JUBILEE YAPONDA RAILA: ‘Baba’ naye amjibu Ruto akome ‘kubwekabweka’ na ‘kutangatanga’

VALENTINE OBARA, MOHAMED AHMED na DPPS

VIONGOZI wa Chama cha Jubilee Jumapili walimshambulia Kiongozi wa ODM Raila Odinga, hatua ambayo inazua masuala kuhusu kujitolea kwa wanasiasa katika kufanikisha maridhiano baina ya Wakenya.

Vigogo hao wa Jubilee waliojumuisha magavana, seneta na wabunge walimwamia Bw Odinga akome kumkashifu Naibu Rais William Ruto kuhusu siasa za 2022.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga naye alimrushia makombora Bw Ruto akimwambia aache “kutangatanga” na “kubwekabweka”akifanya kampeni za 2022 .

Bw Odinga na naibu wake Hassan Joho walitaja ziara nyingi za Bw Ruto kama kampeni za mapema.

“Wacha kurandaranda hapa na pale, kutangatanga ati wewe unasema mimi nitakuwa Rais mwaka 2022. Unajuaje hilo? Ni Wakenya ambao wataamua yule ambaye watamchagua rais wao,” akasema Bw Odinga.

Nao viongozi wa Jubilee wakiongea mjini Thika walidai Bw Odinga ana njama ya kuvuruga chama chao cha Jubilee na kumtaja kama ‘asiye na adabu’.

Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, alikosoa jinsi Bw Odinga alivyopuuzilia mbali ziara za Bw Ruto katika ngome zake za kisiasa na kuzifananisha na kampeni za mapema.

Kulingana na Bw Kindiki, chama cha Jubilee hakina haja ya kufanya kampeni kwa sababu wanachama wanaamini Bw Ruto ndiye atakayemrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapokamilisha hatamu yake ya pili ya uongozi mwaka wa 2022.

“Jubilee haifanyi kampeni za 2022 wala mwaka mwingine wowote, bali tunazuru mashinani kutafuta jinsi ya kutatua changamoto zinazokumba wananchi. Bw Ruto ndiye mgombeaji wetu bila pingamizi atakayechukua mamlaka wakati Rais Kenyatta atakapostaafu mwaka wa 2022 pamoja na Bw Odinga,” akasema Prof Kindiki.

Magavana waliokuwepo ni Ferdinand Waititu na naibu wake James Nyoro, Granton Samboja (Taita Taveta) na Muthomi Njuki (Tharaka Nithi).

Baadhi ya wabunge waliomtetea Naibu Rais ni Kimani Ichungwa (Kikuyu), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Jude Njomo (Kiambu Mjini) Githua Wamashukuru (Kabete), Patrick Wainaina (Thika Mjini), miongoni mwa wengine.

Bw Waititu alidai kuwa Bw Odinga si mwaminifu katika juhudi za kuleta umoja wa taifa kwani anadunisha hatua za viongozi wengine kueneza umoja huo mashinani.

Kwa upande wake, Bw Ichungwa alishangaa kwa nini Bw Odinga anakashifu ziara za Bw Ruto ilhali yeye ndiye aliambia Wakenya waungane baada ya kusalimiana na Rais Kenyatta.

“Si jukumu lake kutuambia kile tunafaa kufanya kuhusu uongozi wa nchi hii. Tuna imani kwa uongozi wa Rais Kenyatta na Naibu Rais,” akasema.

Bw Ruto amekuwa akizuru pembe tofauti za nchi katika siku za hivi majuzi kwa kile anachodai ni juhudi za kukagua miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali mashinani na kupeleka maendeleo zaidi kwa wananchi.

 

Ni mapema mno 

Hata hivyo, ziara hizo zimetazamwa kama juhudi za kujiandaa kwa uchaguzi wa urais wa 2022, huku Bw Odinga akisisitiza bado ni mapema mno kuanza kufikiria kuhusu uchaguzi ujao.

Naibu Rais jana aliepuka mijadala hiyo na kusema serikali imejitolea kufanikisha umoja na maendeleo ya nchi ambayo yatapewa kipaumbele kuliko masuala mengine yote.

Aidha, Bw Odinga aliendelea kumchapa kwa maneno Bw Ruto kuhusiana na ziara zake ambazo ameonekana akihudhuria na kutoa michango ya fedha.

“Kisha watu wanaenda wakipeana pesa hapa, mara kule na tunajua mshahara wanaopata. Ndio maana tunasema wale ambao wanaiba mali ya umma wanajulikana kutokana na vile wanatembea na sura zao zinaonyesha,” akaongeza Bw Odinga huku akisifia tangazo la rais kuhusiana na ukaguzi wa mali ya watumishi wa umma.

Bw Odinga alisifu Rais Kenyatta kwa tangazo lake kuhusu utathmimi wa mali ya maafisa wa Serikali.

“Katika vita dhidi ya ufisadi tutasimama na serikali kuona vinapiganwa mpaka mwisho, na wale wanaohusika katika wizi wa mali ya umma wakamatwe na kutupwa korokoroni,” akasema Bw Odinga.

 

Ukaguzi wa wafanyakazi serikalini 

Katika ziara yake wiki iliyopita wakati wa ufunguzi rasmi wa barabara ya kisasa ya Dongo Kundu, Rais Kenyatta aliapa kupigana na ufisadi na kutangaza kuwepo kwa ukaguzi wa wafanyakazi wa umma ukiongozwa na yeye.

Bw Kenyatta alisema atakuwa wa kwanza kufanyiwa ukaguzi huo wa mali anazomiliki akifuatwa na naibu wake, halafu magavana na mawaziri pamoja na wafanyakazi wengine.

Hapo jana wakati wa sherehe za Idd Baraza ambapo Bw Joho alikuwa ameandamana na Bw Odinga katika eneo la Treasury Square jijini Mombasa, aliunga mkono mwito wa Bw Kenyatta na kusema watasimama pamoja kuhusu vita dhidi ya ufisadi.

Vile vile, kiongozi huyo alipendekeza kuwa ukaguzi wa mali wanazomiliki viongozi ufanywe na mashirika ya kimataifa ambayo hayataweza kushawishika.

“Nilisema hapa mwaka jana kuwa viongozi tufanyiwe ukaguzi huu na mimi naomba sisi viongozi kuanzia rais na naibu wake na magavana tufanyiwe zoezi hilo na wakaguzi wa kimataifa na wale wengine wafanyiwe hapa hapa,” akasema Bw Joho.

Bw Joho pia hakusita kueleza azma yake ya kuwania kiti cha urais 2022.

“Sisi tunataka kuwambia wale ambao wameanza kampeni mapema kuwa hawana mkataba na Mwenyeezi Mungu. Tunasubiri muda mwafaka ufike na watakiona cha mtema kuni,” akasema.

Ghasia zatawala mchujo wa Jubilee Baringo

Na FLORAH KOECH

GHASIA zilikumba mchujo wa chama cha Jubilee eneobunge la Baringo Kusini kabla ya aliyekuwa katibu wa tawi la Baringo wa chama cha walimu nchini Charles Kamuren alipotangazwa mshindi Jumapili alasiri.

Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Bi Grace Kipchoim.

Miongoni mwa waliokuwa wakiwania kiti hicho ni mfanyabiashara anayeishi Amerika Mark Kiptoo, wakili Joseph Tarus na Eunice Lepario kutoka jamii ya Ilchamus.

Kwenye matokeo yaliyotangazwa na afisa aliyesimamia mchujo huo katika ofisi za naibu kamishna, Bw Kamuren alipata kura 13,882, Mark Kiptoo alikuwa wa pili kwa kura 8,919, Eunice Lepario alipata kura 999 naye Joseph Tarus alipata kura 431.

Uteuzi wa Jumamosi ulifanyika katika taharuki na madai kwamba kura hazikupigwa katika zaidi ya vituo 41 ambako masanduku ya kura hayakufika. Ilishukiwa kuwa afisa mmoja alitoweka na masanduku na karatasi za kura na kuyatumia katika vituo vingine.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika kituo cha kujumlisha matokeo katika shule ya wavulana ya Marigat ulionyesha kuwa matokeo ya vituo ambavyo uteuzi haukufanyika yalitangazwa na afisa msimamizi Charles Bowen.

Ghasia zilitokea katika kituo hicho kila upande ukadai ulikuwa umeshinda na polisi wakalazimika kutumia nguvu kuwafukuza wafuasi waliokuwa na hasira kutoka ukumbini.

