Safaricom ilichangia Sh557 bilioni kwa pato la taifa – Ripoti

Na LEONARD ONYANGO

KAMPUNI ya Safaricom ilichangia asilimia 5.2 ya pato la taifa (GDP) katika mwaka wa matumizi ya fedha wa 2020/2021.

Ripoti kuhusu uthabiti wa biashara inaonyesha kuwa kampuni hiyo ya mawasiliano ya simu, ilichangia Sh557.1 bilioni katika uchumi nchi kati ya Aprili 1, 2020 na Machi 31, 2021.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Safaricom, inaonyesha kuwa kampuni hiyo ilitoa ajira za moja kwa moja kwa watu 190,273 ndani ya kipindi hicho.

Mwenyekiti wa kampuni ya Safaricom, Michael Joseph aliyekuwa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo jijini, alisema zaidi ya Wakenya milioni moja walinufaika na ajira zisizo za moja kwa moja kutokana na huduma zinazotolewa na kampuni hiyo.

Safaricom iliyo na zaidi ya wateja milioni 31, inadhibiti asilimia 64 ya soko la mawasiliano ya simu nchini.Ripoti iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano (CA) majuzi inaonyesha kuwa asilimia 68.2 ya Wakenya waliwasiliana kwa kutumia laini ya Safaricom kwa njia ya sauti kati ya Aprili na Juni, 2021.Kati ya Aprili 1, 2020 na Machi 31, 2021, Safaricom ilijipa pato la Sh82 bilioni kutokana na mawasiliano ya sauti

.“Lengo letu kuu ni kuhakikisha kuwa tunabadilisha maisha ya watu,” akasema Bw Joseph.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Safaricom, Peter Ndegwa, alisema kwamba kampuni hiyo imepanda jumla ya miti 650,000 katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Kampuni ya Safaricom inalenga kupanda miti milioni 5 ndani ya miaka mitano ijayo,” akasema Bw Ndegwa.

Muungano wa kaunti umekufa

Na Barnabas Bii

MUUNGANO wa kiuchumi wa kaunti za Kaskazini mwa Bonde la Ufa (NOREB), uliopigiwa upatu kubadilisha chumi za eneo hilo, sasa unaelekea kufa.

Licha ya kwamba ulibuniwa kuvutia wawekezaji wa kimataifa na wa humu nchini ili kuinua kilimo, muungano huo sasa haupo hai na hata sekretariati yake haitekelezi jukumu lolote.

Imebainika kwamba kaunti saba zilizotia saini mkataba wa kuingia kwenye muungano huo tayari zimejiondoa na kuacha tu Uasin Gishu.

Kaunti hizo ni Samburu, Baringo, Turkana, Nandi, Pokot Magharibi, Trans-Nzoia na Elgeyo-Marakwet.Gavana wa Nandi, Stephen Sang’, alikiri kwamba Noreb inakabiliwa na changamoto za kufaulisha baadhi ya miradi iliyokumbatia mwanzoni kutokana na ukosefu wa kifedha.

Bw Sang hata hivyo, alikanusha vikali kwamba kaunti yake imejiondoa Noreb kutokana na hali kwamba pia ipo katika muungano wa kiuchumi wa kaunti za Ziwa Viktoria (LREB).

Kaunti wanachama wa LREB ni Bomet, Bungoma, Busia, Homa Bay, Kakamega, Kericho, Kisii, Kisumu, Migori, Nandi, Nyamira, Siaya, Trans Nzoia na Vihiga“Bado tupo Noreb kutokana na wazo jumuishi la kuinua viwango vya kilimo na ufugaji.

Hata hivyo LREB ndiyo soko ya mazao hayoya kilimo,” akasema Bw Sang.

2020: Waliong’aa na kugusa Wakenya kwa njia ya kipekee

Na BENSON MATHEKA

INGAWA mwaka huu umekuwa mgumu kwa Wakenya, kuna waliong’ara katika nyanja mbalimbali na kugusa wengi kwa kuonyesha utu.Baadhi yao walitambuliwa kimataifa na kutuzwa kwa juhudi zao wakiwemo walimu, wafanyakazi, wanafunzi na wanamichezo.

Michael Munene, Landilodi mkarimu

Wakati wamiliki wa nyumba za kukodisha katika maeneo ya mijini walipokuwa wakihangaisha walioshindwa kulipa kodi kufuatia athari za janga la corona, Bw Michael Munene aligusa wengi kwa kuwasamehe wapangaji wa ploti zake katika Kaunti ya Nyandarua kwa miezi minne na hata kuwapa misaada ya chakula.

“Tunafaa kuwa na utu hata kama tunataka pesa. Ulikuwa wakati wa janga nao wapangaji hawakuwa kazini. Niliamua kuwapa afueni kwa sababu ninaelewa masaibu yao. Kama nilivyosema wakati huo, mimi nimewahi kuwa mpangaji na ninaelewa shida za watu,” asema.

Jane Kimiti, mwalimu bora barani Afrika

Mwalimu mkuu wa shule ya wasichana ya Othaya kaunti ya Nyeri alitawazwa mwalimu bora barani Afrika na muungano wa Afrika mwaka huu kwa kubuni mbinu bora za ufundishaji wa wanafunzi.

Bi Kimiti alitambuliwa kwa mbinu za kuhimiza na kuhakikisha wanafunzi wanadumisha nidhamu. Wakati walimu walikuwa wametulia nyumbani baada ya shule kufungwa, Bi Kimiti alianzisha mfumo wa kuhakikisha wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo.

“Tulishirikiana na machifu wa maeneo husika kuendeleza elimu ya jamii bila kujali shule wanakosomea wanafunzi.

“Tuliwaongoza na kufuatilia kuhakikisha hawapotoki, kuozwa mapema na tabia nyingine zizofaa.Ushindi huu unaonyesha walimu barani Afrika wanaweza kufanya makubwa kupitia ushirikiano,” asema Bi Kimiti aliyetangazwa mshindi Disemba 21.

Stephen Wamukota, 9, alivumbua mashini ya kuosha mikono.

Mnamo Juni, Stephen Wamukota, mvulana mwenye umri wa miaka 9, kutoka kijiji cha Mukwe, kaunti ya Bungoma alivumbua mashini ya kuosha mikono kuepusha watu wengi katika maeneo ya umma kushika sabuni na mifereji.

Uvumbuzi wake ambao imetumiwa na mafundi kuunda mashini sawa, ulisaidia kupunguza hatari ya kusambaa kwa virusi vya corona. Habari zake ziliangaziwa na vyombo vya habari kote ulimwenguni.

“Ilikuwa furaha sana kuona mwanangu akifanya jambo la kusaidia umma. Uvumbuzi wake ulifanya mashini sawa kuundwa kote nchini. Wanahabari wa kimataifa walifika na kuangazia habari zake hadi akapata tuzo la Uzalendo,” asema babake James Wamukota.

Amina Ramadhan, polisi mwenye utu

Ingawa maafisa wa polisi walilaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakitekeleza amri ya kutotoka nje usiku ilipotangzwa Machi mwaka huu kuzuia msambao wa virusi vya corona, mmoja wao aligusa wengi kwa kuwasaidia akina mama waliochelewa kufika nyumbani.

Amina Mutio Ramadhan, aliyehudumu katika kituo cha polisi cha Embakasi, Nairobi aliwasaidia akina mama na watoto wao wakati wenzake walikuwa wakiwadhulumu raia.

“Kama mama na afisa wa polisi, niko na jukumu la kuhakikisha usalama wa kila mmoja. Polisi hutumia nguvu panapohitajika na sio kila wakati. Kuwa na utu ni muhimu,” asema Amina.

Wahudumu wa afya

Katika mwaka ambao corona ilitishia kuangamiza binadamu wote Kenya na ulimwenguni, watu wakiwa nyumbani kwa hofu, wahudumu wa afya walikuwa msitari wa mbele kukagua, kupima, kutibu na kuhamasisha watu jinsi ya kujikinga na virusi vya corona.

Baadhi yao waliambukizwa virusi hivi wakihudumia wagonjwa ambao walinusurika.

Priscilla Kioko, Rebecca Mutua, Faith Mailu

Japo maafisa wengi wa polisi walilaumiwa kwa kutendea raia ukatili wakitekeleza kanuni za kuzuia msambao wa corona, wanawake hawa watatu walijitolea kuwapikia chakula maafisa waliokuwa kwenye kizuizi eneo la Komarock kwenye barabara ya Nairobi,Kangundo.

Maafisa hao waliokuwa wakizuia wakazi kuingia jiji la Nairobi lilipofungwa baada ya maambukizi kuongezeka hawakuwa na mbinu ya kupata chakula baada ya hoteli kufungwa.

Juhudi zao za kuonyesha utu ziliwafanya kukabidhiwa tuzo za Uzalendo mwaka huu. Bi Mailu anasema hawakutarajia kutambuliwa kwa kuwa lengo lao lilikuwa kuwaepusha maafisa hao kuumia kwa njaa wakiwa kazini wakati biashara nyingi zilikuwa zimefungwa.

“Tulitumia mapato yetu kwa shughuli hiyo hadi kizuizi hicho kilipoondolewa,” asema Bi Mailu.

Akothee alilipia kodi wasanii

Msanii Esther Akoth maarufu Akothee alijitolea kuwasaidia wasanii wenzake walioshindwa kulipa kodi ya nyumba na kupata chakula wakati shughuli za burudani zilipigwa marafuku kufuatia janga la corona.

Aliguswa na hali ngumu ambayo wasanii hao walikuwa wakipitia. Aidha alitoa misaada ya chakula kwa wakazi wa maeneo tofauti nchini kupitia wakfu wake wa Akothee Foundation.

“Niliguswa moyo kuona wasanii wenzangu wakiathirika kiasi cha kulala njaa na nikajitolea kuwafaa kwa kidogo nilichopata waweze kulipa kodi na kupata riziki hata kwa siku moja. Siku yangu ya kuzaliwa ilikuwa Aprili na niliamuautu kusaidia wakazi wa baadhi ya maeneo kama Kilifi ambao walikuwa wakiteseka,” asama Akothee ambaye ni mwanachama wa kamati ya kukabiliana na corona ya kaunti za Ziwa Victoria.

Brigid Kosgei, aliwika London Marathon

Alishinda mbio za London Marathon mwaka huu mnamo Oktoba 4 ingawa ulikuwa mwaka mgumu kwa wanamichezo baada ya shughuli za spoti kusimamishwa.

Benard Sang, Diana Chemtai, walishinda Istanbul Marathon

Wanariadha wengine wa Kenya waliowika ziliporejelewa ni Benard Cheruiyot Sang na Diana Chemtai Kipyogei ambao walishinda makala ya 42 ya mbio ndefu za Istanbul nchini Uturuki mnamo Novemba 4.Felix Kimutai, alikuwa wa pili nyuma ya Sang kwenye mbio hizo.

Uhuru awaruka Wakenya kuhusu ushuru nafuu

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliruka ahadi yake kwa Wakenya kuwa ushuru wa VAT ungesalia asilimia 14 hadi Juni 30 mwaka ujao.

Kwa kuweka saini Mswada wa Ushuru jana, Rais aliashiria kuwa ushuru huo utarudi asilimia 16 kuanzia Januari 1, 2021 kinyume na alivyokuwa ameahidi mnamo Septemba mwaka huu.

Hii ni baada ya wabunge mnamo Jumanne kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Ushuru, unaolenga kuondoa afueni ya ushuru ambayo serikali iliwapa Wakenya mwezi Aprili kuwapunguzia makali ya kiuchumi yaliyosababishwa na janga la Covid-19.

Kenya bado haijafanikiwa kukabili kikamilifu virusi vya corona na maambukizi yanaendelea kuongezeka huku mapato ya makampuni na watu binafsi yakipungua.

Hatua ya wabunge na Rais Kenyatta inaipa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) idhini ya kurejesha kiwango cha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya asilimia 16, badala ya asilimia 14 ambayo imekuwa ikitozwa tangu Aprili.

Hatua hii inashiria kuwa huku KRA ikiimarisha kiwango cha ukusanyaji ushuru, wafanyabiashara wataongeza bei ya bidhaa ili kuziba hasara itakayotokana na ongezeko hilo la ushuru; mzigo ambao utabebeshwa wanunuzi au watumiaji huduma.

Mafuta ya kupikia, umeme na salio la kuzungumza kwa simu (airtime) ni miongoni mwa bidhaa na huduma zitakazopanda bei.Nafuu ambayo waajiriwa walipata serikali ilipopunguza ushuru unaotozwa mishahara (PAYE) pia imeondolewa.

Inamaanisha kuwa asilimia 30 ya mishahara itakatwa na KRA kuanzia Januari 1; badala ya asilimia 25 ambayo imekuwa ikitozwa tangu Aprili ili kuwakinga dhidi ya makali ya Covid-19.

Mswada huo ambao uliwasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha, Bi Gladys Wanga, pia umerejesha kiwango cha zamani cha ushuru unaotozwa kampuni (Corporate Tax); ambacho ni asilimia 30.

Katika afueni iliyotolewa na serikali mwezi Aprili, ushuru huo ulipunguzwa hadi kima cha asilimia 25.Hata hivyo, wafanyakazi wanaopokea mshahara wa Sh24,000 kwenda chini, wataendelea kufurahia afueni ya serikali kwani hawatatozwa ushuru wowote, kama ambavyo wamekuwa wakifurahia tangu Aprili.

“Lengo kuu la mswada huu sio kuumiza wananchi bali kuwasaidia kwa kuiwezesha serikali kuongeza mapato yake ili iweze kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi wa umma.

“Wafanyabiashara hawapasi kuongeza bei za bidhaa kwa sababu kimsingi viwango vya ushuru havijaongezwa. Kile mswada imefanya ni kurejesha viwango vya ushuru ambavyo vilikuwepo awali kabla ya afueni ya serikali,” alieleza Bi Wanga.

Lakini Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa alitofautiana na kauli hiyo akisema wafanyabiashara wataongeza bei za bidhaa za kimsingi haswa wakati kama huu wa sherehe za Krismasi.

“Wafanyabiashara huongozwa na uchu wa kutaka kuchuma faida. Nina hakika wataongeza bei kwa kisingizio kwamba KRA imeongeza ushuru wa VAT kutoka asilimia 14 hadi 16, ilhali hili sio jambo jipya,” akasema Bw Ichung’wa.

