Mkewe Trump kuzuru Kenya Oktoba

Na CHARLES WASONGA

MKEWE Rais wa Amerika Donald Trump, Melania Trump amepangiwa kuzuru Kenya mwezi Oktoba atakapozuru mataifa kadha ya Afrika.

Akihutubu Jumatano, Bi Trump alisema atakuwa akizuru mataifa manne “mazuri na yenye sifa za kipekee” barani Afrika ambayo ni; Ghana, Malawi, Kenya na Misri.

Ziara hiyo ni yake ya kwanza barani Afrika tangu mumewe alipochukua hatamu za uongozi wa Amerika mnamo Januari 20 mwaka jana.

“Hii ndio itakuwa ziara yangu ya kwanza barani Afrika na ninafurahi kwamba nitajifunza mengi kuhusu masuala yanayowaathiri watoto katika bara hilo. Pia nitajifahamisha na utajiri wake mkubwa katika nyanja ya utamaduni na historia,” Bi Melania alisema katika mahojiano yake ya awali.

“Sisi ni wanajamii wa dunia na ninaamini kuwa kwa njia ya mazungumzo na kubadilishana mawazo tutapata nafasi ya kufunzana mengi,” akaongeza.

Mama huyo wa Taifa wa Amerika atafanya ziara hiyo peke yake bila kuandamana na mumewe.

Melania alitaja mataifa ambayo atazuru wakati wa halfa iliyoandaliwa kwa heshima ya wake za viongozi wakuu ulimwenguni wanaohudhuria Kongamano la 73 ya Baraza la Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Amerika.

Ziara hiyo itafanyika miezi miwili baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru Amerika kwa mwaliko maalum wa Rais Trump. Rais Kenyatta na mwenyeji wake walijadiliana masuala kadhaa yenye umuhimu kati ya Kenya na Amerika, kama vile biashara, uwekezaji, utalii na usalama.

Tarehe kamili ya ziara ya Bi Trump nchini haijabainishwa japo duru zinasema itafanyika “mapema mwezi Oktoba”.

ZIARA: Mkataba wa kibiashara baina ya Trump na Uhuru

NA PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta na Donald Trump wa Marekani Jumatatu walifanya mazungumzo ya kina kuhusu mbinu za kuimarisha biashara, uwekezaji na usalama baina ya mataifa yote mawili.

Katika kikao cha faragha kwenye Ikulu ya White House, viongozi hao walijadili namna wawekezaji kutoka US wataweza kufanya biashara humu nchini katika mazingira bora zaidi, bila kusumbuliwa.

Aidha, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha biashara ili kufaidi mataifa yote mawili, kwenye ushirikiano wa kisoko baina yao.

Walipofanya kikao na waandishi wa habari jijini Washington DC,  kabla ya mkutano wao, Rais Kenyatta na Rais Trump walieleza matumaini makuu kuwa watafikia maelewano yatakayoleta uthabiti katika sekta hizo.

“Kenya na Marekani zimekuwa na uhusiano thabiti tangu tupate uhuru, tuko hapa kuimarisha ushirikiano huo. Tumekuwa na ushirikiano mzuri haswa katika vita dhidi ya ugaidi,” akasema Rais Kenyatta.

Alisema idadi kubwa ya kampuni za US zinazofanya biashara Kenya zimesaidia katika maendeleo, akiongeza kuwa ziara hiyo itasaidia kuongeza na kuimarisha biashara yao.

“Tuko hapa kufuatilia na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina yetu ili kuona namna tunaweza kuinua tunapoendelea kwa nia ya kufaidi mataifa yetu,” Rais Kenyatta akasema.

Rais Trump aliahidi kutimiza ‘mazuri’ mengi baada ya mazungumzo hayo, mbali na kufanya miradi bora.

“Tunaenda kumalizia vitu vingi vizuri kwenye kikao hicho. Tutakuwa tukifanya dili nzuri kwa mataifa yote mawili,” akasema Rais Trump.

Mbeleni, Rais Kenyatta alikuwa ameshuhudia kutiwa saini kwa mikataba ya kibiashara, ambapo Kenya ilipata zaidi ya Sh23 bilioni kufadhili mradi wa umeme na chakula.

Wake za marais hao Bi Margaret Kenyatta na Bi Melania Trump vilevile walifanya kikao chao kujadili namna ya kuinua miradi wanayosimamia ya ‘Beyond Zero’ (wa Bi Kenyatta) na ‘Be Best’ (wa Bi Trump).

“Bi Kenyatta na Bi Trump walifanya kikao cha wazi kikihusisha malengo yao ya pamoja na miradi yao husika kuhusu watoto. Miradi yao imeungana katika kuinua na kulinda watoto,” ikasema habari kutoka ikulu ya White House.