“Tunasimamisha shughuli hii na hatutaendelea. Tutapeleka masanduku ya kura katika ofisi ya naibu kamishna yakahifadhiwe hadi kesho ambapo tutashauriana na wawaniaji wote,” alitangaza Bw Bowen.

Jana wawaniaji walifanya mkutano kwa saa sita ambao wanahabari hawakuruhusiwa. Mambo yaliharibika Kiptoo na maajenti wake walipoondoka mkutano wakilalamika kuwa matokeo kutoka baadhi ya vituo yalibadilishwa.

Mudavadi na Weta watakiwa kujiunga na Jubilee

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee kutoka magharibi mwa Kenya wamewataka vinara wa NASA Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula ‘kuondoka kwenye baridi’ na kujiunga na serikali.

Mbw Emmanuel Wangwe (Navakholo), Dan Wanyama (Webuye Magharibi) na Didmus Barasa (Kimilili) waliwataka wawili hao kuiga mfano wa wenzao Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kwa kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta.

“Kalonzo alihudhuria Maombi ya Kitaifa na kuwasalimiana na Naibu Rais William Ruto na Bw Odinga licha ya kuachwa nje katika mwafaka wa hapo awali. Sasa Musalia na Wetang’ula hawana budi kujiunga kufuata nyayo za wenzao na kujiunga na Jubilee,” akasema Bw Wangwe.

Naye Bw Wanyama alisema endapo wawili hao wanajiunga na serikali watajiweka katika nafasi nzuri kupata vyeo vya juu katika uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Ikiwa Mudavadi na Wetang’ula watajiunga na serikali watakuwa katika nafasi bora kujadiliana na Naibu Rais William na viongozi kutoka maeneo mengine katika siasa zijazo,” akasema.

Kwa upande wake Bw Barasa alisema njia ya kipekee ya Mudavadi na Wetang’ula kumpinga Raila chenga kisiasa ni kushirikiana na Rais Kenyatta na naibu wake Ruto katika mipango yao ya kuwahudumia Wakenya.

“Njama fiche za Raila zitaambulia patupu ikiwa viongozi hawa wawili watajiunga na serikali katika mchakato wake wa kuunganisha nchi kwa ajili ya maendeleo. Kupitia njia hiyo sisi kama Waluhya tutafaidi,” akasema Bw Barasa ambaye anahudumu muhula wake wa kwanza.

Wabunge hao watatu walikuwa wakiongea Jumamosi katika hafla ya mazishi katika eneo bunge la Navakholo.

Mbw Mudavadi na Wetang’ula hawakuhudhuria hafla ya maombi ya kitaifa katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi. Hata hivyo, Bw Musyoka aliwataka Rais Kenyatta na Bw Odinga kuhusisha wawili hao katika mchakato wa kuunganisha taifa.

“Leo ni siku muhimu zaidi kwa sababu sisi kama viongozi tumeungana hapa kwa ajili ya kupalilia umoja na uthabiti wa taifa letu. Ingekuwa bora zaidi ikiwa wenzetu, Mudavadi na Weta pia watajumuishwa katika mchakato huu ili sote tutembee pamoja,” akasema kiongozi huyo wa chama cha Wiper.

Joho sasa aamua kushirikiana na Uhuru

MOHAMED AHMED Na VALENTINE OBARA

GAVANA wa Mombasa, Hassan Joho, hatimaye amelegeza kamba na kutangaza atashirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Haya ni mabadiliko makubwa ya msimamo wake mkali ambao ameshikilia kwa muda mrefu dhidi ya utawala wa Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto. Ni kutokana na msimamo huo na ukakamavu wa kushambulia wawili hao ambapo gavana huyo amepata umaarufu kitaifa.

Lakini jana akizungumza katika eneo la Shanzu mjini Mombasa alipoongoza hafla ya upandaji miti, naibu kiongozi huyo wa Chama cha ODM alionekana kushawishika kwamba serikali haina ubaya naye.

“Nataka kusema hapa kuwa tuna furaha kufanya kazi na serikali ya kitaifa kwa sababu ni kupitia njia hiyo ambapo watu wetu watapata nafasi ya kufaidika kimaendeleo,” akasema.

Alitamka hayo mbele ya viongozi wa Jubilee, Maseneta Kimani Wamatangi (Kiambu), Charles Kibiru (Kirinyaga) na Millicent Omanga (Seneta Maalum).

Bw Wamatangi aliongoza wenzake kumwomba Bw Joho aweke kando tofauti zake na serikali kuu na kufuata mfano uliotolewa na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa manufaa ya wananchi.

“Viongozi wa Jubilee ni wema na tunataka kuhakikisha tunaleta umoja. Ninataka kumwambia Bw Joho anapoongoza kaunti, anafaa kushirikisha kila mmoja ili tufanye kazi pamoja,” akasema Bw Wamatangi.

Kufuatia wito huo, Bw Joho alisema: “Tumeona kuwa wadosi wetu wamesalimiana, wakashikana mkono. Mimi mdosi wangu ni Bw Raila na hivyo basi tutawaunga mkono na tutaendelea kuwaunga mkono.”

Uhasama kati ya Bw Joho na Rais Kenyatta ulichacha wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka uliopita, ambapo ilibidi serikali itumie polisi kumzuilia kuhudhuria baadhi ya hafla zilizosimamiwa na rais Mombasa.

Matukio yaliyojaa vioja zaidi yalikuwa wakati polisi walipozuia msafara wake asihudhurie uzinduzi wa kituo cha reli mpya ya SGR kilicho Miritini, na uzinduzi wa feri mpya ya Mtongwe.

Rais Kenyatta alidhihirisha ghadhabu yake dhidi ya Bw Joho alipokuwa Mtongwe ambapo alimtaka akome kumfuata kila aendako. “Tunafuatana naye kufanya nini? Mimi sio bibi yake na sina haja naye.

Atekeleze shughuli zake kama anazo, lakini shida yake ni kwamba hakuna lolote ametenda ndiposa anataka kuja kushikilia koti ya serikali ya kitaifa,” akasema rais katika hafla hiyo ya Machi 2017.

Bw Joho amekuwa akipinga hatua ya serikali kuu kujenga bandari kavu katika maeneo ya Embakasi jijini Nairobi na Naivasha katika Kaunti ya Nakuru akidai kwamba mipango hiyo itaathiri uchumi wa Pwani ambao hutegemea sana biashara za Bandari ya Mombasa.

Prof Ghai ataka fedha zilizotumika na Jubilee Ikulu ziwekwe wazi

Na BENSON MATHEKA

SHIRIKA moja lisilo la kiserikali, limeandikia barua Msimamizi wa Ikulu Bw Kinuthia Mbugua, likitaka aeleze kiwango cha pesa zilizotumiwa kuandaa mikutano ya chama cha Jubilee katika Ikulu ya Nairobi na ikulu ndogo nchini mwaka 2017.

Katiba Institute, linataka kujua gharama ya mikutano yote ambayo chama cha Jubilee kiliandaa katika ikulu wakati wa kampeni, aliyeitisha mikutano hiyo na aliyesimamia gharama.

“Dhamira ya barua hii ni kuomba habari kuhusu gharama iliyotokana na mikutano ya chama cha Jubilee katika Ikulu na Ikulu ndogo kati ya Septemba 2, 2017 na Oktoba 2, 2017,” inasema barua iliyotiwa sahihi na mwenyekiti wa shirika hilo Prof Yash Pal Ghai.

Shirika hilo linataka Bw Mbugua kueleza ikiwa Ikulu ni ukumbi wa kukodishwa kuandaa mikutano na ada inayotozwa.

“Je, Ikulu inaweza kukodishwa kuandaa mikutano ya vyama vya kisiasa au hafla zinazoegemea upande mmoja, na ikiwa inakodishwa, ada ni gani?” aliuliza Prof Ghai.

Anataka Bw Mbugua au afisa anayehusika, kueleza aliyelipa gharama ya kukodisha ikulu, vinywaji na mlo katika kila mkutano.

“Unaweza kutukabidhi nakala za risiti, hati za kutoa huduma zilizotolewa kwa kila mkutano,” anaomba kwenye barua aliyoandika Mei 4 mwaka huu.

Profesa Ghai anataka maafisa wa ikulu kueleza iwapo gharama ililipwa na wahusika wengine kikiwemo chama cha Jubilee, pesa walizolipa na risiti za kuthibitisha kwamba walilipa pesa hizo.

“Ikiwa serikali ililipa gharama ya kuandaa mikutano hiyo, ni maafisa gani walioidhinisha malipo hayo. Ikiwa serikali ililipa gharama ya kuandaa mikutano hiyo ilitumia pesa ngapi,” mtaalamu huyo wa katiba anataka kujua.

