Aliyeshtakiwa kwa kumjeruhi mmiliki wa mkahawa jijini kwa kumpiga risasi, afungwa jela miaka 23

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA aliyemmiminia risasi mmiliki wa mkahawa wa Ronalo, almaarufu K’Osewe, William Osewe, wakizozania mwanamke amefungwa jela miaka 23.

Mshtakiwa Tom Oywa Mboya hakufika kortini kwa madai aliugua akiwa katika gereza la Kamiti alikozuiliwa wiki iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumuua Bw Osewe.

Hakimu mkuu, Bi Martha Mutuku alisoma uamuzi wa kumhukumu Bw Mboya kwa njia ya mtandao.

Mshtakiwa alipelekewa kipakatakilishi akiwa kitandani katika sehemu ya wagonjwa, gereza la Kamiti na kusomewa hukumu.

Akipitisha hukumu, Bi Mutuku alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kwamba Mboya alijaribu kumuua Bw Osewe.

Hakimu alikataa kusitisha kusoma hukumu dhidi ya Mboya asubiri uamuzi wa mahakama kuu kufuatia ombi la mfungwa huyo aruhusiwe kuwaita mashahidi zaidi ilhali kesi imefungwa.

Wakili Benjamin Makokha anayemtetea mshtakiwa aliomba hukumu isitishwe hadi leo (Alhamisi) lakini hakimu akatupilia mbali ombi hilo.

Mfungwa huyo anaomba apewe muda awaite mashahidi wanne zaidi.

Miaka 10 ndani yamsubiri Wario kwa ufisadi

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA waziri wa Michezo na Jinsia, Dkt Hassan Wario huenda akasukumwa jela miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya pesa zilizotengewa wanariadha walioshiriki Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro nchini Brazil 2016.

Wario alipatikana na hatia ya kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya na kufuja pesa ambazo zingaliwafaidi wanamichezo.Hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za Ufisadi, Bi Elizabeth Juma, alisema kashfa hiyo ilipelekea zaidi ya Sh55 milioni kupotea.

Wario pamoja na aliyekuwa afisa mkuu wa Kamati ya Olimpiki Kenya (Noc-K) Stephen arap Soi, pia watatozwa faini maradufu ya pesa zinazodaiwa kufujwa.

Wario alipatikana na hatia katika mashtaka matatu. Naye Soi alipatikana na hatia katika mashtaka sita.Wote wawili watajua hatima yao leo, mahakama itakapopitisha hukumu hiyo.

Katika uamuzi uliosomwa kwa muda wa saa tano, hakimu mkuu Bi Juma alisema Wario alitumia mamlaka ya afisi yake vibaya. Aliwapa pesa watu ambao hawakuwa katika orodha ya waliopaswa kusafiri hadi Rio de Janeiro mnamo Julai 2016.

Waliofaidi na ufisadi huo walitajwa kuwa Adan Omar Enow, Richard Abura na Monica Sairo.Soi alipatikana na hatia ya kutofuata mwongozo na utaratibu uliowekwa na sheria ya usimamizi wa pesa za umma.

Hakimu alisema mashahidi 22 walioitwa na upande wa mashtaka, walithibitisha jinsi msimamizi huyo wa timu iliyowakilisha Kenya katika michezo hiyo aliidhinisha matumizi ya Dola za Marekani 151,500 kama marupurupu kwa washiriki wa michezo hiyo.Pia alishtakiwa kwa kusababisha kupotea kwa Sh9.7 milioni.

Pia mahakama ilisema Soi alisababisha kununuliwa kwa tikiti za ndege za thamani ya Sh19.5 milioni na akalipa watu wengine Sh4.9 milioni.

Wafungwa waachiliwa kupunguza msongamano

Na Manase Otsialo

Wafungwa 18 wameachiliwa huru kaunti ya Mandera baada ya hukumu zao kuchunguzwa na Kamati ya Taifa ya Huduma ya Jamii.

Kuachiliwa kwao kunafuatia hatua za kupunguza idadi ya wafungwa magerezani ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Katika Kaunti ya Mandera, idara ya probesheni ya iliwasilisha majina ya wafungwa 36 katika juhudi za kupunguza msongamano katika magereza.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Garissa, Abida Aaron aliachilia tisa mara moja na kuweka watatu katika probesheni.

Aliagiza saba washiriki kazi ya jamii na mmoja akapunguziwa kifungo kutoka miaka mitano hadi mitatu.

Mahakama Kuu ilikataa pendekezo la kuchunguza vifungo vya wafungw wanane.Wakati wa uchunguzi huo, maafisa wa probesheni huwa wanazingatia muda ambao mfungwa ametumikia, tabia yake akiwa gerezani, aina ya makosa aliyotenda na maoni kutoka kwa waathiriwa na jamii.

Wafungwa wa makosa ya kujaribu kuua, uchomaji mali, ulanguzi wa binadamu na watoto na mengine makubwa hawashirikishwi kwenye mpango wa kupunguza msongamano katika magereza.

Baada ya kuachiliwa huru, huwa wanawekwa chini ya usimamizi wa maafisa wa probesheni.

Atupwa ndani wenzake wakiuawa na umati

Na RICHARD MUNGUTI

JAMBAZI  mwenye umri wa miaka 19 aliyejiponya nafsi yake kwa kuruka ukuta na kuingia ndani ya nyumba moja mtaani Lang’ata huku akiwahepa wananchi waliokuwa na hasira wasimle mzimamzima alisukumwa jela miaka sita kwa wizi wa mabavu.

James Okello ambaye wenzake wawili waliuawa na kuteketetezwa pamoja na pikipiki waliyokuwa wanaiendesha na kuchomoka mbio baada ya kutekeleza uhalimu alilia kwa sauti kortini alipoelezwa na hakimu matukio ya siku hiyo Oktoba 11 2020.

Hakimu mkuu Bw Abdul Lorot alimsukuma jela mnamo Jumatano na kumsihi “ajihoji akiwa gerezani kama atabadilika ama ataendelea na maisha ya uhalifu aliomweleza haulipi, hauna faida.”

Okello na washukiwa wengine wawili walimvamia Bi Rose Nduku Kioko na kumwamuru awape simu yake ya kiunga mbali kwenye barabara ya Kitengela iliyoko mtaani Langata, mnamo Oktoba 11, 2020

Bi Kioko alizuiliwa na mwendashaji bodaboda aliyekuwa amewabeba majambazi wawili waliomwamuru awape simu yake ya kiunga mbali la sivyo atajuta maisha yake yote.

Majambazi hao walikuwa Okello na watu wengine wawili waliokuwa wanasafiria kwa boda boda.

Harufu mbaya

Wakati Rose alinyoosha mkono kutoa simu ndani ya mkoba wake chake mmoja wa majambazi hao alichomoa kisu na kumtaka afanye hima la sivyo wamtoboe tumbo machengelele yake yatapakae na kumwaga “kinyesi chake chenye harufu mbaya.”

Rose alidungwa kisu pajani na kwenye tumbo kisha akapiga kamsa kisha mabawabu waliokuwa wanalinda majumba mtaani humo wakakimbia kumwokoa.

Bawabu mmoja alimtandika rungu mmoja wa washambulizi hao wa Rose kisha akamwokoa Rose ambaye tayari anatokwa na damu tumboni na pajani.

Kizaazaa kiliponoga Okello alipata fursha kisha akatoroka na kukwea ukuta na kuingia ndani ya nyumba moja kuponya nafsi yake.

Lakini hakuwa na bahati wananchi walimchomoa hapo na kumtwanga barabara kabla ya kuokolewa na polisi.

Akimuhukumu hakimu alisema ,“mshtakiwa ni mvulana mwenye umri wa miaka 19 tu. Wenzake wawili waliuawa na umati uliokuwa na gadhabu.Natumaini atajirekebisha tabia akiwa gerezani.”

Bw Lorot aliendelea kusema akimuhuku, “Uhalifu uliotekeleza ni mbaya. Ulimdunga mlalamishi tumbo na tako kwa kisu. Kweli ulihatarisha maisha yake. Kifungo cha miaka sita kitakuwa funzo kwako na kwa majambazi wengine.”

Mshtakiwa alilidodokwa na machozi hakimu alipomkumbusha jinsi alitoroka kwa mwendo wa kasi baada ya kukwepa kifo kwa sekunde chache.

Okello aliomba msamaha na wakati huo huo akamshukuru Mungu alimponya na hamaki ya wakazi wa Langata waliokuwa wanalia wamwage damu yake vile alimwaga ya Rose.

Mmoja wa majambazi wenzake alifungiwa kwenye pikipiki waliyokuwa wanaendesha wakitekeleza uhalifu huo kisha akachomwa moto pamoja na boda boda yake aliyokuwa anatumia kuwatorosha wahalifu hao.

Akimlilia hakimu amwonee huruma, Okello alidai alikuwa ametimuliwa kwa nyumba na landlodi na aliingilia uhalifu kusaka pesa za kulipia nyumba.

Hakimu alimweleza , “Uhalifu haulipi. Songa na miaka sita jela.”

Mahabusu zaidi wahepa seli za polisi katika hali ya kutatanisha

Na STEVE NJUGUNA

IDADI ya washukiwa wanaotoroka seli za polisi imeendelea kuongezeka huku 10 wakitoroka katika kituo cha polisi cha Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua mnamo Jumatatu usiku.

Polisi walisema washukiwa hao walitoroka kwa kukata vyuma vya dirisha mwendo wa saa nane za usiku. Wawili walikamatwa baadaye.

Habari zilisema kulikuwa na maafisa wanne wa polisi kazini wakati mahabusu hao walipohepa.

Afisa Mkuu wa polisi katika eneo la Nyandarua Kaskazini, Timon Odingo alisema washukiwa wengine watano waliachwa kwenye seli wenzao walipotoroka.

Polisi katika eneo hilo wamekuwa wakilalamika kutokana na idadi kubwa ya washukiwa wanaozuiliwa kwenye seli.

KAYOLE

Washukiwa wengine sita walitoroka kituo cha polisi cha Kayole mnamo Septemba 3.

Washukiwa hao waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka tofauti ikiwemo ujambazi na unajisi walitoroka kwa kukata vyuma vya madirisha.

Mnamo Agosti 16, washukiwa 11 walitoroka seli katika kituo cha polisi cha Bungoma kwa kutoboa shimo kwenye ukuta.

Polisi walisema kuwa walijulishwa na mahabusu wengine kuhusu kutoroka kwa wenzao mwendo wa saa tisa za usiku.

Mwezi Julai washukiwa wengine akiwemo raia wa Uingereza walitoroka katika hali tatanishi.

Visa hivyo vilitokea maeneo mbalimbali ya nchi, ambapo polisi walishindwa kueleza walivyotoroka.

Visa hivyo vilitokea katika kituo cha polisi cha Mtwapa (Kilifi), mahakama ya Kibera (Nairobi), vituo vya polisi vya Langas (Uasin Gishu), Nyamira na Naiberi (Uasin Gishu).

Wakuu wa polisi wamekuwa wakisita kueleza sababu ya ongezeko la visa vya mahabusu kuhepa.

