Joho atiwa presha atangaze mrithi wake

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho amepuuzilia mbali shinikizo la wanasiasa wanaomtaka atangaze ni nani ambaye angependa awe mrithi wa kiti chake, akiwaambia wanaomezea mate kiti hicho wajitetee wenyewe kwa wananchi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kiti hicho kimevutia wanasiasa watano kufikia sasa wakiwemo Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir (ODM), mwenzake wa Kisauni, Ali Mbogo (Wiper), Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi (ODM), mfanyabishara Suleiman Shahbal (ODM) na aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto.

Akiongea jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Utalii Ulimwenguni katika Hoteli ya Pride Inn eneo la Shanzu, Bw Joho aliwapuuzilia mbali baadhi ya wanasiasa walioanza kujipigia debe wakionekana kutaka baraka zake.“Ndugu zangu ambao mnagombea, ninawatakia kila la heri. Mungu awaongoze,” akasema.

Baadhi ya waliojipigia debe mbele yake ni Dkt Kingi na Bw Nassir, lakini Bw Joho aliwataka waeneze sera zao na kuhakikisha wanadumisha amani katika kampeni.

Alizidi kuwashauri kuwa wahakikishe kampeni zao hazitasababisha mgawanyiko wa kikabila Mombasa kwani wakazi wa makabila tofauti wameishi hapo kwa amani kwa miaka mingi sasa.

Dkt Kingi alimsifu Bw Joho akisema amefanya kazi nzuri kwenye uongozi wake wa mihula miwili akisisitiza kuwa yeye ndiye anayefaa kuendeleza ajenda zake.

“Mimi ndiye ninayefaa kumrithi ili nimalize miradi mikuu ambayo tulianza. Bw Joho aliingia uongozini na kutatua changamoto ya usalama. Hivi sasa tunasherehekea amani kwa sababu ya juhudi zake sawia na kuleta uwiano,” alisema Dkt Kingi.

Kwa upande wake, Bw Nassir alipinga madai kuwa amejiuzulu kwenye kinyang’anyiro hicho na kumwachia Bw Shahbal baada ya kushawishiwa na Bw Odinga na Bw Joho. Hii ni baada ya tetesi kuibuka kuwa Bw Nassir alikubali kuwania useneta badala ya ugavana.

“Huo ni uongo na uzushi. Bado nawania ugavana,” akasema. Wakati huo huo, Bw Joho alitetea uongozi wake kwa kupigania maslahi ya wakazi hasa baada ya wakosoaji wake kumlaumu kuhusu suala la kudorora kwa uchumi wa jiji hilo.

Alimshtumu Dkt Ruto kwa kuwahadaa Wakenya na kumwita kwamba yeye ni ‘mjinga’ alipotoa taarifa kuhusu kuhamishwa kwa bandari ya Mombasa hadi Naivasha.“Sasa wao ndio wanaopiga kelele wakijifanya watakatifu wakiwaelezea vile nyinyi ni maskini.

Alipokuwa kwenye meza ya uongozi hakutamka anayoyasema hivi sasa. Amkeni ndugu zangu msilale, msikubali kuhadaiwa. Mbona hakuleta mabadiliko hapo awali alipokuwa na uwezo?” aliuliza.

Alisifu maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Bw Raila Odingaakieleza namna kaunti ya Mombasa ilivyofaidi kwa mazuri ikiwemo ujenzi wa mabarabara.

Raila tosha 2022, Joho asema

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho ametupilia mbali azma yake ya kuwania urais na kuamua kuunga mkono azma ya kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Joho amesema analenga kuhakikisha kuwa eneo la Pwani linapata uwakilishi kamili katika serikali ijayo.Gavana huyo wa Mombasa jana aliwataka viongozi wa pwani kuunga kwa lengo la kuhakikisha kuwa Chama cha Uniteda Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto hakivurugi umoja wa eneo la pwani kisiasa.

Wakati huu ndoto urais ya Dkt Ruto inaungwa mkono na wabunge wawili pekee waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM. Wao ni mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Kinango Benjamin Tayari.

Viongozi wa Pwani waliokutana na Bw Odinga jana mjini Mombasa walisema wataunga kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Pwani inanufaika katika serikali ijayo.

Gavana Joho, Granton Samboja (Gavana wa Taita Taveta), Dhadho Godana (Gavana wa Tana River) na wabunge Omar Mwinyi (Changamwe), Badi Twalib (Jomvu), Zulekha Hassan (Mbunge Mwakilishi wa Kwale), Asha Hussein (Mbunge Mwakilishi, Mombasa), Ali Wario (Garsen), Teddy Mwambire (Ganze), Ken Chonga (Kilifi Kusini) na mfanyabiashara wa Mombasa Suleiman Shabhal walitangaza kuwa wanaounga mkono azma ya Bw Odinga kuingia Ikulu.

Walifanya hivyo kupitia kile walichokitaja kama Azimio la Pwani.Bw Mung’aru ambaye anataka kuwania kiti cha ugavana wa Kilifi alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo eneo la Pwani.Gavana Joho ambaye anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho alisema kuwa haogopi kustaafu.

Alisema eneo la Pwani litaweza kusuluhisha changamoto zake kama vile za kiuchumi na dhuluma katika umiliki wa ardhi kwa kuwa ndani ya serikali ijayo.

“Wakati huu, pwani haitaki uungwaji bali ushirikiano. Katika kinyang’anyiro cha urais, ikiwa sio Odinga ni Joho. Hatutaki kujiweka katika hali ambapo kila mwaka tunaomba kana kwamba sisi sio Wakenya halisi. Bw Odinga aliunda baraza lake la mawaziri tutakuwa serikalini kisheria wala sio kama waalikwa,” Bw Joho akasema.

Joho na Mucheru waonya wakazi dhidi ya Ruto

Na Winnie Atieno

WAZIRI wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru na Gavana Hassan Joho walimsuta na kumshambulia Naibu wa Rais William Ruto wakisema anaendesha siasa potovu za kuwahadaa vijana kuunga mkono azma yake.

Wawili hao walisema Bw Ruto anawachochea vijana badala ya kutoa muafaka wa changamoto zinazowakabili. Walisema mpango wake wa uchumi kwa wananchi ni ya kuwahadaa Wakenya kumuunga mkono.

“Huu ni wakati wa vijana, jitokezeni ili mpiganie nafasi za siasa. Mkichagua viongozi wachujeni, siasa ni kujipanga ndiyo maana sisi tumejipanga na Rais Uhuru Kenyatta, yule mwingine msimsikize anawahadaa. Hatuwezi kukubali nchi ichezewe,” alisema waziri huyo.

Akiongea eneo la Mombasa kwenye mkutano wa vijana wawili hao walimsuta Bw Ruto kwa kumdhalilisha Rais.Bw Joho naye aliwataka vijana kujitokeza na kupigania uongozi.

Alliwataka vijana kuwa makini na viongozi wabinafsi. “Tumesalia na miezi 11 kabla ya uchaguzi mkuu, chujeni mnachoambiwa. Suala la uchumi ambalo anatangaza kila mahali haiwezifanikishwa humu nchini. Jihusishe na viongozi bora ambao wanawatakia mema sio wale wanaopenda kukosoa bila kutoa jawabu,” alisema. Alimshutumu Bw Ruto kwa ‘kulumbana’ na Rais.

“Kwanini unapigana na Rais ambaye anaenda kustaafu? Unachochea wakenya, tunataka amani katika nchi ambayo watu wanaishi na uwiano. Inauma sana kuona kiongozi akichochea hisia na kuleta chuki na uhasama,” alisema.

Vijana walionywa dhidi ya kupokea hongo ili kuuza kura zao.Aliyekuwa afisa mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Bw Ezra Chiloba aliwataka vijana kugombea viti vya kisiasa.

“Nchi hii iko mikononi mwa vijana, ni wjaibu wenu kujitokeza na kugombea viti vya kisiasa,” alisema Bw Chiloba.

Joho, Ruto waua ndoto ya chama cha Wapwani

Na CHARLES LWANGA

MATUMAINI ya kuundwa kwa chama cha Pwani yanaendelea kudidimia kwa mara nyingine, baada ya wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto na Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuanza kujiondoa kwenye mchakato wa kukumbatia wazo hilo.

Viongozi hao sasa wameanza kutelekeza wazo hilo hasa baada ya Bw Joho ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM, kuwasilisha karatasi zake kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.

Kwa upande mwingine, wabunge wandani wa Dkt Ruto nao wameasi wazo hilo baada ya Naibu Rais kukumbatia chama kipya cha UDA kutokana na misukosuko inayoendelea ndani ya Jubilee.

Wakati Dkt Ruto alipotembelea Pwani mnamo Februari mwaka huu, aliwataka viongozi wa Tangatanga katika kaunti za Kilifi, Mombasa na Kwale wajiondoe katika kuunda chama cha Pwani na badala yake wajiunge naye katika kunadi vuguvugu la Hasla.

Nalo jaribio la wabunge wa Tangatanga Aisha Jumwa (Malindi) na mwenzake wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kufufua chama cha Kadu Asili ambacho kina mizizi yake Pwani liligonga mwamba baada ya kinara wake Gerald Thoya kukataa kuwapokea chamani.

Wabunge wengine wa Tangatanga kutoka Pwani ni Mohammed Ali (Nyali) Khatib Mwashetani (Lungalunga), Sharif Ali (Lamu Mashariki), Jones Mlolwe (Voi), Paul Katana (Kaloleni), Ali Wario (Bura), Benjamin Tayari (Kinango) na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar.

Mnamo Jumamosi iliyopita wakati wa mazishi ya Mzee wa Kaya Kahindi Ngowa, Gavana wa Kilifi Amason Kingi ambaye amekuwa akipigania juhudi za kuundwa kwa chama cha Pwani, aliwalaumu wabunge kwa kumtoroka na kukumbatia vyama vingine kuelekea uchaguzi wa 2022.

“Kuna uwezekano kwamba eneo hili bado litashikwa mateka na vyama kutoka nje kwenye uchaguzi wa 2022. Lazima tufikirie mustakabali wetu,” akasema Bw KingiBaadhi ya wabunge kutoka ODM ambao wamejitenga na wazo la kubuniwa kwa chama hicho ni Teddy Mwambire wa Ganze, Ken Chonga (Kilifi Kusini) Seneta wa Kilifi Steward Madzayo na mbunge Mwakilishi wa Kilifi Getrude Mbeya.

Hata hivyo, Bw Mwambire ambaye ni Katibu Mkuu wa kundi la wabunge wa Pwani, alimpuuzilia mbali Bw Kingi akisema kuwa bado hajajibu maswali waliyoibua kuhusu kuundwa kwa chama hicho.Mbunge huyo alikariri kwamba hawawezi kufuata Bw Kingi kisha mwisho wapoteze umaarufu na wapinzani wao waunge na vyama vinavyodhaniwa kuwa ni vya nje kisha kuwabwaga uchaguzini.

“Ni kweli kwamba tumeandaa mikutano mingi na Gavana Kingi kuhusu hili suala la umoja wa Pwani na kuna masuala ya ndani tuliyoyaibua ambayo majibu yake hatujayapata hadi leo,” akasema Bw Mwambire.

Gavana Kingi naye ameshikilia kwamba ataunganisha vyama vidogo vya Pwani akilenga kuwania urais 2022.

Kaunti yapewa siku 7 kujibu kesi ya wafanyabiashara

Na PHILIP MUYANGA

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imepewa siku saba kujibu kesi iliyowasilishwa kortini na chama cha wenye mabaa, hoteli na nyumba za wageni, kinachopinga Sheria ya Fedha ya Kaunti ya Mombasa 2021.

Jaji Eric Ogola wa mahakama kuu mjini Mombasa pia aliagiza chama hicho kuweka hati ya kiapo ya ziada iwapo wanahitaji wakati watakapopewa majibu na serikali ya kaunti.

