Shoka la Uhuru latua Mlima Kenya

BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

WASHIRIKA wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya, wameingiwa na tumbojoto kufuatia ripoti kuwa shoka la Rais Uhuru Kenyatta sasa linaelekezwa kwao.

Hii ni baada ya kubainika kuwa Rais ameamua kuwazima wanachama wa kundi la ‘Tangatanga’ kwa kuwataka wapigakura kuwafuta kazi.

Mapema wiki hii Rais Kenyatta aliwaondoa wanachama wa kundi hilo, Kipchumba Murkomen na Susan Kihika kutoka nyadhifa za Kiongozi wa Wengi na Kiranja wa Jubilee katika seneti.

Tayari, kama hatua ya kudhihirishia Tangatanga kwamba chuma chao ki motoni, chama hicho kimeanza utaratibu wa kuwaadhibu maseneta watano maalumu waliosusia mkutano ulioandaliwa na Rais katika Ikulu ya Nairobi ambapo ajenda ilikuwa kuwatimua Bw Murkomen na Bi Kihika. Maseneta hao Millicent Omanga, Iman Falhada Dekow, Waqo Naomi Jillo, Prengei Victor na Mary Seneta wanakabiliwa na hatari ya kupokonywa nyadhifa zao kwa kumkaidi Rais.

Duru katika chama hicho zinasema kwamba, Rais Kenyatta anaelekeza shoka lake kwa viongozi waliochaguliwa katika ngome yake ya Mlima Kenya, hasa wabunge, magavana na maseneta ambao wamekuwa wakimkaidi na kumdharau.

Miongoni mwa wabunge ambao wameonekana kuwa mstari wa mbele kumkaidi Rais ni Moses Kuria (Gatundu Kusini), Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira), Alice Wahome (Kandara), Purity Ngirici (Mwakilishi wa Wanawake Kirinyaga), Mithika Linturi (Seneta, Meru) na Kimani Ichung’wah (Kikuyu).

Mnamo Jumatano, katibu mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Raphael Tuju alinukuliwa akisema kwamba, chama hicho kitatangaza majina ya wabunge kinachotaka wapiga kura wawatimue.

“Hivi karibuni tutatoa majina yao. Wale ambao wamekuwa wakimdharau na kumtusi Rais ni miongoni mwa wanaolengwa. Mambo yamebadilika,” Bw Tuju alisema.

Rais Kenyatta ambaye amekuwa akionya viongozi kutoka Mlima Kenya wakome kumtusi, anatarajiwa kuongoza kampeni ya kuhimiza wapigakura kuwatimua.

Hata hivyo, ingawa Katiba inaruhusu wapigakura kuwafuta wabunge, mchakato huo ni mrefu na haujawahi kufanyika tangu Katiba mpya ipitishwe 2010. Vyama vya kisiasa pia vimeshindwa kuwatimua waasi.

Kulingana na sehemu ya 45 na 46 ya sheria ya uchaguzi, mtu au watu wakitaka kumtimua mbunge, ni lazima waungwe mkono na asilimia 30 ya wapigakura waliosajiliwa katika eneobunge analowakilisha wakiwemo asilimia 15 ya wapigakura wa kila wadi katika eneo hilo.

Alhamisi, mmoja wa wanaoegemea kundi la ‘Tangatanga’ alisema ana habari kwamba analengwa kwa sababu ya msimamo wake wa kisiasa.

“Sio siri kwamba tumekasirisha watu kwa misimamo yetu na wanatulenga kwa kila mbinu. Ninachojua ni kwamba, demokrasia katika chama chetu imefifia na tutakabiliana na kila hali,” alisema mbunge huyo aliyeomba tusitaje jina lake.

Duru zetu ndani ya Jubilee zilituarifu kuwa, Rais Kenyatta anataka kuwaonyesha makali yake.

Kulingana na Bw Tuju, chama cha Jubilee kitafuata sheria kuwaadhibu waasi.

Wabunge wanaotimuliwa na vyama vya kisiasa wamekuwa wakikimbia kortini na kupata afueni.

Wakati huo huo, wabunge wanawake, wanachama wa vuguvugu la ‘Inua Mama Jenga Jamii’, sasa wanawataka maseneta watano maalumu walioagizwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama cha Jubilee kukaidi agizo hilo.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome wandani hawa wa Naibu Rais William Ruto, wamewataka maseneta hao kuelekea kortini wakisema hawatapata haki mbele ya kamati hiyo.

“Tunawataka wenzetu walioandikiwa barua na Tuju (Raphael) wasijipeleke kwa kamati hii ambayo ni ‘mahakama bandia’ kwani hawatapata haki. Waende kortini kwa sababu tayari hatima yao imeamuliwa,” Bi Wahome aliwaambia wanahabari katika majengo ya bunge huku akiandamana na wenzake 11.

Bi Wahome alitoa mfano wa mwenzao wa Kilifi, Bi Aisha Jumwa, ambaye alikuwepo Alhamisi, aliokolewa na mahakama baada ya kufurushwa na ODM mwaka 2019.

Murkomen asema habanduki Jubilee

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen ameshikilia hatobanduka chama cha Jubilee na kusema ataendelea kuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Akiongea saa chache baada ya kupokonywa rasmi wadhifa wa kiongozi wa wengi na kumlaumu vikali Rais Kenyatta kwa hilo, Bw Murkomen alisema halaumu yeyote kwa masaibu yake.

“Silaumu yeyote kwa kuondolewa kama kiongozi wa wengi katika seneti na sitaondoka Jubilee kwa sababu hiyo. Nitapambana mle ndani huku nikiendelea kutelekeza wajibu wangu wa kuikosoa serikali na kutetea ugatuzi,” Bw Murkomen amesema alipohojiwa na runinga ya Citizen Jumanne usiku.

“Na kwa kuikosoa serikali haimaanishi siwaungi mkono Rais na naibu wake bali ninachofanya ni kuwasaidia wawajibikie raia. Nimemuunga mkono Rais Kenyatta katika chaguzi za urais mara nne, tangu 2002. Na bado nitaendelea kuunga mkono serikali yake,” akaongeza.

Lakini awali katika seneti, Bw Murkomen alichemka kwa hasira huku akimrushia Rais cheche za lawama kwa kushinikiza mapinduzi dhidi yake.

“Ikiwa mafanikio makubwa ya Rais wa Kenya ni kuwaonyesha wananchi kwamba ‘nimemwondoa kiongozi wa wengi na kweli mimi ni mkubwa’ hiyo haina maana. Bw Spika tayari Rais ni mtu mkubwa lakini mimi ni mtoto wa skwota kutoka Embubut.

“Sasa mnamo wakati ambapo Murkomen si kizingiti, ewe Rais, wafanyie kazi wananchi wa Kenya. Na ukome kuwahadaa Wakenya kuhusu ahadi ulizotoa. Sasa sitakuwa kizingiti, rejesha katika bunge hili miswada yote uliyotia saini kinyume cha Katiba,” Murkomen akafoka.

Kuhusu migawanyiko iliyoko ndani ya Jubilee, seneta huyo amesema hali hiyo inachochewa na wanasiasa wachache pekee.

“Shida katika Jubilee inasababishwa na wafulani wachache, sio familia nzima ya wanachama ambao bado wako pamoja kama zamani. Wanasiasa hao wenye nia mbaya ndio wanawagawanya wanachama na viongozi,” Murkomen akasema.

Amesema amezungumza na Dkt Ruto kuhusu yaliyompata lakini “akaniambia nivumilie tu”.

“Naibu Rais aliniamba yaliyompata yeye na Rais Kenyatta wakati ule ambapo walipelekwa katika mahakama ya ICC ndiyo yaliyokuwa mabaya zaidi. Alisema haya ya seneti ni mambo madogo ambayo hayafai kunikosesha usingizi,” Murkomen akaeleza.

Hata hivyo, alisema kulingana na sheria za seneti angali “kiongozi wa wengi” kwa sababu taratibu za kisheria hazikufuatwa wakati wa kung’atuliwa kwake.

Katika mabadiliko yaliyofanywa wakati wa mkutano wa maseneta wa Jubilee na Kanu katika Ikulu Jumatatu, Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio alipewa wadhifa wa kiongozi wa wengi. Nafasi ya kiranja wa wengi – mnadhimu – ilimwendea Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata baada ya Susan Kihika (Nakuru) kutemwa.

Sasa maseneta 22 wamwandikia Lusaka kupinga kutimuliwa kwa Murkomen na Kihika

Na CHARLES WASONGA

MASENETA 22 wa Jubilee wamemwandikia barua Spika wa Seneti Kenneth Lusaka wakipinga mabadiliko yaliyotekelezwa kwa uongozi wa chama hicho.

Wakiongozwa na Kipchumba Murkomen, aliyepoteza wadhifa wake wa kiongozi wa wengi, viongozi hao pia wamepinga muungano mpya uliobuniwa kati ya chama hicho na Kanu wakisema sio halali kwa sababu haujaidhinishwa na Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama hicho inavyohitajika na Katiba yake.

Maseneta hao wamesema Jumatatu kuondolewa kwa Bw Murkomen na Bi Susan Kihika kutoka nyadhifa zao za Kiongozi wa Wengi na Kiranja wa Wengi, mtawalia, kulifanyika kinyume cha sheria za Seneti nambari 19.

Kulingana na sheria hiyo, mabadiliko kama hayo sharti yaungwe mkono na nusu ya maseneta wanaohudhuria kikao ambako mabadiliko hayo yalifanywa.

Hii ina maana kuwa masenata 18 kati ya maseneta 35 wanafaa kupiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwa wawili hao.

Kulingana na taarifa kutoka Ikulu, mkutano ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta ulihudhuriwa na maseneta 20.

Lakini haijulikani kama wote waliunga mkono mabadiliko hayo au kuna wale waliopinga.

“Tunamweleza Rais kuwa hawezi kuongoza taifa hili kupitia ulaghai. Huwezi kughushi sahihi za wenzetu. Helikopta nne zimetumwa kuwasafirisha baadhi ya maseneta ambao sahihi zao ziliigizwa na kuingizwa kwa njia haramu,” Murkomen akaambia wanahabari baada ya kuvuliwa wadhifa wake.

Barua ambayo aliandikiwa Spika Lusaka imetiwa sahihi na; Bw Murkomen, Bi Kihika, Araon Cheruiyot (Kericho), Millicent Omanga (Seneta Maalum), Samson Cherargei (Nandi), Christopher Langat (Bomet), Michael Mbito (Trans Nzoia), Mahamud Mohamed (Mandera) , Juma Wario (Tana River), Mary Senata (Seneta Maalum), Phillip Mpaayei (Seneta Maalum), Alice Milgos, Victor Prengei (Seneta Maalum, Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Mithika Linturi (Meru), Stephen Lelegwe, Margaret Kamar (Uasin Gishu), Iman Falhada, Naomi Waqo (Seneta Maalum), Anwar Loitiptip (Lamu), John Kinyua (Laikipia) na Christine Wawudi (Seneta Maalum).

Maseneta hao sasa wanadai kuwa hawakupokea mwaliko rasmi kwa mkutano huo ambao ajenda yake kuu ilikuwa ni kuondolewa kwa Murkomen na Bi Kihika.

“Kama maseneta wa Jubilee, hatukupokea mwaliko kwa mkutano wowote wenye ajenda ya kujadili kuondolewa kwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti na Kiranja wa Wengi katika Seneti,” barua hiyo inasema.

Wamesuta sehemu fulani ya uongozi wa Jubilee kwa kujaribu kubuni mirengo ndani ya chama hicho kupitia mabadiliko haramu.

Muungano wa Jubilee na Kanu unalenga kumwondoa Murkomen katika wadhifa wake?

Na CHARLES WASONGA

DURU zinasema huenda mkutano wa maseneta wa Jubilee ambao Rais Uhuru Kenyatta ameitisha katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu utatumiwa kutekeleza mabadiliko katika uongozi wa Seneti, miongoni mwa masuala mengine kuhusu chama hicho.

Wanaolengwa kuvuliwa nyadhifa zao ni Kiongozi wa Wengi Kipchumba Murkomen na Kiranja wa Wengi Susan Kihika ambao wameondokea kuwa ‘wakaidi’ kwa Rais Kenyatta.

Inasemekana kuwa nafasi ya Bw Murkomen huenda ikapewa Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi au Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio.

Na kiti cha Bi Kihika ambaye ni Seneta wa Nakuru huenda kikamwendea Naibu wake Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a.

Haya yanajiri siku ambapo iliripotiwa kuwa chama cha Kanu kimetia saini mkataba wa kubuni muungano wa baada ya uchaguzi na chama tawala cha Jubilee.

Hatua hiyo sasa inamaanisha kuwa maseneta wa Kanu, Mbw Moi, Poghisio na Bi Abishiro Halakhe (Seneta Maalum) watakuwa huru kuhudhuria mkutano wa kundi la maseneta wa Jubilee Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi.

Kulingana na stakabadhi zilizosambazwa mitandaoni na mwandani wa Naibu Rais William Ruto, mwanablogu Dennis Itumbi, stakabadhi za muafaka huo ziliwasilishwa kwa afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (RPP) Anne Nderitu.

Hati hiyo imetiwa saini na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju na mwenzake wa Kanu Nick Salat pamoja na mwenyekiti Seneta Moi (Kanu) na mwenzake Nelson Dzuya.

Hata hivyo, huenda wandani wa Dkt Ruto wanapinga muafaka huo wa muungano kati ya Kanu na Jubilee kwa kuutaja kama unaokiuka Katiba ya chama hicho tawala.

Kulingana na kipenge cha 32 cha Katiba ya Jubilee sharti Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ikutane kuidhinisha pendekezo lolote la kubuniwa kwa muungano na chama chochote cha kisiasa baada ya uchaguzi.

