GWIJI WA WIKI: Dennis Mwima

Na CHRIS ADUNGO

MAISHA huisha. Kabla yaishe, yaishi yaishe. Usiishi kuisha.

Maisha ni safari ambayo mwisho wake ni siri kubwa isiyojulikana kwa binadamu!

Japo utajikwaa, kuteleza na mara nyingine kuanguka katika safari ya maisha, usiogope kitu! Jinyanyue upesi, futa vumbi, pangusa tope na utimke tena. Kuanguka ndiko kuinuka!

Nidhamu, bidii na uvumilivu huchangia pakubwa mafanikio ya mtu. Huwezi kabisa kujiendeleza maishani au kitaaluma iwapo hujiamini. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta!

Usitamauke unapokosa kufaulu. Mtangulize Mungu, endelea kukazana na hatimaye milango ya heri itajifungua yenyewe!

Huu ndio ushauri wa Bw Dennis Mwima almaarufu ‘Mwalimu wa Ulimwengu’ – mwandishi mzoefu wa vitabu ambaye kwa sasa anafundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Providence Academy, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Dennis alizaliwa na kulelewa katika eneo la Butere, Mumias, Kaunti ya Kakamega. Ndiye mwanambee katika familia ya Bw Washingtone Mwima na Bi Sarah Faluma.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Shinamwenyuli, Butere mnamo 1996. Ni katika shule hiyo ambapo hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ilianza kujikuza ndani yake.

Mara si haba, alijipata akiiga sauti za wanahabari maarufu na akapendwa na watu kutokana na ‘sauti yake ya utangazaji’.

Baadhi ya wanahabari aliowaiga ni Jilani Wambura, Leonard Mambo Mbotela na marehemu Billy Omalla.

Kati ya walimu waliotambua utajiri wa kipaji cha Dennis katika utangazaji wa habari na kumpa majukwaa maridhawa ya kukuza na kupalilia talanta yake ni Bw Atita, Bi Susan Kageha na Bw Andrew Were Nyangweso waliomfundisha katika shule ya msingi.

Wengine waliopanda na kuotesha mbegu za utashi wa Kiswahili ndani yake ni Bi Stella Angufu na Bi Agnes Sungu waliotangamana naye kwa karibu sana katika Shule ya Upili ya Musanda, Butere.

Baada ya kufanya mtihani wa KCPE mnamo 2005 kisha KCSE mnamo 2009, Dennis alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Meru (2011-2012).

Alihiari kusomea ualimu baada ya ndoto yake ya kujiunga na chuo cha uanahabari kuyeyushwa na mawimbi ya ufukara yaliyotishia kumzimia mshumaa wa elimu. Hata hivyo, anaishi kwa imani kwamba mvuto wa kipekee uliomo ndani ya mrindimo wa sauti yake utakuja kuwa kitambulisho chake atakapokuwa mwanahabari katika siku za usoni.

UALIMU

Dennis alianza kufundisha mnamo 2013 baada ya kuajiriwa na Kakamega Hill School Junior. Akiwa huko, alikutana na walimu wazoefu wa Kiswahili – Zadock Amakoye na Bw Masika – waliomkuza pakubwa kitaaluma. Alihudumu huko hadi 2015 kabla ya kuhamia Ruai Junior Schools, Nairobi.

Kutua kwake jijini Nairobi kulikuwa mwanzo wa mkoko kualika maua. Alipata fursa za kuhudhuria makongamano mbalimbali ya Kiswahili, akapevuka zaidi kitaaluma na akawa mwalimu bora.

Kabla ya kuajiriwa na Shule ya Msingi ya Providence Academy Ruaraka mnamo Januari 2021, Dennis aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Msingi ya Anas Academy (Eastleigh), Clara Academy (Ruaraka) na Total Care Academy (Pangani).

UANDISHI

Dennis alikuwa mwepesi wa kuandika hadithi bunilizi za watoto alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Insha nyingi alizozitunga chini ya uelekezi wa walimu wake zilimzolea sifa sufufu na kumfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Kufikia sasa, ameandika kitabu cha kiada ‘Kichocheo cha Kiswahili KCPE’ kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Jalada la ‘Kichocheo cha Kiswahili’. Picha/ Chris Adungo

Ametunga pia hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika diwani mbalimbali. Baadhi ya hadithi hizo ni ‘Kuku Mfanyabiashara’ katika mkusanyiko wa ‘Kasuku wa Salome na Hadithi Nyingine’, ‘Udongo wa Hekima’ katika ‘Mtoto wa Dhahabu na Hadithi Nyingine’ pamoja na ‘Ibilisi Mweupe’ katika ‘Kilele cha Mambo na Hadithi Nyingine’.

Dennis ameandika miswada mingi ya hadithi fupi na vitabu vya kiada kwa minajili ya Mtaala wa Umilisi (CBC). Nyingi za kazi hizo zipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu nchini Kenya.

‘Shauku ya Kuishi’ ni novela ambayo Dennis anaiandaa sasa kwa matarajio ya kuchapishwa hivi karibuni.

Miongoni mwa waandishi waliomshika mkono, kumpa motisha ya kujitosa ulingoni kikamilifu na kupiga mbizi katika bahari pana ya uandishi wa vitabu vya Kiswahili ni Ali Hassan Kauleni, Benard Simiyu Mkuyuni, Mathias Momanyi, Tom Nyambeka na Timothy Omusikoyo Sumba.

Wengine waliomshajiisha kukichangamkia Kiswahili kama kiwanda kikubwa cha ajira na maarifa ni Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, marehemu Profesa Ken Walibora, marehemu Sinjiri Mukuba na marehemu Eliud Shihanda Murono.

JIVUNIO

Dennis anaazimia kuvikwea vidato vya taaluma na kuwa miongoni mwa walimu na waandishi maarufu wa Kiswahili. Sawa na alivyoshikwa mkono hadi akafika alipo, naye anajitahidi kuwainua chipukizi katika sanaa ya uandishi.

Mbali na kufanya tafsiri na ukalimani, Dennis huendesha masimulizi na mijadala mingi ya kitaaluma kupitia kumbi mbalimbali za Kiswahili mitandaoni na YouTube (MwalimuTv).

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo sasa inatawala wanafunzi, wanahabari na walimu wengi ambao wametangamana naye katika makongamano anuwai ya kupigia chapuo Kiswahili.

Kwa pamoja na mkewe, Bi Violet Alividza, wamejaliwa watoto wawili – Mishie Nadia Neema na Zarina Zawadi Pendo.

CAPTION 2: Baadhi ya kazi za Mwalimu Dennis Mwima

GWIJI WA WIKI: Fred Mutwiri

Na CHRIS ADUNGO

MSHUMAA hauzimiki kwa kuuwasha mwingine.

Maisha ni safari na safari ni hatua. Safari ya kitalifa kirefu huanza kwa hatua moja.

Kabla ya binadamu kupiga hatua yoyote safarini, huwa tayari ameipiga hatua hiyo akilini mwake. Kwa hivyo, ni dhahiri shahiri kuwa mtu afikirivyo ndivyo alivyo. Uko jinsi ulivyo leo kwa sababu wewe mwenyewe uliamini utakuwa hivyo tangu jana. Vyovyote vile uwavyo, jinsi utakavyokuwa kesho ni matokeo ya jinsi unavyoamini leo kuhusu hiyo kesho yako.

Jihisi kuwa mwenye thamani kwa sababu umeibeba sura ya Mungu aliyekuumba kwa mfano wake mwenyewe. Usikubali kushindwa na lolote maishani.

Katika kila ufanyacho au unachotarajia kutenda, ukitanguliza mawazo ya kushindwa, haitakuwa rahisi kufaulu.

Kama ambavyo neno litokalo kwa Mungu linavyoweza kuumba, ndivyo maneno ya kutoka vinywani mwetu pia yanavyoweza kutujenga au kutubomoa.

Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi. Kila tunachokiri ndicho hutokea. Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mawazo ya mtu na maneno ayanenayo. Ayazungumzayo mtu ndio yanayoujaza moyo wake.

Tofauti kati ya kuku na tai ni nia. Penye nia pana njia. Ni wajibu wa kila mja kuteua iwapo anataka kuwa kuku asiyepaa ama tai anayepaa upeo wa kupaa. Kufaulu kwako ni zao la juhudi. Bahati ni chudi na nidhamu ndiyo dira kamili katika maisha.

Azimia kutimiza ndoto zako kwa kuwa mafanikio hayaji kwa kulaza damu bali kwa kupinda mgongo na kujifunga kibwebwe.

Huu ndio ushauri wa Bw Fred Mutwiri – mwanafunzi wa shahada ya uzamifu na mwandishi mahiri anayefundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Lawrence Nziu Girls, Kaunti ya Makueni.

MAISHA YA AWALI

Mutwiri alizaliwa mnamo 1992 katika kitongoji cha Nkandone, Kaunti ya Meru. Ndiye mtoto wa sita katika familia ya Bi Martha Kabiro na Bw John Ngore.

Hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ilianza kujikuza ndani ya Mutwiri tangu utotoni. Alikuwa mwepesi wa kusoma habari shuleni na kanisani huku akiiga sauti za watangazaji maarufu wa redioni. Alistahiwa pakubwa na wanafunzi na waumini kwa upekee wa kipaji chake cha ulumbi.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Nkandone, Meru. Alisomea huko hadi darasa la saba kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Naathu, Meru. Nusura ndoto zake za masomo ziyeyushwe na pigo la kufariki kwa baba mzazi mnamo 2004.

Kwa imani kwamba penye mawimbi na milango ya heri i papo hapo, Mutwiri alianza kuishi kwa kumtegemea mama mzazi ambaye hakuwa na kazi yoyote ya staha na haiba.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) katika Shule ya Upili ya Igembe Boys, Meru mnamo 2009 na akajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Anakiri kuwa mapenzi yake kwa masomo ya lugha ni zao la kuhimizwa mara kwa mara na Bw Irai aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya upili. Wengine waliochangia ari yake ya kukichapukia Kiswahili ni Prof Rayya Timammy, Dkt Ongarora na marehemu Prof Ken Walibora.

UALIMU

Mutwiri alianza kufundisha mnamo 2013 akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Chuka kuanzia 2015. Alifuzu mwaka wa 2019 baada ya kuwasilisha tasnifu “Muundo wa Sentensi ya Kiigembe: Mtazamo wa Eksibaa” chini ya usimamizi wa Prof John Kobia na Dkt Allan Mugambi.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo 2017 na kumtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya St Lawrence Nziu Girls Makueni. Baada ya kukamilisha shahada ya uzamili, Mutwiri alirejea katika Chuo Kikuu cha Chuka mnamo 2020 kwa minajili ya shahada ya uzamifu (phD). Analenga kufuzu mnamo 2022.

UANDISHI

Mutwiri alikuwa na mazoea ya kuandika hadithi za kubuni pamoja na mashairi alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Utashi wake wa kuandika ulichochewa zaidi na wahadhiri wake wa shahada ya uzamili wakiwemo Prof Kobia, Dkt Erastus Miricho na Bw Bitugi Matundura.

Waliomhimiza aanze kuchapisha kazi zake ni marehemu Bernard Omwega Osano (Kaka Benosa) aliyekuwa mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi na Bw Timothy Omusikoyo Sumba – mwandishi stadi na mhariri mzoefu wa vitabu vya Kiswahili.

Kufikia sasa, Mutwiri amechapishiwa makala ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida ya kitaifa na kimataifa.

Mwalimu Fred Mutwiri. Picha/ Chris Adungo

Alishirikiana na Prof Miriam Mwita wa Chuo Kikuu cha Mashariki ya Afrika Baraton kuandika makala ‘Usawiri wa Wahusika wa Jinsia ya Kiume katika riwaya ya Chozi la Heri’ na yakafyatuliwa katika jarida Mwanga wa Lugha’.

‘Muundo wa Virai vya Sentensi ya Kiigembe’ ni makala aliyoandika kwa kushirikiana na Dkt Allan Mugambi na yakachapishwa na ‘East African Scholars Journal of Education, Humanities and Literature’.

Mbali na riwaya ‘Joka Kitandani’, Mutwiri ameandika kitabu ‘Fumbo la Fasihi’ na msururu wa vitabu vya mazoezi na marudio ‘Futari Njema ya Fasihi Simulizi’, ‘Futari Njema ya Isimujamii’, ‘Futari Njema ya Kigogo’, ‘Futari Njema ya Chozi la Heri’ na ‘Futari Njema ya Tumbo Lisiloshiba’.

Aidha, ametunga hadithi fupi ‘Sumu Tamu’, ‘Karakana ya Upatanisho’, ‘Ningali Hai’, ‘Fumbo la Fumba’, ‘Bibi wa Tajiri’, ‘Si Ndoto Tena’, ‘Joka la Baharini’ na ‘Nzige’.

‘Siri ya Insha’ ni kitabu ambacho Mutwiri aliandika kwa pamoja na Bw Steven Mativo na mwalimu Allan Babashi wa Starehe Boys Centre & School mnamo 2021.

Baadhi ya mashairi yake yamechapishwa katika diwani ‘Malenga wa Afrika’ iliyohaririwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Timothy Omusikoyo Sumba na Fatma Ali Mohammed kutoka Zanzibar.

Mutwiri anatarajia kutoa kitabu ‘Fumbo la Sarufi Mtindo wa KCSE’ mwaka huu 2021.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Mutwiri ni kuweka hai ndoto yake ya kuwa profesa wa Kiswahili na mhadhiri katika vyuo vikuu.

Anajivunia kuelekeza idadi kubwa ya chipukizi katika sanaa ya uandishi kupitia ‘YouTube’ (Mutwiri Fred).

Kwa pamoja na mkewe, Bi Ruth Kaimuri, wamejaliwa mtoto mmoja: Mellisa Gatwiri.

GWIJI WA WIKI: Dkt Deborah Nanyama Amukowa

Na CHRIS ADUNGO

KUNA mwimbaji aliyeimba kuwa: “Maisha ni foleni sisi sote tumejipanga mbele zake Mungu… Kila siku tunasongea polepole. Mwamini Mungu, ipo siku utafanikiwa”.

Hivyo, kufua dafu katika jambo lolote maishani hutegemea jinsi mtu binafsi anavyohusiana na Muumba wake. Mtumainie katika hali zote na mtangulize katika kila hatua. Waswahili husema, kunga za ngoma ya mahepe hufahamika na wanaohusika tu!

Changamoto nyingi za maisha zinaweza kukabiliwa na kila mtu kulingana na uwezo na tajriba aliyo nayo. Jitume katika hicho unachokifanya kwa sababu bahati ni chudi.

Huo ndio ushauri wa Dkt Deborah Nanyama Amukowa ambaye kwa sasa ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maseno.

MAISHA YA AWALI

Deborah alizaliwa katika familia ya Kikristo kijijni Misemwa, eneo la Webuye Mashariki, Kaunti ya Bungoma. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto sita wa marehemu Bi Susan Lumonya Nyukuri na marehemu Bw Wycliffe Wamalwa Cherwenyi waliokuwa walimu katika uzima na uhai wao. Ama kweli, mwana wa mhunzi asiposana huvukuta.

Deborah ilianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Misemwa kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Nakalira alikohamia mama yake mzazi kikazi.

Kati ya 1982–1985, aliendeleza masomo yake ya kiwango cha ‘O-Levels’ katika Shule ya Upili ya Mudavadi – Madzuu Girls. Alihitimu na kujiunga na Shule ya Upili ya Tumutumu Girls (1986–1987).

Deborah alisomea Shahada ya Sanaa (BA) katika tahasusi ya Kiswahili, Historia na Sosholojia katika Chuo Kikuu cha Egerton (Bewa la Njoro) kati ya 1988–1991.

Miongoni mwa wahadhiri waliomtandikia zulia la Kiswahili na kumkuza vilivyo kiakademia ni Profesa Chacha Nyaigotti-Chacha, marehemu Dkt Karisa Beja na marehemu Jay Kitsao.

Deborah alisomea kozi ya stashahada; yaani Diploma ya kuhitimu katika elimu (PGDE) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya Disemba 1996 na Agosti 1997.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Maseno kusomea shahada ya uzamili mnamo 2003 na akafuzu 2005 baada ya kuwasilisha tasnifu “Taswira ya Mtoto wa Kike katika Riwaya ya Kiswahili” chini ya uelekezi wa Profesa Kenneth Inyani Simala na Profesa Wangari Mwai.

Alijisajili kwa minajili ya shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Maseno mnamo 2009 na akafuzu 2013 baada ya kuwasilisha tasnifu “Changamoto za Ujana katika Riwaya za John Habwe” chini ya usimamizi na uelekezi wa Profesa Wangari Mwai na Profesa Florence Indede.

UALIMU

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Deborah kufundisha katika Shule ya Upili ya Chianda Boys, Bondo mnamo 1992. Alihudumu huko hadi mwaka wa 2002 alipopata likizo ya kusomea uzamili 2003–2005.

Alifundisha baadaye katika Shule ya Upili ya Lirembe Girls Ikolomani, Kakamega kati ya Januari na Desemba 2005 kabla ya kuhamia katika Shule ya Upili ya Shieywe mjini Kakamega. Alihudumu huko kati ya Januari na Novemba 2006 kabla ya kuajiriwa na Chuo Kikuu cha Maseno.

UANDISHI

Tangu utotoni, Deborah alikuwa na hamu ya kuchangia makuzi ya Kiswahili kupitia sanaa ya uandishi. Hata hivyo, tatizo kubwa lilikuwa kutojua pa kuanzia, nani wa kumshika mkono na wapi pa kuelekeza kazi zake kwa ajili ya kuchapishwa.

Kati ya watu waliomchochea kujitosa katika ulingo wa uandishi ni walimu wake wa awali waliotia azma ya kupalilia kipaji chake cha utunzi wa kazi bunilizi baada ya kutambua upekee na ukubwa wa uwezo wake katika Kiswahili.

Mwingine aliyemwamshia ari ya kuandika bila kukoma ni Bw Timothy Omusikoyo Sumba anayezidi kumhimiza kuogelea katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, Dkt Deborah amechapisha makala kadhaa katika majarida ya kitaaluma ya kitaifa na kimataifa. Aidha, ametunga pia hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika antholojia mbalimbali.

‘Mwanzo Mpya’ ni hadithi yake nyingine ambayo iko katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika shirika moja la uchapishaji wa vitabu nchini Kenya.

Dkt Deborah amechangia pia utunzi wa kitabu ‘Uandishi na Uhariri: Mbinu na Nadharia’ kwa kushirikiana na wataalamu wengine – Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo, Dkt Jackline Njeri Murimi, Dkt Hamisi Babusa, Dkt David Turuthi, Dkt Wanjohi Githinji, Dkt Evans Makhulo, Bw Henry Indindi, Prof Clara Momanyi na Bw Sumba aliyekuwa msimamizi wa mradi huo.

UANACHAMA

Deborah ni mwanachama wa vyama mbalimbali vya kitaaluma, vikiwemo Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU). Yeye kwa sasa ndiye Naibu wa Katibu Mkuu wa CHAKITA.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Dkt Deborah ni kuweka hai ndoto ya kuwa profesa na mwandishi mashuhuri wa Kiswahili.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Baadhi yao ni Dkt Fridah Miruka (Chuo Kikuu cha Masinde Muliro), Alice Atemo (Shule ya Upili ya Shieywe), Samuel Sinzore, Edwin Atukunda na Martin Mulei. Miongoni mwa wanafunzi wake wa shahada ya uzamili kwa sasa ni Bi Aidah Mutenyo ambaye ni mtaalamu wa Kiswahili nchini Uganda.

Dkt Deborah anajivunia kuwa mwalimu wa lugha. Anaamini kwamba lugha hutawala maisha ya binadamu na ndicho chombo aula cha kumfinyanga, kuelezea fikra zake, kuendeleza mahusiano na kuhifadhi pamoja na kupitisha utamaduni wa jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Kwa pamoja na mumewe Michael Amukowa Ochiel, wamejaliwa watoto wanne: Marvin Justo Ochiel, Murray Oburah, Alverah Lumonya na Shiphrah Nyangasi. Pia wanawalea Melody Nanjala na Elkanah Nyongesa.

GWIJI WA WIKI: Sharon Nafula Wekesa

Na CHRIS ADUNGO

MAFANIKIO ya mtu hayapimwi kwa utajiri wa mali na wingi wa fedha, bali kwa ukubwa wa alama zenye kumbukumbu nzuri anazoziacha katika nyoyo na nafsi za wengine.

Tupo jinsi tulivyo kwa sababu ubora tulio nao umechangiwa na watu wengine. Tazama nyuma uone mchango wa watu hao kisha uwapongeze.

Hakuna aliye na uwezo wa kuzima ndoto zako za maisha isipokuwa wewe mwenyewe. Changamkia fursa adimu utakazozipata za kukupigisha hatua kitaaluma. Jiamini na ufanye hivyo kwa kani na idili.

Huu ndio ushauri wa Bi Sharon Nafula Wekesa – mwandishi chipukizi na mlezi wa vipaji ambaye sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Nakuru Whizzkids.

MAISHA YA AWALI: Sharon alizaliwa Novemba 1994 katika kijiji cha Wehoya, viungani mwa mji wa Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia.

Ndiye mtoto wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bi Margaret – mke wa kwanza wa Bw Peter Wekesa ambaye mkewe wa pili, Bi Veronica, amejaliwa watoto watano.

Sharon alilelewa eneo la Moi Farm Kitale katika utamaduni uliosisitiza ulazima wa mtoto kuadhibiwa na kushauriwa na mzazi yeyote kwa kuwa jukumu la ulezi lilikuwa la jamii nzima. Wavyele wake pia walimrudi kila alipokosea. Hilo lilimfanya kukua akiwa mtoto muadilifu na mwenye bidii.

Hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ni ndoto iliyoanza kujikuza ndani ya Sharon tangu utotoni. Mara si haba, alijipata akiiga sauti za wanahabari maarufu na akapendwa na watu kutokana na ‘sauti yake ya utangazaji’.

Nyanya yake, Leonida Nafula, alikuwa mwepesi wa kumpagaza majina ya watangazaji mashuhuri bila kufahamu kwamba alikuwa akipanda mbegu ya uanahabari iliyoota na kuwa mche maridadi ambao sasa unasubiri kuchanua ndani ya nafsi ya mjukuu wake huyu.

Sharon alisomea katika Shule ya Msingi ya Simatwet hadi darasa la saba kabla ya kuhamia katika Shule ya Msingi ya Mosoriot.

Alikuwa na mazoea ya kuwahi nyumbani kila siku saa saba mchana. Hakufanya hivyo kwa ajili ya chakula cha mchana tu. Maazimio yake makuu yalikuwa kupata fursa adhimu za kusikiliza taarifa za habari zikisomwa na watangazaji aliowastahi na kushabikia.

Japo alifaulu vyema katika mtihani wa KCPE na kuitwa kujiunga na mojawapo ya sekondari za haiba, uchechefu wa karo ulimfanya arudishwe Wehoya kusomea katika shule ya kutwa ya Friends Sirende.

Akiwa huko, alilelewa na ami yake, Andrew Wabwile pamoja na mkewe Everlyne. Sharon aliwaaga nduguze na kuanza ukurasa mpya wa maisha pamoja na binamu zake Florian, Fortune, Fenil na Fidel.

Licha ya changamoto za kila sampuli alizokumbana nazo, alizidi kuuma uzi masomoni. Alibahatika kujiunga na Chama cha Uanahabari shuleni na akapalilia kipaji chake cha utangazaji na utunzi wa kazi bunilizi.

Alifanya mtihani wa KCSE katika mwaka wa 2014 na akajiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Nakuru mnamo Februari 2016.

Akiwa mgeni wa wiki mbili pekee chuoni humo, alipata fursa ya kushiriki kipindi cha makuzi ya Kiswahili katika runinga ya KTN News. Huo ulikuwa mwanzo wake wa kuwa mwendeshaji wa mijadala ya kitaaluma kupitia vipindi vya lugha redioni, runingani na mitandaoni.

MCHANGO KITAALUMA: Baada ya kuhitimu elimu ya chuoni, Sharon alikuwa mtangazaji na ripota wa kujitolea katika stesheni ya Mitume Radio mjini Kitale. Alihudumu huko kwa kipindi cha miezi sita. Akiwa mwanafunzi, alikuwa na mazoea ya kukitembelea kituo hicho mara kwa mara nyakati za likizo na akajifunza mengi katika tasnia ya uanahabari.

Ilikuwa hadi 2018 ambapo alirejea Nakuru kusaka ajira ya ualimu. Maamuzi ya kujitosa katika ulingo wa kiakademia na hata kusomea ualimu ni zao la kuhimizwa na Bi Josephine Onyango aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya upili.

Zaidi ya kumpa kazi ya kuchambua vitabu vya fasihi darasani, Bi Onyango alimteua Sharon mara kwa mara kusoma vifungu vya somo la Ufahamu na kumpa nafasi maridhawa za kuhutubu gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Wazazi nao walimnunulia vitabu vingi vya hadithi. Alipata majukwaa maridhawa ya kunoa kipaji chake cha ulumbi, kuinua kiwango cha umilisi wa lugha na kukichapukia Kiswahili kwa utashi.

UANDISHI: Mapenzi ya kusoma magazeti na vitabu vya hadithi yalimwamshia Sharon hamu ya kuandika kazi bunilizi kila alipokuwa hana shughuli maalumu za kufanya.

Ingawa angezichana tena kurasa alizoandika kwa hofu kwamba alichokisarifu hakikuwa chochote wala lolote, walimu waliotambua utajiri wa kipaji chake walimhimiza apige mbizi katika bahari pana ya utunzi.

