HADITHI: Pengo asononekea hadhi ya chini wanayopewa walimu katika jamii

NA SHIUNDU MUKENYA

VISA vya dharau kwa walimu vilimfanya Pengo awazie upya kuhusu taaluma yake. Alikumbuka jinsi viongozi kwingineko walivyolazimika au kulazimishwa kujiuzulu walipotoa kauli zilizoonekana kukidharau kikundi chochote katika jamii.

Lakini ilivyoonekana, mambo yalikuwa tofauti nchini Kavaluku. Viongozi wa kisiasa walitoa kauli za kuwadhalilisha walimu lakini hakuna lililofanywa zaidi ya kelele za mtandaoni zilizomithilishwa na vituko vya chura visivyomzuia ng’ombe kunywa maji.

Kelele za wananchi kuhusu viongozi waliowadharau walimu kwa kuwaita ‘watu wa vokali na watu wa kushika chaki tu’ zilififia na hatimaye zikatoweka.

Hakuna aliyerejelea kauli hizi. Pengo lakini hakuzisahau, alimkumbusha na kumlalamikia Sindwele kuhusu dharau hii.“Hilo si geni kwa walimu na haswa sisi wa shule za ulimwengu wa tatu, tumezoea dharau hizo. Umesahau msemo kuwa kizuri cha bwana Sweyyid kikiharibika ni cha mwalimu fundi.

Ni sisi mafundi wa kutupiwa vilivyoharibika na kupigiwa mifano ya watu duni katika jamii.” Kauli hii ya Sindwele japo iliuma, ilimkumbusha Pengo aliloambiwa na baba yake siku ile alipoipokea barua ya kuenda chuoni kusomea ualimu.“Una maana kuwa huko pia wanafundisha ualimu?”

Nzeki alimuuliza Pengo na kumjuza kuwa enzi zao watu ambao hawakuweza kuendelea na masomo ya chuo kikuu waliajiriwa kuwa walimu. “Kumbe mambo yamebadilika hivi?”

Mbali na mtazamo huu wa baba yake kuhusu ualimu, Pengo alikumbuka swali alilowahi kuulizwa na mwanafunzi wake mwanzoni kabisa mwa taaluma yake.

Wakati huo Pengo alikuwa barobaro aliyefundisha kwa nguvu zake zote na dhati ya moyo wake. Alipohitimisha kipindi, mmoja wa wanafunzi akaunyanyua mkono akaulize swali.

Mwanafunzi alianza kwa kumpongeza mwalimu kwa kipindi kizuri, “Lakini mwalimu mbona waonekana kuwa msomi hivi na hujawahi kupata kazi nzuri? Mbona ungali unang’ang’ania huu ualimu? Mbona usitafute kazi yenye staha kidogo?” mwanafunzi akauliza hatimaye.

Naam, haya yalitosha kumkumbusha Pengo stihizai walizopitia walimu.“Lakini mbona walimu hawa wasitumie kura zao kuwaadhibu hawa wanasiasa wenye jeuri?” akamuuliza Sindwele.

“Wewe wajua walimu walivyo watu wa kutafuta vijipeni vya ziada. Wao huajiriwa kusimamia uchaguzi na hivyo basi hawapigi kura. Isitoshe, kunayo ile dhana ya ‘mbaya wetu’ kama inavyosawiriwa katika tamthilia ya Ken Walibora. Kwamba kwa pamoja tunamchukia kiongozi yeyote anayetudhulumu, chuki hii hudumu tu hadi wakati wa uchaguzi kila mtu anaposimama na mwanasiasa wa kwao licha ya ubaya wa mwanasiasa huyo,” Sindwele akamfafanulia Pengo.

HADITHI: Sindwele na Pengo wawapa wenzao ‘maagano spesheli’

NA SHIUNDU MUKENYA

SHUGHULI za kawaida zilianza kuchukua sura tena baada ya likizo fupi. Shuleni Sidindi, shughuli ziling’oa nanga Jumatatu asubuhi.

