Wanaosumbua polisi wakati wa kafyu waonywa

Na SAMMY WAWERU

Rais Uhuru Kenyatta ametoa onyo kwa watu wanaohitilafiana na maafisa wa polisi katika jitihada zao kutekeleza kafyu.

Rais Kenyatta aidha amesema hatua kali kisheria zitachukuliwa kwa wanaotatiza shughuli hiyo.

Kwenye hotuba yake kwa taifa mnamo Alhamisi, kiongozi huyo wa nchi alisema kila mmoja afahamu utaratibu na sheria zilizotolewa na serikali zina madhumuni ya kulinda maisha ya Wakenya.

“Yeyote atakayevunja sheria na kutatiza utendakazi wa maafisa polisi, ataadhibiwa kisheria,” Rais akaonya kupitia hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga kutoka Ikulu jijini Nairobi.

Kafyu ya usiku, kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhi inaendelea kutekelezwa kote nchini ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid – 19, unaosababishwa na virusi hatari vya corona. Ilianza kutekelezwa Machi 27, 2020.

Baadhi ya wananchi wanalalamikia inavyotekelezwa, wakinyooshea maafisa wa polisi kidole cha lawama kwa kuwadhulumu. Visa kadhaa vya mauaji na majeruhi yanayohusishwa na utekelezaji wa kafyu vimeripotiwa maeneo tofauti nchini.

Akipongeza utendakazi wa idara ya polisi, Rais Kenyatta hata hivyo amewataka maafisa wa usalama kutekeleza kafyu kwa njia ya utu. “Kwa maafisa ambao wanatulinda usiku na mchana, langu ni kuwapongeza. Pia, mfanye kazi kwa njia ifaayo. Mtekeleze kafyu kwa huruma, muongeleshe anayekosea na mumweleze hatari anayojiwekea yeye mwenyewe na kwa wengine,” Rais akahimiza.

Alisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha maisha ya Wakenya yamelindwa dhidi ya janga la Covid – 19.

Polisi aliyemuua mwanafunzi azuiliwa

Na Richard Munguti

Mahakama Kuu Nairobi Alhamisi iliamuru afisa wa polisi Emmanuel Abunya azuiiliwe hadi Aprili 23 2020 atakaposhtakiwa kwa mauaji ya Carilton Maina miaka miwili iliyopita.

Maina alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Leeds nchini Uingereza.

Jaji Ngenye Macharia aliagiza Abunya apelekwe kupimwa akili katika hospitali ya Mathari.

Upande wa mashtaka uliomba afisa huyo asikubaliwe kujibu shtaka kwa vile utimamu wa akili yake haujulikani.

Wakili Harun Ndubi anayemwakilisha Abunya aliomba mshukiwa aachiliwe kwa dhamana lakini upande wa mashtaka ukapinga.

Jaji Macharia alimweleza mshukiwa atajibu shtaka la kumuua Maina Desemba 22, 2018 mnamo Aprili 23.

KAFYU: Polisi na majambazi sasa wazidisha uhalifu

Na WAANDISHI WETU

VISA vya ukiukaji wa amri ya kutotoka nje usiku na uhalifu vimeendelea kushuhudiwa maeneo tofauti nchini huku maafisa wa polisi wakiwa mstari wa mbele kuvunja sheria wanayopaswa kutekeleza.

Mnamo Jumatatu usiku, maafisa saba wa polisi na raia wawili walikamatwa wakilewa katika baa moja mtaani Mbotela, Nairobi.

Maafisa hao wanahudumu katika makao makuu ya kitengo cha kukabiliana na uhalifu nchini.

Maafisa hao wanazuiliwa katika seli wakisubiri kufunguliwa mashtaka ya kukiuka kafyu ya serikali na kulewa baada ya muda unaoruhusiwa.

Usiku huo, watu watatu walikamatwa katika msako wa polisi kwa kufungua baa katika mitaa ya Lunga Lunga na Mukuru Kayaba, Kaunti ya Nairobi.

Polisi walitwaa mashine kadhaa za kuchezea kamari wakati wa kisa hicho.

Kamanda wa polisi katika eneo la Makadara, Bw Abdikadir Sheikh aliambia Taifa Leo kwamba lengo la msako huo lilikuwa kukabiliana na wanaokusanyika pamoja wakati huu wa janga la virusy vya corona.

“Baa ni moja ya mahali ambapo wananchi hukutania kuburudika pamoja. Serikali imeamuru watu kujiepusha kukaribiana ili ugonjwa wa corona usieneee zaidi, ” Bw Sheikh akasema.

Katika eneo la Nyakoe, Kaunti ya Kisii, polisi wanawasaka washukiwa waliomuua afisa mmoja wa Nyumba Kumi, aliyekuwa akitekeleza agizo la serikali la kuhakikisha maeneo ya burudani yanafungwa kulingana na amri ya serikali.

Afisa huyo aliuawa Jumatatu usiku katika baa moja inayopatikana Mosocho, eneobunge la Kitutu Chache Kusini. Afisa huyo aliyetambulika kama Japheth Mayieka, alikutana na kifo baada ya yeye na wenzake wawili kuingia katika baa hiyo inayodaiwa kutofuata maagizo yaliyowekwa na serikali

Inaaminika kuwa baa hiyo imekuwa ikihudumu usiku kucha na huwafungia walevi ndani.

Wakazi wa sehemu hiyo wamewataka machifu kukoma kutumia vijana kutekeleza maagizo ya serikali.

Kwingineko, katika sehemu za Nyatieko, hatua chache kutoka Nyakoe, wakazi wamelalamika kuwa kuna baa ya mtu maarufu inayohudumu hata baada ya muda ulioruhusiwa.

Katika tukio lingine la Malindi, Kaunti ya Kilifi, wakazi wa eneo la Migingo wanalalamikia kelele kutoka kwa walevi na wametaka hatua za sheria kuchukuliwa dhidi ya wanaofungua vilabu vya pombe usiku.

Akizungumza jan mjini Malindi, mkazi Kalume Chengo, alisema kelele hizo zinawakosesha usingizi wanaoishi karibu na vilabu na kuhatarisha usalama wao.

Kulingana na Bw Chengo, huenda hali hiyo ikawa changamoto dhidi ya vita vya kukabiliana na virusi vya corona na kuweka maisha ya wananchi kwenye hatari.

Wakati huo huo, Bw Chengo ameitaka idara ya polisi kuingilia kati na kuanzisha msako sehemu hiyo na kuwakamata wanaovunja sheria ya kutotoka nje usiku.

“Ninataka polisi waje hapa Migingo kwa sababu tabia hii inatunyima amani, hatulali na hatuwezi kuvumilia wakati tunapozidi kuumia,” alisisitiza Bw Chengo.

Kilifi ni moja ya kaunti nne ambazo wakazi wamepigwa marufuku kusafiri hadi katika kaunti nyingine kwa siku 21 kutokana na idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona.

Ripoti za Sammy Kimatu, Benson Matheka, Wycliffe Nyaberi na Alex Amani

Walioiba bunduki wabambwa

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wa upelelezi wa jinai wamemkamata mwanamume mmoja anayeshukiwa kuwa miongoni mwa majambazi waliovamia kituo cha polisi cha Kibos na kuiba bunduki, risasi kadha na mali nyinginezo.

Kwenye taarifa kupitia akaunti yake ya twitter jana, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema walimkamata mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 19 nyumbani kwake katika kijiji cha Kanyakwar viungani mwa mji wa Kisumu akiwa moja bunduki zilizoibiwa katika kisa hicho mnamo Machi 28, 2020.

“Mshukiwa wa wizi wa kimabavu, mwenye umri wa miaka 19, anayehusishwa na wizi wa silaha kutoka kituo kidogo cha polisi cha Kibos na kisha wizi wa Zaidi ya Sh23,000 kutoka kwa mhudumu wa Mpea katika eneo la Daraja Mbili, Kisumu leo alikamatwa na wapelelezi wa DCI nyumbani kwake katika Kijiji cha Kanyakwar, Kisumu,” DCI ikaandika.

Kulingana na DCI mhudumu wa Mpesa alivamiwa na genge la wanaume watano walikuwa na bunduki aina ya G3 kabla ya kumwibia pesa hizo, simu tatu za mkono na televisheni moja. Kisha walitoroka kwa kutumia pikipiki mbili.

Baada ya tukio hilo maafisa wa upelelezi wa Kisumu wakishirikiana na wenzao kutoka makao makuu ya DCI walianzisha operesheni kali ya kuwasaka washukiwa hao.

Mshukiwa aliyekamatwa jana alipatikana na bunduki moja aina ya G3 nyumbani kwake akiwa ameifunga ndani ya gunia.

“Bunduki hiyo ilitambuliwa kama ile ambayo iliibiwa kutoka kituo cha polisi cha Kibos mnamo Machi 28, 2020 usiku, mvua ikinyesha, watu wasiojulikana walipovunja ghala la silaha na kuiba bunduki tatu, magazine nne na risasi 150,” DCI ikasema.

Iliongeza kuwa baada ya mshukiwa kuhojiwa, aliwaelekeza maafisa hadi nyumba ya mwenzake katika Kijiji hicho hicho.

Katika nyumba hiyo maafisa walipata vitu kadhaa kama vile jaketi tatu za polisi, longi, mishipo, viatu vya maafisa wa usalama, kofia ya polisi na televisheni.

“Vitu hivyo vilitambuliwa kama vile ambavyo viliibiwa kutoka nyumba ya afisa mmoja wa polisi wa cheo cha Inspekta mnamo Machi 10, 2020 alipokwenda Kiganjo kwa mafunzo zaidi, DCI ilisema.

Washukiwa hao wawili wanazuiliwa na polisi huku wapelelezi wakiendelea kuwasaka washukiwa wengine.

KAFYU: Polisi na majambazi sasa wahangaisha Wakenya

Na WAANDISHI WETU

VISA vya uhalifu vimeendelea kutekelezwa na polis pamoja na magenge hatari wakati wa kafyu inayotekelezwa na serikali kuepusha ueneaji virusi vya corona.

Katika kaunti ya Nakuru, mfanyabiashara mmoja analilia polisi baada ya duka lake kuvunjwa na maafisa hao waliokuwa wakitekeleza kafyu.

Kisa hicho kilitokea katika mtaa wa Top Ten, eneo la Langalanga viungani mwa mji wa Nakuru Jumamosi usiku.

Maafisa wakuu wa polisi wakiongozwa na kamanda wao katika kaunti hiyo Bw Stepehn Matu walisema hawakuwa na habari kuhusu tukio hilo.

Katika kaunti ya Uasin Gishu, polisi wanachunguza tukio ambapo walinzi wa kaunti na wale wa kibinafsi waliwavamia vijana wa kurandaranda mitaani na kuwajeruhi watatu Jumapili usiku Eldoret.

Jana, vijana hao walivamia kituo cha Central mjini humo wakitaka walinzi hao wakamatwe.

Katika kaunti ya Laikipia, mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 23 ulipatikana jana asubuhi mtaani Jua Kali mjini Nyahururu.