JUBILEE: Tuju athibitisha kikao cha Rais Kenyatta na maseneta Ikuluni Jumatatu

Na CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amethibitisha kuwa maseneta wa chama hicho wamealikwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa mkutano katika Ikulu ya Nairobi, Jumatatu, Mei 11, 2020.

Hatua hiyo inajiri baada ya wabunge na maseneta wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto kuwa katika malumbano ya mara kwa mara na wenzao wanaoegemea mrengo wa Rais Kenyatta.

Kimsingi, uhusiano wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto haujakuwa mzuri na wa karibu katika siku za hivi karibuni kwani wawili hao hawajakuwa wakionekana pamoja kwa kipindi kirefu.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimshinikiza Rais Kenyatta aitishe mkutano wa Kundi la Wabunge (PG) wa Jubilee ili kujadili masuala ambayo yamekuwa yakileta mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala.

Bw Tuju amenukuliwa akisema kuwa suala kuu ambalo litajadiliwa ni kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu ya Kaunti ya Nairobi hadi Serikali Kuu, ambalo limezua utata.

“Hii ndiyo sababu Rais amewaalika maseneta pekee wala sio wajumbe wa Bunge la Kitaifa, kwani maseneta ndio hushughulikia masuala ya ugatuzi,” amesema Bw Tuju.

Hata hivyo, Katibu huyu Mkuu amefafanua kuwa mwaliko wa mkutano huo ulitoka moja kwa moja kwa Rais Kenyatta na “hivyo siwezi kuelezea mengi kuhusu ajenda yake.”

Mkutano huo unatarajiwa kuanza saa mbili na nusu asubuhi.

“Mnavyojua ni kwamba ni Rais mwenyewe aliyewaalika maseneta. Kwa hivyo, siwezi kutoa mwelekeo kuhusu masuala yatakayojadiliwa. Lakini kila ninachofahamu ni kwamba hali katika Kaunti ya Nairobi itajadiliwa kutokana na shida ambazo zimeizonga tangu kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu kwa serikali kuu,” Tuju ameeleza.

Nairobi

Ingawa amehiari kuachilia majukumu manne makuu ya kaunti hiyo yaendeshwa na Serikali Kuu kwa kutia saini muafaka wa kufanikisha hilo Februari 2020 Gavana Mike Sonko alibadili msimamo juzi.

Anadai Serikali Kuu ilivuka mipaka na kutaka kusimamia hata yale majukumu ambayo yalifaa kusalia chini ya usimamizi wa serikali yake.

Kwa hivyo, ametisha kusambaratisha shughuli katika Kaunti hiyo kwa kujiondoa kutoka muafaka huo.

Hii ndiyo maana Aprili, Sonko alidinda kutia saini mswada ambao ulipendekeza Sh15 bilioni zitengewe mamlaka ya Nairobi Metropolitan Services (NMS) iliyobuniwa na Rais Kenyatta kuendesha majukumu hayo kwa niaba ya Serikali Kuu.

Hatua hiyo ilichangia mgongano kati yake na Ikulu na kuchangia kuondolewa kwa walinzi wake na baadhi ya madereva waliokuwa wakimhudumia.

Maseneta wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kipchumba Murkomen pia wamepinga hatua ya Serikali Kuu kuwapeleka wanajeshi kusimamia NMS.

Afisi hiyo inaongozwa na Meja Jenerali Mstaafu Mohammed Badi kama Mkurugenzi Mkuu. Na majuzi Serikali Kuu iliwatuma maafisa wanne zaidi katika makao makuu ya kaunti ya Nairobi, City Hall.

Mkutano wa mwisho wa PG wa Jubilee ulifanyika mnamo 2017 baada ya Rais Kenyatta kushinda uchaguzi na kuanza kipindi chake cha pili na cha mwisho. Ni katika mkutano huo ambapo wenyeviti na manaibu wenyeviti wa kamati za bunge la kitaifa na seneti waliteuliwa.

Uhuru aundiwa chama kipya?

Na WANDERI KAMAU

IMEIBUKA kwamba mabwanyenye katika eneo la Mlima Kenya wanapanga kukitumia chama cha PNU kuwa “dau mpya” la eneo hilo kwenye uchaguzi wa 2022, ikiwa Chama cha Jubilee (JP) kitasambaratika.

Wadadisi pia wanataja hilo kama mkakati wa Rais Uhuru Kenyatta “kumnyang’anya” Naibu Rais William Ruto udhibiti wa kisiasa katika eneo hilo, ambalo ni ngome yake.

Duru zinaeleza kuwa mipango ya kukibadili jina chama hicho kuwa The National Unity Party (TNU) tayari iko karibu kukamilika na usajili wake rasmi kukabidhiwa Afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa.

Kulingana na ripoti, mabwanyenye hao walikutana katika hoteli moja viungani mwa jiji la Nairobi wiki iliyopita, ambako mchango mfupi wa kufadhili shughuli za chama hicho kipya ulifanyika.

Baadhi ya viongozi wakuu serikalini waliohudhuria ni Waziri wa Kilimo Peter Munya, kwani ndiye amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa sasa.

Na kutokana na hatua hiyo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa huenda hilo likawa mojawapo ya hatua za kichinichini za Rais Kenyatta na waandani wake wa karibu kisiasa katika Chama cha Jubilee (JP) kubuni mkakati watakaofuata kisiasa, ikiwa mustakabali na uthabiti wa JP utaendelea kuyumba kama ilivyo sasa.

Vilevile, wanataja hali hiyo kama “plan B” ya Rais kwenye mpango wa kubuni muungano wa kisiasa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, Seneta Gideon Moi katika Kanu miongoni mwa wanasiasa wengine.

Kulingana na Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, huenda isiwe furaha ya Rais Kenyatta kubuni muungano huo chini ya mazingira ya mafarakano na hali ya kutoelewana kama ilivyo sasa katika Jubilee.

“Si kwamba Rais Kenyatta hashuhudii wala hafuatilii yanayoendelea katika Jubilee. Yeye ni mwanasiasa, ambaye licha ya muda wake kuhudumu kukaribia kuisha, lazima atazame mbele kwa kubuni mazingira, ambapo yeye, familia yake na washirika wake kisiasa watakuwa salama chini yake,” asema Prof Munene.

Wadadisi wanaeleza kuwa kwa kuwashirikisha tena mabwanyenye na watu maarufu kwenye usajili mpya wa PNU, viongozi wakuu katika Mlima Kenya, akiwemo Rais Kenyatta, wanalenga kuanza kukinadi kama “dau” litakalotumika na eneo hilo kufanikisha mipango ya kubuni muungano wa kisiasa na Odinga, Moi miongoni mwa viongozi wengine.

Wanataja hilo kama njia ya pekee kwa Rais Kenyatta kuchukua mwelekeo mpya kisiasa, ikiwa “itakuwa vigumu kwake kutwaa udhibiti” wa Jubilee kutoka kwa Dkt Ruto na waandani wake kisiasa.

Kumekuwa na makabiliano makali kati ya waandani wa Rais na Dkt Ruto kuhusu udhibiti wa Jubilee, pande zote zikiapa kufanya kila ziwezalo “kutetea maslahi yao chamani.”

Waandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimlaumu Katibu Mkuu, Bw Raphael Tuju na Naibu Mwenyekiti, Bw David Murathe, kwa kuendesha njama za kichinichini kumwondoa Dkt Ruto kwenye udhibiti wa chama hicho.

Na kama Rais Kenyatta, Dkt Ruto pia ameripotiwa kubuni vyama viwili vya siasa, ikiwa atapoteza udhibiti wa Jubilee.

Lakini kufuatia uzinduzi mpya wa PNU, wadadisi wanatilia shaka ikiwa juhudi hizo zitafaulu kufuta dhana ya usaliti wa Dkt Ruto na wandani wa Rais Kenyatta katika eneo hilo.

Hili ni kutokana na mpenyo mkubwa ambao alikuwa amefanya, kabla ya kuzuka kwa janga la virusi vya corona, ambalo limesambaratisha shughuli nyingi za kisiasa nchini.

Wadadisi wanasema kuwa ingawa huo ni mpango mzuri kwa Rais Kenyatta, idadi kubwa ya wakazi bado inaona njama hizo kama mpango wa wazi kumsaliti kisiasa Dkt Ruto.

Wanasema kuwa ni sababu hiyo ambapo huenda iwe vigumu kukiuza upya chama hicho, ikiwa baadhi ya viongozi wanaoonekana “kumpiga vita” Dkt Ruto kama Mabwana Murathe na Tuju watakuwa sehemu ya muundo mpya wa TNU.

“Ikiwa Jubilee hatimaye itasambaratika na TNU kuonekana kama chama kipya kitakachookoa jahazi Mlima Kenya, basi lazima viongozi wa zamani katika Jubilee kama Bw Murathe wasionekane hata kidogo. Hii ni kwa kuwa itafasiriwa kuwa wao ni mwendelezo tu wa njama za kumsaliti Ruto kisiasa,” asema Bw Charles Mulira, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Vilevile, uwepo wa vyama vya kisiasa kama Transformation National Party (TNAP) na The Service Party (TSP) vinavyohusishwa na mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini) na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri mtawalia, pia unatajwa kuwa hali itakayowapa waandani wa Rais Kenyatta ugumu kukiuza chama hicho kipya.

Wawili hao ni waandani wa karibu wa Dkt Ruto na wamekuwa miongoni mwa watetezi wake wakuu Mlimani.

Vyama hivyo vilisajiliwa mapema mwaka huu na tayari vimeanza kuwasajili wanachama na kufungua matawi katika sehemu mbalimbali nchini.

Hata hivyo, baadhi ya watetezi wa Rais Kenyatta wanasema kuwa yeye ni mwanasiasa mwenye tajriba, na haitakuwa mara yake ya kwanza kuacha chama na kubuni safari yake huru kisiasa.

“Rais Kenyatta aliacha Kanu na kubuni TNA mnamo 2012 na kushinda urais mnamo 2013, licha ya masaibu yaliyomwandama kama mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Hivyo, huu ni mtihani rahisi kwake,” asema mbunge wa Kieni, Kanini Keega, ambaye ni mojawapo ya watetezi sugu wa Rais.

Viongozi wa Jubilee wakashifu Murathe na Tuju

Na GITONGA MARETE

VIONGOZI wa Chama cha Jubilee kutoka Kaunti ya Meru ambao ni wandani wa Naibu Rais, Dkt William Ruto wameapa kwamba watapigana vikali kudhibiti chama hicho ambacho kwa sasa kinakumbwa na mzozo wa uongozi kati ya mirengo miwili pinzani.

Wanasiasa hao pia walimshutumu Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju na Naibu Mwenyekiti David Murathe kwa kuendesha chama hicho kama mali yao ya kibinafsi.

Kiini cha mzozo wa Jubilee ni uhasama kati ya mrengo wa Dkt Ruto na Mabw Tuju na Murathe ambao wanaaminika kuwa na ‘baraka’ za Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Tuju hivi majuzi alimwandikia msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu akipendekeza maafisa wa chama wabadilishwe na hata kutoa orodha ya washikilizi wapya wa nyadhifa chamani lakini suala hilo likapingwa na wafuasi wa Dkt Ruto.

Upande wa Naibu Rais ulisisitiza kuwa hakuna mkutano wa Baraza Kuu la Chama ulioidhinisha mabadiliko aliyoyapendekeza Bw Tuju.

Seneta wa Meru Mithika Linturi ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa kundi la wabunge wa Kaunti ya Meru, jana alisema wamewekeza sana na kuunga chama hicho tangu kiundwe ndiyo maana hawatakubali kinyakuliwe na mrengo unaopinga Dkt Ruto.

Bw Linturi aliahidi kwamba watatumia njia zote kusalia na chama hicho ikiwemo kuelekea mahakamani kupinga juhudi zozote za kukibinafsisha kwa wanaoegemea mrengo wa Rais Kenyatta pekee.

“Tunaendelea kushauriana kuhusu hatua tunayopaswa kuchukua. Binafsi mimi huchanga Sh10,000 kila mwezi kama mwanachama wa Jubilee na hatutawaruhusu Bw Tuju na Bw Murathe kudhibiti chama hiki. Tutapigana vita hivi kwa njia zote hadi tushinde,” akasema Bw Linturi.

“Chama cha Jubilee kina wanachama na hakifai kuendeshwa kama kioski. Ni kama kampuni ambayo wanachama wana hisa isiyofaa kumilikiwi na watu binafsi. Mtu yeyote anayefikiri kwamba atadhibiti chama, anajidanganya bure. Hawana mamlaka ya kufanikisha mabadiliko yoyote na tutasitisha mipango yao liwalo na liwe,” akaongeza.

Wabunge Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) na Kathuri Murungi (Imenti Kusini) nao waliwashutumu wawili hao kwa kujihusisha na siasa wakati ambapo taifa linapigana na janga la virusi vya corona.

Wabunge hao waliwataka wawili hao wakomeshe chuki na uhasama dhidi ya viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto.

Waliwashutumu Bw Tuju na Bw Murathe kwa kumpotosha Rais na kumfanya asimakinikie vita dhidi ya corona ambayo sasa inatishia kuharibu uchumi wa nchi.

Bw Dawood naye alishikilia kwamba kimya cha Rais Kenyatta kuhusu utata unaozingira kubadilishwa kwa maafisa wa chama kinafaa kufasiriwa kwamba upande wa Naibu Rais ndio msema-kweli.

“Naibu kiongozi wa chama chetu ni Dkt Ruto na tunatii kile anachosema. Rais Kenyatta hataki kuhusishwa na siasa za chama kwa sababu anakabiliwa na suala la kutokomeza corona,” akasema Bw Dawood.

Bw Murungi ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la wabunge kutoka Meru, alisema hawatakubali kushiriki siasa wakati huu taifa liko pabaya kutokana na janga la corona na usalama wa kiafya wa raia wake.