Hata hivyo, baadhi ya walimu hawakuwasili Jumatatu hiyo kwani nao walikuwa wamewapeleka watoto wao shuleni.

Hawa walitua Jumanne. Kinyume na matarajio, walimu wawili walikuwa hawajawasili kufikia Jumanne hiyo, hili halikutarajiwa kabisa. Ilisadifu kuwa wawili hawa walikuwa wale mabinti waliokuwa na miadi na Pengo kule Camp David.

Walimu wetu walipofika shuleni hatimaye, nyuso zao zilidhihirisha kusawijika. Walipoulizwa kilichowasawijisha, walisingizia mavune ya likizo fupi.

Ilipofika zamu ya Pengo kuwaamkua walimu hao, waliupuuza mkono walionyooshewa. Akalazimika kuwaamkua kwa kauli tu.

Walimu wetu walimpa Pengo salamu za shingo upande kwa sauti ya chini mno na ya kujilazimisha. Ilikuwa tu bahati kuwa walimu wengine walikuwepo, vinginevyo Pengo aliamini kuwa hawangezijibu salamu zake.

Akashuku kuwa kusawijika huko kulitokana na miadi yao iliyokwenda tenge wakati wa likizo fupi.

Pengo aliamini kuwa yaliyotukia wakati wa likizo fupi yalitokana na usodai na uchakaramu wa Sindwele.

Ni yuyo huyo Sindwele aliyekuwa nyakanga wa mizungu ya wana wa dunia hii kama Sindwele na wenzake walivyojitapa. ‘Waama hawa si wana wa dunia tu! Hawa ni wana wa giza haswaa!’ Pengo alijiambia.

Papo hapo, darubini yake ikarejea nyuma kumkumbusha yaliyotukia siku hiyo baada ya miadi yao kule Camp David.

Mabinti hao walikuwa wamegusagusa chakula walichoagiza na kilichogharamiwa na Pengo. Sindwele akaahidi kugharamia nauli. Alipiga simu kumwita dereva wa teksi.

Likaja gari moja kachara lililowachukua mabinti hao. Dereva wa gari hilo alinong’onezana na Sindwele faraghani kisha akaondoka na mabinti hao.

Punde tu walipoondoka, Sindwele alimwambia Pengo kuifunga simu yake hadi kesho yake.

Pengo ambaye hadi wakati huu alikuwa kamkabidhi Sindwele hatamu za kuendesha miadi ya siku hiyo aliufyata tu na kufwata aliloambiwa na Sindwele.

Alipoifungua simu kesho yake alikutana na jumbe tumbi nzima kwenye kikasha cha ujumbe. Nyingi ya jumbe hizi yalikuwa matusi yaliyoelekezewa Pengo na Sindwele. ‘Pamoja na uchochole wenu, mumefunguka skrubu za akili.’

Aliandika mmoja wa mabinti hao. Alipoyapeleleza, ndipo alipoambiwa kuwa kumbe Sindwele hakuwa kalipia nauli ya wasichana hao kama alivyoahidi, dereva wa gari hilo kachara aliwajia juu wasichana hao na kuwalazimisha kulipia nauli yao.

Pengo alipojaribu kushauriana na Sindwele kuihusu hili, Sindwele alimwambia kuwa mabinti hao walistahili kuuhisi uzito wa gharama.

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uchambuzi wa hadithi ‘Masharti ya Kisasa’ (Alifa Chokocho)

Na CHRIS ADUNGO

ANWANI ya hadithi hii inasawiri maudhui yaliyomo ndani yake.

Mambo yote yanayomkuta Dadi yanatokana na yeye kutofahamu ni nini kinachoashiriwa na mkewe kila anaposema “masharti ya kisasa”.

Mwishowe anatawaliwa na wivu unaozua matatizo.

Mtunzi anadhamiria kuonyesha jamii kwamba wivu wa kupindukia ni hatari sana kwa maendeleo.

