Wanaraga wa Kenya Simbas wapata mwaliko wa kucheza dhidi ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Simbas, imepangiwa kushiriki mechi mbili dhidi ya kikosi mseto cha Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini mnamo Aprili 2021.

Kocha Paul Odera amesema kwamba ni vyema kwa kikosi hicho kusalia katika hali ya ushindani baada ya kampeni za msimu mzima wa 2020 kufutiliwa mbali kutokana na janga la corona.

Ili kufanikisha kampeni za Kenya Simbas dhidi ya Stellenbosch, kikosi hicho kimewaajiri wakufunzi wawili raia wa Afrika Kusini – Neil De Kock ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Springbok’ na Ernst Joubert ambaye ni nahodha wa zamani wa kikosi cha Saracens.

Huku De Kock akitarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi, maarifa ya Joubert yatategemewa sana katika juhudi za kuboresha makali ya idara ya mbele.

Wakufunzi hao wawili walitarajiwa pia kukinoa kikosi cha wanaraga chipukizi wa Kenya U-20 almaarufu ‘Chipu’ kwa minajili ya kampeni za kipute cha Barthes Cup kilichoahirishwa pia mwaka huu kwa sababu ya corona.

Ni matumaini ya Odera kwamba Wizara ya Michezo itawapa wanaraga wa Simbas idhini ya kuanza maandalizi mnamo Januari 2021 ili kujifua vilivyo kwa kipute dhidi ya Stellenbosch.

“Tunatarajia pia kupata idhini ya Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kuanza mazoezi kwa minajili ya michuano hiyo ijayo nchini Afrika Kusini. Iwapo wachezaji watashiriki mazoezi kwa kipindi cha miezi mitatu au minne kwa kuzingatia kanuni zote zilizopo za kudhibiti maambukizi ya Covid-19, basi tutajiweka pazuri zaidi kutamba nchini Afrika Kusini,” akasema Odera.

Shujaa na Lionesses tayari wamepewa idhini ya kuanza kujiandaa kwa Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mnamo 2021.

“Kwa kuwa sasa hakuna mechi za ligi na wanaraga wengi hawajashiriki michezo yoyote kwa takriban miezi minane iliyopita, tutategemea zaidi wachezaji waliotuwajibikia mwaka uliopita wa 2019. Hao ndio tutakaowaita kambini baada ya kupata idhini ya Serikali kupitia KRU,” akaeleza Odera.

Odera ambaye pia amewahi kuchezea timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, amesema mustakabali wa kampeni za Kombe la Afrika almaarufu Africa Cup utajulikana mwishoni mwa wiki ijayo baada ya makocha wa mataifa wanachama kushiriki mkutano wa mtandaoni na vinara wa Shirikisho la Raga la Afrika (Rugby Africa).

Ili kufanikisha ziara yao ya kutua Afrika Kusini, Odera amesema kwamba kikosi cha Kenya Simbas kitahitaji takriban Sh20 milioni na mipango ya kuchangia kikosi hicho kwa minajili ya mechi za siku 11 nchini Afrika Kusini tayari imeanza.

Odera pia ameshikilia kwamba italazimu vikosi mbalimbali vya Ligi Kuu ya Kenya Cup kuimarisha viwango vyao vya mchezo ili kuwezesha timu ya taifa ya Shujaa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.

“Kuboreka kwa kikosi cha taifa na kusalia hai kwa matumaini ya timu hiyo kufuzu kwa Kombe la Dunia kutategemea kuimarika kwa raga yetu katika viwango vya ligi. Nimekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na baadhi ya wakufunzi wa vikosi mbalimbali vya Ligi Kuu na tumeshauriana kuhusu jinsi ya kuimarisha ushindani katika idara mbalimbali za vikosi vyao,” akasema Odera.

Odera akanusha anataka kutoroka Simbas kujiunga na Shujaa

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji 15 kila upande Paul Odera amepuuzilia mbali madai kuwa anamezea mate wadhifa wa kocha mkuu wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa.

Katika mahojiano Alhamisi, kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 ameambia Taifa Leo: “Kuna uvumi mwingi tu unaenezwa. Mimi sikutuma ombi la kuwa kocha mkuu wa timu ya Shujaa.”

Odera, ambaye ni mwalimu wa shule ya Peponi House Preparatory jijini Nairobi, amesema kuwa lengo lake ni kuongoza Simbas katika kampeni za kufika Kombe la Dunia 2023.

“Lengo langu ni Kombe la Dunia 2023 la raga ya wachezaji 15 kila upande nchini Ufaransa,” anasema kocha huyo aliyeongoza timu ya chipukizi ya Kenya almaarufu Chipu mwaka 2019 kupiga miamba Namibia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2005 na kuingia Kombe la Dunia la daraja ya pili la makinda (JWRT) lililofanyika nchini Brazil.

Alipoulizwa kuthibitisha habari zinazosambaa kuwa Odera yuko mstari wa mbele kutwikwa majukumu ya Shujaa, Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga Kenya (KRU) Oduor Gangla amesema “sina habari kuhusu hilo.”

Wadhifa wa kocha mkuu wa Shujaa uliachwa wazi baada ya raia wa New Zealand Paul Feeney kuondoka Juni 12.

Feeney alisaidiwa na kocha wa klabu ya Mwamba, Kevin ‘Bling’ Wambua ambaye huenda akatwikwa majukumu hayo baada ya Wakenya Benjamin Ayimba, Felix Ochieng’, Innocent Simiyu, Mitch Ocholla na Paul Murunga kuwa kileleni miaka ya hivi karibuni.

KRU inatafuta kocha Mkenya kuongoza Shujaa kwa mashindao ya kifahari ya Raga ya Dunia pamoja na mashindano mengine ya kimataifa.

Kazi hii inahitaji kocha kujukumika wakati wote. Inamaanisha kuwa Odera atalazimika kuacha ualimu kwa muda atakaoongoza Shujaa.

Odera alicheza raga kati ya mwaka 1986 na 2005 alipostaafu uchezaji baada ya kupata jeraha mbaya la shingo. Mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Barclays Bank na Kenya Harlequin alianza kazi ya ukocha mwaka 1994 akiwa mchezaji kabla ya kuzamia shughuli hiyo kabisa alipostaafu kucheza.

Simbas kutumia kipute cha raga ya Afrika kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha kuwania Raga ya Kombe la Afrika mnamo 2022 sasa kitatumiwa na Kenya Simbas kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2023 nchini Ufaransa.

Kivumbi cha Africa Cup hakijafanyika kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita kutokana na uchechefu wa fedha na janga la corona mtawalia. Kampeni hizo zitarejelewa mwakani.

Mshindi wa Africa Cup atajikatia tiketi ya moja kwa moja ya kuingia fainali za Kombe la Dunia huku nambari mbili akilazimika kushiriki mchujo dhidi ya vikosi vingine vitatu kutoka mashirikisho tofauti.

Timu 12 tayari zimefuzu kwa fainali za 2023 nchini Ufaransa baada ya kukamata nafasi tatu za kwanza kwenye kampeni zao za Raga ya Dunia (RWC) katika msimu wa 2019. Hizi ni pamoja na Afrika, Uingereza, New Zealand, Wales, Japan, wenyeji Ufaransa, Australia, Ireland, Scotland, Italia, Argentina na Fiji.

Nafasi nane zilizosalia zitaamuliwa kupitia mchakato wa timu kushiriki mapambano ya mchujo katika kiwango cha kimaeneo. Shughuli hiyo itakamilika kwa mchujo wa mwisho utakaoshirikisha timu nne za mwisho mnamo Novemba 2022. Tarehe za kuandaliwa kwa mashindano ya msimu wa 2021 zitatolewa mapema wiki ijayo.

Kenya Simbas walikosa tiketi ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia mnamo 2019 baada ya kuzidiwa maarifa na Canada kwenye mchujo wa mwisho uliotawaliwa na Ujerumani na Hong Kong nchini Ufaransa.

Chini ya kocha Paul Odera, Kenya Simbas watakuwa wakiwania fursa ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia.

Mnamo 2018, Simbas waliambulia nafasi ya pili barani Afrika baada ya kuwapepeta Uganda, Tunisia na Zimbabwe kabla ya chombo chao kuzamishwa na Namibia jijini Windhoek.

