UDA yaanza kuyumba

 

Na ONYANGO K’ONYANGO

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA), chake Naibu Rais William Ruto, kimekumbwa na sintofahamu mpya kuhusiana na orodha ya majina ya wanachama wa Baraza lake Kuu la Kitaifa (NEC) iliyotolewa wiki jana.

Sababu ni kwamba NEC itatekeleza wajibu mkubwa katika maandalizi ya mwongozo wa uteuzi wa wagombea viti mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Hii ndio maana baadhi ya wanachama wameelezea kutoridhishwa na orodha ya wanachama 34 wa NEC iliyowasilishwa kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Hali hii imempa Dkt Ruto hofu na wasiwasi kwamba huenda kutoridhika huko kukaathiri ushawishi wa UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii ni licha ya kwamba wanaoibua manung’uniko wanafanya hivyo kichichini.Kwa upande wake Katibu Mkuu Veronica Maina ameungama kuwa kuna dosari fulani katika orodha ya majina hayo na kuahidi kuirekebisha.

“Mnamo Oktoba 12, 2021 UDA iliwasilisha kwa wanachama na umma kwa ujumla orodha ya majina 34 ya watu watakaohudumu kama wanachama wa NEC, kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa, 2011.”

“Hata hivyo, chama kingependa kujulisha umma kwamba kulikuwa na dosari isiyokusudiwa katika orodha hiyo na hivyo orodha yenye marekebisho itatolewa hivi karibuni,” Bi Maina akasema Alhamisi.

Chimbuko la malalamishi ni kwamba baadhi ya walioko kwenye orodha hiyo wametangaza azma ya kuwania viti katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Wale ambao wanapania kupambana nao kusaka tiketi ya UDA wanahisi kuwa watu hao watapendelewa wakati wa mchujo wa chama hicho.

Baadhi ya wale ambao wanajumuishwa kwenye orodha ya wanachama wa NEC ni mbunge anayehudumu wakati huu, waziri wa zamani, mbunge wa zamani, meneja wa zamani ya afisi ya kushirikisha kampeni za urais za kiongozi wa ODM Raila Odinga na wataalamu.

Orodha hiyo pia inajumuisha, mwenyekiti wa UDA Johnston Muthama na manaibu wake watatu, Waziri wa zamani Kipruto Kirwa, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako na Nicholas Marete.

Mipasuko UDA na Jubilee yaibua vyama vipya Mlimani

Na GITONGA MARETE

KUPOROMOKA kwa chama cha Jubilee na mng’ang’anio wa tiketi katika chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA) ndizo sababu kuu zinazowasukuma wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya kuunda vyama vidogo kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Ili kujihisi salama, wanasiasa kadhaa wanaogura chama tawala wanaamua kuunda vyama vipya ili walinde nafasi zao katika ulingo wa siasa hapo mwakani.

Mwanasiasa mkuu wa hivi punde kuunda chama kipya ni Gavana wa Meru Kiraitu Murungi ambaye alishinda kiti cha ugavana katika uchaguzi wa 2017 kwa tiketi ya Jubilee.

Ameunda chama cha Devolution Empowerment Party ambacho sasa kimejiunga na orodha ndefu ya vyama vidogo katika eneo la Mlima Kenya, iliyokuwa ngome ya Jubilee.

Vyama vingine vyenye mizizi katika eneo hilo ni Usawa Party kinachohusishwa na Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria, Chama cha Kazi (CCK) cha Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na The Service Party (TSP) kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.

Vyama vingine ni pamoja na; Party of National Unity (PNU) kinachohusishwa na Waziri wa Kilimo Peter Munya, Narc- Kenya cha Martha Karua, Tujibebe Wakenya Party kilichoundwa na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo na The New Democratic kilichoasisiwa na mfanyabiashara wa Nyeri Thuo Mathenge.

Vyama hivyo vimekubalika katika eneo la Mlima Kenya haswa baada ya Bw Kiunjuri, Bw Kuria na Bi Karua kuunda vuguvugu la Muungano wa Mlima Kenya.Mnamo Septemba mwaka huu, viongozi wa Jubilee walikutana na Bw Kiunjuri na Bi Karua katika mkahawa wa Serena, Nairobi ambako ilidaiwa walijadili mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanasiasa wako mbioni kukumbatia vyama hivyo vidogo kutokana na imani kuwa baada ya Jubilee kupoteza ushawishi eneo la Mlima Kenya, itakuwa vigumu kwa mwanasiasa kushinda kiti katika uchaguzi huo kwa kutumia tiketi yake.

Gavana Murungi, ambaye ametangaza kuwa “Jubilee imekufa na kuzikwa” alitwaa chama cha Restore and Build Kenya (RBK) na kugeuza jina lake kuwa DEP. RBK ilitumiwa na aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Elimu Profesa James Ole Kiyiapi kugombea urais 2013.

Chama cha DEP kinatarajiwa kuchota umaarufu katika eneo la Mlima Kenya Mashariki linalojumuisha kaunti za Meru, Embu na Tharaka Nithi.

Bw Murungi ambaye juzi alisema “mwanasiasa yeyote ambaye anataka kupoteza katika uchaguzi mkuu wa 2022 awanie kwa tiketi ya Jubilee” ameibuka kuwa mfalme wa kuunda vyama vipya baada ya kupata idhini ya kutwa chama cha RBK.

Tayari Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu ameidhinisha jina jipya la DEP na alama ya Basi. Alama hiyo ndiyo ilikuwa ya chama cha Alliance Party of Kenya (APK) ambacho Bw Murungi alitumia kuwania ugavana wa Meru 2013 na kushinda.

Ni miongoni mwa vyama 13 vilivyovunjwa mnamo 2016 ili kuunda chama tawala cha Jubilee ambacho sasa kimesalia kigae.

Hii ni baada ya Naibu Rais William Ruto kuongoza kukiasi na kuunda cha cha UDA, Rais Uhuru Kenyatta aliporidhiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo 2018.

Bw Murungi alisema kuwa eneo la Mlima Kenya Mashariki litatumia chama hicho cha DEP kujadiliana na vyama vya ODM, ANC, Wiper na KANU kuhusu ugavi wa rasilimali za kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Mshirika wa karibu wa Shahbal ahamia UDA

NA MWANDISHI WETU

Mwaniaji wa kiti cha Uwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Mombasa Bi Miraj Abdullahi sasa ameachana na mshirika wake mkubwa Suleiman Shahbal wa ODM na kuingia chama cha UDA. Mshirika wake mkuu sasa ni aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa, Bi Miraj alisema kuwa hatafanya kazi na Shahbal kwani ameamua kuendeleza ajenda yake ya kisiasa kupitia kwa chama cha UDA kinachohusishwa na Dkt Ruto.

“Sitashirikiana tena na Bw Shahbal licha ya kwamba tumekuwa pamoja kwa muda wa miaka kumi iliyopita. Wakati umefika kwangu kuendeleza ajenda yangu ya kisiasa ambayo inaonekana kwamba haiungi mkono,” Bi Miraj akasema.

Alifichua kuwa ndoto yake ya kuwania kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Mombasa ndiyo ilivuruga uhusiano wake na Bw Shahbal.

“Urafiki kati yetu unapaswa kuruhusu kila mmoja wetu kujiendeleza. Tunapaswa kuendeleza ndoto zetu. Bw Shahbal hajakuwa akiunga mkono ndoto yangu ya kisiasa tangu tulipokutana mnamo 2013,” Bi Miraj akasema.

Bi Miraj aliandikisha historia kwa kuwa mwaniaji wa kike mwenye umri mdogo zaidi kuwania wadhifa wa udiwani katika Wadi ya Tononoka, Mombasa katika uchaguzi mkuu wa 2013.

Aliwarai wakazi wa Mombasa kuunga mkono ndoto yake ya kisiasa anapojiandaa kuwania kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Wanawake.

Lakini katika ujumbe alioweka kwenye ukurasa wake wa Facebook Shahbal alisema hataruhusu tofauti za kisiasa kuvuruga uhusiano wao.

“Nimemjua Miraj kwa zaidi ya miaka 10. Naheshimu uamuzi wake wa kujiunga na UDA kwa sababu ni wito kutoka katika nafsi yake. Sitaruhusu urafiki wetu wa miaka 10 kuharibiwa na tofauti zetu za kisiasa,” akasema.

“Nawaomba wafuasi wangu wasimharibie sifa kupitia mitandao ya kijamii. Kazi yake katika mradi wa Buxton Point ni tofauti na haitaingiliana hata kidogo na azma yake,” Bw Shahbal alisema katika ujumbe wake.

Hata hivyo, Bi Miraj alitangaza kujiuzulu kutoka wadhifa wake kama Mshirikishi wa Mradi wa Buxton Point.

CCM yakataa kuingia UDA

Na FRED KIBOR

HATUA ya Naibu Rais Dkt William Ruto ya kutaka vyama vyote vinavyounga mkono azma yake ya kuingia ikuluni 2022 vivunjwe kisha vijiunge na UDA, imekashifiwa na Chama cha Mashinani (CCM) ambacho kinaongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto.

Licha ya kuwa CCM imesema kuwa inaunga mkono azma ya Urais wa Dkt Ruto, chama hicho kimesisitiza kuwa hakitavunjwa na kitawasilisha wawaniaji wa nafasi nyingine za uongozi isipokuwa ile ya urais pekee.

