KAULI YA MATUNDURA: Ken Walibora anavyoendeleza taswira ya uana katika ‘Mgomba Changaraweni’

Na BITUGI MATUNDURA

‘MGOMBA Changaraweni’ ni mojawapo ya kazi nyingi za fasihi alizotunga Ken Walibora.

Marehemu Walibora alifahamika sana kwa utunzi wa riwaya na hadithi fupi ingawa pia alichangia mno utanzu wa fasihi ya Kiswahili ya watoto.

Baadhi ya kazi zake ni pamoja na riwaya za Siku Njema (Longhorn,1996), Kufa Kuzikana (Longhorn, 2003), Ndoto ya Almasi (Moran,2007).

Vitabu vyake vya fasihi ya Kiswahili ya watoto ni pamoja na Ndoto ya Amerika (Sasa Sema, 2001) Mtu wa Mvua (Phoenix, 2004) Chapuchapu (Phoenix, 2006), Nimeshindwa Tena (Phoenix) na Mgomba Changaraweni (Phoenix) ambacho ni mojawapo ya kazi ninayoihakiki katika makala haya.

‘Mgomba Changaraweni’ ni hadithi kuwahusu jagina mchunga mifugo anayeitwa Chongameno na msichana kwa jina Alice Kesho ambaye anampenda Chongameno.

Chongameno kwa upande wake anakataa penzi la Alice. Hali hiyo inamfanya Alice kusababisha hasara na mateso makubwa kwa jamii yake kwa sababu Chongameno anakataa kumuoa. Moto aliouwasha ukateketeza msitu wa Suwerwa.

Mwanzo, jamii yake inafikiria kwamba Chongameno ndiye mhalifu aliyetenda kosa hilo na kumtumbukiza gerezani.

Mwishowe, inabainika kwamba kwa hakika Chongameno hana hatia kupitia kwenye ujumbe katika kijikaratasi alichoandika Alice kabla ya kujiua.

Hadithi hii ina sifa za vitabu vya fasihi ya watoto tulizotaja katika sura ya pili.

Ina sura fupi, ni sahili na inasomeka kwa urahisi. Aidha, ina michoro na imechapwa kwa maandishi makubwa na lugha sahili.

Taswira dumifu za uana katika ‘Mgomba Changaraweni’ zinadhihirika hasa tunapoangazia hulka ya wahusika wakuu katika hadithi hii na majukumu yao ya kikazi.

Chongameno ambaye ni mhusika mkuu na wa jinsia ya kiume amesawiriwa kama kijana mwenye nguvu aliyefanya kazi za ushokoa bila kuchoka.

Picha ya Chongameno inayojitokeza katika hadithi hii inaendeleza taswira dumifu katika jamii kwamba mwanamume ni kiumbe mwenye nguvu na uwezo mkubwa wa kutenda mambo anapolinganishwa na mwanamke.

Alice Kesho kwa upande mwingine amesawiriwa kama kiumbe mrembo na safi anayependa kujirembesha kila wakati. Tunafahamishwa: Alisimama wima mbele ya kioo chake, kifua wazi alivyozaliwa. Aliyatazama kiooni madodo yake akayaona yameiva. Akacheka.

“Nani kama mimi?” akajisemea.

Akajipaka mafuta mwilini. Ngozi yake ilikuwa laini. Hakuzoea kazi ya sulubu kama vijakazi wa pale nyumbani, waliojisaga kazini kama watumwa hasa.

Haikuwa ajabu basi kuwa ngozi yake ilikuwa laini na nyororo. Alikuwa na umbo la wastani, si mwembamba sana si mnene sana, na ngozi yake ya maji ya kunde iliwapa vijana wavulana pumbao na tamanisho (Uk. 19).

Hulka ya Alice Kesho kuwa mtegemezi wa Chongameno inajitokeza mwishoni mwa hadithi hasa anapoamua kujiua kwa sababu haoni maana ya maisha baada ya Chongameno kukataa ombi lake la kumtaka awe mpenzi wake.

Hatua ya kujiua inazua maswali mengi kuliko majibu. Je, kulikuwa na haja ya Alice Kesho kujiua?

Hatua hiyo inaonyesha kwa vyovyote udhaifu alio nao mwanamke kutoweza kuishi bila kumtegemea mwanamume?

(Makala yataendelea)

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Mashekhe wanachangia kudorora kwa matokeo ya Kiswahili Pwani ya Kenya?

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA makala yangu yaliyochapishwa kwenye Taifa Leo Juni 16, 2021) niliahidi kuendeleza majadiliano ya wataalamu wa Kiswahili kuhusu chanzo cha matokeo duni ya Kiswahili katika mitihani ya taifa ya shule za msingi (KCPE) na upili (KCSE).

Mdahalo huo ulichukua mkondo ‘mpya’ baada ya msomi wa Kiswahili, Dkt Wambua Kyeu, anayefundisha Marekani kuibuka na nadharia tete kwamba hali hiyo huenda inachangiwa na mashekhe wanaohubiri misikitini kwa ‘kutumia lahaja’. Mdahalo huo ulifanyika katika ukumbi wa WhatsApp wa Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

Ikumbukwe kwamba lugha ya Kiswahili ina takriban lahaja 15. Lahaja hizi ni pamoja na Kiunguja (Zanzibar), Kimakunduchi (au Kihadimu) na Kitumbatu (kinachozungumzwa maeneo ya mashambani, Zanzibar), Kipemba (kisiwa cha Pemba); Kimtang’ata (Tanga); Kimrima (pwani ya Tanzania) na Kimgao (Kilwa).

Lahaja nyingine ni : Kimvita, Kingare na Kijomvu (kisiwani Mombasa na viunga vyake); Kiamu, Kisiu, Kipate, Kibarawa (Kimiini/Chimiini), na Kitikuu (pwani ya kaskazini ya Kenya hadi Somalia kusini), Kivumba na Chichifundi (Wasini na Vanga), Kingwana (DRC na Kongo) na Kingozi (Kiswahili asili).

Kiunguja ndiyo lahaja iliyoteuliwa na wamishionari mnamo miaka ya 1930 kuwa msingi wa usanifishaji wa Kiswahili. Katika mchakato wa uteuzi wa lahaja ya usanifishaji wa Kiswahili, kulikuwa na suala la kukidhi maslahi pamoja na siasa.

Mtaalamu Abdallah Khalid ameliangazia suala hili kwa uketo katika kitabu chake – The Liberation of Kiswahili from European Appropriation (East African Literature Bureau, 1977). Kiunguja ‘kilipendelewa’ kuliko Kimvita na lahaja nyingine kwenye kinyang’anyiro cha uteuzi wa lahaja ya usanifishaji kwa madai kwamba kilikuwa kinatumiwa sana katika shughuli za biashara na vilevile kuwa na maandishi mengi (written corpus). Aidha, mtaalamu Ireri Mbaabu ameandika kwa uketo jinsi Kiswahili kilivyosanifishwa katika kitabu chake – Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili (TATAKI, 2007).

Fasiri ya kimsingi ya dhana ‘lahaja’ kwa mujibu wa wanaisimujamii ni: tofauti katika matamshi, maumbo na matumizi ya maneno katika maeneo mbalimbali yenye asili moja. Kutokana na ufafanuzi huu, wanaisimujamii hujipata taabani katika kuweka mpaka baina ya lugha na lahaja. Mumo kwa mumo katika lugha mna lahaja.

Ubainifu baina ya dhana hizi mbili unaweza kuonekana bayana tunapoangalia ‘lugha’ kwa mkabala wa siasa kimaeneo (Geopolitics of language). Kwa mfano, nchini Kenya, ingawa tuna jamii ya watu wanaoitwa Wameru, hakuna hata mmoja ‘anayeweza kuzungumza Kimeru’. Wanachozungumza watu wa jamii hii ni lahaja za Gichuka, Kimwimbi, Kitigania, Kiigembe, Kitharaka n.k. Kwa hiyo dhana ‘Kimeru’ imefumbata zaidi mwonoulimwengu wa eneo la kijiografia na kisiasa kuliko mwonoulimwengu wa lugha.

Hatua ya usanifishaji wa lugha yoyote ile haiwanyimi wala kuwazuia wasemaji wa lahaja fulani kuizungumza lahaja yao. Kinachosababishwa na shughuli ya usanifishaji ni kuweka tu mipaka ya kuonesha wazungumzaji wa lugha/lahaja ni lini, wapi na vipi wanapaswa kuzungumza lugha sanifu.

Kwa hiyo, nadharia tete ya Mwalimu David Wambua Kyeu kuwa hotuba za Sheikh Izudin Alwy Ahmed misikitini anayesema ‘moya’ badala ya ‘moja’, ‘kitwa’ badala ya ‘kichwa’, ‘ndia’ kwa maana ya njia ina suluhu katika Kiswahili sanifu.

Makala yataendelea…

KAULI YA MATUNDURA: Shabaan Robert na Muyaka walinyanyasa na kudhulumu wanawake katika tungo zao?

Na BITUGI MATUNDURA

NILIPOHUDHURIA Maonesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Kila mwaka jijini Nairobi mnamo 2018, nilizuru ‘kibanda’ cha Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI) kujionea machapisho mapya katika fasihi na Isimu ya Kiswahili.

Maonesho hayo huandaliwa kila mwaka na Chama cha Wachapishaji wa Vitabu cha Kenya (KPA). Mojawapo ya vitabu nilivyovinunua ni Chanjo, Matakwa ya Mwanamume Katika Mwili wa Mwanamke (Muhammed Seif Khatib, 2014). Ingawa kitabu hiki kilichapishwa takriban miaka sita iliyopita, sikupata fursa ya kukisoma kwa sababu sikuwa nimehudhuria maonesho hayo kwa kipindi cha miaka minne. Muhammed Seif Khatib ni mwandishi, mhakiki na vilevile mwanasiasa.

Kazi yake maarufu katika ulingo wa fasihi ni diwani yake ya Wasakatonge (OUP,2003). M.S. Khatib ni mhakiki ambaye misimamo yake katika uhakiki wa fasihi ya Kiswahili imewahi kuzua midahalo miongoni mwa wasomi wa fani hizo. Kwa mfano, msimamo wake katika mdahalo kuhusu Utendi wa Mwanakupona (1850) ni kwamba: “Utendi wa Mwanakupona ni ‘sumu’ inayolenga kuhalalisha dhuluma na ukandamizwaji wa mwanamke katika asasi za jamii.”

Mwengo wa msimamo huu unajitokeza tena katika kitabu chake ambacho nimekwisha kukitaja. Katika kitabu hiki, Khatib anachunguza kwa kina na kufanya uhakiki wa kiulinganifu baina ya washairi wawili mahashumu katika fasihi ya Kiswahili – Muyaka bin Haji na Shaaban bin Robert. Baadhi ya maswali ambayo amejikusuru kuyatalii katika kitabu hiki ni pamoja na: Ni vipi Muyaka bin Haji na Shaaban bin Robert ambao waliishi katika jamii na nyakati tofauti wanafanana na wakati huohuo kutofautiana katika mitazamo na matakwa yao kuhusu taswira ya mwanamke?

Je, zipo athari za kisiasa, kidini, kielimu na kiuchumi kuhusu mitazamo yao kumhusu mwanamke? Mwisho, kitabu chake kimelenga kuchochea mwamko wa ukombozi wa fikra juu ya mwanamke kwa misingi kwamba wanawake ni kundi la kutengwa na kunyanyaswa kwa kipindi kirefu mno – hususani katika asasi za jamii.

Je, Muyaka bin Hajji na Shaaban bin Robert walishiriki na au kuchangia vipi katika ‘ujambazi’ wa kumkandamiza na kumdhalilisha mwanamke katika mashairi yao? Walifanya hivyo kwa kujua au kutojua? Vipi?

Katika kitabu chake, M.S.Khatib anadai kwamba dhamira ya Muyaka bin Haji ya kebehi na dharau inamlenga mwanamke ambaye anakataa udhibiti. Jazanda alizozitumia Muyaka katika tungo zake chambacho Khatib, zinamweka mwanamke katika nafasi ya unyonge na kulazimika kurudi kwa mwanamume kwa shingo upande na kuwa udhibiri wake. Naye Shabaan bin Robert – licha ya kumsifu mwanamke kwa kumumithilisha na ‘ua’ katika mashairi yake mengi kuusifia urembo wake, wakati mwingine anamgeuka (mwanamke huyo) na kumwita ‘malaya’ kwa majina ya kebehi kama vile ‘magune’, ‘pangapunge’, ‘makuyembesa’ na ‘vigwene’.

Kitabu cha Khatib kinachangia upya mdahalo kuhusu suala la taswira ya mwanamke katika fasihi ya Kiswahili. Kwa bahati mbaya, Mohamed Seif Khatib alifariki mapema mwaka huu. Hata hivyo, tunaliwazika na kufarijika kwamba ‘waandishi hawafi’. Huendelea kuishi katika tungo na maandishi yao. Hii ndiyo sababu tungali tunamkumbuka William Shakespeare wa Uingereza – hata ingawa alifariki takriban miaka 400 iliyopita.

KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wamuenzi galacha, mwalimu na mlezi wa wengi Prof Ireri Mbaabu

Na BITUGI MATUNDURA

JUMA lililopita, hafla mbalimbali za kumuenzi na kumsherehekea mwalimu wa wengi – Prof George Ireri Mbaabu zilifikia kileleni kwa kongamano la webina lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Mkuu wa Idaya ya Kiswahili ya chuo hicho – Dkt Pamela Ngugi alisema, mbali na kuandaa dhifa ya kumshukuru na kumuaga Prof Mbaabu ambaye amefundisha Chuoni Kenyatta kwa zaidi ya miongo minne, Idara pia inadhamiria kuchapisha kitabu maalum kitakachowapa fursa wanataaluma wa Kiswahili kuandika makala kumhusu msomi huyo na mchango wake katika tasnia ya Kiswahili.

Mada ya webina hiyo iliyoandaliwa mnamo Machi 2, 2021 ilikuwa ni ‘Ukuzaji na Maendeleo ya Kiswahili’.

Wawasilishaji walikuwa ni pamoja na Prof Chacha Nyaigotti Chacha (Kamisheni ya Vyuo Vikuu, CUE-Kenya), Dkt Musa Hans (Naibu Mkurugenzi, TATAKI, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Maprof Sheila Ryanga, Kitula King’ei na Catherine Ndungo – wote wa Chuo Kikuu cha Kenyatta. Waratibu wa webina hiyo walikuwa ni Dkt Leonard Chacha Mwita, Bi Evelyne Mudhune, Dkt Pamela Ngugi na Dkt Richard Makhanu Wafula.

Akiifungua rasmi webina hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Kenyatta, Prof Paul K. Wainaina alimtaja Prof Mbaabu kuwa mwalimu, mshauri, mlezi na mwelekezi ambaye kwaye wanafunzi na wataalamu wengi walipitia mikononi mwake. Makamu Mkuu wa Chuo cha Kenyatta – Taaluma, Prof Paul Okemo alisema, “Wakati wako umefika kuondoka kwenye ulingo wa ‘kucheza densi’. Umekwisha kuwafundisha wacheza densi wa kutosha – na hata kama umeng’atuka, densi bado itaendelea katika kumbi za mihadhara kwa muda mrefu siku za mbeleni.”

Alimtaja Prof Mbaabu kuwa msomi mwenye nidhamu na bidii aliyetimiza malengo yake.

Prof Paul Wainaina alieleza kwa uketo safari ndefu ya Prof Mbaabu katika ulingo wa usomi. Prof Mbaabu alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mapema miaka ya 1970 – kusomea Kiswahili, Sosholojia na Elimu. Mnamo 1973, alikwenda katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles nchini Marekani kusomea shahada yake za uzamili (Masters) katika taaluma ya isimu.

