JAMVI: Njama ya Jubilee kubadili sheria za uchaguzi

Na LEONARD ONYANGO

HUKU mjadala kuhusu marekebisho ya Katiba kupitia kura ya maamuzi ukiendelea kushika kasi, chama cha Jubilee kimeanza mchakato wa kubadilisha tena sheria za uchaguzi zilizopitishwa kwa haraka siku chache kabla ya uchaguzi wa urais wa marudio mnamo Oktoba 26, 2017.

Wanasiasa wa Jubilee walikimbilia kubadili sheria za uchaguzi kama njia mojawapo ya kuzuia Mahakama ya Juu kubatilisha tena matokeo ya uchaguzi wa urais wa marudio.

Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 baada ya kubaini kwamba uliendeshwa bila kuzingatia Katiba na sheria za uchaguzi.

Hii ilikuwa baada ya Jaji Mkuu David Maraga kutishia kwamba Mahakama ya Juu ingebatilisha tena matokeo endapo Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ingefeli kufuata katiba na sheria katika uchaguzi wa marudio.

Wabunge wa Jubilee walibadilisha sheria ili kuzuia Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo kutokana na kigezo cha IEBC kutozingatia sheria.

Kadhalika, Jubilee walibadili sheria ili kuruhusu naibu mwenyekiti wa IEBC kutangaza mshindi wa urais, tofauti na hapo awali ambapo mwenyekiti pekee ndiye aliyetwikwa jukumu hilo.

Huenda Jubilee walihofia kwamba mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati angejiuzulu hivyo kutatiza uchaguzi wa marudio.

Jubilee pia walisema kuwa si lazima kwa IEBC kupeperusha matokeo kwa njia ya kielektroniki tofauti na awali ambapo matokeo katika karatasi zinazobeba matokeo hayo yalifaa kuwa sawa na yale yanayopeperushwa kwa njia ya kielektroniki.

Sheria hizo zilipingwa vikali na upande wa Upinzani, ulioongozwa na aliyekuwa mwaniaji wa muungano wa NASA Raila Odinga, kutokana na kigezo kwamba zililenga kutoa mwanya kwa Jubilee kuiba kura.

Seneta wa Meru Mithika Linturi sasa anasema kuwa chama cha Jubilee kimeanza mchakato wa kubadili sheria za uchaguzi kwa lengo la kuzuia vurugu katika uchaguzi wa 2022.

Bw Linturi ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Haki za Kibinadamu, anasema kuwa mabadiliko hayo yatahakikisha kuwa Wakenya hawapigani au kuharibu mali baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Tunalenga kubadilisha sheria ili kuzuia uhasama wa kikabila wakati na baada ya uchaguzi. Tutahakikisha kuwa Kenya ina sheria zitakazozuia umwagikaji wa damu au uharibifu wa mali,” akasema Bw Linturi.

“Tunataka kila Mkenya kufahamu kuwa lengo la uchaguzi ni kushindana kwa sera na wala si uadui,” akaongezea.

Hata hivyo, kinara wa upinzani Bw Odinga amesalia kimya kuhusiana na mabadiliko ya sheria za uchaguzi licha ya kuzitaja kama sumu kwa demokrasia zilipopitishwa na wabunge wa Jubilee takriban miaka miwili iliyopita.

Kadhalika, haijulikani ikiwa Naibu wa Rais William Ruto ataunga mkono mabadiliko ya sheria za uchaguzi.

Dkt Ruto alipokuwa akihutubia wasomi katika taasisi ya Chatham jijini London, Uingereza, mapema mwaka huu alisema kuwa sheria za uchaguzi na tume ya IEBC hazifai kulaumiwa kwa machafuko ambayo hushuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi.

Dkt Ruto alisema machafuko hayo yanasababiswa na viongozi wanaokataa kukubali matokeo ya uchaguzi.

“Siasa za Kenya ni safi na wala tume ya IEBC au sheria zetu za uchaguzi hazina dosari. Shida ni wale wawaniaji wanaoingia kwenye kinyang’anyiro lakini hawako tayari kukubali matokeo,” akasema Dkt Ruto huku akionekana kumwelekezea kidole cha lawama Bw Odinga.

Tayari tume ya IEBC imependekeza kuwa Katiba ifanyiwe mabadiliko ili uchaguzi wa rais, wabunge na maseneta ufanyike tarehe tofauti na ule wa magavana na madiwani.

Katika ripoti yake tathmini ya uchaguzi wa 2017, IEBC ilisema ni vigumu kwa maafisa wake kushughulikia kura za viti sita kwa mpigo.

“Kuendesha uchaguzi wa nyadhifa sita kwa mpigo kunasababisha maafisa wetu kuchoka, hivyo kuandika matokeo yaliyosheheni makosa,” ikasema ripoti ya IEBC.

Rais aonywa dhidi ya kuzamisha jahazi la Jubilee

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta sasa ameonywa na baadhi ya wandani wake kisiasa kuwa anahatarisha chama cha Jubilee kuzama kisiasa na kijipate kikiwa hafifu kuwania urais 2022.

Ameonywa kuwa katika siku za hivi majuzi amegeuka kuwa dikteta wa kimaamuzi na ambaye hatii mpangilio wa demokrasia ya vyama vya kisiasa ambapo amegeuza taifa kuwa lisilo na chama chochote cha kisiasa.

Ameambiwa kuwa sera yake ya kukumbatia upinzani ndani ya serikali hata ikiwa ni ya busara katika kusaka umoja na amani ya nchi, vigezo vya demokrasia ya kudumu lazima kiwe ni kuweko kwa vyama vya kisiasa vilivyo thabiti.

Mbunge wa Kapseret, Oscar Kipchumba Sudi katika mtambo wake wa Twitter ameonya kuwa rais Kenyatta amegeuza chama cha Jubilee kuwa mali yake binafsi na ambapo hatambui vyombo vya kufanya maamuzi.

“Wakati mmoja amegeuka kuwa msemaji, mratibu, mkosoaji, kiongozi wa mashtaka, basi hiyo si demokrasia iliyo wazi, ni udikteta,” akasema.

Aidha, Bw Sudi alilia kuwa Jumapili iliyopita Rais alitangaza kuwa sio wanasiasa waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Jubilee ambao walimpa ushindi wa urais.

“Sio wao walinifanya kuwa rais…mimi ndiye niliwatafutia kura na wakawa vile walivyo…Wanacheza na mimi…mimi nitawatoa kwenye wako sasa, ngoja utaona,” akafoka rais akiwa katika kongamano na imani ya Wakorino katika ukumbi wa Kasarani, Nairobi.

Sasa, Sudi anaonya rais Kenyatta kuwa “kuna wengi ambao walijitolea kufa kupona kumpigia debe kwa wapiga kura kiasi kwamba hata wengine walipoteza utajiri na mali katika harakati hizo.”

 

Manung’uniko katika ngome za Jubilee

Na MWANGI MUIRURI

SERIKALI ya Jubilee iliundwa mwaka wa 2013 kwa msingi wa muungano wa Rift Valley na Mlima Kenya kama wanahisa wakuu baada ya vyama vya United Republican Party chake William Ruto na The National Alliance (TNA) chake Rais Uhuru Kenyatta kuungana.

Kama kawaida, wenyeji wa ngome hizi mbili wamekuwa wakitarajia kutuzwa keki kubwa ya kitaifa kwa msingi kuwa “serikali ni yetu.”

Hii ni licha ya kuwa uchaguzi huwa sio wa kusaka wananchi wa kupakuliwa chakula kingi cha serikali kuliko wengine, bali huwa wa kutafuta serikali

ya kitaifa ya kutekeleza usawa wa kiutawala kwa wote.

Lakini baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 ambao ulitekelezwa mara mbili baada ya mahakama kutupilia mbali matokeo ya kwanza, kuyumba kwa usalama kulishuhudiwa ambapo mrengo wa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga uliishia kujiapisha kama ‘serikali ya pembeni’.

Ilibidi Rais Kenyatta amsake Odinga wasalimiane ili kuwe na maridhiano ya kuleta utulivu nchini.

Sasa, salamu hizi, baadhi ya viongozi na raia wananung’unika kuwa ziliingia kuondoa vipande vile vitamuvitamu vya keki ya kitaifa kutoka sahani ya ngome hizo mbili za Jubilee.

Kwa mujibu wa mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri hizi salamu ziliingia kulazimisha maeneo yaliyo na ‘hisa nyingi’ ndani ya hii serikali kutengwa.

“Sisi ndio tulipambana kufa kupona kusaka idadi ya kura tosha za kumweka Rais Kenyatta mamlakani, tukitazamia kuunda serikali lakini leo hii sisi

ndio tumegeuzwa kuwa upinzani,” anasema Ngunjiri.

Wimbo ni uo huo katika ngome za Naibu Rais William Ruto ambapo wenyeji wanateta kuwa hakuna maendeleo wanapata kutoka kwa hii serikali “bali hela na macho ya serikali kwa sasa ni katika ngome za upinzani.”

Ni katika hali hiyo ambapo msanii Ng’ang’a wa Kabari ametunga wimbo ambao ujumbe wake umepakiwa kama radi ukielekezwa kwa serikali ya Jubilee.

Anasema kuwa taswira ya Jubilee kwa sasa kwa wenyeji wa Mlima Kenya na Rift Valley ni ile ya mtoto kuitisha mkate kwa babake lakini anakabidhiwa ‘mtu au mnyama mwingine tofauti’.

“Hii ni serikali ambayo haina haja na masikini. Wakubwa kwa wadogo wanalia serikali. Si wahudumu wa bodaboda, si wa matatu. Kila mtu anakonda na anateseka na kukambwa na njaa kwa sababu ya serikali,” anasema.

Anawaza ni kwa nini watu wa maeneo hayo waliamka asubuhi na mapema kwenda kupigia serikali ya Jubilee kura wakiimba “Tano tena.”

Analia: “Ni Tano Tena ya nini hata afadhali tungekaa nyumbani wengine wakapige kura.”

Anatoa mfano wa mfumkobei.

Analia kuwa umaskini ambao umekumba wengi wa waliopigia serikali hii kura hauna kifani, umaskini ambao umegeuza hata familia kukumbatia

kusambaratika kwa maadili kwa kiwango kikuu.

“Leo hii utapata kuwa baba mzazi ni muuzaji bangi, mama ni kahaba naye mwana wao wa kiume ndiye hupora watu mtaani. Tuliahidiwa kazi kama

vijana; kumbe hatukujua kuwa kazi ni kufungwa jela, kubomolewa vioski na kuhangaishwa tukiitwa wezi!” anatafakari.

Analia kuwa leo hii ni rahisi kwa mwizi wa kuku kufungwa huku wezi wakuu wakiwa serikalini.

 

“Wanjiku wa leo hii anamalizwa na kusukumwa hadi kwa kaburi. Na sasa wametuanza wakituambia kuhusu kura za mwaka 2022. Sioni tukitokea tena kupiga kura. Ni heri mjichague kwa kuwa tumechoka kudanganywa,” anateta.

 

Kuna dalili za machafuko ngomeni mwa Jubilee – Ripoti

Na WANDERI KAMAU

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imezitaja kaunti nane, nyingi zikiwa ngome za chama cha Jubilee (JP) kuwa “maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na ghasia za kisiasa.”

Kaunti hizo ni Kiambu, Kilifi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Baringo, Nakuru, Nyeri na Kakamega.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi Jumanne, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw Hassan Mohamed (pichani), alisema kuwa hali hiyo imesababishwa na ongezeko la mikutano ya kisiasa ambayo imekuwa ikifanyika karibu kila wikendi.

“Tunafahamu kuwa wanasiasa wengi tayari wameanza harakati za kujitayarisha kuwania nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi wa 2022. Hata hivyo, hatutawaruhusu kuendeleza matamshi ya chuki za kisiasa na kikabila,” akasema Bw Mohamed.

Alisema kuwa kampeni hizo hazimaanishi kuwa kiongozi yuko huru kusema lolote alitakalo bila kuzingatia athari zake.

Kutokana na hilo, tume hiyo ilisema kuwa itawatuma maafisa wake wa nyanjani katika kaunti hizo, ili kufuatilia kwa kina matamshi yanayotolewa na viongizi katika mikutano ya kisiasa.

Ili kufanikisha ukusanyaji wa ushahidi, ilitangaza kuongeza mashine 110 za kurekodi na kamera nane maalum kwa maafisa wa usalama katika kaunti hizo.

Mkuu huyo alisema kuwa hatua hiyo vilevile inalenga kuimarisha juhudi za kukusanya ushahidi, kwani kesi nyingi ambazo imekuwa ikiwasilisha mahakamani zimekuwa zikosa kufaulu kwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

“Mahakama zimekuwa zikitushinikiza kutoa mashine ambazo tulitumia kurekodia matamshi ya washtakiwa mbalimbali ambao tumewafikisha mahakamani. Tunataka kuhakikisha kuwa kesi tunazowasilisha zina ushahidi maalum, ili kuona washukiwa wanahukumiwa kulingana na ushahidi tunaowasilisha,” akasema Bw Mohamed.

Kauli hiyo inajiri huku majibizano ya kisiasa kati ya mirengo ya ‘Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke’ yakizidi kuchacha, hasa kuhusu urithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Baadhi ya viongozi pia wamelaumiwa kwa kutoa matamshi yanayozilenga jamii mbalimbali.

Mwezi uliopita, tume hiyo ilimwagiza mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi kufika mbele yake baada ya kutuhumiwa kutoa matamshi dhidi ya jamii fulani.

