Viongozi kukongamana kwa mkutano wa UNGA

Na AFP

NEW YORK, Amerika

VIONGOZI wa ulimwengu wiki hii watakongamana katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, kwa Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Kwa mara ya kwanza tangu mlipuko wa janga la Covid-19 mwaka 2020, viongozi hao wanafanya mkutano wa ana kwa ana kinyume na 2020 ambako walituma taarifa zao kupitia video.

Hata hivyo, thuluthi moja ya mataifa 193 bado yatatuma video kwa mkutano huo.Miongoni mwa mada kuu zitakazojadiliwa katika mkutano huo, ni juhudi mpya za kupambana na athari za Covid-19 na Mabadiliko ya Tabianchi.

Hatua ambazo ulimwengu umepiga katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) pia zitaajdiliwa katika kikao hicho cha UNGA ambacho pia kitahudhuriwa na wakuu wa mashirika ya kimaendeleo ya kimataifa.

Rais wa Amerika Joe Biden atahutubia kikao hicho kesho Jumanne, kwa mara ya kwanza tangu alipoingia mamlakani mnamo Januari 20, 2020.

Balozi wake katika UN Linda Thomas-Greenfield, alisema Biden “atazungumzia masuala yenye umuhimu mkubwa kwetu: kutokomezwa kwa Covid-19, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, kutetea haki za kibinadamu, demokrasia na uthabiti ulimwenguni.”

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Jumamosi aliondoka kuelekea Amerika kuhudhuria mkutano huo ambapo anatarajiwa kuhutubia kikao hicho Alhamisi wiki hii.

Hii ndio itakuwa ziara ya kiongozi huyo nje ya bara Afrika tangu alipoingia mamlakani Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli.

Mara ya mwisho Rais wa Tanzania kuhutubia mkutano wa UNGA ilikuwa mnamo 2015 na alikuwa Rais wa awamu ya nne wa taifa hilo, Jakaya Mrisho Kikwete.

Amerika imesema kuwa kila kiongozi atakayeingia katika ukumbi mkuu wa mkutano sharti athibitishe kuwa amepewa chanjo dhidi ya Covid-19.

Utawala wa jiji la New York pia umeweka kituo cha muda nje ya lango kuu la Makao Makuu ya UN ambako kuna wahudumu wa kuwapa wageni chanjo aina ya Johnson & Johnson, bila malipo.

Chanjo hii hutolewa mara moja.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres , aliwaambia wanahabari kwamba umoja huo unalenga kuhakikisha kuwa asilimia 70 ya watu ulimwenguni watakuwa wamepewa chanjo kufikia Juni, 2022.

Alisema kufikia sasa jumla ya dozi 5.7 bilioni za aina mbalimbali ya chanjo zimetolewa kote ulimwenguni.

Bara la Afrika limepokea asilimia mbili pekee ya dozi hizo.

Biden aipapura Facebook kutozima habari za uongo kuhusu corona

Na AFP

WASHINGTON DC, Amerika

RAIS wa Amerika, Joe Biden ameonya kwamba uenezaji wa habari za uongo kupitia mitandaoni hasa Facebook kuhusu virusi vya corona ndio umechangia kwa vifo vya watu wengi ulimwenguni.

Tangu aingie mamlakani, Rais Biden amekuwa akipiga vita vikali habari feki kuhusu janga la corona kupitia Facebook huku Marekani ikiendelea kuwapa raia wake chanjo ya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

“Wanawaua raia. Janga pekee ambalo tuko nalo ni kuhakikisha kuwa watu wote wanapokea chanjo,” akasema.

Uhasama kati ya Facebook na Rais Biden haujaanza leo. Mnamo Januari mwaka jana akilenga kuwania urais, alinukuliwa na jarida la New York Times akisema mmiliki wa Facebook, Mark Zuckerberg ana tatizo kubwa hasa kuwa kuruhusu kuchapishwa kwa taarifa za kumchafulia jina.

Maafisa wa kitengo cha afya nchini Marekani tayari wameonya kwamba kupanda kwa vifo na maambukizi ya corona, kunawaathiri hasa watu ambao bado hawajapokea chanjo ya corona.

Mapema Ijumaa, Mkuu wa Mawasiliano katika ikulu ya White House, Jen Psaki alisema Facebook na mitandao mingine ya kijamii haijafanya juhudi za kutosha kupigana na habari potovu kuhusu chanjo zinazotolewa za corona.

“Japo wamechukua hatua kupigana na ueneaji wa habari potovu kuhusu corona na chanjo, kuna mambo mengi ambayo bado yanahitaji kutekelezwa na Facebook kuzuia tabia hiyo,” akasema Psaki.

Hata hivyo, msemaji wa Facebook Kevin McAlister amekashifu Rais Biden kwa matamshi yake, akisema kampuni hiyo haitayumbishwa katika utendakazi wake na madai ambayo hayana msingi wowote kutoka Marekani.

“Kama kampuni tuliondoa habari feki milioni 18 zinazohusiana na janga la corona. Pia tumekuwa tukidhibiti na kufuta akaunti za watu binafsi au mashirika ambayo yanakiuka kanuni na kueneza uongo kuhusu janga la corona,” ikasema taarifa ya Facebook.

Mtandao wa Facebook umekashifiwa kwa kutofuta machapisho ambayo yana jumbe potovu kuhusu janga la corona.