Mnamo 2015, walikosa padogo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Uingereza baada ya Zimbabwe kuwazaba 27-10.

Awali, Kenya ilikuwa imewapiga wenyeji Madagascar 34-0 na Namibia ambao hatimaye waliwakilisha bara la Afrika kwa 29-22 katika hatua ya makundi.

Odera amesema kutoandaliwa kwa Kombe la Afrika katika kipindi cha miaka miwili mfululizo ni pigo kubwa kwa maandalizi ya kikosi chake ambacho sasa hakitashiriki mapambano yoyote ya haiba kubwa mwaka huu.

“Yasikitisha kwamba tutakuwa na mwaka mmoja pekee wa kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia. Ingawa jambo hili linatuweka katika hali ngumu, naamini ukubwa wa uwezo wa vijana wangu” akasema.

Mechi za Simbas katika Kombe la Afrika zilitarajiwa kuanza dhidi ya Morocco kisha Ivory Coast, Uganda na Zimbabwe.

Simbas watoa mwongozo mpya wa kuboresha raga nchini Kenya

Na CHRIS ADUNGO

BENCHI ya kiufundi ya kikosi cha raga ya wachezaji 15 kila upande, Simbas, imebuni mwongozo mpya wa ukufunzi na usimamizi utakaosaidia pia klabu mbalimbali kujiimarisha na kuboresha maandalizi yao baada ya shughuli za michezo kurejelewa.

Michezo yote kwa sasa imesitishwa humu nchini na katika mataifa mengi duniani kote kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Mwongozo huo unashughulikia masuala ya afya, jinsi ya kuimarisha mazoezi ya viungo vya mwili miongoni mwa wanaraga na namna ya kuboresha idara za ulinzi, kati na uvamizi za vikosi. Mwongozo huo unapania pia kuwapa maafisa wa mechi mbinu bora zaidi za kukumbatia kila wanaposimamia au kuendesha michuano mbalimbali.

Kocha Paul Odera amekiri kwamba analenga kuutumia mwongozo huo kwa kipindi chote kilichosalia katika mkataba wake na kikosi cha Simbas na kile cha wanaraga chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Chipu.

“Tutakuwa tukifanyia mwongozo huo mabadiliko ya mara kwa mara ili uwiane na mazingira na mahitaji yote ya raga ya humu nchini pamoja na viwango vya kimataifa,” akasema Odera.

Mwanaraga huyo wa zamani wa timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, amesema vikosi vya Kenya vinakosa mtindo ambao ni kitambulisho chao katika ulingo wa raga ikilinganishwa na Afrika Kusini, New Zealand, Uingereza, Australia na Ufaransa ambao ni miamba wa mchezo huo duniani.

“Mfumo na mtindo wetu wa kucheza unastahili kujumuisha upana wa utamaduni wetu bila ya yeyote kubaguliwa kwa misingi ya rangi, kabila au mahusiano ya kijamii. Uwezo wa wanaraga wetu kutumia uchache wa raslimali tulizonazo na kuchuma nafuu kutokana na vipaji vya mbio na ukubwa wa miili unastahili kuwa kitambulisho chetu,” akaongeza.

Simbas walikuwa wameanza kujifua mapema Machi 2020 kwa minajili ya kampeni mbalimbali za raga ya kimataifa kabla ya Serikali kusimamisha kwa muda michezo yote kutokana na janga la corona ambalo limetikisa ulimwengu mzima.

Chini ya Odera, kikosi cha Simbas kilikuwa kimepangiwa kuchuana na Morocco, Uganda na Zimbabwe katika kipute cha kuwania ufalme wa Raga ya Bara la Afrika mwishoni mwa Mei kabla ya kinyang’anyiro hicho kuahirishwa.

Simbas walikuwa pua na mdomo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Raga mnamo 2015 kabla ya kuzidiwa maarifa na Namibia.

Katika makala ya Raga ya Afrika mwaka jana, Simbas waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Namibia barani kabla ya kupepetwa na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika kundi la kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Chipu nao walikuwa wakijifua kwa minajili ya kipute cha Barthes Cup kilichotarajiwa kuandaliwa jijini Nairobi mnamo kati ya Aprili 19-22. Odera aliwahi kukiri kwamba changamoto kubwa anayokabiliana nayo kambini mwa Chipu ni ugumu wa kuoanisha mitindo ya kucheza kwa wanaraga wake.

Hilo lilichochea Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kujinasia huduma za wakufunzi Hans Joubert na Neil De Kock kutoka Afrika Kusini mnamo Februari 2020. Wawili hao walikuwa washirikiane na Odera kuwanoa wanaraga wa Chipu kwa minajili ya kutetea ubingwa wa Barthes Cup mnamo Aprili 2020.

Kenya ilitazamia kutumia mashindano hayo kufuzu kwa Raga ya Dunia kwa Chipukizi (JWRT) nchini Uhispania mnamo 2020 na fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.

Odera ataja kikosi cha Simbas kukabiliana na Zimbabwe raga ya Victoria Cup

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imetangaza kikosi chake cha Simbas kitakacholimana na Zimbabwe katika mechi ya mwisho ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Victoria Cup uwanjani Nakuru Athletic mjini Nakuru hapo Septemba 21.

Kocha Paul Odera amejumuisha Joshua Chisanga, ambaye amekosa mechi mbili zilizopita dhidi ya Uganda, mbili dhidi ya Zambia na Zimbabwe (moja) kwenye Victoria Cup.

Chisanga alichezea Kenya mara ya mwisho katika mchujo wa mwisho wa kuingia Kombe la Dunia uliokutanisha Kenya dhidi ya Canada, Ujerumani na Hong Kong mwezi Novemba mwaka 2018 nchini Ufaransa.

Kenya ilichapwa 30-29 na Zimbabwe ilipozuru mjini Bulawayo kwa mechi ya mkondo wa kwanza mwezi Agosti na itatumai itafanikiwa kulipiza kisasi dhidi ya Zimbabwe, ambayo imeshinda mechi zake tano zilizopita.

Simbas ilianza kampeni kwa kulimwa na Uganda 16-13 mjini Kisumu kabla ya kulipiza kisasi 16-5 jijini Kampala na kisha kupepeta Zambia 43-23 mjini Kitwe na kupoteza 30-29 dhidi ya Zimbabwe kabla ya kunyamazisha Zambia 31-16 jijini Nairobi mnamo Agosti 24.

Kikosi cha Kenya Simbas: Wachezaji 15 wa kwanza – Ian Njenga, Toby Francombe, Melvin Thairu; Emmanuel Mavala, Malcolm Onsando; Joshua Chisanga, Monate Akuei, Elkeans Musonye; Samson Onsomu (nahodha), Charles Kuka; John Okoth, Vincent Onyala; Timothy Okwemba, Geoffrey Okwach na Anthony Odhiambo.

Wachezaji wa akiba – Frank Mutuku, Elisha Koronya, Ian Masheti, Brian Juma, Samuel Were, Barry Robinson, Tony Omondi na Michael Kimwele.

Lazima tujipange kabla ya mechi za marudiano – Odera

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Paul Odera amekiri kuna kazi kubwa ya kufanywa kabla ya Simbas kualika Zambia (Agosti 24) na mabingwa watetezi Zimbabwe (Septemba 21) katika mechi za marudiano za raga ya wachezaji 15 kila upande ya Victoria Cup.

Akizungumza na Taifa Leo baada ya Simbas kuzimwa 30-29 na Zimbabwe mjini Bulawayo, Odera alisema, “Ilikuwa mechi ngumu jinsi nilivyobashiri itakuwa. Tumejifunza jinsi ya kukabiliana na mashambulizi na kulinda ngome yetu pembeni. Hata hivyo, kazi bado ipo kabla ya mechi ya marudiano.”

Kabla ya kucheza na Zimbabwe hapo Agosti 3, Odera alikuwa ametabiri kuwa mechi dhidi ya wapinzani hawa itakuwa kali zaidi katika mashindano haya ya mataifa manne.