Mnamo 1975, aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Kenyatta alikofundisha kama Tutorial Fellow. Mnamo 1981, alikwezwa ngazi kuwa mhadhiri. Mnamo 1988, alikwenda katika Chuo Kikuu cha Howard – Washington DC kusomea shahada yake ya Uzamifu (PhD). Prof Mbaabu amewahi kuwa mshauri wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mbali na kutuzwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili) mnamo 2005. Kwenye wasilisho lake, msomi na mhakiki, Prof Kitula King’ei alisema: “Prof Mbaabu ni mtu mwenye bidii na nidhamu kazini; mtenda haki aliyewasaidia wanafunzi wengi kupata nafasi za ufadhili wa masomo […] alinitia ari ya kuandika na kuchapisha jinsi alivyofanya yeye.”

Mchango wa Prof Mbaabu katika taaluma ya Kiswahili unaonekana bayana katika makala yake kwenye majarida ya kitaaluma barani Afrika, Asia, Marekani na Ulaya.

Baadhi ya vitabu vyake maarufu vinavyotumika kama marejeleo muhimu katika taasisi za elimu kote ulimwenguni ni pamoja na : Sheng –English Dictionary ; aliyoandika kwa ushirikiano na Nzuga Kibande (TUKI,2003), Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili (TUKI,2007), New Horizons in Kiswahili : A Synthesis in Development Research & Literature (KLB,1978) na Language Policy in East Africa: A Dependency Theory Perspective (ERAP,1996). Riwaya yake ya hivi majuzi ni Masomoni California (Longhorn,2017)

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Mshabaha kati ya Rais Magufuli na Kinjeketile Ngwale wa mwanatamthilia Ebrahim Hussein

Na BITUGI MATUNDURA

HAIWEZEKANI kamwe kushiriki diskosi ya siasa za Afrika ya Mashariki katika siku za hivi punde bila angalau kulitaja jina la rais wa Tanzania – Dkt John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki hivi majuzi.

Ninachukua fursa hii kutoa risala zangu za rambirambi kwa raia wa Tanzania kwa kumpoteza rais wao. Kifo cha rais John Magufuli ni pigo kubwa si tu kwa nchi yake – bali pia Afrika ya Mashariki na Kati, maeneo ya Maziwa Makuu na bara zima la Afrika kwa jumla.

Mauko ya rais huyu na hususan mkabala na sera zake za kuukemea ubeberu, ufisadi na vita dhidi ya maradhi hatari ya korona vinanichochea kumlinganisha na mhusika – Kinjeketile Ngwale katika tamthilia maarufu ya Kinjeketile (Ebrahim Hussein, Oxford University Press -1969).

Tamthilia ya Kinjeketile imesukwa na kukitwa kwenye kiunzi cha Kinjeketile wa kihistoria aliyewaongoza Watanganyika katika Vita vya Maji Maji (1904 -1905).

Kwa kuwa fasihi mara nyingi huakisi na kufumbata tajriba na matukio halisi katika maisha ya binadabu, sikosei kudai kwamba si ajabu hulka na sifa za Kinjeketile Ngwale kujitokeza katika rais wa Tanzania – John Pombe Magufuli.

Katika tamthilia ya Kinjeketile, Ebrahim Hussein anasema kwamba Mjerumani alipofika Tanganyika, aliwaamrisha Wamatumbi kulipa kodi. Isitoshe Watanganyika walikabiliwa na dhiki nyingine kama vile njaa, maonevu na kupigwa. Katika hali hiyo, akajitokeza ‘mkombozi’ wao – Kinjeketile aliyeishi kijiji cha Ngarambe karibu na kijito cha Mto Rufiji. Kinjeketile alipandwa na pepo aliyekuwa akiishi katika bwawa hilo.

Akawafundisha Waafrika maana ya umoja, akawatia moyo kwa kuibuka na dhana ya maji. Waafrika wakawa na umoja na nguvu. Watu wengi waliosikia jina lake kwa njia ya ‘nywiywila’ wakaja kumuunga mkono. Maji haya kulingana na matamshi yake yangewazuia watu wasidhuriwe na risasi za Wajerumani ambao waliikalia nchi yao kwa mabavu.

Vivyo hivyo, rais John Pombe Magufuli alikuwa ‘mkombozi’ wa wanyonge na maskini kutokana na ufisadi. Katika kipindi cha miaka sita alichoiongoza Tanzania, alijaribu kadri ya uwezo wake kuwawezesha Watanzania wengi kiuchumi. Katika kipindi hicho, alibadilisha pakubwa amara au miundombinu ya Tanzania. Sawa na Kinjeketile, rais Magufuli alikuwa aliwaelekeza Watanzania katika mkondo wa imani ya maombi kwa Mwenyezi Mungu.

Aliamini kwamba sala ingekuwa silaha kuu katika kukabiliana na ugonjwa wa korona ambao umeutikisa ulimwengu. Akapuuza masharti ya sayansi kama vile kuvaa barakoa na kujiepusha na misongamano na kubanana kwa watu. Akapendekeza kuwa watu wajivukizie.

Mshabaha mwingine kati ya Kinjeketile na rais Magufuli ni kwamba wote wawili walipata ufuasi mkubwa. Jinsi ambavyo dhana ya maji ilivyoteka akili za Watanganyika katika Kinjeketile, ndivyo dhana ya maombi ilivyowateka bakunja raia wengi wa Tanzania. Hata katika hafla ya maombolezo yake, hatukuona raia wengi wa Tanzania wakiwa wamevalia barakoa. Kilele cha tamthilia ya Hussein – Kinjeketile ni kwamba Wamatumbi, Wapogoro, Wazaramo, Wakichi na watu wote wanayaamini ‘dhima ya maji kijinga’ na wanafyekwa na risasi za Mjerumani. Kinjeketile anatiwa mbaroni na kukataa kukana kuwa maji ni uwongo hata baada ya kupigwa mno. Anasema mwishoni mwa mchezo, “Neno limezaliwa […].

Siku moja neno hilo halitakuwa ndoto, bali ukweli. Sawa na Kinjeketile, rais Magufuli amekwisha kufariki. Maneno na azma yake kuhusu Tanzania na bara la Afrika na uhuru wa Mwafrika yatakuwa ya kweli siku moja.

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Kanuni za Kudumu za Bunge hazitasaidia sana ikiwa Baraza la Kiswahili la Kenya halitaundwa

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO Novemba 12, 2020, kwenye hafla ya Hotuba ya Rais Kwa Taifa, Rais Uhuru Kenyatta alizindua tafsiri ya Kiswahili ya Kanuni za Kudumi za Bunge kutimiza mahitaji ya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.

Kwa mujibu wa Katiba hiyo, Kiswahili ni lugha ya taifa na rasmi – sambamba na Kiingereza. Hatua ya uzinduzi huo ilipiga jeki mambo mawili.

Kwanza, ilionesha kwamba Kiswahili kinaendelea kukuzwa Kimakusudi nchini Kenya. Kwa muda mrefu, lugha hii imeachwa ijitafutie mkondo wake. Pili, uzinduzi huo utakivusha Kiswahili hadi ng’ambo ya pili katika kuhakikisha kwamba suala la Sera ya Lugha nchini Kenya – hususan kiutekelezaji linatiliwa maanani. Kwa nini? Kwa sababu masuala ya maendeleo na ustawishaji wa lugha yanafungamana mno na siasa.

Licha ya kuisherehekea hatua hii, ni muhimu kukumbuka kwamba Kenya bado haina Baraza la Kiswahili la Kenya (BAKIKE). Je, kuna faida gani kuwa na Baraza la Kiswahili nchini Kenya? Tangu 1967, Tanzania imekuwa na vyombo vingi vinavyofadhiliwa na serikali. Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967. Kutokana na sheria hiyo, Baraza hilo linaratibu na kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majukumu yake kama yalivyofafanuliwa na Sheria hiyo ni pamoja na: Kuratibu na kusimamia maendeleo ya Kiswahili nchini Tanzania, kushirikiana na vyombo vingine nchini humo vinavyojihusisha na maendeleo ya Kiswahili na kuratibu shughuli zao, kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida na kushirikiana na mamlaka zinazohusika zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi.

Majukumu mengine ni pamoja na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali, mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali na asasi nyingine, kuchapisha jarida au toleo linalohusu lugha na fasihi ya Kiswahili, kushirikiana na mashirika ya kitaifa, asasi na watu binafsi, kufuatilia, kushauri na kusimamia shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili na kushirikiana na mashirika mengine ya kitaifa na kimataifa kusimamia utafiti unaohusu Kiswahili nchini Tanzania.

Vilevile, Baraza hilo hutoa ushauri kwa waandishi na wachapishaji ili watumie Kiswahili fasaha mbali na kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuidhinisha vitabu vinavyotumika shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa.

Muundo wa kiutawala wa BAKITA ni kwamba, kuna idara tano; nazo ni idara ya uhariri na uchapishaji, Idara ya Lugha na Fasihi, Tafsiri na Ukalimani, Istilahi na Kamusi na Idara ya Uhusiano. Idara hizi zote hufanya kazi kwa ushirikiano. Idara ya Istilahi na Kamusi kwa mfano hufanya utafiti wa istilahi zinazotakiwa kusanifiwa na Kamati ya Kusanifu Lugha (KAKULU). Idara hii pia huandaa orodha ya istilahi zinazosanifiwa na KAKULU na kuidhinishwa na Baraza, kuandaa istilahi sanifu kwa ajili ya kuchapishwa katika matoleo ya Tafsiri Sanifu na kufuatilia matumizi yake, kuandaa Kamusi kwa matumizi ya asasi, shule na watu wa aina mbalimbali na vilevile kutoa ufafanuzi wa istilahi kwa wanaoihitaji.

Nchini Kenya, shughuli ya kubuni, kusanifisha, kusawazisha na kusambaza istilahi mpya za Kiswahili limeachiwa watu binafsi na vyombo vya habari. BAKIKE hivyo basi itatoa mwongozo katika maendeleo ya Kiswahili.

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Walibora alivyopagazwa wizi wa miswada

Na BITUGI MATUNDURA

MAKALA ya mwandishi Ken Walibora ‘Ukarimu wa Wallah katika tasnia pana ya Kiswahili’ (Taifa Leo, Machi 9, 2017) yaliibua kumbukumbu muhimu katika akili yangu.

Katika makala hayo, Walibora – ambaye nimewahi kudai kuwa ni mmoja wa waandishi aali wa fasihi ya/kwa Kiswahili Afrika ya Mashariki kuwahi kuonekana mpaka sasa, na katika makala yangu – ‘The Power of an enlightened mass’ (Sunday Nation, Agosti 18, 2012) alishangaa ni kwa nini hajashtakiwa kwa ‘wizi wa miswada’. Wala hakuna mtu aliyejitokeza kudai kuwa kaibiwa m(i)swada u/(i)pi, lini na wapi.

Prof Walibora ameukejeli uvumi huu katika riwaya yake – Kidagaa Kimemwozea ambayo niliiandikia tahakiki katika Sunday Nation mwaka wa 2012. Mnamo 2013, mhariri mmoja alinukuliwa akidai kwamba nilikuwa nimemweleza jinsi Prof Walibora alikuwa ‘hodari sana’ katika wizi wa miswada. Taarifa hizo za kusikitisha zilimfikia Prof Walibora – kwa misingi kwamba, katika enzi hii ya utandawazi, taarifa hasa za tetesi husambaa haraka kama moto nyikani wakati wa kiangazi.

Nilijipata babaya – mithili ya panya kwenye kesi ambapo paka ndiye hakimu. Walibora ni msomi ambaye nimekuwa na mlahaka mzuri sana naye tangu mwaka 2003 nilipokutana naye kwa mara ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Nairobi – wakati huo nikihariri habari za Shirika la Habari la Kenya (KBC). Ilisadifu kwamba marehemu Omar Babu – ambaye wakati wa kuzuka kwa porojo hizo alikuwa mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Cologne – Ujerumani, alikuwa rafiki yetu wa karibu – mimi na Walibora.

Marehemu Omar Babu alinitembelea sana – nikawa ninamualika kutoa mihadhara kwa wanafunzi wangu katika Chuo Kikuu cha Chuka ninakofundisha. Kutokana na mtagusano huo, alikuja kufahamu hulka yangu. Kwa hiyo alimpambanulia Prof Walibora kwamba kamwe hadhi na hulka yangu havikuniruhusu kushiriki midahalo hafifu isiyokuwa na msingi kumhusu Prof Walibora kuwapoka watu miswada.

Tetesi kuwa Prof Walibora aliwaperemba watu miswada zinapotazamwa kwa jicho kali, zinakosa mashiko kwa sababu zifuatazo. Kwanza, wanaodai kuibiwa ni akina nani? Pili, mwandishi huyu lazima awe ‘mwizi hodari sana’ wa kuiba miswada zaidi ya 60 (maanake ameandika zaidi ya vitabu 60). Ukisoma kwa makini riwaya ya mtunzi huyu, kuna mtindo unaotawala tungo zake; ‘Siku Njema’ hadi ‘Nasikia Sauti ya Mama’. Kwa kuwa mtindo ni mtu, miswada iliyoibwa haiwezi kuwa na ruwaza ya mtindo fulani unaotawala.

Madai ya wizi wa miswada si jambo geni katika tasnia ya uandishi wa vitabu. Mtu anapotunga kwa kasi inayokiuka ‘uwezo wa binadamu’ wa kawaida, watu bila shaka watamwonea gere. Je, William Shakespeare alitunga tungo zake zote na za viwango vya juu miaka 400 iliyopita? Je, mashairi yaliyopigwa mhuri kuwa ya Muyaka bin Mwinyi yote ni yake au baadhi ni ya Ali Koti?

Prof Walibora amekwisha kufariki. Waliodai kwamba kawaibia miswada walipoteza fursa ya ama kumshtaki mahakamani au kutoa ushahidi wowote mwandishi huyu alipokuwa hai. Kwa hiyo watalazimika kunyamaza milele.

Swali ambalo mwandishi Walibora aliliuliza mara kwa mara ni: “Tunajenga nyumba moja, kwa nini tupiganie fito?” Ni muhimu wakereketwa wote wa Kiswahili watambue kuwa Kiswahili ni bahari kubwa. Sote tunaweza kutoshea katika bahari hiyo – na kila mtu akaogelea kina chake na kwa kasi yake pasi na kuzozana au kuoneana wivu.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

Buriani mwanasafu mwenza Ken Walibora – Bitugi Matundura

NA BITUGI MATUNDURA

KIPINDI kati ya miaka ya 1980 hadi 1990 kilikuwa ni kipindi kigumu mno kwa fasihi ya Kiswahili kwa jumla na hususan utanzu wa riwaya nchini Kenya.

Hali hii ilitokana na ukweli kwamba ni Wakenya wachache mno – waliokuwa wakitunga kazi za fani hizo. Hali hii ilisababisha wahakiki wa fasihi kudai kwamba ‘fasihi ya Kiswahili ilikuwa imedumaa’.

Katika kipindi hicho, Taasisi ya Elimu ya Kenya (Sasa Taasisi ya Ukuzazi wa Mitaala ya Kenyayaani KICD) ilitegemea sana vitabu vya fasihi vilivyotungwa na Watanzania – kutahiniwa katika mifumo yetu ya elimu.

Hata hivyo, katikati ya mwaka 1990, ustawi wa fasihi ya Kiswahili ulipata msukumo na nguvu mpya wakati waandishi wa Kenya walipojitosa ulingoni. Miongoni mwa watunzi hao walikuwa ni Ken Walibora – ambaye riwaya yake – Siku Njema iliteuliwa kutahiniwa kama kitabu cha lazima katika mtihani wa KCSE.

Tangu wakati huo, mwandishi huyu ambaye pia alikuwa msomi mahiri amechapisha tungo nyingi katika mapana na marefu ya tanzu zote za fasihi ya Kiswahili. Katika Afrika ya Mashariki, sikosei kudai kwamba ni waandishi watatu tu ambao wamefanikiwa kandika tungo za Kiswahili zilizotamba katika tanzu zote za fasihi – riwaya, tamthilia, hadithi fupi, ushairi, novela na fasihi ya watoto. Waandishi hao ni pamoja na Ken Walibora, Said Ahmed Mohamed na Kyallo Wadi Wamitila.