Jumbe hizo bado zimekuwa zikisambazwa, hali ambayo imetia doa uwajibikaji wa kampuni hiyo na kuikasirisha Marekani. Ijumaa, Mkurugenzi wa Kituo cha Afya cha Kupambana na Kuzuia Magonjwa Marekani, Rochelle Walensky aliwatahadharisha raia ambao bado wamekataa kupokea chanjo kuwa afya yao iko hatarini na kuwashauri wabadili mtazamo.

Ni asilimia 67.9 pekee ya Wamarekani ambao wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo huku asilimia 59.7 wakiwa wamechanjwa mara mbili jinsi inavyohitajika. Wengi bado wamekataa kupokea chanjo wakisema hawaiamini na huenda ikawaathiri kiafya.

Mbali na Facebook, mtandao wa YouTube pia umekashifiwa kwa kueneza habari hizo za uongo.

Rais Biden sasa ataka Israeli isitishe mashambulio Gaza

Na MASHIRIKA

GAZA, Palestina

RAIS wa Amerika Joe Biden, Jumanne alieleza hisia zake kuhusu kusitishwa kwa mapigano baada ya siku nane za ghasia za kikatili kati ya jeshi la Israeli na wanamgambo wa Palestina mjini Gaza.

Biden aliambia Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kwamba Amerika inashirikiana na Misri na mataifa mengine kusitisha machafuko hiyo.

Hata hivyo, Amerika kwa mara nyingine ilizuia taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, iliyoitisha kusitishwa kwa mapigano hayo.

Rais wa Amerika Joe Biden. Picha/ AFP

Ghasia hizo sasa zimeingia katika wiki yake ya pili bila dalili zozote za kusitishwa.

Israeli mapema Jumanne iliendeleza mashambulio yake ya angani dhidi ya Gaza.

Jeshi lake lilisema mamia ya roketi zilifyatuliwa katika eneo lake usiku kucha. Watu wasiopungua 212 wakiwemo wanawake na watoto 100 wameuawa Gaza, kulingana na wizara ya afya nchini humo.

Katika taifa la Israeli, watu 10 ikiwemo watoto wawili wameuawa kulingana na idara ya matibabu humo.

Israeli ilisema Jumanne kuwa wanamgambo wapatao 150 ni miongoni mwa waliouawa Gaza.

Kundi la Hamas, ambalo ni wanamgambo wa Palestina wanaotawala eneo hilo, huwa halitoi idadi ya wapiganaji waliojeruhiwa.

Kulingana na taarifa kutoka Ikulu ya White House mnamo Jumatatu, Biden “alihimiza Israeli kujitahidi kwa vyovyote vile kuhakikisha ulinzi wa raia wasio na hatia.”

“Viongozi hao wawili walijadili kuhusu maendeleo katika oparesheni za jeshi la Israeli dhidi ya Hamas na makundi mengine ya magaidi mjini Gaza. Biden alieleza kuunga mkono kusitishwa kwa mapigano na akajadili ushirikiano wa Amerika, Misri na mataifa mengine kuhusu suala hilo,” ilisema taarifa.

Viongozi wa dunia na mashirika ya kutoa msaada wa kibinadamu wameitisha mikakati ya kuzuia vifo vya wakazi na ghasia zinazosababishwa na uharibifu wa majengo na miundomsingi.

Amerika, ambayo ni mojawapo wa marafiki wakuu zaidi wa Israeli, kwa mara nyingine ilizuia juhudi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataiga kutoa taarifa ya kuitaka Israeli kusitisha mashambulizi yake, na badala yake ikasisitiza juhudi zake za kidiplomasia.

“Makisio yetu kwa wakati huu ni kwamba, kuwa na mazungumzo hayo faraghani…ndio mwelekeo mwafaka zaidi tunaoweza kuchukua,” Msemaji wa White House Jen Psaki alieleza wanahabari.

Baraza la Usalama la UN linatazamiwa kushiriki mkutano wake wa dharura kuhusu ghasia hizo Jumanne.

UN pia ilielezea wasiwasi wake kuhusu uharibifu wa miundomsingi katika eneo linaloandamwa tayari na ufukara la Ukanda wa Gaza.

Mbwa wa Biden kupewa mafunzo mapya

Na AFP

MBWA wa Rais wa Amerika Joe Biden, anayefahamika kama Major, atapelekwa kupokea mafunzo zaidi kuhusu jinsi ya kuwa na tabia ya mbwa wa rais.

Msemaji wa Mke wa Rais Jill Biden, Michael LaRosa, alisema Major atapokea “mafunzo ya ziada ya kumsaidia kuzoea maisha katika White House”.

“Mafunzo hayo ya siri yatafanyika katika eneo la Washington, DC na yanatarajiwa kuchukua muda wa wiki chache,” alisema LaRosa.

Mabadiliko hayo ya kuhamia ghafla Ikulu ya White House yalimchanganya mbwa huyo aina ya German Shepherd, aliyekuwa mbwa wa shughuli ya uokoaji.

Mnamo Machi, alirejeshwa katika makao ya familia ya Biden, mjini Delaware, baada ya kuuma watu wasiopungua wawili katika Ikulu.

Rais Biden alieleza vyombo vya habari Machi kwamba rafikiye alikuwa tu akilinda vikali jengo la White House lenye msongamano wa watu.

