Idadi ndogo ya wanaojiandikisha wawe wapigakura yashuhudiwa kwenye vituo mbalimbali

Na SAMMYWAWERU

SIKU mbili baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuzindua rasmi shughuli ya kuwasajili wapigakura wapya, idadi ya wanaojitokeza ingali ya chini mno.

Jumatatu, Oktoba 4, IEBC ilizindua kuanza kwa shughuli hiyo ambapo inalenga kuandikisha wapigakura wapya milioni 7.2.

“Tunahimiza wale ambao hawajasajiliwa wajitokeze kwa wingi,” akasema Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati akiongoza uzinduzi huo katika Kaunti ya Nakuru.

Usajili wa wapigakura wapya unatekelezwa kote nchini, wale ambao wanataka kubadilisha vituo vya kupiga kura pia wakipewa fursa.

Kwa mujibu wa sajili ya IEBC 2017, Kenya ina wapigakura 19,611,423 waliojiandikisha.

Huku viongozi na wanasiasa wakihimiza wapigakura wapya kujisajili ili kushiriki chaguzi mkuu ujao wa 2022, idadi ya wanaojitokeza ingali ya chini.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kwamba katika maeneo kadhaa Nairobi na viunga vyake, makarani wa kuwasajili wapigakura wanashinda mchana kutwa wakisubiri watu kwa sababu wanaojitokeza ni wachache mno.

Kwa mfano, makarani eneo la Mirema, mtaa wa Zimmerman, Nairobi wanaonekana kutulia wakijishughulisha na simu kwa muda mrefu kwa kukosa watu wa kusajili.

Katika uchunguzi wetu, Jumanne kati ya saa tano asubuhi hadi saa saba mchana meza ya makarani hao ilisalia bila kupata mpigakura yeyote wa kujiandikisha.

Hali hiyo haikuwa tofauti na ya Roysambu na Carwash, maeneo yaliyoko Zimmerman.

“Idadi ya wanaojitokeza kujiandikisha ni ya chini mno,” akasema karani mmoja na aliyeomba kutochapisha jina lake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari.

Taswira ya mtaa huo, iliwiana na ile ya Githurai 44, Githurai 45, Kasarani na Mwiki.

Tabia ya Wakenya kuchelea kujitokeza kujiandikisha kama wapigakura siku za kwanza, inaashiria mazoea ambayo yamekuwa yakishuhudiwa miaka ya awali kukimbilia foleni muda unapokaribia kuisha.

Zoezi la mwaka huu linatekelezwa kwa muda wa siku 30.

IEBC hata hivyo inasema haina uhakika endapo itaongeza muda zaidi, kipindi hicho kikikamilika kwa sababu ya uhaba wa fedha kuendesha shughuli hiyo.

“Mgao tuliopata hautatosha kuzidisha siku 30 tulizopangia kuendeleza usajili wa wapigakura wapya,” akasema Prof Abdi Guliye, Kamishna wa IEBC.

Prof Guliye aidha alisema tume hiyo ina uhaba wa mashine za kuandikisha wapigakura, kila wadi ikipewa mitambo tatu pekee. Kenya ina jumla ya wadi 1,450.

Wanasiasa wabuni njama IEBC ikisajili wapigakura wapya

IDADI ndogo ya wananchi walijitokeza Jumatatu katika kaunti za Pwani kwa usajili wa wapigakura wapya, huku baadhi ya viongozi wakidaiwa kutumia mbinu chafu ili waongeze idadi katika maeneobunge yao.

Katika Kaunti ya Kisii, Mbunge wa Mugirango Kusini, Bw Sylvanus Osoro, alitishia kuwanyima basari watoto ambao wazazi wao hawatakuwa wamejisajili kupiga kura kufikia wakati shule zitakapofunguliwa muhula ujao.

Bw Osoro ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, alisema wale watakaojiandikisha kutaka basari watahitajika kuambatisha thibitisho la kuonyesha wazazi wao walijisajili kupiga kura katika ombi lao.

“Hata kama unampenda William Ruto, bila kadi ya kura hutamsaidia. Mugirango Kusini baada ya mwezi mmoja tutatangaza basari. Kama huna kadi ya kura hutapata basari. Badala ya kitambulisho tunataka kadi ya kupiga kura,” akatishia.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inalenga kusajili wapigakura wapya milioni sita kitaifa, wengi wao wakiwa ni vijana ambao hawakuwa wamefikisha umri wa miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Mbunge wa Ganze, Kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire kwa upande wake alidai kuwa baadhi ya wanasiasa walikuwa wakiendeleza njama ya kuwasafirisha wapigakura kutoka maeneo ya nje ili wajiongeze ufuasi kabla uchaguzi ujao.

Bw Mwambire aliambia Taifa Leo kuwa aliarifiwa Jumapili kuhusu mipango hiyo anayodai inaendelezwa na wapinzani wake.

“Niko na watu pembe zote ambao wanafuatilia shughuli hii ili kuhakikisha inafanikishwa ipasavyo. Niliambiwa kuwa kuna magari 10 ambayo yalikodishwa kuwachukua watu kutoka sehemu za Mtwapa, Kilifi, Tezo na sehemu nyingine,” akasema.

Bw Mwambire alisema wanasiasa katika eneobunge hilo wanaogombea kiti cha ubunge wamekuwa na desturi hiyo ambayo huwaacha wakihangaika baadaye.

Katika Kaunti ya Mombasa, vituo vingi vya kusajili wapigakura havikuwa vimepokea watu kufikia Jumatatu mchana.

Kituo kilicho katika uwanja wa Makadara, eneobunge la Mvita kilikuwa kimetembelewa na watu wawili pekee kufikia wakati huo, huku afisi ya IEBC ikipokea mmoja pekee.

Wakazi wengi waliohojiwa na Taifa Leo walisema hawakujua kama usajili ulikuwa unaendelea.

“Nilikuwa nimekuja hapa kwa shughuli zangu ndipo nikafahamu kumbe usajili unaendelea. Lakini nitajisajili siku nyingine, si leo,” Bw Omar Salim, alisema akiwa Makadara.

Mratibu wa uchaguzi katika eneobunge la Mvita, Bi Neema Karisa, alisema watazunguka katika wadi zote ili kufikisha lengo lao la kusajili wapigakura wapya 24,651.

Akizindua shughuli ya usajili katika Kaunti ya Nakuru, Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, alisema usajili utafanywa kila siku ikiwemo wikendi kwa siku 30.

“Tunawaomba Wakenya hasa vijana wajitokeze kwa wingi kujisajili,” akasema Bw Chebukati.

Ripoti za Maureen Ongala, Eric Matara, Valentine Obara na Wachira Mwangi

Wanasiasa wasukuma ngome zao kujisajili

Na WANDISHI WETU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inaanza leo Jumatatu shughuli ya kusajili wapigakura kote nchini huku Naibu wa Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wakiweka mikakati ya kuhakikisha wanapata wapigakura wapya wengi katika ngome zao.

Dkt Ruto ameagiza wandani wake katika Bonde la Ufa, kuanzisha kampeni kabambe kuhakikisha kuwa vijana wanajitokeza na kusajiliwa kuwa wapigakura katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Viongozi hao, wakiongozwa na maseneta Susan Kihika (Nakuru), Aaron Cheruyoit (Kericho); wabunge David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki), Liza Chelule (Nakuru), Samuel Tonui (Kuresoi Kusini), Samuel Gachobe (Subukia), Soipan Tuya (Narok); na magavana Hillary Barchok (Bomet), Paul Chepkwony (Kericho), wanaamini hatua hiyo itasaidia Dkt Ruto ambaye ametangaza kuwania urais kujipatia kura nyingi katika uchaguzi mkuu ujao.

Bi Kihika alifichua kuwa kampeni hiyo inaendelea katika kaunti zote za Bonde la Ufa, ikiwemo Narok na Kajiado.

Wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, wakiongozwa na Gavana Lee Kinyanjui na mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama, pia wameanzisha kampeni ya kuhimiza vijana kuenda kujisajili kuwa wapigakura.

Wandani wa Dkt Ruto wanalenga kuhakikisha kwamba angalau watu 809,583 wanasajiliwa kuwa wapigakura katika eneo la Bonde la Ufa.

Shughuli ya kusajili wapigakura wapya kwa wingi inang’oa nanga leo Jumatatu na itaendelea hadi Novemba 2, 2021.

IEBC inalenga kusajili wapigakura wapya milioni 6 kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Katika ngome ya Bw Odinga, Gavana wa Siaya Cornel Rasanga ameahidi kutunuku watu watakaosajiliwa kuwa wapigakura huku Gavana wa Kisii James Ongwae akitoa ahadi sawa na hiyo.

Wabunge wakiri IEBC imepungukiwa na fedha za uchaguzi

Na CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kulalamikia kupungukiwa na fedha za kufadhili matayarisho ya uchaguzi mkuu ujao, bunge linaonekana kuingilia kati suala hilo.

Mnamo Jumatano, Septemba 29, 2021, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Kanini Kega alitangaza kuwa wanachama wa kamati yake na wale wa Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria watakutana na makamishna wa tume hiyo kujadili suala hilo.

Alitoa tangazo hilo kwenye kikao na wanahabari baada ya kukutana na wanne kati ya makamishna saba wa IEBC wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera.

“Tunakubali kwamba IEBC inakabiliwa na upungufu wa fedha za kuandaa uchaguzi mkuu. Hii ndio maana tumeafikiana na makamishna hawa walionitembelea kwamba tutakutana nao kuchambua bajeti hiyo kwa lengo la kuziba mapengo yaliyopo,” Bw Kega akawambia wanahabari afisini mwaka katika jumba la KICC baada ya kufanya mashauriano na makamishna hao.

“Ninaweza kuthibitisha kuwa katika mwaka wa kifedha uliopita tulitengea IEBC Sh10 bilioni na katika mwaka huu wa kifedha tume hii imetengewa Sh16 bilioni. Sasa inakabiliwa na upungufu wa Sh14 bilioni kutokana na bajeti yake ya Sh41 bilioni,” akeleza.

“Kwa hivyo, tumekubaliana kwamba tutafanya mkutano na makamishna hawa pamoja na wenzetu wa JLAC ili tujadili suala hili la bajeti na masuala yote yanayohusu matayarisho ya uchaguzi mkuu wa 2022. Mkutano huo utafanyika wiki ijao,” Bw Kega, ambaye ni Mbunge wa Kieni akaongeza.

Alisema kuwa katika mkutano huo ambao utafanyika Mombasa, IEBC itapata nafasi ya kuwafafanulia wabunge jinsi itakavyotumia bajeti ya Sh41 bilioni.

“Tukishawishika kuwa bajeti hiyo ina mantiki hatutasita kuiuliza Hazina ya Kitaifa iongezee IEBC fedha katika Bajeti ya kwanza ya ziada itakayowasilishwa mwishoni mwa Oktoba mwaka huu,” Bw Kega akaeleza.

Alisema kuwa haja kubwa ya bunge ni kuiwezesha IEBC kuendesha uchaguzi mkuu kwa njia huru, haki na itakayoaminika na wadau wote.

Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wameisuta IEBC kwa kupandisha bajeti yake kupita kiasi bila sababu maalum.