Haiyumkiniki kusema kila kitu kumhusu Prof Kennedy Atanasi Waliaula – ambaye jina lake la uandishi lilikuwa ni Ken Walibora kwa sababu alikuwa ni mja aliyekirimiwa vipawa vingi. Maisha yake yalizunguka katika vitovu vikuu vinne – uanahabari, usomi, uandishi na ualimu.

Licha ya kubobea katika nyanja hizi, alifahamika mno katika ulingo wa uandishi – hasa utanzu wa riwaya. Riwaya yake maarufu ni Siku Njema ambayo inafumbata kwa uketo taswira ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa. Riwaya hii inaweza kuainishwa kuwa kazi bulibuli (classical). Imetafsiriwa kwa Kiingereza na Kiitaliano.

Riwaya zake nyingine ni Kidagaa Kimemwozea, Ndoto ya Almasi, Kufa Kuzikana. Tawasifu yake, Nasikia Sauti ya Mama inaonesha hulka na changamoto alizopitia kufikia kilele cha juu kabisa katika uanahabari, usomi na uandishi.

Nilifahamiana na Prof Ken Walibora mnamo 2003 nilipokuwa mhariri wa habari katika Shirika la Habari la Kenya (KBC). Tangu kipindi hicho, tumekuwa tukitagusana katika nyanja za taaluma ya uanahabari, uandishi wa vitabu na usomi. Mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Machi 5, 2020 ambapo nilimuuliza anipe fasiri ya neno ‘anihilate’.

“Prof kwema? Naomba tafsiri ya ‘anihilate’. Nimeangukia kitu hapa,’’ nikamuuliza.

Kauli hii ilitokana na makala aliyokuwa ameyaandika katika Taifa Leo akikejeli watu wanaovuruga Kiswahili kwa kutafsiri vibayavibaya.

Prof Walibora alikuwa mwalimu pia. Mbali na kufundisha katika chuo kikuu cha Wisconsin – Madison Marekani, alikuwa pia mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Riara. Tunaweza kudai kuwa alikuwa mwalimu wa jamii pana kutokana na tungo zake za kifasihi.

Taifa Leo

Kwa takriban miaka minne, tumekuwa tukiandika safu ya Kina cha Fikra katika Gazeti la Taifa Leo. Amewahi pia kupendekeza kwamba wanafunzi wa uzamili na uzamifu katika vyuo vikuu wachangamkie utafiti wa makala katika Jarida la Lugha la Elimu katika gazeti la Taifa Leo.

Prof Walibora kwa hakika alikuwa mmoja wa wanariwaya bora zaidi kuwahi kuibukia Afrika ya Mashariki. Mchango wa marehemu Ken Walibora utaendelea kuacha taathira kubwa katika tasnia ya Kiswahili.

Prof Walibora amekwisha kutangulia mbele za haki. Kinachoridhisha mioyo yetu na kutupa ukakamavu na ujasiri wa kuendelea kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Kiswahili ni kwamba watu sampuli yake hutokea mara mojamoja katika kizazi – na gurudumu la maisha haliwezi kusimama. Hatahitaji kujengewa minara ya kumbukumbu.

Mchango wake katika ulingo wa fasihi ya Kiswahili utadumu daima dawamu. Kawape salamu zangu kina Muyaka Al-Ghassanny, Hassan Mwalimu Mbega, Seithy Chachage, Omar Babu, Katama Mkangi, Jay Mashanga Kitsao, Mumamed Said Abdulla, Ben Rashid Mutobwa, Mbunda Msokile, Shabaan bin Robert, Catherine Kisovi, Mzee Sheikh Ahmad Nabhany, Ibrahim Ngozi miongoni mwa waandishi wengine wengi. Buriani ndugu Walibora.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili Katika Chuo Kikuu cha Chuka.

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Mazingira ya kisiasa na kiuchumi katika riwaya ya ‘Haini’ yake Shafi Adam Shafi

Na BITUGI MATUNDURA

HII ni awamu ya nne ya makala kuhusu riwaya ya ‘Haini’ iliyoandikwa na Shafi Adam Shafi.

Mnamo 1982, mtaalamu Farouk Topan alidai kwamba watunzi muhimu wa riwaya ya Kiswahili walikuwa ni Mohamed Suleiman Mohamed na Euphrase Kezilahabi.

Zaidi ya miongo mitatu, madai ya Topan hayana mashiko tena kwa sababu tangu miaka hiyo tumeshuhudia waandishi wengi wa riwaya ya Kiswahili wakijitokeza na kuandika sana.

Mpaka sasa, tuna wanariwaya wapevu kama akina Shafi Adam Shafi, Mwenda Mbatiah, John Habwe, Kyallo Wamitila, S.A. Mohamed, Ken Walibora, Omar Babu miongoni mwa wengine.

Tulivyokwisha kutaja, riwaya ya ‘Haini’ ni mojawapo wa riwaya za mwandishi Shafi Adam Shafi.

Riwaya za mwandishi huyu: ‘Kasri ya Mwinyi Fuad’ (1978) na Kuli (1979), zinaakisi kwa kiasi kikubwa maudhui ya mapinduzi kisiwani Zanzibar yaliyotokea mnamo mwaka wa 1964.

Mapinduzi haya yaliondolea mbali utawala wa Kisultani na kubadili kwa kiasi kikubwa, mfumo wa uzalishaji mali visiwani humo. ‘Haini’ pia inaakisi tukio la kihistoria; kuuawa kwa Rais wa Zanzibar Abeid Amri Karume mnamo mwaka wa 1972.

Kufuatia mauaji hayo, watu wengi wasiokuwa na hatia walisakwa wakakamatwa na kutiwa gerezani kwa kutuhumiwa kuwa mahaini.

Mwandishi amelitumia tukio hilo kuwa kiini cha kuyachunguza matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya nchi za Kiafrika baada ya uhuru. Maudhui yanayotawala katika kazi nyingi za waandishi wa Zanzibar kipindi hicho – mathalan Mohamed Suleimani Mohamed, Said Ahmed Mohamed ni ya kimapinduzi. Katika mapinduzi haya, utawala wa Sultani uling’olewa mamlakani na Waafrika walio wengi wakashika hatamu za uongozi.

Zanzibar ikawa Jamhuri chini ya uongozi wa Amri Abeid Karume. Katika ‘Haini’, mwandishi anamulika historia hii ya Zanzibar kutoka mbali anaposawiri sifa za Chopra, mwendesha mashtaka wa serikali. Anasema: “Jinsi alivyokuwa bingwa wa kazi yake hiyo, aliaminiwa sana na mahasimu wote watatu waliokitawala kisiwa cha Zanzibar.”

Wakati wa Elizabeth wa pili aliaminiwa sana na watawala wa Kiingereza na utiifu wake kwa watawala hao ukawa ni wa kupigiwa mfano. Sultani na wafuasi wake walipofanikiwa kuundoa utawala wa Elizabeth wa pili na kuweka utawala wao, nao pia wakawa na imani kubwa na Chopra wakamfanya kuwa ndiye mshauri wao mkuu wa mambo ya kisheria […] wakwezi na wakulima walipokuja juu wakamtimua Sultani na wafuasi wake kwa mapanga na mashoka na Kigogo akashika usukani wa kuiongoza nchi, Kigogo hakumwona mwanasheria aliyekuwa na kipawa kumshinda Chopra, akambandika cheo cha mwanasheria mkuu wa serikali.” (uk 230 – 231) Amri Abeid Karume aliuawa mnamo mwaka 1972.

Taifa la Zanzibar likashuhudia kilele cha ukiukaji wa haki za kibinadamu katika kile watawala walichokiita ‘usakaji wa mahaini’, wauaji wa Karume. Watu wengi waliteswa, wengi wakauwawa na wengi walifungwa gerezani kwa shutuma za kushiriki mauaji ya Karume.

Taifa likawa kama gereza. Hili ndilo tukio ambalo mwandishi analimulika katika ‘Haini’.

Riwaya ya ‘Haini’ inatufungulia milango ya mazingira yaliyojaa hofu na wasiwasi. Raia wanasakwa, kukamatwa na kutiwa gerezani kwa kosa ambalo wengi wao hawalifahamu.

Sehemu kubwa ya riwaya hii, inasimulia matukio ya gerezani ambamo Hamza pamoja na watuhumiwa wengine wamerundikwa, kuteswa, kuthakilishwa na kutendewa unyama wa kila aina. Hamza na wenzake hawana budi kuumia huku wakiwa hawajui hatima yao.

Wanateswa ili wakiri kwamba walihusika. Baadhi yao hawana budi kufanya hivyo ili kuokoa roho zao. Mkadam, Haramia, Mpakani, Sumbu, Marzuku, Vingosho, Zarkani, Pwacha na Kuchi wanakiri kuhusika kwao. Wanatungiwa visa na ushahidi wa uwongo wa kuwahusisha wale wengine.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Mgogoro wa ushairi wa Kiswahili ulivyomtia matatani mtaalamu Mugyabuso Mulokozi

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO 2017, nilifanya utafiti kuhusu ‘mgogoro wa ushairi wa Kiswahili’ uliozuka mnamo miaka ya 1960.

Mgogoro huo miongoni mwa wataalamu wa Kiswahili ulichochewa na masuala mawili. Kwanza, utata kuhusu maana ya ushairi kwa jumla. Iliki, maana ya ushairi wa Kiswahili. Mgogoro huo ulizua mapote mawili yaliyokinzana. Pote la kwanza lilikuwa na wanamapokeo au wahafidhina.

Pote la pili lilikuwa la wanamapinduzi au wanamabadiliko. Baadhi ya wanamadiliko walikuwa ni pamoja na kina Jared Angira, Euphrase Kezilahabi, Ebrahim Hussein, Crispin Haule, Mugyabuso Mulokozi, Fikeni Senkoro, Alamin Mazrui na Kulikoyela Kahigi – miongoni mwa wengine walioanza kuandika ‘mashairi ya kisasa’.

Wanamapokeo walikuwa ni pamoja na Kaluta Amri Abedi, Abdilatif Abdalla, Shihabbuddin Chiraghdin, Hassan Mwalimu Mbega, Saadan Kandoro, Jumanne Mayoka, Mathias Mnyampala miongoni mwa wengine. Utafiti wangu ulilenga kuutathmini mgogoro huo miaka hamsini baadaye. Je, ulififia? Ungalipo? Hatima yake ilikuwa ni ipi? Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika Jarida la Mwanga wa Lugha Juzuu 1 Na. 2 ; la Idara ya Kiswahili na Lugha nyingine za Kiafrika, Chuo Kikuu cha Moi. Nilidhani kwamba mgogoro huo ulikuwa wa kiakademia tu. Hata hivyo, nilishangazwa wiki iliyopita kwamba mgogoro huo ulivuka mipaka ya kiakademia na kuwaathiri vibaya baadhi ya wanamapinduzi.

Mmoja wa wanamapinduzi aliyeumia kwa sababu ya msimamo aliouchukua kuhusiana na mgogoro huo ni Prof Mugyabuso Mulinzi Mulokozi. Kwenye makala yake: ‘Pambazuko la Taaluma ya Fasihi ya Kiswahili Afrika Mashariki: 1968 -1980’ yaliyochapishwa katika Lugha Na Fasihi : Essays In Honour And Memory of Elena Bertoncini Zubkova (2019). Prof Mulokozi anadai kwamba, kwa sababu ya msimamo wao (yeye na wanausasa wenzake), njama zilifanywa kumzuia asiajiriwe katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili) au Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kuhitimu masomo yake mwaka 1975, licha kwamba alikuwa na sifa zote za kitaaluma zilizohitajika.

Wengine waliojipata matatani kutokana na mgogoro huo ni Kulikoyela Kahigi na Zubeida Tumbo Masabo. Mulokozi anasema kwamba njama hizo zilifanikiwa kwa muda tu. Alikuja kuajiriwa na TUKI mnamo 1979. Mhakiki Elena Bertoncini – Zubkova, ambaye kwa muda mrefu alifundisha katika Chuo Kikuu cha Napoli, nchini Italia alifariki 2018. Kazi ya mtaalamu huyu iliyoacha taathira kubwa mno katika taaluma ni Outline of Swahili Literature: Prose, Fiction and Drama (1989). Kazi hii ambayo aliiandika kwa ushirikiano na Prof S.A. Mohamed, Prof K.W. Wamitila na Dkt Mikhail Gromov ndiyo kazi ya pekee inayojaribu kutoa taswira kamili ya fasihi ya Kiswahili na waandishi wa fasihi hiyo tangu miaka ya 1960.

Mwangwi wa ‘mgogoro wa ushairi wa Kiswahili’ bado ungalipo. Utafiti wangu ulibainisha kwamba licha kwamba mgogoro huo haujabainisha au kujitokeza wazi miaka hamsini baadaye, utaendelea kuathiri kwa kipindi kirefu jinsi au namna utanzu wa ushairi wa Kiswahili unavyotazamwa na wahakiki. Diwani za mashairi zinazotungwa hivi sasa zinajumuisha mashairi yanayofuata arudhi ya yale yasiyofuata kanuni za utunzi wa mashairi alizopendekeza Kaluta Amri Abedi katika Sheria ya Kutunga Mashairi Na Diwani ya Amri (1954).

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka. Yeye pia ni mfasiri wa Moses Series (Oxford University Press).

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Athari ya sera ya udhibiti kwa waandishi wa fasihi ulimwenguni – Sehemu ya tano

Na BITUGI MATUNDURA

HII ni awamu ya tano ya msururu wa makala yangu kuhusu athari ya sera ya udhibiti kwa waandishi wa fasihi.

Mawazo haya yanatokana na makala niliyowasilisha katika kongamano ya kimataifa la Chama cha Kiswahili cha Afrika ya Madharihi – CHAKAMA katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara mnamo Novemba.

Kutokana na makala yaliyopita, imebainika kuwa motifu ya masaibu yaliyomkumba Ngugi wa Thiong’o inajitokeza pia tunapomchunguza mwandishi Abdilatif Abdalla.

Mshairi huyu anayefahamika sana kwa diwani yake ya ushairi ijulikanayo kama ‘Sauti ya Dhiki’ (Oxford University Press, 1973) aliyoitunga akiwa kifungoni tangu Machi 1969 mpaka Machi 1972.

Abdilatif anasema: “Ingawa hapa si mahali pa kueleza sababu ya mimi kufungwa, naona ni dharura niitaje kwa vile ambavyo pengine nisingeyatunga mashairi haya kama nisingekuwa nimefungwa. Sababu ya kufungwa ni kwamba nilipatikana na “hatia ya kuchochea watu kuipindua Serikali ya Kenya kwa kutumia silaha” baada ya kuandika, kuchapisha na kuisambaza kwenye miji kadha wa kadha ya Jimbo la Pwani la Kenya karatasi niliyoiita Kenya: Twendapi?”

Mwandishi mwingine ambaye tajriba zake zinakurubiana na za Ngugi wa Thiong’o na Abdilatif Abdalla ni Katama Mkangi. Mkangi alikuwa mkosoaji mkubwa sana wa serikali ya Moi. Alikuwa ni mmoja wa watu waliopigania sana demokrasia nchini Kenya mnamo miaka ya 1980.

Kutokana na misimamo na maoni yake, Mkangi alikamatwa mnamo Machi 5, 1986 kwa madai ya kuwa mwanachama wa kundi la Mwakenya, na kuwekwa kizuizini kwa miaka miwili. Wasomi wengine waliokamatwa pamoja naye kipindi hicho ni pamoja na Profesa Isaiah Ngotho Kariuki na Maina wa Kinyatti.

Baada ya kuondoka kizuizini, Mkangi alikaa kwa muda mrefu bila ajira kwa sababu hangeweza kurudi katika chuo kikuu kufundisha kwa sababu ya kubandikwa ‘mwasi’.

