Wazazi watozwa ng’ombe 100 kwa utundu wa watoto wao

STEPHEN ODUOR na SIAGO CECE

WAZAZI wawili wametozwa faini ya ng’ombe 100 kwa jumla, baada ya watoto wao wenye umri wa miaka 15 na 17 kupatikana na hatia ya uasherati.

Wazee wa eneo la Kipini, Kaunti Ndogo ya Tana Delta walitoa uamuzi kuwa wazazi wa watoto hao walipe faini ya ng’ombe 50 kila mmoja.Kwa mujibu wa baraza la wazee, tabia ya watoto ilithibitisha wazazi hao, ambao tumewabana majina kwa sababu za kisheria, wameshindwa katika majukumu yao ya uzazi.

Walisema kitendo hicho ni haramu katika jamii na pia hakikustahili katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.Zaidi ya hayo, wazazi waliagizwa kuwapeleka watoto hao kwa shule za bweni zilizopo mbali kwa miaka miwili ili kudhibiti tukio hilo kujirudia.

Endapo wazazi hao watashindwa kutii maagizo ya wazee, familia husika zitatengwa na kufukuzwa kutoka kwa jamii.“Tumeona madhara ya kutosha ya uasherati katika jamii yetu. Imechangia sana kwa ndoa za mapema, mimba za utotoni, na ndoa za utotoni na hata umaskini,” alisema Mzee Sadiq Salat.

Hata hivyo, wazazi waliopewa adhabu wamekata rufaa, wakisema ni zaidi ya uwezo wao kifedha.

“Ni tabia ambayo watoto wamekuwa wakifanya, jamaa wengine hata ?waliwaambia wazazi kuihusu ila wakafanya makusudi kuifumbia macho,” alisema mzee Ramadhan Ishmail.

Wazee walisema walituma vijana eneo hilo kufanya uchunguzi wa siri ndipo walipowafumania watoto hao wawili Jumatatu.Wazazi waliitwa kuelezea tabia ya watoto wao, huku wazee wakiongozwa na Ustadh Salim Maneno wakitanguliza kuwachapa viboko 20 kila mtoto kabla kuwapa ushauri nasaha.

Kwingineko, Serikali ya Kaunti ya Kwale imewahimiza vijana wajitenge na itikadi za kigaidi na utumizi wa mihadarati.Waziri wa masuala ya kijamii na ukuzaji wa talanta kaunti hiyo, Bw Ramadhan Bungale amewataka vijana kujiunga na vyuo vya kiufundi ili kupata ujuzi wa kujiendeleza kimaisha.

Kaunti hiyo ni moja ya zile zilizo na idadi kubwa ya vijana wanaotumia mihadarati inayofanya wengi kujihusisha na uhalifu.“Vijana wengi wanajihusisha na mihadarati kwa sababu ya kukosa kazi, wakipata ujuzi huu wataweza kujitegemea na hawatakua na tamaa ya kutumia dawa hizo,” alieleza Bw Bungale.

Jaji akomesha utata kwa kuwapa wajane ng’ombe

Na BRIAN OCHARO

MAHAKAMA Kuu ya Malindi, Kaunti ya Kilifi imewapa wajane sita ng’ombe wanne kila mmoja baada ya familia kushindwa kukubaliana kuhusu ugavi wa mifugo hao.

Bw Arthur Jeremiah Tsumah ambaye alikuwa na wake sita na watoto 67, alifariki bila kuacha wasia mnamo 2012.

Baada ya kifo chake familia hiyo ililishindwa kukubaliana jinsi ya kugawana ng’ombe 25 wenye thamani ya Sh720,000 aliowacha marehemu.

Ingawaje familia hiyo ilikuwa na makubaliano ya jinsi ya kugawana mali nyingine ikiwemo mashamba makubwa, nyumba za makazi na za kukodisha zote zikikisiwa kuwa na thamani ya Sh30 milioni, walitofautiana katika ugavi wa mifugo.

Jaji Reuben Nyakundi, ambaye alisimamia suala hilo, aliwafungia watoto wao nje kwa sababu ya idadi yao kubwa na akaamua kugawa mifugo bila kujali idadi ya watoto katika kila nyumba.

Familia hiyo ilitaka kila mmoja wa wajane hao apate sehemu sawa ya mali bila ubaguzi.

Wajane wakubaliane

Ni kwa msingi huu ambapo Jaji alibaini kuwa, suala tata la mifugo liamuliwe baina ya wajane hao bila kuhusisha watoto wao.

“Kwa hivyo kila mwanamke atapewa ng’ombe wanne na watakaobaki wauzwe na mapato wagawiwe kwa usawa,” alisema Jaji.

Jaji pia amethibitisha barua za usimamizi zilizotolewa kwa wasimamizi wa mali hiyo na kuamuru kwamba mali ya mwendazake igawanywe kulingana na makubaliano ya ugavi huo.

“Kwa kuwa huu ni mzozo wa kifamilia hakuna amri yoyote kuhusu gharama ya kesi inatolewa katika uamuzi huu,” alisema jaji.

Korti ilibaini kuwa ushahidi uliotolewa awali kuhusu ugavi ulionyesha kuwa wasimamizi wa mali walikuwa na utata kwa sababu ya kulenga kuwaridhisha wahusika wote.

“Kwa hivyo mahakama haina sababu za kuvuruga jinsi ugavi wa mali ulivyopendezwa isipokuwa mzozo kuhusu mifugo. Jukumu la mahakama kwa hivyo ni kuhakikisha kuwa vigezo vya ugavi wa mali ambayo ilikuwa na utata vinaweza kufanywa kulingana na Sheria ya Urithi,” alisema jaji.

Jaji Nyakundi alibaini kuwa jukumu la wasimamizi ugavi wa mali ilifuata Kifungu cha 38 cha Sheria ya Urithi.

“Ni uamuzi wangu kwamba barua za usimamizi wa mali hiyo ithibitishwe na mali ya marehemu igawanywe kati ya walengwa kwa usawa na wajane pia wazingatiwe kama ilivyopendekezwa na wasimamizi na idhini husika,” alisema jaji huyo

Katika kuzingatia ugavi wa hisa za mali sawa kati ya watoto hao, korti ilisema kwamba ilikuwa dhahiri kwamba binti za marehemu pia walijumuishwa na kupewa kiwango sawa na wenzao wa kiume.

Polisi Samburu wapata ng’ombe 14 walioibwa

FAUSTINE NGILA

POLISI katika Kaunti ya Samburu wameokoa ng’ombe 14 ambao walikuwa wameibwa kutoka eneo la Tiamamut, Kaunti ya Laikipia.

Hiyo inafikisha 27, idadi ya ng’ombe walioibwa na kupatikana kuanzia Juli 25.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Samburu Bw Pius Murugu alisema kwamba ng’ombe hao ni kati ya ngo’mbe walioibwa Laikipia na familia ya washukiwa hao ilikuwa ikitafutwa na maafisa wa polisi.

“Maafisa wa usalama walishirikiana kuokoa ng’ombe 14 ambao ni kati ya ng’ombe 80 walioibwa Tiamamut mwezi uliopita,” alisema Bw Murugu.

Katika soko la Wamba afisa huyo alisema kwamba wanatafuta washukiwa saba ambao wanaaminika kuwa miongozni mwa wezi walioiba ng’ombe katika kaunti jirani.

“Juhudi za kutafuta kama kuna ng’ombe wengine ambao wamefichwa mahali zinaendelea,” alisema.

Ng’ombe 24 wa mbunge wafa baada ya kula chakula hatari

NA GEORGE SAYAGIE

Mbunge wa Emurua-Dikir Johanna Ngeno anakadiria hasara baada ya ng’ombe wake wapatao 24 aina ya Holstein Friesian wenye thamani ya Sh2.5 milioni kufa baada ya kula chakula kilichoangizwa kutoka nchi za nje.

Mbunge huyo wa Kanu ametishia kushtaki wauzaji wa lishe hiyo akisema kwamba ng’ombe hao walikuwa wanatoa maziwa lita 40 kila siku.

“Nilienda kwenye maabara ya kitaifa ya dawa na sampuli hizo ili kuchunguza kilochopeleka kifo cha ng’ombe wangu lakini hii lazima niende kortini,” alisema Bw Ngeno.

Katika mazungumzo ya simu na Taifa Leo Jumamosi, mbunge huyo alisema kwamba ng’ombe hao walianza kuanguka mmoja baada ya mwingine baada ya kula chakula hicho.

Kulingana na Bw Ng’eno, chakula hicho hatari kinapatikana kwenye maduka ya kuuza chakula cha mifungo.

Maelezo yaliyochapishwa kwenye magunia hayo yanaonyesha kwamba ni chakula cha mifugo, lakini tarehe ya chakula hicho kuharibika ni Januari 28, 2020.

AKILIMALI: Ifahamu mikate ya ng’ombe kutoka Kalro

NA RICHARD MAOSI

KILOMITA 16 hivi kutoka mjini Nakuru tunawasili katika makazi ya Miriam Wangare, mkazi wa Wanyororo B, eneo la Lanet ambaye ni mkulima mdogo wa ng’ombe wa maziwa.

Huu ni mwaka wa pili tangu aanze kulisha mifugo wake na aina maalum ya nyasi zinazotengeneza lishe ya kisasa, mikate ya ng’ombe, zilizovumbuliwa na Shirika la Utafiri wa Kilimo na Ufugaji (Kalro).

Anasema awali alikuwa akitumia nyasi za kawaida kama vile napier, kulisha ng’ombe wake lakini akahudhuria kongamano la wakulima 2017 kujifundisha nyenzo mbalimbali za kuboresha mazao ya mifugo wake kupitia lishe.

Alieleza Akilimali kuwa lishe hizi hutengenezwa, baada ya kukausha aina ya nyasi zinazojulikana kama Brachiaria (nyasi za kigeni), kisha zikachanganywa na virutubishi vya protini, kuokwa na kukaushwa.

“Mifugo hufurahia aina hii ya lishe kwa sababu ina ladha nzuri kuliko aina nyingine ya nyasi ambazo hazina madini ya kutosha,” anasema.

