Polisi wapoteza mamilioni ya wizi

Na BRIAN OCHARO

KUNDI la maafisa wa polisi limo mashakani baada ya kukosa kuwasilisha mahakamani Sh25.9 millioni ambazo zilikuwa sehemu ya zaidi ya Sh300 milioni zilizoibiwa kutoka kwa kampuni ya G4S mjini Mombasa miaka tisa iliyopita.

Kampuni hiyo ilikuwa ikisafirisha Sh313 milioni kutoka Mombasa hadi Nairobi wakati ziliibiwa, ikidaiwa wafanyakazi wa kampuni hiyo walipanga njama hiyo ya wizi.

Karatasi zilizowalishwa mahakamani zaonyesha polisi walipata pesa hizo kutoka kwa washukiwa lakini hawakuziwasilisha mahakamani kama ushahidi wakati watu wanane walishtakiwa.

Haya yaliwekwa wazi wakati Jacob Mutuku Musau, Sylvester Mbuli Mbuvi na Amos Mutuku Musyoka walifika katika mahakama hiyo kudai fedha hizo ambazo walisema kuwa, zilikuwa zao za biashara na walitaka warudishiwe kuendeleza biashara zao.

Watatu hao walimwambia Hakimu Mkuu Edna Nyaloti kwamba, hawakupatikana na hatia katika kesi hiyo baada ya kukamatwa miaka tisa iliyopita.

Kupitia kwa wakili wao Leonard Mbuvi, watatu hao waliambia mahakama kuwa, fedha hizo hazikuwa sehemu ya zile ambazo ziliibiwa kampuni ya G4S, bali zilikuwa zao za kufanyia biashara.

“Tumejaribu njia zote polisi waturudishie hizo pesa lakini wamekataa licha ya kuwa wanazihifadhi pesa hizo na bidhaa zingine za nyumbani ambazo walichukua katika makazi yetu,” watatu hao walisema.

Watu hao sasa wanataka afisa aliyekuwa akichunguza kesi hiyo, Bw Paul Chebet akamatwe na kufikishwa mahakamani ili kuelezea mahali zilipo fedha hizo.

Mahakama hiyo iliaambiwa kuwa, Bw Chebet amekuwa akidinda kufika mahakamani licha ya kupewa barua za kutaka afike kortini kujibu maswali kuhusu fedha hizo.

Afisa Mkuu wa Upelezi wa Jinai Anthony Mureithi alifika mahakamani na kusema kuwa, ni Bw Chebet anayeweza kuelezea zilipo fedha hizo kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa mchunguzi wa kesi hiyo.

Bi Nyaloti hata hivyo alikataa kutoa amri Bw Chebet akamatwe akisema kuwa, fedha hizo hazikuwasilishwa kortini hivyo basi mahakama yake haina mamlaka ya kutoa amri hiyo.

Hakimu huyo aliwauliza watatu hao watafute njia nyingine ya kufuatilia fedha hizo kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti au kwa kushtaki idara polisi.

Watatu hao ni miongoni mwa washukiwa watano ambao walishukiwa kuhusika katika wizi wa fedha hizo uliotekelezwa Februari 12, 2010.

Walishtakiwa pamoja na wafanyikazi wawili wa kampuni ya G4S Bw Sylvester Mbisi Mutua na Bw Humphrey Wekesa Wanjala.

Wengine ambao walikabiliwa na mashtaka hayo ni Bi Eunice Mwende Musyoka, Bw Francis Kitonyo, Bw Humphrey Kabanga Njau na Bw Patrick Karanja Njau, ambao waliachiliwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yao.

Hata hivyo, Bw Mutua na Bw Wanjala walihukumiwa kifungo cha miaka kumi kila mmoja gerezani mnamo 2017 baada ya kupatikana na hat iya ya wizi wa mali hizo, ambazo zilikuwa zinasafirishwa na mwajiri wao.

Inasemekana kiwango kidogo sana ya Sh313milioni ambazo ziliibwa zilipatikana huku zaidi ya Sh200milioni zikipotea kabisa.

Polisi wahudumia mshukiwa wa ugaidi baada ya kumpiga risasi

Na WACHIRA MWANGI

WAKAZI wa mtaa wa Tudor Mwisho, Kaunti ya Mombasa jana walistaajabishwa na jinsi polisi walivyoepuka kumuua mshukiwa wa ugaidi, wakampa huduma ya kwanza ya matibabu baada ya kumpiga risasi mguuni alipokataa kujisalimisha.

Hofu ilitanda mtaani humo ghafla alfajiri wakati polisi walipoenda kumnasa mshukiwa huyo.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo walieleza jinsi milio ya risasi ilivyotanda kwa karibu dakika 20, polisi walipowaamuru wasitoke nje wakati wa oparesheni hiyo iliyofanywa mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

Polisi hao wa kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU) hatimaye walifanikiwa kumpiga risasi mshukiwa huyo aliyetambuliwa kama Salim Aboud Khalid, 40, almaarufu kama Survivor, wakamjeruhi na kumpeleka hospitalini baada ya kumfanyia huduma ya kwanza ya matibabu.

Mkuu wa polisi wa Mombasa,Bw Eliud Monari alisema maisha ya mshukiwa hayamo hatarini kufuatia jeraha lake la risasi.

Mshukiwa alipigwa risasi mguuni akiwa mafichoni na inadaiwa alijaribu kuwashambulia maafisa wa ATPU waliomtaka ajisalimishe.

Watu walioshuhudia kisa hicho walisema kuwa maafisa wa ATPU wasiopungua 17 waliwasili katika eneo hilo wakiwa wameabiri magari matatu.

“Lengo lao halikuwa kuua. Hii ni kwa sababu mtu mmoja alipojaribu kutoroka nilisikia mmoja wao akiwaambia wenzake: ‘piga mguu’,” akasema shahidi aliyeomba jina lake libanwe.

Maafisa wa polisi walijigawa katika makundi matatu wakati wa oparesheni hiyo. Bw Monari alithibitisha kwamba mshukiwa huyo ambaye sasa yuko chini ya ulinzi mkali hospitalini ndiye alikuwa akisakwa na maafisa wa ATPU.

“Polisi walisikika wakimsihi mshukiwa aliyepigwa risasi kujisalimisha wakisema kwa sauti: ‘inua mikono juu tutakuua weeeee’,” akasema mkazi aliyeshuhudia tukio hilo.

Katika hali ambayo wakazi wengi waliona si ya kawaida, maafisa wa polisi walimpa mshukiwa huyo huduma ya kwanza ya matibabu kabla kumkimbiza hospitalini.

“Tunashukuru Mungu tumemkamata akiwa hai,” maafisa hao walisikika wakisema.

Haikubainika ni lini mshukiwa huyo atafikishwa kortini wala mashtaka yatakayomkabili.

Hata hivyo, duru zilisema wakati mwingi polisi wakiamua kutomuua mshukiwa wa aina yoyote ya uhalifu hata anapokataa kujisalimisha na kuwashambulia, huwa inamaanisha kuna habari muhimu wanazohitaji kutoka kwake.

Wanaoshukiwa kuiba Sh75m waachiliwa kwa Sh1m kila mmoja

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA sita wa wizi wa Sh75.9 milioni za benki ya Standard (SCB) kimabavu Jumatano waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni kila mmoja na wadhamini wawili wa kiasi hicho.

Na wakati huo huo, hakimu mkuu Francis Andayi aliamuru Mamlaka Huru ya Polisi (IPOA) iwachunguze maafisa wa Polisi kutoka kitengo cha Flying Squad waliowatesa na kuwaumiza washukiwa hao sita.

Bw Andayi alisema inasikitisha sana kwa Polisi kuwatesa washukiwa ilhali sheria inakataza washukiwa kuteswa.

“Naamuru IPOA ichunguze madai kwamba maafisa wa polisi waliowatia nguvuni washukiwa waliwatesa washukiwa hao. Ripoti iwasilishwe kortini na Polisi wahusika wachukuliwe hatua kali,” Bw Andayi aliamuru.

Wakili Cliff Ombeta anayewatetea washtakiwa alielezea jinsi polisi waliwatesa na kuwaumiza.

Koplo Duncan Kavesa Luvuga alimwonyesha hakimu majeraha aliyopata alipopigwa , kuzamishwa majini, na kutiwa selotepu mdomoni na kufungwa kichwani kwa karatasi ya nailonu huku akilazimishwa kueleza alikoficha mgawo wake wa pesa hizo.

Bw Andayi alitoa agizo hilo alipowaachilia washtakiwa Konstebo Chris Machogu, Koplo Luvuga, Konstebo Boniface Mutua, Vincent Owuor, Alex Mutuku na Francis Muriuki.

Wakili Cliff Ombeta (kushoto) aonyesha hakimu majeraha ya Koplo Duncan Luvuga. Picha/ Richard Munguti

Aliamuru washukiwa wazuiliwe katika gereza la viwandani ambapo watakuwa wakitolewa kupelekwa kwa afisa wa uchunguzi wa jinai kituo cha polisi cha Langata kuwahoji kwa muda wa siku saba.

Washtakiwa hawa walikanusha mashtaka mawili ya wizi wa mabavu na kuharibu masanduku na vifaa vingine vya kampuni ya G4S zenye thamani ya Sh1,267,000.

Sita hao walikana mnamo Septemba 5, 2019 katika eneo la Nairobi West waliwanyang’anya wafanyakazi wa G4S waliwanyang’anya kimabavu Sh75,949,350.

Shtaka lilisema sita hao walikuwa wamejihami kwa silaha hatari walipotekeleza wizi huo.

Bw Andayi alitupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) la kuwanyima washukiwa hao dhamana akisema “ hajawasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kuwanyima washukiwa dhamana.”

Hakimu alimzomea afisa anayechunguza kesi hiyo kwa kuwasilisha mahakamani beti tisa za afidaviti ambazo hazielezei chochote kuhusu ombi la kuwanyima washukiwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi alisema washukiwa hao walitiwa nguvuni siku tofauti tofauti na mahala mbali mbali na wanahofiwa watawavuruga mashahidi.

Alisema pesa zilizoibwa hazijapatikana.

Polisi Mungiki wanavyotesa wananchi

Na MWANDISHI WETU

HUKU makundi ya wahalifu yakiendelea kuhangaisha raia, baadhi ya maafisa wa polisi wamebuni magenge yao ya kuchukua ada haramu.

Polisi hao wahuni wanawahangaisha wananchi hasa wafanyibiashara, wakidai pesa jinsi kundi hatari la Mungiki lilivyokuwa likifanya.

Biashara wanazolenga ni matatu, vibanda, mabaa na bodaboda.

Wanaokosa kutoa ada hizo huadhibiwa jinsi Mungiki walivyokuwa wakifanya, lakini maafisa hao hutumia mamlaka yao kwa kuwasingizia makosa wananchi, kuwapiga na kuwafungia seli kisha wanaachiliwa wakitoa hongo.

Polisi hawa huzusha hofu miongoni mwa raia kila wanapoonekana na hubidi wawape pesa ili wasichukuliwe hatua hata kama hawana makosa.

