Knec kuanza kusahihisha KCSE wiki hii

Na VICTOR RABALLA

SHUGHULI ya kusahihisha Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka huu itaanza wiki hii huku serikali ikianzisha mpango wa kusawazisha kalenda ya masomo.

Katibu wa Wizara ya Elimu Dkt Julius Jwan alisema, wasahihishaji watawasili Nairobi kuanzia mwishoni mwa Ijumaa kujiandaa kwa zoezi hili huku karatasi ya mwisho ya mtihani huo ikitarajiwa kufanywa Alhamisi wiki ijayo.

Dkt Jwan alisema hayo alipoongoza shughuli ya kufunguliwa kwa konteina na usambazaji wa karatasi za mtihani katika kaunti ndogo ya Bondo jana.

Alielezea matumaini kuwa Wizara ya Elimu itakomboa muda wa masomo uliopotea wakati wa janga la Covid-19. “Kuhusu mitihani iliyofanywa mapema, tunawatarajia wasimamizi wa usahihishaji na manaibu wao kusafiri hadi Nairobi kuanzia Ijumaa wiki hii ili waanze kujiandaa kwa shughuli hiyo muhimu,” akasema.

Dkt Jwan alisema baada ya maandalizi hayo, wasahihishaji wengine watakaoshiriki katika zoezi hilo watasafiri hadi Nairobi.Kulingana na ratiba ya mtihani wa KCSE 2020 iliyofanyiwa marekebisho, karatasi za mwisho za mtihani zitafanywa mnamo Aprili 21.

Karatasi hizo ni pamoja na Sayansi Kimu (Home Science), Sanaa na Maumbo, “Power Mechanics”, “Umeme”, Uchoraji, Teknolojia ya Usafiri wa Angani na Mafunzo ya Kompyuta.

Dkt Jwan vile vile, aliwaonya walimu, wazazi na watahiniwa dhidi ya kupotoshwa na walaghai wanaosambaza karatasi feki za mitihani ya KCSE katika mitandao ya kijamii.

Alisema wale waliokamatwa wiki jana ni miongoni mwa watu hao ambao wamekuwa wakiitisha pesa kutoka kwa watu wasiong’amua ukweli kuhusu uhalali wa karatasi hiyo.

Mmoja wa waliokamatwa ni mwanamke mmoja mkazi wa kaunti ya Machakos.

“Kufikia wakati watahiniwa walikuwa wakifanya mtihani wa Hisabati, karatasi ya Pili, wiki jana, karatasi ghusi zilikuwa zikisambazwa. Kwa bahati mbaya baadhi ya wenzetu walinaswa katika mtego huo na wakatuma pesa kwa walaghai hao,” Dkt Jwan akasema.

Katibu huyo wa Wizara alitoa hakikisho kuwa Wizara ya Elimu imeziba mianya yote ya kufanikisha wizi wa mtihani huo.

MARY WANGARI: Udangayifu katika mitihani ni tishio kwa jamii nzima

NA MARY WANGARI

MITIHANI ya kitaifa imekuwa ikiendelea nchini huku ikiandamwa na sarakasi za kila aina ikiwemo madai ya udanganyifu.

Wakenya wameshuhudia visanga tele kuhusu mitihani ya KCPE na KCSE ambapo Waziri wa Elimu Profesa George Magoha ameripotiwa akisisitiza kuwa hakuna uvujaji wowote wa mitihani hiyo.

KCPE ilikumbwa na sakata ikidaiwa kuwa maswali katika mtihani wa Kiingereza yalidondolewa kutoka jaribio moja lililokuwa limechapishwa mnamo Februari, mwezi mmoja tu kabla ya mtihani huo kuanza.

KCSE haikunusurika huku baadhi ya wazazi na walezi wakiripotiwa kuwalipa watu wawafanyie watoto wao mitihani kikiwepo kisa cha mwalimu aliyechapisha karatasi ya mtihani kwenye mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Ni jambo la kuvunja moyo sana kuona sekta ya elimu nchini ikielekea kuzama licha ya mageuzi yaliyoanzishwa na Dkt Fred Matiang’i. alipokuwa waziri wa elimu.Enzi hizo, wazazi wangefanya chochote hata kama ni kinyume na sheria, ilmradi tu kuhakikisha watoto wao wanapita mitihani na kujiunga na taasisi za kifahari.

Si ajabu baada ya mageuzi hayo, matokeo katika shule nyingi tajika yalianza kudorora ghafla na kuzigeuza dhihaka, huku shule ambazo hata hazikuwa zikisikika zikianza kutia fora.

Kwa kiasi fulani, inaeleweka ni kwa nini wazazi na walezi hujitahidi kwa hali na mali kuhakikisha watoto wao wamenyakua nafasi katika shule nyota za sekondari zinazowahakikishia nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu na hatimaye kupata kazi.

Hata hivyo, kutokana na udanganyifu katika mitihani, wanafunzi wengi werevu hasa kutoka mashinani hufungiwa nje na kukosa fursa ya kujiunga na vyuo huku nafasi zao zikitwaliwa na wasiozistahili.

Matokeo yake ni kuwa na wafanyakazi wasiofaa katika taaluma muhimu kama vile udaktari, uhandisi, ualimu, watumishi wa umma, wanasiasa na waundaji sera, huku sekta ya utafiti na uvumbuzi nchini ikiathiriwa pakubwa.

Udanganyifu katika mitihani hauathiri sekta ya elimu pekee bali jamii kwa jumla.Inahuzunisha kuwa jamii haithamini tena uadilifu na badala yake imegeukia kutukuza ukora ambao matokeo yake ni dhahiri kupitia kuongezeka kwa mafarakano ya kimahusiano, kifamilia ikiwemo ndoa kuvunjika.

Aidha, baadhi ya maafisa wanajinyakulia nyadhifa kuu kwa kutumia vyeti vya kughushi!Tunahitaji mfumo wa mitihani unaoangazia talanta, ujuzi na ari ya kila mtahiniwa kibinafsi ili kuboresha sekta ya elimu nchini na kuondoa ushindani usiokuwa na maana.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

KCSE: Afisa abambwa na Magoha akisaidia watahiniwa kwa udaganyifu

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha kwa mara nyingine ametoa onyo kali kwa watahiniwa wa mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE kuhusu kushiriki udanganyifu katika zoezi hilo linaloendelea.

