Wazee wa Kaya sasa wavuruga karata za Jumwa

Na MAUREEN ONGALA

WAZEE wa Kaya wamezamia siasa za urithi wa kiti cha ugavana Kaunti ya Kilifi, katika hali ambayo itavuruga hesabu za wanasiasa wengi wanaomezea mate kiti hicho mwaka ujao.

Huku wakimtawaza Naibu Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi kurithi kiti hicho, walipitisha uamuzi kuwa kiti hicho kinafaa kuzunguka kutoka kwa kabila moja hadi nyingine.

Kwa msingi huu, uamuzi wao ni kuwa gavana anayefaa kuingia wakati Bw Amason Kingi atakapomaliza kipindi chake cha uongozi, hafai kutoka kwa jamii ya Wagiriama.

Bw Saburi hutoka katika jamii ya Warabai.Idadi kubwa ya viongozi wanaopanga kuwania kiti hicho kufikia sasa ni Wagiriama, akiwemo Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, Mbunge wa Magarini Michael Kingi na Waziri Msaidizi wa Ugatuzi Gideon Mung’aro.

Bw Saburi wiki iliyopita alitangaza rasmi azimio lake kutumia chama cha ODM kwa kinyang’anyiro hicho.

Mratibu wa Chama cha Wazee wa Kaya za Mijikenda, Bw Tsuma Nzai alisema wakati umefika kwa jamii ya Wagiriama kuunga mkono Mrabai kwa wadhifa huo.

“Tunawapongeza Warabai kwa kuunga mkono jamii ya Wagiriama kuongoza kaunti kwa vipindi viwili na tuna hakika wao pia wana viongozi bora. Sasa ni wakati wa Wagiriama kurudisha shukrani na kumkubali naibu gavana wetu aongoze Kilifi,” akasema.

Bw Nzai alisema wazee waliamua kiti hicho si mali ya jamii moja pekee bali kinafaa kushikiliwa na kila kabila katika jamii.

Waliongeza kuwa wameamua kumuunga mkono Bw Saburi kwa vile amekuwa mtiifu kwao kwa miaka mingi na pia amedhihirisha kuwa mwadilifu uongozini.

Walikuwa wameongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wazee Wamijikenda, Mzee Mwalimu Mbwisho kutoka Kaya Digo iliyo Kaunti ya Kwale.

“Naibu gavana wetu amekuwa akitusaidia kwa njia zozote zile bila kuchelewa hata anapokuwa na shughuli nyingi kazini. Hii inaonyesha kuwa yeye si mbinafsi na ataongoza jamii vyema,” akasema.

Hafla hiyo ilifanyika katika Kaya Ribe iliyo Kaunti Ndogo ya Rabai wakati wa kuzindua maombi ya kitamaduni yanayonuiwa kusihi miungu walete mvua, na kukemea kiangazi kilichosababisha ukame na njaa na matatizo mengine katika jamii.

Waliombea pia umoja wa jamii ya Wamijikenda na Pwani nzima kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022.? Mzee Mbwisho alisema hatua yao ya kumuunga mkono Bw Saburi ni mwanzo wa kutafuta umoja wa Wamijikenda.

Kulingana naye, umoja wa Pwani unakumbwa na changamoto nyingi kwa sababu ya viongozi wabinafsi ambao wanajali maslahi yao ya kibinafsi.? “Pwani haitapitia matatizo mengi ikiwa jamii ya Wamijikenda itaungana.

Tunaendelea kuwa nyuma kisiasa na kiuchumi kwa sababu hatuna umoja. Tumekubalia viongozi wa nje ya eneo hili kutugawanya kila mara tunapojaribu kuungana,” akasema.

Hali hiyo ndiyo imelaumiwa kusababisha vikwazo kwa juhudi za kuunda chama cha Pwani kabla 2022 ambazo zinaongozwa na Gavana Kingi.