Pili alieleza kuwa nyasi ya brachiaria hustahimili hali ngumu ya mazingira kama vile ukame uliokidhiri na ukosefu wa rutuba katika mchanga, hivyo basi gharama ya kukuza nyasi hizi mara nyingi huwa ni nafuu. Picha/ Richard Maosi

Pili alieleza kuwa nyasi ya brachiaria hustahimili hali ngumu ya mazingira kama vile ukame uliokidhiri na ukosefu wa rutuba katika mchanga, hivyo basi gharama ya kukuza nyasi hizi mara nyingi huwa ni nafuu.

Brachiaria huchukua miezi mitatu tu kukomaa ambapo mkulima huwa tayari kuzivuna kisha akazihifadhi katika ghala ama kulisha mifugo wake moja kwa moja zikiwa mbichi.

Kwa upande Wangare anasema mkulima anaweza kuongezea lishe hizi thamani kwa kuchanganya molasses, chumvi ya kawaida na kuoka mchanganyiko huu kisha akatengeneza miundo ya mikate .

Miundo hii inaweza kuhifadhiwa katika sehemu yenye joto jingi kama vile ndani ya kitalu ama kwenye jua ili iweze kushikamana vyema na kupoteza unyevu.

Wangare alisema kuwa mara ya mwisho alivuna mazao yake mwezi wa Novemba, mwaka wa 2019 na sasa anasubiri mazao ya pili kufikia mwezi wa Februari mwaka wa 2020.

Miriam Wangare akiwa katika shamba lake la Wanyororo Lanet Nakuru akiwalisha mifugo wake mikate ya kisasa. Picha/ Richard Maosi

Kwa ujumla anaungama kuwa tangu aanze kulisha mifugo wake na Feedblocks, amaeongeza faida kwa mazao yake ya maziwa ambapo yaliongezeka zaidi ya mara dufu chini ya kipindi cha wiki moja.

Awali alikuwa akipata lita 4 za maziwa kutoka kwa ng’ombe mmoja, lakini sasa anaweza kupata baina ya lita 8-10 kwa siku kwa kutegemea yeye huwalisha mifugo wake mara ngapi kwa wiki.

Tatu anasema kuwa ni rahisi kukuza aina hii ya nyasi za barachiaria kwani hahitaji uangalizi mkubwa iwapo shambani, kama vile kuondoa magugu wala kupalilia muradi mkulima awe ametumia mbegu zinazostahili.

Hatua za kutengeneza mikate ya ng’ombe

Hatua chache kutoka kwake Akilimali ilitembelea shirika la Kenya Agricultural and Livestock Research Organisation kupambanua namna ya kutengeneza mikate(feedblocks) inayoweza kudumu kwa muda mrefu.

Gharama ya kukuza lishe hii iko chini. Picha/ Richard Maosi

Tulikutana na Daktari Naftali Ondabu mtafiti wa lishe za mifugo ambaye alitupatia utaratibu wa kuandaa aina hii ya mikate, ambayo ndiyo uvumbuzi wa kwanza kabisa kufanyika humu nchini.

Anasema kuwa katika hatua ya kwanza pindi mkulima anapovuna nyasi zake(brachiaria, lucern ama Desmodium), anaweza kuzihifadhi katika jua ili ziweze kukauka kabla ya kuzioka.

Aliongezea kuwa sio nyasi za aina yoyote zinazoweza kutumika, kwa sababu ya kiwango tofauti cha madini yanayopatikana ndani ya malisho ya ngombe yanayokuzwa.

“Kwa mfano nyasi za brachiaria zinaongoza kwa kiwango cha juu cha protini ambacho kinaweza kufikia zaidi ya asilimia 70,”akasema.

Alieleza kuwa mara tu baada ya nyasi za brachiaria kukauka zinaweza kuchanganywa na molasses, kisha zikahifadhiwa katika sehemu isiyokuwa na unyevu zipate kukauka.

Anasema kwa kutumia maji ya moto ndani ya beseni ya kimo cha kawaida, mkulima anaweza kuchanganya nyasi zake zilizokauka na kuongezea chumvi ya kjawaida ili kuzipatia ladha.

Kutoka kwenye mchanganyiko huo mkulima anaweza kupata baina ya mikate 3-4 yenye kimo cha wastan ambayo inatosha kulisha ng’ombe wawili kwa siku nzima, bila kuongezea lishe nyingine.

Mara nyingi sio vyema kuhifadhi lishe zako katika sehemu yenye majimaji, kwa sababu maradhi ya vimelea vya fangasi yanaweza kuzuka na kuharibu ubora wa nyasi za brachiaria.

Anasema lishe za Feed blocks(mikate) haziwezi kufananishawa na aina nyingine ya lishe kwa sababu zimefanyiwa majaribio ya kimaabara na wakulima wana hakikisho kuwa zimepiku mifano ya hay.

“Wakulima wanaolengwa zaidi wakiwa ni wafugaji kutoka maeneo kame wanaopata changamoto kutafuta lishe wakati wa kiangazi kulisha mifugo wao,” akasema.

Alitaja maeneo kama Samburu, Marsabit ,Wajir , kajiado na Narok kama baadhi ya maeneo ambayo tayari yanaonekana kuja kufaidika na lishe hizi.

Aidha Ondabu alitoa tahadhari kwa wakulima wasitumie makapi ya mahindi kutengeneza lishe hii ,kwa sababu mahindi huwa yamebeba kiwango kikubwa cha sukari na ungaunga.

Nyasi za brachiaria zimeagizwa kutoka nchini Brazili lakini humu nchini zimepatiwa lakabu ya Maasai au Mombasa grass kutokana na kimo chake kirefu.

“Mkulima anaweza kuvuna tani 18 ya nyasi hizi kutoka katika kipande cha ardhi cha ekari moja, lakini akizikausha na kuzihifadhi kisha katengeneza hay uzito hupungua hadi tani 10,”akasema.

Ng’ombe walivyogeuka kuwa kero kwa wafanyabiashara Nairobi

Na SAMMY WAWERU

NG’OMBE huthaminiwa kwa ajili ya maziwa na nyama; bidhaa ambazo ni sehemu ya lishe ya kila siku.

Ngozi yake pia inatumika katika uundaji wa bidhaa mbalimbali.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara – hasa wa bidhaa za kula Kaunti ya Nairobi wanaouzia kandokando mwa barabara – wanatoa malalamiko kwamba mifugo hiyo inawahangaisha hasa ng’ombe wanaporuhusiwa kuzurura kiholela.

Wauzaji wa bidhaa kama mboga, matunda na hata viazi wamesema hawakosi kukadiria hasara inayosababishwa na mifugo hao.

“Kuna ng’ombe wanaoachiliwa kujitafutia lishe na wamekuwa kero kwa sie wafanyabiashara tunaouza bidhaa za kula hususan za mbogamboga,” akalalamika mama nmoja anayeuza mboga, matunda na karoti eneo la Roysambu wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

Kuna baadhi ya wakazi wanaofuga ng’ombe Nairobi na kwa sababu ya uhaba wa mashamba kukuza nyasi za mifugo, huwafungulia kujitafutia lishe kandokando mwa barabara.

Hata ingawa kuna wanaoandamana na wachungaji, wafanyabiashara tuliozungumza nao walisema hawajali bidhaa za watu.

“Hata wakila hawatufidii hasara tunayokadiria,” akasema muuzaji wa viazi mtaani Zimmerman.

Malalamiko hayo ni sawa na ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa za kula barabarani eneo la Githurai.

Katika barabara za mitaa mbalimbali Nairobi na Kiambu, hutakosa kutazama ng’ombe wakivuka.

Mwaka 2018 mbunge mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Kiambu Gathoni Wa Muchomba alikuwa ameahidi kuwasilisha mswada bungeni kuangazia suala la wakulima Kiambu na Nairobi kuhangaishwa na ng’ombe wanaoachiliwa kujitafutia chakula kiholela.

UFUGAJI KIBIASHARA: Amepiga hatua kuu maishani kwa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa

Na SAMUEL BAYA

KIJIJI cha Solai katika Kaunti ya Nakuru kiligusa vichwa vya habari mwaka 2018 wakati maji yalipasua kuta za bwawa la Patel na kuangamiza zaidi ya watu 40.

Hapo ilikuwa ni awali ila kwa sasa, na hasa baada ya mkasa huo, maisha ya wakazi yamekuwa yakiendelea polepole wakijaribu kusahau kilichotukia.

Baada ya dhiki ni faraja na kijiji hiki sasa kimeshuhudia miradi mbalimbali ya kilimo ambayo imeshika kasi huku wakazi wakiwa na lengo la kujikwamua kiuchumi.

Naam, hivyo ukipita mbele kidogo ya kituo hiki cha biashara ukielekea eneo la Kabazi, utakutana na Bw Edward Kiprotich. Yeye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, biashara ambayo inamsaidia kupambana na maisha.

“Nilikuja hapa mwaka wa 1997 ila nikaanza shughuli za ufugaji mwaka wa 2,000 wakati nilipoleta ng’ombe wa babangu mzazi nikiwa ninamchungia. Baadaye babangu aliuza ng’ombe wote kisha tukagawa, na leo hii ninafanya kazi hii kwa ng’ombe wangu wote,” akasema Bw Kiprotich.

Bw Kiprotich kwa sasa anamiliki ngombe sita katika kipande chake cha ekari moja na nusu cha ardhi katika kijiji hicho cha Solai.

Ingawa amepanda nyasi katika baadhi ya sehemu ya ardhi yake, bado nyasi hizo ni chache kulingana na wingi wa mifugo wake hivyo kulazimika kununua chakula cha mifugo ambacho alidai katik mahojiano kwamba ni ghali mno.

Tulipokutana naye, Bw Kiprotich alikuwa katika mkutano wa maendeleo kijijini lakini ari ya kutaka kutuelezea kuhusu biashara yake ilimfanya kuja pindi tu alipofahamishwa kwamba ukumbi wa ‘Akilimali’ ulikuwa umefika bomani mwake.

