Waganda washerehekea kurejeshwa kwa intaneti

MASHIRIKA na CHARLES WASONGA 

RAIA wa Uganda wamesherehekea kurejeshwa kwa huduma za mawasiliano ya intaneti ambazo zilizimwa siku chake kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 14, 2021.

Hata hivyo, mitandao mbalimbali ya kijamii ilisalia kufungwa na ingefikia tu kupitia mtandao wa siri (VPN).

Rais Yoweri Museveni ambaye aliibuka mshindwa na hivyo kupata nafasi ya kuendelea kuongoza Uganda kwa muhula wa sita, aliishutumu mitandao hiyo kwa kupendelea upande wa upinzani na “kutumiwa vibaya kuendeleza ajenda za wageni.”

Hata hivyo, Robert Kyangulanyi, almaarufu Bobi Wine, ambaye alikuwa wa pili katika matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, alidai kuwa serikali ya Museveni ilizima mawasiliano na intaneti na mitandao ya kijamii ili ifanikishe nia yake ya kuiba kura.

Naye Katiba Mkuu wa chama cha National Unity Platform (NUP) kilichodhamini Bw Wine, Joel Ssenyonyi alimshutumu Museveni kwa kuzima huduma za intaneti ili kuwazuia kuwasilisha ushahidi kuhudu udanganyifu katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, aliwaambia wanahabari kuwa chama hicho kinaendelea kukusanya fomu za matokeo ya uchaguzi wa urais, zilizo na ushahidi wa udanganyifu.

Tume ya uchaguzi ilimtangaza Museveni mshindi kwa kuzoa asilimia 58.64 ya kura zilizopigwa huku Wine ambaye alikuwa mpinzani wake wa karibu akipata asilimia 34 ya kura.

Ushindi huo sasa unaashiria kuwa Museveni mwenye umri wa miaka 76 ataongoza Uganda kwa miongo minne (miaka 40) ikizingatiwa kuwa aliingia mamlakani mnamo 1986.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu imeshutumu vikali serikali ya Museveni kwa kuzima mifumo ya mawasiliano.

Wakati huo huo, maafisa wa usalama wanaendelea kuzingira boma la Bobi Wine viungani mwa jiji la Kampala huku mwanasiasa huyo akilalamika kuwa familia yake inakeketwa na njaa kwa kukosa chakula.

Amerika sasa yataka jopo libuniwe kuchunguza matokeo ya uchaguzi wa Uganda

IRENE ABALO OTTO na ANDREW BAGALA

AMERIKA sasa inataka tume huru ya uchaguzi nchini Uganda kukagua matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika wiki iliyopita, huku ikisema kuwa imepokea ripoti kuhusu kuwepo kwa visa vya udanganyifu na vurugu.

Tume ya Uchaguzi (EC) Jumamosi ilimtangaza Rais Yoweri Kaguta Museveni, 76, wa chama cha National Resistance Movement (NRM) kuwa mshindi wa uchaguzi huo baada ya kupata asilimia 58.6 ya kura zilizopigwa.Rais Museveni ambaye amekuwa mamlakani tangu 1986 sasa ataongoza nchi hiyo kwa muhula wa sita.

Shughuli ya kupiga na kuhesabu kura ilifanyika ‘gizani’ baada ya serikali kuzima intaneti na kuzuia kutuma au kupokea fedha kwa njia ya simu.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa wikendi, msemaji wa wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, Morgan Ortagus, alisema kuwa: “Tumeshtushwa mno na ripoti za kuaminika kwamba maafisa wa usalama walisababisha vurugu kabla ya uchaguzi na kulikuwa na visa vya udanganyifu siku ya kupiga kura.”

“Tunahimiza serikali kubuni jopokazi huru ambalo litachunguza ripoti hizo na waliohusika na vurugu hizo wachukuliwe hatua,” akasema Ortagus.

Amerika ilishutumu serikali ya Uganda kwa kuhangaisha wawaniaji wa urais wa upinzani na kugandamiza wanaharakati na mashirika ya kijamii.

“Serikali ya Uganda inastahili kuheshimu haki za kibinadamu za wawaniaji wa urais, ikiwemo haki ya kujieleza,” akasema Ortagus.

Siku ya kupiga kura, maafisa wa usalama wa Uganda walivamia kituo cha kujumlisha matokeo kilichowekwa na mashirika ya kijamii katika Hoteli ya Africana jijini Kampala.

Polisi walikamata maafisa 35 wa mashirika ya kijamii kwa madai ya kuendesha kituo sambamba cha kujumlisha matokeo bila kibali.

Wiki mbili kabla ya uchaguzi mkuu, serikali ilifunga akaunti za benki za baadhi ya mashirika ya kijamii, zikiwemo akaunti za Muungano wa Mashirika ya Kijamii nchini Uganda.Serikali ilidai kuwa mashirika hayo yalikuwa yakifadhili shughuli za ugaidi nchini humo.

Amerika ambayo hutoa msaada wa dola bilioni 1 (Sh100 bilioni) kwa Uganda kila mwaka, ililitaka taifa hilo la Afrika Mashariki kuheshimu demokrasia.

Wawaniaji wa urais walionyanyaswa na maafisa wa usalama ni Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine wa chama cha National Unity Platform (NUP) na Patrick Oboi Amuriat wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) ambao waliibuka katika nafasi ya pili na tatu mtawalia, kulingana na matokeo ya EC yaliyotolewa Jumamosi.

Bobi Wine amekuwa akizuiliwa na maafisa wa usalama nyumbani kwake tangu Alhamisi wiki iliyopita. Wakati huo huo, vijana 60 walikamatwa mjini Nsangi wilaya ya Wakiso, baada ya kuandamana kufuatia habari feki kwamba mbunge wa Mityana Municipality Francis Zaake wa chama cha NUP aliuawa kwa kupigwa risasi.Kulingana na polisi, vijana hao walishambulia basi kwa kutumia mabomu ya petroli.

Facebook yazima ujumbe wa Uhuru kwa Museveni

Na MWANDISHI WETU

MTANDAO wa Facebook jana uliweka onyo kwenye ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta ukidai kwamba ulikuwa wa kupotosha.

Baada ya onyo hilo, Ikulu ya Nairobi ililazimika kufuta ujumbe huo ambao Rais Kenyatta alikuwa amempongeza mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni kwa kushinda uchaguzi wa urais.

Kwenye ujumbe huo, Rais Kenyatta alieleza, kupitia ukurasa rasmi wa Ikulu katika Facebook, kwamba ‘ushindi wa Museveni ulidhihirisha kwamba raia wa Uganda wana imani na uongozi wake’.Ikitoa onyo kuhusu ujumbe huo, Facebook ilidai kwamba ulichunguzwa na kubainika ulikuwa feki.

“Ujumbe huo ulichunguzwa kwingine na wachunguzi huru na ikabainika ni feki,” lilisema onyo la Facebook.

Hatua hiyo ilijiri baada ya mpinzani mkuu wa Museveni, Robert Kyagulanyi anayefahamika kwa jina maarufu la kisanii kama Bobi Wine, ambaye aliibuka wa pili, kudai kwamba uchaguzi ulikumbwa na udaganyifu.

Bw Museveni ametawala Uganda kwa miaka 35 na ataongoza kwa kipindi cha miaka mingine mitano kufuatia ushindi wake kwenye uchaguzi wa Januari 14.Wine, ameahidi kwamba atathibitisha madai yake hivi karibuni.

Tume ya uchaguzi nchini Uganda ilitangaza kuwa Museveni alishinda kwa kura milioni 5.8 huku Wine akifuata kwa kura milioni 3.48.

Onyo la Facebook ni pigo maradufu kwa Rais Kenyatta ambaye alifunga na kufuta anwani zake za kibinafsi za mitandao ya kijamii miaka miwili iliyipota.

Baada ya kuzifuta alidai kwamba alifanya hivyo kwa kuwa watu wanatumia mitandao ya kijamii kueneza udaku na kumtusi.

UGANDA: Demokrasia Afrika bado ni ndoto

NA WACHIRA ELISHAPAN 

Bara la Afrika kwa Mara nyingine limejipata katika hali tata,baada ya rais wa jamhuri ya Uganda Yoweri Museveni kujipata kama mshindi wa uchaguzi wa urais  ulioandaliwa nchini humo.

Museveni alitabiriwa kuwa mshindi hapo awali hata kabla ya shughuli nzima za kuhesabu kura kukamilika. Ushindi wa Museveni hata hivyo ni kero kwa demokrasia ambayo inadhamini haki ya kila mwananchi hata akiwa mchanga,bila kumbagua kwa misingi ya rangi,Vcheo au hata tabaka.

Mgombeaji urais ambaye alionekana kuwa karibu sana na utepe wa kushinda almaarufu Bobi Wine kwa kweli hajakuwa akiishi kwa amani tangu atangaze azma yake ya kuwania urais, na badala yake amekuwa akijifuta machozi ya kukabiliana na polisi ambao waliaminika kutumwa na rais Museveni.

Mapema kabla ya kura kumalizika kuhesabiwa,Mwanaharakati huyo maarufu Bobi Wine alisikika akilalamika maafisa wa jeshi la Uganda walimzingira nyumbani kwake,wakidai kwamba walikuwa wanamlinda yeye.

Katika karne ya ishirini na moja,kuna uwezekano mkubwa Wananchi wanajua haki zao za kimsingi na hapo hawana uwezo mkubwa kuzitwaa,basi wanafanya kinyume na matarajio ya viongozi hao wanaowanyima haki zao.

Afrika huru inahitajika iwapo viongozi wanataka maendeleo na mataifa yaliyostawi. Hayati Rais mstaafu Daniel Moi alifanya kitendo ambacho daima kitakumbukwa na vizazi vingi cha kukubali kustaafu Mara tu alipoongoza taifa hili kwa miaka ishirini na minne,jambo ambalo liliashiria kwamba demokrasia ilikuwa imekwisha kukomaa nchini.

Inasikitisha zaidi kuwaona viongozi wenye Sera za kikoloni bado wakishikilia hatamu za uongozi katika karne hii. Tangu Kenya ilipojipatia katiba mpya mwaka wa 2010,iliashiria mwisho wa uongozi usio wa demokrasia,na hapo ikaashiria mwanzo wa uongozi wa mwananchi.

Tayari matunda ya ugatuzi kama vile usawa wa kijinsia,uongozi wa mihula miwili pamoja na ugavi sawa wa rasilimali za umma kwa hakika yameanza kutundwa.

Hivi majuzi Rais Kenyatta alikiri kwamba uongozi wa Kenya umekuwa ukishikiliwa na jamii mbili,akipendekeza kusema kwamba ni wakati wa jamii nyingine kuongoza taifa hili.

Semi za rais Kenyatta zinaashiria kwamba demokrasia imefika kiwango cha kushabikiwa na kukwezwa hadhi na mataifa yote bila kubagua. Bali na kubadili mfumo wa uongozi,kuna haja kubadili fikra kutoka kwa ukale usio na faida,hadi kwa usasa utakaofaidi watu wote.

Hivyo,umefika wakati mataifa yote ya kiafrika kuamka na kukana viongozi wanaojigandamiza kwenye nyadhifa za uongozi na kuwapa mamlaka wengine wenye maono tofauti.

EU yasifu uchaguzi wa Uganda

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ubalozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Uganda, balozi Atillio Pacifici, ameelezea kufurahishwa na jinsi uchaguzi mkuu nchini humo ulivyopangwa vizuri na kuandeshwa katika mazingira ya amani.

“Tuliona uchaguzi ambao ulipangwa vizuri na watu wakiwa watulivu wakisubiri kupiga kura zao na shughuli hiyo ikaendelea kwa amani. Tumefurahi. Maafisa wa Uchaguzi walioajiriwa na Tume ya Uchaguzi walifanyakazi yao kwa utaalamu mkubwa,” akasema balozi Pacific.