“Viongozi wa chama chetu wanafaa kuonyesha uongozi mzuri na kuwajibikia Wakenya. Inasikitisha dunia nzima inaendelea kuhangaishwa na corona ilhali viongozi wetu wanashiriki siasa za chama,” akasema.

Cositany amrukiaTuju vikali katikamzozo wa Jubilee

 Na PATRICK LANG’AT

UBABE ndani ya chama tawala cha Jubilee unaendelea kutokota, Naibu Katibu Mkuu Caleb Kositany akimshutumu Katibu Mkuu Raphael Tuju kuhusiana na mabadiliko aliyolenga kutekeleza kwa maafisa wa kitaifa wanaosimamia chama hicho.

Bw Kositany ambaye pia ni mbunge wa Soy, kwa mara ya pili ndani ya siku tano, alimshambulia Bw Tuju akipuuza taarifa aliyotuma kwa wanachama awali akitoa ufafanuzi kuhusu mabadilko hayo.

Uhasama kati ya Mabw Tuju na Kositany umefasiriwa na wadadisi wa kisiasa kama wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto. Bw Tuju ni mwandani wa Rais huku Bw Kositany akirindimisha ngoma ya Dkt Ruto ya kuingia ikuluni mnamo 2022.

Kupitia taarifa jana, Bw Kositany aliwataka wanachama wa Jubilee kupuuza mabadiliko aliyoyasema yanasukumwa na Bw Tuju pamoja na Mwenyekiti wa Jubilee Nelson Dzuya kutimiza ajenda zao za kibinafsi.

‘Wanachama wa Jubilee wakiwemo viongozi wanafaa wapuuze taarifa zinazotolewa mara kwa mara na Bw Tuju. Jubilee ni chama kinachozingatia demokrasia na wazo la kila mwanachama linathaminiwa,’ akasema Bw Kositany kupitia taarifa kwa wanachama wote.

Mbunge huyo alitoa wito kwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto kutumia mamlaka yao kuitisha kikao cha Kamati ya Kitaifa inayosimamia chama (NMC) akisema Bw Tuju amekataa au hana nia ya kuitisha kikao hicho.

‘Katibu Mkuu amekataa kuandaa mkutano wa NMC na kiongozi wa chama au naibu wake anafaa kuandaa kikao hicho. Hiyo itasaidia kuzima tofauti zinazoibuka ndani ya chama,’ akaongeza.

Mnamo Jumapili, Bw Kositany alikuwa ameamrisha kuwa Jubilee iandae uchaguzi wake baada ya janga la corona kutokomezwa.

Uchaguzi huo utaisaidia chama kuwachagua maafisa wa kudumu kwa kuwa wa sasa walipokezwa nyadhifa hizo 2017 ili wazishikilie kwa muda.

Kwenye mabadiliko aliyoyapendekeza Bw Tuju, maafisa waliotemwa ni Veronica Maina, Fatuma Shukri na Pamela Mutua.

Tuju, ambaye ni mbunge wa zamani wa Rarieda, aliwateua Lucy Nyawira Macharia, Profesa Marete Marangu, Walter Nyambati, Jane Nampaso na James Waweru kujiunga na NMC.

Kwenye taarifa fupi kwa wanachama, Bw Tuju alisema kuwa mabadiliko hayo yalichochewa na barua kutoka kwa Msajili wa Vyama, Bi Ann Nderitu ambaye alitoa mwongozo wa kufuatwa na chama kuandaa uchaguzi wa maafisa wake.

Kura hiyo ilifaa kuandaliwa mnamo Machi lakini ikaahirishwa hadi baadaye kutokana na janga la corona . Hata hivyo, kwenye barua ya jana, Bwa Kositany alisema Bi Maina, Shukri na Mutua hawajawahi kuwa wanachama wa NMC kwa hivyo kuondolewa kwao kulisukumwa na ajenda fiche ya kisiasa.

Aidha, Bw Kositany alipinga kwamba mkutano wa NMC uliandaliwa Februari 10 akisema wakati huo taifa lilikuwa likimwomboleza Rais Mstaafu marehemu Daniel arap Moi.

Wakati huo huo Kiongozi wa Wengi kwenye Bunge la Seneti Kipchumba Murkomen naye anataka maamuzi yote yaliyokuwa yametolewa na Bw Tuju miezi michache iliyopita, yabatilishwe na kuanguliwa upya.

‘Katibu wa Jubilee amekuwa akiendesha chama kama mali yake ya kibinafsi. Niliona barua zikiandikwa kwa mabunge ya kaunti ya Kirinyaga, Nairobi na Kajiado. Tuju alipata mamlaka wapi ya kuandika barua hizo? Kuanzia leo barua yoyote inayoandikwa lazima iidhinishwe na vitengo vyote vya uongozi wa chama,’ akasema.

Wandani wa Ruto wataka uchaguzi

PATRICK LANG’AT na ONYANGO K’ONYANGO

WAFUASI wa Naibu Rais William Ruto sasa wanataka chama cha Jubilee kuandaa uchaguzi punde baada ya virusi vya Covid -19 kumalizika.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu wiki iliyopita alirejesha mgogoro kuhusu mabadiliko ya Kamati ya Usimamizi Nchini (NMC) kwa chama tawala, akikitaka kisuluhishe suala hilo kivyake.

Kambi ya Dkt Ruto sasa inataka kutumia fursa hiyo kuitisha jambo ambalo wamekuwa wakimezea mate kwa muda: Uchaguzi wa maafisa wa chama, mikakati inayoonekana kumlenga Katibu Mkuu Raphael Tuju na naibu mwenyekiti aliyetangaza kujiondoa, Bw David Murathe.

“Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) iliyopo sasa inaweza kuzinduliwa tena kutekeleza majukumu yake na kupanga chaguzi zifanyike punde baada ya janga la Covid-19 kudhibitiwa. Kwetu sisi, inahitaji tu kiongozi wa chama kuunganisha NEC na tutakuwa tayari, hatimaye kutimiza masharti yote ya Katiba,” Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany alieleza Taifa Leo.

Wakiongozwa na Dkt Ruto, aliyetaja mabadiliko hayo kama ya udanganyifu na haramu, watu hao wapatao 350 wanaojumuisha wabunge na maseneta 146, walimwandikia Bi Nderitu barua ya malalamishi, wakiitaka afisi yake kutokubali hatua ya kubadilisha majina hayo.

Mbunge huyo wa Soy, Bw Kositany, anayeegemea mrengo wa Naibu Rais, alisema kundi hilo lililokuwa limelalamika kwa msajili wa vyama, halioni hali ambapo watahitajika kwenda kwa Baraza la Kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa.

“Sioni sababu yoyote itakayofanya mifumo ya vyama kutofanya kazi. Hatuoni haja yoyote ya kubadilisha NMC kwa sasa, tufanye uchaguzi kisha tuketi chini ili kuibadilisha tena,” alisema. Chaguzi za Chama cha Jubilee zilizopangiwa kufanyika mnamo Machi mwaka huu, ziliahirishwa hadi tarehe isiyojulikana kufuatia mkurupuko wa Covid-19.

Kwa Dkt Ruto na wenzake, kuandaliwa kwa chaguzi hizo si hatua muhimu tu katika kuimarisha ngome yao mashinani, lakini mchakato uliocheleweshwa wa kudhibiti maafisa katika chama hicho wanaonekana kumvunjia heshima Naibu Rais.

“Rais apasa kuadhibu wale ameaminia kuendesha chama lakini sasa wanajitahidi kushirikiana na upinzani na matapeli wa kisiasa kuzamisha chama. Wahuni wasio na haya ambao sasa wanapanga kutumia masaibu ya virusi kuangusha chama sawa na jinsi walivyotaka kufanya wakati wa mazishi ya Moi,”

“Ni sharti sasa turejeshe kikamilifu chama kwa wanachama wake. Ni lazima tuwafukuze waharibifu na matapeli wote waliomo ndani waliokuwa na nia ya kusambaratisha chama. “Tuju na wenzake wanapaswa kujua tunawaandama. Tutawapa hiari ya kuondoka na ikiwa hawatabanduka, tutawafurusha,” alisema Mbunge wa Belgut Nelson Koech.

Nilishauriana na wahusika wote Nairobi, adai Tuju

Na COLLINS OMULO

MABADILIKO ya uongozi katika chama cha Jubilee yaliyotangazwa na Katibu Mkuu, Raphael Tuju kwenye Kaunti ya Nairobi, yaliafikiwa kwa kuhusisha pande zote mbili hasimu.

Imebainika kuwa, Rais Uhuru Kenyatta alihusishwa kwenye kila hatua ya kuafikia orodha hiyo, baada ya mgawanyiko kuibuka kati ya madiwani katika Bunge la Kaunti ya Nairobi.

Uhasama kati ya madiwani ulitokana na ubabe wa kisiasa kati ya Gavana Mike Sonko na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Beatrice Elachi

Uhasama huo ulikuwa unaelekea kuchacha zaidi baada ya Bi Elachi kuanza kushirikiana na msimamizi mpya wa jiji, Jenerali Mohammed Badi.

Hali hii ndiyo ilichangia wakuu wa Jubilee kuandaa mikutano miwili wiki hii kutekeleza mabadiliko hayo na kuhakikisha chama kiko thabiti bungeni.

Kwenye mabadilko hayo, aliyekuwa Kiongozi wa Wengi, Abdi Guyo ambaye pia ni diwani wa Matopeni, alirejeshewa wadhifa wake.

Upande uliotofautiana vikali na ule wa Bw Guyo nao ulitunukiwa wadhifa wa kiranja wa wengi huku diwani wa Mihang’o, Bw Paul Kados akitwikwa jukumu hilo.

Bw Guyo sasa atachukua wadhifa wa kiongozi kwa wengi kutoka kwa Mwakilishi wa wadi ya Dandora Area 3, Charles Thuo, huku Bw Kados akichukua wadhifa wake kutoka kwa diwani maalumu June Ndegwa

Diwani wa Dandora Area 1, Peter Wanyoike atakuwa Naibu wa Bw Thuo huku Waithera Chege ambaye ni diwani wa South B, akiteuliwa Naibu wa Bw Kados.

Bw Thuo na Bi Ndegwa wamekuwa madiwani wa Jubilee ambao wamekuwa wakiunga mkono Bi Elachi huku Bw Guyo na Bi Chege wakiegemea upande wa Bw Sonko ambaye alitofautiana na Bi Elachi.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Bw Tuju alisema pande zote hasimu zimekubali kufanya kazi pamoja na walijuzwa kabla ya mabadiliko hayo kukumbatiwa.

“Niliteua maafisa wa kushikilia nyadhifa hizo kwa muda hadi waelewane wenyewe. Tulifahamu kwamba kulikuwa na mirengo mbalimbali ndio maana tukasawazisha nyadhifa hizo miongoni mwa madiwani wa pande zote mbili,” akasema Bw Tuju.

Hata hivyo, inaonekana tofauti hizo hazitaisha hivi karibuni, baada ya Bi Elachi kutotambua uongozi mpya wakati wa kikao maalumu cha bunge hilo Ijumaa wiki jana. Alisema bado hajapokea barua rasmi kutoka kwa uongozi wa Jubilee.

“Kama Spika, sijapokea barua yoyote kutoka kwa Jubilee. Nitatambua mabadiliko hayo baada tu ya kupokea barua rasmi ya chama,” akasema Bi Elachi.

Bi Ndegwa naye alidai baadhi ya wakuu wa Jubilee wanaohudumu Ikuluni, ndio walichochea kuondolewa kwao kutokana na ushirikiano waliouanzisha na Bw Badi.

“Hatukuwa tumemaliza mashauriano kati ya pande zote mbili. Bado tulikuwa tunashauriana na hata Bw Tuju alifahamu hilo. Iwapo hii ndiyo njia ya kutuliza uhasama kati yetu, basi ameiongeza zaidi,” akasema.

Mzozo katika kaunti ya Nairobi unaendelea, huku chama hicho cha Jubilee kikikumbwa na msukosuko, unaotokana na hatua ya Bw Tuju kubadili baadhi ya viongozi.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu, amewaagiza viongozi wa chama hicho waketi chini na kuafikiana kwanza, kabla ya mageuzi hayo kuidhinishwa.

Kufikia Ajenda 4 Kuu za Uhuru ni ndoto – PBO

Na DAVID MWERE

ITAKUWA vigumu Rais Uhuru Kenyatta kutimiza Ajenda zake Nne Kuu kabla ya kuondoka mamlakani 2022 ikiwa serikali itaendelea kutotimiza malengo yake ya ukusanyaji ushuru, Idara ya Bunge inayoshughulikia masuala ya bajeti (PBO) imesema.

Idara hiyo pia iliitaka serikali ya taifa kusitisha miradi ambayo haileti faida kwa taifa hili na itekeleze mageuzi katika mashirika ya serikali.

Katika ripoti yake kuhusu Taarifa ya Sera kuhusu Bajeti (BPS) ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021 iliyowasilishwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti, PBO inasema malengo yaliyowekwa katika bajeti ya 2019/2020 hayatawezwa kutimizwa.

Idara hiyo inaongeza kuwa mipango ambayo imetekelezwa kufikia sasa, haijachochea maendeleo katika sekta ya utengenezaji bidhaa ambayo mchango wake katika uchumi umekuwa ukididimia.

“Kutimizwa kwa ajenda kuhusu usalama wa chakula hakujashughulikiwa ipasavyo kwa sababu uzalishaji wa chakula umekuwa ukididimia, ukubwa wa mashamba unapungua, kati ya masuala mengine,” PBO inasema katika ripoti hiyo kwa anwani ‘Shut Eye Economy’.

Sekta ya chakula inahitaji angalau Sh105.4 bilioni katika bajeti ya 2020/21 lakini ni Sh51.2 katika bejeti zilizotengewa sekta hii kulingana na BPS.

Idara ya serikali ya Nyumba inahitaji ufadhili wa zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya kujenga nyumba za gharama nafuu kufikia mwaka wa 2022.

