwa kati ya hawa ni wale ambao wanasomea katika shule za sekondari ambao kufikia sasa ni 157,758.

Washukiwa wa ufisadi warushwe rumande kesi zikiendelea – Wabukala

Na VALENTINE OBARA

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) sasa inataka washukiwa wa ufisadi wawe wakisukumwa rumande kesi zao zinapoendelea kusikizwa.

Hata hivyo, msimamo huu wa Mwenyekiti wa tume hiyo, Askofu Mkuu (Mstaafu) Eliud Wabukala ni kinyume cha Katiba, ambayo katika vifungu vya 49 na 50 inasema kila mshukiwa ana haki ya kupewa dhamana, isipokuwa pale kuna sababu kubwa za kufanya azuiliwe kesi ikiendelea.

Askofu Wabukhala alisema kuzuiliwa kwa washukiwa kutasaidia katika vita dhidi ya ufisadi ili kuepusha ufujaji wa mabilioni ya pesa za umma.

Idadi kubwa ya washukiwa wa ufisadi ambao wameshtakiwa wako nje kwa dhamana kesi zao zikiendelea kusikizwa.

“Hivi majuzi, Jaji Mkuu aliahidi kuhakikisha kesi za ufisadi zinaharakishwa. EACC itazidi kuunga mkono msimamo huo na hata kuomba kuwe na maagizo ya kuweka washukiwa ndani wakati kesi zinapowasilishwa mahakamani,” akasema.

Alikuwa akizungumza jana katika hafla ya kuzindua rasmi Taasisi ya Kitaifa ya Mafunzo ya Uadilifu (NICA) jijini Nairobi.

Taasisi hiyo itakuwa ikitoa mafunzo kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta ya kibinafsi kuhusu masuala ya uadilifu, mbinu za kupambana na ufisadi, usimamizi bora, uongozi bora miongoni mwa masuala mengine.

Askofu Wabukala alikariri hatua zilizopigwa na tume hiyo katika kupambana na ufisadi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, akisema hawatalegeza kamba na watazidi kushirikiana na asasi nyingine kumaliza uozo huo.

Katika kipindi hicho, EACC iliripoti kuzima wizi wa Sh4.2 bilioni za umma na ikitambua mali 14 ya umma iliyokuwa imenyakuliwa na watu binafsi inayokadiriwa kuwa za thamani ya Sh2.3 bilioni. Alisema tayari mali ya thamani ya Sh352 milioni imerudishwa mikononi mwa umma.

Tume hiyo pia ilikamilisha uchunguzi wa visa 183 vya ufisadi na kuwasilisha faili hizo kwa Idara ya Mashtaka ya Umma, ambapo ilipendekezwa visa 135 vifunguliwe mashtaka, na 14 vichukuliwe hatua za kinidhamu katika mashirika ambako washukiwa wanahudumu.

Bw Wabukhala jana alisema kwa sasa, kuna zaidi ya visa 3,000 vya ufisadi vinavyochunguzwa na EACC ambavyo vinahusu maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya kitaifa na za kaunti.

“Tunachukulia kwa uzito zaidi kesi zinazohusu maafisa walio na mamlaka ya juu na pia zile zinazohusu wizi wa kiasi kikubwa cha pesa. Tunafahamu kila Mkenya anataka kuona wahusika wa ufisadi wakiadhibiwa kwa hivyo tutaharakisha kasi kuwasilisha faili zetu za uchunguzi kwa DPP, ambaye tunashirikiana naye katika juhudi hizi,” akasema.

Alionya watumishi wa umma waamue kama wanataka kuendelea kutumikia wananchi kwani hakutakuwa na mazingara ya kuendeleza ufisadi na wanaotaka kujitajirisha kwa kufuja pesa za umma ni heri wajiuzulu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Halakhe Waqo, na Katibu wa Wizara ya Elimu anayesimamia ustawishaji wa mafunzo ya kitaaluma, Bw Alfred Cheruiyot miongoni mwa wengine.