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya alisema hali hiyo inaashiria ubadhirifu wa pesa za umma ihali tume hiyo inaweza kuendesha shughuli hiyo kwa kiasi cha chini cha fedha kuliko Sh40.9 bilioni.

“India hutumia kiasi kidogo cha fedha kuendesha uchaguzi ikilinganishwa na Kenya ilhali ina idadi kubwa ya wapiga kura. IEBC inatuchezea shere kwa kuweka bajeti kubwa kiasi hiki,” akasema Bw Kimunya ambaye ni Mbunge wa Kipipiri.

“Hatuwezi kutumia Sh40 bilioni kila baada ya miaka mitano kugharamia uchaguzi. Ina maana kuwa kuna dosari kubwa katika tume hii,” akasema.

Lakini Bw Chebukati ametumia majukwaa kadhaa kutetea bajeti hiyo ya Sh40.9 bilioni akisema fedha hizo zitaiwezesha IEBC kuendesha uchaguzi kwa kuzingatia masharti ya kuzuia kuenea kwa Covid-19.

“Bajeti hii itatuwezesha kuwa na wapiga kura 700 katika kila kituo cha kupigia kura kulingana na mahitaji ya sheria,” akaeleza.

CHARLES WASONGA: IEBC iruhusu Wakenya wote walio ughaibuni wapige kura

Na CHARLES WASONGA

KULINGANA na takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) mwezi jana, Wakenya wanaoishi na kufanya kazi katika mataifa ya ng’ambo walituma nyumbani Sh341 bilioni mnamo 2020.

Kiwango hiki kinawakilisha ongezeko la asilimia 10.7 zaidi ya Sh308 bilioni walizotuma nchini mnamo 2019.Wakenya wanaoishi nje waliongeza kiwango cha pesa wanazotuma nyumbani licha ya makali ya ugonjwa hatari wa Covid-19 yaliyovuruga chumi za mataifa yote ulimwenguni.

Pesa hizi huwekezwa katika miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo humu nchini kando na kugharamia mahitaji mbali mbali ya Wakenya hawa.

Kwa hivyo, Wakenya hawa wana usemi kuhusu namna pesa wanazotuma nyumbani hutumika na serikali iliyoko mamlakani ambayo hukusanya ushuru kutoka kwa miradi na mipango wanayofadhili.

Chini ya kivuli hiki, wenzetu hawa, wapatao 3.5 milioni, wanaoishi na kufanya kazi katika mataifa mbalimbali wana haki ya kushiriki, hususan, katika uchaguzi wa urais.

Isitoshe, baadhi yao hufadhili vyama vya kisiasa na baadhi ya wagombeaji viti mbalimbali.Kwa hivyo, sikubaliani na tangazo la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba ni Wakenya wanaoishi katika mataifa 11 pekee ndio wataruhusiwa kushiriki uchaguzi wa urais 2022.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema kuwa wenzetu wanaoishi Amerika ni miongoni mwa wale ambao wataruhusiwa kujisali kuwa wapiga kura kwa ajili ya kupiga kura za urais.

Wengine watakaoruhusiwa kushiriki shughuli hii ya kidemokrasia ni wale wanaoishi Canada, Uingereza, Muungano wa Milki za Kiarabu (UAE), Qatar na Sudan Kusini.Katika chaguzi za 2013 na 2017 ni Wakenya 3,000 pekee walioko Tanzania, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini waliruhusiwa kupiga kura ya urais.

IEBC inafaa kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa itakapoanza shughuli ya usajili wa wapiga kura wapya mnamo Oktoba 4, 2021 Wakenya katika mataifa yote ambako Kenya ina afisi za ubalozi waruhusiwe kushiriki.

Shughuli hiyo ya usajili iendeshwe katika afisi hizo za kibalozi chini ya usimamizi wa maafisa wa serikali wanaohudumu katika mataifa husika.

IEBC inalenga kusajili jumla ya wapiga kura wapya 9.2 milioni, miongoni mwao ikiwa ni vijana 5.2 milioni ambao watakuwa wametimu umri wa miaka 18 kufikia 2022.

Kwa hivyo, itakuwa makosa kwa IEBC kupuuza sehemu kubwa ya Wakenya 3.5 milioni walioko katika mataifa ya nje kando na 11 ambayo Bw Chebukati alitaja wiki jana.

Hii ni licha ya kwamba watu hawa hutuma mabilioni ya fedha nchini kupiga jeki shughuli za maendeleo.Kuishi au kufanya kazi mataifa ya nje kusiwe sababu ya kumnyima Mkenya haki yake ya Kikatiba ya kushiriki shughuli za kidemokrasia nchini.

IEBC iruhusu Wakenya wote wanaoishi ughaibuni wajisajili kuwa wapiga kura ili washiriki uchaguzi mkuu ujao.

Chebukati aonya dhidi ya kampeni hizi za mapema

Na WINNIE ATIENO

TUME ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), imeonya wanasiasa dhidi ya kampeni za mapema zinazoendelea kuzua joto la kisiasa na taharuki nchini.

Tume hiyo pia imetangaza kuwa haina fedha za kutosha kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Akiongea wakati wa hafla ya kuwakaribisha makamishna wapya wa IEBC, Bi Juliana Cherera, Bw Francis Wanderi, Bi Irene Masit na Bw Justus Nyang’aya, mwenyekiti wa tume hiyo Bw Wafula Chebukati alisema ni sharti wapewe fedha za kuandaa uchaguzi mkuu kulingana na bajeti yao.

Bw Chebukati alisema uchaguzi mkuu ujao utagharimu Sh40.9 bilioni kulingana na bajeti yao.

Hata hivyo, Hazina ya Kitaifa iliwapa Sh26.5 bilioni.

“Tuna upungufu wa fedha za kuandaa uchaguzi na ni lazima tutimize bajeti yetu ili tusimamie uchaguzi mkuu kikamilifu. Tunahitaji Sh14.6 bilioni ili tutimize malengo yetu ya uchaguzi mkuu ujao,” alisisitiza.

Bw Chebukati alionya wanasiasa dhidi ya uchochezi wakati wa kampeni zao za mapema alizosema ni kinyume cha sheria.

Alisema kulingana na sheria, kampeni zinafaa kuanza miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.

Baadhi ya wanasiasa walio na azma ya kugombea urais akiwemo Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, wamekuwa wakifanya mikutano kujipigia debe.

Bw Chebukati alisema kulingana na mipango ya uchaguzi, wanasiasa wanafaa kuanza kampeni miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.

“Kampeni za mapema na joto la siasa zinaendelea kuzua taharuki, tunawasihi wanasiasa kuwa waadilifu na kuhakikisha hawachochei umma,” aliongeza.

Hata hivyo, alisema IEBC inaendelea kushirikiana na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Idara ya Mahakama, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na idara ya polisi kukabiliana na wanasiasa wachochezi.

Alisema wameshirikiana na vyombo hivyo ili pia kuhakikisha usalama unadhibitiwa wakati wa uchaguzi mkuu.

“Tunataka vyombo hivyo kuhakikisha usalama na amani inadumishwa wakati wa uchaguzi. Tumekongamana hapa Mombasa na NCIC, Mahakama, Kiongozi wa Mashtaka na idara ya polisi kujadili namna ya kudhibiti usalama wakati wa uchaguzi,” alisema Bw Chebukati.

Wakati huo huo, Bw Chebukati alitangaza kuwa makamishna hao watashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuendesha uchaguzi huru bila mapendeleo.

Makamishna wa awali walikuwa na mzozo na kulumbana mara kwa mara, chanzo kilichopelekea wengine kujiuzulu na hata aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Ezra Chiloba kusimamishwa kazi.

Hata hivyo, Bw Chebukati alisema kundi jipya la makamishna limetangaza kujitolea mhanga kushirikiana kuendesha uchaguzi wa huru.Makamishna hao wapya waliapa kutekeleza wajibu wao kwa haki.

“Nimejiunga na IEBC kuleta uwiano na tunawaahidi Wakenya mwamko mpya,” alisema kamishna Justus Nyangaya.

Bi Juliana Cherera ambaye alikuwa mfanyakazi katika Kaunti ya Mombasa alisema watashirikiana kutekeleza wajibu wao.

“Tunataka Wakenya watulie waone kazi yetu murwa,” alisema.

Bw Chebukati alisema mwezi ujao IEBC itaanza usajili wa wapiga-kura kote nchini wakitarajia wapiga-kura milioni sita wapya.

Aliwaomba Wakenya walio na umri wa miaka 18 na zaidi wajitokeze kwa shughuli hiyo.

IEBC yakana ‘kumsaidia’ Ruto

Na WANDERI KAMAU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumanne ilikanusa madai kuwa inashirikiana kisiri na mrengo wa ‘Hustler Nation’ wake Naibu Rais William Ruto kumsaidia kuvumisha azma yake kuwania urais 2022.

Madai hayo yalienezwa kwenye mitandao ya kijamii, yakidai kuwa IEBC inausaidia mrengo huo kwenye harakati za kujiandaa kwenye uchaguzi huo.

Madai hayo, ambayo yalisambazwa kwenye mtandao wa Facebook, pia yalidai kuwa tume imefungua akaunti ya YouTube, kuusaidia kupeperusha masuala yanayohusiana na mipango yake.

Lakini kwenye taarifa, tume ilitaja madai hayo kuwa uvumi, ambapo lengo lake ni kuiharibia sifa.

“Madai yanayoenezwa dhidi yetu si ya kweli. Zaidi ya hayo, akaunti ya YouTube tunayodaiwa kuimiliki ni ghushi na si yetu. Tumeuarifu usimamizi wa YouTube kuhusu madai hayo ili kuwachukulia hatua wahusika,” ikaeleza tume.

Madai hayo yanajiri wiki chache baada ya wabunge kadhaa wa chama cha ODM kusema kuwa hawana imani na tume hiyo.

Licha ya kupata makamishna 7, IEBC bado inayumba

Na LEONARD ONYANGO

HUKU ikiwa imesalia chini ya miezi 11 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2021, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ingali inakabiliwa na masaibu tele.

Utata kuhusu kandarasi ya vifaa vya kielektroniki vya kusajili na kutambua wapigakura, uhaba wa wafanyakazi, marekebisho ya baadhi ya sheria zinazohusiana na uchaguzi na sintofahamu kuhusu usajili wa wapigakura, bado ni changamoto kubwa zinazokumba IEBC.

Wito wa kumtaka mwenyekiti wa tume hiyo Bw Wafula Chebukati ajiuzulu kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama cha ODM pia huenda ukatatiza maandalizi ya uchaguzi.

Viongozi wa ODM, wakiongozwa na mwenyekiti wao John Mbadi wanataka Bw Chebukati asisimamie uchaguzi mkuu ujao huku wakidai kwamba Wakenya wamepoteza imani naye.

Viongozi wa ODM wamekuwa wakidai kuwa mwenyekiti wa IEBC anaegemea upande wa Naibu wa Rais William Ruto – madai ambayo Bw Chebukati ameyakanusha vikali.

Tayari IEBC imevuka kizingiti cha kwanza baada ya makamishna wanne; Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya kuapishwa Alhamisi kujaza nafasi zilizoachwa wazi na Roslyne Akombe, Nkatha Maina, Margaret Mwachanya na Paul Kurgat waliojiuzulu miaka mitatu iliyopita.Tangu 2018, IEBC imekuwa ikiendeshwa na Bw Chebukati, Abdi Guliye na Boya Molu.

