Magoha akasirishwa na maafisa wake kwa kufeli kucheza video

Na CHARLES WASONGA

KIOJA kilishuhudiwa Alhamisi katika Taasisi ya Kuandaa Mtaala Nchini (KICD), Nairobi, Waziri wa Elimu alipozomea maafisa wake hadharani kwa kutomakinika kazini.

Hii ni kufuatia hitilafu iliyotokea na kuchagia kutochezwa kwa kanda ya video ya kuonyesha ufanisi wa mpango wa serikali wa kutoa msaada wa masomo kwa watoto kutoka familia masikini, maarufu kama, Elimu Scholaship Programme”.

Mpango huo, ulianzishwa mwaka jana, 2020, hulenga kufaidi wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) na kupata alama bora lakini hawawezi kupata karo.

“Nitaanza kwa kusema kuwa sijawahi kuhusishwa na utovu wa mipango ninaoushuhudia hapa asubuhi ya leo. Hali hiyo ikome kabisa! Nilitarajia maafisa wahusika kucheza video hii mapema kuhakikisha ni shwari. Sitakubali radhi zenu!”, Magoha akafoka.

Waziri huyo alisema hayo baada ya maafisa wa wizara yake kuomba radhi kufuatia video hiyo kufeli kucheza.

Lakini Profesa Magoha alisema tukio hilo iliabisha wizara yake wakati wa shughuli hiyo ambayo ilihudhuriwa na maafisa wakuu katika wizara yake na wanahabari.

Shughuli hiyo pia ilikuwa inapeperushwa moja kwa moja katika mtandao wa Facebook na You Tube ya Wizara ya Elimu.

Jumla ya wanafunzi 9,000 walipfanya mtihani wa KCPE ya 2020 walipata udhamini wa masomo chini ya mpango huo. Gharama zao zote za masomo kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne zitalipwa chini ya mpango huo unaodhaminiwa na serikali kuu kwa ushirikiano na Benki la Dunia.

Wabunge watisha kumtimua Magoha

Na Florah Koech

WABUNGE watatu kutoka Kaunti ya Baringo, wametishia kuwasilisha hoja ya kumtimua Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kutokana na kile walichosema ni kutoa amri zinazovuruga utendakazi wa wizara yake.

Mbunge wa Baringo Kusini Charles Kamuren, Daniel Tuitoek (Mogotio) na Joshua Kandie wa Baringo ya Kati walisema kwamba sekta ya elimu iko katika hatari ya kuporomoka kabisa kutokana na amri na sera za Profesa Magoha ambazo waziri huyo hukumbatia bila kushauriana na wadau wengine.

Wanasiasa hao hasa walisikitishwa na amri ya Profesa Magoha kuwa mabasi ya shule hayafai kutumiwa kwenye hafla za kibinafsi na shughuli za kijamii.

Pia walishutumu amri yake kwamba shule ambazo hazina watahiniwa zaidi ya 40 wa KCPE na KCSE ziunganishwe pamoja na hitaji la walimu wa shule za msingi kuwa na cheti cha Diploma.

“Hatuna taasisi yoyote ya kutoa mafunzo ya ualimu hapa Baringo ya Kati. Pia si wanafunzi wengi kutoka hapa ambaye waliofuzu vyema na kuhitimu kujiunga na taasisi hizo. Amri ya Profesa Magoha kuhusu elimu inakera na inabagua jamii zilizotengwa,” akasema Bw Kandie.

Kusomea ualimu, Wizara ya Elimu imesema kwamba wanafunzi lazima wawe na alama ya C wastani katika KCSE na alama sawa na hiyo katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

“Iwapo Profesa Magoha hatabadili mtindo wake wa uongozi na kuondoa amri hizo alizoziweka, basi niko tayari kuwasilisha hoja ya kumtimua bungeni,” akaongeza Bw Kandie.

Mvulana aliyeitwa shule ya wasichana sasa apata afueni

Na Francis Mureithi

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, amekubali lawama ambapo mwanafunzi mvulana katika Kaunti ya Bungoma aliitwa shule ya upili ya wasichana kujiunga na kidato cha kwanza.

Spencer Wangila kutoka Bungoma alipokea barua ya kujiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Naromoru, Kaunti ya Nyeri.

Ni hali iliyoacha familia ya mvulana huyo katika hali ya kuchanganyikiwa, kwani kijana wao hakuchagua shule ya Naromoru kuwa miongoni mwa zile ambazo angependa kujiunga nazo.

Wangila alifanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) katika Shule ya Msingi ya Misikhu, na kuzoa alama 370.

Lakini akizungumza Ijumaa katika hafla ya kufuzu kwa mahafala wa Chuo Kikuu cha Egerton, Prof Magoha alihakikishia familia hiyo kuwa tatizo hilo limerekebishwa.

“Kama Waziri wa Elimu, ninakubali lawama zote kutokana na kosa hilo. Hata hivyo, ningetaka kuwahakikishia wananchi na wazazi wa mwanafunzi husika kuwa kosa hilo limerekebishwa.

Ni makosa kuwa mvulana huyo aliitwa katika shule ya wasichana japo nina furaha kwani hali hiyo haipo tena,” akasema.

Akaongeza: “Mwanafunzi huyo sasa ameitwa katika Shule ya Upili ya Kibabi, ambayo ni ya wavulana.”

KCSE: Afisa abambwa na Magoha akisaidia watahiniwa kwa udaganyifu

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha kwa mara nyingine ametoa onyo kali kwa watahiniwa wa mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE kuhusu kushiriki udanganyifu katika zoezi hilo linaloendelea.

Prof Magoha alitahadharisha Jumanne kwamba watakaoshiriki wataadhibiwa kisheria.

Waziri huyo pia alitoa onyo kwa walimu na wasimamizi wa mitihani watakaohusishwa na udanganyifu, sheria haitakuwa na budi ila kuchukua mkondo wake.

“Leo Jumanne, tumekamata msimamizi katika shule moja eneo la Migori akisambaza karatasi za mitihani kabla ya wakati wa kuuandika kuwadia. Atafikishwa kortini afunguliwe mashtaka,” akatangaza Prof Magoha, akitoa onyo kali kwa wahusika.

Waziri huyo hata hivyo alihakikishia taifa kuwa mitihani ya KCSE kote nchini ni salama.

“Watahiniwa watakaojaribu kutumia mbinu za hila kupita mtihani, tutawaadhibu kisheria. Hatutasaza mhusika yeyote,” akaonya.

Mtihani huo wa kitaifa kidato cha nne ulianza juma lililopita, Ijumaa, Machi 26, siku chache baada ya ule wa darasa la nane, KCPE kukamilika.

Tetesi ziliibuka kuwa KCPE ilishuhudia udanganyifu. Waziri Magoha hata hivyo alipuuzilia mbali madai hayo.

Kalenda ya masomo 2020 ilisambaratishwa na mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini, ambapo wanafunzi walisalia nyumbani mwaka mmoja.

Aidha, walirejea Januari 2021. Serikali ilichukua hatua ya kufunga shule zote na taasisi za elimu ya juu nchini kama njia mojawapo kusaidia kudhibiti maenezi ya virusi vya corona.

Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa corona Machi 2020.

Watahiniwa wa KCPE na KCSE walirejea shuleni Oktoba 2020 ili kujiandaa kuandika mitihani hiyo iliyoratibiwa kufanyika Machi 2021.

KCSE: Magoha aamrisha polisi wapokonywe simu wasifanikishe udanganyifu wa mitihani

NA MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha Jumatatu ametoa amri kuwa maafisa wa polisi wanaolinda harakati za mtihani wa KCSE unaoendelea kote nchini wawe wakipokonywa simu zao za mkononi ili wasishirikishe visa vya udanganyifu.

Prof Magoha akiongea katika Makao makuu ya Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini alikofika kunyapara usambazaji wa nakala za mtihani huo alisema kuwa maafisa wa polisi wanaoshiriki zoezi hilo wako na uwezo mkuu wa kuhatarisha uadilifu wa mitihani nchini.

Aidha, waziri huyo alipiga marufuku usafirishaji wa mitihani kwa kutumia magari ya kibinafsi akiteta kuwa “kunao walimu wengine ambao wanatumia huduma hata za matatu kuusafirisha hadi mashuleni mwao.”

Alisema kuwa hali kama hiyo inafanya harakati za kulinda uadilifu wa mitihani ziwe ngumu akiongeza kuwa “ninaamrisha magari rasmi ya shule yawe tu ndiyo yatatumika katika usafirishaji huo.”

Aliteta kuwa matatu ikitoka steji moja hadi nyingine ikipitia kwa kila aina ya chochoro huwezi ukawa na uhakika kwamba visa vya udanganyifu havitekelezwi “na baadhi ya wakora tulio nao katika zoezi hili.”

Alisema kuwa maafisa wa polisi wako na uwezo wa kupiga picha nakala za mtihani na kisha kuzituma kwa mitandao ya udanganyifu na kisha kufikia wanafunzi katika shule zingine kwa kuwa hawaanzii kufanya mitihani hiyo kwa wakati mmoja.

Baadhi ya njama ambazo walio katika mtandao huo wa wizi wa mitihani hutekeleza ni kuchelewesha usambazaji wa nakala hadi baadhi ya mashule ndio kwenye zilifunguliwa ziwe zimepigwa picha na kisha kutumwa kwao.

Hapo ndipo nakala hizo zikishapokelewa hujibiwa harakaharaka na walimu au wengine ndani ya njama hiyo na kupewa wanafunzi ili shule zao zing’are katika matokeo au watoto wao wapate alama za juu.