Korti yamfunga nyanya jambazi miaka 35 jela

Na BENSON MATHEKA

NYANYA wa miaka 62 ambaye amekuwa akishiriki ujambazi kwa miaka mingi amefungwa jela miaka 35 baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mabavu. Joyce Wairimu Kariuki alipatikana na hatia ya wizi wa mabavu uliohusisha visa vya unyang’anyi wa magari hasa malori yanayobeba mizigo maeneo ya Nakuru, Mombasa na Nairobi.

Mwanamke huyo ambaye wapelelezi wamemtaja kama kiongozi wa mtandao wa genge la majambazi, alishtakiwa Aprili 23 2019 katika Mahakama ya Loitoktok miezi michache baada ya kuachiliwa kutoka gereza la Shimo la Tewa mjini Mombasa ambako alitumikia kifungo cha miaka 15 na miezi sita kwa kesi nyingine sita za wizi alizotenda maeneo tofuati.

Kushtakiwa kwake Loitoktok kulifuatia uchunguzi ambao ulimhusisha na visa kadhaa vya watu kunyang’anywa magari kaunti za Nakuru, Nairobi na Mombasa kati ya 2018 na Aprili 2019, kumaanisha hakurekebisha tabia licha ya kufungwa jela zaidi ya miaka 15 kwa kesi za awali.

“Kufuatia ripoti za magari kuibwa na hasa malori maeneo ya Nakuru, Nairobi na Mombasa kati ya 2018 na 2019, uchunguzi wa wapelelezi wa DCI katika kesi zote, uliwaelekeza kwa mshtakiwa licha ya kuwa aliachiliwa kutoka gereza la Shimo la Tewa baada ya kukamilisha kifungo cha miaka 15,” DCI ilisema kwenye taarifa.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kwamba mwanamke huyo alifungwa jela kuanzia mwaka wa 2006 baada ya kuhusika na visa vya wizi kaunti za Kilifi, Kwale, Nyeri, Murang’a, Nyahururu na Mombasa.Mnamo Oktoba 16 2006, mahakama ya Kilifi ilimhukumu kufungwa miaka mitatu kwa kosa la wizi, na mwaka uliofuata, mahakama ya Nyeri ilimpata na hatia katika kesi nyingine na kumhujumu kufungwa jela miaka miwili.

Mnamo Novemba 6 mwaka huo, mahakama ya Kigumo kaunti ya Murang’a ilimpata na hatia katika kesi nyingine na kumsukuma jela mwaka mmoja.

Rekodi zake za uhalifu zinaonyesha kuwa mnamo wiki mbili baada ya mahakama ya kesi kuamuliwa Kigumo, mahakama ya Hakimu Mkuu ya Mombasa ilimpata na hatia ya wizi na kumhukumu kufungwa jela miaka miwili.

Kulingana na rekodi za korti, mwaka wa 2008, Wairimu alipatikana na hatia katika kesi aliyoshtakiwa mahakama ya Hakimu ya Nyahururu na akahukumiwa kufungwa jela miaka mitatu.

Mnamo Septemba 23 mwaka huo, akiwa bado gerezani, mahakama ya Hakimu ya Kwale ilimuongezea miaka minne ndani ilipompata na hatia ya wizi. Juhudi zake za kukata rufaa katika kesi hizo ziligonga mwamba Jaji Martin Muya alipoitupilia mbali akisema hangeikubali kwa sababu ilihusu kesi tofauti, zilizoamuliwa na Mahakama tofauti tarehe tofauti.

Katika uamuzi aliotoa Novemba 14 2013, Jaji Muya alisema kwamba rufaa ya Wairimu ilihusu kesi alizoshtakiwa kati ya 2006 na 2008. Baada ya rufaa yake kutupwa Wairumu alikaa jela kwa miaka 15 na miezi sita hadi 2018 alipoachiliwa.

Polisi wanasema waligundua badala ya kuacha uhalifu aliingilia wizi wa mabavu ambao Jumanne wiki hii ulimfanya afungwe jela miaka 35. Mwanamke huyo atakuwa amefungwa jela kwa jumla ya miaka 50 na iwapo hataachiliwa kupitia rufaa atatoka jela akiwa na umri wa miaka 97 Mungu akimjaalia.

Msanii Omar Blondin Diop alivyoteswa akipigania haki za raia wa Senegal

NA FLORIAN BOBIN

Maisha ya mwanaharakati na msanii wa Senegal Omar Blondin Diop, aliyeuawa mwaka 1973 kwa kupigwa risasi chini ya utawala wa Rais Leopold Senghor, yatasaidia kutoa mtazamo wa jinsi siasa za kiukombozi zilivyo katika ukoloni mamboleo.

Mwaka 2013, familia ya Omar Blondin Diop ilifanya utaratibu wa sherehe ya kumbukizi yake, ya miaka arobaini baada ya kifo chake kilichotokea eneo la Gorée. Kwa karne nzima, kisiwa hiki kilikuwa kama kitovu kwa njia ya meli za watumwa waliokamatwa sehemu mbalimbali Afrika kupelekwa Marekani.

Kama sehemu ya maadhimisho ndugu zake waliweka picha wake kwenye kizimba alichokuwa amefungwa ndani ambapo sasa ni sehemu muhimu ya maonyesho katika Jumba la Makumbusho la Senegal. Picha hiyo ilimwonyesha katika mwaka wa 1970, mara tu alipofukuzwa kutoka Ufaransa ambapo alikuwa akiishi kwa mwongo mzima.

Picha hii ilipochukuliwa, alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya udhamifu, akiwa na umri wa miaka 23; katika filosofia. Kama walivyokuwa wanafunzi wengi katika mwaka ule, alikumbana na kadhia ya uasi ya mwaka 1968. Lakini miaka mitano baadaye akiwa mpinzani mashuhuri ; Omar Blondin Diop alibaki kuwa hadithi tu.

Alipokufa gerezani, miezi kumi na minne baada ya kuhukumiwa kwenda gerezani kama mfungwa kwa miaka mitatu kama mtu hatari sana kwa usalama wa taifa, Mamlaka za Senegal zilidai kwamba alijiua.

Lakini wengi walikuwa na sababu nzuri za kuamini kwamba aliuwawa. Na tokea wakati huo, familia yake, bila kuchoka ilitaka haki itendeke, na wasanii pamoja na wanaharakati wengi wamekuwa mstari wa mbele kushikilia kumbukumbu yake.

Kuuawa kwa Omar Blondin Diop, hakuwezi kueleweka kama tukio tu la pekee, lakini kama vipindi vingi vya huzuni katika mfululizo wa ukandamizaji, na uzuiaji wa demokrasia nchini Senegal.

Upinduzi kutoka wakoloni umekuwa ni hadithi ya kawaida kwa kuzaliwa kwa mataifa huru bara la Afrika haswa kuanzia mwongo wa 1960. Hata hivyo kushikiliwa kwa maslahi ya Serikal za kimataifa bado ni sura halisi ya mataifa yote yaliyokuwa chini ya Ukoloni wa Kifaransa.

Hata hivyo katika uhuru uliotajwa tu kisiasa, kuchipuka kwa utawala wa kidikteta (utawala wa mtu mmoja) kwa sehemu kubwa kumedumaza dhana ya mapinduzi ya ukombozi kutoka kwenye ubeberu na ubepari.

Hatusikii sana vikundi vya upinzani Senegali wakati wa Leopald Sedar Senghor aliyetawala kati ya 1960-1980 kwa sababu mfumo wa utawala wake ulifanikiwa kuichora nchi hiyo kama nchi yenye demokrasia iliyofanilikiwa Afrika.

Lakini katika mfumo wa chama kimoja cha Progressive Senegalese Union, mamlaka zilipanga njia ovu za ukatili ; kama vile kuwakamata watu, kuwafunga, kuwatisha, kuwatesa na hata kuwaua. Omar Blondin Diop alikuwa miongoni mwao waliotekwa.

Omar Blondin Diop alizaliwa koloni la Ufaransa la Niger mnamo mwaka 1946. Baba yake alikuwa ni muuguzi na alihamishwa kutoka Dakar, mji wa kiutawala wa Ufaransa kwa Afrika ya Magharibi, na kupelekwa kwenye mji mdogo wa Niamey.

Ingawa hakuwa na nafasi yoyote katika miungano ya mapinduzi, mamlaka za kikoloni zilimshuku kuwa ni mpinzani wa maono au mawazo ya Wafaransa kwa sababu ya kujihusisha kwake na chama cha wafanyabiashara na kusaidia katika kitengo cha kijamii katika chama cha kimataifa cha wafanyakazi.

Ofisi za wakoloni katika mji mkuu Ufaransa zilifuatilia chochote kilichosemekana kupingana na Ufaransa kwa sababu ya hofu kwamba vikundi vinavyopinga ukoloni vingeeneza taabu.

Wakati ambapo familia ya Blondin Diop waliruhusiwa kurudi Senegali, aliishi miaka mingi ya utoto wake katika jiji la Dakar. Alipokuwa na umri wa miaka 14 alihamia Ufaransa, ambapo baba yake alijihusisha kwenye Shule ya udaktari.

Katika mwongo huo wa 1960, Blondin Diop aliishi Ufaransa. Maisha yake wakati wa elimu ya Sekondari yalikuwa Ufaransa, ambapo alihudhuria Chuo cha hadhi cha Ualimu, na kuhitimu katika elimu ya tamaduni za Ulaya na matabaka. Alipokuwa chuoni, Blondin Diop alianza kama mwanasiasa mwenye mlengo wa kushoto.

Huu ulikuwa wakati ambapo vikundi vya kupinga ubepari vilianza kuwa hai kuanzia kwenye tamaduni za kimapinduzi za China, na kupinga kwa nguvu zote uvamizi wa Amerika nchini Vietnam.

Kwa kawaida Waafrika ambao walijiingiza kwenye harakati huko Ufaransa, walikuwa na mitazamo ya kisiasa kutoka kwenye nchi zao wenyewe. Blondin Diop, kwa nafasi yake alikuwa na sehemu pande zote mbili.

Muda mfupi baada ya kusikia kuhusu mwanaharakati huyu aliyetoka Senegali, mtengeza filamu mashuhuri Jean-Luc Godard alimchagua Blondin Diop kushiriki kwenye filamu yake iliyoitwa La Chinoise (1967).

Mnamo 1968, akiwa mwanafunzi-mwalimu wa miaka ishirini na moja, alishiriki kikamilifu kwenye mdahalo ulio tayarishwa na makundi mengine ya mlengo wa kushoto.

Akihuishwa na maandiko ya Spinoza, Marx, na Fanon, akajikita katika kutafuta msimamo wowote ndani na nje ya uhalisia, utawala huria, nadharia ya siasa na matendo ya Mao Tse-Tung. Hakujiweka kando na itikadi moja fulani.

Kwa sababu ya harakati zake katika siasa, Blondin Diop alifukuzwa Ufaransa na kurudishwa Senegali mwishoni mwa mwaka 1969. Pamoja na marafiki zake wengine waliosoma naye Ulaya, alishiriki katika harakati za Vijana wa Marxist-Leninist.

