Rais aongoza Wakenya kuomboleza seneta aliyefariki kwa ajali

Na Mary Wangari

VIONGOZI na wanasiasa mbalimbali wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na naibu wake, Dkt William Ruto jana waliungana na Wakenya kumwomboleza Seneta Mteule, Victor Prengei, aliyefariki katika ajali ya barabarani.

Kupitia kwa taarifa kwa vyombo vya habari, Rais Uhuru alimtaja marehemu kuwa kiongozi shupavu aliyejitahidi kuboresha maisha ya vijana na jamii za wachache nchini.

“Inahuzunisha sana kuwa kifo kimetupoka kiongozi hodari na mchanga aliyejitahidi kuimarisha maslahi ya vijana na jamii za wachache,” taarifa ikasema.

Seneta huyo wa Chama cha Jubilee aliaga dunia baada ya kuhusika kwenye ajali Jumatatu, saa tatu na robo usiku, kwenye barabara ya Kabarak-Nakuru.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyoonwa na Taifa Leo, gari la Bw Prengei lilipoteza mwelekeo katika eneo la Kioto, kabla ya kuyumbayumba na kugonga ukuta.

Seneta huyo aliyekuwa amejeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Moi Memorial ambapo alikata roho alipokuwa akitibiwa.

Marehemu alikuwa miongoni mwa maseneta sita waliofikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu katika chama cha Jubilee mapema mwaka huu.Kupitia rambirambi zake, Naibu Rais alimtaja marehemu kama kiongozi aliyejitolea mhanga kutetea haki za walio wachache.

“Taifa letu limempoteza mwanamme muungwana. Seneta Victor Prengei alikuwa mpole na mtumishi wa umma aliyejitolea kuendeleza maslahi ya walio wachache,” alisema.

Huku akifariji familia na jamaa wa marehemu, Kiongozi wa ODM Raila Odinga alimwomboleza Seneta Prengei akisema “kifo chake cha ghafla ni pigo kuu kwa jamii ya Ogiek na bunge.”

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alituma rambirambi zake akisema jamii ya Ogiek, Seneti na taifa kwa jumla limempoteza kiongozi aliyewakilisha matumaini makubwa.

Akielezea kushtshwa na habari hizo, Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula alisema Bw Prengei alikuwa muundasheria aliyekuwa na uhusiano mwema na wenzake katika seneti huku akitoa wito kuhusu kuimarisha usalama barabarani.

Kwa upande wake, Seneta Mteule Millicent Omanga alimwomboleza marehemu akisema kuwa juhudi zake zitakumbukwa milele.Seneta wa Nakuru Susan Kihika alimtaja marehemu kama rafiki na “mwakilishi wa vijana mwenye unyenyekevu aliyewakilisha wanajamii walio wachache katika Seneti.”

“Kaka yangu.Hii inaumiza sana. Maisha ni nini hasa? Upo hapa leo kesho umeenda. Mwenyezi Mungu aingilie kati…,” aliomboleza Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot..

WANDERI KAMAU: Buriani mhariri wetu mahiri Mauya Omauya

Na WANDERI KAMAU

HUJAMBO msomaji?

Kwa kawaida, nafasi hii huwa ya mwandishi Mauya Omauya kila Ijumaa, ambapo huwa anaandika makala kuhusu masuala mbalimbali kama siasa, historia, falsafa na mahusiano ya kimataifa.

Hata hivyo, nina moyo mzito kuandika makala haya kumhusu, kwani hayupo nasi tena duniani. Bw Mauya alifariki Jumatatu katika mtaa mmoja jijini Nairobi baada ya kuzimia ghafla.

Ripoti ya upasuaji wa mwili wake ilionyesha alifariki kutokana na matatizo ya moyo.

Wakati wa kifo chake, Bw Mauya alikuwa mhadhiri wa masuala ya mawasiliano na mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Moi.

Alikuwa na shahada ya uzamili katika Mahusiano ya Masuala ya Kimataifa kutoka chuo cha School of African Oriental Studies (SOAS), London, Uingereza.

Kando na kuwa mwanahabari, alikuwa msomi, mwandishi na mhariri maarufu, ambapo kando na magazeti ya Kenya, alikuwa akichambua siasa katika magazeti ya kimataifa kama China Daily.

Kama msomi barobaro, kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya uanahabari na usomi nchini.

Kwa muda ambao nilitangamana naye – kati ya 2013 na 2014 – Bw Mauya alidhirisha uelewa mpevu na wa kipekee kuhusu matukio mbalimbali duniani.

Kama msomi, hungemkosa bila kitabu ama kijarida. Alivipenda, akivitaja kuwa “chemichemi na mwanzo wa kuifahamu dunia.”

Bw Mauya pia alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki aina ya Rhumba na waandishi wa Kiafrika.

Katika maandishi yake, hangekosa kumnukuu mwandishi Chinua Achebe, hasa novela ya ‘Things Fall Apart’ (Mambo Huangamia).

Alishikilia kuwa waandishi wa fasihi ya Afrika ndio walioifahamisha dunia nzima kuwahusu Waafrika – tamaduni zao, siasa zao na mpangilio wa kijamii.

Kutokana na imani yake kubwa kuhusu Uafrika, ukombozi na mustakabali wake, alikuwa na mazoea ya kuvaa kijikofia kilichovaliwa na wanasiasa maarufu kama vile Mzee Jomo Kenyatta, Jaramogi Oginga Odinga, Kwameh Nkrumah kati ya wengine.

Sifa yake nyingine ni kwamba alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki wa Reggae.

Aliwapenda wanamuziki walioimba nyimbo zenye maudhui ya ukombozi wa Mwafrika kama Bob Marley, Peter Tosh, Lucky Dube, na Joseph Hill (Mighty Culture).

Mkasa mkuu katika maisha yetu ni kwamba kifo ni sehemu ya matukio tutakayokumbana nayo, kulingana na mwandishi Haruki Murakami kutoka Japan.

Ingawa kifo kimekuwa kikionekana kama mkasa katika maisha ya mwanadamu, imebidi tukubali uhalisia wake, kwani ni njia inayopitiwa na kila kiumbe aliye hai.

Kifo huliza na huatua moyo. Huwa kinavuruga mipango na mielekeo ya maisha yetu. Ni adui tusiyemwepuka hata kidogo.

Tulipotangamana naye akiwa mhariri, alinichochea sana kurudi chuoni kujikuza kimasomo kutokana na ufahamu mpevu aliokuwa nao kuhusu siasa za kimataifa.

Licha ya kuondoka baada ya kuhudumu kama mhariri, tuliendelea kutangamana naye, hasa mitandaoni, nikimwomba mwongozo kuhusu masuala mbalimbali ya kiakademia.

Kama mwalimu na mwanafunzi wake, Bw Mauya alikuwa mwenye roho safi, mjalifu, mwenye huruma na mpenda watu.

Daima, hakujiweka kwenye hadhi ya kiusomi, bali alikuwa tayari kuzungumza na kucheka na yeyote aliyekuwa karibu naye.

Ni Mungu hutoa na ndiye huchukua. Tutamkumbuka daima. Mola amlaze penye wema. Amin.

akamau@ke.nationmedia.com

Raila amwomboleza mwanahabari shupavu Philip Ochieng’

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ameomboleza kifo cha mwanahabari mkongwe Philip Ochieng’ akimtaja kama mtaalamu aliyechochea mabadiliko katika jamii kupitia kazi zake.