Prof Magoha alitahadharisha Jumanne kwamba watakaoshiriki wataadhibiwa kisheria.

Waziri huyo pia alitoa onyo kwa walimu na wasimamizi wa mitihani watakaohusishwa na udanganyifu, sheria haitakuwa na budi ila kuchukua mkondo wake.

“Leo Jumanne, tumekamata msimamizi katika shule moja eneo la Migori akisambaza karatasi za mitihani kabla ya wakati wa kuuandika kuwadia. Atafikishwa kortini afunguliwe mashtaka,” akatangaza Prof Magoha, akitoa onyo kali kwa wahusika.

Waziri huyo hata hivyo alihakikishia taifa kuwa mitihani ya KCSE kote nchini ni salama.

“Watahiniwa watakaojaribu kutumia mbinu za hila kupita mtihani, tutawaadhibu kisheria. Hatutasaza mhusika yeyote,” akaonya.

Mtihani huo wa kitaifa kidato cha nne ulianza juma lililopita, Ijumaa, Machi 26, siku chache baada ya ule wa darasa la nane, KCPE kukamilika.

Tetesi ziliibuka kuwa KCPE ilishuhudia udanganyifu. Waziri Magoha hata hivyo alipuuzilia mbali madai hayo.

Kalenda ya masomo 2020 ilisambaratishwa na mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini, ambapo wanafunzi walisalia nyumbani mwaka mmoja.

Aidha, walirejea Januari 2021. Serikali ilichukua hatua ya kufunga shule zote na taasisi za elimu ya juu nchini kama njia mojawapo kusaidia kudhibiti maenezi ya virusi vya corona.

Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa corona Machi 2020.

Watahiniwa wa KCPE na KCSE walirejea shuleni Oktoba 2020 ili kujiandaa kuandika mitihani hiyo iliyoratibiwa kufanyika Machi 2021.

KCSE: Magoha aamrisha polisi wapokonywe simu wasifanikishe udanganyifu wa mitihani

NA MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha Jumatatu ametoa amri kuwa maafisa wa polisi wanaolinda harakati za mtihani wa KCSE unaoendelea kote nchini wawe wakipokonywa simu zao za mkononi ili wasishirikishe visa vya udanganyifu.

Prof Magoha akiongea katika Makao makuu ya Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini alikofika kunyapara usambazaji wa nakala za mtihani huo alisema kuwa maafisa wa polisi wanaoshiriki zoezi hilo wako na uwezo mkuu wa kuhatarisha uadilifu wa mitihani nchini.

Aidha, waziri huyo alipiga marufuku usafirishaji wa mitihani kwa kutumia magari ya kibinafsi akiteta kuwa “kunao walimu wengine ambao wanatumia huduma hata za matatu kuusafirisha hadi mashuleni mwao.”

Alisema kuwa hali kama hiyo inafanya harakati za kulinda uadilifu wa mitihani ziwe ngumu akiongeza kuwa “ninaamrisha magari rasmi ya shule yawe tu ndiyo yatatumika katika usafirishaji huo.”

Aliteta kuwa matatu ikitoka steji moja hadi nyingine ikipitia kwa kila aina ya chochoro huwezi ukawa na uhakika kwamba visa vya udanganyifu havitekelezwi “na baadhi ya wakora tulio nao katika zoezi hili.”

Alisema kuwa maafisa wa polisi wako na uwezo wa kupiga picha nakala za mtihani na kisha kuzituma kwa mitandao ya udanganyifu na kisha kufikia wanafunzi katika shule zingine kwa kuwa hawaanzii kufanya mitihani hiyo kwa wakati mmoja.

Baadhi ya njama ambazo walio katika mtandao huo wa wizi wa mitihani hutekeleza ni kuchelewesha usambazaji wa nakala hadi baadhi ya mashule ndio kwenye zilifunguliwa ziwe zimepigwa picha na kisha kutumwa kwao.

Hapo ndipo nakala hizo zikishapokelewa hujibiwa harakaharaka na walimu au wengine ndani ya njama hiyo na kupewa wanafunzi ili shule zao zing’are katika matokeo au watoto wao wapate alama za juu.

Prof Magoha alisema kuwa serikali iko macho hasa katika kanda za Magharibi na Nyanza ambako alisema kumezuka habari za ujasusi kuwa njama ya kuiba mtihani huo zinashirikishwa na baadhi ya walimu.

“Tuko na Mwalimu mkuu katika shule moja ya ukanda wa Magharibi ambaye ameshukiwa kuwa na njama ya kupenyeza nakala za kusaidia wizi wa mtihani…Ameamrisha walimu wote waondoke kutoka shule hiyo ndio abakie na mazingara mwafaka ya kuendeleza njama hiyo. Anafaa aaibike sana na nimpe onyo hapa kuwa hataweza kushirikisha ukora huo,” akasema.

Alisema kuna walimu wengine watatu katika Kaunti ya Migori ambao “sijui kama ni wazimu wako nao au ni nini kinawasukuma” kwa kuwa “nao wamefuatiliwa na kutambuliwa kuwa wako na njama hiyo ya kusaidia udanganyifu.”

Prof Magoha aliapa kuwa wote walio katika ajira ya serikali watakaonaswa wakishirikisha wizi wa mtihani huo watafutwa kazi na washtakiwe sambamba na wengine wote ambao watathubutu kushiriki njama hizo.

Mkurugenzi wa Elimu ukanda wa Kati Bi Margaret Lesuda alitoa tahadhari kuwa maradhi ya Covid-19 yashafika katika shule nyingi hapa nchini kwa makali ya ukatili “na ambapo wikendi tu hii imepita tulipoteza walimu wawili wakuu katika shule za msingi huku kwa ujumla tukiwa tumepoteza zaidi ya walimu 15 hadi sasa.”

Alisema kuwa ni suala la dharura kwamba watahiniwa pamoja na wanaoshirikisha zoezi hilo wazingatie masharti ya kiafya hasa katika uvaaji wa maski, kuweka umbali unaopendekezwa na wizara ya afya kutoka mtahiniwa mmoja hadi mwingine, kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji au sanitaiza na pia kuwajibikia dalili za kuugua kwa uadilifu na dharura.

