Jambojet yazindua safari za Lamu

NA KALUME KAZUNGU

KAMPUNI ya ndege ya Jambojet kwa mara nyingine imezindua safari zake kwenye anga ya Lamu baada ya kuzikatiza kwa karibu miaka mitano iliyopita.

Mnamo 2015, kampuni hiyo ilizindua safari zake Lamu lakini ikazikatiza 2017 kwa kile walichodai kuwa ni ukosefu wa usalama na pia hali mbaya ya uwanja wa ndege wa Manda eneo hilo.

Aidha hafla ya kuzindua upya safari za ndege ya Jambojet iliandaliwa Jumatano uwanjani Manda na kuhudhuriwa na Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala, makatibu wa Wizara za Utalii na Uchukuzi, wakuu wa kampuni ya Jambojet miongoni mwa maafisa wengine wakuu serikalini.

Akihutubu kwenye sherehe hiyo, Bw Balala alitaja kurejelewa kwa safari za ndege ya Jambojet Lamu kuwa mwamko mpya kwa sekta ya utalii Lamu.

Bw Balala aliiomba Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) kuharakisha ujenzi na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Manda unaoendelea kwa sasa ili kuuwezesha kupokea ndege zaidi za wageni na watalii wanaozuru Lamu.

Aliisifu serikali kuu kwa juhudi ilizofanya kukabiliana na magaidi wa Al-Shabaab na kuimarisha usalama Lamu.

Alisema ana matumaini kwamba msimu wa juu wa utalii utakapoanza Disemba mwaka huu utavutia watalii wengi kuja Lamu,ikizingatiwa kuwa eneo hilo limeshuhudia usalama wa hali ya juu miaka ya hivi sasa.

“Tunashukuru kwamba Jambojet wamerejelea safari zake Lamu. Huu ni mwamko mpya kwa sekta ya utalii. Natumai KAA itafanya bidi kukamilisha ukarabati unaoendelea wa kiwanja cha Ndege cha Manda kabla msimu wa wageni wengi Disemba ufike,” akasema Bw Balala.

Afisa Mkuu Mtendaji na Meneja wa Jambojet nchini, Karanja Ndegwa alisema hatua yao ya kurejelea safari za Lamu inatokana hasa na kuimarika kwa usalama Lam una pia kuboreshwa kwa uwanja wa Ndege wa Manda.

Bw Ndegwa alisema nauli ya kutoka Nairobi hadi Lamu itakuwa Sh7,100 ilhali ilhali ile ya Mombasa hadi Lamu ikitozwa Sh4,600.

Alisema watakuwa wakitekeleza safari mara nne eneo la Lamu kila wiki.

Alisema kampuni ya Jambojet iliafikia kuzindua safari ya Lamu kutokana na kwamba eneo hilo ni muhimu kwa watalii hapa nchini.

“Kuzinduliwa kwa mradi kama vile Bandari ya Lamu (Lapsset) kutavutia wasafiri na wawekezaji wengi kuja Lamu. Tunataka kurahisisha usafiri waokupitia ndege nah ii ndiyo sababu tukaafikia kurejesha safari zetu hapa,” akasema Bw Ndegwa.

Afisa huyo alisema juma lililopita, Jambojet pia ilizindua safari zake eneo la Goma huko Demokrasia ya Congo (DRC)

Kwa upande wake,Gavana wa Lamu, Fahim Twaha aliomba kampuni nyingi zaidi za ndege kuzindua safari zake za Lamu, akitaja kuwa eneo hilo linafurahikia usalama.

Kenya yasitisha safari za ndege Somalia

Na MWANDISHI WETU

KENYA Jumatatu ilisitisha safari za ndege kwenda na kutoka Somalia kuashiria kuwa uhusiano kati ya mataifa hayo haujarejelewa ilivyotangazwa wiki jana.

Kulingana na notisi kutoka kwa Mamlaka ya Safari za Angani Kenya (KCAA) ndege za kuelekea au kutoka Somalia hazitahudumu kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia jana.

Ni ndege zinazosafirisha misaada ya vyakula na dawa pekee ndio zitaruhusiwa nchini Kenya, mamlaka ya KCAA ilifafanua.

Asasi hiyo haikutoa sababu ya hatua hiyo lakini ikasema kumekuwa na agizo la kuiusalama kutoka serikali kwamba idhibiti usafiri wa anga kati ya nchini hizo mbili..

Uamuzi huo wa KCAA unamaanisha kuwa hata ndege za kukodiwa hazitaruhusiwa kusafiri hadi Somalia.

“Hata hivyo, ndege kutoka Somali, zinazopitia anga ya Kenya kuelekea mataifa mengine hazitaathiriwa na agizo hili,” itasema taarifa kutoka kwa mamlaka hiyo.

Vile vile, agizo hilo halitaathiri safari za ndege za kijeshi ambazo hazisimamiwi na mamlaka ya KCAA.

Tangazo hilo lilitokea wakati ambapo Rais wa Somalia Mohamed Farmaajo alikuwa akisafiri kupitia anga ya Kenya akiwa njiani kuelekea Uganda kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni.

Hatua hiyo, ya kuzimwa kwa safari za ndege kati ya Kenya na Somalia inaathiri juhudi za kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

Wiki iliyopita Balozi maalum wa Qatari Mutlaq al-Qahtani aliingilia kwa nia ya kurejelewa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili. Hii ni baada ya Somalia kukubali kufungua afisi yake ya kibalozi iliyofunga baada ya kukerwa na kile ilichotaja kama hatua ya Kenya kuingilia masuala yake ya ndani.

Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Manda waanza

NA KALUME KAZUNGU

HALMASHAURI ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) limeanzisha ukarabati wa uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu unaokadiriwa kugharimu serikali kima cha Sh 200 milioni.

Mradi huo ambao unahusisha ujenzi na upanuzi wa njia pamoja na mahali pa kupakisha ndege punde zinapotua umepangwa kuchukua muda wa miezi sita kukamilika.

Mkurugenzi wa KAA Ukanda wa Pwani, Peter Wafula, alisema shughuli ya ujenzi na upanuzi wa sehemu hizo za uwanja wa ndege wa Manda inaendelea baada ya kuanza rasmi mwezi Machi mwaka huu.

Bw Wafula alisema wanatarajia shughuli hiyo ya ujenzi kufikia kikomo ifikapo Agosti mwaka huu.

Afisa huyo alisema KAA iliafikia kupanua na kujenga sehemu husika ili kuwezesha ndege zaidi kutua na kupata nafasi ya kupaki kwenye uwanja huo kwa wakati mmoja.

Alisema sehemu zinazokarabatiwa kwa miaka kadhaa zimekuwa katika hali mbaya, hatua ambayo ilichangia baadhi ya kampuni za usafiri wa ndege nchini, ikiwemo Jambojet kukatiza safari zake kwenye eneo la Lamu.

Bw Wafula anasema anaamini kukamilika kwa ukarabati unaoendelea uwanjani humo kutasaidia kuvutia kampuni nyingi zaidi za ndege kuanzisha huduma zake za usafiri Lamu.

Ujenzi ukiendelea kwenye uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu. Jumla ya Sh 200 milioni zimepangwa kutumika kwenye mradi huo. PICHA/ KALUME KAZUNGU

“Tumeanzisha ujenzi na upanuzi wa sehemu za kuegesha na kupaa kwa ndege uwanjani Manda, Kaunti ya Lamu. Sehemu zinazojengwa zilikuwa katika hali duni. Mradi umepangwa kutekelezwa kwa muda wa miezi sita. Shughuli zilianza Machi. Kufikia Agosti kila kitu kitakuwa tayari,” akasema Bw Wafula.

Hatua ya KAA ya kukarabati na kupanua kiwanja cha ndege cha Manda imepokelewa vyema na wadau wa utalii,wawekezaji na wasafiri eneo hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wawekezaji katika sekta ya Utalii, Kaunti ya Lamu, Abdallah Fadhil alipongeza KAA kwa hatua hiyo, akiitaja kuwa yenye natija tele kwa sekta ya utalii Lamu.

“Nimefurahi kwamba KAA imeafikia kukarabati na kupanua kiwanja cha ndege cha Manda. Hii inamaanisha punde shughuli ikikamilika, kampuni nyingi zaidi za ndege zitaanzisha safari zake Lamu. Tutashuhudia watalii wakiingia hapa kwa wingi, hivyo kunogesha sekta hiyo muhimu,” akasema Bw Fadhil.

Mmoja wa wasafiri, Hussein Shukri pia alipongeza ukarabati na upanuzi unaoendelea wa kiwanja hicho cha ndege cha Manda, akisema hatua hiyo itaondoa woga miongoni mwa wasafiri kila wakati ndege zinapotua na kupaa kwenye uwanja huo ambao ulikuwa umesheheni miteremko na mabonde.

Naye Meneja wa Usimamizi na Maendeleo ya Bandari ya Lamu (Lasset), tawi la Lamu, Salim Bunu alisema ujenzi na upanuzi wa uwanja huo wa ndege wa Manda umejiri kwa wakati ufaao ambapo bandari ya Lamu iko kwenye harakati za kuzindua shughuli zake eneo hilo kufikia mwezi Juni mwaka huu.

“Lapsset itakapoanza kufanya kazi itaongeza idadi ya watu eneo hili ambao wengine watakuwa ni wafanyikazi. Wote hao watahitaji usafiri, iwe ni kwa ndege au gari,” akasema Bw Bunu.

Masharti ya safari za ndege yalegezwa

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imetangaza kulegeza masharti ya kupambana na virusi vya corona kwa wasafiri wa ndege nchini.

Tofauti na safari za barabarani na treni ambazo itakuwa ni lazima zifanywe kabla saa tatu usiku kafyu inapoanza, Waziri wa Uchukuzi James Macharia jana alisema wasafiri wa ndege watakubaliwa kuwa barabarani hata saa za kafyu.

Kulingana naye, kuna ndege ambazo zitakuwa zikiondoka usiku kwa hivyo serikali iliamua kanuni za kafyu zisitumiwe kwa wasafiri.’

Anayesafiri akipatikana barabarani saa za kafyu, atahitajika kuonyesha polisi tikiti yake ya usafiri na atakubaliwa kuendelea na safari yake,’ Bw Macharia alisema jana.

Kwa upande mwingine, hitaji la watu kukaa umbali wa mita moja pia halitatumiwa kwa safari za ndege.

Waziri alisema hitaji hilo likitumiwa, itamaanisha ndege zitatakikana kubeba asilimia 50 ya wasafiri wa kawaida na hiyo itakuwa hasara kubwa kwa mashirika ya ndege.

Vile vile, wahudumu wa ndege ambao watakuwa wakiingia nchini kutoka nchi za kigeni hawatatakikana kujitenga kutoka kwa jamii kama ilivyo kwa wasafiri.Jana visa vingine 278 vya maambukizi vilitangazwa na kufikisha idadi hadi 8,528.