Bi Trump anatarajiwa kuzuru Afrika Oktoba.

Rais Kenyatta aelekea Amerika kukutana na Trump

NA PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ameondoka nchini kwa ziara rasmi jijini Washington DC, Amerika, ambapo anatazamamiwa kukutana na Rais Donald Trump mnamo Agosti 27.

Ndege aliyosafiria Rais na ujumbe wake iliondoka Uwanja wa Ndege wa Kimatifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) muda mfupi baada ya saa sita usiku Jumamosi.

Maafisa wakuu serikalini wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na Mkuu wa Majeshi Jemedari Samson Mwathethe walimuaga Rais Kenyatta katika uwanja huo.

Akiwa nchini Amerika, Rais Kenyatta atafanya mashauriano na mwenyeji wake Rais Trump kuhusiana na masuala ya biashara na usalama humu nchini.

Kutoka kushoto: Rais Kenyatta asindikizwa uwanjani JKIA na mkewe Margaret Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, gavana wa Nairobi Mike Sonko na mwenzake wa Kiambu Ferdinand Waititu. Picha/ PSCU

Kwa miaka mingi sasa, Kenya imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika udumishaji amani na usalama katika eneo la Mashariki mwa Afrika, eneo la Maziwa Makuu na Upembe wa Afrika, ambapo Kenya imekuwa katika msitari wa mbele kurejesha amani katika nchi ya Sudan Kusini.

Huko nchini Somalia, vikosi vya majeshi ya Kenya vinashiriki katika mapambano dhidi ya kundi la magaidi la Al Shabaab chini ya  shirika la AMISOM.

Mbali na masuala ya kibiashara na usalama, Rais Kenyatta na Rais Trump watajadiliana kuhusu njia za kuimarisha uhusiano bora kati ya nchi hizi mbili wakizingatia maadili ya kidemokrasia na uelewano.

Mkutano kati ya viongozi hawa wawili unafanyika wakati unaofaa huku Rais Kenyatta akitekeleza mipango ya kuboresha biashara na uwekezaji nchini kupitia Ajenda Nne Kuu za maendeleo.

Rais Kenyatta apanda kwa ndege kuelekea nchini Amerika kwa mkutano wake na Rais Donald Trump. Picha/ PSCU

Aidha, Kenya inanufaika zaidi na  mipango ya kibiashara kati yao muhimu zaidi ukiwa ni mkataba wa AGOA ambao Rais Kenyatta atashauriana upya na Rais Trump.

Uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili umeisaidia Kenya kuthibiti uchumi wake na kudumisha usalama, kutoa huduma bora za afya, elimu , kuimarisha utawala wa sheria na utekelezaji wa kanuni za kidemokrasia.

Mkutano kati ya Rais Kenyatta na mwenyeji wake Trump ni hatua bora ya kuimarisha sekta za utalii na za safari za ndege kwani mkutano kati yao unafanyika majuma machache tu kabla ya kuzinduliwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka uwanja wa JKIA hadi jijini New York mwezi Oktoba 2018.

Hapo Agosti 24, Waziri wa Mashauri ya nchi za Kigeni Dkt Monica Juma ambaye tayari alitangulia Marekani, alifanya mashauriano na mwenyeji wake Michael Pompeo kabla ya mkutano kati ya marais hawa wawili.

Kenya yakataa wito wa Trump kutwaa mali ya wakuu Sudan

Na MWANDISHI WETU

Kenya imekataa shinikizo za Amerika za kutwaa mali ya viongozi wa Sudan Kusini ambayo inadaiwa ilipatikana kwa njia ufisadi, ulanguzi wa pesa na vita.

Maafisa wa wizara ya Mashauri ya kigeni ya Kenya walisema kwamba Kenya inafurahia kubadilishana habari za kijasusi na Amerika kuhusu pesa haramu kutoka Sudan Kusini, lakini inafaa kuthibitisha ikiwa ripoti kutoka nchi hiyo yenye uwezo mkubwa ulimwenguni ni za kweli.

Katibu wa wizara hiyo Macharia Kamau alisema Kenya ina uwezo wa kutwaa mali yote haramu lakini itafanya hivyo kwa kuzingatia taratibu za kimataifa kupitia kanuni za Umoja wa Mataifa na taasisi za kifedha ulimwenguni.

Wiki jana, Kenya ilishinikizwa na serikali ya Amerika, inayotaka kuona mwisho wa vita Sudan Kusini, kuchunguza na kutwaa mali ya viongozi wa Sudan Kusini ambayo inadaiwa huwekeza pesa za ufisadi nchini.

