Asema mume alifaa kufa badala ya mbwa

Na MASHIRIKA

Frankfurt, Ujerumani

MWANAMKE mmoja katika mji huu alishangaza jamaa na marafiki kwa kusema kuwa heri mumewe angekufa kuliko mbwa wake.

Duru zinasema mama huyo mwenye umri wa miaka 48 alikuwa akimpenda mbwa huyo sana, lakini hakuna aliyetarajia matamshi kama hayo kutoka kwake.

Mbwa huyo alifariki baada ya kugongwa na gari akivuka barabara. “Juhudi za madaktari wa wanyama katika mji huu kumtibu mbwa huyo hazikufua dafu na akafariki.

Mama huyo alihuzunika mno. Hakuweza kula kwa siku nne. Jamaa na marafiki walijaribu kumfariji lakini hawakufaulu,” mdokezi aliambia jarida www.dogs.com.

Duru zinasema kwamba mumewe anayefanya kazi mji tofautio aliamua kusafiri nyumbani kumtuliza mkewe.

Hata hivyo, mkewe alipomuona alimkemea: “Heri ungekufa wewe kuliko mbwa wangu ambaye alikuwa rafiki yangu mkubwa maishani. Ukiwa mbali, alikuwa karibu nami, nikimuita alikuwa akiitika ilhali wewe huwa unachukua simu zangu unapotaka,” mama alilia mumewe alipojaribu kumkaribia.

Watu walipigwa na butwaa kufuatia matamshi ya mama huyo ambaye hajajaliwa mtoto na wakadhani mumewe angekasirika.

Hata hivyo, jamaa alipiga magoti mbele ya mkewe na kuomba msamaha kisha akaenda kumnunulia mbwa mwingine wa bei ghali ili kumtuliza.

“Watu walidhani jamaa angekasirika kwa kutakiwa kifo lakini walishangaa alipomuomba mkewe msamaha, akatoka na kurudi na mbwa mwingine ambaye bei yake ni mara tatu ya aliyefariki,” mdokezi alisimulia.

Kulingana na mdokezi, mama alipomuona mbwa huyo alifurahi, akamkumbatia na kurudia shughuli zake za kawaida.

“Mpenzi, kama ningekufa, haungepata mbwa mwingine kama huyu,” mumewe alimtania.

Polo aandaa hafla ya kumtema mkewe

Na TOBBIE WEKESA

WEBUYE MJINI

KALAMENI mmoja kutoka hapa alishangaza watu alipoandaa hafla ya kuachana na mkewe.

Inasemekana polo aliandikia marafiki na majirani barua ya mwaliko akiwaomba kuhudhuria hafla hiyo bila kukosa.

Kulingana na mdokezi wetu, kila mmoja aliyepokea mwaliko alipigwa na butwaa, kwani sababu aliyotoa polo ya kuachana na mkewe haikuwa na mashiko yoyote.

Mkewe alipogundua mpango wa kalameni, pia naye aliamua kuwaalika ndugu zake pamoja na marafiki kwa hafla hiyo.

Inadaiwa kipusa vile vile aliwadokezea wazee wa ukoo kuhusu njama ya mumewe.Siku ya hafla ilipowadia, kila mmoja aliyealikwa alihudhuria.

Polo alishangaa kuwaona mashemeji zake karamuni ilhali hakuwa amewaigta.Duru zinasema katika hafla hiyo, ni jamaa mwenyewe aliyekuwa mfawidhi.

“Mimi nimewaita hapa kuwajuza kwamba kuanzia kesho naanza maisha yangu upya. Nitakuwa kapera mchanga,” alisema wageni wakiangua vicheko.

Mkewe pamoja na ndugu zake walitulia tuli. Jamaa akaendelea: “Nimekaa na mke wangu kwa zaidi ya miaka kumi na wakati umefika wa kila mtu kurudi kwa mama yake. Uchumi umekuwa mbaya.”

Kabla polo kumaliza hotuba yake, wazee wa ukoo walifika. Hata hivyo, polo hakushtushwa na kuwasili kwao.

“Tumesikia mambo yako yote. Hebu tupe sababu nzuri ya kuachana na mkeo,” mzee mmoja alimuuliza mume huyo.

Kulingana na mdokezi, jibu la polo liliwaacha wengi vinywa wazi. “Miaka kumi kuishi na mtu mmoja kwa nyumba si rahisi. Aende kwao atafute bwana mwingine nami nitafute kidosho mwingine,” polo alidai.

Wazee walisitisha mkutano huo mara moja na kuwarai wote waliohudhuria kuachana na porojo za polo.

Kila mgeni aliondoka na kuelekea kwake huku wakistaajabishwa na kisanga cha jamaa huyo.

Mwanamume apokonywa mke na pasta aliyesimamia harusi yake

Na KNA

MFANYABIASHARA mmoja kutoka eneo la Juja Farm, Kaunti ya Kiambu, anasononeka baada ya mkewe wa miaka 26 waliyejaliwa watoto watano kunyakuliwa na pasta aliyesimamia harusi yao.

Bw John Kanyua ameshindwa kuelewa ni vipi pasta aliyewasaidia wakati wa ndoa yao, hata akatia saini cheti chao cha harusi, alimnyelea mkewe wa zaidi ya miongo miwili.

Mwanamume huyo hakutambua kuwa pasta huyo alikuwa akimezea mate mkewe, Leah Wambui, kwa miaka hiyo yote licha ya baadhi ya waliohudhuria harusi yao kubaini ukweli huo.

Hayo yote yalianza wanandoa hao walipoanza kuhudhuria kanisa la pasta huyo eneo la Juja Farm.

Na baada ya kupendezwa na mchango wao kanisani, pasta huyo alimteua Leah kuwa naibu wake katika Kanisa hilo, jambo lililofanya mke wa pasta kuingiwa na wasiwasi.

“Nilipinga uteuzi, lakini alinipuuzilia mbali. Nilimkabili Leah na kumwonya dhidi ya kucheza na mume wangu. Alionekana asiye na hatia, na nikakubali,” alisema Agnes Wangivi, mke wa pasta huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye wamejaliwa watoto watatu.

Urafiki kati ya Leah na pasta uliendelea kunawiri kiasi kwamba, kiongozi huyo wa kanisa angemwalika (Leah) nyumbani kwao kwa hafla za kifamilia, lakini bila kuandamana na mumewe.

“Hapa ndipo nilianza kuuliza maswali kuhusu urafiki wao. Nilimkabili Kinyua na kumwambia amwambie mkewe aachane na mume wangu, lakini hakuwa makini. Hatimaye mume wangu alitelekeza familia yake na kutoweka na Leah mnamo 2015,” Bi Wangivi aliongeza.

Kanyua anasema kuwa hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba, mara kadha pasta huyo angefika nyumbani kwake asubuhi na kusalia mle mchana kutwa na mkewe wakiwa wamejifungia chumbani.

Hii ilimfanya kuwaita maafisa wa utawala na viongozi wa kanisa ili wamsaidia kutatua shida hiyo.

“Hali ilikuwa mbaya kwani pasta alitoroka na mke wangu pamoja na watoto na wakakodisha nyumba katika soko la karibu ambako wanaishi,” alisema.

Wataka kurejesha mahari

Wazazi wa Leah sasa wamewasiliana na Kanyua wakimtaka akubali warejeshe mahari aliyotoa kwao ili kutoa nafasi kwa harusi mpya ya binti yao, lakini mwamume huyo amekataa.

Pasta huyo pia amewaambia watoto wake kwamba, anapanga kuoa mke mwingine na kwamba ametengana na mama yao.

Licha ya kukabiliwa na shida hii, Kanyua bado hulipa karo ya watoto wake kando na kutuma chakula wanakoishi na pasta.

“Hii haiwezekani na siwezi kukaa nikitizama mtu mwingine akichukua familia yangu. Ikiwa serikali haitaingilia kati, nitaamua la kufanya. Nimegharimika pakubwa kutunza familia yangu kwa miaka hiyo yote. Sitaruhusu harusi hiyo kuendelea na nitawasilisha kesi ya kuipinga. Akome kuharibu jina lake na aombe msamaha, na nitamkubali arejee nyumbani,” alisema Bw Kanyua.

Adhani kapata mke kumbe kicheche

 Na John Musyoki

KIAMBERE MJINI

KALAMENI mmoja mjini hapa alijuta baada ya demu aliyemkaribisha kwake kumuibia pesa na simu.

Duru za mtaani zinasema kuwa jamaa alipenda kuwatongoza akina dada mtaani kila mara akilipwa mshahara. Siku chache kabla ya kioja, alifika kwake mwanadada mrembo na kujulisha majirani kwamba alikusudia kumuoa.

“Mwaonaje huyu mrembo? Kwa sasa sina haja ya kuwafuata wanawake wengine. Huyu ni tosha na tena mpole sana. Nitamuoa hivi karibuni kwa hivyo kila mmoja awe tayari kuhudhuria harusi yetu,” jamaa alisikika akijigamba.

Yasemekana baadhi ya marafiki wa jamaa walimpongeza kwa kufanya uamuzi wa busara japo wengi wao walimkosoa kwa kutaka kumuoa demu huyo ilhali hakuwa amemfahamu kwa muda mrefu.

“Utafanya vizuri ukioa kwa sababu tabia unayofanya ya kubadilisha wanawake itakutia matatani lakini mchunguze sana kabla hajakuwa mke wako. Hapa ni mjini na wanawake wengi sio wa kuaminika,” mama mmoja alimwambia jamaa.

Jamaa kwa kiherehere chake, alipuuza ushauri wa busara wa mama huyo.

“Sasa umeamua kunitoa nyama mdomoni. Mwanadada huyu ni mrembo sana na tena namwamini, hawezi kuwa kigeugeu kama wanawake wengine,” jamaa alijibu.

Usiku wa manane siku hiyo, jamaa alisikika akilalamika baada ya kumkosa mwanadada huyo chumbani.