Polisi walisema mwili huo uliotambuliwa kuwa wa John Ngugi uliopatikana na mwanabodaboda ambaye alipiga ripoti kituoni cha polisi.

Nacho chama cha Madereva wa Kusafirisha Mizigo Nchini (KTA), kimeitaka serikali kuchukulia hatua kali maafisa wa polisi waliowapiga madereva wa kusafirisha bidhaa ambao walikuwa wameorodhoshwa kutoa huduma hata baada ya saa za kafyu kufika.

“Polisi hawafai kutumia nguvu nyingi wanapowakabili wananchi na hivyo wote waliohusika wanafaa kuchukuliwa hatua kali,” akasema Newton Wang’oo ambaye ni mwenyekiti wa KTA, katika taarifa.

Huko Siaya afisa wa polisi alikamatwa Jumamosi kwa kukataa kutii kafyu.Afisa huyo, Hussein Abdulahi, alipatikana katika baa akiburundika na wakazi mwendo wa saa mbili na nusu usiku.

Katika mtaa wa Witeithie Juja, Kaunti ya Kiambu, polisi walilazimika kuvunja maskani ya burudani ili kuwafurusha walevi waliokuwa wakijiburudisha na kinywaji baada kafyu kuanza.Ilidaiwa mmiliki wa maskani hiyo aliamua kuwafungia wateja wake ndani ya baa hiyo.

Ripoti za SAMUEL BAYA, DIANA MUTHEU, STEVEN NJUGUNA, LAWRENCE ONGARO, DENNIS LUBANGA, DICKENS WASONGA Na KALUME KAZUNGU

CORONA: Polisi watimua waumini wakaidi makanisani

Na WAANDISHI WETU

POLISI mjini Mombasa Jumapili walilazimika kutimua waumini waliokaidi ushauri wa Serikali Kuu na kuendelea na ibada makanisani.

Katika kanisa la Jesus Celebration Center (JCC) eneo la Buxton, waumini waliokuwa wamejitayarisha kuhudhuria misa ya pili walilazimika kurudi nyumbani, polisi walipoweka ulinzi mkali katika lango la kanisa hilo, huku wakiwazuia waumini kuingia ndani.

Tawi la kanisa la JCC lililoko Bamburi pia lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, ambao baadaye walitimua waumini waliotaka kuhudhuria misa ya pili.

Kamanda wa Polisi Kisauni, Bw Julius Kiragu, alisema kanisa hilo lilienda kinyume na agizo la serikali.

Katika kanisa la Zion Fire Ministries Changamwe, polisi walilazimika kuwatimua waumini walipokataa kutii agizo la kufunga kanisa baada ya misa ya kwanza.

“Tuliwapa wakati wa kumaliza misa ya kwanza na kuwaeleza waende nyumbani. Lakini waliamua kuendelea na misa ya pili. Ndio maana tukawatimua,” alisema kamanda wa polisi Changamwe, Bw Issa Mohammed.

Hata hivyo, polisi wanasema hakuna muumini yeyote aliyejeruhiwa katika shughuli hiyo.

Kasisi wa Kanisa la Kisima cha Neema, Mshomoroni Mary Kagendo, aliiomba serikali ikubali maombi katika makanisa kuendelea.

“Ni muhimu kwa kutatua janga ambalo linashuhudiwa nchini,” akasema.

Katika eneo la Shika Adabu, Likoni, Chifu Athuman Mwakashi aliongoza manaibu wake kuzuia ibada zilizokuwa zikiendelea, huku baadhi ya waumini wakidai walikuwa wakitekeleza matakwa waliyoagizwa na serikali kama njia za kuzuia maambukizi.

Katika kanisa la Life Way Pentecoastal Church, Ujumaa, machifu hao walikuwa na wakati mgumu wa kujaribu kuwahamasisha waumini haja ya kufanyia ibada zao nyumbani jinsi ilivyoagiza serikali.

Naibu Kamishna wa Likoni, Bw Francis Kazungu aliwataka wakazi wa eneo hilo wazingatie maagizo ya serikali, ili kuzuia uwezekano wa maambukizi ya virusi vya corona.

Wavuvi nao waliendelea na shughuli zao maeneo tofauti ya uvuvi katika kaunti, kukiwa hakuna vifaa vya kujikinga kama sabuni na maji safi.

Katika eneo la uvuvi la Ngare, Portreitz, wengi walinawa mikono wakitumia maji ya chumvi kutoka baharini bila kutumia sabuni.

Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa eneo la uvuvi la Ngare, Bw Abdallah Kitondo, alisema kuwa wavuvi hawawezi kubakia nyumbani.

“Hatuwezi kufanyia kazi zetu nyumbani. Tukikaa nyumbani tutakula nini? Kama serikali ingekuwa na mpango wa kutoa chakula kwetu, labda tungebakia nyumbani. Tunaamini viini havikai katika maji ya chumvi,” akasema.

Naye mwenyekiti wa eneo la uvuvi la Old Town, Bw Swaleh Mohammed, alisema kuwa wavuvi wananawa mikono kutumia maji ya bahari ambayo yana chumvi.

Alisema ni vigumu kupunguza idadi ya wavuvi katika boti za kuvulia samaki. Hata hivyo, alisema kuwa amewaagiza wavuvi wasikaribiane, wakae umbali wa mita moja.

Boti moja linaweza kubeba wavuvi watatu hadi wanane kulingana na urefu wake.

“Bado hatuna maji safi na sabuni lakini tumeomba wavuvi na wachuuzi wanaofika katika eneo hili wasikaribiane,” akasema Bw Mohammed.

Taarifa za Siago Cege, Diana Muthey na Hamisi Ngowa.

Seneti yaambiwa raia 210 waliuawa na polisi

Na CHARLES WASONGA

JUMLA ya raia 210 wameuawa na polisi kinyume cha sheria katika kipindi cha miezi 15 iliyopita, hii ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Maafisa wa Polisi nchini (IPOA).

Mwenyekiti wa mamlaka hiyo, Bi Anne Makori jana aliwaambia maseneta kwamba kati ya watu hao, 146 walipigwa risasi hadharani na polisi, 39 walifariki katika vituo vya polisi huku 25 wakipatikana wamefariki baada ya kutekwa nyara na polisi.

Bi Makori aliambia wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Sheria na Haki na Kibinadamu kwamba asasi hiyo imekamilisha uchunguzi kuhusu visa 110 na kuwasilisha faili hizo kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) Noordin Haji ili watuhumiwa wafunguliwe mashtaka.

“Kati ya faili hizo, 75 zimewasilishwa mahakamani na zingine 35 zingali zinashughulikiwa katika afisi ya DPP.

“Vilevile, kuna visa vingine 20 ambavyo tulikamilisha kuchunguza wiki jana na tunatarajia kuwasilisha faili zao kwa afisi hiyo,” akawaambia wanachama wa kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei.

Baadhi ya visa ambavyo IPOA imekamilisha kuchunguza ni mauaji ya mauaji ya mvulana mwenye umri wa miaka mitatu, Dancan Githinji, katika kijiji cha Soweto, mtaa wa Kahawa West, Nairobi, mnamo Novemba 8, 2019.

Kisa kingine ni mauaji ya Bw Carliton Maina katika eneobunge la Kibra, Nairobi mnamo Desemba 22, 2018 ambapo polisi mhusika anasubiri kuwasilishwa kortini kukabiliwa na mashtaki ya mauaji kwa kukusudia.

Vilevile, IPOA imekamilisha uchunguzi wa kisa ambapo polisi walimpiga risasi na kumuua Ahmed Majid mnamo Januari 16, 2020 katika eneobunge la Kamukunji, Nairobi.

Bi Makori aliwaambia maseneta hao kwamba katika kipindi hicho cha miezi 15, maafisa sita wa polisi wamepatikana na hatua ya kutekeleza mauaji ya raia kiholela na kuhukumiwa.

“Watatu kati yao wamepewa adhabu ya kifo,” akasema akiongeza kuwa hiyo ni ishara kwamba IPOA inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Bi Makori alikuwa amefika mbele ya Kamati hiyo pamoja na makundi kadhaa ya kutetea haki za kibinadamu kuangazia hatua ambazo zimechukuliwa na wadau mbalimbali kudhibiti kero hilo.

Miongoni mwa mashirika yaliyohudhuria kikao cha kamati hiyo katika ukumbi wa County, Nairobi ni Amnesty International (AI), Haki Afrika, International Medico- Legal Unit, na Social and Justice Centre.

Mashirika hayo yaliitaka Seneti ipendekeze kuundwe kwa tume ya kisheria ya kuchunguza visa vya mauaji yanayotekelezwa na polisi kinyume cha sheria.

Agizo mabasi yanayohudumu Kaskazini Mashariki yasindikizwe na polisi

JACOB WALTER na MERCY MWENDE

SERIKALI imetoa agizo kwamba mabasi ya uchukuzi wa umma yanayohudumu maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi yawe yakisindikizwa na maafisa wa polisi la sivyo, leseni zifutwe.

Kulingana na kamishna wa kanda hiyo Nick Ndalana, agizo hilo lazima litekelezwe kwani eneo hilo limekuwa likiathirika sana kutokana na mashambulio ya kigaidi.

Ameeleza kuwa madereva na wamiliki wa magari ambao watapuuza agizo hilo watatiwa mikononi mwa sheria wafikishwe mahakamani na kushtakiwa.

Agizo hilo linajiri baada ya shambulio lililofanywa dhidi ya basi moja katika eneo la Sarman mnamo Jumatano ambapo watu watatu waliangamia.

Bw Ndalana alieeleza hayo Jumatano akiwa katika ofisi yake mjini Marsabit akizungumza na wanahabari.

“Kufuatia shambulio katika kaunti ya Mandera hivi leo (jana Jumatano), wamiliki wote wa mabasi katika maeneo haya watahitajika kuhakikisha yanasindikizwa na polisi au kuhatarisha leseni zao kufutwa,” Bw Ndalana akasema.

Afisa huyo wa serikali alieleza kuwa basi lililoshambuliwa lilikuwa linaelekea jijini Nairobi, lakini lilipofika katika eneo la Sarman, kadiri ya washambuiaji 11 ambao walikuwa kwenye pikipiki tatu walimwashiria dereva asimamishe.

Abiria watano walijehuriwa na kuwahiwa hospitalini huku wengine ambao walikuwa wamekimbilia vichakani wakati wa shambulio, wakinusuriwa na maafisa wa polisi kwa kuwekwa kwenye maeneo salama.

Afisa huyo aliwapongeza polisi kwa kufika maeneo hayo kwa haraka na kuwasaidia abiria kwani kwa kufanya upesi, maafisa waliwaokoa abiria wengi.

Bw Ndalama alishangaa kwa nini gari hilo halikuwa na maafisa wa polisi wakati wa shambulio, kwani wakati gari hilo liliondoka katika mji wa Mandera kulikuwa na maafisa wa polisi kwenye basi.