 

Tangatanga washabikia ‘uhasla’ wa Rais Biden

Na BENSON MATHEKA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wamefurahishwa na kauli ya Rais wa Amerika, Bw Joe Biden ya kukumbatia mfumo wa uchumi wa kuinua maskini, mfumo ambao umekumbatiwa na Dkt Ruto.

Rais Biden alitetea mswada wake unaolenga kusaidia watu wa mapato ya chini na ya wastani kujiinua kiuchumi akisema ni mbinu ya kufaidi kila mmoja katika jamii.

“Mnajua nini, kujenga uchumi kuanzia chini kwenda juu ndio mtindo tunaokumbatia kwenye mswada huu na kwa kufanya hivi kila mmoja anafaidi,” alisema Biden.

Alisema hana shida na matajiri kuendelea kujiongezea mapato lakini ipo haja ya mfumo wa uchumi wa kusaidia maskini kupanua uchumi wao.

Seneta wa Kericho, Bw Aaron Cheruiyot alisema kwamba inashangaza mfumo huo ambao Dkt Ruto amekuwa akitumia, unapingwa humu nchini kwa madai kwamba unachochea vita vya matabaka ilhali ndio unaokumbatiwa kote ulimwenguni.

“Kama Rais Biden angekuwa Mkenya, Kalonzo (Musyoka) na wenzake wakishangiliwa na mfadhili wao na washirika wao wangekuwa wakimpiga vita wakisema anachochea vita vya matabaka. Huu ndio mfumo wa uchumi unaotumiwa kote ulimwenguni karne ya 21,” alisema Bw Cheruiyot kwenye Twitter.

Rais Kenyatta na wanasiasa wengine wakuu, akiwemo Kalonzo wamekuwa wakidai kwamba kampeni ya Dkt Ruto inasababisha chuki za kitabaka nchini.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa kampeni ya Hasla Nation, Dennis Itumbi na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwah pia walifurahishwa na kauli ya Biden wakisema kuwezesha raia wa mapato ya chini ndiyo mbinu ya pekee ya kuongeza idadi ya watu wanaolipa kodi na kuimarisha uchumi.

“Huu ndio mfumo wa uchumi ambao unatumiwa kote ulimwenguni ili watu wengi wawe na uwezo wa kulipa ushuru. Watu kama Fred Matiang’i (Waziri wa Usalama) hawawezi kuuelewa,” Bw Ichungwah alisema kupitia Twitter.

Bw Cheruiyot alisema Kenya haiwezi kuepuka mfumo huo iwapo inataka kustawisha uchumi wake.

Wanasiasa wanaompiga vita Dkt Ruto wamemlaumu kwa kutumia kampeni yake ambayo anawapa watu wa mapato ya chini vifaa vya kuwawezesha kuanzisha biashara ndogo ndogo kama wilibaro wakisema anachochea vita vya kati ya matajiri na masikini.

Biden aondoa marufuku ya Trump kuhusu uavyaji mimba

Na AFP

WASHINGTON DC, Amerika

RAIS Joe Biden ameondoa marufuku yaliyozuia Amerika kutoa misaada ya kifedha kwa mashirika ya ng’ambo yanayotoa ushauri kuhusu uavyaji mimba.

Biden alisema hatua hiyo ni miongoni mwa ambazo serikali yake inachukua kuimarisha afya.

“Ni sera ya serikali yangu kusaidia afya na haki ya afya ya uzazi ya wanawake nchini Amerika na kote ulimwenguni,” Biden alisema kwenye amri ya kuondoa marufuku hiyo.

Alisema marufuku hiyo ilihujumu juhudi za Amerika za kutetea usawa wa jinsia ulimwenguni.

Biden pia aliagiza kubadilishwa kwa kanuni zilizoanzishwa na serikali ya mtangulizi wa wake Donald Trump zilizozuia serikali kufadhili kiliniki zinazowatuma wanawake kuavya mimba.

Saa chache baada ya amri ya Biden, waziri wa afya Antony Blinken alitangaza kuwa wizara yake itatoa msaada wa Sh3.25 bilioni kwa shirika la United Nations Population Fund.

Serikali ya Trump ilisitisha ufadhili kwa shirika hilo likidai lililazimisha watu kuhasiwa na kuavya mimba nchini China.

Blinken pia alisema Amerika itaondoa jina lake katika azimio la 2020 Geneva Consensus Declaration ambalo mataifa 30 yalipitisha kupinga uavyaji mimba.

Demokrasia imeshinda, asema Biden baada ya kuapishwa kuwa Rais

CHARLES WASONGA NA MASHIRIKA

NI rasmi sasa kwamba Joe Biden ndiye Rais wa 46 wa Amerika baada ya kula kiapo cha afisi Jumatano, Januari 20, 2021, jijini Washington, Amerika.

“Demokrasia imeshinda,” alisema akihutubu baada ya kulishwa kiapo na Jaji Mkuu John Roberts.

Rais anayeondoka Donald Trump, ambaye hajakubali rasmi kushindwa na Bideni, hakuhudhuria sherehe hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Capitol Hill, Washington. Hata hivyo, makamu wa rais anayeondoka Mike Pence alihudhuria.

Trump ni rais wa kwanza kukosa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais mpya wa Amerika tangu mwaka wa 1896.

Rais huyo mpya ametangaza msururu wa maamuzi rasmi yanayolenga kubatilisha sera kadhaa kuu za Trump.