Kupitia ujumbe katika akaunti zake za mtandao wa kijamii, Bw Odinga alisema Kenya imempoteza mwanahabari wa kupigiwa mfano na mwenye ufasaha katika lugha ya Kiingereza.

“Kupitia weledi wake katika uandishi, Philip aliongelesha watu wetu mamlaka makuu na kuwafanya wanajamii kuchua hatua mbali mbali zenye faida kwa. Alikuwa mwalimu na mshauri wa jamii kupitia kazi zake,” Waziri huyu mkuu wa zamani akasema.

“Philip aliandika mawazo yake na kuwapa sauri wale wasio na usemi. Natuma rambirambi zangu kwa familia na marafiki na jamii ya wanahabari kwa ujumla. Mungu aiweke roho yake pema penye amani,” Bw Odinga akaongeza.

Naibu Rais pia aliwasilisha rambirambi zake akimtaja marehemu Ochieng’ kama mwanahabari ambaye alikuwa na uelewa mpana wa masuala katika nyanja zote za maisha.

“Alikuwa mweledi katika sarufi ya kiingereza na alikuwa nafasi yake magazeti ambapo alitufunza mambo mapya kila mara. Ochieng’ ni mwanahabari msomi ambaye alielimisha wanajamii kupitia makala yake. Mungu aiweke roho yake pema pema wema,” akasema Dkt Ruto.

Familia ya marehemu Ochieng ilithibitisha kuwa mwanahabari huyo mweledi alifariki nyumbani kwake Awendo, kaunti ya Migori baada ya kuugua ugonjwa wa “pneumonia”.

Marehemu alikuwa alikuwa akiandika makala katika gazeti la Sunday Nation ambapo alitumia lugha ya kipekee ya Kiingereza. Makala yake ilijulikana kama “The Fifth Columnist”.

Miaka mingi hapa nyuma marehemu Ochieng’ alihudumu kama mhariri wa magazeti ya Daily Nation na Sunday Nation.

Wakenya wamwomboleza Philip Ochieng’

NA NYAMBEGA GISESA

Wakenya wanaendelea kumwomboleza mhariri na mwandishi mashuhuru wa Makala Bw Philip Ochieng.

Bw Ochieng, 83 ambaye alisomea katika Shule ya Upili wa Alliance alikufa siku ya Jumatano usiku nyumbani kwake Awendo kaunti ya Migori.

Kifo chake kilidhibitishwa na wanafamilia wake ambao walisema kuwa aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa Nimonia.

Viongozi na waandishi mbalimbali wanaendelea kutuma rambirambi zao kufuatia kifo cha mzee huyo ambaye alikuwa na uweldi wa kipekee katika uandishi wa magazeti.

Kifo chake kimewatia majonzi waandishi ambao alikuwa kielelezo kwao. Wanamsifu kutokana na kujitolea kwake na kuwapa mwelekeo katika uandishi.

“Ulinifunza kupenda uandishi na uwanahabari. Uliwashauri na kuwa kielelezo kwa wengi. Ulinipa vitabu viwili; ‘Kenyatta Succession’ na ‘I Accuse the Press’. Ulikuwa msomaji wa makini na mwandishi mashuhuri. Kwaheri Mzee”. Mharirir msimamizi wa Makala maalim katika gazeti la ‘Nation’ Bw John Kamau alimwomboleza.

Kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga pia alituma rambirambi zake akimsifu kuwa mwandishi aliyetangamana na wengi kupitia kalamu.

Kitabu cha ‘The Fifth Columnist’ kilichoandikwa na mfanyikazi mwenzake wa Nation Liz Gitonga- Wanjohi kimeangazia kwa kina maisha ya awali cha Bw Ochieng.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya Sekondari, Bw Ochieeng alienda ng’ambo kuendelea na masomo yake ya Chuo Kikuu.

Amefanya kazi katika Chumba Cha Habari ya Nation Center kama mhariri na mwandishi wa magazeti.

Kati ya Septemba 1988 na Septemba 1991, Bw Ochieng alifanya kazi kama mhariri mkuu wa Kenya Times na hata kujishindia ulinzi wa lango la utawala wa Kanu.

Miaka kadhaa baada ya kutoka kwenye chumba cha habari, Rais wa zamani Mwai Kibaki alimpa agizo la kuwa mshika dau mkuu (OBS) kutokana na kazi yake maalum ya Sunday Nation.

TAFSIRI Na WINNIE A ONYANDO

TANZIA: Mhariri wa zamani wa Taifa Leo afariki

Na LEONARD ONYANGO

MHARIRI msanifishaji wa zamani wa gazeti la Taifa Leo Dennis Geoffrey Mauya, maarufu Mauya Omauya, amefariki baada ya kuzimia ghafla mtaani Donholm, Nairobi.

Kulingana na jamaa zake, Mauya alizimia na kufariki papo hapo Jumatatu mchana, alipokuwa akitoka dukani, mita chache kutoka Kituo cha Polisi cha Savannah, Donholm.

Maafisa wa polisi walifika katika eneo la tukio na kupeleka mwili katika mochari ya Hospitali ya Mama Lucy Kibaki. Lakini saa chache baadaye familia iliwasili na kuhamishia mwili katika Mochari ya Chiromo.

“Nilimpigia simu Mauya lakini ikapokelewa na afisa wa polisi ambaye aliniambia kwenda katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki baada ya kumfahamisha kwamba nilikuwa ndugu yake,” akasema Bw Sam Kiyaka, kaka yake mwendazake.

Kulingana na Bw Kiyaka, Omauya amekuwa akiishi mtaani Zimmerman kwa muda wa miezi minne iliyopita.

“Alikuwa akiishi kwangu mtaani Zimmerman baada ya kutofautiana kidogo na mkewe. Jumatatu asubuhi aliondoka kwenda kutembelea watoto wake wawili na mkewe mtaani Donholm na baadaye alifaa kwenda katikati mwa jiji la Nairobi kununua miwani.

“Lakini hatujui ikiwa alifika au alizimia akiwa njiani kuelekea huko. Hatujui alizuru maeneo yapi kati ya saa 2.00 asubuhi na saa 1.00 mchana alipopatikana akiwa amefariki ,” akasema Bw Kiyaka.

Polisi wanashuku kuwa huenda Omauya alifariki kutokana na matatizo ya kushindwa kupumua kutokana na ugonjwa wa corona.

“Tuna hakika kwamba hakuuawa na corona kwani alidungwa chanjo ya AstraZeneca wiki mbili zilizopita,” akasema Bw Kiyaka.

Mauya alijiunga na kampuni ya Nation Media Group (NMG) kama mhariri msanifishaji wa gazeti la Taifa Leo mnamo 2007. Baada ya kufanya kazi kwa mwaka mmoja, alipata ufadhili na kwenda kusomea Masuala ya Kimataifa, Mawasiliano na Diplomasia kiwango cha Uzamili katika Chuo Kikuu cha London, Uingereza.

Baada ya kukamilisha masomo yake, Mauya alirejea tena katika kampuni ya NMG ambapo aliendelea na majukumu yake ya mhariri msanifishaji wa Taifa Leo kati ya 2012 na 2014.