Katika mtaa wa Donholm jijini Nairobi, wafanyabiashara waliambia Taifa Leo kuwa kila siku maafisa wanaotembea kwa makundi huanza kupiga doria mwendo wa saa moja usiku.

Doria hiyo si kwa minajili ya kuwapa wananchi usalama, bali ni kwa nia ya kukusanya ada ambazo mitaani zinafahamika kama ‘Protection Fees’ (ada za ulinzi).

Mwendo wa saa moja unusu usiku, polisi huonekana wakitembea kwa makundi ya wawili wawili, wake kwa waume, wakiingia katika biashara walizolenga kutoza ada hasa mabaa. Wote huwa wamevaa sare rasmi za polisi na kubeba bunduki.

Wamiliki wa baa, vilabu na maduka ya kuuza pombe waliozungumza na Taifa Leo walisema huwa wanalipa kati ya Sh200 na Sh500 kila usiku kwa maafisa hao.

“Ni hasara kwetu lakini hatuna namna nyingine. Ukikataa kulipa utatafutiwa kosa lolote lile na biashara yako itafungwa,” akasema mfanyabiashara aliyeomba kubanwa jina.

Katika mtaa wa Githurai 44, polisi hutumia gari rasmi na huwa wanaenda kutoka baa moja hadi nyingine. Wanapofika kwenye baa, mmoja ama wawili wanachungulia mlangoni, ambapo mhudumu hutoka nje na kuwapa “ada yao”.

Pia unapofungua biashara ya baa hubidi kuwahonga wakuu wa kituo kilicho karibu.

“Nilipofungua baa mtaani Githurai 45 ilibidi nitoe Sh20,000 kwa wakuu wa polisi eneo hilo. Kila anayefungua biashara hasa ya baa lazima atoe ada hiyo la sivyo utahangaishwa kila mara hadi utoe ama ufunge biashara,” akasema manyibashara mmoja.

Wahudumu walieleza kuwa unapotoa ada hizo haramu huwa unahakikishiwa usalama hata kama utaendelea kuuza baada ya saa zilizokubalika.

Imebainika utapeli huu hufanyika katika karibu kila mtaa jijini, hasa yenye makao ya wananchi wenye mapato ya chini na kadri na sio Nairobi tu bali pia katika miji mingine kitaifa na mashambani.

Kundi la Mungiki lilivuna mamilioni kutoka kwa wahudumu wa matatu wakati wa enzi zake. Lakini sasa polisi wa trafiki wamejaza pengo lililoachwa na sasa ndio wanahangaisha wahudumu hao kwa kuchukua ada hizo.

Wahudumu wa matatu Nairobi, Murang’a, Kiambu, Mombasa na maeneo mengine walieleza kuwa imekuwa kawaida polisi wa trafiki kuchukua ‘protection fee” kila siku kutoka kwao.

“Wengine huwa na vijitabu vya kuandika waliolipa. Hapa Nairobi ada ya kawaida kwa kila gari ni Sh200. Usipolipa utatafutiwa makosa na kuharibiwa biashara,” akasema meneja mmoja wa shirika la matatu Nairobi.

Katika Kaunti ya Mombasa, maafisa kadhaa wa trafiki hulipwa na wasimamizi wa mashirika ya matatu kila wiki ili kuepusha matatu zao kuwekwa kizuizini.

Kwa kawaida matatu huwa zina wasimamizi wao wanaofahamika kama ‘meneja’. Ni jukumu la msimamizi kuhakikisha kuna afisa wa polisi anayelinda magari yale anayosimamia.

“Gari linapokamatwa na polisi fulani kwa kukosa kufuata sheria za barabarani, kile ambacho dereva anahitajika kufanya ni kumfahamisha meneja. Meneja atampigia simu afisa ambaye hupokea ada kutoka kwake, kisha huyu afisa atampigia polisi aliyekamata gari na kumshawishi aliachilie,” akasema.

Kulingana naye, ‘mshahara’ wa polisi huwa kati ya Sh2,500 na Sh5,000 kila wiki ikitegemea maelewano kati yake na msimamizi wa magari ‘anayolinda’. Kiasi hiki ni kikubwa ikizingatiwa kuna uwezekano polisi mmoja hutegemewa na wasimamizi kadhaa wa matatu kulinda magari yao.

Wakati Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai alipoapishwa mamlakani Aprili, aliahidi kupambana na uozo uliokithiri katika idara ya polisi.

Hata hivyo, kufikia sasa juhudi nyingi zimeelekezwa katika kupambana na ufisadi wa polisi wa trafiki, huku mahangaiko ya wafanyabiashara mikononi mwa polisi yakisahaulika.

Polisi lawamani kwa kuua vijana maskini kiholela

Na BENSON MATHEKA

KWA mara nyingine, polisi wamelaumiwa kwa kuwaua kiholela vijana kutoka mitaa masikini jijini Nairobi wakiwahusisha na madai ya uhalifu.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, kuanzia Agosti 2018, polisi wamewaua wanaume na vijana 21 katika mitaa ya Mathare na Dandora jijini Nairobi.

“Mauaji haya ya kiholela yanaonyesha kuna shida kubwa zaidi ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi wakidai kwamba wanadumisha usalama katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi na kukataa kufuata sheria ili kuhakikisha mauaji yanayotekelezwa na maafisa wa polisi yanachunguzwa,” HRW ilisema kwenye taarifa.

Mtafiti mkuu wa shirika hilo barani Afrika, Otsieno Nyamwaya, alisema kwamba polisi hawasaidii shirika huru la kuchunguza utendakazi wa polisi (IPOA) kuchunguza visa hivyo ili kuhakikisha wanaohusika wanachukuliwa hatua.

“Polisi wanawakamata watu ambao hawana silaha na kuwaua kwa kuwapiga risasi na huduma ya polisi au shirika la kuchunguza utendakazi wa polisi hawafanyi chochote kusimamisha mauaji haya,” alisema Bw Nyamwaya.

Afisa huyo anasema kwamba mauaji hayo yanapaswa kuchunguzwa na maafisa wanaoyatekeleza kuchukuliwa hatua za kisheria

Anasema polisi huwa hawaripoti visa vya mauaji ya kiholela au kuanza utaratibu wa kuyachunguza inavyohitajika kisheria.

Msemaji wa polisi, Charles Owino, alisema IPOA inapaswa kuchunguza visa vya mauaji ya kiholela vinavyotekelezwa na maafisa wa polisi.

“Afisa yeyote wa polisi anayekiuka sheria anapaswa kuchukuliwa hatua binafsi. Katika mauaji ya Mathare na Dandora, IPOA inafaa kufanya uchunguzi na kuhakikisha waliohusika wanashtakiwa,” alieleza Bw Owino.

Hata hivyo, HRW inasema kwamba makamanda wa polisi wanaosimamia maafisa wanaotekeleza mauaji hayo hawachukui hatua zozote kuwaadhibu.

“Mauaji haya yanafanyika na makamanda wa polisi wanaosimamia maafisa hao hawachukui hatua kuyazuia au kuwaadhibu wanaohusika,” alisema Bw Nyamwaya.

Kulingana IPOA, polisi huwa hawatayarishi ripoti za kuhusu mauaji hayo ambazo shirika hilo linaweza kutumia kuanza uchunguzi.

Shirika hilo pia lina nguvu za kisheria za kuanza uchunguzi huru kuhusu vitendo vya maafisa wa polisi.

Kulingana na maafisa wa IPOA waliozungumza na HRW, wachunguzi wake hugonga mwamba wakichunguza visa vya mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na polisi kwa sababu mashahidi huwa wanaogopa kuwapa habari muhimu.

Lilimnukuu Bw Owino akitetea maafisa wa polisi katika mitaa ya Dandora na Mathare kwa kusema wamekuwa wakichukua hatua za kulinda umma dhidi ya wahalifu.

Polisi wafurika mitandaoni kuelezea masaibu yao

Na VALENTINE OBARA

MAAFISA wa polisi wamegeukia mitandao ya kijamii kulalamikia mazingira hatari ya kazi huku wakiwasuta wakubwa wao moja kwa moja kwa kuwapuuza.

Idara ya Polisi nchini ni mojawapo ya vitengo vya kiserikali ambavyo maafisa huhitajika kutii amri bila maswali, na hivyo hatua ya baadhi yao kwenda kinyume na matarajio haya inashangaza wengi.

Jumatano, Bw Patrick Safari, ambaye ni askari jela, alifikishwa mahakamani pamoja na mwanablogu Robert Alai kwa madai kwamba walishirikiana kusambaza picha za maafisa waliouawa Wajir.

Polisi wanasema usambazaji wa picha hizo ulikuwa sawa na kushabikia ugaidi.

Kwa muda mrefu, Bw Safari, ambaye ana ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, amekuwa akitoa maoni yake bila uwoga kuhusu masuala tofauti ya kitaifa ikiwemo siasa na usimamizi wa polisi.

Wakati mwingine, yeye huchapisha picha zake akiwa amevalia sare za kikazi na kubeba bunduki huku akieleza anavyoenzi kazi yake ya ulinzi.

Wakati shambulio la Al-Shabaab eneo la Wajir lilipotokea na kusababisha vifo vya polisi 13 wiki iliyopita, alikuwa miongoni mwa walioibua suala kuhusu magari ya kustahimili vilipuzi ambayo yalizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2017.

Alidai idadi kubwa ya magari hayo hayawezi kutumiwa kwa sababu hayana magurudumu na mafuta, ndiposa polisi wanatumia magari ya kawaida katika maeneo yenye hatari ya vilipuzi.

“Maafisa 13 wa polisi walifariki na hadi sasa hakuna mkuu yeyote wa polisi ambaye amezungumza. Ni kana kwamba kila kitu kiko shwari. Ni lini mtu atajitokeza kuwafuta kazi wale wanaohusika na utepetevu huu ambao unasababisha vifo vya maafisa?” akauliza askari huyo wa magereza.

Jumanne, muda mfupi kabla ya kufichua kwamba alipokea habari kuwa polisi wanataka kumkamata, alishangaa kwa nini Bw Alai alikamatwa.

Aliandika: “Nina hakika picha hizo hazikutoka kwake. Lazima zilitoka kwa afisa wa polisi mwenye hasira aliyehusika kwenye operesheni hiyo. Walizisambaza ili kufichua uozo uliopo kwenye idara na kuonyesha masikitiko yao.”

Kando na Bw Safari, afisa mwingine wa polisi aliye miongoni mwa wanaokosoa idara hiyo mitandaoni ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kusimamia Majanga Kitaifa (NDMU), Bw Pius Masai.

Mbali na kulalamika kibinafsi kuhusu hali mbaya ya idara hiyo, Bw Masai huchapisha malalamishi ya maafisa wengine ambao wanahofia kujitokeza wazi.

“Wakati raia wa kawaida anapowasilisha malalamishi, matokeo hutakikana mara moja. Mbona ripoti zinazowasilishwa nasi maafisa wa polisi zinapuuzwa? Kwani sisi si binadamu?” akasema.

