Maswali Ruto akiidhinisha wawaniaji ugavana Pwani

Na WAANDISHI WETU

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kina kibarua kizito kuamua watakaowania uongozi wa kaunti za Pwani katika uchaguzi ujao.

Licha ya chama hicho kuhakikishia wanasiasa mara kwa mara kwamba kutakuwa na haki kuchagua wagombeaji wa UDA, Dkt Ruto aliidhinisha wazi baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuwania ugavana wakati wa ziara yake Pwani.

Chama hicho kimefanya mkutano na wagombeaji watarajiwa leo Jumatatu jijini Mombasa, na inatarajiwa kwamba maafisa wa chama wamejitahidi kutuliza wasiwasi kuhusu uwezekano wa mapendeleo katika mchujo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Dkt Ruto alimwidhinisha Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, kurithi kiti cha Gavana Salim Mvurya. Wawili hao walichaguliwa kupitia kwa Jubilee.

Ijapokuwa Bi Achani alihudhuria mkutano ulioongozwa na Dkt Ruto, hakutangaza kujiunga na UDA.

Tikiti hiyo inawaniwa pia na Bw Mangale Lung’anzi.

“Namshukuru Mama Achani kwa sababu yeye atashikilia ile kazi ambayo ndugu yangu Mvurya amefanya. Sisi wote tunasema kazi iendelee,” akasema naibu rais.

Bw Mvurya ni mmoja wa magavana watatu wanaotumikia kipindi cha pili katika ukanda huo, wengine wakiwa ni Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi).

Katika Kaunti ya Mombasa, Dkt Ruto alimwidhinisha aliyekuwa seneta Hassan Omar kuwania ugavana kupitia kwa UDA alipohutubu katika uwanja wa Allidina.

Baadhi ya wafuasi wa chama hicho humtaka Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, ndiye apeperushe bendera ya UDA katika kinyang’anyiro hicho.

“Sisi kama mahasla Kenya nzima, tumejipanga kupambana na mabepari na mabwanyenye. Ni sisi mahasla ambao tutahakikisha tumeleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya kila Mkenya,” Bw Omar alisema Jumapili.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, kufikia sasa ndiye anayetarajiwa kuwa mgombeaji ugavana Kilifi kupitia UDA.

Hata hivyo, bado anakumbwa na kesi zinazohusu madai ya kushiriki ufisadi na mauaji, hali inayotishia azimio lake iwapo masuala hayo yatatumiwa dhidi yake na wapinzani.

“Tuingie katika mambo muhimu ambayo yanatuumiza. Kwanza tuwekane wazi kuhusu njaa hapa Kilifi, hatujawahi kuona gavana Amason Kingi hata siku moja akija mahali hapa na kuwauliza wala kuwaletea chochote,” alisema Bi Jumwa, wakati wa mkutano wa UDA Kilifi.

Katika Kaunti ya Lamu, mwanzilishi wa shirika la kutoa misaada ya kimatibabu la Safari Doctors, Bi Umra Omar ndiye ameonyesha nia ya kuwania ugavana kupitia kwa UDA.

Dkt Ruto alipokuwa Kaunti ya Taita Taveta, imebainika alikutana na aliyekuwa Gavana John Mruttu na Bw Stephen Mwakesi ambao wote wanawania tikiti ya UDA wakitaka kumwondoa Gavana Granton Samboja mamlakani.

Duru zilisema mkutano huo ulinuiwa kuwapatanisha ili kuwe na mgombeaji mmoja, kuzuia mpasuko chamani.

Hata hivyo, mratibu wa UDA katika kaunti hiyo, Bw Scaver Masale, alisema hakuna aliyeshinikizwa kuweka kando maazimio yake ili kuunga mkono mwenzake.

Katika mahojiano ya awali, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake kaunti hiyo, Bi Lydia Haika, alisema kuna mazungumzo yanaendelea ili Mabw Mruttu na Mwakesi wakubaliane kushirikiana.

“Wakishindwa kukubaliana basi watalazimika kuingia katika kura ya mchujo ambayo itakuwa huru na wa haki,” Bi Haika aliambia Taifa Leo.

Ripoti za Siago Cece, Alex Kalama, Lucy Mkanyika na Valentine Obara

Kaunti za Pwani kusaka ?watalii kama eneo moja

Na SIAGO CECE

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa itashirikiana na kaunti zingine za Pwani kuinua sekta ya utalii ambayo imepata pigo kubwa katika miaka ya hivi majuzi.

Kupitia mpango wa ‘Sister Cities’ ambao hulenga kutafuta ushirikiano wa miji ya kimataifa kuvutia utalii, kaunti hiyo ikiongozwa na Gavana Hassan Joho imeanza kutafuta umoja wa Pwani kitalii, ikianza na Kaunti ya Kwale.

Akizungumza katika Hoteli ya Neptune Beach iliyo Diani, Kaunti ya Kwale, Afisa Mkuu wa Vijana, Jinsia na Michezo katika Kaunti ya Mombasa, Bw Innocent Mugabe alisema mpango huo unakusudia kukuza utalii katika eneo lote la Pwani na kuvutia watalii zaidi wa kimataifa ambao idadi yao imepungua kwa sababu ya janga la corona.“Kaunti ya Kwale ni ya kipekee.

Hatuangalii tu Kaunti ya Mombasa, lakini pia kaunti nyingine jirani kwa sababu hatuwezi kuuza Pwani ya Kenya kupitia kwa kaunti moja tu,” Bw Mugabe alisema.

Alikuwa akizungumza alipoandamana na waandishi wa habari na maajenti wa utalii na usafiri kutoka Ukraine waliotembelea Kwale, ili kugundua vivutio ambavyo vinaweza kuwafuraisha watalii wa Kiukreni.

Kaunti ya Mombasa ilitia saini ushirika wa utalii na serikali ya Ukraine kufufua sekta ya utalii kupitia mpango maalumu wa ‘Sister Cities’.

Bw Mugabe aliongeza kuwa Kaunti za Taita Taveta na Kilifi pia zinalengwa kutokana na vivutio kama vile Mbuga ya Wanyama ya Tsavo ambayo inajulikana kwa wanyama pori na uhamiaji wa nyangumi huko Watamu, Kilifi, ambao kwa muda mrefu umevutia watalii kutoka kote ulimwenguni.

Balozi wa Ukraine nchini, Bw Oleksii Sierkov alisema kuwa tayari, ndege zaidi za kukodisha zimepangwa kuleta watalii kutoka nchi yake ambao watatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi, Mombasa.Wiki hii, watalii zaidi ya 200 wanatarajiwa kuwasili Mombasa.

‘Tangu tuanze ushirikiano huu, zaidi ya watalii 1,000 kutoka Ukraine wamefika Kenya na tunatumaini pia kwamba Wakenya wengi watatembelea Ukraine,’ alisema balozi huyo katika mahojiano akiwa Kaunti ya Kwale.

Mkurugenzi wa mpango huo wa Sister City, Bi Salma Noor alisema angalau miji 22 ya kimataifa imekubali kushirikiana na Kenya kupitia mpango huo wakati miji kutoka Ukraine tayari imeahidi kuwa na ndege zao za kukodi kwenda Mombasa.

‘Miji mingine mingi sasa inavutiwa kujisajili nasi na hii itaongeza idadi ya watalii huko Mombasa ambao pia watatembelea kaunti nyingine,’ alisema, akisisitiza kuwa lengo ni kunufaisha kaunti zote katika eneo la Pwani.

Hivi sasa, utalii wa kimataifa umeanza kuimarika Pwani na hoteli nyingi zinarekodi idadi kubwa za watalii kutoka nchi za nje ikilinganishwa na mwaka jana.

Hofu ya Pwani kususia kura za 2022 yatanda

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI katika ukanda wa Pwani wameeleza wasiwasi wao kuwa huenda idadi kubwa ya wananchi wakakosa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa sababu ya hasira kuhusu ahadi ambazo hawakutimiziwa.

Katika maeneo tofauti ya Pwani, matatizo kama vile ukosefu wa ajira, uhaba wa maji safi ya matumizi nyumbani, ukame, usalama duni na shida ya kumiliki ardhi kihalali yamekuwa yakijirudia kila mwaka licha ya viongozi wa maeneo hayo na kitaifa kuahidi kuyatatua.

Akizungumza wakati wa kuzindua shughuli ya kuhamasisha umma kujisajili kuwa wapigakura, Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, alisema kususia kura hakutasaidia kutatua matatizo yaliyopo.

Alikuwa ameandamana na wanasiasa mbalimbali wa Mombasa wakiwemo madiwani.

“Tunapoanza safari hii, wakumbusheni wananchi kwamba baadhi ya suluhu hazitapatikana kama wanafanya maamuzi kwa hasira. Tusisusie kura kwani ni jukumu letu kama wananchi kushiriki ili kuhakikisha sauti zetu zimesikika. Sasa tujitokeze tuhimize watu wajitokeze kujisajili kuwa wapigakura,” akasema Bw Joho.

Kaunti ya Mombasa ni miongoni mwa maeneo ambayo kufikia sasa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imepokea idadi ndogo ya wananchi wanaotaka kujisajili upya kuwa wapigakura.

Kulingana na takwimu za IEBC, tume hiyo inalenga kusajili wapigakura wapya 234,741 Mombasa, 199,428 Kwale, na 331,889 Kilifi.

Katika Kaunti ya Tana River, tume hiyo inalenga wapigakura wapya 44,771, huku ikilenga watu 18,179 Lamu, na 69,063 Taita Taveta.

Usajili huo ulioanza Jumatatu unafanywa katika kila wadi nchini kwa siku 30, ikiwemo wikendi.

Katika Kaunti ya Kilifi, maafisa wa IEBC walieleza hofu kuwa ukame ambao unashuhudiwa katika maeneo ya kaunti hiyo huenda ukaathiri usajili.

“Kutokana na jinsi hali ilivyo katika eneobunge la Ganze, Kaloleni na Magarini, huenda wakazi wakakosa kujitokeza kujiandikisha kwa sababu mtu hawezi kuja hapa kusubiri kusajiliwa ilhali hajui jioni atakula nini,” alisema afisa mshirikishi wa uchaguzi katika Kaunti ya Kilifi, Bw Abdulwahid Hussein.

Zaidi ya wadi 16 za Kaunti ya Kilifi zimeathirika na ukame uliosababishwa na kiangazi cha muda mrefu.

Afisa huyo alisema kufikia Alhamisi, watu 2,919 walikuwa wamejisajili ilhali lengo ni kusajili takriban watu 3,900 kila siku.

Bw Hassan Kibwana ambaye ni afisa wa mipango katika shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre (KECOSCE) aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kusajiliwa ndipo watimize haki yao ya kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Ninajua kuna changamoto nyingi zinazowakumba wakazi kwa sasa ikiwemo uhaba wa chakula ila ninawaomba jitahidini kujikwamua ili muweze kujitokeza kwa wingi kujisajili. Ni kupitia njia hii ndipo tutaweza kubadilisha hali hii inayowakumba kwa sasa,” alisema Bw Kibwana.

Idadi kubwa ya wananchi wanaolengwa kujisajili ni vijana ambao hawakuwa wametimiza umri wa kushiriki uchaguzi uliopita mwaka wa 2017.

Katika Kaunti ya Lamu, wakazi wa vijiji vya msitu wa Boni ambao umekumbwa na changamoto tele za kiusalama bado hawajaanza kujisajili.

Katika mahojiano, Meneja wa IEBC Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Adan, alisema vifaaa vya kusajili wapigakura wapya havijafika msituni Boni kutokana na hofu za kiusalama.

Bw Adan alisema tayari amezungumza na maafisa wa idara ya usalama ili makarani wa IEBC wapewe ulinzi kuwezesha wakazi kushiriki shughuli hiyo ambayo ni haki yao kidemokrasia.

“Kwa sasa vifaa vya kusajili wapiga kura bado tumevihifadhi katika afisi yetu mjini Faza. Nimezungumza na wahusika wa usalama ili kutusaidia kusafirisha vifaa na makarani wetu msituni Boni ili wakazi wa pale pia waanze shughuli ya kujisajili. Tatizo kuu ni utovu wa usalama ambao umekuwa ukishuhudiwa lakini kila kitu kitakuwa shwari,” akasema Bw Adan.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alisema juhudi zinaendelezwa ili makarani wafikishwe enbeo hilo na wakazi wapate fursa ya kujisajili.

“Tutatumia mbinu zote kuhakikisha wakazi wa msitu wa Boni pia wanashiriki shughuli muhimu kujisajili kupiga kura. Wasiwe na shaka. Tunawashughulikia,” akasema Bw Macharia.

Ukanda wa Pwani ni mojawapo ya maeneo nchini ambayo wagombeaji urais hung’ang’ania kura ikizingatiwa kuwa wakati mwingi hakuna mwenyeji anayewania urais ikilinganishwa na maeneo mengine ya nchi yaliyo na idadi kubwa ya wapigakura.

Ripoti za Wachira Mwangi, Alex Kalama na Kalume Kazungu

Pwani: Kiangazi chaleta maafa

KALUME KAZUNGU na SIAGO CECE

KIANGAZI kimesababisha maafa katika kaunti mbalimbali za Pwani, ambapo watu wameauawa na wanyamapori huku mifugo ikiangamia.

Katika Kaunti ya Kwale, watoto wawili wa umri wa mwaka mmoja na miwili waliuawa na kuliwa na fisi wawili katika kijiji cha Baisa, tarafa ya Kinango.

Kisa hicho kilitokea Jumanne majira ya saa tatu unusu asubuhi, fisi hao walipovamia kijiji hicho ghafla.Watoto hao walikuwa wamelala ndani ya nyumba yao wakati mama akitekeleza shughuli za kawaida mita chache kutoka nyumbani humo.

Afisa Mkuu wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kinango, Bw Fred Ombaka, alisema watoto hao hawangeweza kuokolewa kwa kuwa walijeruhiwa vibaya kichwani.

“Wanakijiji waliwawinda fisi hao na wakafaulu kumuua mmoja. Mwengine alitoroka,” akasema Bw Ombaka.Mama wa watoto hao Mulongo Tsimba alipiga kelele zilizovutia wanakijiji ambao walimkabili mmoja wa fisi hao.