Mbunge huyo alihoji kuwa wafanyabiashara hawakupunguza bei kuendana na afueni ya serikali.Wabunge waliochangia mjadala kuhusu mswada huo waliuunga mkono wakisema itawezesha serikali kuongeza mapato yake na kuondoa hitaji la kukopa fedha. kutoka ng’ambo na katika mashirika ya kifedha ya humu nchini.

“Uchumi wa Kenya uko katika ICU na tukiondoa mpira wa hewa, utaporomoka kabisa. Mzigo wetu wa madeni umefikia Sh7 trilioni na kiwango hicho kinaendelea kupanda. Kwa hivyo, njia ya kipekee ya kuiwezesha serikali kupata pesa ni kuipa idhini ya kutoza viwango vya zamani vya ushuru,” akasema Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale.

Bw Duale ambaye ni kiongozi wa wengi wa zamani aliongeza kuwa hatua ya serikali ya kupunguza VAT, PAYE na ushuru kwa kampuni mnamo Aprili iliwafaidi wafanyabiashara na waajiri na wamiliki wa kampuni husuka wala sio raia wa kawaida.

Mbunge wa Emuhaya Omboki Milemba naye aliitaka serikali kutumia mapendekezo ya mswada huo kukusanya fedha za kupelekwa shuleni chini ya mpango wa elimu bila malipo, fedha za kugharamia mahitaji ya wahudumu wa afya waliogoma, fedha za mgao kwa serikali za kaunti na za kugharamia miradi ya hazina ya ustawi wa maeneo bunge (CDF).

Huenda aina mpya ya corona ikazimisha uchumi wa dunia

WANDERI KAMAU Na BENSON MATHEKA

HALI ya wasiwasi imetanda duniani kufuatia kuchipuka kwa aina mpya ya virusi vya corona, ambavyo vimetajwa kuwa hatari zaidi na wataalamu kuliko ile ambato imekuwa ikihangaisha ulimwengu kwa miezi kumi na moja sasa.

Aina hiyo iligunduliwa kwanza nchini Uingereza siku kadhaa zilizopita na wanasayansi wanasema kwamba, inaenea kwa haraka na kulemea vijana tofauti na iliyoanza kutetemesha ulimwengu kuanzia Desemba mwaka jana na kuathiri zaidi watu wa umri mkubwa.

Tayari, aina hiyo mpya ya corona imeguduliwa katika nchi nyingi za bara Ulaya. Mnamo Jumatatu, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa barani Ulaya (ECDC) kilisema kuwa, aina hiyo ya virusi pia imegunduliwa katika nchi za Australia, Iceland, Denmark, Italia, Uholanzi na Ubelgiji.

Virusi vipya vya corona, pia viligunduliwa Afrika Kusini, ingawa serikali ya taifa hilo imesema ni tofaut nai vilivyopatikana Uingereza.Hata hivyo, serikali nchini humo ilitaja aina hiyo mpya ya virusi kuwa chanzo kikuu cha kuongezeka kwa maambukizi miongoni mwa vijana katika siku za hivi karibuni.

Tayari, nchi kadhaa barani Ulaya na Asia zimesimamisha safari za ndege kwenda Uingereza ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo vipya.Jana, waziri wa afya Mutahi Kagwe alisema, serikali inafuatilia hali kabla ya kuamua kusimamisha safari za ndege kutoka nchi hiyo.

Wizara ya Mashauri ya Uingereza nayo imetoa tahadhari kwa wale wanaopanga kuingia ama kuondoka nchini humo, kuzingatia masharti mapya yaliyotolewa na serikali kudhibiti maambukizi.

“Safari za kimataifa kuingia ama kuondoka Uingereza zimewekewa masharti makali. Nchi zimeanza kufunga mipaka yao na huenda zikatangaza masharti mapya kighafla. Tafadhali shauriana na shirika la ndege unalopanga kusafiria ili kuelewa hali ilivyo,” ikasema wizara hiyo.

Mnamo wikendi, wataalamu nchini Uingereza walitaja virusi hivyo kuwa hatari sana, ambapo vinasambazwa haraka mara saba zaidi ya virusi vya sasa.

Mchipuko huo pia unaonekana kufifisha matumaini ya kupatikana kwa chanjo mpya, hasa baada ya watu waliopewa chanjo hiyo katika nchi kadhaa kuripotiwa kupata matatizo tofauti kiafya.

Haya yanajiri wakati huduma za matibabu zimesambaratika nchini Kenya kutokana na mgomo wa madaktari na wahudumu wa afya.Hofu imezuka kuwa huenda Kenya ikawa mwathiriwa mkuu wa wimbi hilo jipya la maambukizi, kwani ni mshirika wa karibu wa Uingereza na mataifa mengine ya Ulaya.

Kulingana na waziri msaidizi wa Afya Dkt Mercy Mwangangi, virusi hivyo vipya ni changamoto kwa juhudi za kukabiliana na janga ambalo limeathiri sekta ya afya na uchumi.

“Tunafuatilia kwa karibu hali ilivyo Uingereza baada ya kugunduliwa kwa aina mpya ya virusi ambavyo vinaathiri watu wa umri mdogo,” alisema Dkt Mwangangi jana asubuhi.

Mataifa ya Ufaransa, Ujerumani, Italia, Denmark, Uswisi, Ireland, Austria, Ureno, Sweden, Ubelgiji, Bulgaria, Hong Kong, Israeli, Iran, Croatia, Argentina, El Salvador, Chile, Morocco na Kuwait tayari yamepiga marufuku ndege kutoka nchini Uingereza.

Saudi Arabia imesitisha safari zote za kimataifa kwa kipindi cha wiki moja kufuatia kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya corona nchini humo.

Wataalamu wanasema virusi hivyo vinajibadilisha mara kwa mara.Wataalamu sasa wanahofia kuwa chanjo inayoendelea kutolewa kuzuia virusi vya corona nchini humo huenda ikakosa kufanya kazi.

Waziri wa Afya wa Uingereza, Matt Hancock alisema kuwa, virusi hivyo vipya vya corona vinasambaa kwa kasi ya juu na huenda serikali ikalemewa.

Corona inavyoumiza wafugaji wa kuku

Na KEVIN ROTICH

Kabla kuzuka kwa janga la virusi vya corona, biashara ya kuku ilinoga sana nchini ikilinganishwa na hali ilivyo sasa. Ufugaji pamoja na uagizaji wa kuku wa nyama ulikuwa katika kiwango cha juu kufuatia huduma nyingi katika hoteli na sehemu nyingi za kustarehe.

Biashara hiyo ilipigwa jeki na huduma mpya za usafiri kama vile Uber Eats iliyorahisisha kusambazwa kwa bidhaa na kupunguza muda wa kuwafikia wateja.

Lakini mapema mwaka huu, mambo yalibadilika na kubadili mfumo wa kazi na huduma. Baadhi ya mambo yalioathiri shughuli hizi ni pamoja na kusitishwa kwa safari za ndege, kufungwa kwa mipaka, kupungwa kwa safari pamoja na kafiu wakati wa jioni na usiku.

Idadi ya watu wanaotembelea sehemu mbalimbali pia ilidhibitiwa ili kuzuia maambukizi.

Wafanyibiashara katika kaunti ya Nairobi wanasema hali haijarejea kawaida na itachukua muda kabla ya kazi yao kunawiri tena.

“Wakati huu siwezi kusema hali imerejea kawaida ila ninapata matumaini kila baada ya siku. Wateja si wengi ikizingatiwa kuwa bado kila mtu anachunga usalama wake,” akasema mfanyibiashara mmoja jijini Nairobi.

Wamiliki wa hoteli wanasema wamelazimika kupuguza uagizaji wa kuku kutoka kwa wakulima kufuatia idadi ndogo ya wateja na pia masaa chache ya kufamya kazi.

“Wakati huu viwango vya kuaribika kwa bidhaa viko juu. Mara kwa mara unapata wafanyibiashara wengi wanapata hasara haswa wale wanaonunua na kutayarisha michizi vya kuku,” akasema mfanyibiashara mwingine.

Kulingana naye, hali hapo mbeleni wateja wengi walifurika kwenye mikahawa ambapo wengi waliofika kuchelewa walikosa vyakula walivyoitaji.

Bw Solomon Kinyua ni mmoja wa wakulima walioathirika na kulazimika kupunguza idadi ya kuku aliokuwa akifuga kutoka 30, 000 hadi 2, 000.

Katika shamba lake eneo la Marwa kwnye kaunti ya Nyeri, Bwana Kinyua anasema soko ya kuku wake ilipungua ndiposa akapunguza idadi.

“Naweza kusema soko ilipungua kwa asilimia sitini kutokana na masharti yaliyowekwa na serikali na pia kusitishwa kwa soko la kimataifa kama vile katika nchi za Tanzania na Uganda,” akasema.

Aidha, taifa la Uganda limeongeza ada ya mauzo kwa asilimia 25 kwenye bidhaa za kuku kutoka Kenya, asilimia 18 ya VAT, asilimia sita ya kuzuia kodi na asilimia moja ya ushuru wa barabara.

Kwa mfano, kilo moja ya kuku kutoka taifa la Uganda inauzwa kwa Sh200 ilihali iliotoka Kenya ni Sh300.

Kutokana na hayo, mapato ya Bwana Kinyua yamepungua kutoka Sh6 million hadi Sh400, 000 kwa kila msimu wa miezi miwili wa kufuga. ded

Java yawaomba wafanyakazi wajiuzulu kwa hiari

NA WANGU KANURI

Mkahawa wa Java wenye afisi zake kuu jijini Nairobi umewapa wafanyikazi wake notisi ya kujiuzulu  kwa hiari kabla ya wiki mbili kutamatika. Fomu za kujiuzulu zitakuwepo tayari kwa wafanyikazi hapo Novemba 27, 2020.

Kupitia ilani ambayo iliandikiwa wafanyikazi hao, hoteli hiyo ilisema kuwa hata baada ya vikwazo walivyoweka kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19, mauzo yao yamedidimia ikilinganishwa na mwaka jana.

Imesema kuwa kwa wale ambao watajiuzulu kwa hiari yao watapewa marupurupu yao. Mpango huo utakuwa kwa kila tawi la mkahawa huo haswa kwa wafanyikazi ambao wamefanya kazi kwa miaka minne, wafanyikazi ambao hulipwa kutokana na mauzo na wafanyikazi ambao wamefanya kazi kwa miaka mitatu pamoja na wapishi, wanaboda boda, wahudumu na mabawabu ambao wamefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.

Vile vile wafanyikazi hao watapokea mshahara wa siku 15 kwa kila mwaka waliofanya kazi na nyongeza ya mshahara wa mwezi mmoja na nusu ili kufidia siku ambazo hawaendi kazini.

Mkahawa huo wa Java ambao una mikahawa 80 katika nchi zilizoko Afrika Mashariki, umetatizika sana tangu corona ilipobisha. Mnamo Aprili, mkahawa huo uliwakata wafanyikazi mshahara kwa asilimia 40 ili kushughulikia matakwa yaliyowekwa na serikali kwa mahoteli.

Kuwepo kwa kafyu nchini kumetatiza saa ambazo hoteli hufungwa kwa kawaida na hilo likapunguza faida.

LUCY DAISY: Serikali ielewe uchumi umezorota, iwaruhusu wanawake fursa wachuuze bidhaa

Na LUCY DAISY

NCHINI Kenya, kuna wanawake wengi sana ambao hawana namna ya kujipatia riziki. Hawana kazi ilhali wana watoto na familia zinazowategemea. Hivyo basi wanabaki kukimbilia njia mbadala za kujipatia riziki.

Kwa mfano mjini Nairobi, kuna wanawake wengi tu wanauza nguo na chakula kandokando ya barabara. Baadhi wanachuuza huku wamebeba watoto wachanga.

Uchuuzi barabarani ni haramu, na mara kwa mara wanawake hawa hufurushwa na askari wa jiji. Cha kusikitisha ni jinsi askari hawa hutekeleza kazi yao pasina heshima wala huruma.

Wanawachapa viboko akinamama huku wengine wakiwaangusha chini kana kwamba ni vita. Isitoshe, wanamwaga bidhaa zao na kuzikanyagia chini. Unyama huo!

Majuzi nilipokuwa mjini niliwaona askari hawa wakimkamata mwanamke aliyekuwa amebeba mtoto mchanga, wakamcharaza viboko na hata kumuumiza mtoto huyo kando na kuharibu bidhaa alizokuwa akiuza mama huyo.

Mama alilia kwa uchungu akiwarai wamuonee huruma kwani asipofanya kazi ile, hana namna nyingine kabisa ya kuwalisha wanawe na hivyo watakufa njaa.

Ni kweli kwamba kulingana na sheria wachuuzi hawafai kutandika na kuuza bidhaa zao kando ya barabara za mjini.

Lakini serikali haina budi kuelewa kwamba uchumi umezorota na wengi wa wanawake hawa hawana namna nyingine yoyote ya kujipatia riziki.

Ni bora serikali itoea fedha na zile za kaunti zitenge mahali maalum ambapo wachuuzi hawa wanaweza kufanya kazi yao bila bughudha ili angalau wajipatie kibaba cha kila siku.

Wanawake hawa pia hawana budi kufuata kanuni watakapoagizwa kuchuuza bidhaa zao katika maeneo hayo maalum yakatayotengwa, badala ya kuuzia kandokando ya barabara ambapo husababisha msongamano kupindukia wa watu na hatari ya ajali kutokea.

Serikali pia iwaagize askari wake waache kuhangaisha wanawake hawa bila heshima. Wasiwachape na kuwakimbiza kikatili wakiwaumiza na kuwadunisha.

Iwapo lazima wawakamate, wafanye upole na kuwapeleka katika kituo cha polisi ili wafunguliwe mashtaka.

Wateja nao watambue ni makosa kwa yeyote kuuza bidhaa kando ya barabara na pindi wanawake hao watapewa eneo maalum la kuendesha biashara zao, waelekee huko kuendelea kununua bidhaa zao.

Wasiwe wavivu wa kusema sharti waletewe bidhaa katikati ya mji mahali walipo, eti hawataki kusumbuka kwenda mbali kuzinunua.

Uchumi wa nchi yetu umezorota na kila mtu anajaribu juu chini kutafuta riziki.Hakuna aliyechagua kuwa maskini.

Wanawake hawa kama binadamu mwingine yeyote wana haki ya kupewa nafasi ya kujitafutia riziki kwa upole. Polisi na wananchi kwa jumla hawana budi kuwaelewa na kuwaheshimu wanawake hawa.