Kundi hilo baadaye likazaa kundi lingine lililoshawishi sana umoja dhidi ya ubeberu And Jëf (Kufanya Kazi Pamoja), ambalo lililazimishwa kujificha mpaka mwanzoni mwa mwongo wa 1981. Waliporudisha mfumo wa awali, Blondin Diop alikuza maonesho ya sanaa.

Alianzisha mradi wa “Tamthilia mitaani ambayo ingeshughulikia maswala na maslahi ya wananchi” kufanana na tamthilia ya Augusto Boal “Tamthilia ya Wananchi Waliokandamizwa.” Alipotanuka katika sanaa muhimu ya kimapinduzi, Blondin Diop aliandika:

Tamthilia yetu itakuwa ya ubunifu wenye hamasa mchanganyiko. Kabla ya kuchezwa kwa majirani zetu, tutajua washiriki wake, tutatumia muda mwingi pamoja nao, haswa vijana […]. Tamthilia yetu itapelekwa sehemu ambazo zitakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu (masokoni, majumba ya sinema, viwanja vikubwa) […]. Ni muhimu tufanye kila liwezekanalo wenyewe […]. Hitimisho la haki; Ni bora kifo kuliko utumwa.

Senegali huru bado ilikuwa ni eneo la Ukoloni mamboleo. Senghor awali alikuwa amepinga uhuru wa mapema, akijitetea badala yake kuwa na uwezo wa kujitawala kwa zaidi ya miaka ishirini.

Hivyo alipokuwa Rais, mara kwa mara alikuwa akiomba misaada kwa Ufaransa. Mwaka 1962 Senghor aliropoka kumlaumu mshirika mwenzake wa muda mrefu Mamadou Dia, Rais wa baraza la mawaziri la Senegali kwa jaribio la kutaka kumpindua.

Baadaye Dia alikamatwa na kuwekwa kifungoni kwa zaidi ya miaka kumi. Mwaka 1968 wakati mgogoro mkubwa wa Uma ulipolipuka katika jiji la Dakar, polisi waliwakandamiza waandamanaji kwa msaada wa vikosi vya Ufaransa.

Mwaka 1971 kujishikamanisha kwa Senghor na Ufaransa, kulionekana kufikia kileleni kwa ujio wa Rais wa Ufaransa Georges Pompidou, rafiki wa karibu na rafiki waliosoma naye darasa moja.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja jiji la Dakar lilikuwa likiandaliwa kwa mapokezi na ujio wa Pompidou wa saa 24 tu. Katika njia yote ya msafara, mamlaka zilifanya matengenezo ya barabara na majengo, zikijaribu kuficha umasikini wa jiji.

Kwa wanaharakati vijana wabobezi, mapokezi ya Rais wa Ufaransa Senegali yalikuwa uchokozi wa wazi. Wiki chache kabla ya ujio huo kundi lililohamasishwa na makundi mawili ya American Black Panther na Uruguayan Tupamaros walichoma moto kituo cha utamaduni cha Ufaransa kilichopo jijini Dakar.

Walipojaribu kuingilia msafara wa Rais, walikamatwa. Miongoni mwao walioonekana na hatia, wawili walikuwa ndugu zake Blondin Diop. Ingawa aliegemeza matukio haya ya uoinduzi, hakuhusika kwenye mipango.

Alikuwa amerejea Paris miezi michache kabla, baada ya kibali chake cha kuingia kupigwa marufuku. Akiwa na huzuni, Blondin Diop aliamua akiwa na marafiki zake wa karibu, kuondoka Ufaransa kwenda kujifunza mapambano ya silaha.

Wakapanda chombo kuelekea mashariki, wakapita Ulaya yote kwa gari moshi kabla ya kufika kwenye kambi za Syria walipoungana na wapiganaji wa Kipalestina, na askari wa msituni wa Eritrea. Mpango wao ukiwa ni kumteka nyara balozi wa Ufaransa nchini Senegali, ili wabadilishane na rafiki zao waliokuwa wamefungwa gerezani.

Miezi miwili katika mafunzo ya kijeshi, Blondin Diop na washiriki wake wakatoka jangwani kwenda jijini. Walitumaini kupata msaada wa silaha kutoka kwenye kundi la Black Panther Party, ambao walikuwa wamefungua ofisi ya kimataifa katika jiji la Algiers.

Hata hivyo, mgawanyiko kwenye kundi lao, uliwalazimisha kuwaza upya. Baada ya kuyumbishwa Conakry walienda kupiga kambi Bamako ambapo sehemu ya familia ya Blondin Diop iliishi. Na kutokea hapo wakajipanga upya.

Mwezi wa kumi na moja mwaka 1971, Polisi walilikamata kundi hilo siku chache kabla ya ziara ya kwanza ya kitaifa ya Rais Senghor nchini Mali. Watu wa intellejensia wa usalama, walikuwa wakiwafuatilia kwa miezi kadhaa.

Mfukoni mwa Blondin Diop, walikuta barua iliyoeleza mpango wa kundi hilo, kuwatoa rafiki zao wengine waliokuwa wamefungwa. Aliporejeshwa Senegali alihukumiwa miaka mitatu jela. Kwa umaalumu katika siku zao walipokuwa kwenye vizimba vyao, hawakuruhusiwa kutoka humo.

Kupunguza mwingiliano, mwonjo wa mchana ulipunguzwa – wafungwa waliruhusiwa nuru nusu saa tu asubuhi, na nusu saa mchana. Siku zote zilikuwa usiku tu; na usiku ulikuwa hauishi, na mateso yalikuwa ni kawaida.

Omar Blondin Diop aliripotiwa kufariki tarehe 11 mwezi wa tano 1973, akiwa na miaka 26. Taarifa zilitoka kama mlipuko wa bomu. Mamia ya vijana wakafurika mitaani, wakaandika kwenye kuta za jiji “Senghor, katili; wanauwa watoto wenu, amka; Makatili, Blondin ataishi.”

Tangia awali kabisa, Serikali ya Senegali ilificha uhalifu. Kwenda kinyume na maagizo rasmi, majaji waliokuwa wanachunguza wakawashtaki washukiwa wawili.

Katika kitabu cha gereza ilionyesha kwamba Blondin Diop alikuwa amezimia tangu siku moja kabla ya kutangazwa kwake kuwa ameaga dunia. Hata hivyo, utawala wa gereza ulikuwa haujafanya lolote. Kabla jaji kupata muda na nafasi ya kumkamata mshukiwa wa tatu, mamlaka zilimbadilisha jaji na kufunga jalada hilo.

Kila mwezi wa tano tarehe 11 hadi miaka ya tisini, vikosi vya askari vyenye silaha vilizunguka kaburi lake kuzuia aina yoyote ya kumbukizi yake.

Kwa miongo kadhaa, Omar Blondin Diop amekuwa chanzo cha chachu kwa wanaharakati wengi na wasanii huko Senegali, na kwingine duniani.

Katika miaka ya karibuni, maonyesho, michoro, na maigizo yamehusisha simulizi yake ambayo kwa huzuni nyingi inatetema sambamba na siasa. Njia za kimamlaka zinazotumika na uongozi wa sasa wa Senegali zinaonyesha kuepuka adhabu ya zamani.

Mfumo wa utawala wa Raisi Macky Sall, mara kwa mara umetafuta kukandamiza uhuru wa maandamano, ubadhilifu wa fedha za Umma, na kutumia vibaya mamlaka yake. Na kwa kuwa uwajibikaji wa Serikali hauna kusudi lingine lolote isipokuwa kuvutia misaada ya kimataifa, tabia zilezile za kitambo zinadumu kuishi na kuendelea hata sasa.

Hata leo Senegali watu wanafungwa jela wakijaribu kuandamana. Wanaharakati kama Guy Marius Sagna bado wana teswa, wanakamatwa na kinyume cha sheria wanafungwa.

Katika mazingira hayo, na kwa mshangao, bado Serikali imegoma kufungua kwa upya kesi ya Omar Blondin Diop. Hata hivyo, familia yake inashikilia kuwa “haijalishi muda mrefu wa usiku, jua ni lazima litachomoza tu.”

 

Mwandishi ni mwanafunzi wa historia ya Afrika Magharibi katika Chuo Kikuu cha Vancouver nchini Canada. Utafiti wake umegusia mapambano ya uhuru baada ya ukoloni kuanzia miaka ya sitini mpaka sabini katika nchi ya Senegal. Pia, ni mtangazaji wa Elimu PodcastTafsiri ya Kiswahili na JFK Solace, Njoki Mburu na Fainess Mwakisimba.

Mwanamke jela mwaka mmoja kwa kujaribu kumuua mtoto

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 25 atatumikia kifungo cha miezi 12 gerezani kwa kujaribu kumuua mwanawe mwenye umri wa miezi minne.

Rachel Wanjiru alisukumwa jela Jumanne baada ya kiongozi wa mashtaka Winnie Moraa kufichua “mfungwa huyu alikaidi masharti alyopewa na mahakama Aprili kwamba asirudi kubugia chang’aa na vileo vingine.”

Akatoboa siri Bi Moraa, “Rachel amerudia maisha yake ya zamani ya kulewa chakari na kutomjali mwanawe.”

Kiongozi huyo wa mashtaka aliomba mahakama ifutilie mbali kifungo alichopitisha hakimu mwandamizi Bi Martha Nanzushi mnamo Aprili.

“Naomba hii mahakama ifutilie mbali kifungo cha nje cha miezi 13 alichofungwa Rachel na Bi Nanzushi. Mfungwa huyu alikaidi masharti aliyopewa asirudie pombe na kushiriki anasa,” Bi Moraa alimrai Bi Nzibe.

Hakimu alielezwa Rachel aliyewaahidi maafisa wa urekebishaji tabia atabadilika alirudia kubugia pombe ya chang’aa katika mtaa wa mabanda ulioko karibu na mtaa wa kifahari wa Southlands, Nairobi.

Alipoulizwa na hakimu sababu ya kurudia pombe akapata fursa ya kujieleza.

“Mheshimiwa nimejaribu niwezavyo kuacha kulewa chang’aa nimwshindwa,” akasema.

Mfungwa huyo aliomba mahakama imsaidie akapewe ushauri na wataalam

“Nimejaribu kila mbinu niache kulewa pombe nimeshindwa na sasa nahitaji msaada wa mtaalam,” Rachel alimweleza hakimu.

 

Antony Kamau, mumewe Rachel Wanjiru, akabidhiwa mtoto kuendelea kumtunza hadi mkewe atakapokamilisha kifungo cha mwaka mmoja. Picha /Richard Munguti

Hakimu aliuliza ikiwa mtoto huyo wa Rachel alikuwa kortini.

“Mtoto yuko wapi?” Bi Nzibe alimwuliza Rachel.

“Yuko pale kizimbani na mume wangu Antony Kamau,” alijibu Rachel.

“Utaendelea kumtunza huyo mtoto?” Bi Nzibe alimwuliza Kamau.

“Ndio mheshimiwa,” Kamau aljjibu.

Mahakama iliamuru Rachel apelekwe katika gereza la Langata kuanza utaratibu wa kushauriwa jinsi ya kuacha ulevi wa kupindukia.

Atarudishwa kortini tena Mei 30, 2020, kwa maagizo zaidi.