Watu wanne walijeruhiwa kwenye makabiliano hayo.“Bi Mulongo ni miongoni mwa wale waliojeruhiwa. Ana majeraha ya kukwaruzwa mikononi, miguuni na usoni. Kalu Chiti na Mutuku Mutinda pia walijeruhiwa mikononi na miguuni na wamelazwa katika hospitali ya Samburu,” alieleza mkuu huyo wa polisi.

Chifu wa kata ndogo ya Chengoni, Bw Jackson Chengo, alisema fisi hao pia walikuwa awali wamevamia na kujeruhi watu wawili katika kijiji jirani.

Miili ya watoto hao wawili imelazwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ya Kinango.Wakazi wa Kinango, hasa wale wanaopakana na mbuga ya wanyama ya Tsavo, wamekuwa wakihangaishwa na wanyamapori wanaorandaranda mitaani wakitafuta maji na chakula msimu huu wa kiangazi.

Ukame pia umeathiri shughuli za masomo kwani wanafunzi hulazimika kufika shuleni kuchelewa, badala ya kurauka na kisha kuvamiwa na wanyama njiani.

Katika Kaunti ya Lamu, zaidi ya ng’ombe 500 tayari wamekufa katika maeneo ya Witu, Dide Waride, Chalaluma, Kitumbini,Nagelle, Pandanguo,Mavuno, Poromoko, Mkunumbi, Koreni, Mpeketoni, Hongwe, Bar’goni na Hindi.

Mkurugenzi wa Shirika la Kukabiliana na Ukame (NDMA) Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Dahir, alisema juma hili watazuru maeneo yote ya Lamu ambayo yanakumbwa na ukame ili kutathmini hali na kukusanya ripoti kamili.

Watu zaidi ya 100, 000 katika kaunti hiyo tayari wanakeketwa na makali ya baa la njaa pamoja na ukosefu wa maji hata ya kunywa.

Mwenyekiti wa Shirika la Mifugo na Masuala ya soko, Bw Kahlif Hirbae, aliiomba serikali kuzindua mpango wa kuwapa wafugaji lishe ya mifugo wao ili kuzuia wanyama hao wasiendelee kufariki kwa sababu ya makali ya ukame.

Bw Hirbae aliiomba serikali na wahisani kuwafidia wafugaji wote ambao wamepoteza mifugo kutokana na ukame ili wajiendeleze maishani.

“Tunahitaji msaada wa chakula cha ng’ombe. Inasikitisha kusikia taarifa kwamba mfugaji mmoja eneo kama vile Nagelle au Kitumbini amepoteza zaidi ya ng’ombe 100. Tunahitaji pia tufidiwe hasara hii,” akaeleza mwenyekiti huyo.

Chama kipya Pwani kinavyotishia Ruto na Raila

Na MAUREEN ONGALA

MIPANGO ya kuzindua chama kipya Pwani kabla uchaguzi ujao ufike, imeshika kasi na kutishia kugeuza mawimbi ya kisiasa katika ukanda huo.

Chama hicho cha Pamoja African Alliance (PAA) kinahusishwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi na wandani wake ambao husema ukanda wa Pwani unastahili kuwa na chama kikubwa kinachotambulika kitaifa.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba, chama hicho ambacho kilikabidhiwa cheti cha muda cha usajili hivi majuzi kinaendelea kujenga afisi zake katika kaunti mbalimbali kinapojiandaa kusajili wanachama.

Mojawapo ya afisi hizo iko katika Kaunti ya Kilifi, ambayo inatarajiwa kuwa makao makuu yake.Chama cha PAA kitatambuliwa kwa rangi za samawati na manjano, huku nembo yake ikiwa nyumba ya kitamaduni ya Kiafrika.

Kulingana na Bw Kingi, rangi ya samawati ilichaguliwa ili kuashiria thamani ya bahari ambayo ni kitegauchumi kikubwa kinachoweza kukomboa ukanda huo ikiwa rasilimali zake zinathaminiwa na kutumiwa inavyostahili.

“Wakati umefika sasa watu waanze kuzoea rangi ya samawati.Hiyo rangi itatenda maajabu hivi karibuni. Jamii inahitaji nyumba, lakini hatuwezi kuwa tukiita watu waungane ilhali wakati huo huo tunaunga mkono vyama vingine,” akasema Bw Kingi.

Uzinduzi wa chama hicho huenda ukawalazimu Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na Naibu Rais, Dkt William Ruto, kupanga upya mikakati yao wakitaka kupata umaarufu Pwani kabla uchaguzi ujao ufanywe.

Dkt Ruto ambaye anatarajiwa kuwania urais kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA), amefanya ziara nyingi Kilifi tangu wakati alipofanikiwa kuwavutia upande wake wabunge walioasi ODM wakiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa.

Kwa upande mwingine, imebainika baadhi ya wanasiasa waliobaki katika ODM wanasubiri chama kipya kizinduliwe ili wajiunge nacho.

Hivi majuzi, Bw Kingi alipokonywa wadhifa wake wa uenyekiti katika ODM kwa kushikilia msimamo wake wa kutaka kuwe na chama kipya kikuu cha Pwani, wazo ambalo limekuwa likipingwa vikali na Bw Odinga.

Gavana huyo pia alikataa miito ya baadhi ya wanasiasa waliomtaka ajiunge na Dkt Ruto ndani ya UDA, akisema njia pekee ya Pwani kujikomboa kutokana na changamoto ambazo zimedumu kwa karne nyingi ni kupitia kwa chama kilicho na mizizi ukanda huo ambacho kitatambulika kitaifa.

Aliwataka wanasiasa wa Pwani wanaofululiza kuingia UDA wajifunze kutoka kwa wenzao wa eneo la Kati ambao wameshikilia msimamo kuwa watashirikiana na viongozi wengine wakiwa ndani ya vyama vyao wenyewe.

“Mkishaapishwa kuwa wabunge na maseneta, mtapitia yale yale ambayo mliyapitia katika ODM kwa sababu chama ni cha wenyewe. Naibu Rais hakunihusisha alipokuwa anaunda UDA, lakini ananialika nijiunge na chama hicho,” alionya.

“Mimi nitakuwa mgeni nikienda huko na baada ya siku tatu sitafurahia kuwa huko ndani. Ikiwa watu wengi wanaomuunga mkono Naibu Rais wameonelea heri wafanye hivyo wakiwa katika vyama vyao, mbona eneo la Pwani liwe tofauti? Tunahitaji chama ambacho kitatetea kikamilifu masilahi ya eneo hili. Hatutaki kutishwatishwa tena,” akasema.

Hata hivyo, alisema wakati haujafika kwa Pwani kusimamisha mgombeaji urais hadi wakati viongozi watakapokuwa na umoja.

“Wapwani wangapi wamewahi kuwania urais lakini wakapata chini ya kura 200? Nakubaliana na wale wanaotaka tujitose katika siasa za kitaifa lakini tujengeni boma letu kwanza,” akasema.

Uamuzi wa kuunda chama kipya ulifanywa baada ya juhudi za kuunganisha vyama vitano vilivyo na mizizi Pwani kugonga mwamba.

Viongozi wa vyama vya Shirikisho, Kadu-Asili, Republican Congress, Communist na Umoja Summit wangali wanasubiriwa kutoa mwelekeo kwa wanachama wao.

Agizo wanafunzi waliokosa kujiunga na sekondari wasakwe

MAUREEN ONGALA na STANLEY NGOTHO

MAELFU ya wanafunzi hawajajiunga na Kidato cha Kwanza katika kaunti mbalimbali nchini, wiki nne tangu wenzao kuripoti.

Katika Kaunti ya Kilifi, Kamishna wa Ukanda wa Pwani, John Elung’ata, alisema kuwa wanafunzi 12,000 hawajajiunga na Kidato cha Kwanza.

Bw Elung’ata alitoa amri kwa machifu na naibu wao kaunti hiyo kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi amejiunga na kidato cha kwanza kabla ya mwezi wa Oktoba.

Bw Elung’ata aliwaomba wasimamizi husika kuwasaka watoto wote ambao hawajaweza kujiunga na Kidato cha Kwanza kutokana na sababu mbalimbali ili wasaidiwe.

Akizungumza na wadau katika shule ya sekondari ya wasichana ya Wakala, Kaunti ndogo ya Magarini, Bw Elung’ata alisema wasimamizi wahusika wanafaa kusimama kidete kuhusiana na masuala ya masomo.

“Machifu wanafaa kuisaidia wizara ya Elimu kutimiza lengo lake la kuhakikisha kuwa kila mtahiniwa wa KCPE amejiunga na sekondari,” akasema Bw Elung’ata.

Aliwahimiza machifu kuhakikisha kuwa watoto wote wanajiunga na kidato cha kwanza bila kujali hali ya kiuchumi ya wazazi wao.Hata hivyo, kamishna wa Kaunti ya Kilifi alisema kuwa tayari machifu wameanza kutimiza jukumu lao.

“Tunaamini ifikapo wiki ijayo, idadi ya watahiniwa watakaojiunga na sekondari itapanda kutoka asilimia 64 hadi asilimia 80,” akasema Bw Olaka.

Katika Kaunti ya Kajiado, zaidi ya wanafunzi 4,000 hawajaripoti katika shule za sekondari.

Wizara ya Elimu katika Kaunti ya Kajiado ilisema kati ya watahiniwa 21,000 waliofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) ni 17,000 pekee waliojiunga na shule za sekondari.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti hiyo Luka Kangogo, alisema huenda wazazi walikosa kupeleka watoto wao shuleni kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na hatua ya machifu kulegeza kamba.

Kingi azidi kubanwa pembeni

Na ALEX KALAMA

CHAMA cha Kadu-Asili kimetilia shaka nia ya Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kuleta umoja wa Pwani na hivyo kuzidi kumsukuma gavana huyo pembeni kisiasa.

Chama hicho ni moja kati ya vitano ambavyo vilitarajiwa kuvunjwa ili kuunda chama kimoja cha Pwani, lakini viongozi wao wakakataa wazo hilo na badala yake kusema wataunda muungano wa vyama.

Kiongozi wa Chama cha Kadu-Asili, Bw Gerald Thoya alidai kuwa Bw Kingi alifahamu nafasi yake ya kuwa maarufu kupitia kwa Chama cha ODM ilikuwa inakaribia kuisha kwa vile atakamilisha kipindi chake cha pili cha uongozi mwaka ujao, na hivyo wito wake wa kuunganisha vyama vya Pwani ulilenga kumnufaisha kibinafsi.

Bw Kingi, ambaye wiki iliyopita alipokonywa wadhifa wake wa uenyekiti wa ODM Kilifi, alikuwa mstari wa mbele kupigania umoja wa wanasiasa wa Pwani kuelekea kwa uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, mapema mwaka huu, alilalamikia jinsi viongozi wengine walivyomwacha pweke katika safari hiyo na hivi majuzi ripoti ziliibuka kwamba ameamua kuunda chama kingine kipya.

“Tangu mwaka wa 2007 sisi tulikuwa tunashinikiza Pwani isimame na chama chake, lakini Kingi akaendelea kubaki katika ODM hadi leo. Mwaka wa 2017 tulikejeliwa kwamba vyama vyetu vya Pwani ni magogo matano kwa vile hatukuwa na mgombea urais,” akasema Bw Thoya.

Vyama vingine vya Pwani ambavyo vilitarajiwa kuungana ni Shirikisho, Republican Congress, Umoja Summit na Communist.

Bw Thoya alifafanua kuwa majadiliano yangali yanaendelea kuhusu uundaji wa muungano wa vyama vya Pwani, akikariri kuwa azimio lililotangazwa Voi mnamo Julai 17 lilipelekea kubuniwa kwa kamati ndogo ambayo itawapa mwelekeo kamili baadaye.

“Naamini kwamba tutapata mwelekeo mwafaka na msingi thabiti wa muungano huo na tutafurahi kuwaeleza wananchi mambo haya hivi punde,” akasema.

Wakati huo huo, wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wamedai kuwa ODM huenda ikawa hatarini kupoteza umaarufu Pwani baada ya kumpokonya Bw Kingi uenyekiti Kilifi.

“Kingi ndiye gavana pekee kutoka Pwani ambaye alisaidia chama hicho kupata uungwaji mkono kwa asilimia kubwa hasa kaunti ya Kilifi. Ambapo kiongozi huyo alisaidia ODM kunyakua viti vyote vikubwa vya uongozi kuanzia ugavana,useneta, uwakilishi wa wanawake na hata ubunge, kwa hivyo ameacha pengo kwenye chama hicho,” alisema mchanganuzi wa siasa, Bw Alfred Katana.

Viongozi wa chama hicho katika Kaunti ya Kilifi walimshutumu gavana huyo kwa kumsaliti kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, alipoanza kupigania uundaji wa chama cha Pwani. Bw Odinga alikuwa akipinga uundaji wa chama hicho akisema kitasababisha siasa za ukabila.

Vile vile, Bw Kingi, ambaye amekuwa akikosa kuhudhuria mikutano ya Bw Odinga maeneo ya Pwani kwa muda mrefu sasa, alilaumiwa kwa kutotoa uongozi bora chamani wakati ambapo vyama vingine vinazidi kujitahidi kutafuta umaarufu kwa maandalizi ya uchaguzi ujao.

Wapwani wakaushwa tena

Na WAANDISHI WETU

MASAIBU yanayokumba wakazi wa Pwani wanapojitafutia riziki yanazidi kuongezeka, baada ya kubainika kuwa, wavuvi wanaotegemea Bahari Hindi sasa wanasukumwa nje na meli kubwa za makampuni ya kigeni.

Katika miaka ya hivi majuzi, mifuko ya wakazi wengi wa Pwani imekauka kwa vile sekta zilizokuwa zikitegemewa sana kiuchumi zimedorora.

Sekta ya uchukuzi ambayo kwa muda mrefu ilitegemewa kutoa nafasi za ajira kwa vijana na wawekezaji ilianza kulemewa punde baada ya reli ya SGR kukamilika.

Hali hiyo ilisababishwa na sera ya serikali kuu iliyohitaji mizigo yote inayotoka Bandari ya Mombasa hadi Nairobi isafirishwe kwa njia ya reli.