Akiongea jana katika Kaunti ya Makueni, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema wagonjwa 89 walipona, na sasa idadi imefika 2,593.

Waziri Kagwe alithibitisha kuwa wagonjwa wengine wawili wamefariki na kuongeza idadi kufikia 169.

Watu 6 wajeruhiwa katika ajali ya ndege Meru

NA JACOB WALTER

Watu sita walipata majeraha baada ya ndege ya polisi iliyokuwa imebeba maafisa wa usalama kuanguka eneo la Kaithe, Kaunti ya Meru Jumamosi asubuhi.

Kamanda wa polisi eneo la Meru Patrick Lumumba alisema kwamba maafisa hao walikuwa wanaelekea katika mkutano wa usalama Marsabit.

Ndege hiyo ilitua kwenye shamba la ndizi. Wakazi walisaidia kutoa abiria kwenye ndege hiyo. Walioumia walikimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Meru.

Maafisa wa usalama wa eneo hilo wamekuwa wakijaribu kudumisha usalama eneo la Badan Arero baada ya kikundi cha watu kutoka Marsabit kuvuka mpaka na kuingia Wajir na kuiba mifugo zaidi ya 70, na hali hiyo ikachochea vita kati ya jamii hizo mbili.

Watu wanne waliuawa katika vita hivyo Jumatatu.

Maafisa walikuwa wamepanga mkutano Jumamosi wa kurudisha usalama kati ya jamii hizo mbili. Mifugo waliokuwa wamebwa waliikuwa warudishwe kwa wenyewe mbele ya maafisa wa usalama wa eneo hilo, viongozi wa eneo hilo na wazee wa jamii hiyo.

Ajali hiyo ya ndege ilileta kumbukumbu za ndege iliyopata ajali Aprili 10, 2006 eneo la Marsabit ambapo watu kumi na moja wakiwemo wabunge sita walifariki.

Ada za usafiri wa ndege kuongezeka kutokana na athari za Covid-19

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya usafiri ya ndege wanakadiria ada za usafiri huo huenda zikawa ghali mno huku wakipambana kukabiliana na Covid-19.

Aidha Afisa Mkuu wa shirika la Kenya Airways Bw Allan Kilavuka ametangaza kuwa huenda ada ikawa ghali huku wakipambana kuhakikisha abiria hawakaribiani wanaposafiri kwenye ndege hizo.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), uvaaji wa barakoa, kuosha mikono kwa maji na sabuni na kujitenga na umma ni njia maluum ya kukabiliana na ugonjwa huo hatari unaosambaa kwa haraka.

Bw Kilavuka amesema mashirika ya ndege duniani yanaendelea kujadiliana namna ya kuhakikisha abiria hawakaribiani ili kuzuia maabukizi ya virusi vya corona.

Akiongea kwenye mkutano na wawekezaji mbalimbali duniani kujadili namna ya kuanza tena usafiri wa ndege na utalii, Bw Kilavuka amesema usafiri wa ndege utabadilika sana.

“Hali itakuwa tofauti sana; watu watavaa magwanda maalum, barakoa, na kila aina ya kifaa kujidhibiti dhidi ya maambukizi ya visuri vya corona. Tunakadiria asilimia 51 hadi 76 ya soko letu litapotea kuanzia sasa hadi mwishoni mwa Desemba. Lakini baadaye sekta itaimarika,” akasema Kilavuka.

Katika mkutano huo ambao uliwaalika zaidi ya watu 1,400 Bw Kilavuka alisema usafiri wa ndege siku za usoni utabadilika maradufu.

Bw Kilavuka ambaye ni mwanachama wa bodi ya magavana kwenye muungano wa uchukuzi wa ndege alisema walifanya mkutano Jumatatu wiki jana kwa kutumia vyombo vya kiteknolojia na mtandao kujadili maswala ya usafiri wa ndege.

Kwenye mkutano huo, alisema wawekezaji hao walijadili namna ya kuhakikisha sekta hiyo inaweka mikakati ya usafiri wa ndege kwenye sekta hiyo ulimwenguni ili kuzuia maambukizi.

KQ kuwalipia Wakenya nauli kutoka New York hadi Nairobi

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Ndege la Kenya Airways (KQ) limetoa tiketi za bure kwa Wakenya waliotaka kusafiri kutoka jijini New York, Amerika, hadi Nairobi, siku moja kabla ya serikali kuanza kutekeleza marufuku dhidi ya ndege za abiria kutoka nje.

Kwenye ujumbe katika akaunti yake ya Twitter, shirika hilo limesisitiza kuwa Wakenya hao wote watafanyiwa uchunguzi kuhusu maambukizi ya virusi vya corona watakapawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.

Wakenya hao pia watalazimika kujitenga katika mikahawa ambayo imeidhinishwa na serikali, kulingana na maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe mnamo Jumapili jioni.

“Ndege yetu ya mwisho kutoka uwanja wa JFK inaondoka leo na tunatoa tiketi za bure hadi Nairobi kwa Wakenya wenye haja. Kwa habari zaidi, wasiliana na maafisa wetu kwa nambari +1(866)5369224,” ikasema Jumanne.

Ikaongeza: “Zingatia kwamba abiria wote watachunguzwa kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa na Wizara ya Afya. Tutanawiri tena na kuwahudumia kwa mara nyingine tutakaporejelea huduma zetu. Muwe salama.”

Tangazo la shirika hilo ni afueni kwa Wakenya ambao walikuwa wamepanga kurejea nyumbani kwani itawaokolea nauli kiasi cha Sh98,825.

Jumatano, Kenya Airways inatarajiwa kusimamisha “kwa muda” safari zote za kimataifa kama hatua ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Hii ni baada ya kubainika kuwa watu wote 16 wa mwanzo waliogunduliwa kuwa na virusi hivyo ni raia wa kigeni na Wakenya waliowasili nchini kutoka mataifa ya nje ambako visa vya ugonjwa wa Covid-19 vimeripotiwa.

Leo Jumanne waziri Kagwe ametangaza visa tisa mpya vya maambukizi na kufanya idadi ya wagonjwa wa Covid-19 kuwa 25 nchini.

Korti yazuia kukamatwa kwa anayehusishwa na picha ya ndege kutoka China

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imezuia kukamatawa na kushtakiwa kwa afisa wa usalama aliyetimuliwa kazini akikabiliwa na tuhuma za kupiga picha ya video ndege ya shirika la Sourthern China iliyowaingiza abiria 239 kutoka nchini China.

Jaji Weldon Korir aliamuru DPP asimkamate na kumshtaki Bw Gire hadi kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi aliyoshtaki serikali.

Bw Gire Ali aliwasilisha kesi akipinga kukamatwa na kushtakiwa kwa kurekodi video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Wakili Danstan Omari aliyewasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu amesema Bw Ali alidhulumiwa alipotimuliwa kazini kwa kutekeleza kazi yake ipasavyo.

Katika kesi hiyo, Bw Ali anadai video aliyopiga ilisaidia pakubwa ikitiliwa maanani hofu kuu inayokumba mabilioni ya watu ulimwenguni kutokana na kuzuka kwa maradhi ya Corona ambayo yamesababisha vifo vya maelfu na maelfu ya raia wa China.

Katika kesi aliyowasilisha chini ya sheria za dharura, Bw Ali anaomba mahakama itoe agizo ili asikamatwe na kushtakiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

Bw Omari anasema mlalamishi hafai kuchukuliwa alifanya makosa ama kutuhumiwa kuwa tisho kwa vile anatoka eneo la Marsabit.

Hatumjui, KAA yakana habari za Mkenya aliyedondoka London

Na BENSON MATHEKA

MAMLAKA ya kusimamia viwanja vya ndege nchini (KAA), imekanusha habari za shirika la habari la Sky News la Uingereza kwamba mwili wa mwanamume ulioanguka kutoka kwa ndege mjini London ulikuwa wa mfanyakazi wa kampuni inayohudumu katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Kampuni ya Colnet ambayo shirika hilo lilisema mwanamume huyo alikuwa akifanyia kazi, pia lilikanusha habari kwamba alikuwa mfanyakazi wake.

Kauli ya KAA na Colnet inatofautiana na Mamlaka ya Safari za Ndege nchini ambayo awali ilisema huenda mwanamume huyo alikuwa mfanyakazi kampuni moja ya kudumisha usafi katika uwanja huo.

Hata hivyo, usalama katika uwanja huo unatiliwa shaka kufuatia kisa hicho maswali yakiibuka jinsi mwanamume huyo aliweza kuingia uwanjani na kufikia ndege.

Sky News ilimtambua mwanamume huyo kama Paul Manyasi, aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya Colnet, lakini kulingana na KAA na kampuni hiyo, jina hilo haliko katika sajili ya kidijitali ya watu wanaohudumu katika uwanja huo.

“Maafisa wa usalama kutoka vitengo tofauti walianza uchunguzi kuhusiana na madai katika makala ya Sky News kwamba mwanamume ambaye mwili wake ulianguka kutoka kwa ndege alikuwa akifanya kazi katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na inataka kusema uchunguzi huo unaendelea kwa kuzingatia habari zote zitakazopokelewa,” KAA ilisema kwenye taarifa.

Mkurugenzi wa Colnet, Bw Chege Kariuki, alisema kampuni ilishangazwa na ripoti ya Sky News. “Tunashangazwa na habari zilizopeperushwa na Sky News Network zinazohusisha Colnet limited na mwanamume huyo,” Bw Kariuki alisema kwenye taarifa.

Alisema kampuni iliwasilisha rekodi na habari za wafanyakazi wake wote kwa wachunguzi ambao wanaweza kuthibitisha haina mfanyakazi kwa jina Paul Manyasi.

Kampuni hiyo iliwataka watu wanaodai kuwa na habari kuhusu mtu huyo kurekodi taarifa kwa polisi.

Mnamo Jumanne, runinga ya Sky TV ilipeperusha ripoti zilizodai kuwa mwanamume huyo alifahamika kama Paul Manyasi na kwamba alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Colnet inayotoa huduma za usafi katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta.Iliwahoji watu kadhaa akiwemo baba yake Isaac Manyasi, aliyesema kwamba hakuwa amepokea habari zozote kumhusu mwanawe.

Baadhi ya watu waliohojiwa wakiwemo wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema walifahamishwa kwamba mmoja wao alitoweka mwishoni mwa Juni mwaka huu na wakaagizwa kutofichua habari hizo.

Mwanamke aliyedai kuwa mpenzi wa mwanamume huyo alieleza ripota wa Sky News kwamba alienda kazini siku hiyo na hakurudi.

Mwezi jana, polisi wa Uingereza walitoa picha wakitarajia kuwa ingesaidia kutambua mwanamume huyo na familia yake kufahamishwa.