Prof Magoha alisema kuwa serikali iko macho hasa katika kanda za Magharibi na Nyanza ambako alisema kumezuka habari za ujasusi kuwa njama ya kuiba mtihani huo zinashirikishwa na baadhi ya walimu.

“Tuko na Mwalimu mkuu katika shule moja ya ukanda wa Magharibi ambaye ameshukiwa kuwa na njama ya kupenyeza nakala za kusaidia wizi wa mtihani…Ameamrisha walimu wote waondoke kutoka shule hiyo ndio abakie na mazingara mwafaka ya kuendeleza njama hiyo. Anafaa aaibike sana na nimpe onyo hapa kuwa hataweza kushirikisha ukora huo,” akasema.

Alisema kuna walimu wengine watatu katika Kaunti ya Migori ambao “sijui kama ni wazimu wako nao au ni nini kinawasukuma” kwa kuwa “nao wamefuatiliwa na kutambuliwa kuwa wako na njama hiyo ya kusaidia udanganyifu.”

Prof Magoha aliapa kuwa wote walio katika ajira ya serikali watakaonaswa wakishirikisha wizi wa mtihani huo watafutwa kazi na washtakiwe sambamba na wengine wote ambao watathubutu kushiriki njama hizo.

Mkurugenzi wa Elimu ukanda wa Kati Bi Margaret Lesuda alitoa tahadhari kuwa maradhi ya Covid-19 yashafika katika shule nyingi hapa nchini kwa makali ya ukatili “na ambapo wikendi tu hii imepita tulipoteza walimu wawili wakuu katika shule za msingi huku kwa ujumla tukiwa tumepoteza zaidi ya walimu 15 hadi sasa.”

Alisema kuwa ni suala la dharura kwamba watahiniwa pamoja na wanaoshirikisha zoezi hilo wazingatie masharti ya kiafya hasa katika uvaaji wa maski, kuweka umbali unaopendekezwa na wizara ya afya kutoka mtahiniwa mmoja hadi mwingine, kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji au sanitaiza na pia kuwajibikia dalili za kuugua kwa uadilifu na dharura.

Alisema kuwa “mtihani ambao unaweza ukahatarisha maisha ya watoto au ya wanafunzi na wadau wengine ni hatari hivyo basi kila aina ya tahadhari itekelezwe.”

SHULE: Wadau muhimu ngazi zote za serikali waelezea utaratibu ulioko

Na MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema Jumapili kwamba mipango na mikakati yote imewekwa kuhakikisha shule zinafunguliwa kesho Jumatatu.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha amesema hayo huku akiangazia haja ya kuzingatia masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Waziri Magoha amesema mchakato wa kupeana madawati kwa shule kadhaa umefanyika kwa njia nzuri huku akiahidi maseremala na mafundi wengine walioyatengeneza watalipwa.

Inatarajiwa kwamba shule nufaika kwa jumla zitapata madawati zaidi ya 500,000

Waziri Magoha ameahidi kwamba kila mwanafunzi atakuwa na barakoa.

“Kila mwanafunzi shuleni ni sharti awe na barakoa,” amesema Magoha.

Serikali imeahidi itatoa barakoa kwa zaidi ya wanafunzi 3 milioni ambao hawawezi wakapata wao wenyewe ikizingatiwa kipato cha familia za wanakotoka.

Kuhusu umbali, waziri amesikitika kudumisha mita moja na nusu au zaidi kati ya mwanafunzi mmoja hadi mwingine huenda kusidumishwe, lakini akasisitiza ni sharti shule zihakikishe hata wanafunzi wanasomea chini ya miti, katika bwalo na hata sehemu yoyote ya wazi lakini iliyo safi na salama.

Wazazi nao wametakiwa wahakikishe wanawajibika na kulipa karo na wala sio kutumia mwanya wa maagizo ya serikali iliposema wanafunzi kukosa karo usiwe msingi wa wao kurejeshwa nyumbani.

Ni wanafunzi wa kutoka familia zenye changamoto ya kifedha pekee ndio watapewa ruzuku ya ulipaji karo.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangi amesema Rais Uhuru Kenyatta amerefusha utekelezwaji wa kafyu ya usiku ambayo huanza saa nne za usiku.

Mwenyekiti wa Elimu katika Baraza la Magavana aliye pia Gavana wa Kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga amesema yeye na magavana wenzake wanashirikiana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba shule zinafunguliwa tena jinsi ipasavyo.

Wengine waliohutubu katika kikao cha Jumapili na wanahabari ni Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na Waziri wa Uchukuzi James Macharia.

Shule zilifungwa kwa kipindi cha zaidi ya miezi tisa tangu Machi 2020 baada ya janga la Covid-19 kuyumbisha kila sekta.

Huenda baadhi ya watahiniwa wakakosa mitihani ya KCPE, KCSE

Na GEORGE ODIWUOR

WATAHINIWA wa mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) katika shule za kibinafsi ambazo zimefungwa na wamiliki kutokana na makali ya virusi vya corona huenda wakakosa kufanya mitihani hiyo ya kitaifa.

Hii ni baada ya Wizara ya Elimu kusisitiza kuwa watahiniwa waliohamia katika shule za umma watalazimika kurudi katika shule zao za awali wakati wa kufanya mtihani.

Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha amesema kuwa, serikali imeruhusu wanafunzi kutoka shule za kibinafsi kuhamia katika shule za umma kufuatia janga la virusi vya corona.Waziri Magoha, hata hivyo, alisema watahiniwa watalazimika kurejea katika shule zao ambapo walijisajili kufanyia mtihani wa KCPE na KCSE.

Ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya shule 130 za kibinafsi zimefungwa kufuatia makali ya janga la virusi vya corona.

Kulingana na Chama cha Wamiliki wa Shule za Kibinafsi (Kepsa) shule hizo huenda zikakosa kufunguliwa Januari 4, mwaka ujao.Hiyo inamaanisha kuwa, wanafunzi waliojisajili katika shule hizo kwa ajili ya KCPE na KCSE huenda wakakosa kufanya mtihani huo.

“Kuna wazazi ambao walipoteza ajira au biashara zao na watoto wao walikuwa wanasomea katika shule za kibinafsi na hawawezi kulipa karo. Mitihani imetayarishwa na hatuna muda wa kubadilisha shule ambapo wanafunzi watafanyia mitihani yao.”

Prof Magohaa lisema kuwa, serikali itatoa uamuzi wake baadaye kuhusiana na hatima ya watahiniwa wa shule za kibinafsi ambazo zitakosa kufunguliwa.

Waziri alisema kuwa kuruhusu wanafunzi wa shule za kibinafsi kujiunga na shule za umma ni miongoni mwa mikakati iliyowekwa na serikali kuhakikisha kuwa watoto wote wanarejea shuleni Januari.

Serikali yamkata pembe Magoha kwa kumdhulumu afisa wizarani

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Utumishi wa Umma (PSC) Ijumaa ilimpokonya Waziri wa Elimu Prof George Magoha mamlaka ya kusimamia wafanyakazi katika wizara hiyo.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa PSC Browne Kutswa, mwenyekiti wa tume hiyo Stephen Kirogo alipeleka mamlaka hayo kwa Katibu wa Wizara hiyo anayesimamia Elimu ya Msingi Dkt Belio Kipsang’.

Hii ni kufuatia kisa cha wiki iliyopita ambapo Prof Magoha alinaswa kwenye video akimfokea, kumdhalilisha na kumtusi hadharani Mkurugenzi wa Elimu  wa Uasin Gishu Gitonga Mbaka katika shule ya msingi ya Langas, mjini Eldoret.

Ijumaa Bw Kirongo akasema kwenye taarifa hiyo iliyonakiliwa kwa wenyekiti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua kwamba “masuala yote ya wafanyakazi katika Wizara ya Elimu yatasimamiwa na Dkt Kipsang’ hadi wakati usiojulikana.”

Karogo alisema kuwa hatua hiyo inatokana na mamlaka ya PSC na kujitolea kwake kuwakinga watumishi wa umma dhidi ya kukaripiwa na kudhalilishwa bila sababu maalum.

“Utekelezaji wa mamlaka ya tume uliotwikwa afisa fulani sharti undeshwe kwa njia ambayo inajenga imani, heshima na maadili ya utumishi wa umma.” Akasema Bw Kutswa.

Kufuatia kisa hicho, Prof Magoha ameapa kutoomba msamaha kwa kumkosea heshima Bw Mbaka mbele ya maafisa wadogo wake akijigamba kuwa huo ndio mtindo wake wa kufanya kazi.

“Watu hawapaswi kushangazwa na mtindo wangu wa kufanya kazi. Nilihudumu katika Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) ambako nililainisha mambo. Sasa niko hapa kuhakikisha kuwa mahitaji ya wazazi na wanafunzi yanatizwa wakati wowote ule. Ikiwa siwezi kufanya hivyo basi sio haja ya kuendelea kuhudumu katika wizara hii,” akasema siku moja baadaye alipozuru Shule ya Msingi ya Kyamutheke, Kaunti ya Machakos.

Hii ni baada ya Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (KUPPET) tawi la Uasin Gishu kumtaka ajiuzulu kwa kumtusi Bw Mbaka, mkurugenzi wa elimu mwenye tajriba ya miaka mingi. Wakenya mitandaoni pia walimtaka Profesa Magoha ajiuzulu au afutwe kazi na Rais Uhuru Kenyatta.

Mnamo siku ya tukio, Prof Magoha alionekana akimtusi Bw Mbaka, mwenye nywele nyeupe, kwa kutohakikisha kuwa usafi umedumishwa katika shule hiyo ya msingi ya Langa.