Hata hivyo, mbunge huyo aliomba msamaha, ijapokuwa alipewa onyo dhidi ya kutoa matamshi mengine ya kichochezi.

Jana, tume pia ilisema kuwa imeanza kitengo maalum cha kuwanasa wale wanaoendesha matamshi kwa njia za mitandao ya kijamii.

Kitengo hicho kitakuwa kikifuatilia jumbe zinazoandikwa na watumizi wa mitandao.

Na ingawa ilikubali kwamba imekuwa vigumu kuwakabili wale wanaotoa jumbe hizo, ilisema imeanza ushirikiano na asasi kama Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) ili kuzinasa hata vituo vya redio vya lugha za kiasili zinazotumika kuendeleza chuki za kikabila na kisiasa.

“Tunafahamu athari za mitandao ya kijamii katika kusambaza jumbe za chuki za kisiasa na kikabila. Tutakuwa macho kuwanasa wale wanaoweka jumbe hizo,” akasema.

Vituo vya redio vya lugha za kiasili vililaumiwa sana kuwa mojawapo ya sababu kuu ya kuzuka kwa ghasia za 2007/2008. Vingi vililaumiwa kwa kuendesha vipindi vyenye chuki za kikabila, hali iliyochochea mapigano kati ya jamii mbalimbali.

Khalwale sasa mali rasmi ya Jubilee

Na WANDERI KAMAU na SHABAN MAKOKHA

ALIYEKUWA Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, ametangaza kuhama rasmi kutoka chama cha Ford-Kenya na kujiunga na Chama cha Jubilee (JP), akilalamikia “vitisho” kutoka kwa uongozi wake.

Dkt Khalwale, ambaye amekuwa akihudumu kama Naibu Kiongozi wa chama hicho, alikuwa ametakiwa kufika mbele ya kamati yake ya nidhamu Alhamisi wiki ijayo, kujibu tuhuma za kuasi kanuni zake.

Kiongozi huyo amekuwa akimpigia debe Naibu Rais William Ruto, akishikilia kuwa atamuunga mkono kuwania urais mnamo 2022. Hii ni licha ya chama hicho kutotoa msimamo wake kuhusu yule kitamuunga mkono.

Akihutubu nyumbani kwake katika kijiji cha Malinya, Kaunti Ndogo ya Ikolomani, Khalwale alisema alichukua hatua hiyo, baada ya kamati hiyo kutishia kumwondoa kutoka nafasi yake.

“Sitaenda kuaibishwa kwa kisingizio cha nidhamu. Ninahangaishwa kwa kuitafutia nafasi jamii ya Waluhya katika serikali ijayo,” akasema.

Akaongeza: “Nimewaita nyote nyumbani kwangu ili Kenya iweze kufahamu ninakotoka. Nipo hapa kutangaza rasmi kuwa nimehama Ford-Kenya na kujiunga na Jubilee.”

Kujibu tuhuma

Dkt Ruto pia alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria. Chama kilimwandikia barua kwa mara ya kwanza mnamo Machi 26, kikimtaka kujibu tuhuma za kukiuka msimamo wake, lakini akakataa kuijibu.

Aliandikiwa barua ya pili mnamo Jumatatu, ambapo alipewa hadi Jumanne ijayo kujibu tuhuma hizo na kufika mbele ya kamati yake ya nidhamu mnamo Alhamisi.

“Kukosa kuijibu barua hii huenda kukaifanya kamati kukuchukulia hatua, mojawapo ikiwa ni faini,” ikamwonya barua hiyo.

Ijumaa, Dkt Khalwale pia alitangaza kuwania ugavana katika kaunti hiyo mnamo 2022.

Kwa upande wake, Dkt Ruto alisema kuwa nia yake ni kuendeleza umoja wa nchi.

“Nipo hapa kumpokea Dkt Khalwale ili kuungana na viongozi wengine ambao hawataki kuendeleza siasa za kikabila ambazo huzua chuki. Mnamo 2013, niliwaomba viongozi wenzangu kutoka vyama vingine kuvivunja na kubuni chama cha umoja wa kitaifa lakini wakakataa. Leo (nawakumbusha kuwa, ikiwa hawataungana, watashindwa vibaya hata kuliko 2013,” akasema.

JAMVI: Sababu za Uhuru kuogopa kuitisha kikao Jubilee

Na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa Rais Uhuru Kenyatta anasita kuitisha mkutano wa kundi la wabunge wa chama cha Jubilee kwa hofu ya kuaibishwa kwa kuelekezewa lawama kuhusu migawanyiko inayotokota ndani ya chama hicho.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa tuliozungumza nao wanasema Rais Kenyatta anawakwepa wabunge wanaegemea mrengo wa naibu wake William Ruto wanataka ufafanuzi kuhusu dhima ya muafaka kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Wabunge hao ambao ni wanachama wa ‘Team Tanga Tanga’ pia wamebainisha wazi kwamba wangemtaka Rais Kenyatta awaeleze waziwazi ikiwa ahadi yake ya kumuunga Ruto kama mrithi wake 2022 ingalipo au la. Rais anafahamau mipango hii na ndio maana amekuwa akitumia majukwaa mengine kuwajibu wabunge hao,” akasema Bw Javas Bigambo.

Wiki jana, Rais Kenyatta alionekana akijibu madai ya wabunge hao kwamba muafaka huo, maarufu kama handisheki, unalenga kumsaidia Bw Odinga kuingia Ikulu 2022 akisema hawajawahi kujadili suala hiyo katika mazungumzo yao na kiongozi huyo wa ODM.

Aidha, alipuuzilia mbali dhana kwamba uhusiano huo unalenga kuivunja Jubilee na kudidimiza ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

“Huyu Raila hajaniambia anataka kuwa Rais 2022; na sijamwambia ninataka kuwa rais 2022. Tumekuwa tu tukijadili masuala yanayowaathiri watu wetu. Ikiwa ni miundo mbinu, tumekuwa tukijadili kile ambacho tunapaswa kufanya kujenga barabara zaidi.

“Tunajadili, tunasaidiana na kukubaliana,” Rais Kenyatta akasema alipohutubu katika mkutano wa kujadili ufadhili wa miradi ya miundo msingi barani Afrika ulioandaliwa katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Mwenyeji wa mkutano huo alikuwa Bw Odinga, ambayo ni balozi wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundo Msingi.

“Ikiwa ni masuala ya afya, huwa ananielekeza kuhusu kile ambacho tunapaswa kufanya. Sisi huketi, kujadiliana na kukubaliana. Yeye pia hunipa mawaidha kuhusu jinsi ya kuimarisha kile ambacho tunafanya. Sasa kuna kosa gani hapo? Rais Kenyatta akauliza.

Alisema mustakabali wa wananchi na taifa la Kenya kwa jumla ndio nguzo muhimu inayohimili muafaka kati yake na Bw Odinga.

Lakini siku moja baada ya Rais kutoa kauli hiyo, Dkt Ruto alioenakana kumjibu alipodai kuwa, “kuna watu mahali fulani ambao wanawachukulia Wakenya kama wajinga.”

Watu ambao, alisema, aidha wanadhani Wakenya hawajui kinachoendelea au wanaamini kuwa Wakenya hawajui nani atakuwa rais wao.

“Kuna watu fulani ambao wanadhani Wakenya ni wajinga. Wakenya wanajua ni nani atakuwa rais wao. Koma kutuletea siasa. Kuna uhaba mkubwa wa wajinga nchini,” Ruto akasema alipohutubia hafla ya Kanisa mjini Nyeri.

Bw Bigambo anasema ni hali kama hii ambapo Rais Kenyatta na naibu wake wameonekana kukinzana waziwazi kuhusu suala hilo la handisheki ambayo imeendelea kuzua tumbojoto ndani ya Jubilee na kufifisha juhudi zozote za kuitishwa kwa mkutano wa kundi la wabunge wake (PG).

“Isitoshe, Rais na naibu wake wametofautiana hadharani kuhusu suala nyeti la vita dhidi ya ufisadi. Rais ameonekana kuunga mkono uchunguzi unaoendeshwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuhusu sakata ya wizi wa Sh21 bilioni za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer lakini Dkt Ruto anampiga vita Bw Kinoti kwa kudai anatumiwa na mahasidi wake kuhujumu ndoto yake ya urais 2022 kwa kulenga wandani wake,” anasema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maseno Tom Mboya anayeshilikia kuwa ni hali kama hiyo ambayo imelemaza juhudi za kuitishwa kwa mkutano wa PG wa Jubilee.

Akiguzia shinikizo hizo za kuitisha mkutano wa PG, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju anasema hamna “mgogoro wowote ndani ya chama chetu wa kuhitaji kujadiliwa katika mkutano kama huo.”

“Kiongozi wa Jubilee Bungeni Aden Duale hajawasilisha ombi kama hilo kwa uongozi wa chama. Kwa hivyo, wale wanaoitisha mkutano huo kupitia mikutano ya hadhara au ya mazishi wanafaa kuelekeza maombi yao kwa Duale. Kufikia sasa hamna ombi kama hili limepokewa ishara kwamba hamna mgogoro au masuala ya kujadiliwa,” anasema Bw Tuju ambaye pia ni Waziri asiye na Wizara ya Kusimamia.

Kwa upande wake Bw Duale, ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini, anasema wajibu wa kuitisha mkutano wa PG sio wa Rais Kenyatta.

“Wale wanataka mkutano huo wanafaa kuwasilisha maombi yao kwa afisi yangu… kisha nitawasiliana na kiongozi wetu Rais Kenyatta na naibu wake Dkt Ruto ili tukubaliane kuhusu ajenda ya mkutano kama huo. Kufikia sasa hamna sijapokea ombi rasmi kutoka kwa mbunge yeyote,” Duale akaambia jarida la Jamvi.

Lakini kulingana na wabunge wandani wa Dkt Ruto, kutoitishwa kwa mkutano huo ndio sababu ya uwepo wa mgawanyiko unaoshuhudiwa katika chama hicho wakati.

Wanasema kuwa endapo mkutano huo hautaishwa hivi karibuni huenda hali hiyo ikadidimisha nafasi ya chama hicho tawala kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2022.

Mbunge wa Bomet ya Kati Ronald Tonui anasema wabunge wa Jubilee wanakinzana kimawazo kuhusu masuala ya kitaifa kwa sababu mkutano wa PG haujaitishwa ili waweze kuchukua msimamo mmoja kuhusu masuala hayo, hususan utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu ya Serikali.

Bw Tonui na wenzake wanasema kuwa Rais Kenyatta hajawahi kukutana na wabunge wa Jubilee kujadili suala hilo ambalo linavumishwa na serikali katika muhula wake wa pili afisini.

“Tulifanya mkutano wa mashauriano kupanga marudio ya uchaguzi wa urais mnamo Septemba baada ya mahakama ya juu kufutilia mbali ushindi wa raia Kenyatta. Mkutano mwingine ambao tulifanya na Rais ni pale alipokuwa akitaka kuwalazimisha wabunge kupitia Mswada wa Kifedha wa 2018 Novemba mwaka jana,” akasema Tonui.

Kulingana na mbunge huyo, inaonekana Rais Kenyatta anakwepa mkutano wa PG kimakusudi.

“Dhana inayojitokeza ni kwamba Rais ameanza kuwasawiri wabunge kama maadui wake badala ya kuwa washirika katika chama cha Jubilee na katika shughuli za kuendesha serikali.

Naye mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri anasema malumbano baina ya wabunge na Rais kwa upande mmoja na Naibu Rais kwa upande mwingine ni ishara ya kukita kwa migawanyiko ndani ya Jubilee.

“Kutoitishwa kwa mkutano wa PG kumeibua minong’ono na uvumi kuhusu mipango ya chama hiki tawala kuhusu urithi wa kiti cha urais na hatuwezi kunyamaza ikiwa mambo hayaendeshwi sawasawa,” akasema Bw Ngunjiri.

Sawa na wenzake, mbunge huyo anachukulia kuwa muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga pia umechochea mikinzano zaidi ya kimawazao na kimasilahi kati ya Rais na Naibu wake.

Mlima Kenya utahama Jubilee – Moses Kuria

Na NDUNGU GACHANE

MIVUTANO katika Chama cha Jubilee umezidi kutokota huku Mbunge wa Gatundu Kusini akitangaza mipango ya kuunda chama kipya kitakachotetea maslahi ya jamii za Mlima Kenya.

Bw Kuria Jumapili alieleza wazi kwamba uamuzi uliochangia kuvunjwa kwa chama cha zamani cha The National Alliance (TNA) ambacho Rais Uhuru Kenyatta alitumia kuwania urais mwaka wa 2013, uliacha Mlima Kenya bila namna ya kujitetea vilivyo kisiasa.

TNA kilivunjwa pamoja na vyama vingine vya muungano uliokuwepo wa Jubilee, kikiwemo Chama cha United Republican Party (URP) kilichoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kuunda Chama cha Jubilee ambacho kilishinda urais mwaka wa 2017.

Kauli ya Bw Kuria imetokea wakati ambapo joto la kisiasa linachacha katika Chama cha Jubilee kati ya mrengo unaounga mkono azimio la Dkt Ruto kuwania urais 2022, almaarufu ‘Team Tangatanga’, na kundi jingine linalokashifu kampeni za mapema almaarufu kama ‘Team Kieleweke’.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakidai kwamba kuna njama zinazoendelezwa kumzuia Dkt Ruto kufanikiwa katika uchaguzi wa urais ifikapo mwaka wa 2022 ikiwa ni pamoja na kuvuruga Jubilee.