Makamu wa Rais mteule Kamala Harris ndiye aliyeapishwa kabla ya Biden, na kuwa mwanamke wa kwanza wa mweusi na wa asilia ya Asia-Amerika kuhudumu katika wadhifa huo wa pili kimamlaka kutoka wa urais.

Usalama uliimarishwa katika ndani na nje ya ukumbi ambako hafla hiyo iliendeshwa baada ya jengo hilo Januari 6 kuvamiwa na wafuasi wa Trump walioandamana kupinga uhalali wa ushindi wa Biden.

Zaidi ya maafisa 25, 000 wa usalama walimwagwa katika eneo la sherehe hiyo ambayo haikuhudhuriwa na maelfu ya wananchi kama ilivyo ada. Hii ni kutoka na janga la Covid-19.

Katika hotuba yake Biden alitaja siku hiyo kama ya “historia na matumaini”.

‘Roho yangu yote imejitolea kurejesha Amerika mahala ambapo ilikuwa zamani,” akaongeza.

Huku akitaja haja ya kuwepo kwa umoja baada ya utawala wa Trump uliojaa misukosuko mingi, Biden aliahidi kuwahudumia Waamerika wote- wakiwemo wale ambao hawakumpigia kura katika uchaguzi wa Novemba 3, 2020.

Miongoni mwa marais wa zamani wa Amerika waliohudhuria ni; Barack Obama, ambaye Bideni alihudumu chini yake kama Makamu Rais kwa miaka minane, Bill Clinton na George W Bush.

Wasanii Lady Gaga-ambaye aliimba wimbo wa kitaifa- na Jennifer Lopez na Garth Brooks waliongoa watu wachache waliohudhuria hafla hiyo ya kihistoria..

Majira ya asubuhi Jumatano, Bw Biden, 78, alihudhuria ibada ya shukrani katika Kanisa moja Katoliki Washington.

Ulinzi mkali mmoja akinaswa akiwa na bastola, risasi 500 eneo Biden ataapishwa kuwa Rais

Na AFP

MWANAMUME aliyejihami kwa bastola na risasi zaidi ya 500 alikamatwa jijini Washington katika kituo cha ukaguzi wa kiusalama karibu na eneo ambapo rais mteule Joe Biden ataapishwa Jumatano.

Wesley Allen Beeler, kutoka Virginia, aliwasili katika kituo hicho cha ukaguzi mnamo Ijumaa na kujaribu kutumia stakabadhi bandia kuingia eneo hilo lililofungwa na ambalo liko karibu na jumba la Capitol, Amerika, kulingana na nakala zilizowasilishwa katika Mahakama ya Juu, jijini Washington, DC.

Maafisa walipokuwa wakikagua orodha ya watu walioruhusiwa kuingia, mmoja wao aligundua vibandiko vilivyokuwa nyuma ya gari la Beeler vilivyoandikwa “Dhuru Maisha,” na picha ya bunduki pamoja na ujumbe mwingine uliosema, “Wakijia bunduki zako, wape risasi zako kwanza.”

Alipokuwa akihojiwa, Beeler aliwaeleza maafisa kwamba alikuwa na bastola aina ya Glock katika gari lake.Msako ulianzishwa na kufichua bastola, risasi zaidi ya 500, na vifaa vinginevyo vya bunduki, nakala ya korti ilisema.

Beeler alikamatwa na mashtaka kuwasilishwa dhidi yake ikiwemo: kumiliki bunduki ambayo haijasajiliwa pamoja na kumiliki silaha kinyume na sheria, ilisema ripoti ya polisi.

Kufuatia kukamatwa kwake, Beeler alisema lilikuwa “kosa ambalo halikuwa maksudi” na kwamba yeye ni afisa wa ulinzi kutoka shirika la kibinafsi ambaye alipotea njia akielekea kazini karibu na Capitol.

Washington imemakinika mno kabla ya kuapishwa kwa Biden wiki hii, baada ya umati wa wafuasi wa Rais Donald Trump kuvamia jumba la Capitol mnamo Januari 6.

Watu watano walifariki katika shambulizi hilo akiwemo afisa wa polisi.Maafisa wa usalama wameonya kwamba wafuasi sugu wanaomuunga mkono Trump na ambao kuna uwezekano wamebeba vilipuzi, ni tishio kwa Washington pamoja na miji mikuu eneo hilo wakati huu.Maelfu ya vikosi vya polisi vimetumwa Washington huku mitaa eneo hilo ikifungiwa nje kwa vizuizi vya saruji.

Jengo la Kibiashara la Kitaifa ambalo kwa kawaida huwa limefurika watu kila baada ya miaka minne kwa hafla ya kuapisha rais, limetangazwa kuwa marufuku kuingia kufuatia ombi la kikosi cha ujasusi kinachohakikisha usalama wa rais.

Wakati huo huo, msaidizi mkuu wa Joe Biden alisema Jumamosi kwamba rais mpya atatia sahihi takriban mamia ya amri za rais katika siku yake ya kwanza afisini.Polisi wakihofia machafuko kutoka kwa wafuasi wa Trump walianzisha oparesheni ya kiusalama kote nchini humo kabla ya hafla ya uapishaji.

Watu wachache kualikwa kuhudhuria hafla ya Biden kuapishwa

Na XINHUA

WASHINGTON D.C., Amerika

KAMATI ya Bunge la Congress ambalo linahusika na mchakato wa maandalizi ya sherehe za kumwaapisha Rais Mteule Joe Biden, Alhamisi ilisema ni wageni wachache tu watakaoruhusiwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na kupanda kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Rais mteule Biden ataapishwa Januari 20, 2021 jijini Washington japo ni wageni wachache tu kutoka ndani na nje ya nchi watakaoruhusiwa kuhudhuria hafla hiyo.