Kaimu Katibu Mkuu wa CCM Albert Kochei jana aliambia Taifa Leo kuwa uongozi wa chama hicho ulikutana na kuafikiana kuwa watawasilisha wagombeaji katika vyeo vingine vya uongozi mnamo 2022.

“Mwaniaji ambaye tunamvumisha 2022 anasalia kuwa Naibu Rais Dkt Ruto. Kama chama tutapigania viti vingine wala hatutaingia kwenye mkataba wa ushirikiano na chama chochote hata UDA. CCM inasimamia demokrasia, usawa na uhuru wa Wakenya,” akasema Bw Kochei.

Katibu huyo alishikilia kuwa haitakuwa sawa iwapo baadhi ya wanasiasa watawashurutisha wenzao wavunje vyama vyao, akisema hatua hiyo ni kurejesha taifa katika enzi za utawala wa chama kimoja.

“Tunamuunga mkono Dkt Ruto kwa sababu kauli mbiu yake ya hustler inawiana na ajenda ya CCM. Sote tunapigania usawa na kuinuliwa kwa maisha ya Mkenya wa kawaida,” akaongeza.

Alisema CCM ilichukua msimamo huo kutokana na kile ambacho kilitokea baada ya kuvunjwa kwa chama cha Jubilee, alichodai kuwa sasa kimesalia kama kigae.

“Wakenya wamejifunza kutokana na kile ambacho kilifanyika ndani ya Jubilee na raia nao wanatumia vyama ili kuhakikisha viongozi wanawawajibikia. Vyama vya kisiasa huwa ni maarufu sana wakati wa uchaguzi kwa sababu ni kutokana na uwepo wao ambapo raia wapo hiari kuwachagua viongozi bora.”

Aidha, Bw Kochei alisema chama hicho pia hakitawapokea wawaniaji ambao wamehama vyama vyao baada ya kulemewa katika uteuzi wa tiketi hata iwapo watatokea UDA au chama chochote kingine.

“Sisi tunaongozwa na sheria na wale ambao wana manifesto inayoshabikiwa na raia ndio watatumia tiketi yetu,” akasisitiza.Katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wanasiasa wengi wandani wa Dkt Ruto wanapigania kutwaa tiketi ya UDA huku suala kuu likiwa.; iwapo kutakuwa na uwazi katika shughuli za uteuzi.

“Iwapo uteuzi utavurugwa basi UDA itapoteza umaarufu hali ambayo haifai kutokea. Uteuzi unafaa uwe wazi na wandani wa Dkt Ruto hawafai kutumia ukuruba wao kupata tiketi za moja kwa moja,” akasema Jonathan Bii, anayelenga kiti cha Ugavana cha Uasin Gishu.

Hata hivyo, Mshirikishaji wa UDA Uasin Gishu Paul Kiprop aliwahakikishia wote kuwa uteuzi huo utakuwa huru.

“Kiongozi wetu amezungumzia suala hili mara kadhaa na akatuhakikishia kuwa kila mwaniaji atakuwa na nafasi ya kupigania tiketi debeni. Katika ngome za UDA hatutavumilia tabia ya watu kuidhinishwa na kulazimishiwa raia kwa sababu wawaniaji wote ni sawa,” akasema Bw Kiprop.

Wafuasi 13 wa UDA washtakiwa kwa ukiukaji wa kanuni za corona

Na George Odiwuor

WAFUASI 13 wa chama cha UDA katika Kaunti ya Homa Bay, Jumatatu walipigwa faini ya Sh2,000 kila mmoja kwa kukiuka masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Wafuasi hao walikamatwa Ijumaa iliyopita walipokuwa kwenye mkutano katika mkahawa mmoja mjini Homa Bay.Hata hivyo, walilalamika dhidi ya kubaguliwa.

Watu hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Homa Bay, Joy Wesonga, Jumatatu, ambapo walikubali makosa yao.Walishtakiwa kwa kushiriki kwenye mkutano kinyume na kanuni zilizowekwa na serikali.

Viongozi wa chama hicho walilipa faini hizo ijapokuwa walilalamikia “maonevu” dhidi yao na polisi. Viongozi hao walijumuisha mwanaharakati George Ayudi na Mshirikishi wa UDA katika eneo la Nyanza, Bw John Waria.

“Polisi hawapaswi kutumika na wanasiasa. Tuko katika nchi huru ambapo kila mmoja ana haki kujiunga na chama chochote cha kisiasa,” akasema. Aliongeza kuwa washiriki walihakikisha hawakuwa wamekaribiana, kama inavyohitajika na Wizara ya Afya.

Alisema walikuwa wamezingatia masharti hayo yote.Wanaharakati wa kisiasa katika eneo hilo pia walikashifu mtindo wa polisi kuwakamata watu kila mara kwa kisingizio cha kukiuka masharti hayo.

Walisema Mahakama Kuu tayari imefutilia mbali masharti hayo, hivyo watu wako huru kushiriki kwenye mikutano ya kisiasa.

Ruto apigia debe mgombeaji wa UDA Kiambaa kupitia simu

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ametoa wito kwa wakazi wa eneobunge la Kiambaa kujitokeza kwa wingi mnamo Alhamisi, Julai 15, 2021, kuchagua mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Akiongea na wakazi wa eneo hilo kwa njia ya simu, Ruto aliwataka wakazi kumchagua mgombeaji wa chama hicho, John Njuguna Wanjiku katika uchaguzi huo ambao UDA itatumia kusaka mbunge wake wa kwanza tangu ilipopewa jina jipya.

Naibu Rais aliwaambia wakazi kwamba ushindi wa Bw Wanjiku utaonyesha ishara nzuri kwa UDA kuelekea uchaguzi mkuu ujao katika kutekeleza ajenda yake ya kuunganisha Wakenya.

“Safari ya kuunganisha Wakenya wote imeanza. Nawahimiza kwa unyenyekevu kumchagua mgombeaji wa UDA John Njuguna Wanjiku,” akasema kupitia simu ya Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

“Si UDA ni chama? Si mgombeaji ni Wanjiku? Si tarehe ni Julai 15?” akauliza huku wakazi wakiitika kwa mshawasha.

Dkt Ruto aliwataka wakazi wa Kiambaa kuunga mkono chama cha UDA katika azma yake ya kuunda serikali ijayo mnamo mwaka wa 2022.

Uchaguzi mdogo wa Kiambaa umegeuka kuwa uwanja wa mashindano kati ya Dkt Ruto na mkubwa wake, Rais Uhuru Kenyatta.

Kambi ya Rais Kenyatta inapania kushinda kiti hicho cha Kiambaa, kupitia mgombeaji wa Jubilee, Kariri Njama, kuondoa dhana kuwa kiongozi wa taifa amepoteza ushawishi katika ngome yake ya Mlima Kenya.

Kwa upande wake, mrengo wa Dkt Ruto unafanya juu chini kushinda kiti hicho, ili kuthibitisha kuwa ushinda wao katika uchaguzi mdogo wa Juja haikuwa wa kubahatisha bali ni ithibati kuwa ushawishi wa Rais Kenyatta umeshuka zaidi eneo hilo.

Katika uchaguzi huo mdogo wa Juja, mgombeaji wa chama cha Peoples’ Empowerment Party (PEP) kinachohusishwa na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, George Koimbori, aliibuka mshindi.

Bw Koimbori alipata kura 12,159 na kumshinda kwa umbali Susan Njeri wa Jubilee aliyepata kura 5,764. Bi Njeri ni mjane wa aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo marehemu Francis Munyua Waititu, almaarufu, Wakapee.

Wiki jana, Rais Kenyatta alikutana katika Ikulu ya Nairobi na Bw Njama, na viongozi wengine wa Jubilee, ishara kwamba anachukulia uchaguzi huo mdogo kwa uzito.

Matokeo ya uchaguzi huo mdogo unaacha ujumbe mkubwa kuhusu siasa za urithi wa Rais Kenyatta haswa katika eneo pana la Mlima Kenya.

UDA yapigwa rafu Kiambaa

SIMON CIURI na WANDERI KAMAU

CHAMA cha UDA Jumapili kilijipata kona mbaya katika eneobunge la Kiambaa, Kaunti ya Kiambu, baada ya hafla iliyopangiwa kufanya katika uwanja mmoja kufutiliwa mbali katika hali ya kutatanisha dakika za mwisho mwisho.

Polisi walilazimika kufutilia mbali mashindano ya kandanda yaliyokuwa yamepangiwa kufanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Karuri, baada ya kubainika kuwa, Chama cja Jubilee (JP) pia kilikuwa kimepanga kuutumia uwanja huo.

Vyama vilikuwa tayari kuandaa hafla hizo kwani tayari vilikuwa vishapata kibali.

Mashindano hayo, maarufu kama ‘Kiambaa Hustlers’ Cup’, yalitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa UDA, huku yakitumika kumpigia debe mwaniaji ubunge Njuguna Wanjiku, anayewania kwa tiketi ya chama hicho.

Kamanda wa Polisi katika kaunti ya Kiambu, Ali Nuno, aliiambia ‘Taifa Leo’ wanachunguza ni katika mazingira yapi mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw Daniel Oleneya, aliruhusu uwanja huo kutumika na chama kingine ilhali alikuwa ameruhusu kutumika na mrengo wa UDA.

“Nimefutilia mbali mikutano miwili ili kuzuia mafarakano. Tumemwita mwalimu mkuu wa shule hiyo, Daniel Oleneya kutueleza utaratibu uliofuatwa kuruhusu uwanja huo kutumika kwa hafla mbili tofauti katika wakati mmoja,” akasema Bw Nuno kwenye mahojiano.