Lakini Msemaji wa Polisi, Bw Charles Owino alipuuzilia mbali lalama kwamba kuna utepetevu na usimamizi mbaya katika idara ya polisi, akisema serikali imejitahidi sana kuboresha hali ya utoaji huduma za usalama kitaifa.

Mutyambai azima polisi waliozoea hongo katika vizuizi barabarani

Na CHARLES WASONGA

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai Jumatano ameamuru kuondolewa kwa vizuizi na vituo vya ukaguzi wa magari katika barabara kuu kote nchini.

Vizuizi na vituo vya ukaguzi sasa vitawekwa tu kwa idhini ya makamanda wa polisi katika ngazi ya kaunti na sharti viwekwe kwa sababu maalum.

Bw Mutyambai alisema makamanda wa polisi watawajibishwa kwa mienendo mibaya ya maafisa wa polisi chini ya usimamizi yao, mathalan upokeaji wa rushwa.

“Mabadiliko haya tayari yanaendelea kama yanavyoweza kuthibitishwa na idadi ya vizuizi vilivyoko katika barabara kutoka Mombasa hadi Malaba.

“Tunatoa wito kwa Wakenya wenye nia njema kutuunga mkono kwa kutii sheria na kujiepusha na vitendo vya ufisadi,” akasema kwenye taaarifa iliyotumiwa kwa vyombo vya habari Jumatano na afisi yake.

Bw Mutyambai alisema udumishaji wa usalama barabarani ni mojawapo ya masuala ambayo ameyapa kipaumbele.

“Ili kufikia lengo hilo pande husika, wenye magari na polisi, wanapasa kujiepusha na vitendo vya ufisadi na vile vile waripoti visa hivyo kwa asasi husika,” akaeleza.

Hatua hii ya Bw Mutyambai inamaanisha kuwa maafisa wa polisi ambao watahudumu katika barabara kuu watafanya hivyo chini ya amri ya kamanda wa polisi katika maeneo husika kwa sababu maalum.

Tayari baadhi ya makamanda wameamuru kwamba vizuizi vya barabarani viondolewe.

“Maafisa walio ndani ya miji watashauriwa kuhakikisha hamna msongamano wa magari. Na wale walioko nje ya miji waondoke mara moja na wasubiri kushughulikia ajali ambayo yanapaswa kushughulikiwa mara moja huku tukisubiti maagizo zaidi kutika afisa za juu,” akasema barua iliyoandikiwa na kamanda mmoja kwa wadogo wake.

Alipoingia afisini, Bw Mutyambai aliahisi kulainisha idara ya polisi wa trafiki nchini kama sehemu ya mchakato wa kupambana ufisadi katika sekta hiyo.

Kumekuwa na malalamishi kuwa maafisa wa polisi wa trafiki, haswa wale barabara kuu ni wafisadi mno.

Maafisa wote wasimamizi wa vituo (OCS) pia waliamriwa kuhakikisha kuwa sheria za usalama barabarani almaarufu sheria za Michuki, zinatekelezwa.

Juzi, Naibu Inspekta Jenerali Edward Mbugua alisema kuwa operesheni zote za trafiki zimegatuliwa hadi kiwango cha kituoni ili kuhakikisha zinafanikiwa.

Polisi lawamani kwa kuteketeza nyumba tisa

Na CHARLES WANYORO

POLISI katika eneo la Igembe Kusini, Kaunti ya Meru, wamekosolewa vikali kwa madai ya kuchoma nyumba tisa kijijini Thunu, Kaunti Ndogo ya Igembe Kusini.

Wakazi waliopiga kambi katika kanisa la Christ Gospel Mission walisema takriban maafisa 40 wa polisi walivamia eneo hilo mnamo Jumamosi na kupiga risasi hewani kabla ya kuzitia moto nyumba hizo na kusababisha uharibifu mkubwa.

Bi Jane Kaari, 46, mkazi, alieleza jinsi maafisa hao waliokuwa wameandamana na wasimamizi wa eneo hilo (chifu na msaidizi wake) walivyofika mwendo wa saa sita mchana walipokuwa wakitayarisha maakuli ya mchana na kuanza kufyatua hewani.

Alisema maafisa hao walionekana kulenga nyumba fulani kwani walionyesha nyumba zilizofaa kuharibiwa kabla ya kuzivunja na kuzitia moto.

“Walisema walikuwa wamewasili kwa nyumba zilizolengwa kabla ya kuanza kutoa maagizo. Nilitazama mbuzi, vyakula na kuku wakichomeka. Walisema walikuwa wakifukuza wahalifu. Tumefanya nini sisi? Hatuna haki? Tunahisi kubaguliwa,” alisema.

Alieleza kuwa kulikuwa na mzozo kuhusiana na kipande cha ardhi cha ekari 50 na huenda kilikuwa sababu ya kuchomwa kwa nyumba zao, kwa kulenga kuwahofisha wakazi.

Polisi ange kuzima njama za kigaidi

Na MARY WAMBUI

MAAFISA wa polisi nchini wako macho kutokana na uwezekano wa kutokea kwa shambulizi la kigaidi kufuatia kukamatwa kwa washukiwa wanne wa ugaidi katika hoteli za Intercontintal na Hilton, Nairobi mnamo Jumanne na Alhamisi.

Vilevile kitengo cha usalama kiliripoti kwamba vilipuzi na zana hatari zilipatanikana Ijumaa iliyopita katika barabara kuu ya Narok-Bomet, hali inayozidisha hatari ya kiusalama.

Mnamo Jumanne, washukiwa wawili walikamatwa katika hoteli ya Hilton baada ya mienendo yao kuzua maswali huku wengine wawili wenye asili ya Kisomali pia wakinyakwa katika hoteli ya Intercontinental walikoenda kama wageni waliotaka kukodi chumba ilhali hawakuwa na stakabadhi maalum.

Akizungumza na Taifa Leo, Mkuu wa Polisi wa Nairobi Phillip Ndolo alisema maafisa wa usalama wamewekwa katika hali ya tahadhari kuhusu shambulio la kigaidi hata baada ya kukamilika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wakati ambao onyo kuhusu matukio ya kigaidi lilitolewa.

“Onyo tulilolitoa bado linabakia hivyo na litaendelea kwa muda. Hata hivyo, halifai kuzingatiwa katikati mwa jiji pekee bali pia katika maeneo mengine nchini,” akasema Bw Ndolo.

Washukiwa walionyakwa wanaendelea kuhojiwa kuhusu mienendo yao katika vituo mbalimbali vya polisi ambavyo Bw Ndolo hakuvifichua kutokana na sababu za kiusalama.

“Uchunguzi bado unaendelea na huenda ukachukua muda zaidi. Hakuna aliye na stakabadhi za utambulisho kati yao na tunataka kujua walitoka wapi, walikuwa wakienda wapi na lengo lao lilikuwa nini,” akaongeza Bw Ndolo kuhusu washukuwa waliobambwa Nairobi.

Ingawa hivyo, alisema wanne hao huenda wasifunguliwe mashtaka ya kupanga shambulizi la kigaidi lakini watakabiliwa kisheria kutokana na makosa mengine punde tu uchunguzi utakapokamilishwa.

Kufuatia matukio hayo mawili jijini Nairobi, polisi walizidisha doria Jumamosi na Jumapili jijini humo na maeneo ya kuabudu.

Akizungumza akiwa Bomet, Msemaji wa Polisi Charles Owino alisema kuwa maafisa wa polisi siku za nyuma wametibua njama nyingi za kigaidi kwa sababu Wakenya wamekuwa wakiwapasha habari kuhusu watu wenye mienendo ya kutiliwa shaka.

TAHARIRI: Visa vya polisi kujiua nchini vichunguzwe

NA MHARIRI

Tusemezane ukweli. Ongezeko la visa vya maafisa wa polisi kujitoa uhai na kuua watu wa familia zao linatisha. Kuna hatari ya visa hivi kugeuka kuwa janga la kitaifa iwapo hatua hazitachukuliwa kurekebisha hali.

Kwa kufanya chanzo cha maafisa wa polisi kugeuza silaha za kazi yao kujiangamiza ni lazima kibainishwe na hii haitawezekana ikiwa wataalamu kutoka nje ya huduma ya polisi hawatahusishwa.

Tunasema hivi kwa sababu baadhi ya maafisa wanaofungua roho zao kabla ya kujiua huwa wanalaumu presha za kazi na kudhulumiwa na wakubwa wao kazini.

Dhuluma hizi wakati mwingine huwa ni pamoja na kupokonywa wake zao na wakubwa hao, kunyimwa ruhusa na hata kukosa kupandishwa vyeo. Wengi wa wanaotekeleza visa hivi huwa ni maafisa wa vyeo vya chini ambao huwaua wakubwa wao kabla ya kujiua.

Hii inaonyesha kuwa kuna ukweli kwamba wakubwa wanawanyanyasa wadogo wao katika kikosi cha polisi. Katika hali hii, itakuwa bora serikali itafute wataalamu kutoka nje ya kikosi kutoa huduma za ushauri nasaha.

Maafisa wanaopitia wakati mgumu kwa sababu moja au nyingine, ikiwa ni pamoja na kuteswa na wakubwa wao watakuwa na nafasi ya kufungua mioyo yao bila kuwa na hofu ya kudhulumiwa na kwa kufanya hivi hali inaweza kubadilika.

Mara nyingi, wakuu wa polisi huwa wanapuuza ripoti zinazoonyesha matatizo ya maafisa wa polisi ikiwa ni pamoja na kubaguliwa wakiwa kazini na wakubwa wao.

Itabidi Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai kushughulikia hali hii kwa dharura kabla maafisa wake wanaokabiliwa na matatizo ya kiakili kwa sababu ya wanayopitia kazini kugeukia umma na kuwaangamiza.

Ikizingatiwa kwamba kazi yao ni ya kudumisha usalama, inafaa maslahi ya maafisa wa polisi yazingatiwe kikamilifu, wathaminiwe na kushughulikiwa wanapokabiliwa na matatizo.

Kupuuza afisa wa polisi anayesongwa na mawazo kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi au kifamilia ni hatari kwa sababu itakuwa vigumu kwake kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Chembilecho wahenga, ni bora kuziba ufa kwa sababu ni ghali mno kujenga ukuta. Polisi washughulikiwe kabla ya hali hiyo kubadilika na kuwa janga kubwa.

Wizara ya Fedha lawamani kutofidia polisi waliofariki wakiwa kazini

Na DAVID MWERE

WIZARA ya Fedha imelaumiwa kwa kutotoa Sh1.5 bilioni za kulipa fidia maafisa wa polisi waliofariki wakiwa kazini.

Hii ni licha ya maafisa wa polisi kuwa na bima maalum iliyosimamiwa na serikali.