Amerika ni kati ya nchi ambazo ziliathiriwa vibaya na virusi vya corona, na wadadisi wa kisiasa wanasema kushindwa kwa utawala wa Rais Donald Trump kukabili ugonjwa huo ndiko kulikochangia pakubwa kushindwa kwake katika uchaguzi ulioandaliwa mwezi uliopita.

Kulingana na Kamati Jumuishi ya Bunge la Congress (JCCIC) ambayo huhusika na sherehe za upokezanaji wa mamlaka, kila seneta atapokezwa mwaliko pamoja na mgeni mmoja kutoka jimbo lake.

Kwa jumla ni mialiko 1,070 ambayo itatolewa kwa maseneta.

“JCCIC baada ya kushauriana na wataalamu wa kimatibabu na afya ya umma pamoja na kamati inayosimamia hafla ya uapisho wa Rais, imeamua kwamba idadi ya wageni watakaohudhuria kuapishwa kwa Rais Mteule Joe Biden, ijumuishe watu wachache.”

“Hii ni kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona si tu Marekani bali hata katika mataifa mengine duniani,” akasema mwenyekiti wa JCCIC, Seneta Roy Blunt kupitia taarifa. Hii itakuwa hafla ya 59 ya kumwaapisha Rais ambayo kwa kawaida huhudhuriwa na halaiki ya raia pamoja na Marais waalikwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Miaka ya nyuma, kamati hiyo ya Congress ingetoa tiketi 200,000 kwa wageni na kuwapa maseneta nyingine za kuwapa wakazi wachache wa majimbo yao ili wahudhurie sherehe hizo.

Mnamo Jumanne, kamati ya Ikulu inayopanga hafla hiyo kwa ushirikiano na JCCIC, iliwataka raia wa Marekani wafuatilie hafla hiyo nyumbani kupitia runinga zao badala ya kufika jijini Washington moja kwa moja.

Kupunguzwa kwa idadi ya wanaohudhuria sherehe za uapisho kunaonyesha kujitolea kwa Biden na Makamu wa Rais mteule Kamala Harris kusaidia taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi duniani kushinda vita dhidi ya virusi vya corona.

Mnamo Jumanne, kikosi cha Biden kilitangaza kuwa Rais huyo ataapishwa Mashariki mwa mji wa Washington DC.

Biden mwenyewe amewarai raia wa Marekani wasalie nyumbani na kufuatilia uapisho wake kwenye runinga.

Biden kutaja baraza lake la mawaziri Jumanne

Na AFP

WASHINGTON D.C., Amerika

RAIS mteule wa Amerika Joe Biden Jumanne, Novemba 24, 2020, atataja majina ya wale watakaohudumu katika baraza lake la mawaziri, msimamizi mkuu wa afisi yake ametangaza.

Hii ni licha ya kwamba Rais Donald Trump angali anakataa kutambua ushinda wa Biden licha ya kwamba baadhi ya wandani wake wameanza kuutambua ushindi wa mgombeaji huyo wa chama cha Democrat.

Rais huyu mteule ameendelea na matayarisho ya kuapishwa kwake mnamo Januari 20, hata baada ya Trump kuonyesha dalili za kukataa kuidhinisha matumizi ya fedha za umma kufadhili shughuli hiyo.

“Mtawajua wale ambao watateuliwa na Biden katika baraza lake la mawaziri kuanzia Jumanne,” afisa huyo kwa jina, Ron Klain, aliambia makala ya “This Week” (Wiki Hii) yaliyopeperushwa na shirika la habari la ABC Jumapili.

Mashirika kadha ya habari nchini Amerika, yakiwemo Bloomberg na gazeti la The New York Times, yaliripoti kwamba Biden atamteua mwanadiplomasia na mshirika wake wa miaka mingi, Antony Blinken, kuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni.

Rais huyo mteule pia alisema wiki jana kwamba amefikia uamuzi kuhusu ni nani atamteua kuwa Waziri wa Fedha.

Vyombo vya habari nchini humo pia vilibashiri kuwa Biden atamteua Linda Thomas-Greenfield, ambaye alihudumu kama Naibu Waziri anayesimamia masuala ya Afrika katika utawala wa Rais wa zamani Barack Obama, kuwa Balozi wake katika Umoja wa Mataifa (UN).

Idadi kubwa wa viongozi wa Republican wametambua ushindi wa Biden au wametoa wito kwa idara ya General Servive Administration (GSA), itoa fedha za kufadhili hafla ya kumpokeza Bidens mamlaka.

Kwa kuwa Trump amedinda kutambua ushindi wa Biden, Rais huyo mteule amezuiwa kupata habari muhimu kuhusu sera za nyumbani na kigeni, haswa kuhusu janga la corona ambalo limeathiri pakubwa taifa hilo.

MAUYA O’MAUYA: Demokrasia ni kama rinda, kila taifa huvaa linaloifaa

Na MAUYA O’MAUYA

Ukiona vyaelea vimeundwa. Ndivyo ilivyo kwa nchi ya Amerika katika masuala ya utawala wa Kidemokrasia tangu ilipojitwalia uhuru mwaka wa 1776.