Chama hicho, ambacho kinahusishwa na Naibu Rais William Ruto, kilikuwa kimepata kibali kuandaa fainali ya mashindano hayo.

Timu za Thunder Youth na Karura Greens zilikuwa zimepangiwa kucheza saa tano huku timu ya Karuri United na Simba FC zikitarajiwa kukabiliana kwenye fainali.

Hata hivyo, Jubilee pia ilikuwa imepata kibali cha kutumia uwanja huo huo kupitia Muungano wa Makanisa katika Eneo la Kiambaa (KIF).

Muungano huo una ushirikiano mkubwa na Jubilee. Mkutano huo ulikuwa umepangiwa kutumika kumpigia debe Bw Kariri Njama, anayewania ubunge kwa tiketi ya Jubilee.

Bw Nuno alisema ikiwa wangeruhusu hafla yoyote kuendelea, kungezuka mafarakano, upande mmoja ukidai kupendelewa.

Makabiliano hayo yanajiri huku uchaguzi huo unaopangiwa kufanyika Alhamisi ukiendelea kukaribia.

Kampeni za uchaguzi huo zinatarajiwa kukamilika rasmi leo, kulingana na sheria za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kulingana na wadadisi, uchaguzi huo unaonekana kuwa kivumbi kikali cha kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto.

Vyama vya Jubilee na UDA vimekuwa vikifanya kila juhudi kuwavutia wapigakura, huku kila upande ukieleza imani ya kuibuka mshindi.

Alhamisi iliyopita, Rais Kenyatta alikutana na Bw Njama, wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Kanini Keega (Kieni), na Sabina Chege (Murang’a) katika Ikulu ya Nairobi, katika hatua iliyoonekana kuwapa “baraka” zake kwenye kampeni za uchaguzi huo.

Wabunge hao ndio wamekuwa wakiongoza kampeni za Jubilee katika eneobunge hilo. Licha ya mkutano huo, wanasiasa wa UDA wameapa “kuonyesha Jubilee kivumbi” kama ilivyokuwa katika eneobunge la Juja, ambapo chama kilishindwa na Bw George Koimburi, aliyewania kwa tikiti ya PEP, kinachohusishwa na Dkt Ruto.

Kampeni za UDA zimekuwa zikiongozwa na wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira) kati ya wanasiasa wengine wa mrengo wa ‘Tangatanga.’

Kando na Kiambaa, vyama hivyo viwili vinatarajiwa kukabiliana vikali katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Muguga, Kaunti ya Murang’a.

UDA kufanya uchaguzi wa mashinani Oktoba – Muthama

 

Na ONYANGO K’ONYANGO

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA), kinachohushwa na Naibu Rais William Ruto, kitafanya uchaguzi wa mashinani Oktoba mwaka huu, kabla ya mchujo wa wawaniaji wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika Juni 18 lakini ukaahirishwa. Washirika wa Dkt Ruto wamekuwa wakipigia debe chama hicho wakisema, ndicho atatumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao naada ya kutofautiana na Rais Kenyatta.

Wanasema chama kitaandaa uchaguzi wa mashinani kabla ya kuteua wawaniaji hili kuepuka makosa yaliyofanywa na Jubilee.

Kulingana na mwenyekiti wa UDA, Johnstone Muthama, ili mwanachama aruhusiwe kushiriki uteuzi wa chama, ni lazima awe mwanachama, kumaanisha kama vyama vingine, kitahitajika kuwa na orodha ya wanachama

.Bw Muthama anasema hatua hiyo itakipatia chama hicho nguvu kuliko vyama pinzani ambavyo huteua watu kuwa kaimu maafisa.

 

Jumwa akwamilia UDA, adai Ruto ataingia Ikulu 2022

Na VALENTINE OBARA

VIGOGO wa kisiasa ambao wangependa kumvuta Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa upande wao kutoka kwa kikosi cha Naibu Rais William Ruto kabla Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao, huenda wakahitajika kujikakamua zaidi.

Mbunge huyo ambaye amepanga kuwania ugavana wa Kaunti ya Kilifi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao, amepuuzilia mbali madai kwamba ameanza kunyemelea upande wa kisiasa unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Uvumi kuwa Bi Jumwa alipanga kuhama kundi la Tangatanga linaloongozwa na Dkt Ruto ulianza kuenea wikendi wakati alipokutana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli.

Ilifichuka kuwa, wawili hao pamoja na Mbunge wa Msambweni, Bw Feisal Bader walikutana faraghani katika hoteli iliyo Kaunti ya Kilifi.

Baadaye, Bw Atwoli alikutana na Bw Odinga, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, mwenzake wa Rarieda Otiende Amolo na Seneta wa Siaya James Orengo katika kaunti hiyo ikadaiwa Bi Jumwa ndiye aliyewapiga picha iliyokuwa ikisambazwa mitandaoni.

Hata hivyo, Bi Jumwa alijitokeza Jumatatu katika mkutano wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA), kinachohusishwa na Dkt Ruto kusisitiza msimamo wake.

Mkutano huo ulioleta pamoja makundi ya wanawake wa eneobunge la Kiambaa ulikuwa wa kumpigia debe mpeperushaji tikiti ya UDA katika uchaguzi mdogo wa Juni 15, Bw John Njuguna Wanjiku.

Alitumia hotuba yake katika mkutano huo kusisitiza hana nia ya kubadili msimamo wake akiashiria kupanga kutumia UDA kuwania ugavana mwaka ujao.

“Nataka wajue Aisha Jumwa hataondoka katika UDA. Mimi si mpangaji katika UDA bali ni mmiliki. Tunaunda serikali ijayo wapende wasipende,” akasema.

Bi Jumwa ni miongoni mwa wanasiasa ambao walikuwa mstari wa mbele kumpigia debe Bw Odinga kwa urais 2017, kabla ya kubadili msimamo.

Waasi wengi wa ODM pamoja na wengine wa Jubilee waliamua kujiunga na Dkt Ruto ambaye alianza kujitafutia umaarufu mapema akipanga kuwania urais kupitia UDA 2022.

Kwa upande wake, Bw Feisal aliwania ubunge katika uchaguzi mdogo Msambweni akiungwa mkono na kikosi cha naibu rais, akafanikiwa kushinda kiti hicho, baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Suleiman Dori.

Kabla kufariki kwake, Bw Dori pia alikuwa ameanza kukiasi Chama cha ODM ambako alikuwa ni mwanachama.

Bw Atwoli alidokeza kuwa yeye ndiye aliyeitisha mkutano na wabunge hao wawili akathibitisha walijadiliana kuhusu masuala ya kisiasa.

Ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo yao, mikutano aina hiyo huashiria upangaji wa mikakati ya kisiasa wakati huu uchaguzi unapokaribia ndiposa ukaibua gumzo mitandaoni.

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri kuhusu siasa bora zitakazofaidi nchi yetu na tumekubaliana kuhusu mambo mengi. Mimi ni mzee, huwa sialikwi katika mikutano bali mimi ndiye hualika watu,” akasema Bw Atwoli.

Bw Atwoli ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga licha ya kuwa mwanachama wa KANU, amejizolea sifa kwa kupanga mikutano ya kupatanisha wanasiasa wa pande tofauti hasa wanaojaribu kwenda kinyume na misimamo ya waziri huyo mkuu wa zamani.

Mkutano wake na wabunge hao wawili ulitokea wakati ambapo ODM imepoteza wabunge wengi na wanasiasa wengine Pwani, huku idadi ya wanachama wa Jubilee wanaoegemea upande wa UDA katika ngome za Rais Kenyatta ikizidi kuongezeka.

“Kuna watu walikuwa wanasukuma gurudumu la ODM Pwani na sasa hawapo. Jubilee na ODM zimeisha,” alisema Bi Jumwa katika mahojiano ya awali kwa kituo cha redio cha eneo hilo.

Hata hivyo, wanachama wa ODM wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama, wanasisitiza bado chama hicho kina umaarufu Pwani kinyume na jinsi wapinzani wao wanavyofikiria.

Wanachama 500 wagura UDA na kurejea ODM

KNA na CHARLES WASONGA

ZAIDI ya wanachama 500 wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika eneobunge la Karachuonyo wamehamia chama cha ODM kwa madai ya kutelekezwa na chama hicho kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Wanachama hao wanadai kuwa chama hicho kinajihusisha zaidi na shughuli za kutengeneza pesa na kufumbia macho matakwa yao.

Akiongea na KNA, aliyekuwa mshirikishi wa UDA eneobunge la Rachuonyo Duncan Ombat alisema chama hicho kimekuwa kikiendeleza usajili wa wanachama wapya eneo hilo kisiri bila kuwahusisha.

Bw Ombat alisema wanachama waliogura chama hicho walifanya hivyo kwa sababu hawakutaka kuhusishwa na shughuli hiyo haramu na iliyolenga kuwahadaa.

“Hakukuwa na demokrasia ndani ya ODM katika shughuli za mchujo kuelekea uchaguzi mkuu uliopita na ndiposa tukahama na kujiunga na UDA. Tulitarajia kuwa matakwa yetu yangeshughulikiwa katika chama hiki kipya lakini hili halijatendeka,” akasema Ombat.