Aidha, anataka maafisa hao waeleze iwapo pesa za kuandaa mikutano hiyo zilikuwa zimetengwa kwenye bajeti na jina la kila afisa aliyeidhinisha pesa hizo kutumika.

Profesa Ghai anaambatisha orodha ya mikutano 12 ambayo wajumbe wa chama cha Jubilee wakiwemo wabunge walitembelea ikulu kukutana na rais kabla ya marudio ya kura ya urais ya Oktoba 26 mwaka jana.

“Iliripotiwa katika vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na tovuti rasmi ya ofisi ya rais kwamba Rais aliandaa mikutano kadhaa katika ikulu na ikulu ndogo kuhusu masuala ya chama cha Jubilee na kwa kampeni zake pamoja na mikutano ya kundi la wabunge la chama cha Jubilee,” anasema Prof Ghai.

Kulingana naye, Rais alipokea wajumbe wa chama cha Jubilee kutoka maeneo kadhaa kote nchini katika ikulu walioahidi kumuunga mkono.

Anasema anatoa ombi hilo chini ya sheria ya haki ya raia kupata habari kutoka kwa serikali, na haki ya serikali kuchapisha habari kwa manufaa ya wananchi na iwapo haitampa habari hizo ataishtaki mahakamani.

JAMVI: Wito wa Atwoli watikisa msingi wa chama cha Jubilee

Na BENSON MATHEKA

WITO wa kutaka mabadiliko ya katiba ili Rais Uhuru Kenyatta aendelee kuhudumu serikalini baada ya kumaliza kipindi chake cha pili 2022, ni pigo kwa ustawi wa demokrasia nchini na linaweza kusambaratisha chama cha Jubilee.

Na ingawa baadhi ya washirika wa rais wanapinga pendekezo lililotolewa na katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Cotu Francis Atwoli, kwamba katiba ibadilishwe kubuni wadhifa wa waziri mkuu kumwezesha Rais Kenyatta kuendelea kushiriki siasa baada ya 2022, wadadisi wanasema hatua kama hiyo itavunja chama cha Jubilee.

“Pendekezo la Atwoli sio hewa tupu. Katika siasa mambo hubadilika haraka sana. Usisahau washirika wa rais, hasa kutoka ngome yake wanahisi hawana mtu wa kumrithi na wangetaka aendelee kuwa serikalini kwa sababu wanahisi anawakilisha maslahi yao. Siasa za Kenya ni telezi sana,” asema Bw Alloys Mwangi, mdadisi wa masuala ya siasa.

Kulingana naye, mjadala kuhusu kubadilisha katiba kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu baada ya 2022 umekuwepo kwa muda, japo chini kwa chinichini.

“Nahisi kuna mikakati ambayo imekuwa ikiendelea chini kwa chini katika mrengo mmoja wa Jubilee. Hofu ya wakereketwa wa mabadiliko hayo ni azma ya Naibu Rais William Ruto ya kugombea urais 2022.

Rais mwenyewe pia aliahidi kustaafu baada ya kumaliza kipindi chake cha pili na kumuunga Bw Ruto. Hata hivyo, inaonekana kuna shinikizo mpya zilizojiri na muafaka wa Rais Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga,” alisema Bw Mwangi.

 

Uhuru awe Waziri Mkuu 2022

Akiongea kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni katika bustani ya Uhuru Park Jumanne, Bw Atwoli alipendekeza katiba ifanyiwe mageuzi ili kubuni wadhifa wa waziri mkuu utakaoshikiliwa na Rais Kenyatta baada ya 2022.

Kulingana na Bw Atwoli, Rais Kenyatta atakuwa bado na nguvu atakapomaliza kipindi chake cha pili 2022 na anafaa kuendelea kushiriki siasa.

“Tubadilisheni katiba hii na kutumia rasimu ya Bomas ili kuhusisha watu wote kwa sababu sio kila mtu anaweza kuwa rais. Kufanya hivi kutamshirikisha Rais Kenyatta ambaye angali bado chipukizi. Tusipofanya hivyo, tutampeleka wapi?” alihoji Bw Atwoli.

“Nawaambia kwamba hata mtu mwingine akiongoza Kenya, ni lazima atashirikiana na watu wa Mlima Kenya na huo ndio ukweli wa mambo,” alisema Bw Atwoli.

Kulingana na rasimu ya katiba ya Bomas, Kenya ingekuwa na wadhifa wa waziri mkuu ambaye angechaguliwa na bunge na kuwa na na mamlaka makuu.

Wadadisi wanasema pendekezo hilo ni njama ya kuzima azima ya Naibu Rais William Ruto ambaye  amepinga mabadiliko yoyote ya katiba yanayolenga kubuni nyadhifa mpya serikalini. Wanasema si ajabu mabadiliko hayo yalikuwa miongoni mwa masuala ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga walikubaliana katika muafaka wao.

Mchanganuzi Barack Muluka anahisi suala la kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu kama waziri mkuu lilijadiliwa kwenye mikutano iliyotangulia muafaka wake na Bw Odinga.

 

Raila na Uhuru wana maoni sawa

“Odinga anaamini kwamba atakuwa rais pengine akiwa na naibu kutoka  Rift Valley na mwingine kutoka Pwani. Kenyatta anaweza kuwa waziri mkuu akiwa na manaibu wawili kutoka Magharibi na Mashariki. Hawa wawili wana maoni sawa,” Bw Muluka alisema.

Kwenye makala yaliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kabla ya tamko la Bw Atwoli, Bw Muluka  alisema viongozi hao wawili watawaagiza wabunge na madiwani wa vyama vyao kuunga mabadiliko ya katiba wakisingizia wanalenga kuunganisha nchi.

“Kuna wale watakaopinga mabadiliko hayo na kwa hivyo kutazuka makabiliano ya kisiasa na kikatiba nchini Kenya,” alitabiri Bw Muluka.

Kulingana na kiongozi wa wengi katika seneti Bw Kipchumba Murkomen, ambaye ni mshirika wa Bw Ruto, katiba haiwezi kubadilishwa ili kubuni nyadhifa kwa sababu ya watu binafsi.

“Rais ameshughulikiwa ipasavyo katika katiba na hahitaji kutengewa wadhifa,” alisema Bw Murkomen na kuungwa mkono na mwenzake katika bunge la taifa, Aden Duale ambaye pia ni mwandani wa Bw Ruto.

“Rais Kenyatta ametangaza wazi kwamba, atafurahi kustaafu siasa baada ya kumaliza kipindi chake cha pili,” alisema Duale.

Wadadisi wanasema njama zozote za kumzuia Bw Ruto kugombea urais 2022 zinaweza kuvunja chama cha Jubilee.

“Bw Ruto atahisi kuwa amesalitiwa baada ya kumuunga Rais Kenyatta tangu 2013. Amekuwa akilenga urais 2022 na yeye na washirika wake hawatachukulia hatua yoyote ya kuzima ndoto yake kwa urahisi,” asema Bw Doris Chebet wakili na mdadisi wa siasa.

Anasema pendekezo la kumtaka Rais Kenyatta kuendelea kuhudumu ni njama za watu binafsi wanaomzunguka na ambao wanataka kuendelea kufurahia mamlaka.

 

Kuongezwa kwa muhula

“Usishangae kusikia baadhi yao wakipendekeza muda wa kipindi cha rais kuhudumu uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba,” alisema Bi Chebet.

Bw Atwoli alisema kwa sababu Rais Kenyatta atakuwa na umri wa miaka 60 atakapomaliza kipindi chake cha pili, ngome yake ya kisiasa haitakubali astaafu.

Wanaopinga pendekezo hilo wanamhimiza Rais Kenyatta kuiga viongozi wanaoheshimiwa kote ulimwenguni kwa kukataa kukwamilia mamlakani.

Bw Mwangi anasema Bw Atwoli hakuwa wa kwanza kutoa pendekezo kama hilo.

“Nakumbuka mapema mwaka huu, David Murathe, ambaye ni afisa mkuu wa chama cha Jubilee (naibu mwenyekiti) alinukuliwa akisema kuna watu wanaotaka Uhuru astaafu akitimiza miaka 60 ilhali Raila anataka kuwa rais akiwa na miaka 75.

Hii inaonyesha huenda kuna njama pana zinazopikwa kuhakikisha Uhuru anasalia serikalini baada ya 2022” alisema Bw Mwangi na kuongeza kuwa washirika wa Bw Ruto wanaweza kuondoka Jubilee iwapo hilo litatendeka.