Waliotupwa jela kimakosa miaka 36 kufidiwa Sh297m kila mmoja

MASHIRIKA Na MARY WANGARI

WANAUME watatu kutoka Baltimore waliokuwa vijana chipukizi walipohukumiwa kifo kimakosa mnamo 1984 wanatazamiwa kupokea Sh297 milioni kila mmoja kutoka kwa mamlaka ya Maryland.

Hii ni kupitia mpango wa malipo uliopendekezwa ambao Bodi ya Huduma za Umma inatazamiwa kupigia kura mnamo Jumatano.

Mpango huo ulifichuliwa katika vipengele vya ajenda vilivyochapishwa na bodi hiyo mnamo Jumatatu.

Alfred Chestnut, Ransom Watkins na Andrew Stewart walikuwa na umri wa miaka 16 kila mmoja wakati maafisa wa polisi mjini Baltimore walipowalenga kama washukiwa katika mauaji ya Novemba 1983 ya mvulalana mwenye umri wa miaka 14 ndani ya Shule ya Upili ya Harlem Park Junior na kupuuza mashahidi kadhaa na vidokezo vilivyoashiria mtu mwingine.

Wakati mawakili wa upande wa washtakiwa walipouliza ushahidi kuhusu mshukiwa huyo mwingine, mwendeshaji mashtaka wa Baltimore alimdanganya jaji na kusema hakukuwa na ripoti kama hizo.

Hatimaye Chestnut ilivumbua ripoti hizo katika maombi ya rekodi za umma lwa mwanasheria mkuu wa Maryland mnamo 2018, akaziwasilisha kwa wakili mkuu eneo la Baltimore, Marilyn Mosby mnamo 2019, na kitengo cha Uadilifu wa Mashtaka cha Mosby kikajitahidi kuwezesha wanaume hao kuachiliwa huru kabla ya Sikukuu ya Thanksgiving — miaka 36 tangu walipofungwa jela kwa mara ya kwanza.

Maryland haina masharti ya kuwafidia washtakiwa waliohukumiwa kimakosa, badala yake huwaruhusu kuwasilisha malalamishi kwa Bodi ya Huduma za Umma, ambayo “huenda ikaruhusu kiasi fulani” lakini kwa miaka mingi haikufanya hivyo.

Lakini mswada umewasilishwa katika Bunge Kuu la Maryland ambao utahitaji bodi hiyo kuwalipa fidia watu waliohukumiwa kimakosa.

Mswada huo unalenga kuwezesha kufidiwa kwa wale waliohukumiwa kimakosa kiasi fulani cha hela kwa kila mwaka ambao walitumika kifungo cha jela

Aliyezaba polisi kofi atozwa faini Sh500,000 au jela miaka mitano

Na KALUME KAZUNGU

MAHAKAMA ya Lamu imemtoza faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitano gerezani mwanamume aliyepatikana na hatia ya kumzaba kofi afisa wa polisi na kisha kurarua sare yake wakati akijaribu kukwepa kukamatwa.

Kalume Ngumbao alitekeleza kosa hilo mjini Lamu mnamo Mei 1, 2019.

Maafisa watatu wa polisi walikuwa wametumwa kwenye makazi yake kumkamata kwa kufuata amri ya korti baada ya mshukiwa kutoroka na kujificha kwa miezi minane pindi alipopewa dhamana kuhusiana na kesi ya awali iliyokuwa ikimkabili.

Bango la kuelekeza wanaotaka kufika katika mahakama Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Mahakama ya Lamu iliafikia kutoa amri ya kukamatwa kwa mshukiwa huyo baada ya kukosa kuhudhuria kikao chochote mahakamani katika kipindi chote cha miezi minane ambacho ni kinyume na matakwa ya dhamana yake aliyokuwa amepewa.

Mshukiwa alianza kuwatisha kwa maneno polisi na kisha kumwandama mmoja wao aliyemkamata na kuanza kumvurumishia makonde na kuchanachana sare yake.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Lamu, Allan Temba, amesema mshukiwa tayari alikuwa na historia chafu ya kufungwa miaka mitatu kwa makosa mawili ya awali ya kujipatia fedha takribani Sh300,000 kimagendo mnamo 2017.

“Umepatikana na hatia ya kudinda kukamatwa na maafisa watatu wa polisi waliokuwa wakitekeleza amri ya mahakama ya kukukamata. Pia umepatikana na hatia ya kumpiga kofi polisi na kurarua sare yake wakati ukijaribu kukataa kukamatwa. Mahakama imekutoza faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitano gerezani. Una siku 14 za kukata rufaa,” akasema Bw Temba.

Aliyetisha mashahidi ahukumiwa kifungo cha jela miaka 14

Na RICHARD MUNGUTI

MZEE aliyeshtakiwa kwa kutisha mashahidi katika kesi ya ulipuaji matatu kwa gruneti ambapo abiria watatu walifariki Mei 4, 2014, amehukumiwa kifungo cha miaka 14 gerezani bila faini.

Hata hivyo, mahakama imeamuru akae jela miaka 10 kwa sababu alikuwa kizuizizini kwa muda wa miaka minne.

Sar Guracha Haro alipatikana na hatia Ijumaa na Hakimu Mkuu wa Milimani, Nairobi, Bw Francis Andayi.

Bw Andayi amesema kuwa kosa alilofanya Guracha ni baya kwa sababu alivuruga haki katika kesi aliyoshtakiwa pamoja na mwanawe Warque Dejene Sar.

Hakimu amesema makosa aliyofanya yanaweza kufanya haki kutotendeka.

“Makosa aliyofanya mshtakiwa ya kuwatisha mashahidi ni mabaya kwa sababu wahalifu watazoea kutoadhibiwa katika makosa wanayofanya,” amesema Bw Andayi.

Alisema wahalifu watakuwa wanatenda makosa na kuenda nyumbani kuponda raha na kupumzika huku wakijua hakuna hata shahidi mmoja atafika mahakamani kueleza yaliyojiri.

Mahakama imesema kitendo hicho ni cha kuua sheria polepole ili isitumiwe kuwaadhibu wahalifu.

Katika kesi hiyo ya kulipua kwa gruneti matatu hiyo katika barabara kuu ya Thika Superhighway, Guracha na mwanawe Dejene waliachiliwa kwa kukosekana ushahidi.

Akiwaachilia Guracha na Dejene, hakimu alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha kwamba wawili hao waliunga mkono ugaidi licha ya mashahidi kusema wawili hao walipokea Sh85,000 kupitia M-Pesa kutoka kwa ajenti ajulikanaye Cool Breeze katika mji wa Kakuma.

Karibu na mpaka

Hakimu alishutumu upande wa mashtaka kwa kutegemea ushahidi kuwa Guracha alionekana akitembea katika mpaka wa Kenya na Somalia.

Bw Andayi amesema shahidi mkuu katika kesi hiyo alitishwa na hakurudi tena mahakamani.

“Mshtakiwa alifaulu katika azma yake ya kukwepa makali ya sheria kwa kutisha mashahidi,” akasema Bw Andayi.

Akaongeza: “Utatumikia miaka 10 ijapokuwa nimekufunga miaka 14. Miaka minne umekuwa rumande na hii korti inachukulia ulikuwa kizuizini.”

Mgombeaji urais asusia mlo katika jela ya Tunisia

Na MASHIRIKA

MMOJA wa wawaniaji wa urais nchini Tunisia, Nabil Karoui, ambaye alipigiwa upatu kushinda kiti hicho ameanza kususia chakula akitaka aruhusiwe kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa Septemba 15.

Karoui, 56, anayemiliki kituo cha runinga cha Nessma TV alifungwa jela wiki tatu zilizopita kwa madai ya kutolipa kodi na ulanguzi na ‘utakatishaji’ wa pesa.

“Karoui alianza kususia chakula tangu Jumatano akitaka haki yake ya kupiga kura Jumapili,” wakili wake Ridha Belhadj alinukuliwa akisema.

Maafisa wa serikali hawakupatikana kutoa kauli yao kuhusu ripoti hiyo.

Mahakama ya Rufaa inatarajiwa kusikiliza ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana akisubiri uamuzi wa mwisho.

Mfanyabiashara huyo anayepigiwa upatu kushinda urais alikamatwa baada ya kulaumiwa na baadhi ya wanasiasa na mashirika ya serikali kwa kutumia kituo chake kuvumisha azma yake ya kisiasa.

Kura za maoni nchini Tunisia zilionyesha Karoui akiongoza na kwamba kufungwa kwake kuliongeza umaarufu wake.

Wapinzani wake ni waziri mkuu Youssef Chahed, waziri wa ulinzi Abdelkarim Zbidi, aliyekuwa rais Moncef Marzouki, na Abdelfattah Mourou, naibu rais wa chama cha Kiislamu cha Ennahdha party.

Karoui alikamatwa siku ambayo serikali ilitangaza kuwa ilipiga marufuku vituo vitatu vya habari vilivyohusisha chake maarufu cha Nessma TV, kupeperusha habari za kampeni za urais kwa madai kwmba hazvikuwa na leseni.

Masaibu yake yalianza Mei baada ya kutangaza angegombea urais alipowekewa vikwazo na serikali.

Mnamo Juni 18, bunge lilibadilisha sheria ya uchaguzi ambayo ilimzuia Karoui kugombea kwa kumiliki kituo maarufu za televisheni ikisema alikitumia kujipigia debe.

Wadadisi wanasema mabadiliko hayo yalinuiwa kumzuia Karoui kugombea lakini Essebsi alikataa kutia sahihi sheria hiyo kabla ya kifo chake.

Karoui alikuwa msitari wa mbele kuunga Essebi kwenye uchaguzi wa 2014 na amekuwa hasimu mkuu wa waziri mkuu Chahed.

Bwanyenye huyo alikuwa ameeleza hofu yake akisema alikuwa akihujumiwa kwa sababu ya kuongezeka kwa umaarufu wake kabla ya uchaguzi ambao ulifuaia kifo cha Essebsi.

Tume ya uchaguzi ya Tunisia imeidhinisha wagombeaji 26 wakiwemo wanawake wawili na Marzouki.

Nchini Tunisia, rais husimamia masuala ya nchi za kigeni na ulinzi na hugawana mamlaka na waziri mkuu anayechaguliwa na bunge ambalo lina mamlaka ya masuala ya ndani.

Wapiga kura milioni saba wanatarajiwa kushiriki uchaguzi huo baada ya kampeni zilizohusu changamoto za kijamii na kiuchumi katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Wafuasi wa Karoui wanamlaumu Chahed kwa kuchochea kukamatwa kwake, madai ambayo waziri huyo mkuu anakanusha.

Utaenda jela ukikataa sensa

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA watakaosusia shughuli ya kuhesabu watu itakayoanza Jumamosi jioni, wanakabiliwa na hatari ya kutozwa faini ya Sh500,000 ama kufungwa jela mwaka mmoja au adhabu zote mbili.

Kulingana na sheria, ni hatia kukataa kushiriki shughuli hiyo ya kitaifa ya kukusanya takwimu, kuharibu au kuvuruga utaratibu huo.