Nyingi za insha alizozitunga zilimzolea tuzo za kutamanisha kutoka kwa walimu wake. Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali na hata kuchapishwa katika gazeti hili. Uandishi wa Sharon umeathiriwa pakubwa na kazi za marehemu Profesa Ken Walibora.

Kufikia sasa, amechapishiwa hadithi fupi kadhaa katika antholojia mbalimbali kama vile ‘Maisha Karakana na Hadithi Nyingine’, ‘Harufu ya Jehanamu na Hadithi Nyingine’ na Mateka na Hadithi Nyingine’. Amechangia pia mashairi katika diwani za ‘Wosia Na Mashairi Mengine’ na ‘Malenga wa Kenya’ na ‘Tasnia ya Ushairi’.

JIVUNIO: Ndoto ya Sharon ni kufikia upeo wa taaluma yake, kuwa mwandishi tajika na mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Anatambua upekee wa mchango wa Bw Timothy Omusikoyo Sumba anayezidi kumshika mkono kadri anavyojitahidi kupanda vidato vya mafanikio katika safari ya uandishi.

“Hajawahi kuchoka wala haelekei kufanya hivyo. Matarajio yake ni makubwa na matamanio yake ni kuniona nikiendelea kupanua wigo na kuwanda katika ulingo wa sanaa.”

Anamstahi sana ami yake Andrew na mkewe Everlyne ambao walimtwaa udogoni, kumchukua kama mwana wao na kumgharimia masomo yake ya sekondari.

“Mbali na kunishajiisha maishani, walinilea kwa misingi ya kumcha Mungu na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo,” anasema.

GWIJI WA WIKI: Neema Salome Sulubu

Na CHRIS ADUNGO

UIGIZAJI ni kazi kama kazi yoyote nyingine.

Kufaulu katika ulingo huo wa sanaa kunahitaji jitihada, stahamala na nidhamu ya hali ya juu.

Usijitose katika uigizaji kwa lengo la kutafuta fedha na umaarufu. Hutadumu ulingoni kwa muda mrefu!

Hatua ya kwanza katika safari ya mafanikio ni kufahamu unachokitaka, kujielewa wewe ni nani, kutambua unakokwenda na kupiga hatua kusonga mbele kuelekea huko unakolenga kufika.

Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga. Kipende unachokifanya na namna unavyokifanya. Yafanye mambo yaliyomo ndani ya uwezo wako. Yafanye kwa utaratibu unaofaa na kwa wakati unaostahili. Fanya hivyo ili ufike mbali!

Kuwa mwepesi wa kusikiliza na mpole zaidi katika kunena. Hakuna ajifunzalo mtu asiyeuliza. Uliza wajuao ili nawe ujue!

Huu ndio ushauri wa Bi Neema Salome Sulubu – mwanahabari mbobevu na mwigizaji stadi wa vipindi vya runingani.

MAISHA YA AWALI

Neema alizaliwa katika mtaa wa Kisumu Ndogo, eneo la Malindi, Kaunti ya Kilifi. Amekulia katika familia ya Waadventista wa Sabato (SDA).

Ndiye wa saba kuzaliwa katika familia ya watoto wanane wa Bi Janet Dama na marehemu Bw Sulubu Mwagandi Ngala. Nduguze Neema ni Mary Mapenzi, John Kiponda, Lilian Sikukuu, Mercy Rehema, Ashley Asha, Esther Kaneno na marehemu Samson Safari.

Safari yake ya elimu ilianzia katika chekechea ya Al-Fauz, Malindi. Alijiunga baadaye na Shule ya Msingi ya HGM Malindi kisha Shule ya Upili ya Ngala Memorial, eneo la Watamu, Kilifi (2006-2009).

Baada ya kusomea uanahabari katika Chuo cha Mombasa Aviation kati ya 2011 na 2013, Neema alijiunga na chuo cha Kenya Institute of Management (Bewa la Mombasa) mnamo 2017 kusomea masuala ya usimamizi na mahusiano ya umma. Alihitimu katika mwaka wa 2019.

UIGIZAJI

Uigizaji ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Neema akiwa na umri mdogo. Marehemu mwalimu Maulidi alikuwa mwepesi wa kumjumuisha katika makundi ya kutumbuiza wageni kwa nyimbo na mashairi nyakati za hafla mbalimbali shuleni Al-Fauz.

Baadaye katika shule ya msingi, walimu walitia azma ya kupalilia kipaji walichokitambua ndani ya mwanafunzi wao huyu. Bi Munyao alimpa Neema majukwaa mengi ya kuwa ngoi (kiongozi stadi wa nyimbo) katika mashindano ya viwango tofauti.

Alitamba kwa wepesi kutokana na umilisi wake wa Kiswahili.

Uwezo wa Neema katika ulumbi uliwahi kumfanya maarufu sana miongoni mwa wanafunzi wenzake katika shule ya msingi baada ya kuongoza wimbo ‘Katililo’ kwa ukakamavu wa kuajabiwa.

Wengine waliomwamshia ari ya kuthamini na kuchapukia masuala ya uigizaji ni Bw Joseph Akwiri, Bw Kadenge, Bi Maitha na Bw Muye Marembo ambao walitangamana naye kwa karibu sana katika shule ya upili.

Kipaji kinachojivuniwa na Neema katika ulingo wa uigizaji kilipaliliwa zaidi na kutiwa nakshi na Bw Elphas Shitandi na Bw Mbashir Shambi ambao pia walimpokeza malezi bora ya kiakademia katika Chuo cha Mombasa Aviation.

VIPINDI NA TUZO

Neema aliwahi kuongoza makundi mbalimbali ya wanafunzi kutoka Shule ya Msingi ya Malindi, Shule ya Upili ya Ngala Memorial na Chuo cha Mombasa Aviation kushiriki tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Alijizolea tuzo ya Mwigizaji Bora katika michezo ya jukwaani (2008, 2009, 2013) na akatwaa taji la haiba kubwa la ‘Adjudicators’ Award’ mnamo 2007 kwenye tamasha za kitaifa zilizoandaliwa Tumutumu Girls, Kaunti ya Nyeri.

Mnamo 2012, alijiunga na kundi la waigizaji katika Shirika Lisilo la Kiserikali la S.A.F.E Kenya Pwani. Aliwaongoza wenzake kuhamasisha umma kuhusu masuala ya afya, ugaidi pamoja na umuhimu wa kudumisha amani na kuhifadhi mazingira.

Mchezo wa kwanza wa runingani ambao Neema alishiriki ni ‘Utandu’. Aliigiza mhusika Nana katika mchezo huo uliotolewa na Ashiner Pictures mnamo 2013.

Baada ya milango ya heri kujifungua, alipata fursa ya kuigiza mhusika Tumu katika ‘Moyo’ (2014-2016). Huo ndio mchezo uliomkweza kwenye ngazi ya juu zaidi katika ulingo wa uigizaji.

Mnamo Disemba 2018, Neema alitawazwa Mwigizaji Bora wa Kenya Coast Music Awards.

Aliwahi pia kuigiza mhusika Binti katika mchezo ‘Aziza’ (2016-2019) kabla ya kuanza kuigiza Neema katika mchezo ‘Zora’ ambao hufyatuliwa na Citizen TV kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa moja unusu hadi saa mbili usiku.

UANAHABARI

Neema aliajiriwa na redio ya Baraka 95.5 FM mnamo Julai 2013 kuwa prodyusa wa kipindi ‘Bumburuka’ kilichokuwa kikiperushwa hewani kila wikendi.

Umahiri wake wa kuzamia masuala ya kiuchumi ulimfanya pia kuaminiwa fursa ya kuwa mwendeshaji wa kipindi ‘Kurunzi ya Biashara’.

Upekee wake wa kuoanisha talanta na kozi alizozisomea ulimpigisha hatua kubwa katika juhudi za kuwekea taaluma ya uanahabari uhai.

Hadi alipoondoka Baraka FM mnamo Disemba 2018, Neema alikuwa mkuu wa Kitengo cha Matangazo na majukumu yake yalikuwa kuandaa ripoti muhimu na kuratibu matangazo ya biashara.

JIVUNO

Anapojitahidi kujiimarisha zaidi katika sanaa, Neema yuko mstari wa mbele kuwapokeza vijana wenzake kunga za kujinoa vilivyo na kujikuza katika ulingo wa uigizaji.

Hutumia ujuzi wa kuigiza kuwaelekeza waumini wenzake katika Kanisa la Malindi Central SDA kuhusu masuala ya maadili na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali maishani.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo sasa inatawala chipukizi wengi ambao wametangamana naye katika majukwaa mbalimbali ya uigizaji.

Neema anawastahi sana wamiliki wa kampuni ya Jiffy Pictures – Lulu Khadija Hassan na Rashid Abdalla – kwa kumpa fursa ya kudhihirisha utajiri wa kipaji chake cha uigizaji kupitia michezo ‘Moyo’, ‘Aziza’ na ‘Zora’.

GWIJI WA WIKI: Robert ‘Ramtez’ Elijah

Na CHRIS ADUNGO

PANIA kuwa mfano wa kuigwa na wenzako ili hatimaye uache jina zuri duniani.

Lenga kuwa sehemu ya mabingwa watakaotajwa kwa wema waliotenda na ubora wa kazi walizofanya kabla ya kufunga safari isiyo na marejeo.

Jifunze kutokata tamaa, dumisha nidhamu, shindana na wakati, kuwa mtu mwenye msimamo na ujiamini katika kila hali. Jitume katika kazi yako, kuwa na moyo wa kushirikiana na watu wengine na umtumainie Mungu siku zote.

Huu ni ushairi wa Robert ‘Ramtez’ Elijah – mwanahabari chipukizi, mwigizaji, mjasiriamali na mfawidhi wa sherehe ambaye ni mpenzi kindakindaki wa Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Ramtez alizaliwa katika eneo la Mbitini, Kaunti ya Kitui. Ndiye mwana wa pili katika familia ya watoto watatu wa Bi Ruth Robert na marehemu Bw Robert Musee. Nduguze ni Geoffrey na Caleb.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya New Hope Mbitini. Baadaye alijiunga na Shule ya Msingi ya St Stephen’s Kaveta, Kitui alikosomea kati ya 2009 na 2013.

Ramtez alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya St Thomas Aquinas Kalawa Boys, Kitui (2014-2017).

Kwa sasa yeye ni mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika taaluma ya Habari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Egerton (Bewa la Nakuru Mjini). Anatazamia kuhitimu mwaka huu.

Aliyemwamshia ari ya kuchapukia Kiswahili ni mwalimu Nyamai aliyemfundisha katika shule ya upili. “Alinipokeza malezi bora ya kiakademia na akapalilia vizuri mche wa Kiswahili ambao kwa sasa ni mti maridadi,” anasema.

Vipaji vya uigizaji, kucheza vyombo vya muziki na utunzi wa mashairi vilianza kujikuza na kudhihirika ndani ya Ramtez katika shule ya msingi.

Akiwa mwanafunzi wa Darasa la Sita, alimtungia aliyekuwa Waziri wa Maji, Mhe Bi Charity Ngilu, shairi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na akatuzwa Sh5,000. Bi Ngilu kwa sasa ni Gavana wa Kaunti ya Kitui.

Ramtez aliwahi kuongoza makundi mbalimbali ya wanafunzi kutoka Kalawa Boys kuwakilisha shule hiyo katika tamasha za kitaifa za muziki na drama na wakajizolea tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha.

Anatambua pia upekee wa mchango wa Bw Matata anayezidi kumshika mkono kadri anavyojitahidi kupanda vidato vya mafanikio katika safari ya maisha. Bw Matata kwa sasa ndiye msimamizi mkuu wa masuala ya utamaduni na burudani katika Chuo Kikuu cha Egerton.

“Hajawahi kuchoka wala haelekei kufanya hivyo. Matarajio yake ni makubwa na matamanio yake ni kuniona nikiendelea kupanua wigo wa burudani na kuwanda katika ulingo wa sanaa na uanahabari.”

“Mwingine anayenishajiisha maishani ni mama mzazi ambaye alinilea kwa misingi ya kumcha Mungu na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo.”

Ramtez anahisi kwamba fahari zaidi hii leo ingalikuwa kwa baba mzazi kumsikiliza redioni akitema maneno anayoyaita kwa Kiswahili – ajivunie tija, aone fahari na kupata kitulizo kamili cha nafsi kwa kumsherehekea mwanawe.

MCHANGO KITAALUMA

Hata kabla ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu, Ramtez tayari ameanza kujihusisha na taaluma yake. Tangu Oktoba 2020, amekuwa mwanahabari wa Egerton Radio 101.7 FM.

Mbali na kutangaza taarifa, yeye hueendesha kipindi ‘Link-Up Sato’ ambacho hupeperushwa hewani kila Jumamosi. Aliwahi kuhudumu katika idhaa ya Hero Radio 99.0 FM kati ya Disemba 2019 na Machi 2020 akishiriki uendeshaji wa kipindi ‘My Generation My Assignment’.

Kwa kutumia utajiri wa kipaji chake cha ulumbi, Ramtez amepiga hatua kubwa katika juhudi za kuwekea taaluma ya uanahabari uhai. Anapania siku zote kuoanisha talanta na taaluma anayoisomea.

Upekee huo umemvunia fursa nyingi za kuwa mfawidhi wa sherehe pamoja na kutia sauti matangazo ya biashara kutoka kampuni au mashirika mbalimbali.

Ramtez amefanya na anazidi kufanya mambo makuu katika ulingo wa Kiswahili. Zaidi ya kushiriki michezo ya kuigiza, yeye hutunga mashairi kwa ajili mashindano ya viwango mbalimbali katika tamasha za muziki na drama.

CHANJA KIJANJA

Zaidi ya kuwa mfawidhi wa shehere kwa malipo au kwa kujitolea, Ramtez pia huendesha masimulizi kuhusu visa vya wasanii – machale na wanamuziki kutoka Afrika Mashariki – kwenye YouTube (Chanja Kijanja).

Jukwaa hili huwapa mashabiki fursa maridhawa ya kuwafahamu wasanii wao kwa kina – kitaaluma na katika maisha ya kawaida.

Anapojitahidi kuiwekea dira taaluma yake, Ramtez pia amejifunga kibwebwe kuhakikisha kuwa anatamba katika ulingo wa burudani kwa lengo la kuridhisha nafsi na kuwapa mashabiki wake ‘kitu’ cha kujivunia.

Anaishi kwa imani kwamba mvuto na mguso kwenye mrindimo wa sauti yake utakuja kuwa kitambulisho chake katika majukwaa ya burudani, uanahabari na matangazo ya biashara.

Ramtez ni mwanablogu anayeshiriki mijadala mingi ya kitaaluma kupitia vipindi vya redio, runinga na kumbi za Kiswahili mitandaoni. Amezamia pia uuzaji wa sharubati; kazi ambayo humpa tonge la kila siku.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kufikia viwango vya Omary Tambwe Lil Ommy (Wasafi), Mzazi Willy M. Tuva (Citizen) na Chris Da Bass (Milele FM).

GWIJI WA WIKI: Dkt Naomi Musembi

Na CHRIS ADUNGO

HATUWEZI kupiga hatua yoyote ya kusonga mbele bila kuvumiliana.

Jifunze kutokana na yaliyopita ndipo uweze kujenga ya sasa na kukabili yajayo.

Salia imara katika safari ya kufikia malengo yako. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta. Ruhusu mawazo yako yatawaliwe na fikira za ushindi. Mtangulize Mungu, vumilia na ujitume.

Pania kutenda mema, kipende kwa dhati hicho unachokifanya, jiwekee malengo ya mara kwa mara na ujiepushe na watu wasio na maono.

Huu ndio ushauri wa Dkt Naomi Nzilani Musembi – msomi na mwandishi shupavu wa fasihi ambaye kwa sasa ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), Kaunti ya Siaya.

MAISHA YA AWALI

Naomi alizaliwa kijijini Malikini, Kaunti ya Machakos katika familia ya Bw Henry Musembi na Bi Phelis Wanza.

Alianza masomo katika Shule ya Msingi ya Malikini kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Moi High Mbiruri, Embu. Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne na akajiunga na Chuo Kikuu cha Moi kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Anakiri kwamba mapenzi yake kwa lugha hii ni zao la kuhimizwa na Bw Matano aliyemfundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mbiruri. Wengine waliompokeza malezi bora ya kiakademia na kumchochea zaidi kukichapukia Kiswahili ni Prof Clara Momanyi, Prof Kitula King’ei na marehemu Prof Ken Walibora.

“Ken alinichochea pakubwa hasa baada ya kuisoma riwaya yake ya kwanza, ‘Siku Njema’”.

UALIMU

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri Naomi mnamo 1996 na ikamtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya Thome Andu Boys, Kaunti ya Makueni.

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuhamia Wachoro Boys (1999-2000, Embu), Gitaraka Girls (2000-2001, Embu) na Kangaru Girls (2001-2005, Embu).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Dkt Naomi msukumo wa kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Alifuzu mnamo 2008 baada ya kuwasilisha tasnifu “Matumizi ya Taswira na Ukinzano kama Kichocheo cha Zinduko katika Riwaya za G.K. Mkangi” chini ya usimamizi wa Dkt Richard Wafula na Dkt Peter Mugambi.

Alifundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St John’s Kilimambogo, Kaunti ya Kiambu kati ya 2009 na 2010 kabla ya kuajiriwa na Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) mnamo 2011. Alifundisha huko kwa miaka sita kabla ya kuhamia JOOUST mnamo 2017.

Dkt Naomi alihitimu na shahada ya uzamifu (phD) mnamo 2016 baada ya kuwasilisha tasnifu “Mabadiliko ya Maudhui katika Nyimbo Jadiiya za Wakamba” chini ya uelekezi wa Prof Tom Olali na Dkt Pamela Ngugi.

UANDISHI

Sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani yake mnamo 2009. Kufikia sasa, amechapishiwa makala ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa kama vile ‘Mwanga wa Lugha’, ‘Mediterranean Journal of Social Sciences’ n.k

Ametunga pia hadithi kadhaa za watoto zikiwemo ‘Dhiki Yangu’, ‘Malimwengu’, ‘Mkono wa Sheria’, ‘Paka Mtundu’ na ‘Nipe Sababu’. Oxford Publishers ilimtolea kitabu ‘Dhibiti PTE Kiswahili’ mnamo 2010.

Dkt Naomi ameandika miswada mingi ya fasihi ya watoto na hadithi fupi ambayo kwa sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu nchini Kenya.

UANACHAMA

Dkt Naomi ni mwanachama kindakindaki wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). Aliwahi kuwa Afisa Mwenezi wa CHAKITA kati ya 2017 na 2019.

Vyama hivi vimempa majukwaa mwafaka ya kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti, ufundishaji wa Kiswahili.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Dkt Naomi ni kuweka hai ndoto ya kuwa profesa na mwandishi mashuhuri wa fasihi ya watoto.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu. Dkt Naomi kwa sasa ni mwanachama wa Bodi ya Usimamizi katika Shule ya Upili Karaba Boys, Embu.

Kwa pamoja na mumewe Bw Alex Muathe, wamejaliwa watoto wawili – Carol na Steve.

GWIJI WA WIKI: Mhadhiri, mkalimani na mtafsiri anavyochangia kwa makuzi ya Kiswahili

Na WINNIE A ONYANDO

Lugha sio tu chombo cha mawasiliano bali ni malighafi na rasilimali ya jamii ambayo inapaswa kutumiwa kujikuza, kuhifadhi tamaduni zetu kama jamii na kujenga uzalendo wetu hasa tunaporejelea lugha ya Kiswahili.

Kila lugha ina hadhi, hakuna lugha bora kuliko nyingine. Lugha ya Kiswahili inalipa hasa kwa wale wanaoienzi na kuichukua kama lugha yenye hadhi na haiba ya kipeke.

Kiswahili kama lugha kinafaa kutumiwa katika taasisi zote nchini Kenya kama njia mojawapo ya kuwasiliana hasa katika utoaji wa huduma katika ofisi zote za kiserikali.

Lugha ya Kiswahili inafaa kutumiwa nchini Kenya katika vikao vyote. Kila mwajiriwa katika ofisi, kampuni ama taasisi yoyote nchini Kenya anapaswa kutumia lugha ya hiyo kwa uweledi hasa katika utoaji wa huduma kwa umma.

Hayo ndiyo kauli na maoni ya Mhadhiri, Mtafsiri na Mkalimani wa lugha ya Kiingereza, Kiswahili na Kikuyu Bw Vincent Njeru Magugu.

Bw Magugu, 35 ni mpenda lugha aliyebobea katika taaluma ya Tafsiri. Yeye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi (Bewa Kuu) mjini Eldoret anakofunza kozi la Kiswahili hasa Tafsiri.

MAISHA YAKE YA AWALI

Bw Magugu alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Marmanet, eneo la Nyahururu kaunti ya Laikipia, kitindamimba katika familia ya watoto watano.

Anaeleza kuwa japo wengi huchukulia kuwa vitindamimba hudekezwa na wazaziwe, yeye hakudekezwa na wazazi. Alitarajiwa kufanya vizuri shuleni jinsi wenzake walivyohitimu, wazazi wake pia walimtia adabu na kumhimiza atie bidi masomoni.

Wazazi wake marehemu Bw James Magugu na Bi Rose Wamucii ndio kielelezo wa kwanza maishani. Wamekuwa wakimhimiza aendelee kutia bidii masomoni. Mhadhiri huyo anaeleza kuwa ana mke na mtoto mmoja mvulana.

MASOMO

Mhadhiri huyo amaeleza kuwa alianza masomo yake katika shule ya Msingi ya kiserikali ya Kundarilla eneo la Nyahururu, alikosoma hadi darasa la saba na baadaye kuhamishwa katika shule ya Msingi ya kibinafsi ya Amazing Grace eneo la Nyahururu alikomaliza masomo yake ya shule ya Msingi.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya Shule ya Msingi, alijiunga na shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kanjuri, Nyeri.

Anaeleza kuwa japo alikuwa mwanafunzi wa wastani masomoni, alipata mwamko na msisimko mpya masomoni hasa baada ya kukutana na mwalimu wake wa Kiswahili Bi Lucy Mugo. Anaeleza kuwa Bi Mugo hakuchoka kumfuatilia na kumpa mawaidha kila uchao jinsi ya kujiimarisha masomoni na kuwa mwanafunzi bora.

Anaeleza kuwa kupitia mwalimu wake huyo, aliweza kupata alama ya A katika somo la Kiswahili na hata kupasi mtihani wake wa KCSE kijumla.

Magugu anasema kuwa ndoto yake ya kuwa Mwanasheria yalikatizwa baada ya rafiki yake waliyesoma naye pamoja katika shule ya Sekondari Harrison Ngure kumshawishi achague kozi ya Ba Kiswahili.

Hakuchelewa ila akachagua kozi hiyo katika Chuo Kikuu cha Moi (Bewa Kuu) Eldoret. Alijiunga na Chuo hicho mwaka wa 2007.

Chuoni Moi, aliweza kukutana na Prof Nathan Ogechi Mkuu wa Idara ya Kiswahili na Lugha Nyingine za Kiafrika ambaye alimpa ujasiri na kujenga imani yake kuwa BA Kiswahili kinalipa.

Kukutana kwake na hayati Prof Naomi Shitemi ilikuwa nyota la heri kwake. Prof Shitemi alimpa mawaidha kila mara kuhusiana na taaluma ya Tafsiri.

Anaeleza kuwa kwa wakati huo, walikuwa wanafunzi 12 waliojisajili kufanya kozi ya BA Kiswahili. Haya hayakumtia shaka kwa kuwa aliunyakua nafasi huo adimu ili kujiboresha katika lugha ya Kiswahili.

Wakati huo, yeye pamoja na rafiki yake Osinya Okumu walihimizana kila wakati na kudurusu somo la Kiswahili huku wakifanya mazoezi kila mara katika lugha ya Kiswahili.

Kuungana na Chama cha CHAKIMO akiwa katika mwaka wake wa Pili kilimfanya abobee zaidi katika lugha hiyo.

Wakati huo Bw Chris Adungo ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha CHAKIMO Moi naye akachaguliwa Naibu mwenyekiti wa chama hicho mwaka wa 2008.

Chris alipomaliza masomo yake, Bw Magugu alichaguliwa mwenyekiti wa chama hicho. Amekuwa mwenyekiti wa chama hicho akiwa mwaka wa pili hadi mwaka wa tatu.

Baadaye alikuwa mhariri wa chama hicho ampabo walijiendeleza sana kama chama.

Baada ya kuhitimu Shahada ya Digrii, aliendelea na masomo yake ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Moi mwaka wa 2011 ambapo alikuwa mwanafunzi mmoja anayeandaa tasnifu ya Tafsiri. Alisaidiwa na Prof Shitemi na hatimaye kufuzu.

MAENDELEO TANGU AFUZU SHADADA YA UZAMILI

Baada ya kumaliza masomo yake ya Uzamili, alijiunga na Elgon View College ambapo aliajiriwa kama mwalimu. Alifunza somo la Kiswahili, Isimu na Tafsiri kwa muda mchache.

Baadaye, mwaka wa 2013, Chuo cha Moi kilitangaza nafasi ya ajira. Alipeleka barua zake za kuomba kazi na hatimaye akawa mhadhiri Chuoni Moi kuanzia mwaka wa 2014, Januari hadi sasa.

Aliweza kutafsiri kazi nyingi ikiwemo Mradi wa Chuo Kikuu cha Moi ‘Child Health Impact Studies,’ kazi ya Kitivo cha Afya kilichosimamiwa na Prof Omar Egesa.

