Ndoa ya Jubilee na ODM yapigwa mawe

Na BENSON MATHEKA

MUUNGANO unaosukwa wa vyama vya kisiasa vya Jubilee na ODM, unaendelea kukosolewa vikali huku viongozi walioalikwa kujiunga nao ukiiva wakisema, hauwezi kufaulu katika mazingira ya kisiasa nchini.

Mnamo Jumatano wiki jana, vyama hivyo vilitangaza kuwa vimeanza mazungumzo ya kuhalilisha ushirika ambao umedumu tangu handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga Machi 9, 2018 kwa kuungana.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, vyama hivyo vinaunda muungano kwa msingi wa handisheki na vyama vingine vinaweza kujiunga baadaye bila mashartiHata hivyo, vinara wa vyama hivyo na washirika wao wamepuuza muungano huo wakiutaja kama mzaha na unaokiuka sheria.

Kulingana nao, lengo la muungano huo ni kumuandalia Bw Odinga njia ya kushinda urais mwaka ujao.Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alisisitiza kuwa hawezi kushirikiana na Bw Odinga, waziri huyo mkuu akiwa mgombea urais.

Akizungumza akiwa Ithanga kaunti ya Murang’a Jumapili, Bw Musyoka alisema kwamba muungano wa ODM na Jubilee hautafua dafu.

“Tuko na mkataba wa ushirikiano kama Wiper na kiongozi wa Jubilee Party ambaye ni Rais Uhuru Kenyatta na mimi ndiye kiongozi wa chama cha Wiper na siwezi kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga,” alisema.

Mnamo Ijumaa, Naibu Rais William Ruto na washirika wake wa kisiasa walikejeli muungano huo wakiutaja kama wa kikabila.Dkt Ruto alisema muungano huo unalenga kuhujumu azima yake ya urais kupitia Jubilee Party lakini tayari amejipanga na chama cha United Democratic Alliance.

“Wanaweza kuunda muungano wa makabila lakini sisi tumejipanga katika chama cha hasla,” Dkt Ruto alisema akiwa kaunti ya Pokot Magharibi.

Alisema kwamba, Rais Kenyatta na Bw Odinga wanajisumbua bure kuunda muungano wa Jubilee na ODM.Wabunge wa vyama vya Wiper na Amani National Congress (ANC) wanasema kuwa muungano huo hautaweza kuvunja ule wa One Kenya Alliance (OKA).

“Jubilee na ODM wanaharibu wakati kwa kuwa muungano huo hautaenda popote. Ni njama ya kumcheza Odinga kwa kuwa ni wazi haungwi mkono Mlima Kenya,” alisema mbunge wa Lugari, Ayub Savula ambaye ni naibu kiongozi wa ANC.

Muungano wa OKA unaleta pamoja Bw Musyoka, Mudavadi, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa KANU.Bw Musyoka Bw Mudavadi na Bw Wetangula ni washirika wa Bw Odinga katika muungano wa National Super Alliance (NASA) ambao wanasema ungali unadumu.

Bw Mudavadi na Bw Musyoka wamekataa mualiko wa kujiunga na ndoa ya Jubilee na ODM na kusisitiza wako OKA ambao kulingana nao, ni mkubwa kuliko wa vyama hivyo viwili.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye ni mshirika wa Dkt Ruto anasema itahitaji muujiza kwa muungano wa ODM na Jubilee kutikisa siasa Kenya.

“Unahitaji muujiza kwa sababu lengo ni kuafikia muungano wa kikabila,” alisema kwenye kipindi kimoja cha runinga jana asubuhi.

Kulingana na wabunge Dan Maanzo (Makueni na Chris Wamalwa (Kiminini) muungano unaosukwa katika ya ODM na Jubilee kwa sasa, unakiuka sheria kwa kuwa chama hicho cha chungwa kingali katika NASA.

“Vyama tanzu vya NASA haviwezi kuingia katika muungano mwingine lakini vinaweza kuwa na ushirikiano na vyama nje ya muungano huo,” walisema wakizungumza katika hafla tofauti.

Vinara wa OKA sasa waalikwa kwa ndoa ya Uhuru na Raila

Na BENSON MATHEKA

Vigogo wa kisiasa wanaounga handisheki, wamealikwa katika muungano wa kisiasa unaosukwa kati ya vyama vya Jubilee na ODM.

Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju anasema kwamba muungano huo unaosukwa kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga hautawafungia vinara wa vyama vingine vinavyotaka kuungana nao.

Hata hivyo, alisema watakubali tu vyama ambavyo havitawapatia masharti. Vyama vya Wiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka na Kanu cha seneta wa Baringo Gideon Moi vina mkataba wa ushirikiano na Jubilee.

Imeibuka kwamba hatua ya ODM kuungana na Jubilee iliudhi washirika wa Bw Odinga katika muungano wa NASA ambao walitegemea kuidhinishwa na Rais Kenyatta kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Musyoka na kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, wameapa kwamba hawatamuunga Bw Odinga kugombea urais.

Kulingana na Bw Tuju, Jubilee na ODM vimekuwa vikishirikiana ndani na nje ya bunge na vinaandaa mikakati kubuni muungano.

“Sisi, katika mrengo wa Jubilee tunafanya mazungumzo na ODM tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2022 kwa minajili ya kuunda muungano,” Tuju akasema.

Alitangaza Ijumaa kuwa kamati imeundwa, ili kuandaa mikakati ya kubuni muungano.

Tuju alisema kamati hiyo itatoa ripoti chini ya siku 14, na kwamba vyama vingine vya kisiasa vinakaribishwa kujiunga na muungano utakaobuniwa.

“Sio muungano wa kushurutishwa,” alisema. Hata hivyo, duru zinasema kwamba Rais Kenyatta amekuwa akiwarai vinara wenza kwa NASA kuungana nyuma ya Bw Odinga ili kumshinda Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Hatua ya Jubilee kuhalalisha ushirikiano wake na ODM inaashiria kwamba huenda Rais Kenyatta atamchagua Bw Odinga kuwa mrithi wake.

Kalonzo na Raila nao wamekuwa wakitofautiana hadharani kuhusu safari ya kuelekea Ikulu 2022.