Kulingana na  Bi Chebet, mswada wa mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket unaopendekeza katiba ibadilishwe Rais ahudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba na kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka makuu, haufai kupuuzwa.

“Marais wengi wametumia mabadiliko ya katiba ili waendelee kuhudumu, hasa wakiwa na idadi kubwa ya wabunge. Jubilee ina wengi katika bunge na seneti na hata wanaomuunga Ruto wakikosa kuunga mabadiliko, wale wa ODM wanaweza kuyaunga kufuatia muafaka wa Uhuru na Odinga,” alisema.

ODM yaionya Jubilee dhidi ya kuvuruga muafaka

Na BARACK ODUOR

WABUNGE wa Chama cha ODM wameonya wenzao wa Jubilee dhidi ya kujaribu kuvuruga maelewano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Homa Bay, Bi Gladys Wanga, na Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Bw Simba Arati, wamedai kuna wabunge wa Jubilee ambao wanafanya njama kisiri kusambaratisha maelewano ya viongozi hao wawili.

Wakizungumza katika harambee ya kusaidia Kanisa la Gendia Seventh Day Adventist lililo katika Kaunti ya Homa Bay, viongozi hao walisema maelewano yaliyofanywa yamenuia kuleta umoja nchini.

Bi Wanga alimkashifu Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale, kwa kudai kuna wabunge wa ODM ambao wanapinga maelewano hayo.

“Ninataka kumwonya Bw Duale kuhusu matamshi aliyotoa hivi majuzi kwamba baadhi ya wabunge wa ODM hawaungi mkono maelewano. Hii ni kwa sababu sote tunaunga mkono hatua hiyo ambayo ndiyo pekee inayoweza kudumisha amani na utangamano nchini,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Arati aliambia wabunge wa Jubilee wajitenge na matamshi ambayo yanaweza kusababisha mgawanyiko nchini.

Alisema matamshi aina hiyo yanaweza kufanya malengo ya maelewano hayo yasifanikishwe na hali hiyo itasababisha janga la kisiasa nchini.

“Kuna nia ya baadhi ya wenzetu katika Jubilee kuingilia makubaliano kati ya kiongozi wetu na kiongozi wao. Lakini haifai watudharau kwa sababu tunajua tulikotoka,” akasema Bw Arati.

Alitoa wito kuwe na heshima kati ya wabunge wa ODM na Jubilee ili kuendeleza mbele malengo ya makubaliano hayo.

“Kama wanataka kusambaratisha makubaliano hayo, pia sisi tunaweza kufanya hivyo kwa hivyo inafaa tuheshimiane,” akasema.

Bi Wanga pia alitumia nafasi hiyo kusambaza vyakula kwa zaidi ya familia 50 zilizoathirika na mafuriko katika wadi ya Karachuonyo Kaskazini, eneobunge la Karachuonyo.

Alisema maendeleo nchini yanaweza kupatikana tu kama kuna amani na utangamano nchini kote.

Ruto awapa onyo wabunge wa Jubilee

Naibu Rais William Ruto. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais, Bw William Ruto, ameonya wabunge wa Jubilee dhidi ya kuzusha fujo zinazoweza kusababisha mgawanyiko wa wananchi.

Akizungumza Jumapili katika eneo la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga, Bw Ruto alisema mienendo hiyo itafanya iwe vigumu kwa Rais Uhuru Kenyatta kutekeleza ajenda zake za maendeleo kabla kukamilisha hatamu yake ya uongozi.

“Kuna watu wana ushujaa wa kelele ya fujo na fitina lakini sisi katika Jubilee tunajua siasa zetu ni za kuunganisha Wakenya na kuleta maendeleo. Nawaomba viongozi wote hasa wa Jubilee, tujitahidi kutimiza manifesto yetu,” akasema.

Ingawa hakutaja wanasiasa wowote, matamshi yake yalitokea wakati ambapo kuna mvutano kati ya Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, na Mbunge Mwakilishi wa kaunti hiyo, Bi Wangui Ngirici, kufuatia kisa ambapo fujo zilizuka kwenye mkutano wa hadhara wa Bi Waiguru wiki iliyopita.

Katika ziara yake, naibu wa rais alitangaza mipango ya serikali kuimarisha miradi mbalimbali katika kaunti hiyo ikiwemo ya barabara, afya, uzalishaji wa chakula cha kutosha na usambazaji wa maji.

“Nawaomba viongozi wote hasa wa Jubilee, tulikubaliana kwamba mambo yetu ni mawili: Kuunganisha Kenya yote na kuondoa siasa ya mgawanyiko, na pili ni maendeleo. Nataka niwaombe nyinyi nyote muungane, tushirikiane ili tuunganishe Wakenya wote na tuharakishe maendeleo yetu ya Kenya,” akasema.

Viongozi wa Jubilee wamponda Maraga, wamsifu Matiang’i

Na PETER MBURU

VIONGOZI wa Jubilee wamemkabili vikali Jaji Mkuu David Maraga kwa kutetea majaji ambao wanadaiwa kutoa maagizo ya kuzuia shughuli za serikali, huku wakimtetea Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kutokana na vita vya matamshi na Idara ya Mahakama.

Wakiongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Seneta wa Nakuru Bi Susan Kihika, viongozi hao walilaumu mahakama ambazo zimekuwa zikitoa amri za kuzuia maagizo ya serikali wakisema zimechangia kudorora kwa maendeleo nchini.

Viongozi hao aidha walimtetea Dkt Matiang’i kwa madai aliyotoa kuwa maafisa wa mahakama wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya mawakili na watu wanaonuia kusambaratisha serikali.

Walikuwa wakizungumza katika hafla ya mazishi ya nduguye mbunge wa Subukia Samuel Gachobe, marehemu Ibrahim Gachobe aliyeaga dunia wiki iliyopita baada ya kuugua saratani.

“Majaji wamekuwa wakitoa maagizo kuhusu kila kitu wanachoombwa na watu wasiotaka maendeleo. Sisi kama wabunge tuko nyuma ya Bw Matiang’i na tunamrai kusimama kidete. Hatutaki kuingilia utendakazi wa idara ya mahakama lakini suala la kutoa amri za kuzuia mambo kila mara halitoi mwelekeo mwema,” akasema Bw Kuria.

Mbunge huyo alirejelea agizo lililotolewa kuzuia tume ya NTSA kufanya mafunzo ya kisasa kwa madereva, akisema inahatarisha kuongeza ajali za barabarani.
Wabunge wengine waliohudhuria ni Gabriel Kago (Githunguri), John Kiarie (Dagoretti Kusini), Kuria Kimani (Molo), Caleb Kositany (Soy), Liza Chelule (Nakuru) na Jane Njiru (Embu).

Vilevile, Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui, seneta wa Laikipia John Kinyua na mbunge wa EALA Mpuri Aburi walihudhuria.

iongozi hao walizidi kusema kuwa eneo la Mlima Kenya litampigia kura naibu wa rais William Ruto katika uchaguzi wa Urais 2022 na kumtaka rais kuwa makini katika uhusiano wake na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

“Ikiwa Bw Ruto alimuunga mkono rais 2002, kisha akajiunga naye 2013 na kushirikiana naye 2017, basi watu wa Meru na Embu hatuna shaka kuwa tutamuunga mkono ifikapo 2022, hakutakuwa na njia nyingine,” akasema Bw Aburi.

Mwanasiasa huyo aidha alimtahadharisha Rais Kenyatta kujichunga anapotembea na Bw Odinga, akisema hajaamua kujiunga na serikali ila anacheza hila tu.

“Hata mnapoomba naye usifunge macho kwani tunajua kuwa hajabadilika, Raila bado ana hila zake tu,” akasema mbunge huyo.

Jubilee yakiri Cambridge Analytica iliwasaidia uchaguzini 2017

Na WAANDISHI WETU

CHAMA cha Jubilee kimekiri kusaidiwa na kampuni ya Strategic Communications Laboratory (SCL) inayohusishwa na Cambridge Analytica (CA) inayotambuliwa kwa uenezaji wa propaganda hasa katika uchaguzi.

Hata hivyo, chama hicho kimekiri kulipa kampuni hiyo kwa huduma zake za kupatia chama sura ya kipekee -“branding” katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Cambridge Analytica (CA), inakabiliwa na kashfa ya kutumia hila katika uchaguzi ambayo inahusisha Facebook.

Habari hizo zimegonga vichwa vya habari kufuatia mahojiano yaliyorekodiwa ambapo wakuu wake walielezea wajibu wao katika mkondo ambao uchaguzi wa 2013 na 2017 ulichukua, kupitia propaganda kali za kuwagawanya watu na pia ukabila mtandaoni.