Baadhi ya Wakenya wametisha kususia shughuli hiyo wakisema uteuzi wa maafisa watakaoiendesha haukuwa wa haki.

Walioapa kususia shughuli hiyo wanasema watu kutoka maeneo yao walibaguliwa wakati wa kuajiri maafisa wa kuendesha shughuli hiyo.

Kulingana na Sheria ya Takwimu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, adhabu ya kuzuia maafisa wa sensa na kutoa habari za uwongo ni faini ya Sh500,000.

Kulingana na sheria hiyo, watu watakaokataa kujibu maswali ya maafisa watakaoendesha sensa au kutoa habari za kupotosha watatozwa faini au kufungwa jela miezi sita.

“Yeyote ambaye kwa makusudi, anakataa kutoa habari inavyohitajika anavunja sheria na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyozidi Sh500,000, kufungwa jela miezi sita au hukumu zote mbili,” inaeleza sheria hiyo.

Kabla ya sheria kufanyiwa marekebisho, adhabu ya kususia na kudanganya katika sensa ilikuwa Sh100,000 au kufungwa jela mwaka mmoja.

Tayari, serikali imeagiza Wakenya kukaa nyumbani kuanzia Jumamosi jioni hadi Jumapili ili waweze kuhesabiwa.

Itakuwa mara ya kwanza shughuli hiyo kuendeshwa kwa kutumia mitambo ya kidijitali, hatua ambayo serikali inasema itahakikisha habari zitakuwa sahihi na zinaweza kupatikana haraka.

Kila Mkenya atahesabiwa mahali atakuwa na serikali imeonya wanasiasa wanaopanga kusafirisha watu hadi maeneo yao kushiriki sensa.

“Tumepokea ripoti kwamba baadhi ya wanasiasa walifanya mikutano kupanga kusafirisha watu hadi kaunti zao. Hii ni tabia duni inayopaswa kukoma. Tunawatazama na mtakabiliwa na mkono wa sheria,” alionya Bw Matiang’i kwenye kikao cha wanahabari akiandamana na kaimu Waziri wa Fedha, Ukur Yatani na mwenzao wa Habari na Teknolojia Joe Mucheru.

Wanasiasa wakiwemo wabunge na magavana wamekuwa wakihimiza raia kurudi maeneo walikozaliwa kuhesabiwa huko.

Hii ni kutokana na haja ya kuwa na idadi kubwa ya watu kwa ajili ya ugawaji wa pesa mashinani pamoja na mipaka ya maeneobunge.

Mawaziri hao walisema maandalizi ya sensa yamekamilika na wakahakikishia Wakenya kwamba usalama wao umelindwa. Baadhi ya maswali ambayo Wakenya watatakiwa kujibu ni kuhusu umri, jinsia, dini, jamii, eneo la kuzaliwa, elimu na kazi.

Wakenya pia wataulizwa kuhusu mali waliyo nayo ikiwemo mifugo na vifaa vya nyumbani.

Watu wote watakaokuwa nchini kuanzia Jumamosi saa kumi na mbili jioni watahesabiwa.

Serikali yaweka mikakati

Serikali imesema imeweka mikakati ya kuhesabu watu watakaokuwa wakisafiri, watakaokuwa kwenye mahoteli na lojing’i, wagonjwa watakaokuwa hospitalini na wafungwa wote magerezani Jumamosi usiku.

Maafisa wa kuhesabu watu watakuwa wakiandamana na wazee wa vijiji ili watambuliwe kwa urahisi.

Mtu akikosa kuhesabiwa Jumamosi usiku atahesabiwa kwa kurejelea mahali akakuwa usiku wa Agosti 24/25.

Shughuli hii itaendelea hadi Agosti 31 na serikali inasema itatoa nambari ya simu ya kupiga bila malipo ili wale ambao watakosa kusajiliwa katika muda huo wawasiliane na KNBS.

Shirika hilo litatuma maafisa kuhesabu watu hao nyumbani kwao.

Baktash Akasha ahukumiwa kifungo cha miaka 25 jela Amerika

Na KEVIN J. KELLEY na CHARLES WASONGA

MAHAKAMA moja ya Amerika imemhukumu Baktash Akasha kifungo cha miaka 25 jela baada ya kumpata na hatia ya kuhusika katika ulanguzi wa mihadarati.

Kiongozi wa jopo la majaji ambao wamekuwa wakisikiza kesi dhidi ya Mkenya huyo, Victor Marrero, pia amemtoza faini ya dola 100,000 (Sh10.3 milioni).

Baktash na kakake mdogo Ibrahim Akasha walishtakiwa kwa kusafirisha tani kadhaa za dawa za kulevya aina ya heroini hadi nchini Amerika.

Walikiri makosa yao na kukubali makosa yao.

Walikubali kuwa walipanga njama ya kuingiza heroini na dawa aina ya methamphetamine nchini Amerika.

Hukumu dhidi ya Ibrahim itasimwa na Jaji Victor Marrero mnamo Novemba 2019.

Kaka hao walichukuliwa nchini Kenya na kusafirishwa hadi Amerika bila familia zao kujulishwa au mawakili wao na licha ya kuwepo kwa agizo la mahakama la kuzuia kusafirishwa kwao hadi Amerika.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo Julai, jaji huyo alisema kuwa amekubaliana na madai yaliyowasilishwa dhidi ya wana hao wa Akasha.

Bunduki

Kaka hao pia walikiri kubeba na kutumia bunduki aina ya machineguns kuendeleza mipango yao ya kuingiza dawa za kulevya nchini Amerika.

Stakabadhi moja iliyowasilishwa kortini mnamo Julai 25, 2019, ilielezea sababu za kuitaka mahakama isitoe hukumu nyepesi kwa kaka hao wa Akasha.

Sababu hizo zinajumuisha madai kwamba Baktash aliua aliyekuwa mkewe, alimtesa mwanawe wa kiume, alikodi wauaji kumwangamiza babake na kuhusika katika shughuli za ulanguzi wa silaha kwa ushirikiano na kundi la kigaidi la al-Shabaab.

“Kaka wa Akasha walilinda biashara ya mihadarati kwa kutumia ukatili, mauaji, vitisho na mikakati yoyote ya kihalifu waliorithi kutoka kwa baba yao aliyeuawa mnamo mwaka wa 2000,” stakabadhi hiyo iliyotolewa na upande wa mashtaka ilisema.

Wahimizwa wasibague mahabusu wa zamani

Na ELIJAH MWANGI

WAKAZI wa Meru wametakiwa kukoma kuwabagua wafungwa wa zamani.

Machifu wawili; Bi Isabel Mutura wa lokesheni ya Kanyekine na Bi Mercy Mureithi wa lokesheni ya Municipality, Imenti Kaskazini, walisema wakazi wa eneo hilo wamekuwa na mazoea ya kuwabagua wafungwa wanaoachiliwa huru baada ya kukamilisha kifungo chao gerezani.

Bi Mutura alisema kutengwa kwa wafungwa hao wa zamani kunawasukuma kujiingiza kwenye uhalifu na hata kujitoa uhai kwani wanahisi kukataliwa na jamii.

“Wafungwa wa zamani wanachohitaji ni upendo na kusaidiwa kurejelea maisha yao ya awali,” akasema Bi Mutura.

Machifu hao walikuwa wakizungumza katika hafla ya mazishi ya mwanaume aliyejitia kitanzi kwa madai ya kukataliwa na mkewe na watoto wake wawili aliporejea nyumbani baada ya kukamilisha kifungo cha miaka mitano gerezani.

Inadaiwa familia ya mwanaume huyo iliuza shamba alipokuwa gerezani na kuhamia mjini.

Bi Murithi aliwataka wafungwa wanaotoka jela kujiunga na kikundi kilichobuniwa mnamo 2004 kuwasaidia wafungwa wanaorejea baada ya kukamilisha adhabu zao kutangamana na jamii.

“Wafungwa waliojiunga na kikundi hicho wanasaidiwa kuendelea na maisha yao ya hapo awali na kuhimizwa kuwa watu wema,” akasema.

SHAMBULIZI LA GARISSA: Mtanzania jela maisha, Wakenya wawili ndani miaka 41

NA MARY WANGARI

@taifa_leo

RAIA wa Tanzania ambaye ni mmoja wa washukiwa watatu katika mashtaka ya kusaidia utekelezaji wa shambulizi la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa 2015 lililoua wanafunzi 148 Jumatano alitupwa jela maisha.

Rashid Charles Mberesero alipewa adhabau hiyo kwa kuwa alipatikana katika eneo la shambulizi, huku ripoti ya uchunguzi alipokuwa rumande ikionyesha alikuwa na nia ya kujiunga na Al Shabaab akiachiliwa.

Mahakama ya Nairobi iliwazaba kifungo cha miaka 41 gerezani wenzake wawili Wakenya kwa makosa matatu – kushirikiana kupanga kutekeleza ugaidi, kutekeleza ugaidi na kuwa wanachama wa kundi la Al Shabaab.

Hakimu Mkuu Francis Andayi alitoa hukumu hiyo ya kifungo cha jela dhidi ya Mohamed Ali Abdikar na Hassan Aden Hassan.

Kutoka kushoto: Rashid Mberesero, Hassan Edin Hassan na Muhamed Abdi Abikar wakiwa kizimbani Nairobi Julai 3, 2019. Picha/ Richard Munguti

Hukumu hizo tatu ni za kwanza kutokea kutokana na mchakato wa uchunguzi na mashtaka kwa kipindi kirefu.

Magaidi wote wanne walioangamiza Wakenya kwa bunduki waliuawa na vikosi vya usalama.

Mhusika anayeshukiwa kuwa kiongozi wa shambulizi hilo, Mohamed Mohamud almaarufu “Kuno,” aliyekuwa profesa katika mojawapo ya masomo ya mjini Garissa, aliuawa Kusini Magharibi mwa Somalia mnamo 2016.

Mfungwa aliyejifanya maiti kutoroka jela achomwa hadi kufa

MASHIRIKA Na PETER MBURU

Maryland, Marekani

JARIBIO la mfungwa kutoroka gerezani eneo la Maryland, Marekani kwa kujificha katika mfuko wa kusafirisha maiti liligonga mwamba vibaya na kusababisha kifo chake Alhamisi, baada ya wafanyakazi wa mochari kumchoma, wakidhani ni maiti.

Gary Smith, 41, alikuwa amekaa ndani kwa miezi 18 ya miaka 12 ambayo alifungwa, baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki msururu wa wizi uliofanyika 2014.

Alikuwa amekaa katika gereza la Jessup kwa miezi mitano tu, baada ya kuhamishiwa huko alipojaribu kutoroka kutoka jela ya Brockbridge awali mwaka huu.

Anasemekana kutumia fursa ya mfungwa mwenzake ambaye alikufa, kwa kutupa maiti ya marehemu na kujificha ndani ya mfuko wa maiti, kama mbinu ya kupenya kutoroka nje ya gereza.

Japo mpango wake ulikuwa umefanikiwa, bahati yake haikuwa nzuri kwani kwa kile kinashukiwa kuwa alipatwa na usingizi ama kupoteza fahamu akisafirishwa kupelekwa mochari, alichomwa, wafanyakazi wa mochari wakijua ni maiti.