Kiongozi huyo wa ujumbe wa EU alitoa kauli hiyo Ijumaa alipokuw akizungumza na wanahabari katika uwanja wa Kololo Ceremonial Grounds. Ni hapo ambapo kulikuwa kituo cha tume ya uchaguzi ya Uganda cha kujumuisha matokea ya kura za ubunge kutoka kwa tarafa nne za Kampala.

“Inafurahisha kwamba vijana wengi, raia wa Uganda walielimika vizuri, ambao wanahudumu katika uchaguzi huu,” aliongeza wakati alipofanya ziara ya ghafla katika kituo hicho.

Mwaka huu EU haikutuma waangalizi wa uchaguzi, kama ilivyo kawaida yake. Hii ni kwa sababu serikali ya Uganda haijatekeleza mapendekezo yaliyotolewa na waangalizi wa EU katika chaguzi zilizopita.

Badala yake mwaka huu, EU ilituma kundi la wahudumu wa kidiplomasia kutoka afisi za kibalozi za mataifa kadha wanachama wa muungano, zilizoko Kampala.

Wajibu wa wanadiplomasia hao ulikuwa “kuona vila mambo yanavyoendelea katika uchaguzi huo.”

Tofauti na waangalizi wa uchaguzi ambao ni wataalamu, wanachama wa kundi hilo la wanadiplomasia hawatatoa ripoti rasmi na mapendekezo hasusi.

Miongoni mwa maeneo ambako kundi hilo la wanadiplomasia walizuru ni Mbale, Moroto, Arua, Lira na Rukungiri.

Isipokuwa visa vichache kwa makabiliano katika ya makundi hasimu ya wanasiasa na watu kadhaa kukamatwa wakiwemo waangalizi wa makundi ya kijamii, polisi na tume ya uchaguzi walisema kuwa uchaguzi huo wa Alhamisi uliendeshwa katika mazingira ya amani.

Wakati huo huo mnamo Jumamosi saa kumi kamili alasiri, tume ya uchaguzi ilimtangaza Rais Yoweri Kaguta Museveni mshindi kwa kupata jumla ya kura 5,851,037, sawa na asilimia 58.6 ya kura zilizopigwa.

Naye mpinzani wake wa karibu Robert Kyangulanyi, almaarufu Bobi Wine, alipata kura 3, 475, 298, sawa na asilimia 34.8 ya kura zilizopigwa.

Museveni aliyedhaminiwa na chama cha National Resistance Movement (NRM) amekuwa mamlaka kwa miaka 35, tangu 1986 alipoingia afisi kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Hata hivyo, Bobi Wine alipinga matokeo hayo kwa misingi ya kile alichodai ni wizi wa kura na hatua ya serikali kutumia wanajeshi na polisi kunyanyasa wafuasi wake.

Mshindi wa urais Uganda kujulikana kesho

NA DAILY MONITOR

TUME Huru ya Uchaguzi nchini Uganda inatarajiwa kumtangaza mshindi wa kiti cha Urais hapo Jumamosi baada ya kuandaa uchaguzi wake mkuu Alhamisi.

Sheria ya tume hiyo inasisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi lazima yatangazwe saa 28 baada ya upigaji kura kumalizika. Shughuli za uhesabu wa kura bado zinaendelea kote nchini na matokeo ya awali yanaanza kupokelewa leo kutoka vituo mbalimbali vya kupiga kura.

Zaidi ya wapigakura milioni 18 walimiminika katika vituo mbalimbali kumchagua Rais mpya huku ushindani mkali ukitarajiwa kuwa kati ya Rais Yoweri Museveni na Mwanasiasa mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Huduma za mitandao nazo zilisalia kuzimwa kwa siku ya pili mfululizo hatua iliyochukuliwa na serikali ili kuzuia raia kueneza habari ambazo zingezua taharuki na ghasia.

Pia kulikuwa na visa vya mashine za kielektroniki za kuwatambua wapigakura kufeli kufanya kazi katika Wilaya ya Wakiso na pia masanduku ya kupiga kura yalichelewa kufika katika baadhi ya maeneo ya mashinani na hata kwenye baadhi ya vituo jijini Kampala.

Katika kituo cha polisi Gayaza, shughuli za upigaji kura hazikuwa zimeanza kufikia saa tatu asubuhi baada ya mashine za kielektroniki za kuwatambua wapiga kura kukosa kufanya kazi.

“Nimetembelea vituo vingi vya kupiga kura na hakuna chochote kinachoendelea. Baadhi wameondoka kwa hasira huku wengine nao wakiwazomea maafisa wa uchaguzi,” akasema mmoja wa waangalizi Lydia Ainomugisha.

Katika Manispaa ya Kira, watu walisusia kupiga kura baada ya kugundua masunduku yaliyokuwa na karatasi za kupiga kura yalikuwa yamefunguliwa.

Vijana katika kituo cha Wandegeya, nao walikataa kuwapisha wazee na akina mama wajawazito kutangulia kupiga kura wakisema kuwa hata wao walikuwa na haraka ya kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.

“Tumekuwa tukiwaruhusu wazee hawa na akina mama kutangulia kila mwaka wa uchaguzi kisha wanawapigia kura viongozi wakongwe wasiotusaidia kitu. Leo hatutawahurumia wazee hao kwa sababu watakufa hivi karibuni na kutuacha hapa tukiteswa na viongozi hao ilhali wao ndio waliwachagua. Tumekuwa tukiwaheshimu lakini leo wapange laini au warejee nyumbani,” akasema kijana mmoja.

Hapo Alhamisi, usalama uliimarishwa katika vituo mbalimbali vya kupiga kura hasa jiji la Kampala ambalo kwa miaka mingi imekuwa ngome ya upinzani.

Baadhi ya maafisa wa polisi walionekana wakipanda kwenye paa ya majumba marefu wakiwa wamejihami vikali kupambana na utovu wowote wa usalama.

Katika mtaa wa mabanda wa Kamwokya ambako Bobi Wine alilelewa, foleni ndefu zilishuhudiwa huku nao polisi wakiwa ange kuhakikisha kuwa raia wanasimama umbali wa mita moja unusu kuzuia maambukizi ya corona.

“Niko hapa kupiga kura ili kubadilisha uongozi wa nchi. Mara nyingi utawala wa sasa umekuwa ukidai utabadilisha maisha yangu lakini hali bado ni ile ile,” akasema dereva Joseph Ndung’u aliyekuwa kati ya watu wa kwanza kupiga kura.

Mwaniaji huru Henry Tumukunde ambaye alipiga kura yake katika kituo cha Kisementi, jijini Kampala naye alisema hatukubali matokeo hata kabla ya kura kuhesabiwa akisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu.

“Angalia nimepiga kura lakini baada ya kutumia sanitaiza, mkono umekuwa safi na wino umefutika. Watu wanaweza kupiga kura hata zaidi ya mara moja hasa ikizingatiwa mashine nazo zinafeli. Sitakubali matokeo hayo,” akasema.Rais Yoweri Museveni, Wine na wawaniaji wote walipiga kura kwenye uchaguzi huo ambao ulishirikisha nyadhifa za ubunge na udiwani.

TAFSIRI NA CECIL ODONGO

Nitapinga matokeo uchaguzi ukikosa uwazi – Bobi Wine

NA DAILY MONITOR

MWANIAJI urais wa chama cha National Unity Platform (NUP) nchini Uganda Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine amsesma kuwa hatakubali matokeo ya uchaguzi wa Alhamisi iwapo chama chake kitasema uchaguzi haukuwa wa haki na huru.

“Chama changu kitakubali matokeo ikiwa uchaguzi utakuwa wa haki na kura zote kuhesabiwa kwa njia yenye uwazi,” akaambia NTV Uganda katika mahojiano ya kipekee. Isitoshe, alifichua kuwa NUP kina pahali pa huru pa kuhesabu kura dhidi ya uwezo wa kuibwa kwa kura.

“Tutakuwepo na pahali pa kuhesabu kura. Huu ni wakati wa dijitali. Sisi ni kama maji yanayotiririka: wakitusimamisha hapa, tunatokea kutoka upande tofauti,” akasema.

Mwanamuziki huyo amesema kuwa atakataa matokeo ya uchaguzi wa Alhamisi iwapo chama hicho kitaonyesha matokeo hayo kama yasiyo ya kawaida.

Robert Kyagulanyi, aliyekuwa maarufu kupitia uanamuziki wake, kisha akawa mwanasiasa alisema kuwa amejiamini kuwa amefanya ya kutosha licha ya matukio ya kuumiza wakati wa kampeni za uchaguzi.

“Nimekuwa nikiimba kwa miaka karibu 20. Naamini kuwa watu wamenijua toka wakati ambapo nilikuwa nikipitisha jumbe za mabadiliko kupitia mtindo wangu wa muziki wa ‘rab dhaba’,” akaongeza.

Bobi Wine ambaye alikuwa akizungumza kutoka nyumbani mwake, Magere amekuwa kigezo cha matukio ya kisiasa, alikuwa na ujumbe wa matumaini kwa wanaomuunga mkono.

“Wacha Waganda waamini kuwa chama cha NUP kinashinda na uhuru utarejeshwa katika Uganda mpya.” Alipinga mwenendo wa vikosi vya usalama vya nchi siku ya uchaguzi lakini akasema kuwa alikuwa na matumaini kuwa uchaguzi utawaweka huru mamia ya watu ambao wanamuunga mkono ambao walishikwa kiholela.

Bobi Wine amewaona marafiki wake wa dhati wakiuliwa ama kushikwa na chama cha upinzani cha National Resistance Movement kinachoongozwa na rais Yoweri Museveni. “Pahali ambapo watu kama Eddy Mutwe, Dan Magic na Nubian Li wamefungwa bila hatia, wanawakilisha milioni ya wananchi wa Uganda ambao wanahamu ya mabadiliko. Jambo ambalo litadhihirika uchaguzini na watauona uhuru tena,” akasema.

Msimamo wa Wine katika matokeo ya uchaguzi yanalingana sana na yale ya chama cha Alliance for National Transformation’s (ANT) ambacho kiongozi wake ni Genrali Gregory Mugisha Muntu ambaye amesema kuwa upinzani utawaunganisha na kuwakutanisha zaidi ya milioni 45 ya Waganda ili kukataa matokeo ya uchaguzi iwapo yataonyesha udhaifu wowote.

Mgombeaji wa kiti cha Urais kupitia chama cha Forum for Democratic Change, Patrick Oboi aliwiana na matamshi ya wenzake huku akisema kuwa, “Hatutaruhusu kitu chochote isipokuwa uchaguzi huru.”

Karibu wapiga kura milioni 18, ambao wengi ni vijana, watachagua rais wao kutoka wagombeaji wa kiti hicho 11, Januari 14 katika uchaguzi ambao watazamaji wamesema kuwa ni mashindano ya vizazi.

TAFSIRI: WANGU KANURI

Jeshi lamwagwa miji mikuu uchaguzi mkuu ukinukia

NA MASHIRIKA

JESHI la Uganda limeimarisha usalama jijini na nje ya Kampala kabla ya uchaguzi wa urais na bunge uliopangiwa kufanyika kesho. Wanajeshi wanashika doria barabarani huku wengine wakidhibiti hali katika mitaa inayofahamika kama maeneo hatari ya vurugu.

“Muda wa kampeni unaelekea kufika kikomo na sasa tunasonga katika hatua nyingine ya kupiga kura. Sasa tumeimarisha usalama wetu na kuwatuma maafisa wa polisi ambao wanasaidiwa na jeshi. Usalama ni muhumi kuhakikisha haki ya kila mtu kupiga kura na kudumisha imani katika uchaguzi salama na wazi,” Msemaji wa Polisi Jijini Kampala Patrick Onyango, alieleza vyombo vya habari nchini humo.

Aidha, kuna idadi kubwa ya polisi na jeshi wanaotumia magari kushinda ilivyowahi kushuhudiwa katika msimu wa uchaguzi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.’