“Tulikosea wakati tulipovunja chama chetu cha The National Alliance kwa sababu Jubilee ni chama kisicho na mwelekeo ambacho hatuwezi kutumia kufanya mipango yetu ya Mlima Kenya. Nitasajili chama kipya cha kisiasa ambacho kitawapa viongozi wa Mlima Kenya nafasi ya kufanya mipango kuhusu masilahi yetu ya siku za usoni serikalini,” akasema Bw Kuria.

Alikuwa akizungumza katika Kanisa Katoliki la Sabasaba, Kaunti ya Murang’a ambapo aliandamana na viongozi wengine wa Jubilee akiwemo Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome na mwenzake wa Maragua, Bi Mary Waithira pamoja na Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata.

Bw Kang’ata alikiri kwamba siasa zinazoendelezwa zimesababisha mgawanyiko wa viongozi na sasa chama kinaelekea mahali pabaya.

“Chama chetu kinaelekea pabaya kwa sababu pande mbili za Tangatanga na Kieleweke zinasababisha chuki miongoni mwa wale wanaochukuliwa kuwa wapinzani wao,” akasema.

Suala la iwapo Dkt Ruto atatumia Chama cha Jubilee kuwania urais 2022 limekuwa kwenye ndimi za baadhi ya wafuasi wake na wachanganuzi wa siasa kwa muda mrefu hasa tangu misukosuko ilipozidi katika Jubilee kuutokana na muafaka wa Rais Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani, Bw Raila Odinga.

Wakati mmoja, ilifichuka kwamba viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais walisajili vyama vipya na kushukiwa kuwa hayo yalikuwa maandalizi ya kujitafutia makao salama endapo Dkt Ruto ‘atasalitiwa’ na viongozi wa Jubilee wanaotoka Mlima Kenya.

Bi Wahome alitoa wito kwa Rais Kenyatta kuingilia kati ili kutuliza hali chamani na kuepusha mashua ya Jubilee kuzama katika dhoruba kali inayoshuhudiwa.

“Tulipiga kura kwa wingi kuwachagua Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto na tunamtegemea kiongozi wa chama kudhibiti hali iliyopo chamani kwa sasa,” akasema.

Ripoti zaidi na Valentine Obara

TAHARIRI: Mivutano Jubilee ikabiliwe, haifai nchi

NA MHARIRI

SIASA na mivutano ya kimamlaka inayoendelea katika Chama cha Jubilee (JP) inazidi kuongezeka, kwa kiwango ambacho sasa kimeanza kuzua hofu kuhusu uthabiti wa utulivu na amani nchini.

Kila wikendi, wabunge wa mirengo ya ‘Team Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ wamekuwa wakirushiana lawama kuhusu ubabe wa kisiasa na urithi wa Rais Uhuru Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

Hali hii imefikia upeo, kiasi kuwa baadhi ya wabunge wameanza kutusiana hadharani, bila kujali hadhira inayowatazama ama kuwasikiliza.

Kwa kuwa haya yote yanaendelea katika Chama cha Jubilee, ambapo kiongozi wake Rais Kenyatta, imefikia wakati ambapo inapasa aingilie kati na kudhibiti hali.

Mwelekeo huu si salama hata kidogo kwa uthabiti wa nchi, kwani baadhi ya wabunge hata wameanza kuendeleza kampeni za 2022 kiwazi, licha ya agizo la Rais kutofanya hivyo.

Katika majukwaa mengi, Rais Kenyatta amesisitiza kuwa lengo lake kuu katika muhula wake wa pili litakuwa kuiunganisha nchi, ili kupata mazingira mazuri ya kutimiza ahadi zake za maendeleo, hasa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Ni kutokana na hayo ambapo alibuni mwafaka wa kisiasa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ili kuondoa taharuki ya kisiasa iliyokuwepo nchini baada ya uchaguzi tata wa 2017.

Licha ya juhudi hizo, malumbano ya makundi hayo mawili yanatishia kuirejesha nchi pahali ilipokuwa kabla handisheki kupatikana, kwani baadhi wanaunga mkono muafaka huo na wengine wanaupinga.

Historia pevu ya jinsi ghasia hutokea nchini inaonyesha wazi kuwa mbinu kuu ambayo wanasiasa hutumia ni kuanza kujenga taharuki na chuki za kikabila.

Kwa hilo, huwa wanatumia hali hiyo kuvuruga uthabiti wa kisiasa ambao huwepo kujitakasa, huku wakiwalaumu washindani wao kwa athari ambazo baadaye hutokea.

Kama kiongozi wa nchi na Jubilee, Rais Kenyatta ana mamlaka ya kumwadhibu mwanachama yeyote ambaye anakiuka taratibu zilizowekwa.

Si mara moja ametoa maagizo na onyo kwa wabunge kukoma kujenga taharuki zisizofaa.Imefikia wakati ambapo anapaswa kudhihirisha mamlaka yake kwa kuchukua hatua zinazofaa.

‘Tangatanga’ wataka wapinzani watimuliwe Jubilee

NDUNG’U GACHANE na KENNEDY KIMANTHI

MIGAWANYIKO ya kisiasa jana ilizidi kutokota katika Chama cha Jubilee (JP), baada ya kundi moja la wabunge kushinikiza kufurushwa kwa wenzao ambao wanampinga Naibu Rais William Ruto.

Kundi hilo, maarufu kama ‘Team Tanga Tanga’ linakitaka chama hicho kuitisha mkutano wa haraka wa wabunge wote ili kuwaondoa wenzao wa kundi la ‘Kieleweke’ wanalodai linaunga mkono muungano wa Upinzani (NASA).

Wale waliozungumza na Taifa Leo, walisema wataendelea kuushinikiza uongozi wa chama kuhakikisha kuwa kundi la ‘Kieleweke’, limechukuliwa hatua kwa kutomheshimu Dkt Ruto.

Kundi linadai kuwa wanachama wa ‘Kieleweke’ wamekuwa wakitoa kauli za kumkosea heshima, licha ya kuwa mojawapo wa viongozi wakuu wa chama.

Kundi la ‘Kieleweke’ linawajumuisha Mbunge Maalum Maina Kamanda, aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa JP, Bw David Murathe, wabunge Maoka Maore (Igembe Kaskazini), Muturi Kigano (Kangema) na Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), ambaye ndiye mwanzilishi.

Lakini Jumapili, Katibu Mkuu wa JP, Bw Raphael Tuju alipuuzilia mbali pendekezo hilo, akisema kuwa lazima taratibu za chama zizingatiwe katika kumwondoa mwanachama yeyote.

Vile vile, alipuuza uwepo wa makundi hayo mawili, akisema kuwa hayana misingi yoyote ya kisiasa.

“Hakuna kundi lolote ambalo limetangaza kuwa si mwanachama wa Jubilee ama kuanza uhusiano na makundi mengine ya kisiasa,” akasema Bw Tuju.

Kulingana na kipengele 14 (7) cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa, mwanachama wa chama chochote anaweza kuondolewa tu ikiwa amekiuka katiba ya chama husika.

Vile vile, lazima mwanachama apewe nafasi ya kutosha kujitetea kulingana na taratibu zilizowekwa katika katiba hiyo.

Baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikizua migawanyiko katika chama hicho ni ushindani wa urithi wa Rais Uhuru Kenyatta, muafaka wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga na siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

Jumapili, mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, alidai kuwa kundi la ‘Kieleweke’ “linamfanyia kazi Bw Odinga na muungano wa NASA kuisambaratisha Jubilee.”

“Wanachama wengi wa kundi hilo walikuwa washauri na wanachama wa ODM. Tumekuwa wazi kuwa lengo kuu la muungano wa NASA lilikuwa kutumia handisheki ili kuleta migawanyiko Jubilee. Wanalenga kuzua migawanyiko kama walivyofanya baada ya chama cha Kanu kuungana na LDP,” akasema Bw Nyoro kwenye mahojiano.

Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Kirinyaga, Bi Wangui Ngirichi naye alisema kuwa ni kinyume na kanuni za Jubilee kwa mwanachama wake kuunga mkono chama ama kundi lingine la kisiasa.

“Hata ODM walimfurusha mbunge wa Malindi , Aisha Jumwa kwa dai la kuunga mkono Jubilee. Baadhi ya viongozi hawakuchaguliwa na wananchi, lakini wamekuwa wakiupigia debe Upinzani, kiasi cha kushinikiza muungano kati ya Jubilee na ODM. Ni lazima waondolewe katika Jubilee ili wapate muda wa kutosha kumfanyia kampeni Odinga,” akasema.

Hata hivyo, Bw Wambugu alisema kuwa ‘Kieleweke’ haimfanyii kampeni kiongozi yeyote.

Jubilee yakanganya Ruto kuhusu ODM kujiondoa

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Jubilee Jumatano kiliiondolea ODM aibu kilipothibitisha kuwa chama hicho kilijiondoa kutoka uchaguzi mdogo wa Wajir Magharibi, kufuatia makubaliano na uongozi wa vyama hivyo viwili.

Akiongea na wanahabari katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi, Katibu Mkuu Raphael Tuju, alisema hatua hiyo ililenga kupunguza joto la kisiasa nchini, ili kutoa nafasi kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupalilia maridhiano.

“Kujiondoa kwa ODM kunatokana na mashauriano, na makubaliano, kati ya safu ya juu ya uongozi wa vyama hivi viwili. Mashauriano sawa na hayo yalifanya Jubilee kutowasilisha wagombeaji katika chaguzi ndogo za Migori, Ugenya na Embakasi Kusini,” akasema Bw Tuju.

Kauli ya Jubilee inakinzana na kauli iliyotolewa na Naibu Rais William Ruto mnamo Jumanne, kwamba ODM ilijiondoa kutoka kinyang’anyiro hicho baada ya mgombeaji wake Prof Mohamed Yusuf Elmi kujiunga na chama cha Jubilee.

Kwenye taarifa iliyotumwa na kitengo cha habari za naibu rais (DPPS), Prof Elmi alihama ODM baada ya kushauriwa na viongozi na wazee wa ukoo wake wa Degodia.

Kabla ya taarifa ya Prof Elmi, ODM ilikuwa imetangaza kujiondoa kwenye uchaguzi huo kwa kile ilichosema ni katika moyo wa handisheki.

Taarifa hii inafanana na ile iliyotolewa na Bw Tuju, lakini inatofautiana na ile iliyotolewa na Dkt Ruto.

Lakini wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na kiongozi wa wengi bungeni, Bw Aden Duale, walisema ODM ilijiondoa kutoka uchaguzi huo mdogo ili kuzuia aibu ya kushindwa tena sawa na ilivyofanyika katika chaguzi ndogo za Ugenya na Embakasi Kusini.

Wameingia ‘box’ ya Jubilee?

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetangula wameonekana kumezwa na Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, kama Raila Odinga alivyomezwa.

Wiki iliyopita, wawili hao pamoja na Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, walishirikiana na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kuzindua usajili wa watu kidijitali na pia wakahudhuria hotuba ya rais bungeni.

Uwezekano kuwa hata Bw Mudavadi ameamua kufanya kazi na serikali umezua mjadala kuhusu kumalizwa kabisa kwa upinzani nchini.

Bw Mudavadi amekuwa akionekana kuwa mtu pekee aliyeweza kupuuza ushawishi wa Serikali na ndiye amekuwa sauti mpya ya kukosoa serikali.

Hii ni baada ya Bw Odinga kubadili msimamo na akakoma kukosoa serikali, na badala yake kuiunga mkono katika kila suala, kinyume na awali ambapo alikuwa sauti ya mwananchi.

Bw Kalonzo naye alitangaza mwaka jana kuwa atakuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Kenyatta huku Bw Wetangula akibakia kimya.

Lakini bw Mudavadi amekanusha kuwa amemezwa na Serikali: “Sijamezwa. Kilichopo ni kuheshimu ustaarabu wa Rais kutualika kila mmoja kibinafsi katika shughuli hizo mbili za kitaifa.”

Baada ya hotuba ya Rais Kenyatta kwa Bunge mnamo Alhamisi, Bw Mudavadi ndiye pekee aliyemkosoa kwa kukosa kuwaondoa mawaziri wanaochunguzwa kwa madai ya ufisadi.

Mabwana Odinga, Musyoka na Wetangula kwa upande wao walimpa Rais sifa kochokocho kwa hotuba yake, ambayo ilipuuza masuala muhimu zaidi kwa wananchi kama vile gharama ya juu ya maisha na njaa.

Kwa upande wake, Bw Wetangula yanayoshuhudiwa ni matukio ya kisiasa, lakini akasisitiza kuwa taifa haliwezi kutawaliwa kwa handisheki, mbali kinachohitajika ni sera zinazokubalika na wote.

Lakini kulingana na Mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing, kuhusika kwa wawili hao kwenye shughuli za kiserikali ni mbinu ya kisiasa.

“Hatua ya Kalonzo, Mudavadi na Wetangula kuanza kumkaribia Raila ni ishara wazi kuwa kinara wao anaondoka kwenye siasa. Kama fisi anavyofuata mtu akidhani mkono utaanguka aukule, hata hao wanafanya hivyo wakitarajia kunufaika Raila akiondoka,” akasema Bw Pkosing.

Alieleza kuwa mbinu nyingine ni kuwa wanasiasa hao wanataka kukaa karibu na Rais, kwa matumaini kuwa atawaunga mkono kuwania urais 2022.

Mchanganuzi wa siasa, Prof Macharia Munene anasema kuwa uhusiano wa majuzi kati ya Rais Kenyatta na vinara wa upinzani ni jambo ambalo limepangwa vizuri.