“Nina ng’ombe wanane, ndama sita na nzao mbili. Mimi huwa ninauza lita 30 kwa siku kwa sababu nyakati za asubuhi, huwa ninakamua lita 15 na jioni pia hukamua lita zengine 15,” akasema Bw Kiprotich.

Anasema kuwa lita moja inauzwa kwa Sh30 hivyo basi yeye kupata kipato cha Sh900 kwa siku. Hata hivyo mfugaji huyu alisema kuwa kiwango hicho cha bei ya maziwa bado kiko chini na hakimfaidi sana mkulima.

“Shida moja ni bei, au mahali ambapo tunauzia. Mara nyengine tunalazimika kuuza kwa reja reja kwa sababu ile gari ya KCC, huwa inakuja leo unasubiri hata siku mbili gari haifiki tena. Hiyo inamaana kwamba lazima sasa urudi tena kwa kijiji uuze kwa rejareja,” akasema Bw Kiprotich.

Aidha, aliongeza kwamba mara nyingi mojawapo ya changamoto kubwa ni bei ya chakula cha mifugo wake ambayo ni ghali sana.

“Huyu ng’ombe ninamlisha dairy meal kwa afya bora ili kuifanya iweze kutoa maziwa mengi,” akasema.

Kilo hamsini za dairy meal huuzwa kati ya Sh1,800 na Sh2,000 na mfugaji huyu alisema kuwa kila mwezi yeye hununua kilo 100 kwa mwezi. Alisema kuwa bei hiyo iko juu sana na ina gharama kuu kw mfugaji.

“Hii biashara ya ufugaji imenisaidia kusukuma maisha yangu. Imenisaidi kulipa karo za masomo kwa watoto wangu. Mara nyengine kukiwa na shida hata nyumbani, ninachukua mnyama mmoja na kuuza ili kujisaidia,” akasema Bw Kiprotich.

Kaunti yatakiwa isaidie

Anaomba serikali ya kaunti kuangalia hiyo sekta ya ufugaji na kuona ni kwa njia gani ambayo watafanya kuimarisha sekta hiyo wanaoitegemea kujikimu.

“Tunaomba serikali iweze kutoa mikopo kwa wakulima na wafugaji kama sisi. Vile vile tunaomba serikali itusaidie kwa kutupatia mbegu za ng’ombe kwa sababu kwa sasa kupandisha ng’ombe inagharimu kiasi cha Sh2,000 na hiyo ni ghali sana kwa mfugaji,” akasema Bw Kiprotich.

Anasema kuwa kitengo cha mifugo katika kaunti kinafaa pia kuweka pesa kunyunyizia dawa katika maegesho ya mifugo ili waweze kupeleka mifugo wao kuwaogesha kama njia ya kuwaepusha gharama za kuwatibu.

“Hili egesho letu la Solai halina dawa ya kuwezea kutibu maji nasi kupeleka mifugo yetu. Hiyo itatusaidia sisi kuepukana na gharama za kununua dawa za mifugo,” akasema mfugaji huyo.

Bw Kiprotich ambaye ni baba wa watoto sita anasema kuwa kwa siku yeye huuza maziwa kiasi cha Sh2,000 hivyo basi kwa mwezi, huwa anapata pesa kiasi cha Sh50,000.

“Tulikuwa na chama cha ushirika hapa Solai lakini huduma zake zimekuwa duni na mara kwa mara hakifanyi kazi kama tulivyokuwa tukitarajia. Ni kwa maana hiyo basi kuna haja ya kuhakikisha kwamba serikali inaboresha sekta hii ya maziwa ili tufaidi sisi kama wakulima na wafugaji,” akasema mfugaji huyo.

Ufugaji ajira ya maana baada ya kustaafu, Sh165,000 kila mwezi

Na MWANGI MUIRURI

WAKATI Bw Laurence Munyua alistaafu kutoka ajira ya serikali kama mwalimu katika shule za msingi mnamo 1994, hofu yake kuu ilikuwa jinsi ya kuendelea kujipa pato na asiishie kuwa masikini.

Alikuwa na uhakika kuwa kitita cha kustaafu cha Sh90, 000 alichokabidhiwa kama marupurupu ya kuaga kazi yake na pia Sh8, 500 alichokuwa apokezwe kila mwezi kama penseni yake hakikuwa na uthabiti wowote wa kumpa afueni ya maisha ya kustaafu.

“Nilijua tu ikiwa ningekosa kumakinika katika kuwekeza pesa hizo, basi nilikuwa naalika maisha ya mahangaiko na ambayo yangenituma kaburini mapema,” asema.

Katika mawazo yake ya kutumia pesa hizo kama mtaji wa kujiimarisha, alikuwa anahofia kuwa shamba lake ndogo la robo ekari halikuwa na umuhimu wowote katika maisha ya kilimo.

“Nilimwalika mtaalamu wa mipango ya mashamba na ambaye alinifahamisha kuwa shamba hilo lilikuwa kubwa zaidi. Aliniambia kuwa lilikuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya mifugo 200. Sikumwamini na ndipo nikampa kazi ya kunipangia jinsi ya kujenga manyumba ya kuhifadhi ng’ombe wa maziwa 100,” asema.

Mkazi wa kijiji cha Ndenderu katika Kaunti ya Kiambu, Bw Munyua kwa sasa anamilki ng’ombe 41 wa gredi na ambao kwa siku humpa lita 250 za maziwa.

Bw Laurence Munyua akiwa katika shamba lake Kaunti ya Kiambu ambapo kwa sasa anamiliki ng’ombe 41 wa gredi wa maziwa katika shamba lenye upana wa robo ekari. PICHA/ Mwangi Muiruri

“Kwa siku, nikiwa nimeondoa gharama zote za mradi wangu wa ufugaji, mimi huzoa Sh5, 500 kwa siku, kiasi ambacho ni Sh165, 000 kwa mwezi. Hakuna mwalimu ambaye analipwa kiasi hicho cha pesa kwa mwezi,” asema.

Anasema kuwa yeye huuza maziwa yake kwa ushirika wa wafugaji wa Kiambaa katika masaa ya asubuhi huku akiyapeleka sokoni katika mtaa wa Ndenderu jioni.

Huku uzee akisema unamsonga kwa sasa, anaamini kuwa angekosa kumakinika katika uwekezaji wake baada ya kustaafu, miaka 73 aliyo nayo kwa sasa ingekuwa imemtuma kaburini.

“Ni wengi tulistaafu pamoja lakini leo hii hawako tena. Waliokimbilia anasa za ulevi na mahaba mitaani baada ya kupkezwa pesa zao za kustaafu waliishia kuzimaliza haraka na wakapishwa katika maisha ya mauti,” asema.

Anaelezea kuwa alianza mradi huo wake wa ufugaji kwa kununua ng’ombe wawili wa gredi na ambao alizalisha kupitia teknolojia za kisasa hadi akaafikia ubora wa kiwango cha juu.

“Kuanzia 1994, nilikuwa katika harakati hizo za kuwazalisha ng’ombe hao wangu hadi mwaka wa 2006 ambapo nilikuwa nimeafikia kiwango cha juu cha ubora,” asema.

Kufuatia ueledi wake wa ufugaji na pia sifa zake kusambaa kote nchini, wafugaji wengi hujitokeza katika shamba lake ili kueleimishwa kuhusu jinsi ya kutunza ng’ombe wa maziwa.

“Kwa kila mfugaji ambaye hunikujia ili nimwelimishe, huwa namtoza ada ya Sh200 kwa siku, hali ambayo hunizidishia pato hadi Sh200, 000 kwa mwezi mmoja, ukijumuisha na lile pato la Sh165, 000 la maziwa,” asema.

Katika safari yetu katika shamba la Bw MUnyua, tulikumbana na kundi la wafugaji 500 kutoka Kaunti za Narook, Kirinyaga, Murang’a, Nyandarua na Nyeri ambao walikuwa wamemwendea ili waelimishwe jisni ya kutunza ng’ombe wa maziwa.

Bw Laurence Munyua akionyesha jinsi huhifadhi majani ya ng’ombe katika shimo la kuyakausha kama njia ya kujiwekea akiba kwa siku za kiangazi. Picha/ Mwangi Muiruri

Kando na mapato hayo, Bw Munyua huuzia wafugaji limbukeni au walio bado katika uwekezaji huo ndama wa gredi ambao bei yake huwa ni kati ya Sh50, 000 na Sh180, 000.

“Kwa mwaka, naweza kuwa nimeunda pato la Sh2 milioni kupitia mauzo hayo, hali ambayo ni ushuhuda kuwa sekta ya ufugaji wa ng’ombe ina manufaa tele na huwezi ukalia njaa au umasikini wa kustaafu. Mimi naishi maisha kama ya hawa wanasiasa ambao ni lazima waibe kutoka kwetu ili watajirike. Mimi ni bidii na jasho langu,” asema.

Bw Munyua amenunua mashine kadhaa ya kukamua ng’ombe hao wake ili kupunguza gharama za uzalishaji.

“Ukikumbatia teknolojia katika kilimo chako, utapunguza gharama za uzalishaji. Teknolojia humaanisha kuwa utaajiri vibarua wachache na kazi yako itafanyika kwa wepesi na haraka,” asema.

Katika mradi huo wake wa ng’ombe 41 wazima na ndama 28, Bw Munyua ameajiri vibarua watatu tu ambao humsaidia tu katika kufagia boma za ng’ombe hao, kuwapa chakula na hatimaye kumsaidia katika upakiaji wa mitundi ya maziwa inayoandaliwa kuwasilishwa sokoni.

Ili kukimu mahitaji ya chakula cha ng’ombe hao, Bw MUnyua amekodi shamba la ekari tatu na ambalo hupanda nyasi spesheli aina ya Kakamega I na II, na pia mahindi ambayo huvunwa kabla ya kukomaa ili kuwapa mifugo wake nyongeza ya protein muhimu za kuwafanya watoe maziwa mengi.