Kazi nyingine alizotafsiri ni Mradi wa Bunge ya EACC alipotafsiri Kanuni za Kudumu za bunge. Ameweza pia kutafsiri kazi ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Moi Dkt Odiwuori ya ‘Asali Chungu’.

Ameweza pia kutafsiri kazi za wateja. Yeye hupata wateja kutoka nchi mbalimbali. Anasema kuwa kujenga ukuruba na wateja wako na hata kuwafanyia kazi nzuri kwa wakati ufaao ndiyo imekuwa ikimpa wateja wengi.

Mhadhiri huyo ameweza kuwasilisha namna ambavyo DJ Afro anatumia sauti mpachiko katika kuwasilisha kazi zake za video.

Magugu ameweza kutoa wanafunzi waliobobea sana katika tafsiri. Wengi wa wanafunzi wake wanafanya katika mashirika tajika nchini.

Sasa hivi, mhadhiri huyo ameanzisha program ya kutoa mafunzo ya tafsiri ambapo anawaelekeza na kuwashauri watafsiri wachanga Afrika.

Program hiyo ya Mentoring African Traslators umeanzishwa ili kuwakuza watafsiri na kuwapanua akili kiakademia katika taaluma ya tafsiri.

MCHANGO WAKE KATIKA CHAMA CHA CHAKIMO

Bwa Magugu anasema kuwa tangu ajiunge na chama cha Chakimo mwaka wa 2007, waliweza kufanikisha mengi.

Yeye pamoja na wenzake, kama vile Paul Ng’ang’a ambaye alikuwa mhariri wa chama hicho mwaka huo waliweza kuandaa michezo ya kuigiza ya vitabu vya fasihi ya Kifo Kisimani na Utengano. Mwaka wa 2009, alichaguliwa Katibu wa chama cha CHAWAKAMA Kenya.

Mwaka wa 2009 pia alichaguliwa kama Mhazini wa Afrika Mashariki. Waliweza pia kushirikiana na vyama vingene vya Kiswahili kutoka Vyuo vingine na kuandaa kongamano katika Chuo Kikuu cha Nairobi na Uganda.

Wakati wa masomo yake ya Uzamifu, alichaguliwa Kaimu Mlezi wa chama hicho. Hadi sasa Magugu ndiye mwenyekiti wa Taasisi ya Watafsiri na Wakalimani ya muungano wa EATIA.

CHANGAMOTO

Changamoto yaliyomkumba mhadhiri huyo hasa wakati wa masomo yake Chuoni ni ukosefu wa marejeleo ya kutosha. Baadhi ya vitabu vya marejeleo vimeandikwa katika lugha ya Kiingereza. Wakati wa masomo ya Uzamili na Uzamifu, alilazimishwa kutafsiri baadhi ya kazi hizo katika lugha ya Kiswahili.

Anaeleza pia kuwa, katika taaluma yake ya Tafsiri kutoka katika lugha ya Kiswahili, Kiingereza na Kikuyu, vitabu vya marejeleo ni chache sana hasa katika lugha ya Kikuyu. Analazimishwa kutafuta maneno mbadala yanayokaribiana kimaana na lugha lengwa.

Wasomi wengi pia hawajajitokeza kujifunza lugha ya Kiswahili. Wengi katika uzamili na uzamifu wanazamia Fasihi, Isimu na lugha huku wakitupilia mbali taaluma ya Tafsiri wakisema kuwa ni ngmu.

KICHOCHEO

Kilichomchochea mwalimu huyo kuzamia taaluma ya Tafsiri ni mengi sana. Mhadhiri wake marehemu Bi Shitemi alisimama naye na kumwelekeza kila akihitaji mawaidha na maelekezo katika taaluma ya tafsiri.

Wahadhiri wa tafsiri hawakuwa wenge wakati huo, Prof Shitemi na Dkt Odiwuori ndio walikuwa wamezamia sana taaluma ya tafsiri, aliunyakua nafasi huo na kuifanya kuwa kichocheo chake katika kuzamia taaluma hiyo.

Katika darasa lao, walikuwa wanafunzi 12 waliojisajili kufanya kozo ya BA Kiswahili. Hii ilimpa motisha na kumfanya atie bidi katika masomo yake.

Japo alikuwa mwanafunzi wa pekee aliyezamia Tafsiri katika Uzamili na hata Uzamifu, hakutiwa wasiwasi bali aliuchukua kama daraja la kuvuka katika kufikia upande wa mafanikio yake maishani.

Kila moja anaweza kufanikiwa katika daraja lolote maishani, ukakamavu, bidii na kumweka Mungu mbele ndiyo chanzo cha mafanikio maishani.

GWIJI WA WIKI: Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo

Na CHRIS ADUNGO

MAISHA ni safari. Kila hatua ya maisha ya mtu ni muhimu katika kuchangia kuwepo kwake.

Unapozaliwa, unaanza kuandaa makala kukuhusu. Kila unalolitenda – jema au baya – hujenga au kubomoa utu wako.

Lazima tutie bidii na kumakinikia yale tunayokusudia kufanya. Mengine ni ya matokeo ya haraka na mengine yanahitaji utulivu na uvumilivu ili kuyapata.

Ni muhimu kujitia moyo na kujishabikia katika shughuli zako ili uwe na hamu kubwa si tu ya kutaka kuendelea, bali pia ya kukamilisha mradi wowote unaouanza kwa njia bora na yenye ufanisi mkubwa.

Msingi muhimu zaidi katika kila hali ni kumtanguliza Mungu. Yeye ndiye hutukirimia neema na nguvu ya kutuwezesha kufikiria na hata kutekeleza shughuli zetu zote; ziwe kubwa au ndogo. Tuwe wema kwa watu wote tunaotangamana nao nyakati zote.

Huu ndio ushauri wa Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo – mwandishi na msomi wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno.

MAISHA YA AWALI

Asiko alizaliwa mnamo Februari 23, 1979 katika kijiji cha Ikumba, Maragoli ya Kati, Kaunti ya Vihiga. Alilelewa katika familia ya Bi Phanice Nyamanga Liko na marehemu Mzee Sospeter Liko Agufana.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Ikumba kati ya 1983 na 1991 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Butere Girls, Kaunti ya Kakamega. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwishoni mwa 1995.

Alifaulu vyema na kupata fursa ya kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Jiografia) katika Chuo Kikuu cha Maseno kati ya 1997 na 2001.

UALIMU

Baada ya kuhitimu ualimu, Asiko alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya Kegoye, Kaunti ya Vihiga. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Gahumbwa, Vihiga alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya Manor House (2003, Trans Nzoia), Shule ya Upili ya Usenge (2004-2005, Siaya) na Shule ya Upili ya Thurdibuoro (2005, Kisumu).

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri Asiko mnamo 2006 na kumtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya Mahaya, Kaunti ya Siaya. Alihudumu huko hadi mwaka wa 2009.

Asiko alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa minajili ya kusomea shahada ya uzamili mnamo 2005. Alifuzu mnamo 2007 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Uamilishi Dhima wa Nomino katika Sentensi ya Luloogoli” chini ya usimamizi wa Dkt Alice Mwihaki na Dkt Mathooko Mbatha.

Alirejea kufundisha katika Shule ya Upili ya Mahaya kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Maseno kwa shahada ya uzamifu (PhD) mnamo 2008. Alifuzu mnamo 2013 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Uchanganuzi wa Upole katika Majadiliano ya Bunge la Kenya” chini ya uelekezi wa Prof Florence Indede na Dkt Peter Karanja.

Asiko alifundisha katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Cha Tanzania, Bewa la Mwanza, kati ya 2009 na 2010 kabla ya kuajiriwa na Chuo Kikuu cha Maseno kuwa Mhadhiri Msaidizi. Alipanda ngazi kuwa mhadhiri mnamo 2013.

Mnamo 2016, Dkt Asiko alihudhuria Kongamano la Kimataifa la Utafiti wa kithamano katika Chuo Kikuu cha Illinois, Chicago, Amerika.

Akiwa huko, Dkt Asiko alikutana na wasomi wenzake waliokuwa wakitafitia jinsi ambavyo vyombo vya mawasiliano kama vile simu, redio na runinga vinaathiri tabia ya walemavu wa akili na watoto wanaougua usonji (autism).

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Asiko tangu utotoni. Idadi kubwa ya wahadhiri waliomfundisha walimpigia mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na wakamtia motisha ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Miongoni mwa mikota hao wa lugha waliompokeza malezi bora ya kiakademia ni Prof Kenneth Inyani Simala na Dkt Mwihaki.

Kufikia sasa, Dkt Asiko amechapishiwa makala ya kitaaluma katika sura za vitabu majarida mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa yakiwemo ‘East African Journal of Kiswahili Studies’, ‘Journal of Maseno University’ na ‘Kioo cha Lugha’.

Ametunga hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika mikusanyiko mbalimbali na amechangia pia mashairi katika diwani za ‘Wosia na Mashairi Mengine’ na ‘Wasifu wa Timothy Omusikoyo Sumba’ zilizotolewa na African Ink Publishers mnamo 2021.

Mbali na tamthilia ya ‘Mwenye Macho’ ambayo kwa sasa iko katika hatua za mwisho mwisho za uhariri katika kampuni moja ya uchapishaji wa vitabu humu nchini, Dkt Asiko ana mswada wa kitabu cha ‘Mazoezi na Marudio ya Gredi ya Sita’ na hadithi za watoto anazotazamia kufyatua hivi karibuni.

UANACHAMA

Dkt Asiko ni mwanachama kindakindaki anayeshiriki kikamilifu katika shughuli za Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA).

Aliwahi kuwa mlezi wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maseno (CHAKIMA) chini ya mwavuli wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kati ya 2013 na 2016.

Mbali na kuwa mwenyekiti wa masomo ya uzamili na uzamifu katika Chuo Kikuu cha Maseno, Dkt Asiko pia ni mmojawapo wa wadhamini katika Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Malipo ya Uzeeni katika Chuo Kikuu cha Maseno.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Dkt Asiko ni kuweka hai ndoto ya kuwa profesa na mwandishi mashuhuri wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili.

Kwa imani kuwa mfuko mmoja haujazi meza, Dkt Asiko anashughulikia mradi mbadala wa ufugaji wa kuku nyakati za mapumziko.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Dkt Asiko anaistahi sana familia yake inayozidi kumzibia pengo la shaka na kuiwekea taaluma yake mshabaha na thamani. Yeye ni mwanandoa na mama wa watoto watano – Ibrahim, Timothy, Christine, Phanice na Philip. Pia ni mama wa kambo wa watoto wanne – Rose, Valentine, Stephanie na Cornel. Mumewe mpendwa ni Bw Cornel Adede.

GWIJI WA WIKI: Franklin Mukembu

Na CHRIS ADUNGO

KUWA na mwelekeo chanya ni sifa ya lazima kwa binadamu yeyote yule mwenye maono endelevu kushikilia kikiki faulu ndipo afaulu kwa lolote lile analolifanya au analonuia kulitenda.

Yeyote anayelenga kufanikiwa maishani na kitaaluma sharuti atawaliwe na matumaini yasiyofifia ili aweze kuhimili panda-shuka za kila sampuli bila ya kupoteza mwelekeo ambao unadhibiti misingi ya malengo au maazimio yake.

Kama ilivyo katika biashara, kuna wakati wa kupata faida na vilevile kuna wakati wa kupata hasara. Hivyo ndivyo hali ilivyo hata kwa mwandishi. Kuna uwezekano wa kuiandika kazi bila ya kuchapishwa; lakini ukiwa na mwelekeo chanya, utaweza kuvumilia bila ya kukata tamaa wala kusita kuandika tena.

Jambo la muhimu katika kutenda lolote ulifanyalo ni kujiweka katika nafasi ya pili ili kuweza kushughulikia wengine kwanza. Hili litakuondolea ubinafsi na bila shaka matokeo yatawaridhisha wengine kisha utulivu na amani itasheheni katika moyo na nafsi yako.

Mhusika Amani katika riwaya yake Marehemu Ken Walibora ya ‘Kidagaa Kimemwozea’ anashikilia kuwa licha ya mswada wake kuibwa; cha maana mno ni kwamba hatimaye ulichapishwa na ujumbe aliotaka uwafikie wasomaji uliwafikia kwa njia iliyofaa.

Huu ndio ushauri wa Bw Franklin Mukembu – mwandishi chipukizi na mshairi shupavu ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na somo la Jiografia katika Shule ya Upili ya Munithu, eneo la Imenti Kaskazini, Kaunti ya Meru.

MAISHA YA AWALI

Mukembu amewahi kuwaelekeza wengi wa wanafunzi wake kutunga mashairi ambayo yamewahi kuchapishwa katika gazeti la Taifa Leo.

Tangu 2016, Mukembu amekuwa mtahini wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC). Yeye hushughulikia Karatasi ya Kwanza ya Kiswahili (Insha KAR 102/1). Tajriba anayojivunia katika utahini na usahihishaji wa karatasi hiyo imempa fursa ya kuzitembelea shule mbalimbali ndani na nje ya Kaunti za Meru na Tharaka-Nithi kwa nia ya kuhamasisha, kushauri na kuelekeza walimu na wanafunzi kuhusu njia na mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa ya KCSE.

Mukembu amewashirikisha wengi wa wanafunzi wake katika mashindano ya mara kwa mara ya Digital Essay yanayoendeshwa na Shirika la eKitabu. Mnamo 2018, mwanafunzi wake aliambulia nafasi ya tatu na kujizolea zawadi ya rununu na kitita cha Sh10,000 katika Kitengo cha Uandishi wa Insha za Kiswahili yenye mada ‘Teknolojia Katika Kufanikisha Elimu kwa Wote’. Mnamo 2019, mwanafunzi wake aliibuka mshindi nambari tatu katika Kitengo cha Kiswahili kwa kuandika insha iliyohusu jinsi ya kutatua mahudhurio mabaya shuleni kwa kutumia teknolojia.

Makala yake ya kwanza kuchapishwa katika gazeti la Taifa Leo ni Barua kwa Mhariri ambapo aliwashauri wachambuzi wa magazeti katika vituo mbalimbali vya runinga na redio wachambue pia gazeti la Taifa Leo kama walivyokuwa wakifanya kwa machapisho mengine.

Kabla ya kufuzu kwa shahada ya kwanza, Mukembu alipata kazi ya muda ya kufundisha katika Shule ya Wavulana ya Kiriani, eneo la Maara, Kaunti ya Tharaka-Nithi.

Makala yake ya kwanza katika gazeti la Daily Nation yalichapishwa mnamo Novemba, 30, 2009 katika ukumbi wa ‘Letter to the Editor’ ambapo alieleza kuhusu umuhimu wa kuwatayarisha wanafunzi vyema na mapema ili kuzuia visa vya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.

TUZO

Mnamo 2010, Mukembu aliandika shairi la kumtumbuiza Mbunge wa Imenti Kaskazini, Kaunti ya Meru katika hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofaulu vyema katika mtihani wa kitaifa wa KCSE kutoka Shule ya Kutwa ya Munithu. Shairi hilo lililokaririwa na wanafunzi, lilimvunia Mukembu tuzo ya haiba na ya kutamanika mno.

Mnamo 2014, Mukembu alimtungia mwalimu wa shule moja ya msingi katika Kaunti ya Embu shairi ambalo liliwatambisha wanafunzi wake hadi kiwango cha kitaifa katika tamasha za muziki na drama. Shairi hilo lilikuwa lenye mada ‘Mitaa ya Mabanda’.

Mwaka wa 2018, alitunga shairi kuhusu Supa Bima (Bima ya Hospitali ya NHIF). Lilikaririwa na Kundi La wanafunzi 18 kutoka Shule ya Upili ya Munithu hadi kiwango cha kitaifa katika Chuo Kikuu Cha Dedan Kimathi mjini Nyeri.

Mukembu amewahi pia kutambuliwa na kutuzwa pakubwa na shirika lisilo la kiserikali la GEC ambalo liliwahi kudhamini hafla ya kutuzwa kwa wanafunzi waliong’aa katika mitihani na fani nyinginezo.

Mwaka uo huo, alimwongoza mwanafunzi wake kuandika insha ya kidijitali na akaibuka nambari ya tatu katika ushindi uliomvunia Mukembu cheti pamoja na vocha ya Sh1,000. Hafla ya kutolewa kwa tuzo hizo iliandaliwa katika Jengo la Sarit Centre, eneo la Westlands, Nairobi.

JIVUNIO

Zaidi ya kuwa mkereketwa wa lugha ya Kiswahili, Mukembu pia anajivunia natija si haba kutokana na uelekezi wa michezo ya kuigiza, utunzi wa michezo hiyo na uchoraji wa mandhari mbalimbali kwa minajili ya michezo ya drama (back drops).

Nyakati za tamasha za muziki na drama, Mukembu huandikia walimu wa shule za msingi na upili mashairi ya ngonjera, ya kukaririwa na vikundi vya wanafunzi au hata mwanafunzi mmoja kwa malipo ya kati ya Sh2,500 na Sh4,000. Mukembu pia ni mwamuzi stadi wa mashairi na maigizo katika mashindano ya shule, makanisa na mashirika mengine.

GWIJI WA WIKI: Fatma Ali Mwinyi

Na CHRIS ADUNGO

JIFUNZE kuwa na msimamo katika maisha.

Usiwe bendera ifuatayo upepo.

Usiruhusu kamba yako ya matumaini kukatwa na yeyote. Tafuta marafiki watakaokujenga badala ya kukubomoa.

Kubali kurekebishwa ili uboreke zaidi. Jifunze kujifunza na uwe mwadilifu. Usiwe na mtazamo hasi kuhusu maisha. Shukuru ukifanikiwa kupata na ujitume zaidi ukikosa kufaulu. Mtegemee Mungu katika mambo yote!

Huu ndio ushauri wa Bi Fatma Ali Mwinyi – mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret, anayeinukia vyema katika uandishi wa Fasihi ya Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Fatma alizaliwa mnamo Machi 9, 1998 katika mtaa wa Barisheba, Kaunti ya Mombasa. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bw Ali Mwinyi na Bi Najma Omar. Nduguze ni Binti Ali, Khamis Ali, Khadija Ali na Swabra Ali.

Alilelewa na nyanya yake, marehemu Bi Queen Kadiri, katika eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi kabla ya kurejea Mombasa alikoishi na mama yake mkubwa, Bi Rahma Omar.

Hali hiyo ilichangiwa na wingi wa shughuli za kikazi zilizomzonga mamaye mzazi ambaye ni nesi; naye baba alikuwa wakati huo akisomea shahada katika Chuo cha Utalii. Familia ya Bw Mwinyi ilihamia baadaye katika mtaa wa Mtopanga, Mombasa.

Nyanya wa upande wa mama, Bi Khadija Mohammed, amekuwa mstari wa mbele katika kumwelekeza Fatma kimaadili, kumtia katika mkondo wa nidhamu kali na kumshajiisha maishani.

Bi Khadija ambaye ana usuli Pemba, ndiye alimwamshia mjukuu wake huyu ari ya kukichapukia Kiswahili baada ya kumwathiri pakubwa kutokana na upekee wa lafudhi yake.

Ama kweli, jungu kuu halikosi ukoko na kinolewacho hupata!

ELIMU

Fatma alianza safari yake ya elimu mnamo 2000 katika Shule ya Msingi ya Bashiri, Mombasa. Alisomea huko hadi darasa la tatu kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Bahwan, Mombasa mnamo 2004. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwishoni mwa 2011.

Mbali na wazazi, walimu walikuwa wepesi katika kumhimiza Fatma kujitahidi masomoni baada ya kutambua utajiri wa kipaji na uwezo wake katika Kiswahili.

“Fatma jifunge kibwebwe katika somo langu la Kiswahili. Uwezo unao na alama hafifu kwako ni mwiko.” Maneno hayo ya mara kwa mara kutoka kwa Bw Issa Juma yalimpa Fatma msukumo wa kuanza kuthamini na kukichangamkia Kiswahili tangu utotoni.

Wengine waliopanda mbegu zilizootesha ari yake ya kukipigia Kiswahili chapuo ni Bw Luguah, Bw Leakeh na Bw Onyango aliyejitolea kupiga msasa matumizi yake ya lugha kwa kunyosha sarufi, tahajia na hati ya mwanafunzi wake huyu.

Fatma aliishia kuwa miongoni mwa waandishi bora wa Insha za Kiswahili na Kiingereza shuleni na akawa maarufu sana miongoni mwa walimu na wanafunzi wenzake.

Baada ya kuhitimu masomo ya shule ya msingi, alijiunga na Shule ya Upili ya Kwale Girls alikosomea kati ya 2012 na 2015.

Umahiri wa Fatma katika somo la Kiswahili ulidhihirika zaidi katika kiwango hiki cha elimu na akawa mwanafunzi wa kwanza katika mitihani yote ya Kiswahili hadi Kidato cha Nne.

Akiwa huko, alishiriki kikamilifu shughuli za Chama cha Kiswahili cha Kwale Girls na kupata jukwaa maridhawa la kuchangia makuzi ya Kiswahili shuleni. Alikuwa akiandika taarifa za matukio mbalimbali na kuwapa wenzake wasome gwarideni.

Walimu waliazimia haja ya kukuza na kupalilia talanta yake. Bw Jumaine Makoti na Bw Alphonce Kaka walijitolea kumpa Fatma vitabu mbalimbali vya hadithi na kumteua mara kwa mara kusoma vifungu vya Ufahamu darasani.

Chini ya uelekezi wa walimu hawa, Fatma alishiriki mashindano mengi ya kutoa hotuba na kujizolea tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno.

Alivutiwa pia na michezo ya kuigiza na akawa mshiriki wa mara kwa mara wa tamasha za muziki na drama. Fursa hizo zilimwezesha kunoa kipaji chake cha ulumbi na kuinua kiwango chake cha umilisi wa lugha.

Isitoshe, Fatma alitamba sana katika mashindano ya Fasihi ya Kiswahili yaliyohusisha shule mbalimbali kutoka ndani na nje ya Kaunti ya Kwale. Ubora wake katika mashindano hayo uliwahi kumzolea ‘Kamusi ya Karne ya 21’ na kitabu cha ‘Marudio na Mazoezi ya Kiswahili’. Tuzo hizo zilimwamshia ilhamu ya kuzamia kabisa somo la Kiswahili na akazidi kuwa wembe darasani.

UANDISHI

Fatma ni mwandishi anayeinukia vyema katika sanaa ya uandishi wa kazi bunilizi. Aliwahi kushiriki mashindano mbalimbali ya uandishi akiwa mwanafunzi wa shule ya upili na akawapiku wenzake wa vidato vya juu.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali na kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, anajivunia kuandika na kuchapishiwa kazi kadhaa za kibunifu. Baadhi ya hadithi zake ni ‘Ibra’ katika mkusanyiko wa ‘Shaka ya Maisha na Hadithi Nyingine’ (The Writers’ Pen Publishers, 2020) na ‘Mshahara wa Dhambi’ katika diwani ya ‘Maskini Maarufu na Hadithi Nyingine’ (African Ink Publishers, 2020).

Fatma ameandika pia miswada ya riwaya na tamthilia ambayo sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji chini ya mwavuli wa Chama cha Waandishi wa Kiswahili (CHAWAKI). Kazi zake zinazidi kupata umaarufu miongoni mwa washikadau katika sekta ya elimu, hasa walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali nchini Kenya.

KICHOCHEO

Kilichomchochea Fatma kujitosa katika ulingo wa uandishi wa Kiswahili ni ukubwa wa kiwango cha kuathiriwa na kazi za Prof Said A. Mohamed, Mohammed S. Mohammed, Penina Muhando Mlama, Zainab Burhani, Pauline Kea Kyovi na marehemu Prof Ken Walibora.

Wengine ambao wamekuwa wakimchochea pakubwa na kumpa ari ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi wa vitabu ni Dkt Collins Kenga Mumbo, Dkt Harriet Ibala, Bw Vincent Magugu na Dkt Robert Oduori – mikota na walezi wa Kiswahili waliompigia mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi bunilizi.

Fatma amewahi kuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Kwale Boys, Shule ya Msingi ya Bridge(Mtopanga) na Shule ya Mumias Muslim Girls(Kakamega).

Bw Richard Amunga Ondoli ambaye pia ni mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili, amechangia pakubwa kustawisha uandishi wa Fatma anayemstahi sana mwanahabari Hassan Mwana wa Ali (Redio Maisha). Fatma kwa sasa anashirikiana na wanafunzi wenzake – Papaa kombo, Amunga na Said Hamisi kuchangia mijadala ya kitaaluma (Isimu ya Kiswahili) kupitia msururu wa video za ‘Youtube’.

UANAHABARI

Fatma ni mwanachama wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi (CHAKIMO) na huchangia makala, mashairi na habari mbalimbali katika jarida la ‘Dafina Wiki Hii’ ambalo ni chapisho maalumu la CHAKIMO kila Jumatatu na Ijumaa.

Aliwahi kushiriki uendeshaji wa kipindi ‘Dafina ya Lugha’ na kutangaza habari za saa tatu asubuhi kila Ijumaa katika idhaa ya MU-FM (103.9) kwa miaka miwili ya kiakademia (2018-19). Alitawazwa Mtangazaji Bora wa Mwaka katika maadhimisho ya ‘Siku ya Vipawa’ katika Chuo Kikuu cha Moi mnamo 2019.

Ameshirikiana pia na wanafunzi wenzake kuandaa michezo mbalimbali ya kuigiza pamoja na kuandika ‘Miongozo’ ya vitabu teule vya fasihi vinavyotahiniwa katika KCSE Kiswahili.