Aliyekuwa mwenyekiti wa UDA katika eneobunge hilo Jekonia Olango aliunga mkono kauli hiyo akisema wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali kuendesha afisi za tawi la UDA katika eneo hilo.

Muthama atoa masharti makali kabla ya kuridhiana na Kalonzo

Na PIUS MAUNDU

MWENYEKITI wa chama cha UDA, Bw Johnston Muthama ameweka masharti makali kabla ya kushirikiana tena kisiasa na kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka.

Wawili hao walikosana miaka mitatu iliyopita, baada ya Bw Muthama kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha useneta wa Machakos mnamo 2017, na baadaye kuungana na kambi ya Naibu Rais Dkt William Ruto.

“Hatuwezi kushirikiana tena kisiasa hadi pale Bw Musyoka atajiondoa katika BBI pamoja na kuacha kuunga mkono handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga,” akasema Bw Muthama jana.Tofauti kati ya Bw Musyoka na Bw Muthama pia zimeenea kati ya viongozi wa Ukambani hasa kuhusiana na BBI.

Kati ya wale ambao wanapinga juhudi hizo ni Gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana na wabunge wanne wanaosema mabadiliko ya katiba hayafai kwa sasa, kwa kuwa kuna matatizo yanayopasa kushughulikiwa dharura.

Gavana wa Kitui Bi Charity Ngilu na mwenzake wa Machakos Dkt Alfred Mutua pia wanaunga mkono marekebisho ya katiba kupitia BBI ila wawili hao mara kwa mara wamekuwa wakikosana na Bw Musyoka hasa kuhusu siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

Maseneta Mutula Kilonzo Jnr (Makueni) na Enock Wambua wa Kitui pia wamekuwa wakionyesha msimamo wa uvuguvugu kuhusu BBI ili wasije wakakosoa siasa za Bw Musyoka.

Ruto sasa aingia vijijini akilenga kuvumisha UDA

Na ERIC MATARA

NAIBU Rais William Ruto amejitokeza wazi na kuanza kuvumisha chama cha United Democratic Alliance (UDA) vijijini kote nchini.

Chama hicho kimeanza msururu wa mikutano kujiandaa kwa uchaguzi wa mashinani na mchujo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mikutano hiyo pia imetajwa kuwa sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa mashinani wa Juni 2021, kuchagua maafisa wa wadi, maeneo bunge na kaunti.

Maafisa wa kitaifa watachaguliwa na wanachama wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC), baadaye mwaka huu 2021.

Mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa UDA, Bi Veronica Maina, alikutana na mamia ya wawaniaji kutoka eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa katika hoteli moja mjini Nakuru.

Taifa Leo ilifahamu kwamba mikutano hiyo itajumuisha, miongoni mwa mengine, kuelezea wawaniaji wa chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, malengo, manifesto na katiba ya chama.

“Tumezungumzia miongoni mwa mambo mengine, kueleza mfumo wa chama kufanya maamuzi, uteuzi, utatuzi wa mizozo na kanuni za chama,” alifichua Bi Maina baada ya mkutano huo.

Katibu huyo mkuu pia aliwahakikishia wawaniaji kwamba chama kitaandaa uteuzi wa haki na kwa njia ya uwazi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Mkutano huo ulileta pamoja wawaniaji na viongozi kutoka kaunti za Nakuru, Baringo, Bomet, Nyandarua na Narok.

Haya yanajiri wakati chama hicho kimeanza kampeni ya kusajili wanachama wapya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika ngome ya Dkt Ruto ya Rift Valley, wanasiasa wanaomuunga mkono wanajiandaa kupigania tiketi ya chama hicho kabla ya 2022.

Wawaniaji wa viti mbali mbali vikiwemo ugavana, useneta, ubunge na wawakilishi wa wadi wanamezea mate chama hicho kipya wakilenga kukitumia kutetea viti vyao au kuwaangusha wapinzani wao hatua ambayo inaweza kusababisha migogoro kabla ya 2022.

Bi Maina alisema chama cha UDA kitaandaa mikutano sawa na wa Nakuru, huko Meru na Mombasa na maeneo mengine nchini.

“Tunaandaa mikutano katika kumbi kwa kuzingatia kanuni za kuzuia Covid-19 zilizotolewa na wizara ya afya,” alisema Bi Maina.

Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika, mwakilishi wa Kike Kaunti, Bi Liza Chelule ni miongoni mwa waliosimamia mkutano huo.

Diwani wa Wadi ya Kabazi, Dkt Peter Mbae, anayenuia kugombea kiti cha ubunge cha Subukia, aliambia Taifa Leo kwamba UDA kinabadilika kuwa chama chenye nguvu eneo la Rift Valley na kote nchini.

“UDA ndicho chama cha siku zijazo katika Rift Valley kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hii ndiyo sababu tulikutana kuweka mikakati ya siku zijazo ya chama na kuhakikisha uteuzi na uchaguzi utafanyika vyema. Kuanzia sasa, utaona wanasiasa wengi wa Rift Valley wakitaka kujiunga na UDA,” alisema Dkt Mbae.

“Katika Rift Valley, huku ndiko kuporomoka kwa chama cha Jubilee. Kwenye uchaguzi wa 2022, hii itakuwa ngome ya UDA,” aliongeza.

Tayari, vita vya ubabe vya kuthibiti chama hicho Kaunti ya Nakuru vimeshuhudiwa kati ya Seneta Kihika na mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri.

Wilbaro yazoa ufuasi Nyanza na Magharibi

Na DERICK LUVEGA

CHAMA cha UDA kinachohusishwa na Naibu Rais, Dkt William Ruto jana kiliandaa mkutano na wanachama wake waliojisajili katika maeneo ya Nyanza na Magharibi mwa nchi.Maeneo hayo mawili ni ngome za kisiasa za Kinara wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi.

Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wake Johnstone Muthama, Katibu Mkuu Veronica Maina na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale.Walikutana na viongozi ambao wangependa kutumia tiketi ya chama hicho kuwania vyeo mbalimbali Magharibi mwa nchi na Nyanza 2022.

Viongozi hao walitoka katika kaunti za Vihiga, Kakamega, Bungoma, Busia, Kisii na Nyamira.Mikutano kama hiyo pia inatarajiwa kuandaliwa katika maeneo ya Eldoret, Nakuru, Meru na Mombasa mnamo Juni 3.

Viongozi hao waliwataka Mabw Mudavadi na Kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula wauze ajenda zao kitaifa badala ya kuchochea uhasama wa kikabila dhidi ya viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto eneo hilo.

Pia walimtaka aliyekuwa Waziri wa Biashara wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki, Dkt Mukhisa Kituyi aungane na vuguvugu la Hasla wakisema hana uungwaji mkono wowote wa kumwezesha kuwania Urais.

“Tunajua kuna wawaniaji wa kiti cha Urais kutoka eneo hili. Hata hivyo, hawasikiki zaidi ya hapa ndiyo maana wamekumbatia siasa za kikabila. Nawarai washiriki kampeni maeneo mengine badala ya kujikita katika kuwashutumu wawaniaji kutoka nje wanaokuja kusaka kura hapa,” akasema Dkt Khalwale.

Seneta huyo wa zamani wa Kakamega aliwataka wawaniaji hao wavumishe UDA mashinani, akitangaza kuwa atakitumia chama hicho kuwania kiti cha ugavana 2022.

Bw Muthama naye alipigia upato vuguvugu la Hasla akisema linawajumuisha watu wa matabaka yote na akawataka wamuunge mkono Dkt Ruto 2022.

“Hakuna chama chochote ambacho kimekutana na wagombeaji wanaotaka watumie kuwania viti mbalimbali hapa. Tutaelekea katika maeneo mengine kukutana na wanachama wetu nyanjani ili kuimarisha chama chetu,” akasema Bw Muthama.

Viongozi hao pia walimpongeza Jaji Mkuu mpya Martha Koome baada ya kuteuliwa na Rais Kenyatta wiki jana.Japo Mabw Mudavadi na Wetang’ula wapo ndani ya Muungano wa One Kenya Alliance, Dkt Kituyi bado hajatangaza chama atakachokitumia kuwania Urais 2022.

Muungano huo unatarajiwa kuwasilisha mwaniaji moja wa Urais 2022. Kwa sasa unasukumwa na ufanisi walioupata kwa kushinda viti vya ubunge vya Matungu, Kabuchai na Useneta wa Machakos.

Bw Mudavadi amekuwa akisaka uungwaji mkono kwa kuandaa mikutano katika eneo la Mlima Kenya pamoja na kaunti za Uasin Gishu na Kajiado.

Jubilee yapiga kampeni kali za kupangua UDA uchaguzini Rurii

Na WAIKWA MAINA

KUNDI la wanasiasa wa Jubilee wikendi waliendeleza mpango wa kudhoofisha ushawishi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mdogo wa Wadi ya Rurii, Kaunti ya Nyandarua, unaofanyika Jumanne.

Wanasiasa hao walitumia rasilimali nyingi kulipia matangazo katika runinga na redio mbalimbali kwenye jitihadi za kuvumisha mgombeaji wa Jubilee.

Wakiongozwa na Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia, Waziri wa Maji Sicily Kariuk, Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, Kiongozi wa Wengi Bungeni Amos Kimunya na Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, walifanya kila wawezalo kuhujumu kampeni za UDA.