Baada ya kuondoka NMG alienda kufundisha katika vyuo vikuu vya Moi, Nairobi na Karatina. Omauya amekuwa akiandika maoni ambayo yamekuwa yakichapishwa katika gazeti la Taifa Leo kila Ijumaa.

Omauya pia alikuwa mtafiti na mwandishi wa gazeti la China linaloangazia masuala ya Afrika, ‘ChinAfrica’.

Wanahabari wa gazeti la Taifa Leo, wakiongozwa na Mhariri Mkuu Peter Ngare, walimtaja Mauya kama mchapa kazi, mwaminifu, mpenda haki na mweledi wa masuala ibuka ya humu nchini na ngazi ya kimataifa.

Koinange alikuwa kiongozi wa kuaminika, UhuRuto wamwomboleza mbunge

NA MWANGI MUIRURI

MKUKI katili wa mauti umerejea tena katika bunge la kitaifa na kumvuna mbunge wa Kiambaa Bw Paul Koinange baada ya kuugua ugonjwa wa Covid-19—ugonjwa ambao umeonekana kuwa na makali ya kipekee dhidi ya wanasiasa ambao wamegongwa kwa kiwango kikuu na mauti pamoja na maambukizi.

Bw Koinange aliaga dunia Jumatano asubuhi katika hospitali ya Nairobi na ambapo Rais Uhuru Kenyatta alimwomboleza kama kiongozi wa kuaminika na aliyekuwa na maono thabiti kuhusu wema wa nchi hii.

Alimmtaja mwendazake kama aliyetegemewa katika harakati za kuunganisha taifa na ambapo bungeni, alikuwa mwenyekiti wa kamati kuhusu Utawala na Usalama wa Kitaifa.

Amekuwa mbunge wa Kiambaa tangu 2013 na ambaye alifahamika kwa usiri wa kimaisha kwa njia ya hali ya juu, uzalendo usiotingisika kuhusu taifa na uaminifu mkuu kwa rais na serikali yake.

Kwa msingi huo, Bw Koinange alikuwa ameapa hadharani kuwa “hakuna vile hata iwe namna gani mimi ninaweza nikamuunga mkono Naibu wa Rais Dkt William Ruto na hata siasa zigeuke kwa kiwango gani, wa Dkt Ruto ni mrengo ambao siwezi nikajiunga nao kamwe.”

Alisema kuwa Dkt Ruto alikuwa amemuaibisha katika eneo bunge lake akiwa katika mkutano wa hadhara “alipojifanya hata hanijui kwa jina na akauliza watu wangu huwa wananiita nini wala si nani, hii ikiwa ni baada ya hatua yangu ya kumwambia alikuwa anagawa Wakenya na kampeni zake za mapema na za kukaidi rais Uhuru Kenyatta katika mwito wake kwamba kwanza tuwahudumie Wakenya.”

Hata hivyo, Dkt Ruto amemwomboleza mwendazake kama “kiongozi shujaa na ambaye atakumbukwa na wengi kupitia ujasiri wake na ukakamavu katika huduma kwa umma.”

Katika mamlaka yake ya bunge, Bw Koinange aliungana na wengine ambao hivi majuzi walikuwa wamelenga kutunga sheria mpya za kuharamisha vuguvugu la Dkt Ruto la Hasla lakini kukazuka pingamizi kuu kutoka kwa hata kinara wa ODM Raila Odinga na washirika wake baada ya kuibuka kwamba ni mradi ungekuwa na madhara hasi kutoka kwa wapinzani wa Dkt Ruto.

Iliibuka kwamba sheria kama hiyo ingeonekana kama iliyolenga kuharamisha umasikini na ambayo ingezua mawimbi ya ukaidi miongoni mwa wengi nchini ambao kando na siasa, huishi maisha ya Uhasla.

Mauti ya Bw Koinange yanakuja wiki mbili tu baada ya aliyekuwa mbunge wa Kaunti jirani ya Juja Bw Francis Munyua Waititu kuaga dunia baada ya kuugua Kansa ya ubongo—haya yakiwa ni majonzi katika kaunti ya Kiambu yanayofuatana.

Kati ya 1968 na 1970 Bw Koinange alikuwa katika taasisi ya Tarkio nchini Marekani ambapo alijihami na taaluma ya Uzamili kuhusu masuala ya ujamii, Mazingira na siasa na kisha akahamia katika Jimbo la Ohio ambapo alizidisha masomo yake hadi uzamili wa Sheria za Kimataifa.

Mwaka wa 1972 alikuwa katika Wizara ya Spoti akiwa afisa wa nyanjani, kati ya 1974 na 1978 akiwa katika Wizara ya Leba akiwa naibu wa Katibu .

Mwaka wa hadi 1982 alikuwa katika Kampuni ya Mugawa Enteprises Ltd na Suncity Cinema Ltd akiwa Mkurugenzi, 1983 akiwa katika kampuni ya Video Tracts Revival, 1986 akiingia katika kazi ya ushauri katika safu za huduma za umma na za kibinafsi kabla ya kuchaguliwa kama mbunge wa Kiambaa mwaka wa 2013.

Rais Kenyatta atangaza siku 7 za kumwomboleza Magufuli, bendera nusu mlingoti

NA WANGU KANURI

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa risala za rambirambi kwa mkewe Rais Magufuli, Janet Magufuli, watoto wao, jamaa na taifa la Tanzania kufuatia kifo cha kiongozi wa nchi hiyo. Rais Kenyatta aliwahakikishia wanaTanzania kuwa wapo kwenye fikra na maombi yetu.

“Afrika na dunia kwa ujumla imempoteza kiongozi wa kupigiwa mfano ambaye uongozi wake, bidii na maono yake yalifanya nchi ya Tanzania kupiga hatua za maendeleo. Pia Bw Magufuli alipigania umoja wa wanajumuiya ya Afrika Mashariki. Katika nchi za bara, marehemu Magufuli alipigania muungano wa Afrika. Kifo chake kimemnyakua rafiki na kiongozi mwenzangu,” akasema Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta alisema anakumbuka wakati ambapo Rais Magufuli alizuru nchini Kenya kirasmi wakati wa uzinduzi barabara jijiniNairobi. Anakumbuka mazungumzo yao ambayo yalihusu maendeleo ya nchi zote mbili.

Alisimulia pia jinsi Bw Magufuli alisisitiza kwenda kumuona mamake Kenyatta, mama Ngina Kenyatta nyumbani kwao na akafunga safari ya kumtembelea almuradi amtoleee heshima.

Baada ya muda, marehemu Magufuli pia alimpeleka Rais Kenyatta kwao eneo la Chato, Geita, Tanzania na akamsalimu mamake Magufuli na kuongea naye kisha kulala kuko huko.

Safari hiyo iliwapa fursa ya kuzungumza mengi kuhusu uongozi wa nchi ya Kenya na Tanzania na pia uongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki kama wanachama.

Rais Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Jumuiya ya Afrika Mashariki ameagiza kuwa taifa la Kenya litatenga siku saba za kumuomboleza Bw Magufuli. Kwa wakati uo huo bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na ya nchi ya Kenya zitapeperushwa nusu ya mlingoti nchini Kenya na katika ubalozi wa Kenya kwa mataifa mengine.