“Mazingira hapa sio safi,” akasema Waziri. Naye Bw Mbaka akajibu hivi; “Suala hili litashughulikiwa katika ripoti itakayoandaliwa na afisi yangu.”

Ndiposa Magoha akafoka: “Siongei kuhusu ripoti. Nazungumza kuhusu hali iliyoko hapa, uchafu uliotapakaa kote. Nikikuita mjinga, je, nitakuwa nimedanganya?”

Hapa ndipo Waziri huyo alimwamuru Bw Mbaka aondoke kutoka ujumbe ulioandamana naye kukagua hali ya masomo shuleni humo na utekelezaji wa mpango wa usambazaji madawati na kumsindikiza kwa tusi la: “Wewe ni mjinga kabisa.”

Sitaomba msamaha, Magoha awaambia wakosoaji

Na LILLIAN MUTAVI

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, amesisitiza kwamba, hatabadilisha mtindo wake wa kufanya kazi, licha ya kutakiwa kuomba msamaha kuhusiana na kisa ambapo alinaswa akimkaripia afisa wa elimu.

Prof Magoha alinaswa kwenye video akimfokea vikali Mkurugenzi Mkuu wa Elimu katika Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Gitonga Mbaka, katika Shule ya Msingi ya Langas wiki iliyopita.

Akiwahutubia wanahabari jana katika Shule ya Msingi ya Kyamutheke, Kaunti ya Machakos, Prof Magoha alisema baadhi ya maafisa wa elimu walio nyanjani wamekuwa wakizembea katika utekelezaji wa majukumu yao kwa hivyo mtindo anaotumia ndio unafaa ili wananchi wahudumiwe inavyotakikana.

“Watu hawapaswi kushangazwa na mtindo wangu wa kufanya kazi. Nilihudumu katika Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) ambako nililainisha mambo. Sasa niko hapa kuhakikisha mahitaji ya wazazi na wanafunzi yametimizwa wakati wowote ule. Ikiwa siwezi kufanya hivyo, basi sipaswi kuwepo kwenye wizara,” akasema.

Alisema baadhi ya wafanyakazi katika wizara hiyo hawalengi kutekeleza wajibu wao wa kuboresha sekta ya elimu kikamilifu.

Alieleza kuwa, baadhi ya maafisa walio nyanjani hawatembelei shule zilizo katika maeneo wanayosimamia, hivyo hawapaswi kupokea mishahara.

“Ikiwa unasimamia shule 30 katika eneo lako, ambapo kufikia mwishoni mwa mwezi hujatembelea hata shule kumi, hupaswi kupokea mshahara. Maafisa hao lazima wawajibikie majukumu yao, la sivyo nitawafanya kutimiza hayo. Tunapaswa kuwatendea haki watoto wetu kwani serikali inatumia fedha nyingi kutimiza maslahi yao,” akasema.

Wadau mbalimbali, wakiwemo maafisa wa vyama vya walimu, wamemkashifu waziri huyo hasa kwa maneno makali aliyotumia dhidi ya afisa huyo wa elimu.

Baadhi yao walimtaka aombe msamaha, la sivyo wawasilishe ombi kwa Rais Uhuru Kenyatta ili asimamishwe kazi kwa madai ya kukosa maadili.

Prof Magoha amejipata taabani kwa muda sasa, kwani amekuwa akikashifiwa pia kwa jinsi anavyosimamia sekta ya elimu wakati wa janga la corona. Baadhi ya wazazi na walimu hudai kukanganywa na matamshi yake.

Kuhusu suala la uwepo wa madawati shuleni, alisema kufikia sasa wamesambaza vifaa hivyo kwa zaidi ya robo tatu ya shule za msingi na upili nchini. Haya hivyo, alisema Machakos bado haijapokea madawati hayo ipasavyo.

Magoha kuandaa kikao cha wadau kujadili ratiba mpya

Na FAITH NYAMAI

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha ameitisha mkutano wa wadau katika sekta ya elimu wiki hii kujadili kalenda mpya ya masomo shuleni, tarehe za mitihani ya kitaifa na namna ya kufidia miezi iliyopotea kutokana na janga la Covid-19.

Mkutano huo wa dharura, unalenga kujadili na kusuluhisha masuala ibuka kuhusu kalenda ya masomo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa wanafunzi wa madarasa mengine watarejea shuleni Januari, 2021.

Wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne walirejelea masomo ya kawaida mnamo Oktoba 5, 2020, chini ya uzingatiaji wa masharti ya kuzuia maambukizi ya Covid-19.

Ilitarajiwa kuwa wanafunzi wengine wangeripoti shuleni kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 6 lakini mipango hiyo ilisitishwa baada ya visa vya maambukizi ya corona, na vifo, kupanda zaidi ndani ya mwezi wa Oktoba.

Mkutano wa wiki hii pia unatarajiwa kujadili changamoto za kuwa na makundi mawili ya wanafunzi katika madarasa ya tano na kidato cha kwanza katika mwaka mmoja. Suala hilo limeibuka kuwa gumu kutanzuliwa na walimu pekee bila kushirikishwa kwa wadau wengine.

Kucheleweshwa kwa kurejelea masomo kwa wanafunzi wa shule za chekechea, wale wa gredi ya 1 hadi gredi 3, madarasa ya tano hadi saba na kidato cha kwanza hadi tatu kutokana na janga la corona kumeibua wasiwasi miongoni mwa walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe. Hii ni kutokana na muda ambao watakuwa wamepoteza wakiwa nyumbani.

Waziri Msaidizi wa Elimu, Zack Kinuthia aliambia Taifa Jumapili kwamba, wizara inajadili uwezekano wa kuunganisha kalenda ya mwaka ujao na wa mwaka huu ili kubuni mihula minne, badala ya tatu ilivyo kawaida.

“Tunaweza kuamua kuunganisha mihula ya pili na ya tatu kuhakikisha kuwa kalenda ya mwaka huu inatamatika kufikia Juni, 2021,” akaeleza.

Hii itapelekea kila muhula kudumu kwa miezi miwili na nusu pamoja na likizo ya wiki moja au mbili.

Bw Kinuthia pia alisema wanatafakari kuhusu uwezekano wa kuchelewesha usajili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwezi mmoja ili kuepuka uwezekano wa kuwa na makundi mawili ya wanafunzi katika kidato cha kwanza mwaka 2021.

Hii ina maana kuwa huenda wanafunzi watakaojiunga upya na kidato cha kwanza wakaripoti shuleni Julai, baada ya kundi la sasa kujiunga na kidato cha pili.

Wanafunzi wa Kidato cha Nne, Darasa la Nane na Darasa la Nne kurejea shuleni Jumatatu

NA FAUSTINE NGILA

WIZARA ya Elimu imewataka wanafunzi wa Kidato cha Nne, Darasa la Nane na Darasa la Nne kurejea shuleni Jumatatu ijayo kukamilisha masomo ya muhula wa pili wa mwaka huu, yatakayoendelea kwa wiki 11.

Kwenye taarifa iliyotuma kwenye vyombo vya habari Jumanne, wizara hiyo ilifafanua kuwa ilifikia uamuzi huo kufuatia mazungumzo ya kina na washikadau husika.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu alizitaka shule kuendelea kufuata kanuni za kuthibiti maambukizi ya virusi vya corona kama vile kuvaaa maski, kupima joto la wanafunzi na walimu, kunawa mikono na kudumisha hali ya juu ya usafi.

“Shule zote ambazo zilitumika kama vituo vya karantini vimepuliziwa dawa ya kuua viini vya corona kutayarisha madarasa kwa masomo. Walimu wote wanahimizwa kuwapa nasaha wanafunzi watakokuwa na matatizo ya mpangilio huu,” ikasema taarifa kutoka kwa wizara hiyo.

Kulingana na agizo hilo, wanafunzi hao wataenda kwa likizo ya wiki moja siku moja kabla ya Krismasi, hapo Desemba 24, 2020 na kurejea tena mwakani Januari 4, 2021 kwa muhula wa tatu.

Mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE itafanyika kutoka Machi 22 hadi Machi 24, 2021 na Machi 25 hadi Aprili 4, 2021 mtawalia. Matokeo ya mtihani wa KCSE yatatangazwa hapo Mei 2021.

“Wizara ya Elimu itashirikiana na Wizara ya Afya kufuatilia miongozo na mapendekezo ya kufungua shule ili kutambua ni lini wanafunzi wote waliosalia watarejea darasani,” ikasema taarifa hiyo.

 

 

Waziri mtatanishi

Na MWANDISHI WETU

MISIMAMO ya Waziri wa Elimu, Prof George Magoha kuhusu ufunguzi wa shule tangu zilipofungwa Machi kwa sababu ya janga la corona, umewaacha wazazi, walimu na wanafunzi wamechanganyikiwa.

Tangu kisa cha kwanza cha maambukizi ya corona kutokea nchini na kusababisha shule zote kufungwa, Prof Magoha amekuwa katika mstari wa mbele kuarifu umma kuhusu hatua zinazochukuliwa na wizara yake.

Kila mara waziri huyo anapojitokeza kuhutubia umma, wadau wa elimu hasa wazazi na walimu husubiri kwa hamu kusikia wazi kuhusu ni lini shule zitakapofunguliwa.

Hata hivyo, mijadala ambayo hutokea miongoni mwa wadau wa elimu ikiwemo katika sehemu za umma na mitandao ya kijamii kila baada ya hotuba za Prof Magoha huonyesha huwa anawaacha wamekanganyika zaidi kila mara anapohutubu.

Mnamo Julai 1, Prof Magoha alitangaza kuwa uamuzi kuhusu kama shule zitafunguliwa ungetangazwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Julai 6.