Kikosi cha kumpigia debe mwaniaji wa UDA, Muraya Githaiga, kiliongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Nyandarua Faith Gitau, Rigathi Gachagua (Mathira) na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Katika vituo mbalimbali, wanasiasa wa UDA walikumbana na mapokezi mabaya huku wapiga kura wakiwataja kama wasaliti kwa kupinga mswada wa BBI bungeni.

UDA yapinga talaka

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, kimepinga uamuzi wa Jubilee kutaka muungano uvunjwe kutokana na tofauti za kifalsafa kati ya vyama hivyo viwili.

Kwenye barua aliyomwandikia Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu, Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina alisema wanapinga uamuzi huo wa Jubilee kwa sababu ulichukuliwa bila mashauriano na asasi husika za vyama hivyo viwili.

“UDA inapinga uamuzi huo wa Jubilee kwa misingi ya sehemu ya 10 (4) ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2012 na Kipengele cha 6 cha Mkataba wa Muungano. Asasi husika za vyama tanzu zitachukua hatua mwafaka za kusuluhisha mzozo huo na utajulishwa kuhusu matokeo,” Bi Maina akasema kwenye barua aliyomwandikia Bi Nderitu.

Katibu mkuu wa UDA amechukua hatua hiyo siku mbili baada ya chama cha Jubilee kuanzisha mchakato kukatiza uhusiano wake na chama hicho ambacho zamani kilijulikana kama Party of Development and Reform (PDR).

Katika barua aliyomwandikia Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Nderitu, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ya Jubilee iliamua kuwa itakuwa vugumu kukamilisha muungano kati yake na PDR baada ya chama hicho kubadili “jina, nembo, maafisa na sera”.

“Maafisa wote wa PDR waliokuwa wakishiriki katika mazungumzo kuhusu muungano wameondolewa na wale wapya wamedhihirisha uadui na Jubilee kwa kudhamini wagombeaji nje ya kaunti ambazo zililengwa ushirikiano wetu ulipoanza kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017,” akasema Bw Tuju.

Jubilee pia ilipinga kauli mbiu ya Hasla ambayo inaendelezwa na UDA.

Chama hicho tawala kilisemakwamba kauli hiyo inakwenda kinyume na kauli yake ya ‘Tuko Pamoja’ ambayo inadhamiria kuunganisha nchi.

Baadhi ya wanachama wa UDA pia wamekuwa wakilaumiwa kwa kudhamini wagombeaji kupinga wale wa Jubilee katika chaguzi ndogo zilizofanyika katika wadi za London na Hellsgate (Nakuru) na katika uchaguzi mdogo ujao katika eneobunge la Bonchari (Kisii).

Kulingana na mkataba kati ya Jubilee na PDR mnamo Mei, 2017, PDR ingedhamini wagombeaji katika kaunti za Pokot Magharibi, Isiolo, Mandera, Wajir na Garissa.

Wiki jana Naibu Rais Dkt Ruto alikariri kuwa atatumia UDA kuwania urais 2022 kwa sababu ndicho chama ambacho kinashirikiana na Jubilee, endapo hali ya uthabiti haitarejeshwa ndani ya chama hicho tawala.

“Bado nina matumaini kwamba tunaweza kukomboa Jubilee na kuiweka katika mkondo wa maono yake ya awali. Ikiwa hilo haitawezekana, tuko na mpango mbadala. Tuko na chama dada ambacho sasa kinaitwa UDA. Ikiwa mambo yataenda mrama Jubilee, chaguo letu mwafaka litakuwa UDA,” akasema kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen Alhamisi wiki iliyopita.

Jubilee kuvunja uhusiano na PDR ambacho sasa ni UDA

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Jubilee sasa kinapania kuvunja uhusiano wake na chama cha Party of Reforms and Development (PDR) kilichobadilishwa jina na kuwa United Democratic Alliance (UDA), na kuhusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Katika hatua inayoonekana kulenga kumlemaza kisiasa Dkt Ruto, Jubilee imemwandikia barua msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu ikiomba kuzima mkataba wa ushirikiano kati yake na PDR wa Mei 2018.

Kwenye taarifa iliyotolewa Aprili 20, 2021 Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ya chama hicho tawala ilisema ilifikia uamuzi huo kwa sababu PDR imebadili maafisa, nembo, falsafa na hata jina.

“PDR ambacho kimebadilika kuwa UDA sasa ni adui ya Jubilee kwa sababu kulingana na mkataba wa awali chama hicho kilipaswa kudhamini wagombeaji katika kaunti ya Pokot Magharibi, Wajir, Isiolo, Garissa na Mandera pekee. Lakini sasa kinashindana na Jubilee katika kaunti nyingine jinsi ilivyoshuhudiwa Nakuru na sasa Nyandarua na Kisii,” akasema Bw Tuju.

Katibu huyo mkuu ambaye alifafanua kuwa anawasilisha msimamo wa kamati ya NMC, alisema Jubilee imeamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu UDA kinaendeleza ajenda ya uhasla.

“Vile vile, Jubilee imekatiza mchakato wa kukamilishwa kwa uundwaji wa muungano inavyohitajika kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa,” akasema.

“Hata hivyo, wanachama wa muungano huo uliovunjwa ambao wanashikilia nyadhifa za uongozi katika mabunge mbalimbali wataendelea kuhudumu katika nyadhifa hizo, ilivyopangwa katika mkataba wa Mei 2018,” Bw Tuju akafafanua katika barua hiyo.

Hii ina maana kuwa Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo aliyechaguliwa kwa tiketi ya PDR na anashikilia wadhifa wa naibu kiongozi wa wengi katika Seneti ataendelea kuhudumu katika wadhifa huo katika bunge hilo. Madiwani waliochaguliwa kwa PDR pia wataendelea kushikilia nyadhifa zao katika mabunge ya kaunti za Wajir, Mandera, Isiolo na Garissa.

Dkt Ruto adokeza uwezekano wa kuungana na Raila katika uwaniaji 2022

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Dkt William Ruto ametangaza Alhamisi kuwa kuna uwezekano wa yeye kuungana kisiasa na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga kuwania urais wa 2022 japo kwa masharti.

Akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Citizen, Dkt Ruto amesema kuwa Bw Odinga hujiangazia kama aliye na maono ya kitaifa na “ingawa tunatofautiana naye mara kwa mara kuhusu masuala mengi haimaanishi hatuwezi kuwa na mpango.”

Kwa sasa, Dkt Ruto na Bw Odinga wako katika mirengo hasi kuhusu mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), akisema kuwa kila mtu ana haki ya kuwa na msimamo kinzani.

“Haimaanishi hizi tofauti haziwezi zikasuluhishwa na tukawa na umoja. Hii BBI iachiwe wabunge sasa waipige msasa na wapendekeze pa kubadilishwa ndipo kila mmoja awe mshindi. Wanaonisukuma niongoze mrengo wa upinzani kuhusu BBI wamekosa mwelekeo. Ukiwa unataka mrengo huo wa kupinga uwe na kiongozi, wewe chukua jukumu hilo upinge na uache kunishurutisha… Hapo sipo,” akasema Dkt Ruto.

Kuhusu kuungana na Bw Odinga, Dkt Ruto amesema: “Sio sisi katika mrengo wa Hasla tutakuwa wa kuenda kumtafuta tuungane bali ni yeye wa kuja pamoja na wengine ambao wataona kuwa mipango yetu ya 2022 iko shwari.”

Amesema kuwa ni lazima yeyote au chama chochote cha kisiasa katika kusaka kuungana na Hasla kuwa tayari kubadilisha mjadala wa kitaifa kutoka uwaniaji nyadhifa, kabila au eneo na badala yake “tuwe na zile siasa za kulenga kuinua wale walio chini kiuchumi.”

Dkt Ruto amesema kuwa hawezi kamwe akajiunga na mrengo wa kisiasa ambao umekuja pamoja kwa msingi wa kuunganisha vigogo wa kisiasa wa kikabila wakiwa na vyama vyao vya vijiji vya kwao na kuishia kujiita “muungano mtakatifu”.

Ameonekana kulenga muungano wa kisiasa kati ya kiongozi wa ANC Bw Musalia Mudavadi, kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka, mwenzao wa Ford Kenya Bw Moses Wetang’ula na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi.

Dkt Ruto aidha amekashifu uchambuzi wa Bw Mudavadi kuhusu jinsi ya kufufua uchumi wa taifa hasa kutokana na mzigo mkubwa wa madeni kutoka mataifa na taasisi ng’ambo.

“Tunajua kwamba shida yetu kama taifa kwa sasa ni mzigo wa madeni ambapo katika mwaka huu pekee wa kifedha, tutahitajika kulipa Shilingi Trilioni moja kwa wanaotudai. Mzigo huo unaendelea kuwa na uzito kwa kuwa bado tunaendelea kukopa. Suluhu letu sio jinsi ambavyo Bw Mudavadi amekuwa akisema eti tuombe muda zaidi wa kulipa madeni hayo,” akasema.

Kubuni nafasi za ajira

Alisema kuwa dawa ya uchumi wa taifa kwa sasa ni kusaka mbinu za kuwasaidia watu 16 milioni ambao kwa sasa hawana ajira ili wapate nafasi ya kuwa na pato ambalo litalipiwa ushuru ndio uchumi upanuke na kuwe na pesa za kulipa madeni hayo.