ONYANGO: EACC isijifiche kwa Biblia, iweke mikakati inayofaa

Na LEONARD ONYANGO

TUME ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kwa mara nyingine imejaribu kutumia neno la Mungu katika juhudi za kupambana na zimwi la ulaji hongo ambalo ni donda sugu humu nchini.

Tume ya EACC inayoongozwa na Askofu Mkuu mstaafu Eliud Wabukala, kwa ushirikiano na viongozi wa makanisa mbalimbali, wiki iliyopita ilizindua mwongozo wa masomo ya Biblia unaolenga kuwezesha Wakenya kuelewa anayosema Mungu kuhusiana na ufisadi.

Mwongozo huo pia unalenga kuhakikisha kuwa Wakenya wanasoma na kuelewa kwamba Mungu anachukia ufisadi hivyo kuwawezesha kuishi maisha ya uadilifu.

Wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo, tume hiyo ilijitetea kwa kusema kuwa kila Mkenya ana jukumu la kuzuia au kukabiliana na ufisadi.

Hii si mara ya kwanza kwa EACC.Tume ya EACC mnamo Februari mwaka 2017 ilitangaza kushirikiana na viongozi wa kidini kutoka Baraza la Makanisa nchini (NCCK), Baraza la Dhehebu la Wahindu (HCK), Muungano wa Makanisa la Kiinjilisti (EAK) na Baraza Kuu la Waislamu (Supkem) kukabiliana na ufisadi nchini.

Tume ya EACC pamoja na viongozi hao wa kidini waliunda jopokazi la watu 12 ambalo lilitwikwa jukumu la kuhamasisha Wakenya kujiepusha na ufisadi.

Jopokazi hilo pia lilipewa jukumu la kuhimiza Wakenya kujiepusha na vurugu na kuchagua viongozi wenye maadili katika uchaguzi wa Agosti 8.

Jopokazi hilo la ‘watumishi wa Mungu’ lilifeli kwani juhudi zao ziliambulia patupu. Uchaguzi wa mwaka jana uligubikwa na fujo. Madai kwamba baadhi ya wabunge walichukua hongo ya Sh10,000 kila mmoja kutupilia mbali ripoti kuhusu kuingizwa kwa sukari ya magendo nchini inayodaiwa kuwa na sumu ni ithibati tosha kwamba hatukuchagua viongozi wenye maadili.

Wengi wa viongozi wafisadi waliapishwa kwa kutumia Biblia au Koran kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao katika afisi wanazoshikilia lakini hilo halijawazuia kuiba mali ya umma.

Idadi kubwa ya viongozi wanaokabiliwa na sakata za ufisadi wamekuwa wakihudhuria kila ibada katika misikiti na makanisani.

Tumeona wahubiri wa Injili wakinajisi watoto wadogo na hata kuhusishwa na sakata za wizi licha ya kuwa ‘wataalamu’ katika uchambuzi wa Neno la Mungu.

Ni kweli kwamba kila Mkenya ana jukumu la kupambana na ufisadi lakini EACC inafaa kufahamu kwamba wananchi wanalipa ushuru ili kuiwezesha kukabiliana na wezi wa fedha za umma.

Tume ya EACC haina budi kujiepusha na sarakasi na badala yake ikabiliane na ufisadi badala ya kuwabembeleza wafisadi kusoma Biblia ili wabadili mienendo yao.

Wafisadi hawana wakati wa kusoma Biblia kwani wanatumia muda wao mwingi kutafuta mianya na kuunda mipango ya kuiba fedha za Wakenya.

EACC inafaa kuwakamata na kuhakikisha kuwa wafisadi wanaadhibiwa badala ya kuwabembeleza kusoma Biblia.

Washukiwa wote wa ufisadi wanastahili kuchukuliwa hatua kulingana na sheria kwani fedha wanazopunja zingesaidia kupeleka nchi hii mbele zaidi kimaendeleo.

Madiwani waliokataliwa na wapigakura kuchunguzwa na EACC

Na PETER MBURU

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Jumatatu imeandikia wawakilishi wadi wanane wa Kaunti ya Busia wa zamani kufika mbele yake kuhusiana na sakata ya ufisadi kwenye bajeti ya ziada kaunti hiyo.