Aidha, amekuwa mstari wa mbele kuwaongoza wanachama wenzake wa CHAKIMO kuzuru shule mbalimbali kwa nia ya kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

MAAZIMIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Fatma ni kuzamia kabisa taaluma ya Kiswahili na kuweka hai ndoto ya kuwa profesa. Analenga pia kuwa mwanazuoni atakayekuwa kiini cha motisha itakayotawala wanataaluma wengi wa kike watakaoinukia katika bahari ya Kiswahili. Anaazimia kuwa mmliki wa kampuni ya uchapishaji itakayokuwa na malengo mahsusi ya kutambua, kukuza na kulea vipaji vya waandishi chipukizi.

GWIJI WA WIKI: DKT EVANS MAKHULO

Na CHRIS ADUNGO

WATETEZI wa Kiswahili watafanya lugha hii ipendeze na ya kupendeka zaidi iwapo wataacha kulumbana, kujipiga vifua na kujipa lakabu za kutisha!

Ipo haja kwa wapenzi wa Kiswahili kushirikiana kwa lengo moja la kufaulisha makuzi, maendeleo na ustawi wa lugha hii katika sekta mbalimbali za jamii.

Wataalamu wa Kiswahili watawaliwe na kiu ya kusambaza maarifa, waendeleze msingi imara wa lugha na watoe mchango wa kuhimiza na kuchochea kasi ya kutekelezwa kwa malengo mahsusi katika nyanja za uandishi, utafiti, ufundishaji na matumizi ya Kiswahili.

Nyaraka na stakabadhi muhimu za serikali zitafsiriwe kwa Kiswahili, hotuba zote za rais zitolewe kwa Kiswahili na vikao vya mabunge vidhihirishe kwamba Kiswahili kwa kweli ni lugha rasmi ya Kenya. Vinginevyo, urasmi wa Kiswahili utasalia tu kuwa kijisehemu cha maandishi ndani ya Katiba!

Haya ndiyo maoni ya Dkt Evans Makhulo – mshairi shupavu, msomi wa fasihi, mlezi wa vipaji na mjasiriamali anayeinukia vyema katika uandishi wa vitabu vya Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Makhulo alizaliwa mnamo 1986 katika kijiji cha Itete, eneo la Matungu, Kaunti ya Kakamega. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bw Sylvester Makhulo na Bi Lilian Apondi.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Itete kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Nanyeni, Matungu akiwa mwanafunzi wa darasa la nne. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwishoni mwa 2002.

Makhulo alisomea katika Shule ya Upili ya Koyonzo, Kakamega kuanzia mwaka wa 2003. Alifanya Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2006 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kwa shahada ya ualimu (Kiswahili na Historia) mnamo 2008.

Alifaulu vyema kwa kupata daraja ya juu (First Class) mnamo 2012 na ufanisi huo ukampa ufadhili wa kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi kuanzia 2013.

Alifuzu mnamo 2015 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Mamlaka na Itikadi katika Nyimbo Teule za Taraab” chini ya usimamizi na uelekezi wa Prof Rayya Timammy na Dkt James Zaja Omboga.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kwa minajili ya shahada ya uzamifu (phD) mnamo 2016. Alifuzu katika mwaka wa 2019 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Ukosefu wa Upole katika Matini ya Nyimbo za Taarab”.

Makhulo anatambua ukubwa wa mchango wa walimu wake wa awali katika kumhimiza kukichapukia Kiswahili. Baadhi yao ni Bw Joseph Mugera na Bw William Nyangweso waliotangamana naye kwa karibu sana katika Shule ya Upili ya Koyonzo.

“Nilitamani sana ije siku ambapo nami ningekuwa na umilisi mkubwa wa lugha, nikisarifu Kiswahili kama walivyokuwa wakizungumza walimu hawa kwa mvuto, ucheshi na ujasiri. Ama kweli, kinolewacho hupata!”

Wengine waliompokeza malezi bora ya kiakademia katika Chuo Kikuu cha Nairobi ni Prof Kyallo Wadi Wamitilia na Prof John Habwe. Hawa ndio walimwamshia Makhulo ari ya kukipenda Kiswahili tangu walipokuwa waendeshaji wa kipindi ‘Lugha Yetu’ katika Shirika la Habari la Kenya (KBC).

Makhulo anaamini kuwa Kiswahili kina uwezo wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ujuzi, ajira na uvumbuzi.

UALIMU

Makhulo alijitosa katika ulingo wa ualimu mnamo 2012. Alifundisha katika Shule ya Upili ya Koyonzo kwa muda mfupi kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya St Teresa’s Eastleigh, Nairobi mnamo 2014.

Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi. Amewahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya St Francis Rang’ala Girls, Kaunti ya Siaya mnamo 2016. Janga la corona lilimzimia ndoto ya kutua Amerika kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha St Lawrence, New York mwanzoni mwa mwaka wa 2020.

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Makhulo tangu utotoni. Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi na upili, nyingi za insha alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kutoka kwa walimu wake na akawa maarufu sana miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali na kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Ilhamu anayojivunia katika ulingo wa uandishi ilichangiwa zaidi na walimu waliotambua mapema utajiri wa kipaji chake katika utunzi wa kazi bunilizi.

Uandishi wa Makhulo umeathiriwa pakubwa na kazi za Profesa Kithaka wa Mberia na Prof Abdilatif Abdalla – washairi shupavu, wasomi maarufu na mikota wa lugha wanaozidi kumpa ari ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi wa vitabu vya Kiswahili.

Kufikia sasa, Makhulo anajivunia kuandika na kuchapishiwa makala kadhaa ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Ametunga hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika mikusanyiko mbalimbali. Amechangia pia mashairi katika diwani za ‘Wosia Na Mashairi Mengine’ na ‘Malenga wa Afrika’ zilizochapishwa na African Ink Publishers mnamo 2021. Baadhi ya tungo zake huchapishwa mara kwa mara katika gazeti hili la ‘Taifa Leo’.

Baada ya kuchangia uhakiki wa ‘Kamusi Elezi ya Kiswahili’ iliyotolewa na Jomo Kenyatta Foundation (JKF) mnamo 2017, Makhulo aliandika ‘Mwongozo wa Kigogo’ uliofyatuliwa na Phoenix Publishers mnamo 2019.

Baadhi ya hadithi zake ni ‘Siwezi Tena katika mkusanyiko wa ‘Siwezi Tena na Hadithi Nyingine’ (Chania Publishers), ‘Mwisho wa Mwisho’ katika diwani ya ‘Mwisho wa Mwisho na Hadithi Nyingine’ (Mentor Publishers) na ‘Mke wa Jirani’ katika mkusanyiko wa ‘Mkaguzi wa Shule’ uliochapishwa na Education Distinction Publishers mnamo 2021.

Makhulo ameandika pia miswada mingi ya riwaya na tamthilia ambayo sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu.

JIVUNIO

Ndoto ya Makhulo ni kufikia upeo wa taaluma yake na kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi aliowafundisha katika ngazi na viwango tofauti vya elimu. Mmoja wao ni mwanahabari wa KU-TV, Bw Kevin Okello.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Makhulo ni kupanua wigo wake wa ujasiriamali, kufyatua diwani itakayobadilisha sura ya ujifunzaji na ufundishaji wa Ushairi wa Kiswahili na kuwalea waandishi chipukizi wa kazi za kibunifu.

Zaidi ya kuhudhuria makongamano mengi ya kupigia chapuo Kiswahili, Makhulo amekuwa akichangia mijadala ya kitaaluma na kuchanganua masuala ya siasa kupitia runinga mbalimbali nchini Kenya.

GWIJI WA WIKI: Beatrice Gatonye

Na CHRIS ADUNGO

KILA binadamu ana kipaji ambacho ni wajibu wake kukitambua na kutia azma ya kukipalilia. Nidhamu, bidii, uvumilivu na imani ni kati ya mambo muhimu yanayochangia mafanikio ya binadamu.

Jitume katika hicho unachokitenda na umtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga maishani. Fanya hiyo ili ufaulu!

Huwezi kabisa kujiendeleza kitaaluma iwapo utakosa maono. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta. Usilie wala kukata tamaa usipofaulu. Endelea kukazana na milango ya heri itajifungua yenyewe.

Huu ndio ushauri wa Bi Beatrice Gatonye – mpenzi kindakindaki wa Kiswahili, mlezi wa vipaji, mwanahabari shupavu na mwanamuziki chipukizi ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa KBC Channel 1.

MAISHA YA AWALI

Beatrice alizaliwa katika eneo la Kaptagat, Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu. Ndiye mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne wa Bi Jane Wanjiku – mke wa pili wa Bw Joseph Gatonye ambaye mkewe wa kwanza ni Bi Joyce Muthoni.

Beatrice alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Kipsinende, Kaptagat mnamo 1987. Huko ndiko alikosomea hadi mwishoni mwa 1998. Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) na akajiunga na Shule ya Upili ya Naivasha Girls, Kaunti ya Nakuru mnamo 1999.

Baada ya kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2002, alijiunga na Chuo cha Eldoret Aviation alikosomea taaluma ya Habari na Mawasiliano hadi 2004.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo cha Habari Maalum mjini Arusha, Tanzania mnamo 2009. Alifuzu katika mwaka wa 2011 na akarejea Kenya kusomea shahada ya uanahabari katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kati ya 2013 na 2015.

MCHANGO KITAALUMA

Beatrice alipata nafasi ya kuwa mwanahabari wa kujitolea katika kituo cha Sauti Ya Rehema (SAYARE) mnamo 2003. Alihudumu huko kwa muda mfupi akiwa ripota wa runinga ya Sayare TV na mwendeshaji wa kipindi cha jioni cha ‘Evening Drive’ katika Idhaa ya Sayare FM.

Ilikuwa hadi 2008 aliporejea katika kituo hicho kilichomwajiri kuwa mtangazaji wa habari runingani na mwendeshaji wa vipindi vya asubuhi redioni. Kituo hicho ndicho kilidhamini masomo ya Beatrice nchini Tanzania.

Beatrice aliajiriwa na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) mnamo Januari 2012 kuwa ripota wa KBC Channel 1. Aliaminiwa fursa ya kusoma habari za ‘Darubini ya Channel 1’ baada ya miezi miwili pekee na akatawazwa Mtangazaji Bora wa Mwaka katika tuzo zilizotolewa na Baraza la Vyombo vya Habari Nchini Kenya (MCK) mnamo 2014.

Miongoni mwa wanahabari anaowapigia mhuri kutokana na ustadi wao wa kuipa taaluma hii uhai ni Salim Kikeke wa BBC na Jamila Mohamed wa Citizen TV.

KICHOCHEO

Beatrice alianza kuvutiwa na taaluma ya uanahabari katika umri mdogo. Anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa baba yake mzazi katika ufanisi anaojivunia kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili.

Baada ya kubaini utajiri wa kipaji cha mwana wao huyu katika utangazaji na uandishi wa kazi za kibunifu, wazazi wa Beatrice walimpa majukwaa mbalimbali ya kuikuza talanta yake.

Beatrice alikuwa mwepesi wa kujirekodi katika kanda za sauti na kujisikiliza redioni. Babake mzazi alipalilia kipawa kilichoanza kujikuza ndani ya mwanawe kwa kumnunulia nakala ya gazeti la ‘Taifa Leo’ kila siku.

Kati ya walimu waliomchochea Beatrice kukipenda Kiswahili akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni Bw Kariuki aliyemhimiza sana kusoma vitabu vya hadithi.

“Bw Kariuki alipanda ndani yangu mbegu zilizootesha utashi na kariha ya kukichapukia Kiswahili. Alinielekeza kwa idili na akaniamshia ari ya kuthamini masomo.”

Kariha na ilhamu zaidi ya Beatrice katika makuzi ya Kiswahili ilichangiwa na Bw Mbote – mwalimu aliyemtanguliza vyema katika somo la Fasihi na kumpokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya upili.

Chini ya ulezi wa Bw Mbote, Chama cha Kiswahili cha Naivasha Girls kilimpa Beatrice jukwaa maridhawa la kuinua kiwango chake cha umilisi wa lugha. Kilinoa makali yake ya ulumbi na kikachangia ujasiri wake wa kuzungumza mbele ya umma.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa sasa na Beatrice katika Kiswahili ni zao la yeye kufundishwa na wataalamu wabobevu na wapenzi kindakindaki wa lugha hii.

MAAZIMIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Beatrice ni kujikuza kitaaluma, kujifunza Lugha Ishara (KSL) na kuweka hai ndoto ya kuwa miongoni mwa wadau wakuu wa kutoa maamuzi muhimu katika tasnia ya uanahabari.

Anaazimia pia kuwa mmliki wa kituo cha habari kitakachokuwa na malengo mahsusi ya kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanahabari chipukizi watakaoangazia masuala mbalimbali yaliyo na umuhimu katika jamii.

Beatrice anapania kuwa kiini cha motisha itakayotawala wanataaluma wengi wa kike wanaoinukia na watakaoinukia katika ngazi na viwango tofauti vya uanahabari.

HUDUMA KWA JAMII

Beatrice anaendesha kampeni maalum ya kusambaza sodo kwa wanafunzi wa kike kutoka jamii zisizojiweza. Kampeni hiyo inalenga wasichana wa shule za msingi na upili pamoja na wanawake kutoka familia maskini nchini Kenya.

“Inasikitisha kwamba wapo wasichana wanaolazimika kutumia vipande vya magodoro, mablanketi, majani pamoja na karatasi ili kujistiri msimu wao wa hedhi unapowadia.”

Kupitia kampeni hiyo, Beatrice anakusudia kuhakikisha kuwa mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni yanaongezeka hata zaidi.

MUZIKI

Beatrice ni mtunzi wa nyimbo za sifa kwa Mwenyezi Mungu. Kufikia sasa, amecharaza kibao ‘Huniongoza’ alichokirekodi mwaka huu wa 2021. Mbali na kipaji cha uimbaji, pia ana uwezo wa kucheza vyombo na ala mbalimbali za muziki.

JIVUNIO

Beatrice anajivunia wazazi wake waliojihini mengi, wakajitolea kumsomesha na kumzibia pengo la shaka maishani.

Anaistahi sana familia yake inayozidi kuiwekea kazi yake mshabaha na thamani licha ya panda-shuka za kila sampuli.

Beatrice ni mwanandoa na mama wa watoto watatu – Gideon Parselelo, Joshua Lesalon na Tiffany Chemutai. Yeye ni mama wa kambo wa watoto wawili – Ronald Kiprono na Patricia Cheptoo. Mumewe mpendwa ni Bw Zakayo Ng’etich.

GWIJI WA WIKI: Musau Muia

Na CHRIS ADUNGO

MWENYEZI Mungu alipokuumba, alikupangia ramani ya maisha yako. Kila siku fanya jambo ambalo litakupigisha hatua ya kusonga mbele katika barabara ya kutafuta ufanisi.

Kuishi ni matendo. Uzembe si mzuri. Zohali ni nyumba ya njaa. Taa ya mafanikio yako huwaka wakati unapojituma na kujizatiti katika shughuli za kila siku. Guru Ustadh Wallah Bin Wallah husema, “Huwezi kuushika wakati na kuufungia usisonge. Usipoenda na wakati utaachwa na wakati. Wakati ndio mkate!”

Ipande mbegu ya ufanisi kila siku ya maisha yako na mavuno yatakuwa mazuri na mengi ajabu. Kusema kweli, huwezi ukapanda mahindi kisha utarajie kuvuna kahawa! Mtu huvuna anachokipanda. Ukipanda na kupalilia vyema, bila shaka utapata tabasamu ya milele. Jitume sana leo ili kesho ufurahie matunda ya jasho lako!

Ukitaka kufikia kileleta cha mafanikio, nyenyekea na uwastahi wanadamu wengine. Unyenyekevu ni mbolea katika kufanikiwa kwa mtu. Usiwe mwenye magwaji na magumashi. Heri watu wakuone mjinga kutokana na unyenyekevu wako.

Huu ndio ushauri wa Bw Musau Muia – mwandishi chipukizi wa Isimu na Fasihi ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys, Kaunti ya Makueni.

MAISHA YA AWALI

Musau alizaliwa Agosti 8, 1993 kijijini Mang’elete, Makueni. Ni mwana wa katikati katika familia ya Bw James Muia na Bi Ann Mutee.

Amesomea katika shule tatu tofauti za msingi kwa sababu ya uhamisho wa kikazi wa baba yake. Alianzia safari hiyo ya elimu katika Shule ya Msingi ya Mang’elete kati ya 2000 na 2005 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Mtito-Andei mnamo 2006.

Baadaye, alijiunga na Shule ya Msingi ya Emali, Makueni. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwishoni mwa 2007.

Msukumo wa kukipenda Kiswahili ulizidishwa na vitabu vya ‘Kiswahili Mufti’ ambavyo vimeandikwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah. Vitabu hivyo vilimpa ilhamu ya kukichangamkia Kiswahili kutokana na maelezo bora yaliyomo.

Kwa hakika, vitabu hivyo vilichangia zaidi ya asilimia 80 katika alama 96 alizopata katika KCPE Kiswahili. Alifaulu vyema na kupata fursa ya kusomea katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys mnamo 2008.

Ni wakati akiwa Mukaa ambapo aliboresha kiwango chake cha umilisi wa Kiswahili baada ya kuhimizwa pakubwa na walimu wake. Bw Kaula alimfaa sana kwa nasaha zake aula. Aidha ndiye aliyeidhinisha ombi la Musau la kuanzisha Jopo la Kiswahili (kwa sasa ni Chama cha Kiswahili cha Mukaa). Idhini hiyo ilimpa nafasi ya kuwa Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho.

“Bw Kaula alinichochea pakubwa kukipenda Kiswahili. Alipanda ndani yangu mbegu zilizootesha utashi na kariha ya kukichapukia Kiswahili. Alijitolea kunielekeza kwa ari na idili.”

Nasaha za mwalimu mkuu, Bw Francis Mutunga Mutua, zilimpa msukumo chanya katika kuyatambua na kuyachambua maisha.

Kuna kauli ya mwalimu mkuu anayoikumbuka hadi leo. Kwamba, “Failure is a situation, never a person. Notice the difference between what happens when a man says to himself that he failed three times and what happens when he says he is a failure.”

Maneno hayo yalimkosha kwelikweli na kumfumbua macho kabisa.

Bw Kaula ambaye sasa ni Naibu wa Mwalimu Mkuu anayesimamia masuala ya akademia, pia alichangia ufanisi wa Musau. Kauli yake kwamba, “ivitukaniaa kitindioni” iliamsha ari na hamu ya kujizatiti ili aweze kutimiza ndoto zake.

Kauli hii ya Bw Kau ina maana kwamba wanafunzi wanapoenda shuleni, huwa ni wengi na wanafungiwa katika zizi moja (shule). Wanapoendesha shughuli zao shuleni, kuna wale wanaofanikiwa na kunao pia wanaokosa kufaulu kutegemea namna wanavyoutumia muda wao.

Uongozi katika Jopo la Kiswahili ulimpa Musau fursa maridhawa ya kuitafitia lugha ya Kiswahili. Usikivu, umakini na heshima ya wanafunzi wenzake ni miongoni mwa mambo yaliyomshajiisha sana.

USOMI NA UTAALAMU

Musau alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton (Bewa Kuu) mnamo Septemba 2012. Alipania kufanya shahada ya Isimu – Kiswahili na Kiingereza lakini akaarifiwa kwamba isingewezekana na akashauriwa aende Ujerumani kunakofanywa kozi hiyo.

Alipewa michepuo kadhaa ya masomo achague anaotaka. Kwa sababu ya utashi wake wa kusomea Kiswahili, aliishia kufanya shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Akiwa chuoni, alijiunga na Chama cha Kiswahili cha Egerton (CHAKIE). Mnamo 2013, aliingia katika uongozi wa CHAKIE baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu.

Mwanzoni mwa mwaka wa 2015, alichaguliwa kuwa Katibu Mtendaji wa CHAWAKAMA-Kenya. Wadhifa huo wa ulimpa motisha zaidi ya kukichapukia Kiswahili.

Musau amehudhuria makongamano mengi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi. Mnamo 2013, alihudhuria Kongamano la Kimataifa la Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) jijini Kigali, Rwanda.

Mnamo 2016, alihudhuria Kongamano la Kimataifa la CHAWAKAMA nchini Zanzibar katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Mnamo Machi, 2020 aliwapeleka wanachama wa Chama cha Kiswahili cha Mukaa (CHAKIMU) katika Kituo cha WASTA, Matasia, Ngong ambako walijifunza mengi kutoka kwa Guru Ustadh Wallah Bin Wallah. Kwa mujibu wa Musau, nasaha za Wallah Bin Wallah zimechangia pakubwa kuboresha matokeo ya mtihani na kuimarisha nidhamu miongoni mwa wanafunzi wa Shule ya Upili ya Mukaa Boys.

Baada ya kufuzu na shahada ya kwanza, Musau alianza kufundisha Kiswahili na somo la Dini katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys mnamo 2016 na ndiye mlezi wa CHAKIMU. Musau kwa sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

UANDISHI

Musau ni mwandishi chipukizi wa kazi za Kiswahili. Ndoto yake ya uandishi ilichipuza alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Mara si chache aliwahi kushiriki mashindano mbalimbali akiwa katika shule ya upili na kuwapiku wenzake wa vidato vya juu.

Jambo hilo likawa kiini cha msukumo wake wa kujitosa katika ulingo wa uandishi wa vitabu. Kwa sasa anaandikia kampuni ya Spearsharp Educational Publishers vitabu vya Kiswahili kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC). Isitoshe, ana miswada ya kazi mbili ambazo anaamini zitachapishwa mwishoni mwa mwaka huu: ‘Usaili Sahili wa Sarufi’ na ‘Utu na Ubinadamu’. Musau ana imani kwamba nakala hizi zikichapishwa, zitabadilisha pakubwa sura ya ujifunzaji na ufundishaji wa Kiswahili ndani na nje ya Kenya.

JIVUNIO

Musau anaivulia kofia familia yake ambayo imekuwa ikimpa kila sababu ya kujikaza kisabuni. Anastahi sana mkewe Bi Victoria Ndanu ambaye amekuwa akimhimiza sana kukichangamkia Kiswahili.

Isitoshe, anajivunia kuwa na wanafunzi ambao wamekuwa kiini cha mapenzi ya dhati aliyo nayo kwa kazi yake.

GWIJI WA WIKI: Tabitha Manzi

Na CHRIS ADUNGO

USIOGOPE kukosea. Kupotea njia ndiko kujua njia. Jaribu tu. Ipo siku ambapo mghafala utaisha. Zidi kumulika uendako kwa hekima na tabasuri. Utaziona fanaka foko ukivuta subira na kujiamini.

Wengi wanaotaka kuogelea katika bahari pana ya uandishi hutishwa na maji marefu. Huogopa papa na nyangumi wasijue kuwa maji hayabagui.

Mawimbi pia huwatisha wengi wakabaki tu kuchungulia. Je, ni nani asiyejua kuwa mchungulia baharini si msafiri? Sote twajua kuwa penye mawimbi ndipo penye milango – milango ya baraka belele.

Kuandika kwahitaji utafiti na utafitafi mwingi, kusomasoma kwingi na mazoezi mengi ya uandishi. Masuala chungu nzima ya kuandikwa yanajianika katika jamii yetu kila siku. Yatumie kuvitunga visa kwa ubunifu. Soko ni kubwa. Wajibika, jitume na mambo yatajipa.

Siri kubwa ya mafanikio ni kujitolea sabili katika uchapakazi. Kataa ugoigoi na uzembe. Kumbatia bidii ili ufue dafu katika hicho unachokifanya.

Upekee ni muhimu sana katika uandishi. Zama hizi kunao ukuruba mkubwa baina ya kazi zilizochapishwa awali, zichapishwazo na labda zijazo. Huko ni kuonesha jinsi uigaji wa kikasuku unavyotutawala katika ulingo wa uandishi. Nadhani chanzo cha hayo ni tamaa.

Tamaa ya kutaka kuwa jina kubwa kabla ya wakati kuwadia. Tamaa ya kutaka kukimbia kabla ya kutambaa. Tamaa ya kujiweka kwenye hadhi ya juu kabla ya kupanda ngazi hatua kwa hatua.

Kabla ya kuandika, jiulize wataka kuandika nini? Wataka kuandikia nani? Wataka kuandika vipi? Wataka kuandika kwa sababu gani?

Huu ndio ushauri wa Bi Tabitha Mawia Manzi – mwanafasihi chipukizi na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Chuo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Ualimu cha Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

MAISHA YA AWALI

Manzi alizaliwa mnamo Mei 20, 1996 katika kijiji cha Ngungani, eneo la Mwingi, Kaunti ya Kitui. Ndiye mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bi Rosemary Manzi na Bw Timothy Manzi.

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Ngungani alikosomea kati ya 2001 na 2006 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya St Francis Kamuwongo Academy, Kitui mnamo 2007 akiwa mwanafunzi wa darasa la tano.

Alama nzuri alizozipata katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo 2010 zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya Kangaru Girls, Kaunti ya Embu mnamo 2011. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwishoni mwa mwaka wa 2014. Manzi alisomea ualimu (Kiswahili na Dini) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya Septemba 2015 na Julai 2019.

Zaidi ya wazazi wake, mwingine aliyemshajiisha maishani na kumhimiza ajitahidi masomoni ni kaka yake Bw Christopher Kitheka ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Nyanyaa, Kitui.