Kamishna ameitaka Mamlaka ya Usalama Barabarani Nchini (NTSA) kuhakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa ili kuzuia visa vya mashambulio ya kigaidi katika eneo hilo.

Bw Ndalana aliwahakikishia wakazi kuwa serikali ilikuwa imejitolea kupunguza visa vya kigaidi katika eneo hilo.

Alifafanua zaidi kuwa serikali ilikuwa imeongeza maafisa wa usalama ambao waliwekwa haswa katika sehemu zenye matatizo ya kigaidi.

Serikali imepiga marufuku uendeshaji wa bodaboda eneo hilo – kuanzia jana Jumatano – mara ifikapo saa kumi na mbili jioni.

Kamishna wa Mashariki Isaiah Nakoru alipiga marufuku operesheni ya waendeshaji pikipiki kwenye mipaka ya Kenya-Ethiopia-Somalia.

Bw Nakoru alisema kuwa kulikuwa na waendeshaji wa bodaboda ambao walihusika na ugaidi na biashara ya kusafirisha dawa za kulevya katika mikoa hiyo.

“Baada ya kufanya uchunguzi wa mwaka mmoja, tumebaini kuwa waendeshaji wa bodaboda ndio wamechangia sana katika usafirishaji wa dawa za kulevya katika maeneo haya. Hivyo basi, tumepiga marufuku operesheni za bodaboda kutoka saa kumi na mbili jioni,” Bw Nakoru akasema.

Maeneo ambayo yataathiriwa na marufuku hayo ni Kata ndogo ya Moyale, Mandera, Garissa, Wajir na kaunti za Lamu na Turkana.

Maafisa hao wa mkoa huo walikubalina kuwa marufuku hayo yatasaidia katika kulinda maisha ya wakazi kwa sasa hadi wakati ambao visa vya kigaidi vitapunguka katika maeneo hayo.

Kesi za waliouawa na polisi bado zinajikokota -IPOA

Na PETER MBURU

ZAIDI ya mwaka mmoja tangu mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Leeds, Carilton Maina alipouawa na polisi, kesi yake ingali inajikokota na haijafika kortini, licha ya uchunguzi kukamilika awali 2019.

Mamlaka Huru ya Usimamizi na Uangalizi wa Polisi (IPOA) jana ilisema japo iliwasilisha faili ya kesi ya mwanafunzi huyo kwa Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) mnamo Aprili mwaka jana, kesi hiyo haijafikishwa kortini.

Hali ni sawa na hiyo kuhusu kesi ya mtoto wa miaka miwili, Dan Githinji, ambaye alipigwa risasi na polisi waliokuwa wakitafuta hongo kwa watengenezaji wa pombe haramu, katika mtaa wa Kahawa West, Nairobi.

“Bado tunasubiri washukiwa wafikishwe kortini kwani tulikamilisha uchunguzi na kuwasilisha faili kwa DPP,” mwenyekiti wa IPOA Anne Makori akasema jana.

Akiongea wakati wa kikao na wanahabari kutoa ujumbe kuhusu visa vinavyohusisha polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia ama polisi wenzao, Bi Makori alisema mamlaka hiyo imepokea malalamishi mengi kutoka kwa Wakenya, japo uchunguzi wa mengi kati yayo haujakamilika, na kuhusu yaliyokamilika, hayajafikishwa kortini.

“Hadi wakati wa mwisho tulipotoa habari, mamlaka hiyo imepokea malalamishi 13,618 na 1,518 kati yake yakachunguzwa. Tumewasilisha faili za malalamishi 180 kwa DPP, ambapo kesi 75 kati yake ziko kortini sasa,” Bi Makori akasema.

Makamishna wa IPOA walisema katika matukio mengi ambapo polisi wamehusika na uhalifu ama kupiga raia risasi, mashahidi wanahofia maisha yao ama kutishiwa, na hivyo hawajitokezi, jambo walilosema linafifisha uchunguzi.

IPOA aidha iliripoti kuwa miaka ya majuzi kumekuwa na mtindo wa polisi kuwaua wenzao, ama raia kuwajeruhi ama kuwaua polisi, ikisema ni suala ambalo pia inachunguza.

Hata hivyo, mamlaka yenyewe pia haina uwezo zaidi ya kuchunguza visa hivyo kisha kuwasilisha faili za kesi na mapendekezo kwa DPP ama Tume ya Huduma za Polisi (NPSC), kwani mapendekezo yake yasipotekelezwa, haifanyi lolote.

Majuzi, Rais Uhuru Kenyatta aliamrisha wizara ya Usalama wa Ndani kukoma kuwahamisha polisi wanaopatikana wakifanya uhalifu ama ufisadi, na badala yake kuwapiga kalamu.

Mauti na vilio wakazi wakidai haki yao Kasarani

PETER MBURU na MARY WAMBUI

POLISI Alhamisi waliendelea kulaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakilalamikia ubovu wa barabara ya Kasarani- Mwiki jijini Nairobi.

Wakazi hao jana walilaumu polisi kuwa Jumatano waliwapiga watu wawili risasi na mmoja alikufa. Madai tofauti yalisema kuwa watu wawili waliuawa na polisi siku hiyo.

Ripoti zilisema mvulana wa miaka 17, Stephen Machurusi alipigwa risasi kifuani na kuwa alifariki hospitalini.

“Tulimpata akiwa amelala ndipo tukamkimbiza hospitalini lakini tukaambiwa kuwa risasi ilipenyeza mahali hatari. Alikufa muda mfupi baadaye,” akasema Lilian Waringa, dadake marehemu.

Lakini polisi walisema wamethibitisha kifo cha mtu mmoja pekee na kusema bado hawajabaini kilichomuua.

“Kile tumethibitisha ni kuwa mtu mmoja alifariki na maafisa watano wa polisi wakajeruhiwa vibaya. Baada ya upasuaji wa maiti kufanyika ndipo tutajua kilichomuua,” OCPD wa Kasarani Peter Kimani akasema.

Wakati hayo yakijiri, viongozi, wakuu wa usalama Kasarani, maafisa wa Mamlaka ya Ujenzi wa barabara za miji (Kura), maafisa wa vyama vya wenye matatu eneo hilo na Kitengo cha Utekelezaji wa Miradi katika afisi ya Rais (PDU) waliafikiana kusitisha maandamano hayo yaliyoanza Jumatatu na kuanza urekebishaji wa barabara husika mara moja.

Katika mkutano huo ulioongozwa na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, pande zote ziliafikiana kuwa ukarabati wa barabara ya Kasarani- Mwiki ungeanza mara moja na magari kurejelea kazi ya kusafirisha wakazi.

“Malalamishi ya wakazi wa Kasarani ni ya kweli na ni haki yao kwani hali ya barabara ni mbovu sana. Hata hivyo, matukio ambayo yamekuwa yakishuhudiwa siku hizo za maandamano hayakuwa ya kufurahiwa,” Bw Sakaja akasema.

Barabara hiyo ilikuwa imefanyiwa ukarabati 2018 lakini ikaharibika muda mfupi baadaye kutokana na ujenzi duni.

Hali katika barabara nyingi jijini Nairobi ni ya kusikitisha licha ya wakazi kulipa kodi za juu kila mara.

Wanachuo wakabiliana na polisi wakipinga faini

STELLA CHERONO na MERCY KOSKEI

BEWA Kuu la Chuo Kikuu cha Egerton, Jumatatu liligeuka uwanja wa vita, wanafunzi wakikabiliana na polisi wakitaka waruhusiwe kurejea chuoni bila kulipa fidia ya Sh7,000 kwa kuharibu mali ya chuo.

Usimamizi wa chuo ulikuwa umeweka masharti kwamba kila mwanafunzi lazima alipe fedha hizo kutokana na uharibifu wa mali ya chuo mnamo Disemba 4, 2019 baada ya wanafunzi kugoma.

Wanafunzi waliopandwa na mori walipinga hatua hiyo wakisema chuo chao kinatumia kisingizio hicho kupata fedha maradufu kutoka kwao.

“Kiasi wanachotoza ni cha juu mno. Chuo kina zaidi ya wanafunzi 10,000, hiyo ikiwa na maana kwamba zaidi ya Sh70 milioni zitapatikana. Ukitathmini kiasi cha uharibifu, utagundua fedha hizo ni za juu mno,” akasema mwanafunzi mmoja kutoka chuo hicho.

Vurugu hizo zilitatiza usafiri kwenye barabara ya Njoro-Mau Narok, waendeshaji wa magari wakilazimika kuondoa mawe ambayo yalikuwa yamewekwa na wanafunzi kuziba barabara hiyo.

Usimamizi uliwaruhusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa nne pekee chuoni japo kwa masharti kwamba kila mwanafunzi lazima atie saini barua ya kukubali kugharimia uharibifu huo na kuahidi kutoshiriki ghasia tena.

Kufikia saa sita mchana hapo jana, wanafunzi tisa walikuwa wamenyakwa na polisi ambao walitumwa kutuliza ghasia hizo zilizokuwa zinaelekea kusambaa hadi miji ya Njoro na Elburgon.

Wanafunzi waliorejea chuoni walikuwa wameanza kuvamia maduka na kuwaamrisha wafanyabiashara wawape maji na chakula bila malipo.

“Utata unaendelea na serikali inafaa iingilie kati kisha iwatume wakaguzi kutathmini kiwango cha uharibifu kabla hatujaambiwa kiasi cha kulipa. Kiwango ambacho wanaitisha ni cha juu sana,” akasema mwanafunzi mwingine kwa jina Samwel Kimani.

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, chuo hicho kilianzisha matumizi ya kadi maalum ya mtihani kwa wanafunzi waliomaliza kulipa karo.

Wafanyabiashara katika mji wa Njoro nao hawakuwa na budi ila kufunga biashara zao wakihofia maandamano na vurugu hizo zingewasababishia hasara kubwa.

Mfanyabiashara kwa jina Sammwel Macharia ambaye alifunga biashara yake, alisema alikuwa na matumaini ya hali kurejea kama kawaida leo.

Chuo hicho mnamo Desemba ilitishia kuahirisha shughuli za masomo kwa mwaka mmoja kwa wanafunzi wasiokamilisha karo yao, jambo lililochochea maandamano makubwa na kusababisha kufungwa kwake.

Polisi warudisha Kenya enzi za giza

Na MISHI GONGO

CHAMA cha Wanahabari (KUJ) kinataka hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa wa polisi waliomshambulia mpiga picha wa gazeti la Taifa Leo, Laban Walloga akiwa kazini.

Katibu mkuu Bw Erick Oduor, Jumatatu alitishia kuripoti serikali kwa Umoja wa Mataifa (UN) kwa kukosa kulinda uhuru wa wanahabari.

“Wiki moja iliyopita wanahabari watatu walidhulumiwa na polisi. Hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya maafisa hao licha yao kupiga ripoti,” akasema Bw Oduor.

Bw Walloga alikuwa akipiga picha katika maandamano ya kupinga hatua serikali kulazimisha usafirishaji wa mizigo kwa treni ya SGR pekee.