Kwenye mahojiano na runinga ya NTV, Kalonzo alinukuliwa akisema atakuwa mtu mjinga duniani kuunga mkono Bw Raila Odinga 2022 kuwania urais kwa mara ya tatu.

“Kwa sasa, hata haiwezi ikafirika, mimi Kalonzo Musyoka, nitamuunga Raila Odinga mara ya tatu. Nitakuwa mtu mjinga duniani kumuunga mkono mara ya tatu bila ya yeye kurudisha mkono,” akasema.

Kiongozi huyo wa Wiper alilaumu chama cha ODM kwa kile alitaja kama “usaliti” na kusambaratisha NASA, muungano ambao ulileta pamoja Bw Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetangula (Ford Kenya) kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Mnamo Alhamisi akiwa Mombasa, Bw Odinga alisema hajamuomba yeyote kumuunga mkono na kwamba hajatangaza azima yake ya kuwania urais.

“Sijatangaza mimi nataka kusimama urais, lakini wengine wanasema eti hawawezi kuniunga mkono, nimekuuliza wewe uniunge mkono? Mimi sijatangaza, sasa wewe unaanza kutetemeka, unaanza kubwekabweka, subiri bwana mambo bado,” alisema.

Hata hivyo, muungano unaosukwa kati ya chama chake na Jubilee unaonyesha kuwa atakuwa kwenye debe.

Jana, washirika wa Naibu Rais William Ruto ambao wanaunga chama cha United Democratic Alliance walikejeji muungano wa ODM na Jubilee wakisema ni wa makabila na hauwatishi.

Mikakati ya UhuRaila kutuliza mlima

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, sasa wameanza juhudi mpya kutuliza joto la kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya ili “kuitengenezea mapito” ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Hili ni baada ya kubaini kuwa idadi kubwa ya wenyeji bado hawajaikumbatia ripoti hiyo kikamilifu, hali inayotajwa na baadhi ya waandani wa Rais Kenyatta “kuzua wasiwasi miongoni mwao na rais mwenyewe.”

Hatua hiyo pia inaelezwa kuchangiwa na ripoti za kijasusi kuwa juhudi za serikali kuwatumia maafisa wa utawala wa mikoa kama machifu kujaribu kuipigia debe ripoti vile vile hazijazaa matunda.

Tayari, baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakiipigia debe ripoti wamekimya kabisa huku tetesi zikiibuka kuhusu migawanyiko, usaliti na ushindani katika makundi ya kisiasa ya ‘Kieleweke’ na ‘Embrace.’

Makundi hayo ndiyo yamekuwa yakiandaa mikutano katika maeneo mbalimbali ukanda huo kuipigia debe.

Baada ya barua ya Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a kwa Rais Kenyatta kuhusu ugumu wa kuiuza BBI Mlimani, viongozi wengi wanazidi kujitokeza, miongoni mwao akiwemo Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga.

Kwenye mahojiano wiki hii, Bi Waiguru alionya kuwa huenda mchakato huo ukasam- baratika ikiwa viongozi hawatazingatia umo- ja na kutilia maanani malalamishi ambayo yametolewa na wenyeji.

“Ningetaka kuwashauri wale wanaoende- sha mchakato huu kufahamu kuwa hili ni suala la kisiasa. Lazima pawe na mazingira ya kusikilizana na kuwashirikisha viongozi wote hata ikiwa wana maoni au misimamo tofauti. Ikiwa masuala hayo hayatazingatiwa, basi kuna hatari kubwa juhudi zetu zisifaulu,” akaonya Bi Waiguru.

Duru zinasema hatua hiyo ndiyo ilimfanya Rais Kenyatta kubaini hali si shwari katika ngome yake, na kuamua kuchukua jukumu hilo yeye binafsi.

Inaelezwa uhalisia huo ndio ulimfanya Rais Kenyatta kufanya mahojiano ya pamoja na vituo vya redio vinavyotangaza kwa lugha ya Gikuyu mnamo Jumapili. Kwenye hotuba yake ambayo ilipeperush- wa Jumatatu, Rais Kenyatta aliwarai wenyeji “kunyakua kilicho chao kwanza” kwenye ripoti, badala ya kupewa ahadi ambazo hawajui watatimiziwa lini na wale wanaoipinga.

“Sisi (Mlima Kenya) ndio tutakaonufaika zaidi ikiwa Wakenya wataipitisha ripoti. Huu si mpango wa kumfanyia kampeni ndugu yangu [Raila] kama mnavyoambiwa. Je, Raila ana makao yoyote eneo hili? Acheni kupotoshwa na watu wanaoeneza uwongo,” akasisitiza Rais.

Rais pia alimlaumu vikali Naibu Rais Wil- liam Ruto na kundi la ‘Tangatanga’ akisema hawana sababu zozote maalum kuipinga ripo- ti.

“Hii ni safari ambayo tayari nimeianza na hakuna yeyote ambaye atanizuia kufika ninakotaka,” akaeleza. Wandani wake wa karibu walisema hatua yake kutumia vituo vya redio vya Kameme, In- ooro, Coro na Gukena FM kwa pamoja ilikuwa kuhakikisha ujumbe wake umewafikia watu wengi zaidi.

“Huo ulikuwa mwanzo tu. Rais ataanza kampeni kali kuwafikia wenyeji katika mae- neo ya mashinani ili kujaribu kupunguza uasi uliopo dhidi ya BBI,” akaeleza mshirika mmo- ja wa karibu.

Wadadisi wanasema Rais Kenyatta anaon- ekana kushirikiana na Bw Odinga kwenye juhudi hizo kwani tayari, (Odinga) ameanza kufanya vikao na makundi mbalimbali kuto- ka ukanda huo kama wazee, vijana na akina mama.

Kwenye vikao hivyo, Bw Odinga amekuwa akiwarai wenyeji kuwafikia wenzao kwenye maeneo wanakotoka ili kuhakikisha “ujumbe kuhusu manufaa ya ripoti hiyo unawafikia watu wengi zaidi.”

Mapema wiki hii, Bw Odinga alikutana na ujumbe maalum wa wazee wa jamii ya Agikuyu ulioongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Wazee la jamii hiyo (KCA) Bw Wachira Kia- go katika eneo la Ruaka, Kaunti ya Kiambu. Bw Odinga pia alikutana na wafanyabi- ashara kutoka mtaa wa Githurai (Kiambu) ambapo pia aliwaomba kuiunga mkono ripoti.

Kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa, mbinu hizo mpya za Rais Kenyatta na Bw Odinga zi- nalenga kuhakikisha kuwa wametumia “njia tulivu” kushusha uasi huo.

“Rais Kenyatta hana lingine ila kuhakikisha ngome yake imeiunga mkono ripoti hiyo, kwani Bw Odinga amefanikiwa kudhibiti hali miongoni mwa wafuasi wake. Haina pingam- izi zozote miongoni mwao,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kulingana naye, litakuwa pigo kubwa kwa Rais Kenyatta ikiwa Mlima Kenya itakosa kuunga mkono ripoti, hata ikiwa Wakenya wengine wataipitisha.

“Itakuwa ishara Rais amepoteza udhibiti na ushawishi wa kisiasa miongoni mwa wafuasi wake,” akaongeza Bw Bigambo.

Hata hivyo, Prof Macharia Munene, ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa, anasema ingali mapema kudai kwamba Rais Kenyatta ame- poteza usemi wake eneo hilo. Anasema sababu kuu ni kuwa kampeni ras- mi za BBI bado hazijaanza.

“Ilivyo sasa, Rais Kenyatta bado ndiye mse- maji na kiongozi rasmi wa kisiasa Mlima Ken- ya. Hii ni licha ya mirengo tofauti ya kisiasa ambayo inaendelea kujitokeza. Hali halisi ita- julikana kampeni hizo zitakapoanza,” akasema Prof Munene.

Uhuru hawezi kunisaliti – Raila

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga  amepuuza wanaodai kwamba Rais Uhuru Kenyatta hayuko makini kwa handisheki akisema ana hakika kiongozi wa nchi hawezi kumcheza shere.

Alisema kwamba handisheki yake na Rais Kenyatta ilitokana na mazungumzo ya dhati kati yao na wanaosema kwamba atasalitiwa wanadaganya.

“Tuliketi, tukazungumza kwa muda mrefu kabla ya kusalimiana na Uhuru na hawezi kumsaliti Raila. Tulikuwa wawili, wale ambao walikula kiapa cha urais. Wanaotoa kauli kama hizo ni takataka,” alisema Bw Odinga.

Mnamo Jumamosi, seneta wa Siaya James Orengo alinukuliwa akisema iwapo Jubilee haiko tayari kuadhibu wanaopinga BBI, ODM kiko tayari kuchukua nafasi yake ya upinzani.

Alimlaumu Naibu Rais William Ruto ambaye amekuwa akipinga BBI akisema Rais Kenyatta anafaa kumchukulia hatua kuthibitisha amejitolea kufanikisha BBI.

Akihutubia katika kanisa katoliki la Soweto, mtaani Kayole Nairobi jana, Bw Odinga aliwataka Wakenya wasipotoshwe na Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa wapinge marekebisho ya katiba akisema amezoea kueneza uongo kutimiza maslahi yake ya kisiasa.

Bw Odinga alimtaka Dkt Ruto kutimizia Wakenya ahadi alizowapa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017 kabla ya kupinga BBI.

“Kuna watu wanaoeneza porojo na propaganda kuhusu BBI ili wawapotoshwe, msikubali uongo wao kwa sababu amezoea kudanganya,” Bw Odinga alisema.

Aliwakumbusha Wakenya kwamba Dkt Ruto aliahidi Wakenya kwamba serikali ya Jubilee ingetoa vipatakalishi kwa wanafunzi miezi sita baada ya kuingia mamlakani, kujenga viwanja 47 kote nchini ma kubuni nafasi 1 milioni za kazi kwa vijana ambazo kufikia sasa hajatimiza.

“Wakenya hawajasahau ahadi hizo na kwa hivyo haufai kuwaletea ahadi mpya za wilibaro,” alisema.

Bw Odinga aliwaambia vijana kwamba BBI ina mengi ya kuwafaidi na anachofanya Dkt Ruto ni kuwapotosha ili waikatae wasinufaike.

Alisema uongo wa Dkt Ruto umefika ukingoni. “Vijana hawawezi kunufaika kwa kuendesha wilibaro, tunataka kuona Wakenya wanapata ujuzi mpana waweze kujikimu kimaisha,” alisema.

Waziri Mkuu wa zamani alisema BBI itabadilisha uchumi wa nchi kwa sababu itazima ufisadi ambazo viongozi wamekuwa wakipora na kutangatanga nchini wakichanga pesa za wizi.

Uhuru atoa amri miradi Kisumu ikamilike upesi

Na RUSHDIE OUDIA

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa maagizo mapya ya kukamilishwa kwa miradi ya mabilioni ya pesa katika Kaunti ya Kisumu huku zabuni za ujenzi wa barabara muhimu zikitolewa upya kwa masharti makali.

Kutangazwa upya kwa zabuni hizo kunafuatia changamoto za kupata ardhi, kuhamishwa kwa makaburi na mabadiliko ya miundo yaliyofanya gharama kuongezeka.

Wakandarasi wameagizwa kuhakikisha kwamba miradi hiyo ya thamani ya Sh2.1 bilioni imekamilika kabla ya Novemba mwaka ujao wakati jiji la Kisumu linakapotarajiwa kuandaa kongamano la kimataifa la Afri-cities.

Kamishna wa kaunti hiyo Bi Josphine Ouko akifuata amri ya rais, aliagiza mkandarasi anayejenga daraja la Mamboleo kuhakikisha barabara zitakuwa tayari kufikia Aprili mwaka ujao wakati Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga watakapotarajiwa kufungua uwanja wa kimataifa wa michezo wa Jomo Kenyatta unaojengwa kwa gharama ya Sh1.4 bilioni.

Kulingana na meneja wa eneo hilo wa shirika la barabara kuu nchini (KeNHA), Bw Cleophas Makau Mutua, kuna sababu nyingi na changamoto zinazoweza kucheleweshwa kukamilika kwa miradi hiyo.

“Mkandarasi alisimamisha kazi Juni 4, 2019 kwa kukosa kulipwa kazi aliyokuwa amefanya na baadaye akakatiza kandarasi akibakisha asilimia 50 kukamilisha mradi wenyewe,” alisema Mutua.