Naam, inakanganya mawazo ya wengi kuwazia kwamba taifa la nguvu na ukwasi tunaoshuhudia sasa lilikuwa limekandamizwa na minyororo ya ukoloni. Chinua Achebe alinasihi kuhusu hili ‘Utazamapo domo la mfalme, huwezi kuamini naye aliwahi kunyonya matiti ya mamake’. Amerika ilitawaliwa na Uingereza.

Juma lililopita, raia wa dunia waligeuka wataalamu kutoa maoni, kuchanganua na kufuatilia uchaguzi wa Marekani. Hata kina yakhe wa kwetu madongokaporomakani wasiojua tofauti ya Washington na Washington DC walijitwika umahiri wa magwiji wa kuelezea mwelekeo wa mkwaruzano kati ya Donald Trump na Joe Biden.

Mwingine aliniatua mbavu kwa kudai Biden anafaa kwa sababu anaunga mkono BBI. Lahaula! Lililosalia kwetu hasa ni mafunzo muhimu kuhusu utawala wa demokrasia na uendeshaji wa chaguzi za uwazi. Isidhaniwe kwamba Amerika ni paradiso ya demokrasia duniani lakini ilivyo, ni heri nusu shari kuliko shari kamili.

Funzo moja kuu nitaluzungumzia ni usawa na kudumisha hadhi ya kila Jimbo na haki za raia wake. Hii inatokana na mfumo wa kuteua rais kupitia wajumbe 538 wa majimbo licha ya raia mamilioni kupiga kura ya moja kwa moja.

Takriban watu milioni 200 wana haki ya kupiga kura Marekani lakini mgao wa wajumbe 538 kwenye majimbo 50 ya Amerika ndio uamua kiongozi wa nchi.

Mgao huu umeundwa kwa misingi ya idadi ya watu na haja ya kuwakilishwa ili kila Jimbo liwe na sauti katika uchaguzi wa Rais. Demokrasia ni sawa na rinda, vaa linalokufaa.

Mfumo wa Amerika umewafaa kwa kuhakikisha kwamba majimbo yaliyo na idadi kubwa ya watu hayatasakama yale ya wachachache wanapochagua Rais.

Basi, jimbo la California lenye idadi ya watu milioni 40 linatoa wajumbe 55 huku Jimbo la Wyoming la watu nusu milioni likichangia wajumbe watatu kwa mshindi wa kura.

Kwa mtazamo usio makini ungedhani huu ni upuzi lakini ukipiga darubini utagundua mfumo huu ndio umehakikisha uwepo wa muungano wa majimbo 50 na umoja wa kitaifa wa Amerika kwa yakaribia miaka 245 sasa .

Ingekuwa demokrasia ya hesabu ya wingi wa watu pekee, Amerika ingesambaratika kwa sababu ya udikteta wa maslahi ya majimbo makubwa kama vile California, Texas au Florida.

Majimbo madogo yangekandamizwa na tungeshuhudia hata mapigano ya kujitenga au kutangaza uhuru wao. Ili kutwaa urais, kiongozi anahitaji kura za wajumbe 270 au zaidi kutoka majimbo ya nchi. Jinsi Ile kila mpiga kura ni muhimu, kila kura ya mjumbe ni muhimu na zaidi ya yote, kila jimbo ni muhimu.

Ukiwa mgombeaji aliye na kura za wajumbe 267 utahitaji uungwaji mkono na Jimbo kama vile Montana, Vermont, Delaware au Dakota Kaskazini ili kutwaa urais wa Amerika. Majimbo haya yana idadi ndogo ya watu na yanachangia wajumbe watatu kila moja. Haiwezekani kabisa viongozi wa kitaifa kupuuza matakwa ya kitengo cha jamii japo ni wachache.

Nchini Kenya vitengo vyetu vya kigatuzi ni Kaunti zetu 47. Kijamii tuna makundi kadha hasa kwa vigezo vya makabila, jinsia, umri, dini, rangi, wasiojiweza na kadhalika.

Mchango wao usipuuzwe katika uamuzi wa kuchagua utawala. Hata hivyo ni bayana kwamba hatujafaulu kukarabati mfumo wa uchaguzi wa Rais unaohakikisha kila kitengo kinawakishwa. Tumekwama kwenye tope la ukabila.

mauyaomauya@live.com

 

WASONGA: Kenya ifanye kazi na atakayeibuka mshindi Amerika

Na CHARLES WASONGA

WAAMERIKA wanaelekea debeni leo Jumanne kumchagua Rais atakayewaongoza kwa miaka minne ijayo.

Wapigakura wataamua ni nani bora kati ya Rais wa sasa Donald Trump na mpinzani wake mkuu Joe Biden wa chama cha Democrat.

Kenya na Wakenya wamekuwa wakifuatilia uchaguzi huu kwa makini kwa sababu Amerika ni taifa tajiri na lenye nguvu zaidi duniani. Kwa miaka mingi, Amerika imekuwa mshirika wa Kenya katika masuala mbalimbali kama biashara na usalama, hususan, vita dhidi ya ugaidi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika nyanja ya biashara, mnamo 2018, Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh41 bilioni nchini Amerika chini ya mpango wa kustawisha mataifa ya Afrika Kibiashara (AGOA) ulioanzishwa mnamo 2000 chini ya utawala wa aliyekuwa Rais wa Amerika Bill Clinton.