“Uchumi wetu hauhitaji hadaa kuwa Wakenya wengine watapewa likizo ya kulipia ushuru. Wakenya hawana shida na ulipaji ushuru na wako tayari kuanza kwa wakati wowote ule kutozwa ushuru. Ukiwapa mbinu ya kuunda mapato watakuwa tayari kiulipa ushuru. Hao ndio tunafaa tuwainue ili wakishaunda faida zao, walipe mikopo ambayo wametwikwa mabegani mwao na mikopo kiholela,” akasema.

Amesema kuwa vuguvugu lake la Hasla liko tayari kuunda hazina ya Sh60 bilioni ya kuinua uchumi wa walio chini ambapo Sh30 bilioni zitafadhili uendelezaji maeneo bunge huku kitita sawa na hicho kikiundwa cha kuwapa mikopo bila riba wote ambao hawana ajira na wangetaka kuijingiza katika biashara.

Dkt Ruto alisema kuwa kwa sasa ako ngangari, bado ako na imani ya kuibuka rais wa tano wa taifa hili baada ya uchaguzi wa 2022 na kuwa wale wanaopanga njama ya kumfungia nje wajipange kwa kuwa ako na maono na hatalegeza Kamba liwe liwalo.

Alisema kuwa taifa hili lilikuwa katika mkondo sawa kisiasa “kabla ya wageni waliokuja katika nyumba ya Jubilee (Handisheki) na tukaishia kukorofishana ndani ya boma kiasi wengine walianza kutimuliwa eti kwa kuwa wananiunga mkono kisiasa na kutangaza kwamba wao ni marafiki zangu wakaadhibiwa kwa kupigwa teke kutoka vyeo.”

Amesema hizo ni siasa za kipuzi, akiongeza kuwa bado yuko ndani ya chama tawala cha Jubilee “lakini kwa wakati tu unaofaa kwa kuwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) bado ni mradi wetu wa Hasla na ambao utakuwa kimbilio letu iwapo joto litazidi kuelekezewa sisi ndani ya chama tawala cha Jubilee.”

Chama cha Ruto chaaibishwa uchaguzini Machakos

Na PIUS MAUNDU

USHINDI wa Bi Agnes Kavindu Muthama kwenye uchaguzi wa useneta, Machakos Ijumaa umechukuliwa na wafuasi wa chama cha Wiper kuwa pigo kwa juhudi za Naibu Rais William Ruto kujipenyeza kwenye ngome hiyo.

Bi Kavindu alizoa kura 104,352 huku Bw Urbanus Muthama Ngengele wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) akiambulia kura 19,726 pekee.

Mbunge wa Mavoko Patrick Makau alisema chama cha UDA kinachohusishwa na Naibu Rais, kimejifunza kuwa siasa si mchezo wa watoto.

“Chama cha UDA kilikufa siku kilizaliwa Ukambani. Nawashauri wanachama wake waungane na kinara wetu Bw Kalonzo Musyoka tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022,” akasema Bw Makau katika kituo kikuu cha kujumuisha matokeo, Machakos Academy.

Bw Ngengele aliyekubali kushindwa, alitetea kura alizopata ikizingatiwa chama alichotumia.

“Chama cha UDA ni kipya Ukambani. Kupata karibu kura 20,000 si jambo dogo. Tutasonga mbele na juhudi za kujiimarisha,” akasema.

Kwingineko, Mbunge wa Mwala, Bw Vincent Musyoka aliyekuwa miongoni mwa waliompigia debe Bw Ngengele, alidai chama cha UDA kimeonyesha kuwa kinaweza kumaliza umaarufu wa Bw Kalonzo.

Msimamizi wa uchaguzi huo Bi Joyce Wamalwa, aliwahimiza wanasiasa wafanye kampeni za kuwavutia wapigakura wajitokeze kwa wingi siku za uchaguzi.

Kati ya wapigakura 623, 536 waliosajiliwa, ni 131, 940 pekee waliojiteza na kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Kwenye hotuba ya kukubali ushindi wake, Bi Kavindu aliwataka wafuasi wake waache kumchokoza mwenyekiti wa chama cha UDA, Bw Johnson Muthama, akisema ni mzazi mwenzake na yafaa aheshimiwe.

UDA yaelekeza macho yake 2022 baada ya London

ERIC MATARA na CHARLES WANYORO

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Bonde la Ufa sasa wanaamini kwamba chama cha UDA ndicho kitashinda kiti cha Urais 2022 baada ya kushinda uchaguzi mdogo wa wadi ya London.

Mwaniaji wa wadi ya UDA alizoa kura 1,707 na kumshinda mgombeaji wa chama cha Jubilee Francis Njotoge ambaye alipata kura 1,385.

Ushindi wa UDA sasa umeibua mashindano makali ya kisiasa kati ya chama hicho kipya na vyama vingine kama Kanu na Jubilee katika eneo la Kati nchi inapojiandaa kwa uchaguzi wa 2022.

“Naibu Rais na wandani wake walikuwa wakijaribu kuona iwapo chama hicho kimejizolea umaarufu wa kisiasa miezi michache baada ya kubuniwa. Hii ndiyo maana walidhamini mwaniaji na ushindi huo unawapa nguvu zaidi,” akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na wakili Steve Kabita.

Diwani wa wadi ya Kabazi Dkt Petet Mbae alisema ushindi wa UDA ni ishara tosha kwamba umaarufu wa Jubilee unaendelea kufifia na si kipenzi cha raia katika eneo la Bonde la Ufa.

“Ushindi huo umeonyesha kwamba UDA ni chama kitakachokuwa na umaarufu mkubwa hasa katika Bonde la Ufa kuelekea 2022,” akasema Dkt Mbae.

Lakini Katibu Mkuu wa Jubilee eneo hilo Peter Cheruiyot anasema bado Jubilee bado ni maarufu Nakuru na kote Rift Valley. Kwamba ushindi katika wadi moja haufai kuchukuliwa kuwa mizani ya kupima umaarufu wa chama hicho.

“Mwaniaji wa Jubilee alishinda kule Hell’s Gate na katika wadi ya London tulishindwa kwa kura chache mno ambazo ni karibu 200,” akatetea Bw Cheruyoit.

Hata hivyo, alikiri kwamba chama cha Jubilee kina kibarua cha kuweka mikakati ya kujiongezea umaarufu ili kisipitwe na UDA.

Uchaguzi mdogo katika wadi ya London ulionekana kuwa ubabe kati ya Rais Kenyatta na Naibu Rais ambaye alikuwa akimpigia upatu mwaniaji wa UDA. Siasa za BBI na 2022 zilitawala kampeni za uchaguzi huo mdogo.

Seneta wa Nakuru Susan Kihika aliwashukuru wapigakura wa wadi ya London kwa kuvumilia kuhangaishwa na vyombo vya usalama kisha kudhihirisha kuwa Naibu Rais ana ushawishi mkubwa eneo hilo.

Mbunge wa Kuresoi Kusini Joseph Tonui naye alisema kuwa UDA ndicho chama ambacho wakazi wengi wa Nakuru na Bonde la Ufa watakumbatia katika uchaguzi wa 2022.

Akizungumza katika eneobunge la Igembe ya Kati Kaunti ya Meru, Naibu Rais Dkt William Ruto alisema kuwa kuna mpango wa kuiba kura katika uchaguzi mkuu wa 2022 na serikali inapanga kuwatumia polisi kuwatatiza wagombeaji maarufu.

Dkt Ruto alisema Wakenya wana haki ya kujiunga na chama chochote cha kisiasa na wanafaa waruhusiwe kuwachagua viongozi wanaowapenda.

“Kuna watu ambao hawana manifesto na sasa wanapanga watumie nguvu na ghasia ili kuwalazimishia Wakenya viongozi. Polisi wetu hawafai waruhusu wanasiasa wawatumie,” akasema Dkt Ruto.

“Vijana pia hawafai kukubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa. Tunataka kila mwananchi aruhusiwe kumchagua kiongozi anayempenda. Siasa za chuki hazifai hapa nchini,” akaongeza.

Seneta wa Meru Mithika Linturi na wabunge John Paul Mwirigi (Igembe Kusini) Mugambi Rindikiri (Buuri) na Kirima Ngucine wa Imenti ya Kati nao waliwataka wakazi wa Meru wampigie Ruto kura 2022.

Naibu Rais alisema kuwa serikali yake itatoa Sh100 milioni kwa kila eneobunge nchini ili pesa hizo zitolewe kwa watu wa mapato ya chini ili kuwasaidia kuendeleza biashara zao.

Mwaniaji wa udiwani wa UDA akamatwa kwa kuhonga wapigakura

RUTH MBULA Na SAMMY WAWERUUDA

MAAFISA wa polisi katika Kaunti ya Kisii walimtia nguvuni mgombea wa kiti cha udiwani kwa tiketi ya chama cha UDA, mapema Alhamisi kufuatia uchaguzi mdogo unaofanyika wadi ya Kiamokama.

Bw Moses Nyandusi Nyakeremba alikamatwa kutokana na madai ya kuhonga wapiga kura, katika eneo la Moremani.

Mwanasiasa tajika Don Bosco Gichana, ambaye ni mfuasi wa UDA pamoja na wafuasi wengine pia walitiwa nguvuni.

Wapiga kura walianza kumiminika vituoni mwendo wa saa kumi na mbili za asubuhi, foleni ndefu zikishuhudiwa katika vingi vya vituo.

Afisa rejeshi wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) Kiamokama, Bw Mark Manco alisema wadi hiyo ina vituo 22 vya kupigia kura, na jumla ya wapiga kura 10, 853 wliosajiliwa.