“Kuna makundi ya maafisa wa usalama wanaopiga doria kwa miguu, pikipiki na magari. Tumefanya mazoezi kuhusu matukio kadhaa ikiwemo ghasia za kikatili, makundi ya vijana wenye itikadi kali, dhuluma za kimtandao, mapigano kati ya makundi hasimu na kadhalika. Timu hizo zitakabiliana na aina yoyote ya dharura,” alisema.

Wakuu wa mashirika ya kulinda usalama mnamo Ijumaa yalitoa onyo kwa wote wanaopanga kusababisha vurugu wakati na baada ya uchaguzi kwamba wataadhibiwa ipasavayo.

Adolf Mwesige, waziri wa ulinzi na masuala ya wanajeshi waliostaafu alisema, wagombeaji wa kisiasa ni sharti wakubali uamuzi wa watu utakaotangazwa na Tume ya Uchaguzi.

“Mchakato wa pekee tu unaoweza kutumia kupinga matokeo ni mahakama wala si vurugu. Hii si mara ya kwanza kwetu kushiriki uchaguzi,” alisema Mwesige.

Mashirika ya kigeni nchini humo tayari yametahadharisha raia wake kuwa waangalifu zaidi wakati na baada ya uchaguzi, yakionya dhidi ya uwezekano wa kuzuka kwa ghasia za uchaguzi.

“Polisi kwa kawaida huwa wanatumia nguvu kupita kiasi, ikiwemo vitoa machozi, risasi za mipira na risasi halisi kutawanya maandamano. Maandamano Uganda huenda yakasalia jambo la kawaida na kuna uwezekano wa michafuko kuzidi,” Ubalozi wa Amerika uliwatahadharisha Waamerika ukiwahimiza kuepuka maandamano na mikusanyiko ya watu.

Kipindi cha kampeni za urais kilichoanza mwanzoni mwa Novemba na kukamilika jana Januari 12, kimeandamwa na ghasia mbaya za kikatili ambazo baadhi zimesababisha vifo.

Kukamatwa kwa mgombea urais wa chama cha upinzani, Robert Kyagulanyi mnamo Novemba 18 kulizua maandamano katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu 54 waliouawa na maafisa wa usalama.

Rais aliye mamlakani kwa sasa, Yoweri Museveni alipokuwa akizungumza kuhusu maandamano hayo alijutia vifo hivyo akiahidi kuanzisha uchunguzi.

BOBI WINE

Walinzi na wafuasi wa Bobi Wine wakamatwa, siku mbili kabla ya uchaguzi

Na CHARLES WASONGA

MGOMBEAJI wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine Jumanne alifichua kuwa wanajeshi wa serikali walivamia nyumbani kwake na kuwatia mbaroni walinzi na wasaidizi wake siku mbili kabla ya wapiga kura kuelekea debeni kushiriki uchaguzi mkuu.

“Leo asubuhi wanajeshi walivamia nyumbani kwangu na kuwakamata walinzi na mtu yeyote waliyempata karibu,”  Wine, ambaye ndiye mpinzani mkuu Rais wa sasa Yoweri Museveni katika uchaguzi huo wa Januari 14, 2021, alisema kupitia akaunti yake ya twitter.

Mgombeaji huyo ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi alisema hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu sababu ya kukamatwa kwa wasaidizi wake.

Wandani hao wa Wine, 38, ambaye pia ni mwanamuziki mtajika, walikamatwa wakati ambapo mwanasiasa huyo alikuwa akihojiwa na mwanahabari wa Kenya Jeff Koinange katika kituo cha redio cha Hot 96 FM.

Makoa makuu ya polisi na jeshi nchini Uganda hayajatoa kauli zozote kuhusu kisa hicho

Jumla ya wapiga kura 18 milioni nchini Uganda ambao wamesajiliwa wanatarajiwa kushiriki uchaguzi huo wa urais na ubunge mnamo Alhamisi.

Wine ndiye anapigiwa upatu zaidi miongoni mwa wagombeaji urais 10 wanaompinga Rais Museveni ambaye amekuwa mamlakani tangu 1986.

Museveni mwenye umri wa mika 76 amelaumiwa kwa kutumia wadhifa wake kuwadhulumu wapinzani wake na vyombo vya habari.

Kiongozi huyo mkongwe amekuwa wakitumia vikosi vya usalama kuendeleza kampeni za kupambani na wapinzani wake tangu kampeni za kisiasa zilipoanza mwaka jana.

Tangu Novemba 2020 zaidi ya watu 60 wameuawa katika makabiliano kati ya wafuasi wa wagombeaji wa upinzani haswa wale wa Bw Wine. Vitendo hivyo vimelaaniwa ndani ya nje ya Uganda wagombeaji wa urais wa upinzani wakitaka serikali ya Museveni ichunguzwe kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Wiki jana, Wine aliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kumchukulia hatua Rais Museveni kuhusiana na vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Lakini Rais huyo ametetea maafisa wa usalama akisema wamekuwa wakikabiliana na wafuasi wa upinzani wanaokiuka masharti ya kuzuia msambao wa Covid-19 kwa kuandaa mikutano mikubwa ya kisiasa.

Bobi Wine mwenyewe amewahi kukamatwa mara kadhaa wakati wa kampeni na kufikishwa kortini kwa kile maafisa wanasema ni makosa ya kuvunja masharti ya janga la corona.

Mara si moja Museveni amekuwa akishutumu Wine kwa kumtaja kama “mtu anayetumiwa kuendeleza masilahi ya wageni.” Hata hivyo, hajawaji kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Amerika yamshutumu Rais Museveni kunyanyasa Wine

Na DAVID VOSH AJUNA

KAMPALA, UGANDA

UBALOZI wa Amerika nchini Uganda, umekashifu vikali kuendelea kuhangaishwa kwa mwaniaji wa Urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, kwenye kampeni zake za uchaguzi mkuu ujao.

Wine amekuwa akikabiliwa vikali na maafisa wa usalama kwenye msafara wake wa kampeni ambao hutibuliwa na kuishia yeye na wafuasi wake kukamatwa na kuzuiliwa na polisi.

Kisa cha hivi punde ni cha Jumatano ambapo Wine alikamatwa akiwa kampeni katika Kisiwa cha Kalangala. Polisi waliojihami walimnyaka na kumrejesha nyumbani kwake Magere katika Wilaya ya Wakiso ili asiendelee na kampeni zake.

Kukamatwa kwa Wine kulijiri siku 15 pekee kabla ya Uganda kuingia debeni Januari 15, 2021.

“Tukio la Jumatano ambapo polisi walitumiwa kumkamata mwaniaji huyo wa upinzani na wafuasi wake ni ishara kubwa kwamba Uganda haina demokrasia. Inashangaza kwamba kampeni za Rais Museveni hazivurugwi ilhali upinzani unakandamizwa kutokana na amri ya serikali,” ikasema taarifa ya ubalozi huo kupitia ukumbi wa Twitter.

Kando na Wine, polisi wa Uganda pia wamekuwa wakiwahangaisha wanahabari, kuwakamata baadhi yao na kuharibu vifaa vyao vya kazi kwa kupasha umma kuhusu kampeni za Wine.

Kufikia Jumatano usiku, msemaji wa NUP, chama anachotumia Wine kuwania uchaguzi huo alidai kuwa baadhi ya wanachama waliokamatwa na kiongozi huyo bado walikuwa wakizuiliwa na polisi.

“Wanachama wetu ambao walikuwa na mheshimiwa Kyagulanyi eneo la Kalangala walitiwa pingu kisha kurundikwa pamoja kwenye malori ya jeshi. Mmoja wao Eddie Mutwe anashuku kuwa wanapelekwa katika kituo cha polisi cha Masaka Central,” akasema msemaji huyo Joel Ssenyonyi.

“Mheshimiwa Kyagulanyi yupo nyumbani kwake Magere lakini boma limezingirwa na wanajeshi wala hawezi kutoka,” akaongeza Ssenyonyi.

Wine naye jana alidai kuwa wanachama 90 wa NUP walionyakwa Jumatano wanaendelea kuzuiliwa na polisi.

Uhusiano kati ya wanahabari na upinzani kwa upande moja na maafisa wa usalama upande mwingine umekuwa mbaya wakati huu wa kampeni.

Serikali nayo imekuwa ikimlaumu Wine kwa kuandaa misururu ya kampeni inayohudhuriwa na halaiki ya watu hali inayokiuka masharti yaliyowekwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Upinzani hata hivyo, unadai kuwa masharti hayo yanatekelezwa kibaguzi kwa kuwa Rais Museveni mara nyingi amekuwa akihutubia umma bila kuzifuata kanuni hizo.

“Haya masharti ya kuzuia corona yanatumiwa tu na Rais Museveni kuvuruga kampeni za upinzani. Ni masikitiko makubwa polisi wanatumiwa kuhangaisha upinzani na chama tawala kupendelewa,” akasema Msemaji wa FDC Ibrahim Ssemujju katika kikao na wanahabari.

Binti akasirisha baba kwa kuamua kumpinga kisiasa

Na DAILY MONITOR

HUKU joto la uchaguzi likiendelea kupanda nchini Uganda, mwanasiasa mmoja amemuasi bintiye aliyetangaza azma ya kumpinga katika kinyang’anyiro cha wadhifa wa uenyekiti wa Baraza la Mji wa Kasaali.

Bw Godfrey Kimera ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Mji wa Kasaali, wilayani Kyotera, alitaja uamuzi wa bintiye, Reginah Nakiweewa, kuwania kiti hicho kama kitendo cha utovu wa heshima kwake.

Alisema bintiye angewania kiti kingine katika uchaguzi huo, wa mwaka ujao, badala ya kiti hicho anachokishikilia wakati huu.

“Nimemshauri (Nakiweewa) mara kadha ajiondoe katika kinyang’anyiro cha kiti cha uenyekiti wa baraza la mji lakini amekataa. Siwezi nikamvumilia binti kama huyo ambaye hana heshima kwa wazee. Atafute baba mwingine,” Bw Kimera akasema kwa hasira.

Lakini Bi Nakiweewa anasema babake, ambaye ni mwanachama wa chama cha Democratic Party (DP), aliahidi kutowania kiti hicho baada ya kuhudumu kwa mihula miwili. Hii ni baada yake kuchaguliwa kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa 2011.

Wakati huo Kasaali ilikuwa kaunti ndogo lakini ikapandishwa hadhi kuwa baraza la mji mnamo Julai 2017 baada ya Kyotera kutangazwa kuwa wilaya.

“Nilipokuwa mdogo babangu alikuwa akituambia kuwa sisi ndio viongozi wa kesho. Sasa nimekomaa na niko tayari kuchukua usukani kutoka kwake,” Bi Nakiweewa akasema kwenye mahojiano na wanahabari.

“Yeye (Kimera) pia ndiye mmoja wa wale ambao husema Rais Museveni ameongoza kwa muda mrefu na anapaswa kuwapisha viongozi vijana. Je, anataka pia kufuata mkondo huo wa Rais Museveni?” akauliza.

Bi Nakiweewa mwenye umri wa miaka 30 alisema hatavunjwa moyo na vitisho kutoka kwa babake akisisitiza kuendelea na mipango yake ya kuwania kiti hicho.

Anapanga kuwania kiti cha uenyekiti wa Baraza la Mji wa Kasaali katika uchaguzi mkuu wa Januari 2021 kwa tiketi ya chama cha Justice Forum (JEEMA).

“Sina uhasama wowote na Bw Kimera kama mtu binafsi. Atasalia kuwa babangu. Nia yangu ni kuondoa yule mtu ambaye amefeli kutimiza ahadi zake,” akasema.

Katika kisa kingine sawa na hicho, Bw Paul Ssekandi, mwanahabari wa kujitegemea Wilayani Lyatonde, pia ametofautiana na mjomba wake, Bw Elia Ssewandigi.

Hii ni baada ya mwanahabari huyo kutangaza nia ya kushindania kiti kimoja cha kisiasa na Bw Ssewandigi katika uchaguzi mkuu wa 2021.