“Bendera ya Kenya na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zitapeperushwa nusu mlingoti kutoka leo Machi 18, 2021 hadi machweo ya siku ambayo mwili wa rais Magufuli utakapozikwa. Bendera hizi zitapeperushwa katika majengo yote ya umma, nyanja zote za umma na katika ubalozi wa Kenya kwa mataifa mengine,” akasema rais Kenyatta.

Bw Magufuli alifariki Jumatano saa tano usiku huku ujumbe huu ukiwasilishwa naye makamu wa rais mheshimiwa Samia Suluhu. Magufuli alifariki baada ya kuugua ugonjwa wa moyo. Ameaga akiwa mwenye umri wa miaka 61.

Maisha yake

Mwendazake alizaliwa katika eneo la Chato, wilaya ya Geita kaskazini-magharibi mwa Tanzania mnamo Oktoba 1959 na alikuwa rais wa tano kuushika uongozi wa Tanzania tangu 2015 alipomshinda Edward Lowassa katika kinyang’anyiro kikuu nchini humo. Lakini hakulenga usiasa mwanzoni.

Magufuli alipata masomo yake yote nchini Tanzania na alikuwa mwalimu wa sayansi aliyefunza hisabati na kemia kisha baadaye akafanya kazi kama mkemia wa viwanda katika kampuni ya kumudu pamba la Nyanza, eneo la Mwanza kaskazini mwa Tanzania.

Aliteuliwa bungeni mnamo 1995, ambapo alihudumu kwenye baraza la mawaziri nchini Tanzania kama naibu Waziri wa Kazi kutoka mwaka wa 1995 hadi 2000, akahudumu kama Waziri wa Kazi tena kutoka mwaka wa 2000 hadi 2006, akahudumu kama Waziri wa Ardhi na Makazi ya Watu kutoka mwaka wa 2006 hadi 2008, akahudumu kama Waziri wa Mifugo na Uvuvi kutoka mwaka wa 2008 hadi 2010 na mwishowe akahudumu kama Waziri wa Kazi mara ya tatu mnamo mwaka wa 2010 hadi 2015.

Kama Waziri na kisha Rais, alipenda sana kupigiania utendaji bora kwa umma. Kampeni zake zililenga kukomesha ufisadi na kuziokoa fedha za umma pamoja na kulinda biashara za waTanzania.

Uongozi wa kwanza

Baada ya kuuchukua uongozi wa Tanzania mnamo 2015, aliweka mikakati ya kupunguza bei. Alipunguza usafiri wake wa bara na pia usafiri wake katika vikao vya wajumbe wa bara. Kwa mfano, alipunguza mkutano wa wajumbe wa Jumuiya ya madola, Uingereza hadi nne kutoka 50. Zaidi ya hayo, alielekeza pesa zilizonuiwa kuwa za vyakula vya jioni ama sherehe za umma kuwa za kuwasaidia wasiojiweza na wagonjwa.

Magufuli alipunguza mshahara wake kutoka milioni 1.5 kila mwezi hadi sh.400,000 na akawapunguza mawaziri hadi 15 ikilinganishwa na 30 wa Kikwete. Miezi michache baada ya kuteuliwa kwake mnamo mwaka wa 2015, hashtegi ya ‘Ni nini Maghufuli atafanya’ ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku watu wan chi jirani wakipendezwa na utendakazi wake.

Chini ya uongozi wake Magufuli, IMF iliorodhesha Tanzania kama mojawapo wa nchi zilizokuza uchumi wao, kwa asilimia 6. Mwaka jana, benki kuu ya dunia ilikubali nchi hiyo iwe miongoni mwa kitengo cha nchi zenye uchumi wa chini na wa kati, hata ingawa mchakato huo utamalizika mwaka wa 2023.

Magufuli alijenga miundo mbinu kadha wa kadha kama ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, bomba la mafuta kutoka Uganda, reli la SGR na ukuzi wa utaji wa usafiri wa hewani nchini Tanzania. Hata hivyo, cheo chake katika faharisi ya mtazamo wa ufisadi kimekwama. Tanzania ilijizolea nambari 94 kwa nchi 180 katika uratibu uliofanywa mwaka wa 2020. Ripoti kuhusiana na uhuru wa vyombo wa habari kutoka kwa waandishi wa habari wasio na mipaka (RSF) ilisema kuwa Tanzania ilirudi nyuma katika kuwapa vyombo vya habari uhuru wao.

RSF ilisema kuwa, “Hakuna nchi kati ya zile 180 zilizoorodheshwa na waandishi wasio na mipaka katika faharisi ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo imeshuka katika miaka iliyopita,” huku ikimlaumu Magufuli kwa kutostahimili kukosolewa yeye na sera alizounda.” RSF iliorodhesha nambari 124 kwa nambari 180 kwa Tanzania, huku nchi hiyo ikiwa imekuwa chini ya nchi sita hapo awali katika uratibu uliofanywa mwaka wa 2019.

Umaarufu 

Kesi iliyojulikana sana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ilimhusu Erick Kabendera aliyenyooshewa kidole cha lawama kwa kuandika kuhusu ufisadi wa vyombo vya habari vya bara. Kesi yake ilijikokota kwa miezi huku karatasi iliyonakiliwa makosa yake ikibadilishwa mara tatu. Mwishowe Kabendera alitozwa faini kwa utapeli wa pesa haramu, kutolipa ushuru na kuongoza uhalifu. Chini ya majadaliano hayo, Kabendera alilipa $120,000 kabla hajaachiliwa mnamo Februari mwaka jana.

Kundi za kuzitetea haki za binadamu zikiwemo Amnesty International na Human Rights Watch zilisema kuwa hukumu yake ilikuwa ya kisiasa. Licha ya umaaarufu wake wa kwanza nchini, upatanishi wake na wenyeji ulitiliwa shaka. Maghufuli aliwatembelea marais waliomtangulia mara chache sana huku serikali yake ikikwaruzana sana na nchi ya Kenya.

Mkwaruzano kati ya nchi hizi mbili ulisababisha kuzuiliwa kwa mifugo ilivyovuka mipaka, kuwachoma vifaranga walioletwa nchini Kenya, kupiga marufuku kuingia kwa magari ya ziara katika hifadhi na kutoelewana katika kudhibiti ugonjwa wa Covid-19. Katika mambo haya yote, suluhu ilipatikana baada ya muda.

Magufuli ametoa uamuzi unaopigana kwa mfano kubadilisha sheria za uchimabji wa madini ili kuruhusu nchi kutamatisha mikataba iwapo ulaghai unakisiwa na kuzikataza kampuni kushtaki Tanzania katika usuluhishi wa bara. Mojawapo ya kesi zinazoendelea ni kuhusu Acaia Gold ambayo Dar iliwalaumu kwa kuripoti viwango visivyofaa vya mauzo ya nje ya dhahabu.

Baada ya miaka ya maandamano, kampuni hiyo iliamua kufidia ushuru wa dola milioni 100 kwa serikali na ikahitajika kulipia nyongeza ya dola milioni 200 pamoja na kupokeza serikali hisa za asilimia 16. Mabishano mengine ni pamoja na kuagiza jeshi kununua korosho kutoka wakulima ili kuwaondoa walanguzi. Hali kadhalika, jeshi ilishindwa kufikia soko, huku ikishusha bei ya korosho. Pia Magufuli alilaumiwa kwa kuwalazimisha wanafunzi walioshika mimba kubaki nyumbani hata baada ya kuwapata watoto na kuziweka sera bishi za kuwasaka mashoga.