Manzi anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa na aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili katika shule ya msingi, Bw Michael. Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na Bi Kalange wa Kangaru Girls pamoja na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Hawa ni pamoja na Dkt Hamisi Babusa, Dkt Miriam Osore, Dkt Timothy Arege, Dkt Joseph Gakuo, Dkt Jacktone Onyango, Prof Kitula King’ei na Prof Ireri Mbaabu.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa sasa na Manzi katika Kiswahili umechangiwa pakubwa na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao ni wabobevu na wapenzi kindakindaki wa lugha hii.

UALIMU

Kabla ya kuajiriwa na Chuo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Ualimu cha Kitengela mnamo Januari 2020, Manzi alikuwa pia amefundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mwihoko, eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kati ya Januari na Aprili 2019.

Anashikilia kwamba, kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote hutegemea mtazamo wake kuhusu somo husika na mwalimu anayemfundisha darasani.

UANDISHI

Manzi anaamini kuwa safari yake ya uandishi ilianza alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Ni katika kipindi hicho ambapo nyingi za insha alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa kutoka kwa walimu wake wa Kiswahili.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango na ngazi mbalimbali kiasi cha kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, Manzi anajivunia kuandika na kuchapishiwa hadithi fupi kadhaa katika diwani mbalimbali. Ameshiriki pia uhariri wa kazi kadhaa za kibunifu za mwandishi Dominic Maina Oigo pamoja na kitabu cha Gredi ya Nne kilichoandikwa na Dkt Arege mnamo 2019 kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC).

Baadhi ya hadithi ambazo Manzi amechangia vitabuni ni ‘Kifo cha Rehema’ katika diwani ya ‘Kilele cha Mambo na Hadithi Nyingine’ iliyochapishwa na African Ink Publishers, ‘Msafiri’ katika diwani ya ‘Mapenzi ya Pesa na Hadithi Nyingine’ iliyochapishwa na Williams Publishers Ltd na ‘Hali Yangu’ katika mkusanyiko wa ‘Siwezi Tena na Hadithi Nyingine’ uliofyatuliwa na Chania Publishers.

Hadithi nyinginezo ni ‘Wema Hauozi’ katika diwani ya ‘Mtoto wa Dhahabu’ iliyochapishwa na Bestar Publishers na ‘Bamkwe’ katika diwani ya ‘Mkaguzi wa Shule na Hadithi Nyingine’ iliyotolewa na kampuni ya Education Distinction. Ameandika pia kazi nyingi bunilizi zitakazochapishwa hivi karibuni.

Mbali na Bw Oigo na Bw Timothy Omusikoyo Sumba, mwingine aliyemwamshia Manzi ari ya kutunga kazi za kibunifu kwa Kiswahili ni marehemu mjomba wake, Bw Eric Kyallo. Wengine ni Bi Viola Wambui na Bi Linah Ntinyari waliokuwa wanafunzi wenzake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

DRAMA

Zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wake, Manzi amekuwa akiwashirikisha wanafunzi hao wa kiwango cha stashahada (PTE) na diploma (DTE) katika mashindano mbalimbali ya kuigiza.

Yeye mwenyewe aliwahi kushiriki mashindano mengi ya muziki na drama akiwa mwanafunzi wa shule ya upili na akaongoza Kangaru Girls kutawazwa mabingwa wa kitaifa katika tamasha hizo kati ya 2012 na 2014.

Chini ya uelekezi wa Bi Kalange, Manzi alishiriki pia mashindano ya kutoa hotuba na akawa miongoni mwa wanafunzi walioigiza riwaya ya ‘Kidagaa Kimemwozea’ (marehemu Prof Ken Walibora) iliyowahi kutahiniwa katika shule za sekondari nchini Kenya kati ya 2014 na 2017.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, mwandishi maarufu na mhadhiri wa chuo kikuu, Manzi anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala waandishi wengi chipukizi ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya Kiswahili.

GWIJI WA WIKI: Dkt Alexander Rotich

Na CHRIS ADUNGO

USHIKWAPO shikamana na ukiitwa itika.

Usiposhikamana unaposhikwa, anayekushika mkono atachoka na atakuachilia.

Mwishowe utapotea njia, utaanguka na kujuta!

Usipoitika unapoitwa, anayekuita atatamauka na atakupuuza kabisa utakapomhitaji asikie kilio chako ili akuauni!

Kuwa na malengo maishani na uziwanie fursa adimu utakazozipata za kukupigisha hatua kitaaluma. Wapuuze wasiokutakia mazuri, kuwa mtu mwenye msimamo na ushindane na wakati badala ya binadamu wenzako!

Amini kwamba hakuna kisichowezekana, jitume katika safari ya kufanikisha maazimio yako na umtangulize Mungu katika kila jambo!

Huu ndio ushauri wa Dkt Alexander Kipkemoi Rotich – mwalimu mzoefu, mlezi wa vipaji na Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kabianga.

Maisha ya Awali

Rotich alizaliwa mnamo Septemba 9, 1965 katika kata ya Kimuchul, eneo la Chemaner, Kaunti ya Bomet. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto 18 wa Mzee Jonhstone Kiprotich Tuwei na wake zake wawili – Bi Rebecca Chebet na Bi Zipporah Tuwei.

Rotich alianza safari ya masomo katika Shule ya Msingi ya Kimuchul mnamo 1972. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mwishoni mwa 1979.

Alifaulu vyema na kupata nafasi katika Shule ya Upili ya Christ The King, Kaunti ya Nakuru alikosomea kati ya 1980 na 1981 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Tengecha, eneo la Kapkatet, Kaunti ya Kericho mnamo 1982.

Kati ya masomo yote aliyoyafanya Rotich katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCE) mnamo 1983, Kiswahili ndicho kiliongoza. Ingawa alipata nafasi katika Shule ya Upili ya Kabianga kwa minajili ya kiwango cha A-Levels, alihiari kusomea katika Shule ya Upili ya Tengecha kati ya 1984 na 1985.

Anakiri kuwa ilhamu yake ya kukichapukia Kiswahili ilichangiwa na baadhi ya wanafunzi waliomtangulia kimasomo katika Shule ya Upili ya Tengecha, akiwemo Prof John Habwe – mwandishi maarufu wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Ualimu

Rotich alijitosa katika ulingo wa ualimu baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Sita (KACE). Alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya Chemaner mnamo 1986 kabla ya kuhamia katika Shule ya Upili ya Merigi, Bomet alikohudumu kati ya 1987 na 1988.

Ilikuwa hadi Mei 1989 ambapo alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kisii. Alifuzu katika mwaka wa 1991 na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ikamtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya St Michael’s Bomet.

Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kupata uhamisho hadi Shule ya Upili ya Mulot, Bomet (1993-1996) kisha Shule ya Upili ya Chemaner (1996-1997).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Rotich msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea shahada ya kwanza katika ualimu (Kiswahili na Dini) kati ya 1998 na 2001.

Baada ya kuhitimu, TSC ilimtuma katika Shule ya Upili ya Kapsimbiri, Bomet. Alifundisha huko hadi 2005 kabla ya kurejea katika Chuo Kikuu cha Moi kusomea shahada ya uzamili huku akifundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Mosoriot, Kaunti ya Nandi.

Alifuzu katika mwaka wa 2009 baada ya kuwasilisha Tasnifu ‘Nyimbo za Watoto wa Shule za Chekechea na za Msingi katika Manispaa ya Bomet: Uchunguzi wa Kiuamilifu’ chini ya uelekezi wa Prof Issa Yusuf Mwamzandi na marehemu Dkt Hannington Oriedo.

Rotich amewahi pia kufundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kericho (2008-2013). Akiwa huko, alikuwa pia mhadhiri wa muda katika Chuo Kikuu cha Moi, Bewa la Kericho.

Alianza kusomea shahada ya uzamifu (phD) katika Chuo Kikuu cha Moi mnamo 2010 na akaajiriwa na Chuo Kikuu cha Kabianga miaka mitatu baadaye.

Alifuzu mnamo 2018 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Simulizi za Unyanyapaa Unaohusiana na Virusi vya Ukimwi katika Nyimbo za Kenya baada ya Usasa”. Wasimamizi wake walikuwa Prof Mwamzandi na Dkt Mark Mosol Kandagor aliyechukuwa nafasi ya marehemu Prof Naomi Luchera Shitemi aliyeaga dunia mnamo 2013.

Rotich alipanda daraja kuwa Mhadhiri mnamo 2019 na kwa sasa analenga kukwea ngazi za elimu na kuwa Mhadhiri Mwandamizi na kuweka hai matumaini ya kuwa Profesa wa Kiswahili.

Uandishi

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Rotich akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Insha nyingi alizoziandika wakati huo zilimvunia tuzo za haiba kutoka kwa walimu wake.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi ya kizalendo yaliyofana katika mashindano ya viwango na ngazi mbalimbali na kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, Dkt Rotich anajivunia kuandika na kuchapishiwa makala kadhaa ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Ameshiriki pia uandishi wa kitabu cha Gredi ya Tano katika lugha za Kikalenjin kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC).

Uanachama

Dkt Rotich ni mwanachama kindakindaki wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU). Vyama hivi vimempa majukwaa mwafaka ya kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti, ufundishaji na matumizi ya Kiswahili.

Tangu 2017, Dkt Rotich amekuwa Afisa wa Mahusiano Bora wa CHAKAMA–Kenya na yuko mstari wa mbele kuwalea wanachama wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kabianga (CHAKIKA) kwa ushirikiano na Dkt Mohamed Ramadhan Karama, Dkt Emmanuel Simiyu Kisurulia na Prof Mwamzandi.

Katika mengi ya makongamano ya CHAKIKA na Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA), Dkt Rotich amekuwa akitoa ushauri wa kitaaluma kwa wanafunzi na kuwahimiza walimu wenzake kuchochea kasi ya malengo mahususi ya kukuza Kiswahili katika nyanja za ufundishaji, utafiti na uandishi.

Huduma kwa jamii

Dkt Rotich ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Usimamizi wa mojawapo ya shule katika Kaunti ya Bomet na ni mwanachama wa Bodi ya Usimamizi katika shule moja katika kaunti hiyo.

Uzoefu ambao Dkt Rotich anajivunia katika ufundishaji umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kupigia chapuo Kiswahili, kuhamasisha walimu na kuwaelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka za kujikuza kitaaluma.

Jivunio

Dkt Rotich anaistahi familia yake inayozidi kuiwekea kazi yake mshabaha. Kwa pamoja na mkewe Bi Rachael Rotich, wamejaliwa watoto watatu – Winnie Chepkorir, 30, Harriet Chepng’eno, 24 na Collins Kiplang’at, 17.

Dkt Rotich anajivunia wazazi wake waliojihini mengi na wakajitolea kumsomesha licha ya panda-shuka za kila sampuli. Anatambua pia upekee wa mchango wa walimu wake wa awali ambao walimpokeza malezi bora ya kiakademia, kumzibia pengo la shaka na kumchochea pakubwa kitaaluma baada ya kutambua uwezo wake katika Kiswahili.

Hawa ni pamoja na Bw William Sanga, Bw Samuel Kirui, Bw Japhet Chirchir, Bw Gwachi Mayaka, Prof Clara Momanyi na marehemu Clement Busolo. Wengine ni Dkt Allan Lennox Opijah, Prof Nathan Oyori Ogechi na marehemu Davies Muthondu Mukuria.

Dkt Rotich anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi ambao amewafundisha katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

GWIJI WA WIKI: Hussein Kassim

Na CHRIS ADUNGO

USHAURI si ushauri iwapo hautaleta athari chanya katika maisha ya mtu. Iwapo nasaha haimtafaa yeyote, basi nathubutu kusema kuwa huwa ni maneno shinikizi tu. Ashakum si matusi, labda niseme, hiyo huwa porojo!

Kwa yeyote anayetaka kujipa ridhaa ya moyo, basi asichoke kukikumbatia na kukipenda kwa dhati kitu hicho kimoja kinachomridhisha nafsi. Akifuate na kukihangaikia kwa jinsi yoyote iwayo ile, yaje masika au kiangazi!

Aonekane kama ambaye kapagawa kwa namna fulani. Kwanza, aanze kuzoeleka na jamaa zake wa karibu na hata rafikize kwamba kitu hicho ndiyo hewa apumuwayo kila uchao. Kisha, anasibishwe na kitu hicho kokote aendako. Kitajwapo kitu hicho popote, mabongo ya waja yawe yanapata taswira ya fulani huyo – tena na tena na tena, bila kuchoka!

Mwisho wa kwisha, atakuwa amepata mwao na mbinu ya kujipenyeza hadi waliko watu waliofaulu. Siri za kufaulu ni mbili tu – kifanye hicho ukipendacho bila ya kuchoka wala kutamauka na upanie kupata ridhaa na faraja ya moyo kila unapokifanya kitu hicho!

Huu ndio ushauri wa Bw Hussein Kassim almaarufu Bongo Pevu – mtaalamu wa masuala ya afya, mhariri, mtafsiri na mshairi anayeinukia vyema katika uandishi wa Fasihi ya Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Hussein alizaliwa mnamo 1994. Ndiye mwanambee katika familia ya Bw Kassim Mukanda ya wana watano – Suleiman, Mustafa, Leila na Suheila katika usanjari huo. Alilelewa na kupata masomo yake ya awali katika kijiji cha Eshiakhulo kilichoko katika eneo la Mumias Mashariki, Kaunti ya Kakamega.

Hussein alisomea katika shule mbili tofauti za upili – Mumias Boys Muslim (Kakamega) na Laiser Hill Academy (Kaunti ya Kajiado). Alijiunga baadaye na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa kwa masomo ya Shahada ya Kwanza katika taaluma ya Afya ya Jamii na akahitimu mwaka wa 2019.

Mtu wa awali kabisa kuiotesha mbegu ya mapenzi ya Kiswahili ndani yake alikuwa mwalimu Violet Vinaywa aliyemfundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Eshiakhulo. Wengine waliopalilia mche ule na kuwa mti maridadi ni Bi Linah Achieng na Bw Paul Byattah Nambwaya waliomchochea kwa kiwango kikubwa walipokuwa wakimpokeza malezi ya kiakademia katika shule ya msingi.

Marehemu Profesa Ken Walibora! (Roho yake ilazwe pema penye wema.) Alikuwa chanzo kikuu cha mapenzi ya Hussein kwa lugha hii ashirafu ya Kiswahili.

Itakuwa si haki kutotaja na kutambua juhudi za Bw Kassim (babaye) ambaye amemshika mkono siku zote kuhakikisha kuwa anazidi kuvipanda vidato vya mafanikio katika safari ya maisha.

Hakuwahi kuchoka wala haelekei kufanya hivyo, akiwa na matumaini kuwa mwanawe atakuja kuwa mtu wa maana sana katika jamii. Humwamini mwanawe siku zote na anazidi kumlea kwa misingi ya kumcha Mungu na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo.

Bw Kassim ni miongoni mwa watu waliomshajiisha Hussein maishani, kumhimiza ajitahidi masomoni na kumwelekeza ipasavyo katika kila hatua.

MCHANGO KITAALUMA

Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu, Hussein tayari ameshaanza kujihusisha na taaluma yake, ingawa bado hajaajiriwa. Kwa kutumia kipaji chake cha uandishi, amepiga hatua kubwa sana ya kuoanisha talanta na taaluma aliyosomea kwa kuchapisha kitabu cha mashairi ‘Diwani ya Maradhi’.

Ingawa hiki ni miongoni mwa vitabu vingi alivyoandika mnamo 2020, anajivunia sana kazi hii kwa kuwa wazo la kuiandaa lilitoka mvunguni mwa moyo wake. Anaamini kuwa kitabu hicho kitapiga hatua na kuifaa jamii pakubwa mno.

Vitabu vingine alivyoshiriki kuandika katika mwaka wa 2020 ni mikusanyiko ya hadithi fupi ‘Mapenzi ya Pesa’, ‘Shaka ya Maisha’, ‘Makovu ya Moyoni’, ‘Harusi ya Kiharusi’ na ‘Kuku Ameshinda Kura’. Bila shaka, hakuupoteza mwaka huo kama walivyolalama watu wengi duniani kutokana na janga la korona. Ilikuwa fursa yake ya kutamba, naye akaitumia vizuri sana!

Hussein amefanya na anazidi kufanya mambo makuu ili kuikuza lugha hii adhimu ya Kiswahili pamoja na fasihi yake. Mbali na uandishi wa vitabu, pia anafanya tafsiri na ufasiri (Kiingereza-Kiswahili). Umilisi wake wa lugha hizi mbili ni wa kipekee.

Mbali na kuhariri vitabu na makala kwa malipo ama kwa kujitolea tu, yeye ni huendesha masimulizi ya visa kwenye YouTube (Bongo Pevu TV).

Kwa kuwa hakufaulu kuutalii taaluma ya uanahabari, anajifunga kibwebwe kuhakikisha kuwa anafanya mazoezi katika ulingo huo kwa lengo la kuiridhisha nafsi yake.

Anaishi kwa imani kwamba mvuto na mguso wa kipekee uliomo ndani ya mrindimo wa sauti yake utakuja kuwa kitambulisho chake atakapokuwa mwanahabari – taaluma ambayo amekuwa akiiotea tangu utotoni.

Zaidi ya kuandika makala ya kuburudisha na kuelimisha kwenye kaunti ya mtandao wake wa kijamii wa Facebook (Hussayn Qassym), Hussein ni mwanablogu anayeshiriki na kuchangia mijadala mingi ya kitaaluma kupitia vipindi vya redio, runinga na kumbi za Kiswahili mitandaoni.

Anapojitahidi katika ulingo wa uandishi na kuihangaikia taaluma aliyosomea, Hussein amezamia kwa sasa masuala ya biashara ambayo humpa tonge la kila siku.

Anayajaribia maisha biasharani akingoja mlango wa heri ufunguke katika kozi aliyoisomea. Hupata pia fungu la riziki yake kwa kutafsiri katiba, nyaraka na stakabadhi za vyama na mashirika mbalimbali ya humu nchini. Uwezo wake huu umemwezesha kukidhi mengo ya mahitaji yake ya kila siku.

MAAZIMIO

Hussein anaazimia kuvikwea vidato vya uandishi na kuwa miongoni mwa watunzi stadi wa kazi za kitaaluma na bunilizi.

Anapania kuwa kielelezo na mfano wa kuigwa na vijana wenzake ili hatimaye aache jina zuri duniani – atajwe kwa uzuri kama wanavyotajwa mabingwa na mikota wa Kiswahili waliotenda wema kabla ya kufunga safari isiyo na marejeo.

JIVUNIO

Hussein anamstahi sana babaye mzazi, Bw Kassim. Humwombea dua siku zote azidi kuwapo ili aendelee kumfaa. Pia anajivunia watu wengine wa familia yake wanaomwamini siku zote kama vile Imran Hussein, Mustafa Kassim, Rashid Mohammed, Ramadhan Wesonga na Abdul Fibanda.

Pia anajivunia kuwa na marafiki adhimu wanaozidi kumfaa. Hawa ni pamoja na Sylvia Amunga, Suleiman Ofutumbo, Eunniah Mbabazi, Mturi Katana, Nyagemi Nyamwaro Mabuka, Timothy Sumba, Richard Amunga na wengineo wengi.

Hussein amekuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi, wanahabari na walimu ambao wametangamana naye katika warsha na makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo Kiswahili.

Isitoshe, anajivunia kuwashika mikono baadhi ya rafikize, nao wakatia bidii na kupiga hatua kubwa maishani. Kama alivyoshikwa mkono naye akafika alipofika, amefanya juhudi kuwainua wenzake. Miongoni mwao ni Juma Patrick Kurwa, Dorcas Asianut, Emily Gatwiri na Diana Muhandachi.

GWIJI WA WIKI: Rose Okelo

Na CHRIS ADUNGO

KIZURI unachokifikiria ndicho utakachokipata.

Kipende kwa dhati hicho unachokifanya na namna unavyokifanya. Usifanye jambo kwa sababu wengine walilifanya au wanalifanya. Upekee wa mtu ndio ubora wake!

Mwalimu anayeyachangamkia majukumu yake na kulishabikia somo lake huwa kielelezo na mfano wa kuigwa miongoni mwa wanafunzi wake.

Marafiki wanaweza kukujenga au kukubomoa. Teua marafiki wema wenye fikira na uwezo wa kukutoa hapa na kukufikisha pale katika safari yako ya ufanisi. Fanya hivyo ili ufike mbali!

Mwanafunzi anayekubali kuongozwa na kuelekezwa ndiye hufaulu. Anastahili kufahamu uzito wa mzigo aliojitwika na awajibike kuubeba.

Mjenzi bora hujifunza ujenzi akaboreka hata zaidi. Mwandishi husoma kazi za watangulizi wake ndipo awe stadi na hodari kabisa. Huwezi kuwa mwalimu kabla ya kuwa mwanafunzi!

Huu ndio ushauri wa Bi Rose Katiba Okelo – mlezi wa vipaji, mwigizaji hodari na mwandishi wa vitabu ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya The Kenya High, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Rose alizaliwa mnamo 1968 katika eneo la Gwassi, Suba Kusini, Kaunti ya Homa Bay. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa Bi Christine Katiba na marehemu Bw Charles Katiba.

Mbali na Doreen Achia ambaye ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo za injili, ndugu wengine wa Rose ni walimu kitaaluma. Hawa ni Mary Ojuka (Orero, Homa Bay), Deborah Onyango (Nyangubo, Kaunti ya Migori) na Richard Katiba (Kitawa, Homa Bay).

Rose alianza safari yake ya elimu mnamo 1974 katika Shule ya Msingi ya Shimo la Tewa, Mombasa. Alijiunga baadaye na Shule ya Msingi ya Kiabuya, Homa Bay alikosomea kwa mwaka mmoja (1975) kabla ya kurejea Shimo la Tewa kati ya 1976 na 1980.

Alifanya vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Coast Girls, Mombasa kati ya 1981 na 1984. Baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCE), aliendeleza masomo ya kiwango cha ‘A-Level’ katika shule hiyo ya Coast Girls kati ya 1985 na 1986.

Rose alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kagumo, Kaunti ya Nyeri mnamo 1988 na akahitimu katika mwaka wa 1990. Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Fasihi ya Kiingereza) kati ya 1995 na 1999.

Rose anatambua ukubwa wa mchango wa babaye mzazi katika kumlea kwa kumcha Mungu, kumhimiza masomoni, kumshajiisha maishani na kumwelekeza katika mkondo wa nidhamu kali. Miongoni mwa walimu waliomchochea kukichangamkia Kiswahili ni Bi Buko, Bi Ali na Bw Kachila waliotangamana naye kwa karibu sana katika Shule ya Upili ya Coast Girls.

Anakiri kwamba uamuzi wa kuzamia taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa mno na Bi Florence Mukuzi (marehemu) aliyempokeza malezi bora ya kiakademia katika Shule ya Msingi ya Shimo la Tewa.

UALIMU

Baada ya kukamilisha masomo ya A-Levels mnamo 1986, Rose alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Dzitsoni, eneo la Chonyi, Kaunti ya Kilifi.

Aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya Kahuhia Girls, Kaunti ya Murang’a kwa kipindi kifupi kabla ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kumtuma katika Shule ya Upili ya Matuga Girls, Kaunti ya Kwale.

Alihudumu huko kati ya Mei 1990 na Mei 1991 kabla ya kuhamia katika Shule ya Upili ya Luora, Homa Bay alikofundisha hadi Juni 1994 akiwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili.

Rose alifundisha katika Shule ya Upili ya Upper Hill, Nairobi (Julai – Septemba 1994) kabla ya kuelekea Nairobi School (Septemba 1994 – Disemba 2018). Ilikuwa hadi Januari 2019 alipojiunga na Shule ya Upili ya The Kenya High.

Rose amekuwa mtahini wa kitaifa wa Karatasi ya Pili ya Kiswahili (102/2 Matumizi ya Lugha) tangu 1992. Uzoefu anaojivunia katika utahini umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kupigia chapuo Kiswahili, kuhamasisha walimu na kuwaelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa Mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha Nne (KCSE).

Tangu 2004, amekuwa mwanajopo katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaala ya Kenya (KICD) akishughulikia utayarishaji wa nyenzo za kufundishia.

Mbali na kushiriki vipindi vya uchambuzi wa vitabu teule vya fasihi vinavyotahiniwa katika shule za sekondari nchini Kenya, Rose pia amekuwa katika mstari wa mbele kufyatua kanda za video kwa minajili ya mafunzo ya mitandaoni kupitia EDU TV Channel.

DRAMA

Zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili katika shule zote ambazo amefundisha, Rose amekuwa akiwashirikisha wanafunzi wake katika mashindano mbalimbali ya kuigiza.

Aliwahi kuwa Mlezi wa Chama cha Drama cha Nairobi School (2007-2018) na akaongoza waliokuwa wanafunzi wake shuleni humo kutawazwa mabingwa wa kitaifa wa tamasha za drama mnamo 2008 wakiigiza mchezo wa Forty Minutes uliotungwa na Bw Nelson Ashitiva.

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Rose tangu alipojitosa katika ulingo wa ualimu. Kariha na ilhamu zaidi ya kuandika ilichochewa na waliokuwa wanafunzi wake Nairobi School.

Mbali na Bw Ben Wafula, mwingine aliyempigia Rose mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na kumpa motisha ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi wa vitabu vya Kiswahili ni Mkurugenzi wa One Planet Publishers, Bw Kithusi.

Rose alishirikiana na Bw Wafula kuandika kitabu KCSE Homestretch Udurusu na Mitihani ya Kiswahili kilichochapishwa na One Planet mnamo 2014.

Kwa sasa anaandaa miswada ya hadithi fupi za Kiswahili kwa matarajio kwamba kazi hizo zitachapishwa hivi karibuni. Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuandika kazi za ushauri nasaha kwa Kiswahili.