Kwa upande wake, Bw Julius Saha alisema majadiliano kuhusu hitaji la kufanya kiti cha ugavana kiwe kikizunguka kutoka jamii moja hadi nyingine yalianza katika Kayafungo ambayo huwakilisha jamii pana ya Wagiriama.

“Hatua hii italeta umoja kwa jamii ya Wamijikenda. Hatutaki hali ambapo makabila ya watu wachache yataanza kuhisi kama yametengwa uongozini. Kila jamii inafaa kupewa nafasi ya kuongoza,” akasema.

Bw Saburi alitoa wito kwa wazee hao kuwachunguza kwa kina viongozi wote ambao wataenda kwao kutafuta uungwaji mkono.

Wazee wa Kaya watishia kulaani waliosingizia Naibu Gavana

Na CHARLES LWANGA

WAZEE wa Kaya wamewataka wale waliosingizia Naibu Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi mashtaka ya kupotosha wakati wa janga la Corona wamuombe msamaha la sivyo wawalaani.

Wakizungumza na wanahabari baada ya kufanya maombi ya shukrani eneo la Rabai kaunti ya Kilifi, baada ya Bw Saburi kuondolewa shtaka la kuambukiza umma virusi vya corona kiholela, wazee hao kutoka Kaya zote tisa za jamii ya Mijikenda pia waliitaka serikali imfidie Bw Saburi kwa kumtesa kimawazo.

Wakiongozwa na Mzee Stanley Kenga kutoka Kaya Ribe, waliwataka wote waliohusika katika uchochezi uliosababisha kushtakiwa kwa naibu gavana huyo, waombe msamaha.

“Bw Saburi ni mwana wetu na anafaa kuheshimiwa. Wale wote waliohusika katika madai ya urongo kuhusiana na naibu gavana wamuombe msamaha. Wasimpige vita mtoto huyu. La sivyo kutoka mchangani hadi mbinguni walaaniwe,” akasema.

Mzee Erastus Kubo alisema Bw Saburi ameteseka kisaikolojia na kiafya, na serikali inafaa imlipe fidia kutokana na masaibu aliyoyapitia yasiyo na ukweli wowote.

“Kwa sababu kesi hiyo imeisha, tunawataka wale wote waliomletea masaibu hayo wamuombe msamaha,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Tsuma Nzai, ambaye ni mratibu wa baraza la wazee wa Kaya, alisema baadhi ya wale ambao wanafaa kuomba msamaha ni wafanyikazi wa Kaunti ya Kilifi, ambao walichapisha filamu na hadithi za uongo mitandaoni, wakimkashifu Bw Saburi kwa kuambukiza watu virusi vya Corona akijua alikuwa na virusi.

“Kuna filamu ambazo zilivuma katika mitandao ya kijamii. Baadhi ya wakazi wakiwemo viongozi walimkashifu Bw Saburi na kumwita hayawani anayefaa kufungwa au hata kupigwa mawe. Hao ndio baadhi ya watu wanaofaa kuomba msamaha,” akasema.

Alhamisi iliyopita, mahakama ya Mombasa ilimwondolea Bw Saburi shtaka hilo la kukusudia kuambukiza watu Corona.Baada ya kutoka mahakamani, Bw Saburi alihutubia wanahabari na kusema amewasemehe wale waliomchafulia jina.

Lakini Gavana Amason Kingi akiongea na Taifa Leo kwa simu, alikanusha kupokea ripoti za wakora katika serikali yake. Alimshauri naibu wake awasilishe malamishi hayo mbele ya Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC), Mkurugenzi wa Ujasusi (DCI) na idhara nyingine za serikali za kukabiliana na maovu.

Wazee wataka mitishamba itumike kutibu corona

MAUREEN ONGALA na FLORAH KOECH

WAZEE wa Kaya katika eneo la Pwani, wanaitaka serikali ijaribu kutibu virusi vya corona kupitia mitishamba.