Hata hivyo, alipofika mbele ya kamati ya Bunge la Kitaifa mnamo Alhamisi wiki hii, Waziri wa Uchukuzi na Miundomsingi James Macharia alitaja ukosefu wa rasilimali za kutosha kama kikwazo kikuu kwa azma ya serikali kutimiza lengo hilo.

Waziri alisema kufikia sasa ni nyumba 228 pekee kati ya 1,370 ambazo zilipasa kuwa zimejengwa katika awamu ya kwanza ya mpango huo.

Naye Waziri wa Fedha Ukur Yatani aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Uchukuzi kwamba kutokana na uhaba wa fedha, serikali haitaweza kutekeleza miradi yote ambayo ilipangiwa katika mwaka wa kifedha 2019/20.

“Hali hii imechangiwa na hali kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) haikufaulu kutimiza kiwango lengwa cha ushuru,” akasema Bw Yatani.

Na kuhusiana na Agenda ya Afya kwa Wote (UHC), Sh11.4 bilioni zimetengwa katika mwaka ujao wa kifedha wa 2020/21. Mgao huo unapasa kuongezwa hadi Sh130.5 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2022/23.

Ripoti ya PBO inapendekeza kuwa mabadiliko katika Hazina ya Bima ya Matibabu (NHIF) ni muhimu katika kufanikishwa kwa ajenda ya Rais Kenyatta ya Afya Kwa Wote.

“Serikali inastahili kufanikisha mageuzi katika NHIF ili asasi hii iweze kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa gharama nafuu,” inasema.

Ripoti ya PBO pia inaisuta serikali ya kitaifa kwa kutohusisha serikali 47 za kaunti katika mpango wake wa uzalishaji wa chakula.

“Rais Uhuru Kenyatta atakuwa na wakati mgumu zaidi kutimiza Ajenda Nne ikiwa serikali haitatimiza malengo ya ukusanyaji mapato,” idara hiyo ikasema.

Baada ya kuapishwa kuingia afisini kwa kipindi cha pili mnamo 2017, Rais Kenyatta alizindua Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Nguzo zake kuu ni; ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, Uzalishaji chakula toshelezi, Afya kwa Wote na ustawishaji wa sekta ya utengenezaji bidhaa.

Nimemjenga Uhuru – Ruto

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto amedai kwamba ndiye aliyemjenga Uhuru Kenyatta kisiasa hadi akafanikiwa kuwa Rais.

Dkt Ruto alisema alimfahamu Bw Kenyatta mnamo 1998 alipotumwa na Rais Mstaafu Daniel Moi kumrai Bw Mark Too kujiuzulu kama mbunge wa kuteuliwa ili kumpa nafasi Bw Kenyatta.

Kwenye mahojiano na runinga ya NTV Alhamisi usiku, Dkt Ruto alisema kuwa, ndiye mwanasiasa pekee aliyejitolea zaidi ili kumjenga Rais Kenyatta kisiasa hadi pale alipofika.

Alisema haikuwa rahisi kumshawishi Bw Too kujiuzulu.

“Ikiwa kuna mwanasiasa aliyejitolea sana kwa manufaa ya Rais Kenyatta, basi ni mimi. Nimesimama naye hata katika nyakati ngumu zaidi. Kwa mfano, haikuwa rahisi kwangu kumrai Bw Too kujiuzulu kama Mbunge Maalum ili kumpa nafasi Bw Kenyatta,” akasema Dkt Ruto.

Alisema mnamo 2002 baada ya Bw Moi kumtangaza Uhuru kuwa mwaniaji urais wa chama cha Kanu, alimuunga mkono licha ya baadhi ya wanasiasa kuondoka na kubuni chama cha Liberal Democratic Movement (LDP).

Baadhi ya wanasiasa walioondoka Kanu kulalamikia hatua ya Bw Moi ni kinara wa ODM Raila Odinga, Prof George Saitoti, William Ole Ntimama, Joseph Kamotho kati ya wengine.

Hata hivyo, Dkt Ruto alisema alimuunga mkono Rais Kenyatta na hata kumfanyia kampeni hadi pale walikubali kushindwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki aliyegombea kwa tiketi ya muungano wa NARC kwenye uchaguzi mkuu wa 2002.

“Tulipoondoka kwenda kuwahutubia wanahabari kukubali kushindwa, tulikuwa zaidi ya watu 60. Hata hivyo, tulipofika kuhutubu, tulikuwa watu watatu pekee; mimi, Rais Kenyatta na mtu mwingine mmoja,” akasema Dkt Ruto.

Kwa mujibu wa Dkt Ruto, mwaka 2012 ndipo walikumbwa na wakati mgumu zaidi, baada ya aliyekuwa Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Moreno Ocampo kuwataja kuwa miongoni mwa watu sita waliohusika kwenye ghasia za baada ya uchaguzi tata wa 2007/2008 ambapo watu zaidi ya 1,000 walipoteza maisha yao.

“Hata baada ya masaibu yaliyotukumba katika ICC, niliendelea kumuunga mkono bila sharti lolote,” akasema.

Alieleza kuwa imani yake kwa uwezo wa Rais Kenyatta ndiyo ilimfanya kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017, bali si kwa tumaini kwamba, Rais angerudisha mkono kwa kumuunga kuwa mrithi wake.

Kauli yake inajiri huku siasa za urithi wa Rais Kenyatta mnamo 2022 zikizidi kushika kasi, ambapo ameonekana kutengwa, hasa baada ya Rais kumkumbatia kinara huyo wa upinzani.

Dkt Ruto amekuwa akikosolewa na baadhi ya wandani wa karibu wa Rais Kenyatta kwa kuwa kikwazo kikuu kwa utendakazi wake, kwa kuendesha kampeni za mapema za 2022. Hata hivyo, alitaja hali hiyo kuwa ya kawaida, ambayo hutokea kila wakati siasa za urithi zinapokaribia, akirejelea urithi wa Mzee Jomo Kenyatta na Bw Kibaki mnamo 1978 na 2012 mtawalia.

Dkt Ruto alisema kuwa hataondoka katika Chama cha Jubilee (JP) hata baada ya uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika mnamo Machi akisema anaamini katika maono, ajenda na malengo yake.

Tuju aonya viongozi fisadi ndani ya Jubilee

Na JUSTUS OCHIENG’

CHAMA cha Jubilee kimetangaza kwamba kitawafungia nje viongozi wanaohusishwa na doa la ufisadi huku kikitarajiwa kuandaa uchaguzi wake mwaka ujao wa 2020.

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema Jumamosi njia pekee ya kuhakikisha vita dhidi ya ufisadi vinaendelezwa jinsi alivyoamrisha Rais Uhuru Kenyatta ni kuhakikisha kwamba washikilizi wa nyadhifa mbalimbali chamani ni watu wasiohusishwa na sakata yoyote ya ufisadi.

Akishiriki mahojiano na ‘Taifa Jumapili’ nyumbani kwake Asembo, eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya, Bw Tuju pia alisema katiba ya chama hicho haivumilii wafisadi na wanachama ambao wanashiriki uozo huo hawatapewa nafasi ya kuwania au kushikilia cheo chochote.

“Huwezi kutetea ufisadi kisha useme wewe ni mwanachama wa Jubilee ilhali manifesto ya chama inaharamisha ufisadi,” akasema Bw Tuju.

Kwa sasa viongozi mashuhuri ndani ya Jubilee wanaendelea kuchunguzwa kuhusiana na sakata mbalimbali za ufisadi na tangazo la Bw Tuju huenda ikazima nia ya baadhi yao ya kuwania vyeo mbalimbali.

Baadhi ya magavana wa Jubilee wanaokabiliwa na ufisadi ni Ferdinand Waititu(Kiambu), Moses Lenolkulal(Samburu) na Mike Mbuvi Sonko(Nairobi).

Wabunge wengi wa Jubilee pia wanakabiliwa na kesi za ufisadi na usemi wa katibu huyo mkuu huenda ikazima ndoto zao za kuwa maafisa wa chama hicho kubwa zaidi nchini.

Mbunge wa Lamu Magharibi Stanley Muthama anachunguzwa kuhusiana na kukwepa kulipa ushuru unaohusisha zaidi ya Sh400 milioni. Mwenzake wa Embakasi Kaskazini James Gakuya naye ameshtakiwa kwa kupokea Sh40 milioni kutoka kwa Hazina ya Kifedha ya Maeneobunge(CDF) kwa kutoa kandarasi za ujenzi wa barabara bila kufuata sheria.

Wabunge Alfred Keter (Nandi Hills), John Waluke (Sirisia), Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi), Ali Rasso (Saku) na Moses Kuria wa Gatundu Kusini pia wanakabiliwa na kesi za ufisadi.

Bw Keter anakabiliwa na kesi ya kughushi stakabadhi na kupokea Sh633 milioni, Bw Arama anakabiliwa na kesi ya kunyakua ardhi ya manispaa ya Nakuru huku Bw Kuria na Bw Rasso wakiwa na kesi za kutoa matamshi ya kueneza chuki.

Bw Rasso anadaiwa kuchochea ghasia kati ya jamii za Borana na Gabra katika Kaunti ya Marsabit huku Bw Kuria akitoa matamshi ya kuzua chuki kisiasa.

Chama cha kitaifa

Aidha Bw Tuju alisema chama hicho ni cha kitaifa kitahakikisha kuna usawa wa kieneo na uwakilishi wa jamii zote kubwa na ndogo nchini wakati wa uchaguzi wake.

Mbunge huyo wa zamani wa Rarieda pia alifichua kwamba Jubilee itajigatua na itakuwa na mshikilizi wa afisi zake katika kila kaunti hata zile ambazo ni ngome za vyama vya upinzani.

“Kwa mujibu wa katiba yetu, chama chetu kina matawi katika magatuzi 47. Lazima uwepo wetu uhisiwe katika kaunti zote kwa mfano Kilifi ambapo chama cha ODM kilishinda viti vyote kuanzia udiwani hadi ubunge. Wajumbe wa jubilee katika eneo hilo pia watakuwa wanathaminiwa jinsi walivyo wenzao kutoka Kiambu ambayo ni ngome ya chama,” akasema Bw Tuju.

Watetezi kimya Jubilee ikitatiza demokrasia, haki

KIMYA cha Wakenya wakati mafanikio ya demokrasia yanapoendelea kutatizwa na utawala wa Jubilee kimezua wasiwasi wa nchi kurudi katika utawala wa kidikteta.

Hii ni baada ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta kuendelea kuhujumu taasisi kuu za kulinda demokrasia zikiwemo bunge, upinzani, mashirika ya kijamii, vyombo vya habari na mahakama.

Baada ya Rais Kenyatta, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kutuliza ushindani wao wa kisiasa na kuanza kushirikiano, Bunge limekuwa kikaragosi cha Serikali Kuu kwa kupitisha kila kitu inachotakiwa kuidhinisha.

Hii ni baada ya wabunge wa upinzani kuanza kupiga ngoma moja na wenzao wa chama tawala cha Jubilee.

Upinzani nao ulizamishwa baada ya handisheki wakati vigogo Odinga wa ODM na Bw Musyoka wa Wiper walipopata vyeo, hali iliyowapofusha kuhusu maslahi ya wananchi ambayo walikuwa wakidai kutetea.

Mashirika ya kijamii nayo yalizimwa kwa sheria kali ambazo zililemaza shughuli zao pamoja na kukosa ufadhili.

Pia baadhi ya wanaharakati waliokuwa wakiegemea upinzani walinyamaza wakati Bw Odinga na Bw Musyoka walipomezwa na Jubilee.

Navyo vyombo vya habari vimelemazwa hasa kifedha kwa kukosa matangazo kutoka kwa serikali na hali ngumu ya kiuchumi ambayo imetatiza mapato ya kuviwezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Kumekuwepo pia na juhudi za kulemaza mahakama kwa kuingilia utendakazi wake na kukoroga bajeti ya idara hiyo.

Wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi ambao ulitatiza demokrasia, mashirika ya kijamii yakiongozwa na wanaharakati machachari yaliungana na vyombo vya habari kumaliza utawala wa chama kimoja na kuweka nchi kwenye mkondo wa kukua kidemokrasia.

Lakini wakati huu ambapo mafanikio hayo yanaendelea kuzimwa na Jubilee pamoja na uchumi kuzorota, hakujakuwa na wanaharakati wa kushinikiza kuheshimiwa kwa demokrasia na haki kwa Wakenya.

Hii ni kinyume na miaka ya tisini ambapo viongozi kama Seneta James Orengo, Prof Anyang Nyong’o, Marehemu Wangari Maathai, Kaasisi Timothy Njoya, Paul Muite, Gitobu Imanyara, aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga, Bw Njeru Kathangu, Bw Koigi wa Wamerere na wakili Gibson Kamau Kuria waliongoza juhudi za kuleta demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa.

Wanaharakati hawa wamekuwa kimya demokrasia waliyopigania ikihujumiwa na Jubilee isipokuwa Bi Martha Karua ambaye amekuwa akisikika akiikosoa serikali.

“Ni Bi Karua pekee ameonyesha msimamo wa kweli kuwatetea wananchi lakini sauti yake pekee haitoshi. Anahitaji usaidizi wa wanaharakati wengine ili kujaza nafasi ya ukosefu wa upinzani nchini,” asema mchanganuzi wa siasa Bw Wycliffe Muga.

Baadhi ya wadadisi wanasema kimya chao kinatokana na umri wao mkubwa na wengine kujiunga na serikali.Pia viongozi wengi walitosheka na kushawishiwa kwa “minofu” waliyopata baada ya kujiunga na serikali.

Wadadisi wanawataja baadhi ya viongozi hao kama wasaliti, hasa baada ya Bw Odinga kujiunga na Rais Kenyatta kwenye handisheki.Wanasema kuwa sauti ya viongozi hao ingekuwa muhimu wakati kama huu Wakenya wanapoteseka.