Lawama hizi zinajiri baada ya kuibuka kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani ilikuwa imewasilisha ombi la kuitaka Wizara ya Fedha kutoa fedha hizo. Mnamo 2014, Serikali Kuu iliipa kampuni ya Bima ya Pioneer kibali cha kutoa huduma za bima kwa polisi na maafisa wa magereza. Serikali ilitenga Sh3.5 bilioni kuendesha mpango huo.

Malalamishi yaliyowasilishwa na familia zilizoathiriwa katika Bunge la Kitaifa yanaonyesha kuwa familia za polisi waliofariki wakiwa kazini tangu 2017 hazijalipwa fedha zozote.

Kufikia mwezi Mei mwaka huu, vifo 460 vya maafisa wa polisi vilikuwa vimeripotiwa, lakini familia zao bado hazijapokea fidia yoyote.

Zaidi ya polisi 1,200 walikuwa wamejeruhiwa wakiwa kazini kufikia wakati huo. Vifo na majeraha yaliyoripotiwa yalihusiana na ajali za barabarani, kufyatuliwa risasi, vitendo vya ugaidi kati ya masuala mengine.

Kulingana na stakabadhi za malipo zilizo na kampuni hiyo, familia ya polisi anayefariki kutokana na ajali inapaswa kulipwa mshahara wa hadi miaka minane. Hili linamaanisha kuwa kiwango hicho ni kama Sh2 milioni. Polisi anayepata ulemavu kutokana na sababu za kikazi pia anapaswa kulipwa kiasi kama hicho.

Wanaoathiriwa pia wanapaswa kulipwa Sh150,000 kama gharama ya mazishi kwa muda wa saa 24 baada ya kupokea kibali cha mazishi.

Konsitebo wakongwe katika kikosi cha polisi roho mkononi

Na MWANGI MUIRURI

INSPEKTA Mkuu wa Polisi Hillary Nzioki Mutyambai amezindua rasmi msasa wa kuwapandisha ngazi maafisa ambao wamedumu kwa muda mrefu katika ngazi ya chini zaidi ya konsitebo.

Kigezo kikuu katika msasa huo ni kuwa afisa huyo awe ametinga umri wa miaka 50 na hajawahi kupandishwa cheo na hana kesi yoyote ya kinidhamu inayoendelea.

Katika msingi huo, Bw Mutyambai amewaagiza wakuu wote wa vitengo wawasilishe orodha ya maafisa hao afisini mwake, makataa ya kupokezwa orodha hiyo yakiwa ni Mei 9, 2019.

“Barua hii ni ya kuwaagiza makamanda wa stesheni wawasilishe majina ya maafisa walio katika hali iliyoelezewa, wawe wako na zaidi ya miaka 50, wamedumu katika kiwango hicho cha konsitebo ambacho ni kundi la F katika huduma ya umma na wawe hawana kesi za kinidhamu,” barua ya Mutyambai yasema.

Wale ambao watapandishwa cheo hadi kwa mfano kuwa koplo au hata sajini watanufaika na kupanda kwa ujumla wa kitita cha kustaafu wakitinga miaka 60.

Walio na ulemavu hata hivyo hustaafu wakiwa na umri wa miaka 65.

Mmoja wa walio na hamu ya juu kushirikishwa katika kupandishwa cheo ni Konsitebo Joseph Gichuru ambaye aliingia rasmi katika kikosi cha polisi Oktoba 4, 1980, na ambapo tarehe yake rasmi ya kustaafu ni Juni 30, 2020.

“Sijawahi kuwa na kesi yoyote ya kinidhamu. Nimepigwa msasa wa ufaafu mara si haba na hata hadharani nimeomba wakubwa wangu wanipandishe cheo…Wale tulianza nao kazi leo hii wako na mamlaka ya juu na wengine hata ni wakubwa wangu Jijini Nairobi. Mimi huwa najiuliza kwanini nikawa na mkosi huu wote kazini na nimekuwa mwaadilifu kwa kazi yangu,” anasema Gichuru.

Konsitebo Joseph Kimaru Gichuru (kushoto) akiwa na kurutu mwenzake, James Mwangi ambaye leo hii ni Inspekta wa polisi, katika hii picha ya zamani wakiwa katika taasisi ya elimu ya polisi mwaka wa 1980. Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa maisha yamekuwa magumu zaidi kazini kiasi kwamba hata kusomesha watoto wake amepata shida si haba.

“Ina maana kuwa kwa miaka hii yote 39 ambayo nimekuwa kazini sijawahi kupata nafasi ya kuitwa mkubwa na yeyote. Waliojiunga na kikosi hivi majuzi wakiwa sawa na rika la watoto wangu leo hii wengine ni wa kiwango cha Inspekta na ambapo ninafaa kuwanyenyekea na kuwaheshimu kama wakubwa wangu ilhali kwa tajiriba, nilianza kazi wakiwa bado kuzaliwa. Hii dunia mara nyingine haina haki,” anasema.

Sasa, imani yote ya Konsitebo Gichuru ambaye ni mzawa wa Kaunti ya Nyeri katika Kaunti ndogo ya Mathira ni Julai 17, 2019 ambapo afisi ya Mutyambai itatoa orodha rasmi ya wale ambao watapandishwa madaraka.

Bw Mutyambai pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Huduma kwa Polisi (NPSC) Eliud Kinuthia wanakiri kuwa shida hii yote imetokana na ukosefu wa sera maalumu kuhusu kupandisha vyeo maafisa.

Kuna maafisa ambao waliomba wasitajwe ambao wamekiri kuwa kupata madaraka ndani ya kikosi cha polisi ni sawa na kushuka mchongoma.

“Ikiwa wengi wetu wataandika vitabu vya kuelezea mahangaiko yetu tukisaka mamlaka…Wasomaji watashangaa kiasi cha kuzirai…Watasoma vile huwa tunatumia wakubwa wa jamii zetu, kuhongana kwa pesa na hata mahaba… Wengine wakishtaki kesi mahakamani za kushinikiza wapandishwe vyeo. Hii ni kazi ya mawazo na usishangae ni kwa nini visa vya mauti vimejaa ndani ya kikosi ambapo wengine huua wenzao na wengine wakijiua,” anasema mmoja wa makamanda wa Stesheni za polisi hapa nchini.

Taswira ya ukora wa polisi ulioishia mauti ya mshukiwa katika seli Maragua yaibuka

Na MWANGI MUIRURI

IMEANZA kuibuka kuwa Hamuel Muguro Ngugi aliyeaga dunia katika seli za polisi za Stesheni ya Maragua alijipata katika mtego wa uhasama kati ya mwajiri wake na maafisa wa polisi.

Amezikwa Jumatano.

Uhasama huo unasemwa kuwa hata baada ya kukamatwa, kuna maafisa waliodai hongo ya Sh100,000 ili mambo yatulie ndani ya sakata hiyo na baada ya kukataa kuitoa hongo hiyo, mambo yakazidi unga kiasi cha kuishia mauti ndani ya seli.

Taarifa za uchunguzi ambazo zinaendelea kuandikishwa na mamlaka ya kumulika utendakazi wa maafisa wa Polisi (IPOA) zimebaini kuwa kuna afisa mmoja mkuu katika kituo hicho aliyekuwa amesisitiza kumwadhibu mumilki wa baa ya Starehe ambayo marehemu alikuwa mhudumu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bw Wairegi Cheki, maafisa hao walikuwa wameripoti katika biashara hiyo ya pombe asubuhi ya Jumamosi hiyo wakidai hongo lakini wakanyimwa.

“Wakiondoka, waliapa kuwa wangetupa adhabu ya kuwapuuza. Na ndipo usiku huo walituvamia mwendo wa saa tano na dakika tano tukiwa hatuna wateja bali tulikuwa sisi waajiriwa wa baa hiyo tukifunga madirisha ndio tuelekee zetu manyumbani,” akasema Cheki.

Anasema kuwa maafisa hao walipuuza biashara haramu ya uuzaji chang’aa iliyokuwa ikiendelezwa kando mwa baa hiyo na ambayo ilikuwa ikiuzwa na genge la vijana waliokuwa wamejihami kwa mapanga na mipini, lakini wakavamia baa ambayo ilikuwa imefunga kazi kwa mujibu wa sheria.

“Maafisa hao pia walipuuza ushauri kuwa Bw Muguro alikuwa na matatizo ya kimwili na haikukuwa na busara yoyote ya kumtia mbaroni bali hata angeandikiwa bodi ili awe huru.”

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Huduma ya Polisi Bw Eliud Ndung’u Kinuthia, ni haki ya kila mshukiwa wa makosa madogo kupewa bodi wakati wowote ndani ya kituo cha polisi na ikiwa makosa ambayo amekamatiwa hayazui kifungo cha zaidi ya miezi sita gerezani, hufai kufungiwa ndani ya seli.

Anasema kuwa huo ni mwelekeo ambao umetolewa na NPSC na pia afisi ya Inspekta Mkuu wa Polisi (IG) Hilary Mutyambai.

“Hakukuwa na sababu yoyote ya kukataa kumpa bondi mshukiwa huyo kwa kuwa wenzake watatu walikuwa wametiwa mbaroni huku mwajiri wao, Kinuthia Ngai akijitolea kuwa mdhamini wa mshukiwa huyo akiwa huru,” anasema wakili Geoffrey Kahuthu wa mahakama kuu.

Shida ni kuwa hata baada ya mshukiwa huyo kuaga dunia akiwa ndani ya seli hizo, na ambapo mashahidi wanashikilia kuwa mito yao ya kusaka usaidizi ilipuuzwa na waliokuwa katika kituo hicho usiku huo wa mauti, wenzake watatu walifikishwa mahakamani na kushtakiwa.

Ni mashtaka ambayo hata kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua anataja kuwa yenye shaka kuu.

Ikifahamika vyema kuwa washukiwa hao wote walikuwa wahudumu wa baa hiyo, makaratasi ya mashtaka yaliwaorodhesha watatu kuwa wateja wa baa hiyo na mmoja akiwa muuzaji.

“Marehemu Muguro, Waithaka Njeri na Kamari wakieleweka vizuri kuwa walikuwa wahudumu wa baa hiyo waliandikiwa mashtaka ya kuwa wateja. Lakini faili ya marehemu haikufika mahakamani kujibiwa mashtaka. Bw Cheki Wairegi alishtakiwa kivyake kama muuzaji wa pombe kinyume na sheria,” yasema taarifa moja.

Bw Kinyua anasema kuwa huo ulikuwa uamuzi haramu wa kushtaki washukiwa hao kwa makosa yanayoonyesha kuwa yalikuwa ya kulazimisha.

Hicho ndicho kizungumkuti ambacho kwa sasa kinaendelea kuchunguzwa na vitengo kadhaa vya polisi na pia watetezi wa haki za kibinadamu, tayari hata maafisa waliokuwa kazini katika mkondo wa kisa hiki wakiwa tayari wameandikisha taarifa zao.

Marehemu amezikwa katika kijiji cha Gathigia-Irembu kaunti ndogo ya Maragua.

MATHEKA: Heko kwa maafisa wetu wa polisi kwa kazi murua

Na BENSON MATHEKA

IWAPO kuna kitu kilichonifurahisha wiki iliyopita, ni utendakazi wa maafisa wa polisi.