Akionesha muumano na mfanano wa kimawazo na kiitikadi uliopo baina ya Ngugi wa Thiong’o na Abdilatif Abdalla Kresse (2016) anasema: Hiki ni kiungo kati ya Abdalla rafiki na mshirika wake Ngugi wa Thiong’o, ambaye mara nyingi anamwona Abadalla kama kielelezo chema katika ukosoaji wa kisiasa na mwandishi mahiri wa fasihi ya Kiafrika, asiyetetereka katika kuuliza maswali muhimu ambayo yanapaswa kujibiwa.

Wawili hao kwa hakika wanaweza kulinganishwa kwa misingi ya kujitolea kwao kimaadili na katika mapambano ya kisiasa katika nchi yao, na imani yao kwamba nyenzo yoyote ile ya kujieleza kimaandishi – ikiwemo karatasi/makala ni njia ya kutumika katika mapambano hayo.

Wote waliendeleza juhudi hizi wakiwa wangali uhamishoni London (na kwingineko), katika kupinga serikali ya Moi. Tunakubaliana na maoni haya kwa misingi kwamba kuna uwezekano mkubwa wa waandishi walioandika katika kipindi sawa na mazingira sawa kuwa na mwitiko sawa kuihusu jamii yao.

Kitovu kinachowaunganisha Ngugi wa Thiong’o na Abdilatif Abdalla mbali na itikadi yao ya kuegemea Umaksi ni utawala wa Moi ambao watunzi hawa hawakukubaliana nao.

Mhakiki, Mwenda Mbatiah anasema: Ngugi na Mkangi ni waandishi maarufu ambao kazi zao husomwa kote Afrika Mashariki na kwingineko. Watunzi hawa pia ni wasomi, ingawa ni wataalamu katika nyanja tofauti.

Ngugi ni mwanafasihi, mhakiki na mwandishi huku Mkangi akiwa ni mwanasosholojia. Hata hivyo, watunzi hawa huandika kazi zinazosawiri dhiki za umma, ndoto na matamanio yao.

Muhimu zaidi ni kwamba, watunzi hawa wana itikadi sawa ya kisiasa ambayo inaegemea sana Umaksi. Wote wawili walikamatwa na kuwekwa kizuizini. Ingawa waliachiliwa huru hatimaye, hawakuruhusiwa kurejea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Tajiriba za waandishi kuhusiana na sera ya kudhibiti fasihi ulimwenguni – 4

Na BITUGI MATUNDURA

HII ni awamu ya nne ya makala kuhusu sera ya udhibiti wa maandishi kwa waandishi wa fasihi ulimwenguni.

Juma lililopita, nilitaja kwamba Ngugi wa Thiong’o ni mmoja wa watunzi waliofarakana na mamlaka na vyombo vyao vya dola kutokana na sera hii.

Aidha niliangazia maoni ya wakili Issa Shivji wa Tanzania kuhusu jukumu la waandishi, wasomi na wanaharakati katika jamii. Shivji anadai kwamba waandishi wana nafasi muhimu katika mapambano ya kiukombozi. Hata hivyo, isichukuliwe kwamba Ngugi na Euphrase Kezilahabi ndio watunzi pekee ambao kazi zao zimewahi kukabiliwa na udhibiti.

Tuna waandishi wengine kama vile David Maillu ambaye kazi zake pendwa kama vile Unfit for Human Consuption, After 4.30, na My Dear Bottle zilikabiliwa na udhibiti. Nje ya Afrika ya Mashariki, tuna mwandishi Sir Ahmed Salman Rushdie ambaye aliandika Satanic Versers.

Kazi hii ambayo imetumia kiunzi cha maisha ya Mtume Muhammad (SAW) ilipochapishwa nchini Uingereza mnamo 1988, Waislamu wengi walimshutumu Salman Rushdie kwa madai ya kukufuru. Mnamo 1989, kiongozi wa Iran Ayatollah Ruhollah Khomeini alitoa amri ya fatwa kuwataka Waislamu wamuue Rushie.

Mauaji kadha, majaribio kadha ya mauaji na mashambulizi kwa mabomu vilitokea kwa minajili ya kuipinga riwaya hiyo. Serikali ya Iran iliunga mkono fatwa hiyo hadi 1998 wakati serikali iliyoshika hatamu ya rais Mohammad Khatam iliposema kwamba haikuwa inaunga mkono tena suala la kumuua Rushdie.

Masaibu yaliyomkabili Salman Rushdie yanatokana na udhibiti wa maandishi unaotekelezwa na asasi za kidini. Mfasiri wa kazi hiyo kwa lugha ya Kijapani aliuawa kwa kudungwa kisu mjini Tokyo, huku mchapishaji wake nchini Norway akiuawa kwa kupigwa risasi mjini Oslo.

Aidha, mfasiri wa kazi hiyo kwa lugha ya Kiitaliano vilevile aliuawa kwa kudungwa kisu na umati wa watu waliokuwa wakitaka awaeleza alikokuwa amejificha Salman Rushdie.

Nchini Bangladesh, mwandishi wa kike Taslima Nasrin – mshairi na mwanariwaya alilazimika kwenda mafichoni mnamo 1993 baada ya kuaibishwa na kudhulumiwa hadharani (alipigwa na kuvuliwa nguo) na kuandamwa kwa kuandikia masuala ‘yasiyoruhusiwa’ kama vile ‘ubakaji katika ndoa’.

Riwaya yake, Lajja (Aibu) ilipigwa marufuku. Nchi nyingine ulimwenguni ambazo zimewahi kuwafunga waandishi gerezani ni China, Burma, Korea Kusini, Syria na Vietnam. Mwandishi na mshairi wa Malawi, Jack Mapanje alifungwa gerezani mnamo 1987 kwa kuandika mkusanyo wa mashairi Of Chameleons and Gods ambao uliikosoa serikali ya Hastings Banda.

Nchini Nigeria, mwandishi maarufu Ken Sawo Wiwa aliyeandika A Month and a Day: A Detention Diary aliuawa na wanajeshi katika utawala wa Sani Abacha kwa kutetea watu wa jamii yake ya Ogoni dhidi ya dhuluma za kupunjwa na kampuni za kimataifa zilizokuwa zinajishughulisha na uchimbuaji wa mafuta.

Mwandishi mwingine kutoka nchi hiyo, Wole Soyinka alikimbilia uhamishoni nchini Marekani mnamo 1994.

Tajiriba ya Salman Rushdie kufuatia kuchapishwa kwa riwaya yake ya Satanic Verses na waandishi wengine ambao nimekwisha kuwataja zinaakisi mwengo wa masaibu yaliyowahi kumkumba Ngugi wa Thiong’o chini wa utawala wa serikali za Jomo Kenyatta na Daniel Arap Moi.

Ngugi wa Thiong’o anaandika: “Ninafahamishwa, kwa mfano, kwamba mnamo Desemba 1977 watu wawili wenye mamlaka makuu serikalini waliabiri ndege hadi Mombasa na kutaka wakutane kwa dharura na Jomo Kenyatta. Kila mmoja alikuwa na nakala ya vitabu vyangu, Petals of Bloood na Ngahika Ndeenda. Ombi lao lilipokubaliwa, walimsomea Jomo Kenyatta, bila shaka nje ya muktadha, vifungu na sentensi na maneno waliyofasiri kwamba nilikuwa na njama ya kutekeleza maovu.”

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Aina za udhibiti wa maandishi ya kazi za fasihi unaoathiri uandishi na waandishi

Na BITUGI MATUNDURA

JUMA lililopita niliangazia suala la udhibiti wa maandishi (censorship).

Hii ni sifa ya kuyadhibiti maandishi ya kifasihi inayohusishwa na tawala za kimabavu ambazo zinaubana uhuru wa kimaandishi na kusoma. Katika historia ya maendeleo ya fasihi, kuna vitabu vingi ambavyo vimewahi kupigwa marufuku kutokana na sababu za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kimaadili na au kidini.

Riwaya ya kiusasaleo ya Salman Rushdie ya ‘The Satanic Verses’ ilipigwa marufuku kwa sababu za kidini.

Riwaya ya Rosa Mistika (E. Kezilahabi) ilipigwa marufuku nchini Tanzania katika miaka ya 1970s pamoja na Jando na Unyago (J. Mamuya) na novela za D. Maillu kwa sababu zilizodaiwa kuwa za kimaadili.

Kuna mbinu mbalimbali zinazotumiwa na mamlaka na vyombo vya dola katika kutekeleza sera ya udhibiti wa maandishi.

Katika makala haya, tunaangazia takriban aina mbalimbali za udhibiti. Kuzuia ni mbinu itumiwayo ili maandishi yasichapishwe. Kuzuia husitisha maandishi ambayo yanaonekana au kuaminika hayafai kufikia umma au hadhira ya wasomaji. Aidha serikali au kundi fulani linalotetea au kudumisha maslahi fulani hutekeleza aina ya pili ya udhibiti. Aina hii ya udhibiti wa maandishi mara nyingi huhusu afisi au asasi fulani ya serikali, kundi la kidini huwa na mamlaka lenye kumiliki vyombo vya habari au mashirika ya uchapishaji.

Vilevile, kuna mbinu ya kuharibu: Aina hii ya udhibiti huhusu kuharibu vitabu na maandishi mengine kabla au baada ya kuchapishwa ili kuzuia vitabu au maandishi hayo kufikia umma au kuchapishwa upya. Hili hutekelezwa kwa kuteketeza maandishi au kuchanachana kazi husika. Mbinu hii iliwahi kutumiwa na serikali ya Kenya dhidi ya Kampuni ya Uchapishaji ya East African Educational Publishers iliyokuwa inataka kutoa kitabu cha Ngugi wa Thiong’o kiitwacho ‘Matigari ma Njiruungi’ (1987).

Usimbaji (Encryption) pia ni mtindo wa udhibiti ambapo maandishi hudhamiriwa kufikia hadhira au kundi fulani la wasomaji wachache, hasa kwa kubadilisha lugha na kufanya maandishi kuwa magumu kusomeka au kuchochea kimakusudi hamu ya kutosoma kwa kundi fulani nje ya lile linalolengwa na maandishi husika. Kwa mfano, vitabu vingi vya zamani na majarida kuhusu taaluma ya utabibu viliandikwa kwa Kilatini. Ingawa hili lilifanywa kwa sababu kadha, mojawapo ya maelezo ya kimsingi kuhusu hali hiyo ilikuwa ni kuyafanya maandishi hayo yasiwafikie watu wengi, bali kuhakikisha kwamba ni watu wachache waliochukuliwa kuwa wa hadhi na viwango fulani vya elimu ndio wangeweza kusoma maandishi hayo.

Katika uhawilishaji (omission), sehemu au maelezo fulani katika kazi fulani ya kifasihi ambayo yanafikiriwa kuwa hayafai huondolewa kabla ya kazi fulani kuchapishwa. Mbinu hii mara nyingi huweza kuathiri matini asilia. Mbinu hii huruhusu tu kuondolewa kwa kiasi fulani cha matini kwa msingi kwamba kuondoa sehemu kubwa ya matini kunaweza kufanya kazi au maandishi kutoweza kusomeka kwa sababu ya kuvurugika.

Halikadhalika utakasaji ni aina ya udhibiti inayohusu kuacha nje au ‘kutakasa’ matini si tu kwa kuondoa, bali pia kubadilisha maneno, sentensi au sehemu, aya au hata sura za matini iliyokwisha kuchapishwa. Hivi majuzi, kitabu kinachoitwa ‘Blood Ties’ kilichoandikwa na mwandishi wa Afrika Kusini, Zimkitha Mlanzeli kiliondolewa kwenye maduka ya Text Book Centre jijini Nairobi mnamo Septemba, 2019 kwa madai kwamba kilitumia lugha ‘chafu’.

Udhibiti wa kiubunifu huhusisha uandishi upya matini na wadhibiti wenyewe na kubadilisha matini kabisa kiasi kwamba wadhibiti wanaweza kuwa waandishi wenza.

Kuna pia udhibiti wa kutoa kwa orodha ya kupiga marufuku.

KAULI YA MATUNDURA: Ni kweli Nyerere alikuwa tapeli wa tafsiri za tungo za William Shakespeare?

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA ulimwengu wa taaluma, aghalabu huibuka mtu mmoja katika kizazi kizima ambaye mchango wake huwashangaza na kuwafanya watu wengi waajabie michango ya watu hao.

Nchini Uingereza, watu bado wanaajabia upeo wa tungo za mwanatamthilia William Shakespeare ambaye taathira ya tamthilia zake ingali inaonekana takriban mpaka sasa zaidi ya miaka 400 tangu alipoishi, na kutunga na kufa. Shakespeare yadaiwa alitunga tamthilia 36.

Huku Afrika Mashariki, wataalamu wa Kiswahili wanadadisi iwapo Muyaka bin Hajji Al- Ghassaniy ndiye aliyetunga mashairi yote yanayodaiwa kuwa yake.

Je, mbona ni Muyaka pekee aliyetukuka ilihali kulikuwa na malenga wengi wakiwemo kina Ali Koti ambao walitunga katika mazingira sawa na Muyaka?

Kuna uwezekano kwamba baadhi ya mashairi yaliyokwisha kupigwa muhuri kuwa kayatunga Muyaka ni ya akina Ali Koti? Mnamo mwaka 2000, msomi Prof Tigiti Sengo wa Tanzania aliibuka na madai ya kushangaza kuhusu Hayati Rais Julius Kambarage Nyerere na tafsiri ya tungo za William Shakespeare kwa lugha ya Kiswahili.

Katika mojawapo ya mihadhara yake minne ya umma katika Chuo Kikuu cha Egerton, Prof Sengo aliishangaza hadhira yake kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa tapeli na mwongo kuhusu tafsiri ya tungo hizo. Alidai kwamba tungo ‘za Shakespeare’ ambazo zimewahi kuzua mtafaruku na mjadala kuhusu mtunzi wake halisi – Mabepari wa Venisi, Juliasi Kaizari na Makbeth – ambazo yadaiwa zilitafsiriwa na Julius Nyerere – kwa hakika zilikuwa tafsiri zilizofanywa na Abdillahi Nassir.

Kwa mujibu wa Sengo, ‘wizi’ huu ulitekelezwa kwa kupanga na kula njama na kampuni ya uchapishaji ya Oxford University Press. Chambacho Tigiti Sengo, baada ya kulipachika jina la Julius Nyerere kimakusudi kuwa yeye ndiye mtafsiri, waliweka jina la mfasiri halisi; Abdilahi Nassir, kuwa ndiye mhariri.

Sengo alidai kwamba mambo hayakukomea hapo. Alidai kuwa baadhi ya kazi zilizoandikwa katika Kiswahili na kuaminika kuwa za Mwalimu Nyerere pia ni za ‘wizi’.

Kwa hiyo, Prof Sengo alisema kwamba sifa alizopewa Mwalimu Nyerere ambaye ndiye Mwanzilishi wa Taifa la Tanzania kuhusu ufanisi huo zilikuwa si za haki.

Anadai kwamba mwelekeo wa Nyerere kuhusu Kiswahili haukuwa na ukereketwa wa haja na kwamba alichofanya Nyerere ni kukidaka Kiswahili kwa manufaa yake kisiasa.

Sengo alidai kwamba kuna Watanzania ambao walikikumbatia na kukikuza Kiswahili na pindi kilipotia fora, wanasiasa kama Nyerere ‘wakakinyakua’ na kudai kwamba wao ndio watetezi sugu wa lugha hiyo.

Ni kwa nini suala la Nyerere na ‘wizi’ wa tafsiri za Shakespeare ni muhimu? Kwanza, kuna halaiki kubwa ya watu kote duniani waliokwisha kuzisoma tafsiri za Shakespeare kwa Kiswahili zinazodaiwa kuwa za Nyerere.

Wasomaji hao wamekwisha kumwonea fahari Nyerere kwa kazi hiyo. Sijui iwapo wachapishaji wa tungo hizo wanaweza kutoa taswira na habari kamili kuhusu suala hili.

Kuna uwezekano pia kwamba wachapishaji walifanya hivyo kimakusudi kama mbinu ya kisiasa ya kuimarisha mauzo ya vitabu vyao.