Lakini akiendelea kuungua wafanyakazi hao walisikia nduru za kutisha, japo walipogundua walimtia mtu hai walikuwa tayari wamechelewa.

“Kulikuwa na mchungu sana katika sauti yake, nduru hiyo ilikuwa ya kutisha. Tulikimbia kuzima kila kitu lakini alikuwa ameungua kabisa hata kabla tufanye kitu,” akasema mkurugenzi wa mochari hiyo Terence Anderson.

Lakini Anderson alisema kuwa mfungwa huyo alikuwa ameachwa peke yake kwa zaidi ya saa tatu katika kitanda cha kusafirisha maiti, akishuku alikuwa amelala ndipo hakutoroka.

Idara za polisi na magereza zimetangaza kufanya uchunguzi wa pamoja kubaini jinsi Smith alitoroka jela na akafa.

Takriban visa saba vya watu walio hai kuchomwa wakidhaniwa kuwa maiti hutokea Marekani kila mwaka.

Mwanamume aliyepatikana na hatia ya kunajisi wasichana wawili asukumwa jela maisha

Na LAWRENCE ONGARO

MWANAMUME mmoja amepokezwa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuwanajisi wasichana wawili wadogo.

Alhamisi, Mahakama ya Thika ilimpata na makosa James Waita, 36, ya kuwanajisi watoto hao.

Mshtakiwa aliyefikishwa mbele ya hakimu mkuu A. M. Maina katika ushahidi ilielezwa aliwanajisi wasichana hao baada ya kuwahadaa na kuwapeleka katika chumba chake.

Ni kwamba mnamo Januari 14, 2016, akiwa eneo la Githurai 45, Kaunti ya Kiambu, mshtakiwa alikutana njiani na wasichana hao wawili; mmoja akiwa na umri wa miaka tisa na mwingine minane.

Baadaye aliwanunulia bhajia ya Sh20 na kuwahadaa kufika kwa chumba chake.

Baada ya kutenda kitendo hicho wasichana hao walirejea nyumbani lakini hawakusema lolote.

Hata hivyo ilidaiwa kuwa mmoja wa mama wa wasichana hao alishuku msichana wake akionyesha maumivu alipotembea.

Alipomhoji zaidi alipata kuwa alikuwa amenajisiwa vibaya sehemu zake za siri.

Mahakama iliamini jinsi wasichana hao walivyoeleza walivyonajisiwa na mshtakiwa ambaye waliweza kumtambua vyema.

Ubikira

Ripoti ya daktari iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha wazi kuwa wawili hao walinajisiwa ambapo ubikira wao ulitatizwa baada ya kutoneshwa.

Mshtakiwa akijitetea alisema ya kwamba mashtaka hayo ni ya kusingiziwa; jambo ambalo mahakama ilipuzilia mbali ikisema ni kweli alipatikana na makosa.

Baada ya hakimu kutoa uamuzi huo, mshtakiwa alionyesha uso wa huzuni jambo ambalo lilionyesha wazi kuwa alikuwa ameshtushwa na uamuzi huo mkali.

Nao wazazi wa wasichana hao pamoja na jamaa zao waliridhika na uamuzi wa mahakama wakisema kweli haki imetendeka.

Mwekezaji ataka Joho atupwe jela miezi 6

PHILIP MUYANGA Na CHARLES LWANGA

MFANYABIASHARA aliyeshtaki serikali ya Kaunti ya Mombasa kufuatia mzozo wa shamba, sasa anataka Gavana Hassan Ali Joho aadhibiwe kwa kukaidi agizo la mahakama.

Bw Ashok Doshi na mkewe Pratibha, wanataka Gavana Joho, afisa mkuu wa idara ya ardhi Jaffer Mohesh na diwani Benard Ogutu wafungwe miezi sita gerezani kwa kupuuza agizo la mahakama.

Kupitia kwa wakili wao Willis Oluga, Bw Doshi na mkewe wanasema kuwa mahakama ilitoa agizo la kupiga marufuku serikali ya kaunti kubomoa ukuta, jengo au kuharibu mali yoyote iliyoko katika kipande chake cha ardhi.

Mlalamishi anasema kuwa mnamo Mei 10 mwaka huu, maafisa wa serikali ya kaunti wakiongozwa na Bw Joho pamoja wanasiasa wengine kutoka Mombasa, wallikodisha wahuni ambao walivamia shamba lake na kubomoa lango huku wakimshutumu kwa madai kuwa ni mnyakuzi wa ardhi.

“Gavana wa Mombasa alifanya mkutano wa kisiasa ndani ya shamba hilo akidai kwamba yeye ndiye ‘rais’ wa kaunti, na kisha akabatilisha hatimiliki ya ardhi hiyo,” anasema mlalamishi katika stakabadhi zake kortini.

Mlalamishi anasema Bw Joho, Bw Mohesh na na diwani Bw Ogutu walikaidi agizo la mahakama kwa kuvamia ardhi hiyo na kumtatiza kuitumia.

Mlalamishi anasema kuwa Gavana Joho na Bw Ogutu, wakiwa watumishi wa umma, wanafaa kuwa kielelezo bora kwa kuheshimu korti na kudumisha amani badala ya kutumia wahuni kuzua rabsha.

Kwingineko, Hakimu Mkuu katika mahakama ya Malindi, Bi Julie Oseko jana alimshtumu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji, kwa kuchelewa kuwasilisha mashahidi kwenye kesi.

Bi Oseko alisema upande wa mashtaka umewasilisha mashahidi wanne pekee katika kesi ambapo mwanamke na afisa wa polisi wameshtakiwa kwa kuhujumu kesi.

“Kwa nini mashahidi wanne pekee watoe ushahidi katika kipindi cha miaka miwili tangu kesi ianze? ” akasema Bi Oseko.

Alizungumza baada ya kusikizwa kwa kesi ambapo Bi Amina Shiraz pamoja na Sajenti Abdi Sheikh wameshtakiwa kwa kuficha ushahidi wa mauaji ya Bw Jimmy Baburam anayedaiwa kuuawa na mkewe, Bi Shiraz katika hoteli ya Medina Palms eneo la Watamu, mnamo Julai 26, 2015.

Wakati wa kesi kusikizwa, aliyekuwa kamanda wa polisi Watamu, Bw Michael Ndonga alisema kuwa daktari aliyekuwa anashika doria katika hospitali ya Watamu Nursing Home alimwabia kuwa Bw Baburam alikuwa ameshaaga dunia wakati alifikishwa katika hospitali hiyo.

“Nilipofika katika hospitali ambapo marehemu alipelekwa, niliangalia na nikaona kuwa mwili huo haukuwa na alama yoyote ya kuumizwa,” alisema.

Bw Ndonga alisema alienda katika hoteli ya Medina Palms kulitokana baada ya mkuu wa usalama katika hoteli hiyo kumpigia simu ya kuwa mtalii mwanaume amefariki chumbani mwake.

“Aliniambia kwa simu kuwa mtalii aliyekuwa ameabiri chumba mnamo Julai 21, 2015 hadi Julai 27, 2015 amefariki chumbani na alikuwa anataka niende nikaone mahali alifariki,” alisema.

Bw Ndonga ambaye sasa hizi ni Naibu Kamada wa polisi Kaunti Ndogo ya Voi, alisema kuwa aliambatana na polisi mwenzake, Konstebo Mutua hotelini na wakapata damu sakafuni, chupa za pombe, taulo na chupa za kunywea pombe kando ya dimbwi la kuogelea.

Alisema kuwa baada ya hapo walielekea hospitalini ambapo mwili huo unadaiwa kupelekwa na wakampata mwamerika anayesakwa na polisi pamoja na Bi Shiraz akiwa analia.

“Bi Shiraz alikuwa ameambatana na mwanaume ambaye alijitambulisha kama Bw Jacob Schmalze na akasema kuwa yeye ni rafiki wa familia ya marehemu,” alisema.

Bali na shtaka la kunyimana haki, Bi Shiraz pamoja na raia huyo wa Amerika wanakabiliana na shtaka lengine katika Mahakama ya Mombasa ya kumuua Bw Baburam.

Kesi inaendelea kusikizwa.

 

ONYANGO: Idadi kubwa ya vijana waliopo magerezani inashtua sana

Na LEONARD ONYANGO

RIPOTI kuhusu Hali ya Uchumi ya 2019 iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) wiki iliyopita , inafaa kushtua serikali pamoja na wazazi.

Ripoti hiyo ilipotolewa, vyombo vya habari viliangazia tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana licha ya uchumi kuonekana ‘kukua’.

Kulingana na ripoti hiyo, serikali ya Jubilee imefanikiwa kubuni nafasi milioni 1.8 za kazi pekee tangu ilipochukua hatamu za uongozi mnamo 2013, huku mamilioni ya watu wakiwa hawana kazi.

Lakini suala ambalo halikupewa uzito na wanahabari ni kuhusu idadi kubwa ya vijana wa chini ya umri wa miaka 25 wanaotumikia vifungo magerezani.

Ripoti hiyo ya KNBS inaonyesha kuwa karibu nusu ya wafungwa 223,718 waliokuwa gerezani kufikia mwishoni mwa 2018, ni vijana wa chini ya umri wa miaka 25.

Vijana wa umri wa kati ya miaka 16 na 25 ndio wamejazana katika magereza, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Idadi ya watoto wa chini ya miaka 16 ni ya chini japo inaonekana kuongezeka.

Kwa mfano, katika mwaka wa 2016 kulikuwa na vijana 111 wa chini ya umri wa miaka 16 waliozuiliwa magerezani, 114 mnamo 2017 na 131 mwaka jana.

Vijana wa kiume ndio wengi magerezani ikilinganishwa na wenzao wa kike.

Ukitathmini kwa makini utabaini kwamba wengi wa watu waliojazana gerezani walipatikana na hatia ya wizi na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Inasikitisha kwamba vijana wanaofaa kuwa shuleni wakisoma ili kusaidia familia zao katika siku za usoni, wanateseka gerezani!

Kuwepo kwa idadi kubwa ya vijana wa umri wa chini magerezani ni ishara kwamba jamii imewatelekeza watoto haswa wa kiume.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ripoti kuhusu ongezeko la vijana wa umri wa chini wanaojiunga na uhalifu.

Je, ni nini kinasababisha watoto kujiingiza katika magenge ya uhalifu?

Wengi watadai kwamba hali hiyo inasababishwa na ukosefu wa ajira nchini. Lakini ukweli ni kwamba katiba imepiga marufuku ajira za watoto wa chini ya umri wa miaka 18 kwani wanastahili kuwa shuleni.

Wazazi wametelekeza watoto wao na wameshindwa kufunza maadili mema.

Serikali haina budi kufanya utafiti ili kubaini kinachosababisha vijana kujazana katika magereza.

Jela ambapo wafungwa huondoka kila siku kwenda kusaka riziki

MASHIRIKA Na PETER MBURU

KATIKA jela ya Sanganer katika Jiji la Jaipur, India kuna mazingira ya aina yake kwani japo wahalifu hufungwa humo, hawapewi chakula.