Kulingana na taarifa za maafisa hao zilizorekodiwa kisiri na kipindi cha British Channel 4 kilichoonyeshwa Jumatatu, CA ambayo ilitambulika mara ya kwanza kwa kuhusika kwake katika kampeni ya urais wa Donald Trump 2016, pia iliendesha kampeni za Rais Uhuru Kenyatta 2013 na 2017.

Lakini naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe, alipuuzilia mbali kuhusika kwa kampuni hiyo kwa njia kubwa, akisema tu kuwa ilihusika zaidi na huduma za kuiunda sura yake.

 

Jubilee yabana maelezo

Hata hivyo, Bw Murathe hakutoa maelezo zaidi kuhusu kile kampuni ya Cambridge inayohusika na SCL ilifanyia chama cha Jubilee nchini.

Chama cha ODM sasa kinawataka wakuu wa Jubilee kujitokeza na kuweka wazi mchango wa CA katika uchaguzi mkuu wa Kenya uliopita.

“Katika moyo wa mazungumzo ulioanzishwa na vinara wetu wawili, tungependa Jubilee iweke wazi ushirikiano wake na CA ili tuweze kukabiliana na ushawishi wa kisiasa kutoka nje katika siku sijazo na kulinda demokrasia yetu kama nchi,” alisema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

Katika kanda hiyo ya Channel 4 News, meneja Mkurugenzi wa Cambridge Analytica na SCL Elections, amenaswa kwa video akijigamba jinsi kampuni hizo zilivyohusika katika uchaguzi wa Kenya wa 2013 na 2017.

Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Reuters, Cambridge Analytica imekana madai yaliyotolewa na Channel 4 News, ikisema iliwaelekeza wanahabari hao wapekuzi kwa lengo la kujua nia yao.

 

Uchunguzi

Kwa sasa, afisi zake za London zinatarajiwa kuchunguzwa huku kukiwa na maswali pia kutoka kwa wakuu wa Amerika baada ya mfichuzi kueleza jinsi kampuni ilivyosaka habari za kibinafsi za mamilioni ya watu kwa lengo la kusaidia kampeni ya Rais Trump.

Taarifa hizo za kuhusika kwa kampuni hiyo ya Uingereza zimeibua hisia mseto nchini Kenya.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen (Jubilee), alikanusha taarifa kuwa kampuni hizo zilishawishi jinsi uchaguzi ulivyofanyika.

Wakati huohuo aliyefichua sakata ya CA, Christopher Wylie alisema mwenzake alipatikana amekufa katika hoteli moja nchini Kenya.

Alisema Dan Muresan, aliyedaiwa kushiriki katika kampeni za Rais Kenyatta wakati wa uchaguzi wa 2013 alipatikana amekufa katika hali isiyoeleweka.

JAMVI: Dhamira fiche ya Uhuru kuzuia wabunge wa Jubilee kuhojiwa yaanikwa

Kumteua Bw Raphael Tuju kama waziri asiyeshikilia nafasi yoyote ni juhudi za kuhakikisha kwamba maslahi ya Chama cha Jubilee (JP) yanashughulikiwa serikalini, na katika wizara zote. Picha/ Maktaba

Na WANDERI KAMAU

Kifupi:

 • Imefichuka kuwa Jubilee ina mipango madhubuti inayoendeshwa kichinichini kuhakikisha kwamba imedhibiti  habari 
 • Imebainika JP pia inabuni mikakati ya kutoa mafunzo maalum kwa maafisa watakaosimamia chama hicho kutoka ngazi za mashinani hadi za kitaifa
 • Huenda ikawa vigumu kwa Kenya kuwa na chama kimoja ama viwili vya kisiasa, ikizingatiwa kwamba mazingira ya kisiasa nchini ni telezi sana
 • Chama hicho kitageuzwa kuwa chenye asasi thabiti ambazo zitahakikisha kimebaki imara, hata wakati UhuRuto watakapoondoka uongozini

 

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kuwazuia wabunge wa Jubilee kushiriki katika mahojiano yoyote na vyombo vya habari imeibua mkakati wa serikali kuirejesha Kenya katika enzi ya chama kimoja.

Aidha, imefichuka kuwa mkakati huo ni sehemu ya mipango madhubuti inayoendeshwa kichinichini na uongozi wa Jubilee kuhakikisha kwamba imedhibiti jinsi habari muhimu kuhusu maendeleo ya chama hicho yanavyowafikia wananchi.

Mbali na hayo, kuteuliwa kwa Bw Raphael Tuju kama waziri asiyeshikilia nafasi yoyote ni juhudi za kuhakikisha kwamba maslahi ya Chama cha Jubilee (JP) yanashughulikiwa serikalini, na katika wizara zote.

Imebainika kwamba kuwa hiyo ndiyo sababu kuu ambapo Bw Tuju, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa JP, hakupigwa msasa na Bunge, kwani wajibu wake ni ‘mkubwa’.

“Wajibu wa Bw Tuju ni kuhakikisha kuwa utendakazi wa kila wizara unawiana na malengo ya Jubilee, hasa manifesto yake. Ni hali ya kawaida, katika nchi zenye vyama thabiti vya kisiasa kama Afrika Kusini, Uchina, Tanzania, Uganda kati ya nchi nyingine,” zikaeleza.

Duru zimeeleza kwamba ili kuhakikisha kuwa hakuna pengo lolote katika uongozi wa chama, Rais Kenyatta ataendelea kuwa kiongozi rasmi wa JP, hata atakapong’atuka uongozini kama rais mwaka wa 2022.

 

Kugeuza Jubilee kuwa KANU

Na ingawa, hilo lingali kubainika kwa wengi, wachanganuzi wanasema kuwa huo ni mpango wa wazi wa kukikuza chama hicho kufikia kiwango cha chama cha Kanu, ambacho kiliitawala nchi kwa karibu miongo mitano.

“Nadhani ni wazi kwamba Jubilee inairejesha Kenya katika enzi ya utawala wa chama kimoja cha kisiasa,” asema Gabriel Otachi, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

Imebainika kwamba JP pia inabuni mikakati ya kuweka mchakato wa kutoa mafunzo maalum kwa maafisa watakaosimamia chama hicho kutoka ngazi za mashinani hadi za kitaifa.

Kulingana na mwongozo ulioonwa na Jamvi la Siasa, lengo kuu ni kukiwianisha na vyama Chama cha Kikomunisti cha Uchina (CP), African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini, Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kati ya vingine vyenye nguvu.

“Lengo la JP ni kubuni utaratibu thabiti wa usimamizi wa chama, ambao utahakikisha kuwa uongozi wake hautegemei uwepo wa mtu binafsi, basi asasi zitakazokuwepo,” unaeleza mwongozo huo.

 

Ni vigumu

Hata hivyo, wachanganuzi wanatilia shaka mpango huo, wakisema kuwa huenda ikawa vigumu kwa Kenya kuwa na chama kimoja ama viwili vya kisiasa, ikizingatiwa kwamba mazingira ya kisiasa nchini ni telezi sana, ikilinganishwa na mataifa mengine.

“Kenya ni nchi iliyostawi sana kidemokrasia. Hivyo, jaribio lolote la kuirejesha katika chama kimoja huenda lisifaulu, kwani watu wataliasi kwa kutumia vipengele vilivyo katika Katiba kudai haki zao,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Egerton.

Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wanasema kwamba hawajashtushwa na mpango huo, kwani ilidhihirika tangu awali kwamba mpango wa mabw Uhuru na Naibu Raid William Ruto walikuwa na mipango mikubwa kuigeuza Jubilee kuwa chama chenye nguvu.

“Ilidhihirika awali kwamba mpango wao ulikuwa kubuni chama chenye nguvu, hasa baada ya Jubilee ‘kumeza’ vyama tanzu kama vile TNA, URP na vinginevyo. Hii ilikuwa hatua ya kwanza kwamba lengo lao lilikuwa kubwa zaidi,” asema Bw Mutai.

Vile vile, wachanganuzi pia wanataja ukaribu uliopo kati ya uongozi wa Jubilee na CP kutoka Uchina, kama ishara ya wazi kwamba haiangalii nyuma.

Mwezi uliopita, ujumbe kutoka CP uliwasili nchini, ambapo ulitoa mafunzo kwa maafisa kadhaa wa Jubilee. Ilibainika kwamba maafisa hao watatumiwa na chama kuendesha ajenda zake katika kutoka ngazi ya kitaifa hadi mashinani.