“Mechi dhidi ya Zimbabwe itakuwa ngumu kabisa. Motisha yetu iko juu. Wachezaji wazoefu wanashirikiana vyema na wale chipukizi kwa karibu. Tunathamini ujuzi wa wachezaji waliowahi kucheza kombe hili mjini Bulawayo,” alisema Odera kabla ya mechi hiyo ambayo Kenya ilipata alama zake kupitia kwa Monate Akuei (miguso miwili), Anthony Odhiambo (mguso mmoja na mkwaju), Elkeans Musonye (mguso mmoja), Johnstone Mung’au (mguso mmoja) na Charles Kuka (mkwaju).

Nahodha wa Zimbabwe, Hilton Mudariki alifungia timu yake alama 15 nao Takudzwa Kumadiro, David Makanda na Biselele Tshamala wakachangia mguso mmoja kila mmoja.

Kichapo hicho kilikuwa cha kwanza cha Kenya dhidi ya Zimbabwe tangu ilimwe 28-20 uwanjani Prince Edward mwaka 2015.

Tangu wakati huo, Kenya ilikuwa imetawala michuano yake dhidi ya Zimbabwe ikiwemo kubwaga Wazimbabwe mara mbili nchini Zimbabwe na moja jijini Nairobi.

Simbas iliingia nchini Zimbabwe ikitokea Zambia ambako ilikuwa imetamba 43-23 mjini Kitwe.

Majeraha ziarani

Ziara za Kenya nchini Zambia na Zimbabwe zilishuhudia ikipata majeraha matatu.

Isaac Njoroge alipata jeraha la kichwa dhidi ya Zambia mnamo Julai 27.

Hakushiriki mechi ya Zimbabwe baada ya kufeli uchunguzi wa kimatibabu.

Patrick Ouko na Melvin Thairu walipata majeraha ya kifundo dhidi ya Zimbabwe.

Baada ya mechi za wikendi, Zimbabwe inaongoza jedwali la Victoria Cup kwa alama 15.

Iliingia mechi ya Kenya na motisha ya kupepeta Zambia 39-10 (Julai 13) na Uganda 31-26 (Julai 27).

Kenya ni ya pili kwa alama 11 baada ya kupoteza pembamba dhidi ya Zimbabwe na kulima Uganda 16-5 na Zambia 43-23.

Uganda ina alama mbili kwa kupoteza pembamba dhidi ya Zimbabwe. Aidha, mechi kati ya Uganda na Zambia iiliyoratibiwa kusakatwa Agosti 10, imeahirishwa hadi Agosti 17.

Mabadiliko haya, kwa mujibu wa Shirikisho la Raga nchini Uganda, yalifanywa baada ya Zambia kuomba mchuano huo usukumwe mbele kutokana na mabadiliko katika mipango ya usafiri. Simbas ilirejea nchini Jumapili jioni.

Simbas walia kukosa mshahara wa Novemba

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Kenya Simbas inadai Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mamilioni ya fedha ambayo ni mshahara wa mwezi Novemba mwaka 2018.

Ripoti zinasema kwamba wachezaji 30 waliozuru jiji la Bucharest mnamo Novemba 3 na kujipima nguvu dhidi ya Romania pamoja na kushiriki mchujo wa mwisho wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kati ya Novemba 11 na Novemba 23 nchini Ufaransa, wanadai KRU Sh40, 000 kila mmoja.

“Tumelipwa marupurupu ya kusafiri nchini Romania na Ufaransa na pia marupurupu ya mechi. Hata hivyo, bado hatujapokea mshahara wetu wa Novemba,” amefichua mchezaji mmoja wa timu hiyo, ambaye hakutaka kutajwa.

Mchezaji huyo tegemeo aliongeza kwamba benchi la kiufundi la maafisa wanane pia halijalipwa kwa muda unaozidi ule wa wachezaji.

Simbas, ambayo ilimaliza Kombe la Afrika katika nafasi ya pili nyuma ya Namibia mwezi Agosti, ilichabangwa 36-5 na Romania kabla ya kulemewa na Canada (65-19), Hong Kong (42-17) na Ujerumani (43-6). Canada ilipepeta kila timu katika mchujo huo na kunyakua tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Japan.

Nahodha wa Simbas kukosa mechi kali dhidi ya Hong Kong

Na GEOFFREY ANENE

NAHODHA Davis Chenge atakosa mechi ya Kenya Simbas ya kufa kupona dhidi ya Hong Kong ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande mjini Marseille, Ufaransa hapo Novemba 17, 2019.

Chenge, ambaye ni mchezaji wa klabu ya KCB jijini Nairobi, aliumia bega katika mechi ya ufunguzi ya mchujo huu wa mataifa manne dhidi ya Canada mnamo Novemba 11. Simbas iliumizwa kwa alama 65-19 katika mechi hiyo.

Kocha Ian Snook amefanya mabadiliko sita katika kikosi kilichopoteza dhidi ya Canada akilenga kutafuta ushindi wa kufufua kampeni ya Kenya.

Amempa nahodha wa zamani Wilson K’opondo majukumu ya unahodha. Pia ataanzisha K’Opondo pamoja na Elkeans Musonye, Felix Ayange na Nelson Oyoo katika mechi hii. Nao Ephraim Oduor na Dalmus Chituyi wataingia kama wachezaji wa akiba.

Mohammed Omollo, Moses Amusala, Oliver Mang’eni na Darwin Mukidza wamepumzishwa wikendi hii. Benchi la kiufundi linatarajia Chenge kuwa fiti kushiriki mechi ya mwisho dhidi ya Ujerumani hapo Novemba 23. Kutoka orodha hii ya mataifa manne, timu itakayokamilisha juu ya jedwali itaingia Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Japan mwaka 2019. Itamenyana na New Zealand, Afrika Kusini, Italia na Namibia katika Kundi B.

Kikosi cha Simbas kitakachovaana na Hong Kong: Wachezaji 15 wa kwanza – Patrick Ouko, Colman Were, Joseph Odero, Wilson K’opondo (nahodha), Malcolm Onsando, Andrew Amonde, Elkeans Musonye, Joshua Chisanga, Felix Ayange, Samuel Oliech, William Ambaka, Leo Seje Owade, Collins Injera, Nelson Oyoo na Tony Onyango;

Wachezaji wa akiba – Philip Ikambili, Ephraim Oduor, Hilary Mwanjilwa, George Nyambua, Martin Owilah, Samson Onsomu, William Reeve na Dalmus Chituyi.

Historia kati ya Kenya na Hong Kong

Desemba 13, 2011: Hong Kong 44-17 Kenya (Dubai, Cup of Nations)

Agosti 23, 2016: Kenya 24-18 Hong Kong (Nairobi, Kirafiki)

Agosti 26, 2016: Kenya 34-10 Hong Kong (Nairobi, Kirafiki)

Agosti 20, 2017: Kenya 19-19 Hong Kong (Nairobi, Kirafiki)

Agosti 26, 2017: Kenya 34-43 Hong Kong (Nairobi, Kirafiki)

Novemba 18, 2017: Hong Kong 40-30 Kenya (Hong Kong, Cup of Nations)

Romania yataja kikosi kitakachovaana na Simbas Bucharest

Na GEOFFREY ANENE

NCHI ya Romania imetaja kikosi chake kitakachopimana nguvu na Kenya Simbas katika mechi ya raga ya wachezaji 15 kila upande jijini Bucharest hapo Novemba 3, 2018.

Romania haijawahi kukutana na Kenya katika mechi ya raga. Simbas ya kocha Ian Snook iliondoka jijini Nairobi mnamo Oktoba 31 ikipitia Ufaransa. Italimana na Romania kuanzia saa nane mchana Jumamosi.

Mabingwa wa Afrika mwaka 2011 na 2013 Kenya wanatumia mchuano huu, ambao utapeperushwa na runinga ya Romania ya Telekom Sport, kujiandaa kwa mchujo wa mwisho wa kuingia Kombe la Dunia mwaka 2019.

Mchujo wenyewe utafanyika mjini Marseille nchini Ufaransa kati ya Novemba 11 na Novemba 23 ukikutanisha Kenya, Canada, Hong Kong na Ujerumani. Mshindi atajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Japan mwaka ujao.

Kenya, ambayo haijawahi kushiriki Kombe la Dunia katika historia yake, itaanza kutafita tiketi dhidi ya Canada mnamo Novemba 11, imenyane na Hong Kong mnamo Novemba 17 na kukamilisha kampeni yake dhidi ya Ujerumani hapo Novemba 23.