Anajadili kwa kina kiini cha migogoro kati ya wanandoa, ahadi za maisha, elimu, urembo, umbea na masengenyo, itikadi na utamaduni na nafasi ya mapenzi ya dhati.

MAPENZI NA NDOA

Ndoa ni zao la mapenzi na mapenzi huhimili ndoa. Mapenzi na ndoa hukumbwa na changamoto mbalimbali. Baadhi ya wapenzi huwawekea wenzao masharti ya kufuata ili kudumisha uhusiano.

Kidawa alimpa Dadi masharti ya mapenzi ya kisasa kama vile kuosha vyombo, kufagia nyumba, kukuna nazi na kadhalika.

Dadi asingemkataza Kidawa kufanya jambo lolote kwa vile asingesikia wala kutii kwa sasa sababu kila wakati alikumbushwa kuhusu masharti ya kisasa aliyowekewa na Kidawa kabla ya kuoana.

Aliyavumilia masharti haya kwa miaka tisa. Hali hii inamfanya Dadi kuanza kushuku kuwa Kidawa ana uhusiano wa nje kimapenzi, jambo ambalo analifuatilia kijinga na hatimaye kujidhuru.

Wanawake wanateua kupendwa na wanaume wengi, hali inayowalazimu kuwafanyisha mitihani ili waweze kuchagua mume wa ndoa. Ingawa wanaume wengi walimpenda Kidawa, anahiari kuishi na yule ambaye angefuata masharti yake kama vile kuzaa mtoto mmoja.

Ijapokuwa Kidawa alimpa Dadi mitihani mingi na akawashinda wanaume wote, ni dhahiri kuwa hiki si kigezo cha kuchagua mume.

Kuna mambo mengi yanayofaa kuchunguzwa kabla ya watu kula yamini ya ndoa, kwa mfano kiwango cha elimu, ufahamu wa mambo, uhuru wa kusema, na kadhalika.

Kuna ukosefu wa uaminifu kati ya wanandoa.

Dadi anashuku iwapo mkewe anamwendea kinyume kimapenzi. Anashuku kuwa Kidawa ana uhusiano mwingine wa kimapenzi na Mwalimu Mkuu.

Alipanga kumfuata mkewe kazini usiku mmoja kwa nia ya kumfumania na ‘mpenzi wa kando’ ili athibitishe kuwapo kwa uhusiano wa kimapenzi kati yao.

Alipopanda ghorofani na kuchungulia dirishani, alibaini kuwa hakukuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi, ila kwa bahati mbaya alianguka na kuumia vibaya.

Kujipamba na kujirembesha kwa Kidawa kunamtia Dadi shaka. Anashuku kwamba mkewe amejipamba kwa ajili ya kumfurahisha Mwalimu Mkuu. Dadi anapokosa kutambua urembo wa mkewe, Kidawa anakasirika kutokana na fikra potovu za mumewe.

Kuna changamoto tele katika kusaidiana, hasa lijapo suala la majukumu ya nyumbani. Dadi anapokosa kuondoa na kuviosha vyombo baada ya kula, Kidawa anakasirika sana.

Baadhi ya watu huchunguza na kusema mengi sana dhidi ya wanandoa. Bi Zuhura anamuuliza Dadi iwapo amemaliza samaki amuuzie au amebakiza wa kumpikia mkewe nyumbani. Dadi anakasirika kwa vile suala la atakayepika halikufaa kumhusu Bi Zuhura hata kidogo. Aliona kuwa anajipenyeza kwa mambo ya ndani ya ndoa kati yake na Kidawa.

Mwandishi anajadili kazi wazifanyazo wanawake walioolewa. Ni changamoto kubwa kwa Kidawa kufanya kazi ya umetroni ambayo humlazimu kukosekana nyumbani usiku. Mchana huwa akifanya biashara ya kuchuuza bidhaa. Kidawa hana wakati kabisa wa kuwa nyumbani na kumhudumia mumewe.