Wazee hao wameeleza kuwa dalili za virusi hivyo ni sawa na za ugonjwa wa ‘Kivuti’ uliokuwepo katika enzi za zamani, na uliotibiwa kwa mitishamba.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitamaduni cha Wilaya ya Malindi (MADICA) Bw Jospeh Mwarandu, ambaye ni mmoja wazee hao, alisema kuwa ni lazima serikali itumie njia tofauti kukabili virusi hivyo.

“Tuko tayari kujaribu matibabu kwa watu ambao wameambukizwa virusi. Hata hivyo, lazima tupate msaada tunaohitaji na vifaa vya kujikinga ili tusiambukizwe,” akasema Bw Mwarandu.

Alisema kuwa ugonjwa wa ‘Kivuti’ ulikuwa ukitibiwa kwa mchanganyiko wa mizizi, matawi na ngozi kutoka kwa aina mbalimbali za miti.

Aliyeugua ugonjwa huo alikuwa na dalili kama homa, kupiga chafya, kuumwa na mapafu na kushindwa kupumua vyema.

Alieleza kuwa mgonjwa angefariki baada ya siku sita ikiwa hangepata matitabu ya haraka.

Alisema kwamba wagonjwa waliokuwa wanaugua maradhi hayo walitengwa na familia zao na jamii, kwani ulikuwa wa kuambukizana.

Kwingineko, wazee wa jamii ya Tugen katika kijiji cha Cheplaot, Mogotio, Kaunti ya Baringo wameanza kufanya matambiko ya kitamaduni ili kulaani virusi vya corona.

Wazee hao na wanawake zaidi ya 20 walianza harakati za kutafuta usaidizi kutoka kwa mababu zao, ili kukabili virusi hivyo ambavyo vimewaua zaidi ya watu milioni kote duniani.

Walisema kuwa ni kupitia matambiko hayo ambapo watawarai miungu wao ili kuiokoa dunia dhidi ya “maradhi hayo yasiyoeleweka.”

Maombi hayo yalifanywa katika mlima mdogo mtakatifu, yakiongozwa na mzee wa kitamaduni aliyebeba kibuyu, maziwa, asali na miti aina ya minazi huku wakiomba kwa lugha ya Kitugen.

Kwenye maombi, wazee waliwarai mababu zao kuwasamehe dhambi zao na kuiokoa dunia dhidi ya corona.

Wakiongozwa na Mzee Kigen Kiptoo, walisema waliona kwamba huenda virusi hivyo vikaiangamiza dunia nzima ikiwa hakuna hatua za haraka zitachukuliwa kuwaokoa watu.

“Tumefahamu kuwa maradhi hayo hayana tiba na huenda yakakimaliza kizazi cha sasa ikiwa hakuna hatua za haraka zitakazochukuliwa. Tunawaamini mababu zetu, kwani wakati kunapokuwa na kiangazi, huwa tunaomba na mvua hunyesha. Tunaamini kuwa miungu watatuokoa ikiwa tutaomba,” akasema Bw Kiptoo.

Wazee wa Kaya walaumiana kwa kuunga mkono MRC

Na SIAGO CECE

Makundi ya wazee wa Kaya Mzirima na Mzidia yamedai kuwa Kaya Bombo imewaficha wanachama wa kundi la MRC (Mombasa Republican Council), jambo ambalo limefanya maafisa wa usalama waingilie kati.

Akizungumza na Taifa Leo, Mzee Mkoba Gwashe anayewakilisha wazee wa Kaya Rabai, hata hivyo, alipinga madai hayo na kusema hatua ya polisi kuwataka kuripoti kwenye kituo kabla ya kuzuru kaya zao inakiuka haki zao za kuabudu.

Hata hivyo, Wazee wa Kaya Bomba kwa upande wao wamejitokeza kwa kusema madai hayo si ya kweli kwani hawana uhusiano wowote na kundi hilo la MRC.

Wakiongozwa na Mzee Gwashe, walisema kuwa tayari wana mipango ya kuenda kortini ili kutatua ugomvi wao.