Itakuwa mara ya kwanza Kenya kukutana na Canada, lakini imewahi kucheza na Ujerumani mara moja na Hong Kong mara sita.

Romania itakuwa mtihani mkubwa kwa Simbas kwa sababu ina ujuzi wa miaka mingi. Imeshiriki Kombe la Dunia tangu makala ya kwanza mwaka 1987, ingawa haitakuwa nchini Japan mwaka 2019 baada ya kuondolewa ilipopatikana imechezesha mchezaji mmoja ambaye si wake katika mechi za kufuzu. Romania inashikilia nafasi ya 17 duniani nayo Kenya ni ya 28.

Vikosi:

Romania A

Wachezaji 15 wa kwanza – Constantin Pristavita, Eugen Capatana (nahodha), Alexandru Gordas, Marius Iftimiciuc, Marian Drenceanu, Adrian Ion, Cristi Chirica, Damian Stratila, Florin Suruglu, Daniel Plai, Ionut Dumitru, Vladut Zaharia, Ionel Melinte

Wachezaji wa akiba – Andre Radoi, Florin Bardasu, Alexandru Savin, Laurentiu Nica, Vasile Balan, Ionut Muresan, Dumani Mtya, Kuselo Moyake, Valentin Calafeteanu, Tudorel Bratu, Tudor Boldor, Alexandru Bucur, Robert Neagu.

Kenya

Patrick Ouko (Homeboyz), Moses Amusala (KCB), Joseph Odero (Kabras Sugar), Hillary Mwanjilwa (Kabras Sugar), Ephraim Oduor (Kabras Sugar), Colman Were (Kabras Sugar), Philip Ikambili (Homeboyz), Oliver Mang’eni (KCB), Wilson K’opondo (Kenya Harlequins), Malcolm Onsando (Kenya Harlequins), Simon Muniafu (Impala Saracens), Andrew Omonde (KCB), George Nyambua (Kabras Sugar), Dalmus Chituyi (Homeboyz), Elkeans Musonye (Strathmore Leos), Joshua Chisanga (Homeboyz), Davis Chenge (KCB), Martin Owilah (KCB), Samson Onsomu (Impala Saracens), Mohammed Omollo (Homeboyz), Samuel Oliech (Impala Saracens), Darwin Mukidza (KCB), Leo Seje Owade (Impala Saracens), Peter Kilonzo (KCB), Collins Injera (Mwamba), Nelson Oyoo (Nakuru), Felix Ayange (Kabras Sugar), William Ambaka (Kenya Harlequins), Tony Onyango (Homeboyz) na William Reeve (Kenya Harlequins).

Simbas kuraruana na Romania na Namibia kabla ya mchujo wa Kombe la Dunia

Na Geoffrey Anene

KENYA Simbas itasakata mechi nne za kujipima nguvu kati ya Oktoba 7 na Novemba 3 kabla ya mchujo wa kufa-kupona wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande nchini Ufaransa hapo Novemba 11-23, 2018.

Simbas ilikuwa imeomba Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kuitafutia mechi mbili za kirafiki, lakini taarifa kutoka shirikisho hilo zinasema kwamba vijana wa kocha Ian Snook watalimana na British Army kutoka Nanyuki, mabingwa wa Afrika Namibia, klabu ya Blue Bulls kutoka Afrika Kusini na timu ya taifa ya Romania kabla ya kuelekea mjini Marseille.

Kenya inafahamu British Army kwa sababu imefanya mazoezi mara kadhaa nayo katika milima ya Nanyuki. Ilijitayarisha kwa mechi yake ya mwisho ya Kombe la Afrika la Dhahabu dhidi ya Namibia kwa kufanya mazoezi na British Army, ingawa ilipoteza 53-28 jijini Windhoek na kuingia mchujo huu wa mwisho, huku Namibia ikijikatia tiketi ya kuelekea Japan mwaka 2019 kama bingwa wa wa Afrika.

Simbas inajua Namibia kutokana na mashindano ya kila mwaka ya Kombe la Afrika, lakini haijawahi kukutana na Blue Bulls wala Romania.

Simbas itamenyana na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika mchujo wa kuingia Kombe la Dunia. Mshindi wa mchujo huu wa mataifa manne atajaza nafasi ya 24 (mwisho) iliyosalia. Atatiwa katika Kundi B pamoja na New Zealand, Afrika Kusini, Italia na Namibia.

Ratiba na matokeo ya Simbas mwaka 2018:

Oktoba 7

Kenya na British Army (Kirafiki, Nairobi)

Oktoba 21

Kenya na Namibia (Kirafiki, Nairobi)

Oktoba 28

Kenya na Blue Bulls kutoka Afrika Kusini (Kirafiki, Nairobi)

Novemba 3

Romania A na Kenya (Kirafiki, Bucharest)

Novemba 11

Canada na Kenya (Mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, 6.30pm Marseille, Ufaransa)

Novemba 17

Hong Kong na Kenya (Mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, 4.00pm Marseille, Ufaransa)

Novemba 23

Kenya na Ujerumani (Mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, 8.00pm Marseille, Ufaransa)

Juni 23

Morocco 24-28 Kenya

Juni 30

Kenya 45-36 Zimbabwe

Julai 7

Kenya 38-22 Uganda

Agosti 11

Kenya 67-0 Tunisia

Agosti 18

Namibia 53-28 Kenya

Simbas yaomba Wakenya Sh40 milioni kujiandaa kwa mchujo

Na Geoffrey Anene 

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) linahitaji Sh40 milioni kuiandaa Kenya Simbas kisawasawa kwa mchujo wa Kombe la Dunia utakaoandaliwa nchini Ufaransa kutoka Novemba 11-23, 2018.

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Septemba 7, Mkurugenzi wa Raga wa KRU Thomas Odundo amesema KRU inatafuta fedha hizo zitakazogharamia matayarisho, kambi ya mazoezi na ziara ya Simbas mjini Marseille ambapo italimana na Canada, Hong Kong na Ujerumani.

Simbas, ambayo inanolewa na kocha kutoka New Zealand Ian Snook, imekuwa ikifanya mazoezi ya viungo katika jimu ya Alpha Fit kwenye barabara ya Ngong Road hatua chache kutoka makao makuu ya KRU jijini Nairobi.

Kila Ijumaa na Jumamosi, Simbas inafanya mazoezi hayo ya viungo kujiweka fiti. Inafanya mazoezi mepesi ya uwanjani kila Jumamosi. Itaanza mazoezi makali ya uwanjani Oktoba 1.

Inatarajia kusakata mechi mbili za kirafiki jijini Nairobi kabla ya kuelekea Marseille. Kenya imeomba Shirikisho la Raga Duniani (World Rugby) kuitafutia mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Namibia, ambayo iko Kundi B katika Kombe la Dunia.

Namibia ilifuzu baada ya kupepeta Kenya, Tunisia, Morocco, Uganda na Zimbabwe katika Kombe la Afrika la Dhahabu lilokamilika Agosti 18.

Kenya ilifuzu kushiriki mchujo wa mwisho kwa kumaliza ya pili barani Afrika. Mshindi kati ya Kenya, Canada, Hong Kong na Ujerumani ataingia Kundi B linaloshirikisha Namibia, New Zealand, Italia na Afrika Kusini. Kombe la Dunia ni mwaka 2019 nchini Japan.

Simbas kumenyana na mahasidi Namibia Nairobi Oktoba 28

Na Geoffrey Anene

KENYA Simbas itaalika miamba Namibia jijini Nairobi hapo Oktoba 28 kwa mechi ya kirafiki kabla ya kuelekea nchini Ufaransa kwa mchujo wa mwisho wa kuingia Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande utakaofanyika Novemba 11-23, 2018.

Kwa mujibu wa gazeti la The Star, Simbas ya kocha Ian Snook pia huenda ikajipiga msasa dhidi ya Ureno nchini Ufaransa kabla ya kukabiliana na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika mchujo huo, ambao mshindi ataingia katika Kundi B linalojumuisha New Zealand, Afrika Kusini, Italia na Namibia.

Gazeti hilo limesema nyota wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Shujaa, Nelson Oyoo, Andrew Amonde, Dennis Ombachi na Samuel Oliech wameitwa kujiunga na Simbas baada ya majukumu na klabu zao kwenye duru ya raga ya kitaifa ya Dala Sevens mjini Kisumu hapo Septemba 8-9.