 

Uhuru amwomboleza mwanahabari aliyefariki kutokana na corona

CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kwa familia ya mwanahabari Robin Njogu ambaye alifariki Jumatatu usiku baada ya kuugua Covid-19. Marehemu alifariki katika hospitali ya Aga Khan ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu.

Kwenye taarifa ilitolewa na kitengo cha habari za rais (PSCU), Rais Kenyatta alimtaja Njogu kama mwanahabari shupavu ambaye mchango wake katika vitengo vya redio na uanahabari wa mitandaoni umestawisha sekta ya uanahabari na mawasiliano.

Hadi kifo chake, marehemu alikuwa Mhariri Msimamizi wa Habari katika kitengo cha Redio katika Shirika la Habari la Royal Media Services (RMS).

“Robinson alikuwa mwanahabari mwenye tajriba na uzoefu mkubwa ambaye aliwafunza chipukizi wengine katika tasnia ya uanahabari. Daima tutaendelea kuenzi weledi wake, haswa katika kitengo cha redio ambapo alikuwa kielelezo cha ufanisi,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa wa taifa aliongeza kuwa Njogu alikuwa mwanahabari wa kutegemewa zaidi alipohudumu katika kitengo cha habari katika Ikulu kati ya 2013 na 2017.

“Nilifaidi pakubwa katika kutangamana kwangu na Robin wakati ambapo alifanya kazi katika Ikulu pamoja na wanahabari wengine wa kitengo cha habari za rais. Alikuwa mfanyakazi wa kuaminika na kupigiwa mfano,” Rais Kenyatta akasema.

Kwa upande wake Naibu Rais William Ruto alimtaja marehemu Njogu kama mtaalamu aliyependa kazi yake ambayo aliifanya kwa bidii na moyo wa kujitolea.

“Alizingatia maadili ya uanahabari na kutoa mchango wake katika kuendeleza taalamu hii,” Dkt Ruto akasema kwenye taarifa aliyotuma kupitia ukarasa wake wa twitter.corona

Njogu amefariki siku chache tu baada ya kifo cha mama yake.

Pigo mabunge ya Kenya yakipoteza wabunge watano

Na CHARLES WASONGA

JUMATATU, Februari 15, ilikuwa siku yenye mkosi kwa mabunge ya Kenya – Seneti na Bunge la Kitaifa – kufuatia vifo vya Seneta Mohammed Yusuf Haji na baadaye jioni Mbunge wa Bonchari John Oroo Oyioka akakata roho.

Saa moja baada ya Mzee Haji kuzikwa katika makuburi ya Waislamu ya Lang’ata, familia ya Bw Oyioka ilithibitisha kifo chake katika hospitali ya Aga Khan Kisumu ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu baada kuugua.

Mbunge huyo amekuwa akipokea matibabu kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuugua kiharusi kapema mwaka jana. Mapema mwaka huu alilazwa katika hospitali ya Aga Khan Kisumu ambako amekuwa akipokea matibabu.

Bw Oyioka, ambaye ni mwalimu wa miaka mingi, alijiunga na siasa mnamo 2013 ambapo aliwania kiti cha ubunge cha Bonchari.

Kwa bahati mbaya alikuwa wa pili katika uchaguzi huo ambapo alishindwa na Zebedeo Opore kwa kura tano pekee.

Aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Kisii kupinga ushindi wa Opore aliyepata kura 8,992. Na katika uamuzi uliotolewa mnamo Septemba 2013, mahakama ilimtangaza Oyioka kuwa mshindi na kutoa nafasi kwake kuhudumu kama mbunge wa Bonchari.

Hata hivyo, alihudumu kama Mbunge kwa miezi sita pekee kwani Mahakama ya Rufaa iliagiza kufanyike uchaguzi mdogo ambapo Bw Opore alishinda kwa mara nyingine.

Hakukata tamaa kwani mnamo 2017, Bw Oyioka aliwania kiti hicho cha Bonchari na kuibuka mshindi kwa tiketi ya KANU iliyokuwa imeshirikiana na chama cha People Democratic Party (PDP) katika uchaguzi huo.

Kwa bahati mbaya amefariki kabla ya kukamilisha muhula wake wa miaka mitano na kujiunga na orodha ya wabunge ambapo wamefariki katika muhula huu wa Bunge la 12.

Wao ni Justus Murunga (Matungu), James Lusweti Mukwe (Kabuchai) na maseneta Boniface Mutinda Kabaka na Yusuf Haji.

Kando na kuhudumu kama Mbunge wa Bonchari, Marehemu Oyioka amekuwa mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu ambapo alitoa mchango muhimu zaidi haswa kuhusiana na masuala ya utendakazi wa Wizara ya Elimu.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amemuomboleza Oyioka kwa kumtaja kama mbunge ambaye alichukulia kwa uzito wajibu wake bungeni na katika kamati ya elimu alikohudumu.

“Kama bunge la kitaifa tunamkumba Mheshimiwa Oyioka kama mwanachama shupavu wa kamati ya elimu na ambaye alipigania kuimarishwa kwa ubora wa elimu kote nchini. Kwa niaba yangu na Bunge la Kitaifa natoa pole kwa familia na marafiki wa mwendazake,” akasema Bw Muturi

Gavana wa Kisii James Ongwae pia alielezea kuhunishwa na kifo cha Oyioka saa chache baada ya kaunti hiyo kumpa mkono wa buriani kigogo wa siasa za jamii ya Abagusii Simeon Nyachae.

“Rambi rambi zangu na maombi yaendee kaunti ya Kisii kwa ujumla familia, jamaa na marafiki wa mheshimiwa,” Ongwae akasema.

taifa leo

Huzuni tele viongozi wakipoteza wazazi wao

Na WAANDISHI WETU

HUZUNI ilitanda jana katika familia za viongozi mbalimbali waliofiwa na wazazi wao. Rais Uhuru Kenyatta aliongoza taifa kutuma risala za rambirambi na faraja kwa kwa familia ya Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi kufuatia kifo cha Mama Hannah Atsianzale Mudavadi.

Marehemu, aliyekuwa na umri wa miaka 92, ni mjane wa marehemu waziri wa zamani Moses Mudavadi na mama wa aliyekuwa.

Rais alisema Mama Hannah atakumbukwa hususan kutokana na upendo wake kwa elimu na jinsi alivyosaidia watoto wengi werevu kutoka familia zisizojiweza kupata elimu bora.

Rais aliihakikishia familia ya Mudavadi kwamba yupo pamoja nao wakati huu mgumu wa msiba.Akihutubia wanahabari katika hifadhi ya maiti ya Lee jijini Nairobi, Bw Mudavadi alisema mazishi yatafanyika wiki moja baada ya kufungua Mwaka Mpya.

Wakati huo huo, Mbunge wa Mosop, Bw Vincent Tuwei alifiwa na babaye, Zakayo Cheruiyot Chebochok.Kwingineko, Mzee Joseph Kibii Koske ambaye ni baba wa Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kericho, Bi Florence Bore pia aliaga dunia.