“Bado tunatafuta wakili atakayetuwakilisha kortini, si sawa polisi kutuagiza kupiga ripoti kwenye kituo ilhali haya ni masuala ya mila yetu,” alisema.

Alieleza kuwa tatizo hilo lilianza mwanzoni mwa mwaka huu ambapo wazee walienda kufanya matambiko msituni kama ilivyo desturi yao kila mwaka.

Lakini Naibu kamishna wa Kaunti ya Kilifi, Bw Jama Mohamud alisema wazee hao walikuwa na tofauti zao hivyo basi suala la MRC si la kweli.

“Hatujaona vijana wowote wa MRC, hizi tu ni tofauti ambazo wazee wanazo zinazowafanya kulaumiana. Nimewapa wiki mbili ili kutatua suala hilo pamoja na machifu,” alieleza Bw Jama.

Amri hiyo ya wiki mbili ilitolewa baada ya kamishna huyo pamoja na mafisa wengine wa polisi, machifu na wazee wa kaya kufanya mkutano wa dharura.

“Tunaelewa kuwa wazee hawa ni muhimu sana katika jamii na wanasaidia kutunza misitu hii. Kukiwa na jambo kama hili ni bora kulitatua mapema,” alisema Bw Jama.

Bw Jama pia alisema wamefanya mpango wa kuomba usaidizi kutoka kwa Shirika la Uhifadhi wa Misitu (KFS) kulinda misitu ya Kaya dhidi ya kuvamiwa.

Kundi la MRC liligonga vichwa vya habari katika miaka ya hivi majuzi baada ya kuanzisha mchakato wa kutenga eneo la Pwani kama sehemu inayojisismamia, lakini serikali ililiharamisha.

Wazee wa Kaya wamuombea Sonko, waunga mkono BBI

Na FADHILI FREDRICK

WAZEE wa Kaya eneo la Pwani walimfanyia Gavana wa Nairobi Mike Sonko maombi maalumu katika eneo takatifu la Kaya Kinondo mnamo Jumamosi.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wazee wa Kaya za Mijikenda, Bw Abdallah Ali Mnyenze, walimtetea Bw Sonko kwa masaibu yanayomkumba katika Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Walidai gavana huyo anaandamwa na wafanyabiashara tapeli ambao wanataka kumharibia sifa zake za kuwa katika mstari wa mbele kupambana na ufisadi kaunti hiyo.

“Amekuwa akifichua sakata za ufisadi na tunashangaa kwa nini amegeuzwa kuwa mshukiwa,’ akasema.

Katibu wa chama hicho, Bw Juma Hamisi Mwakavi alisema wameamua kumtetea kwa sababu yeye ni mkazi wa Pwani anayeheshimu sana tamaduni za Wapwani.

Wakati huo huo, wazee hao wameapa kuunga mkono na kupigia debe ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) itakapowasilishwa rasmi kwa umma.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na jopo la maridhiano ingali inasubiriwa kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao wa baraza la wazee wa kaya Bw Abdallah Ali Mnyenze walisema ripoti hiyo ambayo ilitokana na kukusanywa kwa maoni kwa wananchi itaisaidia Kenya kuwa nchi yenye utulivu na amani.

Wakihutubia wanahabari katika kaya ya Kinondo huko Diani, Kaunti ya Kwale, Bw Mnyenze alisitiza umuhimu wa mageuzi ya kikatiba nchini ili kuleta usawa kwa kila jamii nchini.

Alisema anamatumaini jopo hilo likusanya maoni ya wakenya na litazingatia maoni hayo kuleta mabadiliko nchini bila ubaguzi wowote.

‘Tuko tayari kuunga mkono ripoti hiyo ambayo tuna uhakika imezingatia maoni ya wakenya,’ akasema.