Ninajua kwamba huwa wanafanya mengi katika kazi yao ya kudumisha usalama kwa wote na haikuwa tofauti na wiki jana.

Hata hivyo, ninataka kutaja matukio matatu ambayo yalinifanya kuwaonea fahari maafisa wetu wa polisi na nitaeleza ni kwa nini. Kwanza, wiki iliyopita ilianza kwa ripoti kuhusu kutoweka kwa mwanaharakati Carole Mwatha mtaani Dandora, Nairobi.

Hofu ya wengi ilikuwa kwamba mwanaharakati huyo ambaye mwili wake ulipatikana katika mochari ya City baada ya siku sita, alikuwa ametekwa nyara na kuuawa kwa sababu ya kulaumu polisi kwa mauaji ya kiholela mtaani humo.

Kwenye mitandao ya kijamii, polisi walirushiwa kila aina ya lawama, watu wakasahau kwamba wanawahitaji kwa usalama wao kila siku.

Kile ambacho raia hawakufahamu ni kwamba wapelelezi walikuwa wakifanya kazi yao kwa kufuatilia simu ya mwanaharakati huyo hadi wakagundua kwamba alikuwa katika hospitali moja mtaani humo na sababu ilikuwa ni kujaribu kutoa mimba.

Cha kusikitisha ni kuwa polisi wasingemuokoa kwa sababu wakati walipopata habari kuhusu kutoweka kwake, alikuwa ameaga dunia.

Licha ya lawama za kila aina, kutoka kwa raia na makataa kutoka kwa wanaharakati, polisi walifanya kazi yao na kuwakamata washukiwa na kuwafikisha kortini kwa wakati.

Joto lilitulia upasuaji wa maiti uliofanywa na mwanapatholojia huru kuthibitisha kwamba mwanaharakati huyo aliaga dunia akijaribu kutoa mimba.

Polisi walibeba lawama lakini walidumisha utaalamu wa hali ya juu kuchunguza mauaji hayo na wanafaa kupongezwa. Naomba kumpongeza kiongozi wa uchunguzi huo, Inspekta Mkuu Joseph Wanjohi wa ofisi ya upelelezi ya Dandora kwa ustadi, utulivu na utaalamu wake katika uchunguzi wa kutoweka na mauaji ya Bi Mwatha.

Funzo

Hapa kuna funzo kwa Wakenya kwamba wanafaa kuwa na subira na kuwapa maafisa wa usalama nafasi ya kufanya kazi yao. Muhimu kwa umma ni kushirikiana na polisi kwa kutoa habari muhimu badala ya lawama.

Aidha, ni wiki jana ambapo aliyekuwa afisa wa cheo cha juu alihukumiwa kunyongwa kwa mauaji, ishara kwamba sheria ikifuatwa kikamilifu haki itatendeka kwa wote.

Katika kisa kingine, Kaunti ya Nyeri wiki jana, polisi walimtia mbaroni mshukiwa wa kujitoa mhanga akielekea katika chuo kimoja kikuu na kumpata na vifaa vilivyoshukiwa kuwa vilipuzi.

Najua kwamba polisi wamefaulu kuzima mashambulio mengi lakini ninahisi kukamatwa kwa mshukiwa huyu huenda kulizuia hasara kubwa hasa ikikumbukwa mkasa wa chuo kikuu cha Garissa.

Tukio jingine ambalo polisi walidhihirisha ustadi wao wiki jana ni kumsaka na kumkamata mshukiwa aliyekuwa akijifanya chokoraa. Picha ya mhalifu huyo iliposambazwa katika mitandao ya kijamii akiwa na bastola, polisi walichukua hatua za haraka na kumnasa.

Hili ni funzo kwa Wakenya kwamba wakitoa habari za kuaminika kwa polisi, visa vya uhalifu vinaweza kukabiliwa vilivyo.

Polisi wapinga ripoti wamewapa silaha maafisa wa akiba

Na PETER MBURU

IDARA ya Huduma za Polisi (NPS)imepinga vikali ripoti kutoka kwa gazeti la The Star kuwa imekuwa ikiwahami maafisa wa polisi wa akiba (KPR), ikitaja habari hiyo kuwa ya wongo na ya kupotosha.

Idara hiyo ilisema kuwa haijawapa silaha wala kuajiri kisiri maafisa wowote wa KPR, ikisema ripoti ya gazeti hilo inatishia kuvuruga amani katika jamii ambapo kikosi hicho hufanya kazi.

Aidha, idara hiyo kupitia akaunti yake ya Twitter ilisema kuwa maafisa wa KPR ambao imeajiri wanajulikana na wakazi ambapo wanahudumu.

“Habari hiyo ni mchanganyiko wa ukweli mchache na uongo mwingi ambao unaleta shaka isiyohitajika miongoni mwa watu. Tunarai umma kupuuza habari hiyo,” idara ya NPS ikasema.

Ilisema kuwa habari yenyewe inaweza kuwa na hatari ya kujenga mjadala kuwa kuna haja ya kupunguzwa kwa maafisa wa kikosi hicho, wakati kwa kweli wanahitajika kwa wingi.

“Tunashauri kuwa haki ya wanahabari kueleza matukio yanayoendelea haifai kutumiwa vibaya kwa kuchapisha habari zisizo za kweli,” NPS ikaasema.

Ilipinga madai kuwa kuna mwingilio wa kisiasa katika shughuli ya kuwaajiri maafisa wa KPR, ikisema “uajiri wa maafisa hao hauhusiani kisiasa kwa njia yoyote.”

“Tunapanga kuongeza idadi ya maafisa katika meneo ambapo wizi wa mifugo umekita,” polisi wakaongeza.

Walisema kuwa hadi sasa, kikosi hicho kina maafisa 11,000 katika maeneo ya kaskazini mwa Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki mwa Kenya, ambao wamechangia kupungua kwa visa vya ukora na wizi wa mifugo katika maeneo hayo.

“NPS haihusiki na haifanyi kitu chochote kinachohusiana na kuhami kisiri maafisa wa KPR na wale walioajiriwa wanajulikana vyema na wakazi wa maeneo ambapo wanahudumu,” ikasema idara hiyo.

Polisi lawamani kwa kumcharaza na kumjeruhi mwanamke

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa polisi Kaunti ya Lamu wamemulikwa kwa mara nyingine kufuatia kisa cha kumpiga mwanamke na kumuumiza raia kaunti ya Lamu.

Bi Mariam Wanjiru ambaye ni mkazi wa kijiji cha Manda, anadai haki baada ya kupigwa na kuumizwa na polisi wakati akitoka dukani kununua bidhaa.

Bi Wanjiru,43, ambaye alikuwa ameandamana na watoto wake watatu, anadai kucharazwa na polisi hao wanaodaiwa kumwangusha chini, hivyo kumsababishia majeraha ya shingo na mashavu.

Bi Wanjiru anaendelea kupokea matibabu kwenye hospitali kuu ya King Fahad mjini Lamu.

Aidha juhudi za mwathiriwa kutafuta fomu ya matibabu (P3) kutoka kituo cha polisi cha Lamu zimegonga mwamba kwani polisi wanadaiwa kumnyima fomu hiyo.

“Nilikuwa nimetoka dukani kununua bidhaa. Ilikuwa yapata saa mbili usiku. Nilikuwa nimeandamana na watoto wangu. Ghafla polisi wanne walitujia na kuanza kunipiga na kuniangusha chini. Waliniumiza shingo yangu na mashavu na tayari nimetibiwa hapa hospitalini King Fahad. Nimejaribu kutafuta P3 kituoni lakinio kila ninapofika ninazungushwa. Ninahitaji msaada ili nipate haki,” akasema Bi Wanjiru.

Dadake Mwathiriwa, Bi Miriam Njeri, al;iambia Taifa Leo kwamba visa vya polisi kuwap[iga na kuwaumiza ovyo wakazi eneo la Manda vimekithiri mno.

Bi Njeri aliwaomba wakuu wa usalama Kaunti ya Lamu kuwachunguza wadogo zao kwa kuendeleza ukiukaji wa haki za binadamu kila wanapokuwa kazini.

“Polisi wafaa kutulinda badala ya kutuumiza siosi raia. Dadangu tayari ni mgonjwa wa moyo na tangu tukio hilo lijiri, hali yake ya kawaida haijarejea,” akasema Bi Njeri.

Hiki ni kisa cha pili cha polisi kuwapiga na kuwajeruhi raia katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kaunti ya Lamu.

Wiki jana, familia moja ilijitokeza kudai haki kwa kijana wao aliyepigwa na kuumizwa vibaya na poliosi eneo la Ndau, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Bw Yusuf Abuu,19, alipigwa na kuumizwa matumbo yake, hatua ambayo ilipelekea yeye kufanyiwa upasuaji wa nyongo yake kwenye hospitali hiyo ya King Fahad.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Kaunmti ya Lamu ili kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kwani hakupokea simu.

LAPSSET: Ujenzi wa bandari ya Lamu ulivyoboresha maisha ya polisi

NA KALUME KAZUNGU

UJENZI unaoendelea wa Mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) katika eneo la Kililana, Kaunti ya Lamu umesaidia pakubwa kuboresha maisha ya maafisa wa usalama wanaohudumu eneo hilo.

Kabla ya mradi huo wa gharama ya Sh 2.5 trilioni kuanza kujengwa, maafisa wa usalama waliokuwa wakipelekwa kuhudumia eneo hilo walijihisi kana kwamba wameonewa, kudhalilishwa, kutelekezwa na kutengwa na wakubwa wao kutokana na hali ngumu ya maisha iliyokuwepo eneo hilo.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, maafisa wa polisi kwenye kituo cha polisi cha LAPSSET kilichoko Kililana wamekuwa wakiishi kwa shida kwenye mahema ambayo yalikuwa yamewekwa  eneo hilo ambalo lilikuwa msitu mkubwa.

Maafisa wa polisi eneo hilo wameishi wakivumilia mvua, kibaridi kikali na kung’atwa na mbu, jambo ambalo baadhi yao waliishia kukosa matumaini na motisha wa kutekeleza majukumu yao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Nyumba, Paul Maringa (kulia) wakati alipozuru Kililana kufungua kituo cha polisi na nyumba za polisi. Picha/ Kalume Kazungu

Aidha ujenzi wa LAPSSET ambao unaendelea eneo hilo sasa umeyapa maisha ya polisi wanaohudumia eneo hilo taswira mpya.

Hivi majuzi kituo kipya cha polisi pamoja na makao mapya ya maafisa hao vilifunguliwa rasmi.

Jengo hilo la kituo cha polisi pamoja na makazi mapya ya maafisa hao viligharimu serikali ya kitaifa kima cha Sh 1.2 bilioni.

Tayari mahema yaliyokuwa yakitumika kama makazi ya polisi yameondolewa  na maafisa wa polisi kuhamia kwenye kituo hicho kipya ambacho kimejengwa kwa muundo wa kisasa na kurembeka, hivyo kukifanya kuwa miongoni mwa vituo bora vinavyovutia kwa macho zaidi nchini.