Ilibainika kwamba jukumu kuu la maafisa hao litakuwa kuwafikia wananchi katika viwango vyote ili kuwafahamisha kuhusu ajenda kuu za chama, hasa manifesto yake.

 

Kuimarisha chama

Katika mojawapo ya mahojiano na kituo kimoja cha televisheni majuzi, mwenyekiti wa JP Bw David Murathe alieleza kuwa chama hicho kitageuzwa kuwa chenye misingi na asasi thabiti ambazo zitahakikisha kwamba kimebaki imara, hata wakati Rais Kenyatta na Bw Ruto watakapoondoka uongozini.

“Hatuna nia mbaya, ila lengo letu kuu ni kuimarisha mfumo wa siasa za nchi, ili kuondoa utegemezi wa watu binafsi, ila uwepo wa vyama ambavyo vitaendeleza malengo yake, hata viongozi hao watakapoondoka,” akasema Bw Murathe.

Mwezi uliopita, Rais Kenyatta alihudhuria maadhimisho ya miaka 106 tangu kuanzishwa kwa ANC, Afrika Kusini, hatua iliyoonekana kuimarisha ushirikiano kati ya vyama hivyi viwili.

Licha ya hayo, wakosoaji wa mpango huo wanautaja kama njama ya kurejesha utawala wa kidikteta nchini. Wanazikosoa mbinu hizo, hasa kuwazuia wabunge kutoa hisia zao kuhusu hali ya nchi, kama ishara ya wazi ya ukiukaji wa haki za kujieleza.

“Sitashangaa ikiwa nitaona maasi kutoka ukanda wa Mlima Kenya (anakotoka Rais Kenyatta) ama Bonde la Ufa (anakotoka Bw Ruto) kwani huu ni udikteta wa wazi,” akasema mwanaharakati wa kisiasa Raymond Mutembei.

 

Mbunge akanganya Kalonzo kuhusu msimamo wa Wiper

Mbunge wa Mwingi ya Kati, Bw Gideon Mulyungi. Picha/ Maktaba

BONFACE MWANIKI na BEN MATHEKA

Kifupi:

 • Bw Mulyungi asema Wiper iko tayari kuhama Nasa wakati wowote iwapo ODM itaendelea kumkosea heshima Bw Musyoka
 • Asema sharti viongozi wa ODM wakome kumtusi Bw Musyoka kwa kuwa haikuwa lazima Kalonzo kuhudhuria “uapisho” huo
 • ODM kimekuwa kikitenga vyama vingine vya muungano huo na hiyo ndiyo sababu ilifanya Wiper kuandikia barua Spika wa Bunge

MBUNGE wa Mwingi ya Kati, Gideon Mulyungi mwishoni mwa wiki alionekana kumkanganya kinara wake katika chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka kuhusu msimamo wa chama hicho katika Muungano wa NASA.

Mnamo Jumamosi Bw Mulyungi aliwaambia wanahabari nyumbani kwake Mwingi kuwa Wiper iko tayari kuhama Nasa wakati wowote iwapo viongozi wa ODM wataendelea kumkosea heshima Bw Musyoka.

Lakini akizungumza jana katika kaunti ya Kilifi, Bw Musyoka alikariri kuwa vinara wa NASA wameungana na kuwa ni Jubilee inayobuni madai ya mgawanyiko katika muungano huo wa upinzani.

Wiki iliyopita, Bw Musyoka alionekana kuwa na msimamo tofauti alipotisha kuwa Wiper inaweza kuondoka NASA iwapo viongozi wake hawataheshimiwa na wenzao.

Bw Mulyungi alieleza kuwa hawajaridhishwa na kukosewa heshima kwa kiongozi wao Bw Musyoka na baadhi ya viongozi wa ODM tangu alipokosa kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Raila Odinga kama “rais wa wananchi” mnamo  Januari 30.

Alisema sharti viongozi wa ODM wakome kumtusi Bw Musyoka akieleza kuwa haikuwa lazima kwake kuhudhuria “uapisho” huo uwanjani Uhuru Park.

 

Furaha ya kunguru

“Tunajua viongozi wa Jubilee wanameza mate wanapoona uwezekano wa kuvunjika kwa NASA wakidhani kuwa tunaweza kujiunga nao.

Ndugu zetu wa ODM wanafaa kuwa waangalifu, la sivyo tutawaachia muungano huo wakiwa na kiongozi wao tuone vile watakavyoendelea kivyao,” akasema Bw Mulyungi.

Kuhusu kugawana viti vya kamati za bunge, Bw Mulyungi alisema ODM kimekuwa kikitenga vyama vingine vya muungano huo na hiyo ndiyo sababu ilifanya Wiper kuandikia barua Spika wa Bunge kutaka mbunge wa Borabu Ben Momanyi kuwa mwanachama wa Tume ya Huduma ya Bunge.

ODM kiliwasilisha majina matatu ya wanachama hicho bila kushirikisha wale wa vyama vingine vya NASA, jambo analosema linaweza kusambaratisha muungano huo.

“Ndugu zetu katika ODM wanachochea mgawanyiko mkubwa katika NASA kwa sababu hatutakubali waendelee kutudhulumu ilhali kulingana na mkataba wa muungano huo tuko sawa,” alionya mbunge huyo.

Alisema Bw Musyoka sio mwoga na yuko tayari kula “kiapo” mradi tu wafuasi wake wanaunga mkono hatua hiyo.

Habari zaidi na BENSON MATHEKA

 

 

 

NGILA: Jubilee ikabiliane na visiki hivi ili kutimiza Ajenda Nne Kuu

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wahutubia taifa katika Ikulu ya Nairobi. Picha/ Maktaba

Na FAUSTINE NGILA

Kwa Muhtasari:

 • Katika mpango wake wa Ajenda Nne Kuu, serikali inalenga kuimarisha sekta za viwanda, afya, ujenzi na kilimo 
 • Mwelekeo ambao taifa hili linafuata ni wa hasara kwa wananchi wote
 • Utawala wa serikali unafaa kutambua kuwa amani hutokana na haki na si kinyume chake
 • Wakenya wanakumbana na gharama ya juu ya maisha, umaskini, ukosefu wa ajira, njaa na utovu wa usalama

SERIKALI ya Jubilee imekariri kuwa itaunda zaidi ya nafasi 1.29 milioni za ajira kutokana na viwanda kufikia mwaka 2022.

Hii ina maana kuwa kwa wastani, serikali itaunda nafasi 706 kila siku ili kutimiza ahadi hiyo. Katika mpango wake wa Ajenda Nne Kuu, serikali inalenga kuimarisha sekta za viwanda, afya, ujenzi na kilimo (chakula).

Kufikia mwishoni mwa 2018, utawala wa Jubilee unalenga kuongeza idadi ya wananchi wenye bima ya afya kutoka milioni 16.53 hadi milioni 25.74.

Serikali pia inapanga kujenga nyumba 500,000 itakazokodisha kwa bei nafuu katika miji mikuu kufiki 2022, mpango ambao inasema utaunda nafasi 350,000 za kazi.

Katika sekta ya ngozi, Rais Uhuru Kenyatta anadhamiria kufanikisha utengenezaji wa viatu milioni 20 nchini kufikia 2022, na kuongeza mapato kutokana na mauzo ya kigeni hadi Sh50 bilioni.

 

Mwelekeo wa hasara

Lakini tukirejelea matukio ya kisiasa humu nchini – kuanzia hatua ya kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga kulishwa kiapo kuwa ‘rais wa wananchi’, hadi mbinu za utawala wa Jubilee za kuzima wazo la marais wawili, Mkenya ataelewa kuwa mwelekeo ambao taifa hili linafuata ni wa hasara kwa wananchi wote.

Katika hali ya sasa ya kisiasa, huenda tukawa na chaguzi mbili sambamba iwapo matatizo yaliyopo hayatasuluhishwa kufikia mwaka 2020.

Hii ndiyo taswira ambayo haifurahishi wengi, lakini ni ithibati kuwa tulicho nacho kwa sasa hapa Kenya, ni changamoto kuu za uongozi katika pande zote za kisiasa, ambazo ni mwiba katika ndoto ya Ajenda Nne Kuu.

Changamoto hizi zinaonekana wazi katika upande wa Rais Uhuru Kenyatta – ikilinganishwa na Bw Raila Odinga – kwa kuwa Rais ndiye nahodha halisi wa chombo hiki kuhusu usimamizi wa ujenzi wa taifa.