Prof Sengo si msomi hivi hivi na hivyo basi madai yake hayawezi kupuuzwa. Lakini pia ni muhimu kukumbuka kwamba, Sengo alipaswa kutoa madai hayo Mwalimu Nyerere akiwa angali hai ili aweze kujitetea. Prof Sengo alizaliwa Morogoro mnamo mwaka 1945.

Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Amendika kazi nyingi zikiwemo Ndimi Zetu, Hisi Zetu, History of Kiswahili Poetry (kwa ushirikiano na Mugyabuso Mulokozi, Fasihi Simulizi ya Mtanzania miongoni mwa tungo nyingine.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Yakini, mikondo ya makuzi ya kamusi za Kiswahili Afrika Mashariki inatia moyo

Na BITUGI MATUNDURA

WAKATI wowote kuanzia sasa, toleo la 3 la Kamusi ya Karne ya 21 (Longhorn Publishers ) litatoka kwenye matbaa.

Nilikuwa mmoja wa wahariri waliotwikwa jukumu la kushiriki katika mchakato wa kuandaa toleo la kwanza la kamusi hiyo iliyotolewa kwa mara ya kwanza mnamo 2010.

Aidha hivi majuzi nilipata fursa nyingine ya kuipitia kamusi hiyo na kushuhudia jinsi ilivyokua na itaendelea kukua kadri miaka inavyosonga.

Kwenye ripoti yangu kuhusu kamusi hii, nilitanguliza shukrani zangu kwa kampuni ya Longhorn Publishers PLC kwa kunipa fursa ya kuipitia Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3).

Kuna historia ndefu baina yangu na mradi wa kuiandaa kamusi hii tangu 2009 jinsi ambavyo nimekwisha kutaja.

Meneja wa Vitabu vya Sekondari, Bw James Mwilaria alinitwika majukumu manne mazito kuhusiana na kazi hii ya Toleo la 3; nayo ni: Kuhariri na kuiboresha Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3), kupunguza idadi ya kurasa kwa baina ya kurasa 80 – 100, kuongeza vidahizo vyovyote vipya ambavyo vinaweza kuwa havikuingizwa katika Toleo la 3, Kutoa maoni yoyote ya matini za nyongeza ambazo zinaambatana na sheria za leksikografia. Nilifahamishwa kwamba madhumuni makuu yalikuwa ni kupunguza kurasa na ‘kubana matini’ ili iwe faafu zaidi. Aidha nilitwikwa jukumu la kutoa mapendekezo mengine muhimu ya kuiboresha kamusi.

Kwa hiyo, ripoti hii inaangazia majukumu niliyofanikiwa kuyatekeleza na vipi na yale ambayo sikufanikiwa kuyatekeleza na kwa nini.

Katika kutekeleza jukumu la kwanza, ilinilazimu nipitie kila kidahizo na namna kilivyotomeshwa (kilivyotolewa maelezo ya kiufafanuzi kwenye kamusi).

Niliongeza ufafanuzi pale ambapo nilipohisi kwamba dhana fulani au neno fulani la kimsingi linalochangia kueleweka kwa kidahizo limeachwa nje. Kadhalika, nilifanya marekebisho ya tahajia au vinginevyo pale ambapo ninahisi kwamba haikuwa sawa.

Katika kutekeleza jukumu la pili la kupunguza idadi ya kurasa kwa baina ya kurasa 80 – 100 nilihisi kwamba Kamusi ya Karne ya 21 tangu awali ilikuwa na mambo yaliyoifanya kuwa na upekee ikilinganishwa na kamusi nyingine zilizoitangulia au zilizoifuatia.

Kamusi ya Karne ya 21 ina nyongeza ya taarifa ambazo kimsingi zinapaswa kuwa katika kamusi za taaluma au nyanja fulani mahususi. Kadri taarifa hizi zilivyozidi kuongezwa ili kuipa kamusi hii upekee wa namna fulani, ndivyo kurasa zake zilivyozidi kuongezeka.

Kwa hiyo, nilipendekeza kwamba kuipunguza kamusi hii kwa kurasa takriban 80 – 100 ina maana kuwa taarifa hizo ziondolewe.

Kurasa hizi haziwezi kupunguzwa kwa kuondoa baadhi ya vidahizo au maelezo ya vidahizo hivyo. Kufanya hivyo kutaifanya Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3) kuwa dhaifu zaidi.

Isitoshe, makuzi na uimarikaji wa kamusi huonekana kupitia kwa kuongeza maneno mapya au yale yaliyosahaulika kila inapotolewa upya – wala si kuondoa taarifa muhimu.

Aidha, nyongeza ya taarifa fulani inatokana na misukumo ya soko ambapo watumiaji wa kamusi hutaka taarifa fulani ziingizwe kwenye toleo jipya la kamusi kama hii. Kwa hiyo, ikiwa lengo hili ni lazima litekelezwe kwenye Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3).

Aidha niliingiza na kutomesha maneno machache ya kimsingi ambayo nilihisi ni muhimu.

Vinginevyo, nilihitimisha kwamba kazi nzuri sana ilifanywa katika kuyaingiza na kuyafafanua maneno ya Kiswahili katika Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3). Ninasubiri kwa hamu na ghamu kuchapishwa kwa toleo hilo la tatu la kamusi hiyo.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Athari ya lugha za kigeni kwa Kiswahili na jinsi zilivyochangia kupanua leksikoni

Na BITUGI MATUNDURA

MOJAWAPO ya vipengee muhimu ambavyo mwalimu na mwanafunzi wa isimujamii anahitajika kujua ni historia ya Kiswahili.

Katika kuangazia historia ya lugha hii muhimu ya Afrika Mashariki na Kati, mwalimu na mwanafunzi wake hawawezi kukwepa suala la jinsi Kiswahili kimeathiri na kuathiriwa na lugha nyingine.

Katika makala haya, ninaangazia jinsi wageni kutoka nje ya bara Afrika walivyochangia katika kuathiri Kiswahili.

Athari ambazo hujitokeza wazi kwenye mada kama hii angalau huwa ni ya kileksikoni au msamiati.

Miongoni mwa wageni wa awali kabisa kuwasili katika pwani ya Afrika Mashariki walikuwa ni pamoja na Waajemi, Wafarsi, Wamisri,Wachina na Waarabu.

Utafiti wa akiolojia au historia chimbo umeonyesha kwamba vyungu vya Wachina, maandishi ya Wamisri na hata athari za wageni wengine kwa wakazi wa Pwani bado zingalipo.

Baadhi ya wageni hawa walipiga kambi na kuishi pwani ya Afrika Mashariki mapema mwaka 900 Baada Kristo.

Wageni hao ambao walihamia pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu wanazozijua wao wenyewe waliishi katika eneo hilo na kufunga ndoa na wenyeji wa sehemu hizo.

Wanavyosema Chiraghddin Shihabuddin na Mathaias Mnyampala katika Historia ya Kiswahili, wahamiaji hao walichangia katika kupanuka na kukua kwa miji ya mwambao wa Washwahili kama vile Pate, Lamu, Mombasa, Kilwa, Vumba, Pemba na Zanzibar.

Wajukuu wa Waarabu wengi pamoja na Waajemi chambilecho Abdalla Khalid walisahau lugha zao baada ya muda mrefu na kuanza kutumia Kiswahili.

Hali ambapo lugha za baadhi ya wahamiaji hao ‘ilimezwa’ na lugha ya wenyeji wa mwambao kimsingi ilitokana na uchache wao.

Hata hivyo, Kiajemi au Washirazi kutoka Irani walipokeza Kiswahili maneno mengi ambayo yanapatikana katika lugha hii hadi leo. Himaya ya Shirazi na makazi yao kuanzia Kisiwa cha Funzi kusini mwa pwani ya Kenya hadi Tanga na Bagamoyo nchini Tanzania ingali inatambulika ingawa si kwa njia ya kinaga ubaga hivi leo. Washirazi walitofautishwa na wakazi wengine wenyeji wa pwani kama vile Wadigo na Wasegeju kwa sababu ya jinsi walivyoishi maisha yao kijumla. Walitegemea uvuvi na kutumia lahaja ya kipekee ya Kiswahili iliyojulikana kama Chichifundi.

Washirazi waliathiri leksikoni ya Kiswahili katika mianda mbalimbali. Mianda na nyanja hizo ni pamoja na utawala ambapo tunapata maneno kama vile jumbe, diwani, amir, waziri, serikali, shehe, akida na Sultan.

Katika mwanda wa biashara, Washirazi walichangia maneno kama vile tajir na bakshish ambayo yameswahilishwa na kuwa tajiri na bakshishi. Kwenye mwanda wa uchukuzi wa vyombo vya majini tunapata maneno kama vile bandali, nanga, tezi na kadhalika.

Katika taaluma ya mimea, Washirazi walichangia maneno kama vile mbangi, mbilingani, mdengu, mgulabi, mharagwe, mpopo, mtambuu, mnansi, mdalasini na derabi. Kuhusu vyakula, walichangia maneno kama birinzi, borohoa, gubiti, sambusa na siki.

Msamiati wa mavazi, mapambo na rangi waliochangia ni pamoja na lasi, seredani, utaji, urujuani, zari,zumaridi na rangi. Aidha, katika taaluma ya ujenzi walichangia maneno kama vile dari, boma, ghala, roshani. Maneno mengine ni pamoja na bahati, beluwa, usafidi, huruma, hoihoi, uhanidhi, ushenzi, barabara miongoni mwa mengine.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

Baruapepe: mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Mbinu za upanuzi wa leksikoni katika lugha ya Kiswahili na changamoto zake

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA kipindi cha majuma mawili yaliyopita, makala yangu yamejikita katika uwanja wa leksikolojia.

Leksikolojia ni taaluma ambayo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uchanganuzi wa msamiati wa lugha pamoja na maana zake.

Uwanja huu vilevile huitwa elimumsamiati. Istilahi ni msamiati katika nyanja maalum za lugha kama vile sheria, tiba, teknohama, biolojia, fizikia, kemia na kadhalika.

Mpaka baina ya msamiati na istilahi ni mwembamba mno kwa msingi kwamba, istilahi inapobuniwa katika lugha fulani na ikawa inakubaliwa na kutumiwa, inakuwa ni msamiati wa ile lugha.

Kwa hiyo, istilahi ni msamiati wa lugha katika uwanja maalum.

Msururu wa makala haya ulichochewa na juhudi za mwandishi na mwanahabari, Bw Geoffrey Mung’ou aliyependekeza istilahi ‘runulishi’ kwa maana ya smartphone. Bw Mung’ou alitumia mchakato wa uhulutishaji wa maneno mawili ‘rununu’ na ‘tarakilishi’ ili kubuni ‘runulishi’.

Mkabala huu umewahi kutumiwa na wataalamu wengine kama vile Prof Rocha Chimerah kubuni maneno kama ‘tarakilishi’. (Hata hivyo, mimi nimekwisha kupendekeza kwamba mtaalamu huyu aifanyie marekebisho istilahi yake ili iwe ‘rununulishi’. Nimekwisha kutoa sababu za kumtaka Bw Mung’ou airekebishe istilahi yake iwe ‘rununulishi’ badala ya ‘runulishi’.

Kiingereza nilivyokwisha kutaja katika makala ya awali ni lugha inayopanua leksikoni yake kwa kuegemea Kigiriki, Kilatini na lugha nyingine kuu ulimwenguni. Lugha hizi zinategemea unominishaji zaidi kuliko uambishaji – unaoonekana zaidi katika lugha za Kibantu.

Nadharia ya Mzee Sheikh Ahmad Nabhany kuhusu upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili ni kwamba lahaja za Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika – hususan lugha za Kibantu ni kanzi muhimu ya kuanzia pale tunapotafuta dhana au neno la kuiita dhana ngeni.

Pale ambapo dhana hiyo inakosa kabisa, Mzee Nabhany anapendekeza kwamba neno au istilahi ibuniwe kwa kuangalia mambo matatu; Kwanza ni muhimu kuangalia umbo la kitu.

Pili, zingatia utenda kazi wa kitu. Tatu, ni muhimu kuzingatia sauti au mlio wa kitu.

Kwa hiyo, tukiirejelea istilahi ya ‘runulishi’ aliyopendekeza Bw Mung’ou, tunagundua kwamba inajikita katika nadharia ya Mzee Nabhany – ambapo muundaji amezingatia utendakazi wa kifaa.

Kwanza, jinsi tulivyokwisha kusema, ‘smartphone’ ni simu (rununu na vilevile inaweza kutenda kazi ileile ya kompyuta au tarakilishi. Kwa mantiki hii, Bw Mung’ou amehulutisha maneno ‘rununu + tarakilishi’ ili kupata ‘runulishi’. Ili kuiepusha istilahi hii (runulishi) na ugiligili na ugumu wa kuitamka, ninapendekeza kwamba iwe ‘rununulishi’.

Je, ‘smart –Tv’ tutaiitaje? Tatizo hili linaturudisha kwenye miundo tofauti ya lugha za Kiingereza na Kiswahili hasa katika suala zima la upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili.

Jambo la kutia moyo ni kwamba, katika ufinyu wake wa kutumia neno moja kurejelea aina mbalimbali za dhana ambazo zimekurubiana, Kiswahili huenda kisihitaji sana au kwa dharura istilahi ya ‘Smart TV’ au hata ‘smartphone’ kwa msingi kwamba dhana televisheni na rununu/ au simu zinaeleweka vizuri pale zinapotumiwa na wasemaji wa Kiswahili. Jambo lililo muhimu ni kwamba, midahalo ya aina hii inakuza Kiswahili kinadharia hata pale ambapo suluhisho la kiutendaji huenda lisipatikane.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Tathmini ya ufaafu wa istilahi ‘runulishi’ kwa maana ya Smartphone – Sehemu ya 2

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA awamu ya kwanza ya makala yangu juma lililopita, niliangazia mdahalo wa wataalamu kuhusu istilahi ‘runulishi’ iliyopendekezwa na mwandishi na mhariri Geoffrey Mung’ou ili itumike kwa maana ya ‘smartphone’.

Nilidai kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia na taaluma nyingine zinahitaji istilahi mahsusi. Nilidai pia kwamba juhudi za watu binafsi kama vile Geoffrey Mung’ou katika kubuni istilahi hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono.

Hata hivyo, nilitahadharisha kwamba shughuli ya kubuni istilahi ni nzito na inayofaa kufuata mchakato au mkondo fulani unaokubalika ili lugha iweze kuwa na istilahi faafu na kuepushwa kuvurugwa.

Baadhi ya wanaleksikoni wapevu nchini Kenya ambao wamekibunia Kiswahili istilahi zinazokubalika ni Mzee Sheikh Nabhany, Prof Rocha Mzungu Chimerah na Prof Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

Vyombo vya habari kama vile Shirika la Habari la Taifa la Kenya (KBC) na Taifa Leo pia vimetoa mchango wa kupigiwa mfano katika kubuni na kusambaza istilahi za nyanja maalum kama vile tiba, sheria na teknohama.

Baada ya kuichunguza kwa makini istilahi ‘runulishi’ aliyoibuni au kuipendekeza Bw Mung’ou, nilihisi kwamba ilikuwa ni istilahi nzuri ambayo ilipaswa kupigwa msasa, ikaboreshwa na labda kuingizwa katika matumizi ya kila siku ya Kiswahili. Kwa hiyo, mimi nilipendekeza kwamba Bw Mung’ou aibadilishe istilahi yake iwe ‘rununulishi’ badala ya ‘runulishi’. Sababu zangu ni pamoja na zifuatazo: Kinadharia, istilahi ‘runulishi’ inatokana na uhulutishaji au uunganishaji wa maneno ‘rununu’ na ‘tarakilishi’.