Kwenye ujumbe wa rambirambi, Naibu Rais William Ruto aliwataja wote kama Wakenya waliojitolea kutumikia nchi kwa moyo mmoja na akatakia familia zao faraja.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Wajir, Bi Fatuma Gedi, naye alimpoteza babake, Gede Ali ambaye alisemekana kufariki ghafla jijini Nairobi.

Mbunge wa zamani wa Kaloleni afariki

Na Mohamed Ahmed

ALIYEKUWA mbunge wa Kaloleni, Gunga Mwinga alifariki jana akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Mombasa.Kwa mujibu wa famili yake, kiongozi huyo alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Hata hivyo, familia hiyo haikufichua ugonjwa aliokuwa akiugua.Akizungumza na wanahabari, mjomba wa marehemu Bw Fredrick Kahindi, alisema kuwa Bw Mwinga aliaga dunia mwendo wa saa tisa usiku wa kuamkia Jumapili.

“Kama familia tunasikitishwa na kufiwa na kijana wetu ambaye alikuwa tumaini kuu kwetu. Kifo hiki ni cha ghafla kwani amekuwa hospitalini kwa muda mfupi tu,” akasema Bw Kahindi.

Ripoti zilieleza kuwa Bw Mwinga alifikishwa hospitalini mnamo tarehe 24 mwezi huu na kukosa kusherehekea sikukuu ya Krismasi na familia yake.

“Tutaanza mipango ya mazishi leo baada ya kukutana kama familia na kutoa taarifa baadaye kuhusiana na kuzikwa kwa marehemu,” akasema Bw Kahindi.

Bw Mwinga alikuwa mbunge wa eneo la Kaloleni kwa muhula mmoja kati ya mwaka wa 2013 na mwaka 2017 ambapo alishindwa na mbunge wa sasa Bw Paul Katana.Bw Katana jana aliungana na familia ya mwendazake hospitalini ambapo alitoa risala zake za rambirambi kwa familia.

“Wakazi wote wa Kaloleni wanaomboleza kwa kuondokewa na kiongozi aliyewahudumia. Alikuwa mshindani wangu lakini tulikuwa marafiki. Tumeshtushwa na kifo chake lakini tunaomba Mungu awape subira watu wa familia yake,” akasema Bw Katana.

Kifo cha Bw Mwinga ni miongoni mwa vya watu mashuhuri katika kanda ya Pwani waliofariki mwaka huu.Miongoni mwa watu hao ni wanasiasa wakongwe akiwemo aliyekuwa mbunge wa Changamwe Ramadhan Kajembe pamoja na wake zake.

Aliyekuwa mbunge wa Likoni Masoud Mwahima pia alifariki mwaka huu na baadaye kufuatiwa na mkewe wiki jana.Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori naye alifariki mwaka huu tukio lililochangia kuwepo kwa uchaguzi mdogo katika eneobunge lake.

Joho apata pigo huku wengi wakimuomboleza Hatimy

MOHAMED AHMED Na MISHI GONGO

KIFO cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha ODM na diwani maalum wa Mombasa, Bw Mohammed Hatimy, kimeacha pengo kubwa katika serikali ya Gavana Hassan Joho.

Bw Joho binafsi alikiri kwamba kifo cha Bw Hitamy ni pigo kwake na Mombasa kwa jumla. “Mombasa imepoteza mwana wake wa kutegemewa ambaye nilikuwa namthamini sana,” Bw Joho alisema kwenye rambirambi zake.

Bw Hatimy alifariki Jumamosi akiwa katika hospitali ya Mombasa ambapo alipelekwa baada ya kupatikana kuambukiwa virusi vya corona.Bw Hatimy ambaye alizikwa jana katika makaburi ya Kikowani, alifariki siku chache tu baada ya mavyaa wake ambaye pia aliripotiwa kufariki baada ya kuugua corona.

Familia yake ilieleza kuwa alifariki Ijumaa saa tisa usiku. Wengi walimsifia Bw Hatimy wakisema hakuwa kama diwani wa kawaida na kwamba aliheshimiwa na kupendwa na wengi.

Kuanzia mwanzo wa serikali ya Bw Joho mwaka 2013, Bw Hatimy ameshikilia wadhfa wa mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kaunti hiyo tangu Bw Joho aliposhinda ugavana 2013.

Bw Hatimy pia alitambulika wakati alipokuwa kwenye usimamizi wa michezo.Jana, viongozi wa chama cha ODM wakiongozwa na kinara wao, Bw Raila Odinga waliomboleza kifo chake na kumtaja kuwa kiongozi aliyejitolea katika utumishi wake.

“Nimezipokea taarifa za kufariki kwa mwenyekiti wa muda mrefu wa ODM tawi la Mombasa Mohammed Hatimy. Alikuwa kiongozi shupavu aliyejitolea katika kila pembe aliyoshikilia. Mungu aipe familia yake subira wakati huu mgumu,” akasema Bw Odinga kupitia mtandao wake wa kijamii.

Gavana Joho alisema kuwa Mombasa imepoteza mmoja wa watu muhimu a kutegemewa.“Kama diwani maalum alihudumu kwa kujitolea na alionyesha matunda ya kazi yake na majukumu aliyokuwa amepewa. Kwa niaba ya watu wa Mombasa natoa rambirambi zangu kwa familia. Mungu awape subira wakati huu wa huzuni,” akasema.

‘Murunga alihudumia wakazi wa Matungu kwa moyo wa kujitolea’

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI kadha wa kisiasa nchini wametuma risala za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Mbunge wa Matungu Justus Murunga.

Wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanasiasa hao walimtaja mwendazake kama kiongozi mchapa kazi, mwenye maoni na aliyehudumia taifa hili na watu wa Matungu kwa moyo wa kujitolea.

“Mheshimiwa Murunga pia alikuwa kiongozi aliyetilia maanani miradi yenye kuwapa uwezo watu wake. Ama kwa hakika watu wa Matungu watamkosa. Sisi kama Wakenya pia tutakosa upendo na mchango wake katika juhudi za kuwaleta pamoja watu wa eneo la Magharibu,” akaeleza Dkt Ruto kupitia Twitter.

Kwa upande wake Bw Odinga alisema: “Nasema pole kwa watu wa Matungu kwa kumpoteza kiongozi wao shapavu wakati ambapo walihitaji huduma zake zaidi; katika muhula wake wa kwanza. Rambirambi zangu ziwefikia familia, jamaa na marafiki wa Mheshimiwa Justus Murunga. Mungu apumzishe roho ya pema daima.”

Gavana wa Kakamega naye alimtaja mwendazake kama kiongozi shupavu aliyeshirikiana naye kutekeleza miradi ya mengi ya maendeleo katika eneo la Matungu.

“Nimehuzunishwa zaidi na kifo chake ambacho kimepokonya kaunti ya Kakamega kiongozi mwenye maoni ambaye atakoswa zaidi kutokana na michango yake katika maendeleo.” akasema Bw Oparanya.

Wengine walituma risala zao ni Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali, Christopher Aseka (Khwisero), aliyekuwa senata wa Kakamega Bonny Khalwale miongoni mwa wengine.

Bw Murunga alifariki Jumamosi jioni alipokuwa akikimbizwa kupelekwa Hospitali ya St Mary’s, Mumia baada ya kukumbwa na matatizo ya kupumua.