Hii imesababisha zabuni ya kukamilisha sehemu iliyobakia kutangazwa upya na kukabidhiwa kampuni ya Zhongmei Engineering Group Limited. Kampuni hiyo italipwa Sh809.9 milioni.

Ilitia saini kandarasi hiyo Septemba 18, 2020 na ikaanza kazi Novemba.Mkandarasi anayejenga barabara ya kilomita 4.5 kutoka shule ya wavulana ya Kisumu hadi Mamboleo ambaye gharama yake ni Sh2.8 bilioni ambayo ilikwama Juni 4, 2019 pia ameagizwa kuikamilisha.

Barabara hiyo ilianza kujengwa Julai 11, 2016.Ilitarajiwa kukamilika Januari 10, 2018, na licha ya muda kuongezwa hadi Disemba 21, 2019, ilikwama baada ya kampuni ya Israeli ya SBI, kusitisha kazi Juni 4, 2019 na baadaye kukatiza kandarasi Septemba 27, 2019 kwa kukosa kulipwa.

Bi Ouko alikuwa akizungumza baada ya kuongoza mkutano wa kamati ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika Kaunti ya Kisumu.

Kaunti hiyo, ambayo ni mojawapo ya ngome kuu za kisiasa za kiongozi wa ODM Raila Odinga, imekuwa ikishuhudia mabadiliko makubwa kimaendeleo katika miaka ya hivi majuzi.

Miradi ya serikali kuu imeshika kasi tangu Rais Kenyatta alipoweka muafaka wa maelewano na Bw Odinga, almarufu handisheki, mnamo Machi 2018 baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Haya yamefanya baadhi ya wadadisi wa kisiasa kutaja miradi hiyo kama ‘matunda ya handisheki’.Mradi mkuu ambao ni ukarabati wa bandari ya Kisumu haujazinduliwa rasmi hadi sasa, licha ya Rais na Bw Odinga kuuzuru mara kadhaa.

Uzinduzi uliotarajiwa uliahirishwa mara nyingi bila sababu mwafaka kutolewa na wahusika.

UGAVANA NAIROBI: Margaret Wanjiru alivyogeuka mwiba kwa UhuRaila

Na CHARLES WASONGA

NI rasmi sasa kwamba uchaguzi mdogo wa ugavana wa Nairobi utafanyika Februari 18 kama ilivyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hii ni baada ya Mahakama Kuu Jumanne jioni kudinda kuzuia tume hiyo kuchapisha notisi kuhusu tarehe ya zoezi hilo na masharti yanayopasa kuzingatiwa na wagombeaji na vyama vyama vitakavyowadhamini.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, kupitia wakili Wilfred Nyamu, alitaka mahakama izuie IEBC kuanzisha mchakato wa kujaza nafasi ya ugavana Nairobi hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.

Alidai sheria ilikiukwa katika hatua zote za kumtimua; kuanzia Bunge la Kaunti ya Nairobi hadi Seneti. Sasa macho yote yanaelekezwa kwa kinyang’anyiro hicho hasusan wagombeaji watakaodhaminiwa na mirengo mikuu ya kisiasa nchini; Handisheki na Tangatanga (au Team Hustler).

Mrengo wa handisheki unashirikisha Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga huku ule wa Tangatanga unaongozwa na Naibu Rais William Ruto ambaye anapania kuingia Ikulu 2022 bosi wake atakapostaafu.

Duru ziliambia jarida la ‘Jamvi la Siasa’ kwamba mrengo wa Jubilee unaongozwa na Rais Kenyatta unapania kutwaa kiti hicho kwa usaidizi wa ODM, kwa moyo wa handisheki.

Chini ya mpango huo, Jubilee itatoa mgombeaji huku ODM ikitoa mgombeaji mwenza, ilivyofanyika wakati wa uchaguzi wa Spika Benson Mutura mnamo Agosti .

Bw Mutura aliungwa mkono na madiwani wa ODM huku Jubilee “ikirudisha mkono” kwa kuunga mkono Diwani wa Baba Dogo Geoffrey Majiwa kutwaa wadhifa wa Naibu Spika.

Wale ambao wanapigiwa upatu kudhaminiwa na mrengo wa Rais Kenyatta na Odinga ni aliyekuwa Mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi Steve Ogolla naye amependekezwa kuwa mgombeaji mwenza wa atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya Jubilee.

Wengine wanaodaiwa kumezea mate kiti hicho kilichosalia wazi baada ya maseneta kuidhinisha hoja ya kumtimu Sonko mamlakani ni aliyekuwa Karani wa iliyokuwa Baraza la Jiji la Nairobi Philip Kisia, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na mfanyabiashara wa Nairobi Agnes Kagure.

Lakini kile ambacho kimewatia mrengo wa handisheki tumbojoto uamuzi wa mrengo wa Tangatanga kumdhamini aliyekuwa Mbunge wa Starehe Askofu Margaret Wanjiru kuwa mgombeaji wake kwa tiketi ya chama chochote kile au hata kama mgombeaji mwenza.

Na kinasemekana kuwakosesha usingizi wapanga mikakati wa kundi la handisheki usingizi na dalili kwamba Askofu Wanjiru, ambaye pia aliwahi kuhudumu kama Waziri Msaidizi wa Nyumba, atapigwa jeki na gavana aliyetimuliwa Mike Mbuvi Sonko.

Kando na kuwa meaneja shupavu mwanasiasa mkakamavu, kiongozi huyo wa Kanisa la Jesus Is Alive Ministries (JIAM) anayo tajriba ya kuwahi kung’ang’ania kiti cha ugavana wa Nairobi 2017 aliposhiriki mchujo wa Jubilee lakini akabwagwa na Sonko.

Isitoshe, kando na ushawishi alio nao kama kiongozi wa kidini, uungwaji mkono atakaoupata kutoka kwa Dkt Ruto, wabunge wa mrengo wa Tangatanga kutoka Nairobi na maeneo mengine utaboresha nafasi yake ya kutwaa kiti hicho.

Kati ya wabunge 17 wa Nairobi mrengo wa wale waliegemea Tangatanga ni watano; James Gakuya (Embakasi Kaskazini), John Kiarie (Dagoreti Kusini), George Theuri (Embakasi Magharibi), Nixon Korir (Langata), James Gathiru (Embakasi ya Kati).