Kiunzi

Fikra za mwandishi Mung’ou hivyo basi zilijikita kwenye kiunzi alichokiegemea Prof Rocha Chimerah katika kubuni istilahi ‘tarakilishi (tarakimu + akili + mashine). Mung’ou alifafanua kwamba umbo na utendakazi wa ‘smartphone’ unakurubiana mno na tarakilishi. Kwamba ‘smartphone’ ina uwezo wa kufanya na kutekeleza mambo ambayo tarakilishi au kompyuta inaweza kufanya. Kwa hiyo, mumo kwa mumo ni simu na tena ni tarakilishi.

Tatizo la istilahi ya Bw Mung’ou (runulishi) ni kwamba lugha ya Kiingereza inategemea sana unominishaji kuzalisha au kupanua leksikoni yake huku lugha nyingi za Kibantu (Kiswahili kikiwemo) zikiwa ni lugha ambishibainishi (agglutinative languages).

Aidha, Kiingereza kimeegemea mno Kigiriki na Kilatini na lugha nyingine kuu ulimwenguni kupanua leksikoni yake.

Mojawapo wa sifa za istilahi nzuri kinadharia ni kwamba sharti istilahi hiyo iweze kuzashisha istilahi nyingine kwa urahisi.

Pili, Kiingereza kina mgao mpana zaidi wa maneno yanayoelezea dhana ile ile moja huku Kiswahili kikiwa na mgao finyu wa msamiati ambao huzieleza zile dhana za Kiingereza kijumla. Kwa mfano katika Kiingereza tuna dhana kama vile: mansion, castle, hut, cottage, house na kadhalika ambazo ni aina mbalimbali za nyuma.

Hata hivyo, mtu anaporejelea aina hizo za nyumba katika Kiswahili kwa neno ‘nyumba’, bado ataeleweka anachokizungumzia.

Vivyo hivyo, dhana ‘simu’/ ‘rununu’ inapotajwa, mawazo ya simu huelekezwa moja kwa moja kwenye simu jinsi tunavyoifahamu pasi na kujali iwapo ni ‘smartphone’ au aina yoyote ile ya simu.

Kwa hiyo kwa maoni yangu, ingawa juhudi za kutafuta neno la Kiswahili la ‘smartphone’ hazipaswi kupingwa, itakuwa vigumu sana kuwadara wasemaji wa Kiswahili waitumie istilahi hiyo kwa sababu hizo ambazo nimekwisha kuzitaja.

Vilevile ni muhimu kukumbuka kwamba lugha haipati hasara pale inapokuwa na leksikoni au maneno yasiyotumika. Katika makala yangu juma lijalo, nitaangazia zaidi changamoto za upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wajadili ufaafu wa ‘runulishi’ kwa maana ya smartphone

Na BITUGI MATUNDURA

WIKI iliyopita, mwandishi na mwanahabari Geoffrey Mung’ou alizua mjadala wa kuchangamsha kuhusu upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili kwa kuibunia lugha hii istilahi mpya.

“ Jina ‘smartphone’ lina dhana ya uwezo wa kiutendakazi sawa na tarakilishi; rununu yenyewe hutumiwa kutekelezea majukumu yote yanayotekelezwa na tarakilishi,” akasema Bw Mungou.

Aliongeza: “Ninajua kwamba yapo majina mengine yaliyobuniwa kwa maana ya ‘smartphone’ ila neno ‘rununulishi’ linaziba sawasawa pengo na mapungufu yote kuhusu tafsiri faafu ya ‘smartphone’.”

Katika makala haya, ninayahakiki maoni ya Bw Mung’ou kuwili. Kwanza, ninayatathmini kinadharia. Pili, nitayapima kwenye mizani ya kiutekelezaji. Maoni ya Bw Mung’ou yalinielekeza katika ukuzaji na upanuzi wa leksikoni ya lugha – hususan Kiswahili. Lugha huhitaji istilahi au msamiati pale inapolazimika kushughulikia mawasiliano katika nyanja maalum ambazo hapo awali ilikuwa haiushughulikii. Baadhi ya nyanja maalum ni pamoja na tiba, sheria, kilimo, fasihi, isimu , teknolojia ya habari na mawasiliano (teknohama) n.k.

Kwa hiyo, dhana ya ‘smartphone’ imejikita katika uwanja wa teknohama. Wakati mwingine, lugha huhitaji kubuniwa leksikoni inapotwikwa jukumu la mawasiliano hasa katika nchi ambazo hapo awali zilikuwa zinatumia lugha za kigeni.

Kwa bahati mbaya, lugha za madola makubwa kama vile, Kijerumani, Kiingereza, Kichina, Kijapani n.k ndizo zinatumika sana aghalabu kuelezea maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa hiyo, ili Kiswahili kiingie katika usemezano wa maendeleo hayo na lugha nyingine za kiulimwengu, lazima kikabiliane na matatizo ya upanuzi wa leksikoni zao.

Ikumbukwe kwamba shughuli ya kubuni istilahi ni nzito – kwa sababu kila istilahi inayobuniwa lazima iwe na mantiki ili iweze kukubalika. Shughuli hii ama inafanywa na watu binafsi, mashirika au vyombo vya habari. Nchini Kenya, baadhi ya wanaleksikolojia wapevu ambao wametoa mchango muhimu katika uwanja huu ni pamoja na Mzee Ahmad Sheikh Nabhany, Prof Rocha Mzungu Chimerah na Kyallo Wadi Wamitila.

Istilahi ‘runulishi’ kwa maana ya ‘smartphone’ Iliyopendekezwa na mwandishi Geoffrey Mung’ou iliibua mwengo wa istilahi ‘runinga’ ambayo ilibuniwa na Mzee Sheikh Ahmad Nabhany kwa maana ya ‘television’ au ‘televisheni’.

Istilahi ‘runinga’ imetokana na uhulutishaji au uunganishaji wa maneno matatu; (1) ‘rununu’ (habari/taarifa), (2) ‘yakuenga’ (kutazama) (3) ‘kwa maninga’ (kwa macho). Kwa Waswahili, neno ‘rununu’ lina maana ya habari zinazotoka mbali na mijini.

Kwa hiyo, chambacho Mzee Sheikh Nabhany, habari hizi huletwa na jinni kulingana na imani ya Waswahili. Kwa hiyo, mtaalamu huyu anadai kwamba taarifa hizo kutoka mbali ni habari (‘rununu’) za kuonwa kwa macho.

Habari za kuonwa

Kwa hiyo, Mzee Nabhany anasema kwamba ‘televisheni’ ni kifaa kinachosambaza habari za kuonwa kwa macho.

Kwa hiyo, alihulutisha maneno haya: rununu + maninga. Katika kubuni istilahi ‘runulishi’, ninafikiri kwamba Bw Mung’ou alikuwa anafuata mchakato aliouanzisha Mzee Sheikh Nabhaby.

Nadharia ya Mzee Nabhany katika kubuni istilahi mpya za Kiswahili ni kuwa, kwanza sharti umbo la kifaa au dhana inayotafutiwa au kubuniwa istilahi izingatiwe’ Pili, sharti utendakazi au uamilifu (function) wa kifaa au dhana utiliwe maanani.

Jambo la mwisho ni kuwa sharti mwanaleksikoni azingatie sauti au mlio wa kifaa cha dhana husika. Baada ya kuikagua istilahi ‘runulishi’ aliyoipendekeza Bw Mung’ou, nilihisi kwamba ingekuwa bora zaidi iwapo angeibadilisha istihahi hiyo iwe ‘rununulishi.

Sehemu ya pili ya makala haya juma lijalo itaangazia sababu za kupendelea ‘rununulishi’ badala ya ‘runulishi’.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Pata mwao wa mchakato wa kubuni na kusambaza istilahi mpya za Kiswahili

Na BITUGI MATUNDURA

MAKALA yangu ya majuma mawili yaliyopita yaliangazia suala la istilahi ‘mzungumzishi’.

Nilikwisha kuangalia istilahi hiyo iliyobuniwa na Seneta Agnes Zani kinadharia na kiutendaji.

Nimekwisha kudai kwamba neno hilo halifai kutumiwa katika nafasi ya ‘spika’.

Mpaka sasa Kenya haina chombo mahususi cha kiserikali ambacho kinaweza kutwikwa jukumu la kuunda, kusawazisha na kusambaza istilahi na msamiati wa Kiswahili.

Hii ni tofauti na ilivyo nchini Tanzania ambako kuna Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) na Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA).

Vile vile, nimekwisha kudai kwamba juhudi za vyombo vya habari na watu binafsi (kama vile Dkt Agnes Zani) wanaojifungata masombo kukibunia Kiswahili istilahi kwa minajili ya matumizi ya nyanja maalumu hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono.

Katika makala ya leo, ninapiga hatua na kutathmini hatari iliyopo Kenya kukosa chombo au asasi maalum ya kuunda au kubuni istilahi, kuzisawazisha istilahi mpya na hatimaye kuzisambaza.

Mchakato wa jumla unaopaswa kufuatwa katika uundaji wa istilahi au msamiati ni kwamba; kwanza, lazima kuwe na haja maalum inayochochea istilahi kuhitajika. Kiswahili kwa mfano kinahitaji kutumiwa katika nyanja maalum kama vile teknolojia ya habari na mawasiliano, bungeni, tiba na mahakamani. Nyanja hizi zinahitaji istilahi maalum. Kwa hiyo, lazima dhana inayohitaji kubuniwa istilahi izuke kwanza.

Pili, baada ya istilahi kubuniwa, inapaswa kujadiliwa na jopo la wataalamu wa leksikoni kubaini iwapo inafaa au haifai. Ikiwa istilahi husika inafaa, chombo au wanajopo wanaohusika huiidhinisha ili ianze kutumiwa rasmi.

Wataalamu au asasi husika inaporidhishwa na istilahi mpya, huichapisha na kusambazwa kwa umma kupitia vyombo vya habari, taasisi za elimu na kadhalika.

Utekelezaji wa hatua ya usambazaji wa istilahi mpya ndiyo hatua ya mwisho inayonuiwa kuipiga muhuri istilahi hiyo kwamba ndiyo inafaa zaidi.

Utundu wa lugha ni kwamba kamwe wasemaji wake hawawezi kushinikizwa kutumia istilahi ambazo wataalamu wamekwisha zibuni na hata zikaidhinishwa kuwa ndizo zinazofaa kutumiwa.

Mifano ambayo inaweza kushadidia kauli hii ni istilahi ‘televisheni/runinga’ (television), ‘kompyuta/tarakilishi’ (computer), ‘kaunti/gatuzi’ (county), chuo kikuu/ndaki/zutafindaki’ (universiry), ‘utandawazi/utandaridhi/ugolobishaji’ (globalisation) na kadhalika.

Kutokana na jozi za istilahi au maneno haya, ni wazi kwamba kuna zile istilahi au maneno yaliyokubaliwa zaidi miongoni mwa wasemaji wa Kiswahili yanapolinganishwa na mengine.

Wasemaji wa lugha wana usemi mkubwa katika mchakato wauundaji, usawazishaji na usambazaji wa istilahi.

Wao ndio wanaoamua ni istilahi au maneno gani yatumiwe lini, wapi na akina nani – hata pale ambapo wataalamu wamekwisha kubuni istilahi nakuipiga muhuri kwamba ndiyo inayofaa zaidi kutumiwa kuelezea dhana fulani.

Baadhi ya wanaleksikoni tajika katika Kiswahili ni pamoja na Mzee Ahmad Sheikh Nabhany wa Mombasa, Prof Rocha Mzungu Chimerah (Chuo Kikuu cha Pwani) na Prof Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Tathmini ya ufaafu wa ‘mzungumzishi’ kwa vigezo vya kinadharia ya Kiisimu

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA makala yangu juma lililopita nilidai kwamba pendekezo la istilahi ‘mzungumzishi’ iliyoubuniwa na seneta maalum – Dkt Agnes Zani haikufaa kwa maana ya ‘spika’.

Hata hivyo, nilimpa kongole Dkt Zani kwa kuthubutu kuisukuma mbele nadharia ya upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili ya kuikuza lugha hii ‘mumo kwa mumo’.

Katika makala ya leo, ninajadili ni kwa nini istilahi ‘mzungumzishi’ haifai kwa tathmini ya kinadharia. Nadharia ya kupanua msamiati wa Kiswahili ‘mumo kwa mumo’ ilipigiwa upatu sana na hayati Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa.

Alidai kwamba kabla ya kukimbilia kutohoa au kukopa maneno kutoka kwenye lugha za kigeni, ni muhimu tuchakurechakure kanzi ya maneno katika lahaja za Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu. Ikiwa tutakosa kabisa neno linaloweza kutumiwa kurejelea dhana ngeni, basi neno libuniwe kwa kuchunguza sifa za dhana ile mpya.

Mimi ninafikiri kwamba mawazo ya kiutendaji ya Dkt Zani yalikuwa yameulenga mkondo huu – ingawa hayakuwa na msingi wa kujikita na ushawishi wa kutosha.

Hatua ya kwanza katika kubuni msamiati au istilahi ni kuwepo haja ya msamiati au istilahi hiyo.

Hapakuwa na haja ya istilahi ‘mzungumzishi’ kwa sababu tayari tuna neno ‘spika’, hili limezoeleka na wasemaji wa Kiswahili na hata kutomeshwa kwenye kamusi.

Profesa Kibuka Kiingi (Uganda) alibuni nadharia ya PEGITOSCA. Anapendekeza kwamba istilahi inayobuniwa ni sharti itimize vigezo vifuatavyo vya PEGITOSCA: Precision (Udhahiri), Economy (Iktisadi), Generativity (Uzalishi), Internationality (Umataifa), Transparency (uwazi), anti-Obsenity (Isomatusi), Systematicity (Umfumo), Consistency (Uangavu) na Acceptability (ukubalifu).

Kimsingi, kila istilahi inayobuniwa sharti iwe dhahiri, fupi na isiyokanganya, iweze kuzaa istilahi nyingine kwa njia ya kunyambuliwa, ikubalike kimataifa, iwe angavu (bila ugiligili), ikubalike kwa urahisi na isisheheni fahiwa ya matusi.

Katika Kiswahili kwa mfano, tuna maneno ‘runinga’ na televisheni ambayo yanatumiwa kama visawe. Ingawa yote mawili yamekubaliwa, ‘televisheni’ ina umataifa zaidi kuliko ‘runinga’.

Aidha, tuna ‘kompyuta’ na ‘tarakilishi’. Ingawa ‘kompyuta’ ni istilahi yenye umataifa zaidi kuliko ‘tarakilishi’, la pili (tarakilishi) linatimiza kiwango cha uzalishi zaidi hivi kwamba linaweza kunyambuliwa na kuunda istilahi nyingi.

Kwa mfano ‘tarakilishia’ (compute for), ‘tarakilishiana’ (compute for one another), ‘nitarakilishie’ (compute for me), tarakilishatarakilisha (compute repeatedly) na kadhalika.

Umataifa

Je, istilahi ‘mzungumzishi’ inatimiza baadhi ya vigezo hivi? Dhana ‘spika’ ina umataifa zaidi kuliko ‘mzungumzishi’.

Kadhalika ‘mzungumzishi’ inakiuka kigezo cha ‘iktisadi’ kwa misingi kuwa neno lenyewe linahitaji kani au nguvu nyingi mno kulitamka.

Maseneta, wakiongozwa na Bw James Orengo walishindwa kabisa kulitamka neno ‘mzungumzishi’ na hiyo ni ishara ya wazi kwamba limekiuka kigezo cha kinadharia cha ‘ikitisadi’ katika lugha.

Vilevile ‘mzungumzishi’ haina uangavu kwa misingi kuwa inazua fahiwa ya kufanyiza na kulazimisha. Kutokana na kitenzi ‘zungumza’ tunaweza kupata maneno kama ‘mzungumziwa’, ‘mzungumzaji’, ‘mzungumzishi’ na kadhalika – nako kumfanya mtu azungumze – yaani ‘kumzungumzisha’ kunaleta dhana ya kutumia nguvu.

 

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Ni kweli neno ‘mzungumzishi’ halifai kwa maana ya‘spika’ lakini seneta Zani ana hoja

Na BITUGI MATUNDURA

JUZI JUZI seneta maalumu, Dkt Agnes Zani, alimtaja Spika wa Bunge la Seneti Bw Ken Lusaka kuwa ‘mzungumzishi’ kwa maana ya spika ambao ni msamiati uliozoeleka.