Kwa muda wa wiki kadha zilizopita, kundi la Tangatanga, chini ya mrengo tawala wa Jubilee na vilevile chama cha ODM, wafuasi wamekuwa wakiendesha kampeni kutafutia wagombea wao kura.

Gavana wa Kisii Bw James Ongwae, Seneta Prof Sam Ongeri, mbunge Mwakilishi wa Wanawake kaunti hiyo, Bi Janet Ongera na mbunge wa Dagoreti Kaskazini, Simba Arati, wamekuwa wakifanyia kampeni mwaniaji wa ODM, Bw Malack Matara.

Nalo kundi la Tangatanga, likiongozwa na Niabu Gavana wa Kisii, Bw Joash Maangi, aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya utekelezaji Katiba Bw Charles Nyachae na kiongozi wa PDP Bw Omingo Magara walipigia debe mgombea wao, Bw Moses Nyakeramba.

Wabunge wengine wa Tangatanga ambao wamekuwa wakisaidia mwaniaji huyo kusaka kura ni pamoja na Mabw Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) na Alpha Miruka (Bomachoge Chache).

Kundi hilo linahusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

Tangatanga iliamua kuunga mkono Bw Nyakeramba baada ya kufanya mkutano na Dkt Ruto, nyumbani kwake eneo la Karen, Nairobi.

Hatua ya Naibu wa Rais kuunga mkono mgombea huyo wa kiti cha udiwani Kiamokama kwa tiketi ya UDA, inalenga kuvumisha umaarufu wake katika jamii ya Abagusii.

“Ni kweli tulikutana na Naibu wa Rais, tukaafikiana kuunga mkono Bw Nyandusi Nyakeramba kama mgombea wa Tangatanga. Hatua hiyo imeondoa shauku kati yetu, ni nani tutaunga mkono,” Bw Maangi akasema.

Awali, Bw Nyandusi, ambaye alikuwa akihudumu kama mkurugenzi mkuu wa kampuni ya majanichai, alikuwa katika njiapanda kufuatia kutoelewana kwa wandani wa Dkt Ruto Kisii ni nani wangeunga mkono.

Waliafikiana kumuunga mkono juma moja kabla ya uchaguzi huo mdogo, na baada ya kufanya kikao na Naibu Rais.

IEBC iliratibu uchaguzi huo kufanyika, Machi 4, 2021 na kuidhinisha wagombea 11.

Kiti cha udiwani Kiamokama kilisalia wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa diwani, Bw Kennedy Mainya, mnamo Novemba 2020.

Bw Daniel Ondabu na ambaye amewahi kuwa mtumishi wa umma ndiye mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya chama kipya cha PED.

“Tuna imani kushinda na kutwaa kiti hiki,” Katibu Mkuu wa PED, Bw Enock Ombuna akaambia Taifa Leo Dijitali.

Wawaniaji wengine ni pamoja na Bw Adams Nyamori Nyakundi (Maendeleo Chap Chap), Stephen Nyakeriga (TND), Dkt Charles Omwega (PEP), Dominic Ateng’a Nyangaresi (KNC), Peter Mwaboto (Narc-Kenya) na mwanaharakati Vincent Gekone kama mgombea wa kujitegemea.

Chama cha ODM kinatetea kuhifadhi kiti hicho kupitia mgombea wake, Malack Matara.

Kampeni za Matungu zaingia hatua ya lala-salama

Na SHABAN MAKOKHA

WAGOMBEAJI wa ubunge katika eneo la Matungu, Kaunti ya Kakamega, wako katika harakati za mwisho za kampeni zao, zinapobaki siku tano pekee kabla ya uchaguzi huo kufanyika.

Katika harakati za kuhakikisha wamefanikisha juhudi zao, wagombeaji hao wamekuwa wakifika katika kila pembe ya eneobunge hilo kuwarai wenyeji kuwapigia kura.

Vyama vya kisiasa vimewatuma wabunge wao kufanya mikutano ya kuwapigia debe wawaniaji wake, huku wagombeaji wakifanya kampeni za nyumba hadi nyumba.

Seneta Cleophas Malala wa Kakamega na mbunge Titus Khamala (Lurambi) wanaongoza kampeni za mwaniaji wa chama cha ANC, Bw Peter Nabulindo, anayetajwa kuwa miongoni mwa washindani wakuu.

Kampeni za Bw Nabulindo zimepigwa jeki na uwepo wa kiongozi wa chama hicho, Bw Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya).

Mwanzoni mwa mwezi huu, Bw Nabulindo aliwaambia washindani wake “kujitayarisha kwa kivumbi”.

Wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Mwambu Mabonga (Bumula), John Waluke (Sirisia), Didmus Barasa (Kimilili), Fred Kapondi (Mt Elgon) na Malulu Injendi (Malava) wameungana na aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, mbunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa, kumpigia debe Bw Alex Lanya, anayewania kwa chama cha UDA.

Hapo Alhamisi, msafara wa UDA ulifanya mikutano katika kijiji cha Sayangwe wadi ya Koyonzo, eneo la Ebubambula katika wadi ya Mayoni na eneo la Makunda katika wadi ya Kholera. Wabunge hao waliwaomba wenyeji kumchagua Bw Lanya, Machi 4.

Msafara wa ANC ulikuwa katika kijiji cha Shibanze (wadi ya Kholera), eneo la Itete katika wadi ya Koyonzo na eneo la Ngaire.

Chama cha ODM kimeanza mkakati mpya, kwa kukutana na makundi mbalimbali katika eneo hilo. Mgombeaji wake ni David Were.

Ghasia katika kampeni za UDA

JOSEPH OPENDA na FRANCIS MUREITHI

KAMPENI za chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika wadi ya London, mjini Nakuru, jana ziligeuka uwanja wa fujo baada ya polisi kurusha vitoa machozi kwa msafara ulioongozwa na Seneta Susan Kihika.

Msafara huo ulikuwa ukimpigia debe Bw Anthony Nzuki, anayewania udiwani katika wadi hiyo kwa tiketi ya UDA.Kufuatia patashika hiyo, barabara ya Kenyatta Avenue iligeuzwa kuwa jukwaa la makabiliano, baada ya polisi waliojihami vikali kuzuia magari kwenye msafara huo kuingia katikati mwa mji huo.

Wenyeji walijipata pabaya baada ya magari ya polisi kufika kwa kasi kwenye barabara hiyo yakiwa tayari kukabili hali yoyote ambayo ingetokea. Hata hivyo, msafara haukusimama kwenye barabara hiyo, hasa baada ya kurushiwa gesi awali kwenye wadi hiyo.

Polisi walichukua udhibiti wa Barabara ya Gusii, huku wengine wakielekea katika Barabara ya Oginga Odinga kuwazuia wanasiasa waliokuwa msafarani dhidi ya kuingia eneo la kati mwa jiji.Masaibu ya wanasiasa na wafuasi wao yalianza wakati walikutana katika mtaa wa Milimani na kujaribu tena kuingia katikati mwa mji.

Majibizano yalizuka kati ya polisi na viongozi hao, ndipo wakalazimika kuwarushia vitoa machozi ili kuutawanya umati ulioandamana nao.Wengine waliokuwa kwenye msafara huo ni Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Nakuru Magharibi, Samson Gathuku, alisema polisi hawakuwa wamefahamishwa kuhusu mkutano huo.

“Hatukupata habari yoyote kuhusu mkutano uliopangwa. Bado tunatekeleza masharti ya serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona,” akasema.Baada ya kutawanywa, wanasiasa hao walilazimika kuandaa mkutano wao kwenye makazi ya kibinafsi.Bi Kihika aliwalaumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuvuruga mkutano wao.

Pigo kwa chama cha UDA Machakos baada ya wandani kutoroka

NA PIUS MAUNDU

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA), kimepata pigo katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos baada ya kutorokwa na wanasiasa wanne waliotegemewa katika kampeni.

Aliyekuwa Naibu Gavana, Bernard Kiala na wanasiasa wengine watatu wamebadilisha msimamo wao wa kumuunga mkono mwaniaji wa UDA, Bw Urbanus Muthama Ngengele katika uchaguzi huo wa Machi 18.

Bw Kiala na watatu hao ambao ni diwani wa zamani wa Matungulu Magharibi, Bi Magdalene Ndawa na wanasiasa Stephen Muthuka na Rita Ndung ni kati ya wawaniaji 13 ambao walikosa nafasi ya kutwaa tiketi ya chama hicho kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, baada ya Bw Ngengele kukumbatiwa bila mchujo wowote kuandaliwa.Walisema hakuwa na imani na kura ya maoni iliyotumika kumpokeza Bw Ngengele tiketi ya chama moja kwa moja.

‘Natangaza kujiondoa katika kampeni za Urbanus Muthama Ngengele kuhusiana na uchaguzi mdogo wa useneta. Mimi bado ni mwanachama wa UDA na ninaunga mkono sera ya kuwainua Wakenya wa mapato madogo kiuchumi,’ akasema Bw Kiala kupitia taarifa.

Jana, Bw Kiala alihudhuria mkutano wa chama cha Wiper hali inayoashiria kuwa atamuunga mkono mgombeaji wa chama hicho Agnes Kavindu Muthama.

‘Nashauriana na wafuasi wangu ili kutathmini mwaniaji ambaye tutampigia kura mnamo Machi 18,’ akaongeza.