Anasema kuwa kinyume na hofu ya wengi kuwa kazi hii ni ngumu, yeye huamka asubuhi mwendo wa saa kumi na nusu ili kunyapara vibarua wake wakiwapa ng’ombe hao chakula na kuwakamua.

Ni katika harakati hizo ambapo masaa hayo ya asubuhi hupulizia kiingilio cha boma lake madawa ya kuua wadudu na viini hatari vya magonjwa ili kukinga shamba lake dhidi ya kuingizwa magonjwa na wageni.

Aidha, amejisajili katika mradi wa serikali wa kupewa mbegu za uzalishaji ili awe na uwezo wa kufuatilia uzalishaji katika mradi wake.

Katika uwekezaji huu wake, anasema kuwa Desemba na Januari za 2007/8 ndiyo miezi aliyokumbana na hatari kubwa ya uwekezaji wake.

“Maziwa yetu yakipokelewa katika ushirika wetu wa Kiambaa, huwa yanasafirishwa hadi Nairobi. Ni katika miezi hiyo ambapo kulizuka utata wa uchaguzi mkuu wa 2007 na ambapo magenge yalijitokeza mitaani. Kwa miezi hiyo ya ghasia, nilipoteza takriban pato la Sh300, 000,” asema.

Anasema kuwa kufikia sasa, sekta ya ufugaji inahitaji sera maalum za kukabiliana na mfumko wa bidhaa.

“Gharama za chakula kwa mifugo imepanda kwa asilimia 130 tangu mwaka wa 2012. Kwa sasa, wafugaji chipukizi wanapata shida sana wanapoingilia sekta hii ya ufugaji ng’ombe wa maziwa. Sisi tunabahatika kwa kuwa tumekuwa tukijiwekea akiba kwa miaka mingi ambayo tumekuwa katika ufugaji,” asema.

AKILIMALI: Siri ya kufaulu katika ufugaji ng’ombe wa maziwa

NA RICHARD MAOSI

NG’OMBE aina ya Jersey ni aina mojawapo ya mifugo maarufu duniani kuwahi kufugwa na wakulima ikiaminika kuwa asili yake ni zaidi ya miaka 1700 iliyopita, nchini Uingereza.

Wanafahamika kutokana na mchanganyiko wa michirizi au mabaka meupe na meusi; rangi inayowatofautisha na Friesian.

Aidha ni wakubwa kwa kimo, watulivu na hawana tabia ya kutembea sana.

Uzani wa mifugo hawa ni zaidi ya ule wa ng’ombe wa kawaida ikiwa ni kati ya kilo 500-800 endapo watalishwa vyema na kuwekwa katika mazingira yenye baridi shadidi yanayoweza kuchangia ukuaji wa lishe ya wanyama (nyasi).

Akilimali ilizuru kaunti ya Nandi kutangamana na wakulima wanaoendesha kilimo cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa almaarufu kama Jersey.

Katika eneo la Biribiriet kaunti ya Nandi, mkulima Erick Kiprotich anaendesha shughuli za ufugaji kama kazi, akisema kazi ya kujiajiri ni bora kuliko ile ya kuajiriwa kwa sababu mfanyabiashara anaweza kujivunia faida yote.

Anaona afadhali wazazi kuwafundisha watoto wao ukulima mapema, na kuwahimiza kuwa na subira ya kuchanika kwa kazi za shambani badala ya kukimbilia kazi za ofisini ambazo ni haba kupatikana siku hizi.

Erick alianza ufugaji kati ya mwaka wa 2007-2009 na ndama wawili na ilichukua muda kabla ya kustawi na kuwa mkulima wa kupigiwa mfano. Alitafuta ushauri wa kitaalam ili kuteua mifugo mwafaka wanaoenda na hali ya anga kwenye Bonde la Ufa.

Aghalabu yeye huwalisha mifugo wake ndani kwa ndani, akisema mkulima anahitajika kuwa na vyakula vya kila aina endapo anatarajia kuvuna pakubwa kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

“Huwezi kuendeleza mradi wa kufuga ng’ombe kwa ajili ya maziwa endapo hauna nyasi za kutosha ambazo ni pamoja na michicha, kunde na wakati mwingine nafaka,” akasema.

Ni jukumu la mkulima kuotesha nyasi za kutosha na ikibidi anaweza kukodisha kipande kingine cha ardhi ili aweze kuotesha malisho ya ziada kisha akayakata na kupelekea mifugo.

Anasema siri kubwa ya kufanya ufugaji huu ni kuwa ni aina ya biashara ambayo haina ushindani wowote muradi mkulima aelewe jinsi ya kutekeleza wajibu wake.

Yeye hukama mara tatu na kiwango cha maziwa hutegemea msimu ambapo majira ya kiangazi lita za maziwa hupungua, na kuongezeka sawia msimu wa mvua nyingi ambapo bei ya lita hupanda na kupungua.

Kwa siku moja Erick anaweza kupata maziwa hadi lita 200 lakini wakati wa kiangazi idadi hii ya lita hupungua hadi lita 150 hivi, lakini bado anasema ni shughuli anayojivunia kwa sababu imemwezesha kuanzisha miradi mingine kama vile ukulima wa mahindi na maharagwe.

Alitufichulia kuwa ng’ombe hawa huwa ni wapole na ameamua kuwafuga katika sehemu tulivu kwani hawafai kutishwa na kitu chochote cha kuogofya kama vile kelele za viwanda na magari.

Ni mifugo ambao huwa na wakati mrefu wa kuishi na mahitaji yao sio mengi. Aidha, wao huchukua muda mrefu kuwanyonyesha ndama wao hadi wakomae na jambo hili hufanya ndama kunenepa na wanaweza kumpatia mkulima hela nzuri anapowauza.

“Pia wanaweza kustahimili hali mbaya ya anga na hawaathiriki na maradhi ya matiti kama ng’ombe wa Friesian wanaougua mara kwa mara maradhi ya miguu na midomo,” akasema.

Alisema kuwa mifugo wa Jersey huchukua muda mfupi kushika ujauzito na baadaye hujifungua kabla ya miezi kumi kinyume na ng’ombe wa kienyeji, wanaoweza kuchukua hadi miaka mitatu kabla ya kushika ujauzito.

Desturi hii imetoa awamu kwa mifugo wake kuzaana haraka baada ya muda mfupi na kufikisha zaidi ya ng’ombe 10 anaomiliki, wanaompatia maziwa, nyama na mbolea.

Anasema pia kuna faida nyingi ambazo mkulima anaweza kupata kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

“Mkulima anaweza kutengeneza hela pale anapouza samadi au anapowauza ndama wake kwa wakulima wanaofanyia majaribio ufugaji kwa ajili ya maziwa,” aliongezea.

Anasema ni lazima mkulima aelewa kuwa uzalishaji wa maziwa katika ng’ombe unategemea umbile la mifugo yako, ng’ombe wazito au wakubwa sana kimwili sana sio bora kwa kukama ila wanafaa kufugwa kwa sababu ya nyama pekee.

Mbali na ng’ombe kuzalisha maziwa anahitaji kuangaliwa kwa ukaribu, alieleza kuwa ng’ombe wa Jersey ambao ni chotara wana uwezo wa kufanya vizuri katika mazingira yoyote hata kama ni magumu.

“Kwa sababu mifugo wa asili si rahisi kupatikana siku hizi, ni vizuri mkulima kuwatafuta ng’ombe wa kisasa na kuwaboresha kutokana na upandikizaji na dume ili kuzalisha mifugo wanaoweza kustahimili uhaba wa malisho,” akasema.

Anasema kama utawafuga wanyama katika sehemu ndogo isiyokuwa na nafasi ya kutosha, basi utakuwa umewaweka katika hali ya usumbufu, ni vyema kuandaa shimo maalum la kuhifadhi samadi kabla ya kuzisafirisha katika shamba.

Kwa jumla, Kiprotich anasema ng’ombe wa maziwa wanahitaji kiwango kikubwa cha lishe na cha mara kwa mara ukilinganisha na mifugo wanaofugwa kwa ajili ya nyama.

Kwa sababu yeye hufuga mifugo wake kwa ndani (zero grazing) anajaribu kuhakikisha kuwa mazingira yao ni safi na pana ili kuwapatia uhuru wa kutembea.

Mapipa ya kuhifadhia maji ameyaweka karibu na vyanzo vya maji safi. Kila ng’ombe anahitaji kunywa lita 5-8 ya maji kila siku ambazo ni ndoo tatu hadi tano hivi.

Anasema ni vizuri kuwa na paa la kuwalinda mifugo dhidi ya hali mbaya ya hewa kama vile jua kali na upepo unaovuma bila mwelekeo maalum.

UFISADI: Kaunti yanunua ng’ombe kwa Sh3.7 milioni!

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI ya Kaunti ya Kisumu ilitumia Sh3.7 milioni kununua ng’ombe mmoja wa maziwa, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Edward Ouko inaonyesha.

Ripoti hiyo ya mwaka wa fedha wa 2017/2018, inaeleza kuwa pesa hizo zililipwa kwa mfanyabiashara mmoja, ambaye kulingana na rekodi alipasa kuuzia kaunti hiyo ng’ombe 27 wa maziwa aina ya “Ayrshire”, lakini uchunguzi ukabainisha ni ng’ombe mmoja pekee aliyewasilishwa.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, mbali na Kisumu, kaunti nyingi zilitumia mamilioni ya pesa kulipia bidhaa na huduma ambazo hazikutolewa.

Kaunti hizo ziliripoti kutumia fedha kwa ununuzi wa bidhaa na huduma tofauti, lakini Mkaguzi Mkuu alipochunguza ilipatikana hapakuwa na huduma ama bidhaa zilizotolewa.

Kwa jumla, Bw Ouko ametilia doa karibu kila kaunti kwa masuala kama vile kuajiri idadi kubwa ya wafanyakazi kupita kiasi, kutotumia mfumo bora wa kuthibitisha uhalali wa matumizi ya fedha, kutokuwepo usawa wa kijamii katika ajira na kutokamilishwa kwa miradi ya maendeleo.