Nyanya na vitunguu ghali zaidi, viazi na karoti zashuka bei

NA CHARLES MWANIKI

BEI ya vyakula imepanda kwa asilimia 10.6 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, ikilinganishwa na asilimia 11.6 hapo Aprili na Machi. Hata hivyo, bidhaa za mapishi zimesalia ghali.

“Licha ya hali ya hewa kusalia shwari, bei ya baadhi ya vyakula imekuwa ghali kwa sababu ya changamoto za uchukuzi kutokana na kanuni za kudhibiti Covid-19,” ikasema taarifa kutoka Benki Kuu ya Kenya.

Takwimu kutoka Shiriki la Kitaifa la Takwimu kuhusu mfumuko wa bei zinaonyesha kuwa katika mwezi  wa Mei, vitunguu, nyanya na maharagwe zilirekodi ongezeko kubwa zaidi la bei kwa kilo, huku viazi, kaorti na spinachi zikipungua bei.

Bei ya kilo moja na vitunguu ilipanda kwa asilimia 21.8 mwezi uliopita ikilinganishwa na 2019. Nyanya zilipanda bei kwa asilimia 15.9 huku kilo moja ya maharagwe ikipanda bei kwa asilimia 10.9.

Kwa upande mwingine, karoti zilishuka bei kwa asilimia 22.5, spinachi kwa asilimia 16.8 na viazi kwa asilimia 10.5 ilikinganishwa na mwaka uliopita.

 

Huenda asilimia 75 ya kampuni zikafungwa Juni – CBK

NA FAUSTINE NGILA

HALI ya uchumi nchini inazidi kudorora kutokana na makali ya janga la Covid-19, huku serikali ikionya huenda Wakenya wengi zaidi wakapoteza ajira kufikia mwishoni mwa mwezi Juni.

Kulingana na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt Patrick Njoroge, huenda asilimia 75 ya kampuni ndogo na zile za wastani zikalazimika kufunga biashara kutokana na ukosefu wa fedha mwezi ujao.

Akihutubu hapo jana kuhusu athari ya virusi vya corona kwa uchumi, Dkt Njoroge alisema kampuni hizo zinafaa kulindwa dhidi ya hatari ya kuporomoka kwani zinachangia pakubwa kwa kuinua viwango vya ajira pamoja na utajiri wa nchi.

“Uchumi ulitarajiwa kupata pigo zaidi kati ya Aprili na Juni, kutokana na mikakati ya kuzuia kuenea kwa Covid-19 iliyoathiri vibaya sekta za uchukuzi, biashara na hoteli. Hivyo, kiwango cha kukua kwa utajiri wa nchi kinaweza kupungua hadi asilimia 2.4 kutoka 5.4 mwaka uliopita,” akasema.

Na wakati huo huo, hoteli ya kifahari ambayo imekuwa ikihudumu humu nchini kwa miaka 116, Fairmont Norfolk, ilifunga hoteli zake na kuwatimua wafanyakazi wote.

Meneja wa hoteli hizo humu nchini Bw Mehdi Morad, alisema uamuzi huo ulifikiwa kutokana na hali kwamba haijulikani ni lini virusi vya corona vitadhibitiwa na watu kuruhusiwa kuendelea na biashara zao.

“Hatuna budi kufunga biashara kwa sasa. Inasikitisha kuwa hoteli zetu za Fairmont The Norfolk, Fairmont Safari Club zimesitisha huduma kutokana na virusi hivi na mafuriko ya hivi majuzi katika hoteli ya Fairmont Mara Safari Club,” alisema.

Katika sekta ya fedha, benki ya Equity jana ilitangaza kuwa faida yake baada ya ushuru imepungua kwa asilimia 14 kutokana na utoaji wa mikopo ya Sh3 bilioni kwa Wakenya kuwasaidia kukabiliana na hali ngumu ya uchumi katika kipindi hiki cha Covid-19.

Hata hivyo, CBK imeweka asilimia 7 kama kiwango cha riba kwa benki za humu nchini, ili kuwezesha wawekezaji kuomba mikopo nafuu, na kuendelea kufanya biashara na kulipa wafanyakazi.

Hata hivyo, kabla ya virusi vya corona fika humu nchini, hali ya uchumi tayari ilikuwa mbaya, kwaani kampuni nyingi zilikuwa zishawafuta kazi wafanyakazi wake, baada ya kulemewa na biashara.

Baadhi ya kampuni hizo ni Tuskys, Mumias Sugar, Tullow Oil, East African Breweries, Sportpesa, Southern Sun Mayfair Hotel, New KCC, Sameer Africa, Mediamax na nyinginezo.

Mabilioni yatengwa kunyanyua uchumi

NA MWANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta ametangaza juhudi atakazoweka ili kufufua uchumi wa nchi. Mikakati hiyo itahusisha mabilioni ya fedha kunyanyua hali ya biashara nchini na kuendeleza miradi ya serikali.

Sh5 bilioni zitatumika kuajiri wafanyikazi wadogo wadogo wa kukarabati barabara na njia wakati wa mafuriko.

Sh6.5 bilioni zimetengewa Wizara ya Elimu ili kuajiri walimu 10,000, kuajiri wakufunzi wa mitandaoni 10,000 na kununua madawati ya wanafunzi.

Sh10 bilioni zitatumika katika uchunguzi wa ulipaji wa ushuru na Sh3 bilioni kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.

“Tutatafuta njia ya kufungua biashara tena huku tukijizoesha kuishi na virusi vya corona”, Rais alisema  Jumamosi.

Sh1.7 bilioni zitatumika kuongeza vitanda hospitalini na kuajiri madaktari 5,000. Sh3 bilioni zimetengwa kwa kusafirishwa mazao ya shambani huku Sh1.5 milioni zikitumika kusaidia wakulima wa maua na masoko ya kimataifa.

Sh2 bilioni zitatumika kusaidia sekta ya hoteli kwa kuwapa wamiliki mikopo huku Sh1 bilioni zikitengewa kukabiliana na mafuriko na Sh850 milioni kutengeneza visima na matangi ya maji.

Sh540 milini zimetengwa kusaidia katika kampeni ya kuhifadhi mazingira, Sh600 milioni kupiga jeki sekta ya viwanda.

“Ninawahimiza Wakenya tuwe wazalendo daima tukiwa na imani kuwa tutashinda,” akasema.

Alisema kuwa bado familia zenye mapato ya chini zinazoathirika zaidi zitaendelea kupata pesa kila wiki.

Tafsiri: Faustine Ngila

 

Jinsi Kenya inavyoweza kuimarisha viwanda vyake

NA SAMMY WAWERU

Kwenye mojawapo ya vitabu vyake, Neglected Value, Roger Wekhomba ambaye ni mtafiti, amechanganua kwa mapana na marefu namna Kenya inavyoweza kuimarika kupitia uboreshaji wa sekta ya viwanda.

Kitabu hicho chenye jumla ya kurasa 131, Wekhomba ametangulia kuorodhesha vigezo muhimu na malighafi yaliyopuuzwa, haswa yakilenga kilimo.

Kwenye simulizi yake, mtafiti huyo anasema ufukara na ukosefu wa kazi hususan kwa vijana, ni masuala yanayoweza kukombolewa ikiwa Kenya itachukua mkondo wa kuboresha viwanda kupitia malighafi ya ndani kwa ndani, badala ya kuyauza nje ya nchi kisha kununua bidhaa zitokanazo nayo.

Wekhomba anahoji, “Kenya ni taifa lenye ukwasi chungu nzima na kuuza malighafi yetu nje ya nchi badala ya kuyaongeza thamani, halafu tunanunua bidhaa kutoka nje, ni sawa na kubunia mataifa hayo kazi”. “Nchi hii tutaikomboa kwa kutambua na kuthamini sekta ya viwanda, ambayo itatuletea utajiri na kubuni nafasi za ajira.

“Huwa tunazungumza jinsi Kenya ilikuwa katika daraja moja na Malaysia, Korea na Singapore mnamo 1968. Tunakosa kubaini mikakati iliyowekwa kuimarisha nchi hizo,” Wekhomba anaeleza kwenye kitabu chake.

Aidha, katika mataifa hayo sekta ya viwanda imepewa kipau mbele, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa teknolojia. Kinachosababisha Kenya kuendelea kusalia nyuma, ni donda ndugu la ufisadi linalosakatwa na viongozi wenye tamaaa ya ubinafsi.

Kwa kiasi kikuu, viongozi tunaochagua na kuteua wanalaumiwa kuchangia masaibu tunayopitia kama taifa lililojaaliwa, kwa kujishughulikia wao wenyewe na kuendeleza ufisadi. Roger Wekhomba anasema, “taifa litaafikia matakwa na maendeleo iwapo tutachagua viongozi wenye maono kutuongoza na kukumbatia uboreshaji wa viwanda”.

Akieleza kuhusu utajiri tulionao, kwa mukhtadha wa Almasi, anasema nishani hiyo kabla kutolewa ardhini haina thamani wala umuhimu wowote, hadi pale itakapochimbwa, isafishwe na kuingia sokoni.

Wekhomba ni mwenye masikitiko tele anapoona mazao ya kilimo yakitupwa kiholela, mengine yakioza na kuishia kutupwa kwa kuwa hayawezi kulika.

Anapofanya ziara kwenye masoko mbalimbali, kinachomuuma zaidi ni kuona maembe, maparachichi, mapapai, machungwa, ndizi, nyanya, miongoni mwa mazao mengine yaliyotupwa na kuchakaa kwenye majaa.

Kabla kufikia kiwango hicho, huwa katika hali shwari lakini kwa sababu ya ukosefu wa soko, wafanyabiashara wanalazimika kuyatupa. Pia, kuna mazao mengine yanayooza kwa sababu ya ukosefu wa njia bora kuyahifadhi.

Hali hiyo inawiana na taswira ya mashambani, ambapo wakulima hukadiria hasara bin hasara kwa ajili ya ukosefu wa soko. Kadhalika, mawakala wanatajwa kuchangia hilo kwa kununua bidhaa kwa bei duni.

Kwa Rodger, hayo yote yanaweza kuepukika. Anapotazama matunda na bidhaa za kilimo zilizotupwa na zingine kuoza, mjasirimali huyo anaona dhahabu.

Anashangaa ni kwa jinsi gani taifa linashuhudia ukosefu wa kazi hasa miongoni mwa vijana, ilhali mazao hayo ni malighafi kuanzisha viwanda. “Kiwanda si majengo makubwa na mashine za bei ghali. Ukiwa na sufuria, kijiko, mwiko, kichujio, vifaa vingine vinavyotumika jikoni na kiini cha moto basi una kiwanda,” Rodger anaeleza.

Mtafiti huyo ni mkufunzi wa uongezaji thamani mazao ya kilimo, ambapo hutumia matunda mbalimbali na mazaohai kuunda mafuta ya kujipodoa, sabuni na viungo vya kuongeza mlo ladha kama vile ‘tomato paste na sauce’, miongoni mwa bihaa zingine.

“Kwa mfano, maparachichi maarufu kama avocado, huyatumia kutengeneza sabuni isiyo na kemikali yoyote,” afafanua.

Matunda kama haya yaliyotupwa baada ya kukosa wanunuzi ni dhahabu kwake. Anahimiza serikali kufanya hamasa uongezaji thamani kwa mazao ya kilimo. Ni mojawapo ya njia kuimarisha sekta ya viwanda nchini. Picha zote/ Sammy Waweru

Nyanya huzitumia kutengeneza viungo, na anasema kinachomkereketa maini ni kuona zikiozea shambani na kwenye masoko. Akitoa mfano wa kisa alichoshuhudia mwaka uliopita, 2019, kwenye soko moja eneo la Athi River, Roger anasema mfanyabiashara mmoja alikadiria hasara ya kreti tatu za nyanya alizodai zimeoza kwa kukosa wanunuzi.

“Nilimpa Sh100 nikazichukua. Hazikuwa zimeharibika alivyosema. Aidha, nilizitumia kama mtihani kutengeneza kiungo kitokanacho na nyanya, tomato sauce,” asimulia.

Anasema nyanya hizo alipoziongeza thamani, kwa muda wa kuku kumeza punje za mahindi alitia kibindoni jumla ya mapato ya Sh12, 000.

Mojawapo ya vifaa vya jikoni anavyotumia kuongeza mazao ya kilimo thamani. Kuanzisha viwanda kulingana naye hakuhitaji maelfu ya pesa.

“Gharama ilikuwa kununua nyanya, maji, kupakia na kuweka lebo. Hebu tathmini hapa, iwapo kila kreti ningeuziwa Sh2, 000, bado ningepata faida ya kuridhisha ya Sh6, 000,” anasema.

Ni hali inayoshuhudiwa katika masoko mengi nchini, wafanyabiashara na wakulima wakiishia kukadiria hasara isiyomithilika. Nyanya, matunda, viazi na mboga zikiwa katika orodha ya mazao yaliyoathirika pakubwa.

“Wakulima na wafanyabiashara wahamasishwe umuhimu wa kuongeza mazao thamani. Hivyo ndivyo viwanda huibuka,” ashauri Steven Mwanzia, mkulima wa matunda na pia mtaalamu wa masuala ya kilimo.

Mwanzia ambaye hukuza matunda aina ya bukini katika Kaunti ya Kiambu, huyaongeza thamani kwa kuunda sharubati na mvinyo. “Matunda tunayolima huyatumia kuunda juisi, mvinyo na divai,” adokeza.

Baadhi ya sabuni alizotengeneza kwa malighafi na mazao ya kilimo, yakiwamo matunda kama vile maparachichi.

Kulingana na maelezo ya Rodger Wekhomba ambaye huendeshea utafiti na gange ya uongezaji thamani mazao ya kilimo eneo la Kiambu, inachopaswa kufanya serikali ni kutilia mkazo suala la uimarishaji na uboreshaji viwanda.

“Maendeleo si ujenzi wa barabara, ila ni kuona kila raia ana kiini cha mapato. Mataifa yaliyoimarika na kukua kiuchumi ni yanayotilia mkazo uimarishaji wa viwanda. Serikali ielekeze mgao mkubwa katika sekta ya viwanda. Mazao ya kilimo pekee yanatosha kutatua suala la ukosefu wa kazi kwa vijana kupitia viwanda vya uongezaji thamani,” Rodger afafanua, akiongeza kuwa hilo linahitaji hamasa kupitia serikali na wadau husika.

Aliingilia shughuli za kuongeza mazao ya kilimo thamani mnamo 2010, na kufikia sasa ana karakana yenye kiwanda cha kazi hiyo. Amebuni nafasi za vijana kadhaa, bila kusahau bidhaa zake pia ziko sokoni, hatua anayoisifia akisema wauzaji wameweza kujiajiri.