Wabunge tisa wanaegemea mrengo wa handisheki huku Charles Kanyi (Starehe), Nancy Gakuya (Kasarani) na Waihenya Ndirangu (Roysambu) hawajajinasibisha na mrengo wowote.

Wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa Wanjiru na Sonko wataupa mrengo wa handsheki kibarua kigumu zaidi ikizingatiwa kuwa wawili hao wako na ufuasi mkubwa zaidi katika mitaa ya mabanda.

“Ikumbukwe Wanjiru na Sonko wamewahi kuwakilisha maeneo bunge ya Nairobi ambako kuna mitaa mikubwa ya mabanda ambao wakazi wao ndio hujitokeza kwa wingi kupiga kura haswa katika chaguzi ndogo. Wanjiru aliwakilisha Starehe ambayo inajumuisha mtaa wa mabanda wa Mathare, Kiamaiko na Huruma huku Sonko aliwakilisha vitongoji kama Mukuru Fuata Nyayo alipohudumu kama Mbunge wa Makadara na alipata kura nyingi zaidi katika mitaa mingine yenye wakazi wengi alipowania kiti cha useneta na ugavana wa Nairobi. Kundi la handisheki lina kila sababu ya kuhofia wanasiasa kama hawa,” akasema Bw Martin Andati ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

“Ikiwa Rais Kenyatta na Raila hawatapanga kampeni zao vizuri huenda wakapokonywa kiti cha ugavana wa Nairobi walivyopokonywa kiti cha ubunge cha Msambweni na vile vya udiwani vya wadi za Lakeview (Nakuru) na Gitugi (Murang’a),” anaongeza.

Huku akitiwa shime na hamasa na ushindi alioundikisha katika majuzi dhidi ya mgombeaji aliyeungwa mkono na Rais Kenyatta na Bw Odinga (Bw Omar Boga) katika eneo bunge hilo lililoko kaunti ya Kwale, Dkt Ruto anatarajiwa kumwaga wandani wake Nairobi katika jitihada zake za kutwaa kiti hicho.

“Msukumo wa Ruto katika kuwasilisha mgombeaji katika kiti cha ubunge cha Msambweni licha ya chama chake kujiondoa ulikuwa ni kupima kama angali na ushawishi katika eneo la Pwani. Hatachelea kurudia mtihani huo huo katika kaunti ya Nairobi yenye maeneo bunge 17 na zaidi ya wapiga kura milioni mbili kutoka jamii zote nchini. Amefanya chaguo bora la kumuunga mkono Askofu Wanjiru mwenye tajriba na uzoefu katika siasa za Nairobi,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo.

Lakini Mbunge wa Makadara George Aladwa anasema kuwa Askofu Wanjiru sio tisho kwa Uhuru na Raila, akisema kuwa mwanasiasa huyo alishindwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evan Kidero 2017.

Bw Aladwa, ambaye ni mwenyekiti wa ODM kaunti ya Nairobi, anasema mrengo wa handisheki una ushawishi mkubwa katika kaunti ya Nairobi ilivyodhihirika wakati wa shughuli ya ukusanyaji wa saini za kuunga mkono mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

“Ikiwa tuliweza kupata zaidi ya sahihi 500,000 kutoka Nairobi licha ya kundi la Tangatanga wakiongozwa na Ruto (Naibu Rais) kupinga, nini kitatuzuia kuwabwaga katika uchaguzi mdogo Februari 18, 2021?” akauliza mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa Meya wa Nairobi.

Lakini wakili Danstan Omari anatofautiana na kauli ya Aladwa akisema ushawishi wa Rais Kenyatta na Odinga umeshuka zaidi haswa miongoni mwa wapiga kura kutoka jamii ya Wakikuyu ambao ndio wengi Nairobi.

“Kura za Wakikuyu zimemwendea Dkt Ruto ambaye ameanzisha mpango wa kuwasaidia vijana na akina mama kibiashara maarufu kama “Hustler Movement”.

Nao wapiga kura kutoka jamii ya Waluhya ambao wamekuwa wakifaidi kutoka kwa mradi wa “Sonko Rescue Team” watafuata mkondo ambao Sonko atawaelekeza.” anasema Bw Omari ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Lakini Mbunge Maalum Maina Kamanda anasema wapiga kutoka jamii za Waluhya, Kisii na Luo wataunga mkono mgombeaji wa handisheki walivyofanya katika uchaguzi mdogo wa Kibra mnamo Oktoba mwaka jana.

Hata hivyo, inakisiwa kuwa huenda Dkt Ruto akajipata pabaya endapo atajitokeza waziwazi kumuunga mkono Askofu Wanjiru wakati ambapo chama chake, Jubilee, kitakuwa kimedhamini mgombeaji wake.

Naibu Rais ndiye Naibu Kiongozi wa chama hicho tawala.Kwa hivyo, ataonekana kumkaidi kiongozi wa chama chake na bosi wake katika serikali ya Jubilee, hali ambayo inaweza kuchochea shinikizo za kutaka akitimuliwe kupitia hoja bungeni.

Ikumbukwe kuwa mwezi Juni mwaka huu Rais Uhuru Kenyatta alishinikiza kutimuliwa kwa wandani wa Dkt Ruto wote walioshikilia nyadhifa za uongozi katika Seneti na Bunge la Kitaifa, pamoja na kamati za mabunge hayo.

Ilidaiwa kuwa viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen na mwenzake aliyeshikilia wadhifa huo katika bunge la kitaifa Aden Duale, walikaidi misimamo na maongozi ya Jubilee ndani ya nje ya bunge.

Mivutano ya UhuRaila, Tangatanga kuwanyima haki watu wa Kirinyaga

Na CHARLES WASONGA

MCHAKATO wa kuchunguza madai yaliyotolewa dhidi ya Gavana Anne Waiguru na madiwani wa Kirinyaga wanaotaka abanduke tayari umetekwa na mvutano wa siasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Hali hii inatarajiwa kuvuruga haki katika mchakato huo.

Wadidisi wanasema inasikitisha kuwa madai ya ufisadi dhidi ya Bi Waiguru sasa yamegubikwa na siasa za ubabe kati ya mirengo ya ‘handisheki’ na ‘tangatanga’ ilivyodhihiri katika Seneti mnamo Jumanne wakati wa kubuniwa kwa kamati ya kusikiza madai dhidi ya Bi Waiguru.