Safari za SGR ziliathiri uchukuzi wa abiria kwa basi, hali iliyopunguza mapato kwa makampuni ambayo yalilemewa zaidi wakati janga la corona lilipozuka.

Hitaji kuwa magari ya uchukuzi wa umma yapunguze idadi ya abiria kama mbinu ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, lilifanya baadhi ya makampuni kama vile Modern Coast na Mombasa Raha kusitisha uchukuzi wa abiria kwa muda usiojulikana.

Hatua hii iliwaacha mamia ya watu bila ajira.Sekta ya utalii iliyokuwa imeanza kufufuka baada ya kupata pigo kutoka kwa mashambulizi ya kigaidi, ilififia tena wakati wa janga la corona.

Kufikia sasa, hoteli nyingi za Pwani bado zinatatizika kurejelea hali ya kawaida kwa sababu ya hasara zilizopatikana tangu mwaka uliopita huku idadi ya watalii pia ikipungua pakubwa kutokana na changamoto za usafiri kimataifa zinazoendelea kushuhudiwa.

Walioathirika si wamiliki na waajiriwa wa hoteli kubwa kubwa pekee bali pia wafanyabiashara wadogo kwa kuwa kufikia sasa, fuo nyingi za umma zilizokuwa zikivutia watalii wa humu nchini zingali zimefungwa.

Viongozi wa kisiasa Pwani hawana msimamo mmoja kuhusu namna ya kutatua changamoto hizi kwa sababu ya tofauti zao za kisiasa.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho ambaye katika miaka iliyopita alikuwa mstari wa mbele kushinikiza serikali ikomeshe dhuluma dhidi ya Wapwani, alibadili mtindo wake baada ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuamua kushirikiana kupitia kwa handisheki.

Katika hotuba zake tangu wakati huo, Bw Joho husema uamuzi wake wa kukumbatia mashauriano na viongozi wa kitaifa, akiwemo rais, kuhusu changamoto za Wapwani ndizo zimewezesha miradi mikubwa ya miundomsingi kufanikishwa eneo hilo.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanasisitiza kuwa, Wapwani bado wanateseka licha ya miradi hiyo mikubwa inayojumuisha ujenzi wa barabara, kutekelezwa na na serikali kuu.

“Nilipokuwa nikizungumzia mambo haya awali, watu walidhani nina wazimu, mimi si wazimu. Tumeingia katika siasa sio eti kwa sababu tunapenda siasa ila tunataka kukomboa watu wetu,’ Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali alisema majuzi.

Licha ya kuwa jamii nyingi Pwani zimetegemea uvuvi kama kitega uchumi tangu jadi, sasa kuna ushindani kutoka kwa meli kubwa zinazotumia mbinu ya kukokota nyavu chini ya maji kuvua samaki.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibainisha kuwa, wavuvi wengi sasa wameamua kuacha kwenda baharini na badala yake hununua samaki kutoka kwa wafanyabiashara Wachina.

Mbali na Wachina, imebainika kuwa meli nyingine kubwa zilizopata leseni kuvua samaki nchini humilikiwa na mashirika kutoka Ushelisheli, Italia, Taiwan, na Hong Kong.

Katika mwaka wa 2020 pekee, meli saba kubwa za Uchina zilisajiliwa kufanya uvuvi katika maji makuu humu nchini na leseni zao zitadumu hadi Desemba 2031.

Samaki sasa huvuliwa na meli hizo kubwa kabla wafike katika sehemu za maji ambapo wavuvi Wakenya walikuwa wakitegemea kwa shughuli zao.

Bw Ngole Mbaji ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa kikundi cha kusimamia wavuvi Mtwapa, Kaunti ya Kilifi alisema, serikali pia imechochea masaibu yao kwa sababu kuna sheria za uvuvi zinazobagua wavuvi wadogo.

“Sasa samaki wote sokoni ni wa kutoka kwa Wachina. Wanawake ambao wanauza samaki huwa lazima waamke alfajiri kwenda katika maghala ya Wachina kununua samaki, wasafishe ndipo wauze,” akasema Bw Mbaji.

Kulingana na Bw Mbaji, serikali kupitia kwa Mamlaka ya kusimamia shughuli za majini nchini (KMA) pia ina masharti mengi yanayogharimu pesa nyingi ambazo wavuvi wanaomiliki meli kubwa ndio wana uwezo wa kugharamia.

Masharti hayo ni kama vile kutafuta cheti cha ukaguzi wa boti mara kwa mara, boti ziwe na ubora unaofikia kiwango cha kimataifa, na waendeshaji boti wapokee mafunzo kutoka kwa taasisi ya Bandari Maritime Academy.

Alisema haya yote yanagharimu zaidi ya Sh100,000 ilhali wavuvi wa Pwani huwa na mapato madogo mno.

“Kile KMA imefanya ni kama kuingiza moshi katika mzinga wa nyuki. Wanatumia udhaifu wetu kutufurusha baharini ili tuwaachie nafasi hawa raia wa kigeni,” akasema Bw Mbaji.

Wale wanaoshindwa kuafikia mahitaji hayo hukamatwa na kushtakiwa.Juhudi zetu kutafuta maoni ya KMA kuhusu suala hili ziligonga mwamba kwani Katibu wa Wizara ya Uchukuzi anayesimamia masuala ya baharini, Bi Nancy Karigithu, na Mkurugenzi Mkuu wa KMA, Bw Robert Njue walikataa kujibu maswali yetu.

Haya yote yanashuhudiwa licha ya jinsi maafisa wa serikali wamekuwa wakifanya ziara nyingi Pwani wakiahidi kustawisha sekta ya uvuvi.Mojawapo ya ziara hizo ilifanywa Februari na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Bw Peter Munya alipozindua meli tatu kubwa za uvuvi.

Meli hizo zilizokabidhiwa kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa ziligharimu Sh60 milioni na zililenga kusaidia wavuvi wa eneo hilo.

Msimamizi wa kikundi cha wavuvi wa Mtwapa, Bw Ndago Gunga alisema walipokea boti lakini limeegeshwa muda wote huo na wala hawajanufaika nalo.

“Nakumbuka lililetwa katika msimu wa uvuvi. Tulifurahi sana kwa sababu tulitumai kuvua samaki wengi katika maji makuu. Lakini kabla tuanze kulitumia, tukabainisha kuna vifaa muhimu ambavyo havikuwepo ndani. Tulihitajika kuchanga takriban Sh1 milioni ili kulifanyia ukarabati na kiwango hicho ni kikubwa sana kwetu,” akaeleza.

Utumiaji wake pia ungehitaji nahodha aliyehitimu kuliko wavuvi hao, mekanika wa kulifanyia ukarabati kila mara na mafuta mengi.Hali si tofauti kwa wavuvi wa Kaunti ya Kwale.

Mmoja wa wavuvi, Bw Omar Bonga alisema maisha ya wavuvi yamekuwa magumu mno kwani wanalazimika kuchagua kati ya kuinua uwezo wao wa uvuvi au kutunza familia zao kwa pesa kidogo wanazopata.

“Inatubidi kupunguza chakula chetu kila siku kwa sababu pesa hazitoshi. Hali huwa mbaya zaidi tunapohitajika kulipia matibabu au karo za shule,” akasema.

Huku msimu mwingine wa uvuvi ukianza mwezi huu, wavuvi Wakenya wanahofia ni wavuvi wa kigeni pekee watakaoendelea kunufaika.

Mtihani manaibu 3 wakiendea ugavana

MAUREEN ONGALA na VALENTINE OBARA

MANAIBU gavana wa kaunti tatu za Pwani wanatarajiwa kukabiliana na mibabe wa kisiasa mwaka ujao katika uchaguzi wa ugavana.

Gavana Hassan Joho wa Mombasa, Amason Kingi (Kilifi) na Salim Mvurya (Kwale) wanatumikia kipindi cha pili cha uongozi ambacho ni cha mwisho kikatiba.

Manaibu wao ambao ni Dkt William Kingi (Mombasa), Bw Gideon Saburi (Kilifi) na Bi Fatuma Achani (Kwale) tayari wametangaza maazimio ya kurithi viti hivyo.

Kufikia sasa, ni Bw Mvurya pekee ndiye ambaye amejitokeza wazi kuunga mkono azimio la Bi Achani kati ya magavana hao watatu.

Mabw Kingi na Saburi wana imani kura ya mchujo itafanywa kwa njia huru na ya haki jinsi walivyoahidiwa na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Katika Kaunti ya Kilifi, Bw Saburi anatarajiwa kumenyana na Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro kwenye mchujo wa ODM.

Bw Mung’aro aliwania ugavana 2017 kupitia chama cha Jubilee, akapata kura 56,547 dhidi ya kura 218,686 za Gavana Kingi.

Mbali na Bw Mung’aro, Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa, balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw Dan Kazungu ni miongoni mwa wanasiasa wengine.

Hata hivyo, alisema hatishiwi na wanasiasa wanaomezea mate kiti hicho.

“Kufikia sasa ni mimi pekee ambaye nimetangaza nia ya kuwania ugavana Kilifi kupitia ODM. Tayari niko ndani ya serikali na nitaendeleza kazi aliyoanzisha bosi wangu,” akasema.

Katika Kaunti ya Mombasa, Dkt Kingi anatarajiwa kupigania tikiti ya ODM dhidi ya Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal.

Bw Shahbal aliwania ugavana 2013 na 2017 kupitia Chama cha Wiper na Jubilee mtawalia lakini akashindwa na Bw Joho.

Mbali na hao, kiti hicho kimevutia pia aliyekuwa seneta wa Mombasa, Hassan Omar na Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo, ambao ni wafuasi wa Chama cha UDA kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto.

“Sote tutakutana debeni na kila mmoja wetu atapigania nafasi yake na nitaibuka mshindi. Nimekuwa naibu gavana kwa miaka minne sasa na tumefanikisha mambo mengi kwa jamii,” akasema Dkt Kingi.

Kufikia sasa, wabunge wengi wa ODM Mombasa wametangaza kumuunga mkono Bw Nassir, huku madiwani na washirika wa karibu wa Bw Joho wakiegemea upande wa Bw Shahbal.

Katika Kaunti ya Kwale, Bi Achani ambaye ni mwanachama wa Jubilee hajatangaza ikiwa atatumia chama hicho kuwania ugavana mwaka ujao au la.

JAMVI: Gavana Kingi aning’inia kisiasa Muungano wa Pwani ukijikokota

?ANTHONY KITIMO na VALENTINE OBARA

HATIMA ya Gavana wa Kilifi Amason Kingi katika enzi ijayo ya kisiasa inaendelea kuning’inia huku mazungumzo ya kuleta umoja wa wanasiasa wa Pwani yakizidi kuchelewa kutamatika.

Licha ya joto la kisiasa kutanda katika kaunti hiyo kwa miezi kadhaa sasa, Bw Kingi aliyekuwa mstari wa mbele kupigania uundaji wa muungano wa Pwani kabla 2022 amejituliza tuli.

Wiki iliyopita, Bw Kingi hakuhudhuria mikutano ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kaunti hiyo licha ya kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa chama hicho Kilifi.

Bw Kingi alionekana tu hadharani wakati Rais Uhuru Kenyatta alipozuru kaunti hiyo kukagua miradi ya maendeleo baadaye Alhamisi.

Bw Odinga hakuandamana na Rais kuelekea Kilifi jinsi imekuwa desturi yao kukagua miradi ya maendeleo wakiwa pamoja katika maeneo mengine nchini.

Hotuba nyingi zilizotolewa katika hafla ambazo Bw Odinga alihudhuria zililenga kuwasuta viongozi walioasi chama hicho cha nembo ya chungwa, huku kukiwa na sisitizo kwamba bado kina umaarufu Kilifi.

Kando na ODM, Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kikiongozwa na Naibu Rais William Ruto pia kimekuwa kikiendeleza ziara nyingi katika kaunti hiyo kwa nia ya kufifisha umaarufu wa ODM kabla uchaguzi ujao.

“Mnafahamu vyema kuwa Kiifi ni ngome ya ODM. Watu wengi watasema watakavyo lakini mwishowe ODM ndiyo itavuma Pwani. Tunajua nani atakuwa Ikulu mwaka ujao na tuna imani atakuwa ni Raila Amolo Odinga,” alisema Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo, alipokuwa akikashifu kampeni za mapema zinazoendelezwa na UDA.

Jumapili iliyopita, vyama vitano vya Pwani ambavyo Bw Kingi amekuwa akishinikiza viungane vilikutana mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta kuendelea kupanga mikakati yao.

Mikutano hiyo imekuwa ikifanyika kwa muda mrefu sasa ila uamuzi wa mwisho kuhusu mwelekeo utakaochukuliwa bado haujatolewa.

Vyama hivyo vya Shirikisho Party of Kenya (SPK), Kadu-Asili, Republican Congress Party of Kenya, Umoja Summit Party of Kenya (USPK) na Communist Party of Kenya vimeamua havitavunjwa kuunda chama kimoja bali vitaungana kuunda muungano wa vyama vya kisiasa vilivyo na mizizi yao Pwani.

Kwa msingi huu, huenda Bw Kingi atalazimika kuhamia mojawapo ya vyama hivyo ikiwa bado anaazimia kuendeleza juhudi za kuleta umoja wa Wapwani kisiasa ifikapo 2022.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Katibu Mkuu wa Chama cha Shirikisho, Bw Adam Mbeto, alisema kufikia sasa uamuzi ambao umefanywa ni kuunda muungano wa vyama vya kisiasa ila uamuzi wa mwisho bado haujafanywa.

“Hatutakuwa na chama kimoja bali muungano wa vyama. Mazungumzo bado yanaendelea kuhusu suala hilo,” akasema Bw Mbeto kupitia kwa mahojiano ya simu Alhamisi iliyopita.

Bw Kingi ambaye ni mmoja wa magavana wa Pwani wanaotumikia kipindi cha pili ambacho ni cha mwisho cha ugavana hajakuwa wazi kuhusu maazimio yake ya baadaye kisiasa akilinganishwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye amekuwa akijiandaa kuwania urais.

Katika Kaunti ya Kwale, Gavana Mvurya ambaye ni mwanachama wa Jubilee pia amekuwa akielezea nia yake ya kujitosa katika siasa za kitaifa wakati atakapokamilisha kipindi chake cha ugavana mwaka ujao.