Takriban wiki tatu zilizopita, mahakama kuu ilizuia kwa muda serikali ya kaunti kulipisha kodi au fedha za adhabu za mwaka jana kama kigezo cha kuruhusu wafanyibiashara kulipia pesa za leseni za mwaka huu.

Wafanyibiashara hao katika stakabadhi za kesi wanasema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa inawalazimisha kulipa pesa za kodi na adhabu zingine za mwaka jana kabla ya kupewa leseni za kufanyia kazi za mwaka wa 2021.

Chama hicho kinasema kuwa serikali ya Kaunti imepuuza suala la kuwa serikali ya kitaifa ilikuwa imeagiza kufungwa kwa biashara mwaka jana kwa sababu ya ugonjwa wa Covid 19 na kwamba kuna biashara ambazo bado hazijafunguliwa hadi sasa.

Wafanyibiashara hao ambao wamewasilisha kesi pamoja na shirika la Coast Legal Aid and Resource Foundation (Clarf), wameshtaki serikali ya kaunti ya Mombasa, katibu wa bunge la kaunti ya Mombasa na wizara ya fedha ya kaunti.Kulingana na walalamishi, umma haukuhamasishwa kuhusu sheria hiyo ya fedha ilipoundwa.

“Washtakiwa waliwanyima wakazi wa Mombasa fursa ya kuhusika katika mchakato wa kutunga sheria hiyo ya fedha,” walisema.

Wanataka mahakama kuamua kuwa hatua za washtakiwa zilikiuka haki zao na katiba kwa kuwa hakukuwa na uhamasishaji wa umma wakati wa mchakato wa kutunga sheria hiyo.

Chama hicho na shirika la Clarf wanataka mahakama kuamua ya kuwa kitendo cha serikali ya kaunti cha kuwafanya walipe kodi na pesa zingine za mwaka jana kabla ya kupokea malipo na kutoa leseni ni kinyume cha sheria.

Pia wanailaumu serikali ya kaunti kwa kuongeza malipo na kodi inayowaathiri wao pamoja na wananchi bila kufuata sheria.Wanaongeza kusema kuwa sheria hiyo ya fedha iliongeza kodi ya vitanda katika hoteli ambayo italipwa kwa serikali ya kaunti licha ya kuwa malipo ya asilimia mbili katika Hazina ya Utalii huwa tayari imeshughulikia ada hiyo. Kesi itasikizwa Mei 27 mwaka huu.

JAMVI: Mkanganyiko mkuu unaogubika siasa za urithi Pwani

Na MOHAMED AHMED

KWA muda sasa magavana watatu kutoka Pwani akiwemo wa Mombasa Hassan Joho, Salim Mvurya wa Kwale na mwenzao wa Kilifi Amason Kingi wameonekana kuweka mipango yao ya kisiasa ambayo itakuja baada ya kumaliza hatamu zao.

Magavana hao wapo kwenye hatamu zao za mwisho kwenye viti hivyo ambavyo itakuwa wamevishikilia kwa muda wa miaka kumi wakati awamu zao zitakapokamilika mwaka 2022.

Wakati viongozi hao wanapopanga kuondoka kwenye nafasi hizo, tayari kuna wale ambao wanamezea mate viti hivyo na kutaka kuwarithi. Baadhi ya wanaomezea mate ni wale ambao magavana hao pia wangependelea wachukue nafasi hizo wakati watakapokuwa wameondoka.

Miongoni mwa viongozi ambao kufikia sasa wameonyesha azma ya kurithi viti hivyo ni pamoja na naibu gavana wa Kwale Fatuma Achani ambaye pia anaungwa mkono na Bw Mvurya

Mpinzani

Kufikia sasa mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani ameonekana kuwa mpinzani wa karibu wa Bi Achani.

Licha ya Bw Mvurya kuwa chama kimoja cha Jubilee na Bw Mwashetani gavana huyo amesisitiza kwamba Bi Achani ndiye anastahili zaidi kumrithi ifikapo 2022

Katika mkutano wa hivi majuzi kwenye mazishi ya Askofu Morris Mwarandu Bw Mvurya alisema ni Bi Achani pekee atakayeweza kuendeleza mafanikio ambayo kaunti hiyo imeshuhudia tangu 2013

“Ni vile hapa ni mazishini sitaongea zaidi. Lakini Askofu aliniambia ‘muda wako unaisha ututayarishie ya mbele’. Naibu gavana ametayarishwa. Mnaona Tanzania hakujakuwa na msukosuko? Katika taasisi ni lazima watu watayarishwe,” akasema.?

Wengine wanaoaminika kumezea mate kiti hicho ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Mtuga Chirau Mwakwere, na katibu wa Wizara ya Kilimo Hamadi Boga.? Mara kwa mara Bi Achani na Bw Mwashetani wamekuwa wakitoleana cheche za maneno ambazo zinaelekezwa na mipango yao ya kurithi Bw Mvurya

Cheche hizo za maneno ya kisiasa pia zimekuwa zikushuhudiwa katika kaunti ya Mombasa ambapo baadhi ya viongozi wanalenga kumrithi Gavana Joho.

Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo na mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambao kufikia sasa ndio viongozi ambao wamejitosa ulingoni wazi wazi wakitaka kumrithi Bw Joho.? Hata hivyo, ukali wa siasa hizo za urithi zimeonekana kuelemea upande wa Bw Nassir na Bw Shahbal ambao ndio mahasimu wa karibu.

Huku Bw Nassir akionekana kusubiri kuidhinishwa na Bw Joho katika azma yake, Bw Shahbal ambaye pia sasa ana uhusiano wa karibu na Bw Joho amekuwa akiendeleza kampeni za mapema kupitia vikao vinavyotambulika kama “Gumzo Maskani”.

Kati ya mwezi wa Februari hadi mwezi jana, kiongozi huyo amefanya mikutano kadhaa katika maeneo bunge ya Mombasa ikiwemo Likoni, Changamwe, Mvita Kisauni na Jomvu kueleza sera zake.

Bw Nassir naye kwa upande amekuwa akitumia nafasi yake kama kiongozi kukutana na wakazi hususan wa eneo bunge lake la Mvita na kueneza azma yake ya kutaka kuwania ugavana.

Hata hivyo, Bw Nassir hajakuwa akionekana zaidi kwenye maeneo bunge mengine kufanya kampeni zake kama vile Bw Mbogo ambaye pia ameshikilia kampeni zake mashinani katika eneo bunge lake la Kisauni.

Uchanganuzi wa Jamvi umeonyesha katika miezi hiyo miwili iliyopita, Bw Nassir amezuru makanisa katika eneo la Changamwe mara tatu huku Bw Shahbal akitekeleza mikutano takriban 20 katika muda huo huo.

Kampeni hizo za mapema pia zimeibua tumbo joto katika chama cha ODM baada ya Bw Shahbal kutangaza kuwa anarudi kwenye chama hicho.

“Walinifungia mlango wakati ule wa nyumba lakini sasa si handisheki imekuja. Si tumerudi nyumbani?” Bw Shahbal alisema katika mmoja ya mikutano yake.? Tangazo hilo la Bw Shahbal lilipelekea Bw Nassir naye kumpiga vijembe mpinzani wake huyo na katika mkutano wa eneo la Jomvu akaonya wakazi dhidi ya kuchagua watu ambao ‘wanazuka saa hizi.’

“Mimi nataka kuwauliza wao walikuwa wapi wakati sisi tulikuwa tunapambana? Mimi nawaambia muwe makini na watu hao,” akasema Bw Nassir.? Licha ya wawili hao kujitokeza kumenyana kwenye kiti hicho, bado haijakuwa wazi iwapo Bw Joho atamuunga mkono yeyote kati yao.

Iwapo Bw Joho atajitokeza wazi kutaka kumuunga mkono kiongozi wa kumrithi basi naibu wake Dkt William Kingi atakuwa miongoni mwa wale wanaotarajia kuungwa mkono.

Dkt Kingi pia amewahi kutangaza kuwa atawania kiti cha ugavana, hata hivyo hakuna mikutano yoyote ya wazi ambayo ameanza kutekeleza.? Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia anatarajiwa kuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo, bado pia yeye hajaanza kujitosa kwenye kampeni za mapema.

Kwa sasa, mwezi mtukufu wa Ramadhan utasitisha kampeni hizo kama ilivyo ada ya wanasiasa wa Mombasa huku kindumbwendumbwe kikitarajiwa baada ya mwezi huu ambao umeanza jana kukamilika.

Kwengineko katika kaunti ya Kilifi mihemko ya kisiasa ya kurithi Gavana Amason Kingi yamevutia aliyekuwa mbunge Gideon Mung’aro na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa

Bado siasa hazijapamba moto eneo hilo lakini Bi Jumwa alikuwa ameonekana kuendesha siasa za chini kwa chini.

Bw Mung’aro naye ameonekana kuwa karibu na Bw Kingi ambaye kwa muda amekuwa akiendesha siasa za chama cha Pwani. Naibu gavana Gideon Saburi pia ametajika katika siasa hizo za urithi.

Ramadhan kupiga breki siasa moto za kumrithi Joho

Na MOHAMED AHMED

MFUMO wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unatarajiwa kutuliza kasi ya siasa za urithi wa kiti cha ugavana cha Mombasa ambazo zimepamba moto.

Kindumbwendumbwe hicho kinatarajiwa kuibuka upya baada ya Ramadhan ambayo itadumu mwezi mmoja.

Siasa hizo za urithi wa Gavana Hassan Joho zimekuwa zikiendelea chini kwa chini licha ya shughuli za kisiasa kuonekana kupungua katika kaunti hiyo.

Kufikia sasa, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo na mfanyabiashara Suleiman Shahbal ndio viongozi ambao wamejitosa ulingoni wazi wazi wakitaka kumrithi Gavana Hassan Joho.

Hata hivyo, ushindani mkali unatarajiwa kati ya Bw Nassir na Bw Shahbal ambao ndio mahasimu wakuu.

Huku Bw Nassir akionekana kuidhinishwa na Bw Joho katika azma yake, Bw Shahbal ambaye pia sasa ana uhusiano wa karibu na Bw Joho amekuwa akiendeleza kampeni za mapema kupitia vikao vinavyotambulika kama “Gumzo Maskani”.

Kati ya Februari na mwezi jana, kiongozi huyo aliandaa mikutano kadhaa katika maeneo bunge ya Mombasa ikiwemo Likoni, Changamwe, Mvita Kisauni na Jomvu kunadi sera zake.

Bw Nassir naye kwa upande wake amekuwa akitumia nafasi yake kama kiongozi kukutana na wakazi hususan wa eneo bunge lake la Mvita na kuvumisha azma yake ya kutaka kuwania ugavana.

Hata hivyo, Bw Nassir hajakuwa akitembelea maeneo bunge mengine kufanya kampeni zake sawa na Bw Mbogo ambaye pia ameshikilia kampeni zake mashinani katika eneo bunge lake la Kisauni.

Uchunguzi wa Taifa Leo umeonyesha, katika miezi hiyo miwili iliopita, Bw Nassir amezuru makanisa katika eneo la Changamwe mara tatu huku Bw Shahbal akiandaa mikutano takribani 20 katika muda huo huo.

Kampeni hizo za mapema pia zimeibua tumbojoto katika chama cha ODM baada ya Bw Shahbal kutangaza kuwa anarudi katika chama hicho.

“Walinifungia mlango wakati ule lakini sasa si handisheki imekuja. Si tumerudi nyumbani?” Bw Shahbal alisema katika mmoja wa mikutano yake.

Tangazo hilo la Bw Shahbal lilipelekea Bw Nassir naye kumpiga vijembe mpinzani wake huyo na katika mkutano wa eneo la Jomvu akaonya wakazi dhidi ya kuchagua watu ambao wanajitokeza wakati huu.

“Nawauliza, wao walikuwa wapi wakati sisi tulikuwa tunapambana? Mimi nawaambia muwe makini na watu hao,” akasema Bw Nassir.