Lakini lazima kama Wakenya tutoe maoni yetu kuhusu suluhu ambazo zitaturejesha katika njia bora ya ukuaji wa demokrasia na uchumi.
Mwanzo, sote twafaa kukubali kuwa tuko chini ya katiba, na wala si juu yake.

Tukirejelea kipengee cha 10 cha katiba na mambo yanayoshikilia taifa letu la kidemokrasia, tutapa kuwa tunafaa kuwa na uzalendo, umoja, ugatuzi wa mamlaka, sheria, demokrasia na kuwashirikisha wananchi.

 

Ubinadamu wa taifa

Kuna yale mambo ambayo yanashikilia ubinadamu wa taifa kama heshima, usawa, haki za kijamii, ushirikishi, haki za kibinadamu, kutotenga wengine na kulinda matabaka ya chini.

Mengine kama maadili, uwazi na uwajibikaji yanaashiria utawala bora.

Utawala wa serikali unafaa kutambua kuwa amani hutokana na haki na si kinyume chake, na kwamba haki inahitaji usalama kwa mkono mmoja na haki zetu kwa mkono wa pili.

Pili, ni kuhusu kuimarisha uchumi wa nchi. Fikiria kuhusu utawala ambao unaangazia kupanua uchumi, maliasili, maarifa na utangamano baina ya jamii mbalimbali.

Kwa sasa, tunashuhudia watu wengi wenye ujuzi na maarifa lakini wamegawanyika katika misingi ya kisiasa. Hii haiwezi kusaidia katika utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu.

 

Ukosefu wa usawa

Tatu, kuna ukosefu wa usawa – matajiri dhidi ya walalahoi – ambao hutokana na kukiukwa kwa mambo manne – usawa wa jinsia, usawa wa maeneo, umri na kushirikishwa kwa jamii zote.

Fikiria kuhusu matatizo ya kila siku yanayowakumba Wakenya – gharama ya juu ya maisha, umaskini, ukosefu wa ajira, njaa, utovu wa usalama.

Hizi ndizo changamoto ambazo Ajenda Nne Kuu za utawala wa Jubilee unafaa kuangazia kwa kina na kuleta sera mwafaka na mipango tekelezi kuzipunguza.

Kenya ikifuata haya hadi 2022, kwa yakini, haitapoteza dira na itapiga hatua kadha katika kuunda nafasi za ajira zipatao milioni 1.29.

 

JAMVI: Uhuru pabaya kwa kusahau baadhi ya maeneo ya Gema katika uteuzi wake

Na WANDERI KAMAU

Kwa Muhtasari:

 • Mirengo mitatu inang’ang’ania ushirikishi zaidi wa kisiasa serikalini, hasa baada ya wanasiasa wenye ushawishi kukosa kutajwa mawaziri
 • Kuchipuka kwa mirengo hiyo mitatu kunaashiria kibarua kipya kwa Rais Kenyatta
 • Rais Kenyatta anakejeliwa kwa kutomteua Bi Martha Karua kama waziri, licha ya kuahidi kwamba angemteua
 • Wanasema kuwa mwelekeo huo ni hatari, ambao huenda ukazua mgawanyiko mkubwa, hasa anapojitayarisha kung’atuka uongozini

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kukosa kuwateua baadhi ya wandani wake imezua uasi wa kichinichini katika ukanda wa Mlima Kenya, hali ambayo imegawanya eneo hilo katika mirengo mitatu ya kisiasa.

Mirengo hiyo inang’ang’ania ushirikishi zaidi wa kisiasa serikalini, hasa baada ya wanasiasa wenye ushawishi kukosa kutajwa katika baraza la mawaziri na Rais Kenyatta.

Mrengo wa kwanza unahusisha kaunti za Meru, Embu, Tharaka-Nithi na Kirinyaga. Mrengo wa pili unahusisha kaunti za Kiambu na Murang’a, huku mrengo wa tatu (Aberdare Group) ukishirikisha kaunti za Nyeri, Nyandarua, Laikipia na Nakuru.

Kulingana na wachanganuzi, kundi la kwanza linadai kutengwa na Bw Kenyatta, hasa baada ya kukosa kuteuliwa kwa Seneta Kithure Kindiki (Tharaka-Nithi) ambapo walimpigania kuteuliwa kama waziri.

Baadhi ya viongozi wa kaunti hizo wamejitokeza kuelezea kutoridhishwa kwao na uteuzi wa gavana wa zamani wa Meru, Peter Munya, wanayedai kutowakilisha maslahi ya wakazi hao.

 

“Ukiritimba wa kisiasa”

Chini ya uongozi wa Gavana Muthomi Njuki wa Tharaka-Nithi, kundi hilo linaamini kwamba kuteuliwa kwa Bw Munya ni uendelezaji wa “ukiritimba wa kisiasa” wa jamii ya Ameru.

“Tunahisi kutengwa kabisa na utawala wa Jubilee, licha ya kujitokeza pakubwa kumpigia kura Rais Kenyatta,” akalalama Bw Njuki.
Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, kundi la Kiambu-Murang’a linaonekana kuridhika na uteuzi wa watu kadhaa katika baraza hilo.

Miongoni mwa walioteuliwa ni James Macharia (Uchukuzi) ambapo anatoka katika Kaunti ya Murang’a na Joe Mucheru (anayetoka katika Kaunti ya Kiambu) ila ana makazi yake katika Kaunti ya Nyeri.

Kundi la tatu, maarufu kama ‘Aberdare Group’ halijafurahia kuteuliwa kwa Bw Mwangi Kiunjuri kama Waziri wa Kilimo.

Kulingana na Profesa Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa, kuchipuka kwa mirengo hiyo mitatu kunaashiria kibarua kipya kwa Rais Kenyatta, ikizingatiwa kwamba msingi wake mkuu ni kushinikiza uteuzi wa watu maarufu ambao waliachwa nje.

“Tathmini ya ndani inaonyesha kuwa msingi mkuu wa makundi hayo ni ung’ang’aniaji wa mamlaka, hasa kwa wanasiasa ambao waliachwa nje,” asema Prof Njoroge.

 

Mgawanyiko

Aidha, anatoa mfano wa kutotajwa kwa aliyekuwa mbunge wa Kigumo, Jamleck Kamau kama waziri ama naibu waziri, kama jambo ambalo huenda likazua uasi na mgawanyiko katika kundi linaloshirikisha kaunti za Murang’a na Kiambu.

“Kuna hatari kubwa ya Bw Kamau kujiunga na wanasiasa wengine waasi kama aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, hivyo kufanya kipindi cha pili cha Bw Kenyatta kuwa kigumu.

Ni wakati wa yeye (rais) kuwatafutia mahali baadhi ya wanasiasa hao, ili kuepuka uwezekano wa msambao wa uasi wa kisiasa,” asema Prof Njoroge.

Msukumo wa ukanda wa Mlima Kenya Mashariki (Embu, Meru na Tharaka-Nithi) ni hisia kwamba Rais Kenyatta ‘aliwazawidi’ watu ‘wasiofaa.’

Mchanganuzi wa kisiasa Daudi Mwenda anasema kuwa uteuzi wa Bw Munya kama Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki ni ishara ya wazi kwamba ni kama Rais Kemyatta hatambui mchango wao katika ushindi wake.

“Matarajio ya wengi yalikuwa kwamba angaa Bw Kenyatta angaliwazingatia baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Tharaka. Hii ni kwa kuwa tayari ‘amezituza’ jamii za Meru na Embu, kupitia uteuzi wa Bw Munya na Bi Cecily Mbarire kama mbunge maalum,” asema Bw Mwenda.

 

Kutomteua Bi Karua

Wengi pia wanamkosoa Bw Kenyatta kwa kutomteua Bi Martha Karua kama waziri, licha ya kuahidi kwamba angemteua, ikiwa angeshindwa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana wa Kirinyaga na Bi Anne Waiguru.

Malalamishi kama hayo ndiyo yaliyo katika kaunti zilizo katika kaunti zinazojumuisha kundi la ‘Aberdare Group.’

Wachanganuzi na viongozi katika eneo hilo wanapinga uteuzi wa Mabw Joe Mucheru na Mwangi Kiunjuri, wakiwataja kuwa “wageni” na kutofaa katika eneo lao.

Baadhi ya viongozi wa Nyeri wamejitokeza kulalamika kwamba Bw Mucheru si mmoja wao, huku Bw Kiunjuri akidaiwa kuwa mwakilishi wa Kaunti ya Laikipia.

“Kwa mara nyingine, Rais Kenyatta ameisahau Kaunti ya Nyeri, licha yake kujitokeza pakubwa kumpigia kura. Hatuna waziri hata mmoja katika baraza lake.