KISUMU

Ripoti hiyo inasema kuwa hapakuwa na stakabadhi zozote za kuthibitisha kaunti hiyo inayoongozwa na Prof Anyang’ Nyong’o ilipokea ng’ombe wengine 26 kama ilivyodai.

Ripoti hiyo imetilia shaka pia Sh9.8 milioni, ambazo zilidaiwa kulipwa kwa kampuni tofauti kuuzia kaunti hiyo mbegu na mbolea. Pia kampuni hizo zilionekana kumilikiwa na mtu mmoja.

NAIROBI

Mpango wa kurembesha jiji la Nairobi ulimeza Sh18.8 milioni kwa malipo ya vibarua pekee, ingawa hapakuwa na stakabadhi zozote za kuthibitisha uhalali wa malipo haya.

Afisi Gavana Mike Sonko na naibu wake (ambaye hajakuwepo kwa zaidi ya mwaka mmoja) ilitumia Sh14.4 milioni na kusema maelezo kuhusu matumizi hayo ni siri, kwa sababu fedha hizo zilitumiwa kwa masuala ya kiusalama.

“Sheria inaruhusu serikali kuu pekee kutumia fedha kwa masuala ya kisiri. Kwa hivyo serikali ya kaunti ilikiuka sheria,” akasema Bw Ouko.

MOMBASA

Kaunti ya Mombasa haijawasilisha Sh3.5 bilioni kwa mashirika mbalimbali zinazokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi kugharamia malipo kama vile ushuru kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), malipo ya uzeeni (NSSF) na ada za Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF).

GARISSA

Kaunti ya Garissa ilimlipa mwanakandarasi Sh3.9 milioni kurembesha mji lakini hakutekeleza majukumu yake. Kaunti hii ilidai pia kutumia Sh6.6 milioni kulipia huduma za hotelini ambazo hazingeweza kuthibitishwa.

EMBU

Kaunti ya Embu ina Sh358,563,651 kwenye akaunti 32 katika benki tofauti za humu nchini. Bw Ouko alisema akaunti hizi zilifunguliwa kinyume na sheria za usimamizi wa fedha za umma katika kaunti na hivyo basi afisi ya gavana ilikiuka sheria.

BARINGO

Serikali ya Kaunti ya Baringo ilinunua dawa za matibabu kwa Sh13.5 milioni ilhali kulikuwa na muuzaji ambaye aliwasilisha ombi kuuzia kaunti dawa hizo kwa Sh6.8 milioni pekee.

MERU

Mfanyabiashara alilipwa jumla ya Sh1.8 milioni kuuzia Kaunti ya Meru mapipa 600 ya plastiki yenye ukubwa wa lita 2,000 kila moja. Mhasibu Mkuu alitilia shaka utumizi huu wa fedha kwani kulingana naye, mapipa hayo yalistahili kugharimu Sh1,000 kila moja na wala si Sh3,000 kila moja. Kwa msingi huu, serikali ya kaunti ingetumia Sh600,000 pekee kwa jumla.

KIAMBU

Kaunti ya Kiambu ilimumunya karibu Sh10 milioni kwa ununuzi wa miche ya parachichi bila kufuata kanuni za kisheria.

Ripoti inasema kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Ferdinand Waititu ilitumia Sh9.97 milioni kununua miche hiyo aina ya ‘Hass’ kwa njia isiyoeleweka.

“Zabuni ya kununua miche hiyo ilipeanwa kwa kampuni mbili pekee. Hapakuwa na maelezo ya kuridhisha kuhusu kwa nini hatua hii isiyo ya kawaida ilichukuliwa,” akasema Bw Ouko kwenye ripoti yake.

NYERI

Serikali ya Kaunti ya Nyeri imekosolewa ilipopatikana na dawa zilizogharimu Sh15.2 milioni ambazo zilikuwa zimeharibika katika hospitali 31.

“Hapakuwa na maelezo kuhusu kwa nini dawa zilikuwa zimenunuliwa kwa wingi kupita kiasi, hali iliyosababisha ziharibike na hivyo kuharibu pesa za umma,” ripoti ikaeleza.

KITUI

Mpango wa kuwezesha wakazi kupanda pojo almaarufu kama ‘Ndengu Revolution’ uliogharimu Sh49.6 umetiliwa shaka.

Afisi ya Gavana Charity Ngilu ilikuwa imesema fedha hizo zilitumiwa kununua mbegu, lakini Mhasibu Mkuu kwenye ripoti yake anaeleza haiwezekani kutambua kama mpango huo umenufaisha wakazi.

Wakati huo huo, mbegu nyingine zilikuwa zikipeanwa na shirika la Kenya Red Cross kwa wakulima na hivyo basi ikawa vigumu kutambua kiwango halisi ambacho kilitoka kwa serikali ya kaunti.

Mama ashinda mashindano bila kumpa fahali wake bangi

Na FAUSTINE NGILA 

Mama Peninah Otuma kutoka kijiji cha Ematetye amefunguka kuhusu vita vya ng’ombe akisema yeye hampi fahali wake chochote kabla ya mashindano.

Akifurahia ng’ombe wake kushinda vita vya ng’ombe katika Shule ya Upili ya Mwangaza katika kaunti ya Kakamega, Bi Otuma anasema kwamba yeye humlisha ng’ombe wake chakula cha kawaida tu kama nyasi na wala si jinsi baadhi ya washindanaji wanavyowapa ng’ombe wao bangi kuwafanya wawe na hasira kali ya kupigana.

Anaongeza kwamba yeye humuombea ng’ombe wake na kumuongelesha kabla ya vita hivyo. Bali na vita vya fahali, mashindano ya kila mwaka ya Toto Cup Cleophas Shimanyula yalijumuisha fani zingine kama kuvutana kwa kamba, soka ya wanaume, soka ya wanawake, voliboli ya wanawake, mpira wa pete na uendeshaji wa baiskeli.

Makala ya mwaka 2018 yalihudhuriwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na Mbunge wa Lurambi, Titus Khamala, miongoni mwa viongozi wengine wa eneo la Lurambi.

AKILIMALI: Jinsi ya kufanikisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa

Na PETER CHANGTOEK

ILI kufanikiwa katika kilimo cha ufugaji wa ng’ombe wanaofugwa kwa ajili ya maziwa, ni jambo aula kufahamu fika kwamba, lishe bora ni muhimu mno.

Kufanikiwa kuzaa kwa ng’ombe kwa njia iliyo salama ni mojawapo ya mambo muhimu katika kilimo cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Kuzaa kwa njia salama kwa ng’ombe kunachangia kuzalishwa kwa maziwa kwa wingi. Hili litawezekana tu, iwapo ng’ombe aliyezaa ndama atatunzwa vyema, kabla, wakati wa kuzaa, na baada ya kuzaa,’’ asema Wytze Heida, mtaalamu wa masuala ya mifugo ambaye pia ni mkurugenzi wa shirika la SNV.

Mtaalamu huyo anasema kuwa, ng’ombe anapozaa, hupitia mabadiliko za kila aina, yakiwemo mabadiliko ya mwilini, kisaikolojia, na kadhalika, na hivyo basi kiwango cha lishe ambazo anafaa kulishwa vilevile, kinafaa kubadilishwa, kuambatana na mahitaji ya ng’ombe.

Bw Heida anafichua kuwa, kwa wakati huo, ng’ombe aliyezaa anastahili kulishwa kwa lishe zinazompa nguvu mwilini, ambazo pia zitamfanya kuyazalisha maziwa kwa wingi.

Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Minnesota, nao wanasema kwamba, zipo awamu tatu ambazo zinaweza kutumika kuwalisha ng’ombe wa maziwa, ili kuhakikisha kuwa wanayazalisha maziwa kwa wingi, na kuwa na afya.

Awamu ya kwanza ni wakati ng’ombe anapozaa hadi siku ya sabini baada ya kuzaa. Kwa wakati huo, maziwa huongezeka upesi mno, hususan katika wiki ya sita hadi ya nane, baada ya kuzaa. Nafaka wanazolishwa ng’ombe wa maziwa kwa muda huo, zinafaa kuongezwaongezwa kidogo kidogo kila siku. Hata hivyo, mkulima ajihadhari asije akawalisha kwa nafaka nyingi kupindukia, kwa sababu zitaathiri afya yao.

Pia, wataalamu hao wanasema kwamba, nafaka nyingi zinazokithiri kiasi kinachofaa, zitaathiri kiwango cha mafuta yaliyoko kwa maziwa. Katika awamu iyo hiyo, lishe zenye nyuzinyuzi zitumike kwa kiasi fulani, kuwalisha.

Isitoshe, lishe zenye protini zitumike kuwalisha ng’ombe hao. Kiwango cha protini chategemea mambo kadha wa kadha, mathalan mbinu za kulisha, uwezo wa uzalishaji wa maziwa kwa ng’ombe, miongoni mwa mambo mengineyo.

Hali kadhalika, mkulima anafaa kuwalisha kwa lishe bora ambazo ni za kiwango cha juu. Vilevile, lishe ziwe na virutubisho vyote vinavyotakikana. Aidha, mkulima ahakikishe kuwa ng’ombe wake hawaathiriwi na usumbufu wa akili, maadamu jambo hilo huathiri kiwango cha maziwa yanayozalishwa.

Awamu ya pili ni kuanzia siku ya sabini hadi siku ya mia moja na arobaini. Huo ni wakati ambapo maziwa yanaanza kupungua. Hivyo basi, ni jambo aula kutumia mbinu zote kuzuia hali hiyo ya kupungua kwa maziwa.

Kwa wakati huo, ng’ombe hawafai kuupunguza uzani, bali wanafaa kuushikilia uzani walionao, au kuuongeza. Kwa hivyo, walishwe kwa lishe zifaazo. Hata hivyo, zisizidi kiasi kinachofaa. Katika awamu hiyo hiyo, ng’ombe hawafai kuwa na mambo yanayowatatiza akili.

Katika awamu ya tatu ya ulishaji wa ng’ombe, ambayo huanzia siku ya 140 hadi siku ya 305, kiwango cha maziwa huwa kinapungua, na ng’ombe anafaa kuwa na mimba.