Alisema kuwa “mtihani ambao unaweza ukahatarisha maisha ya watoto au ya wanafunzi na wadau wengine ni hatari hivyo basi kila aina ya tahadhari itekelezwe.”

Mitihani ya kitaifa ya Gredi 4 yaanza Jumatatu

FAITH NYAMAI na DERICK LUVEGA

MITIHANI ya kutathmini wanafunzi wa Gredi ya Nne inaanza Jumatatu Machi 8. Mitihani hiyo itakuwa sehemu ya matokeo yatakayotumiwa kuamua iwapo watajiunga na shule ya upili baada ya gredi ya sita au la.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha amewataka walimu kuchukulia shughuli hiyo kwa umuhimu mkubwa kwa kuwa itakuwa na asilimia 20 ya alama za mitihani itakayozingatiwa katika gredi ya sita.

Mitihani hiyo imebuniwa na Baraza la Taifa la Mitihani Kenya (Knec) na wanafunzi watatathminiwa na walimu wao na matokeo kuwekwa kwenye tovuti ya Knec.

Shule zinatakiwa kumaliza mitihani hiyo na kuweka matokeo katika tovuti hiyo kati ya Machi 8 na Machi 19.

Prof Magoha alisema kwamba Knec itatoa vifaa vinavyohitajika kwa shule zote kufanikisha shughuli hiyo.

“Tayari KNEC imetoa mwongozo kuhusu mitihani hii muhimu ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mtaala mpya wa Competency Based Curriculum (CBC),” alisema.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC, Mercy Karogo alisema maandalizi ya mitihani hiyo yamekamilika.

“Vifaa vya kufanya tathmini hiyo viko tayari kwa kuwa shule zitavipata katika tovuti na kutekeleza shughuli hiyo kwa kufuata mwongozo uliotolewa,” alisema Dkt Karogo.

Mitihani ya gredi ya nne, tano na sita inatarajiwa kujumuisha asilimia 60 ya matokeo ya kitaifa ya wanafunzi hao watakapohitimu gredi ya sita.

Mtihani wa gredi ya nne utakuwa wa kwanza chini ya CBC jinsi lilivyoshauri Jopokazi kuhusu utekelezaji wa mtaala huo mpya wa elimu.

“Shule zinahitajika kuwasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi ambao kwa sasa wako gredi ya nne kwa KNEC ambayo itakuwa asilimia 20 ya tathmini ya mwisho katika gredi ya sita,” unaeleza mwongozo huo.

Miongoni mwa masomo ambayo yatashirikishwa ni Hisbati, Kiingereza, Kiswahili, Lugha ya Ishara, Sayansi na Teknolojia, Kilimo, Muziki na Sanaa, Somo la Jamii, Somo la Kidini na Afya.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Walimu (TSC), Bi Nancy Macharia aliwataka maafisa wote wa elimu kusaidia shule kuhakikisha walimu hawatatiziki kupata vifaa vya kutumia kutoka kwenye tovuti ya Knec.

“Ninataka kusisitiza kuwa mitihani hii itafanywa wakati wa kawaida wa masomo na wanafunzi hawafai kuwekwa katika mazingira tofauti na waliyozoea katika darasa kila siku,” alisema.

Wanafunzi wafeli majaribio ya KCPE kwa wingi

Na DAVID MUCHUNGUH

WANAFUNZI wengi walianguka mtihani wa majaribio wa Darasa la Nne waliofanya mwaka jana na kuibua wasiwasi kuhusu iwapo wamejiandaa vyema kwa mtihani wa mwisho watakaofanya siku 48 kuanzia Jumatano.

Wanafunzi wa shule za umma walifanya vibaya zaidi katika mtihani huo wa majaribio kuliko wale wa shule za kibinafsi.

Baraza la Taifa la Mitihani (KNEC) linasema kuanguka huko katika shule za umma kulisababishwa na kufungwa kwa shule wakati baadhi ya wanafunzi wa shule za kibinafsi walikuwa wakisoma kupitia mtandao.

Mtihani huo ulifanywa na wanafunzi wa darasa la nane, gredi ya nne na kidato cha nne waliporejea shuleni Oktoba mwaka jana. Wanafunzi wa madarasa mengine walirudi shuleni Januari 4 mwaka huu.

“Moja ya matokeo ya utafiti wa Knec ni kwamba wanafunzi wengi wa darasa la nane walifeli. Hii inathibitishwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawakupata asilimia 50 katika masomo mengi,” inaeleza ripoti.

Wanafunzi walio maeneo kame na yale masikini walipata matokeo mabaya. Knec inahusisha hatua hii na ukosefu wa tekinolojia ya habari na mawasiliano kuwawezesha kusoma wakati shule zilikuwa zimefungwa kutokana na janga la corona.

“Ni wazi kuwa wanafunzi wengi wa darasa la nane hawajafikia viwango vinavyohitajika katika masomo husika,” inaeleza ripoti hiyo.

Mitihani hiyo ilifanywa na kusahihishwa na walimu ambao walituma alama ambazo wanafunzi walipata kwa Knec kuchanganua.

Wanafunzi wengi walifeli hisbati na somo la ishara, Kiingereza na Kiswahili.

WANTO WARUI: Huenda wanafunzi wengi wakakosa mitihani ya KNEC

Na WANTO WARUI

Baraza la mitihani nchini (KNEC) linapanga kuwapa wanafunzi wa Gredi ya 1-3 na madarasa ya 5-7 majaribio ya kutathmini kiwango chao cha uelewa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, 22-01-2021.

Hii ni kutokana na hali iliyowakumba wanafunzi ya kukaa nyumbani kwa kipindi cha miezi tisa kutokana na mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Kwa mujibu wa KNEC, wanafunzi wote wanatarajiwa kuwa shuleni ili waweze kufanya majaribio hayo ambayo tayari yameandaliwa na KNEC na kutumwa shuleni kupitia njia ya mtandao.