Bw Mbeto aliambia Taifa Jumapili kwamba vyama vitano vya Pwani sasa vimeunda kamati ambazo zitatoa mwelekeo wa kisiasa kwa Wapwani hivi karibuni.Imebainika kamati hizo ziko chini ya makundi ya Coast Initiative Development Initiative (CIDI) na Coast Political Parties’ Convention (CPPC) ambayo yatashauriana na kutoa mwongozo wa kiuchumi na kisiasa mtawalia utakaowanufaisha Wapwani.

Vile vile, imebainika kuwa mashauriano hayo yatalenga kutoa mwongozo wa jinsi muungano utafaa kuundwa ili kuunganisha manifesto ya vyama vyote tanzu bila kusababisha migogoro.

Miezi michache iliyopita, Bw Kingi alisuta viongozi wanaokashifu uundaji wa muungano wa vyama ambavyo vina mizizi Pwani kwa madai kuwa mpango huo ni wa kikabila.

Alisema vyama vinavyoendeleza mashauriano vimesajiliwa kama vyama vya kitaifa kwa hivyo vina uhuru wa kutafuta vingine kuunda nao muungano.

“Hakuna chama kinaundwa hapa, ni vyama vya kitaifa vimeundwa kisheria vinakuja pamoja kumiliki ngome yao. Kwa hivyo jambo hili lisichukuliwe kikabila,” alisema Bw Kingi.

Bw Joho ambaye pia ni naibu kiongozi wa ODM alisema Pwani itaendelea kuwa ngome ya kisiasa ya ODM na hakuna nafasi kwa chama kingine chochote, kiwe kipo tayari au kinatarajiwa kuundwa, kuchukua nafasi hiyo.

“Tumeona watu wakijaribu kupenya eneo la Pwani na kujaribu kuwashawishi wanachama wa ODM waondoke chamani. Nataka kuwaambia sisi hatulali na tutalinda wanachama wetu. Tumejifunza kutoka eneo la kati ambapo kuna watu waliohamia vyama vingine bila mpangilio,” akasema.

Alisisitiza kuwa chama hicho ndicho kitaunda serikali ijayo kwa hivyo haitakuwa busara kwa Wapwani kuanza kufikiria kuelekea kwingine wakati huu.

Ukabila sumu ya chama cha Pwani

MAUREEN ONGALA na VALENTINE OBARA

NDOTO ya tangu jadi ya ukanda wa Pwani kuwa na chama kimoja au muungano wa kieneo huenda ikasalia kuwa ndoto daima dahari iwapo vizingiti viwili vikuu havitaondolewa.

Mipango na mikakati ya kuunda ‘chama cha Wapwani’ ambayo imekuwapo kwa miaka na vikaka imekuwa ikiambulia patupu kila mara.

Hata hivyo, imefichuka kuwa kizingiti kikuu katika kufanikisha ndoto hiyo ni ukabila baina ya wanasiasa wanaojiona kuwa Wamijikenda na wale wanaochukuliwa kuwa ‘chotara’, pamoja na ubabe wa kisiasa ambapo kila kigogo anataka awe ndiye anakaa kileleni.

Sababu kuu zilizoleta vikwazo kwa juhudi za baadhi ya wanasiasa kubuni chama kimoja cha Pwani kitakachotumiwa mwaka wa 2022, zimeanza kufichuka.

Kwa mujibu wa wanasiasa wa eneo hili, juhudi hizo ambazo zilishika kasi mapema mwaka 2021 zilianza kufifia ilipobainika kuwa kuna baadhi ya viongozi walioweka mbele masilahi ya kikabila, huku wengine wakiwa na maazimio ya kutumia juhudi hizo kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Imebainika kuwa, ukabila ni mojawapo ya sababu ambazo zilisababisha mgawanyiko kati ya viongozi waliotaka kigogo atakayechaguliwa kuongoza chama hicho kipya awe Mmijikenda, na wale walio na mtazamo kuwa Pwani ina mchanganyiko mkubwa wa makabila ambapo mengine hayafai kubaguliwa.

Mahojiano ambayo Taifa Jumapili ilifanyia baadhi ya viongozi wa kisiasa na wa kijamii wanaofahamu kuhusu mazungumzo ya kutafuta chama kimoja cha Pwani yalibainisha kuwa kikundi hicho cha kwanza kilikuwa kikipendekeza Gavana wa Kilifi Amason Kingi au mwenzake wa Kwale, Bw Salim Mvura ndiye awe msemaji wa kisiasa Pwani.

Magavana hao wawili pamoja na mwenzao wa Mombasa, Bw Hassan Joho wanatumikia kipindi cha pili cha uongozi na wote wanaelekeza macho yao kwa siasa za kitaifa mwaka ujao.

Hii inamaanisha kuwa, mmoja wao tu ndiye aliye na nafasi nzuri kupewa mamlaka ya kushauriana na serikali kuu au wanasiasa wanaopanga kuwania urais 2022 kuhusu mahitaji ya Wapwani, na hata pengine achaguliwe kuwa mgombea mwenza au apewe wadhifa mwingine mkubwa katika serikali ijayo.

Mshirikishi wa muungano wa wazee wa Kaya eneo la Pwani, Bw Tsuma Nzai asema lilikuwa pendekezo la wazee kwamba kinara wa chama kitakachobuniwa awe ni Mmijikenda lakini wazo hilo likachukuliwa vibaya na wanasiasa wengine.

Alilaumu wanasiasa wanaopinga pendekezo hilo kwa kurudisha nyuma juhudi za kuleta umoja wa Pwani.

“Ikiwa sisi tunapigania kuwa na kinara wa Pwani ambaye atakuwa Mmijikenda ilhali Gavana Kingi akiongea, kuna viongozi na wanasiasa wetu wanaompinga na kumpura mawe, ni dhahiri kuwa wao ndio wenye matatizo na wanarudisha safari yetu nyuma kila kukicha,” akasema.

Hii ni licha ya kuwa Bw Kingi amekuwa akisema mipango ya kubuni chama hicho si kwa minajili ya kumwinua yeye binafsi bali kupata nafasi bora ya kutetea masilahi ya Wapwani katika siasa za kitaifa.

Hivi majuzi, Bw Joho ambaye tayari aliwasilisha ombi kwa Chama cha ODM kutaka kupigania tikiti ya kuwania urais 2022, alikashifu siasa za kikabila Pwani.

Alipokuwa akihutubu wakati wa kuzindua kituo maalumu cha matibabu ya moyo katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, Bw Joho alisisitiza kuwa Pwani hujivunia umoja wa makabila mengi na haifai mtu yeyote kuanza kuingiza ukabila.

“Nasikia wengine wakisema mambo ya ukabila. Hapa Mombasa hatutaki ukabila. Tunataka nchi nzima ijifunze kutoka kwetu kuhusu jinsi tunaweza kuinuana kimaisha kwa ushirikiano bila kujali misingi ya kikabila,” akasema.

Kando na haya, imebainika kuwa suala jingine ambalo limetatiza uundaji wa chama cha Pwani ni ubabe wa viongozi wa kisiasa.

Kwa mujibu wa wanasiasa eneo hilo, kulikuwa na mivutano tele hasa kuhusu malengo makuu ya chama ambacho kingeundwa.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, alidai kuwa mvutano mkubwa ulisababishwa na malengo kati ya viongozi wanaopanga kuingia kwa siasa za kitaifa, na wale ambao bado wanatarajia kuwania viti vya mashinani kama vile ubunge, useneta, udiwani na ugavana.

Kulingana naye, viongozi wanaolenga mamlaka katika serikali kuu 2022 walijali sana mashauriano yanayohusu nafasi watakazopata katika serikali ijayo, ilhali wale watakaoendelea kuwania viti vya mashinani walijali jinsi watakavyoshawishi wananchi kuwapigia kura.

Akizungumza katika mahojiano ya redio, Bi Jumwa alisema kwamba kikundi hicho cha pili cha wanasiasa ndicho kilitaka kuwe na chama kitakachotoa kipaumbele kwa majadiliano kuhusu masuala yanayohusu mwananchi moja kwa moja kama vile ugavi wa rasilimali za serikali ya kitaifa.

“Tunachoona kwa sasa ni kuwa hakuna nia. Wale viongozi, hasa magavana wanataka kuzungumza kuhusu Pwani ila wanachowazia ni hatima yao baada ya 2022. Huwa tunazungumza kwa sauti moja tukiwapangia nafasi zao zitakavyokuwa baada ya 2022, lakini hawataki kuongelea kile ambacho mwananchi atafanyiwa. Hapo ndipo tofauti inakuja baina yetu,” akaeleza.

Mbunge wa Magarini, Bw William Kingi alitoa kauli sawa na hii, akiongeza kuwa changamoto nyingine iliyotatiza uundaji wa chama cha Pwani ni jinsi juhudi hizo zilivyoingiliwa na vigogo wa kisiasa wanaotoka nje ya Pwani.

Kwa miaka mingi, eneo hilo limekuwa miongoni mwa yale yanayovutia wagombeaji wa urais lakini huwa laegemea sana upande wa upinzani.

Huku akieleza matumaini yake kuwa chama hicho hatimaye kitabuniwa kabla 2022 na akitumie kuwania ugavana Kilifi, mbunge huyo alisema kuna wanasiasa wa kitaifa ambao wanajua watakuwa hatarini kupoteza kura za urais endapo Wapwani wataamua kusimama kwa umoja jinsi inavyofanyika katika maeneo mengine kama vile Nyanza na eneo la Kati.

Imesemekana kuwa, baadhi ya wanasiasa bado wanalazimika kuwa waaminifu kwa viongozi wa vyama walivyotumia kuingia mamlakani 2017, au vyama ambavyo walihamia tangu wakati huo.

“Ninajua kuna vita vikali dhidi ya wabunge wa Pwani ambao wangali wanaendeleza juhudi za kuunda chama cha Pwani, lakini tutasimama imara. Mazungumzo bado yanaendelea na ifikapo 2022, eneo la Pwani litakuwa na chama chake. Kumekuwa na changamoto kuleta umoja wa eneo hili kwa sababu baadhi ya wanasiasa ni wabinafsi wanaotaka kulinda maslahi yao ya kisiasa,” akasema.

Vyama vinne vya Pwani ambavyo vilitambuliwa ili viongozi wao washauriane kuunda muungano au chama kimoja cha Pwani ni Kadu-Asili, Umoja Summit, Shirikisho na Republican Congress Party.

Hii si mara ya kwanza ambapo viongozi wa Pwani wanashindwa kuungana kisiasa.

Katika mwaka wa 2016, Waziri wa Ugatuzi Gideon Mung’aro ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Kilifi Kaskazini, aliongoza kupitishwa kwa Azimio la Dabaso lililoleta pamoja baadhi ya viongozi wa Pwani ambao walisisitiza wito wa kuunda chama kimoja cha Pwani.

Kaunti pwani zapigwa darubini kuhusu miradi hewa

Na WAANDISHI WETU

BAJETI ya Serikali ya Kaunti ya Tana River, imekosolewa baada ya kubainika kuwa Sh100 milioni zilitengwa kwa ujenzi wa makao makuu ya kaunti katika eneo tofauti na lile ambako ujenzi ulikuwa unaendelea awali.

Kulingana na bajeti hiyo, pesa hizo zitatumiwa kujenga makao makuu katika miji ya Garsen na Madogo. Hii ni licha ya kuwa, kuna ujenzi unaogharimu Sh200 milioni katika kijiji cha Dayate, eneobunge la Galole ambao umefadhiliwa na kaunti hiyo kwa ushirikiano na serikali kuu.

“Hakuna chochote kama makao makuu Garsen na Madogo, na hakuna ushahidi wowote wa ujenzi unaoendelea maeneo hayo ambao unahitaji kukamilishwa,” akasema Katibu Mkuu wa shirika la kijamii la Tana River Civil Association, Bw James Onchaga.

Kando na hayo, miradi mingine haijafafanuliwa itajengwa wapi na hivyo kuibua changamoto endapo kuna wananchi au mashirika huru ambayo yatataka kufuatilia utekelezaji.

Juhudi zetu kutafuta ufafanuzi hazikufua dafu kwani Waziri wa Fedha katika kaunti hiyo, Bw Mathew Babwoya hakushika simu wala kujibu ujumbe aliotumiwa.

Katika Kaunti ya Lamu, Sh33 milioni zilitengewa ujenzi wa makazi ya Gavana huku Sh38 milioni zingine zikitengwa kukamilisha ujenzi wa jengo la makao mkuu ya kaunti ya Lamu lililoko mjini Mokowe.

Katika Kaunti ya Mombasa, idara ya afya imetengewa asilimia 25 ya bajeti ya Sh14.3 bilioni, ambayo ni sawa na Sh3.6 bilioni. Imefuatwa na idara ya maji na usafi (Sh1.23 bilioni), ujenzi na uchukuzi (Sh1.19 bilioni) na elimu na teknolojia ya habari (Sh1 bilioni).

Ripoti za Stephen Oduor, Kalume Kazungu, Siago Cece, Wachira Mwangi na Alex Kalama

WAPWANI WAPIGWA DAFRAU

Na CHARLES LWANGA

MPANGO wa kuunda muungano wa Pwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022, umechukua mkondo mpya baada ya kuibuka kuwa mashauriano yao yameingiliwa na vyama kutoka maeneo mengine ya nchi.

Taifa Leo imefahamu kuwa vigogo wa siasa kutoka nje ya Pwani hawataki Wapwani kuungana wenyewe, mbali vinataka waungane na vyama vyao.

Njama ya vyama vya kitaifa kuingilia mazungumzo ya kuunda chama cha Wapwani zilifichuka baada ya chama cha Kadu-Asili kutangaza kimejiondoa katika mazungumzo hayo wikendi kikidai hakuna hatua zinazopigwa.

Chama hicho ni kati ya vinne vya Pwani ambavyo vilitarajiwa kuunganishwa kwa madhumuni ya kuunda chama kimoja au muungano wa vyama utakaotambuliwa kuwa wa Pwani. Vyama vingine ni Umoja Summit, Shirikisho na Republican Congress Party.