Kenya inafahamu Namibia vyema. Zimekutana mara 11 Simbas ikishinda mara mbili (30-26 mwaka 2006 na 29-22 mwaka 2014) na kupepetwa mechi zingine zote ikiwa ni pamoja na 53-28 zilipokutana katika fainali ya Kombe la Afrika mwezi uliopita wa Agosti.

Simbas imewahi kukutana na Ureno na Ujerumani mara moja pekee. Ilicharaza Ureno katika mechi ya kujipima nguvu mnamo Mei 30 mwaka 2015 uwanjani RFUEA jijini Nairobi. Simbas ilimenyana na Ujerumani mnamo Mei 27 uwanjani RFUEA na kuzabwa japo pembamba 30-29. Haijawahi kukutana na Canada katika raga ya wachezaji 15 kila upande.

Kenya na Hong Kong pia zinafahamiana sana. Mwaka 2017 pekee, zilikutana mara tatu. Hong Kong ilikaba Simbas 19-19 na kuipiga 43-34 mwezi Agosti jijini Nairobi kabla ya kuiongeza kichapo kingine cha 40-30 mjini Hong Kong mwezi Novemba.

Lazima Simbas iimarishe ulinzi ili kupaa – Snook

Na Geoffrey Anene

Kocha Ian Snook amekiri Kenya Simbas ina matatizo katika idara ya ulinzi na kusema haina budi kuimarisha idara hiyo ikitaka kufuzu kushiriki Kombe la Dunia nchini Japan mwaka 2019.

Simbas haikufuzu kupitia mchujo wa Kombe la Afrika ilipomaliza nyuma ya Namibia, lakini ina nafasi ya mwisho ya kujaribu bahati itakapokabiliana na Canada, Hong Kong na Ujerumani mjini Marseille nchini Ufaransa mwezi Novemba 11-23, 2018.

Snook na vijana wake watarejelea mazoezi Septemba 3 baada ya mapumziko ya karibu majuma mawili. Walikamilisha Kombe la Afrika kwa kuzabwa na Namibia 53-28 Agosti 18 jijini Windhoek.

“Lazima tuimarishe idara ya ulinzi kabla ya kuelekea Ufaransa. Ulinzi ni mojawapo ya matatizo tulikuwa nayo katika Kombe la Afrika na lazima tuhakikishe tunarekebisha idara hii,” Snook amenukuliwa na tovuti ya KweséESPN akisema.

“Mchujo hautakuwa rahisi, lakini wachezaji wanafahamu kibarua kinachotusubiri nchini Ufaransa. Tuna uwezo wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, lakini lazima tutie bidii,” aliongeza.

Raia huyu wa New Zealand ameeleza tovuti hiyo kwamba anatumai Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) litatafutia Simbas mechi za kujipima nguvu kabla ya ziara ya Ufaransa.

Kenya, ambayo haijawahi kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande katika historia yake, itafungua mchujo huo dhidi ya Canada (Novemba 11), kisha ilimane na Hong Kong (Novemba 17) na kuukamilisha dhidi ya Ujerumani (Novemba 23).

Mshindi wa mchujo huu ataungana na New Zealand, ambao ni mabingwa watetezi, Afrika Kusini, Italia na Namibia katika Kundi B kwenye Kombe la Dunia.

Snook amejumuisha wachezaji wapya Thomas Okidia, Ephraim Oduor na Elvis Namusasi katika kikosi chake cha watu 33 na kuita tena nahodha wa zamani Wilson Kopondo, ambaye hakushiriki Kombe la Afrika. Amewatema Curtis Lilako, Oscar Simiyu, Isaac Adimo, Edmund Anya na Erick Kerre.

Kikosi cha Simbas:

Patrick Ouko, Thomas Okidia, Philip Ikambili, Dalmus Chituyi, Mohamed Omollo, Maxwell Kang’eri, Zedden Marrow, Tony Onyango (wote Homeboyz), Moses Amusala, Peter Karia, Oliver Mang’eni, Davis Chenge, Martin Owilah, Darwin Mukidza, Jacob Ojee, Peter Kilonzo (wote KCB), Ephraim Oduor, Joseph Odero, Hillary Mwanjilwa, Colman Were, Andrew Chogo, George Nyambua, Felix Ayange (wote Kabras Sugar), Samson Onsomu, Xavier Kipng’etich, Leo Seje, Vincent Mose (wote Impala Saracens), William Ambaka (Kenya Harlequin), Wilson Kopondo, Malcolm Onsando (wote Kenya Harlequin), Elkeans Musonye (Strathmore Leos), Biko Adema (Nondescripts) na Elvis Namusasi (Mombasa).

Simbas yaanza kujipanga kwa mchujo kufuzu kwa Kombe la Dunia

Na GEOFFREY ANENE 

KENYA Simbas itarejelea mazoezi yake Septemba 3 kujiandaa kwa mchujo wa mwisho wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande mwaka 2019 utakaoandaliwa kutoka Novemba 11-23, 2018 mjini Marseille, Ufaransa.

Simbas ya kocha Ian Snook ilipoteza nafasi ya kufuzu moja kwa moja kupitia mchujo wa Bara Afrika iliponyukwa 53-28 na Namibia katika fainali ya Kombe la Afrika la Dhahabu jijini Windhoek mnamo Agosti 18.

Mabingwa wa Afrika mwaka 2011 na 2013, Kenya, watakabana koo na Canada (Novemba 11), Hong Kong (Novemba 17) na Ujerumani (Novemba 23) katika mchujo wa mwisho ambao mshindi atajikatia tiketi ya kumenyana na New Zealand, Afrika Kusini, Italia na Namibia katika Kundi B la Kombe la Dunia.

Kenya haijawahi kukutana na Canada katika historia yake. Inafahamu Ujerumani na Hong Kong.

Ikinolewa na raia wa Afrika Kusini Jerome Paarwater, Kenya ililimwa 30-29 na Ujerumani katika mechi ya kirafiki mnamo Mei 27 mwaka 2017 uwanjani RFUEA jijini Nairobi.

Imekabiliana na Hong Kong mara sita. Simbas ilipepetwa 44-17 zilipokutana mara ya kwanza kabisa katika shindano la mwaliko mnamo Desemba 13 mwaka 2011 mjini Dubai nchini Milki za Kiarabu. Kenya kisha ilizaba Hong Kong 24-18 na 34-10 jijini Nairobi mwaka 2016. Mwaka 2017, Kenya ilikaba Hong Kong 19-19 Agosti 20 na kulimwa 43-34 Agosti 26 jijini Nairobi katika mechi za kirafiki uwanjani RFUEA kabla ya kulemewa tena 40-30 Novemba 17 mjini Hong Kong katika shindano la Cup of Nations.

Katika viwango bora vya raga duniani vya wakati huu, Hong Kong, Canada, Kenya na Ujerumani zinashikilia nafasi za 21, 23, 28 na 29, mtawalia.

Ratiba na matokeo ya Simbas mwaka 2018:

Novemba 11

Canada na Kenya (6.30pm)

Novemba 17

Hong Kong na Kenya (4.00pm)

Novemba 23

Kenya na Ujerumani (8.00pm)

Juni 23

Morocco 24-28 Kenya

Juni 30

Kenya 45-36 Zimbabwe

Julai 7

Kenya 38-22 Uganda

Agosti 11

Kenya na Tunisia

Agosti 18

Namibia 53-28 Kenya

Mastaa warejea kikosini kupepetana na Namibia fainali

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Dalmus Chituyi, Felix Ayange na Curtis Lilako wamerejea katika kikosi cha Simbas kitakacholimana na Namibia katika fainali ya Kombe la Afrika la raga ya wachezaji 15 kila upande hapo Agosti 18, 2018.

Chituyi, ambaye alipachika miguso miwili katika ushindi wa Kenya wa alama 45-36 dhidi ya Zimbabwe mnamo Juni 30, alikosa mechi dhidi ya Tunisia ambayo Simbas ilitawala 67-0 Agosti 11 jijini Nairobi.

Alikuwa na jeraha sawa na mchezaji wa zamani wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande Ayange, na Lilako.

Kocha Ian Snook anaamini watatu hawa wataleta utofauti mkubwa katika mchezo wa Simbas, ambayo inafukuzia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yake.

