Hatimaye mitishamba ya Covid-19 yatua TZ

Na MASHIRIKA

ANTANANARIVO, MADAGASCAR

TANZANIA hatimaye imepokea dawa ya mitishamba inayosemekana kutibu wanaougua Covid-19 kutoka kwa Serikali ya Madagascar.

Akipokea dawa hiyo Ijumaa nchini Madagascar, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Tanzania, Prof Palamagamba John Kabudi alikanusha madai kwamba Tanzania ililegea katika kupambana na janga la corona.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Tehindrazanarivelo Djacoba As Oliva alitoa wito kwa nchi za Afrika kuungana kwa pamoja kupata suluhisho la maradhi ya Covid-19.

Mnamo Mei 3, 2020, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliahidi kutuma ndege Madagascar kwenda kufuata dawa hiyo ya mitishamba.

Wakati huo Dkt Magufuli alisema kuwa amewasiliana na Madagascar baada ya kupokea barua rasmi kutoka nchi hiyo iliyoeleza kuwa wamegundua dawa ya corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema ni muhimu dawa zinazosemekana kuwa na uwezo wa kutibu zifanyiwe majaribio kwanza.

Shirika hilo lilionya huenda watu wakaona wamepata tiba na kujihisi kuwa salama ilhali wametumia dawa ambazo hazijafanyiwa majaribio.

Wakati huo huo, serikali ya Tanzania ilijitetea kwa kusitisha matangazo kuhusu hali ya corona nchini humo kwa takriban wiki moja sasa.

Matangazo hayo yalisitishwa baada ya Dkt Magufuli kutilia shaka shughuli za maabara makuu yaliyotegemewa kupima virusi hivyo.

Kulingana na Magufuli, kulikuwa na shaka kwa vile serikali ilituma sampuli za vitu tofauti kama vile papai na mbuzi, kisha ripoti zikatolewa kutoka kwa maabara kwamba sampuli hizo zilikuwa na virusi vya corona.

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu alisema kimya cha serikali kuhusu maambukizi kilitokana na hatua zinazoendelezwa kuboresha maabara ya taifa.

“Kama mnavyofahamu kuna kazi za kiufundi zinazoendelea kwa hivyo nataka niwaondolee watu hofu tu kwamba ndani ya siku chache kazi itakuwa imekamilika na hivyo tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara,” akasema.

Kitendawili cha ‘dawa’ aina ya chai ya mitishamba kutibu Covid-19 Madagascar

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

ANTANANARIVO, Madagascar

RAIS wa Madagascar Andry Rajoelina amependekeza matumizi ya ‘dawa’ aina ya chai ya mitishamba kwa wagonjwa wa Covid-19 nchini mwake.

Madai ya Rais Rajaelina kwamba ‘dawa’ hiyo, kwa jina Covid Organics (CVO), inayofanana na chai isiyo na maziwa, inawatibu wagonjwa wa Covid-19 yamevutia hisia mseto katika taifa hilo ambalo ni kisiwa kilichoko kilomita 400 kando ya pwani ya Afrika Mashariki.

Kufikia Ijumaa, Madagascar visa 128 vya maambukizi ya Covid-19 vilikuwa vimeripotiwa nchini Madagascar huku watu 82 wakiwa wamepona na hamna vifo vilivyotokea.

Hii ni kulingana na takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Hopkin, Amerika, ambacho hunakili data kuhusu ugonjwa huo.

Kwenye ujumbe kupitia Twitter, Rajoelina amewataka raia wa Madagascar kuwa na imani kwa uwezo wa ‘dawa’ hiyo kulemea virusi vya corona.

Alisema faida yote kutokana na mauzo ya ‘dawa’ hiyo yataelekezwa katika Taasisi ya Utafiti ya Madagascar (MIAR).

“Majaribio yote yamefanywa na imebainika kuwa dawa hiyo inaweza kupunguza na hata kuondoa kabisa dalili za Covid-19 kwa wagonjwa wenye virusi vyake nchini Madagascar,” shirika la habari la Africanews lilimnukuu Rais Rejoelina akisema.

Lakini kwenye taarifa, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeonya dhidi ya tiba kama hiyo likisema kufikia sasa halijaidhinisha tiba yoyote ya Covid-19.

Licha ya onyo hilo kutoka kwa WHO, idadi kubwa ya raia wa Madagascar wanafurika katika vituo ambako ‘dawa’ hiyo inasambazwa bila malipo, ingawa wengine bado wana tashwishi.