“Huyu ameenda wapi? Kwani yeye ni jini ama ninaota. Pesa zangu na simu haziko,” jamaa alisikika akilalamika.

Inasemekana alitoka chumbani na kuanza kuangua kilio huku akijuta baada ya kupuuza ushauri wa mwenzake.

“Naota ama kulikoni? Ako wapi mrembo niliyekuwa naye chumbani?” jamaa alilia na kuwaamsha majirani.

“Ndugu yangu hauoti. Huu ndio ukweli wa mambo. Nilikuambia ukadhani ni ndoto. Sasa unajuta,” mama aliyemshauri awali alimweleza.

Atupa mke kwa kuchoshwa na wakwe

Na John Musyoki

Kiritiri, EMBU 

JOMBI mmoja kutoka eneo hili aliwashangaza wazazi wake alipoamua kumtaliki mkewe akidai wakwe zake ni wasumbufu.

Penyenye za mtaani zinasema kalameni alidai wakwe zake walikuwa wakimtia presha kwa kukosa kuhudhuria harambee waliyoandaa na kutoa mchango wake.

Duru zinasema jamaa aliposusia harambee wakwe walimtisha na kumsuta vikali.

“Mimi nimechoshwa na tabia ya wakwe zangu. Nilipokosa kuhudhuria harambee ya kuchangisha pesa sasa wameeneza udaku kila mahali kunihusu. Sitaki mchezo na wakinichokoza nitampa binti yao talaka,” jamaa alisikika akiwaambia wazazi wake.

Jamaa alizidi kulalamika huku akidai kwamba wakwe zake walikuwa wakimtumia vibaya.

“Nimekasirika sana. Nililipa mahari yote na bado wazazi wako wananifuata waninyonye kila kitu. Wazazi wako wamekuwa wakiniharibia jina langu kila mahali. Hata hawana shukrani kwa kuwalipa mahari chungu nzima. Wakicheza na mimi nitakupa talaka uende ukaishi na wao huko kwenu,” jamaa alimgeukia mkewe na kumfokea.

Inasemekana jamaa aliwapigia wakwe zake simu na kuwakemea kwa kumtisha na kumkosea heshima mtaani. Hata baada ya wazazi wake kumtuliza jamaa aliwaka zaidi.

“Mimi sitaki kisirani. Nitampa mke wangu talaka. Kuishi maisha ya ukapera si hoja kwangu. Ni bora kuliko kuishi na wakwe wanaonikosesha usingizi,” jamaa alisema. Jombi huyo alizidi kuwaka huku watu wakimsihi atulie lakini dua zao ziliambulia patupu.

Ilibidi wazazi wake wafunge safari kwenda kwa wakwe zake ili kujaribu kutatua mzozo huo kwa sababu walikuwa wakimpenda mkaza mwana wao sana. Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya wazazi kutoka pande zote mbili kukutana.

Jombi atoroka mke aliyeletewa na mamake

NA LEAH MAKENA

KANGETA, MAUA

Kalameni wa hapa alilazimika kutoroka nyumbani kuhepa mwanadada aliyechaguliwa na mama yake kuwa mke wake.

Jamaa alikataa kata kata kukubali mwanadada aliyechaguliwa na wazazi wake na walipomshinikiza akaamua kutoroka na kurudi mjini alikokuwa akiishi baada ya kumaliza masomo.

Kwa zaidi ya miaka minne, polo alikuwa chuoni kusoma licha ya wazazi kumtaka kuoa wakidai umri wake ulikuwa umesonga. Alitia masikio nta na kubukua hadi akahitimu ndipo akafika nyumbani kutoa shukrani kwa wazazi.

Hakuamini alipofika nyumbani kwani alifanyiwa kikao na wazee na kutakiwa kumpokea mwanadada aliyekuwa katika nyumba yake kuwa mkewe.

Penyenye zinasema jamaa hakutakiwa kupinga uamuzi wa wazazi wake wa kumchagulia mke.

“Kama unavyojua, imekuwa desturi ya vijana kutafutiwa wachumba kwani tunajua msichana anayekufaa zaidi kama wazazi. Tushalipa mahari na tunachotaka ni wewe kumpokea kama mke wako ili muendeleze kizazi chetu,” wazee walimshauri.

Yasemekana jamaa alikataa akisema alikuwa na mchumba na walikuwa wakipanga harusi.

“Mimi nishapata mpenzi na tunataka kuanza mipango ya harusi punde tu baada ya kupata ajira. Enzi za kutafutiwa wachumba zilipita, naomba mniruhusu nifanye maamuzi yangu binafsi,” kijana alijitetea.

Hata hivyo hakuweza kuwashawishi wazee kubadilisha nia kwani walisisistiza kuwa hawangekubali msichana wa mbali wasiyejua tabia zake.

Hapo ndipo jamaa alikubali agizo lao shingo upande kwa lengo la kuwafurahisha kwa muda. Inasemekana kuwa jioni hiyo, jamaa alitoka bila kuaga na kuishia mjini ambako aliendeleza mipango ya harusi na mpenzi wake bila kufahamisha wazazi.

Vitisho vya wazee kwamba wangemlaani havikumshtua na mwanadada aliyechaguliwa akalazimika kurudi kwao kujaribu bahati kwingine.

Ashangaza kujificha msituni miaka 10 kuhepa ukorofi wa mkewe

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka Uingereza ameshangaza ulimwengu baada ya kuibuka kuwa wakati fulani alipochoshwa na usumbufu wa mkewe, aliamua kwenda kwenye msitu kukaa huko, na akaishia kuishi mwituni kwa miaka 10.

Malcolm Applegate wa miaka 62 na ambaye alikuwa mfanyakazi wa shambani alikuwa amemwoa mkewe kwa miaka mitatu, wakati alipogundua kuwa usumbufu wake unazidi.

“Miaka mitatu ya kwanza mambo yalikuwa shwari, tulikuwa tukiishi vyema na inaonekana kazi yangu ya ukulima ikawa inamtatiza. Kadri nilivyozidi kufanya kazi, naye alikuwa akikasirika kwani hakupenda niwe nje ya boma kwa muda mrefu,” Applegate akaeleza Mashirika.

“Tabia yake ya kutaka kunidhibiti ilizidi na akaanza kunitaka nipunguze saa za kazi,” akaendelea.

Mwanamume huyo alisema ilipofika hapo, aliamua kuondoka katika boma lao na akaamua kuwa hangemfahamisha yeyote kilichokuwa katika akili zake, hata familia na marafiki.

“Niliwatoroka kwa muda wa miaka kumi,” akasema Applegate.

Alisema alitumia wiki tatu kutembea kutoka eneo la Oxford hadi London, ambapo alienda katika msitu mkubwa karibu na eneo la Kingston, kusini magharibi mwa Jiji la London.

Alisema humo alifanya kazi katika eneo la jamii, ambapo wazee wakongwe hukaa.

Applegate alisema katika eneo hilo ambapo alitorokea, kulikuwa na watu wengine ambao walikuwa wamepiga kambi na japo kila mmoja wao alikuwa akifanya kazi kivyake, mara kwa mara wangepatana katika eneo hilo palipokuwa pakiishi wazee, kwani walikuwa wakienda huko kuoga.

“Hakuna aliyejua kuwa tulikuwa huko kwani ni mahali pasipojulikana vyema- hakuna mtu angeenda huko ndani,” akasema.

Mwanamume huyo sasa anasema kuwa anaishi katika eneo pa watu wasio na makao, ambapo anafanya kazi za vibarua vibarua na anachangisha pesa za msaada eneo hilo.

Machozi yamtiririka polo akinyenyekea mkewe asimteme

Na Nicholas Cheruiyot

Kaborok, Kericho

Kulikuwa na kioja katika mtaa huu jamaa alipompata mkewe akitoroka kurudi kwao na kumlilia asifanye hivyo.

Inaarifiwa kuwa polo aligombana na mkewe kuhusu masuala ya kinyumbani hivi majuzi.

“Jamaa alipochoshwa na maneno makali ya mkewe, alimsukuma hadi akaanguka chini kisha akatafuta amani kwa kuenda kutembea mtaani,” mdaku aliarifu.

Hata hivyo, baada ya muda mfupi alipigiwa simu na kaka yake kumfahamisha mkewe alikuwa amefunganya virago na kuondoka.

Mara moja jamaa aliomba pikipiki na kuendesha kwa kasi kwa kuelekea kwa wakwe zake.

Ilikuwa afueni alipopata mkewe njiani akibebwa na pikipiki. Alimuamrisha mwendeshaji kupiga breki naye akafanya hivyo haraka.

Huku akihema, jamaa alishika begi la mkewe na kumlilia asimtie aibu.

“Kwani ulikasirika sana nilipokugusa tu? Si ilikuwa mara yangu ya kwanza kunguruma kama simba? Naomba usinikosee heshima kwa wakwe wangu,” polo alilia machozi huku mkewe akiwa amenuna sana.

“Ulidhani unaweza kunitesa utakavyo na nigandie kwako kama gundi? Baba yangu bado ananipenda sana na kama hunitaki niache. Sirudi ng’o!” mrembo alisema na kutingisha kiuno kwa maringo.

Waendeshaji pikipiki walijiunga na mrengo wa polo na kumshauri mrembo arudi kwake.

“Nyinyi mnaheshimika katika kijiji hiki. Aibu iliyoje watu kusikia mlivurugana! Rudini kwenu na muongee hadi muelewane,” mwanabodaboda mmoja alishauri.

Hatimaye, mrembo alikubali kurudi akiwa ametoa masharti kuwa kamwe yeye si wa kuzushiwa.

“Nikiteleza nataka unieleze kosa langu polepole. Sina mazoea ya kupigiwa kelele na usipobadilika utajua hujui,” kipusa alisema na jamaa akaahidi kuzingatia hayo yote.