Naye Prof Peter Kagwanja anasema kuwa hatua hiyo ni matunda ya handisheki: “Ni dhihirisho kuwa mbinu ya Rais ya kuleta umoja nchini inafanikiwa. Rais amelipatia suala la umoja umuhimu mkubwa katika utawala wake.”

Kwa upande mwingine, hatua ya wakuu wa upinzani kukaribia Rais Kenyatta imezua upinzani kutoka kwa mrengo wa Naibu Rais William Ruto, ambao wanaiona kama yenye lengo la kumtenga zaidi tangu.

Dkt Ruto alikosa kushiriki uzinduzi wa usajili wa kidijitali kutokana na kile wadadisi wanasema ilikuwa kuonyesha kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Rais Kenyatta kuwashirikisha vinara wa upinzani.

Mgawanyiko katika Jubilee

UBASHIRI wa maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Samson Cherargei (Nandi) mwaka 2018 kuwa muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga ungevunja Jubilee, sasa umeonekana kutimia kufuatia migawanyiko inayoshuhudiwa ndani ya chama hicho.

“Ikifanana na mbata, ikitembea kama mbata na kuwika kama mbata, ni mbata. Bw Odinga anatuambia muafaka ni wa kuunganisha nchi, ilhali washirika wake wa kisiasa wanaongea kuhusu 2022. Hii inamaanisha hana nia nzuri katika suala hili,” alisema Bw Murkomen wakati huo.
Naye Bw Cherargei alisema: “Tunajua Raila amezoea kubomoa vyama lakini wakati huu hatutakubali.”
Mwaka mmoja baadaye, Jubilee sasa imegawanyika katika kambi mbili kuu, moja ikimuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na nyingine Naibu Rais William Ruto.

Makundi hayo mawili yamekuwa yakilumbana vikali, ishara kwamba huenda ikawa vigumu kuzima moto unaoteketeza nyumba ya Jubilee.

Mgawanyiko ndani ya Jubilee ulianza kujitokeza mara baada ya mwafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, wakati baadhi ya wanasiasa walipotilia shaka nia ya kiongozi huyo wa ODM hasa alipotuliza siasa kali ghafla, mwezi mmoja tu baada ya kuweka taifa kwenye taharuki kufuatia kiapo cha kuwa ‘rais wa wananchi’.

Wanasiasa hasa wa kambi ya Dkt Ruto, walikaribisha mwafaka huo kwa tahadhari na wameendelea hivyo hadi sasa, wakisema rekodi ya Bw Odinga katika maafikiano ya kisiasa ni ya mtu asiyeweka maagano. Hii ni kufuatia Bw Odinga kusambaratisha Kanu, kuondoka Narc, kuhama Cord na hatimaye NASA.

Vita dhidi ya ufisadi

Mbali na ‘handisheki’, mfarakano wa Jubilee pia umechochewa na vita dhidi ya ufisadi, siasa za urithi wa 2022 na mjadala kuhusu kura ya maamuzi.

“Masuala hayo manne ndiyo yanayomaliza Jubilee. Kufikia mwisho wa mwaka huu, chama hicho kitakuwa kimepasuka vipande vipande,” asema mbunge mmoja kutoka Mlima Kenya wa kambi ya Dkt Ruto.

“Nina hakika kuna mipango ya watu wanaotaka kutimiza malengo yao ya kibinafsi kuvunja Jubilee. Lakini kiini kikubwa ni muafaka ambao kwa kila hali umemtenga Naibu Rais serikalini,” alisema mbunge huyo ambaye aliomba tusitaje jina lake.
Wandani wa Dkt Ruto hasa kutoka eneo la Rift Valley, wanadai kwamba handisheki imevuruga mpangilio uliokuwepo wa chama cha Jubilee kuhusu 2022.

Wanasiasa walio msitari wa mbele kukosoa ‘handisheki’ ni maseneta Murkomen, Cherargei na Aaron Cheruiyot wa Kericho. Wengine ni wabunge Caleb Kositany wa Soy, Oscar Sudi wa Kapsaret na Gavana wa Nandi Stephen Sang.

Mara kwa mara, Dkt Ruto mwenyewe amekuwa akikosoa ‘handisheki’ akisema hailengi kuunganisha Wakenya bali kumtimua kutoka chama cha Jubilee.

“Hatutakubali mlete utapeli serikalini na kuvunja chama cha Jubilee, hili hatutakubali,” Bw Ruto amenukuliwa akisema mara kadhaa.

Kulingana na Seneta Murkomen, mjadala kuhusu kura ya maamuzi na vita dhidi ya ufisadi vinalenga azma ya Dkt Ruto ya kugombea urais.

“Nia ni kuleta mkanganyiko katika chama cha Jubilee ili mpangilio uliokuwepo awali usitimie,” Bw Murkomen amekuwa akisisitiza.

Waondoke Jubilee

Japo amejitenga na siasa, Rais Kenyatta alishangaza wengi kwa kuwaambia wakazi wa eneo la Mlima Kenyatta kwamba watashangaa atakapoteua mrithi wake.

“Hakujakuwa na mkutano wa kamati kuu ya chama au wabunge wa chama tangu ‘handisheki’,” alilalama Bw Cheruiyot majuzi.

Wabunge wa Jubilee wanaomuunga mkono Rais Kenyatta katika vita dhidi ya ufisadi nao wanamshinikiza Dkt Ruto na wandani wake kujiondoa serikalini badala ya kulalamika.

“Kama wanataka kuondoka serikalini waende bila kupiga kelele,” alisema mbunge wa kuteuliwa, Maina Kamanda.

“Hakuna mahali palipoandikwa kwamba ni lazima Ruto awe rais,” alinukuliwa Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu.

Kulingana na mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, Jubilee kimekufa na ni vigumu kukifufua, akiongeza kuwa eneo la Mlima Kenya limeanza kutafuta chama cha kutumia kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mpasuko zaidi Jubilee wabunge wakikabana koo

JOSEPH Beginner bodybuilding program: the coach’s exercises for training at home stanozolol reviews the zone – fitness, bodybuilding and nutrition myprotein. WANGUI na WYCLIFFE MUIA

MPASUKO katika chama cha Jubilee unaendelea kupanuka huku wabunge wa chama hicho tawala wakiendelea kurushiana cheche za maneno kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi.

Siku chache baada ya wabunge wa Jubilee kutoka Rift Valley kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta kwa madai ya kumhujumu naibu wake William Ruto, wenzao wa Kati wamejitokeza kutetea msimamo wa Rais kuhusu vita dhidi ya ufisadi.

Wabunge hao Rahim Dawood (Imenti Kaskazini), Muturi Kigano (Kangema) na Maina Kamanda (maalum), wamewakashifu wenzao wa Rift Valley kwa kuingiza siasa katika juhudi za kupambana na ufisadi nchini.

Viongozi hao wa Kati walimtaka Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi kukoma kumshambulia Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.

“Murkomen na Sudi wanapaswa kukoma kumshambulia DCI. Kwa nini wanapiga kelele hata kabla ya uchunguzi kukamilishwa?,”alishangaa Bw Kamanda.

Bw Kamanda alidai baadhi ya viongozi wa Rift Valley wanataka kutibua uchunguzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer kwa sababu wanahusika katika sakata hiyo.

“Kuna hofu kuwa ukweli utafichuliwa hivi karibuni na wale ambao hawana hatia hawapaswi kutetemeka,”aliongeza Bw Kamanda.

Naye Bw Dawood aliwasuta baadhi ya wabunge wa Rift Valley kwa kulemaza juhudi za kupambana na ufisadi na kutaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) pamoja na maafisa wa DCI wasitishwe na yeyote.

Haya yanajiri siku chache baada ya mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria kudai kuwa chama cha Jubilee kimevunjika tayari.

Siku chache zilizopita, Murkomen na Sudi waliongoza wabunge wa Rift Valley kuwakashifu maafisa wa DCI na DPP kwa madai ya kugeuza vita dhidi ya ufisadi kumhujumu Naibu Rais katika siasa za 2022.

Hata hivyo, Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos Jumatatu alitofautiana na wenzake kuhusu vita dhidi ya ufisadi na kumuomba radhi Rais kuhusiana na matamshi makali yaliyotolewa mwishoni mwa juma na baadhi ya wenzake kuhusu uchunguzi unaoendelea wa sakata ya ujenzi wa mabwawa mawili katika kaunti yake.

Wiki iliyopita, baadhi ya wabunge walitishia kuongoza maandamano dhidi ya serikali ikiwa Rais Kenyatta atathubutu kusitisha ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer kwa sababu ya madai ya wizi wa Sh21 bilioni za kufadhili miradi hiyo.

Wakiongozwa na Daniel Rono (Keiyo Kusini), Kangogo Bowen (Marakwet Mashariki), William Kisang (Marakwet Magharibi) wabunge hao walisema wako tayari kuanzisha uasi dhidi ya utawala wa Rais Kenyatta ikiwa miradi hiyo itasimamishwa kwa sababu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu sakata hiyo.

Spika wa bunge la Elgeyo Marakwet, Bw Philemon Sabulei alisema madai ya ufisadi yanayoelekezwa katika mabwawa ya Kimwerer na Arror yanaongozwa na siasa za ubinafsi wala si vita dhidi ya ufisadi.

Bw Sabulei alidai kuwa vita hivyo vinalenga kuzima azma ya naibu kuelekea Ikulu 2022.

Viongozi hao waliapa iwapo waziri wa fedha Henry Rotich ataachishwa kazi kama ilivyokuwa kwa waziri wa michezo Rashid Achesa, jamii ya Wakalenji haitakuwa na budi ila kujitoa katika muungano wa Jubilee na kutafuta mbinu nyingine ya kumwezesha Naibu Rais kutwaa uongozi wa nchi 2022.

JAMVI: ‘Nyumba ya Jubilee itaporomoka kabla ya 2022’

Na BENSON MATHEKA

Matukio ya hivi punde katika uga wa siasa nchini yanaashiria kwamba huenda chama tawala cha Jubilee kikaporomoka kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wanataja misimamo tofauti ya viongozi wa chama hicho kuhusu vita dhidi ya ufisadi, muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na miito ya kura ya maamuzi kama masuala yanayoweza kuharakisha kusambaratika kwa chama hicho.

Wengi wanahisi kwamba viongozi wa chama cha Jubilee Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Wake William Ruto wametofautiana vikali kuhusu masuala hayo matatu jambo linaloonyesha mpasuko katika chama hicho unaendelea kupanuka.

Kulingana na mwanauchumi maarufu Dkt David Ndii ambaye alikuwa mwanamikakati wa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, ni dhahiri kwamba Jubilee hakiwezi kudumu hadi uchaguzi mkuu ujao.

“Jubilee kilibuniwa kwa sababu ya kesi zilizowakabili viongozi wake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambazo kwa sasa haziko. Hakuna cha kuwaunganisha,” Bw Ndii alisema akihojiwa na runinga moja ya humu nchini Jumatano usiku.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2013, Rais Kenyatta na Bw Ruto waliendesha kampeni yao wakitumia kesi zilizowakabili ICC kurai jamii zao kuwachagua.

Bw Ndii alisema kuna hisia kwamba Bw Ruto ni hatari kuwa rais wa Kenya na hivyo kuna juhudi za kumzuia ili asimrithi Rais Kenyatta jambo ambalo litavunja Jubilee.

Mwishoni mwa mwaka jana, aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe, mwandani wa Rais Kenyatta alitangaza wazi kwamba atahakikisha Bw Ruto hataingia Ikulu.

Rais Kenyatta alijitenga na kauli ya Bw Murathe akisema wakati wa siasa ulipita.

Wadadisi wanasema msimamo wa Bw Ruto na wandani wake kwamba vita dhidi ya ufisadi vimeingizwa siasa ni dhihirisho kwamba nyumba ya Jubilee iko njia panda.

“Hatua ya Bw Ruto ya kulaumu asasi ambazo Rais Kenyatta anasema ana imani nazo katika vita dhidi ya ufisadi na matamshi ya wandani wake kwamba ni jamii moja inayolengwa yanaonyesha nyumba ambayo imegawanyika,” asema Bw Joram Kasumbi mtaalamu wa masuala ya kisiasa.

Katika muda wa wiki moja, Bw Ruto amekuwa akilaumu Idara ya Upelelezi wa Jinai kwa kudai kwamba Sh21 bilioni zilizolipwa kwa ujenzi wa mabwawa mawili Elgeyo Marakwet zilipotea.

Hata hivyo, Rais Kenyatta anasisitiza kuwa idara hiyo inafaa kupatiwa nafasi kufanya kazi yake akisema ana imani nayo.

Ingawa Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa muafaka wake na Bw Odinga ulilenga kuunganisha nchi iliyogawanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Ruto amekuwa akimlaumu kiongozi wa chama cha ODM kwa kuvuruga chama cha Jubilee. Mara kwa mara, amekuwa akimlaumu Bw Odinga kwa kutaka kuvunja chama hicho tawala na kuapa kwamba hatakubali kutimuliwa katika serikali aliyokuwa msitari wa mbele kuunda.

Kulingana na mdadisi wa siasa Bw Ocheing Kadundi, kuporomoka kwa Jubilee kunatokana na muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga. “Muafaka ulitikisa nyumba ya Jubilee ambayo haikuwa na msingi imara na sasa kuporomoka kwake hakuepukiki,” alisema Bw Kadundi.

Kulingana na Bw Kasumbi, nafasi ya salamu zilizotumiwa kama alama ya Jubilee 2017 ilichukuliwa na salamu za Rais Kenyatta na Bw Odinga 2018.

“Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mwisho wa ndoa ya Jubilee,” asema.