Afisa wa ngazi ya juu katika mojawapo ya vyama hivyo, alifichua kwa Taifa Leo kuwa kuna vyama mashuhuri vya kitaifa ambavyo vimeanza kuingilia mazungumzo yao ili kuzuia kuungana kwa vyama asili vya Pwani.

Haikubainika mara moja ni vigogo gani wa kisiasa ambao wameingilia mazungumzo hayo, lakini baadhi wamekuwa wakionyesha nia ya kuthibiti siasa za Pwani kwa ajili ya kura za eneo hilo.

Vyama vya kitaifa ambavyo vimeonyesha nia kubwa ya kukita mizizi Pwani 2022 ni ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, na United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Vingine ni Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka, Amani National Congress (ANC) ambacho kiongozi wake ni Musalia Mudavadi na KANU chake Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Gavana wa Kilifi, Amason Kingi, ambaye amekuwa akiongoza kampeni ya umoja wa Pwani, kusema kuwa huenda juhudi za kuleta umoja wa Wapwani zikasambaratika baada ya wanasiasa kadhaa wa ukanda huo kususia wito wake.

Baadhi ya wanasiasa waliojiondoa katika mipango hiyo wakishuku kuwa Bw Kingi ana nia fiche, madai ambayo amekuwa akiyapinga kila mara.

Juhudi za muungano huo zilianza kuyumbayumba mapema Aprili wakati Bw Kingi na Gavana Hassan Joho walipoanza kuvuta pande tofauti kwa kufanya mikutano miwili sambamba.

Bw Joho anasisitiza kuwa nia yake ni kuunganisha Pwani ndani ya ODM, Kingi anataka kubuniwa kwa chama kipywa ilhali Gavana Salim Mvurya wa Kwale anatarajia kunganisha eneo hilo nyuma ya Naibu Rais William Ruto.

Pigo lingine lilikuwa ni tofauti zilizoibuka kuhusu suala la vyama husika kuvunjwa ili kubuni chama kimoja.

Kinara wa Kadu-Asili, Bw Gerald Thoya alisema chama chake kiliamua kujiondoa katika mipango hiyo baada ya mazungumzo ya umoja wa vyama vya Pwani kukwama.

“Mazungumzo haya yamegonga mwamba kwa sababu hadi leo hatujaelewana na muda unayoyoma. Hatuwezi kuketi tukisubiri mpango ambao vyama vyote vinne vimekosa kuelewana kuuhusu,” akasema.

Hata hivyo, viongozi wa vyama vitatu vilivyosalia walisema mazungumzo yangali yanaendelea na wana matumaini kuwa yatazaa matunda.

Katibu Mkuu wa Chama cha Umoja Summit, Bi Naomi Cidi alisema dhana kuwa Wapwani hawawezi kujisimamia kisiasa wala kufanya uamuzi peke yao lazima ikabiliwe vilivyo.

“Hii ni dhana mbaya ambayo tunaipinga na hivi karibuni tutatangaza uamuzi wetu,” akasema Bi Cidi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Republican Congress Party, Bw Ibrahim Khamisi aliwaomba wakazi wa Pwani wawe na subira mazungumzo yakiendelea.

Naye Bw Adam Mbeto, katibu mkuu wa Chama cha Shirikisho, alisema licha ya misukosuko, jambo la maana ni kuwa vyama vyote vinne vimekubalina kuhusu umoja wa Wapwani, na ana matumani kuwa watafaulu kuunganisha vyama hivyo vinne.

Vigogo wa Pwani lawamani kwa maneno matupu

Na CHARLES LWANGA

VIONGOZI wakuu Pwani wako hatarini kupata sifa mbaya ya kukosa kuonyesha vitendo kwa mipango ya kisiasa ambayo huwa wanahimiza kwa wananchi mara kwa mara.

Miaka mitatu iliyopita, Gavana wa Kilifi Amason Kingi na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho, walifufua wito wa kuitaka Pwani ijitenge na Kenya walipokuwa wakipinga utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, wito huo ulififia baada ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kukubaliana kushirikiana kupitia mpango wao wa handisheki baadaye 2018.

Bw Joho husisitiza kuwa hapakuwa na haja kuendeleza mtindo huo wa kisiasa kwani walipewa nafasi ya kushauriana moja kwa moja na serikali kuu kuhusu changamoto zinazokumba Wapwani.

Hali sawa na hii sasa inaelekea kukumba wito wa uundaji chama au muungano mmoja wa vyama vya Pwani kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Wito huo uliokuwa umeanza kwa kishindo umezidi kufifia baada ya Bw Joho kujiandikisha kupigania tikiti ya ODM kuwania urais 2022.

Kwa upande mwingine, wanasiasa wengine wameashiria kujiunga na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho kinahusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Wanasiasa hao wakiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, tayari wameunda kamati maalumu itakayopendekeza kiongozi wa Pwani ambaye jina lake litawasilishwa kwa Dkt Ruto kumzingatia kama mgombea mwenza wake, na pia itatoa ripoti kuhusu matarajio ya Wapwani kutoka wa naibu rais iwapo ataunda serikali ijayo.

Kando na hayo, juhudi za viongozi wa kaunti sita za Pwani kushirikiana katika sera hasa za kuimarisha uchumi kupitia kwa Jumuiya ya Kaunti za Pwani (JKP) pia zimeonekana kwenda mwendo wa kobe.

Mnamo Februari, wakati Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa JKP, iliwabidi magavana kutoa wito kwa wadau husika wakaze kamba zaidi kufanikisha maazimio ya jumuiya hiyo.

Kulingana na Bw Steve Obaga, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa Malindi, kuna uwezekano wanasiasa Pwani bado hawana hakika kama wana uwezo wa kutosha kushindana na vyama vingine vikubwa kama vile ODM, Wiper na Jubilee ndiposa juhudi zao za kuungana hugonga mwamba.

Bw Obaga anasema kuwa, kuungana kwa wanasiasa hao kutamaanisha watahitajika kushindana na vyama hivyo ambavyo havitakosa wagombeaji uchaguzini.

“Wapwani wana desturi ya kuwa hawaungi mkono vyama vya eneo hilo. Hata marehemu Karisa Maitha aliyekuwa mbunge wa Kisauni, alijaribu kuleta umoja ukanda huo lakini hakufanikiwa,” akasema.

Kando na Maitha, juhudi kama hizi ziliwahi kujaribiwa miaka mingi iliyopita zikiongozwa na aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Kenya African Democratic Union (Kadu), Ronald Ngala.

Uhuru apangiwa kuzuru Pwani baada ya Raila

ANTHONY KITIMO na CHARLES LWANGA

RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzuru Pwani wiki hii, siku chache baada ya Mahakama Kuu kuharamisha urekebishaji katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Ingawa ratiba rasmi kuhusu ziara ya rais haijatolewa, anatarajiwa kutembelea miradi ya maendeleo katika ukanda huo.

Kufikia jana, Rais Kenyatta alikuwa hajaeleza hisia zake kuhusu uamuzi wa majaji watano wa Mahakama Kuu kuharamisha BBI.

Kwa upande mwingine, ilifichuka kuwa mwasisi mwenzake wa BBI aliye kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga tayari alikuwa ametua Pwani wikendi.

Hata hivyo, duru ziliambia Taifa Leo kwamba ziara ya Bw Odinga Kaunti ya Kilifi ilikuwa ya kibinafsi na bado haijulikani kama watakutana na rais atakapowasili.

Mnamo Jumamosi, alikutana na naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe, Katibu Mkuu Muungano wa vyama vya wafanyakazi Francis Atwoli, Magavana Ali Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi) miongoni mwa wanasiasa wengine. Mkutano huo ulitajwa kuwa wa chakula cha mchana.

Matarajio makuu kuhusu ziara yake ya Pwani ni kwamba atasimamia kushuhudiwa kwa meli mbili za kwanza za usafirishaji mizigo zikitia nanga katika Bandari ya Lamu mnamo Alhamisi.

Meli ya Mv CAP Carmel yenye urefu wa mita 204 inayotarajiwa kusafirisha mizigo mbalimbali kutoka Dae es Salaam, itakuwa ya kwanza kutia nanga Lamu kabla ielekee Bandari ya Salalah iliyo Oman baadaye.

Meli ya pili iliyopangiwa kutia nanga hapo dakika chache baadaye ni ile ya Mv Seago Bremen Kaven kutoka Mombasa ambayo itakuwa ikisafirisha parachichi.

Mamlaka ya Kusimamia Bandari za Kenya (KPA) pamoja na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) tayari zimeanza kutamatisha mipango muhimu kabla hafla hiyo inayotarajiwa kubadilisha uchumi wa Pwani na Kenya kwa jumla.

Kapteni Geoffrey Namadoa kutoka KPA alisema MV CAP Carmel ambayo ina bendera ya Singapore, ina uwezo wa kupakia na kupakua mizigo bandarini bila kutumia kreni.

“Kulingana na orodha ya shehena tuliyopokea, tunatarajia kuhudumia kontena 100 za meli katika siku ya kwanza bandarini Lamu. Shehena hizo zitatumiwa kufanyia majaribio barabara inayoelekea bandarini ambayo ujenzi wake umekamilika,” akasema Bw Namadoa.

Alieleza kuwa bandari hiyo imejengwa mahali pazuri ambapo itakuwa mshindani mkubwa wa bandari nyingine zilizoendelea kimataifa kama vile ya Durban, Afrika Kusini.

Kwa upande mwingine, meneja mkuu wa kitengo cha huduma za baharini katika KRA, Bw John Bisonga, alisema wanakamilisha kuweka mitambo ambayo itazuia usafirishaji wa bidhaa haramu kupitia kwa Bandari ya Lamu.

“KRA inafahamu fika kwamba wahalifu huenda wakajaribu kutumia bandari ya Lamu kwa shughuli zisizokubaliwa kisheria lakini tumepeleka rasilimali zote zinazohitajika ikiwemo wahudumu na mitambo,” akasema.

Kando na kutumia mitambo ya kitekinolojia, Bw Bisonga alisema kutakuwa pia na mbwa wa kunusanusa iwapo hilo litahitajika mara kwa mara.

Serikali imewapa wafanyabiashara vichocheo vya kuwavutia ikiwemo uhifadhi mizigo kwa siku 60 bila malipo kwa wanaosafirisha bidhaa kupitia Lamu, badala ya siku 21 ambazo hutolewa katika Bandari ya Mombasa.

Shule za Pwani zakosa kung’aa KCSE

Na WAANDISHI WETU

SHULE za Pwani zilikosa kung’aa katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili yaliyotangazwa jana. Katika orodha ya watahiniwa 15 bora iliyotangazwa na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, hapakuwa na mwanafunzi yeyote kutoka kaunti za Pwani.

Vile vile, orodha ya watahiniwa 10 walioteleza katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) miaka minne iliyopita kisha wakabobea katika KCSE ya 2020, haikuwa na yeyote kutoka Pwani.

Kwa mujibu wa jedwali la matokeo ya shule za Pwani yaliyokusanywa na Taifa Leo, Assya Abubakar Ali ambaye ni msichana aliyesomea Shule ya Upili ya Sheikh Khalifa Bin Zayed, aliibuka nafasi ya kwanza akiwa na Gredi A ya alama 82.

Alifuatwa na Ashraf Mohammed Hassan wa Shule ya Upili ya Memon aliyepata Gredi A ya alama 81, na Sumayya Ahmed Mohammed wa Shule ya Upili ya Qubaa Muslim ambaye pia alipata alama sawa na hizo.Kitaifa, mwanafunzi aliyeibuka nafasi ya kwanza, Simiyu Robin Wanjala, mwanafunzi wa kiume aliyesoma katika Shule ya Upili ya Murang’a, alipata Gredi A ya alama 87.3.

Orodha ya 15 bora kitaifa ilifungwa na Buluma Daizy Nerima, mwanafunzi wa kike aliyepata Gredi A ya alama 86.9.Matokeo yaliyokusanywa na Taifa Leo, yalionyesha kuwa shule za kibinafsi za Pwani ndizo zilizotoa wanafunzi wengi waliopita mitihani hiyo.

Shule hizo ni Sheikh Khalifa Bin Zayed, Memon High, Qubaa Muslim, Abu Hureira na Istiqama High.Kwa upande mwingine, shule za umma zilizong’aa Pwani ni kama vile Dr Aggrey iliyo Kaunti ya Taita Taveta, Kwale High, Mambrui (Kaunti ya Kilifi), na Murray Girls (Taita Taveta).

Katika mahojiano na Taifa Leo, baadhi ya wanafunzi waliopata matokeo bora Pwani walieleza furaha yao huku wakiwa na matumaini kuhusu maisha yao ya usoni.

Nasia alisema kuwa alifanya bidii katika masomo yake na kuhoji kuwa ushirikiano mzuri baina ya walimu, wazazi na wanafunzi wenzake ulichangia kupata matokeo mazuri.

“Sikuwa natarajia kupata alama nzuri hivi kwani nilipata alama ya B kwenye mtihani wa majaribio. Lakini namshukuru Mungu kwa matokeo mazuri,’ alisema.

Alisema kuwa angependa kusomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Nairobi.Ingawaje ugonjwa wa corona ulikatiza masomo shuleni kwa muda mrefu, msichana huyo alisema kuwa alifanya bidii hata akiwa nyumbani.

“Hii ilihakikisha kuwa nimesoma na kuwa tayari kufanya mtihani.Ninashukuru wazazi wangu kwa kufanya bidii kuhakikisha kuwa nilipata muda wa kutosha wa kusoma wakati wa likizo ndefu ya corona,” akasema.

JAMVI: Mkanganyiko mkuu unaogubika siasa za urithi Pwani

Na MOHAMED AHMED

KWA muda sasa magavana watatu kutoka Pwani akiwemo wa Mombasa Hassan Joho, Salim Mvurya wa Kwale na mwenzao wa Kilifi Amason Kingi wameonekana kuweka mipango yao ya kisiasa ambayo itakuja baada ya kumaliza hatamu zao.

Magavana hao wapo kwenye hatamu zao za mwisho kwenye viti hivyo ambavyo itakuwa wamevishikilia kwa muda wa miaka kumi wakati awamu zao zitakapokamilika mwaka 2022.