EACC iliwaandikia madiwani hao Jumatatu asubuhi ikiwataka kufika mbele yake Septemba 12 ili wahojiwe kuhusiana na sakata hiyo, kwa barua zilizoelekezwa kwa karani wa bunge na katibu wa kaunti.

“Tunachunguza madai ya ufisadi na kughushi kuhusiana na bajeti ya ziada ya kaunti,” ikaandika tume hiyo.

Madiwani wanaotarajiwa kupigwa msasa na tume hiyo sasa ni  Philip  Emaset, Tony Opondo, Josephat Wandera, Stephen Ajakait, Godfrey Odongo, Gabriel Okello, Kenneth Ichasi na Margaret Chale.

Hii ni miezi mitatu baada ya gavana wa kaunti hiyo Sospeter Ojaamong pamoja na maafisa wengine wa kaunti kushtakiwa kwa kupotea kwa Sh8milioni mnamo Juni.

Gavana Ojaamong pamoja na waliokuwa mawaziri Bernard Yaite, Allan Ekweny, na Samuel Ombui aliyekuwa wa fedha walikamatwa na kushtakiwa Juni ambapo walikana makosa ya kushirikiana kutekeleza makosa ya kiuchumi, matumizi mabaya ya afisi na kufanya mradi ambao haukuwa umepangwa kwenye bajeti.

Aidha, takriban mwezi uliopita, aliyekuwa gavana wa Nyandarua Daniel Waithaka Mwangi pamoja na afisa mwingine mkuu wa kaunti walishtakiwa kwa sakata za kupotea kwa pesa za umma walipokuwa ofisini.

Hatuwezi kutazama mamilioni ya mafuta yakifyonzwa KPC – Halakhe Waqo

Na CHARLES WASONGA

Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Halakhe Waqo Jumanne alitofautiana vikali na wabunge kuhusu sakata ya Sh660 milioni katika Kampuni ya Mafuta Nchini (KPC).

Huku wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kawi wakidai sio makosa kwa kampuni za humu nchini kuwa maajenti wa kampuni za ng’ambo kuhusiana na suala la utoaji wa zabuni, wanachama wa kamati hiyo walishikilia hiyo sio makosa.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Robert Pukose na mbunge wa Butere Tindi Mwale walidai haikuwa kosa kwa kampuni ya Cla-Val kuiuzia KPC mitambo ya kujaza mafuta kwa ndege (Hydrant Pit Valve-HPV) kwa bei ya juu, Bw Waqo alisema hatua hiyo ni kinyume cha sheria za ununuzi bidhaa za umma.

“Sioni makosa yoyote kwa kampuni ya Cla-Val kutumia kampuni ya Aero Dispenser Valve kama ajenti wake wa kuuza mitambo kama hii, hata kama itakuwa kwa bei ya juu,” akasema Dkt Pukose ambaey ni Mbunge wa Endebess.

Lakini Bw Waqo alishikilia kuwa ilikuwa hatua ya wizi wa waziwazi kwa kampuni ya Aero Dispenser kununua mitambo hiyo kwa Sh72 milioni kutoka kwa Cla-Val kisha kuiuzia KPC kwa bei ya Sh660 milioni, hivyo kuunda faida ya zaidi ya asilimia 800.

“Huu ni wizi ya pesa za umma na sisi katika EACC hatutakaa kitako uovu kama huu ukiendelea,” akasema Afisa huyo alipofika mbele ya kamati hiyo kuelezea hatua ambayo EACC imepiga katika uchunguzi wa kashfa hiyo.

Bw Waqo aliwaambia wabunge hao kwamba tume yake itapendekeza kushtakiwa kwa wahusika wote wa kashfa hiyo ambayo imewaweka pabaya baadhi ya maafisa wa KPC.

Katika sakata hiyo maafisa wa KPC walipeana zabuni ya Sh660 milioni kwa ununuzi wa mitambo ya kujaza mafuta kwa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JKIA) badala ya Sh59 milioni, bei halisi kutoka kampuni ya Cla-Val kutoka Amerika.

Afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Halakhe Waqo jana aliwaambia wabunge kuwa watawasilisha faili ya uchunguzi huo kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ili washukiwa hao washtakiwe kwa wizi wa pesa za umma.

“Tumepata usaidizi kutoka mataifa ya Amerika na Canada katika uchunguzi wetu na sasa tuko ya ushahidi tosha kuhimili kesi mahakama. Mapema wiki ujao tutawasilisha faili yenye ushahidi tosha kwa DPP,” Bw Waqo akasema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Kawi, katika majengo ya bunge.

Afisa huyo aliwaambia wanachama cha kamati hiyo kwamba japo KPC ilipaswa kununua mitambo hiyo kwa Sh59 milioni maafisa wake walishirikiana na kampuni za Aero Dispenser Valve Ltd kukubali bei ya Sh660 milioni.

“Na mnamo Machi 31, 2015 kampuni hiyo ambayo tumebaini ni feki ililipwa malipo ya awali ya Sh262 milioni, kiasi sawa na asilimia 40 ya thamani ya zabuni hiyo huku zilisalia Sh400 milioni” akasema.

Akauliza: “Swali letu ni je, ni nani aliamuru kwamba biashara hiyo ipewe kampuni ya Aero Dispenser Valve ilhali kamati ya zabuni ya KPC ilipendekeza ipewe watengenezaji hali ya mitambo hiyo ambayo ni kampuni ya Cla-Val ya Amerika?.

Bw Waqo alisema japo uchunguzi wao umedumu kwa zaidi ya miaka mitatu hatimaye EACC imebaini ukweli kwamba wafanyakazi wa KPC walishiriki njama ya kuiba pesa za umma kwa kupandisha bei ya mitambo hiyo kupita kiasi.

Maafisa wa kaunti waingia mafichoni kuhepa kukamatwa na EACC

TOM MATOKE NA BARNABAS BII

 

MAAFISA wakuu katika Serikali ya Kaunti ya Nandi wamekimbilia mafichoni kuhepa maafisa wa Tume ya Ufisadi (EACC) wanaofanya uchunguzi wa sakata ya ubadhirifu wa mabilioni ya pesa katika muda wa miaka mitano iliyopita.

Tume hiyo ya EACC imekita kambi katika kaunti hiyo katika muda wa siku tatu zilizopita huku ikiwasaka maafisa wa sasa na waliokuwepo, wanaohusishwa na pesa hizo kwa kutoa kandarasi za ujenzi wa barabara na pia zabuni bila kufuata utaratibu unaostahili.

Wapelelezi wa tume walifanya misako katika nyumba za maafisa hao katika kaunti za Nandi, Uasin Gishu, Trans Nzoia na Vihiga ambapo walichukua stakabadhi muhimu ambazo ni pamoja na hati miliki za ardhi, mashine za kielektroniki, stakabadhi za zabuni na uagizaji miongoni mwa nyingine.

Afisa mkuu wa polisi eneo la Nandi, Bw Patrick Wambani alithibitisha kuwa kundi la maafisa wa EACC liliomba usaidizi wake kuwasaka baadhi ya waliohusishwa na ubadhirifu wa pesa za umma.

Pia walizuru makao ya aliyekuwa gavana Cleophas Lagat ambapo kaunti wakati wa kipindi chake inashukiwa kupoteza mabilioni kati ya 2014 hadi sasa.

Jumatatu, wapelelezi waliwakamata washukiwa zaidi ya 10 waliohusishwa na uporaji wa pesa za umma miongoni mwao wakiwa ni katibu wa kaunti, Bw Francis ominde na aliyekuwa afisa mwandamizi wa fedha, Bw Emmanuel Wanjala na kuchukua stakabadhi za ardhi na nyingine za zabuni.

Taarifa nyingine zilieleza kuwa maafisa hao walipata kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa afisa wa ngazi za juu baada ya kuvamia nyumbani kwake.

Miongoni mwa waliokamatwa na kuandikisha taarifa katika msako wa EACC ni afisa wa fedha katika kaunti, Bi Helen Katam na aliyekuwa mkuu wa fedha, Bw Charles Muge.