Jombi amrithi mke wa ndugu aliyehamia mjini

Na TOBBIE WEKESA

MPELI, BUNGOMA

POLO mmoja kutoka hapa alipigwa na mshangao alipopata mkewe alichukuliwa na ndugu yake mdogo. ? Inasemekana polo alirejea nyumbani kwao baada ya miaka minne kutoka jijini alikokuwa ameenda kutafuta kazi.

Kulingana na mdokezi, polo alipokuwa jijini, alikatiza mawasiliano kati yake na mkewe. Kwa miaka minne, watu wa familia yake hawakuwa wakimpata kwa simu naye hakuwa akiwasiliana nao.

Duru zinasema mkewe alichoka kumngoja na akamuendea shemeji yake na kumuomba amrithi. Penyenye zinasema miaka miwili baada ya jamaa kumrithi kipusa, ndugu yake aliwasili na kupata mkewe alikuwa amejengewa nyumba mpya.

“Hapa si kwako. Nyumba hii hukuijenga. Ni ya ndugu yako mdogo,” kipusa alimueleza polo.

Polo alibaki mdomo wazi. “Unamaanisha nini?” polo aliuliza. Inasemekana kipusa alimkaripia polo huku akimtaka arudi alikotoka.

“Wewe ulipoondoka uliniachia nani hapa nyumbani. Ama ulifikiria nimezeeka sina hisia,” kipusa alimfokea polo.

Inadaiwa kipusa alimueleza polo kuwa ndugu yake mdogo ndiye mwenye nyumba.

“Hapa uliko ni kwa ndugu yako mdogo. Yeye ndiye aliyenioa. Nampenda na sitamuacha. Tafuta mwingine uoe,” kipusa alimwambia jamaa.

Polo alishindwa na la kufanya. “Wewe hukuonyesha dalili za kurudi. Tulikutafuta hata tukadhani ulikuwa umekufa. Haukunitoa kwetu nije kupigwa na baridi kwenu. Mimi nilichukuliwa na ndugu yako akanioa,” kipusa alimhakikishia polo.

Yasemekana ndugu wa jamaa walimlipia mwanadada mahari ambayo jamaa hakuwa amelipa. Inadaiwa polo aliapa kumpa ndugu yake funzo. “Mimi sijafa. Mtoto mdogo anawezaje kumrithi mke wangu! Atajua hajui,” polo aliapa.

Hata hivyo hakufua dafu kwa sababu wazee walimzima na kumwambia alimtelekeza mke kwa miaka minne na ndugu yake alikuwa amechukua usukani hata akalipa mahari.

UNYAMA: Mke kutoka kuzimu alivyompa mumewe upofu daima milele

Na CECIL ODONGO

KILA mwaka Kenya inapowakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi la Westgate lililotokea Septemba 21, 2013, uchungu, ukiwa na masikitiko humvaa Dan Matakaya, mzaliwa wa kijiji cha Shakunga, eneobunge la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega.

Bw Matakaya ambaye ni afisa wa polisi wa hadhi ya konstebo katika kituo cha polisi cha Industrial Area, Nairobi, milele daima hatawahi kusahau siku hiyo ya mauti si kwa Wakenya hao tu bali hata kwake yeye mwenyewe.

Kwake, tukio la kusikitisha alilowahi kukumbana nalo mikononi mwa aliyekuwa mkewe limemfanya kipofu ingawa alizaliwa mzima wa afya tena bila kasoro au tatizo lolote la kimaumbile.

Kama ada, Bw Matakaya ambaye wakati huo alikuwa afisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Kisii ya Kati mjini Kisii siku hiyo alirejea katika makazi yake kituoni humo baada ya kuwajibikia majukumu yake ya kikazi usiku kucha.

Akiwa amevamiwa na uchovu na usingizi mwingi, afisa huyo aliingia chumbani saa 11 asubuhi na kujilaza kitandani ili kupumzika huku aliyekuwa mkewe ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa sababu za kiusalama na kesi iliyoko mahakamani, akiwa anajishughulisha na usafi wa nyumba yao.

Wawili hao walikuwa wamevurugana siku iliyotangulia baada ya Bw Matakaya kumzima mkewe aliyefaa kusafiri kwao siku hiyo kutobeba nguo za marehemu mtoto wao aliyefariki miezi michache ya awali, hadi kwao.

Suala hilo siku iliyotangulia lilikuwa limezua ubishi mkali kati yao.

“Tulikuwa tumejaaliwa mtoto katika ndoa yetu changa lakini kwa masikitiko makuu akafariki miezi michache baada ya kuzaliwa kwake. Mke wangu alifaa kuenda kwao lakini sikuelewa kwa nini alitaka kupeleka nguo za mwanangu kwao. Niliwapigia simu wakwe wangu na kuwaeleza kuhusu suala hilo na wakakubaliana nami kwamba binti yao hakufaa kubeba nguo hizo ndipo nikamkataza,” Bw Mataya akasema wakati wa mahojiano katika jumba la Nation Centre, jijini Nairobi.

Akiwa amepata usingizi wa pono, mkewe, aliyekuwa na umri wa miaka 23 wakati huo na mara nyingi akionekana mnyamavu na mtulivu, alikuja kitandani akiwa amebeba kemikali ya Sulphur aliyotia ndani ya maji moto na kummwagia usoni.

“Nikiwa usingizini nilihisi maumivu makali machoni ila sikuweza kuonana hata baada ya kutapatapa kama mfa maji. Nilijizoazoa kumkabili lakini nikashindwa baada ya kukanyaga nyaya za stima alizokuwa ameunganisha kisha kuzimwagia maji sakafuni ili nichomeke,” akafafanua Bw Matakaya.

Akiwa na maumivu makali, afisa huyo ambaye pia aliwahi kudumu katika kituo cha polisi cha Etabwa mjini Embu alisimulia namna majirani walivyofika na kunusuru maisha yake baada ya kupiga ukemi akilia na kuitisha msaada.

Mkewe naye baada ya kitendo hicho aliingia mafichoni ila akaibuka baada ya siku mbili na kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi kituoni humo ambako alizuiliwa kabla ya kufikishwa katika mahakama ya Kisii kujibu mashtaka ya nia ya kuua. Aliachiliwa kwa dhamana siku chache baadaye.

Akiwa amesononeka, Bw Matakaya alisema kwamba harakati ya kupata haki imekuwa ikijikokota sana. Hii ni kutokana na mazoea ya jaji anayeshughulikia kesi hiyo kuiaihirisha kila mara bila sababu za kuridhisha.

“Kesi imekuwa ikijikokota sana tangu mwaka wa 2013 lakini nina imani kwamba ipo siku nitapata haki,” akasema Bw Matakaya akiwa ameandamana na Wycliffe Manyengo ambaye alimwajiri kama mwelekezi wake baada ya kupofuka.

Katika hali ya kushangaza, afisa huyu anasema kwamba hana kinyongo na mkewe na amemsamehe rohoni lakini hawezi kuondoa kesi kortini maana ameshauriwa kutofanya hivyo.

Anafichua kwamba amekuwa akipokea jumbe za watu kutoka familia ya mkewe wanaosikitikia hali yake na kumwomba amsamehe ila anasisitiza kwamba hawezi kurudiana naye kamwe na wao hukutana tu wakati wa vikao vya kesi wala hawajawahi kuzungumza kwa simu tangu mwaka wa 2013.

Bw Matakaya pia alituelezea kwamba tukio hilo liliathiri sana wazazi wake John Matakaya na Bilha Matakaya ambao walichukua muda sana kukubali kwamba mwanao tegemeo amekuwa kipofu bila kosa wala hatia.

Kikazi, afisa huyo aliwashukuru sana wenzake wa kituoni kwa kumpa msaada mkubwa kila mara anapowahitaji japo alisisitiza kwamba hali yake haijamzuia kutekeleza wajibu wake kama kawaida baada ya kupokea masomo ya namna ya kuwasiliana na kuandika kutumia mashine za Braille zinazotumiwa na wasioona.

“Masomo hayo yamenisadia sana kwasababu naweza kuandika, kusoma, kupiga simu na kazi nyingine za polisi baada ya simu yangu kuwekewa teknolojia ya kisasa inayonirahisishia kuandika na kuongea. Pia maafisa wenzangu na mwelekezi wangu Bw Manyengo wamekuwa wazuri sana kwangu. Kwa kweli namshukuru Mungu na namwomba awazidishie neema,” akaongeza Bw Matakaya.

Akilenga ufanisi na kuwaokoa wanaodhulumiwa, afisa huyo yuko kwenye mchakato wa kuanzisha wakfu kwa jina Dan Shieshie utakaowanusuru waume na wake wanaopitia madhila katika ndoa zao na mambo mengine mabaya yanayotokea katika jamii.

Kulingana naye, wanaume wengi huathirika sana katika ndoa zao japo huwa hawajitokezi kusema kwa hofu ya kuchekwa au kutazamwa tofauti na jamii ambayo huwachukulia kama wakuu wa familia wasiofaa kupigwa na wake.

Hata hivyo yeye amejitolea kuwasaidia kwa kuwapa ushauri na misaada mingine akitumia hela zake.

“Jambo la kweli ni kuwa ndoa nyingi zina pandashuka na wanaoumia zaidi ni wanaume wanaosalia kimya wakiwa na hofu ya kuchekwa. Nimeweka nambari yangu wazi ili waweze kuwasiliana nami kwa sababu niko tayari kuwasaidia hata kwa fedha zangu wasije wakajiua au kufanya mambo yasiyofaa baada ya kuathiriwa kisaikolojia,” akasisitiza afisa huyo.

Ili kudhihirisha matamanio yake ya kuwapa msaada wanaoathirika ndipo yaliyomkuta yasiwapate, Bw Matakaya anasomea shahada ya Ushauri Nasaha katika Chuo Kikuu cha Mlima Kenya bewa la Nairobi.