Ajabu ya ng’ombe kuua simba zizini

Na MWANDISHI WETU

SIMBA ambaye amekuwa akiua mifugo wa wenyeji karibu na Mbunga ya Kitaifa ya Meru aliuawa na ng’ombe Alhamisi usiku katika tukio lisilo la kawaida.

Simba huyo alifariki katika kijiji cha Luciuti, Amwathi, kaunti ndogo ya Igembe Kaskazini, alipojaribu kumla ng’ombe mwingine katika boma la mjane.

Diwani wa Amwathi Bw John M’Ngai, ambaye ng’ombe wake wawili waliangamizwa na simba huyo wiki jana, alisema mnyama huyo wa mwituni alifariki baada ya kunyongwa na kamba ya ng’ombe aliyekuwa akijaribu kumla.

Mlinzi wa Shirika la Huduma za Wanyama Pori (KWS), Bw Nathan Gatundu, alisema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kilichomuua simba huyo.

Inadaiwa njaa na mahangaiko ndizo zilimuua simba huyo.

Bw M’Ngai alisema simba huyo ambaye amekuwa akizurura vijijini usiku baada ya kutoroka mbungani, alifariki baada ya kunaswa katika mtego huku ng’ombe akifanikiwa kujiokoa kutoka kwa kucha zake.

“Simba aliingia katika boma la mjane huyo usiku wa manane na kufululiza hadi zizi la ng’ombe. Lakini alipokuwa aking’ang’ana kumla ng’ombe, alinyongwa na kamba iliyokuwa imefungwa shingoni mwa windo lake. Nadhani huu ni muujiza kwa sababu mjane huyo maskini alikuwa tu na ng’ombe huyo,” akasema.

Diwani aliongeza kuwa simba huyo ambaye amewaua mifugo kadha katika eneo hilo alivamia boma lake Ijumaa na Jumapili wiki jana.

Alieleza: “Aliua ng’ombe mmoja Ijumaa na mwingine Jumapili. Amekuwa akijificha vichakani wakati wa mchana ili kukwepa walinzi wa KWS na wakazi ambao wamekuwa wakimsaka.”

Bw Gatundu alisema uchunguzi wa awali ulibaini simba alikuwa amekula kitu kama ngozi ya mbuzi, lakini sampuli zaidi zimepelekwa kufanyiwa uchunguzi kubaini kiini.

Tukio hilo lisilo la kawaida liliibua msisimko mkubwa katika kijiji hicho ambapo wakazi hulalamikia visa vya uvamizi vya mara kwa mara kutoka kwa wanyapori wanaotoroka mbugani.

Niligonga ng’ombe wala si kuua mwanamke ajalini – Dereva mlevi

Na STELLA CHERONO

Iwapo wasingepata nambari za usajiji za gari karibu na mwili wake, polisi wangechukulia mauaji ya Maureen Wambui Gachagua kama mengine yanayotekelezwa jijini na kukosa matumaini ya kuwapata washukiwa.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu wa chuo kikuu cha Kenyatta, aligongwa na dereva mlevi kisha akaendesha gari lake kwa kilomita tatu mwili ukiwa juu ya gari hilo na kuutupa mtaani South C, Nairobi.

Maureen, 22, alikuwa akitoka kuhudhuria karamu akiwa na rafiki yake Dennis Mburu katika NextGen Mall kwenye barabara ya kuelekea Mombasa.

“Tulitoka NextGen Mall mwendo wa saa kumi Jumapili usiku. Nilifaulu kuvuka mtaro nje ya jumba hilo lakini rafiki yangu aliamua kufuata njia ya kufika barabarani. Nilimsubiri ili tuvuke barabara pamoja lakini alipofika kwenye lami, alianza kuvuka na nikaamua kumfuata kwa sababu barabara ilikuwa shwari. Kabla ya kufika upande wa pili, niliona gari likija kwa kasi na kumgonga,” alisema Dennis.

Alisema mwili wake ulitua juu ya paa la gari na akakimbia akitarajia ungeanguka ili ampeleke hospitalini.

“Lakini gari halikusimama, lilifululiza mwendo nikilifuata mbio hadi nikashindwa kulifikia. Nilijaribu kusimamisha magari mengine kwenye barabara ya Mombasa ili nilifuate lakini hayakusimama,” alisema.

Baada ya nusu saa aliacha kutafuta mwili na kurudi NextGen Mall, ambapo aliomba dereva wa teksi kumsaidia kumtafuta.

“Tulienda katika hospitali za Nairobi West, Nairobi South, Langata, Mater na Kenyatta lakini hatukumpata,” alisema.

Rafiki mmoja aliyempigia simu alimweleza kuna hospitali inayoitwa Mariakani. “Nilienda katika hospitali hiyo na nilipokuwa eneo la kupokea wageni nilisikia mwanamke akisema kuna mwili uliotupwa eneo hilo na mtu asiyejulikana,” alisema Dennis.

Alisema mwili ulikuwa katika hali mbaya bila miguu. Kando ya mwili kulikuwa na nambari za usajili za gari KCN 285B.

Polisi walipofika na umati kukusanyika mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, mtu alichukua nambari hizo na kutoweka.

Afisa anayechunguza ajali hiyo alisema Sajini Dismus Gitenge Motongwa wa idara ya magereza alipotupa mwili alielekea nyumba za makazi za askari wa gereza la wanawake la Langata, akaegesha gari, akang’oa nambari za nyuma za usajili na kuchukua gari tofauti.

Kisha alienda kituo cha polisi cha Langata na kuripoti kwamba aligonga ng’ombe kwenye barabara ya Langata.

Wezi wa ng’ombe wauawa na umma wakiiba nyati

Na GEOFFREY ANENE

WEZI wawili sugu wa ng’ombe walipigwa na umma hadi kufa kwa madai ya kujaribu kuiba nyati katika kijiji cha Bankatti, wilaya ya Godda nchini India, Juni 13, 2018.

Gazeti la Indian Express limeripoti kwamba polisi kutoka kituo cha Deodand walitia nguvuni watu wanne waliohusika na mauaji hayo na pia watu wawili waliodaiwa kuiba nyati.

Ripoti ya polisi kutoka kituo hicho inasema kwamba wafu walikuwa na historia ndefu ya kuiba ng’ombe.Kulingana na polisi, tukio hilo lilifanyika Juni 13, 2018 katika kijiji cha Bankatti kwenye mpaka wa Deodand na Sunder Pahari wilayani Godda.

Inasemekana ‘wezi hao wa nyati’ walipatikana wakitoweka na wanyama hao kutoka kijiji kimoja. Uchunguzi zaidi unafanyiwa waathiriwa hao waliotambuliwa kama Mumtaza Ansari kutoka kijiji cha Taljhari na Charku Ansari kutoka kijiji cha Banjhi karibu na kituo cha polisi cha Poraiyahat.

Uwanja wa ndege sasa wageuzwa malisho ya ng’ombe

Na OSCAR KAKAI

UWANJA wa ndege wa Kishaunet ambao umetelekezwa kwa muda mrefu katika Kaunti ya Pokot Magharibi sasa umegeuzwa kuwa malisho ya mifugo na njia za mkato za wakazi kupitia.

Uwanja huo ambao uko kilomita saba kutoka mji wa Makutano, Kapenguria ni baadhi ya miradi hewa ya serikali katika kaunti hiyo.

Mradi huo ambao ulijengwa na wakoloni miaka ya 1950 ulikuwa ukitumika kama lango la kuelekea Kaskazini mwa Kenya. Ng’ombe na punda ndio ‘abiria’ kwa huonekana wakizurura ndani ya uwanja huo huku wakazi na waendesha bodaboda wakiufanya njia ya mkato kuelekea mijini.

Wakazi wanasema ni aibu kutelekezwa kwa uwanja huo wa ndege ambao una uwezo mkubwa kuwa kitega uchumi kwao. Alipoulizwa ikiwa kuna fedha ambazo serikali imetengea kukarabati uwanja huo, Kamishna wa kaunti hiyo Bw Apollo Okello alisema kuwa hawajapokea fedha zozote kwa ukarabati wa uwanja huo. Bw Okello alisema kuwa wameomba fedha ili waweze kukarabati uwanja huo lakini hadi wa leo hawajapokea.

Gavana wa kaunti hiyo Prof John Lonyangapuo alisema kuwa ukarabati wa uwanja huo uko kwenye manifesto yake na atafanya mazungumzo na Halmashauri ya Viwanja vya Ndege nchini ili waweze kununua shamba lingine kupanua uwanja huo.

“Tuko na ardhi ambayo imetengwa lakini haitoshi,” alisema Gavana Lonyangapuo.

Wakazi walitoa ekari kumi za ardhi kwa ujenzi wa uwanja huo wakiwa na matumaini makuu ya kunufaika lakini ndoto yao bado haijatimia

“Watu mashuhuri hutumia uwanja huu wa ndege. Tungetamani kuona ndege kubwa zikishuka kwenye uwanja huu lakini umesaulika,” alisema mkazi, Daniel Siree.

Mkazi mwingine Meshack Limasya alisema, “Ikiwa serikali itaamua kukarabati uwanja huu itainua uchumi wa kaunti. Maisha yetu yatabadilika kabisa.Hatuelewi mbona uwanja huu umetelekezwa ilihali tunahitaji maendeleo.”

“Tunaishi maisha ya uchochole sababu hatuna kazi ilhali tungeajiriwa kwenye uwanja huu,”asema Bw Limasya.

Genge laiba ng’ombe 8 na kuwachinja kwa mochari

NA PETER MBURU

POLISI mjini Nakuru wanawawinda genge la majambazi ambalo usiku wa kuamkia Jumanne liliiba ng’ombe wanane kutoka shamba la mkulima mmoja na kuwachinja karibu na mochari.

Wezi hao wanasemekana kuvamia shamba la Bi Damaris Njeri, mtaa wa East Gate, Pipeline mwendo wa saa kumi usiku wakiwa wamejihami na mapanga, kabla ya kuondoka na mifugo hao aina ya Friesian.

