Otieno akwezwa cheo FKF huku Muthomi akichunguzwa

Na CELLESTINE OLILO

KATIKA juhudi za kukabiliana na sifa mbaya inayotishia uongozi wake, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limepandisha cheo Afisa wa Mawasiliano na Mauzo Barry Otieno kuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji.

Tangazo hili lilifanywa siku moja baada ya Afisa Mkuu Mtendaji Robert Muthomi, ambaye anachunguzwa kwa madai ya kujaribu kusukuma uhamisho wa mshambuliaji John Avire akiwa bado na kandarasi na Sofapaka FC, kukaa kando akisubiri uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya FKF.

“Robert Muthomi ameomba kukaa kando kutoka wadhifa wake na tumekubali ombi lake, tukitumai kwamba hatimaye madai haya yataondolewa.

“Kamati ya dharura ya FKF ilikutana jana na kuamua kuwa Mkuu wa Mawasiliano Barry Otieno ashikilie wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji kwa muda wakati Robert hayupo kwa sababu lazima FKF iendelee na majukumu yake,” alisema Rais wa FKF, Mwendwa, ambaye aliongeza kuwa kamati hiyo itatoa uamuzi wake kuhusu Muthomi kwa kati ya siku 30 na 35 zijazo.

Kwa Otieno, cheo kipya kitaimarisha wasifukazi wake kwa sababu kinamuinua kutoka kazi ya kukabiliana na matamshi ya umma ya Mwendwa na kumfanya kuwa afisa wa tatu kwa mamlaka katika orodha ya viongozi wa shirikisho hili.

Katika majukumu yake mapya kama mmoja wa viongozi wakuu wa shirikisho, Otieno atashuhudia maslahi yakiboreshwa ikiwemo usafiri wa mara kwa mara barani Afrika kuwakilisha shirikisho, na kutoa uamuzi muhimu kwa niaba ya shirikisho.

Mambo ni tofauti na magumu kwa Muthomi.

Kwanza, atatumai ataondolewa madai hayo yanayotia doa sifa yake. Akirejeshwa kazini, atalazimika kufanya kazi maradufu ili kurejesha uaminifu na uungwaji mkono aliopoteza.

Akitangaza uamuzi wa kamati ya dharura ya FKF katika kikao cha Jumatatu na wanahabari jijini Nairobi, Mwendwa ambaye aliandamana na naibu wake Doris Petra, alionekana mtu aliye na huzuni.

Wandani wake wanasema kuwa uamuzi wa kumwondoa Muthomi kutoka afisi yake, na kuteua Otieno, uliafikiwa baada ya mashauriano ya kina yaliyokamilika usiku.

Supa

Uhusiano wa Muthomi na Mwendwa ulianza miaka kadhaa iliyopita walipokuwa wasimamizi wa klabu katika Ligi ya Supa, ambayo ni ligi ya daraja la pili.

Muthomi alikuwa mwenyekiti wa Nakuru All Stars, naye Mwendwa alikuwa Kariobangi Sharks akihudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji, na pia afisa wa kuweka rekodi za wanasoka nchini Kenya.

Waliingia FKF mwaka 2016 kuchukua uongozi kutoka kwa Sam Nyamweya, ambaye alijiondoa kwenye uchaguzi siku moja kabla ya kura kupigwa.

Uhusiano huu unaonekana kuharibika wakati mbaya, hasa kwa sababu Mwendwa ametangaza kuwa atawania tena Novemba mwaka huu.

Ijumaa iliyopita, FKF ilithibitisha kuwa imeanza kuchunguza Muthomi, ambaye alikuwa amekiri kuandikia Ubalozi wa Misri barua kuuomba umpe Avire kibali cha kusafiri. Hii ilikuwa siku nane tu baada ya mshambuliaji huyu, ambaye kandarasi yake na Sofapaka itatamatika Desemba mwaka 2020, alikuwa nchini Misri akichezea Kenya kwenye Kombe la Afrika (AFCON).

FKF yahamisha kambi ya Harambee Stars kutoka Ufaransa hadi Afrika Kusini

Na GEOFFREY ANENE

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limepiga breki mipango yake ya kuandalia Harambee Stars kambi ya mazoezi na mechi ya kirafiki nchini Ufaransa hadi pale mwenyeji mpya wa Kombe la Afrika la wanaume (AFCON) atakapojulikana kufikia Desemba 31, 2018.

Katika kikao na wanahabari jijini Nairobi, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amesema kwamba Stars itaelekea Ufaransa kombe hili likiandaliwa katika eneo la kaskazini mwa Afrika.

“Majira ya kaskazini mwa Afrika yatakuwa ya joto wakati huo sawa na yale yatakayokuwa Ufaransa wakati huo kwa hivyo hatutakuwa na tatizo kupeleka Harambee Stars nchini Ufaransa. Hata hivyo, Afrika Kusini ikiteuliwa kuandaa makala hayo ya 32, basi tutafutilia mbali kambi ya mazoezi ya Ufaransa pamoja na kusakata mechi za kirafiki barani Ulaya kwa sababu majira yatakuwa baridi nchini Afrika Kusini,” amesema Mwendwa.