Utawala wa Rais Donald Trump umezindua mpango wa kuwekea vikwazo viongozi, familia zao na mitandao ya kibiashara na Kenya na Uganda zinatarajiwa kuhusika.

Mkutano wa Kim na Trump wapongezwa kote duniani

Na AFP

VIONGOZI wa mataifa mbalimbali duniani wamemiminia sifa mkutano wa kihistoria baina ya Rais wa Amerika Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un uliofanyika Jumanne nchini Singapore.

Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in alitaja mkutano huo kuwa wa kihistoria na uliofungua ukurasa mpya’

“Kim na Trump watakumbukwa kama marais walioandikisha historia kwa kudumisha amani ulimwenguni. Tumeacha siku za giza zilizogubikwa na vitisho vya kivita na sasa tumechukua mwelekeo mpya katika udumishaji wa amani,” akasema Moon.

Naye Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema: “Nimefurahishwa mno na maafikiano baina ya Rais Trump na mwenzake wa Korea kaskazini Kim kwa kukubaliana kukomesha utengenezaji wa makombora ya nyuklia.”

Serikali ya Denmark ilipongeza mkutano baina ya viongozi hao wawili lakini ikawataka Trump na Kim kuhakikisha kuwa mkataba wa kukomesha nyuklia uliotiwa saini unatekelezwa kikamilifu.

“Korea Kaskazini imewahi kukubali kusitisha utengenezaji wa makombora ya nyuklia lakini baadaye ikapuuza. Kuna haja ya kuhakikisha kuwa mkataba uliotiwa saini Jumanne unatekelezwa,” akasema Waziri Mkuu wa Denmark Løkke Rasmussen.

Rais wa China, Xi Ji Ping pia alipongeza mkutano huo wa kihistoria baina ya Trump na Kim.

Katika mkutano wa jana, viongozi hao wawili walisalimiana, wakafanya vikao vya faragha na kisha kutia saini mkataba wa maelewano.

Miongoni mwa masuala yaliyoafikiwa katika mazungumzo hayo ni kusitishwa kwa utengenezaji wa makombora ya nyuklia yaliyokuwa yakirushwa mara kwa mara na Korea Kaskazini.

Akihutubia wanahabari baada ya mkutano huo, Rais Trump alisema kuwa mataifa hayo mawili yataendelea na mazungumzo zaidi ili kuhakikisha kuwa mkataba huo unatekelezwa kikamilifu.

Rais Trump na Kim waliafikiana kuachana na vita vya maneno baina yao na badala yake wakaahidi kushirikiana kiuchumi.

Kim Jong-un amekuwa akishutumiwa kwa kuendeleza ugandamizaji wa haki za kibinadamu na mwaka jana alidaiwa kuagiza kuuawa kwa ndugu yake katika uwanja wa ndege nchini Malaysia.

Kim alikubali mwaliko wa Rais Trump wa kumtaka kuzuru ikulu ya White House nchini Amerika.

Ujumbe wa Trump ulijumuisha waziri wa Masuala ya Kigeni, Mike Pompeo, mshauri wa masuala ya usalama John Bolton na mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu ya White House John Kelly. Upande wa kiongozi wa Korea Kaskazini ulijumuisha mwandani wa Kim, Kim Yong Chol, ambaye alikutana hivi majuzi na Rais Trump katika White House.

Wajumbe mbioni kuhakikisha Trump na Kim Jong-Un wamekutana

Na AFP

WASHINGTON, AMERIKA

WAJUMBE wa Amerika na Korea Kaskazini wamekutana kurejelea uwezekano wa kuandaliwa upya kwa kikao kati ya Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong- un.

Kwenye mazungumzo hayo, yaliyofanyika mnamo wikendi, ilidhihirika kwamba Rais Trump ameelezea nia ya kukutana na Kim, licha ya mkutano huo kufutiliwa mbali katika hali tatanishi.

Kwenye jumbe kadhaa alizoandika katika akaunti yake ya Twitter, Bw Trump aliisifia Kaskazini, akiitaja kuwa ni nchi iliyo na uwezo mkubwa kiuchumi. Bw Trump pia alisema kuwa “hatajali kushauriana” na Kim nafasi nyingine itokeapo.

“Naamini kwamba Korea Kaskazini ina uwezo mkubwa sana kiuchumi, ambapo itakuwa nchi ya kupigiwa mfano siku moja,” akasema Bw Trump. Akaongeza: “Kim anakubaliana nawe kuhusu hili. Itatimia!” akasema.

Aidha, alithibitisha kwamba kundi la wajumbe wa Amerika wamefika Kaskazini kufanya maandalizi ya kikao hicho.

Msimamo huo wa Trump unatofautiana na kauli yake siku kadhaa zilizopita, ambapo alifutilia mbali mkutano kati yao wawili.