Tofauti na vituo vingine vya polisi nchini, kituo cha polisi cha LAPSSET pia kiko na zahanati yake mpya ambayo itatumika kuwatibu maafisa wa usalama wanaohudumu eneo hilo.

Zahanati mpya ya polisi iliyojengwa eneo la Kililana. Picha/ Kalume Kazungu

Hali hiyo imepelekea maafisa wengi wa polisi wanaohudumu kaunti ya Lamu kuwa na ari ya kufanya kazi na kuishi eneo hilo la LAPSSET kutokana na makazi na maandhari bora ya maafisa hao kuishi.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, aliisifu serikali kwa kuendeleza mradi wa LAPSSET eneo la Kililana, alioutaja kubadili kabisa hali ya maisha kwa maafisa wake.

Bw Kioi alisema kufunguliwa kwa kituo hicho kipya cha polisi na makazi yao eneo la LAPSSET ni mwamko mpya utakaosaidia kuwapa moyo maafisa wa usalama na kuwafanya kutia bidii zaidi katika kutekeleza majukumu yao.

“Tunafurahia. Ujenzi unaoendelea wa mradi wa LAPSSET eneo hili la Kililana pia umesaidia kubadili maisha ya maafisa wetu. Kwa sasa maisha yameboreka hata zaidi. Maafisa wetu walikuwa wakiishi kwenye mahema lakini kwa sasa wamepata nyumba mpya za kisasa na kituo rasmi cha polisi ambacho pia kina sehemu ya kuwazuilia wahalifu. Hatua hii tayari imewapa motisha maafisa wetu kutia bidiii zaidi kazini,” akasema Bw Kioi.

Mahema ya polisi eneo la Kililana. Picha/ Kalume Kazungu

Kufikia sasa takriba maafisa 100 wa polisi wanahudumia kituo hicho lakini kwa mujibu wa Bw Kioi, zaidi ya maafisa 400 wa vitengo mbalimbali vya usalama wanatarajiwa kusambazwa kituoni humo ili kudhibiti usalama wa bandari ya Lamu punde itakapoanza rasmi shughuli zake.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, ambaye pia ni afisa msimamizi wa Operesheni inayoendelea ya kuwasaka magaidi wa Al-Shabaab ndani ya msitu wa Boni, alitaja kufunguliwa kwa kituo cha polisi cha LAPSSET, makazi mapya na zahanati ya polisi eneo hilo la Kililana kuwa hatua njema itakayowezesha usalama kudhibitiwa zaidi kote Lamu.

“Zahanati iliyoko hapa Kililana ni msaada mkubwa kwa maafisa wetu wa usalama wanaoendeleza operesheni kwenye msitu wa Boni kwani wataweza kuhudumiwa hapa pia. Pongezi kwa serikali yetu. Tutajitahidi kuweka usalama eneo hili ili miradi yote mikuu inayonuiwa kutekelezwa na serikali ifaulu,” akasema Bw Kanyiri.

Kufikia sasa ujenzi wa viegesho vitatu vya kwanza vya LAPSSET umefikia zaidi ya asilimia 60 kukamilika, ambapo kiegesho cha kwanza cha mradi huo kinatarajiwa kukamilika kufikia Juni mwaka huu.

Viegesho vingine viwili vimepangwa kukamilika kufikia mwaka 2020.

Jumla ya Sh 48 bilioni zimekadiriwa kutumiwa na serikali ya kitaifa katika ujenzi wa viegesho hivyo vitatu vya kwanza vya LAPSSET pekee.

ONYANGO: Visa vya polisi kujiua vichunguzwe kwa kina

Na LEONARD ONYANGO

TUNAPOFUNGA mwaka, maafisa wa polisi ni miongoni mwa watumishi wa serikali ambao watakumbuka 2018 kwani walibadilishiwa sare na kupewa za rangi ya samawati.

Maafisa wa polisi watakumbuka mwaka huu kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta kuagiza walipwe marupurupu ya kuwawezesha kutafuta nyumba na kuishi popote wanapotaka mbali na vituo vyao vya kazi.

Hata hivyo, 2018 ni miongoni mwa miaka yenye huzuni kwa maafisa wa polisi.

Mwaka huu ulisheheni visa tele vya maafisa hao wa usalama kuua watu wa familia zao na kisha kujiua kwa kujifyatulia risasi. Mathalani, mwezi uliopita konstabo Cornelius Kipngetich, 28, aliyekuwa akihudumu katika Kituo cha Piave, Njoro alimuua mkewe Eunice Wambui kisha akajitoa uhai kwa kujipiga risasi.

Afisa wa kikosi cha GSU Anthony Lemayan Lenkisol ambaye pia alikuwa miongoni mwa madereva wa Inspekta Jenerali Joseph Boinnet, alijiua kwa risasi alipokuwa likizoni katika eneo la Mwamba, Narok mjini.

Mnamo Aprili Tirus Omondi, afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu katika eneo la Takama, Kaunti ya Mandera alijinyonga nyumbani kwake huko Manyatta, Kisumu kutokana na madai kwamba alilemewa na madeni na hata kunyanyaswa kazini.

Kulingana na ripoti, mwendazake alionekana mwenye mzongo wa mawazo kabla ya kujiua.

Mnamo Oktoba, afisa wa Polisi wa Utawala (AP) wa umri wa miaka 35 alijiua kwa risasi mbele ya wenzake katika eneo laKandutura, Laikipia.

Inadaiwa kuwa afisa huyo wa polisi alikuwa akisumbuliwa na madeni na mizozo ya kifamilia.

Wiki iliyopita, konstabo Boaz Rotich Kipkosgei alijifyatulia risasi shingoni na kufariki papo hapo nje ya kanisa la Faza Fellowship, Kaunti ya Lamu, katika hali ya kutatanisha.

Mnamo Novemba, Konstabo Peter Wambiro Kagunda alijiua kutokana na sababu zisizojulikana katika Kaunti ya Bomet.

Mwezi huo huo, afisa wa polisi Peter Mawira alijitoa uhai katika kaunti ya Kitui kutokana na sababu zisizojulikana.

Hali ya huzuni ilitanda katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet baada ya maiti ya konstabo Michael Kipkoskei aliyekuwa akihudumu katika kituo cha Lokitaung kupatikana ikining’inia nyumbani kwake.

Hao ni baadhi tu ya maafisa wa polisi waliojitoa uhai mwaka huu.

Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba Idara ya Polisi haijachukua hatua kuchunguza kiini cha maafisa hao wanaojitoa uhai kiholela.

Idara ya polisi inafaa kuchukulia suala hilo kwa uzito.

Kwa mfano, ikiwa polisi anajiua kwa kunyanyaswa kazini, nani anawatesa? Idara ya polisi pia inafaa kufahamu sababu ya maafisa wake kujitosa katika madeni kupindukia kiasi cha kujiua.

Idarai hii haina budi kuchunguza kiini cha mizozo ya kifamilia miongoni mwa maafisa wa polisi na kuwawezesha kupata huduma za ushauri nasaha. Polisi ni binadamu sawa na wengine na wanastahili kusaidiwa.

Polisi wajeruhiwa na mwendawazimu kwenye operesheni

John Njoroge Na Macharia Mwangi

ASKARI wawili wa kitengo cha kukabiliana na wizi wa mifugo walijeruhiwa baada ya kushambuliwa na mwanamume mwenye matatizo ya kiakili eneo la Elburgon, Kaunti ya Nakuru.

Maafisa hao wanaohudumu katika shamba la Cheponde, Elburgon, walishambuliwa kwa panga na mgonjwa huyo maafisa hao walipoenda kumsaidia jirani aliyeomba usaidizi.

“Mmoja wa maafisa hao alikatwa mkononi,”alisema mkazi mmoja.

Wauguzi katika hospitali ya wilaya ya Elburgon walisema afisa huyo alipata majeraha mabaya mkononi.

Katika kisa kingine eneo la Gilgil, polisi wanachunguza kifo cha mwanamume ambaye mwili wake ulipatikana ukining’inia ndani ya nyumba ya familia eneo la Elementaita. Mkuu wa polisi wa eneo hilo (OCPD) Emmanuel Opuru alisema uchunguzi wa awali ulionyesha mtu huyo alijitia kitanzi.

Hata hivyo alisema haikubainika mara moja kilichomsukuma mwanamume huyo kujitoa uhai. “Marehemu hakuacha ujumbe kueleza sababu ya kujiua lakini tunachunguza,” alisema.

 

KURUNZI YA PWANI: Wakazi Mombasa wahofia kuishi na polisi mitaani

NA MOHAMED AHMED

MATUKIO ya mauaji ya vijana kiholela mikononi mwa polisi maeneo ya Mombasa, yamefanya viongozi wa kisiasa, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na wakazi kuhofia mpango mpya wa serikali utakaopelekea polisi kuishi mitaani.

Katika mageuzi hayo ambayo yanatarajiwa kuanza rasmi baada ya miezi mitatu, maafisa wa usalama wanatajariwa kutangamana na raia wa kawaida mitaani katika hatua ambayo Rais Uhuru Kenyatta alisema itafanikisha ushirikiano mwema kati ya polisi na jamii.

Mbali na mauaji ya vijana, wakazi pia wanahofia kuwa huenda magenge yakapata njia rahisi ya kulipiza kisasi kwa polisi watakaokuwa mitaani na hivyo basi kusababisha makabiliano ya mara kwa mara kati yao na polisi, na kuweka raia wasiokuwa na hatia hatarini.

Wakazi wa Kisauni, miongoni mwa maeneo ambayo yamekumbwa na visa vya ukosefu wa usalama walisema kuwa kutangamanisha polisi na jamii kutaongeza visa vya mauaji.

“Ni eneo hili ambapo miezi michache tu polisi aliuliwa na vijana wa magenge ya uhalifu. Ukileta polisi karibu na wakazi ni kama kujenga ugomvi,” akasema Bw Said Mbarak.

Seneta wa Mombasa Mohammed Faki, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na maafisa wa mashirika ya kijamii ya Haki Africa na Muhuri walitaka serikali kutekeleza mageuzi hayo kwa uangalifu mkubwa wakisema kutangamana kwa maafisa wa usalama na raia kwa ukaribu huenda kukaleta shida za kiusalama. Bw Faki alisema kuwa ni lazima mpango huo utekelezwe pole pole na si kwa mpigo ili kuruhusu raia kuzoea hali hiyo mpya.

“Tukiamka tu tuseme kuwa maafisa wa usalama waanze kuishi na raia wa kawaida mitaani ni lazima tujue ni mambo yapi tutafanya ili tusilete madhara yoyote hususan ya kiusalama,” akasema Bw Faki.

Bw Nassir kwa upande wake alisema kuwa hali ya utovu wa usalama ilichangiwa na vifo vinavyosababishwa na polisi na magenge ya wahalifu, na hivyo kutangamana huko na raia kutaongeza shida zaidi.