Hivi ni kusema kuwa KNEC inatarajia kila shule nchini iwe na uwezo wa kupata majaribio hayo, iweze kusimamimia wanafunzi wafanye kisha isahihishe kazi hiyo na kutuma majibu yaliyotolewa na wanafunzi kwake (KNEC) kupitia njia iyo hiyo ya mtandao. Hali ilivyo sasa, kuna wanafunzi wengi ambao bado hawajarudi shuleni na hali zao za kuendelea na masomo hazijulikani.

Miongoni mwao ni wasichana ambao walipata mimba, wengi wao sasa wakiwa katika hatua za mwisho za kupata watoto. Kwao itakuwa vigumu mno kuweza kufikia majaribio haya.

Shuleni nako changamoto ni nyingi. Wanafunzi waliorudi shuleni bado hawana madawati ya kutosha. Wengine wanasomea chini ya miti kulikojaa upepo na mavumbi.

Shule nyingi nchini hazina umeme wala kompyuta. Haitakuwa jambo rahisi kwa walimu kuweza kusimamia mitihani hii katika hali kama hizi.Kuna baadhi ya shule ambazo zilifungwa kutokana na mafuriko ya maziwa kama vile Baringo, Nakuru na Naivasha.

Sehemu kubwa ya wanafunzi hao huenda bado iko nyumbani kutokana na hali ya umaskini ya wazazi. Ni wazi kuwa wanafunzi kama hawa hawatapata fursa ya kufanya majaribio haya.

Wati ambapo wanafunzi wa kidato cha nne, darasa la nane na gredi ya nne walipokuwa shuleni, KNEC iliweza kuandaa majaribio kama haya. Ingawaje shule zilijizatiti kusimamia, kuna shule nyingine ambazo hazikutoana matokeo sahihi.

Kufikia sasa, KNEC bado haijaweza kutoa matokeo ya tathmini la Gredi ya 4 kwa walimu.Hivi ni kusema kuwa, majaribio yanayotarajiwa kuanza leo yatakuwa na changamoto kwa walimu na wanafunzi wenyewe.

Kuna wale ambao wataweza tu kufanya nusu ya majaribio hayo huku wengine wakishindwa kabisa. Ijapokuwa KNEC inafanyiza zoezi hili ikiwa na nia nia ya kutathmini kiwango cha uelewa wa wanafunzi tu, itakuwa si vyema kuwakosesha wanafunzi wengi kiasi hiki kushiriki zoezi kama hili.

Mpango huu wa KNEC wa kutathmini wanafunzi kwa njia hii ungefaulu zaidi endapo serikali kufikia sasa ingekuwa ishatekeleza ahadi yake ya awali ya kupeana kompyuta kwa wanafunzi. Hali ilivyo sasa, itabidi wanafunzi wengi waikose mitihani hii.

Umuhimu wa mazingira mazuri kwa watahiniwa

Na SAMMY WAWERU

MAANDALIZI ya mitihani ya kitaifa ya elimu ya msingi KCPE na sekondari KCSE yanaendelea kote nchini.

Jumatatu, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alisema kila kitu kiko shwari linapokuja suala la mitihani hiyo inayotarajiwa kuanza baada ya wiki mbili zijazo.

Ule wa darasa la nane, KCPE utaanza Oktoba 28 na kukamilika Oktoba 31.

Nao wa kidato cha nne, KCSE unatarajiwa kuanza Novemba 4 na kutia nanga Novemba 27.

Akizungumza katika Taasisi ya Mafunzo ya Serikali (KSG), Waziri Magoha alihakikishia taifa kuwa hakutakuwa na visa vyovyote vya udanganyifu wa mitihani wala ufichuzi.

“Hakutakuwa na mtihani utakaofunguliwa kabla ya asubuhi ya siku ya siku,” alisema.

Hata hivyo, Prof Magoha alisema kuna baadhi ya ‘wahuni’ wenye nia ya kutekeleza udanganyifu wakati wa shughuli hiyo ya kitaifa na alionya kuwa serikali itawachukulia hatua kali kisheria.

Wizara ya Elimu, Usalama wa Ndani na Mawasiliano na Teknolojia (ICT) zitashirikiana kufanikisha shughuli hizo za kitaifa.

Walimu 180,000 wameteuliwa kulifanikisha. Pia, kuna helikopta kadhaa zilizotengewa shughuli hiyo hususan kwa maeneo yenye ubovu wa barabara na kushuhudia utovu wa usalama.

Mbali na wizara ya elimu, asasi zingine husika ni baraza la kitaifa la mitihani (Knec) na tume ya waajiri walimu nchini, Tsc.

Wakati serikali inajifunga kibwebwe kuandaa shughuli hiyo ya kitaifa, watahiniwa wanaendelea kubukua vitabu. Kila sekunde, dakika na saa inapoyoyoma, wanahakikisha wanajikumbusha waliyopokea darasani, kuanzia darasa la kwanza hadi nane.

Bi Muriuki Wanjugu, ambaye ni mwalimu mkuu wa shule binafsi ya Kiangai Blessings View Academy iliyoko Kaunti ya Kirinyaga anasema katika muda wa lala salama, wanafunzi wanapaswa kuwa na ukuruba na mlahaka mzuri na walimu.

“Asijalishwe na iwapo ni mwalimu wa somo lake au la, kila mwalimu aliye shuleni anamosomea amfanye rafikiye wa karibu na kuuliza maswali,” anashauri Wanjugu.

Kulingana na mwalimu huyo kipindi hiki kisiwe cha kujipa presha, ila kiwe cha kujikumbusha aliyosoma mtahiniwa awali na kujua mapya ambayo pengine hakuyawahi.

“Ninahimiza walimu pia wawapokee wanafunzi wanaofanya mitihani na wajitolee kuwaandaa sambamba,” anaeleza mwalimu huyo, akishauri kwamba huu ni muda wa kutumia karatasi za mitihani ya kitaifa iliyopita ili kujua muundo wa maswali.

Kujadiliana

Isitoshe, watahiniwa wanatakiwa kuwa katika makundi ya kujadili maswali na masomo mbalimbali, kinachowalemea waalike mwalimu au walimu kuwatatulia.

“Makundi yatawawezesha kubadilishana mawazo na hata maarifa,” anasisitiza mwalimu Pauline Nyaguthii, wa Kiambu.