Uamuzi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kwamba IEBC inahitaji kuwa na angalau kuwa na makamishna watano kuendesha shughuli zake zinazohusiana na sera ulizua hofu kwamba baadhi ya maandalizi ya uchaguzi yaliyofanywa na watatu hao huenda yakafutiliwa mbali.

Bodi ya Kukagua Zabuni za Umma (PPARB) Alhmisi ilifutilia mbali mchakato wa utoaji wa kandarasi ya ununuzi wa vifaa vya kielektroniki vya kusajili na kutambua wapigakura na kupeperusha matokeo (KIEMS).

SHERIA

Bodi ya PPARB ilisema kuwa IEBC haikufuata sheria katika kutangaza zabuni hiyo mnamo Aprili, mwaka huu.Mnamo Agosti 11, mwaka huu, Risk Africa Innovatis Ltd –ambayo ni kampuni ya Kenya – ilishtaki IEBC kwa bodi ya PPARB ikisema kuwa tume hiyo ilikiuka sheria kwa kufungia nje kampuni za humu nchini.

PPARB iliagiza IEBC kutangaza upya kandarasi hiyo ndani ya siku 45 zijazo. Hiyo inamaanisha kwamba shughuli ya utoaji wa kandarasi ya vifaa vya KIEMS huenda ikajikokota hadi Novemba, mwaka huu.

IEBC pia inakabiliwa na shinikizo za kuitaka kutotumia KIEMS za kampuni ya Idemia Securities Ltd (ambayo awali ilifahamika kama OT Morpho) iliyotumiwa 2017 lakini ikafeli siku ya uchaguzi. IEBC inahitaji tableti 55,000 za kusajili na kutambua wapigakura na kupeperusha matokeo katika vituo 53,000 kote nchini.

Mwanakandarasi atakayepewa zabuni hiyo pia atahitajika kununua mtambo wa kuhifadhi taarifa za wapigakura (sava).Sava ya sasa ina uwezo wa kuhifadhi taarifa za wapigakura milioni 20 tu.IEBC inalenga kusajili wapigakura wapya milioni 6 mwishoni mwa mwaka huu.

Kujikokota kwa kandarasi hiyo kunamaanisha kuwa huenda shughuli ya kusajili wapigakura wapya ikafanyika kati ya Januari na Machi mwaka ujao.IEBC tayari imetangaza nafasi 7,540 za makarani wa usajili wa wapigakura, wasimamizi 1,450 na wataalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) 580.

Makataa ya kutuma maombi yalikamilika Agosti 27, mwaka huu, na makarani wa muda watakaoajiriwa kwa muda, watalazimika kungojea kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza kazi.Kulingana na mwongozo wa utendakazi wa 2020-2024, IEBC inakumbwa na uhaba wa wafanyakazi wa kudumu 290.

Kwa mfano, katika idara ya ICT ambayo hushughulika na masuala ya kidijitali, usalama wa sava ya wapigakura, kupeperusha matokeo na masuala ya intaneti, kuna uhaba wa wafanyakazi 13.

Wafanyakazi hao wapya wanahitaji kuajiriwa mapema ili kupata muda wa kutosha kupewa mafunzo kuhusiana na vifaa vipya vya KIEMS vitakavyonunuliwa.Tume ya IEBC pia ilipanga kushawishi Bunge kufanyia marekebisho sheria sita zinazohusiana na uchaguzi kabla ya Agosti 2022.

Miongoni mwa sheria inayolengwa kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022 ni Sheria ya Matumizi ya ICT katika uchaguzi ambayo tume inasema kuwa sheria ya sasa inakanganya.

Sheria nyingine ambayo IEBC iko mbioni kuhakikisha kuwa inarekebishwa ni kuhusu usajili wa wapigakura katika mataifa ya kigeni.

IEBC inasema ukosefu wa takwimu kuhusu idadi ya halisi ya Wakenya walio katika kila nchi ni changamoto kubwa katika usajili wa wapigakura walio ughaibuni.

Idadi ya Wakenya wanaoishi ughaibuni walio katika daftari la wapigakura ni 4,224, kwa mujibu wa IEBC.

Linda Katiba wasema waliopendekezwa kuteuliwa makamishna wa IEBC hawafai

Na CHARLES WASONGA

VUGUVUGU la Linda Katiba limeelezea kutoridhishwa kwake na ufaafu wa watu wanne walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kujaza nafasi nne za makamishna wa IEBC.

Wakiongea jijini Nairobi Jumatano, viongozi wa vuguvugu Bw Martha Karua na Dkt David Ndii walisema wanne hao hawakuwa bora zaidi kielimu na kitajriba kusimamia shughuli za uchaguzi.

Francis Wanderi, Justus Abonyo, Juliana Cherera na Irene Cherop waliopendekezwa na Rais Kenyatta Agosti 5, 2021 kujaza nafasi za Dkt Roselyne Akombe, Consolata Nkatha Bocha, Mary Mwanjala na Dkt Paul Kurgat waliojiuzulu mnamo Aprili 18, 2018.

“Inavunja moyo kwamba jopo hilo halikutupatia watu ambao ndio bora zaidi kwa majukumu ya makamishna wa IEBC. Japo huenda wanne hao wamesoma kiasi cha haja, siamini kwamba wana tajriba hitajika kuendesha uchaguzi,” Bi Karua akasema.

Kwa upande wake Dkt Ndii aliwataka wabunge kuhakikisha kuwapiga msasa wanne hao kuhakikisha kuwa wanne hao ni wale ambao wana uzoefu na weledi wa kuendesha uchaguzi.

“Ikiwa hawatakuwa na sifa hizo, basi wabunge wawakatae na nafasi hizo zipewe wengine wengi waliohojiwa na ambao tunaamini wanahitimu kwa kazi hii,” akaeleza Dkt Ndii bila kutaja wale ambao wanawapendelea kwa nyadhifa hizo.

Jopo la uteuzi wa makamanisha wa IEBC chini ya uongozi wa Bi Elizabeth Muli waliwahoji jumla ya watu 36 mwezi jana katika juhudi zake za kusaka watu wanaohitimu kuhudumu kama makamishna wa tume hiyo.

IEBC motoni kuhusu pesa za kampeni

Na WINNIE ONYANDO

WABUNGE Jumatano waliishutumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kuchapisha kanuni kuhusu ufadhili wa kampeni za uchaguzi mkuu kabla ya bunge kuziidhinisha.

Wakiongozwa na mbunge wa Mbeere Kaskazini Charles Njagagua, wabunge hao walidai IEBC ilitaka kulilaumu bunge kwa kukosa kupitisha kanuni hizo, na kuzichapisha bila kufuata utaratibu ufaao.

“Ni wazi kwamba kanuni hizi zinapaswa kuidhinishwa angalau mwaka mmoja kabla ya uchaguzi. Huwezi kuziwasilisha dakika za mwisho, na hata kuzichapisha katika gazeti rasmi la serikali bila idhini ya bunge. IEBC inataka kutulaumu bure,” akafoka Bw Njagagua, ambaye ni naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu sheria ndogondogo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Funyula, Bw Wilberforce Oundo alisema kanuni hizo zilitayarishwa bila umma kushirikishwa, inavyohitajika kikatiba.

“Mambo yanabadilika kila siku. Mkondo wa siasa na matumizi ya pesa miaka minne iliyopita hauwezi kufananishwa na mwaka huu. Kwa hivyo, maoni ya wananchi yalipasa kushirikishwa wakati wa kuandaliwa kwa kanuni hizi zitakazotumika mwaka ujao,” akasema Bw Oundo.

Kauli yake iliungwa mkono na mwenzake wa Gilgil, Martha Wangari aliyesema IEBC kama tume ya kikatiba, haifai kuonekana kuvunja katiba hiyo.

“Tunafahamu kuwa kanuni hizi hazikubadilishwa tangu zilipotayarishwa mnamo 2016. Ikiwa mabadiliko yatafanywa, sharti bunge lihusishwe. Hilo halikufanyika. Kwa hivyo napinga kanuni hizi,” akasema Bi Wangari.

Hata hivyo, IEBC ilijitetea kuwa ilifuata taratibu zote za kisheria kabla ya kuchapisha kanuni hizo.

“Hatukuwa na nia mbaya katika kuchapisha kanuni hizi. Nia yetu haikuwa kulitenga bunge na umma kama inavyodaiwa. Tunahitaji kuomba msaada wa bunge ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka ujao ni huru na wa haki, ” akasema mwenyekiti Wafula Chebukati mbele ya wabunge hao katika majengo ya bunge, Nairobi.

Meneja wa Ufadhili wa Kampeni, Bi Salome Oyugi, aliyeandamana na Bw Chebukati, pia alitetea IEBC akisema kamati yao ilikuwa tayari kuwasilisha sheria hizo bungeni mwaka wa 2017 ili zijadiliwe, ila bunge likaahirisha mchakato huo.

Ni uchaguzi wa masonko 2022

WINNIE ATIENO na VALENTINE OBARA

MABILIONI ya pesa yataanza kumiminika kitaifa hivi karibuni, baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuchapisha viwango vya fedha ambazo wanasiasa watakubaliwa kutumia kuendesha kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na gazeti rasmi la serikali lililochapishwa jana, wanasiasa wanaotaka kuwania viti mbalimbali kuanzia udiwani hadi urais watakuwa huru kutumia mamilioni ya pesa kwenye kampeni zao.

Ingawa IEBC imeweka viwango vya juu vya pesa, bila shaka kuna wale watakaotumia ujanja kuvipitisha kwa kuwa hakuna mfumo mwafaka wa kufuatilia gharama za kampeni za wanasiasa wote.

Haya huenda yakawafungia nje wananchi ambao hawana uwezo wa kifedha ilhali wana uwezo wa kuwa viongozi wasifika.

Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati jana alitoa wito kwa wabunge kupitisha sheria zinazohusu matumizi ya fedha za kampeni ili mwongozo waliotoa utekelezwe kikamilifu.

“Tunaomba bunge lipitishe sheria hizo ambazo tuliweza kupeleka mswada wao bungeni 2016, ili tuwe na usimamizi bora kuhusu ufadhili wa kampeni za wanasiasa. Sisi tumechapisha viwango ambavyo vinafaa kutumiwa katika gazeti rasmi la serikali inavyohitajika kisheria. Hiyo itawezesha wadau kutoa mchango wao kama wangependa kuwe na marekebisho,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika kongamano la wadau wa uchaguzi lililoandaliwa na Shirikisho la Wahariri la Kenya (KEG) katika Kaunti ya Mombasa, ambapo alizidi kushinikiza serikali iongezee tume yake pesa ili kusimamia vyema uchaguzi unaotarajiwa kugharimu Sh40.3 bilioni.

IEBC itahitaji pia Sh588 milioni kugharamia mahitaji ya kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

Wawaniaji urais watakubaliwa kutumia kiwango kikubwa zaidi cha fedha, ambacho ni Sh4.4 bilioni.

