• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Ken Walibora alivyowaathiri wanafunzi wa kigeni

Ken Walibora alivyowaathiri wanafunzi wa kigeni

Na YUNING SHEN

NINAANDIKA barua hii kwa sababu tu ya kutoa shukrani kwa mwandishi marehemu kwa athari ya vitabu vyake na utu wake kwangu. Mimi ni Mchina na mtaalamu wa Kiswahili anayesomea Ujerumani na kufundisha Nairobi.

Kama mwanafunzi wa Kiswahili, mtu asiye na asili ya Afrika Mashariki (na ya kati) kwa nasaba wala kwa kupitia ahali yangu, mimi sikuwa na tamaa kabisa ya kuandika juu ya historia ya Waswahili, sembuse juu ya hisia zao.

Ni mada ambayo angestahili kuandika mwingine, mada ambayo huenda ikatuangukia sisi watu wa ulimwengu huu begani, kichwani, halafu ikaingia moyoni kama kichomi. Hatujui la kujibu.

Nimeamua kushika kalamu baada ya kusoma makala ya wazee wengi na wasomi wengi juu ya Marehemu Ken Walibora hasa kupitia machapisho ya Kampuni ya Nation Media.

Sehemu ndogo ya makala hii itawalenga Prof. Evan Mwangi na Prof. Austin Bukenya ila nawarejelea kwa unyenyekevu kama aliokuwa nao marehemu Ken Walibora.

Hasa nabishana na mkuu Evan Mwangi aliyetoa wito wa kubuni nafasi kubwa zaidi katika madarasa ya chuoni kwa kabila la “Waswahili halisi” wa mwambao wa Kenya, pwani na visiwani Tanzania na kwingineko.

Vile vile, sibishani na mswahili mtaani mzee Austin Bukenya kwa kupendelea ujuzi wa Kiswahili kama kigezo cha utambulishaji wa Waswahili.

Hata hivyo, ni vyema ieleweke kuwa bado nawatazama na kuwasikiliza, kuwatii na kuandamana nao katika juhudi za kufikisha ugenini maandishi mengi zaidi ya lugha ya Kiswahili pamoja na historia ya Afrika Mashariki.

Ninafikiri kuwa itakuwa bora zaidi ninapoandika sasa kumuenzi mwandishi maarufu Marehemu Ken Walibora Waliaula ni heri niandike kwa lugha ambayo mwenyewe aliitumia. Lugha yake ilikuwa Kiswahili

Kongowea Mswahili

Riwaya ya Siku Njema (1996) aliyoiandika Ken Walibora ni kitabu cha ajabu sana kwangu mimi. Ni kitabu cha Kiswahili cha kwanza nilichokisoma kwa ukamilifu wake wakati nilipokuwa mwanafunzi wa Kiswahili chuoni.

Kitabu chenyewe hakina kurasa nyingi tunapokilinganisha na vitabu vingine kama vile riwaya ya mwandishi maarufu Shafi Adam Shafi, Mbali na Nyumbani (2013) au Harufu ya Mapera cha Kyallo Wamitila. Riwaya ya Siku Njema kimesalia kitabu ‘’kitamu’ zaidi cha Kiswahili kwangu.

Jinsi Ken alivyosimulia visa vya Msanifu Kombo vilikuwa vinagusa watu wengi sana hasa wasomaji ambao wangali katika elimu ya chini.

Msanifu Kombo ambaye amefiwa na mama yake, mwimbaji wa Taarab, akiwa mtoto mchanga sana, halafu kupitia juhudi zake za usomi na uandishi akajiwezesha kukamilisha safari yake kuwa Kongowea Mswahili na kupata kujua alipo baba yake.

Ni hadithi ya kijana aliyejikuta kwenye madhila utotoni mwake akajitoa kutoka katika shimo la umasikini kupitia juhudi, elimu, unyenyekevu na ustaarabu.

Ni hadithi Ken aliyotaka sana hata yeye mwenyewe awe Kongowea Mswahili na ni kitabu kilichoandikwa na yule yule Ken Walibora aliyekuwa anakulia Kitale, Kenya, mji wa mashamba na gereza, mji uliopo mwisho wa reli ya gari moshi.