“Nilinunua mbwa wa kiume mapema mwezi huu na nikampa jina Paul….. Nilikuwa wa kwanza kutangaza azma ya kuwania kiti hicho (uenyekiti) na nitamshinda,” Bw Ssewandigi akasema.

Bw Ssewandigi na Ssekandi watashiriki kinyang’anyiro cha uenyekiit wa Baraza la Mji wa Lyantonde pamoja na mshikilizi wa wadhifa huo sasa Bw Mustapha Kalule.

Mpango wa kuwarudisha nyumbani Waganda waliokwama ughaibuni wakwama

NA DAILY MONITOR

Serikali ya Uganda imeahirisha mpango wa kuwarudisha nyumbani wananchi wake ambao wamekwama nchi za nje, Wizara ya afya ya nchi hiyo imetangaza.

Waziri wa Afya Jane Ruth Aceng alikuwa amesema kwamba watu 300 kati ya 2,392 watakuwa wakirudishwa nyumbani kila wiki na kundi la kwanza linapaswa kufika Jumamosi hii.

Lakini Mamlaka ya Usafiri wa Ndege nchini humo ilisema kwamba haina habari kwamba kuna ndege ya kuleta watu waliokwama nchi za nje.

Baadaye wikendi wizara hiyo ilisema kwamba hakuna ndege itafika humo nchini.

“Huku Waganda zidi ya 2,300 wakirudishwa nyumbani, hakuna ndege inafika nchini kwa sasa. Tarehe halisi itatajwa hapo baadaye.”

Juhudi za kuongea na Wizara ya Afya kuhusiaana na mabadiliko hayo hazikuzaa matunda.

Katibu katika wizara ya afya aliwaelekeza Daily Monitor katika Wizara ya Maswala ya Kigeni.

“Unajua maelezo hayo yana Wizara ya Maswala ya Kigeni, hao ndio wanajua maelezo kuhusiana na usafiri wa wananchi waliokwama nje, kwetu hatuhusiki na usafiri wa ndege,” alisema Dkt Atwine.

Lakini maafisa wa Wizara ya Maswala ya Kigeni hawakupokea simu zetu.

Madereva kutoka Kenya wadai wanawekwa katika vituo duni vya karantini Uganda

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya uchukuzi nchini wameishtumu serikali kwa kushindwa kuwalinda dhidi ya changamoto ambazo madereva wa masafa marefu wanakabiliana nazo wanaposafirisha mizigo hadi nchini Uganda.

Wamesema madereva wamekuwa wakihangaika kila wanapoingia Uganda ikizingatiwa tahadhari kuu iliyoko ya kujaribu kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Wawekezaji hao sasa wanaitaka serikali iingilie kati swala hilo ili madereva wao wasiwekwe katika vituo duni vya karantini ambavyo “haviambatani na kanuni za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Kupitia afisa mkuu wa muungano wa madereva wa masafa marefu nchini, Bw Denis Ombok, wawekezaji hao walidai sehemu za kuwaweka kwenye karantini nchini Uganda ambapo baadhi walipatikana na virusi vya corona ziko katika hali mbaya.

“Kuna uwezekano wa wale ambao wanaendelea kuwekwa kwenye vituo hivyo waambukizwe maradhi mengine kando na Covid-19. Kwanza mazingira na usafi wa sehemu hizo ni duni, hasa vyoo ambavyo viko katika hali mbaya zaidi,” amesema Bw Ombok akizungumza Jumapili mjini Mombasa.

Afisa mkuu wa muungano wa madereva wa masafa marefu Bw Denis Ombok akizungumzia masaibu ya madereva wanaosafirisha mizigo hadi nchini Uganda. Picha/ Winnie Atieno

Bw Ombok alisema inasikitisha kwamba madereva wa humu nchini wanaendelea kupatikana na virusi hivyo wanapofika maeneo ya mipakani.

Amedai kuwa baadhi ya madereva hao wamelazimishwa kusafisha sehemu hizo.

“Sehemu za karantini nchini Uganda hazifai kuwekwa mwanadamu; madereva wetu wana msongo wa mawazo na pia wanahangaishwa kwenye vizuizi huko Uganda na pia kunyanyapaliwa,” ameongeza.

Taharuki UG wafuasi wa upinzani wakikamatwa

Na AFP

IDADI isiyojulikana ya wafuasi wa upinzani Uganda, akiwemo aliyekuwa mgombea urais Dkt Kizza Besigye, wanazuiliwa na polisi kufuatia ghasia katika jiji kuu la Kampala zilizoshuhudiwa Jumatatu asubuhi.

Balaa ilizuka baada ya maafisa wa kulinda usalama kuzuia mkutano uliopangwa wa Forum for Democratic Change (FDC) katika Uwanja wa Mandela mjini Namboole.

Maafisa wa polisi na wanajeshi waliojihami vikali walizingira uwanja huo na kuwalazimu wanachama wa FDC waliojawa na hamaki kuandamana kuelekea makao makuu ya chama chao kwenye barabara kuu yenye shughuli nyingi ya Kampala-Jinja.

Ili kutawanya umati, polisi walitumia vitoa machozi, risasi za maji na risasi za bunduki na kusababisha vita vya kukimbizana.

Dkt Kizza Besigye, aliyekuwa rais wa FDC aliendelea kupungia umati hewani akiwa juu ya gari lake kabla ya polisi kulizuia na baadaye kulivuta katika Kituo cha Polisi cha Naggalama.

Hata hivyo, baadhi ya minyororo iliyotumika kuvuta gari la Besigye ilivunjika huku umma ukimshangilia mgombea huyo aliyewania urais mara nne.

Kisha polisi walitumia risasi za maji kumlazimisha Besigye kutoka garini mwake na kumweka katika gari la polisi, lililoondoka kwa kasi kuelekea Naggalama. Kutokana na vurugu hizo, mbunge wa Manispaa ya Kira, Ibrahim Ssemujju Nganda, alikamatwa lakini akatoweka.

Kupitia taarifa, polisi walisema FDC iliwafahamisha kuhusu mkutano ulionuiwa lakini wakashauriwa kubadilisha eneo, agizo walilopuuza.

“FDC ilitufahamisha kuhusu sherehe hiyo iliyopangwa na tukawajibu tukiwashauri wabadilishe eneo la hafla lakini wakatupuuza. Besigye alikaidi maagizo ya polisi na kuegesha gari lake barabarani katikati huku akiwazuia na kuwahangaisha watumiaji wengine wa barabara,” “Gari lilivutwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Naggalama. Kwa sasa hakuna mashtaka aliyoshutumiwa dhidi yake lakini wapelelezi bado wanakusanya ushahidi,”alisema msemaji wa polisi Kampala Metropolitan Bw Patrick Onyango. Huku uchaguzi wa 2021 ukijongea, vyama vya kisiasa vya upinzani na makundi ya wakereketwa vinapambana kuweka mikakati ya kumkabili Museveni.

Hata hivyo, polisi kila mara wamevunja mikutano yao wakitaja ukiukaji wa Sheria kuhusu Usimamizi wa Utulivu kwa Umma.

Majuzi, Besigye na wafuasi wake kadha walizindua kampeni ya uasi wa umma inayoitwa ‘Tubalemese’, akisema itasaidia upinzani kufanikisha malengo yake.

Besigye, Bobi Wine katika kikao cha siri kuhusu 2021

Na ERIASA MUKIIBI SSERUNJOGI, DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

IMEFICHUKA kwamba Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Dkt Kizza Besigye na Mwanamuziki Mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine wameanzisha mashauriano kisiri kuhusu watakavyoungana kwa nia ya kumshinda Rais Yoweri Museveni kwenye uchaguzi wa 2021.

Inadaiwa mazungumzo hayo yamekuwa yakiendelea kichinichini huku wawakilishi wa viongozi hao wawili wakipanga mikakati maridhawa ya kuhakikisha wanaungana na kumvua Rais Museveni mamlaka ya utawala mwaka huo wa uchaguzi.

Mnamo mwezi Mei, wanachama wa vuguvugu la ‘Serikali ya Wananchi’ linaloongozwa na Dkt Besigye na wenzao wa vuguvugu la ‘Mamlaka ya Wananchi’ linalosimamiwa na Kyagulanyi walitoa tangazo la wazi kwamba watashirikiana kwa lengo la kushinda uchaguzi wa mwaka wa 2021.

Aidha imebainika wawakilishi wa viongozi hao wawili wamekuwa wakiandaa mikutano baada ya tangazo hilo na wameanza kukubaliana kuhusu masuala ya kimsingi huku wakiwa na nia kuu ya kushinda Urais.

Duru zinaarifu kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wawili hao kuungana huku wawakilishi wa Kyagulanyi wakiwarai wenzao wanaomwakilisha Dkt Besigye kukubali na kuunga mkono mwanasiasa huyo chipukizi kwenye uchaguzi huo.

Vilevile imebainika kwamba kuna imani kutoka mrengo wa Kyagulanyi kwamba mwanasiasa huyo chipukizi ana uwezo mkubwa wa kumshinda Rais Museveni ikilinganishwa na Dkt Besigye ambaye ameibuka wa pili kila mara anapowania dhidi ya kiongozi huyo mkongwe.

Aidha inadaiwa kwamba wawakilishi wa Kyagulanyi wamelegeza msimamo na hata kufichua kwamba mwaniaji wao yupo tayari kuhama chama chake na kuwania Urais kwa tiketi ya chama cha FDC kinachoongozwa na Dkt Besigye, iwapo kigogo huyo wa siasa za upinzani atakubali kumuunga mkono.

Wawakilishi

Jopo la wawakilishi wa Dkt Besigye linaongozwa na mwanasiasa Wafula Oguttu ambaye wakati moja alikuwa mbunge, kiongozi wa upinzani bungeni na msemaji wa FDC.

Kyagulanyi naye mara ya kwanza alimteua mbunge wa Butambala, Muwanga Kivumbi kumwakilisha kwenye mazungumzo hayo lakini baadaye alimpiga kalamu kisha akamteua David Lubongoya kuchukua nafasi yake.

Kivumbi ni mwanachama wa chama cha DP na amejizolea sifa kama mwanaharakati ambaye amepinga utawala wa kimabavu wa Rais Museveni kwa miaka mingi.

Pia amekuwa mwanachama wa Vuguvugu la vijana wanaopigania demokrasia Uganda(UYD) tangu wakati alipokuwa mwanafunzi chuoni.

Hata hivyo, Oguttu na Lubongonya walikataa kufichua palipofikia mazungumzo hayo, wote wakisisitiza kwamba waliamrishwa kufanya kazi na kutofichua lolote kwa wanahabari.

Serikali ya Museveni yapitisha kuundwa kwa Baraza Kuu la Kiswahili

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

SERIKALI imeidhinisha hoja ya kutaka kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili litakalotoa mwongozo kuhusu mchakato wa kufanya Kiswahili kuwa lugha rasmi nchini Uganda.

Akihutubia wanahabari kuhusu uamuzi wa Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya Rais mjini Entebbe, Msemaji wa Serikali Ofwono Opondo alisema, kubuniwa kwa baraza hilo kunaambatana na matakwa ya katiba.

Alisema baraza hilo litahakikisha Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya pili nchini Uganda baada ya Kiingereza.

“Katiba inahitaji kwamba tuwe na lugha mbili za kitaifa; Kiingereza na Kiswahili. Lakini hatujakuwa tukitumia Kiswahili. Baraza hilo litaajiri walimu watakaokuwa wakifundisha Kiswahili shuleni,” akasema.

Alisema baraza hilo pia litasimamia kubuniwa kwa sera, mwongozo na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inafunzwa kwa ubora wa juu.

Bw Opondo alisema baraza hilo pia litahakikisha kuwa Kiswahili kinatumika katika wizara na mashirika yote ya serikali na kutoa vifaa vinavyotakiwa kama vile vitabu na kamusi.

Uganda imekuwa ikitumia Kiingereza kama lugha rasmi tangu nchi hiyo kupata uhuru wake mnamo 1962.