Katika viti vilivyosalia, viwango ambavyo wanasiasa wanatakikana kutumia vitategemea ukubwa wa maeneo na idadi ya watu katika maeneo hayo.

Wawaniaji ugavana katika Kaunti ya Turkana ndio watakubaliwa kutumia kiasi kikubwa zaidi cha pesa miongoni mwa wagombeaji wote wa ugavana, ambacho ni Sh123 milioni.

Kaunti hiyo inafuatwa na Nairobi (Sh117.3 milioni), Marsabit (Sh114.8 milioni) na Wajir (Sh103.8 milioni).

Kaunti ambapo magavana watahitajika kutumia kiwango kidogo zaidi cha pesa ni Lamu (Sh21.9 milioni), na Tharaka-Nithi (Sh23.1 milioni).

Mwongozo huo wa kisheria unaonyesha kuwa, viwango ambavyo wabunge wataruhusiwa kutumia ni tofauti kuanzia Sh11 milioni katika baadhi ya maeneobunge kama vile Wundanyi, hadi Sh94 milioni eneobunge la Horr Kaskazini.

Katika wadi zote nchini, wale wanaotaka kuwania udiwani pia watakubaliwa kutumia viwango tofauti kuanzia takribani Sh2 milioni katika wadi nyingi hadi Sh17.9 milioni ilivyo katika Wadi ya Lokori/ Kochodin iliyoko Kaunti ya Turkana.

Kulingana na IEBC, viwango hivyo vyote ni tofauti na kiasi cha Sh17.7 bilioni ambacho vyama vya kisiasa vitakubaliwa kutumia kwa kampeni zao.

Pesa hizo hupangiwa kutumika kugharamia mahitaji kama vile malipo ya viwanja vya kampeni, vyombo vinavyotumiwa, matangazo, malipo ya maafisa na wahudumu wa kampeni na maajenti wa uchaguzi, uchukuzi, mawasiliano, usalama miongoni mwa mahitaji mengine.

Kwa kawaida, kampeni nchini kuanzia mashinani hadi urais huvutia mwembwe za kila aina.

Ni wakati huo ambapo wanasiasa hutaka kuonyesha ubabe wa jinsi wanavyoweza kusafiri kutoka pembe moja ya nchi hadi nyingine kwa saa chache wakitumia helikopta, na uwezo wao kutifua vumbi na tope kila wanapopitia barabara mbovu mashinani wakitumia magari makubwa makubwa.

Hata hivyo, kumekuwa na visa ambapo pesa hutumiwa kwa mambo yanayokiuka sheria za uchaguzi kama vile kugharamia uchochezi wa kisiasa, ghasia na kuhonga wananchi

“Visa vya uhongaji viliripotiwa hata katika chaguzi ndogo ambazo zilifanyika majuzi. Tunatarajia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atachukua hatua kuhusu madai yaliyotolewa. Taratibu za maadili ya uchaguzi zitatumiwa kikamilifu wakati wa kampeni. Wanasiasa watovu wataadhibiwa na vyama vya kisiasa vinavyovunja sheria vitaadhibiwa,” Bw Chebukati alisema Jumatatu.

Kulingana na IEBC, kulikuwa na visa 71 vya uvunjaji sheria ambavyo viliripotiwa mnamo 2017 ambapo watu 31 walishtakiwa na kupatikana na hatia.

Wakati huo huo, Bw Chebukati ameonya vyama vya kisiasa kwamba, orodha za wawaniaji ubunge na useneta watakazowasilisha lazima zizingatie sheria ya usawa wa jinsia, la sivyo hazitaidhinishwa.

Licha ya mjadala unaoendelea kuhusu uwezekano wa uchaguzi ujao kuahirishwa, mwenyekiti huyo alisisitiza kwamba, Uchaguzi Mkuu utaandaliwa Agosti 9 kwa vile ndivyo inatakikana kikatiba.

IEBC yasema iko tayari kutii mabadiliko yoyote ya kikatiba endapo yatatokea

Na WINNIE ONYANDO

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini, IEBC, Bw Wafula Chebukati ametangaza kuwa uchaguzi wa Agosti 2022 utafanyika jinsi ulivyopangwa.

Akitoa makadirio ya bajeti ya uchaguzi mkuu huo, Bw Chebukati alisema kuwa uchaguzi hautaahirishwa bali utafanyika kulingana na Katiba ya Kenya.

“Nimeona mipango ya kujaribu kuahirisha uchaguzi ulivyopangwa. IEBC haitachukua maoni yoyote kutoka kwa mtu yeyote au mashirika kwa kuwa ni tume inayojisimamia,” akasema Bw Chebukati.

Alisema kuwa tume hiyo inaoongozwa na Katiba ya Kenya inayosema kuwa uchaguzi utafanyika Agosti 9, 2022.

Hata hivyo, alisema kuwa ikiwa kutakuwa na mabadiliko yoyote ya kikatiba, basi IEBC itatii.

Uchaguzi huo unatarajiwa kuchukua Sh40.19 bilioni.

Kibarua cha IEBC kuandaa duru ya pili ya uchaguzi 2022

Na WANDERI KAMAU

KENYA inakabiliwa na kibarua cha maandalizi ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais, ikiwa itajipata hapo kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na wadadisi wa siasa, kuna uwezekano mkubwa Kenya kujipata hapo, ikizingatiwa huenda kusipatikane mshindi wa moja kwa moja kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo.

Huo utakuwa uchaguzi wa tatu kufanywa chini ya Katiba ya 2010 nchini, baada ya chaguzi kuu za 2013 na 2017.Kulingana na Katiba, lazima mwaniaji anayetangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa urais kupata asilimia 50+1 ya kura.

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa, kibarua kikuu kinachoziandama taasisi muhimu kama Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni kuhusu mikakati ambayo imeweka kama matayarisho ya hali hiyo.

“Lazima taasisi kama IEBC ijitokeze wazi kuwaelezea Wakenya na wadau wengine muhimu kuhusu juhudi ilizoweka kuona kuwa imejitayarisha kuandaa duru ya pili ya uchaguzi wa urais, ikiwa hilo litatokea,” asema Bw Felix Otieno, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya chaguzi.

Ingawa hadi sasa si wazi kuhusu idadi kamili ya watu ambao watajitokeza kuwania urais, ushindani mkuu unatabiriwa kuwa kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumanne, Dkt Ruto alitangaza kuwa huenda chama cha UDA kisibuni muungano wowote wa kisiasa na vyama vingine, akieleza wanalenga kukikuza chama kuwa cha kitaifa.

“Tumeona jinsi miungano ya kisiasa hugeuka kuwa majukwaa ya usaliti na udhalilishaji wakati inapovunjika. Ili kuepuka tatizo hilo, tunataka kujenga na kukuza chama chetu (UDA) kuwa cha kitaifa. Hili ni kinyume na siasa za awali, ambapo miungano ya kisiasa huwa imekitwa katika ukabila,” akasema Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuwa katika hali ambapo ushindani wa kisiasa utakuwa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga, huenda kusipatikane mshindi wa moja kwa moja.

“Hawa ni viongozi wawili wenye umaarufu karibu sawa kote nchini. Ni vigogo wanaoungwa mkono katika karibu kila pembe ya nchi. Bila shaka, hilo linamaanisha yule atakayeibuka mshindi atamshinda mwenzake kwa asilimia ndogo tu ya kura. Vivyo hivyo, yule atakayeshindwa, atashindwa kwa pengo ndogo sana,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanasema, ikizingatiwa kwa mujibu wa katiba ya sasa lazima kuwe na mshindi wa moja kwa moja, sharti wadau na taasisi husika kuhakikisha juhudi zote zimechukuliwa kuona Kenya haitajipata katika kizungumkuti cha kisiasa kama 2007.

Vile vile, wanafananisha hilo na 2017, ambapo ilimlazimu Rais Uhuru Kenyatta kubuni handisheki na Bw Odinga, kwani alikuwa akiidhibiti nusu moja ya nchi.

“Kuna hatari kubwa ikiwa IEBC na taasisi nyingine hazijajitayarisha kwa uwezekano ambapo Kenya itajipata kwenye duru ya pili ya uchaguzi.

“Sababu kuu ni kuwa kama ilivyoshuhudiwa katika miaka ya 2007 na 2017, huenda ikawa vigumu kwa kiongozi anayechaguliwa kuwa rais kuiendesha serikali, kwani atakuwa tu anaiongoza nusu moja ya nchi.

“Hivyo, itamlazimu kubuni mwafaka wa kisiasa na yule atakayeibuka wa pili kwenye uchaguzi huo, kwani kama yeye, atakuwa anaidhibiti nusu nyingine ya nchi,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Mdadisi huyo anaeleza kuwa taswira hiyo ndiyo iliyowalazimu Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Rais Kenyatta kubuni ushirikiano wa kisiasa na Bw Odinga, kwani licha ya kushindwa kwenye chaguzi hizo, bado alikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakimfuata.

“Tofauti ya ushindi wa Bw Kibaki na Bw Odinga mnamo 2007 ilikuwa ndogo sana, kiasi kwamba baadhi ya wafuasi Bw Odinga waliamini ndiye aliyeibuka mshindi. Vivyo hivyo, mnamo 2017, wafuasi wa Bw Odinga waliamini serikali ilimwibia kura zake, kwani ni kiongozi mwenye ushawishi na ufuasi mkubwa,” asema Bw Muga.

Hata hivyo, anasema hali hizo zingeweza kuepukwa, ikiwa kungekuwa na taasisi muhimu na zinazoaminika na wananchi, kama vile IEBC, Idara ya Mahakama, Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) na Idara ya Polisi.

“Mnamo 2007, Bw Odinga alisema hangeenda mahakamani kwani aliamini hangepata haki. Ni sababu hiyo ambapo aliiomba jamii ya kitaifa kuingilia kati ili kuisaidia Kenya. Vivyo hivyo, kutoaminika kwa Idara ya Mahakama mnamo 2017 ndiko kulikochangia ghasia ambazo zilitokea. Haya yalichangiwa na ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa taasisi muhimu,” asema Bw Muga.

Kwa hayo, wadadisi wanaeleza imefikia wakati wakuu wa idara hizo kuanza kuonyesha ushirikiano wa pamoja miongoni mwa Wakenya ili kujenga imani yao tunapoelekea 2022.

Licha ya hofu hizo, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati anasema wamejitayarisha kukabili hali yoyote itakayotokea, hasa baada ya Rais Kenyatta kuidhinisha majina ya watu wanne watakaojaza nafasi ambazo zimekuwa wazi katika tume hiyo.

Uhuru ajaza nafasi nne za makamishna wa IEBC

Na BENSON MATHEKA

Rais Uhuru Kenyatta jana aliteua watu wanne kujaza nafasi zilizokuwa wazi za makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Rais Kenyatta aliwasilisha kwa bunge majina ya Bi Juliana Cherera, Bw Francis Mathenge Wanderi, Bi Irene Cherop Masit na Bw Justus Abonyo Nyang’aya ili wapigwe msasa na kuidhinishwa.

Wakipitishwa na bunge, wanne hao watajaza nafasi za makamishna waliojiuzulu.Watajaza nafasi zilizoachwa na Roselyne Akombe, Paul Kurgat, Connie Maina na Margaret Mwachanya waliojiondoa baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Tangu kujiuzulu huko, IEBC imekuwa na makamishna watatu ambao ni mwenyekiti Wafula Chebukati, Profesa Yakub Guriye na Bw Boya Molu.