Akieleza sababu ya hatua hilo, Bw Trump alisema kuwa alichukua hatua hiyo kutokana na “msimamo mkali wa Kaskazini kuhusu mpango wake wa urutubishaji wa zana za kinuklia.”

Lakini siku kadhaa baada ya kauli hiyo, Amerika ilianza harakati za kidiplomasia kuondoa dhana hiyo, kwa msingi kwamba “bado kuna nafasi ya mashauriano.”
Mikakati hiyo ililenga kufufua maandalizi mapya ya mkutano huo.

Mnamo Jumamosi, Bw Kim alikutana na Rais Mo Jae-in wa Korea Kusini, katika mpaka wa nchi hizo mbili, ili kuangazia mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati yake na Amerika.

Kulingana na maandalizi mapya, kikao hicho kimepangiwa kufanyika mnamo Juni 12 nchini Singapore.

Mipango hiyo pia imethibitishwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Amerika, kwa kusema kuwa maandalizi ya kikao hicho yanaendelea.

“Tuko katika hatua za mwisho mwisho za maandalizi ya mkutano huo muhimu,” akaeleza msemaji wa wizara hiyo Bi Heather Nauert.

Gazeti la ‘The Washington Post’ liliripoti kwamba ujumbe wa Amerika uliofika Kaskazini uliongozwa na balozi wa zamani wa Amerika katika Korea Kusini na Kaskazini Susan Kim.

Gazeti pia liliripoti kwamba ujumbe huo ulikutana na Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kaskazini Choe Son Hui.

Kwa sasa, Amerika haina balozi katika Kusini, licha ya juhudi zinazoendelea za kurejesha uhusiano wake wa kidiplomasia.

Kulingana na wachanganuzi, cha muhimu kwa sasa ni kungoja matokeo ya mkutano kati ya viongozi hao wawili.

 

Trump aisifu Korea Kaskazini kwa kuharibu kituo cha nyuklia

Na MASHIRIKA

Rais wa Amerika Donald Trump Jumamosi alishukuru Korea Kaskazini kwa kukubali kuharibu kituo chake cha kufanyia majaribio silaha za kinyuklia kabla ya mkutano wake na Rais Kim Jong Un nchini Singapore.

“Korea Kaskazini imetangaza kuwa itaharibu kituo chake cha kufanyia majaribio silaha za kinyuklia mwezi huu kabla ya mkutano mkuu Juni 12,” Trump aliandika kwenye Twitter.

“Asante, hiyo ni ishara nzuri sana,” aliongeza.

Kituo hicho kilichoko Punggye-ri, kaskazini mashariki ya Korea Kaskazini kitaharibiwa mbele ya wanahabari wa kigeni kati ya Mei 23 na 25 kama hatua ya Rais Kim Jong Un ya kujitolea kusitisha silaha za kinuklia.

Hata hivyo, kuna wanaodai kwamba nchi hiyo haijatangaza hadharani kujitolea kwake kuachana na silaha zake ikiwa ni pamoja na makombora yaliyo na uwezo wa kufika Amerika.

Amerika inataka Korea Kaskazini iharibu kabisa silaha za kinuklia na ithibitishwe imefanya hivyo na kusisitiza kuwa ni lazima ithibitishwe.

Buhari kukutana na Trump White House

Na AFP

RAIS wa Nigeria Muhammadu Buhari, Jumatatu atakutana na Rais Donald Trump wa Amerika jijini Washington na kuwa kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kukaribishwa na Trump katika ikulu ya White House.

Trump anapigwa darubini kufuatia tamko lake alilotukana nchi za Afrika ambalo alikanusha baadaye.

Uhusiano wa Trump na mataifa ya Afrika uliingia ndoa zaidi Machi mwaka huu alipomfuta kazi aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Rex Tillerson akiwa Nigeria kwenye ziara yake ya kwanza Afrika.

Hatua hiyo ilifichua machache kuhusu sera za utawala wa Trump kwa Afrika. Ziara ya Buhari inajiri siku chache baada ya Trump kukutana na Chansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Kulingana na taarifa ya ikulu ya White House, mazungumzo ya Buhari na Trump yatahusu vita dhidi ya ugaidi na ukosefu wa usalama, ukuaji wa uchumi na demokrasia nchini Nigeria ambayo itaandaa uchaguzi wa urais Februari mwaka ujao.

Nigeria inapigana na magaidi wa Boko Haram kwa mwaka wa tisa sasa na watu zaidi ya 20,000 wameuawa na magaidi hao.