Nchini Uganda, lugha ya Kiswahili ilianza kutumika katika Baraza la Kifalme la Buganda na Bunyoro, hata kabla ya ukoloni (1862). Kiswahili hutumika katika shughuli za biashara, dini na mila.

Nchini Uganda Kiswahili hutumiwa zaidi na Polisi na Wanajeshi.

Katika miaka ya 1980, raia wengi wa Uganda walikiona Kiswahili kama lugha ya wahalifu ikitumiwa na askari kuwadhulumu na kuwanyang’anya mali yao.

Uganda ndiyo nchi ya hivi karibuni kuidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi. Namibia, Rwanda na Afrika Kusini pia zimeidhinisha Kiswahili kufunzwa shuleni.

Baraza la Mawaziri la Namibia liliidhinisha hoja ya kutaka Kiswahili kufunzwa shuleni Julai, mwaka huu.

Serikali ya Namibia ilianza kujadili suala la kufundisha lugha ya Kiswahili baada ya kiongozi wa Tanzania John Magufuli kuzuru nchi hiyo Mei, mwaka huu. Wakati wa ziara yake, Rais Magufuli alitaka Namibia na Tanzania kudumisha ushirikiano ambao umekuwepo tangu 1991 kwa kufundisha Kiswahili.

Magufuli alisisitiza kuwa kulikuwa na haja kwa mataifa hayo mawili kushirikiana katika sekta ya elimu. Kiswahili kitaanza kufunzwa katika shule nchini Afrika Kusini kuanzia mwaka 2020.

Waziri wa elimu msingi, Angie Motshekga mnamo Septemba mwaka jana alisema kuwa, Kiswahili kitafunzwa kama lugha mbadala kwa wanafunzi nchini humo.

Kisasi Kenya, UG zikionana katika mchujo wa raga

Na GEOFFREY ANENE

KENYA na Uganda zitafufua uhasama wao kwenye raga wakati Lionesses itavaana na Lady Cranes katika mechi yao ya pili ya mashindano ya Afrika ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande ya wanawake leo Jumanne mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Lionesses ilitoka chini mguso mmoja na kurarua Madagascar 35-5 katika mechi yake ya ufunguzi ilitosakatwa Agosti 9 nayo Uganda iliona cha mtema kuni dhidi ya Afrika Kusini ilipopepetwa 89-5 baadaye siku hiyo.

Kenya na Uganda zinafahamiana sana kutoka na kushiriki mashindano ya mataifa mawili ya Elgon Cup.

Tangu makala ya kwanza ya wanawake ya Elgon Cup mwaka 2006, majirani hawa wamekutana mara 18. Kenya inajivunia ushindi 11, Uganda imeshinda Kenya mara sita, huku mechi moja ikiishia sare.

Lionesses itaingia mchuano huu na motisha ya kutopoteza dhidi ya Lady Cranes katika mechi sita zilizopita. Mara ya mwisho mataifa haya yalikutana ni katika Elgon Cup mwaka 2019 pale Kenya ilikanyaga Uganda 44-13 Juni 22 mjini Kisumu na kuilima tena 35-5 Julai 13 jijini Kampala na kuhifadhi taji kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Katika viwango bora vya raga duniani, Kenya inaorodheshwa katika nafasi ya 28 nayo Uganda iko nafasi 16 nyuma.

Baada ya kulima Madagascar, nahodha wa Kenya Philadelphia Olando alionya kuwa Lionesses inastahili kuimarika kabla ya kukutana na Uganda.

“Ilikuwa mechi ngumu kwetu mwanzoni kwa sababu Madagascar ilitubabaisha katika dakika 20 za kwanza. Hata hivyo, tulisalia watulivu katika uzuiaji wa mashambulizi na kuimarisha mashambulizi yetu, na hivyo ndivyo tulifaulu kurejea kwenye mechi na hatimaye kuishinda. Lazima turekebisha jinsi tunavyoanza mechi kwa sababu hatujafurahia jinsi tulicheza dhidi ya Madagascar katika dakika za mwanzo. Ni muhimu tuimarishe sehemu hii ya mchezo wetu kabla ya kurejea uwanjani,” alisema Olando, ambaye alichangia mguso mmoja katika mchuano huo, huku Celestine Masinde akipachika miguso miwili.

Kenya ilipata alama zake zingine kupitia kwa Janet Okelo, Diana Awino, Christabel Lindo (mguso mmoja kila mmoja), Janet Owino (penalti) na Irene Atieno (mkwaju).

Kulemewa

Kenya, ambayo mara ya mwisho ililemewa na Uganda ilikuwa 13-8 mwaka 2013 katika mechi ya marudiano ya Elgon Cup jijini Kampala, itajilaumu yenyewe ikidharau mahasimu hao wake.

Vyombo vya habari nchini Uganda vilinukuu kocha Edgar Lemerigar akiamini kuwa Lady Cranes inaweza kushangaza warembo wa kocha Felix Oloo. “Tulizidiwa maarifa na Afrika Kusini, lakini tunaweza kuchapa Kenya. Tunachohitaji tu kufanya ni kurekebisha makosa tuliyoyafanya dhidi ya Afrika Kusini,” alisema.

Mechi hii itasakatwa saa nane mchana. Itapisha mchuano kati ya Afrika Kusini na Madagascar. Raundi ya mwisho ya mechi za mchujo huu wa mataifa manne ni Agosti 17 wakati Uganda na Madagascar zitalimana saa nane, huku Kenya na Afrika Kusini zikikabiliana saa mbili baadaye.

Mshindi wa mashindano haya ataingia Kombe la Dunia mwaka 2021 nchini New Zealand. Nambari mbili atapata fursa ya mwisho ya kufika New Zealand kwa kumenyana na timu kutoka Amerika Kusini, Ulaya, Asia na Oceania.

JANDONI: Uganda katika mizani raundi ya 16-bora ikianza

Na MASHIRIKA

CAIRO, Misri

MECHI za muondoano za hatua ya 16-bora za AFCON zitaanza rasmi leo Ijumaa hadi Jumatatu katika viwanja mbali mbali ambapo washindi wa mechi hizo watasonga mbele hadi hatua ya robo-fainali.

Uganda Cranes ambayo ndio waliobakia miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki baada ya Kenya, Tanzania na Burundi kuondolewa mapema watamenyana na Senegal ambayo ndiyo timu bora barani Afrika.

Senegal ilimaliza katika nafasi ya pili baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0 na 3-0 dhidi ya Tanzania na Kenya mtawalia na kushindwa 1-0 na Algeria katika mechi za Kundi C.

Katika mechi zingine kali za hatua hiyo ya 16-bora, miamba wawili wa soka barani Afrika, Cameroon na Nigeria watakabiliana jijini Alexandria kesho, Jumamosi, huku wenyeji Misri wakikabana na Afrika Kusini, wakati Ghana ikivaana na Tunisia.

Jumla ya timu nane zimefungasha virago kwa kutolewa katika hatua ya makundi, tatu kati ya hizo zilitingwa mechi zote.

Tanzania ndiyo timu iliyofanya vibaya zaidi katika mashindano hayo kitakwimu, baada ya kufungwa jumla ya magoli nane na kufunga mawili, hivyo wamemaliza wakiwa na uwiano wa magoli sita zaidi ya waliofunga.

Timu inayofuata kwa kufanya vibaya ni Namibia ambayo pia ilifungwa mechi zote na kumaliza na uwiano wa magoli zaidi ya waliyofunga, kisha Burundi yenye alama sufuri pia na uwiano wa magoli zaidi ya waliyofunga.

Timu zingine zilizofungasha virago ni Guinea-Bissau iliyomaliza na pointi moja, Zimbabwe pia pointi moja, Mauritania pointi mbili, Angola pointi mbili na Kenya yenye pointi tatu.

Timu nne zilitinga raundi ya muondoano kama timu bora ambazo ni Guinea, DR Congo, Afrika Kusini na Benin.

Wakati huo huo, aliyekuwa nahodha wa Super Eagles ya Nigeria, Austine Okocha maarufu kama ‘JJ’ amewaonya wachezaji wa kikosi hicho dhidi ya Cameroon zitakapokutana kesho mjini Alexandria.

Nigeria walimaliza katika nafasi ya pili katika Kundi B, nyuma ya Madagascar na sasa watakutana na Indomitable Lions chini ya kocha Clarence Seedorf ambao pia walimaliza katika nafasi ya pili katika Kundi F.

Kujifunza

Okocha, ambaye alikuwa kwenye kikosi kilichoshindwa na Cameroon katika fainali ya 2000 jijini Lagos, amemtaka Gernot Rohr kuhakikisha vijana wake wajifunze kutokana na mechi yao dhidi ya Madagascar ambayo walishindwa na limbukeni hao.

“Nijuavyo, Nigeria wana kibarua kigumu Jumamosi. Cameroon daima wanakuwa wagumu tunapokutana nao mechi inakuwa kama vita,” Okocha alisema.

“Lazima timu yetu ijipange vilivyo kwani lazima mshindi na mshindwa apatikane Jumamosi. Sharti wasahau mechi zilizopita na kuimarisha mchezo wao kwa mtihani mgumu ulio mbele yao.

“Kichapo dhidi ya Madagascar sharti kiwe funzo kwao kabla ya kukutana na Cameroon kwa sababu taifa zima linawategemea. Kwa hakika itakuwa mechi ngumu ambayo kila mtu lazima awe makini daima, wakati huu nchi inasubiri ubingwa wa taji hili,” alisema nyota huyo wa zamani aliyesakatia klabu maarufu nchini Ujerumani na kwenye ligi kuu ya Uingereza (EPL).

Nigeria ni mabingwa wa AFCON wa miaka 1980, 1994 na 2013, na ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mwaka huu.

Mpaka kati ya Rwanda na Uganda wafunguliwa

Na AFP

SERIKALI ya Rwanda hatimaye imefungua mpaka wake na Uganda katika eneo la Gatuna ili kuruhusu magari yanayobeba bidhaa kupita na pia biashara kati ya mataifa hayo kurejelewa.

Mpaka huo ulifungwa miezi mitatu iliyopita kutokana na uhasama kati ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda, na umeathiri shughuli za kibiashara na maisha ya raia wengi wa mataifa hayo mawili.

Hata hivyo, Rwanda ilijitetea kwamba ilifunga mpaka huo ili kupisha ukarabati wa miundombinu na ikakanusha kwamba uamuzi wake ulichochewa na tofauti za kisiasa kati ya viongozi wa mataifa hayo mawili.

Marekebisho

Serikali ya Rwanda pia imesema mpaka huo umefunguliwa upya ili ukaguliwe na kuona iwapo marekebisho yaliyotekelezwa yamerahisisha usafirishaji wa bidhaa.

Uganda imekuwa ikidai Rwanda imetuma majasusi kuchunguza serikali yake, nayo serikali ya Rais Kagame inalalamika kwamba raia wake wamekuwa wakipigwa na kunyanyaswa mpakani na polisi kutoka Uganda.

Warwanda wawili wakamatwa UG wakiendesha ujasusi

Na DAILY MONITOR

MAAFISA wa usalama wa Uganda wamekamata wanajeshi wawili wa Rwanda kwa madai ya kuingia nchini humo kukusanya taarifa za kijasusi.

Kukamatwa kwa wawili hao; Ishimwe Bosose na Peter Sanvura huenda kukazidisha kuzorota kwa uhusiano baina ya mataifa hayo jirani ambayo yamekuwa na uhasama kwa miezi kadhaa sasa.

Wanajeshi hao walikamatwa wakiwa kanisani katika eneo la Kamwezi wilayani Rukiga wikendi iliyopita.

Akizungumza alipopokea mwili wa Mnyarwanda aliyeuawa kwa risasi nchini Uganda karibu na mpaka wikendi iliyopita, meya wa wilaya ya Nyagatare nchini Rwanda, Claudian Mushabe, jana aliitaka serikali ya Rwanda kuachilia mara moja wanajeshi hao wawili.