Hata baada ya wao kuzeeka ama kumezwa na serikali, kumekosekana wanaharakati wachanga wa kuongoza juhudi za kulinda haki na demokrasia.

Ni mwanaharakati Boniface Mwangi pamoja na kikundi cha Haki Afrika kikiongozwa na Hussein Khalid ambao wamesikika wakipinga utawala wa Rais Kenyatta kila mara unapokiuka sheria ama kuchukua hatua za kunyanyasa Wakenya.

Wiper yalambishwa sakafu huku ODM, Jubilee ziking’aa

Na KITAVI MUTUA, CHARLES LWANGA na CHARLES WASONGA

UMAARUFU wa Chama cha Wiper eneo la Ukambani ulitikiswa kiliposhindwa kwenye uchaguzi mdogo wa wadi ya Mutonguni, kaunti ya Kitui na chama cha Maendeleo Chap Chap huku vyama vya ODM na Jubilee vikishinda chaguzi ndogo za udiwani Malindi na Marsabit.

Uchaguzi wa wadi ya Mutonguni uliochukuliwa kama wa kupimana nguvu kati ya viongozi wa vyama hivyo, Kalonzo Musyoka na Alfred Mutua ambao wamekuwa wakipigania ubabe wa kisiasa eneo hilo.

Mhandisi Musee Mati wa Maendeleo Chap Chap (MCC) alizoa kura 2,892 huku mgombeaji wa Wiper Stephen Kithuka akifuata kwa karibu kwa kupata kura 2,147.

Kushindwa kwa Wiper kumesawiriwa kuwa pigo kwa Musyoka ambaye ni kigogo wa siasa katika eneo zima la Ukambani na anatoka kaunti ya Kitui.

Bw Musyoka mwenyewe alifahamu hilo kabla ya uchaguzi huo na ndio maana aliongoza kampeni za kumpigia debe Bw Kithuka akiwasihi wapiga kura wasimwaibishe nyumbani kwa kumkataa mgombeaji wa Wiper.

Chama cha ODM kilishinda uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda kaunti ya Kilifi.

Ushindi wa Reuben Katana umefasiriwa kama pigo kwa mustakabali wa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ambaye ametangaza kuwa atawania ugavana wa Kilifi kwenye uchaguzi Mkuu wa 2022.

Bw Katana alitangazwa mshindi kwa kuzoa kura 4,177 na kumshinda Abdulrahman Mohamed Omar aliyepata kura 2,331.

Bi Jumwa alikuwa akimuunga mkono Bw Mohammed ambaye aliwania kiti hicho kama mgombeaji huru baada ya kugura ODM.

Nacho chama cha Jubilee kilishinda kiti cha udiwani wa wadi ya Loiyangalani, kaunti ya Marsabit katika uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi.

Mgombeaji cha chama hicho tawala Stephen Nakeno alitangazwa mshindi kwa kupata kura 1,522 akifuatwa kwa karibu na Lesiantam Iltele wa Kanu aliyepata kura 1,048.

Mgombeaji wa chama cha Maendeleo Chap Chap Titus Lolmogut Lenguro alikuwa wa tatu kwa kupata kura 663 akifuatia na Tobias Chodow Lenguro wa ODM aliyepata kura 306.

Jubilee yasaliti Kibaki

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI ya Jubilee imemsaliti Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwa kupuuza sera zake za kiuchumi zilizosaidia kuboresha maisha ya mwananchi wa kawaida.

Kutokana na usaliti huo, maisha ya mwananchi wa kawaida yameendelea kuwa magumu kinyume na yalivyokuwa yameimarika wakati wa utawala wa mbunge huyo wa zamani wa Othaya.

Wananchi waliohojiwa na Taifa Leo maeneo mbalimbali ya nchi walieleza kuvunjika moyo kutokana na gharama ya juu ya maisha, ongezeko la umaskini, uhaba wa nafasi za kazi, hali ya kuchanganyikiwa katika sekta ya elimu, huduma duni za hospitali na ukosefu wa mikopo ya kujistawisha kibiashara.

Alipokuwa akikabidhi mamlaka kwa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto mnamo 2013, Mzee Kibaki aliwaambia: “Ninawaachia nchi iliyo tayari kupaa katika ustawi, usawa na umoja. Tunapaswa kulenga darubini yetu katika kujenga Kenya bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”

Deni kubwa

Wadadisi wa masuala ya uchumi na utawala wanasema kwamba badala ya kuendeleza sera za Mzee Kibaki zilizofanya Kenya kufanikiwa kufadhili asilimia 95 ya bajeti bila kutegemea mikopo ghali, serikali ya Jubilee iliamua kutegemea madeni hasa ya kigeni na katika kipindi cha miaka mitano cha utawala wao Kenya ilikuwa ikidaiwa zaidi Sh5.8 trilioni.

Mzee Kibaki alipoondoka madarakani Kenya ilikuwa na deni la Sh1.6 trilioni, ambapo Sh 527 bilioni zilikopwa mashirika ya fedha ya humu nchini.

Mnamo Jumatano, Bunge liliipatia serikali idhini ya kuongeza madeni hadi Sh9 trilioni licha ya mashirika ya wafadhili kuonya kuwa madeni ya Kenya yamevuka mipaka.

Mwanauchumi David Ndii anakosoa sera za serikali ya Jubilee akisema haziwezi kukuza uchumi mbali zinasaidia tu kampuni chache zinazomirikiwa na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Sera za serikali ya Mzee Kibaki zilikuwa halisi na utekelezaji wake ulikuwa ukibainika wazi na zililenga kupunguzia mwananchi wa kawaida gharama ya maisha na kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini.

Mabwanyenye

Wadadisi wanaeleza kuwa kinyume na utawala wa Mzee Kibaki ambao nia yake kuu ilikuwa kusaidia mwananchi wa kawaida, utawala wa Jubilee unajishughulisha zaidi kufaidi mabwanyenye kibiashara.

“Mipango ya maendeleo ya Jubilee huzingatia zaidi ni nani katika serikali ambaye atanufaika kibiashara. Ingawa hata wakati wa Kibaki baadhi ya maafisa wake walikuwa na tabia hii, hali imekuwa mbaya zaidi sasa,” akasema mdadisi mmoja.

Baadhi ya sera za uchumi za serikali ya Jubilee zimerudisha Kenya nyuma huku wawekezaji waliokuwa na imani na nchi hii wakihamia mataifa mengine, tofauti na ilivyokuwa chini ya utawala wa Mzee Kibaki.

Chini ya utawala wa Mzee Kibaki, kampuni zilikuwa zikipata faida kubwa, kupanua shughuli na kuajiri idadi kubwa ya Wakenya. Lakini kwa wakati huu nyingi zinatangaza hasara, kufuta wafanyakazi, kufungwa ama kuhamia mataifa mengine kama Misri, Tanzania na Ethiopia.

Wananchi waliohijiwa na Taifa Leo walisema Jubilee inatoa sera ambazo hazifaidi mwananchi wa kawaida licha ya serikali kushinikiza zitekelezwe.

“Kwa mfano unashangaa nia ya kuagiza mizigo yote isafirishwe kwa SGR. Hii inamaanisha serikali haitujali sisi tuliowekeza katika sekta ya uchukuzi,” akasema mmiliki wa kampuni moja ya mizigo jijini Mombasa.

Kupitia sera za utawala wa Mzee Kibaki, sekta ya fedha ilistawi na benki zikaanza kutoa mikopo nafuu kwa Wakenya wa kawaida kuendeleza biashara.

“Nakumbuka benki zilikuwa zikiwasihi wananchi kuchukua mikopo. Siku hizi ni vigumu sana kwa mwananchi wa kawaida kupata mkopo wa benki,” akasema Anderson Kimani ambaye ni mfanyibiashara Nairobi.

“Hatua hii ilifanya kuwepo kwa pesa nyingi za uzalishaji na biashara, hali ambayo ilichochea ukuaji wa uchumi,” asema mdadisi wa masuala ya uchumi David Kimotho.

Sera bora

Wadadisi wanasema kama serikali ya Jubilee ingeendeleza sera za uchumi za utawala wa Mzee Kibaki, uchumi ungekuwa thabiti zaidi na Kenya haingekuwa na mlima wa madeni.

“Inasikitisha kuwa licha ya utawala wa Mzee Kibaki kupata mafanikio makubwa ya kuboresha maisha ya Wakenya, hatuwasikii viongozi wa Jubilee wakienda kumuomba ushauri,” Janet Mumbua kutoka Kajiado alieleza Taifa Leo kwenye mahojiano.

Ingawa wadadisi wanasema uchumi wa Kenya ulikua vyema katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Jubilee kutoka 2013 hadi 2017, wanasema hii ilikuwa ni matokeo ya sera za Mzee Kibaki.

Chini ya utawala wa Jubilee kodi ziliongezeka na mpya kuanzisha kwa lengo la kupata pesa za kulipa madeni hasa ya China, jambo lililofanya gharama ya maisha kwa mwananchi wa kawaida kupanda.

“Kodi mpya zimechangia mfumko wa gharama ya maisha. Uwezo wa Wakenya wa kununua bidhaa na huduma umepungua tofauti na ilivyokuwa wakati wa utawala wa Mzee Kibaki ambapo sekta kama ya ujenzi ilistawi,” alikiri mwanauchumi mmoja wa serikali.

Wananchi walia

Tofauti na utawala wa Kibaki ambao ulipanua sekta ya elimu kwa kuanzisha elimu bila malipo na kupanua vyuo vikuu nchini, sekta ya elimu kwa sasa inakumbwa na matatizo mengi ikiwemo utekelezaji wa mfumo wa elimu wa CBC.

Japo utafiti wa kubadilisha mfumo wa elimu ulifanywa chini ya utawala wa serikali ya Mzee Kibaki, haikuwa na haraka ya kutekeleza mabadiliko hayo bila kuweka msingi unaohitajika.

Hali ni sawa katika sekta ya kilimo ambapo wakulima wanalia wamepuuzwa.

Alipoingia mamlakani 2003, Mzee Kibaki aliwekeza Sh6.4 bilioni katika sekta ya majanichai na Sh2.5 bilioni sekta ya kahawa ili kuokoa wakulima kutokana na madeni. Hatua hii ilifanya wakulima kupanua kilimo cha majanichai kutoka hektari 131,500 hadi 187,855 kufikia 2011.

Chini ya utawala wa Jubilee wakulima wameanza kung’oa majanichai huku kampuni kubwa zikihamia mataifa jirani ya Afrika Mashariki zikilalamikia sera mbaya na viwango vya juu vya kodi.

Mnamo 2013, serikali iliwanunulia wakulima wa mahindi gunia moja kwa Sh3,000 lakini chini ya utawala wa Jubilee serikali ilitangaza bei ya Sh2,300 kwa gunia la kilo 90 licha ya kuwa gharama za uzalishaji zimepanda tangu 2013.

Hata hivyo Jubilee imeendelea kutekeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na Mzee Kibaki kama SGR, Bandari ya Lamu na ujenzi wa barabara kote nchini. Lakini kumekuwa na malalamiko ya gharama kuongezeka pamoja na kutegemea mikopo ya kigeni kuifadhili.

Tumetumwa na Uhuru kupigia debe ODM Kibra – Kieleweke

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wa Chama cha Jubilee walio katika kundi la Kieleweke wamewataka wakazi wa eneobunge la Kibra kumpigia kura mwaniaji wa ODM Bernard ‘Imran’ Okoth, huku wakidai kwamba anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Mgombeaji wa Jubilee katika uchaguzi huo mdogo ni Bw McDonald Mariga, ambaye wanasiasa hao wanadai anafadhiliwa na ‘maadui’ wa muafaka baina ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Waliongozwa na wabunge Maina Kamanda (Maalumu), Maoka Maore (Igembe Kaskazini), aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi na mbunge wa zamani wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru.

“Mimi ni mbunge maalumu wa chama cha Jubilee na ninaripoti kwa kiongozi wa chama ambaye ni Rais Kenyatta. Siwezi kufanya jambo lolote linalokinzana na kiongozi wa chama. Mkiona ninampigia debe Bw Imran Okoth, mjue yeye ndiye kipenzi cha Rais Kenyatta,” akasema Bw Kamanda aliyekuwa akizungumza katika Kanisa la PCEA, Parokia ya Kibera.

“Imran ndiye mwaniaji wa watu wanaounga handsheki na Mariga ni mwaniaji wa wanaopinga handsheki. Hiyo ndiyo maana hamtaona Rais Kenyatta akija hapa kupigia debe Bw Mariga kwa sababu roho yake iko kwa Imran,” akaongezea.

Hata hivyo, madai hayo hayangethibitishwa kwa njia huru.

Mariga ajipigia debe

Bw Mariga amekuwa akiendeleza kampeni zake Kibra akisaidiwa na wabunge wa Jubilee walio kwenye mrengo wa ‘Tangatanga’ wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Jumapili alikuwa katika maeneo ya Laini Saba ambapo alizidi kuahidi wakazi kwamba akichaguliwa, ataimarisha biashara za vijana na kina mama, na kushirikisha wakazi katika uongozi wake endapo atashinda katika uchaguzi huo wa Novemba 7.

Kwa mara nyingine, Bw Kamanda alidokeza kuwa huenda kukawa na muungano baina ya chama cha ODM na Jubilee kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2022.

“Mnachoona sasa hapa Kibra ndicho kitashuhudiwa 2022, hakutakuwa na chama cha Jubilee wala ODM 2022,” akasema Bw Kamanda.

Bw Maore alisema handisheki baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga imeleta amani na utulivu nchini hivyo wakazi wa Kibra wasiruhusu watu wachache wanaolenga kuvuruga amani kwa masilahi yao ya kibinafsi. Naye Bw Waweru aliwataka wanasiasa wa Jubilee wanaopinga handisheki kujiandaa kuwa katika upinzani 2022.