Wanne hao waliteuliwa kutoka kwa orodha ya watu 36 waliohojiwa na Jopokazi ya kuteua makamisha wa IEBC, ambalo liliongozwa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Dkt Elizabeth Muli.

Jopo kazi hilo lilipokamilisha mahojiano mwezi jana, Dkt Muli alisema kwamba zoezi hilo lilidhihirisha kuwa Kenya ina watu waliohitimu kuhudumia nchi yao.

Uteuzi wa wanne hao unajiri miezi miwili baada ya Mahakama Kuu kuamua kwamba bila kuwa na makamishna wote saba, shughuli za IEBC ni haramu.

Tume hiyo imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo uliotolewa na majaji watano waliozima mchakato wa BBI.

Hatua ya Rais Kenyatta kuchukua hatua za kujaza nafasi za makamishna hao wanne zilionekana kuwa za kuokoa BBI na pia maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao ambao unahitaji tume kuwa imeundwa kikamilifu ili kuendesha uchaguzi kwa utaratibu uliowekwa kisheria.

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa wajiepushe na mjadala wa kuahirisha uchaguzi

Na KINYUA BIN KING’ORI

INGAWA Mahakama ya Afrika ilitoa ushauri kwamba mataifa ya bara hili ambayo huenda yatashindwa kuandaa uchaguzi mkuu kwa sababu ya makali ya janga la virusi vya corona, yanaweza kuzingatia kuahirisha shughuli hiyo, hilo linawezekana tu ikiwa sheria za kitaifa zinakubali uahirishaji wa uchaguzi.

Kwa rai hiyo, lazima katiba ya nchi husika ifanye hivyo. Sasa viongozi wa kisiasa wameanza kutumia muda wao mwingi kulumbana juu ya maoni hayo, wameingiza siasa mapendekezo ya mahakama hiyo.

Lakini ikiwa hawatokoma, watapotosha umma kipindi hiki cha ugumu wa maisha. Inavunja moyo kusikia baadhi ya viongozi hasa wa mrengo fulani wa kisiasa wakizungumza kauli zinazoweza kuvuruga usalama na umoja wetu wakati huu tunapoelekea kipindi cha kampeni mwaka 2022.

Siasa si lazima wanasiasa wapotoshe wananchi, wanapaswa kuwa wajasiri kuelezea ukweli katika mijadala yao kisiasa. Wanaotumia nafasi yao kuendesha porojo na propaganda wanafaa kuwa wa kwanza kuchujwa katika uchaguzi mkuu ujao wa 2022.

Tukizingatia maoni ya majaji wa korti ya Afrika, sijui kwa nini baadhi ya viongozi wetu wameanza kuhisi mchecheto kwenye matumbo yao. Maoni ya korti hiyo yalichapishwa kwa lugha ya wastani ili yaweze kueleweka kwa urahisi na kwa nia njema kwa mataifa yote ya Afrika na ulimwenguni kwa jumla.

Walisisitiza wazi ikiwa taifa fulani, tuseme mfano Kenya, linaweza kuahirisha uchaguzi mkuu ujao wa 2022, ikiwa kutakuwa sababu ya kueleweka inayotokana na janga la corona, lakini lazima katiba tunayoitumia iwe inacho kipengele kinachoruhusu uahirishaji huo.

Tukizingatia katiba yetu ya 2010, uchaguzi mkuu hufanyika Jumanne ya pili ya Agosti, kila baada ya miaka mitano. Kenya inaeleweka wazi uchaguzi mkuu utafanyika siku ya Jumanne, Agosti 9 mwaka wa 2022 na hilo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imethibitisha mara si moja kila wanapoulizwa na vyombo vya habari.

Tukirejelea katiba yetu, haisemi maradhi au janga la njaa linaweza kuchangia uchaguzi mkuu kuahirishwa. Uchaguzi mkuu nchini Kenya waweza kuahirishwa tu ikiwa taifa letu (Kenya) litakuwa katika vita na taifa lingine au mataifa mengine.

Aidha, kubadilsha tarehe ya uchaguzi mkuu lazima Wakenya wenyewe wakubali kwa kubadilsha katiba na kufamyia mageuzi kipengele hicho, na hilo kutimizwa lazima tufanye hivyo kupitia kura ya maoni.

Ingawa si Mara ya Kwanza Kwa viongozi wetu kuzungumzia swala la uchaguzi mkuu kuahirishwa nchini, mazungumzo na kauli wanazotoa Kwa Sasa zimeanza kutia wakenya hofu na wengine kuanza kusadiki kweli huenda njama za kuchelewesha uchaguzi mkuu wa 2022 zikafaulishwa na serikali.

Wanaojifanya kupinga siku ya uchaguzi wa 2022 kubadilshwa hata nukta moja wacha sekondi au dakika, wanajitanua vifua wakisema watawasilisha barua kwa Baraza la usalama katika umoja wa mataifa (UN) kuelezea Kenya haiko vitani na lazima serikali iwe na mikakati bora kufanikisha zoezi la uchaguzi mkuu Kwa mujibu wa katiba.

Katika muktadha huo, ndio nauliza je, kwa nini viongozi watake kuvuruga maisha ya wananchi Kwa kuwasababishia hofu na uoga bure juu ya uchaguzi mkuu? Je, viongozi hao wanajua kuwatia raia hofu ni sawa kuwachochea kujiandaa kwa ghasia? , Je, wanao ushahidi upi kwamba kuna njama ya kuahirisha uchaguzi ujao?

 

Pendekezo vyeti vya kuzaliwa vitumike kusajili wapigakura

Na ALEX KALAMA

MAPENDEKEZO ya kutaka wananchi waruhusiwe kutumia vyeti vya kuzaliwa kujisajili kupiga kura yanaendelea kutolewa huku kukiwa na malalamishi kuhusu ugumu wa vijana kupata vitambulisho vya kitaifa.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imethibitisha kupokea mapendekezo aina hiyo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wanaotaka wananchi walio na umri wa zaidi ya miaka 18 waruhusiwe kutumia vyeti vya kuzaliwa kujiandikisha kupiga kura.

Kisheria, mtu anayetaka kujisajili kuwa mpigakura huhitajika kuwa na kitambulisho cha kitaifa au paspoti halali.

Msimamizi mkuu wa IEBC katika Kaunti ya Kilifi, Bw Abdul Wahid Hussein, alisema wito huo wa wanasiasa tayari umekuwa ukiungwa mkono na baadhi ya wananchi.

Hata hivyo alisisitiza kuwa kwa sasa mfumo huo hauwezi kutumiwa kwani sheria za uchaguzi haziruhusu.

“Tumepokea mapendekezo ya baadhi ya wananchi kwamba wale vijana walio na umri wa zaidi ya miaka 18 wasajiliwe kuwa wapigakura kwa kutumia vyeti vya kuzaliwa. Tunataka kuwaambia kwamba vyeti hivyo vinakosa baadhi ya matakwa yanayohitajika ili kumsajili mtu kuwa mpigakura,” alisema Bw Hussein.

Mapendekezo hayo yalikuwa yametolewa na baadhi ya wanasiasa wakiongozwa na diwani wa wadi ya Gongoni, Bw Albert Kiraga na Kiongozi wa Chama cha Kadu Asili, Bw Gerald Thoya.

Wanaounga mkono pendekezo hilo walidai kuwa inawezekana kutumia vyeti hivyo kwa vile ndivyo hutumiwa na serikali kuwasajili watahiniwa wa mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE bila dosari.

Bw Thoya vile vile alisema kumekuwa na ulegevu katika ofisi husika ya usajili wa vitambulisho, hali inayowafanya wakazi wengi kususia kuenda kuchukua vitambulisho vyao.

“Endapo IEBC itakubali ombi hilo basi wananchi wengi watakumbatia mpango huo wa kujisajili kupiga kura,” akasema.

Wiki iliyopita wakati wa mahojiano ya wawaniaji nafasi ya kamishna wa IEBC, wakili Florence Jaoko aliyehojiwa kwa wadhifa huo pia alitoa pendekezo sawa na hilo.

Bw Hussein alieleza matumaini kuwa wananchi wengi watajitokeza kujiandikisha kupiga kura katika Kaunti ya Kilifi kabla uchaguzi wa mwaka ujao.

Wakati huo huo, Chama cha Kadu Asili kinawataka viongozi wa kisiasa kupunguza cheche za maneno ambazo huenda zikaleta migawanyiko miongoni mwa wananchi.

Akizungumza afisini mwake mjini Malindi, Bw Thoya alionya kuhusu joto la kisiasa na kuhimiza viongozi kuazimia zaidi kuunganisha taifa.

Bw Thoya alishauri jamii kujiepusha na wanasiasa wachochezi wakati huu taifa hili linapojianda kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022 na kudumisha umoja.

“Ningependa kuwasihi wananchi wote kuwaepuka viongozi wachochezi ambao wanakataa juhudi za kudumisha umoja. Pia navisihi vitengo husika kulishughulikia swala hilo,” alisema Bw Thoya.

IEBC imeainisha wazi mazingira ya kituo cha kura – Chebukati

Na SAMMY WAWERU

MACHIFU na manaibu wao hawapaswi kuwa katika kituo au vituo vya kura.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati alisema Alhamisi, wakati uchaguzi mdogo kuchagua mbunge Kiambaa na diwani Muguga ukiendelea, maafisa hao wa serikali hawaruhusiwi kuwa kwenye vituo vya kura.

Hii ni baada ya wafuasi na viongozi wa mgombea wa United Democratic Alliance (UDA) John Njuguna Wanjiku kutoa malalamiko yao kwamba machifu wanatumika kisiasa.

“Nilitaja makundi sita yanayopaswa kuwa kwenye kituo cha kupiga kura na machifu si miongoni mwao. Hawaruhusiwi kuwa humo,” akasema.

Alisema hayo kufuatia kisa cha chifu mmoja Kiambaa aliyefukuzwa, akisisitiza kuingia kituoni kusimamia shughuli za kupiga kura.

Baadhi ya wagombea kiti cha ubunge Kiambaa walizua hofu kuhusu machifu na manaibu wao kuonekana vituoni.

“Mazingira ya kituo cha kura ni hadi mita 400 kutoka jengo linaloendeshewa shughuli, hivyo basi yeyote asiyepaswa kuwa humo awe nje kipimo kilichopendekezwa,” Bw Chebukati akasema.

Zimesalia saa chache vituo vya kupiga kura vifungwe ili shughuli za kuhesabu kura zianze.

Je, IEBC yafaa kuanza kujiandaa kwa kura ya maamuzi kabla ya uamuzi wa mahakama kuhusu rufaa ya BBI?

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inaonekana kuanza maandalizi ya kura ya maamuzi ilhali hatima ya mchakato huo haijaamuliwa na mahakama ya rufaa.

Hii ni baada ya tume hiyo, Jumatano, kutangaza zabuni ya ununuzi karatasi za kupigia kura zitakazotumika katika kura ya maamuzi na uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na tangazo lilichapishwa katika gazeti la ‘Daily Nation‘ IEBC inazitaka kampuni zenye uwezo wa kufanya kazi hiyo ziwasilishe maombi kwa idara ya ununuzi kupitia barua pepe.