SAKATA YA NYS: Uhuru ategemea DCI, DPP kuliko tume ya EACC

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta ameonekana kubadilisha mbinu za kupigana na ufisadi huku akihusisha Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na lile la ujasusi (NIS) kuliko Tume ya Maadili ya Kukabiliana na Ufisadi (EACC).

Hii inadhihirika katika uchunguzi wa sasa wa sakata mbali mbali za ufisadi ambapo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti aliwasilisha faili za uchunguzi wa kashfa ya wizi wa Sh0.5 bilioni kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma DPP moja kwa moja.

Jumanne, DPP Noordin Haji hakutaja EACC kwenye taarifa yake kuhusu washukiwa wa sakata ya NYS waliokamatwa na wanaochunguzwa.

Awali kwenye barua, Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua alimwambia Bw Kinoti kwamba Rais alitaka mashirika yote kushirikiana katika uchunguzi.

Kinachoonyesha kwamba EACC halikuhusishwa kikamilifu ilivyokuwa kwenye sakata ya kwanza ya NYS 2015, tume hiyo haikutumiwa nakala ya barua hiyo.

Kwenye barua hiyo Kinoti na Haji waliagizwa kuwa wakimwarifu Rais kila siku kuhusu hatua za uchunguzi. Kashfa ambazo DCI inachunguza ni yaa NYS, Kampuni ya Mafuta na Kenya Power ambayo inasikisiwa kuwa Wakenya walipoteza zaidi ya Sh10 bilioni.

Na Wadadisi wanasema kuwa rais anaonyesha ana imani na maafisa wa DCI chini ya Bw Kinoti kuliko EACC ambalo limekuwa likijivuta kufanya uchunguzi.

 

 

 

 

Waziri wa zamani ajifungia nyumbani asikamatwe na EACC

Na FRED MUKINDA

MAKACHERO wa Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) wanamsaka aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Michael Kamau baada ya kukosa kumkamata katika msako waliofanya nyumbani kwake Jumanne.

Kulingana na Naibu Afisa Mkuu wa EACC, Michael Mubea, maafisa hao walishindwa kumkamata Bw Kamau kwani alijifungia ndani ya nyumba na akakataa kuwafungulia maafisa hao walipowasili katika makazi ya Windy Ridge mtaani Karen.

“Tulienda kwake kumkamata ili ahojiwe kisha afikishwe mahakamani. Hata hivyo alijifungia ndani na kukataa kutoka nje. Sisi si wale wanaovunja nyumba za watu. Niliwaambia maafisa wangu waondoke kwa kuwa tuna njia nyingi za kushughulikia suala hili,” akasema Bw Mubea.

Alieleza hatua hiyo ilitokana na kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji alipitia faili ya kesi ya waziri huyo wa zamani na alitoa idhini ya kukamatwa kwake Ijumaa iliyopita.

Jamaa wa familia ambaye hakutaka jina lake linukuliwe alieleza Taifa Leo kwamba makachero 10 waliokuwa ndani ya magari mawili waliwasili nyumbani mwa Bw Kamau saa kumi na moja alfajiri asubuhi na kuondoka saa nne mchana.

Hata hivyo mawakili wa Bw Kamau waliokita kambi nyumbani kwake walisimulia vinginevyo. “Makachero ambao hawakujitambulisha waliwasili katika makazi yake kwa lengo la kumnasa na kumhoji.

Mwenzangu Wanja Wambugu alifika na kuwaeleza kuna amri ya Mahakama ya Rufaa ya Julai mwaka 2017 iliyozuia uchunguzi dhidi yake,” akasema wakili Nelson Havi.

Tume ya EACC awali ilimchunguza Bw Kamau na akashtakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa kanuni za zabuni katika kandarasi ya ujenzi wa barabara.

 

Kujinusuru kortini 

Baadaye Bw Kamau alienda kwenye Mahakama Kuu akilenga kuzuia kesi dhidi yake akihoji kwamba tume ya EACC haikuwa na idadi inayotakikana ya makamishna alipofikishwa mahakamani.