“Tunashukuru serikali ya Uganda kwa kutuletea mwili wa raia wetu aliyeaga dunia akiwa huko. Vivyo hivyo, nasihi Uganda kuachilia huru watu wetu wanaozuiliwa huko,” akasema Mushabe.

Bw Mushabe hata hivyo, alikanusha madai kwamba watu waliokamatwa walikuwa wanajeshi.

Aliitaka serikali ya Uganda kuthibitisha madai kwamba Wanyarwanda waliokamatwa ni wanajeshi waliotumwa kukusanya taarifa za kijasusi.

Serikali ya Uganda imeshikilia kuwa wawili hao ni wanajeshi wa Rwanda ambao wamekuwa wakikusanya taarifa za kijasusi na wamepelekwa jijini Kampala ili wahojiwe.

Uhasama baina ya mataifa hayo jirani ulianza mnamo Februari, mwaka huu, Rwanda ilipofunga mpaka wa Katuna na kuonya raia wake dhidi ya kuzuru Uganda.

Rwanda ilidai kuwa Uganda inashirikiana na ‘maadui’ kutatiza serikali ya Rais Paul Kagame.

Mnamo Mei 17, waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uganda Sam Kutesa aliambia mabalozi wa mataifa mbalimbali kuwa wanajeshi wa Uganda wamekuwa wakiingia nchini Uganda bila ruhusa.

“Maafisa wa usalama wa Rwanda wamekuwa wakiingia nchini Uganda bila kufuata utaratibu uliopo,” akasema Bw Kutesa.

Unyanyasaji

Waziri wa Mashauri wa Kigeni wa Rwanda Richard Sezibera, mnamo Aprili pia aliambia mabalozi wa nchi mbalimbali kuwa Uganda imekuwa ikinyanyasa raia wake na hata kufadhili ‘magaidi’ ambao ni tishio kwa serikali ya Rais Kagame.

Wakati wa hafla ya kumwapisha kiongozi wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Jumamosi, Rais Kagame na kiongozi wa Uganda Rais Yoweri Museveni waliketi pamoja.

Huku wakiwa uwanjani Loftus Versfeld jijini Pretoria viongozi hao walionekana wakizungumza, katika hatua ambayo wadadisi walisema kuwa ilikuwa hatua muhimu katika kumaliza uhasama kati yao.

Jumatatu, mamia ya raia wa Uganda na mabalozi wa mataifa mbalimbali walikusanyika katika mpaka wa Katuna kushuhudia Uganda ikikabidhi Rwanda maiti ya mfanyabiashara John Batista Kyerengye aliyepigwa risasi na maafisa wa usalama wa Rwanda.

Mshangao watoto wa miaka 9 na 6 kufunga ndoa

Na PHILIP WAFULA

WAKAZI wa kijiji cha Nakapyata, Baraza la Mji wa Buyende, Wilaya ya Buyende mashariki mwa Uganda, wamestaajabisha wengi kwa kufunganisha ndoa ya watoto wawili.

Harusi hiyo ya kitamaduni iliandaliwa kati ya mvulana mwenye umri wa miaka tisa, na ‘mke wake’ aliye na umri wa miaka sita.

Mvulana huyo, ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Nne katika Shule ya Msingi ya Buyende Light na msichana, ambao wote walisemekana walizaliwa wakiwa na meno mawili, walifanya harusi wiki iliyopita na kupewa chumba watakamoishi pamoja.

Katika sheria za Uganda, ni haramu kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 18 kuozwa au kushiriki ngono.

Ilidaiwa watoto hao walianza ‘kuchumbiana’ wakati mvulana alipokuwa mwenye umri wa miaka mitatu na msichana alikuwa na miezi mitatu pekee.

“Mwanangu alizaliwa akiwa na meno mawili na mke wake pia alizaliwa hivyo. Kuzaliwa kwake kulileta baraka tele na tunatarajia jina lake litaleta umoja kwa makabila ya Baganda na Basoga,” akasema babake mvulana huyo.

Barbra Namulesa, ambaye ni mwalimu wa mvulana huyo, alimtaja kama mvulana mpole, mwenye nidhamu na anayeshirikiana sana na wenzake na pia huongea kama mzee.

“Nadhani huyu ndiye Kintu (anayeaminika kuwa baba wa kwanza ulimwenguni katika jamii ya Baganda) ambaye mababu wetu walihadithia. Yeye hunishauri hata licha ya kuwa mimi ndiye mwalimu wake,” akasema.

Mamake msichana alisema binti yake amekuwa wa kipekee tangu alipozaliwa.

“Alianza kuzungumza mara alipozaliwa. Wakati nilipojifungua niliuliza mtoto wangu ni wa jinsia gani nikaambiwa ni wa kike. Lakini nilishangaa mkunga aliponiambia mtoto amezaliwa akiwa na meno mawili, karibu nimwangushe,” akasema mama huyo wa watoto saba, akieleza alivyohofia kumnyonyesha akiwa na meno.

Katika harusi hiyo ambayo ilijaa nyimbo na densi, baadhi ya waliohudhuria walizirai baada ya kuona mvulana huyo na msichana wameketi kando ya nyoka wawili wenye urefu wa futi tatu kila mmoja. Wazee walidai nyoka hao walinuiwa kulinda ‘wanandoa’ hao.

Msemaji wa polisi katika eneo la Busoga Kaskazini, Michael Kasadha alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

“Ndoa yoyote inapaswa kuwa kati ya watu wenye umri wa miaka 18 kuendelea. Tunataka kubainisha ukweli kuhusu hayo yaliyotokea,” akasema.

FAHARI TELE: Historia mataifa yote ya Afrika Mashariki kutua fainali AFCON

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, TANZANIA

TANZANIA waliwapepeta Uganda 3-0 jijini Dar es Salaam mnamo Jumapili na kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.

Taifa Stars walihitaji ushindi katika mchuano huo wa mwisho katika Kundi L ili kuungana na Uganda katika safari ya kuelekea Misri kwa ajili ya fainali zitakazofanyika kati ya Juni na Julai 2019.

Lesotho waliambulia sare tasa dhidi ya Cape Verde katika mchuano mwingine uliowashuhudia wakibanduliwa kwenye Kundi L.

Ufanisi wa Tanzania una maana kwamba mataifa manne kutoka Afrika Mashariki – Tanzania, Uganda, Burundi na Kenya yatanogesha fainali za AFCON mwaka huu nchini Misri.

Baadhi ya mashabiki wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Picha/ Hisani

Uganda walishuka dimbani kuchuana na Tanzania wakijivunia rekodi ya kutofungwa bao lolote katika kampeni zao za kufuzu kwa fainali za AFCON muhula huu.

Hata hivyo, rekodi hiyo ilifutwa katika mechi yao ya sita baada ya Simon Msuva kumzidi maarifa kipa Denis Onyango na hivyo kuwafungulia Tanzania ukurasa wa mabao kunako dakika ya 21.

Erasto Nyoni aliongeza bao la pili baada ya mapumziko huku Aggrey Morris akizamisha kabisa chombo cha Uganda mwishoni mwa kipindi cha pili.

Hata hivyo, Tanzania wangaliambulia patupu licha ya ushindi huo mnono iwapo Lesotho wangaliwazidi maarifa Cape Verde katika mchuano mwingine wa Kundi L jijini Praia.

Karibu miongo minne nje

Chini ya kocha Emmanuel Amunike ambaye ni winga wa zamani wa Super Eagles ya Nigeria, Taifa Stars kwa sasa watashiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.

Kwingineko, Khama Billiat na Knowledge Musona walifunga mabao muhimu yaliyowapa Zimbabwe tiketi ya kufuzu kwa AFCON baada ya kuwapepeta Congo.

Zimbabwe walijibwaga kwa mchuano huo wakihitaji sare ya aina yoyote ili kuweka hai matumaini ya kufuzu. Kwa upande wao, Congo walikuwa na ulazima wa kusajili ushindi na kujizolea alama zote tatu ili kujikatia tiketi ya kushiriki AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2015.

Bafana Bafana ya Afrika Kusini pia walifuzu kwa fainali za AFCON baada ya kuwapepeta Libya 2-1 katika uwanja wa Taieb Mhiri jijini Sfax.

Wakihitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu, Afrika Kusini walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Percy Tau kunako dakika ya 50.

Ahmad Benali aliwarejesha Libya mchezoni kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 66 na kuwazidishia wageni wao presha.

Ingawa hivyo, Tau alipachika wavuni bao la pili la Afrika Kusini kunako dakika ya 69 na kuwahakikishia Afrika Kusini ushindi uliowawezesha kuungana na Nigeria katika kilele cha Kundi E.

Vikosi vingine ambavyo tayari vimefuzu kwa fainali za AFCON 2019 ni pamoja na Ivory Coast, Madagascar, Mali, Mauritania, Morocco, Algeria, Nigeria, Cameroon, Ghana, Guinea, Angola, Senegal, Namibia na wenyeji Misri.

Burundi walifuzu kwa mara ya kwanza katika historia ya kipute cha AFCON baada ya kuwalazimishia Gabon sare ya 1-1 jijini Bujumbura.

Cedric Amissi aliwafungia Burundi bao kunako dakika ya 76.

Hadi waliposhuka dimbani kwa minajili ya kipute hicho, Burundi walikuwa wakihitaji sare ya aina yoyote ili kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za AFCON nchini Misri mnamo Juni 2019.

Ingawa Omar Ngando alijifunga kunako dakika ya 82, hilo halikutosha kuwapa Gabon waliojivunia huduma za fowadi Pierre-Emerick Aubameyang hamasa ya kupata goli la pili na la ushindi.

Matokeo hayo yaliwasaza Burundi waliokuwa na Saido Berahino wa Stoke City na Gael Bigirimana wa Hibernia, katika nafasi ya pili kwenye Kundi C ambalo linaongozwa na Mali.

Gabon ambao walikuwa wenyeji wa fainali za 2017, wanashikilia nafasi ya tatu.

Raia wa Uganda waliolemewa kulipa hoteli kusukumwa ndani

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wawili wa Uganda Alhamisi walioshindwa kulipa gharama ya malazi katika hoteli moja jijiji Nairobi sasa watalala katika gereza la Viwandani, Nairobi miezi sita wakishindwa kulipa faini ya Sh20,000 kila mmoja.

Mzee Sebowa Kiboigo mwenye umri wa miaka 72 alisababisha kicheko mahakamani aliposema, “Tangu enzi za hayati marais Milton Obote na Idd Amin na hata sasa wakati wa utawala wa Rais Yoweri Museveni nchi ya Kenya imekuwa nzuri kwa raia wote wa Uganda.”

Bw Kiboigo aliyeshtakiwa pamoja na mpwawe Mathias Mgemeso mwenye umri wa miaka 27 alimweleza hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko kuwa ameishi Kenya miaka 40 akifanya biashara za kununua vinyango na kuziuza Marekani na hajawahi fikishwa kortini.”

Akasema, “angu miaka ya 1970 nimekuwa nikifanya kazi nchini Kenya. Nchi hii imekuwa nzuri kwa raia wa Uganda n ahata nyakati machafuko na kisiasa yalipokumba nchi yetu Uganda , Kenya ilitupokea na kutupa kazi za Ualimu , Udaktari na kazi za viwandani.”

Alisema yeye ni Mhandisi wa Masuala ya Kemikali na amekuwa akiishi Kenya tangu alipohitimu masomo yake nchini Amerika miaka ya 1970.

Huku akisakata densi akiwa mchangamfu na mwenye furaha kwa kuruhusiwa kuzugumza mahakamani, Kiboigo alisema hakuwa na pesa za kulipa Comfort Hotel alikolala siku nne.

“Nawashukuru wasimamizi wa wa hoteli ya Comfort kwa kunielewa hata kunipeleka katika benki ya Chase Bank ambapo pesa zangu zimeshikwa baada ya kuwekwa chini ya mrasimu wa Serikali,” Bw Kiboigo alimweleza hakimu.