Maseneta waligawanyika kwa misingi ya mirengo hiyo miwili, ambapo Jubilee na Nasa walitetea kuundwa kwa kamati maalum ya kuchunguza madai dhidi ya Waiguru na ukaibuka mshindi kwa kura 45.

Nao upande uliotaka suala hilo lishughulikiwe katika kikao kizima cha Seneti ulijumuisha wandani wa Naibu Rais William Ruto, ambao walilemewa baada ya kupata kura 14 pekee.

Taswira iliyojitokeza ni kwamba Gavana Waiguru alipata ushindi wa kwanza kutokana na kuwa ni rahisi kwa wanachama 11 wa kamati hiyo “kushawishiwa” kwa urahisi kumtakasa Bi Waiguru.

Kimsingi, suala hilo sasa limechukua mwelekeo wa siasa za kitaifa, wala sio masuala yanayowahusu wakazi wa Kirinyaga, haliambayo itayeyusha masuala muhimu katika hoja hiyo.

Wakili na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa George Ogola, anaonya kuwa uwepo wa mivutano kuhusu suala hilo lenye uzito kwa wakazi wa Kirinyaga itawanyima haki.

“Inasikitisha kuwa tayari kuna madai kuwa makundi haya mawili yalifanya mikutano ya kujadili namna ya kufanikisha malengo yao. Mrengo wa handisheki ulisemekana kukutana kupanga namna ya kumnusuru Waiguru huku wapinzani wao wakipanga namna ya kumsulubisha,” anasema.

Siku chache kabla ya hoja hiyo kusomwa rasmi katika Seneti, Bw Odinga, na wandani wake, waliripotiwa kukutana na Gavana Waiguru katika mkahawa mmoja mtaani Karen kupanga mikakati ya kumwondolea lawama.

Ingawa Bw Odinga alikana ripoti hizo, mwandani wake wa karibu, Junet Mohammed, alitangaza hadharani kuwa chama cha ODM kimeamua “kusimama” na Bi Waiguru bila kujali madai dhidi yake.

Siku moja baada ya mkutano huo, Dkt Ruto naye aliongoza mkutano wa maseneta 16 katika makazi yake rasmi katika mtaa wa Karen, ambapo ajenda kuu ilikuwa na suala lilo hilo la hoja ya kumtimua Bi Waiguru afisini.

Duru kutoka mkutano huo zilisema kuwa Naibu Rais aliwataka maseneta hao, wakiongozwa na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, kuhakikisha kuwa “Waiguru anaangushwa au kuokolewa kwa misingi ya namna atakavyojitetea dhidi ya makosa aliyodaiwa kutenda.”

Wanaodaiwa “kudhamini” msukumo wa kutimuliwa kwa Waiguru mashinani katika kaunti ya Kirinyaga ni pamoja na Naibu wake Peter Ndambiri, Mbunge Mwakilishi wa Wanwake Wangui Ngirici, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho.

Hata hivyo, Dkt Kibicho amekana madai hayo akisema yeye ni mtumishi wa umma na haruhusiwi kushiriki mieleka ya kisiasa.

HANDISHEKI KIZINGITI KWA UTAWALA BORA

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Javas Bigambo anakubaliana na kauli ya Wakili Ogola kwamba misimamo kinzani ya kisiasa ndiyo inatilia shaka uwezekano wa seneti kuishughulikia suala hilo kwa njia huru.

“Madai ya Seneta Orengo kwamba wale wanaotafuta kichwa cha Waiguru hawako katika bunge la kaunti ya Kirinyaga bali wako kwingineko, yalikuwa mazito mno,” anasema Bw Bigambo.

Madai ya Seneta huyo wa Siaya yamewatia hofu madiwani wa Kirinyaga, viongozi wa eneo hilo na mrengo wa Tangatanga ndani na nje ya seneti, kwamba mrengo Rais Kenyatta, Odinga na Kalonzo Musyoka utatumia ushawishi wake kumnusuru Gavana Waiguru.

Hii ndio maana madiwani 23 wakiongozwa na kiongozi wa wengi Kamau Murango walisema hata kama Seneti itamwokoa Bi Waiguru watapambana naye mashinani.

“Tunaweza kuwasilisha hata hoja kumi za kumwondoa mamlakani; hatutachoka,” akasema.

Naye diwani wa wadi ya Mutira David Kinyua Wangui, aliyedhimini hoja hiyo akaongeza: “Ni wazi kwamba kuna njama ya kutupilia mbali uamuzi wetu kama bunge la Kirinyaga. Uhuru na Raila wanafaa kuelewa kuwa hata kama wakimwokoa Waiguru katika Seneti atarudi nyumbani na tutamfunza adabu”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Narc-Kenya Bi Martha Karua, anataja mipango ya kumnusuru Gavana Waiguru kama ithibati kuwa muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga hauna nia ya kusaidfia katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine ya kiutawala.

“Sasa ni wazi kuwa wao ndio kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ufisadi,” anaongeza.

Huku wingu la siasa likigubika mchakato wa kusaka ukweli kuhusu madai dhidi ya Bi Waiguru kupitia Seneti, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeanza kumchunguza gavana huyo na bunge la kaunti ya Kirinyaga kuhusiana na sakata ya upeanaji zabuni na ulipaji marupurupu kinyume cha sheria.

Meneja wa tume hiyo katika eneo la Kati, Charles Rasugu wiki jana aliwaambia wanahabari kuwa malalamishi dhidi ya Bi Waiguru yanahusiana na utoaji wa zabuni ya thamani ya Sh50 milioni na kupokea malipo ya Sh10.6 milioni ya safari hewa ya kigeni.

Watu wa Kirinyaga sasa watasubiri matokeo ya uchunguzi huu wa EACC kupata ukweli kuhusu sakata hiyo kwani mchakato wa Seneti tayari umezamishwa ndani ya bahari ya siasa.

UhuRaila wakejeliwa kwa ‘kutakasa ufisadi’

NA MWANGI MUIRURI

USHIRIKA wa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga chini ya mwavuli wa handisheki umetajwa kama unaolemaza vita dhidi ya ufisadi, huku ukionyesha ubaguzi katika kuandama wezi wa rasilimali za kitaifa.