Wakati viongozi hao wanapopanga kuondoka kwenye nafasi hizo, tayari kuna wale ambao wanamezea mate viti hivyo na kutaka kuwarithi. Baadhi ya wanaomezea mate ni wale ambao magavana hao pia wangependelea wachukue nafasi hizo wakati watakapokuwa wameondoka.

Miongoni mwa viongozi ambao kufikia sasa wameonyesha azma ya kurithi viti hivyo ni pamoja na naibu gavana wa Kwale Fatuma Achani ambaye pia anaungwa mkono na Bw Mvurya

Mpinzani

Kufikia sasa mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani ameonekana kuwa mpinzani wa karibu wa Bi Achani.

Licha ya Bw Mvurya kuwa chama kimoja cha Jubilee na Bw Mwashetani gavana huyo amesisitiza kwamba Bi Achani ndiye anastahili zaidi kumrithi ifikapo 2022

Katika mkutano wa hivi majuzi kwenye mazishi ya Askofu Morris Mwarandu Bw Mvurya alisema ni Bi Achani pekee atakayeweza kuendeleza mafanikio ambayo kaunti hiyo imeshuhudia tangu 2013

“Ni vile hapa ni mazishini sitaongea zaidi. Lakini Askofu aliniambia ‘muda wako unaisha ututayarishie ya mbele’. Naibu gavana ametayarishwa. Mnaona Tanzania hakujakuwa na msukosuko? Katika taasisi ni lazima watu watayarishwe,” akasema.?

Wengine wanaoaminika kumezea mate kiti hicho ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Mtuga Chirau Mwakwere, na katibu wa Wizara ya Kilimo Hamadi Boga.? Mara kwa mara Bi Achani na Bw Mwashetani wamekuwa wakitoleana cheche za maneno ambazo zinaelekezwa na mipango yao ya kurithi Bw Mvurya

Cheche hizo za maneno ya kisiasa pia zimekuwa zikushuhudiwa katika kaunti ya Mombasa ambapo baadhi ya viongozi wanalenga kumrithi Gavana Joho.

Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo na mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambao kufikia sasa ndio viongozi ambao wamejitosa ulingoni wazi wazi wakitaka kumrithi Bw Joho.? Hata hivyo, ukali wa siasa hizo za urithi zimeonekana kuelemea upande wa Bw Nassir na Bw Shahbal ambao ndio mahasimu wa karibu.

Huku Bw Nassir akionekana kusubiri kuidhinishwa na Bw Joho katika azma yake, Bw Shahbal ambaye pia sasa ana uhusiano wa karibu na Bw Joho amekuwa akiendeleza kampeni za mapema kupitia vikao vinavyotambulika kama “Gumzo Maskani”.

Kati ya mwezi wa Februari hadi mwezi jana, kiongozi huyo amefanya mikutano kadhaa katika maeneo bunge ya Mombasa ikiwemo Likoni, Changamwe, Mvita Kisauni na Jomvu kueleza sera zake.

Bw Nassir naye kwa upande amekuwa akitumia nafasi yake kama kiongozi kukutana na wakazi hususan wa eneo bunge lake la Mvita na kueneza azma yake ya kutaka kuwania ugavana.

Hata hivyo, Bw Nassir hajakuwa akionekana zaidi kwenye maeneo bunge mengine kufanya kampeni zake kama vile Bw Mbogo ambaye pia ameshikilia kampeni zake mashinani katika eneo bunge lake la Kisauni.

Uchanganuzi wa Jamvi umeonyesha katika miezi hiyo miwili iliyopita, Bw Nassir amezuru makanisa katika eneo la Changamwe mara tatu huku Bw Shahbal akitekeleza mikutano takriban 20 katika muda huo huo.

Kampeni hizo za mapema pia zimeibua tumbo joto katika chama cha ODM baada ya Bw Shahbal kutangaza kuwa anarudi kwenye chama hicho.

“Walinifungia mlango wakati ule wa nyumba lakini sasa si handisheki imekuja. Si tumerudi nyumbani?” Bw Shahbal alisema katika mmoja ya mikutano yake.? Tangazo hilo la Bw Shahbal lilipelekea Bw Nassir naye kumpiga vijembe mpinzani wake huyo na katika mkutano wa eneo la Jomvu akaonya wakazi dhidi ya kuchagua watu ambao ‘wanazuka saa hizi.’

“Mimi nataka kuwauliza wao walikuwa wapi wakati sisi tulikuwa tunapambana? Mimi nawaambia muwe makini na watu hao,” akasema Bw Nassir.? Licha ya wawili hao kujitokeza kumenyana kwenye kiti hicho, bado haijakuwa wazi iwapo Bw Joho atamuunga mkono yeyote kati yao.

Iwapo Bw Joho atajitokeza wazi kutaka kumuunga mkono kiongozi wa kumrithi basi naibu wake Dkt William Kingi atakuwa miongoni mwa wale wanaotarajia kuungwa mkono.

Dkt Kingi pia amewahi kutangaza kuwa atawania kiti cha ugavana, hata hivyo hakuna mikutano yoyote ya wazi ambayo ameanza kutekeleza.? Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia anatarajiwa kuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo, bado pia yeye hajaanza kujitosa kwenye kampeni za mapema.

Kwa sasa, mwezi mtukufu wa Ramadhan utasitisha kampeni hizo kama ilivyo ada ya wanasiasa wa Mombasa huku kindumbwendumbwe kikitarajiwa baada ya mwezi huu ambao umeanza jana kukamilika.

Kwengineko katika kaunti ya Kilifi mihemko ya kisiasa ya kurithi Gavana Amason Kingi yamevutia aliyekuwa mbunge Gideon Mung’aro na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa

Bado siasa hazijapamba moto eneo hilo lakini Bi Jumwa alikuwa ameonekana kuendesha siasa za chini kwa chini.

Bw Mung’aro naye ameonekana kuwa karibu na Bw Kingi ambaye kwa muda amekuwa akiendesha siasa za chama cha Pwani. Naibu gavana Gideon Saburi pia ametajika katika siasa hizo za urithi.

Mkanganyiko mkuu unavyogubika siasa za urithi Pwani

Na MOHAMED AHMED

KWA muda sasa magavana watatu kutoka Pwani akiwemo wa Mombasa Hassan Joho, Salim Mvurya wa Kwale na mwenzao wa Kilifi Amason Kingi wameonekana kuweka mipango yao ya kisiasa ambayo itakuja baada ya kumaliza hatamu zao.

Magavana hao wapo kwenye hatamu zao za mwisho kwenye viti hivyo ambavyo itakuwa wamevishikilia kwa muda wa miaka kumi wakati awamu zao zitakapokamilika mwaka 2022.

Wakati viongozi hao wanapopanga kuondoka kwenye nafasi hizo, tayari kuna wale ambao wanamezea mate viti hivyo na kutaka kuwarithi.

Baadhi ya wanaomezea mate ni wale ambao magavana hao pia wangependelea wachukue nafasi hizo wakati watakapokuwa wameondoka.

Miongoni mwa viongozi ambao kufikia sasa wameonyesha azma ya kurithi viti hivyo ni pamoja na naibu gavana wa Kwale Fatuma Achani ambaye pia anaungwa mkono na Bw Mvurya. Kufikia sasa mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani ameonekana kuwa mpinzani wa karibu wa Bi Achani.L

icha ya Bw Mvurya kuwa chama kimoja cha Jubilee na Bw Mwashetani gavana huyo amesisitiza kwamba Bi Achani ndiye anastahili zaidi kumrithi ifikapo 2022.

Katika mkutano wa hivi majuzi kwenye mazishi ya Askofu Morris Mwarandu Bw Mvurya alisema ni Bi Achani pekee atakayeweza kuendeleza mafanikio ambayo kaunti hiyo imeshuhudia tangu 2013.

“Ni vile hapa ni mazishini sitaongea zaidi. Lakini Askofu aliniambia ‘muda wako unaisha ututayarishie ya mbele’. Naibu gavana ametayarishwa. Mnaona Tanzania hakujakuwa na msukosuko? Katika taasisi ni lazima watu watayarishwe,” akasema.

Wengine wanaoaminika kumezea mate kiti hicho ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Mtuga Chirau Mwakwere, na katibu wa Wizara ya Kilimo Hamadi Boga.

Mara kwa mara Bi Achani na Bw Mwashetani wamekuwa wakitoleana cheche za maneno ambazo zinaelekezwa na mipango yao ya kurithi Bw MvuryaCheche hizo za maneno ya kisiasa pia zimekuwa zikushuhudiwa katika kaunti ya Mombasa ambapo baadhi ya viongozi wanalenga kumrithi Gavana Joho.

Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo na mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambao kufikia sasa ndio viongozi ambao wamejitosa ulingoni wazi wazi wakitaka kumrithi Bw Joho.? Hata hivyo, ukali wa siasa hizo za urithi zimeonekana kuelemea upande wa Bw Nassir na Bw Shahbal ambao ndio mahasimu wa karibu.

Huku Bw Nassir akionekana kusubiri kuidhinishwa na Bw Joho katika azma yake, Bw Shahbal ambaye pia sasa ana uhusiano wa karibu na Bw Joho amekuwa akiendeleza kampeni za mapema kupitia vikao vinavyotambulika kama “Gumzo Maskani”.

Kati ya mwezi wa Februari hadi mwezi jana, kiongozi huyo amefanya mikutano kadhaa katika maeneo bunge ya Mombasa ikiwemo Likoni, Changamwe, Mvita Kisauni na Jomvu kueleza sera zake.

Bw Nassir naye kwa upande amekuwa akitumia nafasi yake kama kiongozi kukutana na wakazi hususan wa eneo bunge lake la Mvita na kueneza azma yake ya kutaka kuwania ugavana.

Hata hivyo, Bw Nassir hajakuwa akionekana zaidi kwenye maeneo bunge mengine kufanya kampeni zake kama vile Bw Mbogo ambaye pia ameshikilia kampeni zake mashinani katika eneo bunge lake la Kisauni.

Uchanganuzi wa Jamvi umeonyesha katika miezi hiyo miwili iliyopita, Bw Nassir amezuru makanisa katika eneo la Changamwe mara tatu huku Bw Shahbal akitekeleza mikutano takriban 20 katika muda huo huo.

Kampeni hizo za mapema pia zimeibua tumbo joto katika chama cha ODM baada ya Bw Shahbal kutangaza kuwa anarudi kwenye chama hicho.? “Walinifungia mlango wakati ule wa nyumba lakini sasa si handisheki imekuja. Si tumerudi nyumbani?” Bw Shahbal alisema katika mmoja ya mikutano yake.

Tangazo hilo la Bw Shahbal lilipelekea Bw Nassir naye kumpiga vijembe mpinzani wake huyo na katika mkutano wa eneo la Jomvu akaonya wakazi dhidi ya kuchagua watu ambao ‘wanazuka saa hizi.’

“Mimi nataka kuwauliza wao walikuwa wapi wakati sisi tulikuwa tunapambana? Mimi nawaambia muwe makini na watu hao,” akasema Bw Nassir.? Licha ya wawili hao kujitokeza kumenyana kwenye kiti hicho, bado haijakuwa wazi iwapo Bw Joho atamuunga mkono yeyote kati yao.

Iwapo Bw Joho atajitokeza wazi kutaka kumuunga mkono kiongozi wa kumrithi basi naibu wake Dkt William Kingi atakuwa miongoni mwa wale wanaotarajia kuungwa mkono.

Dkt Kingi pia amewahi kutangaza kuwa atawania kiti cha ugavana, hata hivyo hakuna mikutano yoyote ya wazi ambayo ameanza kutekeleza.? Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia anatarajiwa kuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho.

Hata hivyo, bado pia yeye hajaanza kujitosa kwenye kampeni za mapema.Kwa sasa, mwezi mtukufu wa Ramadhan utasitisha kampeni hizo kama ilivyo ada ya wanasiasa wa Mombasa huku kindumbwendumbwe kikitarajiwa baada ya mwezi huu ambao umeanza jana kukamilika.

Kwengineko katika kaunti ya Kilifi mihemko ya kisiasa ya kurithi Gavana Amason Kingi yamevutia aliyekuwa mbunge Gideon Mung’aro na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa Bado siasa hazijapamba moto eneo hilo lakini Bi Jumwa alikuwa ameonekana kuendesha siasa za chini kwa chini.

Bw Mung’aro naye ameonekana kuwa karibu na Bw Kingi ambaye kwa muda amekuwa akiendesha siasa za chama cha Pwani.Naibu gavana Gideon Saburi pia ametajika katika siasa hizo za urithi.

Wanabiashara wapigia debe chama cha Pwani

Na SIAGO CECE

MPANGO wa wanasisasa wa Pwani kuzindua chama cha eneo hilo umepigwa jeki baada ya wafanyabiashara wa eneo hilo kuuunga mkono hatua hiyo.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wanawataka wanasiasa wahakikishe kwamba chama hicho kina sura ya kitaifa, ili kivutie wapigakura wengine kutoka sehemu zote nchini.

Mazungumzo yao yanajiri wakati magavana watatu wa Pwani – Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kwale) na Amason Kingi (Kilifi) – wakikutana majuzi kujadili kuhusu, kinachodaiwa kuwa mipango ya kuunda chama cha Pwani.

Magavana hao watatu wiki jana walikutana na Rais Uhuru Kenyatta, baada ya hapo Jumanne wakakutana katika ofisi za Gavana wa kaunti ya Kwale, licha ya kuwa na tofauti zao za kisiasa hapo awali.

Wakizungumza eneo la Nyali, wafanyabiashra hao wakiongozwa na Fransisca Kitese, walisema lengo lao ni kuwa na usawa katika siasa za eneo la Pwani na nchini nzima.

“Utafiti wetu uligundua kuwa kabila kubwa zaidi hapa Mombasa ni Wakamba, wakifuatiwa na Wamijikenda, GEMA, Waluhya, Wajaluo kisha Waswahili. Licha ya haya, hakuna mbunge yeyote ambaye ametoka katika kabila ambazo si Waswahili au Wamijikenda,” Bi Kitese alisema.

Alisema kabila nyingi za ‘Wabara’ zimebaguliwa kisiasa licha ya wao kuchangia pakubwa katika uchumi wa Pwani.