 

 

FBI wavamia ofisi ya wakili wa Trump kuhusu ulaghai na filamu za ngono

Na CHRIS ADUNGO

WASHINGTON, AMERIKA

KIKOSI maalum cha polisi, FBI kimevamia ofisi ya wakili wa kibinafsi wa Rais Donald Trump,  Michael D. Cohen (pichani) katika Kituo cha Rockefeller usiku wa kuamkia Jumanne na kutwaa rekodi za biashara, baruapepe na stakabadhi kuhusu mada mbalimbali ikiwemo malipo ya filamu za ngono.

Lakini Rais Trump katika mrejesho wake wenye ghadhabu, alikejeli hatua hiyo baada ya kuibuka kuwa ofisi hiyo ilivunjwa ili kumchunguza wakili huyo kuhusu madai ya ulaghai wa benki.

Bw Trump aliisuta Idara yake ya Haki akisema hatu ahiyo inaongozwa na lengo fiche na kusisitia kuwa maafisa wa F.B.I ‘walivunja’ ofisi ya Bw Cohen.

Rais huyo aliyeongea katika ofisi yake ya White House, kabla ya ya kukutana na makamanda wa ngazi ya juu kuhusu uwezekano wa Amerika kuvamia Syria, alitaja uvamizi wa F.B.I kuwa “kitendo cha aibu” na “shambulizi la kikweli dhidi ya nchi yetu.”

Haijabainika iwapo maafisa hao walijitoma ndani ya ofisi ya Bw Cohen, lakini maajaenti hao walikuwa na kibali cha kuchakura ofisi hiyo, na hivyo wangewaarifu wafanyakazi wa hoteli hiyo kuwakubalia kuingia.

Stakabadhi zinaonyesha kibali hicho kilitolewa miaka mingi iliyopita.

Malipo yaliyotolewa kwa muigizaji wa filamu za ngono, Stephanie Clifford, anayejulikana kama Stormy Daniels, ni moja kati ya mda nyingi ambazo zinachunguzwa na FBI.

Kibali hicho ni mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na viongozi wa mashtaka kuingilia biashara za siri za Rais Trump, na kinamkosesha usingizi.

 

Wakenya wengine 20 watimuliwa Amerika

Na MWANDISHI WETU

WAKENYA 20 ni miongoni mwa watu 100 waliofurushwa Marekani kutokana na swala tata la wahamiaji haramu huku wengine wakiwa ni raia kutoka mataifa jirani ya Somali na Sudan Kusini.

Polisi na maafisa wa idara ya uhamiaji uwanjani JKIA walisema ndege hiyo ya Omni International Airline ambayo ni ya kibinafsi ilibeba watu 114 na ilitua uwanjani humo Ijumaa asubuhi.

Wakenya hao baadaye waliruhusiwa kuenda nyumbani huku zaidi ya wasomali 60 na raia 24 kutoka Sudan Kusini waliobaki kwenye ndege hiyo wakisafirishwa hadi miji ya Mogadishu na Juba mtawalia.

Wahamiaji hao ndio mkumbo wa mwisho wa wahamiaji haramu wanaorudishwa hapa nchini kwa muda wa miaka miwili ambayo Rais wa Marekani Donald Triump amekuwa uongozini.

Zaidi ya wakenya 100 walihamishwa kutoka taifa hilo mwaka 2017 ambayo ilikuwa idadi kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mwaka wa 2016 wakenya 63 walirejeshwa kutoka taifa la Marekani. Mwaka jana idadi hiyo iliongezeka hadi 103.

Kulingana na maafisa wa uhamiaji, Marekani waliwatimua raia 2,134 kutoka mataifa yanayopatikana chini ya jangwa la Sahara kufikia Septemba 30 mwaka 2017.

Idadi hiyo ilikuwa mara mbili ya raia 920 waliofukuzwa kutoka taifa hilo mwaka 2016. Jumla ya raia 521 wenye asili ya kisomali walirejeshwa makwao mwaka jana ikilinganishwa na 198 mwaka 2016.

Ripoti kutoka idara ya uhamiaji ya Marekani inaonyesha kwamba raia 226,119 walikuwa nchini humo bila kufuata kanuni za uhamiaji na walirudishwa katika mataifa yao mwaka 2017.

Mwaka 2016 ambapo Rais Trump aliingia uongozini idadi hiyo ilikuwa 240,225 hii ikiwa ni ongezeko la watu 13,106.

Ripoti hiyo inaonyesha Marekani inazidi kuongeza juhudi zake katika kuwatimua raia ambao wanaishi nchini humo kinyume cha sheria. Wengi wa watu hao kwa sasa wanakamatwa na maafisa kutoka idara ya uhamiaji.

Wengi wa wanaorejeshwa haswa kutoka Bara la Afrika, wanasemekana wameishi Marekani zaidi ya muda unaotakikana kulingana na kipindi kilichoandikwa kwenye visa zao za kuishi nchini humo.