Maseneta wengine, wakiongozwa na James Orengo walipinga vikali istilahi hiyo kwa misingi kwamba katika historia ya midahalo bungeni, dhana hiyo kamwe haijawahi kusikika.

Dkt Agnes Zani ni ‘Mswahili’ kindakindaki na binti ya walimu na waandishi mahashumu – Bwana Zachariah M. Zani na Teresa K. Zani.

Kadhalika, Dkt Zani ni msomi wa sosholojia ambaye alipata shahada yake ya uzamifu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Oxford mbali na kuwa mhadhiri wa vyuo vikuu kabla ya kujitoma katika siasa.

Kutokana na rai alizotoa, ninaweza kudai kwamba Dkt Zani alinivutia kuwili.

Kwanza, alionesha raghba ya kukitetea Kiswahili liwe liwalo. Pili, mkabala wake wa kutumia neno ‘mzungumzishi’ badala ya ‘spika’ ulinikumbusha mkabala wa mwanaleksikoni maarufu wa Kiswahili, marehemu Mzee Ahmad Sheikh Nabhany wa Mombasa wa ukuzaji wa Kiswahili mumo kwa mumo.

Nadharia ya Mzee Nabhany kuhusu upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili ni kwamba; kabla ya kukopa na au kutohoa neno au msamiati kutoka lugha za kigeni, ni muhimu tupekuepekue katika lahaja za Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu iwapo kuna neno au dhana inayoweza kutumiwa kuelezea neno au dhana tunayotaka kuikopa.

Nadharia ya Mzee Nabhany inalenga kuepuka ukopaji kiholela kwani kwa kuruhusu hili Kiswahili kinaweza kupoteza upekee wake.

Kwa hivyo, katika kusisitiza kwamba neno ‘mzungumzishi’ litumiwe badala ya ‘spika’, Dkt Zani ana hoja nzito ambayo inapaswa kuungwa mkono.

Lakini je, Kiswahili kina ufukara wa msamiati unaoweza kuchukua nafasi za ‘mzungumzishi’ na ‘spika’? Neno ‘spika’ limetoholewa kutokana na neno la Kiingereza Speaker.

Maana ya kileksika ya spika ni: Mtu anayeongoza majadiliano bungeni; mwenyekiti wa bunge au baraza la wawakilishi.

Msamiati mwingine wa Kiswahili sanifu unaoleta fahiwa inayokaribiana na ‘uspika’ ni ‘longa’ au ‘sogoa’.

Kwa hiyo, seneta Zani hangejipata matatani sana iwapo angependekeza kwamba spika aitwe ‘mlongaji’ au ‘sogoa’ badala ya ‘mzungumzishi’.

Hata hivyo, mdahalo wa seneta Zani na maseneta wengine unatutosa kwenye suala la upanuzi wa leksikoni katika lugha na njia zinazotumiwa na wanaleksikolojia katika kupanua msamiati wa lugha fulani.

Ikumbukwe kwamba lugha hukua kila uchao na hupanuka ili kukidhi haja za maswailiano ya kawaida na katika njanya maalumu.

Lugha hulazimika kupanua msamiati wake pale inapohitajika kushughulikia mawasiliano katika nyanja mpya ambazo awali zilikuwa hazishughulikiwi kwa lugha hiyo.

Hivi sasa, nyanja zinazozishinikiza lugha kupanua mawanda ya kimawasiliano ni maendeleo ya kasi katika sayansi na teknolojia.

Baadhi ya mikabala inayotumiwa katika kupanua leksikoni za lugha mbalimbali ulimwenguni ni pamoja na ‘ukopaji’ au utohozi, uhulutishaji, kubuni maneno mapya kwa kuangalia maumbile na utendakazi wa dhana au kifaa kinachohitaji neno au istilahi, kutumia vifupisho miongoni mwa njia nyingine.

Kwa hivyo, juhudi za Dkt Zani katika kupanua leksikoni ya Kiswahili hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono. Ingawa hakutia fora katika mdahalo wa kutetea msamiati wake kilio chake na ari yake ya kukitetea Kiswahili ilionekana bayana.

KAULI YA MATUNDURA: Matumizi ya Kiswahili na wageni si kigezo faafu cha kupima thamani ya lugha hiyo

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA gazeti la Daily Nation toleo la Julai 11, 2019, kulikuwa na habari kwamba mwanamuziki, mtunzi wa nyimbo na mwigizaji wa Marekani Beyonce Giselle Knowles-Carter alitumia maneno ya lugha ya Kiswahili katika wimbo wake mpya.

Maneno ya Kiswahili yanayosikika katika wimbo huo ni “Uishi kwa muda mrefu mfalme.”

Tukio hili aghalabu lilizua msisimko wa namna fulani miongoni mwa wakereketwa wa Kiswahili Afrika ya Mashariki.

Wakati huo huo, mtaalamu Prof Aldin Kai Mtembei alizua mdahalo katika ukumbi wa WhatsApp wa wanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) alipotuma kauli iliyojaa kejeli na tashtiti kuhusu aina moja ya mvinyo uliotengenezwa nchini ujerumani. “Jinsi Kiswahili kinavyochanja mbuga: Bia imetengenezwa Ujerumani, inauzwa China – na katika melezo yake kuna pia Kiswahili.

Mojawapo ya maelezo katika bia hiyo – Original German Black Beer – Oettinger Schwarz, kuna onyo lililoandikwa kwa Kiswahili – “Unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kudhuru afya yako. Usiuzie yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18. Kunywa pombe kiungwana”.

Mtaalamu Melkiory Fursa aliuliza: Kwa nini walitumia lugha ya Kiswahili? Ni kwa kuwa kinapendwa (Ujerumani)? Wanywaji ni Waswahili na si wazungu? Waswahili hupenda kulewa? Au lugha ya Kiswahili ina mvuto kibiashara?”

Mtaalamu huyu alihisi kwamba Isimujamii ilihitajika mno ili kujibu maswali aliyoyauliza.

Matukio haya mawili – muziki wa Beyonce wenye maneno ya Kiswahili na pombe ya Ujerumani yenye onyo lililoandikwa kwa Kiswahili yanapaswa kutuchochea kutafakari upya kuhusu uzalendo wetu katika kuzikumbatia na kuzienzi lugha zetu za Afrika – hususan Kiswahili.

Mimi nilihisi kwamba hatua ya bia ya Ujerumani kusheheni maandishi ya Kiswahili ni mbinu ya kupanua soko la pombe hiyo.

Upokeaji

Bara la Afrika linapokea na kutumia bidhaa nyingi kutoka nje ikilinganishwa na bidhaa kutoka Afrika zinazouzwa katika maeneo mengine ulimwenguni. Ninahisi kwamba hakuna cha kusherehekea kwamba Kiswahili kimetambuliwa na wazungu. Mbona sisi tusizitambue na kuzienzi lugha zetu – wazungu wawepo au wasiwepo?

Je, wazungu ndio kigezo cha utambuzi wa lugha na tamaduni zetu? Je, vikadiria viwango (rating scale) vya ufanisi wa lugha za Waafrika ni utambuzi wa lugha zenyewe na wazungu?

Nimewahi kudai kwamba ikiwa kuna raslimali kuu ambayo Afrika ya Mashariki inamiliki – basi ni Kiswahili. Kiswahili kinaweza kubidhaishwa na kuuzwa katika mataifa ya kigeni nje ya bara hili kwa namna inayoweza kuziletea nchi za Afrika ya Mashariki mapato makubwa.

Tusidanganyike kwamba Wazungu wanakichangamkia Kiswahili kwa sababu wanakipenda. Mumo kwa mumo katika kukichangamkia Kiswahili kuna maslahi ya kibinafsi.

Kampuni za kimataifa kama vile Microsoft zinapotumia Kiswahili katika mtandao wa intaneti, maslahi yao ya kibiashara ndiyo yamepewa kipaumbele.

Inasadifu tu kwamba katika kuafikia maslahi hayo, wanakitandawazisha Kiswahili bila wao kujua.

Juhudi hizi hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono. Kilichoko ni Waafrika kujifungata masombo kujikomboa kutokana na kasumba za kikoloni ambazo zilichangia mno katika kuwafanya Waafrika kuzionea aibu lugha na tamaduni zao.

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Kila binadamu ana upekee ambao hauwezi kujazwa na mtu mwingine

Na BITUGI MATUNDURA

NILIPOKUWA mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Maseno mnamo miaka ya 1990, mwalimu wangu wa somo la falsafa – Prof Crispin Iteyo aliniambia kauli muhimu ambayo uzito wake unaendelea kunishughulisha na kunifikirisha kadri miaka inavyozidi kusonga na umri wangu kuporomoshwa na wimbi la wakati.

Mwalimu Iteyo alisema kwamba, “Tupende tusipende, lazima tujishughulishe na masuala ya kifalsafa.”

Kadhalika, Prof Iteyo alitugutua kwamba maisha ni mzunguko; ambapo vizazi hupokezana mwenge wa maisha. Pindi mtu anapozaliwa, moyo wake huwa kana kwamba umetiwa majira mithili ya saa.

Hatima ya maisha ya binadamu aijuaye ni Mungu – ila binadamu yule aghalabu huwa ana uwezo wa kuamua mkondo ambao maisha yake yatachukua kutokana na matendo yake ulimwenguni au maamuzi atakayoyafanya. Vivyo hivyo hatuwezi kutilia upofu dhana ya ujaala katika maisha.

Mwalimu na rafiki yangu – Bw Crispine Isaboke ambaye anafundisha somo la falsafa katika Chuo Kikuu cha Chuka ana mtazamo kwamba binadamu hana uwezo wa kudhibiti mkondo ambao maisha yake huchukua.

Anadai kwamba ikiwa mtu fulani ameamua kusafiri kwa ndege kwenda Amerika, uamuzi huo si wake bali ni ujaala.

Ilikuwa imepangwa hivyo.

Mtu huyo akighairi na kuvunja safari, hatua hiyo ilikuwa imepangwa hivyo.

Mawazo ya Bw Isaboke yanaturudisha palepale kwenye udhanaishi (existentialism).

Mwandishi wa fasihi ya Kiswahili ambaye ameegemeza takribani tungo zake zote katika mkabala huu wa udhanaishi ni Euphrase Kezilahabi.

Tatizo la maisha ya mwanadamu linamshughulisha mno Euphrase Kezilahabi katika maandishi yake yote ya kubuni: ‘Kichomi’, ‘Rosa Mistika’, ‘Kichwamaji’, ‘Dunia Uwanja wa Fujo’, ‘Nagona’, ‘Mzingile’ na ‘Dhifa’.

Kezilahabi anamwangalia mwanadamu katika viwango na awamu mbili.

Kwanza, anayahakiki maisha ya mwanadamu katika kiwango cha ubinafsi – yaani mtu binafsi na pili, amamhakiki mwanadamu huyohuyo katika mtagusano wake na watu wengine – yaani jamii.

Kiunzi kikuu kinachofungamanisha tungo za Kezilahabi ni kwamba binadamu huyu – awe katika kiwango cha ubinafsi au jamii pana, anajaribu kutafuta uhuru, furaha, kuusaka ukweli au hata kudadisidadisi iwapo Mungu yupo.

Kwa ujumla, binadamu anajaribu kujiuliza – maisha ni kitu gani? Licha kwamba maswali haya yote ni ya kifalsafa, mtazamo wangu ni kwamba kila binadamu ana nafasi yake muhimu katika dunia hii.

Kwamba kila binadamu amakirimiwa upekee wa namna fulani ambao ni vigumu kuuiga au kuurudufu kwa njia moja au nyingine.

Juha Kalulu

Mfano nitakaoutoa kushadidia upekee wa kila binadamu ni kuhusu mchoraji wa vibonzo vya Juha Kalulu – Edward Gicheri Gitau ambaye aliaga dunia mwaka 2016.

Tangu afariki, hakuna mtu mwingine ambaye amejitokeza kuendeleza kipawa chake cha kuchora vibonzo vya Juha Kalulu kwa mtindo na namna sawa alivyokuwa anachora Mzee Gitau.

Vivyo hivyo, mwandishi mcheshi Wahome Mutahi alipofariki, hakuna mtu aliyeweza kuandika makala ya The Whispers kwa namna na mtindo ule ule alioutumia mwandishi asilia.

Kwa hiyo, sikosei kudai kwamba kila binadamu katika ulimwengu huu anaweza kumtihilishwa na sura mahsusi kwenye jitabu liitwalo maisha.

Unapozaliwa, kuna kitu fulani na upekee wa namna fulani unaouletwa katika dunia hii, na unapofariki, upekee ule hauwezi kufidiwa na mtu yeyote yule.

Kwa hiyo, kila binadamu ana nafasi muhimu katika ulimwengu huu – na anapaswa kutambuliwa na kupewa nafasi ya kuicheza ngoma yake kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

 

Bitugi Matundura ni mtunzi wa riwaya ya ‘Kivuli cha Sakawa’

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Maneno ‘benki’na ‘banki’ hayakufaa kuibua mitanziko yoyote, yote mamoja

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO 2010, Kampuni ya Uchapishaji wa Vitabu – Longhorn Publishers Limited, Nairobi – ilinishirikisha katika mradi wa uandaaji wa Kamusi ya Karne ya 21.

Shughuli hii ilinikutanisha na wanaleksikografia wapevu wa Kiswahili Afrika ya Mashariki kama vile Maprofesa James Salehe Mdee na John Gongwe Kiango.

Kadhalika nilikutana na mwanaistilahi Makih Hassan kutoka Baraza La Kiswahili la Tanzania; BAKITA.

Shughuli hiyo ilinifundisha mambo mengi kuhusu mchakato wa uundaji wa kamusi; hasa uteuzi, uingizaji na utomeshaji wa vidahizo katika kamusi ya kawaida.

Hata hivyo, funzo kuu nililopata ambalo linahusiana na kauli ya makala yangu hivi leo ni kwamba lugha yoyote iwayo ni kwamba uundaji wa kamusi ni shughuli ambayo haina kikomo.

Kwa nini? Kwa sababu lugha ni kitu kilicho hai, kinakua na kuwa kila uchao, kinabadilika na wakati mwingine kufa.

Hii ina maana kwamba, ikiwa Kamusi ya Karne ya 21 imekwenda kwenye matbaa (press) leo, wanaleksikografia huanza kuihariri tena kesho yake ili kubaini iwapo kuna neno lililoachwa nje au kuna neno jipya lililozuka ambalo linapaswa kuingizwa na kutomeshwa kamusini.

Kimsingi, uandaaji wa kamusi ni shughuli ambayo haiwezi kutamatika na kwamba haiyumkiniki kamusi moja kukusanya maneno yote katika lugha yoyote iwayo.

Hulka ya lugha ni kwamba, hata neno ambalo halikufaulu kuingizwa katika kamusi mwaka huu huenda likaingizwa katika siku au miaka ya baadaye kwa sababu watumiaji wa lugha ndio wenye usemi mkubwa na wanahusa na wadau wakuu katika masuala yoyote yanayohusu lugha yao.

Matamshi na tahajia

Mkabala huu unanirejesha kwenye mdahalo wa hivi majuzi kuhusu msamiati ‘Banki’ na ‘Benki’.

Noti za sarafu ya Kenya zimeandikwa ‘Banki Kuu ya Kenya’ ilhali zile za Tanzania zimeandikwa ‘Benki Kuu ya Kenya’.

Kwa hiyo, watu ambao hawana ujuzi wa lugha walitanzika kuhusu hali hii. Neno Banki/Benki limetoholewa kutokana na neno la Kiingereza ‘Bank’ ambalo linatamkwa /benk/.

Kwa hiyo, Tanzania inapoandika kwenye sarafu yake ‘Benki Kuu ya Tanzania’ bila shaka imezingatia matamshi zaidi na kupuuzilia mbali hijai au maendeleo.