Aidha, walichapisha picha za bidhaa ambazo mwanamume huyo alikuwa nazo.Mwili wa mwanamume huyo unahifadhiwa katika mochari moja Uingereza hadi uchunguzi utakapokamilika.

Ndege kadha zazimwa na KCAA

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Safari za Ndege Nchini (KCAA) imeamuru ndege saba za kampuni ya Silverstone Air zisihudumu kwa muda wa wiki moja ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusiana na msururu wa ajali ambazo zimehusisha ndege za kampuni hiyo katika siku za hivi karibuni.

Wakati huo huo, KCAA pia imesimamisha, kwa muda, leseni za kuhudumu za kampuni ya ndege ya Safe Air Company (SAC) ambayo hutoa huduma za usafirishaji wa mizigo na ile ya Adventure Aloft kwa madai ya kukiuka kanuni za usafiri wa angani.

Hayo yametangazwa Jumanne na Mkurugenzi Mkuu wa KCAA Gilbert Kibe alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uchukuzi katika ukumbi wa County, jijini Nairobi.

Hata hivyo, Bw Kibe ameiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing kwamba uchunguzi unaoendeshwa na mamlaka hiyo kuhusu ajali za ndege haulengi kampuni ya Silverstone Air pekee bali kampuni zote za safari za ndege.

“Tuliamua kuanza kuchunguza Silverstone kwa sababu ndiyo ndege zake zilihusika katika ajali hivi majuzi. Nataka kuihakikishia kamati hii kuwa uchunguzi wetu unahusisha ndege zote,” akasema.

Mnamo Jumapili asubuhi ndege ya kumpuni hiyo iligonga na kuharibu ndege nyingine katika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi.

Na Oktoba ndege moja ya Silverstone ililazimika kutua ghafla katika Uwanja wa Kimataifa wa Eldoret, baada ya gurudumu lake moja kupasuka dakika chache baada ya kupaa. Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Lodwar ikielekea Nairobi.

Ndege waharibifu walivyoangamizwa Mwea

Na George Munene  

MAMILIONI ya ndege aina ya quelea ambao wamekuwa wakitatiza wakulima wa mpunga katika shamba kubwa la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga, wameangamizwa.

Serikali kuu ikishirikiana na ile ya kaunti inayoongozwa na Gavana Anne Waiguru ilinyunyiza dawa baada ya maelfu ya wakulima kulalamika wakihofia hasara.

Naibu Gavana Peter Ndambiri alisema hatua ilichukuliwa baada ya idara ya kilimo katika kaunti kufanya upelelezi kwa wiki kadhaa.

“Wakati wakulima walipolalamika kuhusu uvamizi wa ndege hao katika mashamba yao, maafisa wetu walianza kuchunguza mienendo ya ndege hao hadi kutambua tundu zao. Walinyunyiziwa dawa kwa siku mbili mfululizo kwa hivyo sasa wakulima watarajie mavuno mengi,” akasema Bw Ndambiri.

Wakulima walisifu hatua hiyo na kusema kama ndege hawangeangamizwa, mazao yao yote yangeharibiwa msimu huu.

Ndege hao wadogo huorodheshwa kuwa miongoni mwa waharibifu zaidi mashambani kwani huweza kula hadi gramu kumi za nafaka kila mmoja kwa siku.

Gurudumu la ndege ya Silverstone Air ladondoka ikiwa imepaa

Na SAMMY LUTTA

KUMEKUWA na hofu Jumatatu baada ya gurudumu la ndege ya Silverstone Air kudondoka ikiwa hewani ikitoka Lodwar ambapo imelazimika kutua ghafla Eldoret.

Mkasa huo umetokea muda kiasi fulani mara baada ya kupaa ikitokea uwanja mdogo wa ndege uliopo Lodwar, Kaunti ya Turkana.

Gurudumu la nyuma kulia limedondoka kama jiwe na likaanguka umbali wa mita kadhaa wa uwanja huo ulio umbali wa kilomota 500 kutoka jiji kuu la Nairobi.

Nambari za usajili za ndege hiyo ya bombardier Dash 8-300 ni 5YBWG. Ndege hiyo ilikuwa na abiria wanne na wahudumu watano wakati wa mkasa.

“Gurudumu limeokotwa na raia  mita chache nje ya uwanja huo mdogo,” amesema Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Turkana Kati Bw David Mburukwa akiongea na Taifa Leo.

Ameeleza kwamba limechukuliwa na kupelekwa katika ofisi ya meneja wa uwanja huo mdogo wa ndege.

Mara baada ya kupata ripoti za mkasa huo wa ndege, maafisa wa polisi wa Lodwar wamewafahamisha wasimamizi wa uwanja wa kimataifa wa ndege wa Moi mjini Eldoret ambao walihakikisha wanaweka kila kitu shwari ili ndege itue hapo.

Ndgee hiyo iliyokuwa ya safari ya Lodwar hadi Nairobi ilipaa saa tatu na dakika 18 asubuhi, lakini ikatua ghafla Eldoret dakika kadha kufika saa nne za asubuhi, saa za Afrika Mashariki.

Kwenye taarifa Silverstone Air imethibitisha mkasa huo ikisema ndege gurudumu nambari tatu ikilitaja kama “the number 3 wheel assembly”.

“Rubani ameamua kuielerkeza Eldoret kwa ajili ya usalama wa abiria na wahudumu ili kuhakikisha pia inatua salama salimini,” imesema Silverstone Air.

Imesema abiria wamepewa usafiri mbadala na tayari wametua jijini Nairobi.

Oktoba 11, 2019, ndege ya Silverstone ilipoteza mwende ikitaka kupaa katika uwanja wa ndege wa Wilson jijini Nairobi.

Mabaki ya Wakenya walioangamia katika ajali ya ndege Ethiopia yaletwa

Na JAMES KAHONGEH, ERIC MATARA na PHYLIS MUSASIA

MABAKI ya Wakenya 28 kati ya 32 walioangamia Machi 10, 2019 katika ajali ya ndege ya Ethiopia yameletwa; familia zilizofiwa zafanya ibada JKIA

Majeneza maalumu yaliyobeba mabaki hayo yamesafirishwa kwa ndege ya shirika la Ethiopian Airlines iliyotua Jumatatu katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) dakika chache kabla ya saa nne za asubuhi.

Familia na marafiki za wahanga wa ajali hiyo walijumuika katika eneo la watu mashuhuri (VIP) katika uwanja huo ambapo wamepewa ushauri nasaha.

Ni watu wa karibu wa familia ndio wanapewa mabaki hayo ya wapendwa wao.

Kwa muda wa miezi saba tangu ilipotokea ajali hiyo eneo la Bishoftu, Ethiopia ambapo watu wote 157 waliokuwa kwa ndege ya Boeing 737 MAX , familia zilikuwa bado kuzika mabaki ya wapendwa wao.

Maafisa wa Ethiopia walisema miili iliteketea kiasi cha kutotambulika ambapo hata vipimo vya vinasaba, DNA, vilichukua muda wa zaidi ya siku 240 kubainishwa wazi.

Ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Nairobi ilianguka katika eneo la Bishoftu, Ethiopia, dakika chache baada ya kuondoka katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Bole, Addis Ababa.

Jumapili, familia ya Bw John Quindos Karanja ambayo ilipoteza jamaa wao watano, ilisema wanapanga kusafirisha mabaki ya miili ya jamaa zao kwa mazishi Alhamisi.

“Tunashukuru Wakenya wote kwa misaada waliyotolea familia yetu. Tutasafirisha mabaki ya wapendwa wetu baada ya kutambuliwa. Tunapanga kuwazika Alhamisi, Oktoba 17,” ikasema taarifa kutoka kwa Bw Karanja ambaye ndiye msemaji wa familia hiyo.

Bw Karanja, 61, ambaye ni mwalimu mstaafu, alipoteza jamaa zake watano wakiwemo mke wake Ann Wangui Karanja, bintiye Caroline Karanja na wajukuu watatu ambao ni Ryan Njoroge aliyekumbana na mauti akiwa na umri wa miaka saba, Kellie Wanjiku akiwa na umri wa miaka mitano, na Rubi Wangui (miezi tisa wakati mauti yanamkumba).

Jamaa wa familia nyingine kutoka Kipkelion ambayo pia ilipoteza mpendwa wao Cosmas Kipng’etich Rogony kwenye mkasa huo, pia walithibitisha kwamba baadhi yao walisafiri kwenda kuchukua mabaki ya mwili wake ili kuleta nyumbani kwa mazishi.

“Familia ya marehemu Rogony ilisafiri na wanatarajiwa kurejea kesho,” akasema jamaa wa familia hiyo.

Rogony ambaye alikuwa mfanyakazi wa kampuni ya General Electric kitengo cha afya, aliacha binti mwenye umri wa mwaka mmoja na mjane Bi Miriam Wanja mwenye umri wa miaka 27.

Nyumbani kwao ni kijijini Saoset, Kaunti Ndogo ya Kipkelion Magharibi.

Mnamo Machi, familia hizo ziliandaa misa kuashiria msiba na maombi ingawa hapakuwa na miili yoyote kwenye majeneza yaliyotumiwa.

Imechukua zaidi ya miezi saba kwa ripoti ya DNA kuhusu waliofariki kutolewa, na kuruhusu familia kuandaa mazishi inavyostahili kwa wale ambao sehemu za miili yao zilipatikana.

Kufikia sasa, kuna baadhi ya Wakenya ambao wameungana kwenye kesi inayotaka kampuni ya utengenezaji ndege ya Boeing kulipa ridhaa ya Sh100 bilioni.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mahakama ya Amerika na kampuni kubwa za uwakili nchini humo.

Familia hizo zimeuliza kwa nini ndege aina ya Boing 737 MAX 8 hazikupigwa marufuku ilhali kulikuwa na ajali nyingine awali iliyohusisha aina hiyo ya ndege kutoka Indonesia ambapo wasafiri wote 189 waliokuwemo waliangamia.

Hivi majuzi, Boeing ilitangaza kwamba familia zilizoathirika katika mkasa huo zitalipwa Sh15 milioni kila moja.

Ndege yapoteza mwelekeo ikitaka kupaa uwanjani Wilson

Na CHARLES WASONGA

NDEGE ya Silverstone Air imepoteza mwelekeo ikitaka kupaa kutoka katika uwanja wa ndege wa Wilson jijini Nairobi.

Walioshuhudia mkasa huo wamesema ndege hiyo imepoteza mwelekeo ambapo ilifaa kuenda maeneo ya Pwani leo Ijumaa.

Ajali hiyo imetokea majira ya alfajiri.

Ndege hiyo ilikuwa safarini kuelekea Lamu kabla ya kuanguka dakika chache baada ya kupaa angani.

Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini limethibitisha ajali hiyo huku likisema kuwa ndege hiyo huenda ilianguka baada ya kupata hitilafu za kimitambo.