Licha ya wawili hao kujitokeza katika kumenyania kiti hicho, bado haijakuwa wazi iwapo Bw Joho atamuunga mkono yeyote kati yao.

Iwapo Bw Joho atajitokeza wazi kumuunga mkono kiongozi wa kumrithi, basi naibu wake Dkt William Kingi atakuwa miongoni mwa wale wanaotarajia kuungwa mkono.

Dkt Kingi pia amewahi kutangaza kuwa atawania kiti cha ugavana, hata hivyo hakuna mikutano yoyote ya wazi ya kampeni ambayo ameanza kuandaa.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia anatarajiwa kushiriki kwenye kinyanganyiro hicho. Hata hivyo, bado pia yeye hajaanza kujitosa kwenye kampeni za mapema.

Maseneta wakosoa Joho kuhusu matumizi ya feri

Na WINNIE ATIENO

MASENETA wawili kutoka kaunti za Pwani wameishtumu serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kushurutisha zaidi ya watu 300,000 kutumia daraja la Liwatoni wakionya kuwa ni hatari kwa msambao wa virusi vya Corona.

Wiki iliyopita, kamati ya dharura ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19 Kaunti ya Mombasa iliagiza abiria kutumia daraja hilo badala ya feri ambayo ilitajwa miongoni mwa sehemu hatari za maambukizi ya corona kufuatia msongamano mkubwa wa watu.

Hata hivyo, maseneta Mohamed Faki wa Mombasa na mwenzake wa Kwale Issa Boy walionya kuwa, msongamano mkubwa unaoendelea kushuhudiwa katika daraja hilo sasa ni hatari kwa maambukizi ya corona.

Walionya kuwa juhudi za kaunti ya Mombasa, ikiongozwa na Gavana Hassan Joho kupambana na janga hilo hazitafua dafu huku wakitaka agizo hilo libatilishwe.

‘Serikali ya Kaunti ya Mombasa ilikosea kwa kuagiza wakazi kutumia daraja hilo. Isitoshe, hatua hiyo ni kinyume cha sheria kwani wakazi hawakuhusishwa kama inavyotakikana kwa mujibu wa katiba yetu,’ alisisitiza Bw Faki.

Bw Faki ambaye ni wakili aliitaka serikali ya kaunti kuwaruhusu wakazi kutumia feri na daraja kuvuka akisisitiza kuwa watu wanaoishi na ulemavu, wazee na wagonjwa wanataabika.

Kwa upande wake, Bw Boy alisema Kaunti ya Kwale ni mwekezaji mkubwa wa Mombasa na malalamishi yao yanafaa yasikizwe.’Tumepokea malalamishi mengi sana hasa kutoka kwa wafanyibiashara, tunaisihi serikali ibatilishe uamuzi huo,’ akasisitiza.

Wakati huo huo, Idara ya Afya kaunti ya Mombasa imepiga marufuku wakazi kwenda kuvinjari katika ufuo wa umma wa Jomo Kenyatta ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona huku hoteli za Pwani, fuo na viwanja vya ndege vikisalia mahame.

Waziri wa Afya wa kaunti hiyo Bi Hazel Koitaba alisema fuo hiyo kubwa zaidi katika mji huo wa kitalii itafungwa kwa umma kwa muda.Serikali hiyo ya kaunti ilisema fuo hiyo itafunguliwa pindi maambukizi yatakapopungua katika kaunti hiyo.

Haya yanajiri huku wawekezaji wa sekta ya utalii wakilalamika namna biashara imezorota baada ya Rais Uhuru Kenyatta kufunga kaunti tano ambazo zinaongoza kwa maambukizi.

Kufungwa kwa kaunti hizo kulisababisha watalii wa humu nchini kusitisha safari zao za kuzuru Pwani ya Kenya wakati wa Likizo ya pasaka.Mtaalam wa utalii, Bw Mohammed Hersi alisema hoteli nyingi na fuo zilisalia mahame baada ya wakazi wa bara kusitisha safari zao.

Joho alipa Sh1m kuwania tiketi ya urais ya ODM kabla ya Raila

Na JUSTUS OCHIENG

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ndiye mwanasiasa pekee ambaye kufikia sasa amewasilisha ombi la kusaka tiketi ya ODM ili kuwania Urais 2022 huku zikiwa zimesalia siku 10 pekee makataa yaliyowekwa yakamilike.

Kinara wa ODM Raila Odinga na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambao pia wameonyesha azma ya kuingia ikulu kupitia chama hicho mhapo 2022, bado hawajawasilisha maombi yao huku makataa ya Februari 26 yakinukia.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna jana alifichua kwamba ODM imepokea ombi la Bw Joho lakini akasema hafahamu chochote iwapo Mabw Odinga na Oparanya watawasilisha maombi yao kabla ya muda uliowekwa.

“Tumepokea ombi la Gavana Joho na tunatarajia maombi ya wawaniaji wengine yataendelea kumiminika kabla ya makataa kutimia. Hatujasikia kutoka kwa wawaniaji wengine ila tuna matarajio watatii wito huo siku chache zinazokuja,” akasema Bw Sifuna.

Bw Odinga amekuwa kimya kuhusu iwapo atakuwa debeni 2022 au la na sasa amebaki na siku 10 ili ifahamike iwapo atatafuta kurithi kiti cha urais baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu mwakani.

Gavana Oparanya katika mahojiano na Taifa Leo hapo awali alithibitisha kuwa yuko kiny’ang’anyironi kusaka tiketi ya ODM ili awanie urais kwa mara ya kwanza.

Mabw Oparanya na Joho wanahudumu vipindi vyao vya pili kama magavana na katiba haiwaruhusu watetee viti hivyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi wa ODM, Bi Catherine Mumma alikataa kuzungumzia kuhusu iwapo Bw Odinga atawasilisha jina lake, akisema suala hilo litakuwa wazi baada ya Februari 26.

“Wale ambao wana azma ya kuwania urais lazima wawasilishe majina yao kufikia Februari 26. Unaweza kutuma maombi baada ya makataa hayo iwapo muda huo utarefushwa. Baada ya kupokea majina, tutaanza mchakato wa ukaguzi,” akasema Bi Mumma.

ODM inatarajiwa kuandaa uchaguzi wa wanachama mashinani kuanzia mwezi ujao kisha wajumbe watakaoshinda watapewa nafasi ya kumchagua mpeperushaji bendera wa chama hicho.

iwapo maombi ya Urais yatatumwa na zaidi ya mwaniaji mmoja.

Katibu wa ODM Timothy Bosire alieleza Taifa Leo kuwa chama hicho hakitamfungia nje Bw Odinga au wawaniaji wengine wenye nia ya kukitumia kuwania urais 2022.

Naye wabunge Mark Nyamita (Uriri) na Elisha Odhiambo (Gem) walisema Odinga ndiye mwaniaji pekee wa urais wanayemtambua kutokana na umaarufu wake wa kisiasa kote nchini.

“Urais wa Raila haupo kwenye msingi wa iwapo atatuma maombi au la. Lazima atakuwa debeni la sivyo tutaigura ODM na kuachana na siasa kabisa. Ni yeye pekee atakayevunia chama chetu ushindi na mwenye uwezo wa kuunganisha taifa hili,” akasema Bw Nyamita.

Joho, Kingi mbioni kufufua jumuiya ya Pwani

Na LUCY MKANYIKA

MKUTANO wa faragha wa magavana wanne wa Pwani mnamo Jumatano unaonekana kuwa mojawapo ya mbinu za kuwapa uhai wa kisiasa magavana Hassan Ali Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi).

Wawili hao ambao sheria inawazuia kuwania ugavana kwa kipindi cha tatu, waliongoza juhudi za kufufua Jumuiya ya Kaunti za Pwani, iliyofifia baada ya kuanzishwa mnamo 2015.

Kwenye mkutano huo eneo la Mwakishimba, Taita Taveta, wawili hao waliungana na mwenyeji wao Granton Samboja na Gavana Dhadho Godhana (Tana River), kujadili mikakati ya kuendeleza muungano huo ili kuleta maendeleo katika eneo hilo.

Huku vigogo wa kisiasa wa kitaifa waking’ang’ania kura za eneo la Pwani, viongozi hao waliapa kutokubali kutumiwa kisiasa katika uchaguzi ujao.

Alhamisi, Bw Joho alitangaza azma ya kuwania urais kupitia chama cha ODM. Akihutubia wanahabari, gavana Samboja alisema kuwa walikubaliana kuwa eneo hilo halitaendelea kudhalilishwa kisiasa kama awali.

“Tumekubaliana kuwa tutakuwa katika meza ambayo maswala ya nchi yanajadiliwa,” alisema.

“Tutafanya kazi pamoja na tutaongoza ili kuafikia malengo yetu,” akasema Bw Samboja. Jumuiya ya Kaunti za Pwani iliyoanzishwa 2015 ilinuia kuleta pamoja kaunti zote za Pwani ili kuwezesha eneo hilo kufanya maendeleo, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wenyeji.

Hata hivyo, muungano huo ulififia kutokana na tofauti za kisiasa za viongozi wa eneo hilo.

Mkurugenzi wa Jumuiya hiyo ni Bw Emmanuel Nzai.

Gavana Samboja alichaguliwa kama mwenyekiti wa muungano huo ili kufufua mikakati iliyokuwa imekwama kutokana na changamoto za hapo awali.

Wanaonipuuza urais 2022 watashangaa – Joho

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho ametetea azma yake ya kuwania urais akisema hana mzaha kuhusu suala hilo.

Bw Joho alisema Jumatano kuwa ingawa safari yake ya siasa ilianza kama mzaha, alitimiza malengo yake na kushangaza waliokuwa wakimpuuza.

“Nilipotangaza ninataka kuwa gavana, marafiki wangu walinicheka lakini nitashinda. Wanaopinga azma yangu ya urais wajue sina mzaha,” akasema.

Bw Joho alisema atapigania kuteuliwa na chama cha ODM kuwa mwaniaji wake wa urais mwaka ujao.

Bw Joho alikuwa akizungumza ofisini mwake jijini Mombasa alipompokea Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Nairobi, Bi Esther Passaris.

Aliwataka Wakenya kukumbuka ghasia za uchaguzi wa 2007 na kukoma kugawanywa, na badala yake waendelee kuishi kwa amani.

Kwa upande wake, Bi Passaris alimtaka Bw Joho kutangaza ramsi azma yake ya kuwania urais akiwa Nairobi.

 

Joho na Kingi waongoza mipango ya kuhama ODM

Na MOHAMED AHMED

MIPANGO ya viongozi wa kanda ya Pwani kujisimamia kisiasa inazidi kupamba moto huku ripoti zikionyesha kuwa kumekuwa na majadiliano ya viongozi hao kujiondoa katika chama cha ODM.

Magavana Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi, Amason Kingi mnamo Jumatatu walikuatana na wabunge tarkriban 25 katika kikao cha faragha kilichofanyika kwa zaidi ya saa tano.

Mkutano huo ulifanyika katika mkahawa mmoja eneo la Nyali, ambapo majadiliano yalihusisha umoja wa Pwani na iwapo umoja huo unapaswa ufanyike wakati viongozi hao wapo ndani ya ODM ama wakiwa na chama chao kutoka Pwani.

Akizungumza na “Taifa Leo” jana, Bw Kingi ambaye ndiye alikuwa ameongoza kuandaa mkutano huo, alisema majadiliano hayo yalilenga umoja wa Pwani ambao hautaegemea upande wa kinara wa ODM Raila Odinga ama Naibu Rais William Ruto.

“Ajenda yetu kuu ilikuwa umoja wetu. Tumekutana na wabunge ili kuweka mikakati na kwa sababu hiyo hatutakuwa na muungano ambo utaegemea upande wa Bw Odinga ama upande wa Bw Ruto. Hii itakuwa ajenda ya Pwani,” akasema Bw Kingi katika mahojiano baada ya mkutano huo.