Kwa upande wao wazazi wanapaswa kujua kuwa huu si wakati wa kuwapa watahiniwa majukumu ya kinyumbani, kama vile kuosha vifaa vya kula, nguo na kuwaagiza kuenda shambani. Wanahimizwa kushirikiana nao kuhakikisha wanapata muda wa kutosha kudurusu vitabu na hata kupumzika.

“Kipindi hiki wanafunzi wanaofanya mitihani ya kitaifa kama wazazi tunapaswa kuwapenda zaidi na kuwaepusha na kazi za nyumbani,” anasema Elizabeth Wakaguyu ambaye ni mzazi wa mtahiniwa anayetarajiwa kufanya KCPE 2019.

Kiwewe wanachoshuhudia watahiniwa chini ya mfumo wa zamani wa 8-4 – 4 hususan wakati wa mitihani ya kitaifa, huenda kikafikia kikomo mfumo mpya wa CBC ukitekelezwa kikamilifu.

Aidha, CBC ni mfumo unaojiegemeza zaidi katika uamilifu na kukuza vipaji vya wanafunzi badala ya kuwatathmini kupitia mitihani ambayo ni maswali ya yaliyofundishwa darasani.

TAHARIRI: Mawaziri wamulike zaidi maafisa wa KNEC

NA MHARIRI

KWA mara nyingine, ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Wizara za Elimu na Usalama wa Ndani na Baraza la Mitihani ya Kitaifa nchini (KNEC) katika maandalizi ya mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) ni hatua nzuri ambayo itasaidia kukomesha visa vya wizi wa mitihani ambavyo vilikuwa vimeongezeka pakubwa nchini.

Kwa mara ya kwanza, Wakenya sasa wameanza kuwa na imani na vyeti vinavyotolewa na KNEC wakijua kwamba, alama kwenye vyeti hivyo inasheheni uwezo na maarifa sambamba ya mtahiniwa.

Ni jambo la kutia moyo kwamba, Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akifuatilia kwa karibu maandalizi hayo na kutoa onyo kali kwa magenge ambayo yamegeuza mitihani hiyo kuwa kitega uchumi.

Kwa miaka mingi, magenge hayo yamekuwa yakishirikiana na maafisa laghai katika KNEC kusambaza mitihani ya kitaifa mapema kabla ya wakati wake.

Mazingira ya sasa bila shaka yatawatuza wanafunzi wanaotia bidii masomoni na kuwanyima wale wanaotumia fedha kujipatia nafasi ya kujiunga na vyuo taasisi za elimu ya juu.

Isitoshe, hatua hii itakomesha hali ambapo wanafunzi wanazoa alama za juu na kuteuliwa kusomea kozi kama vile udaktari na uhandisi kisha wanalazimika kuzitelekeza ama kutimuliwa kabisa kutokana na ufahamu wao mdogo.

Na katika hali ambapo baadhi wamenusurika kutemwa, matokeo ni kwamba, kumekuwa na wahandisi na madaktari ambao hawakufinyangwa wakaiva vyema.

Wanapoajiriwa, wanaonyesha utepetevu mkubwa pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu ya kimsingi mahali pao pa kazi.

Tunaunga mkono matamshi ya mwenyekiti wa KNEC Prof George Magoha kwamba, wakati wa wanafunzi kupata alama ‘A’ za kishenzi umewadia. Kila mwalimu na mzazi ahakikishe wanafunzi wao wamepewa mazingira bora ya kujinoa ili kukabiliana na maswali darasani bila usaidizi wa aina yoyote kwa njia ya udanganyifu.

Sekta ya elimu imepanuka pakubwa katika muda wa miaka 15 iliyopita, hasa kutokana na sera ya elimu msingi bila malipo iliyoanzishwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki.

Serikali ya sasa imewezeka zaidi katika sekta hiyo kiasi kwamba, sehemu kubwa ya bajeti ya kitaifa inatengewa elimu. Juhudi hizo zote hazipaswi kuruhusiwa kuhujumiwa na walaghai wanaotaka kuvuna wasikopanda.

Na kwa maelfu ya watahiniwa ambao wanajiandaa kufanya mitihani yao ya darasa la nane na kidato cha nne, bila shaka ushauri wetu ni huu: Njia za mkato zina miiba mingi na mara nyingi hazizalishi matunda. Jiandae kikamilifu na ushindi utakuwa ni wetu. Kila la kheri.

TAHARIRI: Wadau washirikiane kufanikisha mitihani

NA MHARIRI

KAULI ya Wizara ya Elimu kwamba wazazi ndio watakaowajibika ikiwa wanao watapatikana wakijihusisha na udanganyifu wa mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) ni ya kuridhisha.

Ni tangazo linalopaswa kuungwa mkono na kila mmoja, ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu wanafunzi wamekuwa wakibebeshwa mizigo ambayo si yao. Wale ambao huwasaidia kujihusisha vitendo vya udanganyifu aghalabu huwa wanasazwa katika mchakato wa utoaji adhabu kwani wanafunzi husika ndiyo huwajibika.

Wizara pia imetangaza kwamba wakati wa mitihani hiyo, wazazi hawataruhusiwa kuwatembelea wanao- hasa wanaosomea katika shule za mabweni. Kimsingi, hii ni hatua nzuri katika kukabili visa hivyo, ila pia pana haja ya mashauriano zaidi.

Kwanza, kuwazuia wanafunzi kuonana na wazazi ama walezi wao huenda isiwe hatua ya busara kwani kuna baadhi ya hali ambazo hutokea na huhitaji uwepo wao. Katika muda huo wa mitihani, baadhi ya wanafunzi huugua au huhitaji dharura fulani maalum ambazo mzazi ama mlezi wake ndiye pekee anazielewa.

Baadhi ya wanafunzi pia hukumbwa na maradhi ya ghafla kama kifafa, hali ambazo usimamizi wa shule wanamosomea huenda ukashindwa kuelewa. Kwa hali kama hizo, si busara kwa Waziri wa Elimu Amina Mohamed kutoa uamuzi huo bila ushirikishi ufaao wa wadau husika.

Hofu kuu inatokana na hali kwamba si mara moja tumesikia visa vya wanafunzi waliougua na kufariki katika hali tatanishi, baada ya uongozi wa shule wanamosomea kutoshughulikia hali zao za kiafya.

