Polisi sita wanaohusishwa na mauaji ya ndugu wawilli wa Embu wakamatwa

Na SAMMY WAWERU

MAAFISA sita wa polisi waliotajwa kuhusika na mauaji ya ndugu wawili Embu mapema mwezi huu wamekamatwa Jumatatu jioni na kusafirishwa hadi Nairobi wakisubiri mashtaka. 

Mamlaka Huru ya Kuchunguza na Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), imependekeza waachishwe kazi mara moja, huku ripoti hiyo ikitarajiwa kuwasilishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) ili kufunguliwa mashtaka.

“Waachishwe kazi mara moja, kufuatia kukamilika kwa uchunguzi wa mamlaka huru na ripoti kuwasilishwa kwa DPP. Kwa sasa maafisa hao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji. Mapendekezo haya hayatabadilika,” IPOA imeeleza kwenye taarifa.

Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha sheria ya IPOA, mauaji yanayofanyika katika kituo cha polisi, kusababishwa na askari au mwanachama wa kikosi cha polisi (NPS), mamlaka hiyo inapaswa kuyachunguza.

“Kifungu cha 29 cha sheria za IPOA pia kinasema endapo uchunguzi unaonyesha kuna tendo la uhalifu, mapendekezo ya kufunguliwa kwa kesi ya mashtaka yawasilishwe kwa DPP.

“Uchunguzi wa mamlaka unaonyesha kuna kesi ya uhalifu kwa maafisa hao sita,” inafafanua.

Kwenye mapendekezo ya IPOA, askari waliotajwa kuhusika katika mauaji ya wavulana Benson Njiru na Emmanuel Mutura, wasalimishe silaha walizonazo mara moja.

“Maafisa na wakuu wa polisi waliohojiwa na kuandikisha taarifa washirikiane na IPOA watakapohitajika kwenye uchunguzi zaidi,” mamlaka inasema.

Mbali na kesi ya mauaji, IPOA imesema inaendelea kushughulikia mashtaka mengine ya utepetevu kazini kwa maafisa waliohusika katika mchakato mzima wa kufariki kwa wawili hao.

Vijana Njiru na Mutura walifariki mikononi mwa polisi, baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka sheria za kafyu.

Walizikwa Ijumaa wiki iliyopita, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi na wanasiasa mbalimbali, wote wakishinikiza maafisa husika kuchukuliwa hatua kisheria.

Simulizi ya mama yashtua mahakama

Na GEORGE MUNENE

Mama mmoja jana alisimulia mahakamani jinsi alivyopata chooni mifupa ya mwanawe na mjukuu wake ambao walikuwa wametoweka katika njia ya kutatanisha kwenye kijiji cha Uriro, Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu.

Bi Pauline Kagendo na mwanawe Johnson Murithi ambaye alizaliwa miezi mitano iliyopita, walitoweka kwa njia ya kutatanisha mnamo Juni 10, 2017.

Mifupa hiyo ilipatikana ndani ya choo cha mpenziwe marehemu ambaye alikuwa afisa wa GSU.

Akitoa ushahidi mahakamani, mamake marehemu Kanini Nyaga alieleza Mahakama ya Embu kwamba mifupa hiyo iliyokuwa imeteketezwa ya mwanawe na mjukuu wakem ilipatikana ndani ya choo na makachero.

Mwanawe Bi Nyaga, alikuwa ameacha masomo katika kidato cha kwanza.Alikuwa akitoa ushahidi kwenye kesi ambapo afisa huyo wa GSU Edwin Mwenda alishtakiwa kwa kumuua Bi Kagendo na Bw Muriithi.

Bw Mwenda ambaye tayari ameachishwa kazi anawakilishwa na wakili Emies Mutegi na inadaiwa kuwa alikuwa mpenzi wa Bi Kagendo.

Bi Nyaga alidai kwamba mwanawe aliacha shule mnamo 2016 baada ya kupachikwa mimba na afisa huyo wa GSU ndipo akajifungua mtoto mvulana.

Alisimulia jinsi Bi Kagendo aliondoka nyumbani ili kumpeleka mwanawe hospitalini baada ya kuugua lakini hakurejea tena.

“Mwanangu alinieleza kwamba alikuwa anaenda kukutana na mpenziwe ili wote wawili wampeleke mtoto hospitalini kupokea matibabu lakini hakurejea nyumbani,” akaeleza mahakama alipokuwa akihojiwa na wakili David Njoroge.