Kiti cha ubunge wa Kibra kilisalia wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth aliyeaga dunia Julai.

Uchaguzi Mdogo wa Kibra utafanyika Novemba 7.

Sakaja: Ni muhimu kukubali Jubilee haiko kama zamani

Na SAMMY WAWERU

SEPTEMBA  7, 2016, vyama zaidi ya 10 vilivunjiliwa mbali kuunda mrengo tawala kwa sasa wa Jubilee, JP.

Vinajumuisha The National Alliance (TNA) kilichoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, United Republic Party (URP) cha Naibu Rais Dkt William Ruto, Alliance Party of Kenya kilichoanzishwa na gavana wa sasa wa Kaunti ya Meru Kiraitu Murungi na New Ford Kenya cha Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, miongoni mwa vingine.

Mbali na ajenda za maendeleo nchini, viongozi wake wakuu Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto walisema kilipania kuleta umoja, utangamano na uwiano wa kitaifa.

Wakihutubu wakati wa kukizindua rasmi Jumatano, Septemba 7, 2016, walisema JP ni chama cha kitaifa, kilicholeta pamoja makabila yote nchini.

Aidha, walieleza kwamba chini ya utawala wa JP, kila jamii itashirikishwa serikalini.

Ni mrengo huohuo kiongozi wa taifa aliutumia kutetea wadhifa wake kwa awamu ya pili na ya mwisho, na ushawishi wao kwa wapiga ulizaa matunda.

Makubaliano yalikuwa Rais Kenyatta aongoze kiti cha hadhi ya juu zaidi nchini kwa muda wa miaka 10, unaotarajiwa kukamilika 2022, kisha naibu wake Dkt Ruto amrithi chini ya JP.

Katika harakati za kampeni, wawili hao walitambuana kama “ndugu yangu”.

Hata hivyo, kitumbua kinaonekana kuingia mchangani hususan baada ya salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, almaarufu Handshake Machi 9, 2018.

JP imegawanyika na kuunda mirengo miwili, Tangatanga kinachoegemea upande wa Rais na Kielewek cha Naibu wake.

Kufuatia mkondo wa siasa unaoshuhudiwa, aliyekuwa mwenyekiti wa TNA na ambaye kwa sasa ni seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja, anasema umoja wa Jubilee uliokuwepo awali umefifia.

“Hakuna haja tudanganyane, umoja uliokuwepo awali haupo. Ingawa Jubilee haijasambaratika, lakini utangamano tulioshuhudia kabla ya 2017 hauonekani,” anasema Bw Sakaja.

Katika kisa cha hivi majuzi ambapo mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro alikamatwa na kuachiliwa huru kwa kile alidai ni idara ya polisi kutumiwa vibaya na baadhi ya viongozi serikalini.

Kuna mrengo ambao umekuja kutambulika  kama Tangatanga na ambao viongozi wake wanamuumga mkono Ruto.

Pia kuna kundi lingine la Kieleweke linalojiegemeza zaidi kwa Rais.

Nyoro anasema anapigwa vita kisiasa kwa sababu ya kuegemea upande wa Naibu wa Rais Ruto.

“Iwapo ningekuwa na hatia, korti haingeniachilia huru. Mimi si mhalifu, na kamwe sijawahi kushiriki kisa chochote cha uhalifu. Hii ni vita ya kisiasa kwa sababu ninaunga azma ya Dkt William Ruto kuingia Ikulu 2022,” akasema mbunge huyo mapema wiki hii baada ya kuachiliwa huru na mahakama ya Murang’a.

Bw Ndindi alitiwa nguvuni na maafisa wa polisi kwa kudaiwa kusambaratisha mchango wa kanisa moja la Kikatoliki Murang’a uliohudhuriwa na mbunge maalum Maina Kamanda na ambaye ni mfuasi wa Kieleweke.

Seneta Sakaja anasema kujiri kwa Tangatanga na Kieleweke ni suala ambalo hakutarajia lingeibuka ndani ya Jubilee. Anasema changamoto zilizoko ndani ya JP zitatatuliwa na Rais Kenyatta na Naibu wake Dkt Ruto, ambao ndio viongozi wakuu.

Jubilee kukosa pesa za matumizi

Na BRIAN OCHARO

CHAMA cha Jubilee kimo hatarini kukosa fedha za matumizi ikiwa ombi lililowasilishwa kwa Jopo la Kusuluhisha Mizozo ya Chama litakubaliwa.

Afisa wa chama hicho katika Kaunti ya Mombasa, Bw Patrick Kabundu ameomba jopo hilo kutoa amri ya muda inayosimamisha afisi ya msajili kutoa fedha za vyama kwa Chama cha Jubilee hadi kesi yake itakaposikizwa na kuamuliwa.

Mlalamishi huyo alitaka pia amri ya kusimamisha mchango wa kila mwezi wa magavana, wabunge na madiwani wa chama hicho hadi kesi yake ikamilishwe.

Endapo jopo litakubali ombi hilo, huenda shughuli za Jubilee zikaathirika vibaya ikiwemo kufadhili kampeni za chaguzi ndogo zitakazoshiriki katika kipindi cha kesi hiyo.

Wakati huo huo, hatua yake imeashiria mikakati ya kumwondoa Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju katika usimamizi wa chama imeanza kushika kasi.

Bw Kabundu ambaye ni katibu wa chama hicho katika Kaunti ya Mombasa, anasema viongozi wa chama ambao pia ni wafanyakazi wa serikali wamekiuka Kipengele cha 77(2) cha katiba na wanafaa kutolewa katika nyadhifa hizo.

“Viongozi kama hao waliapishwa na kuahidi kuheshimu katiba lakini sasa wanaikiuka. Viongozi wa chama cha Jubilee wamekiuka kipengele hicho kwa kushikilia nyadhifa hizo huku wakiwa wafanyakazi wa serikali,” alisema.

Kipengele 77(2) cha katiba ya Kenya kinasema kuwa yeyote aliyeteuliwa kuhudumu serikalini hafai kushikilia ofisi katika chama cha siasa.

Bw Kabundu ameomba jopo hilo kutoa amri kuwa wale wanaohudumu serikalini waondoke katika nyadhifa za chama kwani wameenda kinyume na katiba.

Ameambia jopo hilo la Bw Kyalo Mbobu, Bi Milly Lwanga na Dkt Adelaide Mbithi kuwa chama cha Jubilee hakifuati katiba ya Kenya na hata ya chama kiusimamizi, na kuwa jopo hilo linahitajika kutoa amri chama hicho kifuate sheria.

“Viongozi wote wa Chama cha Jubilee ni wafanyakazi wa serikali. Hii ni kinyume cha sheria,” akasema.

Jopo hilo limepatia chama hicho kinaochoongozwa na Rais Kenyatta muda wa siku 10 kujibu malalamishi ya Bw Kabundu. Kesi hiyo itasikizwa Septemba 27.

Bw Tuju ambaye ni Waziri asiyesimamia wizara yoyote, amekuwa akikashifiwa na wanachama wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, wanaodai ana ubaguzi.

Hivi majuzi, aligonga vichwa vya habari aliposema orodha ya wagombeaji ubunge Kibra ambao walitaka tikiti ya chama hicho iliyowasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikuwa feki, licha ya kwamba ilionekana kuwa na sahihi iliyodhaniwa kuwa yake.

Mnamo Juni, alijikuta taabani na kikundi cha Tangatanga kinachomshabikia Dkt Ruto wakati mawasiliano ya simu kati yake na Bw George Nyanja yalipofichuliwa, wakizungumzia njama zinazoweza kutumiwa kumhangaisha Naibu Rais kisiasa.

Bw Kabundu analaumu chama hicho kwa kukosa kuleta umoja wa wanachama huku akidai kuwa kuna migawanyiko ambayo inaweza kusababisha chama hicho kukosa kutekeleza wajibu wake wa kisiasa.

Mlalamishi ameambia jopo hilo kuwa chama cha Jubilee kimekataa kutii notisi iliyotolewa na msajili wa chama ambayo ilitaka viongozi wanaoshikilia nyadhifa serikalini wang’atuke kwenye vyeo vya vyama.

Pigo kwa Jubilee Mariga kufungiwa nje na IEBC

Na LEONARD ONYANGO

MGAWANYIKO ndani ya Chama cha Jubilee kuhusu ugombeaji wa ubunge Kibra ulizidi kudhihirika Jumanne wakati wakuu wa chama hicho walikosa kujitokeza kumkabidhi rasmi Bw McDonald Mariga vyeti vya uwaniaji, na kuchangia kufungiwa nje kwa mwaniaji huyo na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Tofauti na vyama vingine vya kisiasa ambako wagombeaji walilakiwa na wakuu wa vyama baada ya kuteuliwa kuwania wadhifa huo, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, hawakuwepo katika makao makuu ya Jubilee Bw Mariga alipopewa vyeti.

Badala yake, shughuli hiyo ilisimamiwa na Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju akiandamana na wanasiasa wengine wa chama hicho hasa wa mrengo wa Tangatanga unaomuunga mkono Dkt Ruto.

Tangu kuteuliwa kuwa mwaniaji wa Jubilee, Bw Mariga hajawahi kukutana na Rais Kenyatta ambaye ni kiongozi wa chama hicho.

Duru zilisema, uamuzi wa kuwasilisha mwaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra ulifanywa na Dkt Ruto kwa lengo la kumpinga Bw Odinga.

Ripoti zilisema Rais Kenyatta alikataa mwaliko wa naibu wake aliyemtaka aende kumkabidhi Bw Mariga cheti cha uteuzi katika makao makuu ya chama cha Jubilee.

Viongozi wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Kieleweke unaopinga mienendo ya Tangatanga, wakiwemo Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny na Mbunge Maalumu Maina Kamanda wanadai kuna baadhi ya watu ndani ya Jubilee wanalenga kusambaratisha uhusiano mwema uliopo baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa kusimamisha mwaniaji Kibra.

“Naibu wa Rais anajua kwamba hatashinda kiti cha Kibra na lengo lake kuu ni kutaka kuzua uhasama kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga,” akasema Bw Kamanda.

Wakati huo huo, Bw Tuju pia amethibitisha kuwa Rais Kenyatta hatashiriki katika kampeni za ubunge Kibra.

Viongozi wa Vyama vya ODM, Ford-Kenya, na Amani National Congress ambavyo vina wagombeaji wanaomezea mate kiti hicho kilichoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge, Ken Okoth, wamekuwa mstari wa mbele kutafutia umaarufu wagombeaji wao.

Bw Odinga alimtangaza mbunge wa Suna Mashariki ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM, kuwa kinara wa kampeni za Bw Okoth katika uchaguzi mdogo wa Kibra.

Bw Odinga alifanya kikao cha faragha na wawaniaji wote waliopoteza katika uchaguzi wa kura za mchujo uliofanyika Jumamosi iliyopita ili kuwapatanisha baada ya malalamishi kuibuka miongoni mwa baadhi yao awali.

Baada ya kikao hicho, wawaniaji hao walitangaza kumuunga mkono Bw Bernard Otieno Okoth, almaarufu Imran, aliyeibuka mshindi.

“Hii ilikuwa mechi ya kirafiki, hivyo hakuna uhasama kati yetu. ODM ni chama kinachozingatia demokrasia na sasa tutaunga mkono Bw Imran Okoth na tutahakikisha chama chetu kinahifadhi kiti hicho,” akasema Bw Peter Orero ambaye awali alikuwa amelalamika kuhusu udanganyifu katika kura ya mchujo.

Wawaniaji wengine ambao wamewasilisha stakabadhi zao kwa IEBC ni Eliud Owalo wa chama cha Amani National Congress (ANC), Khamisi Butichi wa Ford Kenya, Malaseh Hamida (United Green Movement) Editar Ochieng (Chama cha Ukweli chake mwanaharakati Boniface Mwangi) na Fridah Kerubo Kingara (mwaniaji wa kujitegemea).

JAMVI: BBI itakuwa msumari wa mwisho kwa jeneza la Jubilee

Na BENSON MATHEKA

Ripoti ya Jopokazi la Maridhiano, maarufu kama BBI, huenda ikawa msumari wa mwisho katika jeneza la chama cha Jubilee ambacho kimekumbwa na mgogoro wa ndani kwa ndani, wadadisi wameonya.

Wanasema kujitokeza hadharani kwa Naibu Rais William Ruto kupuuza jopokazi hilo lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya muafaka wao, ni ishara kwamba ripoti yake itazidisha mpasuko katika chama tawala.

Dkt Ruto na washirika wake katika kundi la Tanga Tanga wamekuwa wakikosoa muafaka huo na pendekezo la kura ya maamuzi tofauti na wale wa Kieleweke wanaompiga vita na ambao wameapa kuzima azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanachama wa Kieleweke wamekuwa wakipigia debe jopokazi hilo na kuunga kura ya maamuzi kubuni wadhifa wa waziri mkuu. Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakipinga kura ya maamuzi inayolenga kubuni nyadhifa zaidi za uongozi.

Wiki jana, Dkt Ruto alipuuza kamati hiyo iliyokusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu marekebisho wanayotaka yatekelezwe kuimarisha uwiano nchini akisema inapotezea wananchi wakati.

Kulingana na Dkt Ruto, BBI haikuwa na haja ya kuzunguka nchini kutafuta maoni ya wananchi, na badala yake ingepata tu maoni ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuhusu namna ya kuzuia ghasia kila baada ya uchaguzi kwa kuwa yeye ndiye amekuwa akipinga matokeo ya kura.

Wadadisi wanasema kauli hiyo ya Dkt Ruto inaashiria kwamba atapinga vikali ripoti ya BBI inayotarajiwa wakati wowote na kuzidisha mgawanyiko katika chama tawala.