“Iwapo polisi watabeba silaha hizo hadi majumbani mwao basi kunaweza kukatokea mauaji zaidi ya kiholela,” akasema Bw Nassir.

Mkurugenzi mkuu wa Haki Africa, Hussein Khalid alisisitiza kuwa kuna haja ya mageuzi hayo kufanywa pole pole la sivyo usalama utazidi kudorora hususan Mombasa.

Alisema kuwa tayari visa vya polisi kuua vijana vimekithiri na utangamano huo huenda utachangia mauji zaidi.

“Tayari tuna kesi nyingi za mauaji, mageuzi haya ni sawa ila yafanywe taratibu,” akasema Bw Khalid.

Mkurugenzi wa shirika la Muhuri kwa upande wake alisema kuwa mageuzi hayo yasiwe ya sare za polisi pekee bali na mienendo yao ya kikazi.

Hata hivyo, Bi Shamsa Hemed ambaye ni mkazi wa Mwandoni alikuwa na maoni tofauti. Asema utangamano wa polisi na raia utaleta usalama karibu na jamii.

Alisema kuwa iwapo polisi hao watakuwa karibu na wakazi basi visa vya vijana kuvamia watu kwa visu na mapanga vitapungua.

“Kutakuwa na hofu miongoni mwa wahalifu na hiyo itaruhusu tupate usalama wa kutosha cha muhimu ni kuhakikisha kuwa maafisa hao pia wanapata usalama wao wa kutosha,” akasema Bi Hemed.

#PoliceReforms: Kero mitandoani kuhusu sare za buluu

Na CECIL ODONGO

BAADA ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mabadiliko kadhaa katika Idara ya Polisi Alhamisi, Wakenya mitandaoni wametoa hisia mseto kuhusu hatua ya serikali kuamua maafisa wote watakuwa wakivaa sare zenye rangi ya buluu.

Wakenya wengi walitoa kauli zao katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter wakikosoa na kukejeli rangi na muundo wa sare hizo.

Wengi wao haswa waligusia zabuni inayotarajiwa kutolewa huku wakiuliza nani atapokezwa tenda ya kuuunda sare hizo ikzingatiwa mchakato mzima unaohusisha utoaji zabuni huwa umejaa ufisadi.

Hata hivyo, katika kikao na wanahabari baada ya uzinduzi huo, Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i aliwahakikishia Wakenya kwamba mchakato huo utaendeshwa kwa uwazi wala hakuna hela zozote zitakazopotea.

“Mabadiliko haya tumekadiria itatugharimu kiasi cha fedha ambacho kilitengwa kwenye bajet. Na kupokezwa kwa maafisa wa polisi sare za aina moja ni mojawapo tu ya mabadiliko yatakayogharamiwa na fedha hizo,” akasema Bw Matiang’i

Kupitia hashtegi ya #PoliceReforms, waliokashifu sare hizo walitaja mwonekano wake kama mbovu zaidi na usioweza kutambua maafisa hao kwa umbali

Wakenya 405 walisambaza posti hii kuonyesha kero lao kwa hatua ya kubadilisha rangi ya sare za polisi. Picha/ Twitter

“Hii sare ni mbovu sana. Na ni vipi polisi watazitumia kuwafukuza wezi na mifuko yao pia ni kubwa kuashiria kwamba zitajazwa hela za hongo?” akasema Abdul Burge.

Mwingine kwa jina Sam Muiga naye akashangaa kama swala hilo ndilo linafaa kupewa kipaumbele. “Hili si suala linalofaa kushughulikiwa kwa sasa, tuna maswala mengine muhimu kuliko sare ya polisi,” akasema.”Hakuna kitu spesheli na hizi unifomu mpya. Bado ziko na mifuko mikubwa ya kujazwa hongo,” akasema yaratibu Weah.

Michael Mburu naye aliuliza kwa nini Rais Uhuru Kenyatta aliamua kuzindua sare mpya kwa maafisa hao bila kuyashughulikia matatizo kama mshahara duni na mauaji ya kikatili mikononi mwa magaidi.

@Kinoti alishangaa kwa nini Rais hakugusia swala la nyongeza ya asilimia 16 ya ushuru wa VAT katika bidhaa ya mafuta jinsi Wakenya wengi walitarajia.

@Rais wa “mnataka nifanyaje?’ amefika kuwahutubia na kuwavalisha polisi.

Hata hivyo wengine walisifu sare hiyo wakiitaja kama hatua kubwa kuleta mageuzi katika idara ya polisi.

“Namvulia Rais kofia. Ulimteua waziri ambaye anazidi kuleta mabadilko ya kuenziwa,” akasema Hannah Mukua.

“Mnakaa vizuri lakini saizi yake ipunguzwe kidogo,” akasema The Disruptor.

TAHARIRI: Polisi watumikie wananchi wote

NA MHARIRI

TUKIO la Jumatatu ambapo maafisa wa polisi walifyatua risasi mazishini na kujeruhi watu kadhaa lazima lishutumiwe.

Maafisa hao walijeruhi watu kwa risasi, wakiwemo polisi wenzao ambao ni walinzi wa wabunge, wakati wa mazishi ya dereva wa mbunge wa Likuyani, Dkt Enock Kibunguchy.

Mazishi ya marehemu Douglas Wakachi yalikumbwa na fujo, huku ikibainika kuwa polisi hawajapiga hatua yoyote kumtia mbaroni hata mshukiwa mmoja.

Dereva huyo aliuawa usiku wa Jumapili, Agosti 12 akiwa ndani ya gari la Dkt Kibunguchy, aliyekuwa ameingia ndani ya Highway Motel eneo la Soy.

Japokuwa Naibu kamanda msimamizi wa polisi eneo la Magharibi, Bw Leonard Omollo alisema maafisa wake walianzisha msako wa kuwakamata washukiwa, inangia wiki ya tatu bila ya kuwepo hata fununu kuhusu watu hao.

Hali hii inaibua maswali kuhusu utendakazi wa maafisa waliokabidhiwa jukumu la kulinda maisha ya watu na mali zao. Inaonekana ni kama polisi hutafuta njia za mkato za kusuluhisha mambo, badala aya kufuata sheria inavyosema.

Hali hii ya kutotaka kufuatilia matukio pia inashuhudiwa katika kaunti ya Kericho, ambapo maafisa wa kituo cha Kericho wanakashifiwa kuwa wanajaribu kuficha ukweli kuhusu kilichosababisha kifo cha manafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Kabarak.

Wazazi wa kijana Edwin Kipkemoi wanadai kuwa polisi wamekataa kushirikiana nao ili kujua ukweli kuhusu kilichomuua. Wanalalama kwamba hawajaruhusiwa kuona ripoti iliyopigwa humo.

Matukio haya yanaibua maswali mengi kuhusu kujitolea kwa polisi kuitikia mwito wao wa Utumishi kwa Wote. Je, polisi sasa wamegeuka kuwa wa kuwatumikia watu wakubwa pekee serikalini? Ni kwa nini suala linapomhusu mtu asiyekuwa na ushawishi huwa halipewi uzito wowote?

Kuna maagizo maalum kwa polisi kwamba wawe wakipuuza malalamishi ya wasiokuwa wanasiasa au watu wasio na pesa? Ikiwa hakuna maagizo, ni kwa sababu gani maafisa hawa wanaruhusiwa kufanya kazi kwa kutumia mwongozo wanaojitungia?

Kuna haja ya kutazama upya utendakazi wa maafisa wa polisi. Hata ikibidi kurejelewa kwa upigaji msasa, ni lazima mwananchi anayelipa ushuru wanaolipwa maafisa hao, apewe hadhi yake kama mwajiri nambari moja wa watumishi wa umma.

Familia ya polisi ‘aliyejiua’ yadai haki

Na SAMMY LUTTA

FAMILIA ya afisa wa polisi aliyedaiwa kujinyonga katika Kaunti ya Isiolo sasa inataka kupata haki baada ya mwili kupatikana na majeraha ya risasi. Konstebo Kelvin Aleper Nyanga, 23, wa Kikosi cha Kukabiliana na Dharura (RDU) alikuwa akifanya kazi katika kambi ya Ngarmara hadi mauti yake Julai 11.

Bi Marcella Karenga, dada ya mwendazake alisema maafisa wa RDU wa Isiolo walidai kuwa Aleper alijitia kitanzi lakini familia imepuuzilia mbali taarifa hiyo.

“Tunashuku kwamba jamaa yetu aliuawa kwa risasi. Tunaomba Tume ya Kitaifa ya Haki za (KNCHR) kuanzisha uchunguzi ili kubaini ukweli kuhusu kilichosababisha kifo cha ndugu yangu,” akasema.

Familia ilishikilia kuwa jamaa yao hakuwa na jambo lolote lililokuwa likimsumbua hadi kufikia hatua ya kujiua.

“Tunaamini kuwa aliuawa na tuna haki ya kujua ukweli,” akasema Bi Karenga.

“Nilipigia simu na Inspekta Hassan kutoka Isiolo aliyenifahamisha kwamba ndugu yangu alijiua. Nilimuuliza ikiwa kweli walishuhudia akijiua, wakanijibu kwamba walipata mwili wake bila kujua kiini cha mauti yake.

“Juzi Inspekta alinieleza kwamba ndugu yangu alienda hospitalini kupimwa na aliporejea alikuwa na huzuni. Madai hayo yote hayana mashiko,” akaongezea.

Familia yake inasema kuwa maafisa wenzake walitelekeza mazishi ya mwendazake, kama ishara ya kuonyesha kuwa alijitoa uhai. Waziri wa Kilimo wa Turkana Chris Aletia ambaye pia ni jamaa ya mwndazake alisema hata maafisa walioleta maiti ya mwendazake nyumbani hawakuvalia sare za polisi.

Viongozi wa Turkana wakiongozwa na kiongozi wa Chama cha Thirdway Alliance Party Ekuru Aukot na mbunge wa Loima Jeremiah Lomorukai walihusisha kifo cha Aleper na operesheni dhidi ya wezi wa mifugo inayoendelea katika Kaunti ya Isiolo.

Wanasiasa hao walidai kuwa huenda aliuawa baada ya kushukiwa kuwa huenda alifichua siri kuhusu wizi wa mifugo kwa watu wa jamii yake ya Waturkana.

Mabwanyenye Mlima Kenya wawanunulia polisi magari ya mamilioni

Na NICHOLAS KOMU

MABWANYENYE kutoka eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na Mwenyekiti wa Benki ya Equity Peter Munga wamenunua magari 26 ya thamani ya Sh100 milioni yatakayotumiwa na maafisa wa utawala katika eneo hilo.

Matano kati ya magari hayo ya kifahari yaliyonunuliwa na Wakfu wa Mlima Kenya yalipokezwa Waziri wa Masuala ya Ndani, Dkt Fred Matiang’i Alhamisi mjini Nyeri.

Magari yaliyosalia yatawasilishwa kwa wizara hiyo baadaye. Bw Munga ambaye ndiye mwenyekiti wa Wakfu huo ndiye aliyewasilisha magari hayo kwa Waziri Matiang’i aliyeandamana na Waziri Msaidizi katika Wizara hiyo, Bw Patrick Ole Ntutu na Katibu wa Wizara Karanja Kibicho.