“IEBC inaalika zabuni za uwasilishaji wa karatasi za uchaguzi, sajili za wapiga kura, fomu za kutangaza matokeo katika vituo vya kupigia kura, fomu za kutangaza matokeo ya uchaguzi na kura ya maamuzi katika vituo vya kuanzia ngazi ya eneo bunge, wadi hadi kitaifa,” likasema tangazo hilo likiongeza kuwa zabuni hiyo itadumu kwa miaka mitatu.

Tangazo hili la IEBC linaonyesha kuwa IEBC inajiandaa kwa kura ya maamuzi kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba ya BBI hata ingawa Mahakama ya Rufaa haijatoa uamuzi wake kuhusu iliyowasilishwa kupinga uamuzi mahakama kuu iliyoharamisha mchakato huo.

Majaji wa mahakama kuu, Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Chacha Mwita na Teresia Matheka katika uamuzi waliotoa Mei 13, pia walisema kuwa mchakato wa BBI ulikiuka Katiba ya Kenya.

Japo ni taratibu ya kawaida kwa IEBC kutangaza zabuni ya uchapishaji na uwasilishaji wa karatasi za kura na bidhaa nyinginezo hitaji uchaguzi mkuu unapokaribia, uagizaji wa bidhaa za kuendesha kura ya maamuzi ni dalili kwamba tume hiyo pia inajiandaa kwa zoezi hilo tata.

Uamuzi kuhusu kesi hiyo ya rufaa iliyowasilisha na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na kiongozi wa ODM Raila Odinga, utatolewa mnamo Agosti 20, 2021.

Tangazo hilo la IEBC limekasirisha wakosoaji wa mchakato wa marekebisho ya Katiba wakisema imetolewa kwa nia mbaya na inakiuka amri ya mahakama kuu “ambayo haitajabatilishwa”.

“Tunaona nia mbaya katika tangazo hili. Aidha ya bidhaa ambazo IEBC inataka kununua zinaonyesha kuwa tume hii imekiuka amri ya mahakama kuu ambayo iliizuia kuandaa kura ya maamuzi,” akasema mawakili Ian Mwiti na Dudley Ochiel waliowakilisha Jack Mwimali aliyepinga kesi iliyowasilishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga katika mahakama ya rufaa.

“Pia kuna agizo la mahakama linalozuia tume kuanza maandalizi yoyote ya kura ya maamuzi. Lakini IEBC imepuuza agizo hili. Imetangaza zabuni ya ununuzi wa bidhaa kuendesha kura ya maamuzi. Hatua hii imechukuliwa kwa nia mbaya,” akasema Bw Mwiti.

Alisema IEBC ilifaulu tu kuzuia utekelezaji wa uamuzi kwamba haiwezi kuendeleza shughuli zake kwa sababu haina idadi tosha ya makamishna.

Na Bw Ochiel alisema kuwa mahakama kuu ilizuia IEBC kufanya chochote kuhusiana na suala la uhalali wa kura ya maamuzi ambalo bado halijaamuliwa na mahakama ya rufaa.

Wakili huyo pia alisema hatua ya IEBC kutangaza zabuni ya ununuzi wa bidhaa za uchaguzi inaonyesha kuwa tume hiyo imeonyesha kuwa inafahamu uamuzi wa mahakama ya rufaa.

“Hatua hii ya IEBC pia inaandaa mazingira bora kwa watetezi wa mchakato wa marekebisho ya katiba, jambo ambalo halionyesha haki kwa upande wa utetezi katika kesi hiyo ambayo uamuzi wake utatolewa Agosti 20,” akasema Bw Ochiel.

Wakili huyo aliongeza kuwa tume hiyo inaweza kushtakiwa kwa kudharau agizo la mahakama.

Kauli hiyo pia ilitolewa na wakili Elias Mutuma ambaye aliwakilisha chama cha Thirdway Alliance katika kesi yake kupinga mswada wa BBI katika mahakama kuu.

“Hatua hiyo ya kutangaza zabuni ni ukiukaji wa wazi wa agizo la mahakama. Hii ni licha ya kwamba IEBC inawajibu waa kuheshimu Katiba hii ambayo inahimiza kuheshimiwa kwa maagizo ya mahakama,” akasema Bw Mutuma.

Lakini kaimu mkurugenzi mkuu wa tume hiyo Hussein Marjan alitetea hatua hiyo ya IEBC ya kutangaza zabuni za ununuzi bidhaa za kura ya maamuzi na uchaguzi, akisema ni sehemu tu ya maandalizi ya tume hiyo.

“Zabuni hiyo inalenga kupata mchapishaji atakayefanya kazi na IEBC katika miaka mitatu ijayo. Tunataka mchapishaji ambaye atatuchapia na kutuwasilishia bidhaa za uchaguzi hitaji likitokea ndani ya kipindi hicho,” Bw Marjan akanukuliwa akisema.

Katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2021/2022 iliyosomwa bungeni Juni 13, mwaka huu, IEBC imetengewa Sh15 bilioni za kufadhili maandalizi ya uchaguzi mkuu. Hazina ya Kitaifa haikutenga fedha zozote kwa ajili ya kura ya maamuzi.

Mnamo Julai 1, 2021 Shirika la Trend and Insights For Afrika (TIFA) lilitangaza matokeo ya kura ya maamuzi yaliyoonyesha kuwa mchakato wa BBI sio maarufu miongoni mwa Wakenya.

Kulingana na matokeo hayo, ni asilimia 19 pekee na Wakenya waliohojiwa waliosema kuwa wako tayari kushiriki katika kura ya maamuzi na kupiga kura ya “NDIO”.

Kulingana na matokeo hayo, asilimia 31 ya waliohijiwa walisema kuwa watapiga kura ya “LA” endapo shughuli hiyo ingefanyika wakati huo, Juni 20 hadi Juni 30, 2021, utafiti huo ulipoendeshwa.

IEBC yalaumu polisi kwa vurugu za chaguzi ndogo

Na WALTER MENYA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati amelaumu polisi kwa kushindwa kudumisha usalama wakati wa chaguzi ndogo za hivi majuzi zilizokumbwa na ghasia.

Haya yanajiri huku ikiibuka kuwa tume imewasilisha ripoti ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Juja kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), ikimlaumu Gavana wa Kiambu, Bw James Nyoro na Mwakilishi wa Kike wa Kaunti hiyo, Bi Gathoni Wamuchomba kwa uhalifu katika uchaguzi na kutaka washtakiwe.

Kwenye hotuba kali katika hafla iliyoandaliwa na Shirika la Elections Observation Group (ELOG) Ijumaa jioni, Bw Chebukati alitaja visa ambavyo maafisa wa polisi waliotumwa kudumisha usalama katika chaguzi ndogo za majuzi walikataa kutii maagizo ya maafisa wa tume, kuhamishwa kwa maafisa wakuu wa polisi siku chache kabla ya chaguzi hizo na kutotumwa kwa maafisa wa kutosha katika vituo vya kupigia kura.

Bw Chebukati alidai kwamba Inspekta Jenerali wa polisi, Bw Hillary Mutyambai, amekataa ombi la kukutana na tume kutafuta njia za kuzuia ghasia kwenye chaguzi ndogo zijazo.

“Moja ya changamoto kuu zinazokabili mfumo wa uchaguzi nchini Kenya ni ukosefu wa usalama wakati wa uchaguzi ambao umefanya ghasia kuongezeka ilivyoshuhudiwa kwenye chaguzi ndogo za majuzi. Hii ni kinyume cha msingi wa uchaguzi huru na wa haki ambao haufai kuwa na ghasia na vitisho kulingana na ibara ya 81(e)(ii). Swali ambalo tunafaa kupata majibu ni wapi au ni nani aliye na jukumu na wajibu wa kuzuia au kukabili ghasia na vitisho wakati wa uchaguzi,” alisema Bw Chebukati.

Hafla ya Elog iliandaliwa kukabidhi mamlaka kutoka kwa aliyekuwa mwenyekiti Bi Regina Opondo hadi kwa mwenyekiti mpya, Bi Anne Ireri.

Maafisa wa polisi wanaotumwa kudumisha usalama wakati wa uchaguzi huwa maafisa wa uchaguzi kulingana na sheria ya uchaguzi ya Kenya ya 2011.

Kama maafisa wa uchaguzi, sheria inawahitaji wafuate maagizo ya IEBC. Hata hivyo, Bw Chebukati alisema kwamba katika chaguzi ndogo za majuzi, tume ilishuhudia maafisa waliotumwa kudumisha usalama wakitazama ghasia zikiendelea katika vituo vya kupigia kura na kujumuisha matokeo.

Kulingana naye, maafisa hao walikataa kuchukua maagizo halali kutoka kwa tume watulize ghasia na pia walikataa kuchukua hatua kuzuia ghasia kutokea.

Chaguzi ndogo zilifanyika majuzi wadi za Ganda, Dabaso, London na Rurii na maeneo bunge ya Msambweni, Matungu, Kabuchai, Bonchari na Juja. Chaguzi hizi zote zikikumbwa na ghasia, kukamatwa kwa maajenti wa baadhi ya vyama vya kisiasa na madai ya hongo.

Kufuatia ghasia zilizotokea kwenye chaguzi ndogo za Bonchari na Juja, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alitoa taarifa akishutumu polisi na maafisa wa serikali ambao hakutaja majina kwa ghasia hizo.

“Tulichoshuhudia katika chaguzi ndogo za Bonchari na Juja ni matumizi mabaya ya nguvu za polisi na onyesho la kutenda makosa pasipo adhabu kulikotekelezwa na maafisa wakuu wa serikali wanaojitakia makuu na kujipiga vifua,” alisema Bw Odinga.

“Vikosi vya usalama ni vya kuhudumia watu na si kutekeleza maslahi ya wale wanaofanya majaribio ya kisiasa,” aliongeza Bw Odinga.

Chebukati ashuhudia maandalizi ya uchaguzi wa Juja

Na LAWRENCE ONGARO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilikamilisha maandalizi yake Jumatatu ambapo katika shule ya upili ya Mang’u High, maafisa wake walihakikisha vifaa vya uchaguzi wa eneobunge la Juja vilikuwa tayari.

Maafisa wa uchaguzi wa IEBC walionekana wakiendelea na mikakati ya kupanga masanduku ya kura na kuyasambaza katika vituo 184.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, alifika katika kituo kikuu cha shule ya upili ya Mang’u High na kusema mipango yote iko shwari.

Alisema chaguzi mbili za ubunge za Juja na Bonchari, Kisii zitaendelea kama kawaida licha ya kizingiti kilichowekwa na mahakama kuu kuwa tume hiyo haistahili kuendesha uchaguzi wowote kutokana na idadi chache ya makamishna walioko afisini. Kwa sasa ina makamishna watatu.

“Uamuzi uliotolewa na mahakama hapo awali, wa mwaka wa 2019, ni kwamba mahakama kuu ilisema ya kwamba afisi ya IEBC inaweza kuendesha uchaguzi na maafisa watatu afisini na kwa hivyo tutaendelea na chaguzi hizo mbili,” alisema Chebukati.