Wadadisi wanakubaliana kwamba kilichowaleta pamoja viongozi wa Jubilee ni kesi zilizowakabili pekee.

“Rais Kenyatta sasa hamhitaji Bw Ruto alivyokuwa akimhitaji walipougana 2013 kubuni muungano wa Jubilee na walipovunja vyama vyao kuunda chama c?ha Jubilee,” aeleza.

Bw Kasumbi asema viongozi wa Jubilee wametofautiana kama ardhi na mbingu kuhusu suala la marekebisho ya katiba. “Ingawa Rais Kenyatta hajazungumzia hadharani miito ya kubadilisha katiba, wandani wake wanayaunga mkono ilhali Bw Ruto na wandani wake wanayapinga. Katika hali kama hii, Jubilee haiwezi kudumu,” aeleza.

Hisia za Bw Ruto na washirika wake ni kwamba marekebisho ya kikatiba yanalenga kumzuia asishinde au asigombee urais ilhali wale wanaomuunga Rais Kenyatta wanasema yatahakikisha Wakenya wataishi kwa amani.

“Rais Kenyatta hajazungumzia miito ya kurekebisha katiba hadharani, mshirika wake katika handisheki, Bw Odinga, hasimu mkuu wa Bw Ruto, anasisitiza ni lazima yafanyike. Ukimsikiliza kwa makini Rais Kenyatta kwenye baadhi ya hotuba zake, utapata dokezo kuhusu msimamo wake kwa vile amekuwa akisizitiza siku za mshindi wa uchaguzi kutwaa mamlaka yote zimepita,” alisema.

Kulingana na Bw Kadundi, Jubilee haiwezi kudumu katika mazingira ya kisiasa yaliyopo nchini kwa wakati huu.

Mdadisi wa siasa Profesa Makau Mutua anasema kusambaratika kwa jubilee sio suala la ikiwa kutatokea.

“Uhuru Kenyatta hana haja na Jubilee kwa sababu anahudumu kipindi cha mwisho na ndio maana itaporomoka na Bw Ruto hataweza kuiokoa,” alisema Profesa Mutua.

JAMVI: Kibarua kigumu kwa Ruto kuokoa jahazi la Jubilee linalozama

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto huenda akawa na kibarua kigumu ‘kufufua’ chama cha Jubilee ambacho kinaonekana kutelekezwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Chama cha Jubilee kimeanza kuonyesha dalili za kusambaratika licha ya viongozi wake kushikilia kuwa kingali imara.

Wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Naibu wa Rais wamekuwa wakishinikiza kujiuzulu kwa viongozi wa sasa wa Jubilee, akiwemo Katibu Mkuu Raphael Tuju.

Wandani wa Dkt Ruto wanadai kuwa viongozi wa sasa wa Jubilee wanahujumu juhudi za naibu wa rais kutaka kuingia Ikulu baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022.

Mzozo unaoendelea kutokota ndani ya Jubilee imesababisha chama hicho kusitisha mpango wake wa kufungua afisi za chama katika kaunti zote 47.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa pia wanaonya kuwa uchaguzi wa viongozi wote kuanzia mashinani hadi ngazi ya kitaifa mwaka ujao huenda ukagonga mwamba iwapo mvutano uliomo chamani hautatafutiwa ufumbuzi upesi.

Chama cha Jubilee kinapanga kuandaa uchaguzi wa viongozi wake, muda wa kuhudumu wa viongozi wa muda utakapokamilika 2020.

Dkt Ruto, hata hivyo, ameshikilia kwamba chama cha Jubilee kingali imara na atakitumia katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Alipokuwa akimpokea mwaniaji wa ubunge wa Wajir Magharibi Ahmed Kolosh aliyegura ODM na kujiunga na Jubilee, Naibu wa Rais Ruto alionnekana kudokeza kwamba angali na nia ya kuhakikisha kuwa chama cha Jubilee kinaendelea kuwa imara.

Dkt Ruto aliyekuwa ameandamana na Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale na Bw Tuju alisema kuwa chama cha Jubilee kimejitolea kwa hali na mali kushinda kiti cha Wajir Magharibi.

“Chama cha Jubilee kitashiriki katika uchaguzi wa Wajir Magharibi kwa kutumia sera na masuala yanayohusu wananchi,” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais anatarajia kutumia chama cha Jubilee kuwania urais 2022 licha ya kuwepo na shinikizo za kumtaka kuuunda chama kipya.

Kulingana na Felix Otieno, ikiwa Dkt Ruto ataunda chama kipya sasa huenda akapoteza kiti cha unaibu rais kwa sababu alichaguliwa pamoja na Rais Kenyatta kwa kutumia .

“Mbali na kuwepo na shinikizo za kumtaka kujiuzulu, itakuwa vigumu kwa chama hicho kipya kupata uungwaji mkono kabla ya 2022,” anasema Bw Otieno.

Hata hivyo, Bw Otieno anasema kuwa Naibu wa Rais atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha kuwa chama cha Jubilee kinaendelea kuwa na ushawishi nchini hadi 2022.

Tangu kuchaguliwa kwa muhula wa pili mwaka jana, Rais Kenyatta amesalia kimya kuhusu hatima ya Jubilee, hatua ambayo imezua hali ya hofu miongoni mwa wanachama.

Kadhalika, Rais Kenyatta haijaitisha kikao na wanachama wa Jubilee ili kuwaelezea kuhusu hatua yake ya kutia mkataba wa ushirikiano na kinara wa ODM Raila Odinga.

Kongamano la viongozi wa Jubilee lilofaa kufanyika Naivasha mnamo Julai mwaka jana mjini Naivasha liliahirishwa na kulingana na Bw Tuju halitafanyika hivi karibuni.

Naibu wa Rais pia anakabiliwa na upinzani na baadhi ya viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya, haswa wanasiasa waliopoteza katika uchaguzi uliopita.

Mwezi uliopita kundi la viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na Maina Kamanda (Maalumu), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Paul Koinange (Kiambaa), Muturi Kigano (Kangema), Naomi Shaban (Taveta) waliwataka wanasiasa wanaompigia debe Dkt Ruto kuhama Jubilee.

Kulingana na wabunge hao, wanasiasa hao hawana heshima kwa Rais Kenyatta ambaye amewataka wanasiasa wa Jubilee kujiepusha na kampeni za mapema za uchaguzi ujao wa 2022.

“Ikiwa wanasiasa hao wanaotembea na naibu wa rais wanadhani kwamba anaweza kuwasaidia wajiuzulu kutoka Jubilee na wawanie tena kwa kutumia vyama tofauti,” akasema aliyekuwa mbunge wa Dagoreti Kusini Dennis Waweru.

Kulingana na mhadhiri wa siasa Prof Macharia Munene, endapo kutakuwa na kura ya maamuzi basi vyama vipya huenda vikajitokeza na huo huenda ukawa mwisho wa Jubilee.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wanataka kufanywa kwa kura ya maamuzi ili kupanua serikali na kujumuisha jamii zote.

Dkt Ruto, hata hivyo, anapinga vikali kwa kusema kuwa hataruhusu katiba kufanyiwa mabadiliko ili kuongeza vyeo.

“Naibu wa Rais amejitokeza na kusema kuwa atapinga rasimu ya katiba endapo vipengee vya kubuni nyadhifa zaidi vitaingizwa. Hiyo inamaanisha kwamba huenda akawa upande tofauti na Rais Kenyatta,” anasema Prof Munene.

“Ikiwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto watakuwa katika mirengo tofauti wakati wa kampeni za kutaka kubadilisha katiba, basi huo utakuwa mwisho wa Jubilee,” anaongezea.

Uhuru awataka wabunge wa Jubilee wasiounga mkono serikali wang’atuke

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amewaonya wabunge waasi wa Jubilee ambao hupinga misimamo ya chama hicho na ajenda za serikali bungeni.

Rais alisema kuwa wabunge kama hao wanafaa kujiuzulu ikiwa hawataki kuunga mkono agenda za chama hicho tawala.

Duru ziliambia Taifa Leo Dijitali kwamba kiongozi wa taifa alitoa onyo hilo Jumatano katika Ikulu ya Mombasa kwenye kikao cha kuratibu ajenda zake bungeni mwaka huu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, maspika Justin Muturi (Bunge la Kitaifa) Ken Lusaka (Seneti) na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju.

Wengine waliokuwepo ni uongozi wa mrengo wa serikalini bungeni; Adan Duale (Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa), Kipchumba Murkomen (Kiongozi wa wengi katika seneti), Moses Cheboi (Naibu Spika bunge la kitaifa), Profesa Kithure Kindiki (Naibu Spika Seneti) na kiranja wengi katika seneti Irungu Kang’ata.

Rais aliukaripia uongozi wa Jubilee bungeni kwa kufeli kuwadhibiti wabunge wa chama hicho, akitoa mfamo wa kisa ambapo nusra Mswada wa Fedha uangushwe.

Hii ni baada ya baadhi ya wabunge wa Jubilee kuungana na wenzao wa upinzani kupinga kuanzisha kwa ushuru wa thamani ya ziada (VAT).

Hata hivyo, njama zao ziligonga mwamba kutokana na hila za wabunge watiifu kwa Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambapo waliondoka nje na kupunguza idadi ya wabunge hitajika kubatilisha pendekezo la Rais kwenye mswada huo.

Baada ya wabunge wa Jubilee waliopinga mswada huo ni James Lomenen (Turkana Kusini), Catherine Waruguru (Mbunge Mwakilishi wa Laikipia), Didmus Barasa (Kimilili), Cornel Serem (Aldai), kati ya wengine.

Ilidaiwa wengi wa wabunge wa Jubilee waliopinga mswada huo ni wale wa mrengo unaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu 2022, maarufu kama wanachama wa “Team Tangatanga”.

“Uhuru amesema kuwa wabunge wote wa Jubilee watahitajika kuunga mkono ajenda za serikali la sivyo wang’atuke,” mbunge mmoja ambaye alihudhuria kikao hicho, lakini akaomba jina lake libanwe, akaambia Taifa Leo.

“Aliwataka wabunge hao kuunga mkono Agenda Nne Kuu za Serikali na kazi ya Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji,” akaongeza huku akiongeza kuwa wabunge walitakiwa kuonyesha umoja bungeni.

Rais alimgeukia Bw Tuju na kumwamuru ahakikishe kuwa kamati ya nidhamu ya chama hicho imeimarishwa ili kukabiliana na wabunge waasi.

“Hii, alisema, inajumuisha, kuwafurusha kutoka chama cha kilichowadhamini bungeni,” mwanasiasa huyo alieleza.

Mapema mwezi huu mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri alimshutumu Rais Kenyatta kutokana na hatua yake ya kushirikiana na Bw Odinga akisema hatua hiyo inalenga kuhujumu nafasi ya Bw Ruto kuingia Ikulu.

Naye mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alionekana kumlaumu Rais Kenyatta kwa kile alichosema ni mwenendo wake wa kupeleka maendeleo kwingineko na kuipa kisogo eneo la Mlima Kenya ambalo lilimpa kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Wazee wapuuza madai ya vurugu Jubilee isiposimama na Ruto

Na FRANCIS MUREITHI

BARAZA la Wazee wa Jamii ya Wakalenjin katika Kaunti ya Nakuru , limepuuzilia mbali madai ya vurugu iwapo Naibu wa Rais William Ruto, hataungwa mkono na chama cha Jubilee katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

“Kaunti ya Nakuru itaendelea kuwa na amani hata kama Naibu wa Rais atakosa tiketi ya Jubilee kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao. Madai kwamba kutakuwa na vurugu hayana msingi na ni porojo zinazolenga kuzua hali ya taharuki,” akasema Mshirikishi wa Baraza la Wakalenjin, Bw Andrew Yatich.

Wakati huo huo, katibu wa chama cha ODM tawi la Nakuru, Bw Hilton Abiola alimshtumu mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri huku akimtaka amheshimu Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

Bw Yatich ambaye ni msimamizi wa masuala ya amani katika baraza hilo, alisema jamii hiyo haifai kuhusishwa na kauli hiyo ya kuchochea vurugu.

“Wazee wa jamii ya Wakalenjin hatuna mawazo hayo potovu kuhusu kuzua vurugu ikiwa Dkt Ruto atanyimwa tiketi ya Jubilee 2022 kuwania urais. Hakutakuwa na machafuko Nakuru,” akasema Bw Yatich. Wazee wa baraza hilo waliitaka serikali kukabiliana na wanasiasa wanaoongoza vijana kufanya maandamano dhidi ya Rais Kenyatta mjini Nakuru.

“Rais ni nembo ya umoja wa kitaifa na wanasiasa kama mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri ambao wameonyesha ukaidi wanafaa kukabiliwa vikali,” akasema Bw Yatich.

Wazee wa Jamii ya Wakalenjin pia walishutumu baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya wanaodai kuwa wametelekezwa na Rais Kenyatta katika miradi ya maendeleo.

“Rais anaitakia nchi hii mema, si kura za Mlima Kenya pekee zilizomfanya Rais Kenyatta kuingia mamlkani. Alipata kura kutoka kila eneo la nchi hii na aliapa kuwatumikia Wakenya wote bila ubaguzi,” akasema Bw Yatich.

Alisema matamshi hayo ya Bw Ngunjiri yanalenga kuzua hali ya taharuki haswa katika maeneo ya Nakuru.

“Wanasiasa wanafaa kukumbatia na mpango wa R ais Kenyatta na Bw Odinga wa kutaka kuunganisha Wakenya wote na kuzika tofauti za kikabila zisiozkuwa na manufaa kwa Wakenya,” akasema.