Anatumai masomo haya yatamwezesha kushughulikia kesi zitakazowasilishwa kwa wakfu wake ama zile atapokea kupitia mawasiliano ili kuwaepusha wengi kukumbana na msiba kama wake.

Pendekezo lake kwa serikali kupitia wizara ya afya ni kwamba mauzo ya wazi ya asidi au kemikali hatari yanafaa kudhibitiwa.

Jombi aomba kanisa limsaidie kutimua mke

Na TOBBBIE WEKESA

KABARI, KIRINYAGA

Kalameni mmoja aliwashangaza waumini wa kainsa moja la hapa alipoingia kanisani na kuomba asaidiwe kumtaliki mke wake akidai alikuwa amegeuka kisirani.

Kulingana na mdokezi, polo alikuwa amechoshwa na tabia za mkewe za kumzomea kila mara. Inadaiwa polo alikuwa amejaribu mbinu zote za kumtimua kipusa lakini hakufua dafu.

Duru zinasema kipusa alipokuwa akienda kanisani, polo aliamua kumfuata polepole. Wakati mahubiri yalipoanza, polo aliingia na kumuomba pasta atulie kidogo.

“Mke wangu hushiriki hapa. Nyumbani hanipi amani wala raha. Niliamua kuzamia pombe angalau nisahau baadhi ya mambo anayonifanyia,” polo alieleza. Kila mtu kanisani alinyamaza kimya kumsikiliza polo.

“Najuta sana kumuoa. Nimejaribu kumfukuza lakini hafukuziki. Naomba talaka,” polo alisema. Mkewe polo alisimama na kumuomba pasta kutomsikiliza mumewe.

“Achana na huyo. Ni mlevi. Wewe endelea na mahubiri,” kipusa alimrai pasta.Inasemekana polo alianza kumzomea kipusa huku akitoboa siri zake zote.

“Acha ujinga. Huyu mwanamke kitandani hatuangaliani. Akiondoka asubuhi yeye hurudi jioni na hataki nimuulize. Mnisaidie nimpe talaka,” polo aliomba. Kulingana na mdokezi, pasta alimuomba polo kurudi nyumbani ili wasuluhishe mgogoro baadaye.

“Tutakuja kusuluhisha hayo mambo baada ya huduma kuisha. Tulia pale kwanza,” pasta alimrai polo. Inadaiwa polo aliamua kuondoka huku akiapa kutumia mbinu zote kumtimua kipusa.

“Sitaki kumuona kwangu. Madharau yake yamenifika kooni. Atafute bwana mwingine wa kumuoa humu kanisani,” polo alisema huku akianza safari kurudi kwake.

Baada ya ibada pasta alielekea kwa jamaa akiandamana na wazee kadhaa na haikujulikana ikiwa walifaulu kusuluhisha mzozo kati yake na mkewe

Atwoli akana kutoroka na mke wa watu

VICTOR OTIENO na PETER MBURU

KATIBU Mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli amejitokeza kujibu uvumi uliotokea hivi majuzi kuwa alimnyanganya mwanamume mwingine mkewe, akisema kamwe hawezi kufanya hivyo.

Akizungumza mjini Kisumu jana, Bw Atwoli alipinga madai kuwa alitoroka na mke wa wenyewe (anayedaiwa kuwa msomaji wa habari za runinga), akisema alishauriwa na babake kutojihusisha na wake za watu.

Bw Atwoli alisema kabla ya kuoa mke mwingine, ni hulka yake kufika kwa wazazi na kutaka kujua ikiwa ameolewa ama yuko huru.

“Kuna mtu hivi majuzi alijaribu kuniharibia jina kuwa nilitoroka na mkewe, ni mwanaume mpumbavu wa aina gani, babangu alinishauri kuwa niwapo uhai nisicheze na wake za watu na hivyo siwezi kufanya hivyo,” akasema Bw Atwoli.

Katibu huyo alisema hata wake wengi aliooa hadi sasa, amekuwa akifuata taratibu zinazofaa kuhakikisha si wake wa wenyewe.

“Jamaa huyu hana akili timamu. Hata wake kadhaa nilio nao nimekuwa nikihakikisha kutoka kwa wazazi wao ikiwa wana wenyewe au la kabla sijawasilisha posa,” akasema Bw Atwoli.

Alisema kuwa babake alimshauri akitaka kuishi maisha marefu asiwahi kucheza na wake za watu.

Hii ilikuwa baada ya tetesi kuibuka kutoka kwa mwanasiasa kutoka eneo la Magharibi kuwa kiongozi huyo wa wafanyakazi alimnyanganya mke na kumtishia kumchukulia hatua kali.

 

Buda amwachia mke uwanja agawe uroda anavyotaka, bila bughudha

Na TOBBIE WEKESA

NETIMA, BUNGOMA

Kalameni mmoja kutoka hapa alitoroka boma lake akidai alikuwa akiwindwa na polo aliyeshuku kuwa mpango wa kando wa mke wake. 

Kulingana na mdokezi, polo alifunganya virago na kutorokea jijini huku akiwaacha wenyeji vinywa wazi.

Inadaiwa kalameni alimlaumu mkewe kwa masaibu yaliyomzonga.

“Mke wangu si mtu mzuri. Heri niondoke nimpe nafasi aendelee na raha yake. Sitaki kuuliwa hapa,” kalameni aliwaambia majirani.

Kipusa alijaribu kumzuia polo asiondoke lakini alilemewa nguvu na polo.

“Kazi yako ni mipango ya kando tu. Juzi umenitusi kuwa mimi sikutoshelezi ndio maana unakimbizana na vijana barobaro,” kalameni alimkaripia mkewe.

Kipusa alipinga madai ya polo huku akidai kuwa yalikuwa uongo mtupu.

“Wewe acha uongo wako. Huyo unayesema si mpenzi wangu bali ni jamaa yangu,” kipusa alijitetea.

Penyenye zinasema polo alikuwa akizozana na mkewe kuhusiana na tabia yake ya kuchovya nje.

Penyenye zilizotufikia zinasema polo alikuwa akipata jumbe za kumtishia maisha akiendelea kumgombeza mkewe.

“Juzi huyo jamaa alinisimamisha njiani na akanipa onyo kali. Aliniambia uhusiano wenu ulianza mkiwa shule ya msingi na nikiwa kizingiti nitanyoroshwa,” kalameni alimfokea mkewe.

Majirani walibaki kutazama sinema ya bure jamaa akifichua masaibu yake.

“Jana usiku nimesikia jamaa akitembea hapa nje. Najua ni mimi wanatafuta. Heri nikuachie boma uendelee na tabia zako nao,” polo alimueleza mkewe.

Baada ya kumaliza kupakia mizigo yake, polo aliitisha bodaboda na kuondoka akiapa kutorudi.

“Sitaki kupigwa na hao watu wako. Ukitaka kuwaleta hapa, basi una uhuru sasa,” polo alimueleza mkewe huku akienda.

…WAZO BONZO…

Mke wa mwalimu aliyeuawa kukaa seli

Na NDUNGU GACHANE

MKE wa mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ambaye mwili wake ulipatikana Jumapili ukiwa umewekwa katika buti ya gari Jumatatu alifikishwa mahakamani pamoja na mshukiwa mwingine wa kiume.

Hata hivyo, Alice Mugechi na Samuel Harrison Gitu hawakujibu mashtaka katika mahakama ya Murang’a, baada ya upande wa mashtaka kuomba muda zaidi wa kuwachunguza.

Mwili wa Bw Samuel Mbogo uligunduliwa ukiwa kwenye buti ya gari eneo la Gakurwe, kwenye barabara ya Murang’a – Kiriaini.

Afisa anayechunguza kesi hiyo Jeremiah Kazungu Ngumbao aliomba mahakama kuwapa polisi muda zaidi kukamilisha uchunguzi, kabla ya kuwafungulia rasmi mashtaka washukiwa hao.

“Naomba mahakama kutupa siku 14 zaidi ili tuweze kukamilisha uchunguzi kabla ya kuwafungulia washukiwa mashtaka kuhusiana na mauaji haya,” afisa huyo akaambia mahakama.

Lakini washukiwa walipinga ombi hilo huku wakitaka mahakama kuwaachilia huru na wakamatwe tena polisi watakapokamilisha uchunguzi.

“Hakuna mtu nyumbani wa kutunza ng’ombe na mifugo wengine. Sikupata wakati wa kufunga mlango wangu nilipokamatwa. Kadhalika, naomba nipewe muda wa kuandaa mazishi ya mume wangu mpendwa.

Polisi wako huru kunikamata tena watakapokamilisha uchunguzi wao,” akasema Mugechi. Gitu aliambia mahakama kuwa yuko tayari kukamatwa tena polisi watakapokamilisha uchunguzi wao.

“Kwa sababu polisi hawajapata ushahidi wa kunihusisha na mauaji hayo, hawafai kuendelea kunizuia. Wanikamate watakapokamilisha uchunguzi wao,” akasema mshukiwa huyo.

Lakini, Hakimu Mkuu, Bi Margaret Wachira alikataa maombi ya washukiwa akisema kuwaachilia huru kutatatiza uchunguzi.

“Nimekubaliana na ombi la upande wa mashtaka. Hivyo naruhusu afisa wa uchunguzi kuzuilia washukiwa kwa siku 14,” akasema Bi Wachira.
Kesi hiyo itatajwa Mei 28.

Mshukiwa wa kiume anadaiwa kuwa mpenzi wa mke wa mwendazake.

Kulingana na afisa mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Murang’a Kaskazini, Bw Japheth Maingi, viatu alivyokuwa amevaa Gitu vilipatikana na damu alipokamatwa. Viatu hivyo vinadaiwa kuwa vya mwalimu mkuu aliyeuawa.

“Tulipomshika Gitu alikuwa na damu katika viatu na nguo zake na tunaamini amehusika na mauaji,” akasema afisa huyo.