Hata hivyo alisema tume hiyo itapinga uamuzi uliotolewa Alhamisi wiki jana na mahakama kuu ambapo majaji watano walitoa hukumu kuhusu uhalali wa afisi yao yenye makamishna watatu walioko kwa sasa baada ya wengine kujiuzulu.

Alisema maafisa wa usalama wamewekwa wa kutosha ambapo ana imani ya kwamba kila kitu kitaendeshwa jinsi ilivyopangwa.

Alisema uchaguzi huo wa Juja ungeng’oa nanga saa kumi na mbili za alfajiri hadi saa kumi na moja jioni ambapo baadaye wataanza kuhesabu kura katika ukumbi mkuu wa shule ya Mang’ u High.

Uchaguzi huo umevutia wawaniaji 10 huku ushindani mkali ukitarajiwa kuwa kati ya Bi Susan Njeri Waititu, mkewe marehemu Francis ‘Wakapee’ Waititu, wa chama cha Jubilee na Bw George Koimburi wa chama cha People Empowerment Party (PEP) kinachohusishwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Kulingana na sheria na kanuni za afya mikutano ya watu wengi ilipigwa marufuku kama njia mojawapo ya kupunguza kuenea kwa Covid-19.

Hali hii ilisababisha wawaniaji wengi kuwa na changamoto ya kukutana na umati mkubwa wa wananchi kuwashawishi.

Afisa mkuu wa IEBC wa Juja Bw Justus Mbithi, amewahimiza wapigakura zaidi ya 115,000 kujitokeza kwa wingi ili kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Hatimaye Uhuru atangaza nafasi za makamishna IEBC

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta hatimaye ametangaza nafasi nne za makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwa wazi. Hatua hiyo imetoa nafasi ya kubuniwa kwa jopo la kujaza nafasi hizo.

Nafasi hizo zilibaki wazi kufuatia kujiuzulu kwa makamishna Roselyne Akombe, Consolata Maina, Margaret Mwachanya na Paul Kurgat.

Kulingana na sheria, Rais Kenyatta anapaswa kutangaza nafasi za makamishna zinazobaki wazi katika muda wa siku saba baada ya kupokea barua za kujiuzulu, lakini hakufanya hivyo.

Hii ina maana kuwa Rais Kenyatta alivunja sheria kwani imemchukua miaka mitatu kutangaza nafasi hizo kuwa wazi. IEBC imekuwa ikihudumu na makamishna watatu ambao ni pamoja na Bw Chebukati, Profesa Abdi Yakub Guliye na Bw Boya Molu.

Kumekuwa na miito ya kujazwa kwa nafasi hizo kutoka kwa wanasiasa lakini hilo halingewezekana bila rais kuzitangaza kuwa wazi au kuvunjwa kwa tume hiyo.

Bw Chebukati amewahi kulaumu bunge kwa kutoweka sheria za kufanikisha kujazwa kwa nafasi za makamishna wa tume.Mwaka jana, Bi Maina aliteuliwa naibu balozi nchini Italia sawa na Bi Mwachanya aliyetumwa Pakistan naye Bw Kurgat akatumwa Urusi.

IEBC yaidhinisha wawaniaji 6 wa ubunge Juja

Na LAWRENCE ONGARO

TUME ya uchaguzi ya IEBC iliwaidhinisha wagombezi sita wa ubunge katika kiti cha Juja. Zoezi hilo lililofanyika mnamo Jumatatu, lilimuidhinisha Bi Susan Njeri Waititu mjane wa marehemu Francis ‘ Wakapee’ Waititu atakaye peperusha mbendera na tikiti ya Jubilee.

Wengine walioidhinishwa huku wakijiandaa kuwania kiti hicho na tikiti ya ( Independent), ni Bw James Marungu Kariuki, Dkt Joseph Gichui, Bw Kariuki Ireri, Bw Chege Kariuki na Zulu Thiong’o.

Bi Waititu alikiri kuwa wao kama wawaniaji kiti hicho watapitia changa moto ya kujumuika na wapigaji kura kwa vikundi vikubwa.

Alisema wakazi wa Juja wangependa kuona mirandi yote yaliyoanzishwa yanakamilika ilivyopangwa.

” Iwapo nitapata hiyo nafasi ya kuwakilisha wakazi wa Juja bila shaka ajenda hizo zitaangaziwa zaidi,” alisema Bi Waititu.

Lakini hata hivyo alisema atatumia njia ya mtandao na mawasiliano na pia kutundika picha zake hadharani.

Afisa mkuu wa IEBC katika kaunti ndogo ya Juja, Bw Julius Mbithi, aliwahimiza wawaniaji wote wafuate mikakati yote iliyowekwa na wizara ya afya ili kukabiliana na homa ya covid-19.

Aliwajulisha wawaniaji hao kuwa sasa wana nafasi ya kuwania kiti cha Juja baada ya kuidhinishwa kirasmi na tume hiyo.

Uchaguzi mdogo wa Juja unatarajiwa kuendeshwa mwezi Mei 18, 2021, huku ukitarajiwa kuwa na upinzani mkali.

Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake Bw Francis ‘ Wakapee’ Waititu, kufariki baada ya kuugua saratani ya ubongo kwa zaidi ya miaka miwili.

Bw Kariuki ambaye pia anawania kiti hicho na tikiti ya (Independent), alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba wanafuata maagizo yote yaliyowekwa na wizara ya afya.

” Tunaelewa vyema kuwa kuna changa moto lakini tutahakikisha tunawafikia wapigaji kura kwa njia ya mitadao na pia kutundika picha maeneo tofauti,” alifafanua .

Kiti cha ubunge cha Juja kimevutia wagombezi 10 ambapo wengine wanne waliosalia wataidhinishwa na tume ya uchaguzi mnamo Jumanne asubuhi.

Baadhi ya waliosalia ni Bw George Koimburi ( People Empowerment Party). Halafu kuna Anthony Kirori (Maendeleo Chap Chap), Eunice Wanjiru ( The National Democrat) na Kenneth Gachuma ( National Liberal Party).

IEBC yasaka ardhi kuhamisha makao

Na PATRICK LANG’AT

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza mpango wa kuhamisha afisi zake hadi nje ya jiji ili kuzuia mali yake kuharibiwa wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi siku zijazo.

IEBC ina afisi zake katikati mwa jiji la Nairobi katika jengo la Anniversary Towers karibu na Chuo Kikuu cha Nairobi na sasa inapendekeza ihamishie makao yake kwenye ekari tano ya ardhi kilomita 20 nje ya jiji ili kuzuia hasara iliyotokea mwaka wa 2017.

Jengo hilo limekuwa makao makuu ya IEBC kwa muda wa miaka 13.

“Ardhi tunayoazimia kuhamia itakuwa kilomita 20 kutoka katikati mwa jiji na itakuwa ekari tano. Pia lazima iwe inaweza kufikiwa kwa urahisi kupitia barabara zilizotengenezwa vizuri.

“Pia lazima iwe na hatimiliki yake na iwapo imekodishwa basi lazima iwe imesalia chini ya miaka 60 kabla ya muda huo kukamilika,” ikasema IEBC kwenye taarifa ya zabuni katika magazeti ya hapa nchini mnamo Machi 16.

Tangazo hilo lilitiwa saini na kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Hussein Marjan. Wale ambao wana ardhi na wanataka kuiuzia IEBC wamepewa hadi Machi 30 ili kuwasilisha fomu zilizojazwa.

“Tume itaendelea kutafuta pesa za kuhakikisha kuwa inafadhili mradi huo. Afisi za sasa ziko katika jengo ambalo lina afisi nyingine pia na lina msongamano mkubwa. Hii huzua changamoto kubwa hasa wakati wa uchaguzi ambapo shughuli huwa nyingi,” akasema Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati alipofika mbele ya kamati ya bunge kutoa ripoti ya kila mwaka ya matumizi ya fedha za tume hiyo.

IEBC imekuwa ikilipa kodi ya Sh100 milioni kila mwaka na kiasi hicho hakijumuishi fedha zinazotumika kuandaa mafunzo kwa wafanyakazi wa tume hiyo pamoja na mikutano mingine.

“Kupatikana kwa ardhi hiyo na kujengwa kwa afisi mpya kutasaidia tume kupunguza gharama zake hasa katika ulipaji kodi na kukodisha maeneo ya kufanyia mikutano na kuandaa mafunzo kwa wafanyakazi wake. Pia kutakuwa na nafasi za kutosha kuhifadhi vifaa vyake,” akasema Bw Chebukati mnamo 2018, wazo hilo lilipokumbatiwa.

Mnamo 2016, kinara wa ODM, bW Raila Odinga aliongoza wafuasi wake kuandaa maandamano karibu na afisi hizo wakimtaka aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC, Issack Hassan abanduke, wakidai hakuwa na uwazi katika kuandaa uchaguzi mkuu wa 2017.

Ripoti ya Muungano wa Wafanyabiashara wa Sekta ya Kibinafsi (KEPSA) ilisema zaidi ya Sh120 milioni zilipotea wakati wa maandamano hayo huku zaidi ya biashara 500 zikivurugwa na kufungwa wakati huo.

Mnamo 2017, mbunge wa Starehe, Bw Charles Njagua alitaka IEBC iondoe makao yake makuu katika jengo la Anniversary Towers ambalo liko katika eneobunge lake.

Echesa akamatwe mara moja – Chebukati

MACHARIA MWANGI Na SAMMY WAWERU

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw Wafula Chebukati amekashifu vikali tukio ambapo aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa alionekana akimzaba kofi afisa mmoja wa tume hiyo eneo la Matungu, Kaunti ya Kakamega mapema Alhamisi.

Kwenye video, Bw Echesa alinaswa akimuangushia kofi afisa huyo wa IEBC kufuatia uchaguzi mdogo unaoendelea eneobunge hilo.

Tukio hilo lilitendeka katika kituo cha Shule ya Msingi ya Bulonga, wakati shughuli za kupiga kura zilikuwa zinaendelea.

Akizungumza baada ya kuzuru kituo cha kupigia kura cha Kiwanja Ndege, Naivasha, Bw Chebukati ameitaka idara ya polisi kumkamata mara moja waziri huyo wa zamani, huku akilaani tukio hilo.

“Uvamizi huo ni hatia, na ninaihimiza idara ya polisi kumtia nguvuni mhusika, achukuliwe hatua kisheria,” Bw Chebukati akaambia wanahabari.

Mwenyekiti huyo wa IEBC alisema chaguzi ndogo zinazoendelea maeneo kadha nchini ni za amani, ila matukio yaliyoshuhudiwa katika eneobunge la Matungu na Wadi ya London, Kaunti ya Nakuru.

Bw Chebukati alisema ni makosa kwa maajenti wa vyama kuzuru vituo tofauti vya kupigia kura kwa madai wanafuatilia shughuli ya upigaji kura.

Duru zinaarifu maafisa wa polisi wamezingira makazi ya Echesa yaliyoko eneo la Shibale, Mumias ya Kati, Kaunti ya Kakamega.

Idara ya polisi inahoji waziri huyo alihepa baada ya kumzaba afisa wa IEBC.

Kwenye video inayosambaa mitandaoni, Bw Echesa anaskika akitaka kuelezwa kwa nini maajenti wa chama cha UDA na ambacho kinahusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, walifurushwa kwenye kituo cha kura.