Mbunge huyo alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Kisumu kwa majuma mawili yaliyopita akiugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Aliondoka hospitalini mnamo Alhamisi na amekuwa akitunzwa nyumbani kwake katika kijiji cha Emakunda, eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega hadi Jumamosi alipoanza kupatwa na matatizo ya kupumua.

Marehemu Murunga alizaliwa mnamo mnamo 1961. Amekuwa akiwania kiti cha ubunge cha Matungu tangu 2002 lakini hatimaye akashinda mnamo 2017 kwa tiketi ya chama cha Amani National Congress (ANC) baada ya kumbwaga David Were. Bw Were alihudumu kati ya 2007 na 2013.

Katika bunge la sasa Bw Murunga amekuwa akihudumu kama mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo na Ufugaji.

TANZIA: Mbunge wa Matungu Justus Murunga afariki

NA SHABAN MAKOKHA na WANGU KANURI

Mbunge wa Matungu, Justus Murungu amefariki Jumamosi usiku alipokuwa akikimbizwa katika Hospitali ya St Mary’s mjini Mumias.

Wiki mbili zilizopita, Bw Murunga aliugua na akalazwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Kisumu ambapo alikuwa akipokea matibabu ya ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Mwenyekiti wa kamati ya NG-CDF, Athman Wangara alisema kuwa mbunge huyo alitolewa hospitalini Alhamisi na akawa anazidi kupata afueni nyumbani kwake Emakunda-Matungu. Mnamo usiku wa Jumamosi ya Novemba 14, alianza kupata matatizo ya kupumua.

“Alishinda siku nzima akiwapokea wageni ambao walimtakia kupona kwema na alikuwa mwenye furaha nyingi huku akiwapa matumaini waliomtembelea kwa kuwaambia kuwa anazidi kupata afueni,” akasema Wangara.

Familia yake ilisema kuwa aliwaonyesha wahandisi pahali ambapo wangejenga tanki la maji katika bustani yake kabla ya chajio. “Alipokuwa akipanda vidato, alikosa nguvu na kuzirai. Alisaidiwa na waliokuwa nyumbani huku wakikimbiza katika hospitali ya Matungu Sub-county lakini hakukuwa na mashine za oksijeni huku ikiwalazimu kumpeleka hospitali ya St Mary’s ambako alifia njiani, ” akaongeza Wangara.

Marafiki na wanafamilia walifurika kwenye mochari baada ya kusikia kifo cha mbunge wao huku majonzi na kilio kikiwajaa moyoni na machoni mwao.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Washiali na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa walifika mochari ambapo mwili wa Murunga ulikuwa umehifadhiwa. Bw Washiali alimuomboleza Murunga akisema kuwa mwendazake alikuwa rafiki yake wa karibu na ambaye hakujua mipaka ya uongozi wa kuwasaidia wananchi wa Matungu.

“Hivi majuzi, marehemu alikuwa amelazwa katika hospitali ya Aga Khan ambako alikuwa akitibiwa ugonjwa wa Kisukari na ugonjwa wa shinikizo la damu lakini akatolewa hospitalini akiwa mwenye siha afadhali. Yasikitisha kuwa ametuacha, ” akaongeza Washiali.

Isitoshe, Bw Washiali alisema kuwa mwili wa mwendazake utasafirishwa katika hifadhi ya mili ya Lee, Nairobi huku maziko yakipangwa.

Bw Echesa alisema kuwa ilimshtua kufahamu kifo cha Murunga. “Murunga alikuwa kiongozi mzuri na ambaye atakumbukwa kwa kuwahudumia wakazi wa Matungu. Ninawapa risala za rambirambi wakazi wa Matungu na chama cha ANC. Mungu awape nguvu mnapopambana na nyakati hizi ngumu,” akasema Echesa.

Marehemu alizaliwa mnamo 1961 na akawa kwenye kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge cha Matungu kutoka mwaka wa 2002 lakini akawania kiti hicho Agosti 2017 katika chama cha kitaifa cha Amani Congress huku akimshinda David Were ambaye alikuwa kiongozi wa Matungu kutoka mwaka wa 2007 hadi 2013.

Viongozi kadhaa wakiwemo  Naibu Rais Dkt William Ruto, gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale, mbunge wa Khwisero Christopher Aseka na Seneta Cleophas Malala walimuomboleza Murunga.

Dkt Ruto alisema kuwa mwendazake alikuwa kiongozi mchapa-kazi na mwenye maono mengi haswa kwa wakaazi wa Matungu. “Mheshimiwa Murunga alikuwa kiongozi mpenda watu na tutaishi kukumbuka uongozi wake na alivyopenda kuwaunganisha watu wa Magharibi,” Daktari Ruto akaandika katika ukurasa wake wa kijamii.

Gavana Oparanya alisema kuwa Murunga alikuwa kiongozi mfanyakazi na aliyejitolea kwa wananchi huku akifanya kazi kwa ushirika sana ili kuboresha eneo la Matungu. “Ninahuzunika sana kwa kifo cha Murunga ambacho kimefanya Kakamega kupoteza kiongozi mwadilifu ambaye mchango wake nchini utakumbukwa. Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi,” akasema.

 

Jinsi viongozi na watumiaji mitandao ya kijamii wamepokea habari za kifo cha Moi

Na SAMMY WAWERU

WATUMIAJI wa mitandao ya kijamii wameelekeza risala za pole kwenye kurasa zao kufuatia kifo cha Mzee Daniel Toroitich Arap Moi ambaye alikuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Kenya.

Mzee Moi ameaga dunia mapema Jumanne katika Nairobi Hospital.

Chini ya utawala wa Rais huyo mstaafu na ambaye kwa sasa ni marehemu, kati ya mwaka 1978 – 2002, anakumbukwa kwa mengi.

Alichukua hatamu baada ya kifo cha Rais mwanzilishi wa taifa hili, Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Neno ‘Nyayo’ linapotajwa, linahusishwa na Mzee Moi.

Katika sherehe za kitaifa, akiingia uwanjani kwa gari maalum la Amiri Jeshi Mkuu, Rais huyo aliinua na kutikisa kidole cha shahada, huku akikariri ‘Nyayo’, wananchi nao wakiiga hilo. Pia alitumia rungu yake kuongoza kukariri jina hilo.

Kwenye mitandao ya kijamii wachangiaji wamefufua kumbukumbu zao kwa mazuri aliyowafanyia katika enzi yake akiwa Rais wa Jamhuri.

Mtumiaji mtandao wa Facebook, Gedion Mwangi Kabugi amechapisha picha za pakiti za maziwa yaliyoasisiwa na Mzee Moi, na ambayo yalikabidhiwa wanafunzi katika shule zote za msingi na za umma nchini miaka ya tisini.

“Watu wa enzi zetu, tunaweza kumsahau Moi kweli? Haya maziwa tulikuwa tunayanywa sana, kisha tunakata vipande vya pakiti na kucheza karata. Nakumbuka 1993 ilisemekana maziwa hayo yana vidole vya binadamu, tukaanza kuyamwaga ila madai hayo yalikuwa uongo mtupu,” anafafanua mchangiaji huyo.