Aliowachagua (Mucheru na Kiunjuri) si wakazi asilia wa Kaunti ya Nyeri. Tunamtaka kutimiza ahadi yake,” akasema mbunge wa Kieni Kaniini Keega.

Mchanganuzi na wakili Wahome Gikonyo anawataja wawili hao kutokuwa “wawakilishi wa kisiasa wa eneo hilo.”

 

Hawapendezi

“Mabw Kiunjuri na Mucheru wamehudumu katika kipindi cha kwanza cha rais, ambapo imedhihirika kwamba hawapendezi. Hawajaonekana kumjenga Rais Kenyatta. Ni wakati rais anafaa kutathmini msimamo wake,” asema Bw Gikonyo.

Wakosoaji wa Bw Kenyatta wanataja uteuzi wake kuwa unaoendeleza “ukiritimba wa kisiasa wa Kaunti ya Kiambu” kama alivyofanya babake, marehemu Mzee Jomo Kenyatta.

Wanasema kuwa mwelekeo huo ni hatari, ambao huenda ukazua mgawanyiko mkubwa, hasa anapojitayarisha kung’atuka uongozini.

“Ni wakati mwafaka azibe nyufa zote ambazo huenda zikaleta mgawanyiko katika ngome yake,” asema mwanaharakati wa kisiasa Linford Mutembei.

 

JAMVI: Onyo utawala wa Jubilee unarejesha Kenya gizani

Wakili mbishi Dkt Miguna Miguna alipowasili jijini Toronto, Ontario, Canada baada ya kufurushwa humu nchini Februari 5, 2018. Picha/ Hisani

Na BENSON MATHEKA

Kwa Muhtasari:

 • Watetezi wa haki za binadamu wanaonya kwamba haki za binadamu zinapuuzwa ili kurejesha Kenya katika utawala wa kiimla wa chama cha KANU
 • Ingawa serikali ilisema kwamba Miguna alikuwa raia wa Canada, iliibuka kuwa walikataza maafisa wa ubalozi wa nchi hiyo jijini Nairobi kumuona
 • Gharama ya ukiukaji wa haki za binadamu ni kubwa. Wanaowajibika wanafaa kuheshimu katiba na kuwa msitari wa mbele kuilinda

MATUKIO yaliyopelekea kufurushwa kwa mwanasiasa mbishi Miguna Miguna yamefanya serikali kushutumiwa vikali na kuonywa dhidi ya kurejesha Kenya katika enzi za giza kwa kupuuza utawala wa sheria, kunyanyasa upinzani na kukiuka haki za raia.

Watetezi wa haki za binadamu na wanauchumi wanaonya kwamba hatua ambazo Kenya ilipiga chini ya katiba mpya hasa kuhusu haki za binadamu, zinapuuzwa kwa lengo la kurejesha Kenya ilivyokuwa chini ya utawala wa kiimla wa chama cha Kanu.

Wanasema dalili za Kenya kurejea katika enzi za giza zinajitokeza kufuatia kukandamizwa kwa vyombo vya habari, kukamatwa na kuzuiliwa kwa watu wanaokosoa serikali na kupuuzwa kwa maagizo ya mahakama.

 

Mwelekeo hatari

Kulingana na Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (KNHRC), serikali imechukua mwelekeo hatari unaoweza kutumbukiza nchi katika msukosuko kwa kutoheshimu utawala wa sheria.

KNHRC inataja ukadamizaji wa uhuru wa wanahabari na maafisa wa serikali na kudharau mahakama kama vitisho kwa utawala wa sheria, upuuzaji wa haki za binadamu na demokrasia.

“Tume inasikitishwa na matukio ya wiki moja iliyopita ambapo kumekuwa na ongezeko la visa vya kudharau utawala wa sheria, vitisho kwa haki za binadamu na haki za kidemokrasia ambazo zimetambuliwa na kuhifadhiwa katika katiba,” asema mwenyekiti wa tume hiyo, Bi Kagwiria Mbogori kwenye onyo kwa waziri wa usalama wa ndani, Dkt Fred Matiang’i, Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet na ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma.

Maafisa hao watatu walipigwa darubini kufuatia kukamatwa kwa viongozi wa upinzani, kuwapokonywa walinzi, silaha na paspoti zao na kuandamwa na maafisa wa polisi.

 

Enzi za giza

“Tunatoa onyo kwamba Kenya inarejea kwa haraka katika enzi za giza na zenye uchungu mwingi. Tunalaani vikali kukamatwa kiholela kwa watu na kudharau mahakama kunakoendelea,” asema Bw Mbogori.

Onyo hilo lilijiri saa chache baada ya serikali kumtimua mwanasiasa Miguna Miguna ikidai hakuwa raia wa Kenya baada ya kukamatwa na polisi na kuhangaishwa kwa siku tano.

Polisi walikataa kutii maagizo kadhaa ya mahakama kumfikisha kortini. Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa upelelezi George Kinoti pia walipuuza agizo la Jaji Luka Kimaru la kufika mbele yake kueleza kwa nini walikataa kutii agizo la mahakama.

Ingawa serikali ilisema kwamba Miguna alikuwa raia wa Canada, iliibuka kuwa walikataza maafisa wa ubalozi wa nchi hiyo jijini Nairobi kumuona akiwa seli hatua ambayo mawakili wanasema ni kilele cha ukatili.

 

Twaelekea wapi?

“Ikiwa polisi wanaweza kumkamata raia wa nchi ya kigeni na kunyima ubalozi wa nchi hiyo nafasi ya kumuona, tunafaa kujiuliza tunaelekea wapi kama nchi na kurekebisha mambo kabla ya kuharibika zaidi,” alisema wakili mmoja aliyeomba tusitaje jina lake kwa sababu ya uhusiano wake na Jubilee.

Anasema matukio ya hivi majuzi yanaonyesha kwamba washauri ambao rais anatengemea. Bi Mbogori anamtaka Bw Boinnet kuhakikisha polisi wanafuata katiba na kutimiza viwango vya haki za binadamu katika kazi yao.

“Agiza maafisa wote wa polisi kufuata katiba kikamilifu na kuheshimu haki za binadamu za watu wanaokamatwa na wote wanafaa kuchukuliwa kuwa sawa bila ubaguzi kwa misingi yoyote,” Bi Mbogori alimweleza Bw Boinnet.

KNHRC ilimwelekezea waziri Matiang’i kidole cha lawama kwa kukandamiza uhuru wa wanahabari na kumuonya kwamba maagizo anayotoa hayafai kukiuka katiba.

“Fuata sheria na ukome mara moja kutoa amri zinazoenda kinyume cha sheria,” tume ilimweleza Bw Matiang’i na kumtaka kufungua vituo vya runinga ilivyoagiza mahakama. Serikali ilifungua vituo vya NTV na KTN News lakini ikachelewa kufungua Citizen Tv na Inooro Tv.

 

Kusambaratisha uchumi

Wadadisi wanasema serikali ikiendelea kukandamiza upinzani, kudharau mahakama na kupuuza utawala wa sheria inaalika msukosuko ambao utalemaza ukuaji wa uchumi.

“Ni mwelekeo mbaya ambao utaathiri uchumi wa nchi, hakuna mwekezaji anayependa nchi isiyo thabiti kisiasa,” asema Dkt Rajnkat Shah, mwekezaji wa kimataifa.

Bi Mbogori anaonya kwamba hali ya kisiasa nchini inaathiri haki za vijana, wanawake, watoto, wazee na watu walio na ulemavu na tayari imeanza kuzua taharuki.

“Ripoti ya tume inaonyesha kuwa kufikia Februari 6, maandamano ya raia yemelipuka katika maeneo ya Kisumu na Migori ambapo mtu mmoja aliuawa Ahero, mali ikaharibiwa na kuibwa. Hali ya sasa inaonyesha jamii inayokumbwa na taharuki na kugawanyika kwa misingi ya kikabila na kisiasa,” anaeleza Bi Mbogori.

Anaonya kwamba maafisa wa serikali wanaohusika hawatajukumika, hali itakuwa mbaya zaidi na kuzaa majuto.

“Tume inawakumbusha wote wanaohusika kwamba gharama ya ukiukaji wa haki za binadamu ni kubwa, gharama ambayo nchi inayong’ang’ana kutimiza mahitaji yake ya kiuchumi na maslahi ya kimsingi ya raia wake haiwezi kumudu. Wanaowajibika wanafaa kuheshimu katiba na kuwa msitari wa mbele kuilinda na kuitetea kwa nia nzuri,” alisema