Wakati huo, alidokeza kuwa shule zitafunguliwa Januari mwaka ujao kwa vile wataalamu wa afya walisema maambukizi ya virusi vya corona yangefika kilele Septemba.

Awali, wizara hiyo ilikuwa imetangaza uwezekano wa shule kufunguliwa Septemba mwaka huu hasa kwa watahiniwa wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne.

Wakati Rais Kenyatta alipohutubia taifa, hakuzungumzia suala hilo na badala yake akalirudisha mikononi mwa Prof Magoha ambaye alihutubu Julai 7.

“Wadau wameamua shule zitafunguliwa tu baada ya idadi ya maambukizi kupungua hadi chini ya asilimia tano ya wanaopimwa kwa wiki mbili mfululizo. Idadi ya maambukizi inapanda sana Kenya kwa sasa. Kwa kuzingatia haya, wadau wameamua kuachana na pendekezo la awali la kufungua shule Septemba,” alisema waziri.

Lakini baadaye mwishoni mwa Agosti, waziri alijitokeza tena na kudokeza uwezekano wa shule kufunguliwa karibuni, aliposema kamati maalumu inatazama hali itakavyokuwa kwa “wiki mbili au tatu zijazo”.

KAMATI MAALUM

Mapema wiki hii, uwezekano huu ulitiwa nguvu baada ya mkutano wa kamati maalumu ya wadau wanaotathmini hali ya elimu wakati wa Covid-19.

Ijapokuwa walikataa kutangaza kama wamekubaliana kufungua shule, Prof Magoha alisema utathmini umefanywa upya kwa vile idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imekuwa chini mno kwa karibu wiki tatu sasa.

“Tumekubaliana kwa pamoja kwamba wakati umefika kufanya utathmini upya kwa sababu idadi ya maambukizi inapungua. Jinsi watoto watakavyokaa darasani bila kukaribiana ndiyo bado ni changamoto,” akasema.

Wanaomlaumu kwa kutapatapa wanasema Wizara ya Elimu inafaa kuwa na msimamo thabiti kuhusu mwelekeo ambao elimu inafaa kuchukua.

“Wizara muhimu kama hii ya Elimu ambayo hutegemewa na mamilioni ya Wakenya haifai kutapatapa. Tunahitaji msimamo thabiti kuhusu masuala yote. Lazima tuwaandae watoto wetu kisaikolojia kama watarudi shuleni Novemba au Januari,” Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu elimu, Bi Florence Mutua alisema wakati kulipokuwa na kikao mapema mwezi huu.

Hata hivyo, wadau wengine wamemtetea Prof Magoha na kusema misimamo yake huongozwa na ushauri kutoka kwa Wizara ya Afya kuhusu hali ya janga la corona ilivyo nchini.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Bw Wilson Sossion, serikali awali ilikuwa imetangaza shule zitafunguliwa Januari 2021 kwa sababu wataalamu wa afya walisema maambukizi yangefika kileleni kati ya Septemba na Oktoba.

TAHARIRI: Pendekezo la vyuo laonyesha ubinafsi

NA MHARIRI

MJADALA kuhusu kurejelea masomo kabla ya Januari mwaka huu, unaibua maswali mazito kuhusu wadau wa sekta ya kibinafsi.

Wamiliki wa shule za Kibinafsi pamoja na vyuo, wamemlaumu Waziri wa Elimu, Profesa Gerorge Magoha kwa kutangaza kwamba hakuna taasisi yoyote ya elimu itakayofunguliwa mwaka huu.

Awali, waziri alikuwa amesema huenda vyuo vingelifunguliwa Septemba.Lakini alipokuw aakibadili msimamo huo, alisema baada ya ukaguzi, ilikuwa wazi kuwa ni vyuo vichache ambavyo vilikuwa vimetimiza masharti ya kukabili maambukizi ya Corona.Chama cha Vyuo Binafsi (Kapco) kinasema vyuo vingi vina viwanja na majengo yanayoweza kuwa na wanafunzi wengi bila ya kuvunja kanuni hizo.

Nao wale wa chama cha shule za kibinafsi (Kepsa), wanasema walimu wengi wanahangaika na baadhi wamejiua kwa kukosa mishahara ya miezi kadhaa.

Kwa hivyo, wasimamizi wa taasisi hizo wanasema ingekuwa vyema kama serikali itawaruhusu wamiliki shule na vyuo vya kibinafsi kuendelea na masomo kuanzia Septemba.Maombi hayo yanaonekana kuwa yanayotolewa bila ya kuzingatia uhalisia wa mambo.

Vyuo na shule za kibinafsi husomesha watoto wa Wakenya, ambao wengi wao wameathirika kiuchumi tangu janga la Corona litokee.Mzazi aliye na mtoto katika shule au chuo cha kibinafsi, ni Mkenya ambaye anajali afya ya mwanawe sawa na yule aliye na mtoto katika shule ya umma.

Kumwambia amwache mwanawe wa shule ya umma nyumbani kisha yule aliye shule ya kibinafsi asome, ni ubaguzi. Mfumo wa elimu nchini haujabagua kwamba kuna elimu ya wanafunzi wa taasisi za kibinafsi na mwingine wa zile za umma. Pili, itaonyesha kuwa hajali afya ya mwanawe bali masomo.

Elimu haina mwisho, mtu anaweza kusoma wakati wowote, bora kuna uhai na hali inaruhusu kufanya hivyo. Kama uchunguzi uliofanywa na serikali unaonyesha kwamba mijengo mingi inaendelea kutumika kama vituo vya kuzuilia watu wanaoshukiwa kuambukizwa virusi vya Covid-19.

Kuiharakisha serikali iruhusu watu wa taasisi za kibinafsi kuendelea na masomo wakati kama huu, kunaonyesha wahusika wanasahau kwamba elimu inahusisha watoto, ambao takwimu za hivi punde zinaonyesha hata wao wako katika hatari ya kuuawa na Corona.

Saidieni shule za kibinafsi zisifilisike, Magoha awarai wazazi

WIZARA ya Elimu imewarai wazazi wenye uwezo kifedha kuwasaidia walimu wa shule za kibinafsi, ili shule hizo zisifilisike kutokana na janga la virusi vya corona.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, alisema wazazi wajitolee kukubaliana na shule za kibinafsi ambako wanao wanasomea kuhusu jinsi wanaweza kuchangia gharama za mahitaji ya shule wakati huu zimefungwa.

Walimu wengi katika shule hizo hawajakuwa wakipokea mishahara tangu Machi wakati shule zilifungwa kutokana na virusi, huku shule nyingine zikihofiwa kufungwa kwa sababu kuna madeni yanayostahili kulipwa.

Akizungumza Jumamosi alipokagua Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Asumbi, Kaunti Ndogo ya Rangwe, Kaunti ya Homa Bay kuhusu kiwango cha kujiyayarisha kwake, waziri alisema shule hizo huwa zinawaajiri zaidi ya walimu 135,000 ambao wako katika hatari ya kupoteza ajira, ikiwa waajiri wao wataamua kuzifunga shule kutokana na ukosefu wa fedha.

“Wazazi wanapaswa kuungana kuhakikisha kuwa shule hizo hazisambaratiki kutokana na hali iliyopo,” akasema.

Na George Odiwuor

Corona yakoroga masomo

NA WANDERI KAMAU

WANAFUNZI wote wa shule za msingi na upili watalazimika kurudia madarasa mwaka ujao, baada ya serikali kufutilia mbali ratiba ya masomo mwaka huu kutokana na janga la corona.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, alitangaza pia kwamba, kutotokana na mashauriano baina ya wadau hakutakuwa na mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) mwaka huu.

Matumaini kwamba shule zingefunguliwa ifikapo Septemba, au angalau watahiniwa kuruhusiwa kurejea shuleni sasa yametokomea kwa kuwa maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kuongezeka, na yanatarajiwa kufika kileleni Septemba.

Taasisi za elimu ya juu pekee ndizo zitaanza kufunguliwa kwa zamu wakati huo, kwa mujibu wa waziri.

Akihutubu jijini Nairobi jana, Prof Magoha alisema maamuzi hayo ya Jopo Maalum la Wataalamu yalimridhisha Rais Uhuru Kenyatta.

“Maagizo haya yatafuatwa na shule zote. Watoto wote ni sawa humu nchini. Hakuna tofauti kati ya mtoto wa (shule ya) umma, kibinafsi wala kimataifa,” akasema Prof Magoha.

Wanafunzi waliokuwa wamesajiliwa kufanya mtihani wa KCSE mwaka huu ni 752,836 huku wale waliosajiliwa kufanya mtihani wa KCPE wakiwa milioni 1.2.

“Ikiwa tungeruhusu wanafunzi wa Darasa la Nane kufanya mtihani wa KCPE mwaka huu, ingemaanisha jumla ya wanafunzi 438,490 hawangepata nafasi katika Kidato cha Kwanza. Kando na hayo, ingekuwa vigumu kuhakikisha wanafunzi hawakaribiani, kulingana na kanuni zilizotolewa na Wizara ya Elimu ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona,” akasema Prof Magoha.

Alieleza kuwa, sababu nyingine ya kuahirisha mitihani ya kitaifa ni kwamba, ingekuwa vigumu kwa wanafunzi walio katika Darasa la Saba na Kidato cha Tatu kukamilisha mihula iliyobaki kwa muda mfupi uliosalia.

“Wanafunzi hao wamepoteza mihula miwili mwaka huu. Je, wangewezaje kukamilisha mihula hiyo katika mwaka 2021 pekee? Hilo halingewezekana,” akasema.