Maandamano hayo yamekuwa yakifanyika jijini Mombasa kila siku ya Jumatatu, ambapo wakazi wanadai hatua hiyo imedidimiza uchumi wa eneo hilo ambalo rasilimali yake kuu ni bandari.

Mpiga picha huyo alieleza jinsi mmoja wa maafisa wa polisi kwenye maandamano hayo alivyompiga kwa rungu bila sababu.

Picha zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha afisa huyo akimrushia rungu Bw Walloga, aliyejaribu kutoroka.

“Nilikuwa kazini na hata nilimuonyesha kitambulisho cha kazi na kamera yangu. Hakutaka kunisikiza. Alinifukuza. Alijaribu kunigonga kwa mkebe wa vitoa machozi lakini nikahepa. Baadaye alinigonga kwa rungu,” akasema.

Wengine waliohangaishwa na kukamatwa wakati wa maandamano hayo ni diwani wa wadi ya Jomvu Kuu, Bw Shebe Mukonoo, na maafisa wa shirika la Haki Afrika wakiwemo Bw Hussein Khalid na Mathias Shipeta.

Jana haikuwa mara ya kwanza kwa mpiga picha huyo kushambuliwa na maafisa wa polisi akiwa kazini.

Mnamo Agosti 2018, Bw Walloga alikamatwa pamoja na mpiga picha wa runinga ya NTV, Bw Karim Rajan walipokuwa wanapiga picha hoteli moja kwenye ufuo wa Bahari Hindi ambayo imekiuka kanuni za mazingira.

Matukio ya wanahabari kunyanyaswa na maafisa wa polisi nchini si jambo la jipya licha ya washikadau mbali mbali kuendelea kupigania uhuru wa uanahabari.

Polisi vidosho sasa marufuku kuvaa wigi

Na NICHOLSA KOMU

MAAFISA wa kike wa polisi watalazimika kuenda saluni ili kuondoa wigi zao za kuvutia punde sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya zitakapokamilika Januari 1, kwa mujibu wa agizo lililotolewa na Tume ya Huduma kwa Polisi (NPSC).

Agizo hilo linataka pia polisi wa kike Waislamu wakome kufunga hijabu za kimapambo, kwani wataruhusiwa tu kufunga za rangi nyeusi.

Idara ya polisi inasema kwamba siku hizi idara ya polisi inakosa heshima machoni pa umma kwani polisi wa kike wameamua kujirembesha kupita kiasi wakiwa kazini.

Kwa mujibu wa Naibu Inspekta Jenerali wa polisi, Bw Edward Mbugua, ambaye alitia sahihi agizo hilo, mienendo hiyo inayoibuka miongoni mwa polisi wa kike inaenda kinyume na maadili ya utendakazi wao.

“Wakati wa ziara yangu kwa muda wa wiki moja katika maeneo mbalimbali ya nchi, nimepata maafisa wa kike wa polisi wanaoshikilia vyeo mbalimbali wakiwa na mitindo isiyofaa ya nywele inayokiuka maadili ya kazi yao,” akasema Bw Mbugua.

Mkuu huyo wa polisi alidai kwamba baadhi ya mitindo ya kisasa ya nywele imewazuia hata maafisa hao wa kike kuvaa kofia zao vyema kichwani wakiwa kazini.

“Hili halikubaliki kamwe kwenye maadili yao ya utendakazi,” akaongeza.

Afisa huyo pia alizua maswali kuhusu vazi la hijabu lenye rangi mbalimbali kwa polisi wa kike Waislamu, akisisitiza kuwa wanafaa kuvaa ya rangi nyeusi pekee jinsi ilivyo kwenye agizo la idara hiyo.

“Polisi wa kike Waislamu wamepuuza hijabu nyeusi inayokubaliwa na sasa wanavaa za rangi mbalimbali. Wanafaa wakome na kufuata sheria,” akasema.

Makamanda wa polisi wanatarajiwa kutekeleza amri hiyo na kuhakikisha kuwa polisi wa kike wenye mtindo wa nywele usiofaa wanatii na kuondoa urembeshaji huo kufikia Desemba 31.

Tume hiyo pia ilishikilia kwamba polisi wote lazima wakumbatie sare mpya ya polisi na mavazi ya kinadhifu, amri ambayo makamanda wote wa polisi watahakikisha inatekelezwa vilivyo.

Polisi mafisi

Na WAANDISHI WETU

VISA vya maafisa wa polisi kushambulia watoto wa kike na kuwanajisi vimeongezeka katika maeneo tofauti ya nchi siku za karibuni.

Katika kipindi cha wiki moja pekee, kumeripotiwa visa visivyopungua vitano ambapo watoto wa umri kati ya miaka 13 na 16 walinajisiwa na maafisa wa polisi.

Katika baadhi ya visa hivyo, watoto hao walikuwa wameenda kutafuta usaidizi kwa polisi bila kujua walikuwa wanajiingiza midomoni ya fisi.

Jumamosi, afisa wa polisi katika Kituo cha Naromoru, Kaunti ya Nyeri alikamatwa kwa madai ya kumnajisi mtoto wa miaka 13 kituoni Ijumaa jioni.

Ripoti ya polisi ilionyesha Konstebo Stephen Wachira alimshambulia mtoto huyo aliyepelekwa kituoni na wasamaria wema ambao walimpata akiwa amepotea.

Msichana huyo alikuwa amepatikana katika steji ya matatu ya Naromoru alikoachwa akiwa anaelekea kumtembelea mjomba wake mjini Nanyuki kutoka mji wa Nyeri.

Alipokewa na maafisa wawili wa kiume kituoni mwendo wa saa mbili usiku lakini keshoye, mwendo wa saa kumi na moja asubuhi, Wachira akaondoka naye akidai anampeleka kituo cha kuabiri matatu ili arudi Nyeri.

“Uchunguzi wa kwanza unaonyesha afisa huyo alimpeleka nyumbani kwake ndani ya kambi ya polisi ambako alimnajisi. Baadaye alimpeleka steji na akampandisha matatu ya kuelekea Nyeri,” ripoti ikasema.

Ni katika matatu hiyo ambapo msichana alieleza wasafiri masaibu yake ndiposa wakampeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nyeri ambapo kisa hicho kiliripotiwa, kisha mshukiwa akakamatwa.

Kamanda wa polisi eneo la Kati, Patrick Lumumba jana alithibitisha hayo, na kusema kesi imewasilishwa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ili kufanyiwa upelelezi zaidi.

Alhamisi iliyopita, msichana wa miaka 15 katika Kaunti ya Kilifi aliripotiwa kupelekwa na wazazi wake katika kituo cha polisi kwa madai ya wizi na utundu ili ashike adabu, lakini polisi akamnajisi.

Kamanda wa Polisi Kilifi Kaskazini, Bw Njoroge Ngigi, alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.

Katika Kaunti ya Migori, polisi walikuwa wanamsaka afisa wa polisi ambaye binti yake wa miaka 12, alimripoti kwa kumnajisi kisha kumfungia katika seli ya Kituo cha Polisi cha Isebania.

Habairi zilisema polisi huyo alimnajisi mtoto wake Novemba 1 na akasaidiwa na maafisa wenzake kuficha kisa hicho ambacho Mkuu wa Polisi wa Kuria Magharibi, Benard Muriuki alithibitisha kinaendelea kuchunguzwa.

Mtoto huyo ambaye alikuwa akiishi na nyanyake. alikuwa ameenda kwa babake kuchukua karo ya shule wakati alipotendewa unyama huo.

Alipohojiwa, alisema wakati alipopiga ripoti katika kituo kidogo cha polisi cha Nyabohanse, kuna afisa wa polisi wa kike ambaye alimwita babake na chifu kisha wakajaribu kumshawishi amsamehe.

Wiki hiyo hiyo Jumanne, Konstebo Kelvin Muturi anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Rangwe alikamatwa kwa kushukiwa kumnajisi msichana wa miaka 15 wa Kidato cha Kwanza.

“Wakati mshukiwa alipokuwa katika zamu ya usiku, inaaminika aliingia katika seli ambayo msichana alikuwepo, kisha akamfungulia na kumpeleka nyumbani kwake ambapo inashukiwa alimnajisi kabla ya kumwambia arudi katika seli,” alisema Mkuu wa DCI Kaunti ya Homa Bay, Bw Daniel Wachira.

Katika Kaunti ya Mombasa, msichana wa miaka 16 alisimulia jinsi alivyotekwa nyara na kunajisiwa na maafisa wawili wa polisi eneo la Nyali.

Msichana huyo alisema alikuwa akielekea kwa nyanyake wakati polisi walipomwamuru kuingia katika gari lao, wakamtishia kwa bastola kisha wakampeleka ufuoni ambako walimtendea unyama.

Ripoti ya NICHOLAS KOMU, IAN BYRON, AMINA WAKO na VALENTINE OBARA

Polisi motoni kumumunya mamilioni ya bima wakidai walikatwa mikono na miguu

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wa polisi wa utawala waliopokea Sh2.4milioni kwa kudanganya kampuni ya bima kwamba walikatwa miguu na mikono kwenye ajali wameshtakiwa katika Mahakama ya Milimani Nairobi.

Konstebo Dominic Lusweti Masengeli na David Ichere Maina walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Peter Ooko.

Walikanusha mashtaka 12 ya upokeaji pesa kwa njia ya udanganyifu na kughushi stakabadhi kuhusu ajali hiyo.

Konst Masengeli aliwakilishwa na wakili Bryan Khaemba, aliyestaafu mwaka huu kazi ya uhakimu.

Bw Khaemba alikuwa anahudumu katika mahakama ya Kiambu. Aliomba aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.

Bw Khaemba alimsihi hakimu atilie maanani kuwa mshtakiwa huyo ni afisa wa polisi asiye na cheo, yeye ni ni Konstebo tu na mshahara wake ni mdogo.

“Mshtakiwa huyu yuko katika kile kiwango cha maafisa wa polisi wasio na cheo. Hawezi kupata dhamana inayozidi Sh100,000,” alisema Bw Khaemba.

Wakili huyo aliomba mahakama itumie mamlaka yake ipasavyo na kuwaachilia kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.’

Mahakama iliwaachilia washtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000 kila mmoja na kuamuru kesi isikizwe Machi 16, 2020.

Kesi itatajwa Desemba 17 2019 upande wa mashtaka ueleze ikiwa umewakabithi washtakiwa nakala za ushahidi.

Shtaka la kwanza dhidi ya washtakiwa lilisema kati ya Septemba 22 2018 na Septemba 5 2019 walifanya njama za kuibia kampuni ya Bima ya Pioneer Sh2,440,320.

Shtaka la pili lilisema mnamo Septemba 5,2019 alipokea kutoka kwa kampuni ya Bima ya Pioneer Sh2,440,320.

Shtaka lilisema washtakiwa hao walidanganya Masengele alipata majeraha mabaya katika ajali iliyotokea kaunti ya Kitui.

Mahakama ilifahamishwa wawili hao waligushi ujumbe wa polisi kuhusu ajali hiyo ulipeperushwa na Kamanda wa Polisi eneo la Mwingi.