Katika ziara yake Naivasha, Bw Chebukati alisisitiza kwamba IEBC imejitolea kuhakikisha chaguzi ndogo zinazoendelea maeneo tofauti nchini ni za huru, haki na uwazi.

Mbali na visa vya Matungu – Kakamega na London – Nakuru, Bw Chebukati alisema hakujaripotiwa matukio yenye uzito.

Aliwataka maafisa wa IEBC kuhakikisha sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao wa ugonjwa wa Covid-19 zinatiliwa mkazo.

Shirika lataka IEBC izuiwe kukagua saini

Na BRIAN OCHARO

SHUGHULI za uthibitishaji saini za wapigakura kuhusu mchakato wa Mpango wa Maridhiano wa BBI, huenda ikakumbwa na changamoto baada ya shirika moja la kutetea haki za binadamu kuishtaki Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Katika kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya Mombasa, shirika la Muslims for Human Rights (Muhuri), linasema kuwa tume hiyo haijaweka wazi mambo maalum ya kisheria na kikatiba yanayoiwezesha kuendesha zoezi la uthibitishaji wa saini.

“IEBC haina hifadhi ya data inayofaa ya wapiga kura kwa ajili ya kutekeleza shughuli hiyo kama inavyotakiwa na katiba,” Muhuri inasema.

Ombi hilo linatokana na mawasiliano kati ya shirika hilo na tume hiyo, ambapo IEBC imeshindwa kutoa majibu ya kuridhisha kwa maswali yake.

Shirika hilo mnamo Desemba 15 liliwasilisha ombi kwa tume hiyo likitafuta maelezo kuhusiana na utaratibu huo wa uthibitishaji saini.

Shirika hilo lilitaka kujua kiwango cha pesa zilizotengwa kuendesha shughuli hiyo.

Katika barua hiyo, shirika hilo lilitaka kujua ikiwa kulikuwa na kanuni au miongozo ya kuendesha mchakato wa uthibitishaji wa saini na pia ikiwa IEBC ina nakala za saini wapiga kura wote waliosajiliwa.

Lakini katika majibu yake, tume hiyo ilisema haina hifadhi ya data ya saini za wapigakura waliosajiliwa, na kuongeza kuwa inahifadhi tu taarifa kuhusu wapigakura waliojiandikisha.

Shirika hilo linasema kuwa katika majibu ambayo IEBC iliipatia, ilizungumza tu juu ya taratibu ambazo imeweka katika shughuli hiyo bila ya kutoa maelezo zaidi jinsi taratibu hizo zitatumika katika uthibitishaji wa saini.

Hazina ya Kitaifa imeidhinisha IEBC kutumia Sh93.7 milioni kwa zoezi hilo. IEBC ilianza mchakato huo mnamo Desemba 30, mwaka jana.

Shirika hilo linashangaa jinsi IEBC itakavyothibitisha saini milioni 4.4 bila hifadhi ya data ya saini za wapigakura wote waliosajiliwa, ambayo imekiri kwamba haina.

“Kwa hivyo mwenendo wa IEBC kuendelea kutekeleza zoezi la uthibitishaji bila hifadhi ya data ya kuaminika ya saini za wapigakura na mfumo wa kuridhisha wa udhibiti wa viwango vya uhakiki ni ukiukaji wa mamlaka yake ya kikatiba.”

Pamoja na mapungufu haya, shirika hilo linasema kuwa kesi yake inastahili kupewa kipaumbele na kusikizwa.

Shirika hilo sasa linataka IEBC izuiliwe kuthibitisha Mswada wa Sheria ya Katiba ya Kenya (Marekebisho) ya 2020 uliowasilishwa kwake na jopo la BBI mnamo Desemba 10.

Pia, Shirika hilo linataka IEBC na Mwenyekiti wake Wafula Chebukati au maafisa wake wazuiliwe kuthibitisha au kuthibitisha kuwa hati hiyo inakifikia matakwa ya Kifungu cha 257 (4) na (5) hadi mfumo kamili wa kisheria, pamoja na kanuni zinazoongoza shughuli hiyo kubuniwa.

Kesi hiyo imeratibiwa kusikizwa Januari 14.

IEBC yaomba radhi kwa kuita BBI ‘Burning Bridges Initiative’

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumatano ililazimika kuomba msamaha baada ya kurejelea mpango wa maridhiano (BBI) kama “Burning Bridges Initiative” badala ya “Building Bridges Initiative”.

Awali, kwenye ujumbe katika akaunti yake ya Twitter, tume hiyo ilitumia maneno hayo kimakosa ilipokuwa ikitangaza kuanza kwa mchakato wa ukaguzi wa sahihi kuunga mkono mageuzi ya Katiba kupitia BBI.

Lakini baada ya Wakenya mitandaoni kulalamika, IEBC ilituma taarifa ikifafanua kuwa ujumbe huo ulitokana na makossa ya tahajia (typographical error) “ambayo haiwakilishi msimamo wa tume hii.”

“Mapema leo (Jumatano), tume hii iliweka ujumbe kuhusu uzinduzi wa zoezi ya ukaguzi wa sahihi za wafuasi wa BBI. Hata hivyo, kulikuwa na hitilafu ya kitahajia kwenye ujumbe huo ambayo hayakukusudiwa. Kosa hili haliwakilisha msimamo wa tume au wafanyakazi wake. IEBC imeomba msamaha kwa wadau wote na umma,” ikasema taarifa hiyo ya kuomba msamaha.

Duru pia zinasema kuwa msimamizi wa akauti ya twitter ya IEBC Jonathan Kiptoo alipiga kalamu kutokana na kosa hilo.

IEBC ilizindua zoezi hilo ambalo litaendeshwa na makarani 400 walioajiriwa kwa ajili ya kibarua hicho baada ya kupokea mafunzo kwa siku moja.

“Makarani hao wamekula kiapo cha usiri ishara kwamba watafanya kazi inavyohitajika kisheria,” mwenyekiti Wafula Chebukati akawaambia wanahabari wakati wa uzinduzi wa shughuli hiyo katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

Makarani hao watakiwa wakilipwa ujira wa Sh1,200 kila siku katika zoezi ambapo litagharimu jumla ya Sh480,000 kwa siku na Sh94 milioni hadi litakapokamilika.

WACHIRA ELISHAPAN: Matatizo yatakayoikumba IEBC ni mwiba wa kujichoma

NA WACHIRA ELISHAPAN

Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya (IEBC) bila shaka inafanya kazi yake itakikanavyo bila kuwa na msukumo wowote kutoka kwa wadau mbalimbali nchini. Hatua hii kwa hakika inadhihirisha kuwa tume hiyo kuwa huru na isiyopendelea upande wowote wa kisiasa wala wa kidini.

Huenda matatizo yanayoiandama tume hii kwa sasa ni mwiba wa kujichoma usioabiwa pole. Masaibu ya tume hii yalianza tangu mwaka wa 2017 ambapo tume hii iliandaa uchaguzi ambao kulingana nao ulikuwa huru.

Uchaguzi huo ulijawa na siasa zisizo na kipimo na baada ya baadhi ya mwaniaji mmoja kukimbilia mahakamani, jaji mkuu Jaji David Maraga baada ya kusikiliza na kukagua ushahidi uliotolewa ,ikabainika wazi kuwa kulikuwa na mushikli katika uchaguzi huo.

Ilibainika wazi kwamba uchaguzi huo haukupangwa kwa njia inayofaa na kwa hivyo malalamishi yote yakaelekezwa kwayo. Tangu hapo Wafula Chebukati amekuwa akionekana kama mtu asiyetaka mazuri kwa serikali.

Uchaguzi wa urais uliporudiwa,na Rais Uhuru Kenyatta kuibuka mshindi pamoja na naibu wake William Ruto,tume hiyo ilionekana kama isiyoutakia mazuri mrengo wa kiongozi wa ODM Raila Odinga na tangu hapo,huenda ndipo uhasama ulitokea baina yao.

Mara tu Raila Odinga waliposalimiana katika salamu za heri njema na rais Uhuru Kenyatta,huenda ndipo mambo yaliigeuka tume hiyo inayoongozwa na Wafula Chebukati.

Tangu uchaguzi huo uliokuwa na utata,kiongozi wa ODM Raila Odinga hajakuwa na imani na tume hiyo na anaitaka kubanduliwa kisha ikaundwa upya ikiwa na makamishna wapya. Hoja ya kuunda ripoti ya jopo la maridhiano la BBI ilipobuniwa,Odinga hakuwa budi kuweka wazi azimio lake la kuibandua tume hiyo.

Hatua ya kwanza ambayo IEBC ilionekana kuchukua baada ya saini za BBI kupokelewa,ilikuwa ni kuitisha fedha za shughuli hizo zote bila hata ya kubaini kwamba itachukua muda gani.

Mzozo kati ya IEBC na Raila Odinga ukatokota upya, tume hiyo ilipodai kima kikubwa cha pesa huku naye Odinga akikisia kiasi cha dola moja kwa kila mpiga kura katika kupiga kura ya maamuzi.

Hatua hii bila shaka huenda ikawa inaonyesha wazi msimamo wa IEBC jambo ambalo halifai kwa tume huru, na tayari tume hiyo imeanza kukagua sahihi hizo japo sasa haijulikani jinsi hali ilivyo katika kambi ya Odinga.

Kenya ina historia ya kubandua tume za uchaguzi kila baada ya uchaguzi,jambo ambalo huibua maswali kuhusu jinsi mfumo wa uongozi unavyotekelezwa.

Mara tu baada ya uongozi wa rais mstaafu Mwai KIbaki kuondoka, tume iliyokuwepo ya ECK ilibanduliwa kasha baadaye ikaundwa tume ya muda ya IIEC na baadaye IEBC tume ambayo inachelea kubanduliwa iwapo mapendekezo ya ripoti ya maridhiano ya BBI yatapitishwa na kuwa sheria.

IEBC yapiga firimbi ya Nairobi

COLLINS OMULO na PIUS MAUNDU

WAKAZI wa Nairobi watapiga kura Februari 18 mwaka ujao kumchagua gavana mpya kufuatia kutimuliwa kwa Mike Sonko.Spika wa Nairobi, Ben Mutura anashikilia cheo cha kaimu gavana.

Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imevipa vyama vya kisiasa vinavyokusudia kushiriki katika uchaguzi huo hadi Desemba 28, kuwasilisha majina ya watu watakaowania mchujo wa vyama husika na pia tarehe ya mchujo.

Baada ya mchujo kampeni zitaanza Januari 18.IEBC ilisema afisa yeyote wa umma anayedhamiria kugombea katika uchaguzi huo mdogo ana siku saba kutoka Desemba 21, 2020 kujiuzulu kutoka ofisi ya umma.

Katika Kaunti ya Machakos, Waziri wa zamani wa Maji, Mutua Katuku jana aliingia katika kinyang’anyiro cha kumrithi seneta wa Machakos, marehemu Boniface Kabaka.

Wengine ni aliyekuwa naibu gavana wa Machakos Bernard Kiala, Musyoka Kala, na mbunge wa zamani wa Kibwezi, Bw Kalembe Ndile.Seneta Kabaka alizikwa Jumanne.