“Mabadiliko kadhaa tumekuwa tukifanya yamezalisha matunda. Washambuliaji wapya ambao tumetumia kama wachezaji wa akiba wamesababisha tofauti kubwa kila wanapoingia dakika za lala-salama.

Tunatumai mambo pia hayatakuwa tofauti tutakapowatumia wakati huo. Felix ataanza kwenye kiti kwa sababu anaweza kucheza katika nafasi nyingi na kufanya vizuri katika nafasi hizo.

Ni mshindani mkali na tunajua yuko tayari kukabiliana kimwili. Biko Adema, ambaye hucheza nafasi hiyo, bado anauguza jeraha. Curtis amerejea kwa hivyo tunaweza kutumia ujuzi na utulivu wake katika dakika za mwisho mwisho katika mchuano huo.”

Snook pia alizungumzia kuhusu matarajio ya Simbas katika mechi ya Namibia akisema, “Matumaini yetu na azma yetu ni kucheza vyema na katika dakika zote 80.

Tumekuwa tukicheza vyema dakika 40 ama zaidi katika mechi zilizotagulia. Imekuwa vigumu sana kwa sababu hatukuwa na mechi za kujipima nguvu kabla ya msimu kuanza. Mechi ya Tunisia ilitusaidia sana kujaribu karibu kila kitu.

Natumai wachezaji walijifunza kutokana na mechi hiyo. Natarajia kwamba wachezaji wangu wako tayari kutia bidii dakika 80 na wanasubiri mechi hiyo kwa hamu kubwa.”

Simbas, ambayo imepigwa vibaya na Namibia katika safari sita imefanya nchini Namibia, itatoka jijini Nairobi mnamo Jumatano asubuhi kuelekea jijini Windhoek kutafuta kufuta rekodi hiyo duni.

Bingwa wa Afrika ataingia Kombe la Dunia litakaloandaliwa nchini Japan mwaka 2019. Atakutanishwa na New Zealand, Afrika Kusini na Italia pamoja na mshindi wa mchujo wa mwisho, ambaye pia anaweza kuwa Kenya ama Namibia.

Mchujo wa mwisho, ambao utafanyika nchini Ufaransa mwezi Novemba mwaka 2018, utaleta pamoja Canada, Hong Kong, Ujerumani na timu itakayomaliza Kombe la Afrika mwaka 2018 katika nafasi ya pili.

Namibia inaongoza mashindano ya Afrika kwa alama 20. Kenya ni ya pili kwa alama 17. Uganda, Tunisia, Zimbabwe na Morocco zinashikilia nafasi nne zinazofuata kwa alama tisa, nne, tatu na tatu, mtawalia.

Mmoja kati ya Tunisia, Morocco na Zimbabwe atapoteza nafasi katika ligi hii ya daraja ya juu ya Afrika almaarufu Gold Cup. Nafasi yake itajazwa na mshindi wa daraja ya pili almaarufu Silver Cup kati ya Zambia na Algeria.

Kikosi cha Simbas kitakachomenyana na Namibia:

Isaac Adimo (Kenya Harlequin), Martin Owilah (KCB), Samson Onsomu (Impala Saracens), William Ambaka (Kenya Harlequin), Darwin Mukidza (KCB), Tony Onyango (Homeboyz), Peter Kilonzo (KCB), Oliver Mang’eni (KCB), Jacob Ojee (KCB), Mohamed Omollo (Homeboyz), Felix Ayange (Kabras Sugar), Dalmus Chituyi (Homeboyz), Curtis Lilako (KCB), Peter Karia (KCB), Elkeans Musonye (Strathmore Leos), George Nyambua (Kabras Sugar), Andrew Chogo (Kabras Sugar), Malcolm Onsando (Kenya Harlequin), Patrick Ouko (Homeboyz), Moses Amusala (KCB), Joseph Odero (Kabras Sugar), Colman Were (Kabras Sugar) na Davis Chenge (KCB, nahodha).

Msiidharau Tunisia, meneja wa Simbas aonya

Na GEOFFREY ANENE

SAA chache baada ya Tunisia kutua jijini Nairobi, Meneja wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya wanaume ameonya vijana wake dhidi ya kudharau Waarabu hao watakapokutana uwanjani RFUEA hapo Agosti 11, 2018.

Katika mahojiano ya simu jijini Nairobi mnamo Agosti 6, Wangila Simiyu amesema Kenya Simbas haifai kuchukulia mechi hiyo yake ya nne ya Kombe la Afrika kuwa “mswaki.”

“Licha ya kupondwa na Namibia (118-0) na Uganda (67-12), Tunisia haifai kudharauliwa hata kidogo. Ilibabaisha Zimbabwe na hata kuwachapa (18-14). Itakumbukwa kwamba Zimbabwe ilitusumbua sana ilipozuru Nairobi. Tunastahili kuheshimu Tunisia na kuchukulia mechi hiyo kwa uzito unaofaa,” Wangila amesema.

Kenya itaanza mchuano huu na asilimia kubwa ya kuushinda. Ina rekodi nzuri katika ardhi yake dhidi ya Tunisia. Julai 8 mwaka 2017 katika kombe hili jijini Nairobi.

Simbas imerarua Tunisia mara sita jijini Nairobi. Iliwika 100-10 Julai 8 mwaka 2017. Kabla ya hapo, ilikuwa imecharaza Waarabu hawa 46-15 mwaka 2015, ikawalima 31-24 mwaka 2012, ikawachapa 16-7 mwaka 2011, ikawakanyaga 25-21 Juni 10 mwaka 2006 na kuwalaza 37-15 Mei 21 mwaka 2005.

Ushindi mbili ambazo Tunisia imepata dhidi ya Kenya tangu mwaka 2000 zimekuwa nchini Tunisia. Ilizaba Kenya 44-15 Agosti 2 mwaka 2008 jijini Tunis na kuilima tena 31-12 Septemba 16 mwaka 2006 jijini humo.

Katika kipute cha mwaka 2018, ambacho pia kinatumika kama mchujo wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2019, Namibia inaongoza kwa alama 20.

Kenya ni ya pili kwa alama 12. Uganda, Tunisia na Zimbabwe zinafuatana katika nafasi za tatu, nne na tano kwa alama tano, nne na tatu, mtawalia. Morocco inavuta mkia kwa alama tatu.

Inatofautiana na Zimbabwe kwa ubora wa magoli. Namibia na Zimbabwe zimesakata mechi nne kila mmoja. Kenya, Uganda, Tunisia na Morocco zimecheza mechi tatu kila mmoja.

Matokeo na ratiba:

Juni 16

Namibia 55-6 Uganda

Zimbabwe 23-23 Morocco

Juni 23

Namibia 118-0 Tunisia

Morocco 24-28 Kenya

Juni 30

Kenya 45-36 Zimbabwe

Morocco 7-63 Namibia

Julai 7

Kenya 38-22 Uganda

Tunisia 18-14 Zimbabwe

Agosti 4

Uganda 67-12 Tunisia

Zimbabwe 28-58 Namibia

Agosti 11

Uganda na Morocco

Kenya na Tunisia

Agosti 18

Tunisia na Morocco

Namibia na Kenya

Uganda na Zimbabwe.

Simbas kujaribu kupiga Cranes nyumbani

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Kenya almaarufu Simbas, itaondoka nchini Alhamisi alasiri kuelekea Uganda kwa mechi ya mkondo wa kwanza ya shindano la Elgon Cup.

Kocha kutoka New Zealand,  Ian Snook amejumuisha wachezaji watano wapya kikosini. Wachezaji hao ni Patrick Ouko kutoka klabu ya Homeboyz, Joseph Odero (Kabras Sugar), Malcom Onsando (Kenya Harlequins), Andrew Chogo (Kabras Sugar) na Xavier Kipng’etich (Impala Saracens).

Katika hafla ya kuzindua kikosi cha wachezaji 23 watakaopeperusha bendera ya Kenya uwanjani Legends jijini Kampala hapo Jumamosi, Snook amesema Simbas imeimarika, ingawa akakiri kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanywa kabla ya timu kuwa fiti kabisa.