Kulingana na mkuu wa jamii ya GEMA Mombasa Crispus Waithaka, wafanyabiashara hao wanashinikiza umoja na ushirikiano kati ya makabila yote ambayo yanayoishi Pwani. Hii ni kwa azma ya kukabiliana na ubaguzi hasa katika uongozi.

“Tunakabiliwa na ubaguzi mwingi na watoto wetu hawazingatiwi katika kupata fursa kwa sababu ya majina yao ambayo si ya Kipwani. Tungependa kushirikiana nao katika hicho chama ili kupunguza ubaguzi kama wa rangi au kabila, ” alisema Bw Waithaka.

Aliongeza kuwa licha ya kuwa wazaliwa wa mkoa huo, wakazi wengi wa Mombasa wamenyang’anywa viti vya kisiasa wakati wa uchaguzi na anataka kujiunga na chama hicho cha Pwani katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, Millicent Odhiambo ambaye ni mkazi na mmoja wa wafanyibiashara hao aliomba kuwa wakati chama cha Pwani kitakapozinduliwa, kiungane na muungano wa ‘One Kenya Alliance’ wa Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Gideon Moi na Moses Wetang’ula.

“Yeyote ambaye hatajiunga na muungano wa OKA ana maslahi ya kibinafsi. Tungependa watu waje pamoja na kumaliza ukabila ili tusiwe na mgawanyiko au vita nchini,” alieleza Bi Odhiambo.

Wakati msimu wa siasa unakaribia, viongozi tofauti nchini wanatengeza miungano ili kuhakisha wamefaulu katika kugombea viti vya uongozi.

Wakazi wa Pwani kuhamishiwa bara

Na MUSA IDDI

WAKAZI wa kaunti za Pwani ya Kenya zinazopakana na Bahari Hindi watahamishiwa bara, baada ya kugunduliwa kwa kiasi kikubwa zaidi cha dhahabu kuwahi kupatikana duniani.

Kulingana na kampuni ya Kenya Coast Gold Exploration and Mining Inc, kaunti ambazo zaidi ya wakazi wake asilimia 80 watahamishwa ni Kilifi, Kwale, Lamu na Mombasa.

Stakabadhi ambazo mwandishi wetu alisoma zinaonyesha kuwa wakazi hao watahamishiwa kaunti za Turkana, Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Kiambu, Nyeri na Kisii

“Tutahakikisha kuwa wakazi wamelipwa fidia kwa kupoteza ardhi na mali yao nyingine ili waweze kutoa nafasi ya uchimbaji wa madini hayo. Mahali wataenda tutawajengea hospitali, shule, kuwawekea stima, maji na barabara za kisasa,” alisema mkuu wa kampuni hiyo, Niklas Saizler.

“Tumekuwa tukifanya utafiti eneo la Pwani ya Kenya kwa muda mrefu na sasa tumethibitisha kuna dhahabu nyingi na ya thamani kubwa,” akasema Saizler.

“Kiasi kikubwa zaidi kinapatikana Lamu chini ya bahari. Dhahabu hiyo ni ya ubora wa juu kuliko nyingine yoyote duniani,” akaongeza.

Alisema mpango huo wa kuhamisha wakazi utaanza kutekelezwa baada ya kushauriana na viongozi wa eneo hilo na kukubaliana kuhusu fidia inayopasa kulipwa wakazi.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi waliozungumza na wanahabari walisema hawatakubali kamwe kuondoka Pwani hata kama watalipwa mamilioni ya pesa.

“Sitotoka hapa mie. Hii ni dhuluma kubwa. Huwezi ukatuhamishia bara eti kwamba unataka kuchimba dhahabu katika mashamba yetu. Mungu alikuwa na sababu alipotupatia makao hapa! Hata nikifa, mwili wangu hautatoka Pwani,” akasema Juma Charo, mkazi wa eneo la Shimo la Kale.

Viongozi wa makundi ya kijamii pia walipinga pendekezo hilo.

“Hao watu wanaota mchana. Hakuna vile utahamisha mamilioni ya wakazi kwa sababu unataka kuiba raslimali zao. Tutapigana nao hadi mwisho,” akaeleza Sheriff Karim kutoka Lamu.

Raila asihi Wapwani wapitishe BBI

Na SIAGO CECE

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga amekamilisha ziara yake Pwani kwa kuwarai wakazi waunge mkono mswada wa BBI, siku ya kura ya maamuzi itakapowadia.

Bw Odinga alisema kupitia mswada huo, masuala ya dhuluma za mashamba ambazo zimewaathiri wakaazi wa Pwani kwa muda mrefu yataangaziwa.

“Niko hapa kuwaambia mpige kura ya ‘ndiyo’ kwa sababu BBI ndiyo suluhu ya shida zenu zote. BBI ikifaulu itawaletea maendeleo mengi,” Bw Odinga Alisema ripoti ya TJRC itatekelezwa chini ya miezi sita baada ya BBI kupitishwa.Masuala mengine ambayo aliahidi wakazi ni kuboresha uchumi wa Bahari ambao ni muhimu kwa wapwani.

“BBI itaboresha uchumi wa bahari na kuwasiaidia wavuvi pia. Kuna njia nyingi za kisiasa za kufanya uvuvi ambazo zitawawezesha wavuvi kuvua kwenye maji ya kina kirefu. Wakati huu ni Wachina ambao wanavua kwenye maji yetu,” alieleza.

Bw Raila alisema mapendekezo ya kubadilisha katiba yataleta mabadiliko kisera na maisha ya wakazi.

Bw Raila pia aliwaandaa wenyeji kuwa tayari kwa kura ya maamuzi.Alisisitizia kwamba kupitia BBI tume itakayosimamia maswala ya vijana itabuniwa ishara kwamba changamoto za ajira kwa vijana itapata sulushisho na kuzikwa katika kaburi la sahau.

Pia, kutwakuwa na maeneo bunge ambayo yataongezwa iwapo BBI itapitishwa, kumaanisha kwamba pesa za maendeleo zitaongezeka na kumfikia mwananchi.

“Wale ambao hawaungi BBI hawataki pesa ziwafikie wananchi. Pesa zitakazotolewa kwa kila kaunti zitaiongezeko kutoka kwa asilimia 15 hadi 35 ambazo asilimia tano zitaenda katika kusaidia miradi ya vijana,” alisema Bw Raila.

Wapwani wataka kummeza Yatani kuhusu Bandari

Na MOHAMED AHMED

AGIZO la kuanzisha upya shughuli ya kumtafuta mkurugenzi mkuu wa bandari ya Mombasa limezua mjadala mkali miongoni mwa wakazi wa Pwani.

Baadhi ya viongozi wa kisiasa na mashirika ya haki za binadamu wameeleza kughadhabishwa kwao na hatua ya waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani kuikataa orodha ya wanaotaka nafasi hiyo akisema kuwa hakuna aliye na uwezo huo.

Katika matokeo hayo watu watatu akiwemo aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa mradi wa Lappset Silvester Kasuku, aliyekuwa katibu mkuu wa Ugatuzi Mwanamaka Mabruki na aliyekuwa kamishna wa tume ya polisi Murshid Mohammed, walikuwa wamefikia hatamu ya mwisho ya kazi hiyo.

Kadhalika, Bw Yatani, mnamo Jumanne alisema watatu hao hawakufikisha asilimia 70 ya alama, ambayo mtu anayetaka nafasi hiyo anapaswa kuipata.Mwenyekiti wa kitaifa wa kundi la Taireni Association of Mijikenda, Bw Peter Ponda alidai kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kwa sababu Wapwani wawili walikuwa kwenye orodha ya watatu hao.Bw Mohammed na Bi Mwanamaka ni wakazi wa Pwani.

Bw Ponda alidai kuwa hatua hiyo ni mpango wa kuzima Wapwani kuchukua nafasi hiyo.“Haya yote yanafanyika kwa sababu ya maslahi ya wale walioko kwenye uongozi wa serikali kuu. Wanataka kuweka mtu wao na kwa sababu kwenye orodha ya hivi majuzi mtu wao hayuko ndiyo maana wanaanza upya,” akasema Bw Ponda.

Aliongeza: “Kitendo hiki ni jambo la kusikitisha. Hii bandari iko Pwani hivyo basi mtu wa Pwani anapaswa kupewa nafasi hii.”

Mkurugenzi wa shirika la Haki Afrika, Hussein Khalid alishangaa iweje shughuli hiyo irejelewe bila sababu mwafaka kuwekwa wazi.Alisema kuwa kuna haja ya wakuu serikalini kutoingilia kati suala hili la kuchaguliwa kwa mkurugenzi wa bandari.

“Kila sehemu nchini humu wakazi wa eneo fulani wanapaswa kupewa kipaumbele. Sisi kama shirika tumeona jambo hili limefanywa kimakusudi kwa sababu kuna Wapwani wawili ambao walikuwa kwenye orodha hiyo,” akasema Bw Khalid.

Bw Yatani alikuwa amedai kuwa watatu hao hawakupata alama hiyo na kuagiza shughuli nzima ifanywe upya.Jana, halmashauri ya bandari (KPA) iliweka tangazo kwenye magazeti na kutangaza kuwa shughuli hiyo itaanza upya na kuwataka wale wanaotaka nafasi hiyo kufikisha stakabadhi zao kabla ya Machi 19.Hii itakuwa mara ya tatu kwa shughuli hiyo kurejelewa.

Mwaka jana, Bw Yatani pia aliagiza shughuli hiyo irejelewe akisema kuwa kuna upendeleoa Siasa za hapo bandarini pia zilikuwa zimetawala shughuli hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kinara wa ODM Raila Odinga Pwani, Seneta wa Mombasa Mohammed Faki alisema kuwa bandari ndiyo sura ya watu wa Pwani na kuna haja ya Mpwani kuchukua nafasi hiyo.

“Hivi sasa hakuna mkurugenzi mkuu na juzi tumesikia kuwa kuna mambo ambayo hayakuwa sawa lakini sisi tunaomba kuwa mtu wa Pwani ndiye anayefaa kushikilia nafasi ile.”

Alimuomba Bw Odinga kusukuma mazungumzo hayo kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha kuwa Mpwani anachukua usukani huo.

Mpango wa kusafisha Pwani wazinduliwa

Na WANDERI KAMAU

SHIRIKA la Petco Kenya na Hazina ya Kuhifadhi Mazingira (WWF) zimetia saini mkataba wa Sh6 milioni, kuimarisha juhudi za kuhifadhi mazingira na uzoaji taka katika ukanda wa Pwani.

Mkataba huo utayawezesha mashirika hayo kupata mashine maalum ya kuboresha taka kupitia teknolojia ya kisasa kutoka Denmark.Mpango huo utaendeshwa kwa ushirikiano na kampuni ya Plastix kutoka taifa hilo, ambayo hujihusisha na kuboresha taka.

Kaunti zinazolengwa kwenye mkakati huo ni Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu.Hilo pia litaendeshwa kwa kuyashirikisha mashirika mengine nchini ambayo yamekuwa yakijihusisha na shughuli za uzoaji taka.

Kulingana na Msimamizi Mkuu wa shirika la Petco nchini, Bi Joyce Gachugi, lengo kuu la mpango huo ni kuimarisha shughuli za uzoaji taka nchini, na kuzigeuza kwa namna zinazoweza kuifaidi jamii.

“Lengo letu ni kuondoa taka aina ya plastiki katika ukanda wa Pwani, kubuni mazingira bora ya kufanyia kazi na kuunga mkono juhudi zinazoendeshwa na wakfu wa WWF katika kusafisha miji, bandari na mito. Mpango huu ni muhimu sana kwetu kwani unapiga jeki juhudi zetu kuwasaidia kifedha watu binafsi na mashirika ambayo yamekuwa yakijihusisha katika uzoaji taka,” akasema.

Mpango pia unalenga kutoa mashine maalum za uzoaji taka na mafunzo maalum kwa zaidi ya watu 800 ambao wamekuwa wakijihusisha katika shughuli hizo.

Mchakato huo mzima utagharimu Sh 6 milioni.Ripoti mbalimbali zimeiorodhesha Pwani kuwa miongoni mwa maeneo yanayokusanya kiwango kikubwa zaidi cha taka nchini.

Taka nyingi huwa vifaa vinavyotengenezwa kwa plastiki.Maeneo ambayo yamekuwa yakiathiriwa sana na tatizo hilo ni fuo za Bahari Hindi, hali ambayo wanamazingira wametaja kuhatarisha maisha ya viumbe wa majini kama samaki.

Wanaharakati wa mazingira wamekuwa wakiwalaumu viongozi wa kisiasa kwa kutolichukulia suala hilo kwa uzito.Wasimamizi wa mkakati huo walisema wanalenga kuchangia katika juhudi za kuendeleza maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya wanawake na wanaume, hasa vijana.

Hili ni kwa kugeuza uzoaji taka kuwa kazi wanayoweza kuifanya kuwa biashara ili kujipatia mapato maishani.Juhudi vile vile zinalenga kuchochea uvumbuzi na kubuni soko la uboreshaji taka.Baadhi ya mashirika yatakayoshirikishwa kwenye mkakati huo ni Plastix, Jil Plastics na Kwale Plastic Plus Collectors (KPPC).

Mashirika hayo yaliungana na kuanza juhudi za kukabili athari za uharibifu wa mazingira unaochangiwa na vifaa vya plastiki katika ukanda huo.Msimamizi Mkuu wa Miradi ya Uhifadhi katika WWF, Bi Nancy Githaiga, alisema kupitia juhudi hizo, wanalenga kubuni ushirikiano wa kimataifa utakaochangia pakubwa katika kuhakikisha uzoaji taka umegeuzwa kuwa mfumo wa kimapato kwa maelfu ya watu.

Raila awaonya Wapwani dhidi ya kuunda chama

LUCY MKANYIKA na MAUREEN ONGALA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amepinga msukumo wa baadhi ya viongozi wa Pwani kuunda chama cha kisiasa cha kutetea maslahi ya eneo hilo.

Akizungumza katika Kaunti ya Taita Taveta alipoanza ziara ya kuvumisha pendekezo la kurekebisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), Bw Odinga alisema pendekezo la kuunda chama cha ukanda huo kitaleta mgawanyiko wa nchi.

Wito wa uundaji chama cha Wapwani umekuwa ukivumishwa na viongozi wengi katika ukanda wa Pwani.