“Shughuli ya uokoaji inaendelea japo inakisiwa kuwa abiria kadha wamejeruhiwa katika ajali hiyo,” shirika hili limesema kwenye ujumbe lililochapisha katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter.

Mamlaka ya Safari za Angani Nchini (KCAA) imesema kwenye taarifa kwamba abiria wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo walioondolewa.

“Wachunguzi kutoka KCAA wako katika eneo la mkasa kuendelea na upekuzi zaidi kubaini chanzo cha ajali hiyo,” ikasema taarifa hiyo iliyotumwa katika ukurasa wa akaunti ya Facebook ya shirika hilo.

Hata hivyo, halikutoa maelezo zaidi kuhusu viwango vya majeruhi waliyopata abiria waliokuwa ndani ya ndege ajali hiyo ilipotokea.

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA) nayo imesema ni watu wawili waliojeruhiwa baada ya ndege ya Silverstone Air kupoteza mwelekeo ikitaka kupaa uwanjani Wilson na kwamba tayari Wizara ya Uchukuzi imeanza uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo.

Ndege hiyo aina ya Fokker F50 yenye nambari ya usajili ya 5Y-IZO ina uwezo wa kubeba abiria 50 kwa wakati mmoja.

Ndege hiyo imehudumu katika uwanja wa ndege wa Wilson tangu Aprili 2018.

Kicheko bungeni abiria wanaochafua hewa kwa ndege wakijadiliwa

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Rangwe Lilian Gogo  (pichani) aliibua kicheko bungeni Jumatano alasiri alipopendekeza kuwa abiria wa ndege wenye matatizo ya tumbo wapewe tembe za kupunguza asidi ili kuwazuia kutoa hewa mbaya (kunyamba) ambayo husababisha usumbufu kwa abiria wengine.

Akichangia mjadala kuhusu Sheria ya Kudhibiti Makosa ambayo hutendwa na abiria kwenye ndege, Bi Gogo alisema kunyamba katika ndege ni usumbufu ambao mara nyingi hupuuzwa.

“Kando na masuala mengine ambayo yanaweza kuhatarisha usalama au kusababisha usumbufu kwa abiria, mnyambo pia ni chanzo cha usumbufu japo hupuuzwa. Kuna abiria ambao hutoa harufu inayokera zaidi baada ya kunyamba,” akasema Bi Gogo.

Mbunge huyo aliongeza kuwa mnyambo pia husababisha machungu kwa abiria wanaosafiri kwa ndege.

“Kunapasa kuwa na sheria inayodhibiti chakula kinachopewa abiria katika ndege kando na mikakati ya tiba ambayo inaweza kupunguza kiwango cha gesi mbaya ambayo mtu anaweza kutoa kwenye ndege,” Bw Gogo akalalamika.

Mbunge huyo alitoa mifano ndege ambazo husafiri kutoka Kisumu kwenda Nairobi akisema ndiko abiria hunyamba kila mara bila kujizuia.

“Hii ndio maana napendekeza kuwa mashirika ya ndege yanayohudumu katika ruti hiyo yawape abiri dawa za kupunguza aside ili kuzuia kero hili,” Dkt Gogo akakariri.

“Sheria iwepo ya kuwazilazimisha mashirika ya ndege kununua dawa kama vile Eno na kuwapa abiria wao ambao huenda wakapata matatizo ya tumbo kwa kula chakula nyingi kupita kiasi,” akaongeza.

Spika wa muda Chris Omulele aliunga mkono pendekezo la Dkt Gogo alisema tabia ya abiria kunyamba imekithiri zaidi katika baadhi ya abiria hulazimika kuvumilia usumbufu wakiwa safarini.

Dkt Gogo pia anapendekeza sheria kuanzishwa na mashirika ya ndege kwa ajili ya kudhibiti kiwango cha pombe ambayo hupewa abiria.

Alisema baadhi ya abiria ambao hudhihirisha tabia mbaya katika ndege wamebainika kuwa walevi baada ya kubugia pombe kupita kiasi.

“Mbona sheria ya kudhibiti kiwango cha pombe ambayo inaruhusiwa kunywewa na abiria kwani baadhi yao hunywa pombe nyingi wanayopewa?

Wabunge waliochangia mjadala huo walisema mabadiliko yanapasa kufanywa na jumuiya ya mataifa kuhusu usalama wa abiria katika ndege, ikiwemo kuimarishwa kwa mafunzo yanayotolewa kwa wahudumu wa ndege.

“Wanafa kufunzwa mbinu bora za kuwadhibiti abiria wanaonyesha mienendo mibaya safarini,” akasema Mbunge wa Kimilili Chris Wamalwa.

Alisema wahudumu wanapasa kufunzwa kwamba abiria hawafai kuruhusiwa kubugia pombe kupita kiasi,” akasema.

UFUGAJI: Ndege wa umaridadi wamemuinua kimapato

Na SAMMY WAWERU

LENGO la kufuga ndege wa umaridadi lilikuwa kurembesha boma lake, na  hatima yake itaishia kuwa kitega uchumi.

Bi Margaret Njeri Maina, anafuga ndege hao chini ya mradi wake wa kuku, Gratia Poultry, ulioko mita chache kutoka Chuo Kikuu cha Wanawake cha Kiriri, Kaunti ya Kiambu.

“Nilipania kurembesha mazingira ya boma langu kwa ndege ambao ni maridadi,” anadokeza Bi Njeri.

Mradi huo, Gratia Poultry, umesitiriwa na kipande cha ardhi chenye ukubwa wa futi 50 kwa 80.

Aidha, umegawanywa kwa sehemu kadhaa hususan kuhifadhi vifaranga anaototoa kwa kiangulio, kuku waliokomaa na ndege.

Kizimba cha nyuni wake kilichoundwa kwa mbao, nyaya na mabati, kimechukua nafasi ya futi 20 kwa 15.

Ndicho makazi ya kanga, bata mzinga (turkey) na batabukini (goose wingi geese).

Njeri pia anafuga bata wa majini (mallards) na njiwa. Kizimba kimegawanywa ili kusitiri kila aina ya nyuni, huku vifaranga wakiwa na makazi yao maalumu.

Kuanza biashara

Bi Njeri 36, alianza ufugaji wa kuku mwaka wa 2016. “Ni kupitia ziara nilizofanya kwa wafugaji wakati nikitafiti kuanzisha mradi wa kuku ndipo nikagundua ndege ni rahisi mno kufuga, pamoja na gharama yao kuwa ya chini,” anaelezea.

Anasimulia kuwa aling’oa nanga na bata bukini wawili, walioanguliwa kutoka kwa mayai matano aliyonunua.

Kila yai aliuziwa Sh200 na anasema kwamba aliyanunua kutoka kwa wafugaji tofauti ili kuepuka kuwazalisha kutoka kwa ‘familia’ moja (inbreeding), suala linalofanya ndege kuwa dhaifu.

“Batabukini walifuatwa na batamzinga mwaka wa 2017, ambapo nilinunua watano kila mmoja nikiuziwa Sh2, 000,” anasema Bi Njeri ambaye ni mama wa watoto wawili.

Anaendelea kueleza kwamba alichinja mmoja na kugundua nyama ya bata mzinga ni tamu sana na yenye ladha ya kipekee.

Ni kufuatia hilo, mfugaji huyu na familia yake walisherehekea wawili zaidi, na kusalia na wawili, wa jinsia ya kike na kiume ili kuwazalisha.

“Hii leo ukizuru mikahawa inayopika nyama za ndege wanaoliwa, uagize ya bata mzinga utajua thamani yake. Ni ghali mno,” anasema.

Bata wa majini, ambao ni maridadi kimaumbile kwa kuwa na kichwa cha rangi ya kijani, manyoya ya zambarau, kahawia au kijivu na kanga-ndege wanaomuingizia pesa kama njugu, aliwanunua mwaka uliopita, 2018.

Mfugaji huyu anafichua kwamba alinunua bata wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike, kila mmoja akigharimu Sh2, 000.

Pia, kutoka kwa wafugaji tofauti, alinunua kanga wawili wa kike na mmoja wa kike, wote akiuziwa jumla ya Sh2, 400. Njiwa aliwaleta baadaye mwaka uliopita, japo anasema furaha yake ni kuona wakipaa na kutua.

Biashara yenye faida tele

Mradi huo umenawiri kutoka wazo la kurembesha boma hadi biashara inayomuingizia maelfu ya pesa, mbali na kutegemea uanguaji wa vifaranga wa kuku.

“Kabla kuanzisha ufugaji, nilikuwa nimewekeza katika biashara ya kuchora na kuchapisha (design & printing). Nilipoona shughuli za ufugaji zina mapato, nilisitisha kazi hiyo, ili kuuvalia njuga kikamilifu,” Njeri anasema.

Ana viangulio vitatu, cha kutotoa mayai 2112, 1056 na 500.

Kwa wiki, huangua vifaranga wa kuku wasiopungua 6, 000 na ni kupitia biashara hiyo wateja wake wameinua kwa kiasi kikubwa ufugaji wa ndege.

“Wateja wa vifaranga wa kuku ndio walewale wanaonunua ndege ninaofuga. Wanapokuja, hufurahishwa na mandhari yaliyotwaliwa na rangi maridadi ya ndege na kelele zao zinazohinikiza mazingira na kuyafanya yavutie. Huagiza ndege hata kabla watage na kuanguliwa,” anafafanua.

Wakati wa mahojiano alisema huwa hauzi mayai ila huyazalisha vifaranga (value addition).

“Uuzaji wa vifaranga una faida kuliko mayai,” anasema.

Huangua vifaranga kwa viangulio anavyotumia katika kuku. Alisema huuza vifaranga wa ndege walio na umri wa kati ya siku moja hadi wiki moja. Wanaopitisha umri huo, huwahifadhi ili kuimarisha jitihada zake.

Idadi ya ndege

Kwa sasa ana batamzinga tisa wa kike na wawili wa kiume. Kanga, ni jumla ya saba – wawili wakiwa wa kiume. Idadi ndogo ya kanga inatokana na soko lake ambalo ni mithili ya mahamri moto sokoni.

Bata bukini ni 12, wawili wakiwa wa kiume. Bata wa majini ni 10 wa kike na 5 wa kiume.

Ana njiwa zaidi ya 15. Wakati wa mahojiano tulipata akiwa na vifaranga 10 wa ndege anaofuga, na alisema wote wana oda na hata kulipiwa ada.

Alifichua kwamba siku kadhaa zilizopita, alileta ndege wawili wanaojulikana kama vulturine guinea fowl, aina ya kanga maridadi na machachari.

Kwa mujibu wa takwimu za mfugaji huyu, batabukini hutaga wastani wa mayai 20 kwa mwezi. Anapoyaangua kwa viangulio, kifaranga wa siku moja hadi wiki moja humuuza Sh500.