“Kwa kukosoa jopokazi ambalo Rais Kenyatta alihusika kuunda ni kuonyesha kuwa hayuko tayari kukubaliana na ripoti yake iwapo itatoa mapendekezo ya kubadilisha muundo wa serikali. Hii inaweza kuvunja Jubilee kabisa. Kumbuka chama hicho kimegawanyika huku Dkt Ruto na washirika wakilaumiana na wale wa Rais Kenyatta kuhusu kila kitu,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Dkt Ruto na wandani wake wanahisi kwamba BBI inatumia rasilimali za serikali kutimiza malengo ya kuzima azima yake, kumaanisha kuwa hawatambui na hawatatambua mapendekezo yake.

“Kwa msingi huu pekee, kinachoweza kutarajiwa ni mvutano zaidi ndani ya chama cha Jubilee wandani wa Dkt Ruto wakikataa mapendekezo ya jopokazi hilo. Kwao, halikufaa kubuniwa na halina maana kwa sababu wanahisi linanuiwa kummaliza naibu rais kisiasa,” aeleza Bw Kamwanah.

Wadadisi wanasema uwezekano wa ripoti ya BBI kupendekeza kura ya maamuzi, ndio unaomkera Dkt Ruto ambaye amekuwa akidai pendekezo hilo linalenga kunufaisha watu au jamii chache.

“Kauli hii inalenga wanachama wa kundi la Kieleweke ambao wamekuwa wakiunga mkono maridhiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na hii imekuwa ikimwasha Dkt Ruto na wandani wake. Wanahisi kwamba Bw Odinga amezua msukosuko katika chama cha Jubilee kwa lengo la kumwekea Ruto vikwazo, madai ambayo Rais Kenyatta mwenyewe amekanusha akisema muafaka wao haukuhusu uchaguzi wa 2022,” asema mdadisi wa siasa, Peter Wafula.

Anasema ishara kwamba ripoti ya kamati hiyo itazamisha chama cha Jubilee ni hatua ya wandani wa Dkt Ruto ya kuunga mswada wa kura ya maamuzi wa Punguza Mizigo ambao unapendekezwa na chama cha Third Way Alliance.

“Ikiwa kutakuwa na kura ya maamuzi kutokana na mapendekezo ya BBI, kutakuwa na kivumbi katika chama cha Jubilee, Dkt Ruto na washirika wake wakiyapinga. Sio kwa sababu mapendekezo hayo yatakuwa mabaya, yanaweza kuwa mazuri kwa nchi, lakini watayapinga kwa sababu Bw Odinga na Wanakieleweke watayaunga mkono,” asema Bw Wafula.

Anatoa mfano wa bunge la kaunti ya nyumbani ya Bw Odinga ya Siaya kukataa mswada wa Punguza Mizigo huku bunge la kaunti ya nyumbani ya Dkt Ruto ya Uasin Gishu ikipitisha mswada huo.

Kulingana na wandani wa Dkt Ruto, BBI inatumiwa kusambaratisha ndoto yake ya kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na hawawezi kuunga mapendekezo.

Wadadisi wanasema Dkt Ruto anahisi kuwa hakushirikishwa kwenye BBI licha ya kuwa nguzo muhimu katika serikali ya Jubilee na siasa za humu nchini.

Wandani wake wamekosoa kamati hiyo wakidai kwamba inalenga kutimiza maslahi ya watu wachache wanaotaka kutenga jamii nyingine.

“Kwa chama ambacho kimekumbwa na migogoro ya ndani kwa ndani na madai ya usaliti kama Jubilee, ripoti ya BBI inaweza kukivunja kabisa ikizingatiwa tangu mwanzo, Dkt Ruto ambaye ni mshirika mkuu katika chama hicho hakuchangamkia muafaka uliozaa jopokazi hilo,” asema Bw Kamwanah.

Mikakati ya Dkt Ruto kudhibiti Jubilee

Na CHARLES WASONGA na GEOFFREY ANENE

NAIBU Rais William Ruto ameamua kudhibiti chama cha Jubilee kwa kuhakikisha ameshawishi maamuzi muhimu.

Haya yamebainika huku kukiwepo madai kwamba Dkt Ruto alisukuma Jubilee kudhamini mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra kama sehemu ya mikakati yake wa kukita usemi wake chamani na kufanikisha ndoto yake ya kuingia Ikulu mwaka 2022.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba uongozi wa chama awali haukutaka kudhamini mgombeaji Kibra ili usiathiri uhusiano mzuri uliopo kati ya kiongozi wake, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia handisheki.

Lakini chama hicho kililazimika kukubaliana na uamuzi wa Dkt Ruto ili kuzuia uwezekano wa viongozi wa Jubilee kuunga mkono wagombeaji tofauti katika uchaguzi huo wa Novemba 7 hali ambayo ingepanua zaidi ufa uliopo ndani ya chama tawala.

Mnamo Ijumaa wiki jana, mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEC), Andrew Musangi, alithibitisha kuwa mwanasoka McDonald Mariga, ambaye anapendelewa na Dkt Ruto, ni miongoni mwa watu 16 wangepigwa msasa ili katika harakati za kusaka anayehitimu kuwa mgombeaji wa Jubilee.

Kama ilivyodhihirika katika chaguzi ndogo za Wajir na Embakasi Kusini, Dkt Ruto anataka mgombeaji anayependelea ndiye aibuke mshindi katika uchaguzi mdogo wa Kibra ili kuimarisha nafasi yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hata hivyo, saa chache baada ya Jubilee kutangaza Mariga atapeperusha bendera ya chama, kiungo huyu aliyesakata soka yake katika mataifa ya Italia, Uhispania na Uswidi kati ya mwaka 2006 na 2018, amepuuzilia mbali madai hayo.

“Mimi si mradi wa mtu yeyote. Nawania kiti cha ubunge cha Kibra kwa sababu nataka ‘kurudisha mkono’ kwa jamii. Pia, nafahamu maisha ya watu wa eneo hili na kile wanachopitia,” akasema Mariga.

Enzi yake kama mchezaji, Mariga, 32, alichezea Enkopings SK na Helsingborg (Uswidi), Parma, Inter Milan na Latina Calcio (Italia) na Real Sociedad na Real Oviedo (Uhispania). Hajakuwa na klabu tangu Julai 1, 2018, hali ambayo pengine imemsukuma katika siasa kujaribu bahati yake.

Mariga alibwaga watu 15 kupata tiketi ya kupeperusha bendera ya Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra utakaofanyika Novemba 7. Aliwabwaga Morris Kinyanjui, Walter Trenk, Ibrahim Said, Doreen Wasike, Oscar Kambona, Bukachi Chapia, Jane Githaiga, Jack Owino, Omondi Rajab, Daniel Adem, Daniel Orogo, Ramadhan Hussein, Fank Amollo, Timothy Kaimenyi na Geoffrey Mwangi.

Atapambana na mgombea wa ODM, ambaye atajulikana baada ya mchujo utakaofanyika Septemba 7, Eliud Owalo (Amani National Congress) na wagombeaji huru kadhaa.

Kiti hiki kiliachwa wazi baada ya Ken Okoth kuaga dunia Julai 26, 2019 jijini Nairobi baada ya kuugua kansa.

Duru kutoka ndani ya Jubilee zasema Dkt Ruto pia anapanga kudhibiti chama hicho kwa kuhakikisha kuwa wandani wake wanashinda viti vingi katika uchaguzi ambao utafanyika kuanzia Machi 2020. Uchaguzi huo utafanyika kutoka ngazi ya mashinani hadi kitaifa.

Itakumbukwa kuwa alitumia mbinu kama hii kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017, alipoingilia mchujo wa Jubilee na kuhakikisha kuwa wanasiasa wandani wake waliibuka washindi, hasa katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya.

Uchaguzi wa chama unapokaribia, wandani wa Dkt Ruto katika matawi ya Jubilee kote nchini sasa wanaamini wana idadi tosha ya wajumbe ambao wataweza kumuondoa Bw Raphael Tuju kutoka wadhifa wake wa Katibu Mkuu.

Dkt Ruto hafurahishwi na jinsi Bw Tuju anaendesha shughuli za chama hicho na Agosti alimtaja kama Katibu Mkuu wa chama tawala ambaye amepoteza mwelekeo na kugeuka mpanga mikakati wa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

“Kwa sababu ameonekana kuunga mkono Raila Odinga, tunahisi kuwa Bw Tuju anafaa kuiga mfano wa Bw David Murathe na kujiuzulu mapema. Asipofanya hivyo, tutahakikisha ameong’olewa mamlakani katika uchaguzi wa chama mwaka 2020,” mbunge wa Belgut Nelson Koech alisema juzi.

Hofu

Dkt Ruto anahofia kwamba wanaopinga azma yake kama Bw Murathe wanaweza kusambaratisha chama anachoamini ni maarufu miongoni mwa Wakenya.

Lakini ieleweke kwamba licha ya kutangaza kujiuzulu, jina la David Murathe bado liko katika orodha ya maafisa wa Jubilee, ambapo anaorodheshwa kama Naibu Mwenyekiti.

Inasemekana kuwa Rais Kenyatta alipinga nia yake ya kujiuzulu.

Yapo madai kwamba wafuasi wa Dkt Ruto pia wanapanga kumiliki jina la Jubilee kwa kuunda chama kipya cha Jubilee Republican Party ambacho atakitumia katika safari yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hii ni baada ya kubainika kuwa viongozi wa Jubilee wanaounga mkono handisheki wanapanga kukihama kubuni muungano mpya wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 na kukatiza uhusiano kati yao na Dkt Ruto.

Juzi Mbunge Maalum Maina Kamanda alifichua muungano huo utashirikisha chama cha ODM pamoja na “vyama vingine vyenye sera sawa na zetu”.

Jubilee yamtangaza Mariga mgombea wake wa ubunge Kibra

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Jubilee kimemteua mwanasoka McDonald Mariga Wanyama kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra mnamo Novemba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho Andrew Musangi alisema Jumatatu kwamba uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuwahoji watu 16 waliosaka tiketi hiyo.

“Baada ya kuwahoji kwa makini jumla ya watu 16 waliotuma maombi ya kutaka kuwa wawaniaji wa kiti cha ubunge cha Kibra kwa tiketi ya Jubilee, bodi yangu umemteua Bw McDonald Mariga Wanyama. Hii ni kwa sababu tumeridhika kuwa ana ufahamu wa hali ya eneobunge hilo, ameonyesha bidii, nguvu na kujituma; sifa ambazo Jubilee inahitaji kwa mpeperusha bendera yake,” Bw Musangi akasema kwenye kikao na wanahabari saa moja usiku katika makao makuu ya Jubilee, mtaani Pangani, Nairobi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) Andrew Musangi akimtangaza McDonald Mariga kuwa mgombeaji wa kiti cha ubunge Kibra kwa tiketi ya Jubilee. Hapa ni katika makao makuu ya Jubilee, Pangani, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

Sasa ni rasmi kwamba Bw Mariga atakupambana na mgombeaji wa ODM ambaye atajulika Jumamosi baada mchujo wa chama hicho.

Vilevile, atakabana koo na mgombeaji wa chama cha Amani National Congress (ANC) Eliud Owalo na wagombeaji huru kadhaa.

Kiti cha Kibra kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge Bw Ken Okoth mnamo Julai 26, 2019 katika Nairobi Hospitali baada ya kuugua kansa ya utumbo.

Umri

Bw Mariga mwenye umri wa miaka 32 amewahi kuichezea timu ya taifa Harambee Stars na miamba wa soka nchini Italia Inter Milan.

Vilevile, amewahi kuchezea timu zingine duniani miongoni mwao ikiwa ni Real Sociedad, Parma, Helsingborge na Real Oviedo.

Wengine waliong’ang’ania tiketi ya Jubilee kwa kinyang’anyiro hiki ni pamoja na Morris Kinyanjui, Walter Trenk, Ibrahim Said, Doreen Wasike, Oscar Kambona, Bukachi Chapia, Jane Githaiga, Jack Owino, Omondi Rajab, Daniel Adem, Daniel Orogo, Ramadhan Hussein, Fank Amollo, Timothy Kaimenyi na Geoffrey Mwangi.

WANDERI: Jubilee ikome kutumia kifua dhidi ya Wakenya

Na WANDERI KAMAU

UHESABU wa watu ni shughuli ambayo imekuwepo kwa miaka mingi. Ni shughuli muhimu ambayo ilichukuliwa kwa uzito na falme nyingi ambazo ziliweka msingi kwenye mfumo wa utawala duniani.

Ni kutokana na ufahamu wa watu ambapo watawala wa falme hizo waliweza kuendesha shughuli muhimu kama uajiri wa watu katika jeshi.

Katika falme kama Ugiriki na Roma, watawala wake walitumia takwimu za watu waliopata kuzigawanya katika maeneo ya kiutawala ambayo yaliwasaidia sana katika utoaji wa huduma muhimu kwao.

Sensa vile vile ni zoezi ambalo linakubalika kidini, kwani katika Ukristo, Yesu alizaliwa wakati mtawala Herode wa Israeli alikuwa ameagiza watu wote katika ufalme huo wahesabiwe.

Hivyo, zoezi hili ni muhimu sana kwa nchi ama falme yoyote ile duniani.

Hii ikiwa sensa ya sita tangu Kenya kujinyakulia uhuru kutoka kwa Waingereza mnamo 1963, kuna maswali mengi ambayo Wakenya wengi wanajiuliza licha ya kukubali kuhesabiwa.

Baadhi ya maswali hayo ni kuhusu umuhimu wake, ikizingatiwa kuwa inafanywa miezi miwili tu baada yao kuagizwa na Serikali ya Kitaifa kujisajilisha kupata Huduma Namba.

Zoezi hilo liliendeshwa kwa uzito mkubwa kiasi kwamba Rais Uhuru Kenyatta alilazimika kuongeza muda wa usajili wake kwa wiki moja ili kuwaruhusu Wakenya ambao hawakuwa wamejisajilisha kufanya hivyo.