Kenya inapanga kusakata kati ya mechi mbili na tatu kabla ya AFCON. Mojawapo ya mechi hizo ni dhidi ya Reggae Boys ya Jamaica jijini London, ambayo imekuwa ikipangwa tangu Februari 2018. Mechi itaondolewa kwenye ratiba ya Kenya ikiwa Afrika Kusini itatwikwa majukumu ya kuandaa AFCON mwaka 2019.

Aidha, Mwendwa alisema kwamba FKF ilitaka Stars ikipige kambi Ufaransa kwa sababu mataifa mengi ya magharibi mwa Afrika hupenda nchi hiyo.

“Itakuwa vigumu sana kuwa na kambi nchini Ufaransa ikiwa Afrika Kusini itachaguliwa kuandaa AFCON kwa sababu ya tofauti hiyo ya majira. Tulitaka kambi hiyo iwe Ufaransa ili tuweze kuzungumza na timu kutoka magharibi mwa Afrika inayoenda AFCON tujipime nayo nguvu ikiwa kambini Ufaransa. Huenda isiwezekane ikiwa Afrika Kusini itachaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na tofauti ya majira,” amesema Mwendwa. 

Mwendwa aahidi Harambee Stars donge nono wakiilima Ghana

Na Geoffrey Anene

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa ameahidi Harambee Stars “zawadi nono” ikibwaga Black Stars ya Ghana katika mechi ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) uwanjani Kasarani jijini Nairobi hapo Septemba 8, 2018.

Tofauti na Ghana, ambayo imtangaza wazi kila mchezaji atatia mfukoni Sh504,300 kwa kuchapa Kenya, Mwendwa hajafichua donge ambalo vijana wa kocha Sebastien Migne watapata. Amesema, “FKF ilikuwa na kikao na wachezaji kuzungumzia suala la kuwapa motisha ya kuwatuza wakipata ushindi. Tuliamua zawadi yenyewe isalie kuwa siri, lakini ningependa kuwahakikishia kwamba ni zawadi ya kudondosha mate. FKF itawatunuku na pia mimi nitafanya mifuko yao iwe mizito kwa kuongeza zawadi hiyo.”

Mwezi uliopita wa Agosti, vyombo vya habari nchini Ghana viliripoti kwamba Kamati ya muda inayoendesha soka nchini Ghana inayojumuisha maafisa kutoka mashirikisho la soka duniani na bara Afrika haijabadilisha motisha ya Sh504,300 kwa kila mchezaji wa Black Stars ikicharaza Kenya.

FKF, ambayo inakabiliwa na wakati mgumu kifedha na kesi 12 mahakamani zinazoigharimu zaidi ya Sh100 milioni ikiwa ni pamoja na kutoka kwa makocha wa zamani wa Harambee Stars Adel Amrouche na Bobby Williamson, haitarajiwi hata kidogo kukaribia kitita cha Ghana.

Mwendwa afichua FKF inadaiwa Sh100m na makocha wa zamani wa Harambee Stars

Na Geoffrey Anene

Madeni ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kwa makocha wa zamani wa Harambee Stars yanatisha hali yake ya kifedha.

Rais wa FKF, Nick Mwendwa amefichua Jumanne jijini Nairobi kwamba shirikisho lake linadaiwa zaidi ya Sh100 milioni kutokana na kesi 12 zilizowasilishwa dhidi yake mahakamani.

Kocha Mbelgiji Adel Amrouche, ambaye aliongoza Stars kati ya Februari mwaka 2003 na Agosti 4 mwaka 2014 alipotemwa baada ya Kenya kukosa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2015, anadai FKF Sh60,390,000 (dola 600, 000 za Marekani). Mzawa huyu wa Algeria alikuwa amesaini kandarasi ya miaka mitano na FKF.

Mapema mwaka 2018, alishinda kesi ya kupigwa kalamu kabla ya kandarasi yake kutamatika mahakamani. Korti iliamua alipwe mamilioni hayo, ambayo FKF bado inapambana kuona yamepunguzwa.

FKF ilielekea katika mahakama ya kuamua kesi za michezo (CAS) kutafuta haki baada ya kulalamika kwamba kesi ya Amrouche dhidi ya FKF ilisikizwa na jaji mmoja.

Mrithi wa Amrouche, Bobby Wiliamson anadai FKF Sh55 milioni. Raia huyu wa Scotland alijiunga na timu ya taifa ya Kenya mnamo Agosti mwisho mwaka 2014 kama kocha mkuu akitokea klabu ya Gor Mahia.

Baada ya msururu wa matokeo duni, Williamson alifurushwa na FKF mapema mwaka 2016. Alishtaki FKF mnamo Mei 2016 akitaka fidia kwa sababu ya kutimuliwa kabla ya kandarasi yake kukamilika.

FKF pia inaandamwa na kesi ya kukwepa kulipia ushuru ya zaidi ya Sh40 milioni, ingawa Mwendwa amesema shirikisho hili litaendelea kuzungumza na Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) kuhusu tukio hilo lilofanyika kati ya mwaka 2011 na 2012 wakati hakuwa ameingia ofisini. Mwendwa alichaguliwa kuongoza FKF mwezi Februari mwaka 2016.