Ingawa hajaweza kuibuka na mkondo sambamba wa utagaji wa kanga, Njeri anasema ndege hawa hutaga sana msimu wa baridi na ule ya wastani ikilinganishwa na wakati wa joto.

“Ni ndege wa mwituni, ambao wakiachiliwa hutaga popote. Nilishangaa kuona hutagia mchangani na kuficha mayai. Kuyapata huwa vigumu iwapo mkulima hatawafuatilia kwa umakinifu wa hali ya juu.

“Kinyume na bata bukini na bata wa majini, ambao ni watulivu, wanaotafuta mahala maalum pa kutagia na kusalia hapo, kanga wanahitaji kuongozwa. Hata hivyo, kanga ndio ndege nambari moja katika mauzo yangu,” anaelezea mfugaji huyu.

Anadokeza kuwa, kwa mwezi kanga mmoja hutaga zaidi ya mayai 15 huku kifaranga mmoja akigharimu zaidi ya Sh1, 000.

Batabukini, ndege watulivu na wanaoandamana pamoja kila wakati, utagaji wake si wa kuridhisha vile kwani kwa mwaka hutaga kati ya mayai 20 hadi 40.

Bi Margaret Njeri Maina akiwa na ndege anaofuga nyumbani. Picha/ Margaret Maina

Hata hivyo, ni ndege bora katika uatamiaji wa mayai na kutunza vikembe wake, ingawa Njeri huyaangua vifaranga kwa vifungulio.

Mbali na bata mzinga ambao hujiatamia mayai yake na kuangua vifaranga, mayai ya wale ndege wengine huyaangua kwa mashine (viangulio).

Bw Okuta Ngura, mtaalamu wa masuala ya ufugaji wa kuku na ndege, anasema maganda ya batamzinga ni magumu mno na yanawahitaji wenyewe kuyaatamia.

“Batamzinga wa kike husaidiana na wa kiume kuyaatamia,” anasema Bw Ngura ambaye hutoa huduma za kuku na ndege nchini na ukanda wa Afrika Mashariki kupitia kampuni yake ya Ngura Poultry Care.

Kwa mwaka, bata mzinga hutaga karibu mayai 100.

Kifaranga wa ndege huyu, Bi Njeri humuuza zaidi ya Sh1,000.

Uanguaji wa mayai ya ndege wengi huchukua muda wa kati ya siku 21 hadi 30.

Ndege wa umaridadi waliokomaa hununuliwa kwa pea, kiume na kike. Bata wa majini na kanga, pea moja hugharimu takriban Sh5, 000, huku bata bukini na mzinga ikigharimu Sh10, 000. Hukomaa miezi mitano baada ya kuanguliwa.

Lishe na changamoto

Njeri anasema ndege wanaofugwa tu kwa ajili ya umaridadi ni miongoni mwa nyuni rahisi zaidi kufuga;na biashara yenye faida ya haraka.

Kando na kuwalisha chakula maalumu cha kuku, na ambacho ni bei ghali, mfugaji huyu hupunguza gharama kwa kuwapa masalia ya chakula cha binadamu.

“Wanapenda ugali, punje za mchele na masalia mengine ya chakula. Pia, wanapenda majani kama ya mboga,” asema.

Wataalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji wanapendekeza ndege na kuku walishwe chakula chenye madini kamilifu.

“Vifaranga walishwe chick mash, wanaokua growers na wanaotaga layers mash,” anashauri Bw Okuta Ngura ambaye ni mtaalamu.

Mdau huyu, pia anahimiza umuhimu wa kuwanywesha maji mengi na safi.

Kulingana na Njeri, ndege anaofuga ni nadra kuathiriwa na magonjwa.

Bw Ngura hata hivyo, anasema magonjwa yanayoshuhudiwa kwa ndege ni kama vile; yanayoathiri sehemu za kupumua, kwa Kiingereza Chronic Respiratory Disease (CRD), Coccidiosis na Coryza.

Magonjwa mengine ni Newcastle na Salmonella.

Muhimu ni kwamba magonjwa hayo yanahitaji chanjo na matibabu.

Vimelea ni; viroboto, kupe, mchwa na minyoo.

Ili kuwadhibiti, Bi Njeri hudumisha kiwango cha juu cha usafi katika vizimba vya ndege na kuku, na hata katika mazingira.

Kando na kupulizia dawa dhidi ya vimelea, humwaga maji sakafuni na ukutani, ili kuwafurusha.

Mfugaji anashauriwa kuondoa ndege au kuku kizimbani wakati wa kupulizia dawa ya vimelea.

Njeri anasema kuwa, akiondoa gharama ya leba, chakula na matibabu, ndege hao humpa zaidi ya asilimia 50 ya mapato.

Ni muhimu kukumbusha kwamba ili kuruhusiwa kufuga ndege wa umaridadi na kurembesha boma, unapaswa kupata kibali kutoka kwa shirika la huduma ya wanyamapori nchini (KWS).

AKILIMALI: Ufugaji kanga unamdumisha kimaisha bila bughudha yoyote

Na CHARLES ONGADI

SIKU njema huonekana asubuhi , ndivyo hali inavyoashiria katika mtaa maarufu wa Makande Railways karibu sana na makazi ya wafanyikazi wa Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA) ya Makande, Mombasa.

Hapa tunamkuta Bw Joseph Juma, 51, maarufu kama ‘Jeyjey’ akiwa katika pilkapilka za kila siku za ufugaji wa ndege aina ya kanga.

Bw Juma ambaye ni afisa mshirikishi wa mipango katika shirika la kutetea haki za kibinadamu la Christian Human Rights na pia mshauri wa kisheria katika shirika la Wasioona la Vision of the Blind, ni mfugaji maarufu wa kanga Pwani.

Bw Joseph Juma akiwa na kanga anaofuga katika eneo lake la makazi katika mtaa wa Makande Railways, Mombasa. Picha/ Charles Ongadi

Kanga ni ndege wa jamii ya kuku ambaye mara nyingi huishi porini, mwenye rangi ya kijivu iliyokoza madoadoa meupe.

Bw Juma hata hivyo amevunja mwiko kwani anafuga aina tatu ya kanga, weupe pepepe wenye rangi ya kijivu iliyokoza madoadoa meupe na weusi tititi.

“Ninapenda kufuga aina tofauti ya kanga nikilenga wateja wa aina zote,” asema Bw Juma alipotembelewa na Akilimali hivi majuzi.

Huchukua kipindi cha kati ya miezi minne hadi mitano kwa kanga kukua na kukomaa kabla ya kuanza kutaga mayai akiwa na miezi sita.

Kulingana na Bw Juma, tofauti na kuku, kanga ana uwezo wa kutaga mayai 40 na kuyaangua yote baada ya mwezi mmoja bila hata moja kuharibika.

Bw Juma anasema mara baada kanga kuangua mayai na kupata vifaranga humpa muda wa mwezi mmoja u nusu kisha anawatenganisha na vifaranga hao ili aanze kutaga tena.

Bw Juma anafichua kwamba mbinu hii umhakikishia mfugaji kupata idadi kubwa ya kanga kwa kipindi kifupi.

Mbinu nyingine ya kupata idadi kubwa ya kanga ni kutomwacha kanga kulalia mayai yake pindi muda wa kulalia mayai unapofika.

“Wakati mwingine siachi kanga kulalia mayai yake na badala yake nawapa kuku wa kienyeji kulalia mayai hayo na kanga anapokosa kuona mayai yake anaendelea kutaga mayai zaidi na hata kufikisha 60,” afichua Bw Juma.

Anaongeza kwamba katika kipindi hicho anahakikisha kila kuku wa kienyeji analalia mayai 15 ya kanga hadi pale atakapoyaangua.

Kulingana na Bw Juma, hii inaleta uhusiano thabiti kati ya kanga na kuku ambapo utapata kuku akilea vifaranga vya kanga pasi na bughudha kati yao.

Hupata chakula cha kanga kutoka katika soko kuu la Kongowea ambayo mara nyingi huwa ni nyanya, mboga na wishwa au kununua katika maduka ya vyakula vya mifugo yaliyoidhinishwa.

Aidha, Bw Juma anaiambia AkiliMali kwamba wateja wake wengi ambao huwa ni wenye hoteli kubwa za kitalii mwambao wa Pwani hupenda kununua kanga weupe kuliko wale wa kawaida na weusi.

“Wanavutia na tena nyama yao ni nyororo na tamu kupindukia,” asema Bw Juma.

Anauza kanga mweupe aliyekomaa kwa Sh6,000 wakati kanga mwenye rangi ya kawaida na mwenye rangi nyeusi akichukuliwa kwa Sh3,000.

Wakati biashara inaponoga, ana uwezo wa kuuza kati ya kanga 10 hadi 15 kwa siku.

Hata hivyo, anakiri kwamba amekuwa akikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nafasi ya kutosha ya kuendesha ufugaji wake barabara.

“Niko katikati ya makazi na mara nyingi huwa ni rahisi sana kanga hawa kuibwa pasipokuwa na ungalizi wa kutosha,” asema.

Mkurupuko wa magonjwa mara nyingi humsababishia hasara hasa hatua ya haraka inapokosa kuchukuliwa kuokoa hali.

Anampongeza Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho kwa kumpa sapoti katika ufugaji wake ila anaomba kutengwa kwa eneo wazi kwa ufugaji huu ambao ni nadra kupatikana eneo la Pwani.

Anashauri wafugaji hasa wa ndege mkoani pwani kukumbatia ufugaji wa kanga akisema unalipa vyema huku akishauri vyuo na shule kumtembelea kupata mbinu bora ya ufugaji wa kanga.

Familia za waliokufa Ethiopia zahangaishwa na mawakili

Na PHYLIS MUSASIA

MAWAKILI wakiwemo wa kutoka ng’ambo, wameanza kuziandamana familia za waliopoteza jamaa zao kwenye mkasa wa ndege ya Ethiopian Airlines mapema mwezi huu.

Familia za waathiriwa zinasema zimechoka kupokea simu kutoka kwa watu waonajitambulisha kama mawakili, huku wengine SMS zinazowaarifu waungane kwa pamoja na wenzao ili waweze kusaidiwa kupata fidia.

Hii ni licha ya Ethiopian Airlines kusema kuwa itawalipa fidia jamaa za watu 157 waliongamia Machi 10 kwenye ndege hiyo wakiwemo Wakenya 36.

Familia moja mjini Nakuru iliambia Taifa Leo kuwa, wiki jana ilitembelewa na kundi la watu waliojitambusha kama mawakili tajika Nairobi.

“Walitwambia wamekuja kuomboleza nasi na wamejitolea kutusaidia tupate fidia. Walipoondoka, nilipata ujumbe mwingine kwenye simu yangu uliotoka kwa mtu aliyejitambulisha kwa jina la Richmond. Alinieleza kuhusu kampuni yake ya uwakili, akidai imejitolea kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapata fidia bila kulipia chochote,” akaeleza.