Kutokana na hilo, inawabidi wafungwa kila siku kwenda kutafuta kazi za vibarua ili kupata riziki, nje ya gereza.

Jela hiyo, ambao iko taifa la Rajasthan, magharibi mwa India haina kuta, vizuizi wala walinzi kwenye lango. Wafungwa huhimizwa kwenda jijini kila siku kujitafutia riziki.

Ilianzishwa miaka ya 1950 na kila wakati ina wafungwa 450. Ni moja ya taasisi nyingine za aina hiyo takriban 30 katika taifa hilo la Rajasthan.

Watu waliohukumiwa kwa makosa makubwa kama kuua, wizi wa mabavu na mengine hupata makao humo.

Taifa hilo limekuwa likizidisha juhudi za kuwepo kwa magereza wazi, kampeni inayoongozwa na Bi Smita Chakraburtty, akitaka iwe kawaida kote India.

Bi Chakraburtty amefikisha kesi katika mahakama ya juu India, ambapo anataka mataifa madogo tofauti ndani ya nchi pana ya India kuanzisha jela za aina hiyo.

Tayari mataifa mengine manne huko India yameanza kutekeleza mfumo huo wa magereza, kwani mwaka uliopita yalifungua jela za aina hiyo.

“Muundo wa utoaji haki katika sheria za kijinai ni wa kushughulikia vitendo lakini mtendaji huwa haangaziwi,” akasema Smita.

Hakuna walinzi katika jela hizo na kila anayetaka kutembea humo ndani huwa yuko huru.

Wengi wa walio katika jela ya Sanganer ni wale waliofungwa kwa makosa ya mauaji. Wafungwa katika jela hiyo huona maisha yakiwa rahisi na kila wakati wamefurahi.

Lakini kabla ya kupelekwa katika jela hiyo, wote sharti wawe wamehudumia thuluthi mbili za muda wa kifungo katika jela ya kudhibitiwa, wakiona jela hiyo ya kisasa kuwa uhuru kabisa.

Kukatalia ndani

Tangu kuundwa kwa jela hiyo, serikali inasemekana kuwa na wakati mgumu wakati vifungo vya wafungwa vinapokamilika kwani wengine wao wanakatalia humo.

Katika nyakati fulani, serikali inalazimika kuwafukuza wafungwa kutoka gerezani kwa lazima, kwani wanakataa wanapoona kuwa kuna shule na mazingira mazuri humo ndani.

Wafungwa hao huendesha maisha kikawaida humo ndani kwani wanaweza kununua vitu kama simu, pikipiki na runinga wanapofanya kazi.

Aidha, hawavai sare yoyote ya jela na wanaishi kwa vikundi vidogo. Hata hivyo, jela haiwapi kitu kingine kama chakula, pesa wala maji na hivyo inawabidi kuondoka kutafuta kazi.

Ni kwa sababu hii ndipo kila siku utawapata wengi wao wakiondoka kutoka jela hiyo kwenda kutafuta riziki, japo ni wafungwa.

Wanaume waliofungwa kwa mauaji hufanya kazi za ulinzi, wa viwanda na vibarua vingine vya kila siku.

Wanaadhibiana

Sheria ya pekee ni kuwa wafungwa hao sharti kila siku jioni waangaliwe ikiwa wako wote. Ni mfungwa ambaye huendesha zoezi hili. Kwa kawaida, ni wafungwa wenyewe ambao hujiongoza na kuadhibiana panapokuwa na makosa.

Mfungwa akijaribu kutoroka kutoka jela hii anahatarisha kurudishwa katika jela ya kufungiwa ndani.

Wafungwa wengi, hata hivyo, bado huadhiriwa na hali kuwa watu wengi wa kawaida huhusisha mazingira wanamoishi ya jela kuwa yasiyo mazuri na hivyo huwaona kama watu wasiokuwa wa kuaminika. Baadhi ya watu huwanyima kazi wanapotoa vitambulisho vyao vya jela.

Lakini kwa wanawake, wengi wao wamesema kuwa angalau mazingira hayo ya jela hiyo yamewafaa kwa kuwawezesha kukutana na wanaume ambao wamewapenda.

Wanawake wengi walikiri kuwa wamepata waume ambao wameanzisha familia nao, hivyo wakijihisi wakamilifu.

Ndani miaka 105 kwa kulawiti wavulana watatu

Na CHARLES WANYORO

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 36 Jumatano alifungwa jela miaka 105 kwa kuwalawiti wavulana watatu kwa siku tatu mfululizo katika kijiji cha Makengi, Kaunti ya Embu.

Hakimu Mkuu Mkazi, Vincent Nyakundi alimhukumu Paul Muriithi Karuga kifungo cha miaka 35 jela kwa mashtaka matatu yaliyomkabili. Kwa jumula, Muriithi anafaa kuishi jela miaka 105 lakini mahakama ikaamua hukumu zote zitatumika wakati mmoja.

Muriithi alishtakiwa kwamba kwa siku tatu mfululizo kati ya Mei 20 na Mei 22 2017 katika kijiji cha Kanjau, Makengi, Kaunti ya Embu, kwa makusudi na kinyume cha sheria, aliwalawiti wavulana watatu waliokuwa na umri wa kati ya miaka 9 na 12.

Alikabiliwa na mashtaka matatu mbadala ya kushirikisha wavulana hao katika kitendo cha aibu.

Mahakama iliambiwa kwamba siku ya kwanza, mshtakiwa alimuotea mvulana wa kwanza akitoka kanisani na kumtaka washiriki mapenzi lakini akatoroka. Alimkimbiza mtoto huyo na kumkamata kisha akampeleka kichakani akamlawiti.

Siku iliyofuata, Muriithi aliwavamia ndugu wawili waliokuwa wametumwa dukani na nyanya yao jioni, akawanyang’anya tochi na mmoja alipotoroka, alimshika mwenzake na kumlawiti.

Siku iliyofuata alikutana na mwathiriwa wa tatu ambaye alikuwa akienda dukani na akamwambia apande kwenye mkokoteni wake uliokuwa ukivutwa na fahali amsindikize kisha akampeleka kichakani na kumlawiti.

Wavulana hao waliwaeleza wazazi wao ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Manyatta na Muriithi akakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Pendekezo wafisadi wote wasukumwe jela maisha

Na HAMISI NGOWA

MBUNGE wa Likoni, Bi Mishi Mboko amependekeza watu wanaopataikana na hatia ya ufisadi wafungwe gerezani maisha na kisha mali zao kutwaliwa na serikali.

Anasema ni kupitia kwa adhabu kali kama hiyo ambapo taifa hili litaweza kufaulu kwenye vita vyake dhidi ya ufisadi.

“Wakati umefika kwa taasisi za kisheria ikiwemo Idara ya Mahakama kuhakikisha zinawapa adhabu kali wanaopatikana na hatia ya ufisadi ili kuwa mfano kwa wenye hulka hiyo,” alisema.

Akizungumza mwishoni mwa wiki akiwa Likoni, mbunge huyo wa chama cha ODM alikemea vikali sakata ya mpya ya ufisadi iliyofichuliwa hivi majuzi katika Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) pamoja na ile ya mahindi akisema zinalemaza ajenda nne kuu za serikali.

Alisema inasikitisha kuona idara hiyo muhimu inayotegemewa kumaliza matatizo ya vijana ikihusishwa tena na sakata kubwa ya wizi wa mabilioni ya pesa.

“Ninaona wakati umefika kwa sheria kali kuchukuliwa dhidi ya watu wanaopatikana na hatia ya uporaji  mali ya umma. Wanafaa wafungwe gerezani maisha na mali yao kutaifishwa na serikali,” akasema.

 

Mwanamke ndani miaka 15 kwa kunajisi tineja

Na RUSHDIE OUDIA

KATIKA kisa kisicho cha kawaida, Mahakama ya Kisumu Jumatano ilimhukumu mwanamke wa miaka 24 kifungo kikali cha miaka 15 gerezani kwa kufanya mapenzi na mvulana tineja wa miaka 15.

Hukumu hiyo ilizua mjadala mkali miongoni mwa watumizi wa mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook kwani mara nyingi visa vingi kuhusu ubakaji na unajisi huhusisha wanaume kuwadhulumu wasichana na wanawake.

Bi Judith Wandera (pichani) alipatikana na hatia ya unajisi na kumfanyia mtoto kitendo kichafu kinyume na sheria mnamo Julai 5, 2017 katika Kaunti ya Kisumu.

Mashahidi saba walitoa ushahidi dhidi yake kwenye kesi hiyo huku Bi Wandera akijitetea kivyake.

Kwenye uamuzi wake, Hakimu Mkuu wa Kisumu, Bi Joan Wambilyanga alisema wawili hao walikamatwa Julai 17, mwaka mmoja baada ya kuanza uhusiano wa kimapenzi.

“Wote wawili walikiri kushiriki mapenzi, wakati mwingine walitumia kinga na wakati mwingine hawakutumia,” akasema Bi Wambilyanga alipokuwa akitoa hukumu.

Akijitetea, mshtakiwa alidai hangeweza kujua umri wa mvulana huyo walipokutana kwani alipomtazama hakuonekana kama mwenye umri wa chini ya miaka 18, na pia alikuwa ni mwendeshaji wa bodaboda.

Sheria inayohusu makosa ya vitendo vya ngono huruhusu mshtakiwa kujitetea kuwa hakufahamu umri wa mtu kutokana na maumbile, lakini mahakama ilipata kuwa Bi Wandera hakuweka juhudi zozote kubainisha umri wa tineja huyo.

Hakimu alipuuzilia mbali tetesi za mshtakiwa na kumwambia angethibitisha iwapo alichukua hatua yoyote kutambua umri wa mlalamishi.

“Hapakuwa na ushahidi wowote kuonyesha kuwa mlalamishi alidanganya kuhusu umri wake na utetezi wa mshtakiwa umetupwa nje kwa sababu alishindwa kuthibitisha hatua alizochukua kubainisha kama mvulana huyo alikuwa na umri wa chini ya miaka 18,” akasema Bi Wambilyanga.

Mshtakiwa aliambia korti kuwa tineja huyo alikuwa akitumia dawa za kulevya na alionekana tu mwenye umri mdogo alipokuja mahakamani kutoa ushahidi.

 

Aliacha masomo

Katika ushahidi wake, tineja huyo alieleza mahakama jinsi alivyoacha shule alipokuwa katika darasa la saba mwaka wa 2016 na akawa mhudumu wa bodaboda.

Hakimu alisema wawili hao walikamatwa mara mbili awali, mshtakiwa akaambiwa akomeshe uhusiano huo baada ya mama ya mvulana kulalamika kuhusu tofauti ya umri wao lakini mshtakiwa akapuuza hayo yote.

Bi Wandera aliomba asamehewe kwa sababu ana mtoto, kaka na mama ambao wanamtegemea kimaisha. “Mimi pekee ndiye ninategemewa. Tafadhali nisamehe sitarudia kosa hilo,” akaomba. Lakini ombi lake halikufua dafu.

Hukumu iliposomwa alijikuna kichwa huku macho yake yakionekana kana kwamba alitaka kulia, kisha akamtazama dadake aliyekuwa mahakamani.
Wakati wote kesi ilipokuwa ikisikilizwa, Bi Wandera alikuwa mtulivu lakini hukumu iliposomwa alibadilika kwani ni kama hakutarajia adhabu kali kiasi hicho.