Hata hivyo, kesi nyingi zilizowasilishwa na wahamiaji katika mahakama za Marekani zinachangia kujikokota kwa mchakato wa kuwarejesha wengi wao.

 

Trump atarajiwa kuzuru Kenya

Na PRAVINDOH NJUGUNATH

RAIS wa Amerika Donald Trump anatarajiwa kuzuru Kenya wiki ijayo katika ziara yake ya kwanza barani Afrika.

Trump anapaniwa kuzindua barabara Kuu ya Mombasa- Nairobi inayoendelea kupanuliwa kwa ufadhili kutoka serikali yake na ile ya Kenya.

Serikali ya Kenya imekaa kimya kuhusu ziara hiyo ya siku tatu ya Rais Trump kwa sababu ya usalama wa kiongozi huyo wa taifa lenye uwezo zaidi duniani.

Uchunguzi wa Taifa Jumapili umebainisha kuwa tayari maafisa wa Federal Bureau of Investigation (FBI) kutoka Amerika wamewasili nchini na wanaendelea kushirikiana na wenzao wa Kenya kulainisha usalama wa Trump.

“Tayari tumepokea zaidi ya maafisa 100 wa FBI na tumewatuma maeneo ambayo Trump atatembelea wakati wa ziara yake,” alisema Mkuu wa Polisi jijini Nairobi Seetanoh Lutchmeenaraidoh.

Bw Lutchmeenaraidoh hata hivyo, hangethibitisha iwapo maafisa hao wa FBI wamekuja kwa sababu ya ziara hio ya Trump, lakini alisema Kenya inatarajia ‘mgeni mashuhuri.’

Duru ziliambia Taifa Jumapili kuwa kutimuliwa kwa Balozi wa Amerika humu nchini Robert Godec kulikuwa sehemu ya kutayarisha ziara ya Trump,kwa kuleta balozi mwingine ‘anayekubalika’ na Wakenya wote.

Hivi majuzi, aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Rex Tillerson alifika nchini kwa kile kilionekana kama kuandaa ziara ya kiongozi huyo.

Barabara Kuu ya Mombasa- Nairobi imepanuliwa kwa gharama ya Sh380 bilioni na kiasi kikubwa cha fedha hizo kimefadhiliwa na serikali ya Trump.

 

Trump amtimua Godec, ateua Kyle McCarter kutwaa nafasi yake

Na WYCLIFFE MUIA

RAIS Donald J. Trump Alhamisi amemfuta kazi Balozi wa Amerika nchini Kenya Robert Godec na nafasi hiyo akampa Seneta wa Illinois, Kyle McCarter.

Taarifa kutoka White House alisema Bw McCarter ana ufahamu kuhusu Kenya baada ya kuhudumu kama mmishonari na Mkurugenzi wa kampuni ya Each One Feed One International,iliyokuwa na afisi yake eneo la Mukothima,Kaunti ya Tharaka-Nithi.

“Seneta McCarter amefanya kazi na shule za kibinafsi za K-8 ambapo alisaidia watoto masikini na mayatima. Alitoa huduma za matibabu kwa zaidi ya watu 15,000 kila mwaka alipokuwa mkurugenzi wa Each One Feed One International,” ilinukuu taarifa ya Ikulu.

Katika mtandao wake wa Twitter, McCarter alimshukuru Rais Trump kwa uteuzi huo na kuelezea furaha yake ya kutumwa kuhudumu Kenya.

“Ni heshima kubwa kwa kutumwa na Rais Trump na taifa la Amerika kwenda kurudi kuhuduma taifa ambalo nimeishi na kufanya kazi,”alisema Bw McCarter.

Seneta huyo alisema anakusudia kukuza uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ili kuacha wosia unaompendeza Mungu na raia wa mataifa yote.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Amerika, McCarter na mkewe wanaongea Kiswahili sanifu baada ya kuishi Kenya kwa muda.

Uteuzi wa seneta huyo unatarajiwa kuidhinishwa na kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Kigeni nchini Amerika.

“Nina upendo mkubwa kwa Kenya,” McCarte aliambia gazeti moja nchini Amerika.

Baada ya kuidhinishwa na Seneti, McCarter atachukua mahali pa Bw Godec ambaye muhula wake nchini Kenya ulikumbwa na shutuma kutoka kwa muungano wa upinzani NASA uliodai kuwa anaegemea upande wa serikali.

Godec aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama mnamo 2012 kuwa balozi wa Kenya na kabla ya hapo alihudumu kama balozi wa Amerika nchini Tunisia kutoka 2006 hadi 2009.