Aliongezea kuwa, ujumbe huo ulimtaka pia azifikishie ujumbe familia za waathiriwa wengine.

Familia nyingine iliyoomba kutotajwa, ilisema ilijiwa na kundi moja lililojitambulisha kufanya kazi na kampuni ya upelelezaji wa kibinafsi Nairobi, na kudai kuwa limepewa kibali cha kukusanya familia za waathiriwa wa mkasa huo wa ndege ili waweze kusaidiwa kwenye kesi ya fidia dhidi ya kampuni ya Boeing.

Mmoja wa familia hiyo alisema alipokea ujumbe kwenye WhatsApp uliosemekana ni kutoka kwa kampuni moja ya mawakili kutoka Marekani, ukidai kushirikiana na Ethiopia Airlines kuishtaki kampuni ya Boeing ili iwalipe waathiriwa fidia.

Waathiriwa wanaomba serikali kuingilia kati suala hilo ili kuwalinda dhidi ya matapeli.

Wakili Steve Ogolla amekashifu vitendo hivyo vya mawakili, na kuomba familia za waathiriwa ziwe na uangalifu na kuwasilisha malalamishi yao haraka iwezekanavyo katika ofisi za sheria nchini kuhusu kuhangaishwa huko.

Familia hizo ziko kwenye majonzi zaidi baada ya kukosa kupata miili ya wapendwa wao, kwani iliharibiwa kiasi cha kutotambulika kwenye ajali hiyo.

MKASA WA ETHIOPIA: Dhiki ya kuzika mchanga

NA MASHIRIKA

SHIRIKA la ndege la Ethiopia limewapatia jamaa wa familia za watu 157 waliokufa kwenye ajali wiki iliyopita, mifuko yenye mchanga kwenda kuzika. Hii ni baada ya mabaki ya walioangamia kukosekana.

Shirika la habari la BBC lilinukuu shirika la AP Jumapili likiripoti kuwa kila familia ilipewa kilo moja ya mchanga uliochukuliwa kutoka eneo ambapo ndege hiyo ilianguka, ilipokuwa ikielekea Nairobi kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Hii ilifanyika huku idadi ya Wakenya waliokufa ikiongezeka kutoka 32 hadi 36, baada ya kufahamika kuwa wanne zaidi walikuwa wametumia paspoti za mataifa ya kigeni kusafiri.

Hapo jana, mmoja wa familia ya Cosmas Rogony, ambaye ni miongoni mwa walioangamia, aliambia Taifa Leo kuwa jamaa wao waliokuwa wamesafiri Addis Ababa walirejea wakiwa na mchanga waliopewa Ethiopia.

Alisema kuwa wazee wa ukoo wa marehemu watafanya kikao leo kuamua kitakachofanyika baada ya mwili wa mpendwa wao kukosekana.

BBC ilisema kuwa Ethiopian Airlines ililazimika kuwapa mchanga jamaa wa waliokufa baada ya kuwa vigumu kutambua miili.

Familia zimeambiwa kuwa itachukua hadi miezi sita kutambua mabaki ya miili ya 157 walioangamia.

Wachunguzi wamekusanya vipande vidogo vidogo takriban elfu tano vya mabaki ya miili ya binadamu katika eneo la ajali. Vipande hivyo ni kama vile vidole na mifupa. Ripoti zinasema sehemu kubwa zaidi ya mwili ambayo ilipatikana ni mkono.

Haijafahamika kiini cha ajali hiyo kufikia sasa huku uchunguzi unaoshirikisha Ethiopia, Ufaransa na Amerika ukiendelea.

Hapo jana, maelfu ya waombolezaji walilazimika kufanya ibada ya wafu mbele za majeneza yaliyokuwa tupu baada ya kukosa miili ya wapendwa wao.

Majeneza 17 yalifunikwa kwa bendera ya kitaifa ya Ethiopia na kuzungushwa katika barabara za Addis Ababa, huku baadhi ya jamaa za marehemu wakizimia.

Wasafiri kutoka mataifa zaidi ya 30 walikuwa kwenye ndege hiyo ilipoanguka katika eneo la Bishoftu, kilomita 60 kutoka Addis Ababa.

“Upelelezi wa kisa kikubwa namna hii huhitaji uchanganuzi wa kina na muda mrefu kufahamu ukweli,” akasema Waziri wa Uchukuzi wa Ethiopia, Dagmawit Moges.

Vifaa vya kurekodi shughuli za ndege almaarufu kama ‘black box’ vilipatikana na kupelekwa Ufaransa ili habari zilizomo zitolewe na kuchunguzwa.

Wapelelezi nchini Ufaransa walisema Jumamosi kuwa walifanikiwa kutoa habari zilizokuwemo kwenye vyombo hivyo na kuzikabidhi kwa wapelelezi wa Ethiopia.

Ilikuwa imefichuka awali kwamba rubani wa ndege hiyo aliwasiliana na kituo kikuu cha uwanja wa ndege wa Bole, na akaeleza alikuwa anakumbwa na matatizo kudhibiti ndege. Aliruhusiwa kurejea uwanjani humo lakini ndege ikaanguka kabla arudi.

Idara ya Uchukuzi wa Ndege Amerika, ilisema uchunguzi wake kuhusu mienendo ya ndege hiyo umeonyesha dakika zake za mwisho zilifanana na zile za ndege ya Lion Air, ambayo ilianguka Indonesia mnamo Oktoba mwaka uliopita na watu 189 wakafariki.

Ndege zote mbili zilikuwa aina ya Boeing 737 MAX 8, ambazo sasa zimepigwa marufuku kusafiri katika mataifa mengi ulimwenguni ikiwemo Amerika, ambako ndege hizo hutengenezwa.

NGILA: Teknolojia inayoua wanadamu yafaa kukomeshwa

NA FAUSTINE NGILA

KWA mara ya pili chini ya miezi sita, ndege aina ya Boeing 737 MAX 8 ilianguka dakika chache baada ya kupaa angani na kuua watu 157 Ethiopia.

Oktoba mwaka uliopita, watu 189 waliangamia kwenye aina sawa ya ndege nchini Indonesia. Kiufundi, lazima kuna tatizo katika aina hii ya ndege inayosababisha maafa miezi michache baada ya kununuliwa.

Huku familia zikizidi kuomboleza jamaa na marafiki waliopoteza maisha, maswali yameibuka upya kuhusu usalama wa aina hiyo ya ndege, ambayo ni muhimu kwa Amerika katika mipango yake ya teknolojia ya angani.

Kutokana na hili, mataifa ya Uchina, Indonesia, Singapore, Australia, Brazil, Argentina, Mexico na Ethiopia yamechukua hatua muhimu ya kusitisha usafiri kwa aina hiyo ya ndege kwa kuwa usalama wake umejaa shaka.

Uchunguzi wa mapema kutoka kwa tovuti ya Sweden wa kufuatilia ndege zote angani, flightradar24, imefichua kuwa ndege hiyo aina ya Boeing 737 MAX 8 ilikosa udhibiti wakati wa kupaa.

Ajali ya Indonesia pia ilitokea dakika chache baada ya kupaa, huku uchunguzi zaidi ukionyesha kuwa ndege hiyo ina programu ya ambayo haipo kwa aina zingine za ndege, ambayo huwatatiza marubani.

Programu hiyo mpya inafaa kusaidia ndege hiyo kupaa bila tatizo, lakini wakati wa ajali ya Indonesia, ilikuwa inailazimisha ndege kwenda chini kila mara licha ya juhudi za rubani kuisitiri hewani.

Baada ya ajali hiyo, kampuni ya Boeing ilituma ilani ya dharura ikionya marubani kuhusu tatizo katika programu hiyo, huku ikiahidi kuunda programu nyingine ya kuondoa tatizo hilo.

Ingawa siwezi kusema kuwa programu hiyo ndicho kiini cha ajali ya Ethiopia, kwa kuwa makosa ya kibinadamu pia huchangia kwa ajali, teknolojia ambayo inaletea wanadamu maafa inafaa kuondolewa kwa vifaa vinavyonunuliwa kwa matumizi ya watu, hasa usafiri.

Ninatambua kuwa teknolojia ni nguzo kuu ya maendeleo ya kila taifa, lakini iwapo uvumbuzi au utekelezaji wake una shaka, basi teknolojia hiyo inafaa kurudishwa jikoni na kuundwa vyema kwa kuzingatia usalama wa wanadamu, wanyama na mazingira.

Kampuni ya Boeing yaweza kuomba radhi kwa vifo vya watu 346 ambao waliangamia kwa ndege iliyounda, lakini haiwezi kuwafufua watu hao, wala kuzipatia familia zilizotegemea watu hao matumaini mbadala kwa maisha ya usoni.

Ni jambo la busara kwa wavumbuzi kuwa makini zaidi wanapotengeneza teknolojia ya kutumika na wanadamu, kwa kuzingatia usalama wake katika nyanja zote za maisha.

fmailu@ke.nationmedia.com

Ndege mbili aina ya Boeing 737 MAX 8 zapiga abautani angani

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

NDEGE mbili aina ya Boeing 737 MAX 8 za Shirika la Ndege la Uturuki ambazo zilikuwa zikisafiri kuelekea Uingereza zililazimika kupiga abautani hewani baada ya Uingereza kuweka marufuku dhidi ya ndege hizo kusafiri katika anga yake Jumanne.

Ndege hizo zilikuwa zimeanza safari katika Uwanja wa Kimataifa wa Instanbul, Uturuki, kabla ya Mamlaka ya Kusimamia Safari za Angani nchini Uingereza kutangaza marufuku hiyo. Hii ilikuwa ni dakika chache baada ya saa saba mchana saa za Uingereza.

Na kufuatia hatua hiyo, takriban watu 300 ambao walikuwa wamepanga kusafiri kutoka Uingereza kwenda jijini Instanbul waliachwa wakihangaika katika viwanja vya ndege vya Birmingham na Gatwick.

Hatua hii imechukuliwa na Uingereza baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia Airlines ya aina hiyo kuanguka na kuwaua watu 157 mnamo Jumapili dakika sita baada ya kupaa angani.

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka uwanja wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Nairobi.

Zaidi ya mataifa 13 yamepiga marufuku ndege hizo zinazotengenezwa Amerika kufikia sasa. Miongoni mwao ni China, Australia, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ireland, Ufaransa, Indonesia, Brazil, Afrika Kusini, Mexico, Ujerumani na Ethiopia.

Hatuhitaji marubani tena – Trump

Na WAANDISHI WETU

RAIS  wa Amerika Donald Trump, ametilia shaka uwezo wa marubani kuendesha ndege za kisasa.