Hakimu alifahamishwa mnamo Julai 10 2019 katika afisi za kampuni ya Bima ya Pioneer Assurance barabara ya Harambee wakiwa na nia ya kulaghai walipeana ujumbe feki kuhusu ajali hiyo kwa Bi Irene Njagi wakidai umetayarishwa na kamanda huyo.

Pia walishtakiwa kwa makosa ya kujitengenezea cheti cha ajali Ref:P/AL807/0004550 wakidai kimetayarishwa na Idara ya Polisi.

Wananchi wakamata na kutandika polisi walevi kisiwani

KALUME KAZUNGU na JOSEPH NDUNDA

POLISI kisiwani Lamu walilazimika kutimua umati uliokuwa ukiwatandika wenzao wawili waliokamatwa na kufungwa kwa kamba na raia kwa madai ya kuhangaisha watu wakiwa walevi.

Maafisa hao yadaiwa walikuwa wamekunywa pombe ya mnazi katika kijiji cha Mararani kinachotambulika kwa biashara ya vileo vya kienyeji.

Yadaiwa wakiwa wanapepesuka, polisi hao waliovaa kiraia walianza kuhangaisha wakazi kwa kuwalazimisha kujitambulisha kwa kuonyesha vitambulisho vyao vya kitaifa.

Waliokaidi amri ya maafisa hao walitandikwa, jambo lililowakasirisha wakazi ambao walikusanyika na kuwapiga maafisa hao. Baadaye waliwafunga kamba mikononi na kuwaitia polisi wenzao kuwachukua.

Kiongozi wa Nyumba Kumi kijijini humo, Bw William Diwa, alisema kundi la polisi waliobeba bunduki na marungu liliwasili na kuanza kuwapiga wanakijiji kabla ya kuwakamata zaidi ya 10 na kuwapeleka kituo cha polisi cha kisiwa cha Lamu.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alithibitisha tukio la kupigwa kwa maafisa wa polisi eneo la Mararani na akasema tayari uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanzishwa.

“Mmoja wa polisi anadai kuibiwa Sh7,000 wakati wa tukio hilo ilhali kijana mmoja akidai kupokonywa simu yake ya mkononi na maafisa hao. Wote wamekamatwa na kufikishwa kituoni kuandikisha taarifa huku uchunguzi ukiendelea,” akasema Bw Macharia.

POLISI WATEKAJI

Jijini Nairobi, Idara ya DCI jana ilipata agizo la mahakama la kuwazuilia maafisa wawili wa polisi waliokamatwa katika mtaa wa Eastleigh mnamo Jumamosi kwa jaribio la kumteka nyara polisi mwenzao.

Hakimu Mwandamizi wa Makadara, Stephen Jalang’o aliruhuru polisi kuwazuilia Abdikadir Daiche na Ali Shukri Galgalo katika kituo cha polisi cha Pangani kwa siku saba ili wakamilishe uchunguzi.

Daiche ni afisa anayefanya kazi katika kituo cha polisi cha Muthaiga huku Galgalo akihudumu katika kituo kidogo cha polisi cha Quarry eneo la Embakasi.

Wawili hao walikamatwa gari wanalodaiwa kuteka nyara lilipokwama mwendo was saa saba za usiku.

Wanadaiwa walikuwa wameteka gari la dereva wa Uber ambaye ni afisa mwenzao wa wa polisi mara baada ya kushukisha abiria kwenye barabara ya Juja, eneo la Pangani.

Idadi ya maafisa wa usalama wanaokamatwa kwa kuhusika katika visa vya uhalifu imekuwa ikiongezeka katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Polisi wasifiwa kwa juhudi za kuzima uhalifu

KALUME KAZUNGU na LUCY MKANYIKA

TUME ya Huduma kwa Polisi nchini (NPSC) imepongeza juhudi zinazoendelezwa na maafisa wa vitengo mbalimbali vya usalama katika kukabiliana na wahalifu.

Mwenyekiti wa NPSC, Bw Eliud Kinuthia, alisema kupitia juhudi hizo, Lamu kwa sasa ni miongoni mwa maeneo yanayoshuhudia amani na utulivu nchini.

Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu mwishoni mwa juma, Bw Kinuthia aliwataka wageni, watalii na wawekezaji ambao wamekuwa wakisitasita kutembea na hata kuwekeza eneo hilo kwa sababu za kiusalama kubadili fikra zao kwani Lamu iko na usalama wa kutosha.

Akitaja sherehe ya Maulid iliyoandaliwa mjini Lamu na kukamilika Ijumaa, Bw Kinuthia alisema hafla hiyo ilivutia maelfu ya wageni na watalii kutoka sehemu mbalimbali za nchi na ulimwenguni waliofika Lamu kujumuika na wenyeji katika maadhimisho ya hafla hiyo.

Aliwasifu maafisa wa usalama wakiwemo wanajeshi wa nchi kavu (KDF) na wale wa vitengo mbalimbali vya polisi ambao wamejitoa kikamilifu na hata kuhatarisha maisha yao katika kudhibiti usalama wa Lamu.

“Niko na furaha kubwa jinsi Lamu ilivyodhibitiwa kiusalama. Kuna amani ya kutosha ikilinganishwa na miaka iliyopita. Ninawashukuru maafisa wetu wa usalama wanaoendeleza operesheni ya Linda Boni kwenye msitu wa Boni kwa kujitolea mhanga katika kudhibiti usalama eneo hili.

“Ningewasihi wawekezaji na watalii ambao wamekuwa wakihofia kutembea Lamu kuondoa shaka. Lamu ni shwari. Ni amani tupu hapa,” akasema Bw Kinuthia.Mwenyekiti huyo wa tume ya kuajiri polisi aidha alisema serikali itaendelea kujitolea kikamilifu katika kudhibiti usalama kote nchini ili maendeleo yaafikiwe hata zaidi.

Operesheni ya Linda Boni ilizinduliwa Septemba, 2015 baada ya kuzidi mashambulizi na mauaji ya mara kwa mara yaliyokuwa yakitekelezwa na magaidi wa Al-Shabaab dhidi ya raia na walinda usalama kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu.

Kwingineko, zaidi ya familia kumi zinakadiria hasara baada ya nyumba zao kuharibiwa na maporomoko ya udongo katika kijiji cha Sungululu, kaunti ndogo ya Wundanyi, Taita Taveta.

Familia hizo ziliepuka mauti Ijumaa usiku baada ya udongo kuzika nyumba zao na baadhi ya mifugo na mali zingine.Wakaazi hao wanakadiria maafa hayo, huku wakisalia bila makao kutokana na mkasa huo.

Milima ya Taita imekuwa ikishuhudia mvua nyingi tangu wiki iliyopita. Wenyeji sasa wanaishi kwa hofu wakihofia maafa zaidi, huku mvua nyingi ikiendelea kunyesha katika eneo hilo.

Bi Linet Nyambu alisema kuwa alinusurika kifo baada ya kufunikwa na udongo huo. Alisema kuwa watoto wake walimuokoa baada ya kuangukiwa na udongo usiku huo.

“Nilikuwa nasaidia kuondoa vyombo ndani ya nyumba yangu ndio udongo ukaporomoka juu yangu,” akasema nyanya huyo wa miaka 70.Mwenyeji mmoja Bw Moses Mwanake alisema kuwa mifugo na kuku walikuwa wamefunikwa na udongo.

Alisema kuwa hawana mahali mbadala pa kuhamia huku mvua ikiendelea katika eneo hilo. Familia hizo sasa zimeitaka serikali kuwasaidia ili waweze kujenga nyumba zao tena.

EACC yatofautiana na polisi kuhusu ufyatulianaji risasi na hongo

NA JUSTUS OCHIENG’

TUME ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi(EACC) na polisi wametofautiana vikali kuhusu kisa cha kupigwa risasi wa maafisa wa tume hiyo waliokuwa wakiendesha operesheni ya kuwanyaka maafisa wa trafiki kuhusu hongo mjini Kisumu.

Maafisa hao wa tume hiyo walikuwa wamevamia mzunguko wa Mamboleo kwenye barabara ya Kisumu-Kakamega ambapo polisi walikuwa wakitekeleza wajibu wao.

Juhudi za maafisa wa EACC za kuwanyaka polisi waliodaiwa walikuwa wakipokea hongo ziliishia ufyatulianaji wa risasi huku polisi wawili wakinyakwa wakati wa kisa hicho.

Maafisa wa EACC pia walikuwa wameandaa operesheni kama hiyo katika kituo cha kibiashara cha Riat karibu na uwanja wa ndege wa Kisumu.

Kwenye kisa cha Mamboleo, afisa wa polisi wa trafiki kwa jina Gladys Chemutai alisalia na majeraha ya risasi kwenye mguu wake wa kulia huku mwenzake Fredrick Matunda pia akisalia na majeraha kwenye goti lake.

Afisa mwngine kwa jina Marwa Mwita naye alikamatwa. Kando na maafisa hao, polisi wengine wa trafiki waliokamatwa ni Meshack Munyendo, Wesley Koech na Benjamin Tuwei. Watano hao bado hawajafikishwa mahakamani, wiki moja baada ya kukamatwa.

Kulingana na Mkuu wa EACC ukanda wa Nyanza Aura Chibole, Bi Chemutai hakuwa kati ya walionyakwa na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Avenue baada ya kufanyiwa upasuaji mguuni.

Bw Matunda pia yupo kwenye hospitali hiyo akiganguliwa. EACC tayari imewaondolea lawama maafisa wake kuhusiana na tukio hilo na kuwashutumu polisi wa trafiki kwa kuwapiga risasi maafisa wenzao.

Bw Chibole wikendi alikuwa na wakati mgumu kueleza namna kisa hicho kilivyotokea, akisema tu kwamba bunduki zote za maafisa waliohusika zimetwaliwa ili kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu kujua ni ipi iliyotoa risasi iliyomdhuru Bi Chemutai.

“Maafisa wetu hawakufyatua risasi. Hayo ni madai ya polisi wa trafiki japo bunduki zote zilizotumika zimetwaliwa kufanyiwa uchunguzi wa kitaalam,” akasema Bw Chibole.

Kulingana na ripoti ya tukio hilo katika kituo cha polisi cha Kondele iliyoonekana na Taifa Leo, maafisa wa EACC wamehusishwa na ufyatulianaji wa risasi kama njia ya kuwaadhibu polisi wa trafiki wakati wa kukamatwa kwao.

Ripoti hiyo ya OCS wa Kondele James Nderitu iliyoandikwa kwa makao makuu ya polisi inasema kwamba maafisa wa EACC ndio walifyatua risasi kama njia ya kuwatia maafisa hao uoga ndipo wawakamate.

Taifa Leo imebaini kwamba Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu(DCI) imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo huku Bw Chibole akiomba muda zaidi wa kumalizwa uchunguzi kwenye bunduki zilizotwaliwa.

Baadhi ya mashahidi tayari wameandikisha taarifa na DCI , taarifa zinazodaiwa kulaumu EACC kutokana na kosa hilo.