Mwaka 1968 Kenya ilikuwa katika daraja moja na nchi kama vile Korea, Malaysia na Singapore. Mataifa hayo kupitia uongozi bora yamepiga hatua nyingi mbele, ambapo sekta ya viwanda imepewa kipau mbele, yote hayo akiyaangazia kwenye kitabu chake ‘Neglected Value’ akiyalinganisha na Kenya.

Hata ingawa amefanikisha azma yake, anasema changamoto inayozingira sekta ya viwanda nchini ni wanunuzi haswa wenye maduka ya kijumla kukosa kuthamini bidhaa za ndani kwa ndani. Anahimizia serikali kubuni sheria zitakazopiga jeki bidhaa zilizotengenezewa humu nchini, kama vile sokoni ziwakilishe asilimia 60.

Kwenye kitabu chake, ‘Neglected Value’, Rodger anasema Kenya ina utajiri wa kutosha kuanzisha viwanda chungu nzima, ila muongozo na hamasa, ni vigezo vinavyokosa. Mazingira duni ya biashara, mtafiti huyo anataja kama vizingiti vinavyochangia wawekezaji wa ndani kwa ndani kuhofia kuwekeza utajiri wao kwenye viwanda.

Kupitia kitabu chake, Neglected Value, ameipa serikali mwongozo wa vigezo inavyopaswa kuzingatia ili kuboresha sekta ya viwanda.

Akicharura viongozi, anasema wanajishughulisha kusambaza utajiri wenyewe kwa wenyewe. “Serikali itathmini namna ya kubuni utajiri kupitia uboreshaji wa viwanda, ambavyo vitabuni nafasi za ajira. Iweke mikakati kabambe kuimarisha utendakazi wake,” amenukuu kwenye kitabu hicho.

Pia, anaendelea kupendekeza ugatuzi utumike kufanikisha sekta ya viwanda, kupitia mgao wa fedha ambazo serikali za kaunti hupokea kila mwaka wa fedha.

CORONA: Wauzaji nguo walia hela hazipatikani

NA SAMMY WAWERU

WAFANYABIASHARA wa nguo wameathirika kwa kiasi kikuu tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Covid-19 kuripotiwa nchini.

Katika eneobunge la Ruiru, Kiambu, ambapo masoko yaliamriwa kufungwa wiki iliyopita kuanzia Machi 26, wauzaji wa mitumba wamelalamikia hali duni ya uchumi, wakisema hela hazipatikani.

Wafanyabiashara katika masoko ya Ruiru Mjini, Jubilee na Migingo yaliyoko mtaa wa Githurai na yaliyo pembezoni mwa barabara wamesema hali ikiendelea hivi huenda wasipate hata pesa za kununua chakula.

“Kiwango cha mauzo kilianza kushuka, hatua iliyoendelea visa vilipozidi kuongezeka. Hali hii inamaanisha riziki hatupati sasa,” Simon Kagombe, muuzaji wa nguo za mitumba aliambia Taifa Leo Dijitali.

Licha ya kuwa maduka ya huduma za utoaji na uwekaji pesa zinaruhusiwa, Antony Kabui, mhudumu WA M-Pesa, anasema idadi ya wateja imeshuka kwa kiasi kuu.

“Awali kabla ya janga hili ningehudumia zaidi ya wateja 50 kwa siku. Kwa sasa wameshuka hadi chini ya 20,” mfanyabiashara huyo akasema.

Wenye maduka ya M-Pesa, ndio wanaruhusiwa kuendesha biashara. Picha/ Sammy Waweru

Hali ni sawa katika maeneo mengine ya Kiambu, kama vile Thika.

Hatua ya kufunga masoko inanuia kusaidia kudhibiti ueneaji zaidi wa virusi hatari vya corona, ambavyo kulingana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe vinaendelea kuenezwa ndani kwa ndani.

“Visa vya maambukizi tunavyoshuhudia sasa si vya kutoka nje, virusi sasa vipo kati yetu,” akasema Bw Kagwe katika mojawapo ya kikao na wanahabari.

Mengi ya masoko, hasa ya mavazi tuliyozuru eneobunge la Ruiru yamesalia kuwa mahame.

Wafanyabiashara wanaoruhusiwa kuendesha kazi ingawa wanatakiwa kuwa waadilifu kwa kuzingatia utaratibu na kanuni zilizotolewa na serikali kuzuia maambukizi ya Covid – 19, ni wauzaji wa bidhaa za kula pekee pamoja na maduka yanayotoa huduma za uwekaji na utoaji pesa.

Wauzaji wa vyakula wanaruhusiwa kuendesha biashara ingawa kwa kuzingatia sheria na utaratibu. Picha/ Sammy Waweru

Soko la Jubilee, Githurai na ambalo ni maarufu kwa bidhaa za bei nafuu, vibanda vingi vimesalia mahame.

Hata ingawa amri iliyotolewa haikupokelewa vyema na wafanyabiashara hao, tangu kisa cha kwanza cha Covid – 19 kiripotiwe nchini mwezi Machi 2020, sekta ya biashara ilianza kudididmia.

Wauzaji wa vyakula wametakiwa kutilia mkazo umbali baina yao, ikiwa ni pamoja na kudumisha kiwango cha juu cha usafi. Pia, hawapaswi kuchuuza, ila wasalie eneo moja kuhudumia wateja.

Masaibu hayo ya sekta ya biashara yanashuhudiwa huku kafyu kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi moja asubuhi ikiendelea kutekelezwa.

 

Ni kubaya!

Na VALENTINE OBARA na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameingiwa na wasiwasi tele kuhusu watakavyojikimu kimaisha kutokana na idadi kubwa ya kampuni zinazoendelea kufungwa zikilalamikia sera duni za serikali.

Hali hii imeathiri sekta zote na inatilia shaka mustakabali wa uchumi wa nchi.

Idadi ya kampuni za kibinafsi zinazofungwa au kuvunjwa kwa kushindwa kuhimili mazingira ya kiuchumi imeongezeka maradufu.

Takwimu katika afisi ya msajili wa kampuni zinaonyesha kuwa, kampuni 388 za kibinafsi zimefungwa au kuhama Kenya katika kipindi cha miezi sita kufikia Septamba 21, mwaka huu.

Hali ni mbaya hivi kwamba, katika kipindi cha miezi kumi na sita, zaidi ya kampuni kumi, zikiwemo za kimataifa na za humu nchini zimefuta wafanyakazi baada ya kupata hasara.

Kampuni ya East African Breweries iliwafuta wafanyakazi 100 huku ile ya kutengeneza simiti ya East African Portland ikitangaza kuwaachisha kazi wafanyakazi wote zaidi ya 1,000.

Shirika la Ndege la Kenya ambalo limekuwa likipata hasara ya mabilioni ya pesa liliwafuta wafanyakazi 38.

Katika sekta ya fedha, benki ya Stanbic iliwastaafisha mapema wafanyakazi 200 nayo kampuni ya Finlays iliyobobea katika ukuzaji wa majanichai na maua ikiwatimua wafanyakazi 1,700 mwaka 2018.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya kiuchumi, hali hii inatokana na sera za serikali ambazo zimefanya uwezo wa kiuchumi wa Wakenya kudorora.

Kampuni nyingine ambazo zilifunga na kuacha maelfu ya Wakenya bila kazi ni Deacons Limited. Nayo Nestle Foods ilifunga afisi yake jijini Nairobi, hatua ambayo iliathiri wafanyakazi wake 100.

Vile vile, sekta zinazotegemewa na wananchi kujiajiri zinaendelea kukumbwa na misukosuko tele inayofanya wajasiriamali kufunga biashara zao kwa sababu ya hasara wanazopata.

Inahofiwa hali hii huenda ikazorotesha zaidi uchumi wa kitaifa kwani bila mapato, wananchi hawatakuwa na uwezo wa kugharamia mahitaji yao muhimu na hivyo basi biashara tele zitaathirika.

Kwa wiki chache zilizopita, sekta ya kilimo ambayo imekuwa ikisifiwa kuwa kitega uchumi kikuu cha taifa imepitia changamoto tele zinazotia hofu wadau.

Wakulima wa majani chai na kahawa walishtushwa na matangazo ya mashirika yanayosimamia shughuli zao kwamba, faida watakazopata zitapungua kwa kiasi kikubwa mwaka huu.

Ingawa sababu zilizotolewa ni kuwa ushindani wa uzalishaji mazao hayo kimataifa ulizidi, swala ibuka ni kwa nini wakulima wa humu nchini hawakuwezeshwa kufaidika katika ushindani huo ilhali serikali hujisifu kuhusu inavyopiga jeki sekta hii.

Hali sawa na hiyo imo katika kilimo cha miwa na mahindi ambapo masaibu ya wakulima yanaongezeka kila kukicha.

Kampuni zawekwa chini ya mrasimu

Wiki iliyopita, matumaini ya kufufua sekta ya miwa yalididimia wakati usimamizi wa kiwanda kikubwa zaidi cha sukari cha Mumias ulipotwaliwa na Benki ya KCB kwa kushindwa kulipa madeni yake.

Kampuni nyingine iliyowekwa kwenye usimamizi wa mrasimu ni Athi River Mining ambayo ilikuwa ikiajiri maelfu ya wafanyakazi, nayo Telkom Kenya ikafuta asilimia 72 ya wafanyakazi wake.

Unilever Tea Kenya iliwasimamisha wafanyakazi vibarua 11,000 kuanzia mwaka 2018.

Wiki jana, kampuni kubwa za michezo ya bahati nasibu za Sportpesa na Betin ziliamua kufunga biashara zao nchini kwa sababu ya mizozo iliyodumu kwa muda kati yao na serikali kuhusu madai ya kukwepa kulipa ushuru.

Kampuni ya Sportpesa pekee iliwafuta kazi wafanyakazi 400 na kusitisha ufadhili wa miradi mbali mbali ambayo vijana walitegemea kujiajiri ikiwa ni pamoja na spoti.

Betin ilikuwa imefungulia maelfu ya vijana nafasi za kujiajiri kupitia maduka yake kote nchini.

Athari za hatua hiyo ni vijana hao kukosa ajira, wachezaji wa vilabu vikubwa vya michezo vilivyofadhiliwa na kampuni hizo kukosa kupata mishahara na marupurupu yao.

Wakuu wa kampuni hizo walisema mandhari ya kibiashara yamekuwa mabaya mno nchini kwa hivyo ni vigumu kufaidika kibiashara.

Viwanda vya utengenezaji pombe na sigara navyo viliashiria uwezekano wao kufunga biashara zao nchini au kufuta kazi baadhi ya waajiriwa wao, kwa sababu hizo hizo.

Ilani iliyotolewa na mashirika ya British American Tobacco (BAT), Kenya Wine Agencies (Kwal), Alcoholic Beverages Association of Kenya (Abak) na Mastermind Tobacco ilionya kwamba, sera za ushuru zisiporekebishwa, kutakuwa na athari kubwa kwa ajira kwani maduka na kampuni za usambazaji bidhaa zao zitaathirika.

“Italemaza sekta ya kiviwanda na kuathiri hali ya maisha kwa maelfu ya Wakenya,” mashirika hayo yakasema kwenye taarifa ya pamoja.

Katika Kaunti ya Mombasa, wakazi, wanasiasa, mashirika ya kijamii na wakurugenzi wa kampuni za uchukuzi mizigo wamekuwa wakiandamana kwa wiki kadhaa sasa wakilalamikia jinsi uchumi ulivyodorora tangu serikali ilipoagiza mizigo isafirishwe kwa reli ya kisasa ya SGR.

Imebainika kwamba hatua hiyo haikuathiri wakazi wa Mombasa waliotegemea ajira katika kampuni za uchukuzi wa malori pekee, bali pia Wakenya wengine waliofanya biashara katika barabara ambazo lori hizo zilikuwa zikipitia kama vile Mtito Andei.

“Wakazi wengi wanashindwa hata kulipa kodi ya nyumba. Nyumba zinabaki tupu bila wapangaji kwani wengi wameamua kuhamia miji mingine,” Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisema majuzi.

Mjini Kisumu, mamia ya wakazi wanahangaika baada ya maeneo yao ya biashara kubomolewa kiholela serikali ikijiandaa kufanyia ukarabati bandari ya Ziwa Victoria kwa haraka.

Nafasi za ajira zimepotezwa pia katika sekta ya maduka ya jumla baada ya kampuni kadhaa kama vile Choppies na Nakumatt kufungwa.

Kampuni ya Nakumatt ililazimika kuwafuta kazi wafanyakazi 800 huku kuporomoka kwake kukiathiri maelfu ya wafanyabiashara waliokuwa wakiitegemea.

Kampuni za kimataifa ambazo zilihama Kenya zikilalamikia mazingira magumu ya kibiashara ni benki ya Hong Kong Shanghai Banking Corporation (HSBC), Reckitt & Benkiser, Procter & Gamble, Bridgestone, Colgate Palmolive na Johnson & ?Johnson.

“Kinachotendeka ni hatari kwa Kenya kama nchi na kama mbabe wa uchumi Afrika Mashariki. Tunapaswa kulinda himaya yetu ya kibiashara kwa kuwapa motisha wawekezaji wa humu nchini na kimataifa,” asema mwanauchumi Solomon Njoroge.

Anasema kufungwa kwa viwanda na makampuni kunapunguza uwezo wa uchumi wa nchi.

“Serikali ikikosa kuweka mazingira ya kukuza biashara zilizopo na zile mpya, basi nchi itapoteza nafasi yake ya kuwa na uchumi thabati eneo hili,” asema.

Wadadisi wanasema itakuwa vigumu kwa serikali kushawishi Wakenya kwamba, uchumi unakua wanapopoteza kazi.

“Watu wanashangaa serikali inaposema mambo yako shwari wakati maelfu ya watu wanapoteza kazi kampuni zikifungwa na wafanyabiashara kuchelea kuwekeza Kenya kwa sababu ya sera za serikali,” anasema mtaalamu wa masuala ya uchumi David Kimotho.

Uhuru kimya hali ya nchi ikizorota

BENSON MATHEKA Na SAMMY LUTTA

KIMYA cha Rais Uhuru Kenyatta wakati serikali yake na nchi kwa jumla inakabiliwa na changamoto nyingi, kimechochea kila aina ya uvumi miongoni mwa wananchi kuhusu yanayoendelea serikalini.