SHANGAZI: Nataka kumsahau mpenzi lakini nalemewa na hisia

Na SHANGAZI SIZARINA

Kwako Shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 22. Sijaolewa lakini nilizaa mtoto na mwanamume tuliyekuwa wapenzi. Punde tu nilipojifungua, tulianza kukosana na hatimaye tukaachana aliponitambulisha kwa mpenzi wake mwingine. Muda si mrefu, waliachana na tangu hapo tumekuwa tukikutana na kufurahia mahaba kama awali. Hata hivyo, nataka kumsahau ili niendelee na maisha yangu lakini nimeshindwa kwa sababu nampenda sana. Nipe ushauri.
Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, nahisi kuwa unajaribu kubishana na moyo wako. Ukweli ni kwamba, hutaki kumuacha mwanamume huyo kama unavyodai kwa sababu unamalizia kwa kukiri kuwa unampenda sana. Na hiyo ndiyo sababu yako kumkaribisha tena katika maisha yako baada yake kuachana na mpenzi aliyemfanya akuache. Kama yuko tayari mrudiane, acha maringo. Isitoshe, ndiye baba ya mtoto wako.

 

Kumbe ni kiruka njia
Vipi Shangazi. Nina kijana mpenzi wangu ninayempenda sana. Hata hivyo, juzi niliona kwenye mitandao msichana mwengine aliye na jina sawa na langu ambaye wanaitana wapenzi. Je, nimuache?
Kupitia SMS

Kama unayosema ni ya kweli, basi ina maana kuwa huyo unayemuita mpenzi wako si mwaminifu bali ni ndumakuwili. Sasa umejua kuwa ana mpenzi mwingine kwa hivyo utaamua mwenyewe iwapo utamuacha ama utaendelea kumvumilia na tabia yake hiyo.

 

Baba mzazi aniwinda
Shikamoo Shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 16 na nina tatizo ambalo nataka unisaidie kutatua. Baba yangu mzazi amekuwa akitaka tushiriki mahaba na nimeshindwa nitafanya nini.
Kupitia SMS

Maajabu ya ulimwengu hayo! Siamini kuwa baba mzazi anaweza hata kufirikia kushiriki tendo hilo na binti yake mwenyewe. Usikubali kamwe kwani kitendo hicho ni mwiko katika jamii nzima ya binadamu. Pili, mfahamishe mara moja mama yako kuhusu jambo hilo. Kama mama yako hayupo, mwambie jamaa yako mwingine uliye karibu naye ili akupe mwelekeo zaidi.

 

Mimi kivutio kwa vipusa
Hujambo Shangazi. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 22. Ninashangaa kwamba, warembo wanapenda sana kunifuata wakinitaka, si kwa simu, si kwa mitandao. Sijui nina jini la kupendwa ama vipi. Nishauri.
Kupitia SMS

Je, ina maana kwamba unalalamika kwa kupendwa ama nini? Mimi ninaamini kuwa mtu hupendwa kutokana na maumbile au tabia yake. Hayo yako eti una jini la kupendwa mimi siyajui. PiIi, unafaa kushuruku badala ya kulalamika kwa sababu kuna wenzako ambao wamekuwa wakisaka wapenzi kwa muda mrefu bila kufaulu.

 

Nifanyeje nipate mpenzi?
Kwako Shangazi. Nina umri wa miaka 26 na natamani sana kuwa na mpenzi. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Kazi yangu katika safu hii ni kutoa ushauri wala si kusaidia watu kutafuta wapenzi. Kama wewe ni mwanamume, itabidi ujitahidi kutafuta mpenzi la sivyo utaishi pweke. Kama wewe ni mwanamke, kuwa na subira na ujaribu kutangamana na wanaume wala si kuketi kitako nyumbani ukitarajia mpenzi aanguke kutoka angani.

 

Mke alianza kuzurura nje
Shangazi naomba ushauri wako. Nilikuwa na mke na tukajaliwa mtoto mmoja ambaye ninampenda sana naye pia ananipenda. Lakini mke wangu alianza kutembea sana nje na nikalazimika kumuacha. Alirudi kwao na mtoto na sijui nitafanya nini ili nimpate mtoto wangu. Nisaidie tafadhali.
Kupitia SMS

Wazazi wanapotengana na kukosa kupatana kuhusu ni nani kati yao anayefaa kuishi na mtoto au watoto, mzozo huo hutatuliwa mahakamani. Kama mke wako amekataa na mtoto na unahisi wewe ndiye unayefaa kuishi naye, itabidi utafute suluhisho kortini.

 

Nikimkumbuka nalia
Nina miaka 45. Mpenzi wangu alifariki. Usiku silali. Nikimkumbuka nalia tu. Nitafanya nini?
Kupitia SMS

Pole zangu nyingi kwa kumpoteza mwenzako. Kuombeleza na kukubali kwamba umempoteza mwenzako sio jambo la siku moja. Huchukua hatua moja hadi nyingine hadi pale akili na mwili wako vitakapokubali kwamba mwenzako hayuko tena. Lia pale unapojisikia kufanya hivyo, mwandikie barua pale unapohisi unashindwa kumtoa mawazoni. Zungumza na watu wa karibu nawe kuhusu unavyojisikia. Lakini ukiona haya yote hayasaidii, ni vizuri umuone mshauri nasaha.

 

Mwanamume kumlipa mkewe wa zamani Sh127,000 kila mwezi

Na RICHARD MUNGUTI

JUHUDI za mwanaume za kupunguziwa mzigo wa kumtunza na kumpa mkewe aliyemtaliki kitita cha Sh127,000 kila mwezi maisha yake yote hapa ulimwenguni iligeuka kuwa kufukuza kifuli baada ya mahakama ya upeo kumwamuru abebe mzigo wake.

Jaji Mkuu David Maraga pamoja na majaji wengine wanne walimwamuru Charles Michael Angus Walkers Munro aendelee kumlisha vinono mkewe ambaye ndoa yao ilijikwaa kisha wakatalikiana.

Majaji hao walikataa kukubalia ombi la Munro kwamba yeye ama mwanaume mwingine yule aliyetalikiana na mkewe hapasi kumsaidia ama kumtunza ikiwa yuko na mapato.

Lakini majaji hao walikataa na kusema vinono na maisha ya bashasha ambayo mwanaume humzoesha mkewe atavigharamia hadi kifo kitakapowatenganisha.

“Hili ni suala la kijamii linalohusu mtu na mkewe. Hatuna mamlaka kisheria kuingilia na kuvuruga maagizo mume awe akimlipa mkewe kiasi kilichowekwa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama kuu,” walisema majaji watano wa Mahakama ya Juu wakiongozwa na Jaji Mkuu (CJ) David Maraga.

Uamuzi huo ulitowesha matumaini ya Bw  Bw Charles Michael Angus Walkers Munro kupunguziwa gharama za kumtunza mkewe aliyemtaliki.

Pia wanaume wengine waliokuwa wanasubiri kwa hamu na ghamu uamuzi huo ndipo wapunguziwe gharama za kuwatunza wake wao waliowapiga teke ziligonga mwamba.

Jaji Maraga na Majaji Jackton Ojwang , Njoki Ndung’u na Smokin Wanjala walikataa kubatilisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ambapo Bw Munro aliagizwa awe akimtunza mkewe na kumpa vinono alizomzoesha nchini Uingereza na humu nchini.

Majaji hao walisema suala la talaka sio suala la kikatiba bali ni suala la kijamii na  “hawana mamlaka kisheria kuvuruga uamuzi uliopitishwa na mahakama ya rufaa na mahakama kuu.”

Majaji hao walisema lazima Bw Munro aendelee kufadhili raha za mkewe waliyetengana.

Bw Munro ambaye ni raia wa Kenya alikuwa amewasilisha rufaa kupinga agizo awe akimlipa mkewe Bi Pamela Ann Walker Munro kitita cha Sh127,000 kila mwezi baada ya kumtaliki.

Bi Pamela Ann ambaye ni raia wa Uingereza alikuwa amefunga ndoa na Bw Munro na ndoa yao haikujaliwa watoto.

 

Mapato ya juu

Katika rufaa yake,  Bw Munro alikuwa amesema mkewe huyo waliyetangana  “anaweza kujikimu kimaisha kwa vile alikuwa na mapato ya juu.”

Bw Munro alikuwa amedokeza Pamela Anne alikuwa na nyumba nchini Uingereza na alikuwa anapokea pensheni ya mumewe wa kwanza aliyekuwa afisa wa Kijeshi.

Alisema jumba hilo la kifahari liko ulaya na alilikodisha walipokuwa wanahamia nchini Kenya. Makazi yao humu nchini yalikuwa kaunti ya Kilifi.

Lakini walipotengana mwaka wa 2013 Jaji Christine Meoli aliambiwa Bw Munro alihama na kurudi Uingereza na kumwacha mkewe Kilifi.

Mkewe huyo alimweleza Jaji Meoli mumewe alimwacha kwa upweke na kushikana na wanawake wengine kuponda raha.

Pamela alikuwa ameomba mahakama iamuru Bw Munro awe akimlipa Sh250,000 kila mwezi.

Bw Munro alisema yeye ndiye mume wa pili kumuoa Pamela na kwamba “hastahili kumuongezea pesa juu ya pesa.”

Katika rufaa aliyowasilisha mbele ya Majaji Milton Asike Mahakhandia,William Ouko na Kathurima M’Inoti , Bw Munro alilalamika Sh127,000 alizoagizwa na Jaji Meoli awe akimlipa mkewe ni nyingi zapasa kupunguzwa.

Wakauliza, “Mbona sasa Bw Munro anataka kubanduka ilhali alikuwa amemzoesha mkewe maisha ya juu. Lazima aendelee kumweka katika maisha aliyomzoesha.”

Majaji hao walisema hawatakuwa na utu endapo watabatilisha uamuzi wa Jaji Meoli.

“Ulimzoesha mkeo vinono na maisha ya kifahari, endelea kuyagharamia,” waliamuru majaji hao.