Shughuli hiyo iliendeshwa katika makazi rasmi ya Mshirikishi wa eneo la Kati. Magari hayo ni aina ya Toyota Land Cruiser TX na Mercedes Benz S350.

Bw Munga alisema hatua iliyochukuliwa na wakfu huo inalenga kurejeshwa sifa ya zamani ya utawala wa mkoa.

“Maafisa wa mkoa walikuwa watu wenye mamlaka makuu na ambao waliwakilisha Rais katika maeneo ya mashinani. Tunafaa kuwasaidia kwa kuwapa magari ya kuwawezesha kusafiri katika maeneo wanayosimamia kwa urahisi,” Bw Munga akasema.

Chini ya mpango huo, Washirikishi katika eneo zima la Mlima Kenya watapewa magari aina ya Mercedes Benz huku makamishna wa kaunti wakipewa magari aina ya Land Cruiser na Land Rover.

Magari hayo yataongezea yale ya serikali ambayo maafisa hao wamekuwa wakitumia.

Dkt Matiang’i alishabikia msaada huo huku akitoa wito kwa Wakenya wengine kuiga mfano huo kwa kuchangia katika uboreshaji wa utendakazi wa idara za serikali.

“Huu ni mfano mzuri na kielelezo cha uzalendo. Nyakati nyingi huwa tunalalamikia kutohusishwa kwa umma katika mipango ya serikali. Kila Mkenya ana uhuru wa kushiriki vitendo walivyofanya viongozi wa Wakfu huu,” akasema.

TAHARIRI: IPOA ilikosa kuafikia matarajio ya wengi

Na MHARIRI

Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Polisi ilimaliza hatamu yake Jumatatu ikiwa imekamilisha uchunguzi wa kesi 752 kati ya 9,248 zilizofikishwa kwenye meza yao.

Kulingana na ripoti yao ya mwisho, visa vya utumizi mbaya wa mamlaka vilichukua asili mia 45.1 ya kesi zote zilizoripotiwa huku asili mia iliyobakia ikiwa ni visa kuhusu unyanyasaji unaofanywa na maafisa wa polisi, mauaji ya kiholela na dhuluma za kimapenzi zinazofanywa na maafisa wa usalama.

Kwa kuangalia utendakazi mzima wa bodi hiyo kwa jumla, unaweza kuhisi kwamba haikuafikia matarajio makubwa Wakenya waliokuwa nayo kwa taasisi kama hiyo.

Kufaulu kuhukumu polisi kwa makosa katika visa vitatu pekee katika kipindi cha miaka sita, ni mzaha mkubwa mbali na kuwa kinaya kikuu katika taifa linalosema linafuata sheria.

Ni siri iliyo wazi kwamba katika taifa hili, kitengo cha polisi kiko miongoni mwa taasisi zinazohusishwa na hujuma, dhuluma, mauaji, utepetevu na ukandamizaji wa haki za kimsingi za kibinadamu.

Na kama kunaye anayehitaji mfano mzuri wa jinsi idara ya polisi inavyokandamiza haki za kimsingi za binadamu, basi anahitaji kusoma habari za mauaji ya mwanamke katika Bustani ya City, Nairobi, wikendi iliyopita.

Bi Janet Waiyaki, mama wa watoto watatu wachanga, alimiminiwa risasi na kuuawa akiwa kwenye gari na mwanamume mmoja, ambaye baadaye alifahamika kuwa jamaa yake, Bw Bernard Chege.

Polisi wanasema walishuku wawili hao walikuwa wahalifu waliokuwa ‘katika mazingira ya kutatanisha’ kwa jinsi walivyokosa kufungua dirisha la gari walipotakiwa kufanya hivyo.

Lakini familia inashangaa jinsi maafisa hao wa polisi kutoka Makadara, walivyomiminia gari hilo zaidi ya risasi 15 bila kuwa na ushahidi kwamba wawili hao walikuwa wahalifu.

Kisa hiki kingelikuwa muhimu kwa bodi ya IPOA kuthibitisha umuhimu wa kuweko kazini wakilipwa kitita cha pesa na mlipa ushuru, lakini kwa bodi iliyoshindwa kutoa majibu kuhusu mauaji ya Mtoto Pendo mjini Kisumu, mwaka 2017, pamoja na kuuawa kwa risasi kwa watoto Stephanie Moraa na Geoffrey Mutinda waliokuwa wanacheza nyumbani kwao wakati wa patashika katika ya wafuasi wa NASA na polisi Nairobi, kwa kweli ilikuwa vigumu kutarajia lolote la tija kutoka kwao.

 

Polisi ashtakiwa kumuua mwenzake

Wyclife Nyandisi Motanya (kulia) ambaye ni afisa wa polisi wa zamani akiwa na kondakta Dengah John Lenda kizimbani Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUINGUTI

ALIYEKUWA afisa wa polisi alishtakiwa Alhamisi kwa wizi wa mabavu uliopelekea kuuawa kwa afisa wa polisi.

Wyclife Nyandisi Motanya (afisa wa polisi wa zamani) alishtakiwa pamoja na kondakta wa matatu Dengah John Lenda mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Walikanusha mashtaka kumi na mawili ya kuwaibia abiria katika eneo la Baba Ndogo, Ruaraka kaunti ya Nairobi.

Walikana kuwa mnamo Aprili 28, 2018 walimnyang’anya Koplo Martin Korir bastola.

Wakitekeleza wizi huo, washtakiwa yadaiwa walikuwa na bastola na visu.

Walizuiliwa rumande hadi afisa wa urekebishaji tabia awasilishe ripoti kuwahusu ndipo wawasilishe ombi la kuachiliwa kwa dhamana.

Kesi itatajwa Mei 25.

Polisi wanatumiwa kututishia – Wahadhiri

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Muungano wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini (UASU) na Chama cha wafanyakazi wa vyuo hivyo (KUSU) wameshtumu serikali kwa kutumia polisi kuwashambulia na kuwanyanyasa wahadhiri wanaoshiriki mgomo.

Katibu Mkuu wa UASU Dkt Constantine Wasonga alisema kwamba dhuluma hizo katu hazitawalazimisha kusitisha mgomo huo na kuitaka serikali na manaibu chansela wa vyuo kutumia njia zinazokubalika ili kufikia makubaliano yatakayowarejesha madarasani

Baadhi ya vyuo vikuu alivyovitaja kwamba usimamizi wao umechukuliwa na Polisi ni Masinde Muliro, Maasai Mara, Pwani na Kenyatta.

“Tunalaani kwa kinywa kipana kuendelea kutumiwa kwa wakora na maafisa wa polisi katika vyuo vyetu ili kuwalazimisha wahadhiri kurejea darasani. Mgomo unaendelea wapende wasipende hadi watutatulie maslahi yetu,” akasema Dkt Wasonga.

Katibu huyo pia aliulaumu uongozi wa vyuo vyenyewe wakiwemo manaibu chansela kwa kutumia swala la mgomo kuzua uhasama mkubwa kati ya wahadhiri na wanafunzi. Katika siku za hivi karibuni wanafunzi wa baadhi ya vyuo wamekuwa wakiandamana na kupinga mgomo huo huku wakiwakabili wahadhiri wanaogoma.

“Serikali sasa imeamua kutugonganisha na wanafunzi ambao ni watoto wetu wakifikiria hilo litatutia uoga. Tunawaomba wanafunzi wasiende vyuoni kwa sababu wakora na polisi watawadhuru,” akasema

Aidha, katika onyo kali kwa serikali, kiongozi huyo alisema endapo mwanachama yeyote wa vyama hivyo viwili atajeruhiwa au kufariki kutokana na vitendo vya kihalifu vya polisi basi serikali iwe tayari kupokea lawama kubwa.

Kwa upande wake Dkt Charles Mukhwaya ambaye ni katibu mkuu wa chama cha KUSU alishangaa haja ya wao kuendelea kushirikishwa kwenye mikutano mingi na jopo lililoundwa na waziri wa elimu Amina Mohamed ilhali hawajawasilishiwa pendekezo mbadala la matakwa yao.

“Tunashinda katika vikao na jopo hilo ilhali wanachama wake hawajawahi kutupa pendekezo lao lakini wanatarajia mgomo usitishwe. Dhuluma wanazotenda dhidi ya wahadhiri ndizo zinazidi kutonesha vidonda vyetu,” akasema Dkt Mukhwaya

Wawili hao walikuwa wakizungumza katika mkutano na wanahabari katika makao makuu chama katika Jumba la Unafric mjini Nairobi.

 

Polisi waonya huenda Al-Shaabab watekeleze uvamizi Ramadhan

Na BERNARDINE MUTANU

POLISI wamewatahadharisha Wakenya kuhusu uwezekano wa magaidi wa Al-Shabaab kutekeleza mashambulio wakati wa mwezi mtakatifu wa Ramadhan.

Katika taarifa Jumanne, Polisi walisema makundi ya kigaidi, likiwemo al-Shabaab, yalikuwa yametoa onyo kuhusu mashambulizi kuanzia Mei 15.

“Tunapoelekea mwezi mtakatifu wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza Mei 15, 2018, makundi ya kigaidi yametoa tahadhari na kuwarai wanachama wake kuzidisha mashambulizi wakati huo,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa NPS, Bw Charles Owino katika taarifa.

Makundi mengine yaliyo na mipango hiyo ni ISIS na al-Qaeda, “Ingawa uwezo wa al-Shabaab umelemazwa, tuna habari za kuaminika zinazoashiria kwamba kundi hilo linapanga kutekeleza mashambulizi nchini,” alisema.

Al-Shabaab mara kwa mara waibuka kutekeleza mashambulizi nchini wakati wa Ramadhan hasa katika maeneo ya Pwani na Kaskazini Mashariki na sehemu za miji nchini.

Hivyo, NPS iliwaomba wananchi kuwa makini hasa katika maeneo yaliyo na watu wengi vikiwemo vituo vya mabasi, mahoteli, makanisa, na shule.

Idara hiyo iliwahakikishia wananchi kwamba vikosi vya usalama viko makini, “Tunakagua kwa umakini shughuli zote zinazoendelea katika mpaka wa Kenya na Somalia ili kusambaratisha mashambulizi yoyote dhidi ya Kenya,” alisema Bw Owino.

Wakati huo huo, alisikitikia wananchi walioshambuliwa Mandera katika mgodi wa Shimbir Fatuma. Wakati wa kisa hicho, wananchi wanne walipoteza maisha yao, “Tunaomboleza na familia za waliotuacha na tunaendelea kuwasaka waliotekeleza shambulizi hilo,” aliongeza.

Kulingana na taarifa hiyo, vikosi vya usalama tayari vimewakamata baadhi ya washukiwa wanaosaidia katika uchunguzi wa shambulizi hilo.

Alisema visa vya mashambulizi ya kigaidi nchini vimepungua pakubwa.