Hali hii pamoja na kujirembesha kwake hasa anapoenda kazini kunamfanya Dadi aanze kushuku kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na Mwalimu Mkuu.

Kuna tofauti kubwa katika viwango vya elimu. Inabidi Kidawa ambaye amesoma hadi darasa la kumi na mbili amtafsirie Dadi baadhi ya maneno ya Kiingereza.

Wivu unamfanya Kidawa kutotaka kumwona Dadi akiwatazama na kuvutiwa na wanawake waliojipamba kwa mavazi na vipodozi. Anamuonya mumewe akome kuwatazama wanawake wa aina hiyo.

Tatizo la mawasiliano ni changamoto nyingine. Dadi alisongwa na fikra iwapo Kidawa alijipamba kwa ajili yake au Mwalimu Mkuu. Kidawa alipomweleza ni kwa ajili yake, hakusema lolote. Kidawa alipomweleza Dadi kuwa ilifaa aviondoe vyombo na kuviosha maadamu yeye alipika, alinyamaza. Hakumuuliza Kidawa iwapo alimpenda Mwalimu Mkuu. Badala yake, anapanga njama ya kuwafumania kisiri ambapo matokeo yake ni yeye kujidhuru.

MIGOGORO NA SHAKA

Dadi anavutana na hisia ndani yake. Anashuku iwapo Kidawa ana uhusiano wa kimapenzi na Mwalimu Mkuu. Hali hii inamfanya kununa na kupanga kuwafumania wawili hao wakila uroda, ambapo alianguka na kuumia vibaya.

Kuna mvutano hasa Dadi anapomtaka mkewe Kidawa aache kazi ya umetroni. Anashuku kwamba Kidawa humwendea kinyume kimapenzi kila anapoelekea kazini usiku. Pia kuna mgogoro kati ya Kidawa na Dadi kwa sababu ya biashara anayoifanya ya kuchuuza bidhaa. Dadi alitaka kumkataza mkewe asitembeze bidhaa tena. Kidawa asingekatazika kwa vile daima alimrejesha Dadi kwa masharti ya ndoa ya kisasa.

Mvutano mwingine unatokana na mavazi yanayovaliwa na wanawake. Dadi anawatazama na kuvutiwa na wanawake kutokana na mavazi yao pamoja na kujirembesha kwao. Kidawa anamkataza ila anasongwa na fikra hasa akikumbuka jinsi mwanamke aliyeolewa anavyojipamba na kujipeleka kwa mwanamume mwingine.

Kuna mgogoro unaotokana na majukumu ya nyumbani. Kidawa anataka Dadi aviondoe vyombo mezani na kuviosha maadamu yeye alipika. Anataka wasaidiane. Dadi anapokataa, Kidawa anamkasirikia. Kujirembesha na kujipamba kwa Kidawa kunamtia Dadi wasiwasi tele. Kidawa alijirembesha ili ampendeze mumewe. Badala yake, Dadi anawaza kwamba kujirembesha huko kwa Kidawa ni kwa sababu ya Mwalimu Mkuu.

Mvutano unasababishwa pia na tofauti za viwango vya elimu na ufahamu wa mambo kati ya Kidawa na Dadi. Inabidi Kidawa ayatafsiri baadhi ya maneno katika lugha ya Kiswahili ili Dadi aelewe. Dadi angezumgumza na Kidawa ili aiondoe shaka ya kwamba mkewe anahusiana na Mwalimu Mkuu kimapenzi, ila aliongozwa na ujinga. Anaparamia paipu ili athibitishe hayo. Hatimaye anaanguka na kuumia.

ELIMU

Ili kufanikisha elimu, Mwalimu Mkuu hana budi kutia bidii kazini. Anakwenda kufanya kazi usiku ili kuzipunguza. Walinzi waliwajibika kuwalinda wanafunzi shuleni. Walipowasikia watu wakimtaja mwizi, walifika ghafla jengoni na walipomuona Dadi amepanda juu ya paipu, walidhani ni mwizi aliyekuwa akiwachungulia wasichana.