Aidha, Kenya inapoandika kwenye noti zake: ‘Banki Kuu ya Kenya’ imezingatia zaidi hijai (mwendelezo) kuliko matamshi.

Kamusi yoyote nzuri itayatomesha maneno haya kuwa ni visawe.

Mdahalo kuhusu ‘Banki’ nchini Kenya na ‘Benki’ nchini Tanzania ulipozuka, mimi sikuona sababu yoyote ya kujadili suala hilo.

Hata hivyo, mdahalo huo ungekuwa wenye mashiko mno ikiwa baadhi ya noti nchingi Kenya zingekuwa zimeandikwa ‘Banki’ na ‘Benki’ au za Tanzania kuandikwa ‘Benki’ na ‘Banki’ kwa sawia.

Hii ina maana kwamba, ikiwa nchi imeamua kutumia mkabala wa hijai, haiwezi kutumia mkabala wa matamshi kwa wakati mmoja.

Vivyo hivyo, halitakuwa kosa kwa Kenya kuandika ‘Benki’ kwenye noti zake miaka ijayo – wala haitakuwa kosa kwa Tanzania kutumia ‘Banki’ kwenye noti zake.

Ikumbukwe kwamba ingawa Kiswahili ni lugha sambazi Afrika ya Mashariki, hatuwezi kuufumbia macho ukweli kwamba kuna ‘Kiswahili cha Kenya’ na ‘Kiswahili cha Tanzania’ kwa sababu ya suala linalojulikana kama ‘lahaja za kijiografia’ (georaphical dialects).

Maelezo aliyotoa Gavana wa Benki Kuu, Dkt Patrick Njoroge kwamba Kenya inatumia neno ‘Banki’ kwa sababu ati lilipendekezwa na Tom Mboya si ya kitaalamu.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Nilivyomrai Prof Senkoro kuitoa upya riwaya yake ya ukombozi ya Mzalendo iliyochapishwa na Shungwaya 1977

Na BITUGI MATUNDURA

HIVI majuzi, katika pekuapekua ya maktaba yangu, nilipata riwaya ya Mzalendo (Shungwaya Publishers, 1977) iliyoandikwa na Fikeni Senkoro wa Tanzania.

Prof Fikeni Senkoro ni mmoja wa waandishi na wahakiki wa fasihi ya Kiswahili walioacha taathira kubwa mno katika taaluma hizo mbili; uhakiki na uandishi wa kubuni.

Mzalendo ni riwaya ambayo kimsingi imesheheni maudhui ya juhudi za siasa za ukombozi kutokana na utawala dhalimu wa wabeberu.

Kwa bahati mbaya, kampuni ya Shungwaya Publishers Ltd ilisambaratika baada ya kuitoa riwaya ya mwandishi huyu.

Mara yangu ya kwanza kukutana na Prof F. E. M. K Senkoro ilikuwa ni katika kongamano la wataalamu wa Kiswahili lililofanyika mjini Arusha, Tanzania mnamo 2002.

Kipindi hicho, nilikuwa ndio ninainukia katika usomi.

Hivi majuzi, sadfa ilinikutanisha naye tena kwenye kundi la WhatsApp la wataalamu wa Kiswahili ambao ni wanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

Kwa hiyo, nilisema naye chemba: “Shikamoo Prof Senkoro! Natumai hujambo. Riwaya yako hii (Mzalendo) uliichapisha mnamo 1977 na Shungwaya. Kampuni hii iliporomoka. Je, mbona usiitoe upya kazi hii na mchapishaji mwingine?”

Prof Senkoro alinishukuru kwa ushauri huo alioutaja kuwa mzuri.

Hata hivyo, alinifahamisha kwamba mimi si mtu wa kwanza kuwahi kumpa ushauri wa aina hiyo.

“Watu wengi wamekuwa wakinishauri hivyo lakini ninasita kidogo. Labda nitakaporudia kuisoma tena na tena nitaitolea uamuzi,” akasema.

“Salamu za huko Kenya?” akaniuliza.

“Kenya kwema Prof. Tumefanya maombi juzi kuukemea ufisadi. Hapa wizi tu. Unasita kwa nini Prof?” Nikasaili.

“Riwaya hiyo ni ya zamani. Nilikiandika kitabu hicho nikiwa kijana mno,” akasema Prof Senkoro.

“Mimi ninaamini kwamba huo ndio ulikuwa mchango wako kipindi hicho. Kwa hiyo, riwaya yako inaonyesha jinsi ulivyokuwa unafikiria kipindi hicho. Mimi ninapendekeza ukitoe kitabu hicho upya jinsi kilivyo. Wasomi tunajua kwamba mawazo na mitazamo ya Prof Senkoro vimebadilika. Kwa hiyo, wahakiki wataiangalia riwaya yako kwa mkabala huo – wasomaji wataisoma riwaya yako kwa jicho la Senkoro wakati huo, na Senkoro hivi sasa,” nikamrai.

Kufumbata mambo ya kipindi

Aidha nilishadidia kwamba fasihi hufumbata mambo ya kipindi pamoja na mazingira kazi hiyo inamotungwa.

Prof Senkoro alionekana kukubali ushawishi wangu wa kuitoa upya riwaya hiyo na kusema kwamba atanitwika jukumu la kuliandikia dibaji toleo jipya.

Kazi nzuri za fasihi ambazo zilichapishwa na makampuni ya uchapishaji ambazo zilisambaratika ni nyingi.

Tungo nyingi za Shaaban Robert kwa mfano zilichapishwa na kampuni ya Nelson Brothers, Uingereza.

Kwa zaidi ya mwongo mmoja vitabu vya Shaaban Robert ambaye yadaiwa kuwa ni mmoja wa watunzi maarufu kushinda wote Uswahilini – Afrika ya Mashariki na Kati havikupatikana kwa urahisi.

Kwa sababu hiyo, kuna uwezekano kwamba kuna vijana ambao hata hawamjui Shaaban Robert.

Hata hivyo, kampuni ya Mkuki na Nyota, Dar es Salaam, Tanzania ilianza kuvitoa vitabu hivyo ili kufufua tena katika mawazo ya kizazi chipukizi mchango wa mwandishi huyo muhimu.

Kwa hiyo, ni muhimu waandishi wa wachapishaji kuwazia upya hatua ya kuchapisha upya maandishi yao ambayo ama hayapatikani kwa urahisi kwa sababu ya kampuni kusambaratika au kwa sababu nyingine zile.

Kampuni ya Vide Muwa nchini Kenya imetoa mchango muhimu katika kutoa tungo za Euphrase Kezilahabi kama vile Nagona na Mzingile – ambazo zilikuwa hazipatikani Kenya.

Ninaamini kwamba Prof Senkoro atalivalia njuga pendekezo langu la kutoa upya riwaya yake – Mzalendo.

mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Urasmishaji wa Kiswahili nchini Rwanda badala ya Kifaransa hauna upya wowote

Na BITUGI MATUNDURA

JUMA lililopita, wabunge wa Rwanda waliidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi na ‘kuitupilia mbali’ lugha ya Kifaransa na kukiweka pembezoni Kiingereza.

Hatua hiyo ilipokelewa kwa hisia mbalimbali; baadhi ya watu wakiisherehekea na wengine wakionyesha masikitiko.

Baadhi ya watu walisema kwamba hatua hiyo ni nzuri; ingawa kuna wasiwasi kuwa huenda ikaighadhabisha Ufaransa.

Athari za hatua hiyo kwa mujibu wa wataalamu zitaanza kuonekana ikitarajiwa kwamba Ufaransa huenda ikaiadhibu Rwanda kwa kufadhili vyama vya upinzani kupinga utawala wa Rais Paul Kagame.

Baadhi ya wataalamu walihisi kwamba hatua hiyo ni ishara na mfano maridhawa unaopaswa kuigwa na nchi za Afrika ambazo bado zinakumbatia lugha za watawala wao wa zamani na hivyo basi kuendelea kudumisha ukoloni mamboleo.

Nilimuuliza Afisa Mkuu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) – Prof Inyani Simala – atoe kauli kuhusu hatua hiyo ya Rwanda kukikumbatia Kiswahili badala ya Kifaransa.

Hatua hiyo inaashiria nini?

Athari yake katika Sera ya Lugha Afrika ya Mashariki na Kati ni ipi?

Prof Simala alisema kwamba hatua hiyo haikuwa ngeni kwa sababu maamuzi hayo yalifanywa mnamo mwishoni mwa 2017 na mwanzoni mwa 2018.

Prof Simala alitahadharisha kwamba kabla ya kuisherehekea hatua hiyo ambayo haina upya wowote, ni muhimu kuelewa muktadha mzima kwanza uliochangia katika nchi hiyo kufikia maamuzi hayo.

Alisema kwamba maamuzi hayo yalichukuliwa na nchi zote za Afrika ya Mashariki.

Alifafanua kwamba Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imekwisha kuweka na kuimarisha mikakati ya kukiendeleza Kiswahili.

Alisema, kwa sasa, Kiswahili si lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa sababu hiyo Kamisheni ilishirikiana na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na kupitisha kwamba Kiswahili kiwe lugha rasmi.

Mwongozo wa kisera

Baada ya tamko hilo, KAKAMA ilishauri Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki kutoa mwongozo wa kisera wa utekelezwaji wa azimio hilo. Baraza hilo chambacho Mwalimu Simala lilitoa maelekezo matano kwa nchi zote wanachama.

Kwanza, kila nchi ikitangaze Kiswahili kuwa lugha rasmi.

Pili, kila nchi ianzishe Baraza la Kiswahili.

Tatu, kila nchi iwe na Chama cha Kitaifa cha Kiswahili. Nne, Kiswahili kitumiwe katika Nyanja rasmi ikiwa ni pamoja na mifumo ya elimu na vyambo vya habari.

Mwisho, shughuli za Kiswahili zifadhiliwe pale inapowezekana.

Kwa hiyo, Prof Simala alifafanua kwamba nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimo katika hatua mbalimbali za utekelezwaji wa mambo haya.

“Rwanda ikitangaza Kiswahili kuwa lugha rasmi, inachofanya ni kutekeleza maazimio hayo kupitia elimu.”

Alifafanua pia kuwa, sera ya lugha nchini Rwanda inatoa nafasi kwa lugha nne rasmi: Ikinywarwanda; Kiingereza; Kiswahili na Kifaransa.

Kutokana na maelezo na ufafanuzi wa Prof Simala, sikosei kudai kwamba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinajikokota katika kusukuma mbele ajenda ya Kiswahili.

Nchini Kenya kwa mfano, hatua za kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili la Kenya (BAKIKE) zimekwama.

Mchakato wa kuandaa Rasimu ya Sera ya Lugha ya Kenya (Kenya Language Policy Draft Bill) ulikwama miaka mingi imepita sasa.

Prof Kimani Njogu, mtaalamu wa lugha na utamaduni pendwa anasema kwamba mchakato huo umekuwa ukizunguka kwenye mduara.

Anapendekeza kwamba Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) kijifungate masombo kuhakikisha kwamba mchakato huo unaanzishwa tena.

Kiswahili ni lugha muhimu sana katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa ndiyo lugha ya mawasiliano mapana.

Baruapepe: mwagechure@gmail.com

KAULI YA MATUNDURA: Huu ndio mtazamo wa mwandishi Ayi Kwei Armah kuhusu sanaa ya uandishi wa kubuni

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO Januari 2005 nilihudhuria mhadhara wa mwandishi Ayi Kwei Armah wa Ghana kwenye ukumbi wa Taifa Hall, Chuo Kikuu cha Nairobi.

Katika kipindi hicho, raghba yangu ya kutaka kuwa mwandishi ilikuwa katika upeo wake.

Riwaya yangu – Mkasa wa Shujaa Liyongo ilikuwa imekwisha kuchapishwa na Phoenix Publishers Limited – baada ya vuta n’kuvute kali ambayo mara nyingi huwakatisha tamaa waandishi chipukizi.

Nisingalikuwa na moyo wa chuma kipindi hicho, labda ningaliachana kabisa na uandishi.

Lakini ninapovuta taswira kuhusu safari yangu ya uandishi, ninahisi kwamba kamwe sina majuto.

Yaliyonisibu labda ni kisa nitakachokisimulia wakati mwingine. Kwa hiyo, malengo ya kuhudhuria mhadhara wa mwandishi huyu yalikuwa ni mawili.

Kwanza, nilitaka kusikia tajriba yake na mtazamo wake kuhusu sanaa na fani ya uandishi.

Pili, nilitaka kukutana na mwandishi mwenyewe baada ya kusoma tungo zake kama vile The Beautiful Ones Are Not Yet Born (1968), Two Thousand Seasons (1973), The Healers (1973) na Why Are We So Blest? (1973).

Kazi nyingi za mwandishi huyu ziliwahi kuorodheshwa katika msururu wa tungo za African Writers Series (AWS) – ambao kwa yakini ulionesha nani ndiye nani katika uandishi wa fasihi ya Kiafrika punde tu baada ya mataifa mengi ya bara hili kujinyakulia uhuru.

Saa nane juu ya alama, ukumbi wa Taifa Hall, chuoni Nairobi ulikuwa umejaa pomoni.

Wahadhiri, wanahabari na wanafunzi walikuwa wameketi tayari kumsikiliza Ayi Kwei Armah. Mhadhara wake ulitamba kwenye mawanda mapana kuhusu historia na mahusiano ya Afrika, utamaduni wake na ukoloni.

Alidai kwamba katika mtagusano wa watawala wa kikoloni na Waafrika, wakoloni waliwadhalilisha Waafrika kwa namna ambayo iliwafanya wadharau tamaduni zao.

Alidai kwamba mpaka sasa, dhana ya uhuru wa Mwafrika ni dhana ya kimzaha tu.

Alisisitiza kwamba uhuru wa kisiasa kamwe hauwezi kuwa na manufaa ikiwa Waafrika hawatakuwa na uhuru wa utamaduni wao. Mwandishi huyu alizungumzia kuhusu mikabala mine ambayo inaweza kumfaa zaidi mwandishi yeyote – hasa mwanndishi chipukizi (kama mimi wakati huo) katika kuandika tungo za ‘masafa marefu’.

Kwanza, alisema kuwa uandishi ni sanaa ambayo inahitaji kukabiliwa na ufundi wa namna fulani.

Pili, alishauri kwamba sharti mwandishi awe na raghba (inspiration) ya kutaka kuandika.

Tatu, alisema kwamba lazima mwandishi awe mtu makini na anayefanya kazi kwa bidii. Alikariri kwamba mwandishi mara nyingi ni mtu mwenye ukiwa kwa sababu ndiyo kawaida ya kuandika.

‘Sisi wenyewe’

Aliendelea kusema kwamba matatizo ya bara la Afrika yana suluhisho mumo kwa mumo katika bara hili – kwamba hatuwezi kutarajia suluhisho kutoka popote isipokuwa Afrika.

Mwisho, mwandishi huyu aligusia suala nyeti kuhusu lugha inayopaswa kutumika kutungia fasihi ya Afrika.

Mhadhara ule ulipomalizika, kipindi cha maswali kilijiri. Niliuinua mkono wangu kutaka kumuuliza swali kuhusu nafasi ya Kiswahili katika uanndishi wa fasihi ya Kiafrika – na mstakabali wa lugha yenyewe katika ulingo wa kimataifa pamona na usemezano wa utamaduni wa Mwafrika na staarabu nyingine ulimwenguni.

Kwa bahati mbaya, mkono wangu ulipotelea kwenye ‘misitu ya mikono’ mingine iliyoinuliwa na watu wengine waliotaka kuuliza maswali.

Liwe liwalo, nilijifunza kutoka kwa mwandishi Ayi Kwei Armah kwamba uandishi ni taaluma inayohitaji subira na uvumilivu.

Ikiwa mtu hana hulka ya kudumisha mambo haya mawili, nafikiri ni muhimu ‘ ajipe shughuli’ ya kufanya mambo mengine tofauti.

Vinginevyo, atavunjika moyo bure bilashi.

mwagechure@gmail.com