Hii ni baada ya Rais Kenyatta kuendelea kunyamaza wakati ikiwa wazi chama chake cha Jubilee kimegawanyika, Baraza la Mawaziri haliko pamoja tena, uhusiano kati yake na Naibu Rais William Ruto umeharibika, wadogo wake serikalini wanampuuza, shughuli za kaunti zinakaribia kukwama na bei ya unga inazidi kupanda miongoni mwa masuala mengine.

Wadadisi wa siasa wanasema sauti ya kiongozi wa taifa inahitajika katika masuala haya na mengine yanayokumba taifa ili kukomesha uvumi ambao umeongezeka miongoni mwa wananchi kuhusu yanayoendelea serikalini.

Wanaeleza kuwa Wakenya wanamtazama yeye kama rais wao na wala sio mawaziri ama maafisa wengine, na makosa ya mawaziri ni makosa yake kwa sababu ni yeye aliyewateua.

Kwa muda sasa imekuwa wazi Jubilee kimegawanyika katika mirengo: ‘Tangatanga’ inayounga mkono Naibu Rais William Ruto, ‘Kieleweke’ kinachopigia debe handisheki ya Rais na Raila Odinga na ‘Team Wanjiku’ wanaodai kutetea mwananchi wa kawaida.

Licha ya tofauti hizi kuwa wazi, Rais Kenyatta hajachukua hatua za kurekebisha mambo na amekataa miiti ya kuitisha kikao cha kujadili hatima ya Jubilee akisema hana wakati wa kupiga siasa.

Tatizo lingine ambalo kiongozi wa taifa amenyamazia ni ukaidi wa wazi wa Dkt Ruto na mrengo wake wa ‘Tangatanga’ wa kuwataka wakomeshe siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

Sio mara moja ambapo Rais Kenyatta amewakemea ‘Tangatanga’ kwa kampeni hizo, lakini amekosa kufuatilia maneno yake kwa vitendo.

Wadadisi wa siasa wanasema japo kila Mkenya ana haki ya kutoa maoni, Rais anahitajika kutuliza hali hii ya kupuuzwa na wadogo wake kwa kuhakikisha nidhamu inadumishwa na kila mmoja serikalini.

Rais Kenyatta pia anakabiliwa na tatizo la migawanyiko katika Baraza la Mawaziri, ambapo duru za kuaminika zinasema kuna makundi matatu: Lake Rais Kenyatta, la Dkt Ruto na wachache wasioegemea upande wowote.

Hali hii ilizorota ilipodaiwa kuwa mawaziri wanne, Peter Munya, Joe Mucheru, Sicily Kariuki na James Macharia walikuwa na njama ya kumuua Naibu Rais.

Rais pia amenyamazia mvutano kuhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje, ambalo ni suala muhimu kwa mwananchi wa kawaida kwani linahusisha unga ambao ni chakula kinachotegemewa na wengi.

Rais Kenyatta pia amekuwa kimya kuhusu mvutano kati ya magavana na serikali kuu kuhusu mgao kwa kaunti.

Hapo jana Gavana wa Kaunti ya Turkana, Josphat Nanok almtaka Rais alisema alichangia kuzuka kwa mzozo huo: “Rais Uhuru alitia sahihi sheria ya kuruhusu Serikali Kuu kutumia pesa katika bajeti ya 2019 bila kufuata utaratibu unaofaa,” akasema Bw Nanok.

Suala lingine ambalo Rais Kenyatta amekosa kuweka wazi ni mjadala wa wakereketwa wake ambao wanapendekeza atafutiwe wadhifa mkuu serikalini kupitia mageuzi ya kikatiba, wakisema angali na nguvu za kuendelea kuhudumu.

Japo hizi zinaweza kuwa siasa duni ambazo hafai kujihusisha nazo, wachanganuzi wanahisi kuwa ni suala la umuhimu kwa taifa na sauti yake inahitajika ili kuweka msimamo wake wazi.

ODONGO: Rivatex ichangie katika ufufuzi wa kilimo cha pamba

Na CECIL ODONGO

KUFUFULIWA kwa kiwanda cha kutengeneza nguo cha Rivatex kumewapa matumaini mapya wakulima wa pamba kutoka iliyokuwa mikoa ya Nyanza, Bonde la Ufa na Magharibi.

Kiwanda hicho kilichofunguliwa upya na Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa iliyopita kilisifika miaka ya themanini na tisini kwa kutengeneza nguo na kubuni nafasi nyingi za ajira kwa Wakenya.

Tunaposifia kufufuliwa kwa Rivatex, ni vyema kuhakikisha kwamba matatizo yaliyoizonga miaka ya nyuma na kusababisha kuporomoka kwake hayarejelewi ili mara hii ifane katika utendakazi wake.

Hata hivyo, ufanisi huo utafikiwa tu iwapo serikali itatekeleza mikakati kadhaa ambayo ikitiliwa manani basi kiwanda hiki kitafanikisha maazimio yake nchini.

Kwanza, serikali inafaa kuhakikisha kwamba maafisa wakuu wa kiwanda hiki ni watu wenye maadili na wasiojawa na tamaa ya kufuja mali ya umma wakiwa uongozini.

Imebainika kwamba viwanda vilivyoporomoka na kushindwa kurejea ulingoni kama Mumias na Webuye vilianguka kutokana na uongozi mbaya na wasimamizi wafisadi, ambao baadaye walijiuzulu na kutumia mali waliyoiba kuyoyomea katika siasa.

Vile vile wanasiasa pia wasiruhusiwe kuingilia usimamizi wa kiwanda cha Rivatex kwa sababu watatumia ushawishi wao kuhakikisha washirika wao wanaajiriwa na wengine wanashikilia nafasi za juu kiwandani, kisha kuwatumia kukifilisi kifedha hasa nyakati za kampeni.

Pili, maslahi ya wakulima ambao watakuwa na mchango mkubwa katika uendeshaji wa Rivatex kwa kushiriki kilimo cha pamba yaangaliwe vizuri na serikali.

Kwa sasa ni ukweli kwamba kilimo cha pamba kimekufa hasa katika maeneo yaliyosifika kwa ukuzaji wa mmea huo kama Nyando, Kisumu, Nyanza Kusini na maeneo mengine ya Bonde la Ufa na Magharibi mwa nchi.

Itailazimu serikali kuwahamasisha wakulima, ambao wengi wao bado wanauguza machungu ya kutolipwa fedha kwa pamba walizowasilisha kwa kampuni za KIKOMI mjini Kisumu na Rivatex, kurejelea kilimo cha pamba.

Uhamasisho huo unafaa kujumuisha hakikisho kwamba wakulima hawa watalipwa malimbikizi wanayodai Kikomi na Rivatex, kisha waafikiane na usimamizi wa kampuni hizo kwamba watakuwa wakilipwa kila mara wanapowasilisha pamba badala ya mtindo wa zamani walipolazimishwa kusubiri kupokea fedha zao baada ya miezi kadhaa.

Tatu, jinsi alivyosema Rais Kenyatta, Rivatex inafaa ianze kuzamia matangazo ya nguo na mavazi mengine inayotengeneza ili Wakenya wayanunue.

AJIRA: Mwiba wa kujichoma unavyoitesa serikali

Na LEONARD ONYANGO

TANGAZO la Serikali mnamo Jumanne kuwa kuanzia Julai itaajiri wafanyikazi wake kwa kandarasi ili kubana matumizi yake, ni hatua nyingine kati ya nyingi zilizokosa kuzingatiwa awali.

Hii ni kutokana na kuwa juhudi zote za awali za kupunguza matumizi serikalini zimeshindwa, na gharama hiyo imekuwa ikipanda badala ya kushuka.

Kulingana na bajeti iliyosomwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Henry Rotich, serikali itatumia Sh790 bilioni kuwalipa mishahara watumishi wa serikali kati ya Julai 1 mwaka huu na Juni 30, 2020.

Ni kutokana na kiasi hicho kikubwa cha pesa ambapo Serikali imetangaza kuwa kuanzia Julai 1 itakuwa ikiwaajiri watumishi wa umma kwa kandarasi za miaka mitatu.

Lakini hii si mara ya kwanza kwa Serikali kutangaza mikakati ya kupunguza mzigo wa malipo ya wafanyikazi wake, ila jitihada hizo zote zimekuwa kazi bure.

Hii ni kutokana na kuwa viongozi wakuu wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wamekuwa wakitenda kinyume cha sera za Serikali za kupunguza gharama za matumizi katika sekta ya umma.

Kuongezea mzigo

Mara baada ya kuchaguliwa kuhudumu muhula wa pili mnamo 2017, Rais Kenyatta alibuni wadhifa wa Waziri Msaidizi (CAS) akisema kuwa watasaidia kuboresha huduma katika wizara, licha ya kuwa kila wizara ina katibu (PS) na nyingine hata zaidi ya mmoja.

Wengi wa CAS hao ni wanasiasa waliokataliwa na wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa 2017. Wadhifa huo umewaongezea Wakenya mzigo zaidi wa kuwalipa CAS hao 22 mishahara, marupurupu, magari, ofisi na wafanyikazi wanaowahudumia.

Mbali na kila mmoja kulipwa mshahara wa zaidi ya Sh700,000 kwa mwezi, CAS pia wanalipiwa bima ya matibabu ya zaidi ya Sh10 milioni.

Hatua nyingine ambayo imefanya sera za Serikali za kupunguza matumizi yake kuwa domo kaya ni kushindwa kuunganisha mashirika ya serikali kama ilivyokuwa imeshauriwa na jopo kazi lililoongozwa na Abdikadir Mohamed.

Mnamo 2013, Rais Kenyatta alibuni jopokazi hilo kutoa mwelekeo wa mageuzi katika mashirika ya umma.

Jopokazi hilo lilipendekeza mashirika ya umma yanayofanya kazi sawa yaunganishwe ili kuyapunguza kutoka 262 hadi 187.

Lakini hadi sasa serikali haijatekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo huku ikiendelea kulipa mamilioni ya fedha kwa wanachama wa bodi za mashirika yaliyostahili kuvunjwa.

Hawajui majukumu

Ripoti hiyo ya Abdikadir ilibaini kuwa wengi wa wajumbe wa bodi katika mashirika ya umma hawajui majukumu yao. Hii ni kutokana na kuwa wengi wa wanaopewa kazi hizo ni wanasiasa walioshindwa kwenye uchaguzi, washirika wa wanasiasa wakuu na jamaa zao ambao hawana ujuzi wa majukumu yao.

Hatua nyingine inayotilia shaka nia ya serikali kupunguza matumizi ni ile ya 2014 wakati Rais Kenyatta alipoagiza Wizara ya Ugatuzi kukagua watumishi wote wa serikali ya kitaifa ili kuondoa wafanyakazi hewa.

Rais alitoa agizo hilo baada ya kubainika kuwa Kenya inapoteza Sh1.8 bilioni kila mwaka kuwalipa mishahara wafanyakazi hewa. Mwishoni wa shughuli hiyo, serikali ilitangaza kufichua wafanyakazi hewa 12,500 katika sajili yake ya mishahara.

Wafanyakazi hewa

Akisoma bajeti wiki iliyopita, Bw Rotich alisema kuwepo kwa wafanyakazi hewa katika sajili ya mishahara ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha serikali kutumia mamilioni ya fedha kulipa mishahara, hivyo kumaanisha shughuli hiyo ya 2014 ilikuwa ya kupoteza wakati kwani wahusika hawakuondolewa.

Rais Kenyatta alipokuwa Waziri wa Fedha mnamo 2010, alipiga marufuku maafisa wa serikali kutumia magari yenye injini zilizozidi ukubwa wa 1800cc.

Agizo hilo limepuuzwa na serikali, kaunti na mashirika huku wengi wakiendesha magari makubwa yanayonunuliwa kwa bei ya juu, kutumia mafuta mengi na gharama za juu za kuyatengeza.

Uthabiti wa shilingi ya Kenya watajwa kuwa ‘sumu’ Jumuiya

Na MWANGI MUIRURI

UTHABITI wa Shillingi ya Kenya katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umetajwa kama kiini cha wafanyabiashara wa hapa nchini kuhangaika katika ushindani.

Wabunge katika bunge la jumuia hiyo (EALA) wakiongozwa na Bw Simon Mbugua wanasema kuwa suluhu la usawa katika soko hili pana ni kuzinduliwa kwa sarafu moja ya kutumika na wote.

“Shida kubwa kwa Wakenya ni kuwa, wafanyabiashara kutoka mataifa mengine wanaingiza bidhaa zao hapa nchini na kuuza kwa bei za chini, lakini wakishabadilisha pesa hizo hadi kwa sarafu za kwao, wanajipata wameunda faida za juu,” anasema Bw Mbugua.

Kwa mfano, Shilingi ya Uganda imekuwa ikibadilishwa kwa kiwango cha Sh36 za Kenya, ile ya Tanzania ikiwa katika kiwango cha Sh22, Franc ya Rwanda ikibadilishwa kwa Sh8 na ile ya Burundi kwa Sh17.

“Ukiangalia mtindo huu, utapata kuwa wafanyabiashara kutoka mataifa hayo wataingiza bidhaa zao hapa nchini kwa kuwa kuna maelewano ya soko huru, wauze kwa bei za chini ikilinganishwa na ushindani wa Wakenya, lakini wakiishia kwa benki na wabadilishe pesa hizo hadi kwa sarafu za kwao, wanawaacha Wakenya hoi kifaida,” anasema Bw Mbugua.

Anasema kuwa Wakenya wengi wanaachwa wakiwa wamepokonywa nafasi ya kushiriki biashara huru iliyo na usawa, uchumi unapokonywa sarafu za kigeni kwa kuwa wafanyabiashara hao hurejea makwao wakiwa na hela zilizobadilishwa hadi za mataifa yao na hatimaye bidhaa za Kenya zinabakia bila uteja kwa kuwa ni za bei za juu.

Anasema kuwa taifa la Kenya limekuwa na mazoea ya kukumbatia maelewano hayo ya biashara huru lakini bila kuzingatia athari zile  zinazoandamana na kulegeza masharti ya sarafu.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiteta kuwa wale maafisa wa Kenya ambao wanafaa kuwakinga wafanyabiashara wa Kenya dhidi ya miskumo hii wamekuwa wabutu kiasi cha kutelekeza uchumi wa taifa.

“Si hawa maafisa waelewe kuwa kuna njia nyingi za kuua paka… Unaweza ukasema kuwa bidhaa hizi hazijaafikia vigezo na unazifungia nje au unaweka masharti ya juu kuliko yale yanayotekelezewa bidhaa asili,” Rais amewahi kunukuliwa akiteta.