Aliongeza kusema kuwa ametumiwa pesa kupitia Benki ya Western Union na ndugu yake na sasa “niko tayari kulipa hoteli hiyo.”

Mzee huyo alieleza mahakama kuwa umri wake wa miaka 72 haumruhusu kufanya ukora wa njia yoyote ile.

Karani wa mahakama awasomea mashtaka washukiwa mbele ya hakimu Peter Ooko. Picha/ Richard Munguti

Alikiri maelezo ya kiongozi wa mashtaka Bi Celestine Oluoch kuwa kati ya Machi 10 na Machi 19 alikuwa amekodisha chumba cha kulala akiwa na mwanawe.

“Mshtakiwa alitoroka hoteli hiyo bila kulipa lakini akarudi tena Machi 18 na 19 na kupokewa kwa mikono miwili lakini akashtakiwa aliposhindwa kulipa ada ya malazi,” alisema Bi Oluoch.

Mshtakiwa huyo alieleza korti hana la kusema ila kushukuru nchi ya Kenya kwa kumpa makao kwa zaidi ya miaka 40 lakini akadokeza kufilisika kwa benki ya Chase Bank kulimfanya akumbane na makali ya sheria.

Mshtakiwa huyo aliomba msamaha na kusema hangelipenda kuchokoza nchi hii ambayo inaishi na amani na majirani wake.

“Mimi sisemi eti mimi ni mtu mtakatifu nisiye na udhaifu. La hasha. Mimi ni binadamu kama wengine walio na udhaifu kama huu ambao umenifanya kufika mahakamani nikiwa na umri mkubwa,” alisema mshtakiwa.

Aliongeza kusema kwa maisha yake hapendelei watu wanaowalaumu watu wakifanya makosa hata ikiwa wako na umri wa miaka 10.Mtu anaweza kufanya makosa wakati wowote.

“Ulikuja Kenya kufanya nini?” Bw Ooko alimwuliza Mzee huyo.

“Nilikuwa nimemleta mpwa wangu kutembea katika soko ya Maasai kununua ushanga,” Kiboigo alitoboa siri.

Akaendelea, “Mpwa wangu ameanza kuuza ushanga ng’ambo na nilikuwa nimemleta kumtembeza aone kule zinatengenezwa na kuuzwa. Miaka yangu yote nikiishi Kenya nilikuwa nauza vinyango na vikapu nchini Amerika. Nilipata ufanisi mkubwa na pesa zangu nilikuwa naziweka katika benki ya Chase Bank.”

Bw Kiboigo aliendelea kusema wasimamizi wa benki hii iliyowekwa chini ya mrasimu kutoka Benki Kuu ya Kenya (CBK) walimwandikia barua pepe na kumtaka awasilishe pasi yake ya kusafiri na kitambulisho ndipo pesa zake zilipwe.

UCHUMI: Uganda yapaa Kenya ikichechemea

Na BENSON MATHEKA

Kwa Muhtasari:

  • Wakenya wanaendelea kununua bidhaa kwa wingi kutoka Uganda badala ya kununua zinazotengenezewa humu nchini
  • Bidhaa kutoka Uganda zinazoagizwa na Wakenya ni mayai, maziwa, sukari na maharagwe
  • Kwa sababu ya mazingira bora ya kibiashara, kampuni zilizokuwa na makao Nairobi zimehamia Kampala
  • Haya yote yametokana na serikali ya Kenya kuongeza ushuru wa bidhaa za humu nchini na zile za kutoka nje ya nchi

KENYA imo hatarini kupoteza nafasi yake kama simba wa uchumi Afrika Mashariki baada ya mataifa jirani hasa Uganda kufanikiwa kuuza bidhaa zaidi nyingi hapa nchini kuliko inazonunua.

Hii inamaanisha kudidimia kwa viwanda vya Kenya, watu zaidi kupoteza nafasi za kazi na kupotea kwa ushuru.

Ingawa Rais Museveni anasema Uganda imefanikiwa kuafikia haya kutokana na amani iliyoletwa na jeshi la nchi hiyo, wadadisi wanasema mazingara bora ya kiuchumi nchini humo ndiyo yamechangia hali hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa Wakenya wanaendelea kununua bidhaa kwa wingi kutoka mataifa jirani hasa Uganda na Tanzania badala ya kununua zinazotengenezewa nchini au zinazoigizwa nchini moja kwa moja kutoka ng’ambo kama vile India na China.

Margaret Wanjiru anasema kwamba huwa anaenda Uganda kununua nguo anazouza Nairobi kwa sababu ya bei nafuu: “Huwa ninaenda Kampala mara tatu kwa wiki kununua nguo ambazo hapa Kenya ni ghali mno. Tangu nianze miaka mitatu nimekuwa nikipata faida kubwa kuliko mbeleni,” asema Bi Wanjiru.

Kwa kipindi cha miaka minne sasa, Uganda, ambayo haina bandari kama Kenya, imekuwa ikiuzia Kenya bidhaa za mabilioni ya pesa kuliko inazonunua hapa nchini.

Bidhaa hizo ni pamoja na zinazotoka ndani ya uchumi wa Uganda kama vile mayai, maziwa, sukari na maharagwe. Pia wafanyibiashara wa Kenya wanasafiri Uganda kununua nguo, bidhaa za urembo, mbao na vipuri vya magari kwa ajili ya kuziuza nchini.

Kulingana na mtaalamu wa uchumi, Robert Kamande, Uganda imefanikiwa kuuzia Kenya bidhaa za kilimo kutokana na mfumo bora wa kusaidia wakulima na kupunguzwa kwa ushuru wa fatailaiza, mbegu na pembejeo. Hii ni kinyume na Kenya ambapo gharama za kilimo ziko juu.

Gharama ya chini ya uzalishaji 

“Ndio maana maziwa yanayotoka Uganda yanauzwa Sh40 kwa pakiti ilihali ya Kenya ni Sh50. Hii inamaanisha gharama za uzalishaji Uganda ni nafuu sana ukizingatia kuwa wanauza Sh40 wakiwa wameweka gharama za usafiri,” asema Bw Kamande.

Mwaka 2018, takwimu za Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) zilionyesha kuwa Uganda iliendelea kuuzia Kenya bidhaa nyingi zaidi, tofauti na awali ilipokuwa ikinunua bidhaa hizo kutoka Kenya.

“Kwa sababu ya mazingira bora ya kibiashara, kampuni zilizokuwa na makao Nairobi zimehamia Kampala. Na kwa sababu ya hali nafuu ya kibiashara na ushuru, gharama ya kutengeneza bidhaa huwa ya chini Uganda, na hivyo basi kuvutia wafanyabiashara wa humu nchini,” aeleza mtaalamu wa biashara Robert Kamande.

Takwimu za KRA zinaonyesha kuwa bidhaa ambazo Kenya huuzia Uganda zimekuwa zikipungua kwa kiwango kikubwa tangu 2015.

Wafanyabiashara kutoka Kenya wanachagua kusafiri hadi Uganda kununua bidhaa kwa bei nafuu kuliko kuziagiza moja kwa moja kutoka China au kuzinunua nchini ambako zinauzwa kwa bei ghali baada ya serikali kuongeza ushuru.

Uganda inavyokwepa bandari

Ili kurahisisha biashara, wafanyabiashara wa Uganda wamekuwa wakisafirisha bidhaa kwa ndege moja kwa moja kutoka China hadi Kampala badala ya kuzipitishia bandari ya Mombasa ambapo zinatozwa ushuru mkubwa kabla ya kuzisafirisha kwa reli na matrela hadi Uganda.

Kulingana na Bw Kamande, baadhi ya bidhaa inazoagiza kutoka China huwa pia zinatengenezewa nchini lakini wafanyabiashara huamua kuzinunua Kampala kwa sababu ya bei nafuu.

“Uganda haiwalimbikizii wafanyabiashara mzigo wa kodi kama Kenya. Masharti ya biashara ni nafuu na ndiyo sababu hata magari na vipuri vya magari ni bei nafuu kuliko Kenya,” aeleza Bw Kamande.

Bali na magari, Wakenya wamekuwa wakinunua nguo, bidhaa za urembo, maziwa na mayai kutoka Uganda, jambo ambalo wadadisi wanasema ni tisho kwa uchumi wa nchi kwa sababu kununua bidhaa hizi kutoka nchi jirani ni kuua viwanda vya humu nchini na kunyima Wakenya nafasi za kazi.

Ingawa Kenya ina viwanda vikubwa vya bidhaa za chuma Afrika Mashariki na Kati, Wakenya wamekuwa wakinunua bidhaa hizi kutoka Uganda kufuatia ushuru wa asilimia 35 uliowekwa na serikali kwenye bajeti ya 2018/2019.

Kwenye bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Herny Rotich aliweka ushuru wa asilimia 35 kwa mavazi na viatu kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda viwanda vya humu nchini.

Sekta ya samani iliuawa

“Kwa sababu ya ushuru mpya wa bidhaa za mbao, serikali iliua kampuni kadhaa zilizokuwa zikihusika na fanicha na baadhi zikahamia Uganda na kuacha maelfu ya Wakenya bila kazi,” asema Bw Raju Shah, ambaye alifunga kampuni yake nchini mwaka jana.

Anasema baada ya serikali kuchukua hatua hii ikisema ililenga kulinda viwanda vya humu nchini, bidhaa hizo zinaendelea kuingia Kenya kutoka Uganda kwa bei nafuu zaidi.

Wadadisi wanasema baada ya Kenya kuongeza ushuru wa bidhaa kutoka nje ya nchi, Uganda iliwafungulia milango wawekezaji wa Kenya kwa kupunguza kodi.

“Matokeo yamekuwa ni kuongezeka kwa bidhaa zinazouzwa nchini kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Uganda na Tanzania,” asema Bw Kamande.

Grace Msalame kushtaki UG kwa kutumia picha zake kuvumisha utalii

Na WYCLIFFE MUIA

MPANGO wa serikali ya Uganda wa kugeuza wanawake wanene kuwa kivutio cha kitalii, umeingia doa baada ya mtangazaji Grace Msalame wa Kenya kusema atashtaki wasimamizi wa mpango huo kwa kutumia picha zake kutangaza kampeni hiyo.

Mashindano hayo maarufu kama ‘Miss Curvy Uganda’ yalizinduliwa mnamo Jumatano na Waziri wa Utalii wa Uganda, Godfrey Kiwanda.

“Tuko na wanawake warembo waliobarikiwa kwa unene na umbo la kutamanika. Mbona tusiwatumie kuimarisha sekta ya utalii,” alisema Waziri Kiwanda akizindua kampeni hiyo.

Alipokuwa akizindua mashindano hayo, Bw Kiwanda alisambaza mabango yenye picha ambazo Bi Msalame anadai ni zake, na kuwataka wanawake wa Uganda wenye umbo kama la Mkenya huyo kushiriki kampeni hizo ambazo shabaha yake ni kuvutia watalii kuzuru Uganda.

Katika taarifa yake Alhamisi, Bi Msalame alijitenga na mashindano hayo akisema yanadunisha hadhi ya wanawake na kuwa matumizi ya picha zake yamemkera sana.

“Nimeudhika sana kwa picha zangu kutumika kueneza dhuluma dhidi ya wanawake. Sikubaliani kamwe na dhana kuwa mwili wa mwanamke unaweza kugeuzwa kuwa kivutio cha kitalii,” alisema Bi Msalame katika taarifa yake kwa vyombo ya habari.

Mwanahabari huyo alisema matumizi ya mwili wa mwanamke kuvutia watalii ni ukiukaji wa haki za kibinadamu na akatangaza kuwachukulia wasimamizi wa mashindano hayo hatua za kisheria.

“Nimefanya bidii nyingi katika kazi yangu ili kulinda hadhi yangu na bila shaka nimeanzisha mchakato wa kisheria dhidi ya wahusika wa mashindano hayo,” alisema Bi Msalame.