JIVUNIO

Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Rose amefundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali nchini.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika hafla mbalimbali za makuzi ya Kiswahili.

Rose aliwahi kuchangia mijadala ya kitaaluma kupitia vipindi ‘Kiswahili Kitukuzwe’ (2004-2010, KBC TV) na ‘Kamusi ya Changamka’ (2004-2005, QFM na QTV).

Kwa pamoja na mumewe Bw James Okelo, wamejaliwa watoto watano – Jan Okelo, 28, Sydney Katiba, 27, John Okelo (marehemu), Ben Ambrose, 20, na Beavan Okelo (marehemu). Rose anawastahi sana wajukuu wake – Jamal Kumu na Waridi Katiba.

GWIJI WA WIKI: Geoffrey Mung’ou

Na CHRIS ADUNGO

MSIMAMO ni mhimili wa ufanifu; usiwe bendera ya kufuata upepo.

Msimamo kuhusu yaliyo na mantiki – si upotoshi. Tabasuri na uandame mkondo wenye tija, ukupao maarifa, kisomo pia kipato!

Kulaza damu na kupenda anasa ni ubatili…ubatili wa kuhiliki, halafu majuto na vilio vya mbwa mdomo juu!

Msingi wa yote, mtegemee aliyekuhuluku (Mungu); ambaa makatazo na utii maagizo yake. Kutenda mema kwazaa mema. Kutenda mawi kwazaa mawi! Adui mpende, ila usile akupacho. Usitie fundo moyoni. Maudhi ya leo yaishe leo; ukilia leo, cheka kesho na ugange yajayo!

Huu ndio ushauri wa Bw Geoffrey Mung’ou (Simba) – mwalimu, mwanahabari, mhariri na mwandishi mbobevu wa vitabu vya Kiswahili.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Maisha yangu ya awali yalikuwa ya kifaranga ambaye usingejua kwamba angekuwa jogoo. Nililelewa na wazazi wakali kama simba; waliadilisha kwa mijeledi. Nami nikajua kujituma, kuthamini utiifu, utu, bidii na ucha Mungu. Marehemu mama (mzawa wa Seguton, Baringo) hakunilea kwa mikate ya siagi. Nilikulia vijijini, kupeleka mifugo malishoni na mtoni kuwanywesha maji vilevile kuwasaidia wazazi katika kazi za shambani.

Nilichana mbuga miguu mitupu kule vijijini Elgon kama kilomita tano kila siku, kwenda na kutoka shuleni. Mwanzoni, nilijiokotaokota tu kimasomo kwa kutomakinika, sikwambii sarakasi za kila nui za utotoni. Nisingekosa ‘kumfungia mtu shule’ na kupewa noma (disk) hata mara mia kwa kuzungumza lugha ya kwanza.

Ndoto yako ya uanahabari ilianza lini?

Tangu chekechea, nilikuwa kasuku wa kuwaiga watangazaji wa ndani na nje ya nchi. Wazazi wangu walipenda sana kusikiliza habari. Hapo ndipo ndoto ya utangazaji iliponijia. Nikawa nawatumbuiza wanafunzi wenzangu kwa kuwasomea taarifa ya habari na kubadilibadili sauti iwiane na ya mtangazaji huyu au yule. Kufikia darasa la saba, nilikuwa moto wa kuotea mbali!

Ulisomea wapi?

Safari yangu ya elimu ilianzia Shule ya Msingi ya Kapsokwony, Elgon. Nilianza kujielewa kimasomo nilipofikia darasa la saba. Nikawa kidedea hadi sasa. Nilifanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika Shule ya Msingi ya Kibuk. Nilifaulu vyema kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Cheptais, halafu Shule ya Wavulana ya Kimilili nilikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Sekondari (KCSE). Niliweka rekodi ya kupata gredi ya ‘A’ tena ya pekee katika somo la Kiswahili shuleni humo, mnamo 2001. Halafu nikajiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea Shahada ya Ualimu. Lisingekuwa janga la UVIKO-19, ningehafili mwaka wa 2020 katika shahada ya uzamili, kisha nizamie uzamifu. Ndiyo mipango yangu ya mwakani, Inshallah!

Nani aliyekuchochea kujitosa katika ulingo wa uandishi wa vitabu?

Ni miaka ayami sasa tangu niotee ndoto tasnia hii; angaa nami nitie guu…nitembee mumo kwa mumo. Kwa umbuji, niibue tungo adhimu, zitue machoni pa wasomaji na kukubalika katika nyoyo zao. Nilikuwa kidato cha pili ambapo ilhamu ya kuwa mwandishi ilinijia baada ya kuisoma riwaya ya kusisimua ya ‘Siku Njema’ ya Ken Walibora (kwa mauko yale, Dayani ni mlifi!)

Mgomo wa wahadhiri uliochukua muda mrefu nilipokuwa chuoni ulinipa fursa ya kudariji mswada wa ‘Mkakasi’. Mashallah! Ndoto ikatimia punde baada ya Bw Ochoi wa Jomo Kenyatta Foundation (JKF) kuupitia mswada wenyewe ulionichukua miaka mitano hivi kuuandika, na mingine minne ya kujaribu kuwafikia wachapishaji. Baadhi walinipuuza; baadhi hawakunijibu, baadhi wakaniweka katika ngojangoja. Wiki moja tu baada ya Bw Ochoi kutia kiganjani ule mswada, akanipigia simu na kuniambia hivi, “Tutachapisha. Kwa hakika ni mswada mzuri!” Sauti ile ingali hai masikioni mwangu hadi leo. Iliamsha ile ilhamu. Nikanuia kuchovya asali tena na tena katika buyu hili la uandishi.

Umechapishiwa vitabu vingapi kufikia sasa?

Vingi tu. Mnamo 2013, novela ya ‘Falme Tisa’ (Oxford) yenye falsafa tele ilifuata. Huachi ng’o uanzapo kuisoma! Kabla ya kuchapishiwa novela ya ‘Ufalme wa Mende’ (Queenex), kalamu yangu ikawa tayari imetia vitabuni hadithi nyingine – ‘Raha za Peponi’ katika mkusanyiko wa ‘Kigoda cha Simanzi na Hadithi Nyingine’, vilevile ‘Safari ya Ahadi’ katika mkusanyiko wa ‘Safari ya Ahadi na Hadithi Nyingine’ (One Planet), kutaja tu baadhi.

GWIJI WA WIKI: Dkt James Ontieri

Na CHRIS ADUNGO

KUFAULU katika jambo lolote ni zao la jitihada, nidhamu, imani na stahamala.

Siri ya kuwa mwalimu bora ni kutawaliwa na upendo wa dhati kwa taaluma, kuchangamkia masuala yanayohusiana na mtaala na kuwa mwepesi wa kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji.

Hakuna mafanikio utakayoyapata bila ya kujituma. Shindana na wakati, jiwekee malengo mapya ya mara kwa mara na uzoee kuangusha jasho ndipo upate.

Hatua ya kwanza katika safari yoyote ya mafanikio ni kufahamu kile unachokitaka, kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unakokwenda. Jiamini, jikubali na ukatae maisha ya kujihukumu.

Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga na uwe na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika mambo unayoyafanya.

Huu ndio ushauri wa Dkt James Ontieri – msomi wa isimu, mhariri shupavu, mtafiti stadi, mwandishi mahiri, mwanataalamu msifika na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Rongo, Kaunti ya Migori.

MAISHA YA AWALI

Ontieri alizaliwa mnamo 1970 katika kijiji cha Nyabiosi, eneo la Keumbu, Kaunti ya Kisii. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto kumi na mmoja wa Bw Benedicto Omari na Bi Hellen Nyang’ara.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Nyabiosi mnamo 1976. Alisomea huko hadi 1978 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Kamwaura, eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru mnamo 1979. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mwishoni mwa 1982.

Alifaulu vyema katika mtihani huo na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Mong’oni, Kaunti ya Nyamira kati ya 1983 na 1986. Alijiunga baadaye na Shule ya Upili ya Nyambaria, Kaunti ya Nyamira kwa minajili ya masomo ya kiwango cha ‘A-Levels’ mnamo 1987 na akafanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Sita (KACE) katika mwaka wa 1988.

Mnamo 1989, Ontieri alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Historia). Alihitimu mwishoni mwa 1992.

Miongoni mwa wahadhiri waliompokeza malezi bora ya kiakademia na kumtandikia zulia zuri la kukichangamkia Kiswahili ni Dkt Allan Lennox Opijah, Profesa Said A. Mohamed, marehemu Davies Muthondu Mukuria, marehemu Dkt Hannington Oriedo, marehemu Prof Abel Gregory Gibbe na marehemu Ibrahim Ngonzi.

Wengine waliomchochea pakubwa kwa imani kwamba Kiswahili ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni Prof Isaac Ipara Odeo, Prof Miriam Mwita na Mwalimu Luganda.

Ontieri anakiri kuwa ilhamu zaidi ya kukichapukia Kiswahili ilichangiwa na baadhi ya wanafunzi waliowatangulia kimasomo chuoni, akiwemo Prof Nathan Oyori Ogechi ambaye kwa sasa ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Moi.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Ontieri msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton kusomea shahada ya uzamili katika mwaka wa 2002. Hatua hiyo ilikuwa zao la kuhimizwa pakubwa na Dkt Samuel Obuchi.

Alihitimu mnamo 2005 baada ya kuwasilisha Tasnifu ‘Matumizi ya Lugha katika Magazeti ya Kiswahili mfano Gazeti la Taifa Leo’ chini ya uelekezi wa Dkt John Kimemia na Prof Aswani Buliba.

Ilikuwa hadi 2007 ambapo Ontieri alirejea katika Chuo Kikuu cha Egerton kwa minajili ya kusomea shahada ya uzamifu (PhD). Aliandaa Tasnifu ‘Uchanganuzi wa Makosa katika Insha za Wanafunzi wa Shule za Upili mfano wa Wilaya ya Nakuru’ chini ya uelekezi wa Prof James Onyango Ogola na marehemu Prof Mwenda Mukuthuria. Alifuzu katika mwaka wa 2010.

UALIMU

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Ontieri kufundisha katika Shule ya Upili ya Kamobo, Kaunti ya Nandi mnamo 1993. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Koitalel Samoei, Nandi (1994-1999).

Ontieri aliwahi pia kuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Moi Tea Girls, Kericho (1999-2002) na Kericho Boys High (2004-2008) kabla ya kufundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Murang’a kati ya 2008 na 2009.

Hadi alipojiunga na Chuo Kikuu cha Rongo mnamo Februari 2020, Ontieri alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Kaunti ya Narok. Kabla ya kupanda ngazi kuwa Mhadhiri Mwandamizi mnamo 2015, alikuwa Mhadhiri (2011-2015) na Mhadhiri Msaidizi (2009-2010).

Ontieri amewahi pia kufundisha katika Chuo Kikuu cha St John’s (SJUT), Dodoma, Tanzania (Mei – Agosti 2018) chini ya mradi wa kubadilishana wahadhiri wa Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA).

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Ontieri tangu alipoanza kufundisha. Idadi kubwa ya walimu wenzake walimpigia mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na wakamtia motisha ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Baada ya kuchapishiwa ‘Mwongozo wa Visiki’ (Khaemba Ongeti), Ontieri alishirikiana na Dkt Obuchi kuandika ‘Mwongozo wa Siku Njema’ (Ken Walibora).

Hadi kufikia sasa, Ontieri amechapishiwa makala tisa katika sura za vitabu mbalimbali na kuchangia makala mengine 14 ya kitaaluma katika majarida ya kimataifa.

Mbali na kuwa miongoni mwa wahariri wa ‘Jarida la Mwanga’ (Chuo Kikuu cha Moi) na ‘Jarida la Mnyampala’ (Chuo Kikuu cha St John’s); Ontieri amewahi pia kuwa mhariri wa vitabu mbalimbali vya Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA).

Alishirikiana na Dkt Mark Mosol Kandagor, Dkt Leonard Sanja na marehemu Prof Mukuthuria kuhariri kitabu ‘Kiswahili na Maendeleo’ (2015) kabla ya kushirikiana na Prof Ernest Sangai Mohochi na marehemu Prof Mukuthuria kuhariri kitabu ‘Kiswahili katika Elimu’ mnamo 2019.

UANACHAMA

Ontieri ni mwanachama wa vyama mbalimbali vya Kiswahili vikiwemo Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). Vyama hivi vimempa majukwaa mwafaka ya kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti, ufundishaji na matumizi ya Kiswahili.

Ontieri ameongoza CHAKAMA katika nyadhifa mbalimbali. Amewahi kuwa Afisa wa Ushirikiano (2011-2013), Afisa Mwenezi (2013-2015), Naibu Mwenyekiti (2015-2017) na Mwenyekiti (2017-2019). Tangu 2015, amekuwa Mwenyekiti wa CHAKAMA–Kenya na anahudumu sasa katika Kamati Tendaji ya Afrika Mashariki.

Amewahi pia kuwa Mlezi wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara (2010-2015) na Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kati ya 2017-2019.

Katika mengi ya makongamano ya vyama hivi, Ontieri amekuwa akitoa ushauri wa kitaaluma kwa wanafunzi na kuwahimiza walimu wenzake kuchochea kasi ya malengo mahususi ya kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika; pamoja na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote mathalan uandishi na uchapishaji wa vitabu na majarida.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, Ontieri anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi ambao amewaelekeza katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Baadhi yao ni Bw Aggrey Katima, Bi Fridah Oiko, Bi Martha Nyangweso, mwanariadha Wilfred Bungei, Dkt Mark Odawo, Dkt Stanley Kevogo, Dkt Jackline Ogolla na Seneta wa Kaunti ya Kericho, Aaron Cheruiyot.

Ontieri amewahi pia kuchangia mijadala ya kitaaluma kupitia vipindi vya ‘Bahari ya Lugha’ (Radio Citizen) na ‘Ramani ya Kiswahili’ (KBC Radio Taifa).

Kwa pamoja na mkewe Bi Joyce Kemunto, wamejaliwa watoto watatu – Sylvia Mandere, 24, Sheilah Kwamboka, 22, na Catherine Moraa, 13.

GWIJI WA WIKI: Paskali Watua

Na CHRIS ADUNGO

WENGI wetu huona shida ikiwa na uhasi katika maisha ya mwanadamu.

Hata hivyo, shida ndizo humfanya mtu kuwa mbunifu nao ubunifu ukamfanya mwanadamu aanze kusowerea katika njia ya mafanikio.

Mafanikio nayo huhitaji matumaini na uvumilivu. Bidii, matumaini na stahamala huoana na huhitajiana ili mtu afaulu katika chochote anachokifanya.

Japo tumeaminishwa kuwa bidii na kujituma ni kati ya mambo yanayochangia mafanikio, dhana hii ina ukweli tatanishi kwani, mafanikio ni ubunifu tu unaohitaji akili nyingi na nguvu kiasi. Au wewe, hapo ulipo, umewahi kumwona punda aliyefanikiwa?

Aidha, si kwamba mafanikio huja kama ajali. La hasha! Kati ya vitu vilivyo na uwezo wa kumfaulisha mtu au kumzuia asifanikiwe kabisa, ni fikra zake! Fikra hasi huzaa hasara nazo fikra chanya huzaa ubora. Fikra ni kama mbegu inayopandwa gizani na ikaota mchana wa jua! Hivyo, maisha anayoishi mtu, huwa ni zao la mawazo yake.

Usikate tamaa! Wewe unayepania kufanikiwa, jambo muhimu kwako ni kudumisha matumaini, kujiwekea malengo na kuruhusu fikra chanya zitawale ndani ya ubongo wako. Ukiwa unaazimia kufaulu, ni busara kujenga taswira ya mafanikio yako kwenye fikra na kuyatazama kila leo kwa darubini ya akili kichwani mwako.

Iwapo mafanikio yangekuwa mepesi jinsi baadhi yetu tunavyoyachukulia, basi kufaulu kusingekuwa na maana yoyote!

Huu ndio ushauri wa Bw Paskali Null Watua almaarufu Mwanafalsafa – mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa anasomea Teknolojia ya Mawasiliano nchini Ireland.

MAISHA YA AWALI

Paskali alizaliwa mnamo Februari 16, 1996, katika kijiji cha Matuguta, kata ya Githiga, kaunti ndogo ya Githunguri, gatuzi la Kiambu. Yeye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano wa Bw Stephen Watua na Bi Beatrice Watua. Nduguze Paskali ni Irene Nafuna Watua, Thomas Wadabwa Watua, Jackline Nandudu Watua na Susan Kainza Watua.

Paskali alianza kuhudhuria masomo ya chekechea mnamo 2001 katika Shule Msingi ya Githiga Centre Junior Academy ambayo kwa sasa inaitwa PCEA Githiga Academy, Kaunti ya Kiambu.

Baada ya kusoma kwa kipindi cha mwaka mmoja, alijiunga tena na chekechea ya Shule ya Msingi ya Matuguta, Kiambu mnamo 2002. Alisomea huko kwa miaka miwili kabla ya kujiunga na Darasa la Kwanza katika shule hiyo hiyo.

Paskali alifanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo 2011 na akawa miongoni mwa watahiniwa bora kutoka Shule ya Msingi ya Matuguta na eneo pana la Githunguri.

Ingawa aliitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Gathiruini, Kiambu, uchechefu wa karo ulimnyima nafasi ya kusomea katika shule hiyo maarufu na akalazimika kujiunga na shule ya kutwa ya Gikang’a Kagece, Kiambu mnamo 2012.

Mnamo 2014, aliteuliwa kuwa Naibu Kiranja Mkuu wa maktaba ya shule. Ni katika mwaka huo ambapo alijumuishwa katika kundi la wanafunzi walioshiriki mashindano ya somo la Hisabati katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Githiga, Kiambu.

Aliibuka miongoni mwa wanafunzi bora na akateuliwa kuhudhuria kongamano la wanafunzi katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance, Kikuyu.

Paskali alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2015 na akawa wa pili katika orodha ya mwa watahiniwa waliotia fora zaidi kutoka Shule ya Upili ya Gikang’a Kagece.

Baada ya hapo, aliajiriwa katika duka la jumla jijini Nairobi kabla ya kujiunga na Chuo cha Teknolojia cha Murang’a mnamo 2016. Baada ya mwaka mmoja, safari yake ya masomo ilikatika ghafla kutokana na hali ya mbaya ya kiuchumi ya wazazi wake. Hata hivyo, hakukata tamaa.

Mnamo 2019, Paskali alijiunga na Chuo cha Microsoft Training Academy (MTA) kuendeleza kozi yake ya Teknolojia na Mawasiliano. Kwa sasa, anasoma kwa njia ya mtandao katika chuo hicho cha MTA kilichoko nchini Ireland.

UANDISHI

Zaidi ya kuwa mwanafunzi wa Teknolojia na Mawasiliano, Paskali ni mwandishi wa kazi za kibunifu kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Ingawa kipaji cha uandishi kilianza kujikuza ndani yake akiwa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu mnamo 2014, aliyemchochea zaidi kujitosa katika ulingo wa sanaa ya utunzi ni mwandishi chipukizi raia wa Tanzania, Lovi Pius Kijogoo.

Paskali alianza kwa kuandika mashairi, simulizi na nudhuma za kimapenzi mnamo 2018 huku akizipakia kwenye makundi ya mtandaoni yanayomilikiwa na watunzi wa Tanzania.

Mwaka uo huo, aliandika riwaya mbili – ‘Ngumu Kuelewa’ na ‘Mwisho wa Mwanzo’ ambazo anatazamia zitachapishwa mwaka huu. Paskali pia ameshirikishwa katika utunzi wa mikusanyiko mbalimbali ya hadithi fupi.

Hadithi yake ‘Jinamizi la Uhuru’ ilichapishwa na kampuni ya The Writers’ Pen Publishers, Eldoret katika mkusanyiko wa ‘Shaka ya Maisha na Hadithi Nyingine’ mnamo Julai 2020.

Paskali ndiye mwandishi wa hadithi ‘Kauli ya Mwisho’ katika mkusanyiko wa ‘Harusi ya Kiharusi na Hadithi Nyingine’ uliofyatuliwa na kampuni ya Bestar Publishers mnamo Julai 2020.

Kampuni ya African Ink Publishers imemtolea pia hadithi ‘Shani ya Kiama’ katika mkusanyiko wa ‘Maskini Maarufu na Hadithi Nyingine’ na hadithi ‘Panya Mlafi’ katika antholojia ya ‘Kasuku wa Salome na Hadithi Nyingine’ mnamo Agosti, 2020.

Baadhi ya mashairi yake yamejumuishwa katika ‘Diwani ya Maradhi’ iliyochapishwa na The Writers’ Pen mnamo Agosti 2020.

Kwa sasa anatazamia kampuni ya African Ink imchapishie hadithi ‘Takbiri’ na ‘Samahani Mke Wangu’ katika antholojia ya ‘Mapenzi ya Mwanaharamu na Hadithi Nyingine’ wakati wowote kuanzia sasa.

Paskali amechangia pia mashairi ya Kiingereza katika diwani ya ‘When I Marry Rimanto’ (The Writers’ Pen, Julai 2020) na ‘Shackles Of Pain’ (The Writers Pen, Februari 2020). Zaidi ya hayo, ameandika diwani ya mashairi ya Kiingereza kwa jina ‘Games Of Witches’ iliyochapishwa na Elong’o Publishers mnamo Machi 2019.

Baadhi ya kazi za Paskali zimejumuishwa katika majarida mbalimbali nchini likiwemo Jarida la The Writers’ Pen. Amepokea vyeti na tuzo kadhaa za haiba kubwa kutokana na uandishi wake wa mashairi ya Kiingereza.

Paskali anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali.

Anamstahi pakubwa mkewe Bi Rosa Nyaboke ambaye amekuwa nguzo muhimu katika juhudi zake za kuchapukia sanaa ya uandishi. Kwa pamoja, wamejaliwa mtoto wa kike – Elora Beatrice Watua.

Ni naima kwa Paskali kujumuishwa kati ya magalacha wa kazi za fasihi. Lengo lake kuu ni kushirikiana na wenzake katika kundi la Writers Unity kuwalea na kuwakuza chipukizi wanaoibukia katika uandishi wa kazi bunilizi na kuwashirikisha katika mashindano mbalimbali ya fasihi.

GWIJI WA WIKI: Emily Gatwiri

Na CHRIS ADUNGO

MAFANIKIO ni zao la bidii, imani na stahamala.

Usipoteze dira ya maono yako maishani hata unapokumbana na changamoto. Kuwa na matumaini hata pale ambapo mambo yanakwenda kinyume na matarajio yako na uvute subira kwa imani kwamba siku njema itafika.

Mtangulize Mungu katika kila hatua ya maisha, kuwa radhi kuwajibikia matendo yako na ukipende hicho unachokifanya kwa moyo wa dhati.

Kipimo cha mafanikio ya mtu si utajiri wa mali na wingi wa fedha; bali ni ukubwa wa alama zenye kumbukumbu nzuri anazoziacha katika nyoyo na nafsi za wale anaowatumikia au kuwaongoza.

Ndoto zako haziwezi kabisa kutimia iwapo hutajitolea kuzifanyia kazi. Amua pa kuanzia baada ya kufanya maamuzi sahihi. Jitume bila ya kutafuta visingizio. Amini unaweza na usichoke kutafuta!

Mungu alipokuumba, alikupa kipaji na uwezo wa kukitumia vyema. Kulaza damu na kushindana na watu ni upumbavu. Badili mtazamo wako na ujiwekee malengo mapya ya mara kwa mara.

Huu ndio ushauri wa Bi Emily Gatwiri – mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Sukari Presbyterian Academy, eneo la Kahawa Sukari, Kaunti ya Kiambu.

MAISHA YA AWALI

Emily alizaliwa mnamo Mei 2, 1989, katika kijiji cha Ntua, eneo la Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watatu wa Bw Zaverio Baariu na Bi Benedicta Naita. Nduguze Emily ni Yvonne Mukiri ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Upili ya St Francis Mang’u, Kiambu na Victor Muriithi anayesomea katika Shule ya Msingi ya Ahadi Presbyterian, eneo la Kenyatta Road, Kiambu.

Emily pia ni mama wa wavulana wawili – Lameck Mwangi, 6, na Alex Mwenda, 4. Wote hao wanasomea katika Shule ya Sukari Presbyterian.

Mnamo 1996, Emily alijiunga na Shule ya Msingi ya St Kizito, Kaunti ya Isiolo. Anakumbuka alivyokuwa chini kimasomo wakati huo.

“Nikiwa mwanafunzi wa Darasa la Kwanza, sikujua kusoma kabisa. Sikung’amua chochote ila kwa msaada wa mwalimu wangu, Bi Ntoribi aliyekuwa akisalia nami shuleni ili anisaidie kusoma baada ya wenzangu kuondoka na kurejea nyumbani adhuhuri.

“Bi Ntoribi alikwenda nami nyumbani kwake mara kwa mara kwa masomo ya ziada. Upendo wake kwangu ulinitia ari ya kuchangamkia masomo. Kuanzia hapo, historia yangu iliandikwa upya, nikawa miongoni mwa wanafunzi bora zaidi darasani.”

Kutokana na kumbukumbu hiyo, Emily anaamini kuwa kila mwanafunzi ana uwezo wa kufaulu vyema masomoni. Anakiri kuwa mwalimu wake angekosa kumwamini, kumwelekeza ipasavyo na kumpokeza malezi bora ya kiakademia, basi masomo kwake yangesalia usiku wa kiza.