Mwandishi Ken Walibora bila shaka ni mswahili wa aina yake. Nafikiri riwaya zake zilishakuwa mwanga kwa watu wengi waliokuwa wakisoma vitabu vyake shuleni.

Nathubutu kusema kuwa, pengine hata watu waliokuwa wamemtambulisha kuwa mwandishi aliyejaa vipaji vingi wamejiona ndani ya mioyo yao labda wao pia wangekuwa ni Waswahili kwa njia moja au nyingine. Si hata Mzee Austin Bukenya alijitambua kuwa Mswahili mtaani?

Isitoshe, wazee waliohariri kitabu cha Siku Njema na waliotaka kumshangilia Ken kuwa mwandishi wa Kiswahili wa kizazi kipya wakati ule, bila shaka wameshatabiria majengo yake.

Sigmund na Lourenco

Nilipoandika kwamba nilisoma Siku Njema chuoni, nilimaanisha chuo kikuu yaani “university” siyo shule ya upili.

Mimi sikupata muda wangu wa kujiunga na shule Kenya wala sikuweza kukulia Dar es-Salaam kama mswahili mtaani mzee Austin Bukenya, lakini, nimefunzwa lugha kwa ustaarabu na hali ya uswahilini, madarasa yapo katika mataifa mengi yakiwemo Uingereza, Ujerumani, Marekani, Urusi, Ufaransa, Uchina, Japani, Korea Kusini.

Orodha hii haina mpangilio maalum ila nilijaribu kuipangilia kwa mujibu wa ujenzi wa kitengo cha ufundishaji wa Kiswahili.. Kwa ufupi, maandishi ya Kiswahili yanasomwa, tena na watu wengi hata kama wanayasoma kwa kuchelewa.

Msomi Evan Mwangi alipomuingiza mbwa wake Sigmund, katika barua yake ya kuenzi Ken Walibora bila sababu wazi.

Nafikiri jina hili alilenga litokee kama Sigmund Freud, mtaalamu wa saikolojia kutoka nchini Austria ambaye nadharia yake ilichangia pakubwa katika falsafa ya Ulaya, nadharia ya jinsia, na vile vile katika kuhakiki fasihi ya Kiingereza, Kifaransa na lugha zingine za Ulaya.

Mkuu Evan Mwangi pengine amesahau ni pale pale Austria palipopandisha fasihi ya Kiswahili si haba. Jina la yule mwalimu ni Lourenco Noronha.

Mwalimu Lourenco alifundisha lugha ya Kiswahili na fasihi yake katika Chuo Kikuu cha Vienna, Austria, miaka thelathini na mitano kamili (1974-2009).

Alishuhudia waandishi wengi ya lugha hii azizi na adimu kupanda jukwaani kutoka Farouk Topan, Ebrahim Hussein, Mohamed Suleiman Mohamed hadi Euphrase Kezilahabi na wengine wengi.

Yeyote akipitia tovuti yake kwenye Chuo Kikuu cha Vienna na baada ya kujua wasifu wa waandishi hawa mmoja baada ya mwingine bila usajili wala hitaji la malipo, atashangaa kwa nini mwalimu mmoja tu aliyefunza Austria nzima Kiswahili.

Na si “Wa-Lurecho” pekee palikuwa pia na Prof Thomas Geider (1953-2010) aliyeorodhesha maandishi ya Kiswahili na uhakiki wa fasihi ya Kiswahili mtandaoni katika Swahili Forum (2003) na (2011), Orodha hii ndefu ya zaidi ya kurasa 130 yapatikana mtandaoni, pia bila malipo, hadharani kabisa. Kama si hawa tungepata wapi orodha kama hii.

Ningekuwa na mbwa wangu, afadhali nimuite Walurecho badala ya Sigmund. Najuta sana wakati nilipoelezewa maana ya kila neno la ngoma kwenye makamusi mbali mbali ya Kiswahili nyumbani kwake Ahmed Sheikh Nabhany huko Mombasa, mbwa wangu ninayemfuga sasa hakuwa amezaliwa.

Wasomi hawa wageni wanawafuata kwa makini sana kina Kyallo Wamitila, Kithaka wa Mberia, Mahmoud Mau, Rocha Chimera, Ahmed H. Ahmed na watu wengi wasiohesabika kuweka nguzo ya fasihi ya Kiswahili.