Katika ujumbe wake wa kwaheri, Godec alisema anajivunia ushirikiano aliokuza mataifa hayo mawili katika nyanja za kilimo, afya, biashara, uwekezaji, usalama pamoja na uongozi.

“Kenya ina mahali pazuri katika moyo wangu. Ningependa kusema asanteni sana kwa serikali ya Kenya, raia wa Kenya na wenzangu katika ubalozi kwa ushirikiano mzuri wa zaidi ya miaka mitano niliyohudumu hapa,”alisema Bw Godec katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

 

Walanguzi wote wa dawa za kulevya wanyongwe – Trump

Na AFP

RAIS Donald Trump wa Amerika sasa anataka walanguzi wa dawa za kulevya wanyongwe kama njia mojawapo ya kukabiliana na mihadarati nchini humo.

Rais Trump alizindua rasmi pendekezo hilo alipokuwa akihutubu katika eneo la Manchester jimboni New Hampshire.

“Walanguzi wa mihadarati ni watu wabaya na tunahitaji kuwachukulia hatua kali. Ikiwa tutawahurumia basi mihadarati itaendelea kutuathiri, wanyongwe,” akasema Rais Trump.

Jumla ya watu milioni 2.4 ni waraibu wa dawa za kulevya ambazo zinajumuisha heroini. Inakadiriwa kuwa dawa za kulevya huua watu 115 kwa siku, kulingana na takwimu za Idara ya Afya.

Rais Trump aliahidi kukabiliana na tatizo sugu la dawa za kulevya lakini kufikia sasa hajapiga hatua yoyote.

Kulingana na sheria mpya, watu wanaoua baada ya kutumia dawa za kulevya wanastahili kuhukumiwa adhabu ya kifo. Lakini kufikia sasa hakuna mshukiwa amehukumiwa kwa kutumia sheria hiyo.

Tafiti ambazo zimewahi kufanywa zinaonyesha kuwa, asilimia 55 ya Waamerika wanaunga mkono adhabu ya kifo dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya.

 

 

Trump ampiga kalamu Rex Tillerson akiwa Afrika

Na BENSON MATHEKA

RAIS wa Amerika, Donald Trump alimfuta kazi waziri wake wa mashauri ya nchi za kigeni, Rex Tillerson, siku moja baada ya kuzuru Kenya.

Mnamo Jumatatu, Bw Tillerson alikatiza ziara yake barani Afrika na kurudi Amerika katika kile kilichotajwa kama kushughulikia masuala ya dharura.

Kwenye ujumbe wa Twitter punde tu baada ya Bw Tillerson kurejea Amerika, Bw Trump alitangaza kwamba alikuwa amemteua Mkurugenzi wa shirika la ujasusi (CIA) Bw Mike Pompeo kuwa waziri mpya wa mashauri ya kigeni.

“Mike Pompeo, Mkurugenzi wa CIA, atakuwa waziri wetu mpya wa mashauri ya nchi za kigeni. Atafanya kazi nzuri. Asante Rex Tillerson kwa huduma zako,” Trump alisema kwenye Twitter.

Bw Tillerson aliwasili Nairobi Ijumaa muda mfupi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na hasimu wake wa kisiasa Raila Odinga.

Alikutana na kushauriana na Rais Kenyatta kabla ya kushauriana na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Kenya, Dkt Monica Juma na mwenzake wa utalii Najib Balala.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi, alisema alifurahishwa na mkutano wa Rais Uhuru na Bw Odinga akitaja hatua hiyo kuwa muhimu kukuza uwiano nchini.

Mnamo Jumamosi, alipangiwa kuhudhuria kikao pamoja na waziri wa afya Sicily Kariuki katika hospitali ya Pumwani lakini kilifutiliwa mbali dakika za mwisho ikisemekana alikuwa ameugua. Alitarajiwa kuzuru Somalia lakini akafutilia mbali ziara hiyo.

Aliondoka Kenya Jumatatu kuelekea Chad na Nigeria.

Trump akiri Urusi iliingilia uchaguzi wa Amerika 2016

Na AFP

WASHINGTON, AMERIKA

RAIS Donald Trump, alikiri Jumanne kwamba Urusi na ‘nchi nyingine’ ziliingilia uchaguzi wa urais uliofanywa mwaka 2016 ambao alitangazwa mshindi, lakini akaahidi hilo halitawahi kufanyika tena.

Akizungumza kwenye kikao cha wanahabari ambapo aliandamana na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, alidai pia kuwa uingiliaji wa Urusi haukuathiri matokeo katika uchaguzi huo.