Viongozi wengi waliohudhuria mkutano huo ni wa kutoka ODM. Wabunge ambao wanamuunga mkono Dkt Ruto hawakuwepo kwenye mkutano huo.

Bw Kingi alisema kanda ya Pwani imeamua kuchukua mkondo wake wa kisiasa kwa sababu kwa muda mrefu eneo hilo limekuwa likiachwa nyuma kwa sababu ya kuwacha wengine kuwasimamia.

Alisema ili kuipa nguvu ajenda hiyo ya umoja wa Pwani, magavana wote sita wa kanda hiyo watakutana Februari 9 katika kaunti ya Taita Taveta kujadiliana kuhusu mpango huo.

“Tumekuwa tukiwakilishwa na ODM kama eneo lakini sasa tunataka kujiwakilisha wenyewe na kujisimami. Kwa muda mfupi ujao utaona matunda ya mikutano hii ambayo tumepanga,” akaongeza Bw Kingi.

Bw Joho juzi pia alisema kuwa ni wakati wa viongozi wengine wa chama cha ODM akiwemo Bw Odinga kumuunga mkono yeye katika azma yake ya kuwania Urais mwaka wa 2022.

Joho ashauriwa kuhusu urais 2022

Na WINNIE ATIEO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho ametakiwa kuwapatanisha viongozi wote wa Pwani kabla hajatangaza azma yake ya kuwania urais mwaka ujao.

Mbunge wa Kisauni, Ali Mbogo alimsihi Bw Joho kuhakikisha umoja wa Pwani umepatikana kwanza ili aweze kupata uungwaji mkono.

“Kama kinara wa ODM Raila Odinga atakubali kumwachia nafasi Bw Joho na kuunga mkono azma yake, itakuwa jambo bora sana kwa wapwani. Lakini ni sharti Bw Joho na magavana wenza Salim Mvurya (Kwale) na Amason Kingi (Kilifi) wakae chini na kutafuta atakayepeperusha bendera ya urais eneo la Pwani. Lazima wazungumze lugha moja,” akasema Bw Mbogo.

Pia alimtaka Bw Joho afanye kikao na wanasiasa wote wa Mombasa, hasa wabunge, ili waweze kumsaidia katika safari yake ya uongozi.

“Lazima wakubaliane ni nani atawania urais ili Wapwani wote wampigie debe. Bw Joho huwezi kutembea peke yako kama wataka urais. Shirikiana na wabunge Mohammed Ali (Nyali), Mishi Mboko (Likoni), Omar Mwinyi (Changamwe), Badi Twalib (Jomvu) na Abdulswamad Nassir (Mvita) na MCA wa Mombasa,” akasema.

Wiki iliyopita, Gavana Kingi alisema hivi karibuni atatangaza mkondo ambao Pwani itafuata kisiasa.

Bw Kingi amekuwa akipigania kuanzishwa kwa chama cha Pwani, ambacho alisisitiza kiko katika mkondo wa mwisho.

Mbunge amtaka Joho ajiuzulu ODM

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE muasi wa Chama cha ODM, Bw Owen Baya amemtaka Gavana wa Mombasa, Hassan Joho ajiuzulu kama Naibu Kinara wa ODM ili wasukume azma ya kuunganisha eneo la Pwani pamoja.

Kauli yake inajiri baada ya Bw Joho na mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi wiki jana kutangaza katika hafla tofauti maeneo ya Garsen na Kaloleni, wakisema kuwa wakati umefika ambapo eneo la pwani linafaa kujisimamia kisiasa na hata kumsimamisha mgombeaji wa urais.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Bw Baya pia alimtaka Gavana Kingi ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha ODM kaunti ya Kilifi pamoja na wabunge wote waliomuidhinisha Bw Joho kama kinara na msemaji wa pwani atakayepeperusha bendera ya urais 2022 kujiuzulu katika viti na majukumu yao katika chama

.’Wanafaa wajiuzulu katika majukumu yao ya chama ndio tuhakikishe kuwa hawatani na wanamaanisha wanachokisema au sivyo tutajuwa ni njama ya kuvuruga mpango wa kuunda chama cha kipwani na baadaye kurudisha wapwani kwa ODM,’ alisema.

Akijieleza ni kwa nini wanafaa kujiuzulu katika nafasi zao za chama, Mbunge huyo wa Kilifi Kaskazini alisema yeye mwenyewe aliondolewa katika ODM kama Naibu katibu mpangakazi kwa ajili ya maoni yake ya kuunda chama cha kipwani.

Wakati huo huo, Bw Baya ambaye ni mmoja wa wabunge katika mrengo wa Tangatanga inayoongozwa na Naibu Rais William Ruto, alisema wanatambua mbinu za uongozi wa kinara wa ODM Raila Odinga za kutenganisha ili kutawala ambazo huenda wanapanga kutumia kurudisha eneo hilo kwa chama cha ODM katika uchaguzi mkuu ujao.

‘Lakini wakati huu hutatukoga kwa kitumia matambiko wala pesa. Tuko tayari na imara kukomboa eneo la pwani bila wewe,’ alisema.

Viongozi wengine wa mrengo wa Tangatanga ni Mbunge wa Nyali Mohamed Ali, Khatib Mwashetani (Lungalunga), Sharif Ali (Lamu East), Jones Mlolwe (Voi), Ali Wario (Bura), Benjamin Tayari (Kinango), aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar na Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa juwa ambaye ameweka macho yake kwa chama cha Kadu-Asili atakachokitumia kugombea ugavana wa Kilifi mwaka wa 2022.

Jumamosi iliyopita katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga, Gavana Kingi ambaye ni mwandani wa Bw Joho alisema eneo hilo lina kura takribani 3 milioni na wakati umefika eneo la pwani linafaa kujisimamia kisiasa na kuwacha kutegemea vyama ya maeneo mengine nchini.

“Kwa ajili ya haya, ninataka kuhakikishia wakazi wa pwani kuwa ifikapo Juni mwaka huu, tutakuwa na chama chetu wenyewe ambacho kitaongoza kampeni za uchaguzi,” alisema.

Wiki mbili zilizopita, wabunge wa Tangatanga walimuidhinisha gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya kama kinara na msemaji wao eneo la Pwani.

Lakini Jumatano iliyopita, wabunge 25 na waziri msaidizi wa usalama, Bw Hussein Dado waliambatana na Bw Joho eneo la Garsen kupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI), na wakamuidhinisha Bw Joho kama kinara na msemaji wao atakayeunganisha pwani.

Akizungumza katika hafya hiyo, Bw Joho alisema wakati umefika ambapo wapwani wanafaa pia nao wasikizwe na maeneo mengine ya Kenya na kufanya misimamo zao wenyewe za kisiasa.

“Wakati umefika tutafanya uamuzi wetu wa siasa, tumekuwa tukitumiwa na watu kwa manufaa yao ya kisiasa na wakati wa kuwa wafuasi wa watu wengine umepita,” alisema na kuongeza “ukiniangalia mimi Hassana Joho au kiongozi mwengine wa pwani, kwani hatutoshi kuwa rais wa Kenya? Tumekuwa tukitumiwa vibaya kisiasa lakini wakati huu mambo yamebadilika.”

Lakini Bw Baya huenda ukubadilishaji wa uamuzi wa Bw Joho kisiasa huko Garsen ni baada ya kugunduwa mrengo wa Tangatanga umekita mizizi na kusambaa eneo la pwani.

‘Ili (Bw Joho) apate umaarufu, lazima avamia njama zetu na sasa anaitisha umoja wa wapwani pamoja na mgombeaji wa urais na yeye akiidhinishwa kama mpeperushaji bendera ya pwani,’ alisema.

Njama ya Joho, Kingi ‘kupiga chobo’ vinara wa Tangatanga

Na CHARLES LWANGA

MIBABE wa chama cha ODM eneo la Pwani sasa wamepanga njama kuwapiku wafuasi wa Naibu Rais William Ruto eneo hilo, wanaotaka kubuni chama kipya cha Wapwani.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, na mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi, wametangaza mipango ya kuzindua chama ambacho Wapwani watajitambulisha nacho kuanzia uchaguzi wa 2022.

Tangazo lao kwamba watazindua chama hicho mwezi Juni, lilikujia saa kadha baada ya wafuasi wa Dkt Ruto katika ukanda huo wametia moto wito wa kubuni chama cha Wapwani.

Mwishoni mwa wiki, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, alifichua kuwa chama cha Kadu Asili ndicho wamepiga msasa ili wakitumie katika chaguzi zijazo, bila kutegemea vyama ambavyo vigogo wake si Wapwani.

Lakini Bw Joho alipinga mpango wa Bi Jumwa na wenzake akidai ni mbinu ya kutia kura za Wapwani katika kapu moja kwa manufaa ya Dkt Ruto.

Mnamo Jumamosi katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kaloleni, Gunga Mwinga, Gavana Kingi – ambaye ni mwandani wa Bw Joho – alisema eneo hilo lina kura takribani milioni tatu na wakati umefika kwao kujisimamia kisiasa.

“Nataka kuhakikishia wakazi wa Pwani kuwa ifikapo Juni mwaka huu tutakuwa na chama chetu wenyewe ambacho kitaongoza kampeni za uchaguzi,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Kingi alikashifu viongozi wa Pwani kwa kupigana wenyewe kwa wenyewe akisema hicho ndicho kizuizi kikuu cha umoja wa kanda hiyo.

“Changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba hata tukiitisha umoja wa Wapwani tunaendelea kupigana wenyewe kwa wenyewe kisiasa, na hata kupigia debe wagombeaji wa kutoka maeneo mengine ya Kenya,” alieleza.

Wiki mbili zilizopita, wabunge wa Tangatanga walimuidhinisha Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, kama kinara na msemaji wao eneo la Pwani.

Lakini Jumatano iliyopita wabunge 25 na waziri msaidizi wa usalama, Bw Hussein Dado, wakiandamana na Bw Joho eneo la Garsen kupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI), walimuidhinisha Bw Joho kama kinara na msemaji wao atakayeunganisha Pwani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw Joho alisema wakati umefika Wapwani pia wasikizwe na maeneo mengine ya Kenya na kufanya misimamo yao wenyewe ya kisiasa.

“Wakati umefika kufanya uamuzi wetu kisiasa. Tumekuwa tukitumiwa na watu kwa manufaa yao; wakati wa kuwa wafuasi wa watu wengine umepita,” akasisitiza.

Alisema matumaini yake kwamba Kiongozi wa ODM Raila Odinga ataunga mkono mgombeaji urais kutoka Pwanii, kwani eneo hilo limemuunga mkono kwa miaka mingi.

“Kuna wale wanadai ati tunataka kiti cha naibu waziri mkuu, hayo si kweli kwa sababu tunalenga kiti cha urais,” alisema.Bw Joho alisema watajaribu mahojiano na wapinzani wao Pwani ili wawarudishe upande wao na wasonge pamoja nao kwa madhumuni ya kuunganisha eneo zima.

Matokeo ya uchaguzi mdogo Kwale yalivyowapa maadui wa Joho sauti

Na MOHAMED AHMED

SIASA za uchaguzi mdogo wa Msambweni, Kwale uliofanyika mwezi uliopita, zilikuwa zimechukuliwa kama kipimo cha umaarufu na ufuasi miongoni mwa viongozi wa Pwani.

Kati ya viongozi hao ni pamoja na Gavana Hassan Joho na baadhi ya wabunge ambao zamani walikuwa maswahiba wa Bw Joho lakini baadaye wakamtoroka.

Wabunge hao wanaongozwa na Bi Aisha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Mohammed Ali (Nyali) na Khatib Mwashetani wa Lunga Lunga.

Wabunge hao walikuwa wameshikana pia na kusukumwa na aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar ambaye ni mpinzani mkubwa wa Bw Joho.

Katika uchaguzi huo, wapinzani hao walikuwa wanamuunga mkono Feisal Bader ambaye alinyakua kiti hicho dhidi ya Bw Omar Boga ambaye alikuwa anaungwa mkono na Bw Joho.

Kuanzia kumalizika kwa uchaguzi huo, moto wa kisiasa ulianza rasmi kati ya Bw Joho na viongozi hao wenzake wa Pwani. Mzozo huo wa kisiasa baina ya pande hizo mbili pia umelenga kumuondolea Bw Joho sifa za kuwa kiongozi ama “Sultan” wa Pwani kama anavyojiita.

Sasa, wabunge hao wamezamia kwa nguvu mpya, kuendeleza ‘injili’ yao ya kutaka kuwepo kwa chama cha Pwani huku baadhi yao wakimpendekeza Gavana Salim Mvurya wa Kwale kuwa ndiye anayestahili kuwa kiongozi wa Pwani.

“Sisi hatukuogopi. Wewe kama unataka siasa za kujipiga kifua na majivuno basi tunakwambia tuko tayari. Tutapambana na wewe. Kama ulisema huu ndio mwaka utakaoongoza Pwani basi sisi tuko tayari kupambana,” akasema Bi Jumwa wiki jana kufuatia kauli ya Gavana Joho kuwa chama cha ODM kitaanza rasmi kampeni zake mwaka huu.Aidha, wabunge hao wakiongozwa na Bw Baya walisema nembo na rangi za chama wanachotaka kusajili ziko tayari.

Chama hicho kipya, wabunge hao walisema, kinalenga kuendeleza umoja wa Pwani na kujitoa kwenye utawala wa ODM ambapo Bw Joho ndiye naibu kiongozi.

Chama hicho kulingana nao pia kitaungana na vuguvugu la Hustler Nation ambalo linaongozwa na Naibu Rais William Ruto.Wabunge hao walitoa matamshi hayo yote baada ya Bw Joho kutoa taarifa ya akiikashifu mipango yao ya kuunda chama kipya cha Pwani akisema kuwa tayari kuna vyama vya kutosha Pwani.

Badala yake, Bw Joho alidai kuwa viongozi hao wanapanga mipango hiyo ili kumridhisha Dkt Ruto ambaye ndiye kiongozi wao wa mipango hiyo.Mnamo Alhamisi alipozuru Kaunti ya Tana River, Bw Joho kwa mara nyingine aliwafokea wabunge hao na kusema kuwa umoja huo wa Pwani haufai kuelemea kwa kiongozi ambaye wanamtaka wao.

“Msiambiwe tu kushikana kwa sababu ya mtu fulani. Kama ni kushikana, tushikane kwa sababu yetu wenyewe. Mimi nataka kubadilisha hayo mawazo ya kufuata watu wengine. Safari hii sisi tusikubali kuwa wafuasi, ni lazima sisi pia tufuatwe,” akasema Bw Joho.

Alisema kuwa kusimama kwa Pwani na Bw Raila Odinga ni kwa matarajio kuwa ataunga ukanda huo siku za usoni. Bw Joho alisema ukanda wa Pwani unapaswa kulenga kuwa na kiongozi atakayewakilisha eneo hilo katika mjadala wa kitaifa na si kuendelea kuwakilishwa kila mwaka.

“Sisi tutafanya mashauriano na watu wetu.  Hatuwezi kuendelea kufuata kila siku. Tunataka kuwa tunakaa kwenye meza na kuwa na sauti na si kila siku sisi tuwe ndio ‘menu’. Haiwezi kuwa kila hesabu zikipigwa sisi hatumo. Sisi pia tuna uwezo,” akasema Bw Joho.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Pwani, Prof Hassan Mwakimako viongozi hao wote wamekuwa na tabia ya ubinafsi na kwa muda sasa wanaangalia maslahi yao kuliko yale ya Pwani.

Katika mahojiano, Prof Mwakimako alisema kuwa umoja wa Pwani utasimama iwapo wanasiasa watakuwa na nia safi na wakazi na si kupitia vyama.

“Sioni kama wanasiasa hawa wana nia ya ukweli kuhusiana na umoja wa Pwani. Kama ni umoja si lazima pawepo chama kipya ama tuendelee kukaa kwenye vyama vinavyoongozwa na wengine. Nia ikiwa safi basi hapo ndipo watakapofaulu,” akasema.

Ukiwa umesalia mwaka mmoja hadi kufikia uchaguzi mkuu ujao, itaangaliwa ni vipi ukanda huo utakavyoenda kuhusiana na siasa za 2022 kwani kwa muda eneo hilo limekuwa likiongozwa na wanasiasa wakuu kwa sababu ya mgawanyiko na kutoshikana kwa viongozi kama ilivyo sasa.

Viongozi hao wakuu wameendelea kunufaika na kukosekana kwa umoja wa Pwani ambayo huajawa na kiongozi wa kuiendesha na kuwa na sauti moja kama jamii.

Joho ataka Raila aunge Mpwani kuwania urais

STEPHEN ODUOR na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa, Hassan Joho ameeleza matumaini kwamba Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ataunga mkono mgombeaji urais kutoka Pwani katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Huku akiwajibu mahasimu wake wa kisiasa wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, gavana huyo aliye pia naibu kiongozi wa ODM alisema Pwani itakuwa na mgombeaji urais mwaka wa 2022 na anaamini Bw Odinga ataunga mkono mgombeaji atakayetajwa.

Kulingana naye, eneo hilo limekuwa likimuunga mkono Bw Odinga kwa muda mrefu kwa sababu waziri mkuu huyo wa zamani anajua eneo hilo linatarajia atarudisha mkono.

Kufikia sasa, Bw Odinga hajatangaza iwapo atawania urais katika uchaguzi ujao huku Bw Joho akiwa tayari ameeleza azimio lake kuwania wadhifa huo.

“Hatuwezi kuunga mkono watu wengine kila mwaka wa uchaguzi. Tunataka kukaa kwenye meza. Hatuwezi kuendelea kuwa menyu. Hatuwezi kuwa katika hali ambapo wakati wowote kuna mipango inayofanywa, hakuna hata mmoja wetu kutoka eneo letu aliyepo. Hatuwezi kuendelea kuwakilishwa. Huu ni wakati wa kiongozi kutoka eneo hili kuwa kwenye debe la urais na matokeo ya kinyang’anyiro hicho yaamuliwe mbele mbele hata iweje,” akasema.

Hata hivyo, alionya kwamba hilo halitawezekana iwapo viongozi wa eneo hilo wataendelea kujibizana kwa njia inayoashiria ubinafsi.

Alisema mfumo wa siasa za Pwani unapaswa kuwa tofauti, kwa hivyo viongozi hawapaswi kuwa wepesi kutoa wito kwa umoja wa mkoa huo bila mipango kabambe.

“Hatutafanikiwa ikiwa tutaonekana kutoelewa kile tunachohitaji kama eneo,” alisema hayo wakati wa ziara katika Kaunti ya Tana River.

Aliwakashifu viongozi wa Pwani wanaoegemea upande wa Naibu Rais akisema wana nia mbaya wanapodai kwamba wanataka kuwaunganisha Wapwani.

Kwa mujibu wa Bw Joho, umoja wa Pwani haupaswi kuwa kwa msingi wa kuunga mkono kiongozi mmoja, bali kwa madhumuni ya kuwafaidi watu wa Pwani na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.

“Hatupaswi kuambiwa kwamba tunahitaji kuungana kwa sababu ya kiongozi fulani. Ikiwa tunatafuta umoja, basi iwe kwa mkoa wetu na kwa ajili ya Wapwani. Tunapaswa kuungana kwa sababu ya changamoto tunazokabiliana nazo kama wakaaji wa eneo hili,” alisema Bw Joho.

Wito kuhusu uundaji wa chama kimoja cha Wapwani umeshika kasi tangu uchaguzi mdogo wa Msambweni ufanyike, ambapo ODM ilishindwa na upande wa Dkt Ruto licha ya kutarajiwa na wengi kunyakua kiti hicho.

Matokeo hayo yalifanya baadhi ya viongozi wa eneo hilo kumtaka Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, atwikwe jukumu la kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa Wapwani. Jukumu hilo limekuwa mikononi mwa Bw Joho kwa muda mrefu.

Wabunge wasiopungua 11 wa Pwani na Seneta wa zamani wa Mombasa Hassan Omar ambao wanamuunga mkono Dkt Ruto ndio wako katika mstari wa mbele kushinikiza kuundwa kwa mavazi mapya ya kisiasa kabla ya mwaka wa 2022.

Shahbal aonekana kufaidika na siasa za kumrithi Joho

Na MOHAMED AHMED

SIASA za urithi wa kiti cha Gavana wa Mombasa Hassan Joho zimeonekana kuchukua mkondo tofauti ambao unaonekana kumfaidi mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambaye anawinda kiti hicho mwaka 2022.?

Kufikia sasa, kiti hicho kimevutia wagombeaji kadha wakiongozwa na Bw Shahbal pamoja na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ambao ndio wameonekana kuwa washindani wa juu zaidi.

Wawili hao wote wanatarajia kupata kuidhinishwa na Bw Joho wakati uchaguzi huo utakuwa unakaribia mnamo 2022.? Licha ya Bw Joho kuonyesha dalili kuwa atamuunga mkono Bw Nassir, watu wake wa karibu ambao wamehusika katika mipango yake ya siasa wameonekana kuelemea upande wa Bw Shahbal, hatua ambayo inaibua masuali mengi kuliko majibu.

Miongoni mwa watu hao wa karibu wa Bw Joho ni washauri wa kisiasa wa gavana huyo akiwemo Rashid Bedzimba ambaye alikuwa mbunge wa Kisauni na aliyekuwa mshauri wa Bw Joho, Idriss Abdurahman ambaye sasa ni mshauri wa masuala ya usalama katika afisi ya gavana.

Bw Bedzimba ambaye ana ushawishi wa kutosha katika eneo bunge la Kisauni alipanga mkutano na viongozi wa kampeni zake na kuwakutanisha na Bw Shahbal.

Hatua hiyo ni baada ya kubainika kuwa Bw Abdurahman naye ndiye aliyechukua uongozi wa mipango ya kampeni ya Bw Shahbal.? Kwa upande Bw Bedzimba analenga kumkusanyia Bw Shahbal kura za Kisauni kulingana na ufuasi alionao.

Bw Bedzimba amehudumu eneo bunge hilo kwa zaidi ya miaka 15 kama diwani na mbunge.? Hata hivyo, mwaka 2017 alipoteza kiti hicho kwa mbunge wa sasa Ali Mbogo ambaye kwa sasa analenga kiti cha ugavana.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia analenga kiti hicho.? Siku za hivi karibuni, ni Bw Shahbal na Bw Nassir ambao ndio wameonekana kuzunguka zaidi kuuza sera zao mapema kwa wananchi.

Akizungumza katika ukumbi wa Sheikh Zayed eneo la Bombolulu baada ya kukutana na wafuasi hao wa Bw Bedzimba, Bw Shahbal alisema kuwa ana matumani kuwa kushikana na Bw Bedzimba kutamuezesha kunyakua kiti hicho cha ugavana.

Alisema pamoja watapigana na changamoto za utovu wa usalama, utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana na ukosefu wa kazi.

“Nataka kumshukuru Bw Bedzimba kwa nafasi hii ya kunikutanisha na majemedari wake. Mimi nawaomba tushikane mkono ili tuhudumie watu wetu wa Kisauni na Mombasa kwa jumla tukiwa pamoja,” akasema Bw Shahbal.

Bw Bedzimba kwa upande wake alisema kuwa ameaumua kumuunga mkoni Bw Shahbal kwa sababu miongoni mwa wale wote ambao wanataka kuwania kiti hicho yeye yupo mbele.

Alimtaja Bw Shahbal kuwa kiongozi mwenye maono na mwenye azma ya kuhudumia wakazi wa Mombasa kwa hali na mali..? ? ? “Mimi madhali alikuja akaniomba anataka kukutana na nyinyi nikasema tumpe nafasi. Kwa sababu hata tukiangalia kwa wote wale ambao wanataka kiti hicho Bw Shahbal yupo mbele yao tayari,” akasema Bw Bedzimba.

Hayo yalijiri huku mbunge wa Mvita Bw Nassir akionekana kuondeleza siasa zake katika maeneo bunge ya Kisauni, Nyali na Changamwe.? ? ? Bw Nassir amekuwa akifanya mikutano na kujipigia debe ili apate nafasi hiyo baada ya kumaliza hatamu yake kama mbunge wa Mvita.

Aidha, mbunge wa Kisauni Ali Mbogo naye ameonekana kushikilia siasa za mashinani ambapo amekuwa akiendesha kampeni zake za kiti cha ugavana.

Ikiwa imesalia zaidi ya mwaka mmoja, wandani wa masuala ya siasa wanatazama iwapo wale ambao wameanza mapema siasa zao watatoboa hadi mwisho wa ushindani huo wa mwaka 2022.

Hii pia ni kwa sababu inatarajiwa kuwa kutaibuka wawaniaji wengine katika kumezea mate kiti hicho.? ? Ikisubiriwa hilo, kwa sasa viongozi waliopo wamepata wasaa wa kujipigia debe na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata kiti hicho ifikapo mwaka wa uchaguzi.

Ubunge kuokoa vigogo kisiasa

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA ambao wanahudumu kwa muhula wa pili, na wa mwisho, watalazimika kuwania nyadhifa za ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2022 ili wawe katika nafasi bora ya kuteuliwa kwa nyadhifa za juu serikalini.

Hii ni baada ya mswada rasmi wa marekebisho ya Katiba kupitia Muafaka wa maridhiano (BBI) kutopendekeza kubuniwa kwa serikali za majimbo, ambazo baadhi ya magavana hao walipania kuongoza. Vilevile, BBI imedumisha vipengele vya katiba vinavyosema kuwa rais na magavana watahudumu kwa mihula miwili pekee.

Kulingana na mswada huo, uliozinduliwa Jumatano, Nairobi, Waziri Mkuu, manaibu wa waziri mkuu, sehemu ya mawaziri na manaibu waziri watakuwa wabunge, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo mawaziri hawapaswi kuwa wabunge.

Baadhi ya magavana 22 watakaostaafu 2022, walikuwa wameweka matumaini yao kwa marekebisho haya ya Katiba, kwamba wangepata mwanya wa kuwania nyadhifa za magavana wa majimbo.

Wengi wao waling’amua kuwa nafasi ya kuwania urais au kuwa mgombea-mwenza 2022 utakuwa finyu.

Mapema mwaka huu, magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Ali Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi) walitetea kubuniwa kwa serikali za majimbo, kwa kile kilichofasiriwa kama nia ya kuendeleza kuwa na ushawishi wa kisiasa. Magavana hao, ambao awali walikuwa wametangaza nia ya kugombea urais, walitoa mapendekezo hayo wakati wa mikutano ya hamasisho kuhusu BBI katika uwanja wa Tononoka (Mombasa) na ule wa Bukhungu (Kakamega).

Wakili wa masuala ya kikatiba, Bw Bobby Mkangi anasema kuwa japo wadhifa wa ubunge unaonekana kuwa wenye hadhi ya chini kuliko ugavana, mswada wa BBI sasa umeufanya kuwa kivutio kwa magavana watakaokamilisha kipindi chao cha kuhudumu 2022.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba baadhi ya magavana, wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho, watalazimika kuwania nyadhifa za ubunge ili wazitumie kucheza karata zao za kuteuliwa katika nyadhifa za Waziri Mkuu, manaibu wa waziri mkuu, mawaziri na manaibu wa mawaziri. Hii ni kwa sababu wengine wao hawataki kusalia katika baridi ya siasa baada ya kuondoka afisini,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Alhamisi.

Kauli sawa na hii ilitolewa na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora, aliyesema kuwa haitashangaza kuona baadhi ya magavana wanaotaka kuwania urais, wakiendea nyadhifa za ubunge kama ‘daraja’ la kukwea juu serikalini.

“Ukweli ni kwamba mswada wa BBI umewaacha magavana wanaohudumu kipindi cha pili katika hali ya kujikuna kichwa hasa baada ya wazo la kubuniwa kwa serikali za majimbo kutupiliwa mbali. Kwa hivyo, itawalazimu kuwania nyadhifa nyingine kuanzia ubunge, useneta na hata urais ili waendelee kuwa na usemi katika ulingo wa siasa,” akasema Bw Manyora, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alisema kuwa pendekezo la kubuniwa kwa maeneobunge mengine 70 zaidi litawafaa zaidi magavana hawa 22 kupata nafasi za kushindania nafasi hizo mpya.

Orodha ya kaunti 28 zilizogawiwa maeneobunge hayo mapya ina kaunti 15 zilizo na magavana wanaohudumu kwa awamu ya pili.

“Kwa mfano, Bw Oparanya anaweza kuwania kimojawapo cha viti viwili vya maeneobunge yatakayobuniwa katika Kaunti ya Kakamega. Naye Bw Joho anaweza kuwania katika mojawapo ya maeneo matatu mapya ambayo yatabuniwa katika Kaunti ya Mombasa endapo mswada wa BBI utapitishwa na Wakenya katika kura ya maamuzi,” akaeleza Bw Manyora.

Hata hivyo, wachanganuzi hao wanaonya kuwa magavana watakaowania nyadhifa za ubunge kwa lengo la kuteuliwa mawaziri watakuwa na kibarua kikubwa kujinadi kwa wapigakura.

Kulingana na Bw Mkangi, itabidi waweke matumaini yao kwa uwezekeno wa chama au muungano watakaotumia kisiasa kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu.

Hivi majuzi, Gavana Oparanya, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), alitangaza kuwa hatastaafu siasa baada ya kipindi chake kukamilika ila atapigania kiti cha kitaifa.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye alikuwa akiongea katika Shule ya Upili ya Shiatsala, eneobunge la Butere, hakufichua wadhifa atakaopigania.

“Kipindi changu cha kuhudumu kama gavana kinakamilika 2022. Nimeamua kuwa sitaenda nyumbani lakini nitaendelea kupambana katika siasa za kitaifa. Sijui ni kiti kipi, lakini ninaamini kuwa nitakuwa katika meza ambako keki ya kitaifa inagawanywa,” akasema.

Magavana wengine wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho ni pamoja na Jackson Mandago (Uasin Gishu), Sospeter Ojaamong (Busia), Martin Wambora (Embu) na Paul Chepkwony (Kericho).

Wengine ni Josephat Nanok (Turkana), Mwangi wa Iria (Murang’a), Okoth Obado (Migori), Samuel Tunai (Narok), James Ongwae (Kisii), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) miongoni mwa wengine.

Joho apata pigo huku wengi wakimuomboleza Hatimy

MOHAMED AHMED Na MISHI GONGO

KIFO cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha ODM na diwani maalum wa Mombasa, Bw Mohammed Hatimy, kimeacha pengo kubwa katika serikali ya Gavana Hassan Joho.

Bw Joho binafsi alikiri kwamba kifo cha Bw Hitamy ni pigo kwake na Mombasa kwa jumla. “Mombasa imepoteza mwana wake wa kutegemewa ambaye nilikuwa namthamini sana,” Bw Joho alisema kwenye rambirambi zake.

Bw Hatimy alifariki Jumamosi akiwa katika hospitali ya Mombasa ambapo alipelekwa baada ya kupatikana kuambukiwa virusi vya corona.Bw Hatimy ambaye alizikwa jana katika makaburi ya Kikowani, alifariki siku chache tu baada ya mavyaa wake ambaye pia aliripotiwa kufariki baada ya kuugua corona.

Familia yake ilieleza kuwa alifariki Ijumaa saa tisa usiku. Wengi walimsifia Bw Hatimy wakisema hakuwa kama diwani wa kawaida na kwamba aliheshimiwa na kupendwa na wengi.

Kuanzia mwanzo wa serikali ya Bw Joho mwaka 2013, Bw Hatimy ameshikilia wadhfa wa mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kaunti hiyo tangu Bw Joho aliposhinda ugavana 2013.

Bw Hatimy pia alitambulika wakati alipokuwa kwenye usimamizi wa michezo.Jana, viongozi wa chama cha ODM wakiongozwa na kinara wao, Bw Raila Odinga waliomboleza kifo chake na kumtaja kuwa kiongozi aliyejitolea katika utumishi wake.

“Nimezipokea taarifa za kufariki kwa mwenyekiti wa muda mrefu wa ODM tawi la Mombasa Mohammed Hatimy. Alikuwa kiongozi shupavu aliyejitolea katika kila pembe aliyoshikilia. Mungu aipe familia yake subira wakati huu mgumu,” akasema Bw Odinga kupitia mtandao wake wa kijamii.

Gavana Joho alisema kuwa Mombasa imepoteza mmoja wa watu muhimu a kutegemewa.“Kama diwani maalum alihudumu kwa kujitolea na alionyesha matunda ya kazi yake na majukumu aliyokuwa amepewa. Kwa niaba ya watu wa Mombasa natoa rambirambi zangu kwa familia. Mungu awape subira wakati huu wa huzuni,” akasema.

Kivumbi chaanza Joho akitua Msambweni

Na MOHAMED AHMED

KIVUMBI kinatarajiwa katika uchaguzi mdogo wa Msambweni baada ya Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na mwenzake wa Kwale, Salim Mvurya kuunga wagombeaji wawili wapinzani.

Huku Bw Joho akimuunga mkono mgombeaji wa chama cha ODM, Omar Boga, Bw Mvurya ametangaza yuko nyuma ya mgombeaji huru Feisal Bader ambaye pia anapigiwa debe na Naibu Rais William Ruto.

Viongozi wengine wa Kaunti ya Kwale ambao wako upande wa Bw Bader ni wabunge wa Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Benjamin Tayari (Kinango) na naibu wa Bw Mvurya, Bi Fatuma Achani.

Viongozi wengine ni pamoja na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, Owen Baya (Kilifi Kaskazini) Didmus Barasa (Kimilili) na waliokuwa maseneta Hassan Omar (Mombasa), Johnson Muthama (Machakos), Boni Khalwale (Kakamega) miongoni mwa wengine.

Baada ya Bw Bader kuwasilisha stakabadhi zake mnamo Alhamisi viongozi hao walifululiza pamoja na mgombea huyo katika uwanja wa Sawa Sawa eneo la Ramisi ambapo waliuza sera zake.

Viongozi hao walitaka wakazi kumpigia kura Bw Bader kama hisani kwa mjombake Bw Suleiman Dori ambaye alifariki na kuacha wazi kiti hicho ambacho kinapiganiwa saa hii.

“Sisi tulifanya kazi na Bw Dori na tumeona kuwa katika chaguzi ndogo za hapo nyuma ndugu za marehemu wanapewa kiti lakini hapa tunaona upande ule mwengine umedinda kufanya hilo, hivyo basi nawaomba mrejeshe hisani kwa familia hii,” akasema Bw Mwashetani aliyekuwa anaongoza mkutano huo.

Bw Tayari pia alisisitiza hilo na kusema kuwa licha ya yeye kuwa mwanachama wa ODM ameamua kumpigia debe Bw Bader kwa sababu ya hisani yake kwa Bw Dori.

Viongozi hao wengine pia walimpigia debe Bw Bader na kusema kuwa watakita kambi eneo hilo la Msambweni kuhakikisha kuwa wanaibuka washindi.

Kwa upande wao, viongozi wa ODM wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho jana alisema kuwa watakita kambi eneo hilo kuhakikisha kuwa Bw Boga anashinda kiti hicho.“Sisi kama chama tupo tayari kwa ushindani huu.

Na ninaamini tutashinda kwa sababu tupo na ajenda kwa watu wa Msambweni. Bw Boga ndiye kiongozi anayestahili nafasi hiyo. Sisi hatushindani na watu ambao wanafanya siasa zao Nairobi,” akasema Bw Joho.

Bw Joho alimshambulia Dkt Ruto akisema kuwa kama yeye ni mkali kweli na anajiamini basi aende eneo la Pwani wapimane nguvu. Alisema kuwa yeye hatashindana na wale wanaotumwa na Dkt Ruto kwani hao ni watu ambao hawapo ngazi yake ya kisiasa.

Seneta James Orengo naye alisema kuwa Bw Boga atashinda kiti hicho kwa sababu eneo la Msambweni ni ngome ya ODM.“Tukiwa na Joho ndiye anaongoza kampeni na Boga kama mgombea wa ODM na handisheki basi tutashinda kiti hicho. Nawaomba tufanye kampeni za amani sisi sote,” akasema.

Bw Mvuvra ambaye ni gavana wa Jubilee alisema kwamba Bw Bader ndiye anayeweza kuwafaa wakazi wa Msambweni kwa sababu alifanya kazi kwa karibu na marehemu Dori.

Joho kumenyana na Ruto Msambweni – ODM

Na JUSTUS OCHIENG

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimesema kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge cha Msambweni, Kaunti ya Kwale kitakuwa ushindani kati ya naibu kiongozi wa chama hicho Hassan Joho na Naibu Rais William Ruto.

Chama hicho kilitangaza jana kuwa kinyume na ripoti kwamba ulikuwa ushindani kati ya kiongozi wake Raila Odinga dhidi ya Naibu Rais, ni Gavana wa Mombasa atakayeongoza kampeni zake katika uchaguzi mdogo uliotengewa kufanyika Disemba 15.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, Jumatatu alieleza Taifa Leo kuwa kiti hicho kitakuwa mapambano kati ya manaibu wawili.

“Itakuwa naibu dhidi ya naibu. Tuna jumla ya chaguzi tatu ndogo katika eneo la Pwani na tunapanga kutwaa viti vyote,” alisema Bw Sifuna.

Wadi ya Dabaso katika Kaunti ya Kilifi na wadi ya Wundanyi/Mbale katika Kaunti ya Taita Taveta ni miongoni mwa maeneo matatu ya upigaji kura ambapo IEBC itaandaa chaguzi hizo eneo la Pwani.

Maeneo mengine ni Wadi ya Kisumu Kaskazini katika Kaunti ya Kisumu na Wadi ya Kahawa Wendani katika Kaunti ya Kiambu.

Katika eneo la Msambweni, ODM inampigia debe aliyekuwa diwani wa Wadi ya Gombato/Bongwe Omar Boga, atakayepimana nguvu na mgombea wa kujitegemea Feisal Bader.

Uongozi wa Joho wazua zogo bungeni

Na WINNIE ATIENO

WAWAKILISHI wa wadi katika Bunge la Kaunti ya Mombasa wametofautiana kuhusu wajibu wa Gavana Hassan Joho, huku baadhi wakikiri ni watu wake wa mkono.

Baadhi ya madiwani hao wamedai hawana uhuru wa kujadili hoja yoyote bila ya ruhusa ya Gavana Joho, ambapo wenzao walioteuliwa wamekuwa wakipitisha hoja au mswada unapopendekezwa na serikali ya kaunti hiyo bila kuidadisi.

“Sipendi ukandamizaji wa wanyonge. Kamati za bunge letu zinateuliwa kulingana na wale wanaotii amri ya bwana mkubwa. Sioni haya kuwaambia ukweli,” alidai diwani wa Kipevu, Bi Faith Mwende.

Alitoa mfano wa diwani wa Kongowea, Bw Abrary Mohammed Omar ambaye alikuwa naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge inayosimamia ardhi lakini akatimuliwa.

“Ukisema kitu tofauti na wenye mji unang’atuliwa kutoka kamati za bunge. Nitakuwa nawaambia ukweli. Wenyeviti wote wanaimba wimbo wa Joho. Ninasikitikia sana bunge letu. Tuombe Mungu kwa miujiza lakini hamuwezi kupata haki bungeni,” aliongeza.

Diwani wa Freretown, Bw Charles Kitula aliwataka wakazi, hasa wafanyabiashara, wasusie kulipa ushuru hadi pale Bw Joho atakapowaeleza namna alivyotumia fedha za ugatuzi.

Diwani huyo ambaye alitimuliwa kutoka kwawadhifa wa Kiranja wa Wengi, alisema kosa lake kubwa ni kuuliza maswali magumu kuhusu ufujaji wa fedha.

“Ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu na matumizi ya fedha za umma ilipotoka, niliona dosari katika kaunti yetu ya Mombasa. Kati ya 2013 na Machi 2020, serikali yetu imetumia Sh15 bilioni kwa maendeleo. Nina stakabadhi zote za kuthibitisha ninayoyasema. Haya maendeleo yako wapi?” akauliza Bw Kitula.

Lakini kiongozi wa vijana wa ODM tawi la Mombasa, Bw Moses Aran alimtetea Gavana akisema haingilii bunge hilo.

“ODM ina idadi kubwa ya wawakilishi wa wodi bungeni na hatufai kuonewa gere wala kulaumiwa kutokana na hilo. Bunge linaendeshwa na idadi ya waliowengi. Kati ya wawakilishi 42 wa bunge letu, mbona ni wanne tu ambao wanapiga kelele. Niliteuliwa na ODM na lazima niwe mwaminifu kwa chama,” alisema.

Bw Aran alisema Bw Joho hajawahi kuwashurutisha wala kuwaita mkutanoni ili wamuunge mkono kwenye maswala yake katika bunge.

“Sisi kama wabunge wateule 12, tumekuwa katika mstari wa mbele kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa sharia.

Madiwani 27 walichaguliwa na wananchi kupitia chama cha ODM, mmoja anatoka Wiper, Ford Kenya na mwingine alikuwa mgombea huru. Bw Kitula na wenzake ni watu wa maslahi,” alisema Bw Aran.

Spika wa bunge la Mombasa, Bw Aharub Khatri alikanusha madai hayo akisema haongozi wanaopiga muhuri kwenye uongozi wa bunge hilo.

“Haya ni masuala ya kisiasa, hayanihusu. Mimi sina kura wala siko kwenye kamati za bunge. Kazi yangu ni kama jaji na kutoa uamuzi, huwa sipendelei upande wowote,” akasema.

Hata hivyo wawakilishi wa wodi teule wakiongozwa na Bi Fatma Kushe walikiri kuwa wao ni wapiga muhuri wa Bw Joho na chama cha ODM.

“Niliteuliwa na Gavana Joho kupitia ODM ambaye ni naibu kinara wa chama hicho. Siwezi kwenda kinyume na ODM wala Bw Joho. Bw Kitula alichaguliwa kupitia ODM kama yeye ni mwanamume kweli ajiuzulu na agombee kiti chake kupitia chama cha hasla. Alikuwa kiranja wa bunge, alitekeleza mangapi? Tunajua hao wasaliti wanatumika na wapinzani wetu kuzua vurugu bungeni,” alidai Bi Kushe.

Madiwani sasa watishia kumtimua Joho

Na FARHIYA HUSSEIN

BAADHI ya madiwani wa Kaunti ya Mombasa, wametishia kumtimua ofisini Gavana Hassan Joho, wakimlaumu kwa ufisadi na kuwadharau.

Haya yanajiri siku chache baada ya madiwani hao kumshtaki Bw Joho kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), wakitaka achunguzwe kwa madai ya matumizi mabaya ya pesa.

Diwani wa wadi ya Jomvu Kuu, Bw Athman Shebe, alisema kwamba wanatumia sheria kumuondoa Bw Joho ofisini.

Hata hivyo, wanaomuunga Bw Joho walipuuza tisho hilo wakisema wanaolalamika hawana idadi ya kutosha kufanikisha mswada wa kumuondoa ofisini.

“Iwapo wataweza kuwasilisha mswada katika bunge la kaunti, watahitaji kuuungwa na theluthi mbili ya wawakilishi,” alisema diwani wa Likoni, Bw Athman Mwamiri.

Alisema ili mswada wao uweze kukubaliwa, watahitajika kukusanya sahihi za madiwani 14.Bw Shebe alisema kwamba madiwani wengi wanaunga mkono kutimuliwa kwa Joho japo wanaogopa kutamka hadharani.

“Wawakilishi wengi wa wadi wanaogopa kuonekana ama kusikika hadharani wanataka kumuondoa gavana. Hii ndio sababu kuu ya sisi kufuata njia za kisheria na tayari tumeanza kukusanya sahihi,” akasema Bw Shebe.

Mwenyekiti wa Chama cha ODM kaunti ya Mombasa, Bw Mohammed Hatimy, ambaye anasimamia fedha katika kaunti ya Mombasa, alisema kwamba Bw Joho yuko tayari kujitetea kortini.

“Ikiwa ni kweli wana ushahidi, basi wauwasilishe. Pesa wanazotushtumu kwa matumizi mabaya zilitumika kuwalipa wafanyakazi mshahara, kumaliza miradi, na baadhi ya maswala mengine,” alisema.

Madiwani Bw Charles Kitula (Freretown), Athman Shebe (Jomvu Kuu), Abarari Omar (Kongowea), Fahad Kassim (Mjambere) ni miongoni mwa wanaotaka Bw Joho kuondolewa ofisini.

Wanne hao walipokonywa nyadhifa za uongozi katika bunge la kaunti kwa kumshtaki Bw Joho kwa EACC.

Madiwani waliosema Joho ni mfisadi watimuliwa

Na FARHIYA HUSSEIN

MADIWANI wa Kaunti ya Mombasa ambao walimshtaki Gavana Hassan Joho kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa madai ya utumizi mbaya ya fedha za umma, wameadhibiwa kwa kutupwa nje ya Kamati za Bunge.

Akiongea na Taifa Leo jana, diwani wa Jomvu Kuu, Athman Shebe, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira, alithibitisha kuwa yeye ni mmoja wa walioondolewa katika kamati za bunge.

‘Tulitolewa kwa sababu tulijitokeza wazi kuzungumzia jinsi fedha za umma zinavyotumika na serikali ya kaunti, ‘akasema Bw Shebe.

Mwakilishi mwingine ambaye alipata pigo ni Charles Kitula wa wadi ya Freretown, ambaye alikuwa kiranja wa wengi katika bunge la kaunti: ‘Tumeondolewa kwenye kamati zote za bunge bila kupewa taarifa yoyote,’ akasema Bw Kitula.

Mwenzake wa wadi ya Kongowea, Abrari Omar naye alisema imekuwa shida kubwa kwao kuwasilisha hoja yoyote bungeni.

“Kamati ya biashara bungeni inaendeshwa na washirika wa gavana. Lakini tumeamua hatutakaa kimya tena. Tutatumia njia zote za kisheria kwani tuna ushahidi wote unaohitajika kumuondoa gavana wa kaunti yetu madarakani,’ Bw Omar alisema.

Diwani mmoja aliambia Taifa Leo kuwa walifanya mkutano mnamo Jumatatu ndani ya majengo ya bunge kuamua adhabu kwa madiwani wanaomkosoa Bw Joho’Mkutano wa madiwani wa ODM ulifanyika kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mitatu iliyopita mnamo Jumatatu.

Kusudi kuu lilikuwa kujadili jinsi wawakilishi wa wadi wanaozunguka wakimshutumu gavana wa kaunti wataadhibiwa,’ alisema diwani ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kaunti, Bw Mohammed Hatimy alipinga madai ya madiwani wanaomlaumu Bw Joho akisema hayana msingi.

Mnamo Jumanne, Mkuu wa EACC eneo la Mombasa, Bw Mutembei Nyaga alithibitisha kuwa amepokea ripoti kutoka kwa madiwani kuhusu madai ya matumizi mabaya ya pesa katika kaunti hiyo.