Kumekuwa na tetesi nyingi kuwa Wakenya wamegeuzwa kuwa washindani wa wenzao wa Afrika Mashariki katika soko la hapa nchini lakini likiwa halina usawa wowote kwa kiwango kikuu uhasi ukiwa dhidi ya Wakenya.

Jaa la taka

Ni katika hali hiyo ambapo kuna wadadisi ambao wanashikilia kuwa Kenya imegeuzwa kuwa kama pipa la taka ambapo linapokezwa kila aina ya bidhaa kutoka kila pembe ya Jumuia lakini bidhaa zake zikiwa  bado zinatekelezewa masharti katika mataifa hayo.

Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua anasema kuwa ndio sababu amewasilisha mswada bungeni wa kuzima biashara ambayo  haina usawa katika soko hili la Jumuia ya Afrika Mashariki.

“Tunataka kuwe na utaratibu wa kibiashara. Ukiwa na mayai ya kuuza hapa nchini, unafaa utengewe eneo ambalo halina uzalishaji wa bidhaa hiyo. Na wafanyabiashara wa Kenya nao watengewe bidhaa za kuuza kwa soko za wengine. Kuwe na mikakati za kupiga jeki uzalishaji ili kusiwe na udhaifu kwamba Wakenya wanaweka bei zao juu kwa kuwa gharama za uzalishaji ziliwasinya nao wale washindani wakiwa katika hali ya kuwa na uhuru wa kuteremsha bei kwa kuwa serikali zao ziliwapiga jeki,” anasema Rigathi.

Ukosefu wa mvua kulemaza ukuaji wa uchumi

Na BERNARDINE MUTANU

Ukuaji wa uchumi nchini Kenya utatatizika kutokana na upungufu wa mvua nchini.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge ambaye alionya kuwa ukame utaathiri ukusanyaji wa ushuru na ukuaji wa nafasi mpya za kazi.

Dkt Njoroge alisema athari za ukame kwa kilimo itafanya ukuaji wa uchumi kwenda chini 2019 hadi asilimia 5.3 kutoka asilimia 6.3 zilizokadiriwa.

Utakuwa ukuaji wa pili wa chini zaidi katika uchumi tangu serikali ya Jubilee kuingia mamlakani 2013.

Dkt Njoroge alisema hayo wakati wa mahojiano na Bloomberg, “Kama kutakuwa na ukame, basi ukuaji wa uchumi utashuka hadi asilimia 5.3 au chini au zaidi kidogo ya kiwango hicho,” alisema.

Ukuaji wa chini wa uchumi utaathiri mapato ya makampuni, na kusababisha kiwango cha ushuru kinachokusanywa kwenda chini, hivyo kuathiri zaidi nafasi za kazi.

Alisema hali huenda ikawa ilivyokuwa 2017 ambapo ukuaji wa uchumi ulikuwa ni asilimia 4.9 kutoka asilimia 5.9 mwaka uliotangulia.

Hii uni kutokana na kupungua kwa kiwango cha mazao ya shambani kwa asilimia 1.6 mwaka wa 2017 kutoka asilimia 4.7 mwaka uliotangulia na asilimia 5.3 mwaka wa 2015.

Kilimo ndio uti wa mgongo wa Kenya na huchangia thuluthi moja ya ukuaji wa uchumi wa Kenya. Pia, uhimili robo tatu za bidhaa za Kenya zinazouzwa nje ya nchi.

Wakenya wengi hawaweki akiba, hukopa marafiki – Ripoti

EDWIN OKOTH Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi mwaka huu licha ya serikali kusema hali ya uchumi iko imara.

Kwenye hotuba yake kwa bunge kuhusu hali ya nchi Rais Uhuru Kenyatta alisema uchumi wa Kenya umeimarika kwa asilimia 6.1

Hata hivyo, utafiti wa hivi punde uliofanywa na Benki Kuu ya Kenya na Shirika la FSD Kenya, umeonyesha kuwa hali ngumu ya maisha inawasukuma Wakenya wengi kuomba na kukopa majirani, marafiki na watu wa familia.

Utafiti unasema hali ambayo inalemea watu walioajiriwa ambao wako na umri wa kati ya miaka 27 na 34.

Kulingana na utafiti huo watu wengi wanashindwa kuweka hazina na kukosa kujiandaa kukabiliana na jambo la dharura litatokea.

Utafiti huo ulionyesha kuwa, zaidi ya nusu ya Wakenya wanalalamika hali ya maisha iliwaharibikia 2019, ikilinganishwa na 2018. Wakazi wa maeneo ya mashambani ndio waliathirika zaidi.

“Asilimia 51 ya watu kitaifa waliripoti kuwa hali yao ya kifedha iliharibika 2019, ikilinganishwa na asilimia 23.8 ya watu ambao waliripoti kuwa hali yao iliimarika. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa wakazi wa mashambani, ambapo asilimia 53.3 walisema hali yao iliharibika,” utafiti huo unasema.

Idadi ya watu ambao wamekuwa wakikopa katika maduka ilipanda kutoka asilimia 9.9 mwaka wa 2018 hadi asilimia 29.7 mwaka 2019, huku asilimia 45.4 wakishindwa kulipa na kuathiri wafanyabiashara wadogo.

Kitaifa, watu wanaoorodheshwa kuwa sawa kifedha ni asilimia 21.7 pekee mwaka huu, ikilinganishwa na asilimia 39.4, ilivyokuwa 2016.

Utafiti huo ambao ulihusisha maboma 11,000 katika maeneo ya mijini na mashambani aidha ulibaini kuwa asilimia 62.1 ya Wakenya hawawezi kukimu matumizi yao ya kila siku, ikilinganishwa na mapato yao.

Wanapoishiwa na pesa, watu hao hutafuta marafiki, watu wa familia ama waajiri wao kutafuta msaada kwa sababu hawaweki akiba. Asilimia 24.7 ya wanaowatafuta marafiki huenda kuomba na asilimia 6.5 kukopa.

Asilimia 10.9 huamua kukaa ngumu na kutofanya chochote, japo mtu wa familia aliye na uwezo anaweza kuingilia kati na kuwasaidia.

“Marafiki na familia ndio suluhu kubwa ya kifedha ambayo Wakenya wengi wanatumia wanapoishiwa na pesa kukidhi mahitaji ya kila siku,” utafiti huo unasema.

Utafiti huo ulibaini kuwa, matajiri huwa wanaathirika kifedha wakati mtu wa familia anapofariki, ikilinganishwa na masikini.

Kukosa mikopo na kushindwa kuweka akiba kulitambuliwa kama kunakoharibu hali na kurejesha Kenya nyuma kimaendeleo.

Hali hii inakinzana na ripoti kuwa uchumi wa Kenya umekua kwa asilimia 6.1 katika kipindi cha miezi tisa 2018.

“Wakenya wamekuwa na uwezo wa kupata mapato kwa miaka mingi lakini hawawezi kuweka akiba kwa sababu huwa hawana uhakika wa watapopata pesa. Utafiti unaonyesha kuwa, asilimia 59 ya Wakenya wanalenga kutumia elimu kutimiza ndoto zao kimaisha,” utafiti huo ukasema.

Kwa Wakenya wasio na elimu na wakazi wa mashambani, kutafuta chakula ndilo lengo kuu maishani na kwa wakazi wa mijini afya ndilo lengo kuu.

Hapa hujuma tu!

Na VALENTINE OBARA

MABILIONI ya pesa za umma yameharibiwa kwenye miradi mikubwa ya Serikali ya Jubilee, ambayo imekwama au imeshindwa kuwa ya manufaa kwa umma.

Mradi wa hivi majuzi kupata pigo ni wa vipakatalishi kwa watoto wa darasa la kwanza, ambao ulivumishwa vikali na wakereketwa wa Jubilee walipoingia madarakani 2013.

Hii ni baada ya Wizara ya Elimu kusema imebadilisha sera kuhusu mradi huo, na kwa hivyo itakoma kuwapa watoto laptopu hizo.

Badala yake, alisema Katibu wa Wizara ya Elimu, Belio Kipsang, watajenga maabara za tekinolojia katika shule zote 25,000 za umma nchini.

“Sera imebadilika kutoka kumpa kila mwanafunzi kipakatalishi, na sasa itakuwa ni ujenzi wa maabara ya kompyuta kwa mafunzo ya ICT,” alinukuliwa.

Kulingana na Ripoti ya Wizara ya Elimu mnamo Desemba mwaka 2018, mafanikio ya mradi huo ni asilimia tano pekee. Hii ni licha ya Sh42.3 bilioni kutumika katika mradi huo.

Haya yalitokea siku chache baada ya kugunduliwa kwamba mradi mkubwa wa unyunyizaji maji katika shamba la Galana Kulalu, Kaunti ya Tana River pia umekwama, baada ya serikali kutumia Sh5.9 bilioni kulipa kampuni ya Israeli iliyokuwa ikijenga miundomsingi katika shamba hilo.

Mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa alisema wabunge wataitisha ripoti kutoka kwa serikali ili ifafanuliwe jinsi fedha zilizotengewa miradi hiyo.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo kuhusu vipakatalishi, Bw Wamalwa alisema: “Tulisema wazi tulipokuwa katika Muungano wa Cord na NASA kwamba mpango huo ulibuniwa bila nia ya kusaidia wananchi, bali kujaza pesa mifuko ya watu wachache. Tunataka uwajibikaji kuhusu jinsi fedha zilivyotumiwa.”

Ripoti zilisema kampuni iliyohusika katika Galana iliondoka kabla ya kukamilisha ujenzi wa miundomsingi kwani haikuwa imelipwa pesa zote.

Kwa upande wake, Bodi ya Kitaifa ya Unyunyizaji (NIB) ilidai kampuni hiyo ya Green Arava, ilikiuka makubaliano na haikutekeleza kazi kama ilivyotarajiwa.

Utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulikuwa umenuia kutumia mradi huu kama mfano wa mbinu za kisasa za kilimo zitakazofanikisha uzalishaji wa chakula kitakachotosheleza mahitaji ya umma.

Awali, Wizara ya Elimu nayo ilimulikwa kwa madai ya ubadhirifu wa fedha katika usambazaji wa vitabu vya kusoma kwa shule za umma, huku ikihofiwa karibu Sh10 bilioni zilifujwa.

Mradi mwingine mkuu ambao Rais alitumaini kuutumia kuacha sifa bora kabla aondoke mamlakani 2022, ni wa usambazaji wa maji safi kwa wananchi kupitia ujenzi wa mabwawa katika sehemu mbalimbali za nchi.

Lakini hili pia linaonekana kukumbwa na dhoruba kali kwani imebainika kuwa kampuni iliyopewa zabuni ya ujenzi wa mabwawa matano maeneo ya Rift Valley na Kaunti ya Meru kwa gharama ya Sh104.5 bilioni haina uwezo wa kutekeleza ujenzi huo.

Jana, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliagiza wakurugenzi wa kampuni 107 zinazoaminika zilihusika katika ufujaji wa fedha katika ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, wafike katika idara hiyo ili kusaidia katika uchunguzi ulioanzishwa.

Mradi mwingine ambao umekwama ni utoaji wa mbegu na fatalaiza kwa bei nafuu, ambao Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri tayari amesema hautatekelezwa mwaka huu kutokana na ukosefu wa ufadhili. Hii ni licha ya kuwa ulitengewa pesa kwenye bajeti ya 2018/2019.

Tangu ulipoanzishwa mnamo 2014, jumla ya Sh19.3 bilioni zimetumika kwa ununuzi wa mbegu na mbolea za bei nafuu.

Hata hivyo, mradi huo umekuwa ukikumbwa na madai ya ulaghai wa mbolea na mbegu mbovu, pamoja na maafisa kuuza fatalaiza hiyo kwa wafanyibiashara, ambao baadaye wanawauzia wakulima kwa bei ya juu.

Kwa upande mwingine, lengo kuu la kusaidia vijana kubuni nafasi za kazi kupitia kwa Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) na Hazina ya Vijana (YEF) imetatizika kutokana na wizi wa pesa katika mashirika hayo.

UCHUMI: Uganda yapaa Kenya ikichechemea

Na BENSON MATHEKA

Kwa Muhtasari:

  • Wakenya wanaendelea kununua bidhaa kwa wingi kutoka Uganda badala ya kununua zinazotengenezewa humu nchini
  • Bidhaa kutoka Uganda zinazoagizwa na Wakenya ni mayai, maziwa, sukari na maharagwe
  • Kwa sababu ya mazingira bora ya kibiashara, kampuni zilizokuwa na makao Nairobi zimehamia Kampala
  • Haya yote yametokana na serikali ya Kenya kuongeza ushuru wa bidhaa za humu nchini na zile za kutoka nje ya nchi

KENYA imo hatarini kupoteza nafasi yake kama simba wa uchumi Afrika Mashariki baada ya mataifa jirani hasa Uganda kufanikiwa kuuza bidhaa zaidi nyingi hapa nchini kuliko inazonunua.

Hii inamaanisha kudidimia kwa viwanda vya Kenya, watu zaidi kupoteza nafasi za kazi na kupotea kwa ushuru.

Ingawa Rais Museveni anasema Uganda imefanikiwa kuafikia haya kutokana na amani iliyoletwa na jeshi la nchi hiyo, wadadisi wanasema mazingara bora ya kiuchumi nchini humo ndiyo yamechangia hali hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa Wakenya wanaendelea kununua bidhaa kwa wingi kutoka mataifa jirani hasa Uganda na Tanzania badala ya kununua zinazotengenezewa nchini au zinazoigizwa nchini moja kwa moja kutoka ng’ambo kama vile India na China.

Margaret Wanjiru anasema kwamba huwa anaenda Uganda kununua nguo anazouza Nairobi kwa sababu ya bei nafuu: “Huwa ninaenda Kampala mara tatu kwa wiki kununua nguo ambazo hapa Kenya ni ghali mno. Tangu nianze miaka mitatu nimekuwa nikipata faida kubwa kuliko mbeleni,” asema Bi Wanjiru.

Kwa kipindi cha miaka minne sasa, Uganda, ambayo haina bandari kama Kenya, imekuwa ikiuzia Kenya bidhaa za mabilioni ya pesa kuliko inazonunua hapa nchini.

Bidhaa hizo ni pamoja na zinazotoka ndani ya uchumi wa Uganda kama vile mayai, maziwa, sukari na maharagwe. Pia wafanyibiashara wa Kenya wanasafiri Uganda kununua nguo, bidhaa za urembo, mbao na vipuri vya magari kwa ajili ya kuziuza nchini.