Sehemu za ngombe zilizosalia kama idhibati baada ya wezi kuiba na kuwachinja kando ya chumba cha kuhifadhi maiti cha Umash, Nakuru Juni 12, 2018. Picha/ Peter Mburu

“Nilipigiwa simu saa kumi alfajiri na mfanyakazi wangu wa shambani na akanieleza kuwa wezi wamewavamia na wakaiba ngombe wote wa maziwa. Baadaye nilimpigia chifu wa eneo hilo ambaye aliahidi kufahamisha polisi,” akasema Bi Njeri.

Mwanamke huyo alieleza Taifa Leo kuwa baada ya saa mbili alifika kwenye kituo cha polisi cha Mwariki kuripoti, ijapokuwa mkuu wa polisi kituo hicho alidai ‘kuwekewa mafuta’ kwenye gari la kazi kabla ya kwenda kutafuta mifugo hao.

Kichwa cha mmoja wa ngo’mbe walioibwa na kuchinjwa karibu na mochari Nakuru. Picha/ Peter Mburu

“Nilipopiga ripoti mwendo wa saa kumi na mbili, Bw OCS alinitaka kutoa Sh1,000 akisema ni za kuweka gari la polisi mafuta, ilinibidi nitoe kwani nilihitaji msaada wao,” akasema mwanamke huyo.

Mkulima huyo alieleza ghadhabu yake na tabia ya polisi hao, ambao hawawezi kuwasaidia wananchi kabla ya kupewa rushwa.

“Si vyema hata kidogo kuwa ili kuhudumiwa na polisi wananchi wanahitajika kuwahonga kwanza. Huenda hii ndiyo sababu visa vya wizi vimezidi katika mtaa huu,” Bi Njeri akasema.

Kichwa na ngozi zilizosalia baada ya wezi kubeba nyama. Picha/ Peter Mburu

Naibu wa OCPD Nakuru Bw Daniel Kitavi alisema hakuna takwa lolote katika huduma za polisi linalohitaji wananchi kulipia gharama za kusaidiwa kuweka ulinzi na polisi.

“Siku hizi, magari ya polisi yanawekwa mafuta kwa kutumia kadi wala si pesa taslimu, ikiwa afisa huyo aliitisha pesa, hicho ni kinyume cha maadili na sharia na atachukuliwa hatua za kisheria,” akasema Bw Kitavi.

Kinaya cha yote kilikuwa, baada ya ‘kupokea pesa za mafuta’ polisi hawakufanikiwa kuwapata mifugo hao kwani walipata baadhji ya sehemu za mizoga yao, baada ya kuchinjwa na wezi kuondoka na nyama.

Mguu na ngozi zilizopatikana katika eneo ambapo ng’ombe walichinjwa. Picha/ Peter Mburu

Wezi hao waliwachinjia ngombe wa mkulima huyo kando ya chumba cha kuhifadhi maiti cha Umash, lakini hawakubeba vichwa, kwato na ngozi.

“Ngombe wote walikuwa wamechinjwa, tulipata vichwa, ngozi na kwato pekee lakini nyama zilikuwa zimebebwa,” akasema Bi Njeri.

Hadi wakati wa kuandika taarifa hii, hakuna mwizi aliyekuwa amekamatwa na polisi.

VITUKO UGHAIBUNI: Mwislamu aliyeua ng’ombe auawa na umati

Na AFP na VALENTINE OBARA

NEW DELHI, INDIA

MWANAMUME Mwislamu aliyekashifiwa kwa kuua ng’ombe alipigwa hadi kufariki na umati katika eneo la kati mwa India, polisi walisema Jumapili.

Tukio hilo limeongeza idadi ya mauaji yanayotendwa na halaiki dhidi ya watu wanaochinja wanyama ambao huabudiwa na Wahindi.

Siraj Khan ambaye alikuwa mshonaji nguo mwenye umri wa miaka 45, alishambuliwa katika Wilaya ya Satna iliyo Jimbo la Madhya Pradesh mapema Ijumaa iliyopita, akafariki papo hapo, kwa mujibu wa afisa wa polisi wa eneo hilo Arvind Tiwari.

Rafiki yake, Shakeel Maqbool, ambaye pia alishambuliwa, alilazwa hospitalini akiwa katika hali mahututi.

Polisi karibu 400 walipelekwa eneo hilo Jumamosi kuendeleza uchunguzi, kulingana na gazeti la Press Trust of India.

“Tumekamata watu wane, na wameekwa kizuizini. Tunachunguza kilichosababisha shambulio hilo,” akasema Tiwari.

Aliongeza kuwa polisi walipata nyama na mzoga wa beberu katika eneo la mkasa lakini hakutoa maelezi zaidi kwani uchunguzi ungali uanendelea.

Wahindi huchukulia ng’ombe kama viumbe vitakatifu na ni hatia kuchinja au kupatikana au kula nyama ya ng’ombe katika majimbo mengi nchini humo.

Uchinjaji wa ng’ombe katika Jimbo la Madhya Pradesh hupokea adhabu ya kifungo cha miaka isiyozidi saba gerezani lakini katika majimbo mengi India adhabu ya kisheria huwa ni kifungo cha maisha gerezani.

Polo agutusha kijiji kuficha ng’ombe kwa kimada

Na TOBBIE WEKESA

EKERENYO, NYAMIRA

KALAMENI mmoja aliwashangaza wenyeji wa hapa alipoamua kuwahamisha ng’ombe wake hadi kwa mpango wake wa kando.

Inasemekana katika tukio hilo lililowaacha wengi vinywa wazi, polo alichukua hatua hiyo akidai kwamba mke wake haaminiki kabisa.

Duru zinasema kalameni alianza kumshuku mkewe mashemeji wake walipoanza kwenda kwake bila kumfahamisha.

“Tangu ninunue hawa ng’ombe, ndugu zako wamekuwa wakija hapa kila wakati. Mbona huniambii wakija na sababu yao ya kuja,” polo alimkaripia mkewe.

Kulingana na mdokezi, sababu aliyoitoa mkewe haikumridhisha polo. “Nahofia sana ng’ombe wangu. Sioni hawa watu wako wakiwa na nia njema,” polo alidai huku akielekea zizini na kuwafungulia ng’ombe.

“Naona leo umewafungulia mifugo mapema sana. Kwani unawepeleka malishoni umbali gani na hii mvua?” mkewe alimuuliza kalameni. Inasemekana polo alimkanya mkewe kuingilia mambo ayafanyayo.

“Achana na mali yangu kabisa. Ikiwa ni malishoni nawapeleka haikuhusu. Ni mimi niliwanunua,” kalameni alimkaripia mkewe.

Maneno ya polo yalimshtua kipusa. “Nahofia sana ng’ombe wangu kuchukuliwa na watu wa kwenu. Heri niwafiche mahali salama,” polo alimueleza mkewe.

Alipotaka kujua mahali salama alikodai kuwapeleka ng’ombe, polo alimueleza mkewe kwamba alikuwa akiwapeleka kwa mwenzake.

“Hii mali yangu naipeleka kwa mwanamke mwenzako ambaye hana njama na watu wao kama wewe. Acha maswali mengi,” kalameni alimueleza mkewe huku akienda.

Duru zinasema baada ya kuwafungulia ng’ombe wake, polo alianza safari kuelekea kwa mpango wa kando katika kijiji jirani kuwaficha humo.

…WAZO BONZO….

Mafunzo muhimu kuhusu ufugaji wa kuku na ng’ombe

Na FAUSTINE NGILA

FEBRUARI 24, 2018, Akilimali ilijumuika na jarida la kilimo kwa lugha ya Kiingereza Seeds of Gold katika kituo cha utafiti cha Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo nchini (Kalro), kilomita moja kutoka mjini Kitale, kaunti ya Trans Nzoia.

Mamia ya wakulima kutoka kaunti za Nairobi, Nyeri, Nakuru, Kakamega, Uasin Gishu, Bungoma, Kisumu na Trans Nzoia walimiminika katika kituo hicho, kila mmoja akitazamia kuelimishwa kuhusu mbinu bora za kilimo na jinsi ya kukabiliana na visiki vya ufugaji na ukuzaji mimea.

Wataalamu wa kilimo, wavumbuzi, kampuni mbalimbali na wapenzi wa kilimo walihudhuria hafla hiyo inayoandaliwa baada ya kila miezi miwili, kwa lengo moja la kuimarisha kilimo nchini.

Kipindi cha maswali na majibu kilianza kuhusu ufugaji wa ndege wa nyumbani, ambapo zaidi ya wafugaji kumi waliuliza maswali mbalimbali ambayo yamekuwa kitendawili kwao kwa muda mrefu.

Mkulima mmoja wa kundi la wafugaji la Shamba la Wanyama kutoka kaunti ya Kakamega aliuliza sababu ya kuku wake wa kienyeji kutoangua asilimia 100 ya mayai wanayolalia, vifaranga kufa ovyoovyo na jinsi ya kutokomeza mazoea ya kuku kula mayai.

Katika jibu lake, mkurugenzi wa kituo cha Kalro cha Kakamega Dkt Luvodicus Okitoi alianza kwa kuwauliza wafugaji mbinu zao za kufuga kuku.

“Ni mayai mangapi kuku wa kawaida anaweza kutaga kabla ya kuyalalia?” aliwauliza. Wakulima walitoa idadi iliyo kati ya 15 na 25, na kukubaliana 18 kama idadi ya wastani.

“Kuku yeyote wa kienyeji anayetaga zaidi  mayai 20 hawezi kuyalalia na yaangue yote. Idadi ya wastani ni mayai 14 na idadi ya vifaranga watakaoanguliwa itakuwa 10 na watakaofikisha umri wa kukomaa ni sita,” wakulima walikubaliana na kauli hiyo.

Mtaalamu huyo alielezea kuwa bei ya kuku mmoja mjini Bungoma ni Sh500, na ikizingatiwa kuwa kuku hawa hutaga mayai mara tatu kwa mwaka, mkulima hupata Sh9,000 kwa mwaka.