Simbas imekuwa mazoezini wiki sita pamoja na kufanya mazoezi na wanajeshi kutoka Uingereza (British Army) mjini Nanyuki. “Hii ndiyo timu nzuri tuko nayo wakati huu nchini,” Snook amesema na kufichua kwamba Kenya itakosa huduma za nahodha Wilson K’Opondo na Joshua Chisanga.

“K’Opondo anauguza jeraha naye Chisanga bado ana majukumu na klabu yake nchini Poland. Watakosa ziara ya Uganda, lakini tunawatarajia kabla ya kambi ya mazoezi nchini Afrika Kusini,” alifichua.

Meneja wa Simbas, Wangila Simiyu alisema timu ya Kenya itatafuta kupiga Uganda kwao, ingawa akakiri Cranes si wachache katika ardhi yao. Aliongeza kwamba makocha wapya kutoka New Zealand wameleta mabadiliko makubwa kikosini hasa katika idara ya mazoezi na anaamini mbinu zao mpya zitasaidia Kenya kupambana na wapinzani.

Aidha, Mkurugenzi wa timu za taifa za raga nchini, Raymond Olendo amesema Simbas pamoja na timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanawake Kenya Lionesses zimepokea tiketi za ndege kutoka kwa serikali kusafiri nchini Uganda na Botswana, mtawalia.

Hata hivyo, Olendo alikiri Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) bado linasubiri fedha za kufanikisha mahitaji ya timu hizo kama chakula na malazi. Simbas inahitaji Sh2 milioni nchini Uganda na Sh8 milioni katika kambi ya mazoezi nchini Afrika Kusini.

Inajiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia nchini Japan mwaka 2019. Kombe la Afrika la Dhahabu (Gold Cup) mwaka 2018 litatumika kuchagua timu itakayowakilisha Afrika nchini Japan.

Gold Cup itakutanisha Kenya, Morocco, Uganda, Tunisia, Zimbabwe na mabingwa watetezi Namibia. Lionesses itakuwa jijini Gaborone nchini Botswana wikendi hii ya Mei 25-26 kuwania ubingwa wa Afrika.

Kikosi cha Kenya Simbas:

Wachezaji

Patrick Ouko*(Homeboyz), Philip Ikambili (Homeboyz), Joseph Odero* (Kabras), Malcolm Onsando* (Kenya Harlequins), Oliver Mang’eni (KCB), George Nyambua (Kabras), Elkeans Musonye (Strathmore), Tony Onyango (Homeboyz), Martin Owilah (KCB), Samson Onsomu (Impala), Isaac Adimo (Kenya Harlequins), Leo Seje (Impala), Peter Kilonzo (KCB), Darwin Mukidza, Jacob Ojee (KCB), Peter Karia (KCB), Vincent Mose (Impala), Curtis Lilako (KCB), Andrew Chogo* (Kabras), Davis Chenge (KCB), Xavier Kipng’etich Bett* (Impala), Biko Adema (Nondies) na Oscar Simiyu (KCB).

*Mbioni kuchezea Kenya kwa mara ya kwanza kabisa

Benchi la kiufundi:

Ian Snook (Kocha Mkuu), Murray Roulston (Kocha msaidizi), Dominique Habimana (Kocha wa safu ya mbele), Richard Ochieng (kocha wa mazoezi ya viungo), Christopher Makachia (daktari wa timu), Simiyu Wangila (meneja wa timu)

Ratiba ya Simbas mwaka 2018:

Mei 26 – Uganda vs. Kenya (Elgon Cup, Kampala)

Juni 23 – Morocco vs. Kenya (Africa Gold Cup, Casablanca)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (Africa Gold Cup, Nairobi)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (Africa Gold Cup, Nairobi)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (Africa Gold Cup, Nairobi)

Agosti 18 – Namibia vs. Kenya (Africa Gold Cup, Windhoek)

Hatua kwa hatua, Simbas wajinyanyua viwango vya raga

Na GEOFFREY ANENE

KWA wiki ya pili mfululizo, Kenya imeimarika katika viwango bora vya raga ya wachezaji 15 kila upande duniani bila kuteremka uwanjani.

Katika viwango vipya ambavyo Shirikisho la Raga duniani (World Rugby) imetangaza Jumatatu, Simbas, timu ya Kenya inavyofahamika kwa jina la utani, imeruka juu nafasi moja hadi nambari 29.

Vijana wa kocha Ian Snook waliimarika kutoka nafasi ya 31 hadi 30 hapo Mei 7 baada ya Chile kulazwa 28-12 na Brazil katika Kombe la Amerika Kusini mnamo Mei 5. Wameimarika tena kutokana na Korea Kusini kupepetwa 30-21 na Hong Kong katika Kombe la Bara Asia hapo Mei 12.

Simbas haijacheza mechi ya kimataifa tangu ziara yake ya Hong Kong mwezi Novemba mwaka 2017. Itafungua mwaka 2018 dhidi ya majirani na mahasimu wa jadi Uganda katika Kombe la Elgon hapo Mei 26 jijini Kampala. Vijana wa Snook wanatarajiwa kuingia kambini Mei 18 katika eneo la Nanyuki.

New Zealand, Jamhuri ya Ireland, Uingereza, Australia, Scotland, Afrika Kusini, Wales, Ufaransa, Argentina na Fiji zinashikilia katika nafasi 10 za kwanza duniani, mtawalia. Zimesalia katika nafasi hizo.

Mabingwa wa Afrika, Namibia wamesalia katika nafasi ya 24 duniani. Namibia inashikilia nafasi ya kwanza Afrika baada ya Afrika Kusini, ambayo haishiriki Kombe la Dhahabu la Afrika (Gold Cup).

Kenya inafuata Namibia katika viwango bora vya Afrika, huku Uganda ikisalia katika nafasi ya 34 duniani na nambari tatu Afrika. Morocco imetupwa chini nafasi moja hadi nambari 40 duniani baada ya Paraguay kuzima Colombia 28-26 katika Kombe la Amerika Kusini.

Tunisia imenufaika na Colombia kupoteza. Imepaa nafasi moja hadi nambari 42 duniani. Zimbabwe inasalia katika nafasi ya 44 duniani. Namibia, Kenya, Uganda, Morocco, Tunisia na Zimbabwe zitawania ubingwa wa Kombe la Dhahabu la Afrika mwaka 2018 ambalo litatumika kuchagua mwakilishi wa Afrika katika Kombe la Dunia mwaka 2019.

Ratiba ya Simbas mwaka 2018:

Mei 26 – Uganda vs. Kenya (Elgon Cup, Kampala)

Juni 23 – Morocco vs. Kenya (Africa Gold Cup, Casablanca)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (Africa Gold Cup, Nairobi)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (Africa Gold Cup, Nairobi)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (Africa Gold Cup, Nairobi)

Agosti 18 – Namibia vs. Kenya (Africa Gold Cup, Windhoek)

Kikosi cha Simbas: Patrick Ouko (Homeboyz), Oscar Simiyu (KCB), Moses Amusala (KCB), Joseph Odero (Kabras), Nelson Nyandat (KCB), Curtis Lilako (KCB), Peter Karia, (KCB), Phillip Ikambilli, (Homeboyz), Coleman Were (Kabras), Oliver Mangeni (KCB),Malcolm Onsando (Quins),Eric Kerre (Impala),Wilson Kopondo, (Quins),Andrew Chogo (Kabras),George Nyambua (Kabras), Dalmus Chituyi (Homeboyz), Peter Misango (Quins), Elkeans Musonye (Strathmore), Martin Owila (KCB), Davis Chenge (KCB),  Samson Onsomu (Impala), Xavier Kipng’etich (Impala), Mohammed Omollo (Homeboyz),Isaac Adimo (Quins), Biko Adema (Nondies), Leo Seje (Impala), Maxwell Kangeri (Homeboyz), Peter Kilonzo (KCB), Zedden Marrow (Homeboyz), Tony Onyango (Homeboyz),Felix Ayange (Kabras), Jacob Ojee (KCB), Darwin Mukidza (KCB), Edmund Anya (Strathmore),Vincent Mose (Impala).

Simbas washuka viwango vya raga duniani

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Simbas imetupwa nje ya mataifa 30-bora kwenye viwango bora vya raga ya wachezaji 15 kila upande duniani Jumatatu.

