Sofapaka yamtimua Waliaula baada ya Ssimbwa kujiuzulu

Na CHRIS ADUNGO

SIKU moja baada ya kocha mkuu Sam Ssimbwa kujiuzulu, Sofapaka Jumanne imempiga kalamu meneja wa timu hiyo Willis Waliaula.

Afisa wa klabu hiyo aliyesema na Goal.com alithibitisha taarifa hizo akisema: “Ndiyo, Waliaula si meneja wetu tena. Nafasi yake kwa sasa imetwaliwa na Hillary Echesa.”

“Ni uamuzi ambao ulifikiwa na usimamizi wa timu ili kuleta amani na maelewano kwa timu. Kumekuwa na  migogoro baina ya benchi la kiufundi na wachezaji.”

“John Baraza atasalia kuwa kocha wetu mkuu kwa sasa, lakini mipango ipo kumleta kocha mwenye uzoefu na tajriba katika soka.”

Batoto ba Mungu kwa sasa wako katika nafasi ya nne ligini wakiwa na pointi 16.

John Baraza sasa kuwaongoza ‘Batoto Ba Mungu’

Na CHRIS ADUNGO

MCHEZAJI wa zamani wa Harambee Stars John Baraza amepata nafasi ya pili kuongoza kikosi cha Sofapaka baaada ya kocha Sam Ssimbwa kujiuzulu. Taarifa kutoka kwa klabu hiyo imethinitiha haya.

Taarifa hiyo inasema kuwa Baraza, ambaye alipata ufanisi akiichezea ‘Batoto ba Mungu’, atakuwa kocha mkuu wa muda hadi pale klabu hiyo itapata kocha wa kudumu katikati ya msimu.

Baraza, ambaye alishinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2009, alichangia pakubwa timu hiyo kuponea 2016 wakati ilipitia wakati mgumu ligini na kupewa nafasi ya naibu kocha mkuu baada ya SSimbwa kuwasili Januari 2017 kutoka Uganda.

“Sofapaka ingependa kutangaza kuwa kocha kutoka Uganda Sam Ssimbwa alijiuzulu akilalamikia matokeo duni ya timu na kulemewa kuiletea ushindi.

“Nafasi ya Ssimbwa itachukuliwa na John Baraza kwa muda, hadi katikati ya msimu ambapo uongozi wa klabu utatathmini matokeo ya timu na kikosi cha ufundi. Baraza amekuwa naibu kocha wa timu hii,” ataarifa hiyo ilisema.

 

 

Ssimbwa ajiuzulu akilalamikia wachezaji kumgomea

Na CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI wa Batoto Ba Mungu, Sam Ssimbwa amejiuzulu nafasi ya kocha mkuu Jumapili.

Kocha huyo mzaliwa wa Uganda aliamua kugura kazi hiyo kufuatia kichapo cha 2-1 mikononi mwa Thika United ambayo imedhalilishwa mno katika Ligi Kuu ya Kenya.

Mwenyekiti wa Sofapaka Elly Kalekwa amethibitisha habari hizo, akisema Ssimbwa aliomba kujiondoa akilalamikia tabia ya wachezaji kutojituma kwa mechi ili wamuaibishe.

 

“Amejiuzulu. Amewapa wachezaji buriani ya kuonana na tunaheshimu hilo. Anadai kuwa wachezaji wanamgomea, hawataki kusikiza anachosema,” akasema.

“Hakuna haja kwake kuandika barua ya kujiuzulu, tumekubali uamuzi wake.”

“Hakuna uhusiano mbaya kati yetu naye, jinsi amesema mwenyewe, atasalia kuwa mwandani na kututakia mema kwa mechi,|” akaongeza.

 

Kufikia sasa, Sofapaka imeshinda mechi tano, ikapata sare moja na kulimwa mechi tatu.