Mbali na Bi Ntoribi, mwingine aliyemchochea na kumhimiza Emily kujitosa katika ulingo wa ualimu ni Bi Saba aliyemfundisha kuanzia Darasa la Nne hadi Darasa la Nane. Ingawa Emily hakuwa na maazimio ya kuwa mwalimu hapo awali, alijenga upendo wake katika taaluma hiyo hatua kwa hatua, na amekuwa na msukumo wa kujiboresha kila uchao.

Baada ya kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika Shule ya Msingi ya St Kizito mnamo 2003, Emily alijiunga na Shule ya Upili ya Mfariji Girls iliyoko Mutuati, Kaunti Meru mnamo 2004. Alisomea huko kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Akithii Girls, Tigania Magharibi. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwishoni mwa 2007.

Kati ya walimu waliomtia ilhamu ya kuchangamkia masomo ya lugha ni Bi Victoria na Bi Kaibung’a ambao walimtanguliza vyema katika Fasihi ya Kiingereza na kutambua utajiri wa kipaji chake katika uandishi wa kazi bunilizi. Mwingine aliyemchochea pakubwa kwa imani kwamba Kiswahili ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi; ni Bi Makena Muriungi.

Bi Victoria alimpigia Emily mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na kumpa motisha ya kujitosa kikamilifu ulingoni na kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa fasihi baada ya kutathmini mswada wake wa kwanza wa riwaya ya Kiingereza mnamo 2014.

Emily alisomea ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Murang’a kati ya 2008 na 2010. Ilikuwa hadi 2015 ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

UALIMU

Kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Sukari Presbyterian anakofundisha kwa sasa, Emily aliwahi kuwa mwalimu katika shule za Juja St Peters, Tulivu Junior Academy, North Riara Ridge na Ahadi Presbyterian.

Amewahi pia kuwa mkutubi msaidizi katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Thogoto, Kiambu kati ya 2012 na 2014. Akiwa huko, alipata fursa ya kuwa karani wa Baraza la Mitihani ya Kitaifa nchini Kenya (KNEC) kati ya 2012 na 2013.

UANDISHI

Emily alishiriki uandishi wa vitabu kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC) mnamo 2019. Tangu wakati huo, ameandika vitabu vingi vya hadithi za watoto ambavyo vitachapishwa hivi karibuni. Ameshirikiana pia na waandishi chipukizi na waliobobea kuchapisha antholojia mbalimbali za hadithi fupi.

Hadithi yake ‘Chovya Chovya’ ilichapishwa na kampuni ya The Writers’ Pen Publishers, Eldoret katika mkusanyiko wa ‘Shaka ya Maisha na Hadithi Nyingine’ mnamo Julai 2020.

Emily ndiye mwandishi wa hadithi ‘Kosa La Baba’ katika katika diwani ya watoto ya ‘Kuku Ameshinda Kura na Hadithi Nyingine’ iliyofyatuliwa na kampuni ya Williams Publishers, Kisumu mnamo Septemba 2020.

Kabla ya Chania Publishers kumchapishia hadithi ‘Jambazi wa Chuoni’ katika antholojia ya ‘Siwezi Tena’ na Hadithi Nyingine mnamo Oktoba 2020, Emily alikuwa amechangia mashairi katika ‘Diwani ya Maradhi’ iliyotolewa na The Writer’s Pen mnamo Agosti 2020.

Sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani ya Emily tangu akiwa mtoto mdogo. Babaye mzazi alikuwa akimnunulia magazeti kila siku na kumuongoza kushiriki mashindano mbalimbali ya uandishi kwenye kumbi za watoto magazetini. Pia alimnunulia vitabu vingi vya hadithi vilivyompa kariha ya kuandika insha zilizovutia na kustaajabisha walimu na wanafunzi wenzake kwa ufundi wa lugha na ubunifu wa kipekee.

Kati ya waandishi, wasomi na wataalamu waliomwamshia Emily ari ya kuzamia uandishi wa vitabu ni Bw Mutahi Miricho, Bw Sam Mbure na Bw Moses Murithi Murega ambaye ni mhariri katika Shirika la Uchapishaji la Kenya Literature Bureau (KLB).

Weingine ni Bw Kinyanjui Kombani, Bw Richard Ondoli Amunga, Bw Angira O. Angira, Hussein Kassim, Timothy Omusikoyo Sumba na Bw Gabriel Dinda ambaye ni mwanzilishi na mkurugenzi wa Shirika la Writers’ Guild.

GWIJI WA WIKI: Mtetezi wa Kiswahili ndani ya Seneti

LEONARD ONYANGO na CHRIS ADUNGO

KITI cha Naibu wa Spika wa Seneti kiliposalia wazi baada ya Seneta wa Tharaka Nithi Profesa Kithure Kindiki kubanduliwa Mei 22, mwaka huu, Seneta Maalumu Isaac Mwaura alikuwa miongoni mwa maseneta waliotuma maombi ya kutaka wadhifa huo.

Wengine walioidhinishwa kuwania wadhifa huo ni Seneta wa Kirinyaga Bw Charles Kibiru, Prof Margaret Kamar (Uasin Gishu), Bw Stewart Madzayo (Kilifi) na Bi Judith Pareno (Maalumu).

Lakini siku chache baadaye, Bw Mwaura, Bw Kibiru, Bw Madzayo na Bi Pareno walijiondoa kutoka kwenye kinyang’anyiro baada ya kufanya mashauriano, hivyo kumwezesha Prof Kamar kuchaguliwa bila kupingwa.

Kuchaguliwa kwa Prof Kamar, hata hivyo, ilikuwa baraka kwa Seneta Mwaura.

“Kamar alikuwa katika jopo la wasaidizi wa spika. Alipochaguliwa kuwa naibu wa spika, kulitokea nafasi katika jopo hilo. Mnamo Juni 24, mwaka huu, nilichaguliwa kujaza nafasi hiyo,” anaelezea.

Jopo hilo la watu sita, hujumuisha spika, naibu spika na wasaidizi wanne ambao wanaweza kuongoza vikao vya Seneti.

Wasaidizi hao wanne wanaweza kuendesha vikao spika na naibu wake wasipokuwepo.

Bw Mwaura ambaye ni msaidizi wa spika mwenye umri mdogo zaidi, anasema kuwa wadhifa huo umetimiza ndoto aliyokuwa nayo kabla ya kuingia bungeni 2013 kwamba siku moja angeongoza vikao vya bunge.

“Nilitamani kuwa spika wa Bunge hata kabla ya kuingia bungeni 2013. Ninashukuru sana kwa sababu hiyo ni ndoto ambayo imeafikiwa,” anasema.

Kati ya wasaidizi hao wanne wa spika, Bw Mwaura amekuwa kivutio cha wengi kutokana na hatua yake ya kuendesha vikao vya Seneti kwa kutumia Kiswahili.

“Nilipoanza kutekeleza majukumu yangu kama msaidizi wa spika sikuanza kwa lugha ya Kiswahili. Lakini baadaye nilitafakari kwa kina nikaamua nitumie lugha ya Kiswahili katika vikao vyangu.

“Lakini jambo la kutia moyo ni kwamba Wakenya wamependezwa sana na hatua yangu ya kutumia Kiswahili kuongoza vikao vya Seneti. Nimekuwa nikipokea arafa tele za kunimiminia sifa,” anasema Bw Mwaura.

Seneta Mwaura ndiye alikuwa akiongoza kikao cha Seneti wakati wa kupitisha Mswada wa Ugavi wa Fedha kwa Kaunti (CARB) 2020 mnamo Octoba 6 hivyo kuingia katika daftari la kumbukumbu kwa kuwa spika wa kwanza kutumia Kiswahili kupitisha sheria.

“Hata Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alinieleza kuwa alipendezwa sana na hatua yangu kupitisha sheria kutumia lugha ya Kiswahili. Hakuna spika ambaye amewahi kutumia Kiswahili nchini Kenya na kuendesha vikao vya Bunge na hatimaye kupitisha sheria.

“Maseneta wanashangaa kwa sababu ninapewa ratiba ya shughuli za Seneti za siku zikiwa zimeandikwa kwa Kiingereza lakini mimi nazitafsiri kwa Kiswahili wakati wa kuzungumza,” anasema.

Tofauti na Bunge la Kitaifa ambalo kanuni zake zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, kanuni za Seneti hazijatafsiriwa. Lakini kuna jopokazi linaloendelea na shughuli ya kutafsiri kanuni za Seneti kwa lugha ya Kiswahili.

Seneta Mwaura, hata hivyo, anasema kuwa ni wabunge wachache mno wanaotumia Kiswahili wakati wa mijadala licha ya kanuni za Bunge la Kitaifa kutafsiriwa kwa Kiswahili.

HOFU YA KUZUNGUMZA KISWAHILI BUNGENI

Bw Mwaura anasema kuwa maseneta wengi wanasema kuwa hawazungumzi Kiswahili kwa sababu wanaogopa kuboronga lugha.

“Wanahisi kuwa hawataweza kuzungumza kwa ufasaha. Lakini jambo la kushangaza mbona wanatumia Kiswahili kuomba kura kutoka kwa Wakenya wakati wa uchaguzi na hawaoni haya?” anauliza.

Seneta Mwaura ambaye ni mtu wa kwanza mwenye ulemavu kuhudumu katika jopo la maspika, anasema kuwa pongezi ambazo amekuwa akipata zimemtia mshawasha wa kuendelea kutumia Kiswahili kuongoza vikao.

“Tangu nilipoanza kutumia Kiswahili kuongoza vikao Wakenya wamekuwa wakiniambia kuwa sasa wanafuatilia matukio katika Seneti kwa sababu wanaelewa kinachoendelea ndani ya Bunge,” anasema.

ELIMU

Anasema kuwa aliipenda lugha ya Kiswahili alipokuwa kinda katika Shule ya Msingi ya Wasioona ya Thika. Mnamo 1996, Mwaura alitunukiwa tuzo kwa kuwa msemaji bora wa hotuba ya Kiswahili nchini katika mashindano ya wanafunzi wa shule ya msingi.

“Nilifana kuanzia kanda hadi ngazi ya kitaifa na nilitunukiwa cheti katika jumba la KICC na aliyekuwa waziri wa Elimu JJ Kamotho. Wakati huo nilikuwa mwanafunzi wa Darasa la Nane,” anaeleza.

Baada ya kukamilisha elimu ya shule ya msingi, Mwaura alifaa kujiunga na Shule ya Upili ya Starehe lakini akanyimwa nafasi kwa kuwa mlemavu.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya sekondari, Bw Mwaura alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea Elimu ya Watu wenye Mahitaji Maalumu na Kifaransa ambapo alihitimu 2006.

Alipokuwa mwanafunzi aliongoza maandamano dhidi ya shirika lisilokuwa la kiserikali lililokuwa likitumia wanafunzi wasioona kujinufaisha.

Mnamo 2006, aliunda chama cha kutetea masilahi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Mwaka huo alikutana na mwigizaji mahiri Lupita Nyong’o katika Jumba la Maonyesho ya Sanaa (KNT) alipokuwa akijiandaa kutengeneza filamu yake iliyofahamika kama My Genes.

“Niliomba Bi Nyong’o kunitambulisha kwa baba yake Prof Anyang’ Nyong’o aliyekuwa Katibu Mkuu wa ODM. Baadaye Prof alikuwa mlezi wa Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngozi (ASK),” anasema.

Mwaura alihudumu kama mshauri wa Waziri Mkuu Raila Odinga kati ya 2010 na 2012. Alimshauri Bw Odinga kuhusu sera zinazohusiana na watu wenye ulemavu.

Mnamo 2013, aliteuliwa kuwa mbunge maalumu aliyewakilisha walemavu.

Bw Mwaura pia alisomea katika Chuo Kikuu cha Leeds cha Uingereza kati ya 2011 na 2012, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Metropolitan (2010 -2012) na Chuo Kikuu cha Presbyterian East Africa (2003-2012).

MATAZAMIO

Bw Mwaura anahimiza Wakenya, haswa viongozi kukumbatia Kiswahili kwa sababu mawanda yake yanazidi kuenea kote barani Afrika.

“Kiswahili kinazidi kukua barani Afrika. Kiswahili sasa kinafundishwa mataifa mbalimbali barani Afrika kama vile; Afrika Kusini, Rwanda, Burundi, Namibia na Dr Congo,” anasema.

Anasema kuwa Kiswahili kinafaa kuzungumzwa na wabunge wote bila kujali maeneo wanayotoka.

“Kwa mfano, katika Seneta wa Laikipia John Nderitu Kinyua hutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha sana pale katika Seneti. Lugha ya Kiswahili hakifai kuwa tu ya wabunge na maseneta kutoka Pwani. Kiswahili kinastahili kuenziwa na kila seneta au mbunge,” anasema.

“ Ninashangazwa kwamba hakujawahi kutokea spika ambaye amewahi kukumbatia Kiswahili bungeni. Hata Spika wa kwanza wa Seneti Timothy Chitasi Chokwe aliyehudumu kati ya 1963 na 1966, hakuwa akitumia Kiswahili kuendesha shughuli za Bunge licha ya kuwa mzaliwa wa maeneo ya Pwani,” anaongezea.

Anasema kuzungumza Kiswahili Bungeni ni ishara ya kuonyesha kuwa wabunge wanamjali mwananchi wa kawaida.

“Mara nyingi tunapozungumza Kiswahili watu huelewa zaidi. Hii ni kwa sababu idadi kubwa ya Wakenya wanaelewa Kiswahili ikilinganishwa na lugha ya Kiingereza.

Haja kubwa hapa si lafudhi au ufasaha bali na kujieleza. Hatufai kuendeleza kasumba ya wakoloni ambao walikichukulia Kiswahili kuwa lugha ya watu ambao hawajasoma na watumwa. Kiswahili ni lugha ya kila mtu; kuanzia wale hawakupata fursa ya kwenda shuleni hadi wale wamesoma hadi kiwango cha uzamifu (PhD),” anasema.

Anasema kuwa tangu alipoanza kuongoza vikao vye Seneti kwa lugha ya Kiswahili baadhi ya maseneta wamepata ujasiri wa kuwasilisha hoja kwa kutumia lugha hiyo ambayo inatumika humu nchini kama lugha rasmi na lugha ya kitaifa.

Anasema kuwa kanuni za sasa zinazotumika katika Seneti na Bunge la Kitaifa pia zinachangia katika kufanya wabunge kutozungumza Kiswahili.

“Tunafaa kubadilisha kanuni za Bunge ili kuruhusu maseneta kuchanganya Kiswahili na Kingereza wakati wa kutoa hoja bungeni. Kwa sasa kanuni za Bunge zinasema kuwa unapoanza kuzungumza kwa Kiingereza ni sharti umalize hotuba kwa Kiingereza. Ukianza kwa Kiswahili unamalizia kwa Kiswahili – wengi hupendelea kuanza kwa Kiingereza,” anasema.

Bw Mwaura anasema kuwa ili kuwatia mshawasha wa kuzungumza Kiswahili maseneta wenzake: “Ninapokuwa kwenye kiti cha Spika maseneta wanapozungumza kwa Kiingereza mimi nawajibu kwa Kiswahili.”

Anasema kuwa viongozi wakuu serikalini wanafaa kukumbatia Kiswahili.

“Rais Uhuru Kenyatta, kwa mfano, anasoma hotuba yake ya Kiingereza na kisha mwishoni anafafanua mambo aliyoyasoma kwa Kiswahili. Huko ni kudunisha Kiswahili.

“ Natamani siku ambayo Rais Kenyatta atasoma hotuba yake rasmi kwa Kiswahili bila kuchanganya na Kiingereza. Huo si uzalendo tu bali itawafikia Wakenya wengi,” anasema.

Patrick Mukanga: Mtangazaji, mwalimu na mshauri wa lugha

Na PETER CHANGTOEK

Patrick Michael Mukanga ni mja mwenye vipaji vingi. Yeye ni mtangazaji, mwalimu, mwandishi wa vitabu na pia mshauri na hutoa nasaha kuhusu masuala ya lugha za Kiingereza na Kiswahili.

Alizaliwa mnamo mwaka 1990, katika kitongoji cha Bujwang’a, kaunti ndogo ya Butula, Kaunti ya Busia.

Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi ya Khunyangu, iliyoko katika Kaunti ya Busia, mnamo mwaka 1996, kabla hajajiunga na nyingine ijulikanayo kama St. Teresa Nelaa, akiwa katika Darasa la Nne, alikofanyia mtihani wa KCPE, mnamo mwaka 2005.

“Baadaye, nikajiunga na shule ya Upili ya Lugulu A.C, kuanzia mwaka 2006 hadi 2007. Mnamo mwaka 2008, nililazimika kukaa nyumbani kwa sababu ya kukosa karo,” afichua Mukanga.

Huku akiwa nyumbani baada ya kukosa karo, alishurutika kujihusisha na shughuli ainati za kilimo, ili apate hela za kulipia karo.

Juhudi zake zilimlipa. Baada ya kuyauza baadhi ya mazao ya shambani, alijiunga na shule tofauti mnamo mwaka 2009, ili kuyaendeleza masomo yake.

“Mnamo mwaka 2009, nilijiunga na St. Mathias Secondary School, Busia, kuanzia Kidato cha Tatu hadi cha Nne, na kufanya mtihani wa KCSE mwaka 2010,” asimulia Mukanga, mwenye umri wa miaka 30.

Mnamo mwaka 2011, baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya upili, aliendeleza shughuli za kilimo.

“Mnamo Mei, 2012, nilijiunga na Kenya Institute of Media and Technology, iliyokuwa katika Taveta Road, Nairobi, ambapo nilisomea diploma katika kozi ya uandishi wa habari na utangazaji,” adokeza Mukanga, ambaye alikamilisha masomo hayo mwaka 2014.

Mnamo Juni, 2014, alijiunga na Around The Globe (ATG) Radio, ili kuhudumu kwa mafunzo ya nyanjani, kwa kipindi cha miezi miwili. Baada ya muda huo kukamilika mnamo Agosti mosi, aliajiriwa kuko huko, kwa muda wa mwezi mmoja, ambapo alikuwa akichukua na kuzihariri video zilizokuwa zikitumiwa katika runinga ya Deliverance TV, inayomilikiwa na shirika la habari la ATG.

Mnamo Septemba, 2014, alijiunga na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), ili kupata mafunzo mengine ya nyanjani, hadi Disemba. Akiwa kule, alipata fursa ya kufanya kazi na akina Charles Otunga, Kennedy Epalat, Franco K. Lusaka, miongoni mwa wengine.

Mbali na kukiandaa kipindi cha Darubini, Mukanga pia alikuwa ametwikwa jukumu la kuziandika na kuzisoma habari, katika Radio Ingo, iliyokuwa ikimilikiwa na KBC.

Hata hivyo, kipaji chake kilianza kuonekana mapema, akiwa katika shule ya msingi ya Nelaa, na hata mwalimu wake mmoja akamwambia kuwa, angekuwa mwanahabari baadaye.

“Nilikuwa nikiwaiga watangazaji kama vile Charles Otunga, Hassan Ali (Radio Maisha), marehemu Waweru Mburu na Mohamed Ali,” asema Mukanga, ambaye ni mzawa wa saba, katika aila ya watoto kumi na wawili.

Anasema kuwa alianza kuandika alipokuwa katika Kidato cha Kwanza. Hata hivyo, hajaanza kuichapisha mingi ya miswada yake.

Kwa sasa, amekichapisha kitabu kimoja, Mwerevu Mjinga, kilichochapishwa na Onmove Publishers. Alikiandika kitabu hicho kwa kuutumia mwangaza wa mshumaa.

Kitabu hicho kinamhusu kijana mmoja anayejulikana kama Mworia, ambaye ni mhusika mkuu, aliyekuwa mwerevu darasani, ila akaja kunaswa kwenye ulimbo wa mihadarati.

Alikuwa na miswada kumi na mitatu, lakini ameuchapisha mmoja, na ana kumi na miwili iliyosalia. Anaongeza kuwa aliliona pengo katika uandishi wa vitabu vya watoto, na akaamua kulijaza

Mbali na kuwa mtangazaji na mwandishi wa vitabu, Mukanga pia ni mshauri wa lugha za Kiswahili na Kiingereza, si tu katika shule za msingi, bali pia katika shule kadha wa kadha za sekondari.

Miongoni mwa shule ambazo amewahi kuzuru na kuwapa wanafunzi nasaha ni: Kids Village Academy (South C), Nairobi South Primary School (South B), Winka Academy (South C).

Pia, amewahi kutoa nasaha na mwongozo katika shule kadhaa za upili nchini, zikiwamo BDS Secondary School (Industrial Area), Kingandole Secondary School (Busia) na Bukhalalire Secondary School (Butula).

Mwandishi huyo anawasihi wale ambao wana azma ya kujiunga na uanahabari kuwa na mtazamo na kutositasita. Isitoshe, Mukanga anawashauri kufanya utafiti, na kukumbuka kuwa hakuna ndoto yoyote ambayo itatimia, endapo mja hatatia bidii za mchwa.

Anaazimia kupata masomo ya juu, hususan ya lugha ya Kiswahili. Aidha, ananuia kushirikiana na waandishi wengineo wenye tajriba pana, kuviandika vitabu, katika siku za usoni.

GWIJI WA WIKI: Jane Angila Obando

Na CHRIS ADUNGO

KUFAULU maishani na katika taaluma kunahitaji mtu kujituma, kujiamini na kuvuta subira.

Tupo jinsi tulivyo kwa sababu ubora wetu umechangiwa na watu wengine. Hatua ya kwanza katika safari yoyote ya mafanikio ni kufahamu kile unachokitaka, kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unakokwenda.

Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga, uwe na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika mambo unayoyafanya na uithamini sana familia yako. Jitabirie mambo mema katika siku za usoni na usikubali kushindwa na jambo lolote zuri maishani.

Huu ndio ushauri wa Bi Jane Angila Obando – mwandishi maarufu, mhakiki wa fasihi, mlezi wa vipaji na mwigizaji stadi ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Jane alizaliwa mnamo Novemba 21, 1961 katika kijiji cha Ebulako, Kaunti ya Vihiga. Ndiye wa kumi kuzaliwa katika familia ya watoto kumi na wawili wa marehemu Bi Rumonah Obando na marehemu Bw Nelson Obando.

Mzee Nelson Obando aliyeaga dunia mnamo 1977, aliwahi kuwa Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya Ebusakami, Vihiga na Inspekta wa Elimu katika eneo la Kavirondo Kaskazini.

Jane alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Ebusakami mnamo 1967. Alisomea huko hadi darasa la tatu na kujiunga na Shule ya Msingi ya Misikhu Girls, Kaunti ya Bungoma mnamo 1970. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mwishoni mwa 1973.

Alifaulu vyema katika mtihani huo na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Nangina Girls, Kaunti ya Busia kati ya 1974 na 1975. Baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (KJSE), alijiunga na Shule ya Upili ya Tigoi Girls, Vihiga mnamo 1976 na akafanya Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Kidato cha Nne (EACE) mnamo 1977.

Kifo cha baba mzazi kilimtikisa Jane pakubwa na kikatishia kumzimia mshumaa wa elimu ulioning’inizwa kwenye uzi mwembamba wa matumaini.

Alilazimika kusalia nyumbani kwa zaidi ya miaka miwili hadi 1980 ambapo alijiunga na Shule ya Upili ya Matuga Girls, Kaunti ya Kwale kwa minajili ya masomo ya kiwango cha ‘A-Levels’.

Baada ya kukamilisha Mtihani wa Kidato cha Sita (EAACE) mwishoni mwa 1981, Jane alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Hobunaka Boys, Vihiga. Alihudumu huko hadi mwishoni mwa 1983 kisha akajiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Siriba, eneo la Maseno, Kaunti ya Kisumu kusomea Diploma (Kiswahili na Historia) kati ya 1984 na 1985.

Anakiri kwamba maamuzi ya kusomea taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa mno na Bi Kago aliyempokeza malezi bora zaidi ya kiakademia katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Siriba.

UALIMU

Jane aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) mnamo Aprili 1986 na akaanza kufundisha katika Shule ya Upili ya Mbale Boys, Vihiga. Alihudumu huko hadi Januari 2000 alipopata uhamisho hadi Shule ya Upili ya Mutuini Boys, eneo la Dagoretti Kusini, Kaunti ya Nairobi. Ilikuwa hadi Januari 2013 ambapo alijiunga na Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi.

UANDISHI

Uandishi ni sanaa ambayo Jane anakiri kwamba ilianza kujikuza ndani yake tangu alipoanza kuwa mtahini wa kitaifa wa KCSE mnamo 1989. Alitambua makosa mengi yaliyokuwa yakifanywa na wanafunzi katika mitihani na akaazimia haja ya kutunga kazi za kuwasaidia kujibu maswali.

Bi Amina Mlacha Vuzo ni miongoni mwa walimu waliompigia Jane mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na kumpa motisha ya kujitosa kikamilifu ulingoni na kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Jane ameandika ‘Miongozo’ ya vitabu vyote teule vya Fasihi ya Kiswahili ambavyo vimekuwa vikitahiniwa katika shule za sekondari za Kenya tangu 1998.

Ameandika pia vitabu vingi vya mazoezi na marudio kikiwemo ‘KCSE Score More’ alichochapishiwa na kampuni ya Storymoja Publishers jijini Nairobi mnamo 2015.

Zaidi ya ‘Mwongozo wa Insha’, ‘Mwongozo wa Isimujamii’, ‘Mwongozo wa Mashairi’ na ‘Udodosi wa Fasihi Andishi’; msururu wa vitabu ‘Marejeleo Halahala’ katika Sarufi na Matumizi ya Lugha, Isimujamii, Mashairi na Fasihi Simulizi ni miongoni mwa kazi zake nyinginezo. Vitabu hivi vimechapishwa na kampuni ya Nyapunyi Publishers iliyoanzishwa na Jane mnamo 1998.