Wafugaji wa kuku waliuliza kila aina ya maswali kwenye kliniki ya Seeds of Gold iliyofanyika katika kituo cha Kalro, Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kuongeza mapato
Akielezea jinsi ya kuongeza kiwango hiki cha pesa kutoka kwa kuku mmoja, alisema, “Iwapo kuku atalishwa vizuri, vifo vitapungua. Badala ya kumpa kuku mayai 14, mpe mayai 10 na ataangua yote na vifaranga wote wafikie umri wa kukomaa.”

Mkulima mwingine aliuliza kuhusu kuku kufikia kikomo cha kutaga mayai.

“Unaweza kupyesha uwezo wa kuku kutaga mayai. Mtumbukize kuku ndani ya maji baridi. Baada ya hapo, homoni zake zitabadilika na kuanza kutaga mayai tena.

Kwa kufanya hivi, kuku wako anaweza kutaga mayai mara kumi kwa mwaka, ikilinganishwa na mara tatu bila mbinu hii,” akajibu.

Kwa hilo, wakulima waliduwazwa na mbinu hiyo, na baada ya kupiga hesabu za haraka, waligundua kuwa badala ya Sh9,000 wanazopata kila mwaka, wanaweza kuuza kuku kumi mara kumi kwa mwaka na kutia mfukoni Sh50,000.

Mfugaji auliza swali kwenye kliniki ya Seeds of Gold iliyofanyika katika kituo cha Kalro, Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kuku mlezi
Ili kudumisha ubora wa ndege wanaofuga, wakulima walishauriwa kuvalia njuga ufugaji wa kuteua kuku mmoja ambaye atawalea vifaranga wote.

“Chagua kuku wako bora kwa kulea vifaranga na ataweza kukulelea vifaranga wote 100 walioangaliwa na kuku kumi tofauti,” akashauri mtaalamu huyo.

“Je, hili litawezekanaje?” akauliza mfugaji mmoja aliyeshangazwa na mbinu hiyo.

Daktari huyo alielezea kuwa ingawa kila kuku anajua vifaranga wake kwa harufu, vifaranga wa kuku wengine wanaweza kuletwa kwa kuku mlezi usiku kwa kutumia mikono safi.

Kufikia asubuhi, harufu hiyo itakuwa imeyeyuka na kuku mlezi atawakubali vifaranga wote. Akikataa, basi ujue ulikuwa na marashi kwa mikono yako.

Francis Mathai aonyesha nduma aina ya Dryland aliyopendekezewa na maafisa wa Kalro Mei 2017. Alikuwa amehudhuria kliniki ya mafunzo ya kilimo mjini Kitale Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kugeuza kuku kuwa kiangulio
Mtafiti huyo pia alielezea wakulima jinsi ya kugeuza kuku wao kuwa mashine ya kuangua vifaranga. Aliwashauri kuteua kuku aliye na rekodi nzuri ya kuangua mayai yote.

“Mpe kuku huyo mayai 10 baada ya kila siku 21. Mpe mayai yaliyotagwa na kuku wengine alalie katika siku ya 22. Baada ya kila siku 21, vifaranga 10 walioanguliwa watakuwa na afya njema mpaka waishi mpaka ukomavu. Hivyo, kuku huyu anahitaji chakula na maji ya kutosha.”

Kwa mwaka mmoja, utaangua vifaranga mara 17 watakaolelewa na kuku walezi, na hivyo mfugaji atapata Sh85,000 akiwa mashinani.

Kuhusu utata wa ufugaji wa kuku wa umri tofauti na kuwatibu, Dkt Okoiti alianza kwa kuwakumbusha wafugaji kuwa yai la kwanza kutagwa haliwezi kuangua kuwa kifaranga.

“Pasua yai hilo na ujaze changarawe na ufunike ganda lake. Yai hili feki utaliweka kwa kiota baada ya kuchukua yai lililotagwa. Kuku hupata motisha wa kutaga akiona yai kiotani.”

Aliwataka wafugaji kutia alama mayai yote kuhusu siku yaliyotagwa. Baada ya kati ya siku7-10 tangu kutagwa, mayai yatakuwa tayari kulaliwa na kuangua vifaranga wa umri sawa.

Mkurugenzi wa kituo cha Kalro kaunti ya Kakamega Dkt Ludovicus Okitoi akiwaelimisha wafugaji wa kuku kuhusu mbinu mbalimbali za kuongerza mapato mjini Kitale Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila.

Kupunguza vifo
Ili kukomesha tatizo la vifaranga kufa, aliwashauri kufuga jogoo mmoja kwa kila kuku 10 ambaye hana ukoo na mamake ili kuimarisha uwezo wa mayai kuangua na kuepuka vifaranga kufa.

Kuku wanaokula mayai na kuwala wenzao manyoya, inamaanisha wamesongamana sana na mwangaza huwa mwingi katika kiota ambamo mayai hutagiwa.

Wakigundua ni tamu, hii sasa huwa tabia yao. Kwa hivyo, unafaa kuwakata midomo ukitumia kisu moto ili iwe butu, na watakomesha tabia hiyo kwa muda wa wiki mbili.

Wakiwachanja kuku dhidi ya ugonjwa wa Newcastle, wafugaji walishauriwa kufanya hivyo mwishoni mwa kiangazi au mwishoni mwa msimu wa mvua.

“Je, kuku anaweza kuishi kwa muda gani kwa maisha yake?” mtafiti huyo akatupiwa swali.

“Maisha ya kuku yanategemea mbinu za mfugaji,” alianza.

“Kama nyoka, kuku huondoa magamba yake. Ukiona manyonya yakimtoka, mlazimishe kutoa maganda. Manyoya mengi huashiria ukosefu wa maji na chakula. Mnyime maji na chakula kwa wiki nzima, hawezi kufa. Baada ya hapo atapyesha homoni za kukua na kuanza kutaga mayai upya. Hivyo ndivyo unaongeza maisha yake.”

Wakuzaji wa miche ya matunda, mitishamba na mboga waonyesha ubunifu wao. Picha/ Faustine Ngila

Chakula cha ng’ombe
Maswali sasa yaliegemea ufugaji wa ng’ombe. “Je, ni nafaka zipi bora zaidi kwa kutengeneza chakula cha ng’ombe?” akauliza mfugaji wa kike.

Mkurugenzi wa kituo cha Kalro, Kitale Dkt F Lusweti alijibu kuwa mtama na mahindi ni chaguo bora.

“Kalro inapendekeza mahindi aina ya KH5500-43A kwa kuwa inakomaa haraka na unaweza kukuza alizeti baada ya kuvuna.

Iwapo unataka chakula chenye proteini, basi tumia mahindi mbichi wakati yameanza kuunda maziwa.

Lakini kama unataka chakula kingi kisicho na proteini nyingi, tumia mahindi yakiwa kiwango cha kuchemshwa. Nyasi ya Rhodes pia ni nzuri.”

Swali liliibuka kuhusu nyamakondo (placenta) kukwama ndani ya baadhi ya ng’ombe baada ya kuzaa.

Mtaalamu huyu alisema sababu kuu ni ya kiukoo, jua kali au ndama kuwa mkubwa kupita kiasi. Aliwashauri wafugaji kusaka fahali wanaozalisha ng’ombe ndama wa wastani.

Kampuni ya Simba Corp iliwaelezea wakulima trakta na mashine bora za kilimo na ufugaji inazounda. Picha/ Faustine Ngila

‘Hongo kwa ng’ombe’
Watafiti walionya wafugaji dhidi ya ‘kuwahonga’ ng’ombe kabla ya kumkama, kwa kumlisha chakula cha ng’ombe wa maziwa. Walisisitiza kuwa inafaa ng’ombe watunukiwe kwa kumpa mfugaji maziwa, na si kinyume chake.

Wafugaji pia walionywa dhidi ya kufuga fahali ikiwa wana ng’ombe watano pekee. Gharama ya kumfuga iko juu, hivyo mkulima anafaa kutumia mbinu ya kiteknolojia kuwatunga mimba ng’ombe.

Chuo Kikuu cha Egerton kilitangaza kuwa kimevumbua aina mpya ya mtama inayoweza kutumika kwa uokaji wa mikate. Kilisema kinashirikiana na kampuni za uokaji ili kuitangaza sokoni.

Wote waliohudhuria darasa hilo la elimu ya kilimo walifurahia kupata ujuzi na mbinu mpya za kupunguza gharama, kukabiliana na magonjwa, kuongeza mavuno na kuepuka hasara katika kilimo chao.

 

Baruapepe: fauzagila@gmail.com

 

Taabani kwa kukosa kulipia ngozi ushuru

Godfrey Bosire akiwa kizimbani aliposhtakiwa kwa uuzaji ng’ambo zaidi ya kilo milioni 3 za ngozi za ng’ombe na kukwepa kulipa mamlaka ya ushuru nchini (KRA) Sh204 milioni. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Jumatatu kwa kuuza ngozi za ng’ombe kilo 3,862,264  ng’ambo na kukwepa kulipa serikali ada ya forodha iliyopelekea serikali kupoteza ushuru wa Sh204 milioni.

Bw Godfrey Bosire alikanusha shtaka hilo mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya miliamni Bw Francis Andayi.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha aliomba kesi hiyo dhidi ya Bw Bosire itajwe Jumanne kwa lengo la kuiunganisha na  nyingine ambapo Bi Clare Marisiana Odimwa alishtakiwa kwa kosa kilo hilo.

Bw Naulikha alisema nakala za mashahidi katika kesi hiyo ziko tayari na kuwa Bw Bosire anaweza kuzipokea aandae tetezi zake.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa katika kesi dhidi ya Odimwa mahakama ilimwachilia kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Pia alisema mshtakiwa huyo  alipewa dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000.

Wakati huo huo Bi Margret Awino Magero alishtakiwa kwa kupokea sabuni na mafuta ya kupikia za thamani ya Sh 17 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Mabw Jeremiah Kiplangat Kendagor na Bw  Lukas  Oketch Mandagi Desemba 2016.

Alikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu.