TAHARIRI: Shule zisiwafukuze wanafunzi kiholela

KITENGO CHA UHARIRI

WANAFUNZI wanapofungua shule hapo Jumanne, wazazi wengi wanakabiliwa na mzigo mzito wa kulipa karo.

Mzigo mzito hasa ikizingatiwa kuwa muhula wa kwanza ulikamilika siku 10 tu zilizopita.

Kutokana na ufupi wa muhula huo, kuna uwezekano mkubwa kuwa wazazi wengi hawakumaliza kulipa karo ya muhula huo, au wengine waliomaliza walifanya hivyo katika siku za mwisho mwisho za muhula.

Kutokana na hali hiyo, ni muhimu serikali kupitia kwa Wizara ya Elimu iingilie kati kwa kuzikataza shule na walimu wakuu kuwafukuza wanafunzi mwanzoni mwa muhula.

Ni kweli kuwa kila mzazi au mlezi anafaa kujitahidi kulipa karo ya shule.

Hata hivyo, ni bayana kuwa wapo baadhi ya wazazi au walezi ambao huenda wakalemewa kukamilisha ada hiyo mapema jinsi inavyohitajika hasa kutokana na makali ya janga la Covid-19.

Jinsi ya kuwasaidia wazazi hao ni kuwapa muda wa kutosha kukamilisha malipo hayo bila kuwafukuza watoto wao wasije wakakosa masomo.

Hiyo itasaidia pande zote kunufaika kwani shule zitapata pesa kuendeshea shughuli za masomo nao wanafunzi watasoma bila kukosa kipindi chochote.

Ili kufanikisha hilo, serikali inahitajika kutoa mwelekeo kwa shule kuwavumilia wazazi watakaoshindwa kuwalipia watoto wao ada za shule hasa kwa kuzingatia hali ngumu ya uchumi iliyoko sasa.

Kwa upande mwingine, wazazi nao wahimizwe kutozembea katika utafutaji wa pesa za kulipa karo.

Kauli hii inahusu hasa shule za upili, vyuo na shule zote za kibinafsi zinazohitaji malipo ya karo.

Inapozingatiwa pia kuwa muhula umepungua kwa zaidi ya mwezi mmoja, zipo baadhi ya ada kama vile chakula cha wanafunzi na michezo zinazohitajika kupunguzwa ili kuwapa wazazi nafuu ya mzigo huo.

Mbali na masuala ya karo, itakuwa muhimu shule na wadau wakuu hasa Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa wanajitahidi kufundisha sehemu kubwa ya silabasi.

Inafahamika kuwa uwezo wa binadamu kunasa mambo mengi akilini kwa muda mfupi ni mdogo, lakini ipo haja ya kutumia muda huo mfupi kuhakikisha wanafunzi wananasa mambo mengi iwezekanavyo ya kielimu.

Huenda pia ikawa muhimu kupunguza majaribio ya mitihani ili muda huo uweze kutumiwa kufundisha kwa dhamira ya kukamilisha silabasi ambayo kwa kawaida inafaa kumalizika katika muda wa miezi tisa badala ya sita ya sasa, kwa mwaka.

TAHARIRI: Hakuna raha tena kushabikia Stars

KITENGO CHA UHARIRI

KWA mara nyingine timu ya taifa Harambee Stars ililambishwa sakafu katika mechi ya kimataifa, raundi hii kichapo kikitolewa na Mali nchini Morocco.

Kipa Ian Otieno alitolewa kijasho kuanzia dakika ya nane Mali walipofunga bao la kwanza.

Mtindo ukawa ni kutoa ndani bao baada ya kila dakika 10 katika kipindi cha kwanza.

Kufikia mapumziko tulikuwa tumeoshwa mabao manne.

Mali walipunguza makali yao kipindi cha pili, lakini hata kwa hilo hatukufanikiwa kufunga bao la kufutia machozi.

Kufuatia kichapo hicho, Kenya sasa imeshuka hadi nafasi ya tatu kundini tukiwa na alama mbili pekee.

Stars watawakaribisha tena wapinzani wao kwa mechi ya marudiano siku ya Jumapili kuanzia saa kumi jioni.

Masaibu ya Stars yanatarajiwa kuongezeka zaidi Jumapili watakapowakaribisha tena wapinzani hao kwa mechi ya marudiano, ugani Nyayo kuanzia saa kumi jioni.

Bado vichapo vingine vinanukia mikononi mwa wenzetu wa Kundi E – Uganda, ambao siku hizi tumekuwa mboga kwao hamna tena ushindani wa zamani tuliokuwa tukiwapa.

Kwa mwelekeo huu, hata Rwanda – wanaoshikilia nafasi ya mwisho kundini – watatulambisha sakafu.

Kikosi cha akina dada wasiozidi umri wa miaka 20 jana Ijumaa pia kilibanduliwa nje ya michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022 nchini Costa Rica.

Hii inafuatia kichapo cha jumla cha mabao 10-3 dhidi ya Uganda.

Ni masaibu ya kusikitisha kwa wapenzi wa soka nchini, na yameletwa hususan na masihara ya Rais wa Shirikisho la soka Nchini (FKF), Nick Mwendwa.

Udikteta, ubadhirifu wa fedha rasilimali, ukosefu wa mikakati ya kukuza soka mashinani na usimamizi duni wa timu ya taifa umekuwa wimbo tangu Mwendwa achukue hatamu za kusimamia soka nchini.

Hata kwa hayo, kinara huyu haoni cha kumfanya ajiondoe kwa hiari.

Mashabiki mitandaoni tayari wameanza kujikusanya pamoja na wapenzi wengine wa soka nchini, kumtia presha Mwendwa aondoke.

Itakuwa vyema akikunja jamvi mwenyewe la sivyo shinikizo zitamuondoa.

TAHARIRI: Vijana wakatae hila, hadaa za wanasiasa

KITENGO CHA UHARIRI

UMESALIA karibu nusu mwaka hivi tuingie katika uchaguzi mkuu wa 2022, nalo joto la siasa linaendelea kusambaa kama moto katika kichaka kikavu.

Wanasiasa wanajipanga kuwamwagia vijana ‘sera zao tamu’, maneno ya mvuto na pesa za kuwashawishi kuwapigia kura.

Maazimio yao waliyoshindwa kuyatimiza na ile miradi bandia waliyowaanzishia vijana, wanarudi tena kuwalaghai ili wawape nafasi nyingine ya kuwatimizia malengo hayo.

Hii yote ni kero ya kura. Waliwashawishi vijana vivyo hivyo miaka mitano iliyopita, wakawaamini na kuwapa kura zao.

Walipopata uongozi wakawaona kinyaa. Wakawatoroka na kujificha wakiponda raha na familia zao.

Wakawatelekeza wale waliowapa vyeo.

Sera zile zile walizowaongopea mwanzoni, wakashindwa kuwatimizia matakwa yao, hivi wanarudi tena kuwahadaa kwazo.

Tunapaswa kutambua kwamba asilimia kubwa ya wapigakura nchini ni vijana. Mataifa mengi yakitaka kutekeleza ajenda zao kwanza lazima waulize, ‘kwani wao wanasemaje?’

Vijana hapa ndio wanaorejelewa kwani ndio nguvukazi ya jamii na nchi nzima kama vijana walengwa wakuu wa wanasiasa tuwe na msimamo thabiti dhidi yao.

Waliwaahidi ajira, hawakuziona. Wakaajiri wafanyakazi hewa na vitita vya pesa kujilimbikizia.

Hivi sasa mirengo mbali mbali ya kisiasa inaweka mikakati jinsi itakavyowatumia vijana ili kuwapenyeza kwenye debe.

Siku zote wanasiasa hawa huwashawishi vijana kufanya mambo fulani kama kuzua ghasia na rabsha kwa kuwaahidi malipo manono ama nafasi za ajira baadaye.

Lakini huwa ni uongo mtupu na wanawatumia vijana tu kwa maslahi yao kwa kuwa wana nguvu na ushawishi mkubwa katika jamii. Huu ndio wakati wa vijana kuungana na kupinga udhalimu huo unaofanywa na wanasiasa kila wakati wa kupiga kura.

Kura isiwatie tamaa ya kula. Wanasiasa nia yao ni kuwagonganisha vijana na kuwaharibia uhusiano mwema baina yao, wapigane na kusababisha vurugu nchini ilhali wanasiasa wapo kwenye makasri yao wanawatazama wakisagana na kuchinjana hovyo.

Ni wakati wa vijana kukengeuka na kupinga hadaa za wanasiasa. Ni jukumu la vijana kulilinda taifa lao dhidi ya wanasiasa madhalimu na wachochezi.

TAHARIRI: Serikali iwakinge wananchi maskini

KITENGO CHA UHARIRI

BAADA ya vilio vya muda mrefu kuhusu gharama kubwa ya mafuta na maisha kwa jumla, hatimaye serikali inaonyesha dalili za kuwapunguzia raia wake, hasa maskini mzigo huo.

Juma lijalo bunge litajadili kuhusu viwango vya ushuru kwa dhamira ya kuvirejesha chini kwa angaa nusu

Kwa sasa ushuru wa VAT pekee kwa mafuta na gesi ni asilimia 16 na ndiyo sababu ya kupaa kwa bei za bidhaa hizo muhimu ambazo miaka kadhaa iliyopita ushuru wake ulikuwa chini mno.

Nyongeza ya bei za mafuta na gesi, iliyotokana na ushuru huo wa asilimia 16, inatishia kuwasukuma raia katika umaskini zaidi hasa inapozingatiwa kuwa tayari wamefinywa na makali ya janga la corona.

Kwa sasa, mtungi mdogo wa gesi (kilo 6) uliokuwa ukiuzwa karibu Sh1,000 hadi kufikia Mei mwaka huu sasa unauzwa kwa Sh1,400 huku mkubwa (kilo 13), uliokuwa ukiuzwa Sh2,100, sasa ukifika kati ya Sh2,500 na Sh2,900.

Mbali na VAT, kwa bidhaa za kimsingi, iliyokuwa imeongezwa kuanzia Julai 1, kupaa kwa bei za bidhaa hizo hasa mwezi huu kunatokana na hatua ya serikali ya kubuni ushuru wa ziada kwa bidhaa za kimsingi ikiwemo maziwa, sukari, mkate na nyinginezo mnamo Oktoba 1.

Japo bei ya mtungi wa gesi ilikuwa tayari imepanda kabla ya Oktoba 1, kuanzia juma hili, bei hiyo imeongezeka tena kwa angaa Sh200 kwa mtungimdogo na Sh400 kwa mtungi mkubwa.

Naam wapo watakaosema kuwa gesi ni ya watu wanaojiweza, lakini ukweli ni la; hilo si kweli.

Gesi siku hizi inatumika na watu wa matabaka yote hata mashambani ambako kawi iliyozoeleka kwa mapishi ni kuni.

Hiyo ina maana kuwa kuongezeka kwa bei ya bidhaa hizo kutaathiri vibaya hata watu wa tabaka la chini.

Kadhalika, kuongezeka kwa bei ya mafuta kunaathiri Wakenya wote maadamu shughuli nyingi za kiuchumi kwa sasa zinaendeshwa na mafuta; viwanda, magari ya uchukuzi na kadhalika.

Shughuli hizo humhusu kila Mkenya.

Kwa hayo yote, ushauri wetu ni kuwa bunge linapoketi juma lijalo kujadili bei za mafuta, vivyo hivyo, pawepo mjadala wa kupunguza bei za bidhaa nyingine muhimu hivi karibuni kabla ya madhara kuanza kushuhudiwa kote nchini.

Ni heri serikali ikose kiasi fulani cha ushuru lakini mwananchi aweze kuishi kwa kumudu riziki.

TAHARIRI: Ukora katika kusajili wapigakura uzuiwe

KITENGO CHA UHARIRI

SHUGHULI ya usajili wa wapigakura kitaifa inaingia siku ya tatu leo huku juhudi nyingi zikianza kutekelezwa kuhakikisha wananchi wengi hasa vijana wanasajiliwa.

Ni habari za kufurahisha serikali kutangaza kuwa inalenga kuwapa angaa wanafunzi 20,000 wa shule za upili vitambulisho ili waweze kujisajili.

Hatua hiyo itasaidia Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufikisha au kukaribia kusudi lake la kusajili angaa wapigakura milioni saba wapya katika mikumbo miwili ijayo ya usajili.

Hata hivyo, pamezuka malalamiko kuwa wanasiasa wenye uwezo wameanza ukora wa kuhamisha wapigakura kutoka pale walipojisajili hadi kwingine ili wawapigie kura wanasiasa hao katika uchaguzi ujao huku wengine wakiwashiwishi wakazi wa maeneo ya mbali kujisajili katika maeneo wasiyoishi kwa kusudi hilo hilo la kuwapigia kura mwaka ujao 2022.

Sharti Serikali kupitia kwa wizara ya Usalama wa Ndani pamoja na wadau wengine husika wazuie mbinu za aina hiyo.

Mbali na kikwazo hicho, ni sharti usajili huo uendeshwe kwa njia itakayohakikisha, lengo la IEBC la kusajili mamilioni hayo ya wapigakura mwezi huu Oktoba na hapo Januari limetimia.

Je, idadi hiyo itafikiwaje bila kuwawezesha vijana ambao ndio wengi wanaolengwa katika usajili huu?

Zaidi ya asilimia 90 ya wanaotazamiwa kusajiliwa ni vijana. Changamoto kuu ambayo imejitokeza kuhusu kufaulisha azimio la kusajili angaa wapigakura hao wanaolengwa ni ukosefu wa vitambulisho.

Hii ni kwa sababu shughuli ya vijana kupewa vitambulisho imeanza siku chache zilizopita, hali inayomaanisha kuwa haitakuwa rahisi kusajiliwa kama wapigakura katika usajili wa mwezi huu kwa sababu shughuli hizo zote mbili zinaenda sambamba.

Vitambulisho huchukua angaa mwezi mmoja kabla ya kuwa tayari kuchuliwa na waliotuma maombi ya kupewa.

Katika muda huo wa kusubiri, vijana hupewa stakabadhi ya kuonesha kuwa wanangoja kupewa vitambulisho kamili.

Haieleweki ni sababu gani serikali, katika enzi hii ya kidijitali bado inajikokota katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama vile kuwapa vijana na raia wake vitambulisho.

Wengi wao wanaoshika vitambulisho sasa wataweza tu kujisajili kama wapigakura kwenye mkumbo wa Januari.

Maadamu IEBC imelenga jumla ya wapigakura milioni saba katika mikumbo hii miwili ya usajili, basi itakuwa vigumu kufikisha idadi hiyo iwapo wengi hawatapata vitambulisho hivi kwa sasa ndipo wajisajili.

Inapozingatiwa kuwa upigaji kura ni haki ya kidemokrasia ya kila Mkenya, iwapo vijana hao hawatakuwa wamepata vitambulisho vya kuwawezesha kujisajili kwa madhumuni hayo, basi watakuwa wamenyimwa haki yao; jambo ambalo si zuri.

Mbali na vijana, IEBC inahitajika kujitahidi kuhakikisha kuwa shughuli nzima ya usajili wa wapigakura imeendeshwa vyema bila hila zozote zinazoweza kutokea.

Kwa mfano, wapo baadhi ya watu ambao tayari wameanza kulalamika kuwa kuna wanasiasa fulani ambao wameanza kuhamisha wapigakura kutoka maeneo wanakostahili hadi kwenye maeneo yao kwa nia ya kujipa ushindi katika uchaguzi wa 2022.

Sharti njama kama hizo zizimwe.

TAHARIRI: Vijana wapewe vitambulisho upesi

KITENGO CHA UHARIRI

SHUGHULI ya usajili wa wapigakura kitaifa ilianza jana ambapo Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inalenga kusajili zaidi ya Wakenya milioni nne.

Usajili huo ukifanikiwa, Kenya itakuwa na jumla ya angaa wapigakura milioni 24 bila kuzingatia awamu nyingine ya usajili inayotarajiwa kufanyika Januari 2022.

Je, idadi hiyo itafikiwaje bila kuwawezesha vijana ambao ndio wengi wanaolengwa katika usajili huu?

Zaidi ya asilimia 90 ya wanaotazamiwa kusajiliwa ni vijana.

Changamoto kuu ambayo imejitokeza kuhusu kufaulisha azimio la kusajili angaa wapigakura milioni nne wanaolengwa mwezi huu wa Oktoba ni ukosefu wa vitambulisho.

Hii ni kwa sababu shughuli ya vijana kupewa vitambulisho imeanza siku chache zilizopita, hali inayomaanisha kuwa haitakuwa rahisi kusajiliwa kama wapigakura katika usajili wa mwezi huu kwa sababu shughuli hizo zote mbili zinaenda sambamba.

Vitambulisho huchukua angaa mwezi mmoja kabla ya kuwa tayari kuchuliwa na waliotuma maombi ya kupewa.

Katika muda huo wa kusubiri, vijana hupewa stakabadhi ya kuonesha kuwa wanangoja kupewa vitambulisho kamili.

Haieleweki ni sababu gani serikali, katika enzi hii ya kidijitali bado inajikokota katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama vile kuwapa vijana na raia wake vitambulisho.

Wengi wao wanaoshika vitambulisho sasa wataweza tu kujisajili kama wapigakura kwenye mkumbo wa Januari.

Maadamu IEBC imelenga jumla ya wapigakura milioni saba katika mikumbo hii miwili ya usajili, basi itakuwa vigumu kufikisha idadi hiyo iwapo wengi hawatapata vitambulisho hivi kwa sasa ndipo wajisajili.

Inapozingatiwa kuwa upigaji kura ni haki ya kidemokrasia ya kila Mkenya, iwapo vijana hao hawatakuwa wamepata vitambulisho vya kuwawezesha kujisajili kwa madhumuni hayo, basi watakuwa wamenyimwa haki yao; jambo ambalo si zuri.

Mbali na vijana, IEBC inahitajika kujitahidi kuhakikisha kuwa shughuli nzima ya usajili wa wapigakura imeendeshwa vyema bila hila zozote zinazoweza kutokea.

Kwa mfano, wapo baadhi ya watu ambao tayari wameanza kulalamika kuwa kuna wanasiasa fulani ambao wameanza kuhamisha wapigakura kutoka maeneo wanakostahili hadi kwenye maeneo yao kwa nia ya kujipa ushindi katika uchaguzi wa 2022.

Sharti njama kama hizo zizimwe.

TAHARIRI: Vijana wajisajili wasikike 2022

KITENGO CHA UHARIRI

IDADI kubwa ya watu wanaolengwa katika shughuli ya usajili wa wa wapigakura kwa wingi inayoanza leo, ni vijana.

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya 2019, takribani vijana milioni 6 wamehitimu umri wa miaka 18 kuanzia Agosti 2017 hadi sasa. Hiyo inaamana kwamba vijana waliokuwa watoto waliokuwa na kati ya umri wa miaka 13 na 17 katika uchaguzi wa 2017 sasa wamehitimu kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Katika uchaguzi wa marudio wa urais wa Oktoba 26, 2017, Rais Kenyatta alishinda kwa kura milioni 7.4 milioni. Hiyo inamaana kwamba iwapo vijana hao wote milioni 6 watajitokeza kusajiliwa kuwa wapigakura na kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao, watakuwa na usemi mkubwa katika kuamua kiongozi wa tano wa Kenya.

Takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zilionyesha kuwa asilimia 51 ya wapigakura katika uchaguzi wa 2017, walikuwa vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 35. Iwapo vijana hao wote milioni 6 watajisajili basi asilimia ya wapigakura vijana itaongezeka hadi asilimia 65.

Kati ya vijana 3,428 waliowania viti mbalimbali vya kisiasa ni 314 tu walioshinda ilhali wao ndio wapigakura wengi.

Kwa miaka mingi, vijana wamekuwa wakilalama kwamba wameachwa nje katika masuala ya uongozi. Vijana wamekuwa wakilalamika kwamba wamechoka kuambiwa kuwa wao ni viongozi wa kesho.

Ikiwa kweli vijana wamechoka kuambiwa kwamba wao ni viongozi wa kesho, hawana budi kujitokeza kwa wingi na kusajiliwa kuwa wapigakura.

Inasikitisha kusikia baadhi ya vijana wakiapa kwamba hawatapiga kura kwa sababu hawajaona viongozi waliochaguliwa awali wakileta mabadiliko. Wakati wa kuleta mabadiliko ambayo vijana wanahitaji ni sasa. Mabadiliko hayaji kwa kulalamika bali kwa kupigakura ambayo ni haki ya kidemokrasia kwa kila Mkenya ambaye amehitimu umri wa miaka 18 na zaidi.

Vijana wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha watu ambao hawajasajiliwa kuwa wapigakura kwenda kujisajili.

Vijana wanafaa kuongoza juhudi za kuhakikisha kuwa vitambulisho vya kitaifa ambavyo havijachukuliwa katika afisi za usajili wa watu vinapelekewa wenyewe ili wasajiliwe kuwa wapigakura.

TAHARIRI: Sekta ya elimu yahitaji mageuzi

NA MHARIRI

SHULE zinafunga wiki hii ili kukamilisha muhula wa kwanza katika kalenda mpya ya elimu nchini. Kalenda ya elimu ilivurugwa kutokana na ujio wa janga la corona ambalo limetatiza shughuli mbalimbali katika ulimwengu kwa jumla.

Ili kufidia muda uliopotea, kalenda ya shule imebadilishwa kwa kupunguzwa pakubwa ili kuerejesha hali ya kawaida. Kutekeleza mabadiliko hayo kumeibuka kuwa changamoto kuu kwa wanafunzi, walimu na wazazi.

Hata hivyo, mabadiliko hayo ni ya muda mfupi tu, makusudio yakiwa kuhakikisha kwamba kalenda ya zamani ya masomo shuleni inachukua mkondo wake.

Hata hivyo, serikali inapaswa kutathmini utaratibu huo. Baada ya mwaka mzima wa utekelezaji wa mpango huo, mambo mengi yameibuka na yanapaswa kuibua mafunzo tele kwa wadau wanaoutekeleza kwa manufaa ya wanafunzi katika siku zijazo.

Changamoto kuu inayokabili wazazi kwa sasa ni suala la karo. Wanapaswa kulipa karo kwa mfuatano mfupi na pia kuwapa nauli ya watoto wao wanaporejea shuleni, zaidi ya kuhakikisha kwamba mahitaji yao yote ya kiakademia yamekidhiwa barabara.

Masaibu haya yote yanatokana na ujio wa tandavu la corona, ambalo limevuruga kila sekta ya kitaifa, ya elimu ikiwa yenye kuvurugwa pakubwa.

Hivyo basi, Wizara ya Elimu inapaswa kuwazia njia mwafaka za kusaka suluhu za matatizo yanayoikabili kwa sasa.

Ikumbukwe kuwa Wizara hii ilipunguza karo mwanzoni mwa muhula na itakuwa busara tupu iwapo karo hiyo itaendelea kupunguzwa hivyo hadi mwisho wa mwaka ili kuwapa wazazi nafasi ya kutafuta pesa.

Shule ambazo zimeongeza karo zinapaswa kumulikwa na kuadhibiwa na serikali kwa kuwapa wazazi zigo zaidi ya lile linalowaelemea sasa hivi.

Serikali pia inapaswa kuhakikisha kwamba likizo fupi za kati ya mihula zinaondolewa kwa muda kwa sababu zina gharama pia kwa mzazi. Si sawa kwa wanafunzi kufunga kwa likizo fupi, ilhali mihula yenyewe imefupishwa.

Utoaji wa basari nao pia unapaswa uende sambamba na kalenda ya shule na wanafunzi zaidi waweze kupokea ufadhili huo, kutokana na ukweli kwamba familia nyingi zimepoteza mapato kutokana na corona.

Muhimu zaidi ni kuwaandaa watahiniwa wa kidato cha nne na darasa la nane kwa mitihani ya kitaifa ambayo inajongea.

TAHARIRI: Sakata ya Kemsa inakatisha tamaa

KITENGO CHA UHARIRI

KAMATI ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) iliyokuwa ikichunguza sakata ya wizi wa mabilioni ya fedha kupitia kandarasi zilizotolewa kiholela na Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Tiba nchini (Kemsa), janga la corona lilipovamia Kenya mwaka jana, haikufanya kazi ya kuridhisha.

Katika ripoti yake, kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, haikutoa mapendekezo ya kushtakiwa kwa baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi serikalini waliotajwa wakati wa uchunguzi.

Sh7.8 bilioni zilitengwa na serikali kupambana na virusi vya corona lakini takribani Sh3.2 bilioni zinaaminika kuishia katika mifuko ya mabwanyenye wachache licha ya hospitali kukosa mitungi ya oksijeni na mavazi ya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya virusi.

PIC ilipendekeza kampuni zilizopata kandarasi hizo zilizokuwa zikitolewa kiholela, zirejeshe fedha.

Wakati kamati hiyo ilipokuwa ikihoji wakurugenzi wa kampuni 102 zilizofanya biashara na Kemsa, walionufaika na kandarasi hiyo walikiri kukiuka sheria.

Wakenya walistaajabishwa kusikia baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo wakidai kwamba waliomba Mungu kuwapa kandarasi.

Wengine walidai kwamba walikuwa wakipita karibu na jumba la Kemsa wakaitwa na kupewa kandarasi hiyo.Ukweli ni kwamba, ni vigumu kwa raia wa kawaida kupata kandarasi bila kuwa na ushawishi serikalini.

Kulikuwa na dalili kwamba kampuni hizo zilimilikiwa na watu wenye ushawishi serikalini waliojificha nyuma ya wakurugenzi hao.Sakata hiyo ilipoibuka, Rais Uhuru Kenyatta, mnamo Agosti 2020, aliagiza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufanya uchunguzi na kuukamilisha ndani ya siku 21.

EACC ilikamilisha uchunguzi wake baada ya siku 21 kupita na kuwasilisha ripoti yake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Bw Haji, hata hivyo, alikataa faili ya uchunguzi huo huku akiitaka EACC kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ushahidi wa kutosha.

EACC ilikuwa imependekeza kushtakiwa kwa wakurugenzi wa kampuni za Accenture Kenya, Gadlab Supplies, Meraky Healthcare, Steplabs Technical Services, Wallabis Ventures, Shop n Buy na Kilig Ltd ambayo Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe alikiri kuisimamia kuchukua mkopo katika Benki ya Equity.

Mbali na PIC, sakata hiyo imechunguzwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya pamoja na Seneti.

Inaonekana sakata hiyo imeingia kwenye orodha ndefu ya visa vya ufisadi ambapo walipa ushuru wamepoteza mabilioni ya fedha bila wahusika kuchukuliwa hatua.

Idata ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) haina budi kuingilia kati kuhakikisha kuwa fedha zote zilizopotea katika sakata hiyo zinarejeshwa na wahusika wanakamatwa.

TAHARIRI: Ripoti ya Kemsa inakatisha tamaa

KITENGO CHA UHARIRI

KAMATI ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) iliyokuwa ikichunguza sakata ya wizi wa mabilioni ya fedha kupitia kandarasi zilizotolewa kiholela na Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Tiba nchini (Kemsa), janga la corona lilipovamia Kenya mwaka 2020, haikufanya kazi ya kuridhisha.

Katika ripoti yake, kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, haikutoa mapendekezo ya kushtakiwa kwa baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi serikalini waliotajwa wakati wa uchunguzi.

Sh7.8 bilioni zilitengwa na serikali kupambana na virusi vya corona lakini takribani Sh3.2 bilioni zinaaminika kuishia katika mifuko ya mabwanyenye wachache licha ya hospitali kukosa mitungi ya oksijeni na mavazi ya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya virusi.

PIC ilipendekeza kampuni zilizopata kandarasi hizo zilizokuwa zikitolewa kiholela, zirejeshe fedha.

Wakati kamati hiyo ilipokuwa ikihoji wakurugenzi wa kampuni 102 zilizofanya biashara na Kemsa, walionufaika na kandarasi hiyo walikiri kukiuka sheria.

Wakenya walistaajabishwa kusikia baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo wakidai kwamba waliomba Mungu kuwapa kandarasi.

Wengine walidai kwamba walikuwa wakipita karibu na jumba la Kemsa wakaitwa na kupewa kandarasi hiyo.Ukweli ni kwamba, ni vigumu kwa raia wa kawaida kupata kandarasi bila kuwa na ushawishi serikalini.

Kulikuwa na dalili kwamba kampuni hizo zilimilikiwa na watu wenye ushawishi serikalini waliojificha nyuma ya wakurugenzi hao.

Sakata hiyo ilipoibuka, Rais Uhuru Kenyatta, mnamo Agosti 2020, aliagiza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufanya uchunguzi na kuukamilisha ndani ya siku 21.

EACC ilikamilisha uchunguzi wake baada ya siku 21 kupita na kuwasilisha ripoti yake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Bw Haji, hata hivyo, alikataa faili ya uchunguzi huo huku akiitaka EACC kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ushahidi wa kutosha.EACC ilikuwa imependekeza kushtakiwa kwa wakurugenzi wa kampuni za f Accenture Kenya, Gadlab Supplies, Meraky Healthcare, Steplabs Technical Services, Wallabis Ventures, Shop n Buy na Kilig Ltd ambayo Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe alikiri kuisimamia kuchukua mkopo katika Benki ya Equity.

Mbali na PIC, sakata hiyo imechunguzwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya pamoja na Seneti.

Inaonekana sakata hiyo imeingia kwenye orodha ndefu ya visa vya ufisadi ambapo walipa ushuru wamepoteza mabilioni ya fedha bila wahusika kuchukuliw hatua.Idata ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) haina budi kuingilia kati kuhakikisha kuwa fedha zote zilizopotea katika sakata hiyo zinarejeshwa na wahusika wanakamatwa.

TAHARIRI: Usimamizi wa soka umedorora

KITENGO CHA UHARIRI

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Soka (KPL) unaanza hii leo ukigubikwa na sintofahamu kubwa jinsi ligi itafadhiliwa, baada ya kampuni ya Odibet kuwa ya hivi punde kuondoa udhamini wake.

Wiki hii Odibet ilitangaza rasmi kuagana na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kwa kile kinachosemekana ni kutoridhishwa na juhudi za shirikisho kukuza soka mashinani.

Kampuni hiyo ya kamari ilikuwa ikitoa ufadhili wa Sh127 milioni katika mkataba wa miaka mitatu uliotangazwa Desemba 2019. Ufadhili huo ulikuwa kwa Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza, Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili na Ligi ya Kaunti.

Madhumuni yalikuwa kuimarisha kandanda mashinani ili kuwa na timu thabiti zinazokuza chipukizi watakaowika kesho na mtondogoo.

Kujiondoa kwa Odibet kunakujia miezi kadha baada ya wafadhili wa Ligi Kuu, Betking, kukatiza uhusiano wake na FKF kuelekea mwisho wa msimu jana Agosti.

Betking, kutoka Nigeria, ilikuwa imetoa ufadhili wa Sh1.2 bilioni katika mkataba wa miaka mitano kuanzia Julai 2020.Kwa sasa ni kampuni moja pekee iliyosalia ya Betika, inayofadhili Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Hata huko mambo ni hatihati huku kukiwa na minong’ono kwamba pia inawazia kuondoa ufadhili wake wa Sh45 milioni kwa miaka mitatu, ulioanza Novemba 2019.

Ni wazi kwamba wafadhili hawana imani tena jinsi Rais Nick Mwendwa anavyosimamia soka ya Kenya.Kinara huyo amejawa na kiburi, haambiliki hasemezeki. Hataki kuwajibikia mabilioni ya fedha ambazo FKF inapokea kuendesha soka.

Isitoshe, amekuwa kama dikteta – alilazimisha klabu za soka kutia saini mkataba wa kupeperusha mechi kupitia Star Times, la sivyo zinyimwe posho la ufadhili wa Betking.

Akajipata katika mvutano na vigogo wa soka nchini, Gor na AFC, kuhusu Sh3 milioni za kombe la Betway Cup ilhali siku chache tu alizindua mnara wa KPL la Sh5 milioni.

Juzi aliibuka na jipya alipotangaza kocha mpya wa timu ya taifa Harambee Stars kwa mkataba wa miezi miwili! Ni matukio ya kushangaza jinsi usimamizi wa soka unavyozidi kudorora kila uchao. Je, nani atawaondolea mashabiki madhila haya?

Wanachama wa Baraza Simamizi la Kitaifa (NEC) ndio wenye kuamua jibu la swali hili. Wako na uwezo wa kupiga kura ya kumuondoa Mwendwa ofisini kwani hatokubali kubanduka. Wataweza?

Tunasubiri kuona iwapo watatimiza wajibu huo ipasavyo ili kuokoa soka ya Kenya.

TAHARIRI: Midahalo endelevu itachochea ustawi

KITENGO CHA UHARIRI

NYAKATI za kampeni za kisiasa husheheni matumizi tele ya propaganda za kisiasa ambapo washindani mbalimbali huzitumia kuwaumbua wenzao, hasa uchaguzi unapokaribia.

Ni mtindo ambao umekuwepo kwa muda mrefu tangu mwanzo wa tawala zilizojikita kwenye mfumo wa kidemokrasia katika maeneo kama Ugiriki na falme ya Roma.

Nchini Ugiriki, washindani wa nyadhifa mbalimbali za uongozi katika miji ya Athens na Sparta walitumia majarida maalum kuelelezea mikakati ambayo wangetumia kuboresha uongozi.

Kando na kujumuisha mikakati yao, walikosoana, japo kwa njia ambazo zilizua midahalo ya kuvutia miongoni mwa wenyeji wa miji hiyo miwili mikuu.

Mfumo huo ndio uliokua na kupanuka kabisa kiasi cha kuigwa na nchi kama Amerika na Uingereza.

Lengo kuu la tathmini hii ni kubuni msingi kuhusu chimbuko na athari za matumizi ya propaganda kwenye siasa.

Nchini Amerika, midahalo ambayo hufanyika miongoni mwa washindani wa urais huwa ni kuumbuana na kukosoana, ingawa huendeshwa kwa njia ya kuwazindua wafuasi wa kila upande.

Hapa Kenya, tumeona majaribio kadhaa ya maandalizi ya mdahalo wa kitaifa miongoni mwa wawaniaji wakuu wa urais.

Jaribio la kwanza lilikuwa mnamo 2013 huku zoezi la pili likiwa 2017.

Kwenye mdahalo uliofanyika 2013, Wakenya walipata nafasi ya kufuatilia kwa kina mipango ambayo wawaniaji husika walikuwa nayo ili kuiboresha nchi.

Jambo lilo hilo lilifanyika mnamo 2017, ingawa halikufaulu kama 2013 kutokana na migawanyiko ya kisiasa iliyokuwepo nchini, hasa kati ya mrengo wa Jubilee, ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Nasa, ulioongozwa na Raila Odinga.

Tunapokaribia uchaguzi mkuu wa 2022, Baraza la Wahariri Kenya (KEG) limetangaza Julai 12 na 26 kuwa tarehe ambapo midahalo hiyo itafanyika. Hata hivyo, swali ni: Midahalo hiyo itafaulu kutokana na migawanyiko ya kisiasa iliyopo nchini?

Kosa kubwa ambalo vigogo wakuu wa kisiasa nchini wanafanya ni kuumbuana na kukosoana isivyofaa. Wengine hata wanatusiana hadharani kwa kisingizio cha kushindana.

Matumizi yafaayo ya propaganda hukitwa kwenye sera za mgombea husika wala si mwenendo wake, familia, marafiki au jamaa zake.

Nchini Amerika, wawaniaji hukosana kwa misingi ya sera na manifesto zao wala si sifa au familia zao.

Kosa hilo ndilo hujenga taharuki na migawanyiko ya kikabila isiyofaa.

Ni wakati wanasiasa wafahamu kuwa propaganda huwa njia ya kuzua midahalo endelevu wala si kutusiana.

TAHARIRI: TSC idhibiti zogo la shule haraka

KITENGO CHA UHARIRI

RIPOTI kuhusu uchomaji wa shule kubwa za upili humu nchini siku mbili zilizopita zinaibua hofu kuu kwa wazazi hasa ikikumbukwa kwamba mwaka huu wa masomo ni mfupi mno na wanafunzi, walimu wana kazi nyingi kukamilisha kabla ya Machi 2022.

Kando na miaka ya awali, wadau sasa wanahitajika kusomesha silebasi ya mwaka mzima katika wakati mfupi uliowekwa na wizara ya Elimu.

Katika hali hii, shule zinafaa kuwa na mazingira matulivu yatakayoyawezesha kufikia maazimio na malengo yao kimasomo, kama kupasi mitihani ijayo kwa alama za juu.

Serikali, walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wote katika shule kwa jumla wanafaa kujukumika kufanikisha haya kwa ushirikiano.Matukio yalishuhudiwa katika Shule ya Upili ya Sigalame iliyoko kwenye Kaunti ya Busia ni kinyume cha matarajio haya.

Mojawapo ya mabweni ya shule hii iliripotiwa kuchomwa na wanafunzi kuagizwa kwenda nyumbani hadi uchunguzi kamili kuhusu tendo hilo la uhalifu huo ukamilike na suluhisho kamili na kudumu kupatikana.

Mbali na hasara kutokana na uharibifu wa vifaa vya wanafunzi katika bweni, hakuna madhara ya kiafya yalitoripotiwa kuwakumba wanafunzi.

Hali inayotamausha katika tukio hili ni kwamba, hii ni bweni la nne kuchomeka ndani ya mihula miwili pekee na bado kiini cha uhalifu huu hakijafichuliwa licha ya uchunguzi kufanywa kila wakati.

La wazi ni dai kwanza wanafunzi hawahusiki kabisa!Kulingana na Bodi ya Usimamizi (BOM) katika shule hii, tayari imewasilisha kwa Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC) malalamiko na ushauri kuhusu jinsi ya kukabili tatizo hilo lakini hatua ya dharura ilivyokatikana haikuchukuliwa na TSC kwa wakati uliofaa.

Kuna malalamiko chungu nzima ya usimamizi mbaya na ufisadi katika utoaji tenda ambapo kidole cha lawama kinaelekezewa Mwalimu mkuu na naibu wake.

Ni aibu pia kuona Shule ya Upili ya Ofafa Jericho katika Kaunti ya Nairobi ikijipata katika orodha hii ya uchomaji bweni siku moja baada ya wenzao wa Sigalame.

Tume ya TSC ikishirikiana na wizara ya Elimu inafaa kuingilia kati masuala ya kinidhamu kama haya kabla hayajaenea nchini ili kuhakikisha shule zinasimamiwa na walimu wenye maadili ya kipekee.

TAHARIRI: Sarakasi hazimfai raia anayeumizwa

KITENGO CHA UHARIRI

WANANCHI wanapoendelea kuumizwa na bei ya juu ya mafuta, kila mtu anajaribu kujiondolea lawama.

Maseneta, kwa kutaka kujipendekeza kwa wapigakura, jana Jumanne walijaribu kufurahisha umma kwa kutaka kuwahoji mawaziri wawili. Mawaziri hao John Munyes (Petroli) na Charles Keter (Kawi) walipuuza mwaliko huo.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, ambaye aliongoza Bunge mwaka 2018 kupitisha Mswada wa Fedha, safari hii amejitokeza kuwa mkosoaji.

Akizungumza wikendi eneo la Runyenjes, Embu, Bw Muturi aliwataka wabunge wawasilishe bungeni marekebisho ya sheria hiyo.Siku walipopitisha, Bw Muturi alionekana kusukuma wabunge waharakishe shughuli hiyo, bila kusikiza waliokuwa na pingamizi.

Maseneta, kwa kutaka kujipendekeza kwa wananchi, walichukua jukumu lisilo lao. Waliwaita mawaziri kujadili kuhusu Sheria ya Fedha (2018), ambayo ushuru uliopendekezwa umeanza kuonekana athari yake.

Wakenya wanapopambana na ugumu wa maisha kutokana na janga la Corona, ipo haja ya kuangalia upya sheria hiyo. Kwa sababu ya ushuru kupita kiasi kwenye bei ya mafuta, bidhaa hiyo ni ghali humu nchini kuliko ilivyo Uganda.

Taifa lisilokuwa na bandari, linalotoa mafuta yake kwenye bandari ya Mombasa na kuyapitishia nchini, linauza lita moja ya petroli Sh4300 za Uganda, sawa na Sh131 za Kenya.

Hiyo ndiyo bei ya juu zaidi Uganda, ikilinganishwa na Sh147 mjini Mandera.

Maseneta wanafahamu kwamba Katiba inalipatia Bunge la Taifa jukumu na mamlaka ya kuhusika na masuala ya fedha. Mswada uliopandisha ushuru wa mafuta unaweza tu kurekebishwa na wabunge.

Si maseneta wala mawaziri.

Ndio maana mawaziri Munyes na Keter ambao ni maseneta wa zamani, walikataa kufika mbele ya Seneti.

Walijua mwaliko huo ni sarakasi tupu.

Ingawa Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga aliamua kwamba sheria hiyo ya ushuru ni batili, Serikali imeonyesha siku za nyuma kuwa haiheshimu maamuzi ya korti.

Kinachohitajika sasa ni mbunge yeyote kuunda mswada wa marekebisho ya sheria hiyo.

Mswada huo ujadiliwe kwa haraka na kuondoa sheria inayotoza ushuru zaidi kwa mafuta.

Bila hivyo, agizo la Spika kwamba Kamati ya Fedha ichukue wiki mbili kuangalia suala hilo, ni sarakasi isiyowaondolea dhiki wananchi.

TAHARIRI: Ushuru zaidi ni mzigo usiofaa

KITENGO CHA UHARIRI

HATUA ya mahakama kuu kuharamisha sheria iliyonuia kuanzisha ushuru wa mapato wa asilimia moja ambao ungeshuhudia biashara na kampuni zikitozwa kodi hiyo hata wakati ambapo zimepata hasara, ni jambo la kujivunia.

Hatua hiyo ya mahakama inafaa kuizindua serikali kuhusu mipango yake ya kujiongezea mapato. Si vyema serikali kuongeza pato lake huku biashara hasa ndogondogo ambazo zingeipa hata ushuru zaidi zikianguka.

Je, biashara hizo zikishaanguka, serikali itatoza nani asilimia hiyo ya ushuru?

Naam, hamna serikali yoyote ulimwenguni inayoweza kuhudumu bila kutoza raia wake na mashirika ya kibiashara ushuru maadamu ni kutokana na kodi hiyo ambapo miradi ya maendeleo hufanikishwa mbali na watumishi wa umma kama vile walimu na madaktari kupata mishahara yao.

Ila pia hakuna taifa lililoendelea kiuchumi au kijamii kwa kuwatoza raia wake ushuru wa kupindukia kama huu ambao serikali ya taifa hili imekuwa ikipanga kuanzisha.

Hii ni kwa sababu unapowatoza raia ushuru mwingi, wanakosa uwezo wa kununua bidhaa mbalimbali jinsi ambavyo wangependa na hivyo basi biashara nyingi ambazo huwategemea raia hao kama wateja kukosa mapato.

Katika hali kama hiyo, watu wengi hukosa riziki na shughuli za kiuchumi kupungua, jambo linalodororesha viwango vya maisha.

Cha kusikitisha ni kuwa hata katika hali ambapo ushuru huu vinginevyo ungetumiwa kufadhili, kwa njia ya ruzuku, huduma nyingi za kimsingi, fedha nyingi zinazotokana na ushuru wa mwananchi huliwa kifisadi na Wakenya wachache walio katika nafasi zao.

Katika mataifa mengine ambapo ushuru mwingi hutozwa raia, huduma muhimu kama vile elimu, afya na hata usafiri huwa ni za hali ya juu mbali na kuwa nafuu zaidi.

Tatizo jingine kuu la kutoza ushuru mwingi ni kutoroka kwa wawekezaji wa kigeni ambao huhamia mataifa yaliyo na mazingira bora ya kufanyia biashara.

Kwa ufupi, utozaji ushuru usiokuwa na mipaka una athari nyingi hasi kuliko manufaa hasa kwa mataifa yanayostawi kama vile Kenya.

TAHARIRI: Vijana wasikubali siasa za vurugu

KITENGO CHA UHARIRI

WAKAZI wa Kaunti za Siaya na Kisumu wanastahili pongezi kwa jinsi walivyoshughulikia ziara ya mfanyibiashara Jimmy Wanjigi.

Kwa kawaida mapokezi ya heshima kwa mtu ambaye ametangaza kuwa atampinga Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ndani ya chama chake, hayangefanyika.

Hili lilionekana Ijumaa katika Kaunti ya Migori, ambapo vijana walimrushia mawe Bw Wanjigi huku wakikatiza hotuba yake. Walisikika wakisema ‘Baba! Baba!’

Hiyo ilikuwa ishara kwamba eneo hilo ni ngome ya Bw Odinga pekee.

Kwa hivyo ni vizuri kwamba chama cha ODM kilikashifu kitendo hicho na kutaka Idara ya Polisi uchunguze waliokidhamini.

Tunaungana na ODM kumhimiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai aamuru uchunguzi. Watakapatikana na hatia ya kuwafadhili vijana kuzua vurugu hizo, washtakiwe.

Kenya ina sheria.

Katiba inatoa hakikisho kwamba kila Mkenya atakuwa na haki ya kushiriki katika kampeni na kuwaomba watu kura.

Kumzuia mtu au kumshambulia kwa mawe kwa sababu amepeleka kampeni zake eneo fulani, ni uhalifu.Ndio sababu viongozi wa Baraza la Wazee wa Luo kupitia mwenyekiti wake Mzee Willis Opiyo Otondi wanastahili pongezi.

Mzee Otondi alimkaribisha Bw Wanjigi Siaya, nyumbani wa Bw Odinga na akampa maneno ya kumtia moyo.

Aliamini kwamba Bw Wanjigi akiwa mwanachama wa maisha wa ODM, ana kila haki ya kuwania uteuzi wa chama hicho.Yeye si wa kwanza kufanya hivyo.

Manaibu vinara wa ODM Wycliffe Oparanya na Hassan Joho walifanya hivyo. Magavana hao wawili walilipa Sh1 miliono kila mmoja kwa chama cha ODM na kueleza azma zao za kutaka kuwania uteuzi wa kupeperusha bendera ya urais.

Ingawa Bw Joho wikendi alitangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro, viongozi na wanachama wa ODM waliheshimu kujitokeza kwake kutaka ateuliwe.

Bw Wanjigi jana Jumapili pia alipata mapokezi mazuri jijini Kisumu, kitovu cha siasa za ODM.

Wakazi hao walitambua kuwa, Bw Odinga pia atataka kuomba kura katika maeneo yaliyo nje ya Nyanza. Kumvuruga Bw Wanjigi lingekuwa kosa kubwa kwa kiongozi mwenye hadhi ya kutaka kuwa urais wa Tano.

TAHARIRI: Lalama kuhusu CBC zisipuuzwe

KITENGO CHA UHARIRI

MJADALA kuhusu ufaafu na utekelezaji wa Mtaala mpya wa Umilisi na Utendaji (CBC) umedumu kwa muda sasa huku wazazi na walimu wakilalamika.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha amesisitiza kuwa mtaala huo utaendelea kutekelezwa na kwamba serikali imeweka mikakati ya kuufanikisha kikamilifu.

Kulingana na Prof Magoha, wanaolalamika kuhusu mtaala huo wanautakia mabaya usifaulu akisema serikali haina nia ya kuutupilia mbali.

Hata hivyo, malalamishi ya wazazi na wadau wengine si ya kutaka mtaala huo ukomeshwe bali uboreshwe zaidi kwa manufaa ya wanafunzi na wazazi pia.

Wazazi wanahisi kwamba wamelimbikiziwa majukumu mengi ya kuwasaidia wanafunzi wao ilhali kuna baadhi yao ambao japo wana muda, hawana ufahamu wowote kuhusu wanayotakiwa kutekeleza.

Kuna wale ambao hawakusoma ilhali wanatakiwa kusaidia watoto wao kwa kazi za shuleni na kuna wale ambao wamesoma lakini hawana ufahamu wa masuala ya teknolojia ambayo yamepewa umuhimu katika mtaala huo.

Kuna pia gharama ya vitabu na vifaa ambayo waziri alipuuza lakini ni muhimu sana.

Ingawa anasema serikali imenunua vitabu vya kutosha katika shule zote za umma, kuna suala la usawa ambalo linafaa kushughulikiwa.

Hii ni kwa kuwa wanafunzi wote hawawezi kutoshea katika shule za msingi za umma.

Huu ni ukweli ambao hauwezi kupuuzwa. Muhimu kabisa ni mipango ya serikali ya kuhakikisha wanafunzi wa kwanza wa gredi ya sita wataendelea na masomo ya shule ya upili bila kutatizika.

Licha ya walimu kutilia shaka uwezo wa kufanikisha wanafunzi wa gredi ya sita kujiunga na shule za msingi, Prof Magoha anasema wanaolaumu serikali wanafaa kusubiri kuona mikakati ya serikali.

Kauli ya waziri huyo inaashiria kuwa huenda kuna mipango ambayo serikali imekuwa ikifanya bila kuwahusisha walimu ambao inategemea kufanikisha mtaala huo.

Ikiwa huo ndio ukweli, serikali itakuwa imekosea kwa kuwaacha walimu gizani ilhali inawategemea kutekeleza mtaala huo.

Ili kuepuka malalamishi na sintofahamu, uwazi unahitajika kwa kuwa mtaala wa elimu huwa si mali ya watu wachache bali huwa unabuniwa kustawisha nchi.

Mtaala huo unaweza kuboreshwa kwa kusikiliza malalamishi yanayoibuka na kuyajibu au kuyashughulikia kikamilifu na si kwa kuyapuuza.Kwa kufanya hivyo, mtaala huu utafaulu na kunufaisha nchi.

TAHARIRI: Tuwekeze katika soka ya kina dada

KITENGO CHA UHARIRI

ILIKUWA shangwe, vigelegele, hoihoi na nderemo pale wasichana wa kikosi cha soka cha Vihiga Queens walipofuzu kwa dimba la Klabu Bingwa Afrika (CAF) ambalo linachezwa kwa mara ya kwanza nchini Misri baadaye mwaka huu.

Mafanikio hayo yalitokana na hatua ya Vihiga kuibuka mabingwa wa kandanda ya Baraza la Shirikisho la Soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) iliyotia nanga Alhamisi jijini Nairobi.

Vihiga alichabanga Commercial Bank of Ethiopia mabao 2-1 kwenye fainali kali iliyosakatwa katika uwanja wa Kasarani, Nairobi.

Hakika soka ya Kenya, upande wa kinadada imekuwa ikipanda hadhi katika miaka ya hivi karibuni hasa tangu kikosi cha taifa cha Harambee Starlets kifuzu kushiriki fainali za Kombe la Afrika mnamo 2018, hii ikiwa mara ya kwanza kabisa kwa taifa hili.

Tangu wakati huo, mchezo wa kinadada wa Kenya umekuwa ukistawi aste aste kila mwaka licha ya ligi ya wanawake nchini kukumbwa na misukosuko ya kila aina hasa kutokana na ukosefu wa ufadhili.

Je, iwapo hadhi ya kabumbu ya Kenya imekuwa ikipaa hivyo ilhali hamna ufadhili wa kutosha, sembuse ufadhili huo ukizidishwa?

Waama, sawa na Harambee Starlets, Vihiga Queens wametupa kila sababu ya kuhakikisha kuwa tunamakinikia zaidi mchezo wa vipusa.

Ni wakati muhimu kwa mashirika mbalimbali hasa ya kibiashara kama vile benki, kampuni za mawasiliano, fedha, usafiri na kudhalika kujitokeza kuinua mchezo wa wasichana wetu.

Wala hii haina maana kuwa macho yaondolewe kwa mchezo wa wavulana; la hasha.

Fani hiyo bado pia inahitaji kukuzwa maadamu ina umuhimu mkubwa hasa kwa maisha ya vijana hao wa kiume.Ufadhili huu una umuhimu nomi kwa maisha ya vijana wa taifa hili.

Kwa kuwekeza katika mchezo huu wa soka hasa upande wa vigoli, tutazuia matatizo mengi nchini yanayowakubwa watoto wa jinsia hiyo.

Wataepuka maovu kama vile mapenzi ya kiholela, ndoa za mapema na hata mihadarati kwa kujishughulisha zaidi na mpira.

Mpira wa mguu, kama shughuli ya kuwatafutia vijana ajira, inastahili kuzingatiwa zaidi na serikali pamoja na wadau ili kuhakikisha kuwa pengo kuu la uhaba wa kazi linazibwa.

Mafanikio ya Vihiga Queens yaibue mwamko mpya kwa wadau katika sekta hii mbali na wawekezaji ambao kwa hakika huvuna pesa nyingi kama faida kila mwaka kutokana na mauzo wanayofanya ambayo hufanikishwa na wateja ambao hasa ni raia wa Kenya.

TAHARIRI: Ahadi ya kazi kwa vijana iko wapi?

KITENGO CHA UHARIRI

KISA cha wasomi watatu waliohitimu na shahada ya uzamifu (PHD) kulazimika kufunza shule za chekechea na msingi kwa kukosa kazi katika shule za upili, vyuo vikuu na taasisi husika za serikali kinatamausha na kukatisha tamaa wanafunzi wengi waliofuzu na digrii ya kwanza katika vyuo vikuu nchini.

Dkt John Timon Owenga, Dkt Violet Otieno na Dkt Daughty Akinyi wanasema kwamba wamelazimika kufunza shule za msingi licha ya kubobea katika taaluma zao kwa kuwa hawajafaulu kupata kazi au kupandishwa vyeo.

Licha ya watatu hao kutumia nguvu, muda, pesa na kujitolea kufikia kiwango cha juu zaidi cha elimu Kenya, hawajaweza kupata kazi zinazowiana na elimu yao katika serikali za kaunti, serikali ya kitaifa, vyuo vikuu au mashirika ya serikali. Hii ndio taswira kamili ya watu wengi waliofuzu chuo kikuu humu nchini.

Wengi hawana kazi na wamesalia kufanya vibarua ili kujikimu kimaisha.Juzi, habari za wanachuo watatu wanaofanya kazi timboni wakilipwa Sh100 zimezagaa kote mitandani.

Amos Kimutai, aliyefuzu katika Chuo Kikuu cha Kisii na digrii ya Kemia ya Mafuta alisema kwamba yeye na rafiki zake hutengeza kokoto wakilipwa Sh100 kwa siku kwa sababu hawakupata kazi baada ya kufuzu.

Ni mahafala wangapi wanafanya kazi kama walinzi wa usiku mijini? Ni wangapi ni mayaya? Kuna tatizo kubwa la ukosefu wa kazi nchini, ingawa tatizo hili laweza kutatuliwa kwa juhudi za pamoja.

Mojawapo ya manifesto na ajenda ya serikali ya Jubilee ilikuwa kuunda ajira milioni moja kila mwaka kwa vijana wetu ili kupunguza kiwango cha ukosefu wa kazi miongoni mwao.

Hilo halikutimia, kilnachoshuhudiwa sasa hivi ni malumbano ya kisiasa yanayopandikiza chuki na uhasama miongoni mwa Wakenya badala ya siasa safi zenye kuboresha hali na maisha yao.

Serikali ya Rais Kenyatta imefanya mengi kuhusu miundomsingi, barabara nyingi zimejengwa katika maeneo mengi nchini, mitaani na mashinani.

Juhudi zizo hizo zilihitajika kupiga jeki sekta za kilimo, utalii, teknolojia, elimu na kwa jumla tasnia ya uzalishaji ili kujenga nafasi tele za kazi.

Wanachuo waliofuzu nao pia wanaweza kutumia maarifa waliopata vyuoni kubuni nafasi za kazi badala ya kutegemea serikali kuwaajiri. Elimu ya juu inapaswa kutanua ubongo na maarifa ya mtu ili afikirie zaidi ya kuandikwa kazi.

TAHARIRI: Kikosi maalumu kitumwe Laikipia

KITENGO CHA UHARIRI

UFICHUZI kwamba majangili wanaohangaisha wakazi wa Kaunti ya Laikipia wanatumia bunduki za maangamizi makubwa kuliko zile zinazotumiwa na polisi, unahofisha.

Kulingana na Kamishna wa Bonde la Ufa, Bw George Natembeya, majangili hao wanatumia bunduki za M16 ambazo kwa kawaida hutumiwa na majeshi ya kigeni ambayo yamekuwa yakifanyia mafunzo katika Kaunti ya Laikipia.

Bw Natembeya pia alifichua kwamba serikali haina ufahamu kuhusu mahali majangili hao walikopata silaha hizo hatari.

Kwa upande mwingine, maafisa wa humu nchini wanatumia bunduki aina ya AK47 na G3 hivyo kuwa vigumu kuwamaliza majangili hao.

Watu wasiopungua 12 wameuawa na zaidi ya nyumba 50 kuteketezwa kufikia jana katika eneo hilo. Kwa mujibu wa ripoti, shule zisizopungua sita zimefungwa kufuatia machafuko hayo.

Inaogofya kwamba majangili hao wamekuwa wakitekeleza mashambulio usiku dhidi ya raia licha ya kuwepo kwa vikosi mbalimbali vya usalama kama vile maafisa wa kupambana na wizi wa mifugo (ASTU) na GSU.

Mnamo Julai 28, 2021, waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i alipozuru Kaunti ya Laikipia alitoa onyo kali dhidi ya majangili na kutoa makataa ya siku saba kwa wafugaji waliokuwa wakichunga mifugo yao katika mashamba ya kibinafsi, kuondoka.

Lakini makataa hayo ya Waziri Matiang’i hayakuwa na athari yoyote kwani majangili hao wangali wanaendelea kuhangaisha wakazi.

Kulingana na Katibu wa wizara ya Usalama, Dkt Karanja Kibicho, suala la usalama katika Kaunti ya Laikipia limeingizwa siasa – hali ambayo imetatiza juhudi za kudhibiti majangili.

Jambo la kushtua zaidi ni kwamba majangili hao wamekuwa wakijitokeza tu kila mara uchaguzi unapokaribia tangu 1992.

Suala la ukosefu wa usalama katika Kaunti ya Laikipia limegeuka donda ndugu sawa na eneo la Kapedo (mpakani mwa Kaunti za Baringo na Turkana) ambapo serikali imeshindwa kudhibiti majangili ambao wamekuwa wakihangaisha watu kwa miaka na mikaka.

Serikali haina budi kuchukua hatua kali kwa kuzindua kikosi maalumu cha kukabiliana na majangili hao katika eneo la Laikipia sawa na ilivyofanya 2008 dhidi ya wanamgambo wa Sabaot Land Defence Force (SLDF) katika eneo la Mlima Elgon kupitia ‘Operation Okoa Maisha’.

TAHARIRI: Serikali iviondoe vizingiti vya CBC

KITENGO CHA UHARIRI

SUALA kuhusu mfumo mpya wa elimu (CBC) limejitokeza tena, safari hii hata walioshirika kuubuni wakilalama kuwa unakandamiza wazazi.

CBC ambayo serikali inaipigia debe kuwa njia bora kwa watoto kujitegemea siku za usoni, imekosolewa kuwa inayosababisha usumbufu.

Wazazi wengi wanasema ni kama walioshiriki kuja na fikra za mfumo huo walikuwa wakiwawaza matajiri pekee.

CBC si mfumo wa elimu kwa mtu maskini kama ilivyokuwa 8-4-4.

Tofauti kubwa ni kwamba, wakati wa 8-4-4 watoto walitakiwa kupeleka shuleni vifaa vilivyokuwa viko kwenye nyumba zao.

Mmoja angeagizwa apeleke viatu vya ngozi. Mwenzake angeitishwa rangi ya viatu. Mwengine angeagizwa apeleke taa ya chemni na jivu na kadhalika.

Wanafunzi hao wangefundishwa jinsi ya kusafisha kioo cha taa au kupiga rangi viatu.

Lakini CBC inamchukulia kila mzazi kuwa mwenye uwezo wa kununua bidhaa.

Mwalimu huitisha darasa zima lipeleke mrundo wa vitu.

Gharama nyingine ipo kwenye vitabu.

Ingawa vitabu vya CBC bei yake ni ya wastani, kila mzazi hutakiwa kununua angalau vitabu kumi na kimoja.

Hata somo la mazoezi ya viungo (PE) limeandikiwa kitabu.

Katika mfumo wa sasa, mbali na vitabu wazazi huitishwa vitu vingi. Kuna udongo wa kununuliwa madukani, kuna makasi, nyuzi na vitu vingine vingi.

Walimu bila kujali hali ya kifedha ya wazazi, hutaka vifaa vyote vipatikane kwa wakati mmoja.

Mtu yeyote anayeelewa taaluma ya ualimu anatambua kwamba, vifaa vyote haviwezi kutumika kwa pamoja.

Kwenye mpango wa ufundishaji, Mwalimu hufundisha jambo moja kwa kipindi. Iwapo wanafunzi watakuwa hawajaelewa, humbidi arejelee somo hilo au afanye marudio mafupi kabla ya kusonga mbele.

Kuwaitisha wazazi kila siku ni usumbufu unaoweza kuepukwa.

Wizara ya Elimu katika kupanga ratiba ya mihula, imeongeza masaibu kwa wazazi kwa kuwa na mapumziko mafupi.

Mzazi kumtumia mwanawe nauli aende nyumbani wikendi pekee kwa mapumziko kisha arejee shuleni ni gharama isityostahili.

Wakati huu ambapo watu wanakabiliwa na gharama ya masisha kutokamna na Covid-19, ni muhimu kwa wadau kufikiri upya jinsi ya kuondoa usumbufu kwenye mfumo wa CBC.

TAHARIRI: Polisi wakabiliane na sarakasi za siasa

KITENGO CHA UHARIRI

SARAKASI na fujo zilizoshuhudiwa katika Kaunti ya Nyeri jana wakati wa ziara ya Naibu Rais William Ruto hazikustahili.

Dkt Ruto na wafuasi wake walidai kushambuliwa na kurushiwa mawe na watu waliowashuku kuwa wafuasi wa Mbunge wa eneo la Kieni, Kanini Kega.

Baadhi ya wakazi wa Nyeri waliyakana madai hayo, wakisema waliwaona vijana ambao mara kwa mara huandamana na Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua kwenye misafara yake.

Hatuna namna ya kuyathibitisha madai ya pande zote mbili.

Kwa hivyo, tutajikita zaidi kwenye matukio yenyewe.

Msimu wa siasa, wanasiasa hutumia kila mbinu kuungwa mkono na wapigakura, ikiwemo kuzua fujo au kubuni matukio ya kuwafanya waonewe huruma.

Vyovyote iwavyo, ghasia, fujo au watu kudai eneo fulani ni lao na mwanasiasa wasiyekubaliana naye kifikra hafai kulizuru, ni mambo yanayofaa kukemewa.

Katiba inaruhusu na kukubali Mkenya kuwania uongozi na kuomba kura katika pande zote za nchi, hasa akiwa anawania urais.Dkt Ruto ameshatangaza kwamba atakuwa debeni Agosti 2022.

Kujitokeza katika maeneo ya nchi kuomba kura ni haki yake. Kama kweli waliomrushia mawe walikuwa wa upande wa viongozi wa mrengo wa Kieleweke, basi hayo ni makosa.

Licha ya yeye, hata Kinara wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na wengine ambao hawajatangaza azma zao, wana haki ya kuzuru Nyeri na kwingineko Kenya.

Lakini pia kama ni kweli viongozi wa mrengo wa Tanga Tanga walibuni tukio hilo ili kujinufaisha kisiasa, basi wakome.

Siasa sawa na dini, huibua hisia kali miongoni mwa wananchi. Mtu kwa kuunga mkono upande mmoja wa siasa, anaweza kusahau ukoo na kutengana na jamaa zake. Huhitaji kuchochewa kidogo tu ili kulipuka.

Kwa hivyo wanasiasa wanapaswa kuwa makini na kuepuka visa vyovyote vya kuibua hisia za wananchi.

Aidha, idara za usalama twazihimiza zichunguze matukio kama ahaya na kuchukua hatua hadharani, ili watu wengine wenye nia ya kusababisha fujo wapate funzo.

TAHARIRI: Serikali isuluhishe uhaba wa walimu

KITENGO CHA UHARIRI

JUHUDI za Waziri wa Elimu Prof George Magoha kuhakikisha wanafunzi wa Kidato cha Kwanza wamesajiliwa katika shule za upili hivi majuzi ni za kupongezwa hasa wakati huu ambapo baadhi ya wazazi wamekabwa na ukosefu wa karo kutokana na athari ya janga la corona na njaa.

Waziri Magoha wiki hii alionekana akiwa katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Pwani na Magharibi kukagua kiwango cha wanafunzi waliopelekwa shuleni za sekondari walikopata nafasi.

Hii ni kuendana na lengo kuu la serikali kuhakikisha kwamba kila mwanafunzi anapata masomo ya sekondari ambayo imeyafadhili. Ili kufikia lengo hili, wazazi wameagizwa wawapeleke watoto wao shuleni huku machifu wakitwikwa jukumu la kuhakikisha amri hiyo imetekelezwa kikamilifu.

Maafisa hawa wanatakikana wawafichue wanaokaidi ili kuchukuliwa hatua faafu kisheria.

Ingawa hatua hii ya serikali ni ya kutia moyo hasa kwa watoto kutoka kwa familia maskini, ripoti kuhusiana na upungufu wa walimu wa baadhi ya masomo ni jambo la kusikitisha na kutaumsha kweli kweli.

Katika mojawapo ya taarifa zetu za toleo la leo, imefichuka kwamba shule 27 nchini zimeathirika kabisa na uhaba wa walimu wa baadhi ya masomo na huenda masomo hayo yakaacha kufunzwa kabisa.

Baadhi ya masomo haya ni ya lazima kama vile Hisabati na Kiswahili. Uhaba huu ulisababishwa na waliosomea ualimu kukosa kutuma maombi ya kazi katika shule hizo husika.

Wengine walituma lakini hawakufika kwa mahojiano hata baada ya kualikwa. Kwingineko, waliohojiwa walikosa kufikia viwango vya kuhitimu vilivyohitajika.

Shule zinazoathirika zinapatikana katika kaunti za Laikipia, Siaya, Nakuru, Kisumu na Kakamega.Ingawa serikali kupitia Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ilitimiza jukumu lake la kutenga fedha katika bajeti kugharimia uajiri wa walimu 8,914 mwaka huu 2021, ili kukabiliana na uhaba ulioko nchini, tatizo la shule kadhaa kupuuzwa linafaa kuvaliwa njuga na likabiliwe ipasavyo.

Ni wajibu wa wataalamu wa elimu katika wizara kuhakikisha kuna walimu wa kutosha nchini na fauka ya haya kuhakikisha kuna usawa katika uajiri ambapo kila shule itapata walimu wa kutosha bila kujali eneo, kaunti ndogo au kaunti.

Serikali kupitia wizara ya Elimu iibuke na mikakati mahususi kuhakikisha walimu wanapelekwa shuleni ambazo zinakabiliwa na upungufu bila kujali ziko mashambani, vijijini, mashinani au mijini.

Si ajabu kwamba kuna baadhi ya shule ambazo zina walimu wa ziada huku nyingine zikiendelea kuhangaika.

Ni sharti serikali itimizie kila mwanafunzi haki ya kusomeshwa na kupata elimu kwa usawa bila kubagua la sivyo itaonekana kama serikali inayoendeleza maonevu dhidi ya watoto wake.

Hili linawezekana kwani penye nia pana njia. Kazi kwako Profesa Magoha!

TAHARIRI: Spoti: Serikali iwazie miundomsingi zaidi

KITENGO CHA UHARIRI

HERI nusu shari kuliko shari kamili; hiyo ndiyo tamathali inayofaa kuambiwa serikali ya Jubilee.

Ni msemo unaohitaji kuzingatiwa katika masuala ya ukuzaji wa michezo nchini hasa kuhusiana na miundomsingi.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto, mnamo 2013 na 2017, kama njia ya kujipigia debe ili wachaguliwe katika nyadhifa hizo kuu, waliahidi wananchi makuu, yakiwemo yanayohusiana na viwanja na miundomsingi mbalimbali ya michezo.

Rais aliahidi kujenga angaa viwanja vitano vyenye hadhi ya kimataifa mbali na kujenga vingine vyenye hadhi kuu katika kila mojawapo ya kaunti 47 nchini.

Hali ilivyo sasa ni kwamba taifa hili linajivunia uwanja mmoja pekee wenye hadhi ya kimataifa ambao unaweza kutumiwa kuandaa mashindano ya kimataifa – uwanja huo ni Kasarani.

Uwanja mwingine wenye hadhi japo hauwezi kutumiwa kwa mashindano ya hadhi kubwa ni Nyayo.

Hivi ndivyo viwanja maarufu nchini. Kinaya kikuu ni kwamba ni viwanja vilivyojengwa zamani sana, katika enzi ya rais wa pili wa Kenya, marehemu Daniel Toroitich arap Moi.

Katika enzi ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki, kisha mrithi wake Rais Uhuru, hakuna uwanja wowote wa thamani uliojengwa.

Hiki kwa hakika ni kinaya kwa sababu uchumi wa Kenya katika enzi za watangulizi wa Rais Uhuru, ulikuwa chini.

Kwa sasa taifa hili lina bajeti ya takribani Sh3 trilioni ilhali linashindwa kujenga uwanja wowote wa ziada.

Kinachosikitisha hata zaidi ni kuwa mataifa yenye uchumi mdogo ukilinganisha na Kenya mathalani Rwanda na Tanzania, yanajivunia miundomsingi ya hadhi.

Inapozingatiwa kuwa Rais Uhuru anastaafu mwaka ujao wa 2022, inavunja moyo zaidi kuwa hata uwanja mmoja kati ya hivyo vitano alivyoahidi, haujajengwa. Ndiyo maana tunasema, heri nusu shari kuliko shari kamili.

Heri Rais angeisukuma serikali yake kujitahidi kujenga angaa uwanja mmoja wa hadhi hiyo. Kwa kufanya hivyo, ataeleweka kwa urahisi atakapotaja changamoto zilizomzuia kumudu ujenzi wa viwanja hivyo.

Naam, twafahamu kwamba serikali kadhaa za kaunti chini ya utawala wa Rais Uhuru zimejenga viwanja vya hadhi ya kujivunia.

Hata hivyo, itakuwa bora zaidi iwapo serikali kuu itajaliza juhudi za kaunti hizo kwa kuwapa Wakenya uwanja mmoja wenye thamani kubwa.

TAHARIRI: Serikali ikabili baa la njaa mapema

KITENGO CHA UHARIRI

RIPOTI kwamba janga la njaa tayari limeanza kukatiza maisha ya Wakenya kaunti 12 zikiathirika, ni suala la kuhofisha na linalofaa kuchukuliwa kwa uzito na viongozi nchini.

Vile vile hatua za dharura zinafaa kutekelezwa kwa haraka.

Kwa kawaida, kila mara zinapochipuka taarifa kuhusu vifo kutokana na njaa, serikali hukimbia kuzipinga huku ikijiondolea lawama.

Aidha hakuna takwimu kuhusiana na idadi ya waliofariki au kuathirika na njaa.

Si ajabu wakati mwingine maafisa wa serikali hutoa taarifa ya jinsi walivyo tayari kupambana na baa la njaa ilhali kwa hakika huwa ni siasa na ahadi tupu za kuwafunga wananchi macho.

Maisha ya Mkenya mmoja yanapopotezwa yana thamani kubwa kiasi kwamba kila mbinu inafaa kutumiwa kuyalinda.

Hii ni kwa sababu yanapotoweka, hakuna njia hata moja inayoweza kutumika kuyarerejesha tena upya.

Wakati mwingine serikali huwa inasubiri hadi pale watu kadhaa wanafariki na janga la njaa kukithiri ndipo ianze kuchukua hatua za kuokoa raia wake.

Utaona serikali ikitegemea mashirika yasiyo ya serikali kama Red Cross, World Vision kuwafaa waathiriwa huku ikiwatazama tu!

Miaka ya hapo nyuma Wakenya walionekana kuungana pamoja kuchangia wenzao ili kuwanusuru kutokana na makali ya njaa.

Tayari vifo kutokana na njaa na ukosefu wa maji vimeripotiwa katika Kaunti ya Samburu. Hali ya ukame imetajwa maeneo ya Kaskazini Mashariki, Pwani na Mashariki mwa Kenya.

Maeneo mengine ni Turkana, Baringo na Bonde la Ufa kwa ujumla ambapo wanyama wa mifugo kadhaa wamefariki kutokana na kiangazi kikali. Si siri kwamba mifugo ndio asili ya mlo na tegemeo la kifedha la wafugaji nchini.

Ni haki ya Wakenya kupewa hakikisho la usalama wa chakula. Pia ni haki ya kila Mkenya kupata maji safi.

Kwa upande mwingine ni jukumu la serikali kulinda raia wake dhidi ya njaa. Vivyo hivyo inafaa kutoa maji safi kwa wananchi bila kushurutishwa.

Kutokana na miradi duni iliyoanzishwa na serikali kuu, zikiwepo zile za kaunti, baadhi ya Wakenya wamejipata katika hali ya kusononeka kwa madhara ambayo hawajui asili wa fasili yake.

Mingi ya miradi ya mabwawa nchini ilizinduliwa miaka kadha iliyopita na fedha nyingi kuwekezwa humo lakini matokeo yake yamekuwa ya kusikitisha. Badala ya miradi hii kukamilishwa na kufaidi wakazi, hatimaye husambaratika na mamilioni kuishia katika mifuko ya watu binafsi kwa misingi ya ufisadi.

Miradi mingine ya unyunyiziaji maji mashamba nchini ilipitia mkondo huo huo na kuacha raia na matumani hewa.Serikali ziungane mara moja kuokoa maisha ya Wakenya kutokana na makali ya njaa sasa hivi.

Mikakati ya kukomesha janga hili kabisa ifufuliwe na kukelezwa. Taifa linaloheshimiwa ni lili linalowajali raia wake hasa kuwatosheleza mahitaji ya kimsingi ikiwepo hitaji la chakula.

TAHARIRI: Serikali isidunishe uvaaji sare shuleni

KITENGO CHA UHARIRI

JUHUDI za serikali kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi na upili zinafaa kupongezwa.

Serikali imedhihirisha kwa vitendo kwamba inathamini elimu.

Waziri wa Elimu George Magoha amekuwa mstari wa mbele kuwasaka watoto ambao kufikia leo hawajaenda shuleni, karibu mwezi mzima tangu wenzao wajiunge na Kidato cha Kwanza.

Prof Magoha alipigwa na butwaa katika Kaunti ya Mombasa, alipowaona vijana wawili waliopata kati ya alama 350 na 395 wakiwa wangali nyumbani.

Picha zilimuonyesha waziri akiwa kwenye nyumba ya matope ya chumba kimoja, ambamo msichana aliyepata alama 355 alikuwa hajaenda shuleni kwa sababu ya matatizo ya kifedha nyumbani kwao.

Tukio hilo lilimthibitishia waziri yale ambayo Taifa Leo tumekuwa tukiyaangazia kuwahusu wanasiasa.

Viongozi wengi wamekuwa wakitumia basari na pesa nyingine za hazina wanazosimamia, kuwatuza wapambe wao wa kisiasa, watu waliowafanyia kampeni, marafiki, washirika katika biashara na matajiri walio na uwezo wa kulipa hata karo ya mwaka mzima.

Kama si hivyo, basi ilikuwaje mtoto aliyepata alama 394 au huyo wa 355 hakufanikiwa kupata basari katika eneobunge lake?

Mbali na basari ya mbunge, kuna basari ya kaunti. Hizo zote pamoja na wabunge wawakilishi wa kike hazikupatikana.Wasimamizi wa basari wanadai kwamba ili mtoto kupata ufadhili, ni sharti awe alisoma katika shule ya msingi ya umma.

Fikra hizo ni za kutaka kuonyesha kuwa wazazi wa mtoto aliyesoma shule ya kibinafsi wana uwezo. Si kweli. Hali ya maisha hubadilika. Covid-19 iliathiri biashara na shughuli mbalimbali.

Ingawa serikali inafanya kazi nzuri ya kuhakikisha watoto wote wamefika shuleni, yapaswa kutenga pesa za kuwanunulia sare wale walio na hali ngumu kabisa. Kuwaamuru walimu wakuu wawapokee wanafunzi wote hata kama hawana sare, si suala la busara.

Shule ni pahali ambapo watoto wote hutakiwa wawe sawa kupitia sare.

Kufanya hivyo hufanya iwe rahisi kwa walimu kuwatambua wanafunzi wao, hata kunapokuwa na mkusanyiko wa shule mbalimbali.

Kuvaa sare pia huepusha wahuni na watu wasiokuwa wanafunzi kuingia shuleni.

Kwa hivyo serikali itafute mbinu nyingine za kuwasaidia watoto maskini, lakini si kusoma bila ya sare.

TAHARIRI: Heko chipukizi kuitawala dunia

KITENGO CHA UHARIRI

KUKAMILIKA kwa mashindano ya vijana wasiozidi umri wa miaka 20 kumerejesha tabasamu nyusoni mwa Wakenya.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa humu nchini na kuyaleta pamoja mataifa ya ulimwengu, yamedhihirishia dunia kwamba Kenya ingali hodari katika riadha.

Kinyume na mambo yalivyokuwa kwenye Olimpiki jijini Tokyo, Japan, chipukizi wetu walijikakamua na kumaliza katika nafasi ya kwanza.

Vijana hao walizoa jumla ya nishani tisa za dhahabu, moja ya fedha na saba za shaba.

Kivumbi hicho kilifanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika na mataifa hodari kama vile Jamaica, Ethiopia, Botswana, Uganda kati ya mengine, hayakuwa na chao mbele ya chipukizi wetu.

Labda wasiotupenda watasema kwa kuwa mcheza kwao hutuzwa, vijana wetu walistahili kushinda. Huo si ukweli.

Ushindani uliotoka kwa nchi mbalimbali, ulionyesha kuwa hapakuwa na suala la vijana wetu kuwa kwao nyumbani.

Walijitolea na kupambana, hasa walipokaribia kwenye utepe.Mafanikio haya yanatuonyesha kuwa tunapofanya maandalizi mazuri na tukaweka malengo yetu ipasavyo, hakuna linalotushinda.

Vijana hao wametuletea fahari kama taifa. Walipokuwa wakishinda na wimbo wetu wa taifa ukiimbwa, mara moja tulisahau tofauti zetu za kisiasa na kudondokwa na machozi ya furaha.

Michezo ni kiungo muhimu katika kuwaleta watu pamoja, kujenga undugu wa kweli na kumaliza tofauti ndogo ndogo.

Wizara ya Michezo chini ya waziri Amina Mohammed inapaswa kushirikiana na ile ya Elimu, kutambua vipaji vingi katika shule za msingi na upili.

Ingawa janga la Corona limesimamisha michezo katika shule zetu, wadau wa wizara za Elimu, Michezo na Afya wanapaswa kutafuta mbinu za kuendeleza mashindano shuleni.

Wakufunzi, bila ya ubaguzi au mapendeleo, wazunguko katika kaunti zote 47 kutambua vijana walio na vipaji katika riadha pamoja na michezo mingine.

Kufanyika kwa mashindano haya katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani bila shaka kumetoa fursa kwa ulimwengu kuona viwanja vyetu.

Serikali iendeleze ujenzi wa viwanja vyenye hadhi ya kimataifa kama cha Kasarani, ili siku za usoni tuandae mashindano makubwa kama Olimpiki na hata Kombe la Dunia.

TAHARIRI: Mauaji ya vijana yatia hofu

KITENGO CHA UHARIRI

KWA muda wa wiki mbili, vijana sita wameuawa kwa njia ya kutatanisha kwenye visa tofauti nchini na kuibua hofu kwamba vijana wa nchi hii wako kwenye hatari kubwa.

Familia mbili zimeongezwa katika orodha ya zile zinazopokonywa vijana waliokuwa na matumaini makubwa kwao na hata kwa nchi.

Kaka wawili waliouawa baada ya kukamatwa na maafisa wa polisi katika kijiji cha Kianjakoma, kaunti ya Embu kwa kukiuka kafyu walikuwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Naam, familia ilipokonywa wavulana wawili iliyotumia nguvu, kujinyima na rasilmali ili kuwapa elimu bora.

Ingawa uchunguzi kuhusu jinsi wawili hao walivyokufa unaendelea, polisi hawawezi kuepuka kidole cha lawama.

Kabla ya Wakenya kusahau mauaji ya vijana hao, familia nyingine eneo la Syokimau inaomboleza baada ya vijana wawili kuuawa kikatili kaunti ya Kajiado kwa madai finyu kwamba walikuwa wezi wa mifugo.

Kulingana na polisi, hakukuwa na mifugo walioibwa eneo hilo wakati huo na isitoshe, vijana hao walikuwa na pikipiki ambazo haziwezi kubeba ng’ombe.

Vijana wa mama mmoja, ambao walikuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa ya rafiki yao. Kwamba vijana hao walioondoka katika nyumba yao ya kifahari waliuawa kwa kushukiwa kuwa wezi wa mifugo katika eneo lililo na maafisa wa usalama na utawala ni jambo la kuatua moyo.

Visa hivi na vingine vya vijana kutekwa na kutoweka, kuuawa kwa kupigwa risasi kiholela na maafisa wa polisi kwa kudaiwa kuhusika na uhalifu bila ushahidi vinatoa mwelekeo hasi kwa jamii tunayoishi. Mwelekeo ambao ni hatari kwa usalama wa taifa na jamii kwa jumula.

Vijana, ambao ni tegemeo la nchi siku zijazo wakiangamizwa na maafisa wa polisi wanaofaa kuwalinda ni ishara ya nchi isiyojali ustawi wake.

Ni sawa na kukatiza siku zijazo za nchi. Ni mtindo unaofaa kuzimwa. Awali ilikuwa ni vijana kutoka mitaa ya mabanda inayoishi watu masikini waliouawa na polisi kwa kushukiwa kuhusika na uhalifu lakini sasa, hali imebadilika hivi kwamba hata wale wa matabaka ya juu, walio na taaluma zao wanauawa na polisi.

Hii inawafanya vijana kuwachukulia maafisa wa usalama kuwa maadui. Maafisa wa polisi wanafaa kufahamu kuwa vijana wanaoua kiholela ni sawa na watoto na ndugu zao.