Kiti hicho kilisalia wazi baada ya mauti ya Boniface Kabaka mnamo Disemba mwaka jana.Wawaniaji wengine wanaomezea mate useneta huo ni John Mutua Katuku (Maendeleo Chap Chap Party), Dkt John Musingi (Muungano Party), Stanley Masai Muindi (Party of Economic Democracy), Edward Musembi Otto (Ford Asili) na Simeon Kioko Kitheka (Grand Dream Development Party).Wengine ni Sebastian Nzau, Jonathan Maweu na Francis Musembi ambao ni wawaniaji huru.

Ruto apangia UDA mikakati ya chaguzi ndogo

Na ERICK MATARA

NAIBU Rais William Ruto ameanza mikakati ya kuhakikisha chama chake kipya cha United Democratic Alliance (UDA) kimeshinda viti vya udiwani katika chaguzi ndogo zijazo.

Tayari Dkt Ruto amekutana na Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika kuweka mikakati ya UDA kutwaa ushindi katika chaguzi ndogo za wadi za Hell’s Gate na London, Kaunti ya Nakuru.

Viti hivyo, vilisalia wazi kufuatia vifo vya diwani wa London, Samuel Mbugua na mwenzake wa Hell’s Gate, John Njenga mnano Novemba mwaka uliopita.

Chaguzi hizo ndogo zitafanyika Machi 4.

Huku wandani wa Dkt Ruto wakiwapigia kampeni kali wawaniaji wa UDA, Gavana Lee Kinyanjui na Mbunge wa Nakuru Magharibi,Samuel Arama wamekuwa wakivumisha wawaniaji wa Jubilee.

Jubilee imekuwa ikidhibiti siasa za Nakuru tangu 2013, lakini sasa huenda ikapoteza umaarufu kwa kuwa wabunge wengi wa eneo hilo pamoja na Bi Kihika wamehamia mrengo wa Dkt Ruto.

Ruto azidisha uasi dhidi ya bosi wake

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ameendeleza uasi dhidi bosi wake, Rais Uhuru Kenyatta kwa kuidhinisha wagombeaji katika chaguzi ndogo zitakazofanyika katika maeneo mbalimbali mwezi Machi mwaka huu.

Jana, Dkt Ruto aliongoza uzinduzi wa mfanyabiashara Urbanus Mutunga Muthama kuwa mgombeaji wa useneta wa Machakos kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Machi 18.

Kando na Machakos, Dkt Ruto pia amewadhamini Mbw Evans Kakai na Alex Lanya ambao watapeperusha bendera ya UDA katika chaguzi ndogo za maeneo bunge ya Kabuchai na Matungu, mtawalia.

Chaguzi hizo ndogo zitafanyika Machi 4. Shughuli hiyo ambayo ilihudhuriwa na wandani wake kutoka Machakos, wakingozwa na mwenyekiti wa UDA Johnstone Muthama, ilifanyika katika makazi rasmi ya Dkt Ruto mtaani Karen, Nairobi.

Hii ni licha ya chama cha Jubilee kutangaza kwamba kitaunga mkono wagombeaji wa vyama washirika wake katika handisheki katika chaguzi ndogo za Machakos na maeneo bunge ya Matungu na Kabuchai.

Lakini jana, siku moja tu baada ya Jubilee kutoa tangazo hilo, Dkt Ruto alimwidhinisha Bw Muthama, maarufu kama Ngengele ambaye anatarajiwa kushindana na mgombeaji wa Wiper, Bi Agnes Kavindu Muthama, Waziri wa zamani Mutua Katuku wa Maendeleo Chap Chap miongoni mwa wengine.

Bi Kavindu, ambaye alikuwa mwanachama wa Jopo la Maridhiano (BBI) anapigiwa upatu na Rais Kenyatta, ikizingatiwa aliwania kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Machakos katika uchaguzi mkuu wa 2017 kwa tiketi ya Jubilee.

Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka alisema Bw Muthama ndiye aliibuka bora miongoni mwa wagombeaji 10 waliosaka tiketi ya UDA kulingana na kura ya maoni iliyoendesha na chama hicho ambacho alama yake ni wilbaro.

Katika siku za majuzi, Dkt Ruto amejitokeza kimasomaso kukaidi Rais Kenyatta. Mwishoni mwa wiki alimrukia bosi wake kwa kupendekeza rais atakayechaguliwa 2022 hapaswi kutoka jamii za Agikuyu ama Kalenjin.

kwa misingi kuwa ndizo pekee zimekuwa uongozini tangu Kenya ilipopata uhuru mnamo 1963.

UDA chajiuza kama chama kisichobagua Mkenya yeyote

Na LEONARD ONYANGO

WANDANI wa Naibu wa Rais William Ruto wametangaza kuwa wameanza harakati za kutumia chama cha United Democratic Alliance (UDA) kubomoa Jubilee.

Wakiongozwa na aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen na aliyekuwa naibu Kiranja wa Wengi katika Seneti Susan Kihika, viongozi hao Ijumaa wamewataka wafuasi wa Jubilee kuhamia chama cha UDA ambacho wamedai kuwa hakina ubaguzi.

Wamesema walilazimika kuhamia katika chama cha UDA baada ya kutengwa na kupigwa marufuku kuenda katika makao makuu ya chama cha Jubilee.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza wakati wa kutoa vyeti kwa wawaniaji wa kiti cha ugavana wa Kaunti ya Nairobi, ubunge katika maeneobunge ya Kabuchai na Matungu; na Wadi za Kiamokama (Kisii), London (Nakuru) na Hells Gate (Nakuru).

Askofu Margaret Wanjiru amekabidhiwa tiketi ya chama cha UDA kuwania ugavana katika Kaunti ya Nairobi katika uchaguzi mdogo uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 18, 2021.

Uchaguzi huo mdogo ulisitishwa kwa muda baada ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuenda kortini kupinga kutimuliwa kwake na Seneti hadi pale kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Lakini Ijumaa, viongozi wa ‘Tangatanga’ wamedai kuwa kesi ya Bw Sonko ni njama ya serikali ya Jubilee kuchelewesha uchaguzi mdogo wa Nairobi ‘baada ya kuhofia kuwa watabwagwa na mwaniaji wa UDA’.

Askofu Wanjiru sasa atamenyana na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru anayepigiwa upatu kupeperusha bendera ya Jubilee.

Chama hicho pia kimekabidhi tiketi Bw Evans Kakai Masinde na Bw Alex Lanya kuwania ubunge katika maeneobunge ya Kabuchai na Matungu mtawalia.

Maeneobunge hayo yalisalia wazi baada ya vifo vya Justus Murunga (Matungu) na James Lusweti (Kabuchai).

Hatua ya UDA kusimamisha wawaniaji wake inamaanisha kuwa Dkt Ruto atakuwa anaendesha kampeni dhidi ya wawaniaji wa Jubilee na huenda akamenyana na Rais Uhuru Kenyatta katika kampeni haswa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi.

Hatua hiyo pia ina maana kwamba Naibu wa Rais Ruto amepuuzilia mbali ombi la viongozi wa chama cha Amani National Congress chake Musalia Mudavadi na Ford Kenya kinachoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula ambao walimtaka asisimamishe wawaniaji katika chaguzi ndogo za Matungu na Kabuchai.

Wakizungumza Alhamisi katika ibada ya kumuaga Mama Hannah Mudavadi, mama ya kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi jijini Nairobi, viongozi wa ANC na Ford Kenya walimsihi kiongozi wa ODM Raila Odinga na Dkt Ruto wasisimamishe wawaniaji wao katika chaguzi hizo ndogo.

Chama hicho cha Wilibaro pia kilitoa tikiti kwa wawaniaji wa udiwani Antony Wachira (London), Jonathan Warothe (Hells Gate) na Moses Nyakeramba (Kiamakoma).

“Wawaniaji wetu wote watakuwa wanatumia chama cha UDA kuanzia sasa. Sisi hatuogopi kujihusisha na UDA kwa sababu hata wao (viongozi wa Jubilee) wamekuwa wakijihusisha na shughuli za chama cha ODM bila kuadhibiwa. Kadhalika, chama cha Party for Development Reform (PDR) kilichobadilisha jina lake kuwa UDA kilikuwa mshirika wa Jubilee na hivyo basi hatujakiuka sheria,” akasema Bw Murkomen.

Wanasiasa sasa wako huru kutumia chama hicho cha ‘Wilibaro’ kuwania viti katika chaguzi mbalimbali baada ya watu kukosa kuwasilisha pingamizi dhidi ya chama hicho kinachohusishwa na Naibu wa Rais William Ruto.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Ann Nderitu, mapema wiki hii alisema hakuna mtu aliyejitokeza kupinga hatua ya chama cha Party for Development Reform (PDR) kubadili jina lake kuwa United Democratic Alliance (UDA).

Bi Nderitu pia alisema kuwa afisi yake haijapokea pingamizi za kutaka kuzuia chama cha UDA kutumia nembo ya ‘Wilibaro’ au kaulimbiu yake ya ‘Kazi ni Kazi’.

UDA inayoongozwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama, ni kati ya vyama sita ambavyo Naibu wa Rais Ruto analenga kutumia kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Vyama vingine ambavyo Dkt Ruto analenga kutumia ni The Service Party (TSP) cha aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, New Democrats kinachohusishwa na aliyekuwa mbunge David Kiprono Sudi na People’s Empowerment Party (PEP) kinachohusishwa na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Vingine ni The United Green Party (UGP) na Grand Dream Development Party (GDDP).