Kidawa anafanya kazi ya umetroni kwa bidii ili awalinde wasichana bwenini wakati wa usiku. Tofauti katika viwango vya elimu husababisha kutoelewana na mvurugano katika ndoa.

VITUKO: Sindwele amfurusha Msodai nyumbani kwa Pengo kwa kukerwa na maudhi yake

NA SAMUEL SHIUNDU

MSODAI alipochapuka kutoka nyumbani mwa jiraniye Pengo, alibisha kwa Pengo. “Karibu ndani shemeji, naelekea madukani narejea.” Alikaribishwa na Felistus aliyezoea kumshemeji kila mtu. Msodai alifumwa na gere dhidi ya Pengo kwa bahati hii ya mke mzuri.

Msodai aliwakuta Pengo na Sindwele wakizungumza. Sindwele alimtazama mgeni huyu na akili yake ikamwambia kuwa aliwahi kuwona japo hakukumbuka ni wapi haswa walipoonana. ‘Haikosi tulikutana katika hizi lewa lewa zangu’ alijiambia akijaribu kukumbuka.

‘Lakini malevini wapi hasa? Huku Sidindi? La!’ aliendelea kujiuliza na kujijibu. Hakuwa na mazoea ya kulewa nje ya mipaka ya Maka. Alikuwa jogoo wa Maka ambaye hakudiriki kulewa Sidindi. ‘Potelea pote, itanisaidia nini nikijua tulikokutana?’ alijiambia hatimaye.

“Nimerejea kukujulia hali” Msodai alimjuza Pengo. Sindwele aligundua kuwa sauti ya mwanamume huyo haikubeba huruma hata kidogo. Akazidi kushawishika kuwa aliwahi kuisikia mahali fulani.

“Naona ungali tu ulivyokuwa tulipokuwa hapa” Msodai aliendelea kuroroja kwa sauti iliyobeba uchokozi na kero. Hakujua kuwa alikuwa anaupanda mchongoma ambao kuushuka ingekuwa noma. Sindwele hakumvumilia, “Hivyo sivyo mtu azungumzavyo. Kumbe hilo jichwa lako tupu?.” Alimuuliza.

“Kwani utado?” Msodai alimuuliza Sindwele kwa dharau. Sasa Sindwele alimkumbuka huyu mwanamume asiye na nidhamu. Waliwahi kukutana katika baa ya Jamhuri.

Alikumbuka jioni ile Pengo alipozindua kampeni za kuwania ukatibu wa chama cha walimu hapo baani Aliyakumbuka maneno ya bwana huyu yaliyobebwa na sauti la kilevi, ‘Pengo gani nazo zisizokwenda kwa daktari zikachopekwa meno?’ ndivyo alivyobwata mwanamume yuyu huyu jioni hiyo huko Jamhuri.

Sindwele alikumbuka jinsi mwanamume huyu alivyoapa kuwa hangempa Pengo kura hata kwa uchawi. Sasa alimfuma barabara kwa jicho la chuki. “Usiniangalie hivyo wewe!” Msodai alibwata

“Fanya heshima ndugu Msodai. Huyu ni rafiki yangu na hapa ni kwangu” Pengo alimkumbusha Msodai. “Usijali bwana Pengo. yaelekea amesahau kilichompata miaka mawili iliyopita .”Sindwele alikaulisha. Kwa hakika Pengo na Msodai hawakukumbuka hayo ya miaka mawili iliyopita.

“Akili yako imelegeza skrubu. Mimi sikujui wala sikumbuki lolote lililotukia miaka mawili iliyopita.” Msodai alijibu kwa takaburi. “Yangu imelegeza skrubu na yako ikakwenda mafyongo. Si wewe ndiye yule mlevi aliyetumwa na Kadenge kuuvuruga mkutano wa ndugu Pengo hapa. Umesahau ulivyonyanyuliwa vibaya vibaya na kufurushwa pakashume?” Sindwele alimkumbusha.