Chama cha Jubilee chasimama na ‘Baba’

CHARLES WASONGA Na WANDERI KAMAU

CHAMA cha Jubilee Jumatano kilijitokeza kumtetea kiongozi wa ODM, Raila Odinga dhidi ya shutuma za baadhi ya viongozi kuwa ndiye kiini cha mizozo inayokikumba kwa sasa.

Katibu Mkuu Raphael Tuju alitetea muafaka wa maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga akisema unaafikiana azma ya Jubilee ya kuunganisha Wakenya wote na kamwe hahusiki katika mzozo wa chama hicho.

“Azma ya chama chetu, ambayo imekuwa ikikaririwa na Rais Kenyatta kila mara ni kuunganisha Wakenya wote bila kujali misingi yao ya kidini, rangi, kabila au vyama vya kisiasa. Ni moyo huu ambao ulimwongoza Rais kuweka muafaka kati yake na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga,” akasema Bw Tuju.

Chama cha Jubilee kimekumbwa na mizozo ya ndani kutokana na suala la urithi, huku baadhi ya wakuu wake wakisisitiza Naibu Rais William Ruto hatapewa tiketi ya moja kwa moja kuwania urais 2022, nao wafuasi wake wakiitisha uchaguzi na mageuzi ya chama.

Bw Tuju alisema mzozo unaokumba Jubilee unatokana na wanachama ambao wanaongozwa na siasa za kikabila na hawataki kukubali ukweli wa mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Kauli hiyo iliungwa mkono na viongozi wa eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na waliokuwa wabunge Peter Kenneth na Martha Karua, ambao walimsifu Bw Odinga na Rais Kenyatta kwa kuweka tofauti zao kando kwa ajili ya amani na umoja wa taifa.

“Ni maoni yetu kuwa baadhi ya wanasiasa wasio na uzalendo wana nia ya kuvuruga juhudi za maridhiano ili kujinufaisha binafsi kisiasa,” akasema Bw Kenneth kwenye taarifa.

Wanasiasa wanaoegemea kilichokuwa chama cha URP kabla ya kuingia Jubilee, wamekuwa wakilalamika kuwa Bw Odinga anatumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kuingia kwenye serikali na kuvuruga umoja wa Jubilee.

Tangu mwafaka huo, Rais ameonekana kuwa na urafiki wa karibu na Bw Odinga na wamekuwa wakiandamana kwenye hafla nyingi za kiserikali na za kibinafsi, huku akimwita “ndugu yangu” kwenye hotuba zake.

Suala hilo limeonekana kuwakera baadhi ya wanasiasa wa Jubilee ambao wanaonelea kuwa rais anaegemea zaidi kwa Bw Odinga, ambaye alikuwa adui yake mkuu kisiasa kwenye uchaguzi wa 2017, na kumtenga naibu wake William Ruto.

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri mnamo wikendi alimshutumu rais akisema amesahau mchango wa Bw Ruto katika kampeni zake za urais 2013 na 2017.

Mzozo huo pia umechochewa na maoni kuwa Bw Odinga anataka kuvunja chama hicho tawala kwa lengo la kujiweka katika nafasi bora ya kushinda urais 2022. Lakini Bw Odinga amekuwa akikanusha madai hayo.

Baadhi ya wakosoaji wake wanasema historia yake ya kuvuruga vyama na miungano ambayo amekuwa nayo awali ndiyo inayowatia wasiwasi kuwa nia yake ni kusambaratisha Jubilee.

Mzozo wa sasa ulipamba moto kufuatia matamshi ya aliyekuwa naibu mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe kwamba hakukuwa na maafikiano kuwa Bw Ruto atakuwa mgombea urais kwa tiketi ya Jubilee 2022.

Matamshi ya Bw Murathe yalisababisha cheche ndani ya Jubilee huku baadhi ya viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru wakitaka yeye na Bw Tuju watimuliwe na maafisa wapya wachaguliwe. Bw Murathe alijiuzulu wiki jana.

Mzozo huo wa Jubilee unatishia kufanikiwa kwa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo pamoja na uboreshaji wa maisha ya Wakenya kutokana na migawanyiko ambayo imeibuka serikalini.

Katika maeneo mbambali ya nchi kumeibuka kambi ambapo moja inaegemea upande wa Bw Ruto maarufu kama “Team Tanga Tanga” na nyingine inayompinga. Maeneo ambako kambi hizi zimeshamiri ni Mlima Kenya, Magharibi na Pwani.

Migawanyiko hii hasa miongoni mwa wabunge, imepatia siasa kipa umbele kuliko maendeleo, hali ambayo imezima matumaini ya wananchi kutimiziwa ahadi ambazo waliahidiwa kwenye uchaguzi wa 2017.

Eneo la Mlima Kenya ndilo limeonekana kutatizwa zaidi na siasa za 2022 huku viongozi wakigawanyika na kutumia muda wao mwingi kwenye siasa.

Jubilee ijifunze kutokana na ODM – Murkomen

Na WYCLIFFE MUIA

SENETA wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen sasa anataka chama chake cha Jubilee kuiga mfumo wa usimamizi wa chama cha ODM na kusema anatamani sana iwapo Jubilee ingekuwa na mfumo wa uongozi kama chama hicho cha upinzani.

Akihojiwa katika televisheni moja ya humu nchini jana asubuhi, Bw Murkomen alisema chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kina nidhamu zaidi kuliko Jubilee.

“Ninatamani sana uongozi wa ODM licha ya changamoto nyingi chama hicho kinapitia,”alisema Bw Murkomen.

Bw Murkomen ambaye pia ni kiongozi wa walio wengi katika Seneti alisifu jinsi chama cha ODM kilivyodhibiti mawimbi ya kisiasa yaliyoibuka baada ya Bw Odinga kuanza kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018.

“Hata wakati wa handisheki, Waziri huyo Mkuu wa zamani aliwaita wanachama wake na kuwaelezea walichozungumzia na Rais Kenyatta,”alisema Bw Murkomen akiashiria makosa ya Rais Kenyatta kushindwa kuelezea wanachama wa Jubilee makubaliano yake na Bw Odinga.

Alisema kuna haja ya Jubilee kuiga miundo ya uongozi ya ODM ili kulainisha mizozo na kuweka mfumo mwema wa kufanya maamuzi muhimu ya chama.

“ODM imedumu kwa miaka 10 na sisi tumehudumu tu kwa miaka mitano. Kuna haja ya kujifunza mengi kutoka kwa ODM,”akasema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe kujiuzulu na kusisitiza kuwa Naibu Rais William Ruto hafai kuwania urais 2022.

Msimamo wa Bw Murathe umezua joto jingi katika Jubilee huku baadhi ya wabunge wakimtaka Rais Kenyatta kujitokeza na kueleza wazi msimamo wake kuhusu mzozo ndani ya chama chake.

Bw Murkomen alisema uongozi wa Jubilee unapaswa kuleta maridhiano ili kuzuia chama kuporomoka.

“Murathe bado ni mwanachama wa Jubilee na tunamhitaji chamani. Kuna haja ya kuwepo na maridhiano ili kuzima migawanyiko zaidi,” alisema Semeta huyo.

Naye Seneta maalum wa Jubilee Isaac Mwaura alisema ni wazi chama hicho kinaendelea kuporomoka na kumlaumu Bw Odinga kwa masaibu hayo.

“Ukweli mchungu ni kuwa ndoa ya Jubilee imefika mwisho. Raila alifanikiwa kuvunja NASA na sasa baada ya kujiunga na Jubilee, matokeo ni yale yale,”alisema Bw Mwaura.

Mbunge wa Sirisia John Waluke aliunga mkono kauli ya Bw Mwaura akisema muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga umekuwa laana kwa chama cha Jubilee.

“Kazi haijakuwa ikifanyiki tangu Raila aungane na Rais Kenyatta…Rais hashughulikii chama cha Jubilee tena. Tunataka tumsaidie Rais aondoke katika hii nyororo ambayo amewekwa na Raila,” alisema Bw Waluke.

Mzozo ndani ya Jubilee ni hatari kwa muafaka, mashirika yaonya

Na VALENTINE OBARA

MASHIRIKA mbalimbali yameonya kuwa mizozo ya Chama cha Jubilee inahatarisha mafanikio yaliyopatikana kufikia sasa kutokana na muafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga.

Mwafaka huo wa Machi 9, umekuwa ukisifiwa na wengi kuleta utulivu wa kisiasa kwa kiwango cha kutoa mandhari bora ya kibiashara.

Chama cha Kitaifa cha Biashara na Viwanda (KNCCI) kimesema siasa za urithi wa 2022 na kura ya maamuzi zinaweza kuathiri ukuaji wa uchumi.

Kulingana na Mweneyekiti wa Kitaifa wa chama hicho, Bw Kiprono Kittony, biashara nyingi zingali zinatatizika kurejelea hali ya kawaida baada ya kuathirika wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa 2017 na hivyo basi ni muhimu utulivu udumishwe.

“Tunaomba wanasiasa waepuke kampeni za mapema tunazoshuhudia. Bado ni mapema mno kuruhusu siasa za urithi kuteka midahalo yetu ya kitaifa,” akasema, kwenye taarifa.

Aliongeza: “Tutumieni 2019 na 2020 kujenga uchumi wetu na kuleta umoja wa nchi kupitia kwa mipango tofauti kama vile hadnsheki.”

Msimamo sawa na huu ulitolewa na Baraza la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Mwenyekiti wa kitaifa wa baraza hilo, Bw Stephen Cheboi, alikosoa wanaoingiza siasa kwenye mwafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga na kuwataka watazame mwafaka huo kama njia ya kusaidia wananchi.

Alizidi kuambia viongozi wajiepushe na kutusi wenzao hadharani.

Mvutano katika Chama cha Jubilee umezidi kushuhudiwa wiki hii kufuatia malumbano kati ya Rais Kenyatta na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wanaodai amepuuza eneo hilo kimaendeleo licha ya kumwezesha kushinda urais mara mbili mfululizo.

Jubilee pia kinakumbwa na misukosuko baada ya aliyekuwa Naibu Mwenyekiti, Bw David Murathe, kudai hapakuwa na maelewano yoyote kwamba Naibu Rais William Ruto ataungwa mkono kuwania urais na jamii ya Wakikuyu ifikapo mwaka wa 2022.

Matamshi ya Murathe yaipasua Jubilee

Na WAANDISHI WETU

MATAMSHI ya Naibu Mwenyekiti wa chama tawala cha Jubilee, David Murathe kuwa eneo la Mlima Kenya halitamuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 yamezua joto kali ndani ya chama hicho.

Mnamo Jumatano Bw Murathe alisema hakuna mkataba wowote kati ya Dkt Ruto na jamii ya Mlima Kenya kuhusu uchaguzi wa 2022, matamshi ambayo yalipandisha joto katika kambi ya Naibu Rais jana.

Wandani wa Dkt Ruto na wabunge kutoka Mlima Kenya walimkashifu Bw Murathe na kupuuzilia matamshi yake kama yasiyo na msingi huku wengine wakitaka atimuliwe chamani.

Seneta wa Nandi, Samuel Cherargei na Mbunge wa Soy, Caleb Kositany walimkashifu Bw Murathe wakidai amelipwa na mahasimu wa Dkt Ruto kumchafulia jina.

“Tunajua Murathe ni tapeli wa kisiasa ambaye anatumiwa kumharibia Naibu Rais jina,” akasema Bw Cherargei.

Mbunge wa Kuresoi Kusini, Joseph Tonui na mfanyabiashara Shadrack Koskei nao walimkashifu Bw Murathe na kumtaka kuomba msamaha kufuatia matamshi yake.

“Matamshi ya Bw Murathe hayakufaa kwani Dkt Ruto ndiye aliyeongoza kampeni za Rais Kenyatta katika chaguzi za 2002, 2013 na 2017. Tayari ana uungwaji mkono kote nchini,” akasema Bw Koskei.

Baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya pia walimkashifu Bw Murathe na kutaka avuliwe mamlaka katika Jubilee. Viongozi hao pia walimtaka Rais Kenyatta kujitokeza kukanusha matamshi ya Bw Murathe.

Wabunge Gichunge Kabeabea (Tigania Mashariki), Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) na Kathuri Murungi (Imenti Kusini) walisisitiza kuwa eneo hilo lilifanya uamuzi wa kuunga mkono Dkt Ruto katika azma yake ya urais 2022.

“Uhuru anafaa kuitisha uchaguzi wa chama mara moja ili Murathe aondolewe kwani analeta utengano katika chama,” akasema Bw Dawood.

Katika Kaunti ya Nyeri, Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua alimkashifu Bw Murathe akisema matamshi yake hayakuwakilisha eneo la Mlima Kenya, msimamo ulioungwa mkono na Mwenyekiti wa Jubilee Kaunti ya Kirinyaga, Muriithi wa Kang’ara na Mbunge wa Mukurweini, Anthony Kiai waliotaja matamshi ya Bw Murathe kuwa yake binafsi.

Wabunge Patrick Munene wa Chuka/Igambang’ombe na Gitonga Murugara wa Tharaka nao walisema wabunge wa Jubilee hawajawahi kujadili kuhusu mambo aliyozungumzia Bw Murathe.

Lakini Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu na aliyekuwa Mbunge wa Maragwa, Elias Mbau waliunga mkono matamshi ya Bw Murathe.

SIASA ZA 2022: Nyumba ya Jubilee inavyoyumba

Na GRACE GITAU

MGOGORO mpya umeibuka miongoni mwa viongozi wa Jubilee na kuibua hali inayotishia kusambaratisha chama hicho huku siasa za urithi wa urais 2022 zikizidi kutokota.