Sababu nyingine ya hatua hiyo ni kuwa, ikiwa wanafunzi wangeruhusiwa kusafiri kurejea katika shule zao kwa kuabiri magari, hilo lingewaweka kwenye hatari ya kuambukizwa na kusambaza virusi hivyo.

Hatua hii itakuwa pigo kwa walimu wa shule za kibinafsi na wale wanaoajiriwa na bodi za usimamizi wa shule ambao wengi wao hawajapokea mishahara tangu Machi. Wadau wa elimu waliozungumza katika kikao hicho cha wanahabari walieleza kuridhika na hatua hiyo ya serikali.

“Usalama wa watoto na walimu shuleni ni muhimu. Kwa hivyo, Wakenya wanafaa kuunga mkono uamuzi huu. Raia wote na wazazi hakikisheni watoto wakiwa nyumbani wako salama hadi wakati watarudi shuleni,” akasema Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Bw Wilson Sossion.

Kauli hii iliungwa mkono na mwenzake wa Chama cha Walimu wa Sekondari (KUPPET), Bw Akello Misori ambaye alisisitiza kutakuwa na changamoto kubwa endapo maambukizi ya corona yatazidi watoto wakiwa shuleni.

Mwakilishi wa shule za kibinafsi katika kamati hiyo, Bi Mutheu Kasanga alisema mashauriano yataendelezwa kuhusu jinsi walimu wa shule za kibinafsi na wale wa bodi za usimamizi wa shule watakavyosaidiwa shule zikiwa zimefungwa.

Kuhusu vyuo vikuu na anwai, Prof Magoha alisema wizara hiyo itatoa mwongozo kuhusu tarehe ambapo taasisi hizo zitafunguliwa. Kulingana na waziri, Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) vilevile litatoa ratiba mpya kuhusu mitihani katika taasisi hizo.

Magoha amrushia Uhuru kiazi moto cha kufungua shule

Na FAITH NYAMAI

UAMUZI kuhusu lini shule zitakapofunguliwa, sasa umo mikononi mwa Rais Uhuru Kenyatta.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, Jumatano alisema kutokana na mashauriano na wataalamu wa afya, imetambuliwa kuna uwezekano mkubwa idadi ya watu wanaoambukizwa corona itafikia upeo wake Septemba.

Rais alikuwa ameambia Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na idara nyingine zinazoshiriki katika juhudi za kupambana na virusi vya corona, watafute jinsi watoto wanavyoweza kurudi shuleni kuanzia Septemba.

Jana, Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman alitangaza idadi kubwa zaidi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa kwa siku moja.

Watu 307 walipatikana na virusi hivyo na kufikisha idadi ya wagonjwa hadi 6,673.

Idadi ya waliopona ilifika 2,089 baada ya wagonjwa 50 kuruhusiwa kwenda nyumbani. Hata hivyo, idadi ya waliofariki ilifika 149 baada ya mgonjwa mwingine kufariki dunia.

Kwa kuzingatia takwimu za sasa, Prof Magoha alisema itakuwa vigumu kuamua shule zote zifunguliwe Septemba kwani imetabiriwa maambukizi yataanza kupungua Januari mwaka ujao.

“Kuna maelewano tumefanya na hilo litatangazwa na yule anayesimamia mikakati yote (Rais) kwa hivyo tusubiri hadi atakapohutubia nchi,” akasema.

“Mnamo Jumatatu, Julai 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta atatoa tangazo rasmi kuhusu ni lini shule zitafunguliwa,” aliongeza waziri Magoha.

Akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa sekta ya elimu katika taasisi ya ukuzaji wa mitaala (KICD), Profesa Magoha alisema wizara haitaweka afya ya wanafunzi hatarini.

Alisema msimamo wa wadau, wakiwemo wazazi na magavana ni kwamba, shule hazifai kufunguliwa hadi maambukizi yatapoanza kupungua.

Mkutano wa jana ulihudhuriwa na maafisa wa vyama vya walimu vya Knut na Kuppet. Chama cha wahadhiri wa vyuo vikuu (Uasu), chama cha walimu wwanawake (Kewota), chama cha walimu wakuu wa shule za sekondari (Kessha) na chama cha walimu wakuu wa shule za msingi (Kepsha) miongoni mwa vingine.

Mjadala kuhusu ni lini shule zinafaa kufunguliwa umekuwa ukiendelea tangu Juni.

Mitihani ya kitaifa tayari imeahirishwa hadi Aprili 2021.

Rais Kenyatta alikuwa ameagiza wizara ya elimu kufanya maandalizi ya shule kufunguliwa Septemba. Kama sehemu ya maandalizi, Profesa Magoha alisema shule zitapatiwa maski 24 milioni zitakazogawiwa wanafunzi.

Waziri Magoha pia amesema kila shule itakuwa na matangi ya maji kuwezesha wanafunzi kunawa mikono mara kwa mara.

Magoha asisitiza mitihani ya kitaifa ingalipo mwaka huu

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha angali anasisitiza kuwa watahiniwa wa mitihani ya kitaifa – KCPE na KCSE – wataifanya mwishoni mwa mwaka huu wa 2020.

Ingawa hivyo, amesisitiza kuwa hawezi kuitaja tarehe kamili ya kufunguliwa kwa shule.

“Ikiwa hali itakuwa mbaya, basi shule zinaweza kusalia zimefungwa hata kwa mwaka mmoja. Hili ni janga ambalo limekumba ulimwengu mzima,” amesema Magoha.

Ameongeza kwamba shule zikifunguliwa walimu wataanza kutekeleza silabasi sehemu ambazo waliachia Machi 15.

“Hii ni kwa sababu masomo ya sasa kupitia mitandao ni ya ziada tu na sio wanafunzi wote wanaofaidi,” amefafanua Prof Magoha.

COVID-19: Magoha abadili kalenda ya masomo

Na CHARLES WASONGA

LIKIZO ya mwezi Agosti itafupishwa kwa majuma mawili, vipindi vya masomo kuendeshwa kwa saa nyingi na likizo fupi ya muhula wa pili kufupishwa kwa siku nne.

Hizi ni baadhi ya hatua ambazo Wizara ya Elimu inapanga kuchukua kukabiliana na athari za janga la Covid-19 kwa kalenda ya masomo shule zitapofungiliwa jinsi inavyotarajiwa Juni 2020.

Katika stakabadhi iliyowasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, Wizara hiyo inasema kuwa hatua hizo ni baadhi ya mikakati ya kufidia muda ambao wanafunzi walipoteza baada ya mlipuko wa virusi vya corona.

Vilevile, mabadiliko hayo kwa kalenda ya masomo yanalenga kuwawezesha wanafunzi kukamilisha silabasi.

Waziri wa Elimu George Magoha alisema janga la Covid-19 limeathiri masomo ya wanafunzi 15 milioni katika shule za msingi, shule za upili lakini akaelezea matumaini kuwa mtaala wa masomo utakamilishwa.

“Tumefanya marekebisho kadhaa katika kalenda na masomo na hivyo tuko na imani kuwa walimu wetu watakamilisha silabasi kwa wakati,” Profesa Magoha akaeleza.

Hii ni ithibati tosha kuwa Serikali haina nia ya kuahirisha mitahani ya kitaifa ambayo imeratibiwa kufanywa mwishoni mwa mwaka 2020.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Baraza la Kitaifa la Mitahini (KNEC) Desemba 20, 2019, Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) unapasa kuanza Novemba 2 na kikamilishwa Novemba 3. Na Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KSCE) imepangiwa kuanza Novemba 7 na kukamilishwa rasmi mnamo Novemba 30.

Kumekuwa na hofu kuhusu hatima ya mitahani hiyo mlipuko wa virusi vya corona ulipochangia kufungwa kwa shule mnamo Machi 17, wiki tatum kabla ya kukamilika kwa muhula wa kwanza.

Hatua hiyo imesababisha watahiniwa kupoteza muda mwingi wa masomo ya kawaida ya darasani.

Japo, Wizara ya Elimu, kupitia Taasisi ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) imekuwa ikiendesha vipindi vya masomo mitandaoni, redioni na kwenye runinga ya Edu TV, imebainika kuwa idadi kubwa ya wanafunzi, hasa kutoka jamii za kipato cha chini, wameachwa nje.

Vilevile, Wizara ya Elimu imesema kuwa ratiba ya masomo katika shule za kutwa za upili pia itafanyiwa mabadiliko ili vipindi vya masomo viendeshwe kwa saa nyingi.

Hii ina maana kuwa wanafunzi watahitajika kuripoti shuleni mapema na kurejea nyumbani kuchelewa, majira ya jioni.

“Sawa na sekta zingine nchini, Covid-19 imeathiri pakubwa sekta ya elimu ikiwemo ratiba ya masomo,” Profesa Magoha akasisitiza.

SEKTA YA ELIMU: Magoha atoe mipango thabiti ya mageuzi katika vyuo vikuu

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Waziri wa Elimu Profesa George Magoha ya kupiga marufuku mwenendo wa vyuo vikuu vya umma kubuni mabewa sehemu mbalimbali nchini sio geni.

Vilevile, sio mara ya kwanza kwa Waziri huyo, watangulizi wake, kuviamuru vyuo hivyo vifutilie mbali kozi ambazo hazisaidii kufanikisha mipango ya maendeleo yaliyotangazwa na serikali.

Itakumbukwa kwamba mnamo mwaka 2017 aliyekuwa Waziri wa Elimu Fred Matiang’i (sasa Waziri wa Usalama wa Ndani) aliviamuru vyuo hivyo vikome kuanzia mabewa mapya na kuapa kufunga yale aliyoyataja kama “feki”.