Maswali pia yameibuliwa kuhusu kucheleweshwa kwa mchakato wa kuwafikisha mahakamani maafisa watano wa polisi siku tano baada ya kisa hicho huku ikisemekana EACC bado haijaamua itawashtaki kwa kosa lipi.

Hata hivyo, Mkuu wa Polisi eneo la Nyanza Dkt Vincent Makokha alisema watashtakiwa mahakamani baada ya afisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma kuipa EACC ruhusa.

Rais Kenyatta aagiza timu za uokozi KDF na idara ya polisi zipelekwe Pokot Magharibi

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ameagiza timu za uokozi kutoka kwa wanajeshi wa ulinzi Kenya (KDF) na idara ya polisi kupelekwa katika Kaunti ya Pokot Magharibi iliyokumbwa na maporomoko ya ardhi katika juhudi za kuzuia maafa zaidi.

Kufikia Jumamosi jioni watu zaidi ya 30 walikuwa wamethibitishwa kufariki katika mkasa huo, kulingana na ripoti za Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi, Rais Kenyatta ametoa hakikisho kuwa serikali yake inafanya kila iwezalo kutoa msaada kwa waathiriwa kwa ushirikiano na mashirika mengine.

“Nimeamuru kwa walinda usalama wetu wapelekwe katika maeneo yaliyoathirika na mkasa wa maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Pokot Magharibi ili kuchukua hatua za kuokoa maisha. Operesheni hiyo itaendelezwa na Wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya (KDF), maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na wahudumu kutoka Idara ya Mipango Maalum hadi hali ya kawaida itakapoanza kushuhudiwa,” Rais amesema.

Aidha, kiongozi wa nchi amesema amepokea habari za kuhuzunisha kuhusu maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Hali hiyo imesababishwa na mvua iliyopitiliza inayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali humu nchini.

“Ninawapa pole waliopoteza wapendwa wao katika mkasa huo na nawatakia waliojeruhiwa na wamepelekwa katika hospitali mbalimbali, afueni ya haraka,” amesema Rais Kenyatta.

Mkasa huo ulitokea mwendo wa nane na nusu alfajiri – yaani usiku wa manane kuamkia Jumamosi – kulingana na Shirika la Msalaba mwekundu na maafisa wa utawala katika maeneo yaliyoathirika. Mojawapo ya maeneo hayo ni kijiji cha Nyarkulian katika kaunti ya ndogo ya Pokot Kusini ambako familia moja ya watu wanane iliangamia walipozikwa hai na matope katika nyumba yao.

MAKALA MAALUM: Idara ya polisi haijapiga hatua kubwa katika kuleta mageuzi

Na STELLA CHERONO

SWALI la iwapo mageuzi ambayo yamekuwa yakitekelezwa katika idara ya polisi yamefanikiwa au la bado ni kitendawili, iwapo matukio yanayoendelea kuzingira maafisa hao wa usalama nchini ni ya kuzingatiwa.

Aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet ambaye kwa sasa ni Waziri Msaidizi, alipigia debe mageuzi hayo wakati akiondoka ofisini baada ya kukamilisha muda wake wa kuhudumu kulingana na Katiba.

Bw Boinnet alisema idara hiyo ilishuhudia mageuzi makubwa chini ya uongozi wake. Alitaja kuunganisha kwa idara za polisi wa kawaida na wale wa utawala kama mojawapo ya ufanisi alioafikia, akisema hilo lilisaidia kufanikisha utoaji wa huduma bora na kuhakikisha kwamba majukumu ya vitengo hivyo viwili havigongani.

Mtaala

Mafanikio mengine aliyoyataja ni kubadilishwa kwa mtaala wa mafunzo kwa makurutu wanaoajiriwa kama polisi, kuimarika kwa mbinu ya kuhakikisha kwamba maslahi ya maafisa yanaangaliwa, makazi bora na kupewa huduma za bima ya matibabu kwa polisi binafsi pamoja na familia zao wanapougua.

“Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imepitia mageuzi makubwa kutoka kwa miundombinu bora hadi mishahara ya polisi, vifaa, mavazi na kujihami kwa maafisa kupambana na utovu wa usalama unaochipuka mara kwa mara nchini,” akasema Boinnet alipokuwa akitoa hotuba hiyo ya mwisho.

Msingi wa kauli ya Boinnet ulitokana na sheria iliyopitishwa mwaka 2011, ambayo ilitoa mwongozo jinsi ambavyo idara hiyo inaweza kuasi dhana ya kutumia mamlaka kuadhibu raia bila makosa, na badala yake polisi kufanya kazi yao kulingana na kanuni za taaluma yao.

Hata hivyo, miaka minane baada ya mchakato wa mageuzi hayo kung’oa nanga, polisi wengi bado wanahangaika na kupitia changamoto tu kama zamani, licha ya serikali kutumia zaidi ya Sh10.3 milioni kwenye bajeti ya mwaka 2015-2018 kuwajengea makazi mapya.

Ni kutokana na hayo ambapo mashirika ya kijamii, wachanganuzi wa masuala ya usalama na watetezi wa haki za kibinadamu wanaamini kwamba, mageuzi katika idara ya polisi yamefeli pakubwa licha ya serikali kuwekeza mabilioni ya fedha kubadilisha kitengo hicho muhimu cha usalama.

Kulingana na mwenyekiti wa kundi ambalo limekuwa likifuatilia mageuzi hayo PRWG-K, Bw Peter Kiama, hakuna hatua kubwa zilizopigwa katika mageuzi yaliyolengwa, kutokana na uhasama na ubinafsi wa wakuu wa polisi. Hii ni licha ya baraza la mawaziri mnamo 2009 kupitisha ripoti ya Ransley iliyotoa mwongozo wa kufanikisha mageuzi katika idara hiyo.

“Kuna tabia za uhalifu zinazoendelezwa katika idara ya polisi. Uchunguzi, mohajiano na ukaguzi wa maafisa wa polisi ambao ulipangwa kutekelezwa ili kusafisha idara hiyo, ulikosa kuzaa matunda. Asasi ambazo zinaangazia utendakazi wa polisi zimekuwa zikisimamiwa na watu wanaoongozwa na maslahi yao ya kibinafsi, na kusahau kutekeleza majukumu yatakayosaidia kuboresha idara hiyo,” akasema Bw Kiama.

Katika muda wa miezi michache iliyopita, Wakenya wameshuhudia kukamatwa kwa maafisa wa polisi ambao walihusika katika visa vya wizi wa fedha katika benki, hoteli na barabarani. Wengine nao walipatikana na pembe za ndovu, miongoni mwa maovu mengine.

Tume kama Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi (Ipoa), Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) na asasi ya Huduma kwa Polisi (NPS), zote zimefeli kutekeleza wajibu wao. Utepetevu huo umekashifiwa mno na mashirika ya umma pamoja na yale ya kutetea haki za kibinadamu chini ya mwavuli wa PRWG-K, ambazo zimelaumu idara ya polisi kwa ubadhirifu wa pesa za mlipa ushuru bila kutimiza malengo yoyote.

Jeruhi mwanafunzi

Kudhihirisha namna idara ya polisi bado ni ile ile, maafisa watano wa usalama Jumatatu wiki hii waliwapiga na kuwajeruhi vibaya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), waliokuwa wakishiriki maandamano chuoni humo.

Watano hao walinaswa kwenye video wakiwaangushia wanafunzi hao kipigo kikali, na kumfanya Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i pamoja na Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) wa sasa Bw Hillary Mutyambai kushutumu kitendo hicho. Vile vile, waliwasimamisha kazi polisi hao ambao walikuwa wameshutumiwa vikali kwenye mitandao ya kijamii kwa ukatili wao.

Kupitia taarifa, Dkt Matiang’i alieleza kughadhabishwa na jinsi maafisa hao walikabili wanafunzi ambao walikuwa tu wakilalamikia ukosefu wa usalama ndani na nje ya chuo hicho.

“Nimefuatilia matukio katika chuo cha JKUAT na nimeshangazwa na mkondo wa mambo. Polisi walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wanafunzi hao kinyume na amri ya idara,” akasema Dkt Matiang’i.

IPOA nayo ilishutumu kisa hicho na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya maafisa waliohusika.

“IPOA inakemea vikali tukio la JKUAT ambapo polisi walinaswa kwenye kamera wakiwapiga wanafunzi bila huruma,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa IPOA Anne Makori.

Hata hivyo, IPOA imekuwa na vita vya ndani kwa ndani vilivyosababisha kutimuliwa kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Maina Njoroge, miezi mitano tu baada ya kuchukua wadhifa huo kutoka kwa Joel Mabonga ambaye alistaafu mwaka jana.

Utendakazi

Ni kutokana na vita hivyo ambapo maafisa wa PRWG-K wameeleza wasiwasi wao kwamba, utendakazi huru wa mamlaka hiyo unavurugwa na maafisa wanaochimbiana na kuendeleza uhasama kati yao.

“Bodi ya IPOA haiwajibiki ipasavyo. Wameangazia sana nyongeza ya mishahara, ulinzi na masuala mengine ambayo yanawahusu binafsi,” alieleza Bw Kiama.

Anaongeza kwamba, mahojiano na uchunguzi wa polisi ambao unalenga kuleta uwajibikaji katika idara hiyo, ni kati ya mambo yaliyofeli kabisa.

Ni wiki jana tu ambapo maafisa wa polisi waliokuwa na kesi baada ya kuhojiwa na NPSC, walirejeshewa kazi zao licha ya Sh800 milioni kutumika kuwachunguza na kuwasimamisha kazi.

NPSC pia ilitangaza kwamba maafisa hao hawatachukuliwa hatua zozote za kinidhamu kutokana na uchunguzi huo uliofanywa kabla yao kuingia ofisini.

Mwenyekiti mpya wa NPSC Eliud Kinuthia alisema tume hiyo imeamua kutupilia mbali mapendekezo ya mtangulizi wake Johnstone Kavuludi dhidi ya maafisa hao, na kwamba kuhojiwa na kuchunguzwa kwa maafisa wa vyeo mbalimbali umesimamishwa mara moja.

“Tutawapa nafasi nyingine ya kujitetea. Kulingana na maafisa wapya wa tume, mapendekezo yaliyotolewa baada ya kuhojiwa na kuchunguzwa kwao hayana mashiko na yametupiliwa mbali,” akasema Bw Kinuthia.

Mageuzi katika idara ya polisi, ambayo yana nia ya kutumia teknolojia katika idara hiyo, yametumia zaidi ya Sh450 bilioni kuwekeza miundomsingi ya kisasa kwenye idara hiyo.

Miundombinu hiyo ni katika sekta ya mawasiliano ya kisasa, magari ya polisi, vituo vya kuongoza operesheni, helikopta mpya kati ya mingine.

Mashirika ya umma na yale ya haki za binadamu kupitia mwavuli wao wa PRWG-K, sasa yanapendekeza kutekelezwa kwa kifungu cha sheria ya Polisi kinachompa Inspekta Jenerali mamlaka ya kusimamia bajeti ya maafisa wake, ili kuhakikisha kila kituo cha polisi na vitengo vyote viko na fedha za kutosha kuendesha shughuli zao.