Katika siasa zinazoendelea katika ung’atuzi wa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Rais na Bw Odinga wamekosolewa pakubwa kwa mapendeleo yao ya wazi ya kukinga baadhi ya washukiwa huku wakiwaandama wengine.

Hii ni baada ya bunge la Seneti kuonekana wazi kuwa lina mirengo miwili ya kisiasa ambayo inamenyana kumzamisha au kumnusuru Bi Waiguru, ule wa handisheki ukionekana wazi kuwa hauzingatii sana ushahidi wa bunge la Kaunti ya Kirinyaga bali unazingatia tu masilahi ya umoja wa Raila na Uhuru.

Tayari, mwandani wa Raila ambaye ni Seneta wa Siaya James Orengo ametangaza kuwa “kesi dhidi ya Waiguru haina msingi bali anawindwa kisiasa na mahasidi wa handisheki. Wanatafuta kichwa cha Waiguru!”

Naye kiranja wa wengi katika bunge hilo la Seneti Irungu Kang’ata ametangaza kuwa “mimi naunga mkono msimamo wa Rais wetu na kinara wetu wa chama cha Jubilee kuwa suala hili la Kirinyaga litatuliwe haraka ili kaunti hiyo itulie.”

Aliyekuwa Waziri wa masuala ya kikatiba na haki, Martha Karua amesema kuwa ushirika huo wa handisheki umepotoka kutoka nia njema ya kuleta amani na utengamano nchini na kugeuka kwanza kuwa mauti kwa demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa na hatimaye kuondoa ule uwajibikaji wa upinzani kuwa nyapara wa utawala wa serikali.

Bi Karua aliye pia kinara wa chama cha Narc-Kenya aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kwa sasa hakuna uwezekano wa ushirika huo kuwafaa Wakenya na uchumi wao katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine ya kiutawala.

Alisema kuwa “wawili hawa wamekuwa wakidai kuwa idara ya mahakama ndiyo imekuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ufisadi, lakini kwa sasa ni wazi kuwa hata katika fikira na utendakazi wa wawili hawa, hata wao ni visiki katika vita hivi.”

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alisema kuwa kuna visa kadhaa ambapo akiwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu bajeti alipata shinikizo za kutengea miradi ghusi pesa za kimaendeleo kutoka mrengo wa Handisheki.

“Kuna wizara za mawaziri wa handisheki ambazo zilikuwa zinasukuma pesa za kimagendo kutengewa miradi yao…Mimi nilikuwa nikikataa na mojawapo ya miradi hiyo ya ukora ni kuhusu utapeli wa shamba la Ruaraka ambapo Wizara ya Elimu ikiwa kwa wakati mmoja mikononi mwa Dkt Fred Matiang’i  ambapo hadi sasa hakuna taasisi inayofuatilia kesi hii kwa kuwa huyu Matiang’i ni wa Handisheki,” akasema.

Ni msimamo ambao ulitiliwa mkazo na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen aliyesema kuwa “vita dhidi ya ufisadi kwa sasa ni silaha ya kisiasa mikononi mwa baadhi ya mirengo ya kisiasa.”

Amesema kuwa wale ambao humuunga mkono naibu wa Rais Dkt William Ruto wakisingiziwa ufisadi huwa wanasukumwa mbio hadi nje ya nyadhifa huku wale wa handisheki wakiwa sasa na idhini rasmi ya kutapeli, kufuja, kuiba na kufisadi watakavyo kwa kuwa wako katika kambi ya wadosi.

Alisema kuwa Raila amekuwa akijipendekeza kama mpiganiaji wa haki za Wakenya na utawala bora lakini “amegeuka kuwa wa kutakasa wale ambao wamehusishwa na ufisadi bora tu watangaze kuwa wanamuunga mkono.”

Alisema kuwa Raila ameambukiza Uhuru msimamo huo dhidi ya ufisadi ambapo “ukionekana kuwa unaunga mkono muungano wa handisheki bila masharti, unatakaswa katika idara za kuchunguza ufisadi.”

Katika hali hiyo, Murkomen aliteta kuwa watu wa Kirinyaga sawia na wengine ambao wako katika mirengo tofauti ya kisiasa waelewe kuwa “vita dhidi ya ufisadi ni kwa wale ambao watakataa kujumuishwa katika mrengo mmoja wa kisiasa hapa nchini kwa lazima.”

Aliyeandaa mswada wa kumng’atua Bi Waiguru katika bunge la Kirinyaga, Kinyua wa Wangui alisema kuwa “mimi sitaki kuhusika kamwe na ukora na unafiki huu ambao umeonekana katika bunge la Seneti.”

Alisema kuwa “ni wazi kuwa kumeandaliwa njama ya kutupuuza kama bunge la Kaunti na Uhuru na Raila wanafaa waelewe kuwa hata wakimwokoa Waiguru katika Seneti, bado atakuja hapa Kirinyaga na tutawafunza adabu za kutuheshimu.”

Kiranja wa bunge hilo la Kirinyaga Pius Njogu alisema kuwa “huu ni utawala wa giza, ushirikiano wa hujuma na uliojaa unafiki wa kupambana na vita dhidi ya ufisadi,” huku aliyekuwa kiranja wa wengi, Kamau Murango akisema kuwa “Uhuru na Raila hawajaonyesha nia ya kuwa na uwazi dhidi ya kupambana na ufisadi.”

Uhuru amtembeza Raila jijini usiku

Na BENSON MATHEKA

Yaonekana Jumatatu ilikuwa siku ya Rais Uhuru Kenyatta kuyafurahisha makundi mawili hasimu ya kisiasa yanayounga mkono kinara wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Mchana baada ya kushiriki maadhimisho ya Sikukuu ya Madaraka ambapo alitagusana na naibu wake, Dkt Ruto kwa bashasha na uchangamfu, usiku ilikuwa zamu ya Rais kumtembeza Bw Raila kwenye gari lake jijini Nairobi.

Rais Uhuru na waziri huyo mkuu wa zamani waliwagutusha Wakenya walipoamua kutembelea barabara za jiji la Nairobi usiku wakati wa kafyu.