Kulingana na mtaalamu wa uchumi, Robert Kamande, Uganda imefanikiwa kuuzia Kenya bidhaa za kilimo kutokana na mfumo bora wa kusaidia wakulima na kupunguzwa kwa ushuru wa fatailaiza, mbegu na pembejeo. Hii ni kinyume na Kenya ambapo gharama za kilimo ziko juu.

Gharama ya chini ya uzalishaji 

“Ndio maana maziwa yanayotoka Uganda yanauzwa Sh40 kwa pakiti ilihali ya Kenya ni Sh50. Hii inamaanisha gharama za uzalishaji Uganda ni nafuu sana ukizingatia kuwa wanauza Sh40 wakiwa wameweka gharama za usafiri,” asema Bw Kamande.

Mwaka 2018, takwimu za Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) zilionyesha kuwa Uganda iliendelea kuuzia Kenya bidhaa nyingi zaidi, tofauti na awali ilipokuwa ikinunua bidhaa hizo kutoka Kenya.

“Kwa sababu ya mazingira bora ya kibiashara, kampuni zilizokuwa na makao Nairobi zimehamia Kampala. Na kwa sababu ya hali nafuu ya kibiashara na ushuru, gharama ya kutengeneza bidhaa huwa ya chini Uganda, na hivyo basi kuvutia wafanyabiashara wa humu nchini,” aeleza mtaalamu wa biashara Robert Kamande.

Takwimu za KRA zinaonyesha kuwa bidhaa ambazo Kenya huuzia Uganda zimekuwa zikipungua kwa kiwango kikubwa tangu 2015.

Wafanyabiashara kutoka Kenya wanachagua kusafiri hadi Uganda kununua bidhaa kwa bei nafuu kuliko kuziagiza moja kwa moja kutoka China au kuzinunua nchini ambako zinauzwa kwa bei ghali baada ya serikali kuongeza ushuru.

Uganda inavyokwepa bandari

Ili kurahisisha biashara, wafanyabiashara wa Uganda wamekuwa wakisafirisha bidhaa kwa ndege moja kwa moja kutoka China hadi Kampala badala ya kuzipitishia bandari ya Mombasa ambapo zinatozwa ushuru mkubwa kabla ya kuzisafirisha kwa reli na matrela hadi Uganda.

Kulingana na Bw Kamande, baadhi ya bidhaa inazoagiza kutoka China huwa pia zinatengenezewa nchini lakini wafanyabiashara huamua kuzinunua Kampala kwa sababu ya bei nafuu.

“Uganda haiwalimbikizii wafanyabiashara mzigo wa kodi kama Kenya. Masharti ya biashara ni nafuu na ndiyo sababu hata magari na vipuri vya magari ni bei nafuu kuliko Kenya,” aeleza Bw Kamande.

Bali na magari, Wakenya wamekuwa wakinunua nguo, bidhaa za urembo, maziwa na mayai kutoka Uganda, jambo ambalo wadadisi wanasema ni tisho kwa uchumi wa nchi kwa sababu kununua bidhaa hizi kutoka nchi jirani ni kuua viwanda vya humu nchini na kunyima Wakenya nafasi za kazi.

Ingawa Kenya ina viwanda vikubwa vya bidhaa za chuma Afrika Mashariki na Kati, Wakenya wamekuwa wakinunua bidhaa hizi kutoka Uganda kufuatia ushuru wa asilimia 35 uliowekwa na serikali kwenye bajeti ya 2018/2019.

Kwenye bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Herny Rotich aliweka ushuru wa asilimia 35 kwa mavazi na viatu kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda viwanda vya humu nchini.

Sekta ya samani iliuawa

“Kwa sababu ya ushuru mpya wa bidhaa za mbao, serikali iliua kampuni kadhaa zilizokuwa zikihusika na fanicha na baadhi zikahamia Uganda na kuacha maelfu ya Wakenya bila kazi,” asema Bw Raju Shah, ambaye alifunga kampuni yake nchini mwaka jana.

Anasema baada ya serikali kuchukua hatua hii ikisema ililenga kulinda viwanda vya humu nchini, bidhaa hizo zinaendelea kuingia Kenya kutoka Uganda kwa bei nafuu zaidi.

Wadadisi wanasema baada ya Kenya kuongeza ushuru wa bidhaa kutoka nje ya nchi, Uganda iliwafungulia milango wawekezaji wa Kenya kwa kupunguza kodi.

“Matokeo yamekuwa ni kuongezeka kwa bidhaa zinazouzwa nchini kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Uganda na Tanzania,” asema Bw Kamande.

Kaunti 10 zenye bidii ya kuiletea Kenya mapato

Na BERNARDINE MUTANU

Kaunti ya Nairobi ndiyo iliyoipa Kenya mapato mengi zaidi ikilinganishwa na kaunti zingine.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ya Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), Nairobi ilitoa asilimia 21.7 ya mapato yote katika muda wa miaka mitano.

Uchunguzi wa kwanza kuhusu mapato ya jumla ya kaunti (GCP) 2019 ulionyesha kuwa kaunti zingine zilizoipa Kenya mapato zaidi ni Nakuru, Kiambu na Mombasa.

Uchunguzi huo ulihusu thamani ya bidhaa na huduma zilizotolewa katika kila kaunti nchini.

Kaunti zingine zilizo katika nafasi ya 10 bora ni Nakuru (asilimia 6.1), Kiambu (asilimia 5.5), Mombasa (asilimia 4.7), Machakos (asilimia 3.2), Meru (asilimia 2.9) na Kisumu (asilimia 2.9),Nyandarua (asilimia 2.6) Kakamega (asilimia 2.4) na Uasin-Gishu (asilimia 2.3).

Isiolo ilitoa asilimia 0.2 ilhali Samburu ilitoa asilimia 0.3 na kushikilia mkia katika ripoti hiyo inayoonyesha kiwango cha mapato ya serikali kutoka katika maeneo ya kaunti.

UBABE: Hatari ya vita baina ya Amerika na Uchina yanukia 2019

NA FAUSTINE NGILA

KATIKA taarifa za kimataifa za miaka ya hivi karibuni, vita vya kiuchumi baina ya Amerika na Uchina zimetawala kwenye vyombo vya habari tangu Rais Donald Trump aingie Ikulu ya White House.

Lakini msimamo mkali dhidi ya sera za kiuchumi za Uchina wa Bw Trump ulianza wakati wa kampeni za uarais hapo 2016 na amezidi kuzipinga kufikia mwaka huu.

Tofauti na marais wa zamani wa Uchina ambao serza zao zililenga kufaidi mataifa yote mawili, Trump amebadilisha siasa za kiuchumi na kuwa za ushindani mkali wenye uadui ndani yake.

Hapo 2018, usimamizi wa Trump ulipandisha joto la siasa hizo, ulipowekea bidhaa zote kutoka Uchina ada ya juu ya ununuzi ya Sh2.5 trilioni. Hatua hii iliisukuma serikali ya Beijing kupiga bidhaa za Amerika ada ya Sh1.1 trilioni.

Na kuanzia Januari mosi mwaka huu, ada ya asilimia 10 ya Amerika kwa bidhaa kutoka Uchina ilipandishwa hadi asilimia 25, ambayo sasa imekuwa kisiki katika ukuaji wa sekta za bidhaa husika.

“Sarafu ya Uchina imedidimia dhidi ya dola ya Amerika. Kampuni zinaweza kupata hasara kubwa sana wakati ada imepanda hadi asilimia 25, na hii itakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Dunia,” akasema mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa Edward Alden.

Umaarufu wa Trump

Licha ya hayo, Trump amejizolea umaarufu zaidi katika ngome zake, na kuweza pia kuwashawishi wanasiasa wa Democrat katika kampeni yake ya ‘Kurudisha Hadhi ya Amerika.’

Uchina na taifa ambalo limeanza mapinduzi ya viwanda majuzi, ikilinganishwa na Amerika, na imetumia teknolojia nyingi za Amerika kujiimarisha kiuchumi. Kulingana na Trump, Uchina imeiba maarifa ya Amerika na kujitapa nayo kimataifa huku ikijiboresha kiteknolojia.

Amerika hudai kuwa Uchina imeiba siri zake kuu za kibiashara, ikakiuka sheria zinazolinda teknolojia, michakato ya uundaji bidhaa viwandani, na kulazimisha kampuni za Amerika zilizowekeza Uchina kutoa siri zake za ufanisi wa kiteknolojia huku ikidukua taarifa muhimu zinazolinda viwanda vya Amerika.

“Hizi ndizo mbinu za hila ambazo Uchina inatumia kujiimarisha kiteknolojia. Wanataka kuwa magwiji katika mustakabali wa teknolojia duniani, kuanzia magari ya kielektroniki hadi teknolojia zote za kiroboti,” anasema Alden.

Ruwaza ya Uchina kuhusu nia yake ya kutawala Dunia kiuchumi ilianza hapo 2015 ilipozindua kampeni ya Made in China 2025 Initiative, na inalenga kuibadilisha nchi hiyo kutoka weledi wa viwandani hadi gwiji wa teknolojia ulimwenguni.

Ikumbukwe kuwa wiki iliyopita Uchina ilituma chombo cha kwanza kutua karibu na mwezi katika harakati zake za kutafiti kuhusu anga nje ya sayari ya Dunia, ishara ya uwezo wake wa ubunifu wa kisasa.

Tisho kwa usalama

Amerika kwa upande wake imesema hatua hizi za Uchina ni tisho kubwa sana kwa usalama wake katika miaka mingi ijayo.

“Iwapo Uchina itaafikia udhibiti wa teknolojia inayolenga, itakuwa tisho kubwa kwa jeshi la Amerika kuliko ilivyo sasa. Masuala ya kiuchumi na kiusalama yako sambamba,” anasema Alden.

Lakini Uchina imejitetea vikali dhidi ya malengo yake ya kujitegemea kiuchumi na kiteknolojia, ikisema inadhamiria kuboresha uwezo wake kukabili vizuizi vya kiuchumi kutoka mataifa ya Magharibi.

Utawala wa Trump umekejeli mtindo wa Uchina kuzima viwanda vya kampuni za Amerika nchini humo, na kukataa kuruhusu kampuni za mataifa ya Magharibi kuwekeza katika nchi yao.

Tangu mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia, kumekuwa na uhusiano wa kibaridi baina ya mataifa ya kikomunisti na yale ya kikapitalisti, huko yote yalaumiania kwa sera zake kuhusu masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Tatizo hapa ni kuhusu ushindani katika teknolojia na Nyanja nyingine ambazo Uchina inafaa kukabiliwa vikali. Hii ndiyo taswira ya Amerika. Inafaa kutiba bidii zaidi katika ubunifu wa kiteknlojia kuzima uwezo wa Uchina,” anasema mwanauchumi wa mradi wa Asia na Pasifiki katika Jumba la Chatham, Bw Kerry Brown.

“Fikra za masoko kutawalwa na taifa la kikomunisti linaikera Amerika na inataka kuona mabadiliko makuu. Hili ndilo suala zima. Sina hakika kama inawezekana katika mkutano mmoja wa marais wa pande zote. Suala hili la uadui huenda likazidi kutokota kwa miaka mingi ijayo,” anasema.

Kando na ada za uagizaji wa bidhaa, Amerika pia imeiwekea Uchina shinikizo za kisiasa, na kuongeza imani kuwa hivi sasa vitakuwa vita vya moja kwa moja kupitia Nyanja mbalimbali, sawa na Vita vya Baridi baina ya Amerika na Urusi miaka ya themanini.

Vikwazo zaidi 

Agosti 2018, Amerika ilizidisha vikwazo dhidi ya Uchina, na kuzima mauzo ya bidhaa za teknolojia ya hali ya juu nchini humo. Pia ilipitisha sheria mpya ambayo inazuia Wachina kuwekeza Amerika katika sekta ya teknolojia.

Hapo Septemba mwaka uliopita, Trump alikiwekea vikwazo kitengo kimoja cha jeshi la Uchina kuhusu ununnuzi wa ndege za kivita kutoka Urusi na mabomu ya kutoka ardhini hadi angani.

Katika siasa, Amerika ilidai Uchina ilijaribu kuvuruga Uchaguzi wa mwaka uliopita wa mabunge. Uchina ilikana madai hayo, na badala yake kuikejeli Amerika kwa maandalizi ya majeshi yake katika bahari ya South China.

Kwenye kongamano la muungano wa Asia-Pasifiki hapo Novemba 2018, Naibu Rais wa Amerika Mike Pence aliikosoa Uchina kwa miradi yake ya ufadhili wa ujenzi wa barabara na madaraja akasema ni njia moja kubwa ya kuyasukumia mataifa yanayoendelea madeni makubwa ili yaiunge mkono kwa sera zake.

Akihutubu katika kongamano hilo, rais wa Uchina Xi Jin Ping alijitetea kuwa ufadhili wake ni ‘mtego’ na kwamba Beijing haina ‘ajenda fiche’ huku akikejeli sera ya ‘Amerika Kwanza’ kuhusu vikwazo.

Amerika sasa imeapa kuzidisha vikwazo dhidi ya bidhaa kutoka Uchina na hatimaye kupiga marufuku bidhaa zote, iwapo taifa hilo halitafuata masharti inayotaka.

Maafisa wakuu serikalini Amerika wamepuuzilia mbali uwezekano wa suluhu kwa zogo hili, huku wadau wa masuala ya kimataifa wakisema kuwa “masuala yanayohusu Trump hayawezi kutabiriwa, na huenda suluhu ya kiajabu ikapatikana.”

Ikikosekana, basi uhasama huu huenda ukafikia kiwango cha kuigawanya Dunia zima kwa mirengo miwili mwaka huu – Ule unaounga mkono Amerika, na ule utakaoshikilia kuwa Uchina ina sera bora za kiuchumi.

Wakenya waliteseka 2018, watarajia hali bora 2019

NA LILYS NJERU

JAPO mwaka uliopita wa 2018 ulikuwa na changomoto chungu nzima kwa wananchi, Wakenya wengi mwaka huu wa 2019 wameomba kila mmoja awe na utu na roho ya kusaidia wengine.

Ukosefu wa kazi, kufutwa kiholela na waajiri na kukosa kutimiza ahadi kwa wapendwa wao kutokana na gharama ya juu ya maisha ni baadhi tu za changamoto nyingi zilizowakosesha Wakenya usingizi mwaka 2018. Kulingana na Wycliffe Asuga, 32 ambaye ni baba wa mtoto mmoja, alishuhudia kwa masikitiko akiba yake yote ya Sh100,000 ikiisha vivi hivi asibakie hata na senti mwaka uliopita.