Msodai sasa alikumbuka yaliyompata. Sindwele akamshauri kuufyata na kuondoka au afurushwe kwa mara nyingine.

Msodai hakusubiri yafike huko. Akaondoka.

VITUKO: Nia fiche ya Farida kumfichulia Pengo njama ya Mwinyi na Tumbo

Na SAMUEL SHIUNDU

Walifika faraghani na kuagiza chakula. Pengo hakula nyama kwa sababu za kidini. “Huu ni mwezi mtukufu wa pasaka aisee! Lazima tususie kila jambo linalotupa raha’ Hili lilimgutusha Farida.

Akatambua kuwa kakutana na mwanamume mwenye msimamo mkali wa kidini. Hakujua kama hii kauli ya Pengo kuhusu ‘kila jambo la raha’ ilihusisha pia yale yaliyomsumbua roho.

Hapo naye akaomba apewe soda baridi kwa keki. Hakutaja pombe asije akadhaniwa mhuni na muumini huyu. Hakuna mwanamke ambaye hujiachilia na kuonyesha udhaifu wake kwa mwanamume kwa mara ya kwanza. Kwake stara ilikuwa ngao iliyomsaidia kuvishinda vita vingi vya aina hii. Akajitunza na kunyenyekea.

Baada ya jambo-sijambo, Farida alimfichulia mwenzake lililowakutanisha katika mkahawa huo. Alimweleza jinsi alivyoyasikiliza mazungumzo kati ya Tumbo na Mwinyi.

“Nilisikia wakizungumzia kitu kama ‘interdiction’. Mwanzoni sikujua maana ya neno hilo. Lakini baada ya kulitafitia, nikagundua kuwa ni jambo kama, kufutwa kazi.” Farida alimfafanulia mwenzake kabla ya kuendelea, “Na anayepangiwa njama hii si mwingine ila wewe mpenzi” akampasulia mbarika hatimaye.

‘Yakoje haya masikio basi?’ Pengo alijiuliza kwa mshangao. Alijua kuwa Mwinyi hakumpenda, lakini hakujua kuwa uhasama wao ulikuwa umefikia kiwango hiki. Akameza mate machungu huku akimsikiliza Farida aliyekuwa akirogonya kama muumini aliyepandwa na roho wa ndimi, “Nilipogundua hili nikajiambia kuwa si haki kabisa!

Si haki kwa kijana mwema kama wewe kupatwa na nakama hii! Ndipo nilipoikumbuka methali ya kikwetu isemayo kuwa, asiyetahadhari hugaagaa kwenye mapito ya majitu.

Nimekuita nikujuze utahadhari kabla ya hatari. Wajua tena ilivyo vibaya kukumbwa na balaa huku mwenyewe huna habari? Wanasema wahenga kuwa, nzi asiye na mshauri huuandama mzoga hadi kaburini. Singetaka uwe nzi huyu.”

Pengo alikumbuka siku aliyokutana na huyu binti Farida kwa mara ya kwanza. Hakuwahi kufikiria kuwa angemfaa. Aliaibika kwa kumpuuza awali. “Sasa nitafanyaje maskini?” Pengo alishangaa.

Kwa kulisikia swali hili la Pengo, Farida alijiwa na matumaini ya kuvuna alilolilenga. Akampa habari nyingine nzuri. “Swala lako lilinikeshesha na kuniliza hadi kisima changu cha machozi kikakauka. Nimekwishazungumza na mkuu wa shule ya Baraka kule Sidindi. Akaniambia umwone.

Mwinyi aliposema wewe wa nini kumbe kunao wanaojiuliza watakupata lini?” Farida alimliwaza kwa misemo ya kikwao.

Pengo alimshukuru Farida kwa fadhila zake. Shilingi mia tatu zikamtoka kulipia chakula chao. Wakaagana na kuahidiana wakutane kesho yake Pengo atakaporejea kutoka Sidindi.