Viongozi katika chama hicho ambao ni wandani wa Rais Uhuru Kenyatta, jana waliwakemea wenzao ambao ni washirika wa Naibu Rais William Ruto, kwa kile walichodai ni mazoea ya kumdharau Rais.

Walieleza hisia zao kutokana na jinsi wenzao kutoka Rift Valley walivyoondoka ghafla katika hafla iliyoongozwa na Rais katika Kaunti ya Bomet mnamo Jumatatu.

Wabunge saba kutoka Kaunti ya Bomet, Jumatatu waliondoka katika mkutano uliosimamiwa na rais kwa hasira, wakilalamika kuwa hawakutambuliwa wala kutengewa nafasi ya kuzungumza au hata kuwapungia mkono wenyeji.

Wenzao kutoka eneo la Mlima Kenya jana walitaja kitendo hicho kama dharau kwa Rais huku wakiongeza kwamba vitendo vya kumdhalilisha rais vimekuwa vikishuhudiwa kwa muda tangu Rais alipoamua kushirikiana na Kiongozi wa ODM Raila Odinga. Walitaja pia tukio la Jumapili wakati wanasiasa wa eneo hilo walijaribu kumshinikiza Rais kumtaja mrithi wake alipokuwa Kapsabet.

Wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri mjini) Rigathi Gachagua( Mathira), Johnson Sakaja (Seneta, Nairobi) na Maoka Maore (Imenti Kaskazini) walidai kuna njama za kumhujumu Rais Kenyatta katika kipindi chake cha pili na cha mwisho uongozini.

“Kuna uwezekano kwamba hatua yao ilikuwa imepangwa mapema. Vitimbi walivyotuonyesha Jumapili havikuwatosha. Hakuna mtu yeyote anayefaa kuthubutu kumsawiri rais kama kiongozi asiye na mamlaka,” akasema Bw Maore.

Awali, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Rais Kenyatta, aliambia wanachama kuwa hawana namna nyingine ila kuunga mkono mwafaka wa rais na Bw Odinga.

Wandani wa Bw Ruto kwa muda mrefu wamekuwa wakidai handsheki hiyo inalenga kumharibia naibu rais nafasi ya kushinda urais ifikapo 2022 ndiposa wao humtaka rais afafanue kama makubaliano yake na naibu wake bado yangali imara.

“Handsheki ipo kati ya rais na aliyekuwa waziri mkuu na tunaiunga mkono kwa sababu ni jambo jema kwa nchi. Kama Raila ataitumia kuwania urais, kuna shida gani?” akasema.

Bw Wambugu ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Naibu Rais alisema baada ya yale yaliyoshuhudiwa Jumapili, ilikuwa vyema wabunge hao kunyimwa nafasi ya kuzungumza kwa sababu ya jinsi wanavyosisitiza Rais anafaa kutangaza kwamba atamuunga Bw Ruto 2022.

Kulingana naye, kitendo cha wabunge hao kilianika wazi jinsi wanavyomchukulia Rais.

Lakini licha ya hayo yote, Bw Gachagua alisema kitendo cha Jumatatu hakikuathiri uamuzi wa viongozi wa eneo la Mlima Kenya kumuunga mkono Bw Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

JUBILEE YATOKOTA: Joto kali huku wandani wa Uhuru na Ruto wakikabana

BENSON MATHEKA Na GRACE GITAU

KUIBUKA kwa mirengo miwili mikuu ndani ya chama tawala cha Jubilee kumezua tofauti zinazotishia kuvuruga chama hicho.

Tofauti hizo zimetokana na masuala manne makuu ambayo ni: Jinsi vinavyoendeshwa vita dhidi ya ufisadi; misako ya kunasa bidhaa feki; mwafaka wa Rais Kenyatta na Raila Odinga, na kukosekana kwa uhakika wa iwapo Rais Kenyatta na wafuasi wake watamuunga mkono naibu wake kuwania urais mwaka 2022.

Joto linaripotiwa kuwa jingi ndani ya chama hicho kutokana na tofauti kati ya mrengo wa kilichokuwa chama cha TNA kilichoongozwa na Rais Kenyatta dhidi ya URP kilichosimamiwa na William Ruto. Vyama hivyo vilivunjwa mwaka 2017 na kuungana kubuni Jubilee.

Katika kile kinachobainika kuwa kujiandaa kwa talaka inayoweza kutokea ndani ya Jubilee wakati wowote, baadhi ya wabunge washirika wa Naibu Rais wameunda vyama vya kisiasa na kutangaza wazi kwamba wanamwandalia kinara wao chama cha kuingia ikulu, iwapo wandani wa Rais Kenyatta “wamsaliti” na kukosa kusimama naye 2022.

Wadadisi wanasema japo Bw Ruto ameepuka kuzungumzia suala hilo hadharani, washirika wake wa kisiasa wamechukua hatua zinazoweza kuvunja chama cha Jubilee, alichotarajiwa kutumia kugombea urais 2022.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei amenukuliwa akisema wanalenga kutayarisha chama ambacho Bw Ruto atatumia kugombea urais 2022. “Kama marafiki wa William Ruto, tunapanga kuunda chama chetu. Tunafikiria kumwachia Rais Uhuru na watu wake chama cha Jubilee,” alisema Bw Cherargei.

Naye mwandani wa Bw Ruto, ambaye aliomba asitajwe alisema: “Subiri tu, tunaandaa mikakati, ndoa yetu na upande wa Rais Kenyatta katika Jubilee inayumba, na sio siri.”

Hatua ya Rais Kenyatta kuingia kwenye mwafaka na Bw Odinga mapema mwaka huu nako kumeonekana kuongeza kasi ya mtafaruku katika Jubilee, baada ya mrengo wa Naibu Rais kutafsiri hatua hiyo kama mbinu ya kuhujumu ndoto yake ya kuwa rais.

Vita dhidi ya ufisadi viliposhika kasi, washirika wa kisiasa wa Bw Ruto walianza kulia ngoa wakidai vinaendeshwa kwa ubaguzi.

Msukosuko huo ulizorota baada ya Rais Kenyatta kutangaza kuwa watumishi wote wa umma wafafanue walivyopata mali yao katika juhudi za kupigana na ufisadi.

Bw Cherargei, Mbunge Oscar Sudi na kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen walijitokeza na kupinga agizo hilo wakidai lilimlenga Bw Ruto.

Siku tatu baada ya Bw Murkomen kujitokeza kimasomaso kudai Bw Ruto ndiye mlengwa wa tangazo kuhusu ufafanuzi wa mali, iliibuka kuwa wandani wa Bw Ruto wamesajili vyama vipya vya kisiasa vya United Green Party (UGP) na Grand Dream Development Party (GDDP).

Mgawanyiko wa Jubilee umepenya hadi bungeni. Mnamo Jumanne, Mbunge wa Aldai, Cornelly Serem alidai kuwwa nduguye Rais Kenyatta, Muhoho Kenyatta ni mmoja wa walioagiza sukari mbaya, jambo ambalo Wizara ya Kilimo imekanusha ikisema jina lake liliingizwa na watu wenye nia mbaya kwenye orodha iliyowasilishwa.

Hapo jana, Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu, alimtaka Murkomen na mwenzake katika bunge Aden Duale kujiuzulu kwa kile alichosema ni kuvuruga vita dhidi ya ufisadi.

Bw Wambugu aliwalaumu Duale na Murkomen kwa madai ya kuhujumu juhudi za Rais Kenyatta kupigana na uovu huo akidai wanawatetea baadhi ya wanaolaumiwa kwa kuingiza sukari yenye sumu nchini, na kupinga wanasiasa na watumishi wa serikali walivyopata mali yao.

“Hatuwezi kuwa na viongozi wa wengi wanaotumiwa kumshambulia Rais. Walipatiwa nyadhifa hizo kutetea sera za Rais na sio kuzipinga. Wanafaa kujiuzulu au tuwatimue,” alisema Bw Wambugu.

Mbunge huyo, ambaye mapema mwaka huu alizua mjadala kwa kudai si lazima wafuasi wa Rais Kenyatta wamchague Bw Ruto 2022, alitisha kuwarai wabunge na maseneta wengine wa Jubilee kuwatimua wawili hao kutoka nyadhifa zao na kuteua watu wengine.

Alisema hatua ya Bw Serem, ambaye ni mwandani wa Ruto ya kutaja jina la Bw Muhoho kwenye kikao cha kamati ya bunge mnamo Jumanne, ilikuwa ni njama ya kumtisha Rais Kenyatta ili aache vita dhidi ya ufisadi.

Bw Wambugu alidai baadhi ya wabunge wenzake wanawalenga jamaa za familia ya rais ili kuhujumu vita dhidi ya ufisadi na biashara ya magendo ili kulinda baadhi ya kampuni.

Naye Bw Duale, ambaye pia ni mwandani wa Bw Ruto, amekuwa akikosoa juhudi za kusaka sukari ya magendo zinazoendelezwa na serikali.

Bw Wambugu alisisitiza kuwa viongozi hao wawili wanafaa kuunga mkono ajenda za Rais badala ya kuzipinga akisema hawafai kushikilia nyadhifa za viongozi wa wengi.

Aliyechaguliwa kwa ODM atangaza kuwania kwa Jubilee 2022

Na Magati Obebo

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Kisii, Joash Maangi ametangaza kuwa atawania ugavana wa kaunti hiyo kupitia chama cha Jubilee ifikapo 2022.

Mnamo Jumatatu, Bw Maangi alimwambia Naibu Rais William Ruto kuwa yuko ODM kwa muda tu na kuwa ameanzisha safari ya kurudi Jubilee.

Akiongea mjini Nyamiria, Bw Maangi alisema ana uhusiano wa karibu sana na chama cha Jubilee licha ya kuwa upinzani.

“Ningetaka kukuambia naibu rais kuwa sina amani moyoni kuwa katika upinzani. Wakati ukifika nitajiunga nawe katika chama tawala na kukufanyia kampeni za kuwa rais,” Bw Maangi alimwambia Bw Ruto wakiwa eneo la Rigoma, Kaunti ya Nyamira.

Bw Ruto alikuwa katika ziara ya siku moja eneo hilo kwa mwaliko wa wabunge Shadrack Mose (Kitutu Masaba) na Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini).

Viongozi hao waliapa kumuunga mkono naibu rais katika kampeni za urais ifikiapo 2022.

Mwaka jana Bw Maangi alijiunga na Jubilee kabla ya kujiunga tena na ODM akidai mawimbi ya upinzani yalikuwa mazito Kisii na huenda yangemmeza kisiasa.

Alisema hatua yake ya kurejea ODM ilitokana na ushauri kutoka kwa viongozi pamoja na wakazi wa Kaunti ya Kisii.

Bw Maangi alipokelewa tena chamani na kinara wa ODM Raila Odinga na kuahidiwa kusalia naibu gavana wa Kaunti ya Kisii baada ya uchanguzi wa Agosti 2017.

Alipojiunga na Jubilee mnamo 2015, Bw Maangi alipanga kutumia chama hicho kumng’oa Gavana James Ongwae lakini akashawishiwa na wakuu wa Jubilee kutoa nafasi hiyo kwa Chris Obure ambaye alibwagwa na Ongwae katika uchaguzi wa Agosti 2017.

Wasiwasi mpya wa mgawanyiko wazuka Jubilee

WYCLIFF KIPSANG, ONYANGO K’ONYANGO na LUCY KILALO

MATAMSHI yanayokisiwa kuwa ya mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, yameendeleza hofu ya kuwepo kwa mgawanyiko katika chama cha Jubilee.

Bw Kuria amesikika kwa rekodi ya sauti hiyo inayosambazwa mitandaoni akidai kuwa viongozi wa Mlima Kenya wanaomuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto wamepata vitisho.

Bw Kuria anawahakikishia wenyeji wa bonde wa ufa kwamba Mlima Kenya utamuunga mkono naibu wa rais mwaka wa 2022.

“Wengine wetu mkituona hapa tunapokea vitisho kila siku eti tunamfuata Ruto. Nilifikiria kumuunga Naibu wa Rais ni sehemu ya ajenda ya Jubilee,” Bw Kuria anasema kwa sauti hiyo katika sehemu fulani katika kaunti ya Nandi.

Kulingana na Bw Kuria, Rais Uhuru Kenyatta hajabadilisha nia yake ya kumuunga mkono naibu wa rais 2022.

“Hakuna wakati rais ametuambia sisi kama viongozi wa mlima Kenya kutomuunga mkono naibu wa rais,” alisema Bw Kuria.

Bw Kuria alisema kuwa hawapingi hatua ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuungana na Rais Kenyatta.

“Tunaunga mkono salamu kati ya viongozi lakini hatua hiyo isiwafaidi watu wachache,” alisema Bw Kuria.

Kumekuwa na minong’ono katika muungano wa Jubilee kufuatia madai kuwa baadhi ya viongozi wako na nia ya kuhakikisha kuwa Bw Ruto hashindi urais mwaka wa 2022.

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen amethibitisha kuwa mambo si sawa katika muungano wa Jubilee.

“Tuko na habari kuwa kuna baadhi ya watu katika afisi ya rais ambao wanatumia muda wao mwingi kuhakikisha kuwa Jubilee inasambaratika,” Bw Murkomen alisema kwenye mahojiano ya moja moja katika runinga ya Citizen Jumapili usiku.

Kulingana na Bw Murkomen, wanaompiga Ruto vita ni wale hawataki yeye atwae urais mwaka wa 2022.