Jane alikuwa miongoni mwa walimu walioshiriki utunzi wa kitabu ‘Mwandani wa Mwanafunzi’ kilichotayarishwa na Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi mnamo 2015. Kwa sasa anaandaa riwaya ambayo anatazamia ichapishwe hivi karibuni.

DRAMA

Jane alitambua kipaji chake katika sanaa ya uigizaji akiwa mwanafunzi wa A-Levels katika Shule ya Upili ya Matuga Girls. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliowakilisha shule hiyo katika tamasha mbalimbali za kitaifa za muziki na drama na kupata fursa ya kuigiza kwenye majukwaa ya maeneo mbalimbali ya humu nchini.

Mbali na kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi, Jane amekuwa mstari wa mbele kushirikisha wanafunzi wake katika mashindano ya kufyatua filamu na kuigiza. Amewahi kutambuliwa kwenye tuzo za kimataifa za Kalasha zilizoandaliwa katika ukumbi wa KICC mnamo 2015 na akaongoza Moi Girls Nairobi kushiriki drama za kimataifa katika Mkoa wa Lira (2018) na eneo la Fort Portal (2019) nchini Uganda.

JIVUNIO

Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Jane amefundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali za maendeleo ya jamii.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo Kiswahili.

Tajriba pevu na uzoefu mpana anaojivunia katika utahini wa Kiswahili umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuelekeza na kuhamasisha wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa. Ziara hizo zimempa pia majukwaa ya kuhimizana na walimu wenzake kuhusu umuhimu wa kuandika vitabu. Jane anamstahi sana mjukuu wake Rumonah Maloba, 23. Jane anaazimia sasa kuzindua shule ya kimataifa ya mtandaoni ya ‘The International Swahili Mastery Academy’ kufikia Januari 2021.

GWIJI WA WIKI: Prof Kithaka Wa Mberia

Na CHRIS ADUNGO

WAKATI ndiyo raslimali na hazina ya pekee muhimu zaidi ambayo sisi binadamu tunayo kwa kiwango sawa.

Ukitumia hazina hii vizuri, utafaulu katika shughuli zako na utafika mbali.

Kila binadamu ana kipaji ambacho ni wajibu wake kukitambua na kupalilia. Huwezi kujiendeleza maishani iwapo hujiamini. Kujiamini ni chanzo cha ubunifu wa aina yoyote.

Kupiga hatua katika taaluma yoyote kunahitaji mtu kujiheshimu na kuongozwa na subira. Haiwezekani kabisa kwa mambo yote kuja kwa wakati mmoja. Ufanisi ni zao la bidii, nidhamu, imani na stahamala. Milango ya heri hujifungua yenyewe kwa watu wenye sifa hizi.

Chagua maono yenye matarajio, ota ndoto kubwa zenye thamani na uwe tayari kuzitolea jasho. Ndoto hukua na kunawiri iwapo itanyunyiziwa jasho! Jifunze kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo kisha teua kushindana na wakati. Thamini hicho unakichokifanya, jitume na waulize wajuao zaidi yako.

Huu ndio ushauri wa Prof Kithaka wa Mberia – mshairi, mwanaisimu, mwandishi na msomi na mtetezi wa haki ambaye kwa sasa ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Kithaka wa Mberia alizaliwa mnamo Agosti 8, 1955 katika kijiji cha Keraka, Kaunti ya Tharaka-Nithi.

Alianza safari yake ya masomo mnamo Mei 1963 katika Shule ya Msingi ya DEB Karethani, Tharaka alikosomea kwa miaka mitatu kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Gatunga, Marimanti, Tharaka kwa miaka minne.

Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mnamo 1969 na akapata nafasi ya kusomea katika shule maarufu ya Chuka Boys, eneo la Karingani, Tharaka-Nithi kuanzia 1970.

Baada ya kuufanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (EACE) mnamo 1973, Kithaka wa Mberia alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance, Kaunti ya Kiambu kuendeleza masomo yake ya kiwango cha ‘A-Levels’ katika mwaka wa 1974. Aliufanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Sita (KACE) mwishoni mwa 1975.

Mnamo 1976, alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya B.A katika Isimu na masuala ya Jamii, Siasa na Utawala. Alihiari kuzamia zaidi masomo ya Isimu na akapata fursa ya kufundishwa na mikota wa lugha wakiwemo Prof Mohamed Hassan Abdulaziz, Prof Karega Mutahi, Prof Mohamed Bakari, Prof Lucia Ndonga Omondi, Prof Francis Katamba (Chuo Kikuu cha Lancaster, Uingereza) na marehemu Prof Jay Kitsao.

Baada ya kufuzu mnamo 1979, Kithaka wa Mberia alianza kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi chini ya usimamizi wa Prof Karega. Alifuzu mnamo 1981 baada ya kuwasilisha Tasnifu, “The Consonants of Kitharaka” na akaanza kufundisha kozi za Fonolojia katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Baadhi ya wanafunzi wake wa kwanza ni Dkt Mungania Basilio Gichobi, Dkt Hanah Chaga Mwaliwa na Prof Kineene Wa Mutiso.

Kithaka wa Mberia alianza kusomea shahada ya uzamifu (phD) katika Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 1985. Kutokana na shughuli nyingi za uandishi, alichukua kipindi kirefu cha muda kukamilisha utafiti wa nyanjani.

Ilikuwa hadi Agosti 1988 alipoanza kuandaa Tasnifu ‘Segmental Morphophonology of Kitharaka with Special Reference to the Noun” chini ya uelekezi wa Prof Karega na Prof Bakari. Aliiwasilisha mnamo 1992 na akafuzu mwaka uliofuata wa 1993.

Mbali na kuwa mtahini katika vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya Kenya, Prof Kithaka wa Mberia amewahi pia kufundisha katika Chuo Kikuu cha Virginia State, Petersburg (Amerika), Chuo Kikuu cha Warsaw (Poland) na Chuo Kikuu cha Hankuk (Korea Kusini).

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Kithaka wa Mberia tangu utotoni. Akiwa mwanafunzi wa Kidato cha Pili, alitunga shairi ‘The Bell’ lililochapishwa katika Jarida la Shule ya Upili ya Chuka Boys, ‘The Voice of the Mountain’.

Aliacha kabisa kuandika alipoingia Kidato cha Tatu kwa lengo la kupata fursa ya kumakinikia masomo. Ilikuwa hadi 1982, baada ya kutunukiwa shahada ya uzamili, ambapo alirejelea uandishi wa mashairi na michezo ya kuigiza.

Baada ya kampuni ya Marimba Publishers kumfyatulia diwani ‘Mchezo wa Karata’ (1997), Kithaka wa Mberia alichapishiwa tamthilia ‘Natala’ (1997), tamthilia ‘Kifo Kisimani’ (2001), ‘Bara Jingine’ (2002), ‘Redio na Mwezi’ (2005), tamthilia ‘Maua Kwenye Jua la Asubuhi’ (2007), ‘Msimu wa Tisa’ (2007), ‘Rangi ya Anga’ (2014), ‘Doa’ (2019) na ‘Mvumo wa Helikopta’ (2020) ambayo ni diwani yake ya saba.

Sita kati ya vitabu hivyo vya Prof Kithaka wa Mberia, vimetafsiriwa hadi kwa Kiingereza: ‘A Game of Cards’ (Dkt Zaja Omboga, 2011) ‘Another Continent’ (Dkt Richard Makhanu Wafula, 2011), ‘Death at the Well’ (Khalfan Kasu na Marami V. Marami, 2011), ‘Flowers in the Morning Sun’ (Khalfan Kasu, 2011), ‘Natala’ (Khalfan Kasu, 2013) na ‘The Ninth Season’ (Zaja Omboga, 2013).

Vitabu hivi vyote ambavyo vimechapishwa na kampuni ya Marimba Publishers – iliyoanzishwa na Prof Kithaka wa Mberia mnamo 1997 – vimeidhinishwa na Taasisi ya Kenya ya Ukuzaji wa Mitaala (KICD) kutumiwa kufundishia Fasihi katika shule za upili na vyuo vya humu nchini.

Mbali na ‘Natala’ iliyotahiniwa kwa muda mrefu zaidi katika Vyuo vya Mafunzo ya Ualimu nchini Kenya (2005-2015), tamthilia nyingine ya Prof Kithaka wa Mberia iliyowahi kuteuliwa kutahiniwa katika shule za sekondari za Kenya ni ‘Kifo Kisimani’ (2005-2012).

Mbali na tamthilia zake zote tatu, mengi ya mashairi ya Prof Kithaka wa Mberia yamewahi kuigizwa jukwaani kwenye Ukumbi wa Kitaifa wa Michezo ya Kuigiza (The Kenya National Theatre). Mtaalamu huyu wa Isimu anajivunia machapisho mengi ya kitaaluma katika vitabu na majarida ya kimataifa.

HUDUMA KWA JAMII

Prof Kithaka wa Mberia amehudumu katika Bodi za Usimamizi wa shule mbalimbali katika eneo la Tharaka Kusini, ikiwemo Shule ya Upili ya ABC Nkondi Girls. Kwa sasa ni kinara katika Baraza la Uongozi la Parklands Sports Club, Nairobi.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Prof Kithaka wa Mberia ni kuendelea kuandika zaidi kazi za Isimu na Fasihi ya Kiswahili na kuhudhuria makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo makuzi ya Kiswahili.

Mbali na fahari ya kuhudhuria idadi kubwa ya michezo ya kuigiza, Prof Kithaka wa Mberia amewahi kuwa mwasilishaji na mwamuzi mkuu katika mashindano mbalimbali ya tamasha za kitaifa za muziki na drama. Anajivunia tajriba pevu kuhusu jinsi sanaa za kila sampuli zinavyozamiwa na watu wa tamaduni mbalimbali.

Zaidi ya Amerika, Korea Kusini na Poland, Prof Kithaka wa Mberia amewahi pia kuzuru mataifa ya Ujerumani, China, Tanzania, Iran, Italia na Nchi ya Milki za Kiarabu (UAE).

Kwa pamoja na mkewe Anne Mberia, wamejaliwa watoto wawili – Gacheri Mberia na Nyaga Mberia.

GWIJI WA WIKI: Lilian Gathoni

Na CHRIS ADUNGO

JIFUNZE kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo, jiamini na upende kushindana na wakati.

Ujasiri wa kukabiliana na changamoto mbalimbali na imani kuwa hakuna lisilowezekana ni siri kubwa ya kufanikiwa maishani na katika kitaaluma.

Kufaulu katika jambo lolote ni zao la jitihada, nidhamu, imani na stahamala.

Upo mahali ulipo kwa sababu kuna mtu aliyetambua ukubwa wa uwezo wako na akakuchochea kufikia kilele cha ndoto zako.

Uwajibikaji, ari ya kufanya kazi kwa kujituma pamoja na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika mambo unayoyafanya, ni sifa muhimu na za lazima kwa mtu kuwa nazo ili afanikiwe. Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga na usonge mbele kwa mwendo na kasi yako.

Huu ndio ushauri wa Bi Lilian Gathoni Wambui –mwanafasihi chipukizi, mhariri na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na somo la Dini katika Shule ya Upili ya Royal Star, eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado.

MAISHA YA AWALI

Gathoni alizaliwa katika kijiji cha Iruri, eneo la Kamacharia, Kaunti ya Murang’a akiwa mwanambee katika familia ya watoto wanne wa Bi Agnes Wambui. Nduguze Gathoni ni Glorious Chelang’at, Davis Kiplang’at na Alex Kipkoech.

Gathoni alilelewa katika utamaduni uliosisitiza ulazima wa mtoto kuadhibiwa na kushauriwa na mzazi yeyote kwa kuwa jukumu la ulezi lilikuwa la jamii nzima.

Baada ya kupata elimu ya msingi shuleni Iruri kati ya 2002 na 2010, alijiunga na Shule ya Upili ya Kiria-ini Girls, Murang’a mnamo 2011 na akahitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 2014.

Gathoni alisomea ualimu (Kiswahili na Dini) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya Septemba 2015 na Disemba 2019.

Zaidi ya nyanya na mama mzazi kuwa walimu wake wa awali maishani, wawili hawa walimshajiisha sana Gathoni na kumhimiza ajitahidi masomoni.

Anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa na aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili katika shule ya msingi, Bi Mwangi. Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Zaidi ya Bw Stephen Wamalwa, wengine waliomchochea pakubwa kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote ni Dkt Hamisi Babusa, Dkt Miriam Osore, Dkt Timothy Arege, Dkt Joseph Gakuo, Mwalimu Mudhune na marehemu Mwalimu Kamunde.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa sasa na Gathoni katika Kiswahili umechangiwa pakubwa na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao ni wabobevu na wapenzi kindakindaki wa lugha hii.

UALIMU

Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Gathoni alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Kenswed iliyoko katika eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kati ya Mei na Agosti 2019 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Royal Star.

Gathoni anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote hutegemea mtazamo wake kwa somo husika na kwa mwalimu anayemfundisha darasani.

UANDISHI

Gathoni anaamini kwamba safari yake ya uandishi ilianza alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Ni katika kipindi hicho ambapo nyingi za insha alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa kutoka kwa walimu wake wa Kiswahili.

Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Kiria-ini Girls na wadhifa huo ukachangia kunoa kipaji chake cha ulumbi na kuinua kiwango chake cha umilisi wa lugha.

Chini ya uelekezi wa Mwalimu Daniels, Gathoni alishiriki mashindano mengi ya kutoa hotuba na kujizolea tuzo za haiba.

Kati ya waandishi waliomwamshia ari ya kutunga kazi za kibunifu kwa Kiswahili ni Bw Dominic Maina Oigo, Bw Wafula wa Wafula, Bw Djibril Adam, Bi Pauline Kea Kyovi, Bw Almasi Ndangili, Dkt Babusa na marehemu Profesa Ken Walibora.

Tangu 2017, Gathoni ameandika idadi kubwa ya miswada ambayo kwa sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu.

Kampuni ya Bustani Language Solutions (BLS) Nairobi ilimchapishia Gathoni hadithi ‘Kamari ya Maisha’ katika diwani ya ‘Mama Amerudi na Hadithi Nyingine’ mnamo Juni 2019.

Hadithi zake ‘Huba la Dhati’ na ‘Umdhaniaye Siye’ zilichapishwa na kampuni ya Bestar Publishers Nairobi katika mkusanyiko wa ‘Kitovu cha Shibiri na Hadithi Nyingine’ mnamo Disemba 2019.

Gathoni ndiye mwandishi wa hadithi ‘Vita vya Nafsi’ katika mkusanyiko wa ‘Hakimu wa Kifo na Hadithi Nyingine’ uliofyatuliwa na kampuni ya Bestar Publishers mnamo Februari 2020.

Gathoni ameshiriki pia mradi wa uandishi wa ‘Tusome Kenya’ kupitia kampuni ya Queenex Publishers Nairobi iliyomtolea kitabu ‘Mwati na Swale na Hadithi Nyingine’ mnamo Agosti 2020.

Gathoni kwa sasa anatafsiri riwaya ‘Son of Fate’ ya mwandishi John Kiriamiti hadi ‘Hatima Yangu’. Kazi hiyo itafyatuliwa na kampuni ya East African Educational Publishers (EAEP).

UHARIRI

Uhariri ulianza kujikuza ndani ya Gathoni tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Alikuwa mwepesi wa kuwakosoa wenzake waliovuruga lugha kila Jumatano ambayo ilikuwa ‘Siku ya Kiswahili’ shuleni mwao.

Kufikia sasa, amehariri makala mbalimbali ya kitaaluma, vitabu vya kiada na antholojia za hadithi fupi ambazo zimechapishwa na kampuni mbalimbali nchini Kenya.

Diwani yake ya kwanza kuihariri ni ‘Mama Amerudi na Hadithi Nyingine’ kabla ya kushirikiana baadaye na John Wanyonyi Wanyama kuipiga msasa diwani ‘Hakimu wa Kifo na Hadithi Nyingine’.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, mwandishi maarufu na mhadhiri wa chuo kikuu, Gathoni anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala waandishi wengi chipukizi ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya Kiswahili.

GWIJI WA WIKI: Meja Bukachi

Na CHRIS ADUNGO

MWANADAMU lazima awe na malengo maishani. Pania kuyatimiza hayo maazimio yako kabla ya kufa. Usiondoke duniai bila kuacha lolote lenye mashiko.

Kabla ya maisha kuisha, hakikisha kwamba lipo jambo – japo moja – ambalo waliosalia duniani watakukumbukia nalo.

Ukiwa mwimbaji, imba angalau ubeti mmoja tu utakaosikilizwa wakati wa kupumzika kwako ukiwadia. Ukiwa kiongozi, jenga daraja bora la mapatano na ulizindue; na iwapo umejaliwa mkono wa kuandika, basi andika na uandike bila hofu!

Kumbusha watu kuhusu umuhimu wa maisha na waeleze ubora wa kutenda mema kabla hawajaisha!

Huu ndio ushauri wa Bw Meja S. Bukachi – mwalimu wa Kiswahili, mwandishi wa vitabu, mwanahabari na mjasiriamali ambaye kwa sasa ni mhariri wa miswada katika kampuni ya Bestar Publishers na mhariri wa Chama cha Kiswahili cha Nakuru (CHAKINA).

MAISHA YA AWALI

Meja amelelewa katika familia ya walimu. Mbali na nduguye Elphaz Shigugu Bukachi wa Shule ya Msingi ya Ingotse, Kakamega; nduguze wengine wawili kati ya saba pia ni walimu.

Hawa ni Philip Masaga Bukachi na Duncan Bukachi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Ebutenje katika Kaunti ya Kakamega. Nduguze wengine ni Violet Bukachi, Hoglah Bukachi, Daniel Bukachi na Byrum Sunguti ambaye ni Luteni wa Kanisa la Jeshi la Wokovu katika Jimbo la Vihiga.

Meja alizaliwa kijijini Eshilakwe, eneo la Lurambi, Kaunti ya Kakamega. Ni mwana wa saba katika familia ya watoto wanane wa Bw John Bukachi Sunguti almaarufu ‘Mzee wa Job’ na Bi Gladys Mmbone Bukachi.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya Eshilakwe alikolainishwa na Mwalimu Mary Namayi ambaye alimpokeza malezi bora ya kiakademia. Meja alifanyia mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) shuleni Eshilakwe mwishoni mwa 2004.

Licha ya kufaulu vyema katika KCPE na kupata nafasi katika Shule ya Wavulana ya Kakamega na Shule ya Wavulana ya Lubinu, Kakamega; uchechefu wa karo ulimlazimu kujiunga na Shule ya Upili ya Sirigoi katika eneo la Navakholo, Kakamega akiwa mwanafunzi wa kutwa. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2009.

Meja anatambua jitihada za wazazi wake katika kumlea kwa kumcha Mungu, kupenda amani na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo.

Anakiri kuwa asingekuwa ‘Meja’ mwenye mapenzi kwa taaluma yake isingekuwa kwa ushajiishaji na uelekezi wa Bw Geoffrey Furechi, Peter Cetera Okova, Bw Khakali, Bw Josephat Matikho na Bw Shadrack Nashilobe waliomfundisha shuleni Sirigoi na Bi Violet Chimika na Bw Njuguna waliomtandikia zulia zuri la elimu shuleni Eshilakwe.

Wengine waliomchochea zaidi kitaaluma ni Bw Mugo Maina almaarufu ‘Balozi Ustadh’, Bw Mugendi Mutegi almaarufu ‘Msafiri Makini’, Bi Shelmith Weru wa Moi Forces Academy – Lanet, Bw Brian Kimutai Rop, Bi Terry Ambundo na Bw Nahashon Akunga Nyangeri ambaye alikipalilia kipaji chake katika sanaa ya uandishi.

UALIMU

Meja alihitimu stashahada katika ualimu (Kiswahili na Historia) kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Lanet, Nakuru mnamo 2014 na kuanza kufundisha katika Shule ya Upili ya Anestar, Nakuru.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimfanya kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) mwaka uo huo wa 2014 na akahitimu Shahada ya Ualimu mnamo 2016.

Meja pia amewahi kufundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Ematiha, Kakamega kwa kandarasi ya bodi pindi tu alipokamilisha KCSE. Yeye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na Historia katika Shule ya Upili ya Anestar Premier, Nakuru.

UANAHABARI

Moto wa Meja katika fani ya uanahabari uliwashwa na aliyekuwa mwanahabari mahiri wa kipekuzi, Mohamed Ali ‘Jicho Pevu’ ambaye sasa ni Mbunge wa Nyali, Kaunti ya Mombasa. Kutoka utotoni, Meja alipenda masuala ya kijasusi na ndoto yake ilikuwa kuwa kachero.

Ilhamu yake katika uanahabari ilichangiwa pia na vipindi vya Kiswahili kama vile Ramani ya Kiswahili (KBC) iliyokuwa Bahari ya Lugha (Radio Citizen) na Nuru ya Lugha kinachoendeshwa na Ali Hassan Kauleni wa Radio Maisha.

Kariha zaidi ilikuwa zao la kuhimizwa na mwanahabari Mugendi Mutegi alipokuwa Radio Fahari (Nakuru) akiendesha kipindi cha ‘Upeo wa Lugha’. Meja alianza kushirikishwa kama mchambuzi na mchanganuzi wa masuala ya Kiswahili kabla ya kupewa fursa ya kuwa mwelekezi mwenza wa kipindi akiwa msaidizi wa Mugendi.

Nafasi hii ilimtia ari ya kujiunga na Chuo cha East Africa Institute of Certified Studies (ICS) alikofuzu na stashahada ya uanahabari mnamo 2018.

Haja ya kujiendeleza zaidi katika taaluma hii ilimfanya kujiunga na Chuo Kikuu cha Multimedia anakosomea shahada ya uanahabari kwa sasa.

Meja pia ameanzisha kampuni ya masuala ya Habari na Mawasiliano ya Simba Media Services ambayo analenga kuisajili rasmi mwakani.

Akishirikiana na Mugendi Mutegi, wamezindua huduma za matangazo ya biashara na habari, uuzaji na ununuzi wa vitabu na huduma nyinginezo kupitia mtandao. Huduma ya Koupon City (KC) inawawezesha waandishi na watoaji huduma kama vile wanahabari na walimu kuuza na wanunuzi kununua bidhaa kwa bei nafuu na tena kwa starehe zao.

UANDISHI

Meja anashikilia kuwa uandishi ni talanta iliyoanza kujikuza ndani yake akiwa mwanafunzi wa darasa la sita. Huo ndio wakati alipoandika ‘mfano’ wa mswada wa riwaya aliouita ‘Raha Karaha’ japo hakuukamilisha hadi sasa. Insha nzuri alizoziandika na kumzolea tuzo za haiba wakati huo ni ushahidi wa utajiri wa kipaji chake katika uandishi.

Hamu ya kuandika ilimkaba koo zaidi kutokana na mapenzi yake ya kusoma kazi bunilizi za waandishi Prof Said A. Mohamed, Dkt Robert Oduori, Prof K.W. Wamitila, marehemu Prof Ken Walibora, marehemu Prof Euphrase Kezilahabi na marehemu Prof Katama G.C. Mkangi.

Waandishi wengine waliomtia Bukachi hamu ya kutunga ni Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Geoffrey Mung’ou na Dkt Hamisi Babusa.

Kampuni ya Uchapishaji wa Vitabu ya Maxwel Publishers Limited ilimchapishia Meja ‘Uketo wa Fasihi’ toleo la kwanza mnamo 2017, mwaka mmoja kabla ya Smart Publishers kumfyatulia ‘Mwongozo wa Kigogo’ na ‘Mwongozo wa Tumbo Lisiloshiba’ mnamo 2018.

Mnamo 2019, Maxwel Publishers Limited ilimtolea Bukachi ‘Mwongozo wa Chozi la Heri’ kabla ya Bestar Publishers kuzamia uchapishaji wa msuru wa ‘Uketo wa Sarufi’, ‘Uketo wa Fasihi’, ‘Uketo wa Ushairi’, ‘Uketo wa Fasihi Simulizi’, ‘Uketo wa Insha, Ufahamu, Ufupisho na Isimujamii’.

Meja pia ameandika kazi za kibunifu zikiwemo riwaya ya ‘Hawakuziki Mama’ (2019) na ‘Mola Mkuu’ (2020) ambazo zimechapishwa na Bestar Publishers. Miswada miwili ‘Ameavya Tena’ (riwaya) na ‘Pepo Tusitusi’ (tamthilia) inashughulikiwa na Gateway Publishers Limited na African Ink Publishers mtawalia.

Meja ameshirikiana na John Wanyonyi Wanyama kuhariri antholojia ya hadithi fupi ya ‘Wingu Limetanda na Hadithi Nyingine’ iliyochangiwa na wanachama wa CHAKINA na kuchapishwa na Bestar Publishers mnamo Machi 2020.

Ameshirikiana pia na Mugendi Mutegi kuandika diwani mbili za ushairi – ‘Diwani ya Kupe’ na ‘Uketo wa Ushairi’.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa malengo yake, Meja anaazimia kutumia kampuni ya Simba Media Services na mtandao wa Koupon City kupigia chapuo Kiswahili na kuwasaidia vijana.

Anajivunia kufundisha vijana wengi ambao wamezamia uanahabari na taaluma nyinginezo katika sekta mbalimbali za maendeleo ya jamii. Meja anajivunia kuwa kielelezo kwa vijana wanaotambua kuwa kutenda jambo hakutegemei umri.