Na alipokuwa akisoma bajeti ya kitaifa Juni 2019 aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich alitangaza kuwa serikali inapanga kuviunganisha baadhi ya vyuo vikuu kando na kufunga mabewa kadhaa.

Alitaja hatua hiyo kama sehemu ya mageuzi ambayo serikali inapania kutekeleza katika sekta ya vyuo vikuu katika mwaka huu wa kifedha wa 2019/2020.

Hii ni baada ya kubainika kwamba baadhi ya vyuo vikuu haviwezi kujisimamia kwa sababu ya kupungua kwa ufadhili kutoka kwa serikali ya kitaifa, kupungua kwa idadi ya wanafunzi, uhaba wa vifaa vya mafunzi na wahadhiri waliohitimu.

Lakini akihutubu alipofungua rasmi kongamano kuhusu elimu ya vyuo vikuu jijini Nairobi mapema wiki hii, Profesa Magoha hakufichua mikakati ambayo wizara yake imetekeleza kufanikisha mabadiliko yaliyotangazwa awali na mawaziri wenzake.

Ni muhimu kwa Waziri huyu pia kutangaza hatua ambayo wizara yake imepiga kwamba kwa mfano, kahakikisha kuwa kozi ambazo zimetajwa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) kama zinafaa.

Vile vile, Magoha anapaswa kutoa mipango ya serikali katika kufadhili elimu ya vyuo vikuu vya umma nchini kwani vyuo hivi vinakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha. Kwa mfano, mapema wiki hii, Chuo Kikuu cha Kenyatta kililazimika kukopa Sh450 milioni kutoka kwa benki baada ya kushindwa kuendesha baadhi ya mipango yake.

Hii ndiyo maana mwaka 2019 manaibu chansela wa vyuo vikuu vya umma waliitaka serikali kuongeza karo inayotozwa wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali.

Baraza la Manaibu Chansela lilipendekeza wanafunzi hao wawe wakilipa karo ya mafunzo ya Sh48,000 kila mwaka badala ya Sh16,000 wanazolipa sasa, pendekezo ambalo lilipingwa vikali na wanafunzi.

Hii ni kwa sababu tangu 2016 idadi ya wanafunzi wanaojifadhili wenyewe (self-sponsored) imepungua kwa kiwango kikubwa baada ya idadi ya wanafunzi wanaopata alama ya C+ kwenda juu kupungua. Awali, vyuo vikuu vya umma vilikuwa vikivuna hela nyingi kutokana kwa tapo hili la wanafunzi.

Mwishoni mwa 2019 Katibu Mkuu wa Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) Constantine Wasonga aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kwamba vyuo hivyo vinakabiliwa na changamoto ya kifedha kiasi cha kushindwa kuwasilisha michango ya wahadhiri kwa hazina ya Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) na ya pensheni (NSSF).

Isitoshe, aliiambia wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly kuwa kuwa kufikia Aprili mwaka huu vyuo hivyo havikuwa vimewasilisha jumla ya Sh481.3 milioni kwa mashirika ya akiba na mikopo ya (Saccos) hali ambayo imeathiri uwezo wa wahadhiri kupata mikopo ya kujiendeleza.

Badala ya Profesa Magoha anapaswa kutoa mpango madhubuti kuhusu ufadhili wa elimu ya vyuo vikuu, badala kutangaza marufuku kiholela.

Magoha na wenzake waitwa bungeni

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha, Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) Nancy Macharia sasa wametakiwa kufika mbele wa wabunge kuelezea hali iliyochangia kuondolewa kwa walimu Kaskazini Mashariki ya Kenya.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi Jumanne alisema watatu hao sharti wafike kibinafsi mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu wiki hii na wala wasiwatume wawakilishi wao.

Huku akitaja suala hilo kama la dharura na lenye umuhimu wa kitaifa, Bw Muturi aliitaka kamati hiyo kuwahoji watatu hao ili iwasilishe ripoti bungeni Jumanne juma lijalo.

“Hili ni suala nzito na lenye umuhimu wa kitaifa. Kwa hivyo, linapasa kushughulikia kwa dharura na ripoti iwasilishwe bungeni na kwa Wakenya Jumanne wiki ijayo,” akasema.

Bw Muturi alimwagiza mwenyekiti wa kamati hiyo Julius Melly kuhakikisha kuwa Profesa Magoha na Dkt Macharia wameelezea kamati yake ikiwa uamuzi huo uliidhinishwa na Bodi ya TSC.

“Tunataka kujua ikiwa ni kweli kwamba asasi moja ya serikali ilifanya maamuzi bila kuzingatia sheria ya taratibu. Au ikiwa TSC ilichukua uamuzi huo bila kushauriana na wizara ya Elimu au Idara ya Polisi,” akasema.

Bw Muturi alitoa amri hiyo kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Wajir Magharibi Ahmed Kolosh aliyetaka maelezo kuhusu sababu iliyopelekea TSC kuwahamisha zaidi ya walimu 1,000 wasio wenye kutoka kaunti za Wajir, Garissa na Mandera.

Bw Kolosh aliyedai kuwasilisha viongozi wa kisiasa kutoaka eneo zima la kaskazini mashariki alilalamika kuhamishwa kwa walimu hao kutaathiri eneo hilo kielimu.

“Tunataka kujua vigezo vilivyotumika kuwahamisha walimu hao na ikiwa Inspekta Jenerali wa Polisi alifahamishwa. Hii kwa sababu hatua hiyo sasa imeathiri masomo katika shule zetu na haswa utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu (CBC),” akasema mbunge huyo.

Mwezi Januari, TSC iliwahamisha walimu zaidi ya walimu 1,000 wasio wenyeji wa kaunti za WajiR, Garissa na Mandera kufuatia uvamizi wa kigaidi uliowalenga.

Hii ni baada ya wahalifu waliodaiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabaab kuvamia kuwaua walimu watatu katika kituo cha Kamuthe, kaunti ya Garissa.

Hata hivyo, viongozi wa eneo hili wakiongozwa na magavana Ali Korane (Garissa), Ali Roba (Mandera) na kiongozi wa wengi bunge Aden Duale walipinga hatua hiyo wakisema imelemaza masomo katika shule za umma maeneo hayo.

UoN: Pigo kwa Magoha

Na CHARLES WASONGA

PROFESA Stephen Kiama ataendelea kuhudumu kama Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) baada ya mahakama kukataa ombi la Waziri wa Elimu George Magoha la kutaka uteuzi wa Kiama ufutiliwe mbali.

Waziri Magoha aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Masuala ya Ajira na Mahusiano ya Leba akitaka uteuzi wake wa Profesa Isaac Mbeche kama kaimu Naibu Chansela udumishwe.

Alisema Jaji wa mahakama hiyo, Maureen Onyango, alipotoshwa na Profesa Kiama alipotoa amri kwamba aendelee kuhudumu kama Naibu Chansela baada ya kuteuliwa na Baraza la Chuo hicho chini ya uongozi wa Profesa Julia Ojiambo.

Lakini Alhamisi, Jaji Onyango ameamuru kuwa kesi hiyo isikizwe Ijumaa katika kikao ambapo wawakilishi kutoka pande zote inatarajiwa watahudhuria. Aliorodhesha kesi hiyo kama ya dharura.

Kwenye kesi aliyowasilisha, Magoha alisema kuwa wadhifa wa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi bado uko wazi.

“Mahakama inafaa kuondoa amri iliyotoa Jumatatu ili Waziri aweze kuteua naibu Naibu Chansela na Msaidizi wa Naibu Chansela ili chuo kiweze kuendelea na shughuli muhimu za usimamizi. Mahakama isipotoshwe na Prof Kiama kwamba yeye ndiye mkuu wa taasisi hiyo,” zikasoma stakabadhi ambazo waziri aliwasilisha mahakamani na wakili wa Profesa Magoha ambaye ni Evans Monari.

Profesa Magoha alisema amri ya Jaji Onyango iliyotolewa Jumatatu itaathiri utendekazi wa chuo, wakati huu ambapo kuna pengo katika afisi ya Naibu Chansela na baraza la chuo hicho.

“Licha ya kuwepo kwa pengo hilo, Prof Kiama ameendelea kujiwasilisha kama Naibu Chansela na kufanya mabadiliko makubwa kuhusu usimamizi wa chuo na kuhadaa umma,” akasema wakili Monari.

Mnamo Jumatatu mahakama hiyo ilisitisha uamuzi wa waziri Magoha wa kubatilisha uteuzi wa Profesa Kiama kama Naibu Chansela.

Jaji Onyango alitoa uamuzi huo baada ya Profesa Kiama kuwasilisha kesi ya kupinga hatua ya Profesa Magoha kufutilia mbali uteuzi wake na badala yake kumteua Profesa Isaac Mbeche kama Kaimu Naibu Chansela.

Kufikia sasa Profesa Kiama ametangaza teuzi mpya katika taasisi hiyo, na kumtuma Profesa Mbeche kwa likizo.

Katika taarifa aliyotoa Januari 21, 2020, Profesa Kiama alimteua Profesa Madara Ogot, ambaye ni Msaidizi wa Naibu Chansela (DVC) anayesimamia Utafiti, kuwa kaimu Msaidizi wa Naibu Chansela anayesimamia Masuala ya Fedha.

Maprofesa wenye tajiriba pevu wanahitajika vyuoni – Magoha

Na LAWRENCE ONGARO

VYUO vikuu vya masomo vinastahili kuwa na maprofesa waliohitimu ili kuboresha elimu ya juu.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesema hadhi ya Profesa ni ya kuheshimiwa na ni wale waliotambulika ndio wanastahili kupata cheo hicho.