Hatua ya Wizara ya Utalii nchini Uganda kutumia picha ya Mkenya katika mashindano hayo imewakera pia raia wengi wa Uganda waliolalamika kuwa huko ni ‘kukosewa heshima’ na serikali yao.

“Ni aibu kwa Uganda kutumia picha ya mgeni katika mashindano ya ‘Miss Curvy Uganda’. Kwani hakuna wanadada walioumbwa vyema Uganda?” alilalamika Noah Kisemi, katika mtandao wa Twitter.

Mashirika ya kijamii ya wanawake nchini Uganda vilevile yameapa kuzima mashindano hayo yakisema kuwa yanadunisha hadhi ya mwanamke katika jamii.

“Hatua hii ni ya kuhalalisha dhuluma dhidi ya wanawake. Tumeshuhudia mara nyingi wanaume wakiwapapasa kwa lazima wanawake mitaani Uganda na hatutakubali vitendo hivyo kuidhinishwa kuwa vya kitalii,” alisema mwanaharakati Primrose Murungi wa Uganda.

Bi Msalame anatarajiwa kuanzisha shoo mpya katika runinga ya NTV, Kenya.

UG sasa kutumia wanawake warembo kuvutia watalii

DAILY MONITOR Na PETER MBURU

SERIKALI ya Uganda kupitia Wizara ya Utalii imeamua kuwatumia wanawake wenye mili ya kuvutia na umbo mduara kama kivutio cha watalii wa kigeni.

Waziri wa Utalii nchini humo Godfrey Kiwanda alianzisha shindano la urembo la ‘Miss Curvy Uganda’ Jumanne kama hatua ya kuinua utalii wa taifa hilo.

Wanawake wanaojiamini kuwa warembo wanatarajiwa kushindana kuhusu yupi mrembo na mwenye makalio ya kuvutia, kisha baadae mshindi washindi watakaotumika kuvutia watalii watangazwe mnamo Juni.

Waziri huyo alianzisha shindano hilo katika hoteli moja Jiji kuu la Kampala, wakati alipeperusha bendera huku wanawake waliovalia mavazi ya kubana wakizunguka kando ya kidimbwi cha kuogelea, wakipigwa picha na waandalizi wa shindano hilo.

“Tumekuwa tukiwatuza wanawake wanaovutia na ambao ni warembo kuangaliwa kila siku. Kwanini tusiwatumie kama mbinu ya kuinua utalii wetu?” Bw Kiwanda akasema.

Sekta ya Utalii ndiyo huipatia nchi ya Uganda pesa nyingi zaidi za kigeni, kwani mwaka uliopita ilipata zaidi ya S100milioni (za Kenya), kulingana na rekodi za serikali.

Watalii wengi huzuru mbuga kutazama wanyama na ndege, mbali na ziwa Victoria ambalo ndiyo chemichemi ya Mto Nile.

Lakini sasa Uganda imeamua kupanua nyanja za kupata hela zaidi za kigeni, sasa kwa kuongeza bidhaa nyingine katika menyu ya utalii, wanawake wenye makalio ya kuvutia na warembo kabisa.

Mwandalizi mkuu wa shindano hilo la urembo Ann Mungoma alisema kuwa ana matumaini kuwa litawaangaza watu wa Uganda na kuwafanya kuvutia ulimwengu.

“Ni shindano ambalo litaonyesha urembo halisi wa mwanamke Mwafrika. Litawafanya wanawake wa umri mdogo kuonyesha weledi na makalio yao ya kuvutia,” akasema Bi Mungoma.

Watakaohusika katika shindano hilo, hata hivyo, ni wale wa kati ya umri wa miaka 18 na 35 pekee, wengine wakifungiwa nje.

Mfanyakazi adukua mitambo ya serikali ya Museveni na kuhepa na data ya siri

DAILY MONITOR Na PETER MBURU

MADAI yameibuka kuwa mtu aliyedukua mitambo ya Wizara ya Leba nchini Uganda na kuiba taarifa za siri zenye umuhimu kuhusu uajiri ni mfanyakazi wa serikali.

Inaripotiwa kuwa wadukuzi waliiba habari na nakala za umuhimu mkuu kuhusu ajira ndani ya serikali.

Mitambo ya wizara ambayo hukagua kampuni za kutoa ajira za nje ya nchi, kuonyesha ikiwa kuna nafasi za ajira na kupigana na suala la watu kusafirishwa kwa njia haramu ilikosa kufanya kazi kwa njia ambazo hazikueleweka.

Mitambo hiyo iliwekwa baada ya malalamishi kuwa raia wa Uganda wanaofanya kazi Uarabuni wanateswa kuzidi.

Serikali iliamua kukaza kamba katika mbinu zake za kukagua habari kuhusu namna watu wanasafiri, kazi wanazoenda kufanya na ikiwa zinapatikana. Kila kampuni inayofanya biashara hiyo inapewa akaunti ambapo inasema watu inaohitaji.

Lakini wafanyakazi wa serikali wamedai kuwa ni mfanyakazi wa wizara ya Teknolojia na mawasiliano ambaye kwa ushirikiano na baadhi ya kampuni za kutafutia watu kazi walitekeleza kitendo hicho, ili kupitisha ukaguzi wa baadhi ya wafanyakazi wao.

Kamishna wa Leba katika wizara hiyo David Mugisha alisisitiza kuwa mitambo ‘ilianguka’ tu, akipinga kuwa ilidukuliwa.

“Ninawaambia kuwa mitambo ilianguka tu, sijui mlikotoa habari kuwa ilidukuliwa,” akasema Bw Mugisha.

Lakini mdokezi mmoja alieleza gazeti  la Daily Monitor kuwa wizara inamfahamu aliyedukua mitambo hiyo. Alisema, hata hivyo, wizara bado haijamchukulia hatua zozote.

Mitambo ilikuwa imeundwa kwa namna kampuni ikipokea ombi la kutafuta mfanyakazi kutoka mataifa ya nje, ingewasilisha ombi hilo kwa wizara ya Leba kabla ya kuruhusiwa.

Baada ya kuruhusiwa, kampuni inatafuta mfanyakazi na kumfanyia mahojiano, kasha anayefuzu anawasilishwa kwa wizara tena ili akaguliwe.

Majina ya wanaoruhusiwa yanawasilishwa kwa idara kadha za serikali hadi wakubaliwe kusafiri kutoka nchini.

Wadokezi walieleza kuwa tangu serikali kuanza kutumia mtindo huo, maombi mengi ya kazi yamekuwa yakikataliwa, baada ya kubainika kuwa zilikuwa feki.

Wadokezi waliendelea kuel;eza kuwa maafisa wa kampuni kwa ushirikiano na wale wa usalama na uhamiaji huwasafirisha watu kuvuka mipakani kinyume na sheria kwa kutoa hongo ya kati ya Sh300,000 na nusu milioni (za Uganda) kila mtu.

“Kampuni ambazo zinamilikiwa na wakuu wa usalama na maafisa wa serikali zinahudumiwa hata bila kulipa pesa hizo,” akasema mdokezi.

Baada ya kisa hicho cha udukuzi, serikali ya Saudi Arabia inasemekana kufahamisha wizara hiyo ya Jinsia na Leba kuwa kazi hiyo ilifanywa na watu wa ndani ya wizara yenyewe.

Wadokezi walisema kuwa maafisa wa Saudi walimtambua mdukuzi kama mfanyakazi katika wizara na kujitolea kusuluhisha tatizo hilo, lakini wizara ya Leba ikakataa msaada wake.

Mitambo hiyo ilikuwa imeundwa hibi kwamba Saudi ikiwa na nafasi za ajira ingetangaza hapo, na kampuni zikihitaji wafanyakazi pia kutangaza hapo.

Baada ya matukio hayo, kampuni ambazo zilikuwa zimehudumiwa na wateja wao kuruhusiwa kusafiri kwenda Saudi bado hazijawasafirisha.

Wadokezi walisema kuwa udukuzi ulitekelezwa kwa ushirikiano kati ya idara ya usalama na maafisa wa uhamiaji katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

Serikali ya Saudi ilibaini kuwa kulikuwa na kisa cha aina hiyo baada ya mitambo hiyo, inayoitwa MUSANED kuruhusu watu 1660 wa Uganda kusafiri kwenda kufanya kazi, bila kukaguliwa na wizara.

Kaimu waziri wa Leba na Jinsia Peace Mutuuzo aliandikia serikali ya Saudi baada ya kubaini, akitaka maelezo kuhusu namna Waganda hao waliruhusiwa bila kupitishiwa mchakato wa kawaida.

Serikali ya Saudi, hata hivyo, ilisingizia matatizo ya kimitambo ya MUSANED kuwa sababu, ikisema kuwa timu yake ilirekebisha kosa hilo mara moja.

Wanachama wa muungano unaoshughulika na uajiri wan je ya nchi Uganda sasa wameitaka serikali kumtafuta na kumkamata mdukuzi aliyefanya hivyo.

UGANDA: Onyo kwa viongozi dhalimu mapinduzi yaja!

Na WANDERI KAMAU

KATIKA historia, mapinduzi ya kiraia yamechangia pakubwa kung’atuliwa ya viongozi wa kiimla wanaokwamilia mamlakani.

Mapinduzi hayo hutokea wakati wananchi wanapochoshwa na udhalimu wa viongozi hao, ambapo huungana kwa kusahau tofauti zao za kikabila, kidini, kisiasa na kitamaduni.

Nchini Kenya, kuungana kwa wananchi kupitia muungano wa Narc, ulioongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2002, ndiko kulipelekea kushindwa kwa utawala wa Kanu.

Rais Mstaafu Daniel Moi, hakuwa na lingine ila kukubali uamuzi wa Wakenya, japo shingo upande.

Vivyo hivyo, mwelekeo huo ndio unaonekana kutokea nchini Uganda, ambapo Rais Yoweri Museveni anakabiliwa na wimbi kali linalotishia kuyumbisha utawala wake wa kiimla.

Wimbi hilo linaloongozwa na mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine nalinaonekana kusambaa kote kote nchini humo.

Hii ni baada ya vikosi vya usalama kumkamata mwanasiasa huyo na wabunge kadhaa wa upinzani, kwa kisingizio cha “kutishia usalama wa kitaifa.”

Hadi sasa, hali ya taharuki ingali tete, huku baadhi ya nchi za kigeni kama Uingereza, zikitoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya kusafiri Uganda.

Cha kushangaza ni kwamba, Bw Museveni anaonekana kujitia hamnazo kuhusu wimbi hilo, analodai kuwa la “warusha mawe.”

Undani wa maasi dhidi ya Museveni ni kuwa unaongozwa na wabunge vijana, ambao wamechoshwa na utawala wake wa zaidi ya miaka 30.

Kile kiongozi huyu anaonekana kutofahamu ni kuwa mawimbi haya husambaa kama moto wa nyikani, ambapo mwishoni, huwa wanageukwa hata na washirika wao wa karibu.

Mifano dhahiri ya viongozi waliowahi kung’atuliwa mamlakani na mapinduzi ya kiraia ni aliyekuwa rais wa Haiti, Papa Dok, Ferdinard Marcos (Ufilipino), Hosni Mubarak (Misri), Zine Idine Ben Ali (Tunisia), Muammar Gadaffi (Libya) kati ya wengine.

Ingawa baadhi ya mapinduzi hayo yaliendeshwa na nchi za kigeni kama Amerika, ukweli ni kuwa uingiliaji mataifa hayo huwa ni kuwasaidia raia kujikomboa dhidi ya utumwa wa kisiasa.

Uhalisia uliopo ni kuwa katika enzi hii ya mitandao ya kijamii, ni hadaa kubwa kwa kiongozi yeyote kujidanganya kwamba anaweza kuzima mawasiliano ya raia kuhusu mikakati watakayochukua ili kujikomboa.

Mapinduzi hayo ni onyo kwa viongozi wote Afrika kuwa enzi ya udhalimu wa kisiasa zimepitwa na wakati.

akamau@ke.nationmedia.com