Hata hivyo, katika wiki chache zilizopita, wengi wao waliachana na mipango hiyo ambayo sasa inaonekana kuendelezwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi na wandani wake pekee.

Bw Odinga alisema kuwa katiba inawapa Wakenya haki ya kuunga mkono mrengo wowote bila kueneza ukabila nchini.Viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto katika ukanda huo walitangaza wataingia katika Chama cha United Democratic Alliance badala ya kuendeleza mipango ya awali ya kuunda chama cha Wapwani.

Kwa upande mwingine, Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho alisema aliwekeza sana katika uundaji wa chama cha ODM kwa hivyo hana nia ya kukihama chama hicho kwa sasa, anapolenga kutafuta tiketi yake kuwania urais 2022.

Bw Odinga alionya kuwa, kutakuwa na hatari ya kusababisha migawanyiko endapo viongozi wa Pwani wataunda chama ambacho hakitakuwa na mtazamo wa kitaifa.

“Katika katiba, Kenya ni demokrasia ya vyama vingi na tunataka kuwa na vyama vya kitaifa. Tukianza kuwa na vyama vya majimbo, tutagawanya Kenya. Kama unataka kuunda chama, katiba haikuruhusu kuanzisha chama cha ukoo au kikabila. Huo ni ushauri ningetaka kuwapa watu wa Pwani,” akasema.

Hapo jana, balozi huyo wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU), alifanya mikutano mbalimbali Kaunti ya Taita Taveta.Alikuwa ameandamana na viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Gavana Granton Samboja.

Katika mikutano ya hadhara, viongozi waliohutubu waliahidi wananchi kwamba mswada wa BBI ukipitishwa utaleta manufaa kwa maendeleo na uongozi bora.

Kulingana nao, mapendekezo kama vile kuongeza mgao wa fedha kwa kaunti na kutengea madiwani pesa za maendeleo ya wadi, yatasaidia kustawisha nchi katika maeneo ya mashinani.Msafara wa Bw Odinga leo umepangiwa kuelekea Kaunti ya Kilifi ambayo imegeuka kitovu cha wito wa uundaji chama cha Wapwani.

Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire, alisema kuwa ziara ya Bw Odinga haihusu masuala ya chama bali BBI.Jumatatu wabunge wa chama ODM Kaunti ya Kilifi pamoja na wajumbe wa Kaunti hiyo walifanya kikao kirefu na Bw Kingi kujiandaa kwa ziara ya Bw Odinga.

 

Raila atua Pwani kufunza wakazi kusakata Reggae

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Raila Odinga leo amepangiwa kuanza rasmi ziara yake eneo la Pwani kupigia debe mswada wa marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Bw Odinga jana alitua katika Kaunti ya Taita Taveta lakini hakufanya mkutano wowote wa hadhara ilivyotarajiwa na wengi.Amepangiwa kuzuru kaunti za Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River ili kuendeleza kampeni za BBI katika ukanda huo.

Bw Odinga leo amepangiwa kukagua soko la kisasa la Mwatate, mradi wa ujenzi wa hospitali ya ugonjwa wa corona mjini humo kisha kuhutubia wenyeji wa mji huo kabla ya kufungua shule ya Mwakinyungu katika eneo la Rong’e.

Baadaye atahutubia wenyeji wa Voi kabla ya kuendeleza safari yake Kaunti ya Mombasa.’Safari yake inalenga kuzindua kampeni za BBI katika eneo la Pwani,’ alisema mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Taita Taveta, Richard Tairo.

Kiongozi huyo pia atakutana na viongozi wa kaunti hiyo ili kujadili mikakati ya kuendeleza kampeni za BBI katika eneo hilo.Baadhi ya viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni gavana Granton Samboja, seneta wa kaunti hiyo Jones Mwaruma, wabunge Jones Mlolwa (Voi), Andrew Mwadime (Mwatate), aliyekuwa mbunge wa Wundanyi Thomas Mwadeghu na madiwani.

Vilevile ziara ya kiongozi huyo inapania kufufua umaarufu wake unaotishiwa kudidimia viongozi wengi wakipigania chama huru cha Wapwani.

Chama cha ODM, ambacho kimekuwa kikipata uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo, kilipata pigo baada ya baadhi ya wanasiasa kuhamia mrengo wa Tangatanga unaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto.

Viongozi hao vilevile wamekuwa mstari wa mbele kupinga BBI na hivyo kuzua tumbojoto ikiwa mswada huo utapenya ifikapo kura ya maoni mnamo Juni.

Ziara ya kiongozi huyo inajiri baada ya Dkt Ruto kuzuru eneo hilo wiki chache zilizopita. Bw Raila ananuia kupoza ziara ya Bw Ruto ambaye anaaminika kuwa anaendelea kupata umaarufu katika eneo hilo.

Pwani yasisitiza itakaa ODM hadi mwisho, haitaunda chama

Na Mohamed Ahmed

WABUNGE kutoka Pwani wametetea msimamo wao kukwamilia Chama cha ODM hata wakati ambapo wito umezidi kutolewa kuhusu uundaji chama maalumu cha Wapwani.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Kwale, Bi Zuleikha Hassan, amesema mpango wa kuunda chama Pwani hauna msingi kwa sasa.Badala yake, alisema mpango huo unakoroga wananchi pamoja na viongozi ambao wanatilia mkazo jambo hilo.

“Kwa sasa tumechelewa kabisa na pia kisheria hatupaswi kuwa na chama ambacho ni cha sehemu moja pekee. Hivyo basi ningewaomba viongozi wenzangu waache kutukoroga sisi wengine pamoja na wakazi wetu,” akasema Bi Hassan.

Alisema kuwa viongozi ambao wanataka Pwani ijitoe katika chama cha ODM wanapoteza wakati kwani chama hicho ndicho kinachowafaa Wapwani.Alisema ni kupitia kiongozi wa chama hicho cha ODM, Bw Raila Odinga, Pwani imeweza kufaidika kimaendeleo.

“Sisi kama Wapwani tulikuwa tunalilia ugatuzi na ni Bw Odinga alipigania nchi hii nzima kupata ugatuzi. Sisi tunafaa kusalia ndani ya ODM na tusikubali kuambiwa vingine,” akasema.

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir pia alisema kuwa Pwani haitatoka ODM na kuongeza kuwa viongozi wake wamechangia kukijenga na kukipa sifa chama hicho.

“Mimi binafsi na Gavana Hassan Joho pamoja na viongozi wengine tunasema kwa ujasiri kuwa tumechangia kuunda chama hiki. Hivyo basi sisi tuko ndani ya ODM mpaka mwisho,” akasema.

Bw Joho pia amesisitiza kuwa atapigania Urais kupitia chama hicho cha ODM.

 

Kingi aungama mambo si shwari kwa ODM Pwani

Na MOHAMED AHMED

KAUNTI ya Kilifi ambayo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 ilichagua viongozi wote kwa chama cha ODM, imeanza kuyumba na kuchukua mwelekeo tofauti dhidi ya kinara wa chama hicho Raila Odinga.

Kilifi ndiyo kaunti pekee nchini ambayo Gavana, wabunge, Seneta, Mbunge Mwakilishi wa Kike na wawakilishi wadi (MCAs) walichaguliwa kupitia ODM.

Lakini sasa Gavana Amason Kingi ambaye ndiye mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Kilifi, ameingia kwenye kampeni dhidi ya chama hicho, hatua ambayo itakuwa ni pigo kuu kwa Bw Odinga.

Akizungumza katika mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Bw Kingi alisema kuwa kwa muda sasa Pwani imekosa uwakilishi mzuri katika meza ya kitaifa, kwa sababu ya kuwakilishwa kupitia vyama vingine kikiwemo ODM.

Bw Kingi alisema hayo huku akiweka wazi kuwa hatawania tiketi yaUrais kupitia chama cha ODM.

“Mimi sitawasilisha ombi langu la kuwania kiti hicho kupitia ODM. Hilo liwe wazi kabisa. Azma ya kuwania kiti hicho bado ipo, lakini haitatimia kupitia ODM. Kwa sasa mwelekeo wangu ni kuhakikisha kuwa tunapata chama chetu cha Pwani,” akasema Bw Kingi.

Alisema kuwa mpango wake ni kuhakikisha kuwa vyama vyote ambavyo vipo Pwani vinakuja pamoja na kuwa kitu kimoja, na kusisitiza kuwa ni katika muungano huo ndipo Pwani itaweza kusikika na sio kuendelea kutegemea watu wengine kama vile imetegemea ODM kuwakilisha matakwa yake kwa muda.

Taifa Leo imegundua kuwa kuna mpango wa magavana wa Pwani pamoja na viongozi wengine kutoka kanda hiyo kukutana wiki hii ili kujadiliana kuhusiana na umoja huo wa Pwani ambao umeonekana kubabaisha viongozi.

“Ni kweli kutakuwa na mkutano wa viongozi lakini mpango wetu ni kufanya mambo bila kupiga fujo maana kuna wale maadui zetu ambao wanatishiwa na kuungana kwa Pwani. Hivyo basi, tusubiri tu ndani ya siku hizi chache na watu wetu wataona mwelekeo,” akasema Bw Kingi kuhusiana na mkutano huo ambao unatazamiwa kuleta mwelekeo mpya.

Mwito wa umoja huo umepelekea Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kujiondoa katika kumuunga mkono Bw Odinga.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana ambaye pia alipata kiti chake kupitia ODM anavutia upande wa wabunge hao wawili.

Wabunge wengine wa Kilifi akiwemo Michael Kingi (Magarini), Teddy Mwambire (Ganze), William Kamoti (Rabai) na Ken Chonga (Kilifi Kusini) wanavutia upande wa Bw Kingi na wanaunga mkono mwito wa umoja wa Pwani.

Bw Kingi alisema mpango wake ni kuvileta pamoja vyama vya Kadu Asili, Shirikisho, Umoja Summit na Devolution Party of Kenya (DPK) miongoni mwa vyengine pamoja.

Mpango huu unatazamiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu kulingana na Bw Kingi.

“Tayari tupo kwenye mazungumzo na viongozi tofauti na washikadau. Maongezi hayo yanahusisha viongozi wa vyama hivyo ambavyo vipo tayari Pwani,” akasema.

Hatua hii inatazamiwa kukisambaratisha chama cha ODM ambacho siku za hivi majuzi kilipata pigo katika kaunti ya Kwale kwa kushindwa kunyakua kiti cha Msambweni katika uchaguzi mdogo.

Kushindwa kwenye uchaguzi huo na kuja kwa mwito unaoongozwa na Bw Kingi kunakiweka pabaya chama cha ODM wakati siasa za 2022 zinapopamba moto.

Joho ataka Raila aunge Mpwani kuwania urais

STEPHEN ODUOR na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa, Hassan Joho ameeleza matumaini kwamba Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ataunga mkono mgombeaji urais kutoka Pwani katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Huku akiwajibu mahasimu wake wa kisiasa wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, gavana huyo aliye pia naibu kiongozi wa ODM alisema Pwani itakuwa na mgombeaji urais mwaka wa 2022 na anaamini Bw Odinga ataunga mkono mgombeaji atakayetajwa.

Kulingana naye, eneo hilo limekuwa likimuunga mkono Bw Odinga kwa muda mrefu kwa sababu waziri mkuu huyo wa zamani anajua eneo hilo linatarajia atarudisha mkono.

Kufikia sasa, Bw Odinga hajatangaza iwapo atawania urais katika uchaguzi ujao huku Bw Joho akiwa tayari ameeleza azimio lake kuwania wadhifa huo.

“Hatuwezi kuunga mkono watu wengine kila mwaka wa uchaguzi. Tunataka kukaa kwenye meza. Hatuwezi kuendelea kuwa menyu. Hatuwezi kuwa katika hali ambapo wakati wowote kuna mipango inayofanywa, hakuna hata mmoja wetu kutoka eneo letu aliyepo. Hatuwezi kuendelea kuwakilishwa. Huu ni wakati wa kiongozi kutoka eneo hili kuwa kwenye debe la urais na matokeo ya kinyang’anyiro hicho yaamuliwe mbele mbele hata iweje,” akasema.

Hata hivyo, alionya kwamba hilo halitawezekana iwapo viongozi wa eneo hilo wataendelea kujibizana kwa njia inayoashiria ubinafsi.

Alisema mfumo wa siasa za Pwani unapaswa kuwa tofauti, kwa hivyo viongozi hawapaswi kuwa wepesi kutoa wito kwa umoja wa mkoa huo bila mipango kabambe.

“Hatutafanikiwa ikiwa tutaonekana kutoelewa kile tunachohitaji kama eneo,” alisema hayo wakati wa ziara katika Kaunti ya Tana River.

Aliwakashifu viongozi wa Pwani wanaoegemea upande wa Naibu Rais akisema wana nia mbaya wanapodai kwamba wanataka kuwaunganisha Wapwani.

Kwa mujibu wa Bw Joho, umoja wa Pwani haupaswi kuwa kwa msingi wa kuunga mkono kiongozi mmoja, bali kwa madhumuni ya kuwafaidi watu wa Pwani na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.

“Hatupaswi kuambiwa kwamba tunahitaji kuungana kwa sababu ya kiongozi fulani. Ikiwa tunatafuta umoja, basi iwe kwa mkoa wetu na kwa ajili ya Wapwani. Tunapaswa kuungana kwa sababu ya changamoto tunazokabiliana nazo kama wakaaji wa eneo hili,” alisema Bw Joho.

Wito kuhusu uundaji wa chama kimoja cha Wapwani umeshika kasi tangu uchaguzi mdogo wa Msambweni ufanyike, ambapo ODM ilishindwa na upande wa Dkt Ruto licha ya kutarajiwa na wengi kunyakua kiti hicho.

Matokeo hayo yalifanya baadhi ya viongozi wa eneo hilo kumtaka Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, atwikwe jukumu la kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa Wapwani. Jukumu hilo limekuwa mikononi mwa Bw Joho kwa muda mrefu.

Wabunge wasiopungua 11 wa Pwani na Seneta wa zamani wa Mombasa Hassan Omar ambao wanamuunga mkono Dkt Ruto ndio wako katika mstari wa mbele kushinikiza kuundwa kwa mavazi mapya ya kisiasa kabla ya mwaka wa 2022.