Baada ya kumsaka mwanawe na mjukuu wake kwa muda wa mwezi moja, Bi Nyaga alipiga ripoti kuhusu kisa hicho katika kituo cha polisi cha Ishiara na uchunguzi ukaanza ndipo mifupa ya wawili hao ikapatikana kwenye choo ndani ya boma la Bw Mwenda.

‘Ukeketaji bado unaendelea Embu’

NA CHARLES WANYORO

Wasichana wanne waliokeketwa Kaunti ya Embu Kijiji cha Gitugi wameruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitalini na kupelekwa kwa nyumba spesheli ili kupewa nasaha. 

Wasichana hao watajiunga na wenzao walionusuriwa wakiwa wanatayarishwa kukeketwa. Ukeketaji huo uliendeshwa na wauguzi waliostaafu.

Diwani mteule Sicily Warue alisema kwamba wanaendelea kuchunguza jinsi wasichana hao wanavyoendelea, ambao wana umri kati ya miaka 8 na 12.

Bi Warue alisema kwamba watatunga sheria itakayosaidia kumaliza ukeketetaji wa wasichana wa shule.

Madiwani ambao ni wanachama wa kamati ya jinsia, utamaduni, watoto na huduma za jamii walisema kwamba vitendo hivyo vilivyopitwa na wakati vilikuwa bado vinatekelezwa katika kaunti hiyo kwa sababu ya kukosa sheria  zitakazochukuliwa dhidi ya ngariba.

Huku akiongea baada ya kutembelea hospitali hiyo ya Embu, Bi Warue alisema kwamba kamati itatengeneza sheria itakayoeleza adhabu itakayochukuliwa wakeketaji hao wa zamani. Diwani huyo alisema atawahimiza madiwani wote wanawake waunge mkono mswada huo.

Bi Warue alisema kwamba madiwani wanaume waliahidi kuhakikisha kwamba mswada huo umepitishwa.

Diwani mteule Elizabeth Kibai aliwahimiza pia wenzake waunge mkono mswada huo ili kuokoa wasichana kutokana na unyama huo.

Kaunti za Meru na Embu zapigania miraa

DAVID MUCHUI na CHARLES WANYORO

SERIKALI za Kaunti za Embu na Meru zinazozania Sh2.2 bilioni zilizotolewa kuwafaa wakulima wa miraa katika kaunti hizo.

Huku gavana wa Embu Martin Wambora akisema serikali yake iko tayari kuzungumza na serikali ya Meru kuhusiana na jinsi ya kugawanya pesa hizo, serikali ya Meru imesema kuwa hakuna mazungumzo yoyote ya aina hiyo.

Wambora Jumatano alisema wajumbe kutoka Embu walikuwa katika Kaunti ya Meru kuzungumzia jinsi ya kugawanya pesa hizo na jinsi zitakavyotumiwa.

Alizungumzia Sh1 bilioni, lakini jumla ya Sh2.2 bilioni zilitolewa katika mwaka wa 2016/2017 ambapo Sh1 bilioni zinashikiliwa na Hazina ya Fedha ili kungoja Wizara ya Kilimo kuunda kamati kutekeleza ripoti ya jopo kuhusu miraa iliyotolewa mwaka 2017.

Wambora alisema Embu ililenga kutumia mgao wake kununua miche ya mimea tofauti kwa lengo la kukuza aina tofauti za mazao ili kuepuka kutegemea miraa.

Biashara ya miraa imehusishwa na kiwango kikubwa cha vijana wanaoacha shule eneo hilo.

Alisema uongozi wake ulikuwa umetoa miche 5,000 ya makadamia kwa wakulima katika maeneo wanakopanda miraa.

Hata hivyo, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na chama cha wauzaji miraa cha Nyambene (Nyamita) alipuzilia mbali madai hayo kwa kusema pesa hizo zitatumika kufufua masoko ya miraa.

Bw Kiraitu alisema pesa hizo zitatumika kuambatana na mapendekezo ya jopo kuhusiana na miraa.

“Kwa sasa, Mbunge wa Igembe Kasakazini Maore Maoka ndiye anayefaa kufuatilia suala hilo kwa serikali ya kitaifa kuhusu wakati zitakapotolewa pesa hizo,” alisema.