Pasta amfurusha mke kwa kutisha kusambaratisha kanisa

Na CORNELIUS MUTISYA

NZAIKONI, MACHAKOS

PASTA wa kanisa moja eneo hili alimfurusha mkewe akidai alikuwa amechoshwa na tabia yake ya udaku. Jamaa alisema tabia ya mkewe nusura isambaratishe kanisa lake na hangemvumilia.

Kulingana na mdokezi, pasta alifungua kanisa hapa na likavutia watu wengi. Waumini walikuwa wakifurika kanisani kupata chakula halisi cha roho.

Inasemekana kwamba mkewe alipewa jukumu la kuwapa ushauri nasaha wanawake kanisani.

Hata hivyo, wanawake hao hawakuwa na imani na uongozi wake wakidai alikuwa mwenye kiburi na mjeuri kupindukia.

Yasemekana alikuwa akiwasengenya akina mama hao kokote alikoenda.

Hata akiwa saluni, ama akinunua mboga sokoni, alikuwa akieneza porojo kuhusu vile wanawake wa kanisa la mumewe walikuwa wachoyo, washamba na waliokosa hadhi ya kuitwa wanawake kwa sababu ya kutojua kujipodoa.

Kulingana na mdokezi, wanawake hao walipochoshwa na udaku mke wa pasta, walianza kususia ibada.

Hata hivyo, mmoja wao aliwashauri wamjulishe pasta wao kabla ya kuchukua hatua yoyote.

“Akina mama hao walimwendea Mtumishi wa Mungu ofisini na wakamueleza malalamishi yao. Pasta aliwaomba radhi na akawaahidi kuchukua hatua muafaka,’’ akasema mpambe wetu.

Duru zaarifu kuwa, pasta alifululiza hadi nyumbani na kumuamuru mkewe kufunganya virago vyake na kutokomea kwa kumharibia sifa.

“Siwezi nikakubali kanisa langu lisambaratike kwa sababu ya sususu na umbea wako. Nenda zako. Wewe ni bure kabisa!’’ pasta alimfokea mkewe.

Twaarifiwa kwamba, mke wa pasta alifunganya virago vyake na kutokomea kusikojulikana. Aliacha nyuma watoto wawili ambao wanaendelea kutunzwa na baba yao huku kanisa likizidi kushamiri.

…WAZO BONZO…

 

 

Atwangwa na mkewe kama mburukenge kwa kutomnunulia nyama

Na BENSON MATHEKA

GITHUNGURI, KIAMBU

WAKAZI wa hapa, waliachwa vinywawazi baada ya jombi kupokonywa mboga na kutandikwa na mkewe kama mburukenge akimlaumu kwa kutomnunulia nyama.

Mwanadada huyo huwa anauza bidhaa sokoni kuchuma riziki.

Yasemekana kidosho huyo hakuweza kwenda kufanya kazi yake sokoni kwa sababu ya mvua mkubwa na mumewe akachukua jukumu la kununulia familia yake ilichohitaji.

Siku ya kisanga, jamaa alienda kazini ilivyokuwa desturi yake.

“Aliomba ruhusa kazini na kuondoka mapema kuliko kawaida na akiwa njiani kurudi nyumbani, aliamua kupitia katika kituo cha biashara ili ajirudishie mkono kwa kuchapa kazo nzito siku nzima,” alisema mdokezi,

Inasemekana kuwa jamaa alijitosa kilabuni na kuagiza vikombe kadhaa vya ‘Keg’ ndipo akalewa chakari.

Kulingana na mdokezi, hata baada ya kulewa, jamaa hakusahau jukumu lake la kununulia familia chakula. Alielekea dukani akanunua unga na mboga.

Inasemekana alipofika nyumbani badala ya mkewe kumpokea, alianza kumrushia cheche za matusi.

“Kitu gani mbaya na wewe? Kwa hivyo badala ya kutununulia vitu nzuri kama nyama unanunua mboga.

Kwani unafikiri sisi ni sungura wa kutafuna matawi kila siku? Mwanamume gani usiye na akili wewe. Nitakuonyesha jinsi wanaume kama wewe hufunzwa na kupata akili,” alichemka mama huyo.

Inasemekana kuwa mama watoto alimpokonya mumewe mboga na kurushia kondoo wake kabla ya kumtwanga mangumi na mateke. “Jamaa alipiga nduru zilizowavutia majirani,” alisema mdokezi.

Iliwabidi majirani hao kungilia kati na kumuokoa jamaa huku wakimlaumu mama kwa kumdharau mumewe.

Haikujulikana uhusiano wake na mkewe ulivyoendelea baada ya kisa hicho.

…WAZO BONZO…

Ajuta kujaribu kumtia mumewe kiganjani

Na LEAH MAKENA

GITEMBENE, MERU

Mama wa hapa alipatiwa talaka  kwa kuweka akiba kisiri ili ajenge nyumba ya kifahari. Mama alikuwa na mshahara mnono na akaamua kuweka pesa akiwa na lengo la  kujenga nyumba na kumweleza mumewe baada ya kuikamilisha. 

Mumewe hakuwa na kazi nzuri na mapato yake yalikuwa kidogo mno.

“Nia ya mama ilikuwa kumpunguzia mumewe mzigo kwa sababu mapato yake yalikuwa ya chini sana. Alitaka familia yake kuwa na maisha mazuri,” alisema mdokezi.

Inasemekana kuwa mama alichukua mkopo  benki ili kuharakisha ujenzi wa nyumba hiyo na akaamua kulipa madeni yote bila kumhusisha polo.

Haikujulikana jinsi mumewe alivyogundua siri ya mama ila alimpigia simu akiwa kazini na kumtaka kujipanga kuondoka kwake.

Jioni ya kisanga, mama alifika na kupata begi la nguo nje huku jamaa akitetemeka kwa hasira.

“Yaani unanifanya kutoa jasho kushughulikia mahitaji yote ya nyumbani ilhali unachukua loni kujengea uwapendao majumba makubwa? Huu uwe mwisho wangu na wewe kwani umekuwa kero kwangu,” jamaa aliteta.

Juhudi za mama za kujaribu kujitetea hazikufua dafu kwani polo aliendelea kubishana akidai jengo lililokuwa likikamilika halikuwa lao.

“Siwezi kuishi katika nyumba ambayo sikuhusika kujenga. Ulikuwa unaficha nini iwapo ulikuwa na nia nzuri?” mzee aliwaka.

Ilibidi mama kuzoa kilichokuwa chake na kuondoka huku polo akiapa kulisha watoto pekee yake na kumlaumu mkewe kwa kuficha siri kubwa kama hiyo.

Haikujulikana iwapo jamaa alibadilisha nia  baadaye mkewe kuwajulisha wazee wazungumze naye apate kujua ukweli wa mambo.

…WAZO BONZO…

FUNGUKA: Nachuuza mke wangu nipate hela

 

Na PAULINE ONGAJI

Japo mwanzoni nilionekana kukerwa na tabia hii, mke wangu alinishawishi akisema kwamba ingekuwa fursa murwa ya kuangamiza ufukara uliotukodolea macho kwa kumwalika mwanamume huyo kwenye meza yetu na kumhadaa kuwa mimi ni dadake – Vitalis

Kuna dhana kuwa kati ya jinsia mbili zinazotambulika, hakuna watu waliojawa na wivu kama wanaume.

Hii ni hasa inapowadia katika masuala ya mahaba ambapo ni dhahiri kuwa wanaume hupata maumivu makali mwanamke wampendaye anapoamua kugawa asali pembezoni.

Kwa mfano ni rahisi kwa mwanamke kumsamehe mwanamume anapomlaghai katika uhusiano, lakini huwia vigumu wanaume kufanya hivyo.
Hili linadhihirishwa kila tunaposikia visa vya wanaume kuwaua wapenzi wao kwa sababu ya udanganyifu katika uhusiano.

Lakini kwa Vitalis mambo ni tofauti sana. Huku wanaume wengi wakiwakinga wapenzi, wachumba na wake zao kutokana na macho ya madume wenye tamaa, bwana huyu anafanya kila awezalo kuwavutia madume wenzake kwa mkewe Rita.

Wawili hawa wameoana kwa miaka minne na wana watoto wawili lakini penzi lao ni la kushangaza ajabu. Kwanza kabisa hawana ajira na wamekuwa wakitegemea fedha kutoka kwa wanaume wengine kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Vitalis amekuwa akimchuuza mkewe kwa wanaume hasa wa kizungu huku wawili hawa wakijifanya kuwa mandugu kila wanapokutana na windo lao.
Kulingana na Vitalis tabia hii ilianza miezi michache baada ya kuoana.

“Nilikuwa nimefanya kibarua na kupata senti kidogo ambapo niliamua kumpeleka mke wangu angaa katika mkahawa wa kifahari ili kupata kikombe cha kahawa.

Kutokana na umbo lake la kupendeza na urembo wake wa kipekee alivutia macho ya wengi mle ndani. Hasa alinasa macho ya bwana mmoja wa kizungu ambaye alikuwa akimkodolea macho bila haya.

Japo mwanzoni nilionekana kukerwa na tabia hii, mke wangu alinishawishi akisema kwamba ingekuwa fursa murwa ya kuangamiza ufukara uliotukodolea macho kwa kumwalika mwanamume huyo kwenye meza yetu na kumhadaa kuwa mimi ni dadake.

Kwa hivyo tulimualika na hata kuagiza vinywaji kwa pamoja. Baadaye ilikuwa kawaida kwa dume hilo kututembelea nyumbani kwetu ambapo alimchumbia mke wangu kwa miaka miwili tukiwa pamoja.

Mojawapo ya maagano kati ya yake na mke wangu ilikuwa kununua nyumba na kuwekeza hapa Kenya. Kutokana na kuwa kaka huyo alikuwa ameduwazwa na penzi la mke wangu, katika kipindi cha miezi sita alikuwa ashatimiza haya lakini pindi alipoanza kusisitiza amzalie mtoto, binti akachana mbuga na kutoweka na mali yote.