Rais Rajoelina ameamuru kuwa kinywaji hicho kisambazwe bila malipo kwa wananchi maskini na kiuzwe kwa bei nafuu kwa wananchi wengine.

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, hata wanajeshi wamekuwa wakitembea nyumba hadi nyumba kusambaza ‘dawa’ na CVO.

“Napendelea kunywa chai hii ya mitishamba ili niimarishe afya yangu. Vilevile, tangu zamani nimekuwa nikitumia dawa za kienyeji,” Josette, bibi – bikizee – mwenye umri wa miaka 60 anayeishi katika kitongoji cha Tsimbazaza jijini Antananarivo aliambia shirika la habari la Anadolu.

Maduka ya jumla na yale ya kuuza dawa jijini Antananarivo yameanza kuuza dawa ya CVO ambayo imepakiwa kwa chupa za kuanzia mililita 200 na zaidi. Na zinanunuliwa kwa haraka kwa sababu wateja ni wengi.

“Tulitaka kununua dawa hiyo. Lakini tulipoenda kwa duka la jumla lakini chupa za dawa hiyo zilikuwa zimeisha,” anasema Judith, mama wa mtoto mmoja. Ingawa hajaambukizwa virusi vya corona, ana hamu kubwa ya kuweka akiba ya dawa hiyo nyumbani kwake.

Taasisi ya Kutoa Mafunzo kuhusu Dawa Madagascar (ANAMEM) inasema imetambua uwezo wa dawa kama tiba ya virusi vya corona. Taasisi hiyo inatafakari kuanzisha mfumo wa kufuatilia hali ya watu waliotumia chai hiyo ya mitishamba.

Taasisi hiyo haipingi matumizi ya CVO na imewaachia wananchi kujiamulia kama wataitumia au la mradi wazingatie vipimo vilivyopendekezwa, haswa kwa watoto.

Rakoto Fanomezantsoa, mwanajeshi daktari na mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Soavinandriana, jijini Antananrivo, akisema kiungo kimoja cha CVO kinaimarisha kinga ya mwishi na hutokomeza virusi.

Dawa hiyo inatengenezwa kutoka na mmea kwa jina Artemesia Annua, kutoka China na kuingizwa nchini Madagascar katika miaka ya 1970s kwa ajili ya kutibu malaria.

Kufikia sasa, dawa hiyo inasambazwa katika maeneo matatu nchini humo, ambayo ni Analamanga, Haute, Matsiatra na Atsinanana ambayo yameandikisha visa vingi vya maambukizi ya virusi vya corona tangu Machi 19.

Kulingana na taarifa kutoka Afisi ya Rais wa Madagascar, mataifa matatu ya Afrika kama vile Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Guinea Bissau yamesaka maelezo kuhusu CVO.

Rais wa Senegal Macky Sall ameagiza dawa hiyo baada ya kuwasiliana na Rais Rejoelina, kulingana na vyombo vya habari nchini Senegal.

Kuna zaidi ya visa 33,000 vya maambukizi ya virusi vya corona, vifo 1,469 na jumla ya wagonjwa 10,152 waliopona katika mataifa 52 kati ya 54 bara Afrika, kulingana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Maganjwa Afrika.

Pwani wasaka dawa ya corona mitini

Na MISHI GONGO

WAKAZI katika maeneo tofauti ya Pwani wameanza kutumia dawa za miti-shamba wakiamini zitawakinga wasiambukizwe virusi vya corona.

Haya yamefichuka siku chache baada ya uvumi mwingine kuenea Pwani na kusisimua wengi kwamba chai ya rangi bila sukari ni kinga dhidi ya corona.?Mbinu hizo hazijathibitishwa kisayansi kuweza kukinga wala kuponya ugonjwa huo ulioangamiza maelfu ulimwenguni.

Wataalamu wanasema uenezaji wa imani hizo za kitamaduni unatishia kuvuruga vita dhidi ya maradhi hayo.

Tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona nchini China mnamo Desemba mwaka uliopita, wanasayansi hawajafanikiwa kupata dawa wala chanjo dhidi yake.

Bw Hassan Mohammed kutoka eneo la Kizingo, wadi ya Tiwi, Kaunti ya Kwale alisema mababu zao walitumia miti-shamba kupigana na maradhi mbalimbali ikiwemo ukambi na homa.