Mapema mwaka huu 2020 Rais Uhuru Kenyatta alianzisha mazungumzo mapya na Rais Trump kuhusu uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Amerika alipomtembelea Ikulu ya White House Februari 2020.

Hiyo ilikuwa ziara ya pili ya Rais Kenyatta nchini Amerika baada ya ile kwanza ya Agosti 2018.

Lakini tangu Trump aingie mamlakani baada ya kushinda uchaguzi mnamo Novemba, 2016, utawala wake haujakuwa na uhusiano mzuri na mataifa ya Afrika na watu weusi kwa ujumla.

Ametumia sera yake ya “Amerika Kwanza” kupunguza uhusiano kati ya utawala wake na Afrika pamoja na kuzuia wakimbizi kutoka bara hili (haswa mataifa ya kiislamu) kuingia Amerika. Aidha amekuwa akitumia lugha chafu kurejelea mataifa fulani ya Afrika.

Licha ya hayo, inatarajiwa kuwa ushindi wa Trump katika uchaguzi wa leo Jumanne utatoa nafasi ya kufanikishwa kwa mkataba wa kibiashara kati ya Amerika na Kenya.

Chini ya mpango huo wawekezaji kutoka Amerika wanatarajiwa kuanzisha biashara nchini Kenya, hatua ambayo imesawiriwa kuwa tishio kwa mpango wa kuanzishwa kwa eneo la biashara huru barani Afrika -Africa Continental Free Trade Area-AFCFTA.

Lakini Kenya isivunjike moyo endapo Biden ataibuka mshindi kwa misingi kwamba haifahamu sera zake kuhusu Afrika, na haswa taifa la Kenya.

Naamini kuwa hakuna Rais wa Amerika anaweza kupuuza Kenya katika mipango na sera zake za kigeni, kwa sababu taifa hili ni nguzo kuu katika mipango ya Amerika ya kupambana na ugaidi katika ukanda huu.

Kando na hayo Kenya ni mdhamini mkuu wa mchakato wa amani nchini Sudan Kusini na eneo zima la Maziwa Makuu ambako Amerika imekuwa ikiendeleza maslahi yake (ya kusaka soko kwa bidhaa zake).

Kwa hivyo, Kenya iwe tayari kufanyakazi na kiongozi yeyote ambaye Waamerika wataamua kuchagua leo kwa manufaa ya raia wa mataifa hayo mawili.

MUTUA: Itakuwa kibarua kudhibiti Trump na Biden mijadalani

Na DOUGLAS MUTUA

NIMETAFAKARI kuhusu mojawapo ya mbinu ambazo zinapendekezwa ili kumdhibiti Rais Donald Trump wa Marekani wakati wa midahalo ya urais nikajipata nikiangua kicheko na kusema ‘kila la heri’!

Tume inayoandaa midahalo ya urais nchini Marekani imependekeza kuzima kipaza sauti cha ama Bw Trump au mpinzani wake, Bw Joe Biden, mara tu mmoja wao anapopewa fursa ya kuzungumza.

Haja ya kuzima kipaza sauti kimoja imeibuka ghafla baada ya mdahalo wa wiki jana kutokea kuwa kituko kitupu kutokana na kelele za Bw Trump.

Kila mshiriki alipewa dakika mbili pekee za kuzungumza kwa zamu na mfawidhi Chris Wallace, lakini Trump alifoka kiholela na kumtatiza Bw Biden, ambaye wakati mmoja alipandwa na wa kwao na kumwambia Rais wa watu: “Fyata mdomo bwana!”

Juhudi za Bw Wallace kuingilia kati kama msimamizi wa mdahalo wenyewe hazikufaa kifu; Trump alikwenda sambamba naye, mwishowe akaishia kuizamisha sauti ya mfawidhi huyo.

Watu wengi waliotazama mdahalo huo walisema haukuafiki kuitwa mdahalo wa urais bali kelele za kitoto kwa sababu haukuwa na ustaarabu wowote.

Baadhi yao walilalamika kuwangwa na vichwa, wengine kuumwa na masikio, sikwambii hata wapo walioshangaa walipoteza usingizi wao kwa dakika 90 wakitizama kitu gani.

Wote waliokasirishwa na yaliyotokea usiku huo walimlaumu Trump, mtu asiye na subira hata ya sekunde mbili, kwa kuigeuza shughuli hiyo muhimu kuwa kioja cha kuudhi. Nilisema ‘kila la heri’ pale tume inayosimamia midahalo ya urais ilipotishia kuzima kipaaza sauti kimoja kwa sababu namjua Trump: haambiliki hasemezeki!

Hata kipaza sauti chake kikizimwa, atafoka kama kichaa sokoni na kumtatiza mwenzake atakayekuwa umbali wa mita mbili pekee.

Bila shaka vipaza sauti vya enzi hii ya dijitali vina wigo mkubwa hivi kwamba hata ukiangusha sindani vinanasa sauti ya mwanguko huo na kuuvumisha mbali.

Ikiwa sauti ya sindano inasikiza, seuze kelele za Trump ambazo kawaida hufanywa makusudi kuwatishia na kuwadhalilisha watu asiokubaliana nao? Hapo pana kibarua kigumu tu.

Trump si mwanasiasa wa kawaida anayehofia kujiharibia sifa; dakika mbili ni nyingi mno kwake, hivyo anaweza kuamua kujongea kipaza sauti cha mwenzake na kutema tusi au kuvuruga mambo ilmuradi tu utawala wake mbaya wa miaka minne iliyopita usikosolewe.