#JkuatLivesMatter: Majina ya polisi katili yatolewa

NA MARY WANGARI

KISA cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) aliyepigwa kikatili na polisi kimechukua mkondo mpya huku Mamlaka Huru ya Uangalizi (IPOA) ikiwatambua maafisa wote 50 waliohusika na oparesheni hiyo na baadhi ya majina ya maafisa hao kutangazwa.

Haya yamejiri huku Tume ya Kitaifa kuhusu Huduma ya Polisi (NSPC) hatimaye ikitaja majina ya maafisa wanne walioibua hasira nchini na kimataifa waliponaswa kwenye video iliyosambazwa mno mitandaoni, wakimpiga kinyama mwanafunzi ambaye hakuwa amejihami.

Akihutubia wanahabari jana, Mwenyekiti wa NSPC Bw Eliud Kinuthia aliwatambulisha maafisa hao kama Koplo George Wathania, Makonstebo wa Polisi Jonathan Kibet na Boniface Muthama.

Bw Kinuthia alisema kuwa afisa wa nne alikuwa bado hajatambuliwa na kufafanua kuwa Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Thika, Koplo Mathew Masaga aliyeongoza oparesheni hiyo, alikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa katika kisa hicho.

Kulingana na taarifa ya Tume ya Kungazia Utendakazi wa Polisi (IPOA) iliyotiwa sahihi na Mwenyekiti, Anne Makori, maafisa hao wanne wamesimamishwa kazi huku uchunguzi kuhusu kisa hicho ukiendela.

Ripoti hiyo ilisema kuwa wanafunzi wasiopungua 22 walijeruhiwa wakati wa kisa hicho.

“IPOA imewasiliana na kuchukua taarifa kutoka kwa walioshuhudia kisa hicho. Kutokana na ripoti hii, mamlaka sasa imeanza uchunguzi kamili kuhusu tukio hilo,” akasema Bi Makori.

Haya yamejiri siku moja tu baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi, Hilary Mutyambai kutoa amri ya kuwakamata maafisa hao walionaswa katika videoya kisa hicho.

Mnamo Jumanne, Wakenya pamoja na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za kibinadamu walijitosa mitandaoni kuelezea hasira zao kuhusu kisa hicho cha kushtusha ambapo maafisa wanne wa polisi walinaswa wakimpiga kinyama mwanafunzi.

Tukio hilo lilijiri wanafunzi wa JKUAT walipokuwa wakishiriki maandamano ya amani nje ya chuo hicho wakilalamikia ukosefu wa usalama chuoni humo.

#JkuatLivesMatter: Polisi waliopiga mwanachuo watemwa

MARY WANGARI Na MARY WAMBUI

POLISI wanne walionaswa kwenye video wakimpiga kinyama mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) Jumatatu wakati wa maandamano ya amani wamesimamishwa kazi.

Kulingana na taarifa kutoka kwa msemaji wa polisi, Charles Owino kwa vyombo vya habari, “maafisa wawili wanatoka Kituo cha Polisi cha Makongeni huku mmoja akitoka Kituo cha Polisi cha Juja.”

Haya yamejiri saa chache tu baada ya kisa hicho kuibua hisia kali nchini na kimataifa.

Wakenya waliojawa na ghadhabu walimtaka Waziri wa Usalama wa Nchi Fred Matiang’i na Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambia kuwachukulia hatua kwa haraka maafisa waliohusika.

Punde baada ya video hiyo iliyoonyesha maafisa wa polisi waliovalia magwanda yao wakimvamia na kumpiga kinyama mwanafunzi huyo, Allan Omondi, Dkt Matiang’i alijitosa mitandaoni na kuahidi kuwachukuliwa hatua wahusika katika muda wa saa 24.

“Nimetazama matukio ya JKUAT leo kwa wasiwasi usioelezeka. Utumiaji nguvu kwa polisi wafafanuliwa wazi katika Sheria kuhusu Polisi wa Kitaifa. Nimezungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi na sote tumekubaliana kuwa hatua kali na thabiti zitachukuliwa kwa afisa yeyote aliyetumia nguvu kupita kiasi, katika muda wa saa 24 zijazo,” aliandika Waziri Matiang’i kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Dkt Matiang’i alisema hayo akijibu kilio cha maelfu ya Wakenya waliofurika mitandaoni kulaani kisa hicho cha kinyama kilichowakumba wanafunzi wa JKUAT walipokuwa wakilalamikia ukosefu wa usalama chuoni humo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za kibindamu la Amnesty International lilijiunga na Wakenya kulaani kisa hicho.

Irungu Houghton ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo alikemea visa vya ukatili wa polisi katika maandamano akisema: “Ukatili wa polisi katika maandamano ni sharti ukome. Ni vigumu kwa Jamhuri kutofautisha wahuni wakiwa wamevalia au bila kuvalia magwanda ya polisi.

“Maafisa wanaokiuka kanuni za taaluma yao ni sharti waadhibiwe binafsi kwa kukosa nidhamu, kusimamishwa kazi na kulazimishwa kuwalipa wahasiriwa.”

Tukio hilo liligonga vichwa vya habari nchini na kimataifa baada ya polisi watatu kumpiga vibaya mwanafunzi ambaye hakuwa amejihami huku afisa mmoja akionekana akimponda kichwa kijana huyo aliyelala chini akijaribu kujikinga kwa mikono yake.

Wakenya walijitosa kweye mtandao wa kijamii wa Twitter jana ambapo kupitia heshitegi #jkuatlivesmatter na #stoppolicebrutality, walilaani vikali kisa hicho.

“Polisi wana nguvu ya kumpiga mateke mwanafunzi ambaye hana silaha lakini hawawezi kuwakamata majambazi Kasarani,” alisema Papi Chulo.

“Wahuni hao waliovalia sare ni sharti wakamatwe! Hakuna ufafanuzi wowote utaelezea ukatili huu,” Raymond Ofula alichangia.Baadhi ya Wakenya walihoji kuwa ni vitendo kama hivyo vya polisi vinavyofanya raia kutowaheshimu na kukosa imani na idara hiyo ya utekelezaji sheria nchini.

“Ni vigumu kuheshimu afisa wa polisi Mkenya. Ama ni fisadi, hana utu na ni katili na kwa jumla hafahamu chochote kuhusu wajibu wake,” alihoji Elijah Mokua.

“Hawa ndio maafisa wa polisi tunaoaminia maisha yetu? Haiwezekani. Ni sharti wafurushwe kutoka NPS na waadhibiwe,” alieleza Victor Kipng’eno.

Polisi wageuka wanyama ghafla wakizima maandamano JKUAT

Na Leonard Onyango

MAAFISA wa polisi waliokuwa wakizima maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha JKUAT mjini Juja, Kaunti ya Kiambu Jumatatu waliacha kuwa binadamu na kugeuka wanyama wasio na akili.

Katika moja ya video iliyotiwa katika mitandao ya kijamii, polisi wanne wakishirikiana na wahuni wanaonekana wakimkanyaga mwanafunzi wa kike na kumpiga kila sehemu ya mwili, hata kichwani, kwa bakora na mateke akiwa amelala chini.

Mmoja wa polisi hao wanyama alikuwa ameshikilia bunduki na wenzake wakiwa na bakora.

Wengine walimkanyaga na kurukaruka kwenye kichwa chake huku wengine wakimshambulia kwa bakora sehemu zingine za mwili.

Video hiyo imezua hisia kali mitandaoni miongoni mwa Wakenya ambao wanataka maafisa hao wa polisi wasiokuwa na utu wakamatwe, wafutwe kazi kisha wafikishwe mahakamani.

Wanafunzi hao walikuwa wakilalamikia kuzorota kwa usalama katika eneo hilo. Hii ni baada ya wahalifu kudunga kisu mmoja wa wanafunzi alipokuwa akielekea chumba cha malazi.

Polisi majambazi

Na BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

WAKENYA wana kila sababu ya kuhofia uhai na usalama wao kwa jumla baada ya kuibuka kuwa magenge ya wahalifu yanayowahangaisha yanahusisha maafisa wa polisi.

Baadhi ya maafisa waliopatiwa mafunzo kuwalinda raia, wanatumia mafunzo hayo kuongoza magenge ya majambazi na wanakodiwa kutekeleza mauaji au kukodisha silaha zao kutumiwa na majambazi kuiba na kuua Wakenya.

Hali ni mbaya hivi kwamba maafisa hao wamekuwa na ujasiri wa kukaidi maagizo ya wakubwa wao kinyume na kanuni za kikosi cha polisi.

Katika kisa cha hivi punde, afisa wa kikosi cha kukabiliana na fujo (GSU), Anthony Kilonzo, alikamatwa na anazuiliwa na polisi, ili uchunguzi uendelee kuhusu kukiri kwake mahakamani kwamba alilipwa kutekeleza mauaji eneo la Katani.

Polisi walisema kwamba alikuwa mwanachama wa genge la majambazi wakiwemo maafisa wa usalama waliokuwa wakihangaisha wakazi wa Katani na maeneo yaliyo karibu.

Ilibainika kuwa haikuwa mara ya kwanza kwa afisa huyo kutekeleza mauaji. Alihusishwa na mauaji ya afisa wa polisi katika uwanja wa ndege wa Wilson mapema mwaka 2019.

Aidha, polisi waligundua kuwa alikuwa amesajili vijana raia katika genge lake la majambazi na kuwapa silaha hatari.

Mmoja wao aliuawa kwenye ufyatulianaji wa risasi na wapelelezi mtaani humo mapema wiki huu na silaha hatari zikapatikana.

Wiki jana, maafisa wa upelelezi walimkamata afisa wa polisi mtaani Mihango, Embakasi ambaye amekuwa akihusishwa na visa vya wizi.

Afisa huyo, David Odhiambo, alikuwa kiongozi wa genge la majambazi ambao wapelelezi walihusisha na visa vya uhalifu nchini. Sare kadhaa za polisi zilipatikana katika nyumba yake.

Polisi pia walipata risasi 30, jaketi mbili za kukinga risasi, vitambulisho vya kitaifa, leseni za kuendesha gari, noti feki za thamani ya Sh29,000 na dola za Amerika 8,800 na vitabu kadhaa vya rekodi za polisi, ishara kwamba afisa huyo alikuwa akishiriki uhalifu kwa muda mrefu.

Wizi Eastleigh

Mapema Oktoba 2019 maafisa wa idara ya upelelezi waliwakamata maafisa watano wa polisi waliohushishwa na wizi wa Sh6 milioni kutoka kwa wafanyabiashara wawili katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi.

Wao ni Simon Mwaniki, Catherine Waithera Wairimu wa vyeo vya konstebo na Wilson Cheruiyot, Daniel Kiokorir na Alex Kandie wa cheo cha koplo. Maafisa hao wote wanahudumu katika kituo cha polisi cha Kayole, Nairobi.