Katika baadhi ya matukio, wanafunzi hufikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa au hata kupewa dawa zisizofaa, hivyo kuhatarisha hali zao zaidi.

Ili kuepuka matukio kama hayo, wizara inapaswa kulegeza kamba kuhusu agizo lake ili kutoa mwanya wa kushughulikia hali maalum zitakazowakumba wanafunzi. Mojawapo ya mikakati inayopaswa kuwekwa ni wizara kuwaagiza maafisa wake wanaosimamia shule mbalimbali ama vituo vya mitihani kunakili wanafunzi ambao watahitaji hali zozote za dharuta mitihani hiyo ikiendelea.

Hilo litabuni ushirikiano mzuri ambao utahakikisha kuwa pande zote mbili zinashirikiana kwa manufaa ya wanafunzi, ila si kuwaumiza.

PEPO WA MIGOMO: Shule 30 zafungwa, wanafunzi wachoma mali ya mamilioni

Na WAANDISHI WETU

PEPO ya migomo imeitembelea tena Kenya huku Waziri wa Elimu Amina Mohamed akitaja hofu ya mitihani kama kiini kikuu cha fujo zinazoshuhudiwa shule nyingi hasa za sekondari.

Katika miaka ya majuzi imekuwa jambo la kawaida kwa migomo na uharibifu wa mali katika shule za sekondari kushuhudiwa.

Waziri Mohamed alisema hayo huku shule zaidi ya 30 zikiathiriwa na migomo na mabweni kuchomwa.

Shule hizo ni pamoja na Maranda High, Kisumu Girls, Ng’iya, Ambira, Maliera, Onjiko, Otieno Oyoo, Chulaimbo, Oriwo, Ngere, Kandiege, Usenge, Barding, St Augustine Nyamonye, St Marys Girls, Mumias na Litein Boys.

Pia kuna Kitondo, Nduluku Good Shepherd Girls, Kikuumini, Kyeemundu kutoka Mashariki. Zingine ni Kathera Boys, Thuura, Mukuiru, Kisima, St Lukes na Meru.

Katika visa vya majuzi vya migomo hiyo, wanafunzi 30 wa shule ya kibinafsi ya Kenyenya katika Kaunti ya Kisii walikesha kwenye baridi usiku wa kuamkia jana baada ya shule hiyo kukumbwa na moto.

Kwa mujibu wa wanafunzi, bweni moja liliteketea wakati wanafunzi walipokuwa madarasani kwa masomo ya ziada.

Nayo shule ya Upili ya Wavulana ya Chewoyet, Kaunti ya Pokot Magharibi ilifungwa kwa muda usiojulikana baada ya bweni moja kuchomeka jana asubuhi.

Mali yenye thamani isiyojulikana iliteketea katika bweni la Longonot ambalo huwa na wanafunzi 115.

OCPD wa Kapenguria Bw Anthony Wanjuu alisema moto huo ulianza majira ya saa kumi na moja alfajiri wakati wanafunzi walipokuwa kwenye masomo ya ziada .

Katika juhudi za kukabiliana na migomo hiyo, alisema Bi Mohamed, wanafunzi watatu wa shule ya Siakago High iliyoko Kaunti ya Embu wamefungwa jela kwa mwaka mmoja huku wanafunzi 125 wa shule mbalimbali wakikamatwa kuhusiana na migomo inayoendelea.

Haya yanajiri wakati Idara ya Upelelezi (DCI) imetangaza kukusanya habari kuhusu wanafunzi wanaochochea migomo na kujaribu mali kwa lengo la kuweka rekodi ambazo zitatumiwa wakati wa maombo ya Vyeti vya Tabia Njema wanapomaliza masomo. Vyeti hivyo huhitajika na waajiri wengi.

Bi Mohamed alisema mikakati iliyowekwa kuzuia udanganyifu katika mitihani ya kitaifa imechangia pakubwa migomo hiyo. Pia ameeleza kuwa ukosefu wa nidhamu kwa jumla unachangia matukio hayo.

Waziri alieleza kuwa ripoti ya mapema ya wizara imeonyesha hilo huku akitoa mfano wa tukio katika shule ya Chalbi, Marsabit ambapo wanafunzi waliwavamia walimu ambao si wenyeji.

“Wanafunzi hao pia walimtaka mkuu wa shule kuwahakikishia kuwa watasaidia wizi wa mitihani,” alieleza, akisema jambo hilo linastahili kumtia hofu kila mmoja.

“Hii ndiyo sababu nitasafiri Nyanza kubaini chanzo cha baadhi ya shule ambazo hazijawahi kushuhudia fujo kuwa na hali hiyo sasa. Ninataka kujua ni nini kilifanyika na nini kilichochea. Ikiwa ni mitihani, basi ieleweke kuwa sote lazima tufanye bidii kupita mitihani yetu,” alisema.

Alieleza kuwa wizara inaunga mkono hatua ambazo zimechukuliwa na idara ya upelelezi nchini kuwa wanafunzi wanaojihusisha na migomo shuleni watakabiliwa na mashtaka ya uhalifu.

“Hii ni kuonya kila mwanafunzi kuanzia shule ya msingi, sekondari, vyuo vya kadri na vikuu kuwa DCI inaweka maeleo ya kila tukio la uhalifu na kuunganisha mashtaka ambayo huenda yakapendekezwa kwa kila mwanafunzi anayehusika na uhalifu,” idara hiyo ilieleza.

Idara hiyo ilieleza kuwa matukio hayo yatawaathiri wakifuta vyeti vya nidhamu njema, mbali na kuwa rekodi ya uhalifu itadumu katika maisha yao na huenda ikawazuia hata wanapotafuta ajira.

LUCY KILALO, JADSON MANDUKU NA OSCAR KAKAI

FUNGUKA: Sihitaji urembo kunyaka wahadhiri chuoni na kuwalambisha asali nipite mitihani

Na Pauline Ongaji

Ni ndoto ya kila mwanafunzi wa chuo kikuu kufanya vyema katika mtihani wake na hata kuhitimu.

Na ni ndoto ambayo Valerie anaifuata kwa udi na uvumba na ananuia kuitimiza. Hata hivyo tofauti na wanafunzi wengine wa kawaida wanaotia bidii kimasomo kuafikia ndoto hii, binti huyu anayesomea shahada ya uzamili katika masuala ya kibiashara katika chuo kikuu kimoja hapa nchini amebuni mbinu kunufaika.