Kumbuka wakati wa mojawapo wa midahalo aliyoshiriki na Bi Hillary Clinton mnamo 2016, Trump alimfuata nyuma Bi Clinton kwa njia ya kutishia pindi Bi Clinton alipokuwa akihutubia watu waliohudhuria hafla hiyo.

Bi Clinton alisema baadaye kwamba aliingiwa na woga sana alipogundua Trump alikuwa nyuma yake kwa sababu chochote kingeweza kutokea.

Trump na jeuri yake ni mtu asiyetabirika kwa hakika. Unachoweza kutabiri kumhusu ni kwamba wakati wote atafanya mambo visivyo.

Jambo linalozuga akili za kila mtu mstaarabu ni kwamba Trump na ukorofi wake huo anavutia mamilioni ya watu! Wafuasi wake, na hata baadhi ya washauri ambao ni wahafidhina kindakindaki, wanampenda alivyo, tena wangetaka aendelee kuvuruga mambo.

Je, akijongea kipaza sauti, au afoke kwa mbali na kutatiza mjadala utakaofanyika wiki mbili zijazo, waandalizi watamfanyia nini? Hamna!

Bila shaka hawawezi kumwitia polisi wamdhibiti kwa maana hiyo itakuwa aibu ya kimataifa. Njia ambayo kwayo Trump anaweza kudhibitiwa vizuri ni kumweka yeye na Biden kwenye vyumba viwili tofauti ila vyenye mafundi wa mitambo wa tume husika ili kila mmoja asipate fursa ya kukaribia kipaza sauti cha mwenzake hata kidogo.

Wote wawili wanaweza kuwekuwa viwambo kama vya runinga mbele yao ili waonane na kuhisi kana kwamba wanazungumziana.

Njia nyingine ila hatari ni ya kuwaweka kwenye chumba kimoja, kipaza sauti cha asiyezungumza kizimwe, Trump akijongea cha mwenzake tu mdahalo umalizwe ghafla kwa maelezo kwamba Rais hadhibitiki. Hapo atapata fedheha na lawama kwa mkumbo mmoja, hali atakayojutia mno kwa kumnyima ushindi kura zikipigwa Novemba 3.

mutua_muema@yahoo.com

Trump taabani huku spika akiidhinisha achunguzwe

Na AFP

SPIKA wa Bunge la Amerika, Nancy Pelosi ameagiza kuanzishwa kwa harakati za kutaka kumng’oa ofisini Rais Donald Trump kutokana na madai ya kutumia mamlaka yake vibaya.

Inadaiwa kwamba, Rais Trump ameunda njama ya kutaka kumaliza wapinzani wake wa kisiasa kwa kushirikiana na serikali ya Ukraine.

Taarifa zasema Rais Trump alimshinikiza Rais wa Ukraine kuanzisha uchunguzi dhidi ya aliyekuwa makamu wa Rais Joe Biden ili kumwezesha kutumia sakata hiyo katika kampeni zake za urais 2020.

Biden ambaye alikuwa naibu wa rais wa Barack Obama, tayari ametangaza kuwania urais kupitia chama cha Democratic na anapigiwa upato wa kumto kijasho Trump katika uchaguzi mkuu ujao.

Spika Pelosi alisema Trump ni sharti awajibishwe.

Kiongozi huyo wa Amerika, hata hivyo, amepuuzilia mbali madai hayo akisema anawindwa na mahasimu wake wa kisiasa.

Wabunge wengi wanaunga kutimuliwa kwa Rais Trump lakini hoja hiyo huenda ikagonga mwamba katika Seneti kwani wengi wa maseneta ni wa chama tawala cha Republican.

Rais Trump ameahidi kuchapisha mambo aliyozungumza na kiongozi wa Ukraine kwa njia ya simu.

Endapo hoja ya kumtimua Trump itapitishwa, basi kiongozi huyo wa chama cha Republican atakuwa rais wa tatu kung’olewa mamlakani katika historia ya Amerika.

Idadi ya wabunge, maseneta

Chama cha upinzani cha Democratic kina idadi kubwa ya wabunge lakini kina maseneta wachache.

Hiyo inamaanisha kuwa huenda ikawa vigumu kwa hoja hiyo kupitishwa katika Seneti.

Pelosi amekuwa akishinikizwa kuidhinisha uchunguzi utakaosababisha Trump kung’olewa mamlakani kufuatia madai ya kutumia mamlaka yake kumshinikiza Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuanzisha uchunguzi dhidi ya Biden.

Inadaiwa kwamba, Rais Trump alimtaka Rais Zelensky kuanzisha uchunguzi dhidi ya Biden kuhusu sakata ya ufisadi ndiposa apatie nchi hiyo msaada wa kijeshi.

Rais Trump amekiri kujadili Joe Biden katika mazungumzo yake na Rais Zelensky mnamo Julai 25 lakini amekanusha madai kuwa alitaka mwanasiasa huyo wa chama cha Democratic achunguzwe.

Marais wawili ambao bunge limewahi kupitisha kura ya kuwang’oa afisini ni Andrew Johnson (1868) na Bill Clinton (1998). Wawili hao, hata hivyo, walinusuriwa na Seneti.

Richard Nixon alijiuzulu mnamo Agosti 1974 kabla ya wabunge kumng’oa kutoka afisini.