“Mwaka jana nilikuwa na lengo la kununua kipande cha ardhi ili nijenge nyumba yangu kwa kuwa familia yangu imekuwa ikiishi katika nyumba ya kukodisha. Nilianza kudunduiza fedha mwanzo wa mwaka huo ila kila kitu kilienda mrama baadaye,” akasema Bw Asuga.

Baba huyo na mkewe wanafanya kazi ya upigaji rangi viatu jijini Nairobi na kwa pamoja walilenga kutimiza ahadi hiyo ila katikati ya mwaka wa 2018 mambo yaliwaharabikia baada ya mkewe kukumbwa na maradhi.

“Katikati ya mwaka wa 2018, aliugua ghafla na hangeweza kuendelea na kazi yake. Akiba yangu yote iliishia kwenye gharama za matibabu. Kwa sasa anatarajiwa kufanyiwa oparesheni mwisho wa mwezi huu na nina wingu la matumaini oparesheni hiyo itafaulu,” akasema Bw Asuga.

Kilichotia msumari moto kwenye kidonda cha Bw Asuga hata hivyo ni jinsi idadi ya wakazi wa jijini wanaofika kwenye vibanda vyao vya upigaji rangi ili kuhudumiwa ilivyopungua pakubwa.

“Mimi ni maskini kwa sababu kile ninacholipwa sasa ni ya kujikimu tu. Hata hivyo mambo yakinyooka 2019, huenda nikaanzisha kilimo cha ufugaji katika kijiji changu mashinani, “ akaongeza Bw Asuga.

Masaibu yayo hayo pia yanamkumba Collins Ouma, 26 ambaye kwa sasa anatafuta ajira. Kwa wiki kadhaa Bw Ouma amekuwa akitembelea ofisi nyingi jijini Nairobi akiwa amejihami na vyeti vyake akiomba ajira ila bado hajafanikiwa.

Kulingana naye, mwaka wa 2018 ulikuwa mgumu sana. “Nilianza biashara ya kuuza nguo mwezi Juni ila ikaporomoka Agosti. Baadaye nilipata kandarasi ya kuwa mlinzi na kampuni moja ya usalama. Kwa sasa nasaka ajira kwa udi na uvumba,” akasema Bw Ouma. Vile vile kijana huyo anatia dua usiku na mchana ili aweze kupata fedha za karo ili arejee Chuo Kikuu cha Kenyatta kukamilisha shahada ya elimu aliyokuwa akisomea.

Wengine kama Peris Muthoni, afisa wa usalama hata hivyo alishabikia mno mwaka wa 2018 baada ya kufaulu kumsajili mwanawe kusomea Chuo Kikuu cha Nairobi. “Ingawa sikuweza kufikia malengo yangu ya kifedha niliyojiwekea, nafurahi sana kwamba niliweza kumsajili mwanangu chuoni ili aweze kusoma. Natumai mwaka wa 2019 utakuwa wa heri,” akasema Bi Muthoni. Kulingana na matokeo ya utafiti wa kampuni ya TIFA, asilimia 56 kati ya Wakenya 1,267 waliohojiwa walikemea sana mwaka wa 2018 wakiutaja kama mbovu zaidi.

Hii ilitokana na changamoto kama gharama za juu ya maisha, ukosefu wa ajira na umaskini.

MWAKA MPYA 2019: Wito wa amani na umoja Kenya

BENSON MATHEKA na BRIAN OCHARO

WAKENYA wamehimizwa kuishi kwa umoja na amani mwaka huu ili nchi ipate ustawi wa kiuchumi.

Viongozi wa mirengo yote ya kisiasa na kidini walitoa wito kwa Wakenya kukumbatia undugu na kuungana ili kustawisha nchi yao 2019. Akiwa Mombasa, Rais Uhuru Kenyatta aliwataka Wakenya kuishi kama ndugu na kuheshimiana.

“Sisi ni familia moja ya watu wa Kenya na taifa la Kenya. Tunapaswa kujifunza kuishi, kufanyakazi pamoja na kuheshimu kila mmoja kwa lengo la kujenga nchi yetu,” alisema.

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, alisema ana matumaini kwamba mwaka wa 2019 utakuwa wa ustawi nchini. “Ninajiunga nanyi Wakenya wenzangu katika matumaini yenu na kuwatakia mwaka wa 2019 wenye ustawi. Ingawa 2018 ulianza kwa hali ngumu, tuliumaliza kwa matumaini. Niko na hakika siku zijazo zitakuwa bora zaidi kwetu,” alisema Bw Odinga kwenye risala ya mwaka mpya.

Aliwakumbusha Wakenya kwamba, walimaliza mwaka wa 2018 kwa utulivu kwa sababu ya kuchagua amani.

“Kama kuna kitu tulichojifunza 2018 ni kwamba, watu huwa kile wanachochagua kuwa. Tunaweza kuchagua kugawanya au kuunganisha nchi, kupigana wenyewe kwa wenyewe kwa misingi ya kikabila au kuungana kama jamii moja iliyo na mwelekeo mmoja, tunaweza kuungana kupigana na ufisadi na kuepuka adhabu au kukubali maovu haya ambayo yametuangamiza kwa muda mrefu,” alisema Bw Odinga.

“Ninajitolea kuendelea na chaguo nzuri za 2018 na kufanya chaguo sawa mradi tu ni kupeleka Kenya na Afrika mbele 2019,” akaongeza.

Kwenye risala yake, Rais mstaafu Daniel Moi aliwataka Wakenya kukumbatia amani na umoja. “2019 uwe mwaka wa amani na umoja wa taifa,” alisema na kuongeza kuwa nchi haiwezi kupata maendeleo ya kiuchumi ikiwa imegawanyika.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alisema 2019 utakuwa mwaka wa mabadiliko makubwa kwa maisha ya Wakenya chini ya muafaka wa viongozi wa serikali na upinzani. Katika risala yake ya mwaka mpya, mwenyekiti wa chama cha Kanu aliye pia Seneta wa Baringo, Gideon Moi aliwataka Wakenya kuishi kama watu wa taifa moja.

Gavana wa Mandera Ali Roba alitoa wito kwa Wakenya kutetea na kulinda ugatuzi mwaka huu mpya wa 2019. Kwenye taarifa, Bw Roba ambaye ni mwenyekiti wa baraza la maendeleo la kaunti za kaskazini mwa Kenya aliunga marekebisho ya katiba lakini akasema yanafaa kushirikisha maslahi ya Wakenya wote.

Alisema ugatuzi umesaidia kubadilisha nchi na unafaa kulindwa. “Ni matumaini yangu kwamba ugatuzi utatiwa nguvu zaidi na kulindwa na wote,” alisema Bw Roba.

Viongozi wa dini ya Kiislamu eneo la Pwani nao waliwaomba Wakenya kuhubiri amani wanapoendelea na sherehe za mwaka mpya wa 2019. Wakiongozwa na Katibu Mwandalizi wa Baraza la Waislamu na Wahubiri wa Kenya, Sheikh Mohamed Khalifa, waliwaomba wanasiasa kuepuka siasa za ukabila na kuunganisha Wakenya ili kuwe na maendeleo nchini.

Raia wa Argentina wagoma kulilia hali mbaya ya uchumi

Na AFP

SHUGHULI zilikwama Argentina kufuatia mgomo wa umma Jumanne uliosababishwa na matatizo ya kiuchumi yanayokabili taifa hilo.

Wakati huo huo, rais wa benki kuu nchini humo alijiuzulu huku serikali ikijitahidi kushauriana na Hazina ya Kimataifa ya Fedha (IMF) ili ipate mkopo wa dharura.

Huku Rais Mauricio Macri akiendeleza mashauriano ili kupokea ufadhili wa dola bilioni 50 kutoka kwa IMF, thamani ya sarafu ya nchi hiyo (peso) ilizidi kudorora huku habari zikicipuka kwamba Guido Sandleris alichukua mahali pa Luis Caputo kuwa msimamizi mpya wa benki kuu.

Raia karibu wote wa Argentina walifanya mgomo na baadhi wakaandamana kuonyesha ghadhabu yao kuhusu jinsi gharama ya maisha imekuwa ngumu kufuatia jinsi thamani ya pesa ilivyoshuka kwa karibu asilimia 50 dhidi ya dola mwaka huu.

Maduka mengi, mabenki na afisi za umma zilifungwa huku wahudumu wa uchukuzi wa umma na teksi wakilemaza shughuli za usafiri.

Baada ya maandamano ya Jumatatu yaliyoandaliwa na vyama vya wafanyakazi, waandamanaji wa upande wa upinzani waliungana nao Jumanne kukawa na makabiliano kati yao na maafisa wa usalama Buenos Aires mnamo Jumanne.

Barabara za katikati mwa jiji zilikuwa tulivu mno kwani hapakuwa na watu walioenda kazini.

Viwanja vya ndege pia havikuwa na watu wengi kutokana na kuwa usafiri wa ndege kuingia na kuondoka katika nchi hiyo ulifutiliwa mbali.

Mfumko wa kiuchumi unatarajiwa kupanda kwa asilimia 40 kufikia mwisho wa mwaka.

Hali ilianza kuwa mbaya Argentina kuanzia Aprili wakati thamani ya peso iliposhuka kwa kasi na serikali ikaomba mkopo wa dola bilioni 50 kutoka kwa IMF.

Hatua hii haikuleta afueni na Macri akatangaza Agosti kwamba ataomba mkopo uliotarajiwa kutolewa kwa awamu za miaka mitatu utolewe haraka mwaka huu.

Macri pia alitangaza mikakati mingine ya kupunguza matumizi ya fedha za umma ikiwemo kupunguza wizara za serikali kwa asilimia 50, na kurudisha ushuru wa nafaka zinazouzwa nje ya nchi.

Benki Kuu ilitoa taarifa kudai kuwa Caputo alijiuzulu “kwa sababu za kibinafsi” huku ikieleza matumaini yake kuwa “makubaliano mapya na IMF yatarudisha imani kwa hali ya kifedha na ubadilishanaji wa hisa za kigeni”.

Baadhi ya wachanganuzi walisema kulikuwa na uvumi Ijumaa iliyopita kwamba angejiuzulu kwa sababu ya “tofauti kati yake na IMF kuhusu sera za kifedha”.

Sandleris ni mwanauchumi ambaye aliwahi kufanya kazi katika Benki ya Dunia. Alikuwa naibu waziri wa fedha kabla kutangazwa kuwa rais wa benki kuu.

WANDERI: Muda umefika Wakenya kuungana ili kujikomboa

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Agosti 10, 1792 mfumo wa kifalme ulifikia mwisho nchini Ufaransa, baada ya maandamano makubwa ya wakulima dhidi ya viwango vya juu vya kodi walivyokuwa wakitozwa.

Wakulima waliandamana na kupiga kambi katika Ikulu ya Mfalme Louis 16, wakilalamikia kiwango kikubwa cha fedha ambacho ufalme ulikuwa ukitumia ili kuendesha maisha ya kifahari, huku wao wenyewe wakiishi katika maisha ya kichochole.

Ujumuisho wa raia wa Ufaransa wakati huo ni kuwa zaidi ya asilimia 80 walitegemea kilimo, hivyo walihisi makali ya kiwango hicho cha kodi.

Kwa ghadhabu ya kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama mkate, maandamano hayo yalipelekea kuisha kwa mfumo wa kifalme na kuanza kwa utaratibu mpya wa kiutawala uliowashirikisha raia wote.

Cha msingi ni kwamba, watu hawakuungana tu; ila kando na matatizo ya kiuchumi yaliyowakabili, waliwategemea sana wasomi na wanafalsafa ambao waliwapa mwanga kuhusu udhalimu wa mfumo wa kifalme.

Baadhi ya wanafalsafa hao wenye mawazo ya kimapinduzi ni kama Voltaire, Jean-Jacques Rousseau, Denis Diderot kati ya watu wengine wengi.

Mapinduzi hayo ya kiraia yalichangia pakubwa katika ujio wa viongozi kama Napoleon Bonaparte, aliyeibukia kuwa maarufu sana katika historia ya kimapinduzi ya Ufaransa.

Kwa sasa, Kenya iko katika njia panda ya kisiasa, hasa inapoelekea mwaka 2022.

Wengi wanalalamikia ugumu wa maisha, hasa baada ya Serikali kuongeza asilimia 16 ya kodi kwa mafuta na kuathiri bidhaa zote zinazohusiana nayo.

Hili bila shaka limewaacha Wakenya katika njia panda ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kuhusu wanakoelekea kutokana na ugumu wa kimaisha.

Kwanza, kilicho dhahiri ni kwamba, kama ilivyokuwa Ufaransa, kuna uwezekano mkubwa kwamba safari ya mapinduzi ya kiraia nchini itaanza karibuni.

Huu ndio wakati mwafaka zaidi ambapo Wakenya wanapaswa kuungana dhidi ya mfumo wa kitabaka ambao umetumiwa na famillia za kisiasa kuwakandamiza kwa msingi wa kuwafarakanisha.

Kwa mfano, wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga walijawa matumaini kwamba mwafaka wa kisiasa kati yao ungezaa matunda.

Kuna wale walioshangilia kwamba hatimaye ‘matunda’ waliyokuwa wakitafuta wameyapata. Wengine walifurahi kwamba “usumbufu” wa adui yao umeisha.

Ni maswali mengi ila hali ilivyo, imefikia wakati Wakenya kuzinduka na kuanza mapinduzi ya kiraia.

Kama anavyorejelea msomi Frantz Fannon (kwenye kitabu Wretched of the Earth-Watengwa wa Dunia) tabaka la kundi la chini litabaki mateka wa mabwanyenye waendesha uchumi ikiwa halitajitokeza na kupigania haki zao.

Katika maasi ya Kiarabu yaliyoanza mnamo 2011, uchunguzi wa kina umebainisha kwamba ingawa kulikuwa na shinikizo za kisiasa, mojawapo ya sababu kuu ilikuwa ni shinikizo za kupanda kwa bei za msingi kama mkate jinsi Kenya ilivyo kwa sasa.

Imefikia wakati Wakenya kuungana bila kujali tofauti zao za kikabila, kisiasa, kidini, kitamaduni kusema “Yametosha”!

Si Uhuru, Raila ama Ruto atawaokoa. Njia ni moja; kuungana na kuanza safari ya ukombozi.

akamau@ke.nationmedia.com