Katika viwango vipya vilivyotangazwa na Shirikisho la Raga duniani (World Rugby), Kenya imeteremka nafasi moja na sasa inashikilia nambari 31 kwa alama 54.24.

Imerukwa na Korea Kusini, ambayo ilititiga wenyeji wa Kombe la Bara Asia Malaysia 35-10 jijini Kuala Lumpur hapo Aprili 28, 2018 na kupaa nafasi moja.

Kenya inasalia katika nafasi ya tatu barani Afrika nyuma ya Afrika Kusini, ambayo imesalia nambari sita duniani nayo Namibia imekwamilia nafasi ya 24 duniani.

Uganda ni ya nne barani Afrika na 34 duniani. Morocco, Tunisia na Zimbabwe zinafuatana katika nafasi za tano, sita na saba barani Afrika, mtawalia. Zinashikilia nafasi za 38, 43 na 44, duniani, mtawalia.

Kenya, Namibia, Morocco, Tunisia, Uganda na Zimbabwe zitawania taji la Kombe la Afrika la Dhahabu kati ya Juni 16 na Agosti 18 mwaka 2018.

Simbas, ambayo ina kocha mpya Ian Snook kutoka New Zealand, itaanza kampeni yake dhidi ya Morocco jijini Casablanca mnamo Juni 23.

Itakabana koo na Zimbabwe, Uganda na Tunisia mnamo Juni 30, Julai 7 na Agosti 11 jijini Nairobi kabla ya kukamilisha kampeni yake dhidi ya mabingwa watetezi Namibia jijini Windhoek hapo Agosti 18.

Kocha mpya wa Simbas atambulishwa

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA mpya wa timu yake ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas, Ian Snook, ametambulishwa rasmi kwa umma jijini Nairobi, Alhamisi.

Raia wa New Zealand, Snook ameajiriwa kwa kandarasi ya mwaka mmoja. Atafanya kazi na raia mwenzake wa New Zealand, Murray Roulston pamoja na Wakenya Wangila Simiyu, Charles Ngovi, Christopher Makachia, Richard Ochieng’ na Dominique Habimana.

Snook na Roulston waliwasili nchini Kenya hapo Aprili 9. Snook anajaza nafasi ya raia wa Afrika Kusini, Jerome Paarwater, ambaye Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilimtema Desemba mwaka 2017.

Taarifa kutoka KRU zinasema kwamba majukumu makubwa ya raia hao wa New Zealand ni kuongoza Kenya katika kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2019.

“Wana ujuzi wa zaidi ya miaka 50 kati yao katika kazi ya ukufunzi katika viwango mbalimbali kutoka mataifa yanayokuwa na pamoja na timu ya taifa ya New Zealand,” KRU imesema.

Snook na Roulston watashughulikia idara za mashambulizi na ulinzi, mtawalia. Hata hivyo, Snook ndiye kocha mkuu.

Ratiba ya Simbas ya Kombe la Afrika (2018):

Juni 23 – Morocco vs. Kenya (ugenini)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (nyumbani)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (nyumbani)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (nyumbani)

Agosti 18 – Namibia vs. Kenya (ugenini)

KRU yatangaza kikosi cha wachezaji 35 wa Simbas 2018

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limetangaza kikosi cha wachezaji 35 kitakachowakilisha Kenya kimataifa kwenye raga ya wachezaji 15 kila upande mwaka 2018 likiwemo Kombe la Afrika.

Kuna wachezaji saba wapya kabisa kikosini ambao ni Coleman Were, Patrick Ouko, Peter Waitere, Michael Wanjala, Mohamed Omolo, Johnstone Mung’au na Aggrey Kitoi. Wachezaji Joseph Odero na Levy Amunga wamerejea katika kikosi cha mazoezi.

Amunga, ambaye alishiriki mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Victoria Falls nchini Zimbabwe mnamo Machi 24-25, alikuwa muhimu katika kampeni ya Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kumaliza Ligi Kuu ya msimu 2017-2018 katika nafasi ya 10. Kitoi ndiye mchezaji wa pekee kikosini ambaye hayuko kwenye Ligi Kuu.

Alishiriki Ligi Kuu ya msimu 2017-2018, lakini timu yake ya Kisii iliteremshwa daraja baada ya kumaliza ndani ya mduara hatari wa kutemwa.

Kikosi hiki kitanolewa na kocha mpya kutoka New Zealand, Ian Snook, ambaye anatarajiwa kuingia Kenya wakati wowote mwezi wa Aprili. Snook alichukua nafasi ya raia wa Afrika Kusini, Jerome Paarwater, ambaye alitimuliwa Desemba mwaka 2017.

Kombe la Afrika litatumika kama shindano la kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2019.

KIKOSI CHA KENYA SIMBAS

Washambuliaji:

KCB – Moses Amusala, Oscar Simiyu, Curtis Lilako, Peter Karia, Oliver Mang’eni, Davis Chenge, Martin Owila, Peter Waitere

Kabras Sugar – Joseph Odero, Coleman Were, George Nyambua

Impala Saracens – Dennis Karani, Eric Kerre

Homeboyz – Patrick Ouko, Philip Ikambili, Steve Otieno

Kenya Harlequins – Wilson K’Opondo (nahodha)

Decazevillois (Ufaransa) – Simon Muniafu

Strathmore Leos – Elkeans Musonye

Mabeki:

Impala Saracens – Samson Onsomu, Nato Simiyu, Leo Seje, Vincent Mose

KCB – Michael Wanjala, Jacob Ojee, Peter Kilonzo, Darwin Mukidza

Homeboyz – Mohamed Omollo, Tony Onyango

Blak Blad – Levy Amunga

Nondescripts – Biko Adema

Kenya Harlequins – Dennis Muhanji

Mwamba – Brad Owako

Kabras Sugar – Johnstone Mung’au

Kisii – Aggrey Kitoi

Ratiba ya Simbas ya Kombe la Afrika (2018):

Juni 23 – Morocco vs. Kenya (ugenini)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (nyumbani)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (nyumbani)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (nyumbani)

Agosti 18 – Namibia vs. Kenya (ugenini)

Simbas hatimaye wapata kocha mpya

Kocha mpya wa Simbas Ian Snook kutoka New Zealand. Picha/ Hisani

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas hatimaye imepata kocha mpya Ian Snook kutoka New Zealand, wiki 15 baada ya kutengana na raia wa Afrika Kusini Jerome Paarwater.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilitangaza Machi 19 kwamba Snook amekubali kuinoa Simbas kama kocha mkuu na kuongeza kwamba atawasili nchini wiki ya kwanza ya mwezi ujao wa Aprili.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, KRU imemsifu Snook ikisema “Analeta ujuzi wa miaka mingi kikosini baada ya kufanya kazi ya ukufunzi na kupeana ushauri nchini New Zealand, Australia, Uingereza, Jamhuri ya Ireland, Laos, Japan, Croatia, Italia na Afrika Kusini.”

Snook, ambaye amekuwa kocha kwa zaidi ya miaka 30, atasaidiwa na raia mwenzake wa New Zealand Murray Roulston, ambaye pia amefanya kazi ya kocha na kutoa ushauri kwa timu ya Highlanders na mataifa ya New Zealand, Japan, Trinidad & Tobago na Romania.

“Wawili hawa wakati huu wanashirikiana na benchi la kiufundi la Kenya linalojumuisha Dominique Habimana, Charles Ngovi, Richard Ochieng, Chris Makachia na Simiyu Wangila kuunda ratiba ya mazoezi. Watawasili mapema Aprili,” KRU ilitangaza.

Shughuli ya kutafuta mrithi wa Paarwater imekuwa ikiendelea kwa muda na hata kuzua wasiwasi kikosini baada ya kuonekana kuchukua muda mrefu sana.

Wakati huo huo, KRU imefichua kwamba inalenga kutafutia Simbas mechi kadhaa za kujipima nguvu dhidi ya timu kutoka Bara Ulaya kabla ya Kombe la Afrika la mwaka 2018 litakalotumika kuchagua mwakilishi wa Afrika katika Kombe la Dunia mwaka 2019.

Ratiba ya Simbas ya Kombe la Afrika (2018):

Juni 23 – Kenya vs. Morocco (ugenini)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (nyumbani)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (nyumbani)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (nyumbani)

Agosti 18 – Kenya vs. Namibia (ugenini)