Katibu wa wazee hao wa kaya Bw Hamisi Juma Mwaviko alitoa wito kwa Wakenya kuiunga mkono ripoti ya BBI akisema italeta manufaa kwa wananchi kwani ripoti hiyo natokana na mkusanyiko wa maoni ya wakenya wa kila tabaka.

Bw Mwaviko alisema ripoti hiyo itakapotolewa rasmi lazima kuwe na uhamasisho zaidi kwa wananchi kujua kweli mapendekezo hayo yalizingatia maoni ya wakenya.

‘Kuna uwezekano katiba huenda ikarekebishwa lakini tunaomba hamasisho mashinani ili kueleza ripoti hiyo imependekeza nini,’ akasema.

Bw Mwaviko alisema kumekuwa na tetesi katika ripoti hiyo ambayo haijayolewa rasmi na hivyo kuomba baadhi ya viongozi kutowapotosha wakenya.

Na naibu mwenyekiti la baraza hilo Bw Stanley Kenga alisema kama wazee wa kaya wanaunga juhudi za kuwapatanisha wakenya kupitia jopo la maridhiano na kuwasihi wananchi kusubiri mapendekezo la jopo hilo.

‘Tutapigia debe ungwaji mkono kwa mapendekezo hayo katika ripoti hiyo ya BBI endapo kutakuwa na mapendekezo ya kurekebisha baadhi ya vipengele katika katiba,’ akasema.

Hatua hiyo ya wazee hao wa kaya kuunga mkono ripoti hiyo yanajiri huku joto likizidi kupanda kuhusu ripoti hiyo ambayo haijatolewa rasmi.

Magavana pia wana mchakato wao wa marekebisho ya katiba ambao ni Ugatuzi Initiative kwa lengo la kuimarisha serikali za kaunti.

KURUNZI YA PWANI: Thamani ya misitu ya Kaya kwa Mijikenda

Na KAZUNGU SAMUEL

MISITU ya kaya katika ukanda wa Pwani ni muhimu sana katika uhifadhi wa mazingira na kuulinda utamaduni.

Katika makabila tisa ya jamii ya Wamijikenda, kila kabila liko na msitu wa kaya ambao hutumika katika shughuli mbalimbali za kitamaduni ikiwemo maombi ya kiasili ambayo yalithaminiwa sana na jamii.

Jamii ya Wamijikenda inashirikisha Wagiriama, Wakauma, Wachonyi, Waribe, Wadigo, Waduruma, Wakambe, Wajibana na Warabai. Kila jamii kati ya hizi inahifadhi msitu wa kaya na kuuthamini katika shughuli za kitamaduni.

Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni,uharibifu wa makaya haya kutokana na uwepo wa shughuli nyingi za kibinadamu umeanza kuzua hali ya sintofahamu.

Zaidi ni hofu ya kuangamia baadaye kwa misitu hiyo endapo hakutakuwa na hatua za haraka zitaazochukuliwa kuhifadhi misiti hii ya kaya.

Mojawapo ya misitu ambayo inakumbwa na hofu ya kuangamia ni ule wa kaya Chonyi ulioko katika kijiji cha Mwarakaya, Vwevwesi, kaunti ya Kilifi. Msitu huo ambao unahifadhiwa na jamii ya Chonyi umeharibiwa sana.

Takribani asilimia sabini ya msitu huo imegeuka kuwa mashamba baada ya wenyeji kuingia ndani na kuanza kufanya shughuli za ukulima.

Hata hivyo katika juhudi za kuhakikisha kwamba misitu hiyo inahifadhiwa, shirika la Umoja wa Mataifa linahohusika na kuhifadhi utamaduni la UNESCO limeanzisha mpango wa kuhakikisha kwamba kaya zote tisa Pwani zinahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kile kitakachokuja. UNESCO imeanza mikakati ya kutoa zawadi kwa makaya ambayo yatahifadhi vyema misitu na mazingira yao.