Kicheko mahabusu kumlilia hakimu aongezwe ugali rumande

TITUS OMINDE na BRIAN OCHARO

MAHABUSU aliye katika rumande ya Gereza Kuu la Elodret alisababisha kicheko mahakamani Jumatano alipodai kuwa maisha yake yamo hatarini kutokana na kipimo kidogo cha ugali ambacho anapewa kizuizini.

David Shikoli ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kubaka mwanamke, alimwambia Hakimu Mkuu, Bw Harrison Barasa kuwa mwili wake unaendelea kudhoohofika kutokana na ugali mdogo anaopewa huko.

“Mheshimiwa huu mwili wangu haukuwa hivi. Nimepungua kutokana na chakula kidogo ambacho napewa kule jela. Sikuzoea maisha ya kula ugali kidogo. Tafadhali nitetee,” akasema Shikoli.

Aliiambia mahakama kuwa juhudi zake za kutaka kusikizwa na wasimamizi wa gereza hilo zimegonga mwamba, kwani maafisa husika wamekuwa wakimwambia kuwa jela si nyumba ya mama yake.

Hata hivyo, hakimu alimshauri awasilishe malalamishi yake kwa maafisa wa maslahi kutoka katika idara ya mahakama, ambao watazuru gereza hilo mwishoni mwa juma hili.

Shikoli alishtakiwa pamoja na wenzake ambao hawako mahakamani kwa kubaka mwanamke mmoja mnamo Desemba 23, 2017 katika kijiji cha Kambi Miwa kwenye kaunti ya Uasin Gishu.

Kesi yake itasikizwa Mei 7.

Katika mahakama ya Mombasa, mwanamume aliwaacha watu vinywa wazi, alipokiri kuiba vijiko 108 vya thamani ya sh3,780 kutoka duka kuu la Uchumi.

Theophilus Mutunkei Sakaya hata hivyo hakufafanua sababu za kitendo hicho.

Alishtakiwa kuiba vijiko hivyo kutoka kwa duka hilo kwenye barabara ya Moi mnamo Aprili 21 mwaka huu.

Hata hivyo, Sakaya aliachiliwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Edgar Kagoni baada ya kusema kuwa alitaka kwenda kwa mazishi ya mama yake ambaye alikufa wiki moja iliyopita.

“Nimesikia malilio ya mshukiwa na kuzingatia kwamba vijiko vyote vimepatikana, nitamuachilia huru chini ya kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu ya Jinai,” alisema Bw Kagoni.

Inasemekana kwamba siku hiyo, Sakaya aliingia katika duka hilo saa tatu na nusu asubuhi akijifanya kuwa mteja.

Ripoti za polisi zasema alielekea moja kwa moja kwenye rafu ambapo vijiko vilikuwa na kuchukua rundo tisa za vijiko na kuziweka katika mfuko wake wa mbele.
 

Rais wa zamani aanza kutumikia kifungo cha miaka 12 katika jela

Na AFP

RAIS wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, alianza siku yake ya kwanza kutumikia kifungo cha miaka 12 gerezani Jumapili. 

Ingawa marais wengi waliowahi kuongoza Brazil wamekuwa wakikumbwa na matatizo ikiwemo kung’atuliwa mamlakani kupitia uamuzi wa bunge au mapinduzi, na kisa kimoja cha rais kujitoa uhai, Lula ni wa kwanza kuwahi kuhukumiwa kwa ufisadi na kufungwa jela.

Makao yake mapya sasa ni ya ukubwa wa futi 160 kwa mraba pekee, katika makao makuu ya idara ya polisi yaliyo Curitiba, jiji la kusini mwa nchi ambapo upelelezi kumhusu ulikuwa ukifanywa hadi alipokamatwa.

Lula alipatikana na hatia mwaka uliopita kwa kuchukua jumba la kifahari kama hongo kutoka kwa kampuni ya ujenzi, ingawa anasema hukumu yake si ya haki.

Rais huyo aliyehudumu kwa awamu mbili kuanzia mwaka wa 2003 hadi 2011, aliwasili gerezani Jumamosi jioni kwa helikopta iliyotua kwenye paa la makao makuu ya polisi Curitiba.

Wakati helikopta ilipokuwa ikitua, waandamanaji nje ya jengo hilo waliwasha fataki huku polisi wa kupambana na ghasia wakiwarushia gesi ya kutoza machozi, na kupelekea hewa kujaa moshi na milio ya vilipuzi.

Watu wanane walipata majeraha madogo katika maandamano hayo, ikiwemo mmoja ambaye alipigwa risasi ya mpira, kwa mujibu wa idara ya zimamoto.

Lula, ambaye licha ya sakata zinazomkumba anaongoza kwenye kura za maoni kuhusu uchaguzi wa urais wa Oktoba, alijaribu kufanya hukumu yake icheleweshwe kwa kuwasilisha msururu wa rufaa katika Mahakama Kuu ya Brazil mnamo Jumatano iliyopita.

Wakati hatua hiyo ilipogonga mwamba, alianza kuzozana na maafisa wa serikali katika mtaa wa Sao Bernardo do Campo anakotoka, viungani mwa Sao Paulo.

Huku akiwa amezingirwa na maelfu ya wafuasi katika jumba la chama cha wafanyakazi wa vyuma, alipuuza agizo la mahakama lililomtaka ajisalimishe Ijumaa.

Ilipofika Jumamosi, alikubali kupelekwa jela, lakini msafara wake ukazuiliwa na wafuasi wake ambao walikuwa wakiwika “usijisalimishe, baki hapa Lula!”.

Ilibidi ashuke kwenye gari akazingirwa na walinzi na kutembea hadi kwenye gari la polisi ambalo lilimpeleka katika uwanja wa ndege wa Sao Paulo, na kusafirishwa hadi Curitiba.

Hata hivyo, seli alimofungwa ina mandhari bora ikilinganishwa na zingine, ikiwemo bafu ya kibinafsi yenye maji moto na choo.

Mwanamke alilia haki kufuatia mateso Uarabuni

Na MOHAMED AHMED

MACHOZI ya furaha yalibubujika kutoka machoni mwa mzee Ndolo Baya baada ya mtoto wake wa mwisho aliyekuwa anatumikia kifungo nchini Saudi Arabia kurudi nchini.

Mawazo ya Bw Baya, 71, kuwa ataenda kupokea maiti ya bintiye yaligeuka Jumapili baada ya kitinda mimba wake kurudi nchini salama.

Levina Mapenzi, 27, alirudi nyumbani baada ya kukaa nchini humo miaka minne.

Baada ya kufanya kazi kwa mwaka mmoja na nusu alikamatwa na kufungwa jela kwa madai ya kufanya zinaa.

Aidha katika mahojiano na Taifa Leo Jumapili,  Bi Mapenzi alidai kuwa alibakwa na dereva wa tajiri yake.

levina Mapenzi Ngolo akihadithia wanahabari Aprili 8, 2018 yaliyomsibu alipokuwa Saudi Arabia. Analilia haki baada ya kutupwa jela kwa mwaka mmoja nchini humo kwa kile alichokitaja kuwa madai ya uongo dhidi yake. Picha/ Laban Walloga

“Nilifungwa kwa madai ya kufanya ngono. Lakini sikuwa nimefanya hilo. Nilibakwa na jamaa huyo ambaye yeye alichapwa viboko kama ilivyo kulingana na sheria za kule,” akasema huku akitokwa na machozi ya uchungu.

Bi Mapenzi alitumikia mwaka mmoja jela ambapo alijifungua mtoto wake wa kiume aliyerudi naye baada ya kupatikana na masaibu katika nchi hiyo ambayo imeshutumiwa mara nyingi kufuatia kuteswa kwa Wakenya wanaoenda kufanya kazi hususan wanawake.

“Kwa sababu niliiambia mahakama kuwa nilifanyiwa dhuluma za kimapenzi ndio nikapewa adhabu hiyo ya kifungo cha mwaka. Nashukuru nimerudi salama lakini sikupata lile nililoendea,” akasema.

Bi Mapenzi aliondoka humu nchini mwaka 2014 bila ya ruhusa ya babake ili kutafuta riziki na aweze kukimu mahitaji ya mtoto wake wa kwanza aliyemuacha humu nchini.

Alieleza kuwa baada ya kupatikana na mimba ya miezi miwili na tajiri yake aliweza kuwapeleka yeye pamoja na mwanamume huyo polisi na baadaye kuhukumiwa.

 

Wakili Mutinda aponea kusukumwa jela kwa kuwa ‘mwongo’

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI wa Serikali Charles Mutinda yuko na bahati kama mtende kwa vile aliponyoka kusukumwa jela kwa madai hakuwaarifu Waziri wa Usalama Fred Matiang’I, Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Meja mstaafu Gordon Kihalangwa wamfikishe wakili mbishi Miguna Miguna makamani Alhamisi.

Mawakili Cliff Ombeta, John Khaminwa , Harun Ndubi na James Orengo waliomba Jaji George Odunga amsukume Mutinda jela kwa kukaidi agizo la korti kwa “kutowakabidhi agizo la korti wafike kortini wakiandamana na Dkt Miguna.”

“Huyu wakili wa Serikali anadanganya. Ni mdanganyifu. Alikaidi agizo la hii korti kwamba Miguna afikishwe kortini leo,” alisema Khaminwa.

Dkt Khaminwa alisema Mutinda hakuchukulia suala hilo kwa makini ndipo washtakiwa hawakufika kortini. “Naomba uamuru Mutinda asiwahi kuhudumu kama wakili na kwamba asithubutu kufika mbele ya mahakama yoyote kwa vile amekaidi sheria kama wakuu hao wa serikali waliokwepa mahakama.”

Bw Ombeta alisema Mutinda ni “mwongo na hata hafai kusimama kortini bali anatakiwa kufukuzwa aende nyumbani.”

Ombeta alishangaa jinsi Bw Mutinda hakuwaona Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet ilhali waliapa afidaviti aliyotumia kukata rufaa na kesi nyingine ya kuomba maagizo ya Jaji Roselyn Aburili yatupiliwe mbali. “Huyu wakili Mutinda ni mdanganyifu.”

Bw Orengo alisema Bw Mutinda anapasa kupewa adhabu moja na Matiang’i, Boinnet na Kihalangwa kwa vile wote wamekaidi agizo la hii mahakama.

“Je, Matiang’i na wenzake wako wapi. Uliwaambia wanatakiwa kufika hapa kortini?” Jaji Odunga alimwuliza.

“Sikuwafikia kwa simu. Nilipiga simu mara 16 na sikujibiwa,” alisema Mutinda.

Bw Mutinda alijililia na kuomba korti isiamuru akome kutoa huduma za uwakili katika afisi ya mwanasheria mkuu ama kama wakili wa kibinafsi.

“Naomba hii mahakama iwachukulie hatua Matang’i, Kihalangwa na Boinnet. Nihurumie. Mimi ni wakili tu na kamwe sijakaidi agizo ka mahakama,” alijitetea Murinda.