Inadaiwa walitekeleza wizi huo kwa ushirikiano na raia mmoja wa Cameroon, Esome Baptist na Bi Petronila Njeri Ngaara ambaye ni mhudumu katika duka lililo kituo cha polisi cha Kayole.Katika kisa kingine kilichotokea mwezi Septemba 2019,

Afisa mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na maafisa watatu wa polisi wa utwala (AP) walikamatwa kuhusiana na wizi wa Sh72 milioni katika mtambo wa ATM wa Benki ya StanChart katika mtaa wa Nairobi West.

Maafisa wa DCI walisema waliwakamata AP hao Simon Gachuhi Karuku na mkewe Carolini Njeri Waithira katika eneo la Thogoto, kaunti ya Kiambu. Baada ya kuhojiwa, wawili hao waliwaelekeza polisi nyumbani kwa dadake Karuku, Wangari Karuku, ambaye ni afisa wa KDF katika kambi ya jeshi ya Kahawa, ambaye walimkabidhi pesa walizoiba.

Naye Wangari aliwaelekeza maafisa hao wa DCI kwa Bi Florence Wanjiru Karuku, ambaye pia ni afisa wa AP.

Mapema mwaka 2019 wapelelezi kutoka kitengo cha polisi wa kupambana na wahalifu sugu (SCPU) walipewa wajibu wa kumsaka afisa wa polisi wa Kiambu kwa tuhuma za kukodi bunduki yake kwa wahalifu.

Afisa huyo wa cheo cha Sajini Mkuu katika Kituo cha Polisi cha Kiambu alitoweka saa chache baada ya majambazi wawili kuuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Viwandani Nairobi na batola mbili zikapatikana.

Kizaazaa polisi kufurika kortini kuokoa mwenzao aliyetupwa seli

Na TITUS OMINDE na SETH MOIBEN

KIZAAZAA kilishuhudiwa katika mahakama ya Eldoret maafisa wakuu wa polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, walipofurika kortini kujaribu kumshawishi hakimu amwachilie mmoja wao aliyezuiliwa kwa kukosa kuheshimu agizo la mahakama.

Maafisa wapatao 10, wakiongozwa na kamanda wa polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Johnstone Ipara, walifika mahakamani ili kujaribu kumtetea mwenzao.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Eldoret, Linus Kaissan, aliamuru Bw Solomon Wamai ambaye anasimamia kituo cha polisi cha Eldoret Magharibi azuiliwe seli kwa kukosa kufuata agizo la mahakama kufikisha washukiwa wawili kortini.

Washukiwa hao walikamatwa kwa madai ya kupatikana na katoni zaidi ya 200 za sigara zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria.

Wakili wa washukiwa hao alipata agizo lililomtaka afisa huyo kuwafikisha washukiwa hao mahakamani Alhamisi.

Korti hiyo ilitoa amri Bw Wamai afike mahakamani kuelezea kwa nini alikosa kuwafikisha washukiwa hao alivyoagizwa.

Alipofika kortini, afisa huyo alikubali kwamba alikuwa amepokea agizo la mahakama kutoka kwa wakili wa washukiwa hao, Bw Collins Akenga.

Alipokuwa akijibu maswali, Bw Wamai alisema alishuku agizo hilo kwani lilikuwa na saini mbili tofauti.

Alipoulizwa na hakimu ni kwa nini alikaidi agizo hilo, alijitetea kwamba aliagizwa na kamanda wao, Bw Ipara, kutozingatia agizo hilo kwa sababu walishuku uhalali wake.

Juhudi za Bw Ipara kujaribu kumtetea afisa wake hazikufua dafu kwani hakimu huyo alishikilia kuwa afisa huyo alikuwa amekaidi amri ya mahakama na angezuiliwa hadi awafikishe washukiwa hao wawili kortini.

“Kwa heshima na unyenyekevu, tunaomba korti hii imwachilie mwenzetu kwani agizo la kwanza la mahakama liliiamuru washukiwa wazuiliwe kituoni kwa muda wa siku 14 ili uchunguzi unaoendelea ukamilike,” alirai Bw Ipara.

Licha ya hayo, mahakama ilishikilia msimamo wake wa kumzuia afisa huyo. “Nimeamuru kuwa afisa huyu azuiliwe kortini hadi pale atakapowafikisha kortini washukiwa hao. Mtu yeyote ambaye anakaidi agizo la mahakama lazima aadhibiwe,” hakimu alisema.

Maafisa wa polisi kortini walikuwa na wakati mgumu kumuamrisha mkubwa wao kuingia katika seli na badala yake wakamuacha azurure kortini wakubwa wao wakijikuna kichwa. Afisa huyo alipata afueni wenzake walipopata agizo la Mahakama Kuu kufuta agizo la hakimu.

Koplo Caroline Mango Atieno aachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi, Koplo Caroline Mango Atieno amekanusha mashtaka 20 yanayohusu kukosa kulipa zaidi ya Sh8 milioni za ushuru kutokana na biashara aliyofanya na Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).

Mango ambaye amefikishwa mahakamani jijini Nairobi ameachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni pesa taslimu.

Kesi imeratibiwa kusikizwa Novemba 28, 2019.

 

Tunaandaa habari kamili…

Polisi waliofutwa waamriwa warejeshe sare

Na KNA

POLISI wa akiba nchini (NPR) waliopokonywa silaha na serikali, sasa wameamrishwa kusalimisha sare zote walizo nazo.

Kamishna wa eneo la Bonde la Ufa, Bw George Natembeya alisema polisi yeyote wa akiba nchini ambaye bunduki yake ilitwaliwa na ambaye huenda alikuwa amepewa sare ya serikali, ni sharti arudishe.

“Wanaozurura wakiwa wamevalia sare wanajifanya tu kama NPR. Serikali imefunga ukurasa wa kikosi cha zamani cha KPR ambapo walioteuliwa walikuwa wakiishi katika jamii wakiwa na bunduki,” alisema kamishna huyo.

Akizungumza mjini Eldoret Ijumaa wakati wa ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na serikali kuu akiandamana na kamati ya maendeleo eneo hilo, Bw Natembeya alisema kikosi kipya cha NPR kitateuliwa na kupokea mafunzo na uteuzi wao hautafanywa kwa misingi ya eneo au kabila.

“Baada ya mafunzo polisi hao wa akiba wataishi kambini ambamo watasimamiwa na afisa mkuu wa polisi,” alisema.

Aidha, alitangaza kuwa watu wanaomiliki bunduki kinyume na sheria katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa walikuwa na juma moja pekee kusalimisha silaha hizo kwa hiari kabla ya kupokonywa kwa nguvu.

“Kuanzia wiki ijayo tutapiga kambi Baragoi eneo la Samburu, Baringo, Turkana na Bonde la Kerio kuchukua silaha zote haramu zilizo mikononi mwa Wananchi. Ningependa kuhimiza mtu yeyote eneo hili anayemiliki bunduki kinyume na sheria kuisalimisha kwa hiari kwa serikali kabla ya muda wa makataa kuisha,” alisema.

Mwanajeshi, polisi 3 ndani kuhusiana na wizi wa Sh72m

Na STELLA CHERONO

AFISA mmoja wa Jeshi la Kenya (KDF), na maafisa watatu wa polisi kutoka familia moja, wanazuiliwa kuhusiana na wizi wa Sh72 milioni kutoka benki ya Standard Chartered katika eneo la Nairobi West, Kaunti ya Nairobi.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema kuwa makachero walimkamata Bw Simon Gichuhi Karuku na mkewe, Bi Caroline Njeri, ambao wote ni maafisa wa polisi eneo la Thogoto, Kaunti ya Kiambu.

Makachero waliwakamata wawili hao katika afisi moja ya wakili, walikokuwa wameenda kumwagiza awasilishe ombi kortini kuzuia wasikamatwe.

Baada ya kukamatwa, washukiwa waliwapeleka makachero nyumbani kwa dada ya Bw Karuku, aliyetambuliwa kama Eunice Wangari Karuku. Bi Wangari ni mwanajeshi katika kambi ya kijeshi ya Kahawa jijini Nairobi. Bi Karuku ndiye alikabidhiwa pesa hizo.

“Afisa huyo alikuwa amesafiri mjini Nyahururu kuhudhuria mazishi,” walisema polisi.

Bi Wangari aliwaelekeza kwa dada yake, Bi Florence Wanjiru Karuku kuchukua fedha hizo. Bi Wanjiru pia ni afisa wa polisi ambaye alikuwa akilinda ATM ya Benki ya Equity, iliyo karibu na benki ya StanChart, wakati fedha hizo zilipoibwa.

Wakati polisi walipofika kwake, aliwaambia kuwa alipopata fedha hizo, alimpa mpenzi wake, aliyetambuliwa kama James Macharia, aliyetorokea sehemu isiyojulikana.

Makachero pia walipata gari aina ya Toyota Mark X, lenye nambari ya usajili KBX 779 kutoka kwa Bi Wangari, wanaloamini lilinululiwa kwa fedha hizo.

Wanne hao wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata, huku polisi wakiendelea kumsaka Bw Macharia, anayeaminika kuwa na fedha zilizobaki.

Wizi huo ulifanyika mnamo Septemba 5, ambapo kulingana na taarifa za walinzi, “ulitekelezwa na watu waliovalia sare za polisi wa utawala.”

Fedha hizo ziliibwa baada ya wafanyakazi wa kampuni ya G4S kuziweka kwenye mashine ya ATM.

Walinzi wa G4S walikuwa wamesafirisha fedha hizo kutoka makao yao makuu yaliyo katika eneo la Industrial Area hadi Benki ya Standard Chartered tawi la Nairobi West.

Wezi wadhaniwa polisi

Taarifa kutoka kwa walinzi hao zilisema kuwa walidhani kuwa wezi hao walikuwa polisi waliokuwa wamesindikiza fedha hizo.

Wezi hao walipakia fedha hizo katika magunia 13, na kuyaweka kwenye gari ndogo walilokuwa nalo na kuondoka.

Siku chache baada ya wizi huo, polisi waliwakamata maafisa wawili wa polisi waliotambuliwa kama Chris Ayienda na Vincent Owuor, waliopatikana na Sh7 milioni. Vilevile walipata gari.

Makachero pia walipata Sh1 milioni katika zizi la ng’ombe katika eneo la Lurambi, Kaunti ya Kakamega.

Mfanyakazi mmoja wa kampuni ya G4S aliyetambuliwa kama Bernard Sewanga, aliyekuwa ameenda mafichoni baada ya wizi huo pia alikamatwa.

Aidha, walipata Sh2.3 milioni katika nyumba ya Bi Mary Kyalo, mwenye umri wa miaka 60 katika Kaunti ya Machakos.

Mjukuu wake, Bernard Mwendwa pia alikamatwa.

Washukiwa wengine waliokamatwa kufikia sasa ni Musa Rajab, Abraham Mwangi Njoroge, Ascar Kemunto, Dancun Luvuka, Wilfred Nyambane, Natahn Njiru, Danmark Magembe, Boniface Mutua, Alexander Mutuku na Francis Muriuki.