Bw Nyaga alisema EACC itaamua hatua za kuchukua baada ya kuchunguza madai yaliyowasilishwa, ambayo yanahusu utumiaji mbaya wa takribani Sh30 bilioni zilizokuwa kwenye bajeti ya kaunti tangu 2017.

Joho awindwa na EACC

MOHAMED AHMED na FARHIYA HUSSEIN

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inachunguza madai ya ufujaji wa pesa katika Serikali ya Kaunti ya Mombasa inayoongozwa na Gavana Hassan Joho.

Mkuu wa EACC jijini Mombasa, Bw Mutembei Nyaga jana alithibitisha kupokea ripoti kutoka kwa madiwani wa kaunti hiyo kuhusu utawala wa Bw Joho, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Nyaga alisema EACC itaamua hatua Za kuchukua baada ya kuchunguza madai yaliyowasilishwa, ambayo yanahusu utumiaji mbaya wa takribani Sh30 bilioni zilizokuwa kwa bajeti ya kaunti tangu 2017.

Haya yamefichuka siku chache baada ya kubainika kuwa Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed, pia anaandamwa na makachero wa EACC kuhusu kashfa ya ufisadi katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) iliyotokea mnamo 2015.

“Tulipokea barua hiyo juzi na bado tunaangalia madai hayo kutoka kwa madiwani,” akasema Bw Nyaga.

Katika barua yao kwa EACC, madiwani wanadai kumekuwa na ubaridhifu wa fedha katika utekelezaji wa bajeti za kaunti kuanzia 2017.

Wakiongozwa na Diwani wa Wadi ya Mjambere, Bw Fahad Kassim pamoja na mwenzake wa Frere-Town Charles Kitula, waliitaka EACC kuhakikisha usimamizi wa kaunti unapeana ripoti zake za fedha bungeni ipasavyo.

‘Tulimpa gavana muda atueleze jinsi pesa zilitumiwa. Tuliomba pia Idara ya Fedha kupitia kwa mwenyekiti wake itupatie angalau sababu ya kuridhisha kuhusu jinsi pesa zilitumiwa lakini hatujawahi kujibiwa hadi sasa. Tunasema tumechoka, wacha EACC ishughulikie hilo suala,’ akasema Bw Kitula.

Bw Kassim alidai kaunti hiyo ilikuwa inapanga kutumia Sh64 milioni kuweka maua katika kaunti na Sh3.4 milioni nyingine kuchimba visima akisema pesa hizo ni nyingi kwa miradi hiyo.

Kando na kupeleka kesi kwa EACC, walitishia kuwasilisha hoja ya kumng’oa Bw Joho mamlakani wakisema, pesa hutengewa maendeleo kwenye bajeti lakini hakuna miradi inaonekana mashinani.

“Kwa miaka mitatu hakujakuwa na uwasilishaji wa ripoti kuhusu matumizi ya fedha bungeni kama inavyotakikana kisheria,” akasema Bw Kassim kwenye mahojiano.

Aidha, viongozi hao wameitaka afisi ya fedha za kaunti kuhakikisha kuwa ripoti za fedha zinatumwa bungeni na kupelekwa katika afisi za serikali kuu kama inavyotakikana.

Viongozi hao wamedai hilo halitekelezwi ipasavyo kwa sababu ya njama za kuficha matumizi ya fedha za umma.

Uwasilishaji ripoti hizo ni hitaji la kisheria ambalo linapaswa kutekelezwa na kila kaunti nchini; jambo ambalo wawakilishi wa Mombasa wanadai halijakuwa likitekelezwa.

“Mambo yanafanywa tofauti hapa na ndio sababu hatuna imani na kamati ya fedha ambayo ndio imekuwa ikichangia kuwepo kwa shida hizi zote,” akasema Bw Kassim.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kaunti, Bw Mohammed Hatimy amepinga madai ya madiwani hao akisema hayana msingi. A

lisema ripoti hizo ambazo madiwani hao wanataka zimekuwa zikipelekwa katika afisi za wakuu wa fedha jijini Nairobi kama inavyotakikana.

“Serikali kuu inapata ripoti za kaunti kupitia kwetu, na bunge limekuwa likiwasilisha ripoti hizo ndio maana hakujakuwa na shida yoyote na afisi za serikali kuu zinazoangalia masuala ya fedha,” akasema Bw Hatimy.

Alieleza kuwa, pesa za kaunti zimekuwa zikitumiwa vyema kwa miradi ya maendeleo na kulipa mishahara ya wafanyakazi.

‘Kuna miradi katika kaunti, ilhali wanadai hakuna chochote kimefanywa. Pesa hutumiwa pia kulipa wafanyakazi mishahara yao miongoni mwa mahitaji mengine,’ akasema.

Kaunti yaambiwa ianze kufunga vituo vya corona

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuhamisha vituo vyote vya wagonjwa wa Covid-19 vilivyo katika taasisi za elimu huku wizara ya elimu ikijitayarisha kwa ufunguzi wa vyuo vikuu na vile vya mafunzo ya anuai.

Serikali ya kaunti ya Mombasa imejipata njia panda kwenye vita vyao dhidi ya virusi hivyo baada ya kutakiwa kuhama kwenye chuo kikuu cha Mombasa na ile ya Kenya National Coast Polytechnic ambapo wagonjwa wenye akili taahira wanaopambana na virusi hivyo wanatibiwa.

Chuo Kikuu cha Mombasa ndicho kituo kikubwa zaidi cha wagonjwa wa corona chenye vitanda 300.

Hivi majuzi waziri wa afya Bw Mutahi Kagwe aliipongeza serikali ya Mombasa kwa kuwa na kituo cha kipekee nchini cha kuwapa huduma za afya wagonjwa wenye akili taahira wanaokabiliana na janga la corona.

Lakini huku serikali ikijitayarisha kwa ufunguzi wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu, serikali ya Gavana Joho itatakiwa kutafuta suluhu ya sehemu itawapeleka wagonjwa wa corona.

Kamishna wa Mombasa ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa kamati ya kukabiliana na janga hilo kaunti hiyo Bw Gilbert Kitiyo aliwahakikishia wanafunzi wa vyuo hivyo na wahadhiri kwamba sehemu zilizotumika kama vituo vya kuhifadhi wagonjwa vitanyunyuziwa dawa maalum. ili kuhakikisha usalama wao.

‘Tumewaandikia barua serikali ya kaunti ya Mombasa kuhamisha kituo chao kilichoko pale chuo kikuu na kile cha ufundi ili tuanze matayarisho ya ufunguzi wa vuo hivyo mnamo Septemba. Hata hivyo tutanyunyuzia sehemu hizo dawa, kufanya marekebisho kabambe kabla ya kufungua. Tutachukua tahadhari zote,’ alisema Bw Kitiyo.

Aprili mwaka huu gavana wa Mombasa Hassan Joho alizindua rasmi kituo hicho cha kuwatibu wagonjwa ambao si mahututi.

Hata hivyo kwenye mahojiano na kituo cha radio hivi majuzi, afisa wa afya Dkt Khadija Shikely alisema serikali ya kaunti imeanza kuweka mikakati ya kutafuta sehemu mbadala ya kuwahamisha kituo hicho.

“Tunaanza kuweka mikakati ya kutafuta sehemu mbadala lakini tunaona hospitali ya Port Reitz ikiwa mwafaka,” alisema Dkt Shikely.

Joho na Junet waendea ‘Baba’ Dubai

Na VALENTINE OBARA

WAFUASI wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, sasa wana matumaini kwamba hatimaye kiongozi huyo atarejea nchini hivi karibuni.

Hii ni baada ya Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, kufunga safari jana kuelekea Dubai ambako Bw Odinga alifanyiwa upasuaji majuzi.

Tangu wiki iliyopita, wafuasi wa Bw Odinga wamekuwa wakisubiri kwa hamu habari za kurudi kwake nyumbani, huku duru zikisema chama chake cha ODM kinajiandaa kumkaribisha nchini ‘kifalme’.

Matumaini yalianza kuongezeka wakati bintiye, Bi Winnie Odinga, alipotoa video iliyomwonyesha balozi huyo wa miundomsingi wa Muungano wa Afrika (AU) akiwa mchangamfu.

Mkewe, Bi Ida Odinga pia alithibitisha wiki iliyopita kwamba, mumewe anaendelea vyema na anatarajiwa kurudi nyumbani wakati wowote sasa.

Bw Joho na Bw Mohamed jana walitangaza safari yao kupitia mitandao ya kijamii.

Walipigwa picha wakiondoka katika uwanja wa ndege, na baadaye wakiwa ndani ya ndege ya kifahari ambayo haijabainika iligharimiwa na nani.

Kwa mujibu wa kampuni za kukodisha ndege, aina hiyo ya ndege ya Airbus 318 hugharibu takriban Sh500,000 kukodisha kwa saa moja pekee.

Pia, haikujulikana jinsi wawili hao waliidhinishwa kuondoka nchini ilhali kungali kuna marufuku ya safari za ndege isipokuwa za mizigo na masuala ya dharura.

“Tunaelekea Dubai na Junet Mohamed kumwona Baba,” akasema Bw Joho bila kutoa maelezo zaidi.

Tovuti ya kufuatilia safari za ndege ya FlightRadar24 ilionyesha ndege hiyo ilitoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi saa sita na dakika 45 mchana.

Ufahari wake unadhihirika kwa maelezo kuihusu, kwani ina vyumba mbalimbali vya kifahari kama vile chumba cha kubarizi, chumba cha kutumiwa na watu mashuhuri (VIP), chumba cha kulala na afisi ya kibinafsi.

Sehemu zote zimeundwa kwa vifaa vya gharama ya juu.

Bw Odinga alienda Dubai mwishoni mwa mwezi uliopita kufanyiwa upasuaji mguuni, kwa mujibu wa familia yake.

Kutokana na safari hiyo, jopo lililobuniwa kukusanya maoni kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) halijafanikiwa kuwasilisha ripoti yake iliyokamilika mwishoni mwa Juni kwa kuwa wanafaa kuiwasilisha kwa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Safari hiyo ya Bw Odinga pia imeibua mdahalo miongoni mwa wataalamu wa siasa za kimataifa, ikidaiwa huenda anafuatilia masuala kuhusu uhuru wa Somaliland.

Taifa hilo lililojitenga kutoka kwa Somalia limekamia kutambuliwa rasmi kuwa nchi huru kimataifa, hasa kwa Milki ya Kiarabu (UAE). Bw Odinga kwa miaka mingi amekuwa akitetea wazo hilo la kujipatia uhuru.

Mjadala kuhusu nia yake halisi ya kuendelea kukaa Dubai licha ya kutangaza amepona, ulizidi baada ya Bw Mohamed, ambaye ni mwandani wake wa kisiasa, kuzuru Somaliland siku chache zilizopita.

Duru zilisema kuwa, Bw Odinga anatarajiwa kutembelea nchi hiyo hivi karibuni. Haijabainika kama amepanga kuelekea huko moja kwa moja akitoka Dubai, au atakuja Kenya kwanza.

Hayo yalitokea huku pia ripoti zikisema Chama cha ODM kimepanga kuwasilisha hoja bungeni ili Kenya itambue Somaliland kama nchi huru.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya kidiplomasia wanasema hatua hiyo itakuwa hatari kwani inaweza kuchochea zaidi uhasama kati ya Kenya na Somalia. Vile vile, itakuwa kinyume na matakwa ya sheria za kimataifa kwa Kenya kutambua nchi iliyojitenga kutoka kwa nyingine kama taifa huru.

“Kenya haiwezi kukosa busara hadi itambue nchi ambayo ilizaliwa kwa kujitenga na nyingine,” wakili Ahmednassir Abdulahi ambaye ni mmoja wa wanaofuatilia kwa karibu siasa za Somalia, akasema.