Amehimiza umuhimu wa kufanya utafiti katika masomo na nyanja tofauti na kuwashauri wanaoendesha utafiti huo kuwa wenye ujuzi wa hali ya juu katika masomo.

“Hakuna haja ya ya kuwa na maprofesa wengi katika Chuo kimoja kwa vile wana gharama kubwa. Kwa hivyo, ni vyema kuwa na wasomi wachache ambao wana ujuzi wa kuendeleza chuo kwa njia ifaayo,” amesema Prof Magoha wakati wahitimu mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) mjini Thika wamefurahia sherehe – mahafali – ya kufana Ijumaa, Desemba 6, 2019.

Wahitimu wamekuwa 5,000 wa na hafla imeandaliwa katika uwanja wa Happy Valley Pavilion eneo la Landless mjini Thika.

Waziri amesema mabadiliko makubwa yanastahili kuonekana katika masomo ya juu ili kuwa na ubora wa elimu nchini.

“Hakuna haja ya kuwa na kabila moja kwenye Seneti ya vyuo vikuu kwani hiyo ni njia moja ya kukuza ukabila masomoni,” amesema waziri huyo.

Kuhusu mwongozo wa serikali wa karo za shule za upili, amesema wakuu wa shule hawastahili kuongeza karo kwa vyovyote vile.

Amesema wahitimu wote wanaopata vyeti vya uzamifu ni sharti wawe wamefanya utafiti wa kutosha na wawe wamekaguliwa vilivyo katika masomo yao.

Alisema serikali imesitisha ufunguzi wa vyuo vipya kote nchini.

“Vyuo vilivyoko kwa sasa hata ni vingi kupita kiasi. Kote nchini kuna vyuo 79.

Kuchagua ajira

Amesema mzazi yeyote atakayepata kuwa ana shida ya karo kuongezwa apige ripoti mara moja.

Amewahimiza wahitimu hao wasiwe watu wa kuchagua ajira.

” Kama ningekuwa mmoja wenu ningefanya hata kazi ya kuendesha trekta. Kwanza kubali kufanya kazi yoyote iliyoko mbele yako halafu jipange polepole,” amesema Prof Magoha.

Mwenyekiti wa bodi ya Chuo cha Mount Kenya Prof Simon Gicharu, amewashauri wahitimu hao kujiamini wakati wowote wanapotekeleza wajibu wao.

“Msikubali kuvunjwa moyo kwa yale mnayotenda. Mtu unastahili kuwa mkakamavu na wa kujiamini,” amesema Prof Gicharu.

Amesema Chuo hicho kimewafadhili wanafunzi watano kufanya utafiti kwa gharama ya kitita cha Sh4 milioni huku pia Sh460 milioni zikitengwa kuwatuza watafiti waliofanikiwa katika utendakazi wao.

Amesema wataendelea kutilia mkazo maswala ya mafunzo na utafiti ili kuboresha maswala ya elimu chuoni humo.

Wakati wa hafla hiyo wahitimu 10 wamepokea shahada za uzamifu. Halafu 119 walihitimu kwa shahada ya uzamili.

Wahitimu wengine walipata vyeti katika shahada za biashara, elimu, uandishi, na maswala ya uchumi huku wakipata vyeti vya digrii na vya diploma.

Wakati wa hafla hiyo naibu Chansela mpya Prof Peter Wanderi amekaribishwa kuchukua mahali pa Prof Stanley Waudo ambaye atastaafu rasmi ifikapo Aprili mosi , 2020, baada ya kutumikia chuo kikuu hicho kwa miaka 11 mfululizo.

Magoha awataka wazazi Migori waache kulialia baada ya eneo kutajwa ‘ngome ya wizi’

Na DERICK LUVEGA

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha amepuuzilia mbali madai ya Muungano wa Wazazi katika Kaunti ya Migori kwamba amepitiliza katika kusema kwamba eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yenye mazoea ya watahiniwa kufanya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.

Akiongea Alhamisi asubuhi katika Shule ya Chavakali, Kaunti ya Vihiga, waziri Magoha amesema ni wazi mwaka 2018 matokeo ya watahiniwa katika baadhi ya vituo Migori yalifutiliwa mbali kwa sababu ya kubainika kulikuwa na udanganyifu.

“Mwaka 2018 matokeo katika vituo Uriri na Nyatike. Hatutaki hilo litokee tena,” amesema Magoha wakati akijionea jinsi ambavyo mchakato mzima wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne unavyoendelea.

Mtihani huo ulianza rasmi Jumatatu wiki hii na umeingia siku yake ya nne.

 

Magoha kuongoza kikao kuhusu mitihani

Na CECIL ODONGO

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha leo Jumatatu anatarajiwa kukutana na wadau katika sekta ya elimu kupanga namna ya kuendesha mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE inayonukia, mkutano utakaofanyika katika Kenya School of Government eneo la Kabete.

Prof Magoha anatarajiwa kukutana na Washirikishi wa elimu kutoka maeneo yote nchini pamoja na wakurugenzi wa elimu katika kaunti na kaunti-ndogo kote nchini.

KCPE inatarajiwa kuanza Oktoba 28 hadi Oktoba 31 huku KCSE ikianza Novemba 4 hadi Novemba 27.

Wanafunzi 1,089,671 wanatarajiwa kufanya mtihani wa KCPE huku wengine 698,935 wakifanya mtihani wa KCSE.

Baadhi ya mambo yanayotarajiwa kujadiliwa ni namna mitihani hiyo itakavyosafirishwa, usalama wa karatasi za mitihani na namna ya kuzuia visa vya udanganyifu.

Aidha, waziri huyo amekuwa akitoa onyo kali kwa walimu wakuu wanaoshirikiana na baadhi ya watu kisha kuwahadaa wanafunzi kuchangisha fedha kununua mitihani hiyo kwamba wataadhibiwa vikali.

Watahiniwa njiapanda kuhusu amri ya Magoha

Na WANDERI KAMAU

HATIMA ya maelfu ya wanafunzi wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne katika baadhi ya shule za kibinafsi nchini haijulikani, baada ya serikali kuapa kufunga shule ambazo zitapatikana kutozingatia kanuni zifaazo za ujenzi.

Wanafunzi hao wanajitayarisha kufanya mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) baadaye mwaka huu.

Kwenye agizo kwa wakuu wa elimu wa kanda na wakurugenzi wa elimu katika kaunti, Katibu wa Elimu Dkt Bellio Kipsang alisema kuwa serikali itafunga shule zote za kibinafsi ambazo hazijasajiliwa na Wizara ya Elimu.

Agizo hilo linafuatia mkasa uliotokea Jumatatu iliyopita katika Shule ya Msingi ya Precious Talent jijini Nairobi, ambapo wanafunzi wanane walifariki baada ya mojawapo ya madarasa kubomoka.

Tangu mkasa huo, wizara hiyo imeanza msako mkali, ambapo shule kadhaa zimefungwa kwa kutozingatia kanuni zifaazo za ujenzi.

Baadhi ya shule ambazo zimefungwa kufikia sasa ni Shule ya Msingi ya St Catherine Bombolulu iliyo katika mtaa wa Kibra, Pama Academy iliyo katika mtaa wa Kangemi kati ya nyingine.

“Shule zote ambazo hazijasajiliwa na Wizara ya Elimu zitafungwa na wanafunzi wake kuwekwa katika shule za umma,” akasema Katibu.

Vilevile alisema kuwa shule ambazo zitapatikana kutokuwa na miundomsingi bora zitafungwa na kunyang’aywa vyeti vyao vya usajili.

Kulingana naye, shule nyingine ambazo zitafungwa ni zile ambazo zitapatikana kuongeza idadi ya wanafunzi wake kuliko kiwango ambacho zilikubaliwa.

Kutokana na hayo, aliwaagiza wakuu hao kufanya ukaguzi wa shule hizo katika maeneo wanakosimamia na kuwasilisha ripoti kwake kabla ya Oktoba 25, ambapo shule hizo zitafungwa.

Wizara hiyo pia imetangaza hatua kali kwa shule ambazo hazijawaajiri walimu ambao wamesajiliwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC).

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema kuwa operesheni hiyo itaendelea hadi pale watakapohakikisha kuwa kila mwanafunzi anasomea katika mazingira salama.

Hata hivyo, wadau mbalimbali wa elimu wamesema kuwa ingawa hatua hiyo ni nzuri, wizara inapaswa kuwashirikisha walimu na wazazi ili kuhakikisha haiwaathiri wanafunzi katika matayarisho ya mitihani yao.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Kenya (KEPSHA), Bw Nicholas Gathemia aliunga mkono hatua hiyo, akisema kuwa maisha ya watoto yanapaswa kupewa kipaumbele.

“Mpango huu ni mzuri, kwani unalenga kuhakikisha kuwa maisha ya wanafunzi yanalindwa. Maisha yao ni muhimu kuliko mitihani ya kitaifa. Mpango huu haupaswi kuonekana kumlenga yeyote kwani hakuna mtoto wa kibinafsi ama wa umma,” akasema.

Ni hali inayoonekana kuzua mgawanyiko kwani baadhi ya wazazi katika Shule ya Msingi ya Precious Talent wameiomba wizara kubatilisha uamuzi wake wa kuifunga.

Mtihani wa KCPE utaanza hapo Oktoba 28 hadi Oktoba 31 huku ule wa KCSE ukianza Novemba 4 na kumalizika Novemba 27.

Magoha apiga marufuku shughuli zisizo za masomo muhula wa tatu

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu George Magoha amepiga marufuku shughuli zozote zisizohusiana na masomo wakati wa muhula wa tatu kama sehemu ya mikakati ya kuzuia visa vya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.