“Kuna miti kama murubaini, mzunje, vumbamanga, mmachomacho, mrehani na mtseketse ambayo wazee wetu walitumia kujitibu na kuimarisha kinga ya miili yao. Tumeamua kutumia dawa za asilia kupambana na ugonjwa huu wa corona,” akasema Bw Mohammed.

Mkazi mwingine Bi Asha Mgayu, alisema japo wanafuata masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya kama vile kunawa mikono na kuepuka maeneo yenye watu wengi, wameamua kupiga hatua zaidi kukabiliana na virusi hivyo kwa kujitafutia kinga za kiasili.

“Mwarubaini unaaminika kuwa tiba ya magojwa 40 na ni maarufu sana kote duniani, kinyume na dawa za kutengenezwa katika maabara. Dawa za kienyeji hazina madhara yoyote,” akasema.

Katika Kaunti ya Kilifi, Mwenyekiti wa Chama cha Utamaduni wa Mijikenda Joseph Mwaradandu, alidai kuwa katika miaka ya 1950s, ugonjwa wenye dalili sawa na virusi vya corona uliwakumba wakazi wa Pwani.

Kulingana naye, ugonjwa huo uliofahamika kama kivuti, uliathiri viungo vya mwanadamu vya kupumua jinsi corona inavyofanya.?Alieleza kuwa mgonjwa aliyeugua kivuti alipata matatizo ya kupumua, kikohozi kikavu na kupatwa na joto kali mwilini.

Sawa na ilivyo kwa Covid-19, mgonjwa wa kivuti alitengwa na jamii ili kuepusha maambukizi, kisha kufanyiwa matibabu kwa kutumia miti-shamba.

Kwa msingi huu, aliitaka serikali iwazie kushauriana na wataalamu wa miti-shamba ili kupambana na virusi vya corona.

“Kuna baadhi ya watu wanahusisha miti-shamba na uchawi na ushirikina. Huu si uchawi bali ni kutumia miti asilia kutengeza tiba,” alisema Bw Mwarandu.

Bw Mwarandu alisema matibabu yalihusisha kuchemshwa kwa majani ya miti ya mdungu, mhirihiri, mberandu na mwarubaini.

“Baada ya majani hayo kuchemka mgonjwa angeketishwa kwenye kiti karibu na chungu kilichotokosewa majani hayo kisha kufunikwa na nguo zito ambayo hairuhusu moshi kutoka nje,” akasema Bw Mwarandu.

Alieleza kuwa mgonjwa angeachwa kuketi ndani ya nguo hiyo kwa muda wa dakika 20 hadi atoke jasho kisha kutolewa katika zoezi lililojulikana kama cheruko.

“Baada ya kutokwa jasho, mtabibu angetumbukiza kitambaa kwenye jungu la mitishamba kisha kumkanda mgonjwa katika sehemu za mbavu, mgongo na koo,” akaeleza mzee huyo.

Kujikinga na kuambukizwa, anayemuhudumia mgonjwa pia alitengenezewa dawa sawia na ya mgonjwa.

Hayo yanaendelea huku maambukizi yakizidi kuongezeka nchini. Jana, watu sita zaidi walitangazwa kuambukizwa na kufanya idadi kufika 197.

Wanne ni wakazi wa Nairobi, mmoja wa Mombasa na mwingine wa Siaya, ambaye alifariki.

Kufikia jana watu milioni 1.8 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo katika mataifa 210 duniani, nusu milioni kati yao wakiwa wako Amerika.

Amerika pia ilipita Italia kwa idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo ikiandikisha vifo zaidi ya elfu 21, nayo Italia ikiwa na elfu 19. Uhispania nayo ni ya tatu kwa elfu 16.

Wazee wataka mitishamba itumike kutibu corona

MAUREEN ONGALA na FLORAH KOECH

WAZEE wa Kaya katika eneo la Pwani, wanaitaka serikali ijaribu kutibu virusi vya corona kupitia mitishamba.

Wazee hao wameeleza kuwa dalili za virusi hivyo ni sawa na za ugonjwa wa ‘Kivuti’ uliokuwepo katika enzi za zamani, na uliotibiwa kwa mitishamba.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitamaduni cha Wilaya ya Malindi (MADICA) Bw Jospeh Mwarandu, ambaye ni mmoja wazee hao, alisema kuwa ni lazima serikali itumie njia tofauti kukabili virusi hivyo.