Ingawa Mahakama Kuu ilikataa kuzuia kushtakiwa kwake, alikimbilia Mahakama ya Rufaa na majaji watatu wa mahakama hiyo wakafutilia mbali uamuzi wa korti ya hakimu. Uamuzi huo ulisababisha mahakama hiyo ya chini kumwachilia.

Waziri huyo wa zamani tena alikimbilia Mahakama Kuu akidai mahakama ya hakimu ingemwondolea kesi kabisa badala ya kumwaachilia lakini mwezi Aprili mahakama hiyo ilikataa pendekezo lake na kuiruhusu EACC ianze uchunguzi mpya dhidi ya madai ya kushiriki ufisadi yanayomkabili.

Pia Jaji wa Mahakama Kuu Hedwig Ongudi alikataa maombi yake ya kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali.

“Mahakama ya rufaa haikumwaachilia kwa sababu yeye anadai kwamba alikamatwa kama tume haikuwa na makamishna wa kutosha. Sasa wapo na kesi iendelee. Madai ya mawakili wake ni propaganda tupu,” akasema Bw Mubea.

Wakili Havi alisema makachero hao walisema walipata maagizo kutoka juu kufanya upekuzi katika nyumba ya Bw Kamau lakini hata baada ya kuruhusiwa kufanya hivyo walionekana kuwa na malengo tofauti.

Aidha alilamika kwamba EACC inalenga kukiuka sheria na amri za mahakama katika kumshtaki waziri huyo wa zamani.

 

Wakazi wafunzwa mbinu mpya ya ‘kumulika hongo’

PETER MBURU na MERCY KOSKEY

VIONGOZI wa usalama waliungana na maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kaunti ya Nakuru Jumatano kuongoza matembezi na uhamasishaji kwa umma ili waripoti visa vya ufisadi kupitia simu za mkononi.

Wakiongozwa na kamishna wa kaunti hiyo Joshua Nkanatha na kamanda wa polisi Hassan Barua, viongozi hao walishirikiana na shirika la ‘Mulika Hongo’ kuhamasisha umma kuhusu namna bora, mpya na salama ya kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.

Kulingana na mratibu wa shirika hilo wa kitaifa Bi Grace Wanjohi, wananchi ndio nguzo muhimu katika kupigana na ufisadi nchini, endapo watakubali kuripoti visa hivyo wanapokumbana navyo, ama kukataa kutoa rushwa.

Walizindua mbinu ya kutumia ujumbe mfupi kwa simu ya rununu ama apu kwa simu za kisasa zenye mifumo ya Android kuripoti visa hivyo kwa haraka na kwa njia salama.

“Kupitia njia hii, zaidi ya macho milioni 40 yameweza kuona na kuripoti visa vyote vya ufisadi popote, wakati wowote na dhidi ya yeyote. Mafanikio yetu mkuu ni uwezo wa kuzuia ufisadi kwani waendeshaji wanaripotiwa kwa njia salama,” akasema Bi Wanjohi.

Kulingana na kamishna wa kaunti ya Nakuru Bw Joshua Nkanatha, ni jukumu la kila mtu kupigana na ufisadi na wote, anayetoa na anayepokea rushwa watakabiliwa kisheria, ila lawama haipaswi kuwaangukia wanaopokea pekee.

“Kamati ya usalama Nakuru ilifanya mikutano mingi na ikaamua kupigana na suala la ufisadi ana kwa ana na hafla hii itaandaliwa kila mwaka ili kufanikisha vita hivi.juhudi sasa ni kujumuisha wananchi katika vita dhidi ya ufisadi kwani ndio wanaoumia zaidi na visa vya ufisadi,” Bw Nkanatha akasema.

Naibu mkurugenzi wa EACC eneo la South Rift Bw Gilbert Lukhoba alisema kuwa Mulika Hongo ilikuwa mbinu muhimu ya kupigana na ufisadi, akirai wakenya kushirikiana na mashirika yote yanayofanikisha vita hivyo.

“Viongozi wa dini, wazazi, walimu na wote wanafaa kueneza maadili mema ili taifa lijivunie mazao mema siku za usoni,” akasema Bw Lukhoba.