“Warusi hawakuathiri kura zetu kwa njia yoyote ile lakini kwa hakika, kulikuwa na uingiliaji na pengine pia kutoka kwa nchi nyingine na watu wengine binafsi,” akasema Trump, ambaye amekuwa akipuuzilia mbali ushawishi wa Urusi kwake na amekuwa akipinga vikali madai kwamba wasimamizi wa kampeni zake walishirikiana na Urusi.

Alipoulizwa kama anahofia kitendo hicho kitashuhudiwa tena, rais huyo alisema, “Tutazuia chochote watakachojaribu kufanya kwa kila njia tuwezavyo. Huwezi kukubali mfumo wa uchaguzi kuvurugwa kwa njia yoyote na hatutaruhusu hilo lifanyike.”

Aliongeza: “Hatujasifiwa na mtu yeyote lakini ukweli ni kwamba tunajitahidi sana kuandaa chaguzi zijazo.”

 

Tisho

Wakati huo huo, rais huyo alikashifu sheria za kibiashara za Muungano wa Ulaya (EU) na kusema muungano huo umefanya iwe vigumu mno kwa kampuni za Amerika kuendeleza biashara zao na akatishia kuongeza ushuru wa bidhaa za mataifa ya EU zinazoingizwa Amerika.

Trump, ambaye ametishia kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa vyuma vinavyoingizwa kutoka nchi za kigeni na asilimia 10 kwa mabati alisema haogopi hata kama kutazuka mgogoro wa kibiashara.

Alionya pia kwamba yuko tayari kuongeza ushuru wa magari ya Ulaya yanayoingizwa Amerika, mengi yakiwa yanatoka nchini Ujerumani.

“Wanafanya iwe vigumu sana kwetu kufanya biashara nao, ilhali wanaleta magari yao na kila kitu kingine Amerika. Wanaweza kufanya chochote kile watakacho lakini wakifanya hivyo, basi tutaweka ushuru mkubwa wa silimia 25 kwa magari yao na mniamini nikisema hawataendelea kwa muda mrefu,” akasema.

Kwa upande wake, Lofven alionya kwamba uhuru na uwazi wa kibiashara ni muhimu sana kwa Sweden na EU.
Aliongeza kuwa ushuru mkubwa utaathiri viwanda vya Ulaya hali wao hutengeneza tu asilimia 10 ya vyuma ulimwenguni huku Uchina ikitengeneza asilimia 50.

“Ninaamini ushuru ukiongezwa tutaumia katika siku zijazo. Hakika, ninaunga mkono juhudi za Uropa kuendeleza biashara chini ya mfumo usiokuwa na vikwazo vingi,” akasema waziri huyo mkuu.

Manusura akejeli Trump kwa kuzembea kudhibiti umiliki wa bunduki

Na MASHIRIKA

MANUSURA wa shambulio katika shule ya Parkland, Jumamosi alimlaumu Rais Donald Trump kwa kuwa na uhusiano na chama cha taifa cha bunduki (NRA) huku maelfu ya watu wakikusanyika Florida kushinikiza hatua za haraka zichukuliwe kudhibiti umiliki wa silaha.

Siku tatu baada ya mvulana aliyekuwa na bunduki kufyatua risasi na kuua watu 17 katika shule ya upili ya Marjory Stoneman Douglas, Emma Gonzalez 18, alitoa hotuba kwa wanafunzi, wazazi na wakazi wa mtaa ulio karibu wa Ft. Lauderdale.

“Kwa kila mwanasiasa anayepokea michango kutoka kwa NRA, aibu kwako!” alisema mwanafunzi huyo na kumshtumu Trump kwa kupokea mamilioni ya pesa kutoka kwa chama hicho kufadhili kampeni yake ya uchaguzi. Umati ulijibu kwa kusema : “Aibu kwake!”

“Haya yatakuwa mauaji ya mwisho ya kufyatuliwa risasi. Tutabadilisha sheria,” aliapa na kumshutumu Nikolas Cruz 19 ambaye alinunua bunduki halali licha ya kujulikana kwamba alikuwa na tabia ya kuzua ghasia.

“Suala la iwapo watu wanafaa kuruhusiwa kumiliki silaha si suala la kisiasa. Ni suala la uhai na kifo na linapaswa kukoma kuwa suala la kisiasa,” alisema Gonzalez.

Jijini Washington, wanasiasa walisema kwamba NRA halitaguswa huku Trump mwenyewe akisema sababu ya watu kuwamiminia risasi wengine linahusu matatizo ya akili bila kuzungumzia suala la kuthibiti umiliki wa silaha.

“Ikiwa rais anataka kuja na kuniambia ana kwa ana kwamba huu ulikuwa mkasa mbaya na kwamba hakuna hatua zitakazochukuliwa, basi nitafurahia kumuuliza ni pesa gapi alizopata kutoka kwa NRA,” alisema Gonzalez kwenye hotuba yake.