Tokea tuanze biashara hii tumehadaa wanaume watano wa kizungu na hata kuna wengine ambao wanazidi kukidhi mahitaji yangu na mke wangu huku wakidhani kuwa mimi ni kakake.

Tumekubaliana kufanya hivi huku mke wangu akihitajika kuwa mwangalifu asishike mimba za hawa madume wala kuwazia suala la ndoa.

Tuliamua kufanya hii kazi baada ya kujaribu kutafuta ajira kwa miaka bila mafanikio na kutokana na kuwa tulikuwa tunapendana na hatungeachana kwa sababu ya ufukara, tulitafuta mbinu mbadala kujipatia riziki.

Kupitia kazi hii tumefanya mambo kadha ikiwa ni pamoja na kununua majumba mawili ya kifahari jijini Nairobi na Mombasa, bali na kununua magari kadha na kuwapeleka watoto wetu katika shule za kifahari.

Sasa tumeanza kupanga mikakati ya kuwekeza ili angaa tutulie kama familia”.

Taabani kwa kugeuza kondoo wa babake mke na ‘kurina asali’ mara saba

Na TITUS OMINDE

MWANAMUME wa umri wa miaka 30 alifikishwa katika mahakama moja mjini Eldoret kujibu mashtaka ya kushiriki ngono na kondoo wa babake.

Mlalamishi Sang Kibii ambaye ni baba wa mshtakiwa alisababisha kicheko kortini alipodai kuwa mwanawe amekuwa akishiriki tendo hilo na kondoo wake kwa zaidi ya mara saba.

Maelezo ya mashtaka yalisema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Aprili 13 mwaka huu kaitka eneo la Chepkanga viungani mwa mji wa Eldoret.

Mshtakiwa William Kipchirchir Kibii ambaye alikana mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu wa Elodret Bw Charles Obulutsa, alionekana kujikanganya pale alipokiri kuwa amewahi kushiriki ngono na kondoo huyo mara moja wala si mara mbili kama ilivyodaiwa.

Juhudi za mahakama kushawishi pande mbili husika kutafuta suluhu nje ya mahakama ziligonga mwamba kwani babake mshtakiwa aliambia mahakama kuwa tabia ya mwanawe ilikuwa imezidi ambapo alitaka apate funzo kupitia kwa sheria.

“Mheshimiwa nimechoshwa na kijana wangu ameshindwa kutafuta mke badala yake amebadilisha kondoo wangu kuwa mke wake,” aliambia mahakama  mzee mwenye ghadhabu.

Mahakama iliamuru mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu ya Sh10,000, kesi hiyo itasikizwa Aprili 25 mwaka huu.

Tetesi kasisi alitumia ndumba kupora mke

Na CORNELIUS MUTISYA

NZAIKONI, MACHAKOS

Pasta mmoja wa eneo hili ameingiwa na kibaridi baada ya tetesi kutanda mtaani kuwa alitumia nguvu za giza kumzamisha mume wa muumini wake aliyekuwa hasimu wake mkuu ili amchukue mkewe!

Kulingana na mpambe wetu, pasta huyo alikuwa akishukiwa kuwa na uhusiano wa kimahaba na mke wa jamaa huyo.

Tetesi hizo zilitanda mitaani mithili ya cheche za moto nyikani na zikamkera mno kalameni huyo.

“Uvumi kuwa pasta alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa polo huyo zilimchongea. Uadui ulizuka baina ya mtumishi wa Mungu na mume wa mwanamke huyo,’’ alieleza mdaku wetu.

Inasemekana kwamba, ili kulipiza kisasi, mume wa mwanamke huyo aliyekuwa ameteuliwa kiongozi wa wanawake kanisani humo alianza kuambia watu eti pasta huyo alikuwa Mfarishayo aliyekuwa akihubiri maji na kubugia mvinyo!

“Alieleza watu kwamba pasta alikuwa mzinifu mkuu na kwamba alitumia wadhifa wake kuvuruga boma za watu.

Aliapa kumkomesha pasta huyo kwa mbinu ambazo hakueleza watu,” alisema mdokezi.

Uhasama wa polo na pasta ulizidi na kufikia kilele walipokutana kisadfa njiani na polo akamchapa akimlaumu kwa kumnyemelea mkewe.

Hata hivyo, pasta alimuambia polo ya kwamba baada ya muda wa wiki mbili, angekiona cha mtema kuni.

“Vitisho vya pasta huyo vilitimia kikamilifu wakati polo huyo alipoanza kudhoofika mwili na kutatizika akili,’’ alisema mdaku wetu.
Wakazi walidai alimroga jamaa huyo ili amnyakue mkewe.

Kwa sasa, pasta huyo anaogopewa mno eneo hili na hakuna mtu yeyote anayethubutu kumchezea wengi wakimtaja kama “moto wa kuotea mbali.”

…WAZO BONZO 1…
…WAZO BONZO 2…
…WAZO BONZO 3…

Ajitia kitanzi akilalamikia kuchoshwa na mkewe

BARACK ODUOR na CHARLES WASONGA

MWANAMUME mmoja katika kaunti ya Homa Bay Alhamisi alijiua katika mti wa maembe kwa madai kuwa alikuwa “amechoshwa” na mkewe.

Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Kowuor, kaunti ndogo ya Rachuonyo Mashariki.

Chifu wa eneo hilo Kennedy Otieno alisema kuwa mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 30 alijua kwa kamba ya mkonge nyumbani kwake baada ya kumtumia dadake ujumbe mfupi akimwambia kuwa “nimechoshwa na mke wangu.”

Kulingana na chifu huyo mwanamume huyo hakufafanua sababu iliyopelekea yeye kusinywa na mkewe kiasi cha kujinyonga.

Kamanda wa Polisi kaunti ya Homa Baye Marius Tume alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa maafisa wake wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kifo hicho.

Mwili wa marehemu umepelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Rachuonyo Kusini kufanyiwa upasuaji.

 

Buda afumania mkewe peupe akigawa asali sebuleni

Na BENSON MATHEKA

EMBAKASI, NAIROBI

KALAMENI wa hapa hakuamini macho yake alipompata mkewe akigawa asali kwenye kochi katika sebule ya nyumba yake.

Inasemekana badala ya kuaibika baada ya kufumaniwa, mwanamke huyo ambaye ni mama ya watoto wawili wanaosomea shule za mabweni alimkabili mumewe na kumlaumu kwa kutomkata kiu ya uroda.

Kulingana na mdokezi wetu, jamaa ambaye ni afisa katika shirika moja la kiserikali, alikuwa na tabia ya kutumia muda wake vilabuni akipiga soga na marafiki na mkewe alikuwa akidai kwamba akifika nyumbani alikuwa akilala fofofo.

“Mkewe aliamua kutafuta mwanamume wa kumtimizia mahitaji yake ya uroda. Alidai kuwa mumewe alikuwa ameshindwa na majukumu yake ya unyumba na akafaulu kumpata jamaa ambaye alikuwa akimwalika nyumbani mumewe akiondoka,” alieleza mdokezi.

Siku ya kisanga,  mumewe aliondoka kwenda kazini lakini  wakubwa wake wakamweleza alitakiwa kwenda nje ya nchi jioni kwa ziara ya kikazi.

Walimwambia arudi nyumbani kujiandaa kusafiri jioni hiyo. Ni alipofika nyumbani alipompata mkewe akiendelea kurushana roho na mpango wake wa kando.

Kulingana na mdokezi, hata kabla ya kalameni kutamka lolote, mkewe alimkabili kwa maneno huku jamaa aliyefumaniwa akiramba asali ya mwenyewe akitulia.

“Usijaribu kumguza huyu jamaa.  Umeshindwa na kazi na  ni mimi niliyemwalika hapa kunishughulikia. Unafaa kuniuliza mimi kama una la kusema,” mama alimwambia mumewe.

Kalameni alihema kwa hasira, chozi likamtoka, kisha akamweleza mkewe kwamba amempa ruhusa ya kuendeleza nderemo zake na jamaa huyo.

Hata hivyo, aliwaambia hiyo ilikuwa siku ya mwisho kutumia nyumba yake kama danguro.

Alimsimamia mkewe akakusanya virago vyake kisha akaondoka na jamaa huyo na haikujulikana kilichojiri baada ya jamaa kurejea kutoka ziara ya kazi.

…WAZO BONZO…

 

SHANGAZI: Kila niendapo kwa duka lake, hulalama kuhusu mumewe

Mimi ni kijana na nilioa miaka mitatu iliyopita. Nina mtoto mmoja. Tatizo ni kwamba, kuna mwanamke mwenye biashara ya nguo. Niendapo kununua wakati ninapotoka, yeye huniandama na kunilalamikia kuhusu mume wake. Nifanyaje?
Kupitia SMS

Watu hulemewa na matatizo na huwa wanatafuta jinsi ya kutua mzigo wa mawazo na hofu. Hivyo labda huyu dada ameona unaweza kumsikiliza na kumsaidia kutua aliyo nayo. Hata hivyo ni muhimu kuwa mwangalifu ili usijipate umetekwa kimapenzi. Ni vizuri kufafanua kwake kwamba nia yako ni kumsikiliza na labda kumpa usaidizi wa kupata suluhu na wala sio vinginevyo.

 

Natafuta mke wa mtu
Naitwa Maguta kutoka Narok. Nina mke na watoto wawili. Natafuta wanawake wanene na pia wake za watu. Aliye tayari ajitokeze. Kupitia SMS

Nadhani unatamani kupigwa, ama umechoka kuishi.

 

Nashuku nina mimba
Mimi ni msichana wa umri wa miaka 24. Nina mume ambaye nikilala naye natokwa na maji na nina mimba ya miezi sita. Niko Mombasa. Kupitia SMS

Unapokuwa mjamzito ni muhimu mno kuwa makini na kinachoendelea mwilini mwako hasa inapohusu burudani. Siwezi kujua kwa uhakika kama hali hiyo ni kawaida ama la. Bali itakuwa vyema umuone daktari,akuangalie na akupatie jibu la kitaalamu. Kwa sasa pumzisha burudani na mumeo hadi utakapomuona daktari.