Na licha ya kumalizika kwa mchakato huo, maswali yangalipo kuhusu umuhimu wake. Je, umuhimu wake ulikuwa upi? Maelezo ambayo Wakenya walitoa yatatumiwa vipi? Yatakuwa na manufaa yoyote kwao?

Tashwishi hizi zinachangiwa na hali kuwa hata Wakenya wanaoishi ng’ambo waliagizwa kujisalilisha, la sivyo wangekumbwa na vikwazo vingi, hasa kwenye taratibu za kuchukua upya stakabadhi kama paspoti.

Serikali ilitoa maagizo kwa mabalozi katika nchi mbalimbali kuhakikisha kuwa kila Mkenya anajiandikisha.

Ingawa zoezi hilo lilitumia jumla ya Sh8.8 bilioni, asilimia kubwa ya wananchi hawana ufahamu wowote kuhusu umuhimu na maana yake.

Hii ni kwa kuwa baadhi ya maswali ambayo wanaulizwa kwenye zoezi la sensa ni yale yale waliyoulizwa walipokuwa wakijisajilisha kwa Huduma Namba.

Hofu hizi zinapojiri wakati ufisadi umegeuka kuwa jinamizi kuu kwa utawala wa Jubilee, ni muhimu kwa asasi husika kujitokeza wazi kuwafafanulia Wakenya kuhusu uhusiano wa zoezi hizi mbili.

Baadhi ya Wakenya wenye ghadhabu wamesikika wakitishia kususia kuhesabiwa, wakilalama kwamba hawaoni mabadiliko yoyote kwa maisha yao licha yao kutoa maelezo mengi kwa Serikali.

Ni kinaya kwa Serikali kuendesha mazoezi hayo bila kuwafafanulia Wakenya umuhimu wake, ikizingatiwa pia huwa inachukua maelezo muhimu ya mtu anapojisajilisha kupata stakabadhi muhimu kama paspoti ama kitambulisho cha kitaifa. Pia mtoto anapozaliwa, anapoingia shule husajiliwa na pia kila anayekufa huandikishwa.

Imefikia wakati uongozi wa Rais Kenyatta ufahamu kuwa kuendeleza sera kimabavu kwa wananchi bila kutoa ufafanuzi kuhusu maana yake ni njia ya kuongeza hasira miongoni mwao. Utawala shirikishi unapaswa kuwachukulia raia kama washikadau, lakini sio kama maadui wachapwao kwa viboko.

akamau@ke.nationmedia.com

Jubilee yaruka Mariga katika Kibra

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha Jubilee kimekanusha kwamba kiliorodhesha jina la mwanasoka wa kimataifa MacDonald Mariga miongoni mwa wanaotaka tiketi yake ili kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa Kibra hapo Novemba 7.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju alikanusha Jumanne kwamba aliandika barua yenye jina la Bw Mariga na watu wengine wanne huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikikataa barua hiyo na kuirudisha kwa usimamizi wa Jubilee.

Mwanasoka huyo pamoja na ndugu yake Victor Wanyama waligonga vichwa vya habari nchini mwezi jana baada ya kumtembelea Naibu Rais William Ruto katika ofisi yake wakati wa kupanga mashindano ya soka ya Wanyama Royal Cup yanayodhaminiwa na wawili hao.

Ni kutokana ziara hiyo ambapo barua iliyoorodhesha jina la Bw Mariga ilionekana na wengi kuwa azma yake ya kuwa mbunge wa Kibra inapigwa jeki na Dkt Ruto.

Wengine waliotajwa kama wanaomezea mate kiti cha Kibra kwa tiketi ya Jubilee kwenye barua hiyo tatanishi ni Said Abraham, Morris Peter Kinyanjui, Mukinyingi Walter Trenk na Doreen Nangame Khayanga Wasike.

“Tume ilipokea barua Jumatatu Agosti 26 saa kumi na moja jioni ikipendekeza majina ya wawaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra. Hata hivyo, tume imeelezwa kwamba Jubilee haikuidhinisha barua hiyo. Tume imeandikia chama na kuambatanisha nakala ya barua hiyo ili chama kichukue hatua inayofaa,” ikasema taarifa ya IEBC.

Bw Tuju mnamo Jumatatu jioni alieleza kutofahamu lolote kuhusu barua hiyo iliyochipuka punde tu baada yake kutoa taarifa kwamba chama hicho kitawasilisha mwaniaji kuchuana na mgombeaji wa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga ili kutafuta mrithi wa marehemu Ken Okoth.

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Dijitali katika Afisi ya Rais, Dennis Itumbi alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kusambaza barua hiyo na kusema ilikuwa na saini ya Bw Tuju kama thibitisho kwamba aliidhinisha.

“Nasimama na barua niliyosambaza kuhusiana na uchaguzi wa Kibra. Jubilee itaandaa kura ya mchujo. IEBC ina barua ambayo nimeambatanisha hapa,” akaandika Itumbi kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mchujo

Huku hayo yakijiri, Bw Tuju alikanusha kwamba chama hicho kitafanya kura ya mchujo, akisema wenye nia ya kutumia Jubilee kupigania kiti cha Kibra watakaokuwa wamewasilisha vyeti vyao watachujwa Ijumaa hii kisha uamuzi wa mgombeaji wa kupewa tiketi ya moja kwa moja uafikiwe na chama.

Wakati huo huo Bw Tuju alieleza Taifa Leo kwamba hatua ya chama hicho kumwasilisha mwaniaji kukabiliana na ODM Kibra haitavuruga ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga maarufu kama handisheki.

Visiki vizito katika azma ya Jubilee kufanya uchaguzi

Na WANJOHI GITHAE na BENSON MATHEKA

CHAMA cha Jubilee kinakabiliwa na kibarua kigumu zaidi kinapojiandaa kwa uchaguzi kote nchini huku wafuasi wa Naibu Rais wakilalamika kuwa kuna njama ya kuwafungia kugombea nyadhifa za uongozi.

Kulingana na katiba ya chama hicho, uchaguzi unafaa kufanyika Machi 2020.

Maafisa wa chama hicho walifahamisha Taifa Leo kwamba Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) litakutana hivi karibuni kuweka mikakati ya uchaguzi ambayo wanachama wanapaswa kufuata.

Kulingana na katiba ya Jubilee, uchaguzi unapaswa kuanzia mashinani hadi kongamano la kitaifa la wajumbe ambapo maafisa wa kitaifa watachaguliwa.

Kwa wakati huu, chama hicho kimegawanyika katika makundi mawili; ‘Tangatanga’ linalomuunga Dkt Ruto na ‘Kieleweke’ linalopinga azma yake ya kugombea urais.

Chama hicho kinakabiliwa na msukosuko ambao baadhi ya wanachama wanasema unachangiwa na viongozi kutokutana kuzungumza kwa sauti moja.

Dkt Ruto amekuwa akitengwa serikalini na wandani wake wa kisiasa wanadai kwamba wanahangaishwa na serikali. Wiki hii, Rais Kenyatta alitoa tamko la wazi kuashiria kwamba hatamuunga mkono kuwa mrithi wake kwenye uchaguzi mkuu ujao aliposema ni Mungu anayejua atakayechaguliwa Rais.

Naibu rais ameendelea na kampeni zake na amekuwa akiashiria kwamba anafahamu kuna njama za kumzuia kuwa rais kupitia uchaguzi wa chama.

Uchaguzi wa Jubilee unafuatiliwa kwa karibu na wanachama wa mirengo yote miwili ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ ambao wameapa kutohama chama hicho.

Wanachama wa Kieleweke wamekuwa wakipendekeza kuwa viongozi waliochaguliwa wasiwanie nyadhifa za uongozi wa chama, msimamo ambao Tangatanga inapinga.

Kulingana na Tangatanga, wabunge wa zamani wanataka kuchukua nyadhifa za uongozi chamani ili wamzime Ruto na wafuasi wake kwenye uteuzi wa wagombeaji wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Hivi majuzi, chama hicho kilipokea Sh190 milioni ambazo Katibu Mkuu Raphael Tuju anasema zitatumiwa kuandaa uchaguzi.

Bw Tuju ambaye majuzi alishambuliwa na wafuasi wa Dkt Ruto wakitaka atimuliwe alisema maandalizi ya uchaguzi yanaendelea.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa wanaowania nyadhifa za uongozi lazima wahudhurie mafunzo kwanza ili waelewe malengo yake.

“Hakuna atakayeruhusiwa kugombea wadhifa ikiwa anaendeleza chuki za kikabila. Malengo ya chama ni umoja wa kitaifa,” alisema.

Alisema ni lazima viongozi wote waliochaguliwa na wanachama wanaowania nyadhifa chamani wahudhurie mafunzo hayo.

“Warsha hizo zitakuwa sehemu ya maandalizi ya uchaguzi,” alisema na kuongeza kuwa watawasajili wanachama kabla ya uchaguzi.

Maafisa wapya

Naibu katibu mkuu wa chama hicho Caleb Kositany alisema ni lazima kiwe na maafisa wapya kufikia Machi 2020 ili kijiandae kumteua mgombea urais 2021.

“NEC itakutana hivi karibuni kujadili na kutoa mwelekeo,” alisema.

Uchaguzi huo unaandaliwa huku Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee Party akipuuza miito ya ‘Tangatanga’ ya kuitisha kikao cha wabunge.

Bw Tuju alikiri kwamba chama hicho kitakabiliwa na changamoto katika kuandaa uchaguzi huo.

ODM yafifia Jubilee ikivuna ngome zake

Na BERNARDINE MUTANU

CHAMA cha ODM kimepoteza umaarufu kwa Jubilee katika ngome zake za Pwani, Nyanza na Magharibi.

Kwa sasa, Jubilee ndicho chama maarufu zaidi kulingana na ripoti ya utafiti uliofanywa na kampuni ya utafiti ya Infotrak.

Ripoti hiyo iliyotolewa jana, ilionyesha kuwa Wakenya wengi zaidi (asilimia 40) wanajihusisha na chama cha Jubilee dhidi ya asilimia 21 wanaojihusisha na ODM.

Ni asilimia tatu pekee ya wote waliohusishwa katika utafiti huo waliounga mkono na chama cha Wiper Democratic-Movement Kenya (WDM-K).

Nayo asilimia moja pekee inaunga mkono Amani National Congress (ANC) na pia FORD-Kenya.

Cha kushangaza ni kuwa, licha ya Jubilee kuendelea kupata umaarufu katika ngome za ODM, chama cha Chungwa kimepoteza ufuasi katika maeneo kinakotarajiwa kuwa na wafuasi wengi zaidi.

Kwa mfano, katika eneo la Nyanza, ni asilimia 47 waliosema ni wafuasi wa ODM dhidi ya asilimia 24 waliounga mkono Jubilee.

Kwa upande mwingine, umaarufu wa Jubilee eneo la Kati umesalia imara kwa asilimia 61, dhidi ya umaarufu wa ODM wa asilimia saba pekee.

Katika eneo la Pwani, vyama hivyo maarufu zaidi nchini vina uwezo sawa, ambapo asilimia 33 ya wakazi wa eneo hilo (kwa kila chama) walisema wanaviunga mkono.

Na katika eneo la Magharibi, umaarufu wa ODM umedidimia dhidi ya umaarufu wa Jubilee ambapo ni asilimia 25 pekee wanaounga mkono chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga dhidi ya asilimia 27 wanaounga mkono Jubilee.

Hali ni kama hiyo katika Kaunti ya Nairobi ambapo ODM kina umaarufu wa asilimia 27 dhidi ya asilimia 23 ya Jubilee.

Chama cha Jubilee kina wafuasi wengi zaidi eneo la Bonde la Ufa kwa asilimia 57 dhidi ya asilimia 12 wanaounga mkono chama cha ODM.

Licha ya mgogoro wa ndani ambao umetishia kusambaratisha Jubilee, bado chama hicho ni maarufu zaidi eneo la Kaskazini Mashariki (asilimia 42) na Mashariki (asilimia 39).

Viongozi wataka Uhuru atatue shida za Jubilee

Na ERIC MATARA

KUNDI la viongozi kutoka Rift Valley limehimiza chama cha Jubilee kuandaa mkutano wa wanachama wake ili kuzima tofauti kati ya kambi za Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Viongozi hao walisema ni muhimu kwa Rais na naibu kuelewana na watangaze kusitisha siasa za 2022, ambazo walisema zinaathiri ajenda za serikali.

Wakiongozwa na Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui, kundi la wabunge, wazee wa baraza la wazee wa Bonde la Ufa na madiwani, viongozi hao walisema wanataka mkutano wa haraka uandaliwe ili kutatua matatizo yanayokumba Jubilee.

Akizungumza katika mazishi ya mbunge wa zamani wa eneobunge la Rongai, Willy Komen, Gavana Kinyanjui alisema siasa kuhusu urithi hapo 2022 ambazo zinaendelea kwa sasa, hazina umuhimu kwani zinanyima taifa maendeleo.

“Makundi ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ yanagawanya taifa na hii ni hatari kwa Jubilee. Tunafaa tuandae mkutano na tujadili masuala haya,” Bw Kinyanjui akasema.

“Watakaochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu ujao itakuwa ni kwa misingi ya kutimiza ahadi ambazo tulitoa wakati wa kampeni. Kwa sasa tunahitaji kufanya kazi ya kutimiza ahadi hizi,” akasema gavana huyo.

Wabunge waliozungumza na Taifa Leo walisema joto lililoko ndani ya Jubilee litatulizwa tu kwa kuandaliwa kwa mkutano wa viongiozi.

“Namrai Rais Kenyatta aitishe mkutano ili kumaliza hatari ya kusambaratisha chama,” mbunge wa Kuresoi Joseph Tonui akasema.

Mwenyekiti wa baraza la wazee eneo la Rift Valley, Gilbert Kabage naye alisema siasa za 2022 zinapandisha joto na hofu eneo hilo, akisema siasa za majibizano zinaathiri hali ya maisha.