Sawa na msemo wa Kiingereza “The end justifies the means,” Valerie hajali atakachofanya kiwe kibaya au kizuri, mradi apate matokeo anayotaka. Mbinu ya binti huyu ni kuwanasa wahadhiri ili wamdokezee kuhusu maswali kwenye mtihani kabla siku yenyewe.

Kwanza kabisa binti huyu mwenye umri wa miaka 33 sio wale mabinti ambao kwa viwango vya kawaida unaweza waita warembo sana. Valerie sio mmojawapo wa mabinti wanaojirembesha. Kwa hivyo ni kawaida kukutana naye akiwa ameachilia shungi la nywele na ni nadra kwake kujipaka vipodozi.

Badala yake amewekeza nguvu na rasilmali zake kwingineko.

“Nimenoa akili yangu kiasi cha kwamba hilo ndilo lango la kwanza ninalotumia kunasa windo langu kabla ya kuliingiza katika mtego wa mahaba.

Kwangu urembo ni mchuuko sana. Mtu yeyote anaweza kuwa mrembo. Siku hizi kwa mapeni kadha ya kununua vipodozi ghali na nywele za kubandika waweza shindania tuzo ya ‘slay queen’.

Nawe ukiwa hivi, ni vigumu kwa mhadhiri kukuchangamkia na kuwa na makini kwako kwani kuna wengi kama wewe. Ukishamuonjesha, basi ni hivyo anasonga na kumwendea mpumbavu mwingine kama wewe.

Badala yake nimewekeza katika akili yangu, rasilmali ya kipekee ya kuwanasa hawa wahadhiri ambao ni ada kwao kunipa alama za juu kwenye mtihani. Badala ya kununua nywele za kubandika, mimi hutumia pesa zangu kununua vitabu na kuhakikisha kuwa nahudhuria mihadhara yote muhula unapoanza.

Kadhalika mimi hufuatilia mada kuu za kimasomo kabla ya mhadhiri kuingia, kumaanisha kuwa anapoingia kufunza mimi, ni mmojawapo wa wanafunzi wachache wanaochangamkia maswali, mbinu ambayo imenisaidia kunasa wahadhiri wengi, hasa wanaovutiwa na akili ya binti badala ya masuala sahili kama vile sura na umbo la kupendeza.

Lakini mtego wangu haukomei hapo tu kwani nimehifadhi uhondo pindi nikishawakaribisha kwenye ubongo wangu ambao ni sawa na sebule ya nyumba.

Sawa na mgeni maalum, akishaingia ukumbini lililosalia ni kumvuta hadi chumbani ambapo pia nimehakikisha kuwa kibuyu cha asali kimehifadhiwa vilivyo, na nakuhakikishia kuwa pindi anapoonjeshwa sitatumia nguvu nyingi kumshawishi ashughulikie masuala yangu wakati wa mtihani.

Nilianza tabia hii nilipokuwa nikisomea shahada yangu ya kwanza ambapo katika mtihani wa mwaka wa kwanza, licha ya kutia bidii, kuna mabinti wazembe waliofanya vyema zaidi yangu kutokana na uhusiano waliokuwa nao na wahadhiri.

Natarajia kukamilisha masomo yangu mwisho wa mwaka huu ambapo tayari nishapita katika masomo ya nadharia na katika tasnifu ninayoandika kuna ishara kubwa kuwa nitapata alama ya A.

Pia najiandaa kuanza kusomea shahada ya uzamifu pindi baada ya kukamilisha masomo na mtindo utakuwa huo huo hadi mwisho”.

Mitihani ya mwigo yapigwa marufuku Baringo

Na Florah Koech

SERIKALI imepiga marufuku mitihani ya pamoja ya majaribio almaarufu ‘Mock’ katika shule za upili za Kaunti ya Baringo.

Akihutubia mkutano wa chama cha walimu wakuu wa shule za sekondari (KESHHA) mjini Kabarnet, Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo Bw Willie Machocho alihusisha mitihani hiyo na visa vya migomo shuleni.

Alisema wanafunzi wengi katika eneo hilo hugoma wakati wa maandalizi ya mitihani hiyo.

“Shule kadhaa eneo hili zimekumbwa na ghasia kwa sababu ya maandalizi ya mitihani hii. Kwa sababu hii, tunapiga marufuku mitihani yote ya majaribio katika shule zote za sekondari ili kuzuia hali hiyo,” alisema Bw Machocho.

Alitaja shule zilizogoma muhula huu kama ya wavulana ya Tenges, Reuben Cheruiyot, Maji Moto , Rosoga, Kisanana na Timboroa.

Alisema mbinu nyingine ambayo wanatumia kuzima migomo ya kila mara ni kuhakikisha walimu wakuu na manaibu wao wanaishi shuleni

Tangazo hilo lilijiri wiki mbili baada ya mali ya mamilioni ya pesa kuteketea katika bweni la shule ya wavulana ya Tenges iliyoko Baringo ya Kati. Moto huo ulizuka wanafunzi walipokuwa madarasani jioni.

Visa vingi vya migomo hushuhudiwa muhula wa pili kutokana na kile washikadau katika elimu wanahusisha na mitihani ya mwigo.

 

 

KNEC yaonya kuhusu hatari ya wizi wa mitihani kurudi

Na WANDERI KAMAU

BARAZA la Kitaifa la Mitihani (KNEC) Jumatano limeonya kuhusu kuchipuka tena kwa mtandao mkubwa wa wizi wa mitihani unaohusisha baadhi ya maafisa wake, walimu, wazazi na wanafunzi.

Imebainika kwamba walimu wanaohusika katika njama hizo wamekuwa wakipokea pesa kutoka kwa wanafunzi kwa ahadi za kuwapa karatasi za mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) itakayofanywa katika miezi ya Oktoba na Novemba 2018.

Akiwasilisha ripoti kuhusu hali ya matayarisho ya mitihani Jumatano katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaala Kenya (KICD) jijini Nairobi, Mwenyekiti wa baraza hilo Prof George Magoha alisema wako macho kuhakikisha kwamba wamesambaratisha mitandao hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba wameanza mikakati ya kijasusi ambayo itahakikisha kwamba wale ambao wanahusika katika njama hizo wamenaswa na kukabiliwa kisheria.