Mwaka jana, msitu wa Kayafungo ulioko katika kaunti ya Kilifi ulitunukiwa kitita cha Sh 750,000 kwa kuibuka kuwa msitu uliotunzwa zaidi.

Msitu huo ni ngome ya jamii ya Wagiriama na unafahamika kwa kulinda mazingira yake dhidi ya uharibifu wa aina yoyote. Msitu huo unapatikana katika kijiji cha Gotani na mbali na fedha, ulipatiwa vifaa vyengine kama vile wilbaro ambazo zitatumika katika kuuhifadhi.

Fedha hizo zilitolewa na tume ya kitaifa ya KNATCOM kwa niaba ya UNESCO ili kuhakikisha kwamba misiti hiyo haiharibiwi tena.

Katika hafla hiyo, ambayo iliongozwa na maafisa wakuu wa KNATCOM akiwemo katibu wa bodi Dkt Evangeline Njoka msitu wa Kaya Gandini/Mtswakara kutoka kaunti ya Kwale uliibuka wa pili. Msitu wa kaya Gandini ulipongezwa kwa kuweka rekodi nzuri kuhusu shughuli zake za kuuhifadhi.

Msitu wa Kaya Chonyi ambao umeharibiwa sana uliibuka nambari ya mwisho na mwito ukatolewa kwa jamii ya Wachonyi kutia bidii ili kuhakikisha kwamba msitu huo hauharibiwi tena.

Mwaka wa 2009, UNESCO ilitoa jumla ya Dola 126,580 za Marekani kwa serikali ya Kenya. Fedha hizo zilitolewa mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi misitu ya kaya na vile vile kuhakikisha kwamba maeneo yenye historia za utamaduni yanahifadhiwa.

Pesa hizo zilitolewa kupitia kwa kitengo cha utamaduni katika wizara ya michezo na utamaduni.

Kulingana na Dr Njoka, shirika la KNATCOM linapanga kuangazia juhudi za kuhakikisha kwamba misiti ya kaya inalindwa dhidi ya uharibifu ambao unachochoewa na idadi ya watu ambao wanaingia misituni aidha kulima au kufanya makao.

“Lazima tulinde misiti yetu kwa sababu ndani yake kuna historia ya kale ambayo tutaipoteza endapo tutaiacha ikiangamia,” akasema Dkt Njoka.

Hivi majuzi, mwenyekiti wa Kayafungo Mzee Charo Mlewa aliambia Taifa Leo kuwa wanaendelea na juhudi za kuuhifadhi msitu wa Kayafungo ambao ni maarufu sana katika jamii ya Wagiriama.

“Tangu tuongoze kati ya kaya zote tisa, tumeendelea na juhudi zetu bila kurudi nyuma. Lengo kamili ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwa bora kwa uhifadhi,” akasema Mzee Mlewa.

Juhudi hizi za kuhifadhi misitu ya kaya pia zimepongezwa na washika dau mbalimbali likiwemo shirika la World Wildlife Fund (WWF) ambalo limekuwa likiongoza juhudi nyingi za kuhifadhi misitu kote nchini.

Akiongea na Taifa Leo afisa wa miradi katika WWF anayesimamia kaunti za Kilifi na Kwale Bw Elias Kimaru, alisema mpango wa KNATCOM kuanza kutoa zawadi kutasaidia pakubwa katika kuhakikisha kwamba misitu inahifadhiwa bila tatizo lolote.

“Mpango huu wa kutoa tuzo kwa misitu bora ya kaya italeta ushindani mkubwa ambao hatimaye utawafanya wazee na jamii ya Wamijikenda kuhifadhi misitu na hili ni jambo la muhimu sana,” akasema Bw Kimaru.

Naye afisa wa misitu katika makavadhi ya kitaifa NMK anayesimamia kaunti ya Kilifi Bw Lawarence Chiro aliponfgeza mpango wa KNATCOM kuanza kutoa tuzo utazifanya jamii ziendelee kuhifadhi misitu bila kuharibu.