Akizungumza siku mbili baada ya ndege ya Ethiopia kuanguka na kuua watu 157 wakiwemo Wakenya 32, rais huyo mbishi alisema ndege zimekuwa ngumu zaidi kuendesha, na hivyo zinahitaji wataalamu wa teknolojia za kisasa zaidi kuliko marubani.

“Marubani hawahitajiki tena, mbali wanasayansi wa kompyuta kutoka MIT (Massachusetts Institute of Technology),” akasema kwenye mtandao wa Twitter.

Alisema hayo huku serikali ya Amerika ikitetea usalama wa ndege za Boeing 737 MAX 8, nayo mataifa zaidi yakipiga marufuku utumizi wa ndege hizo baada ya ajali iliyosababisha vifo vya watu 157 Jumapili.

Jana Uingereza, Australia, Malaysia, Singapore, Australia, Afrika Kusini, Brazil na Mexico zilijiunga na mataifa ambayo yalizuia utumizi wa ndege hizo huku ikiripotiwa marubani Argentina walisusia kuziendesha wakihofia usalama wao.

Lakini Mamlaka ya Kitaifa ya Ndege nchini Amerika (FAA) ilituma taarifa kimataifa kuhakikisha usalama wa ndege hizo.

Ajali ya Jumapili ilikuwa ya pili ya aina hiyo ya ndege katika kipindi kifupi. Oktoba mwaka uliopita, ndege aina hiyo iliyomilikiwa na shirika la Lion Air ilianguka Indonesia na kuua watu 180.

Ilibainika kuwa baada ya ajali ya Indonesia, Boeing iliagizwa na FAA kurekebisha programu za ndege hiyo ambazo zinashukiwa na wataalamu kusababisha ajali.

Imefichuka pia kampuni hiyo imekuwa ikiendeleza mikakati ya kutengeneza upya miongozo ya mafunzo kwa marubani.

Kufikia sasa, kuna jumla ya ndege 387 za aina hiyo zinazomilikiwa na mashirika mbalimbali ulimwenguni.

Huku hayo yakijiri, familia na marafiki wa rubani Yared Getachew walianza kumiminika Mombasa kwa ajili ya swala za mwisho za Kiislamu kwa mwendazake ambaye ni raia mwenye asili ya Kenya na Ethiopia.

Mjombake marehemu, Bw Khalid Shapi alisema swala za mwisho zitafanyika katika msikiti wa Baluchi.

Katika Kaunti ya Kisii, familia katika kijiji cha Mesisita, Kaunti ndogo ya Kisii Kusini, inaomboleza mpendwa wao. Bi Ann Birundu aliyekuwa akisomea uhandisi katika chuo cha Boku, Austraria.

Tuliiona ndege ikichomeka ikiwa angani – Mashahidi

VALENTINE OBARA Na MASHIRIKA

UCHUNGUZI wa kujua chanzo cha ajali ya ndege iliyotokea Jumapili na kusababisha vifo vya watu 157, wakiwemo Wakenya 32 nchini Ethiopia, umeshika kasi baada ya chombo muhimu cha ndege hiyo kupatikana.

Hayo yalijiri huku wachunguzi wakitathmini kuhusu uwezekano kwamba ndege iliangushwa, ikizingatiwa Serikali ya Amerika ilikuwa imeonya raia wake Ijumaa kutosafiri katika uwanja wa ndege wa Bole nchini Ethiopia mnamo Jumapili.

“Raia wa Amerika wameshauriwa wasiwasili wala kusafiri katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Bole, Machi 10, na wafanyakazi wa ubalozi pia wamekatazwa kwa muda kutosafiri kuelekea Oromia,” ilani hiyo ikasema.

Ndege hiyo ilianguka katika eneo la Oromia, ambako kumekuwa na maandamano dhidi ya serikali ya Ethiopia. Hata hivyo, wataalamu walisema ukweli utajulikana baada ya upelelezi kukamilika.

Maafisa walipata kifaa cha kurekodi shughuli za ndege almaarufu kama ‘black box’ kutoka kwenye vifusi vya ndege ya shirika la Ethiopian Airlines, aina ya Boeing 737 MAX 8 huku uvumi ukienea kuhusu chanzo cha ajali.

Kwa kawaida, wapelelezi wa ajali za ndege huchunguza masuala kama vile ubora ndege, weledi wa marubani, hali ya hewa na uwezekano kwamba ndege iliangushwa kusudi pengine na magaidi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Ethiopian Airlines, Tewolde GebreMariam alipohojiwa Jumapili alisema hawatapuuza uwezekano wa ugaidi katika uchunguzi utakaofanywa.

Mbali na maafisa wa Serikali ya Ethiopia, upelelezi huo unashirikisha wapelelezi wa Serikali za Kenya na Amerika na wataalamu wa ndege kutoka kampuni ya Boeing iliyo Amerika.

Walioshuhudia kisa hicho katika eneo la Bishoftu, kilomita 60 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bole, ambapo ndege nambari ET302 ilikuwa imetoka, walisema ilianza kuwaka moto ikiwa angani.

“Ndege hiyo ilikuwa tayari imeshika moto kabla ya kuanguka. Ilipoanguka kulikuwa na mlipuko mkubwa. Moto ulikuwa umewaka katika upande wa nyuma na ndege ilikuwa ikiyumbayumba kwa kishindo,” akasema shahidi Tegegn Dechasa, aliyehojiwa katika eneo la mkasa.

Shahidi mwingine, Sisay Gemechu alisema: “Ilionekana rubani alilenga kutua kwenye uwanja tambarare ulio hapa karibu lakini ndege ikaanguka kabla ifike hapo.”

Waziri wa Uchukuzi, James Macharia alisema Kenya imetuma mpelelezi wake Ethiopia kwa vile ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya raia walioaga.

Mataifa 13 yasitisha safari za Boeing 737 MAX 8

Na VALENTINE OBARA

MASHIRIKA ya ndege katika nchi mbalimbali, yamesitisha utumizi wa ndege aina ya Boeing 737 MAX 8, kufuatia ajali iliyotokea Jumapili nchini Ethiopia na kuangamiza watu 157 wakiwemo Wakenya 32.

Huku uchunguzi ukianzishwa kujua chanzo cha ajali ya ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Nairobi kutoka Addis Ababa, mashirika katika nchi 13 yamesitisha utumizi wa ndege hizo mara moja kwa sababu za kiusalama.

Mashirika ya ndege ya mataifa ya Uchina, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Ireland, Malaysia, Mexico, Brazil, Singapore, Australia, Cayman, Indonesia na Ethiopia yalisema hatua hiyo itadumu kwa muda usiojulikana.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Meneja wa Ethiopian Airlines hapa Kenya, Bw Yilma Goshu, alisema hatua hiyo ilianza kutekelezwa Jumapili.

“Hii haimaanishi kwamba ajali ilisababishwa na muundo wa aina hii ya ndege bali ni hatua ya tahadhari huku uchunguzi ukiendelezwa. Tunalenga zaidi kushughulikia uchunguzi kwa ubora wa kimataifa mbali na kufariji na kuwapa ushauri nasaha jamaa na marafiki wa waathiriwa,” akasema.

Uamuzi wa mashirika kusitisha utumizi wa ndege hizo umetokana na kuwa hii ni mara ya pili kwa aina ya ndege ya Boeing 737 MAX 8, ambazo zilizinduliwa mwaka wa 2016, kupata ajali dakika chache baada ya kupaa.

Ajali nyingine ilitokea Oktoba mwaka uliopita Indonesia na kuua watu 180, ikasemekana kulikuwa na hitilafu ya programu za kiteknolojia.

“Tutachukua hatua zote zinazohitajika kwa usalama wa ndege zetu kabla zirudi kuhudumia wateja wetu,” Afisa Mkuu Mtendaji wa Cayman Airways, Bw Fabian Whorms akasema.

Shirika la Air China ambalo lilianza kutumia ndege za Boeing 737 MAX 8 katika mwaka wa 2017, lilisema ajali ya Ethiopia ilifanana sana na ile ya Indonesia na hivyo basi ndege hizo zitaendelea kutumiwa tu baada ya kuthibitishwa zina usalama wa kutosha.

Mashirika mengine ya ndege yalisema yanafuatilia hali ilivyo kabla yafanye uamuzi wa iwapo yatandelea kutumia ndege hizo huku ikiripotiwa bei ya hisa za kampuni ya Boeing ilianza kushuka kwa kasi jana.

“Nilikasirika sana nilipofungiwa nje ya ndege ya mauti Ethiopia’

Na LEONARD ONYANGO

KUCHELEWA kwa dakika mbili pekee kulimfanya raia wa Ugiriki kunusurika kifo katika ajali ya ndege iliyosababisha vifo vya watu 157.

Antonis Mavropoulos, sasa angekuwa mwathiriwa wa 158, endapo angewasili mapema na kuabiri ndege hiyo.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 MAX iliondoka jijini Addis Ababa saa 2:38 asubuhi na kupoteza mwelekeo dakika sita baadaye. Ilianguka karibu na mji wa Bishoftu takribani kilomita 60 kutoka Addis Ababa.

“Nilikasirika sana nilipofika katika lango nikakuta limefungwa na hakukuwa na mtu wa kunisaidia,” akasema Mavropoulos kupitia mtandao wa Facebook ambapo ameweka picha ya tiketi yake.

Mavropoulos, ambaye ni rais wa shirika la International Solid Waste Association, alikuwa akielekea Nairobi kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), kulingana na shirika la habari la Ugiriki, Athens News Agency.

“Nilipelekwa katika kituo cha polisi kilichoko katika uwanja wa ndege. Afisa wa polisi aliniambia niwe mpole na kuomba Mungu kwa sababu sikupanda ndege hiyo,” akasema Mavropoulos.

Polisi walimzuilia kwa muda wakimhoji ni kwa nini hakupanda ndege hiyo iliyopata ajali: “Walisema hawangeweza kuniachilia huru kabla ya kunihoji na kujua sababu yangu kukosa kupanda ndege iliyoanguka,” akasema.

Wakati huo huo, mkazi wa Dubai, Ahmed Khalid pia ameelezea furaha yake huku akidai kuwa alifaa kuabiri ndege iliyopata ajali.

Alifaa kuabiri ndege ya kuunganisha lakini akaabiri mbadala alipopata ndege iliyoanguka ikiwa imeondoka.

Majonzi, vilio baada ya ajali ya ndege Ethiopia

Na WAANDISHI WETU

MAJONZI yalitanda maeneo mbalimbali ya nchi, jamaa na marafiki wakiomboleza wapendwa wao waliofariki kwenye ajali ya ndege nchini Ethiopia, na kuwaua watu 157, wakiwemo Wakenya 32 mnamo Jumapili.

Katika kijiji cha Kwa Amos, eneobunge la Bahati katika Kaunti ya Nakuru, familia moja inaomboleza vifo vya watu watano.