“Tumefahamu kwamba kuna baadhi ya walimu ambao wanawaitisha wanafunzi pesa za kuwawezesha kupata karatasi za mitihani. Lakini tunawaambia kwamba tuko macho. Uchunguzi wetu umebaini kwamba baadhi wanaitisha hadi Sh20,000,” akasema Prof Magoha.

Alisema kuwa wameimarisha juhudi zao katika usimamizi wa mitihani hiyo, kwa kuongeza maafisa wa usalama na mitambo ya teknolojia.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha kwamba walimu wakuu lazima wawepo katika ufunguzi wa kontena za mitihani. Walimu hao pia lazima wahakikishe kwamba hakuna mtu asiyetakikana anayekuwa karibu na mazingira ya kituo husika wakati mitihani hiyo inaendelea.

Kwa sasa, walimu 60 wanaendelea kuchunguzwa kwa tuhuma za kushiriki katika wizi huo mwaka uliopita.

Kwa muda wa miaka miwili iliyopita, KNEC kwa ushirikiano na idara nyingine za serikali ilifanikiwa kupunguza udanganyifu kwenye mtihani, hatua ambayo imefurahiwa na Wakenya wengi.

Wizara ya Elimu pia imeonya kwamba shule ambazo zitapatikaba kuhusika katika aina yoyote ya udanganyifu zitafungwa mara moja.

Akihutubu katika taasisi hiyo, Waziri wa Elimu Amina Mohamed alisema kwamba hiyo ndiyo itakuwa hatua pekee ya kuhakikisha kwamba wanaopaswa kusimamia mitihani hiyo wamewajibika ifaavyo

“Hatutaketi kitako kuona watu wachache wakiwaharibia watoto wetu maisha ya baadaye. Tutafunga shule hizo ili kutotumika tena kama jukwaa la kuendeleza udanganyifu,” akaonya waziri.

Mwaka uliopita, matokeo ya wanafunzi 1,200 yalifutiliwa mbali na baraza hilo baada ya kubainika kwamba walishiriki katika udanganyifu.

Mwaka huu, jumla ya wanafunzi 1,060,703 wamejisajilisha kufanya mtihani wa KCPE, huku wanafunzi 664,585 wakisajiliwa kufanya ule wa KCSE.

Kulingana na KNEC, hilo linaashiria ongezeko la wanafunzi zaidi, ikizingatiwa kwamba mnamo 2017, watahiniwa 1,002,922 waliufanya mtihani wa KCPE, huku 577,253 wakifanya mtihani wa KCSE.

Wizara pia iliahidi kufanya ukarabati wa shule ambazo ziliharibiwa na mafuriko na zitatumika kama vituo vya kufanyia mitihani, ili kuhakikisha kwamba hakuna wanafunzi ambao wanakosa nafasi ya kuufanya.

 

TAHARIRI: Majaribio ya kuiba mitihani yazimwe

Na MHARIRI

HABARI za hivi majuzi kwamba mikakati kabambe imewekwa kuiba mtihani wa kitaifa kwa shule za upili(KCSE) zinatamausha mno na ni sharti serikali iingilie kusitisha mpango huo.

Imefichuka kwamba baadhi ya wakuu wa shule za sekondari wanashirikiana na baadhi ya wazazi kukusanya hela za kununua karatasi za mtihani wa KCSE wa mwaka huu.

Baada ya mianya ya kuziba wizi wa mitihani kuwekwa, wahuni sasa wanaingilia mifumo ya ulinzi wa shule ili kufanikisha wizi huo.

Mpango wa wizi wa mitihani ni mkubwa mno na ni sharti serikali iwekeze pakubwa iwapo inataka kutangua shughuli hiyo inayoweza kuzamisha ndoto za watoto milioni 1.7 ambao watafanya mtihani huo mwezi Oktoba.

Ni hatia kubwa iwapo wanafunzi nao watafahamu kuhusu mpango huu wa wizi wa mitihani na kuendelea kushirikiana na wahuni hao na wasifanye lolote.

Mwaka 2017, Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani(KNEC) Bw George Magoha alidokeza kuwa wahuni wanafanya juhudi kuhakikisha kwamba mtihani wa KCSE 2018 unafichuliwa mapema.

Wizi wa mitihani uliripotiwa mwaka jana baada ya jaribio la kufungua masanduku yaliyotumiwa kubeba karatasi za mitihani kabla ya kuanza kufanywa.

Huku maandalizi ya mitihani yakiendelea , ikiwa imesalia miezi mitano tu, KNEC yapaswa kuchukua hatua madhubuti kuzuia wizi huo.

Yapaswa kuwa zaidi ya kuwaita maafisa wakuu katika wizara ya elimu, Tume ya Kuajiri Walimu TSC na wakurugenzi wa elimu katika kaunti kujadili maandalizi ya mitihani ya kitaifa. Mkutano huo utafanyika Mei 31 katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (KICD), Nairobi.

Prof Magoha alionya kuhusu mikakati hiyo ya wizi wa mitihani lakini pia akatahadharisha kuhusu adhabu kwa watakaopatikana.

Haijalishi kwamba walimu wamefanya juhudi zote kuwaandaa wanafunzi kufanya KCSE halafu matokeo yao yakataliwe kutokana na wizi wa kura. Huu ni ufisadi wa hali ya juu na ndio maana jinamizi hilo linaendelea kuzonga nchi.

Mbali na matokeo yao kukataliwa, wale wanaopenya kuingia vyuoni wanakuwa mbumbumbu hawawezi kumudu masomo ya chuo kikuu yanayohitaji kiwango cha juu cha kisomo. Hatimaye tunapata marubani ambao hawaifahamu kazi yao barabara, madaktari wasiomudu udaktari nk. Wizi wa mitihani ukomeshwe!

Ni tovuti ya Gazeti la Kampuni ya Nation Media Group
Mkurugenzi Mkuu: STEPHEN GITAGAMA
Mhariri Mkuu: TOM MSHINDI
Mhariri : PETER NGARE