Wakati huo huo, Mbunge wa Cherangany, Joshua Kutuny alipuuzilia mbali kuwepo kwa mgawanyiko katika Jubilee, huku akitahadharisha wafuasi wa Naibu Rais dhidi ya kujitenga na salamu kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Bw Kutuny alisema Jumanne kuwa mrengo wa naibu una nafasi kubwa ya kunufaika kutokana na salamu hizo, lakini ukiendelea na matamshi yanayoonekana kama ya kuwagawanya Wakenya huenda ukatengwa na kutorokwa na Wakenya wengine.

Bw Kutuny alikuwa akijibu madai ya Kiongozi wa Wengi katika Seneti, ambaye ni Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, kuwa vita dhidi ya ufisadi vinamlenga Naibu Rais William Ruto.

 

Angefuata taratibu 

Alisema kuwa iwapo kuna tatizo lolote, Bw Murkomen kama mmoja wa viongozi hata kwa kundi la wabunge wa eneo la Rift Valley, alikuwa na nafasi ya kuwasilisha suala hilo kwa kufuata utaratibu wa chama wa kusuluhisha masuala yake.

“Anahitaji kuonyesha tofauti ziko wapi katika chama lau sivyo ni yeye dhidi ya chama,” alisema.

“Naibu Ruto mwenyewe anatambulika na hahitaji watu kuzungumza kiholela ili kumpigia debe.

“Kwanza wakizidi kuongea kuhusu uchunguzi wa maisha wanaibua maswali mengi zaidi kushinda majibu. Nawahimiza wenzangu kutoka Rift Valley kukoma kuzungumzia masuala ya Naibu Rais na rais.

Alisema kuwa Bw Ruto ni mtu ambaye amejijenga na mwenye tajriba ya kisiasa na ana mbinu zake za kuendesha mambo yake. Pia alitaja kuwa Bw Ruto mwenyewe ametangaza kuwa atakuwa wa kwanza pamoja na rais kuchunguzwa jinsi walivyopata mali.

zao.

“Wachunge ndimi zao, wanavyozungumza ndivyo wanaweza kuzamisha azimio la Naibu Rais la kutafuta urais,” alisema akiongeza kuwa kwa sasa ni yeye Bw Ruto pekee ambaye ametangaza nia ya urais, rais Kenyatta akitarajiwa kujiuzulu.

Hata hivyo, alitaja kuwa wafuasi wake naibu rais lazima pia umtambue Bw Raila Odinga ambaye angali katika siasa.

“Tushikilie hizi salamu, huyu baba tumbembeleze, huwezi kumpiga vita na utarajie kushinda,”

Pia alisema wanaozungumzia harakati za kuzima ufisadi wajue wanamhujumu Rais na “watangaze rasmi kwamba hatuko na Uhuru tena.”

Mbunge wa Nandi Hills, Alfred Keter na mwenzake wa Moibeni Silas Tiren pia walieleza kuunga mkono juhudi za kukabiliana na ufisadi zinazoendeshwa na rais Kenyatta.

Wandani wa Ruto walia vita dhidi ya ufisadi vinalenga kusambaratisha ndoto yake 2022

Na LEONARD ONYANGO

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wameendelea kudai kuwa vita vilivyopamba moto dhidi ya ufisadi ni njama inayomlenga ili kumharibia sifa asiwe rais 2022.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen kuwa vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi ni njama ya kuzima ndoto ya Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022.

Pia alisema tangazo la Rais Uhuru Kenyatta kuwa watumishi wa umma watatakiwa kufafanua walivyopata mali yao, pamoja na ushirikiano kati ya rais na kiongozi wa ODM Raila Odinga ni kati ya mbinu zinazolenga kumzima Bw Ruto.

Msimamo wa Bw Murkomen unalingana na wandani wengine wa Bw Ruto, Seneta wa Nandi Samson Cherargei na wabunge Nelson Koech (Belgut) na Oscar Sudi (Kapseret), ambao wameshikilia kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga watu wachache kwa sababu za kisiasa na wala si kwa manufaa ya Wakenya.

Bw Murkomen, na ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Ruto, alisema vita dhidi ya ufisadi vinatekelezwa kwa lengo la kumpaka tope Naibu Rais ili kudidimiza umaarufu wake.

Kulingana na Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet, juhudi hizo, ambazo zimeshika kasi katika siku za majuzi, ni njama ya washauri katika Ofisi ya Rais kusambaratisha ndoto ya Bw Ruto kuingia Ikulu.

“Walipogundua kwamba umaarufu wa Naibu Rais unaongezeka kwa kasi nchini waliketi chini na kutafuta mbinu za kumzima. Vita dhidi ya ufisadi ni miongoni mwa mbinu walizobuni ili kumchafulia sifa,” Bw Murkomen aliambia runinga ya Citizen mnamo Jumapili.

Alisema watu hao, ambao hakuwataja, wametumia raslimali nyingi kuhakikisha kuwa Bw Ruto hatakuwa rais 2022.

“Lengo lao ni kuzua uhasama na mgawanyiko baina ya Rais Kenyatta na Bw Ruto,” akasema Bw Murkomen.

Alidai kuwa wito uliotolewa na Rais Kenyatta wa kutaka watumishi wa serikali kufafanua walivyopata mali yao ni miongoni mwa njama za kumzima Bw Ruto.

“Tumefanya uchunguzi na kubaini kuwa stakabadhi iliyokuwa na pendekezo la kutaka utajiri wa watumishi wa umma uchunguzwe iliandaliwa na watu hao wanaompinga Bw Ruto,” akasema Seneta huyo.

Alisema mrengo wa Bw Ruto haukushauriwa kuhusiana na mpango huo wa kutaka kuchunguza utajiri wa watumishi wa umma. “Wito wa kutaka kuchunguza utajiri wa watumishi wa umma unalenga mtu mmoja ambaye ni Naibu wa Rais,” akadai.

Alieleza pia kuwa hatua ya Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta ni njama ya kusambaratisha chama cha Jubilee.

“Lengo la Rais Kenyatta lilikuwa kuunganisha nchi lakini lengo kuu la Bw Odinga lilikuwa kubomoa Jubilee,” akadai.

Seneta huyo pia alieleza kuwa mrengo wa Bw Ruto ulishtushwa na kauli ya Rais Kenyatta aliyotoa akimrejelea naibu wake kama “Kijana wa Kutangatanga’.

“Rais alipotoa kauli hiyo tulishtuka. Hatufai kufuata mkondo huo wa kudunisha baadhi ya viongozi,” akasema.

Bw Murkomen, hata hivyo, alisisitiza kuwa uhusiano baina ya Rais Kenyatta na Bw Ruto ungali imara.

Bado tuko pamoja, Ruto apuuza mpasuko ndani ya Jubilee

ABDIMALIK HAJIR na LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto amepuzilia madai ya mgawanyiko baina yake na Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na siasa za 2022.

Bw Ruto, ambaye alikuwa akizungumza Jumapili katika eneobunge la Narok Kusini, alisema madai ya mgawanyiko ndani ya Jubilee yanaendeshwa na wale aliowataja kama ‘manabii wa uongo’ kwa nia ya kugawanya Kenya kwa misingi ya kikabila.

Kumekuwa na madai ya mgawanyiko kati ya Bw Ruto na Rais Kenyatta, ambao unaonekana kusambaa hadi katika chama cha Jubilee.

Hali hii ilianza kujitokeza baada ya Rais kuafikiana kufanya kazi na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, jambo ambalo lilionekana kumwathiri Naibu Rais hasa kuhusiana na siasa za 2022.

Majuzi Bw Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakirushiana maneno licha ya wao kuahidi hadharani kuzika tofaurti zao na kuunga mkono juhudi za kufanya kazi pamoja.

Wanasiasa kutoka ngome ya Bw Ruto ya Rift Valley pia wamekuwa wakilalamika kuwa vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi vinafanywa kwa ubaguzi.

Lakini jana Bw Ruto alisisitiza Jubilee iko imara: “Mimi sijalalamika na ninaendelea kuchapa kazi na Rais Uhuru Kenyatta amefurahishwa na kazi hiyo,” akasema Bw Ruto.

Bw Ruto, ambaye alikuwa ameandamana Narok na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, magavana Joseph ole Lenku (Kajiado) na Samuel Ole Tunai (Narok), alisema Jubilee hakikubuniwa kwa lengo la kushinda uchaguzi bali kuboresha maisha ya Wakenya.

Wengine waliokuwepo ni wabunge Lemanken Aramat (Narok Mashariki), David Ole Sangok (Maalum), Johana Ng’eno (Emurua Dikirr), Gabriel Ole Tongoyo (Narok Magharibi), Dominic Kosgey (Sotik), Joyce Korir (Mwakilishi Wanawake Bomet) na Soipan Tuya (Mwakilishi Wanawake Narok).

“Ninahimiza hao manabii wa mgawanyiko kuachana na Jubilee. Tunajua tulipotoka, tulipo saa hizi na tuendapo. Katika chama cha Jubilee tungali pamoja na lengo letu ni kuunganisha Wakenya wote na tuna mpango wa kufanikisha hayo,” akasema.

Naye Seneta Sakaja alisema Jubilee hakitatikisika: “Wale wanaodai mgawanyiko ndani ya Jubilee wamezoa siasa za kuzozana. Jubilee ni imara na kazi tuliyoanza 2013 inaendelea hadi baada ya 2022.”

Kiongozi Garissa, Kiongozi wa Wengi Bungeni, Aden Duale alisema Rais Kenyatta na Bw Ruto wangali marafiki na na wanaendeleza ajenda ya chama cha Jubilee.

“Rais anatoa mwelekeo wa chama na sisi, akiwemo Naibu Rais, tunafuata,” akasema Bw Duale.

Hamtaniweza, Ruto awaambia mahasidi

ERIC WAINAINA na ALEX NJERU

NAIBU Rais William Ruto amesema anajitayarisha kukabiliana na viongozi wanaomlenga kwa propaganda kupitia vyombo vya habari, katika harakati zake za kuwania urais mwaka wa 2022.

Bw Ruto ambaye alikuwa akiongea katika hafla ya kuchangisha pesa katika Shule ya Sekondari ya St Joseph’s Githunguri, Kaunti ya Kiambu Ijumaa, alisema anajua kuhusu makundi ambayo yameanzisha juhudi hizo za kueneza propaganda ili kuchafua sifa ya serikali.

Alieleza kuwa hatishwi na juhudi hizo ambazo alisema zinaendeshwa na watu ambao hakuwataja, akisema rekodi ya serikali ya Jubilee inaonekana dhahiri na kwamba yuko tayari kukabiliana na wanaohusika nazo kwa msingi wa ufanisi wa serikali.

“Kuna jaribio la kuhujumu rekodi ya Jubilee, lakini ukweli huwa haufichiki, hauwezi kufuta rekodi ya serikali ya Jubilee kwa kuwa ni ya kweli. Kwa hivyo, wale wanaoendesha propaganda, wacha waendelee lakini tutakutana nao siku ya kiama (uchaguzi wa 2022) na wapigakura wataamua ni nani mchapa kazi na nani mwenye propaganda,” alisema.

Naibu huyo alieleza kuwa anafahamu vyema kinachoendelea hasa kuhusiana na siasa, na kwamba kuna makundi ambayo yamejipanga kueneza uongo kupitia kwa vyombo vya habari kwa lengo la kuwagawanya Wakenya, lakini akasema vitendo vyao havitamshtua.

Bw Ruto alikuwa ameandamana na viongozi wa eneo la Kati ambao walisema watatimiza ahadi yao ya kumuunga mkono.

Viongozi hao walijumuisha Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi, Naibu Gavana James Nyoro, wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Kago wa Lydia (Githunguri), N’gan’ga Kin’gara (Ruiru), Jonah Mburu (Lari), Jude Njomo (Kiambu Mjini), Rigathi Gachagua (Mathira), Mwakilishi Mwanamke Wambui Ngirichi (Kirinyaga), Faith Gitau (Nyandarua) na Faith Mukami (Nyeri)

Hata hivyo, akiendelea kujitayarisha, wanasiasa kutoka eneo la kaskazini mwa Mlima Kenya wamesema kwamba watamuunga mkono Bw Ruto tu iwapo aatamchagua Senata wa Tharaka -Nithi, Prof Kithure Kindiki, kama naibu wake.

Wakizungumza wakati wa sherehe za ufunguzi wa ofisi mpya ya gavana wa kaunti hyio katika mji wa Kathwana, viongozi hao walisema wanahitaji kuketi na Bw Ruto ili kuhakikisha kwamba wamesikilizana.

Wakiongozwa na Gavana Muthomi Njuki, Seneta wa Meru Mithika Linturi, wabunge Patrick Munene (Chuka /Igambangombe), Kareke Mbiuki (Maara), Gichunge Kabeabea (Tigania Kaskazini) na Moses Kirema (Imenti ya Kati) walisema ni wakati wa eneo hilo kupata kiti cha unaibu rais.

Bw Mbiuki alisema kuwa Prof Kindiki ndiye mwanasiasa mtajika kutoka eneo hilo na ndiye wanayemtarajia awe naibu rais.

“Lazima tuongee kwa kauli moja ili tutoe naibu rais mwaka 2022 na huyo si mwingine bali Prof Kindiki ambaye wamefanya kazi na Bw Ruto kwa wakati mrefu, ” alisema Bw Mbiuki.

Bw Munene alisema kuwa viongozi wa eneo hilo wako tayari kufanya kazi na Bw Ruto na wamejitolea kuwa wanachama wa ‘Team Tangatanga ‘.