“Tuko tayari kujaribu matibabu kwa watu ambao wameambukizwa virusi. Hata hivyo, lazima tupate msaada tunaohitaji na vifaa vya kujikinga ili tusiambukizwe,” akasema Bw Mwarandu.

Alisema kuwa ugonjwa wa ‘Kivuti’ ulikuwa ukitibiwa kwa mchanganyiko wa mizizi, matawi na ngozi kutoka kwa aina mbalimbali za miti.

Aliyeugua ugonjwa huo alikuwa na dalili kama homa, kupiga chafya, kuumwa na mapafu na kushindwa kupumua vyema.

Alieleza kuwa mgonjwa angefariki baada ya siku sita ikiwa hangepata matitabu ya haraka.

Alisema kwamba wagonjwa waliokuwa wanaugua maradhi hayo walitengwa na familia zao na jamii, kwani ulikuwa wa kuambukizana.

Kwingineko, wazee wa jamii ya Tugen katika kijiji cha Cheplaot, Mogotio, Kaunti ya Baringo wameanza kufanya matambiko ya kitamaduni ili kulaani virusi vya corona.

Wazee hao na wanawake zaidi ya 20 walianza harakati za kutafuta usaidizi kutoka kwa mababu zao, ili kukabili virusi hivyo ambavyo vimewaua zaidi ya watu milioni kote duniani.

Walisema kuwa ni kupitia matambiko hayo ambapo watawarai miungu wao ili kuiokoa dunia dhidi ya “maradhi hayo yasiyoeleweka.”

Maombi hayo yalifanywa katika mlima mdogo mtakatifu, yakiongozwa na mzee wa kitamaduni aliyebeba kibuyu, maziwa, asali na miti aina ya minazi huku wakiomba kwa lugha ya Kitugen.

Kwenye maombi, wazee waliwarai mababu zao kuwasamehe dhambi zao na kuiokoa dunia dhidi ya corona.

Wakiongozwa na Mzee Kigen Kiptoo, walisema waliona kwamba huenda virusi hivyo vikaiangamiza dunia nzima ikiwa hakuna hatua za haraka zitachukuliwa kuwaokoa watu.

“Tumefahamu kuwa maradhi hayo hayana tiba na huenda yakakimaliza kizazi cha sasa ikiwa hakuna hatua za haraka zitakazochukuliwa. Tunawaamini mababu zetu, kwani wakati kunapokuwa na kiangazi, huwa tunaomba na mvua hunyesha. Tunaamini kuwa miungu watatuokoa ikiwa tutaomba,” akasema Bw Kiptoo.

Wataka bunge lipitishe sheria kulinda tiba za kiasili

Na TITUS OMINDE

MADAKTARI wa tiba za kiasili wanataka bunge kupitisha sheria kuhusu tiba hizo. 

Madaktari hao walisema kupitishwa kwa sheria hiyo kutakabiliana na matapeli katika sekta hiyo mbali nakutoa mazingira bora ya wahudumu wa tiba za kiasili.

Daktari Shadrack Moimet wa zahanati ya Koibatek mjini Eldoret alisema kukosekana kwa sheria na sera kuhusu tiba hizo kumechangia katika ongezekeo la matapeli katika tiba husika.

Dkt Moimet alisema iwapo wabunge watapitisha sheria hiyo Wakenya wataondoa dhana potovu kwamba tiba za kiasili ni uchawi.

“Ikiwa sheria hii itapitishwa matapeli ambao wamevamia sekta hii watadhibitiwa mbali na kuondoa dhana potovu kwamba tiba za kiasili ni ushirikina na uchawi.”

Anataka wahudumu katika tiba hizo kushirikiana ili kuona kwamba matakwa yao yanatekelezwa.

Mswada kuhusu tiba hizo umekuwa bungeni tangu bunge la tisa ambapo umekuwa ikihairishwa mara kwa mara.

Madaktari wa tiba za kiasli wanadai kuwa iwapo watapewa mazingira bora ya kuendelezea kazi zao watashirikiana na madaktari wa tiba za kisasa kukubiliana na changamoto ya maradhi tata.

“Dawa zetu zina uwezo wa kutibu ugonjwa kama vile saratani na maradhi mengine ambayo hayana tiba zakisasa, kile tunataka ni kutambuliwa na kushirikishwa vilivyo katika utafiti wa maradhi husika,” akasema.

Vile madaktari hao wanataka serikali kuwatengea fedha za kuendeleza utafiti kupitia tiba za kiasili kama ilivyo nchini Uchina.