 

Namtafuta kidosho
Mimi ni kijana wa umri wa miaka 25. Natafuta mpenzi. Awe anajiweza na umri wa miaka 30. Awe Muislam hasa Muarabu. Kama uko jitokeze.
Mohamed. Mombasa. Kupitia SMS

Natumaini unayemtafuta atajitokeza.

 

Ninachukia wanaume
Nina umri wa miaka 19. Sina mpenzi na wanaume watatu wananiandama. Nawachukia wanaume. Je, hii ni sababu ya kukosa mpenzi? Nifanyaje waache kunifuata? Kupitia SMS

Inawezekana pia umri wako unachangia pakubwa hiyo chuki uliyo nayo kwa wanaume. Ingawa pia inaweza kuwa mambo yaliyokutokea wakati unakua ama yale ambayo uliyashuhudia kuhusiana na wanaume. Jipatie wakati ukue, ukomae zaidi.

 

Kuna dawa ya chuma?
Chuma changu ni nchi nne unusu. Je, ni kidogo? Na kuna dawa? Kama ipo inaitwaje? Niipate wapi? Hussein Ali. Umri wangu ni miaka 24.
Kupitia SMS

Haya maswali yako ni kama ya afisa wa upelelezi. Huna haja ya kujiuliza haya yote, bali unatakiwa kulenga mbinu na jinsi za kutumia ulicho nacho kumfurahisha mwenzako. Kwani raha ya mapenzi sio ukubwa wa chuma, bali mbinu za kukitumia.

 

Niko tayari kumwoa
Nina umri wa miaka 20. Jina langu ni Bihija. Niko tayari kuishi na Twaha. Kupitia SMS

Natarajia huyo mwenzako amesikia mwitikio wako.

 

Nampenda lakini hajui
Naitwa James kutoka Thika. Kuna mrembo ninayempenda sana lakini sijamwambia. Kwani yuko sekondari na nataka kumpa muda amalize. Lakini naogopa atapatwa na mwingine.
Kupitia SMS

Kama kweli unampenda, mpatie nafasi amalize masomo, kabla ya kuchafua akili yake na masuala ya mahaba.
Naogopa lakini namtaka

 

Naogopa wa kando sababu nimeokoka
Nimeolewa na nina mtoto mmoja wa kike. Mume wangu ananipenda sana. Lakini kuna jamaa ana mke na mtoto mmoja alinipenda. Lakini hatujakutana kimwili. Tatizo ni kwamba naogopa sababu nimeokoka lakini nisipoona sura yake sina raha.
Kupitia SMS

Majaribu na vishawishi ni kawaida katika ndoa na hata mahusiano. Tofauti inakuja jinsi unavyosuluhisha roho yako na uweze kuishi na amani. Kitu gani hasa unachokosa kwa mumeo ambacho unadhani utakipata ukienda nje. Labda hilo ndilo swali kubwa la kujiuliza na ujijibu na kisha uamue.

 

Ana wivu ajabu
Nimeolewa na mume wangu ana mwanamke pembeni. Na akiniona na mwanaume anakasirika. Niko Mombasa.
Kupitia SMS

Ina maana mmeoana na nyote wawili mnachakachua nje? Hii ni ndoa ama maradhi?

 

Ni ugonjwa ama nini?
Mimi nina mke na umri wangu ni miaka 22. Nikirushana roho ni raundi moja tu. Huu ni ugonjwa ama uzima? Kupitia SMS

Kwa kweli hapo mwanangu siwezi kujua. Wewe wajielewa na mwili wako vyema zaidi.

 

Pasta ashangaza kuomba waumini idhini afurushe mkewe

Na TOBBIE WEKESA

KABATI, MURANG’A

PASTA wa kanisa moja la hapa aliwaacha wengi vinywa wazi alipowaomba ruhusa waumini ili amtimue mke wake.

Inasemekana pasta alitangazia waumini masaibu aliyokuwa akipitia mikononi mwa mkewe na akawaomba ruhusa aweze kumfurusha.

Kulingana na mdokezi, pasta alichukua nusu saa kuelezea kanisa sababu za kufikia uamuzi huo. Kulingana na pasta, mkewe alikuwa mtu asiyeaminika  katika ndoa.

“Nikiondoka kwenda semina, mke wangu pia huondoka. Haendi kwao. Anakoenda mimi sijui,” pasta alieleza.

Kila mtu kanisani alikuwa ange kumsikia pasta. Wengi waliofahamu tabia  za mkewe walitabasamu. Penyenye zinasema mkewe alikuwa  akimcheza pasta  kwa muda mrefu.

Kila wakati pasta akiondoka nyumbani kwenda mikutano ya maombi, kipusa alikuwa akiondoka kwenda kwa mipango ya  kando.

Pasta alieleza namna alivyong’ang’ana na majukumu nyumbani hata mkewe akiwa.

“Ni Mungu tu amenitunza. Nimepitia mengi. Naomba idhini yenu ili nimtimue,” pasta alieleza.

Duru zinasema kabla ya kanisa kuanza, mwanadada huyo alikuwa amegundua mipango ya pasta. Aliamua kuondoka mapema akihofia kuaibishwa.

“Kama ni hayo unayopitia, pasta ruhusa tumekupa na utafute mwanadada mwingine atakayekutunza,” muumini mmoja alisimama na kumueleza pasta.

“Nimechoka kusikia hadithi mtaani. Jina langu limeharibika. Mke wangu hatulii. Sijui ameingiliwa na shetani gani,” pasta akasema.

Kulingana na mdokezi, waumini wote walikubaliana kwa kauli moja kumuunga pasta.

“Mfukuze. Tutakusaidia kupanga harusi nzuri. Huyo mke hata sisi tunajua mienendo yake,” muumini mmoja alisema kwa sauti huku wenzake wakikubaliana naye.

…WAZO BONZO…

Mke wa mwanamume achukuliwa na mwenzake baada ya kupoteza ubashiri wa mechi

Na CHRIS ADUNGO

MWANAMUME mmoja atatazama kupoteza mkewe na kulala chumbani kwa rafiki yake wa kamari kwa wiki nzima baada ya kupoteza ubashiri wa mechi ya Man City dhidi ya Man United Jumamosi.

Kwenye makubaliano waliyoandikiana kwa mkono kwenye kijikaratasi, wanaume hao wawili kutoka Tanzania, kila mmoja aliapa kumpa mwenzake mkewe kwa muda wa wiki moja endapo angeshindwa kwenye utabiri wa matokeo ya mechi hiyo.

Ingawa Taifa Leo haiwezi kuthibitisha ukweli wa makubalino hayo yaliyosambazwa mitandaoni, mmoja wa wanaume hao sasa huenda akampoteza mkewe baada ya Man United kupigana kufa kupona na kuweza kuilaza Man City 3-2 katika mechi iliyochezwa uwanjani Etihad.

Makubaliano kati ya Amani Stanely na Shilla Tony kabla ya mechi ya debi ya Manchester. Picha/ Hisani

Katika kijikaratasi hiki hapa juu, Amani Stanley, ambaye ni shabiki sugu wa Man City, aliweka mkewe kama dhamana kabla ya timu yake kupigwa, huku mwezake Shilla Tony pia akikubali kupena mkewe Man United ingelimwa.

Ikiwa makubaliano haya yalikuwa ya kweli, basi utakuwa ni mfano wa hivi karibuni wa mashabiki sugu kusahau thamani ya pesa na badala yake kutumia wake zao kama dhamana katika ubashiri wa mechi.

 

 

Polo aliyeokoka afichulia waumini yeye ni mpenziwe mke wa pasta

Na SAMMY WAWERU

KANDARA, MURANG’A

WAUMINI wa kanisa moja mtaani hapa walipigwa na mshangao jamaa aliyeamua kuokoka alipodai alikuwa na mpango wa kando wa mke wa pasta.

Jamaa alimwaga mtama na kuaibisha mke wa pasta huku mumewe akitoka na kupoteza fahamu.

Inasemekana polo alijiunga na kanisa hilo kufuatia ushawishi wa pasta na mkewe kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Pasta na mkewe walikuwa wakialika kalameni kwao kumhubiria aokoke,” alieleza mdokezi wetu.

Siku ya kioja pasta alieleza washirika wa kanisa hilo kuwa alikuwa na ujumbe maalum kwao.

“Leo tumejaaliwa kuwa na mgeni, ni kijana ambaye mimi na mke wangu tumefanya kila tuwezalo kumnusuru kutoka ulevini,” alisema mhubiri huyo akialika jombi kutoa ushahidi.

Jamaa alijitambulisha, na kushukuru mtumishi wa Mungu kwa dhati kwa kumgeuza kuwa kiumbe mpya. Alikuwa mcheshi, ambapo kanisa liliangukia kicheko kutokana na aliyosimulia.

Hata hivyo, kanisa lilitulia kama maji mtungini aliposema ana ujumbe maalum aliotaka ujulikane. “Kusema ukweli nina kila sababu ya kutabasamu na kumshukuru pasta kwa kunikomboa.

Naomba mtumishi wa Mungu unisamehe kwa kuwa nusura nivunje ndoa yako kwa kuwa nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wako, nilikuwa mtenda dhambi lakini naungama makosa yangu,” alitangaza kalameni.

Waumini walijishika tama, kwa siri iliyofichuka wakifahamu fika kuwa mama huyo alikuwa katika mstari wa mbele kanisani kukashifu usinzi kwenye ndoa.

Pasta alipoteza fahamu na kupelekwa katika chumba maalum ili kufanyiwa huduma ya kwanza. Mkewe alionekana akimwaga machozi na kuomba msamaha kwa kanisa.

…WAZO BONZO…