Mwanafunzi wa Kiswahili ughaibuni

Prof. Ken Walibora ana marafiki wengi nje ya Afrika Mashariki, labda umaarufu wake utaweza kushinda alivyosifiwa nchini Kenya.

Baada ya mazishi yake, wasomi wa Kiswahili kote duniani walijumuika kwenye mkutano maalum wa Zoom ili kusherehekea maisha yake. Ukurugenzi wa Chama cha CHAUKIDU (Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani) waliandaa kikao hicho.

Vile vile nafikiri kuna mashabiki wengi tu wa Kiswahili kama mimi tuliojificha na kujinyamazisha kwenye mkutano huu angalau kimya tushuhudie kazi njema aliyofanya Ken kwa kukuza lugha ya Kiswahili na heshima ya waliotoka uswahilini.

Mwanafalsafa mkubwa toka uswahilini, Shaaban Robert (1909-1962), alikuwa akiandika “wakati mmoja nilifikiri kuwa yote yaliyo azizi au bora kwa mtu ni matendo yake aliyotenda zamani;… wazo hili lilibatilishwa na fikira kuwa pengine ubora wa mtu huwezekana kuwa katika wakati ujao. (Shaaban Robert 1949/1966:1)”

Katika mfano wa maisha ya Ken Walibora, tayari amehitimu mitihani hii miwili. Naomba tukumbushwe tu nia yake ya kuwa Mswahili wa aina yake haiathiri juhudi zake za kuwabunia Waswahili wengine jukwaa mwafaka wapate kusikilizwa sauti zao na hisia zao.

Kazi yake Ken ya mwanzo kabisa niliyoijua katika kuhakiki fasihi ya Kiswahili ililenga kuweka ushairi wa Sauti ya Dhiki (1973) tungo za Abdilatif Abdala sehemu ambapo ingestahili kuonekana kwenye ulimwengu wa fasihi. “Msanifu Kombo” alikuwa na unyenyekevu huu kwa fasihi ya Waswahili.

Mara ya mwisho nilipokutana na Ken ana kwa ana ilikuwa mwishoni mwa mwaka jana, tuliposalimiana kwenye lango la nyumba yake mtaani Lavington, Nairobi tukiwa na rafiki yake Hezekiel Gikambi.

Ken alinitania akiniita “mkubwa” na halafu akanizawidia kitabu chake kwa wanafunzi wa darasa la kwanza Kalamu ya Maria Imepotea (2019). Wakati ule chapa ya kitabu hiki ilikuwa bado ni toleo kwa mwandishi na mhariri yaani hakijatolewa rasmi. Nilishangaa ati ukarimu wake hauchagui mtu, siku wala mwaka.

Wiki moja iliyopita, msomi mmoja wa CASS (Taasisi ya Taaluma ya Sayansi ya Jamii ya taifa nchini China), baada ya kuandikiwa buriani ya Ken Walibora, akaniuliza kuwa atapataje njia ya kutafsiri kitabu cha Siku Njema hadi Kichina, kwa sababu alimuahidi Ken katika kongamano moja lililoandaliwa na Umoja wa Afrika (CODESRIA), Dakar, Senegal, kutafsiri kitabu hiki na hata amepewa nakala ya Kingereza A Good Day (2019). Akazidi kuniomba nimsaidie kuhariri kutoka toleo la Kiswahili ikiyumkinika.

Pia akisema alikuwa anashangaa kwani Ken alikatiza mawasiliano naye wiki chache zilizopita juu ya mada ya uhusiano wa mataifa aliyoifundisha Chuo Kikuu cha Riara. Nikamjibu “Pole, Tutajaribu.”

Naamini labda hicho ndicho Shaaban Robert alichosema ni ubora wa mtu utakaogoma kufa katika wakati ujao.

Bw Yuning Shen ni Mtafiti Maalum wa ZJNU (Zhejiang Normal University), Mkufunzi wa Shahada ya Uzamivu katika UHH (Chuo Kikuu cha Hamburg-Ujerumani), Mhadhiri Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Baruapepe: [email protected]

You can share this post!

Ebola yazuka upya DRC

Mudavadi bado ndiye msemaji wetu – Atwoli

adminleo