Familia hiyo ya Mzee John Quindos Karanja, ilipoteza mkewe Wangui Quindos, bintiye Caroline Nduta Karanja na wajukuu Ryan Njoroge (7), Kelly Paul (5) na Ruby Pauls (miezi tisa).Watano hao walikuwa miongoni mwa Wakenya 32 waliangamia kwenye ajali iliyohusisha ndege ya kampuni ya Ethiopian Airways, iliyokuwa ikienda Nairobi kutoka mjini Addis Ababa.

Hapo jana kifaa cha kurekodi habari za safari za ndege (Black Box) kilipatikana kwenye vifusi.

“Sina amani na bado nimechanganyikiwa. Nimepoteza familia yangu. Niko Nairobi nikijaribu kufuatilia mambo hapa na pale kabla ya kurudi nyumbani hapo baadaye,” akasema Bw Karanja.

Mmoja wa majirani wake aliambia Taifa Leo kuwa, Bw Karanja alikuwa ameenda Nairobi Jumapili asubuhi kupokea familia yake iliyokuwa ikisafiri kutoka Canada, ambako mkewe amekuwa tangu mwaka jana akimtembelea bintiye.

“Mkewe Karanja alisafiri Canada mwaka uliopita kwa mwaliko wa bintiye aliyekuwa akiishi Canada pamoja na mumewe,” akasema Bw Martin Muchiri, ambaye ni rafiki wa karibu wa familia ya Bw Karanja.

Bw Karanja alikuwa ameondoka nyumbani Jumapili asubuhi kuelekea Nairobi kuwalaki wapendwa wake, kabla ya kupokea habari hizo za majonzi.

Bw Muchiri alisema walikuwa wameandaa karamu ya kukaribisha familia hiyo lakini ilipofika jioni Bw Karanja alimpigia simu akimweleza mipango yote ilikuwa imeharibika kufutia vifo vya wapendwa hao.

Mjini Homa Bay, maombolezo yalitanda katika boma ya Mzee Philip Jaboma Akeyo, ambaye bintiye Isabela Jaboma alikuwa miongoni mwa walioangamia.

Alisema alikuwa alipokea habari hizo kutoka kwa mwanawe wa kiume, Alan Onyango, aliyempigia simu kutoka Nairobi mnamo Jumapili alasiri.

Isabela, aliyekuwa na umri wa miaka 31, alikuwa akisafiri kutoka Cairo nchini Misri, alikokuwa ametumwa kikazi na shirika la Hope for Cancer Kids.

Mzee Jaboma alisema alizungumza na bintiye kwa simu mara ya mwisho wiki iliyopita alipokuwa akipanda ndege kuelekea Misri.

“Nduguye alikuwa uwanja wa Jomo Kenyatta kumpokea wakati alipofahamishwa kuwa Isabela alikuwa miongoni mwa waliofariki,” akaeleza.

Katika kaunti za Vihiga na Trans Nzoia, familia ya Cedric Galia Asiavugwa wa miaka 32, ilikuwa kwenye majonzi baada ya kupokea habari za kifo chake.

Marehemu Cendric alikuwa akirudi nyumbani kutoka mjini Washington nchini Amerika, kuhudhuria mazishi ya mmoja wa jamaa zake. Alikuwa akisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Georgetown.

Alizaliwa katika kijiji cha Luzu kilichoko Chamakanga katika Kaunti ya Vihiga, kabla ya familia yake kuhamia eneo la Mawe Tatu, Kaunti ya Trans Nzoia.

Dadake, Beatrice Achitsa alisema babake, Govedi Asiavugwa yumo Nairobi kufuatia habari hizo za kuhuzunisha alizosema zimetikisa familia yake.

Rafiki za marehemu walisema alikuwa na nia ya kuwa padre kabla ya kubadili mawazo na kusomea sheria. Amemuacha mjane na mtoto

Katika Kaunti ya Kakamega, familia ya Derick Lwugi Kivia ilikuwa ikiomboleza kifo cha mwanao wa miaka 54, waliyemtaja kama tegemeo kuu kwao.

Marehemu Lwugi, ambaye alizaliwa katika kijiji cha Naliaba eneobunge la Ikolomani, alikuwa na uraia wa Kenya na Canada.

Mamake, Elizabeth Chumazi, alisema mwanawe alikuwa ameahidi kumpeleka hospitali kwa matibabu maalum baada ya kufika Kenya.

Alisomea katika shule ya msingi ya Naliaba, Kakamega High, Chavakali High na Chuo Kikuu cha Jepun alikopata digrii ya Uhasibu.

Familia yake ilisema alikuwa akiwafadhili kimasomo wanafunzi 25 wa sekondari kutoka Kakamega na Vihiga. Amemuacha mjane na watoto watatu.

Taarifa ya Phylis Musasia, Derick Luvega, George Odiwuor and Shaban Makokha

Dakika za mwisho kabla ya mkasa wa ndege ya Ethiopia

ALLAN OLINGO Na PETER MBURU

KENYA inaomboleza vikubwa kufuatia ajali ya ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Ethiopia kuelekea Nairobi, ambapo Wakenya 32 waliangamia, kati ya abiria 157 ambao walikuwa katika ndege hiyo.

Iliripotiwa kuwa ndege hiyo ilionyesha dalili za hitilafu dakika mbili tu baada ya kupaa kutoka uwanja wa Kimataifa wa Bole, Jijini Addis Ababa saa 2: 38 (asubuhi) ya Jumapili.

Baada ya mitambo ya usafiri wa ndege kudokeza kuwa haikuwa ikipaa kwa njia inayofaa, hali hiyo inaripotiwa kuendelea kwa dakika tatu na mnamo saa 2:42 asubuhi, ndege hiyo ikakosekana katika mitambo ya kufuatilia usafiri.

Rubani wa ndege hiyo Yared Getachew anaripotiwa kuwa alifahamisha idara ya kufuatilia usafiri wa ndege katika Ethiopia kuwa alikuwa akikumbana na matatizo baada ya kupaa na alitarajiwa kurejea uwanjani Bole kutua tena.

Ndege hiyo ilianguka karibu na kijiji cha Tulu Fara, Bishoftu, takriban kilomita 60 kusini magharibi mwa Addis Ababa na kuua wasafiri wote, marubani wawili na wahudumu sita.

Ndege hiyo ilianza kufanya kazi nchini Ethiopia Oktoba 2018.

Waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni raia wa mataifa 33, na kati yao ni Kenya iliyopata pigo kubwa zaidi.

Raia 18 wa Canada waliangamia, tisa wa Ethiopia, kisha Italy, China na Marekani kulingana na wingi wa waliofariki.

Waliokufa walikuwa wa kutoka mataifa 11 ya Afrika na 13 ya bara Uropa.

Wasimamizi wa usafiri wa ndege hiyo walisema bado haijabainika chanzo hasa cha mkasa huo, wakisema uchunguzi umeanzishwa.

“Bado ni mapema sana kubaini kiini cha ajali na uchunguzi zaidi utafanywa kwa ushirikiano na washikadau, ikiwemo kampuni iliyotengeneza ndege hiyo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji Tewolde Gebremariam.

Aliitaja siku ya ajali hiyo kuwa “ya huzuni sana na ya mkasa.”

Ndege hiyo ilikuwa imesafiri kutoka Johannesburg hadi Addis Ababa, ambapo ilikaa saa tatu kabla ya kupaa tena kuelekea Nairobi, Bw Gebremariam akasema.

Ilikuwa imefanyiwa ukaguzi wa kina mnamo Februari 4, baada ya kununuliwa Oktoba.

Maafisa wa mashirika ya kimataifa kama Katibu Mkuu wa Muungano wa UN Antonio Guterres waliomboleza pamoja na familia za walioangamia.

Waziri wa Uchukuzi humu nchini James Macharia alisema kuwa timu kutoka Kenya ikiongozwa na Katibu katika wizara hiyo Esther Koimett ilitumwa Ethiopia Jumapili kufuatilia hali.

Ajali hiyo ilikuwa ya tatu kama hiyo ikihusisha ndege za Ethiopia, ambapo ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Beirut, Lebanon mnamo 2010 ilianguka punde tu baada ya kupaa na kuangamiza watu 90.

Mnamo 1996 vilevile, moja kati ya ndege za Ethiopia ilitekwa nyara ilipokuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi, kisha ikaanguka katika kisiwa cha Comoros, katika Bahari Hindi na kuua wasafiri 125.

MKASA WA ETHIOPIA: Ruto, Mudavadi na Maraga watuma risala za rambirambi

Na PETER MBURU

VIONGOZI mbalimbali Jumatatu waliendelea kutuma jumbe za rambirambi kwa familia za watu walioangamia katika mkasa wa ajali ya ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Ethiopia kuelekea Jijini Nairobi, Kenya, wote wakieleza kuwa vifo hivyo vya watu 157 ni pigo kwa dunia.

Baada ya ajali hiyo ambayo iliacha familia nyingi kwa huzuni, viongozi hao wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga walitumia mitandao ya kijamii kufariji familia hizo, na kuziombea amani.

“Wakenya wenzangu ambao wamepoteza wapendwa wao katika mkasa mbaya wa ajali ya ndege #ET302, Mungu awape nguvu ya kukabiliana na hali hii ngumu. Tunaelewa uchungu mnaopitia na tuko nanyi katika maombi,” akasema Bw Odinga, kupitia mtandao wa Twitter Jumatatu.

Jaji Mkuu David Maraga aidha alijiunga na viongozi waliokuwa wakiomboleza na familia hizo, akisema ajali hiyo ni mkasa wa kuhofisha.

“Najiunga na Wakenya na ulimwengu mzima kuomboleza walioangamia katika ajali ya ndege iliyokuwa ikitoka Ethiopia. Mawazo yangu yako kwa familia na washirika wa wale wote waliopoteza maisha yao. Mungu awape amani na nguvu ya kukabili hali hii,” akasema Bw Maraga.

Naibu Rais William Ruto Jumapili jioni naye alisema “Nimehuzunishwa na habari kuhusu ajali ya ndege iliyokuwa ikitoka Ethiopia kuelekea Nairobi asubuhi ya leo, mawazo yetu na maombi yako kwa familia za wale wapendwa wao walikuwa wakisafiri katika ndege hiyo.”

Rais Kenyatta pia Jumapili alisema “Tumehuzunishwa na habari kuhusu ajali ya ndege iliyokuwa ikitoka Ethiopia ambayo iliripotiwa kuanguka dakika sita baada ya kupaa, ikielekea Kenya. Maombi yangu yanaelekezwa kwa familia na washirika wa wale waliokuwamo.”

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi aidha aliomboleza pamoja na waliopoteza wapendwa, kama viongozi wake walivyotuma jumbe, pia naye akitumia mtandao wa Twitter kutuma rambirambi zake.