Akiongea katika katika Shule ya Wanafunzi wanaoishi na ulemavu ya Machakos, Machakos School for the Physically Disabled Profesa Magoha alisema shughuli za maombi kwa watahiniwa, shule kupokea wageni mbalimbali kwa ajili ya kutoa hotuba za uhamasisho au wazazi kutembelea shule hazitaruhusiwa.

“Na walimu wakuu pia wanaonya dhidi ya kusaidia katika utekelezaji wa wizi wa mitihani au kutowachulia hatua walimu watakaoshiriki uovu huo,” akasema Waziri alipokuwa akikagua shughuli inayoendelea ya mafunzi kwa walimu kuhusu ufundishaji wa mtaala mpya wa umilisi na utendaji (CBC).

“Nafahamu kwamba baadhi ya walimu wakuu wanapanga kuiba mitihani, lakini nawaonya wasithubutu kwani tumeweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wanakamatwa,” Profesa Magoha akaongeza.

Waziri huyo pia aliwaonya watahiniwa dhidi ya kushawishiwa kushiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa ya darasa la nane (KCPE) na ile ya kidato cha nne (KCSE).

“Wale watakaopatikana na hatia ya kuiba mitihani watakamatwa na kusukumwa jela, sawa na wahalifu wengine. Vilevile, matokeo ya wale watakahusika udanganyifu wa mtihani yatafutuliwa mbali,” akasema.

Profesa Magoha alisema kuwa mwezi wa Novemba utakuwa mwezi mahsusi wa mtihani kwani wanafunzi wa madarasa mengine watafunga kwa likizo ndefu mnamo Oktoba 28.

Mtihani wa mwaka 2018 wa KCPE unaanza Novemba 1 na kuisha Novemba 3.

Kwa upande mwingine ule wa KCSE utaanza Novemba 7 hadi Novemba 30, 2019.

Magoha adinda kutetea wanavyuo wanaokosa hafla

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha ametetea wahadhiri wa vyuo vikuu kwa kuondoa wanafunzi ambao hawajafuzu wasishiriki kwenye mahafali.

Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali kwamba wahadhiri huwafanya kukosa kufuzu kutoka vyuoni kwa sababu zisizo na msingi.

Chuo Kikuu cha Moi ndicho kimeibuka kuwa na malalamishi mengi zaidi ya aina hii, ikiwemo majuzi ambapo mamia ya wanafunzi waliokuwa wanatarajia kushiriki kwenye mahafali walikuta hawamo kwenye orodha.

Ijumaa, chama cha wanafunzi (KUSO) kilitishia kwenda mahakamani kushtaki chuo kikuu cha Moi baada ya wanafunzi 700 kukosekana kwenye orodha hiyo huku wenzao wakiwa wanatarajiwa kufuzu mnamo Alhamisi wiki hii.

Jana, Prof Magoha alisema wahadhiri wana mamlaka ya kuamua iwapo mwanafunzi amehitimu kufuzu au la.

“Tunakaa kana kwamba nia yetu kuu ni kuwapa wanafunzi vyeti. Hivi sasa kuna wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi ambao wanalalamika kuwa majina yao hayamo kwenye orodha ya mahafala. Suala muhimu si la jina lako kuwa kwenye orodha, hii inahusu mhadhiri wako kutosheka kwamba umepata ujuzi wa kutosha ili ufuzu,” akasema Prof Magoha.

Aliwataka wakufunzi wawe na ujasiri wa kuwaambia wanafunzi kwamba hawatafuzu kwa ajili ya suala hili au lile.

Wakati huo huo, wizara ya elimu imetangaza kuwa muundo wa mtaala utakaoongoza mafunzo katika taasisi za mafunzo ya walimu kuhusu mtaala mpya utakuwa tayari kati ya wiki tatu na miezi mitano ijayo.

Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa warsha ya chama cha walimu wakuu wa vyuo vya elimu nchini inayoendelea katika hoteli ya Travellers mjini Mombasa, Prof Magoha aliwashauri walimu hao kutia bidii katika kuelimisha walimu watarajiwa mtaala huo.

“Ili kuwaelimisha watoto wetu kutumia mfumo mpya mnapaswa kwanza kuelewa nini kinahitajika kabla yenu kupitisha ujuzi huo kwa walimu ambao watafundisha madarasani,”alisema.

Zaidi ya walimu wakuu 300 kutoka kwa vyuo vya serikali na vile vya kibinafsi, chama cha walimu,Taasisi ya kushughulikia mtaala walikongamana Mombasa kwa kusudi la kuangazia mtaala mpya.

Waziri huyo aliwashauri walimu kujivunia kazi wanayoifanya.

“Najivunia kuwa mwalimu kwa sababu ya watu wengi wakubwa kama madaktari wa upasuaji waliopitia mikononi mwangu. Wananitambua kuwa mimi si mtu rahisi lakini wanajuwa kuwa ni ugumu wangu uliowafanya wao kufaulu katika masomo yao,” akasema.

Kongamano hilo ambalo ni la nane mada yake ikiwa kuboresha mwalimu wa karne ya 21, linapanga kuangazia masuala ibuka katika mafunzo ya walimu katika mtaala mpya.

Mwenyekiti wa chama cha vyuo vikuu, Bw Barasa Wafula alisema kongamano hilo limefanyika wakati muafaka ambapo serikali imeanzisha mtaala mpya.

Muungano huo pia ulihakikishia serikali kuwa utaiunga mkono katika kutekeleza mfumo mpya wa elimu.

Aliomba serikali kuajiri walimu zaidi ili wanafunzi wapokee elimu bora.

Vilevile, Bw Wafula alisisitiza kuwa ni muhimu walimu wanaofanya diploma kupokea mafunzo ya mtaala mpya ili wawe tayari kuyatumia.

Sossion apata fursa ya kuponda Magoha kwenye kizaazaa

Na WANDERI KAMAU

KIZAAZAA kilizuka Alhamisi kwenye kikao cha Kamati ya Bunge Kuhusu Elimu baada ya Waziri wa Elimu Prof George Magoha kujibizana vikali na Mbunge Maalum Bw Wilson Sossion.

Bw Sossion, ambaye ni mwachama wa kamati hiyo, alimtaka Prof Magoha kueleza mikakati ambayo wizara yake imeweka ili kukabili ukosefu wa usalama katika shule za msingi katika wadi ya Kiunga Mashariki katika Kaunti ya Lamu.

Kikao hicho kilikuwa kikiendelea katika Ukumbi wa County Hall, jijini Nairobi, ambapo waziri huyo alikuwa akiieleza kamati hiyo kuhusu hali ya elimu nchini.

Swali hilo lilikuwa limeulizwa na Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruveida Obo, ambaye pia ni mwanachama wa kamati hiyo, akilalama kuwa hali hiyo imeathiri shughuli za masomo katika karibu shule zote za wadi hiyo.

“Ningemtaka waziri kuelezea hatua ambazo serikali inachukua kuimarisha usalama katika shule hizo, kwani hakuna shughuli za masomo ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miaka minnne kufikia sasa,” akauliza Bi Obo.

Mbunge huyo alisema kuwa wale ambao wameathiriwa sana na hali hiyo ni watu wa jamii ya Waboni, aliodai idadi yao ni chini ya 1,000 kote nchini.

Alipoelekezewa swali hilo, Prof Magoha alisema kuwa hawezi kulijibu, kwani suala la usalama wa taasisi zozote, hata zile za elimu ni jukumu la Wizara ya Usalama wa Ndani.

“Ndugu Mwenyekiti (Sossion) naomba kutojibu swali hilo, kwani hilo si jukumu langu. Kuna maafisa wa usalama na ujasusi ambao wako katika eneo hilo lakini huwa hawaripoti kwangu. Hivyo siwezi kulijibu swali hilo,” akasema Prof Magoha.

Hata hivyo, Bi Obo alilalamika, akimtaka huyo waziri kufafanua zaidi, kwani hali ya usalama katika maeneo yanayopakana na wadi hiyo hayana matatizo yoyote ya kiusalama.

“Ningemtaka waziri kutufafanulia zaidi, kwani wadi jirani ya Basuba haina tatizo hilo. Walimu huwa wanatoka katika eneo hilo kuja katika wadi ya Kiunga kwa shughuli za kimasomo, lakini huwa wanarejea makwao. Ningemtaka kueleza mbona hali ni tofauti katika wadi hizo mbili zinazopakana,” akarai mbunge huyo.

Akionekana kumuunga mkono Bi Obo, Bw Sossion alimshinikiza waziri kutoa ufafanuzi kamili kuhusu inavyofanya wizara yake, akisema kuwa duniani kote, jukumu la usalama wa taasisi za elimu huendeshwa na wizara hiyo.

Bw Sossion pia aliungwa mkono na Mbunge Mwanamke wa Kaunti ya Migori, Dkt Rosemary Odhiambo, ambaye pia alimrai Prof Magoha kueleza wizara inavyofanya.

Waziri alipandwa na mori, akisisitiza kuwa hatajirudia. “Siwezi kurudi kwa swali hilo!” akafoka Prof Magoha.

Akionekana kuridhika, japo shingo upande, Bw Sossion alimrai Bi Odi kutafuta ufafanuzi zaidi kutoka kwa wizara za elimu na usalama wa ndani kuhusu yule anayepaswa kusimamia usalama.

Kwa kuona hali ilivyokuwa, Bw Sossion aliamua kuendelea na maswali mengine.

Wadau mbalimbali wa elimu wamekuwa wakilalamika kuwa imekuwa vigumu kufikia misimamo ya pamoja na waziri huyo, wakimtaja kutekeleza yale anayoamini yanafaa.