Kabugi kwenye simulizi yake, anakumbuka wakati baba yake akiwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi aliyosomea, alikuwa akiingia ofisini kisiri na kuyanywa maziwa ya Nyayo. “Ningekunywa zaidi ya pakiti tatu. Mungu ailaze roho yake mahali pema Mzee Moi, hatutakusahau,” anaeleza.

Mchangiaji mwingine, Wa Biashara Simon, anasema tangu Rais Moi astaafu, ameyakosa maziwa hayo ya Nyayo.

Susan Mwangi naye anataja marehemu kama kiongozi ambaye aliwapa wanafunzi motisha ya kusoma.

“Hatukuwa tukikosa shuleni kwa sababu ya maziwa,” Susan amemsifu Moi.

Nasrin Naserian anamuomboleza kama kiongozi aliyehubiri utangamano na amani.

“Kama kuna mtu niliyekosea, ninaomba anisemehe,” Nasrin anamkuu Mzee Moi akisema kauli hiyo ni ishara kuwa alikuwa kiongozi aliyethamini amani.

Mwili wa kiongozi huyo umehifadhiwa katika chumba cha Lee Funeral jijini Nairobi, ambapo viongozi na wanasiasa mbalimbali wanaendelea kumiminika kuutazama mwili.

Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, kwa upande wake amesema alikuwa mmoja wa mawakili wa Mzee Moi.

“Moi aliniteua mnamo 1993 kuingia bungeni. Nilikuwa na fursa ya kipekee kuwa mmoja wa mawakili wake,” akasema Bw Wetang’ula akitoa salamu zake za pole.

Marehemu pia ametajwa kama kiongozi ambaye hakutaka mzaha kazini.

“Alikuwa mcha Mungu na kabla kuanza kazi lazima angesoma Biblia. Alikuwa akiamka alfajiri na mapema kuhudumia taifa,” anasema Franklin Bett ambaye alihudumu chini ya serikali ya Mzee Moi.

Marehemu pia anatajwa kama profesa wa siasa, Bett akisema alielewa bayana mchakato na mikakati ya siasa. Licha ya sifa zake, baadhi walimlaumu kwa utawala wa kidikteta.

Wakati wa usomaji habari, ambapo Voice of Kenya (VoK) kwa sasa ndiyo KBC Radio Taifa, ndicho kilikuwa kituo cha redio cha kipekee, sharti taarifa ya kwanza ingekuwa ya Rais Moi.

Japo inaelezwa alizaliwa 1924 mwandani wake wa karibu Lee Njiru amesema Mzee amefariki akiwa na umri unaozidi miaka 100.

Vilevile Raymond Moi amesema Mzee alikuwa na umri unaozidi miaka hii ya 95 na 96 inayosemwa.

KAULI YA MATUNDURA: Ni pigo kwa ulimwengu wa Kiswahili kumpoteza Prof Mwenda Mukuthuria

Na BITUGI MATUNDURA

Mhariri. Naomba unipe idhini niitumie safu hii kumuomboleza mwalimu na rafiki yangu Prof Mwenda Mukuthuria  (pichani anayepokezwa mikrofoni) ambaye alitutupa mkono Jumamosi, juma lililopita. Jumamosi ambayo ni ya mkosi.

Maombolezo haya pia ni kwa niaba ya wanataaluma wengine wa Kiswahili ambao waliwahi kutangamana na kutagusana na Prof Mukuthuria, ambaye hadi mauko yake alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Narok.

Mara yangu ya kwanza kukutana na Prof Mukuthuria ilikuwa ni mwaka 2001 katika kongamano la ‘Lugha na Utandawazi’ mjini Nyahururu. Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA).

Mwaka mmoja baadaye, tulikutana naye tena katika kongamano la Kiswahili mjini Arusha, Tanzania ambapo Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki – CHAKAMA kilizinduliwa.

Urafiki tuliouanzisha Nyahururu uliota mizizi na kushamiri. Katika kipindi hicho, alikuwa mhadhiri katika Chuo cha Kiisilamu cha Uganda.

Mnamo 2010, ujaala ulitukutanisha tena nilipokwenda kutafuta ajira katika Chuo Kikuu cha Chuka ambapo tulihudumu pamoja kwa miaka mitatu kabla hajaguria Chuo Kikuu cha Mount Kenya ambapo alikwezwa hadhi na kuwa Profesa Mshiriki wa Kiswahili.

Baada ya kuhudumu katika chuo hicho kwa muda, Prof Mukuthuria alihamia Chuo Kikuu cha Maasai Mara ambapo alihudumu wadhifa wa Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Fani.

Wataalamu mbalimbali wa Kiswahili walipokea taarifa kuhusu kifo cha Prof Mukuthuria mnamo Jumamosi 28, 2018 kwa masikitiko makubwa. Prof Kimani Njogu – mwenyekiti mwasisi wa CHAKITA alimtaja Prof Mukuthuria kuwa msomi mwadilifu, mwaminifu na mtu wa kutegemewa.

Prof Mukuthuria aliwahi kuwa mhazini wa Chama cha Kiswahili cha Taifa – ambacho ni chombo kilicho katika msitari wa mbele kutetea makuzi ya Kiswahili nchini Kenya.

Wataalamu wengine walioomboleza mauko ya Prof Mukuthuria ni pamoja na Dkt Mark Kandagor (Mwenyekiti, CHAKITA), Prof Clara Momanyi, Prof Kineene wa Mutiso (Nairobi), Prof Chacha Nyaigotti Chacha , Prof John Kobia (Chuo Kikuu cha Chuka), Prof Ken Walibora, Prof Sangai Mohochi (Chuo Kikuu Rongo). Wengine ni Prof Obuchi Moseti (Moi) Prof Ipara Odeo miongoni mwa wengine. Marehemu Prof Mwenda Mukuthuria alizaliwa katika kijiji cha Mwigele, Kata ya Nkomo tarafa ya Kilenchune – Tigania Mashariki alisomea katika shule za Lubunu Primary, na St Kizito Secondary (O Level) na Friends School, Kamusinga (A Level).

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi mnamo 1987 alikohitimu Shahada ya Ualimu akimakinikia masomo ya Kiswahili na Jiografia. Mnamo 1995, alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton alikosomea shahada ya uzamili na Uzamifu.

Prof Mukuthuria aliwalea wataalamu wengi chipukizi waliopitia katika mikono yake. Alikuwa na kalamu yenye utelezi mno na hivyo basi kuchangia zaidi ya makala 30 ya kitaaluma yaliyochapishwa katika majarida mbalimbali ulimwenguni – barani Afrika, Asia, Ulaya na Marekani.

Kaulimbiu aliyoichangamkia mno katika uhai wake ni kwamba maarifa na habari ni mambo ambayo hayakuwa na umuhimu wowote yakihodhiwa na mtu mmoja.

Aliamini kwamba vitu hivyo vilikuwa muhimu kwa jamii pindi vingesambazwa na watu wengi kuvipokea. Kwa hiyo, Prof Mukuthuria alikuwa radhi kuwagawia wataalamu wengine kanzi ya taarifa kutoka kwenye maktaba yake kubwa.

Taaluma ya Kiswahili imempoteza msomi wa isimu ambaye alitegemewa sana. Marehemu atazikwa tarehe 4 Jumamosi ijayo, 2018, Jumamosi ijayo.

Buriani ‘mufti’.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katicha Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com