Ziara hiyo iligunduliwa baada ya video iliyonaswa na kamera za usalama kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwenye video hiyo, gari moja linaonekana likisimama kwenye barabara ya Kenyatta Avenue kabla ya Rais Kenyatta kushuka kutoka kiti cha dereva na kufuatwa na Bw Odinga anayeshuka kiti cha mbele kando ya dereva.

Bw Odinga anaungana naye kando ya barabara huku maafisa kadhaa wa kikosi cha ulinzi wa rais wakikaa chonjo kuhakikisha usalama.

Magari mengine mawili yanayoaminika kuwa ya walinzi wa rais yanafika na kusimama nyuma ya gari ambalo viongozi hao wawili walishuka.

Video hiyo pia inaonyesha afisa wa usalama aliyejihami kwa bunduki akishika doria kwenye barabara hiyo.

Viongozi hao wawili wanaonekana wakitembea kwa miguu ishara kwamba huenda walikuwa wakikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika la Huduma la jiji la Nairobi na viunga vyake (NMS) ambalo Rais Kenyatta alibuni kufuatia mkataba wake na Gavana Mike Sonko wa kuhamisha majukumu hadi serikali ya kitaifa.

Wawili hao wanaonekana wakitembea huku magari hayo yakiwafuata. Ziara hiyo pia ilimpa Rais fursa ya kubaini iwapo marufuku ya kutotoka nje usiku yalikuwa yakitekelezwa jijini.

Ingawa video hiyo haionyeshi tarehe iliyonaswa, inaaminika kuwa ilikuwa Jumatatu usiku baada ya sherehe za Madaraka Dei zilizofanyika ikulu ya Nairobi.

Kuonekana kwao pamoja katika barabara za Nairobi kunaonyesha ukuruba wao tangu handisheki yao ya Machi 9 2019, umeendelea kuimarika. Kabla ya kufika barabara ya Kenyatta Avenue, wawili hao walikuwa wametembelea sehemu kadhaa za katikati mwa jiji.

Baadhi ya walinzi walisema waliona msafara wa magari matatu katika barabara ya Waiyaki.

Walinzi wa usiku katika barabara za jiji ambao hawakutaka majina yao yachapishwe walisema wawili hao walionekana wachangamfu wakikagua hata mitaro ya maji taka na taa za barabarani.

Rais Kenyatta amekuwa akifanya ziara za ghafla kukagua miradi ya maendeleo lakini hajawahi kuonekana na Bw Odinga katika barabara za Nairobi usiku.

Amewahi kutembelea Kaunti ya Nyeri kukagua ukarabati wa reli na akatembelea uwanja wa Nyayo kukagua maandalizi ya uwanja huo wakati wa ibada ya wafu ya hayati Daniel Moi.

Aliwahi kuzuru bandari ya Kisumu akiwa na Bw Odinga bila kutarajiwa.

Mapema siku hiyo, kiongozi huyo wa nchi alikuwa pamoja na Naibu Rais katika sherehe za Madaraka, hali iyozua furaha miongoni mwa wafuasi wa Dkt Ruto waliodhani Uhuru alikuwa na mpango wa kumsaliti mdogo wake serikalini.

Hata hivyo, matukio hayo mawili yanashadidia kauli ya Rais kuwa nia yake ni kuunganisha taifa badala ya kuligawanya.

ONYANGO: Raila atumie ukuruba na Uhuru kuleta mageuzi

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa Wengi Bungeni Aden Duale amegonga ndipo kwa kuhimiza Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kutekeleza ripoti ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC).

Wito huo wa Bw Duale umeshutumiwa vikali na wakosoaji wake kwa sababu amekuwa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa Jubilee ambao wamekuwa wakipinga kutekelezwa kwa ripoti ya TJRC kutokana na kigezo kwamba itatonesha vidonda vya zamani.

Hata hivyo, wito huo wa Bw Duale unastahili kukumbatiwa na wanasiasa wote kutoka Jubilee na mrengo wa Upinzani; kuhakikisha kuwa ripoti hiyo ambayo imetelekezwa tangu 2013 inatekelezwa kikamilifu.

Rais Kenyatta alipokuwa akihutubia bunge la kitaifa mnamo 2015, aliomba msamaha kwa dhuluma zilizotekelezwa na serikali za marais waliomtangulia.

Katika hotuba yake kwa taifa mnamo 2017, Rais Kenyatta aliagiza Bunge kujadili ripoti hiyo. Lakini baadaye chama cha Jubilee kiligeuka na kusema kuwa utekelezwaji wa ripoti hiyo utazua uhasama dhidi ya baadhi ya jamii.

Kutekelezwa kwa ripoti ya TJRC ni miongoni mwa ajenda kuu ambazo Bw Odinga aliahidi kutekeleza endapo angefanikiwa kuingia Ikulu katika uchaguzi wa Agosti 8, mwaka jana.

Bw Odinga pia aliahidi kutoa elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, kurejeshwa kwa maziwa kwa wanafunzi, kupunguzwa kwa kodi ya nyumba, kuwapunguzia wananchi gharama ya maisha, kuhakikisha wazee wanapata msaada wa fedha kila mwezi kati ya ahadi nyinginezo.

Wiki iliyopita, Bw Odinga katika mahojiano na runinga moja ya humu nchini alifichua kuwa siku hizi anakemea na kuripoti sakata za ufisadi kwa kumpigia simu Rais Kenyatta.

Bw Odinga alisema tangu kutia saini mwafaka wa ushirikiano na Rais Kenyatta amesitisha mbinu yake ya zamani ambapo aliita wanahabari kufichua sakata ya ufisadi na badala yake anampigia simu Rais Kenyatta moja kwa moja.

Ni kweli kwamba Rais Kenyatta ameorodhesha miradi yake mikuu minne; ujenzi wa nyumba nafuu, matibabu bora ya gharama ya chini, uboreshaji wa viwanda na uzalishaji wa chakula cha kutosha, anayopanga kushughulikia kabla ya kustaafu 2022.

Lakini, Bw Odinga anaweza kutumia ukuruba wake na Bw Odinga kushinikiza kutekelezwa baadhi ya ahadi alizotoa mwaka jana kama vile kutekelezwa kwa ripoti ya TJRC, elimu ya bure kutoka shule za msingi hadi sekondari, kupunguza kodi ya nyumba kati ya ahadi nyinginezo.

Baadhi ya ahadi zilizotolewa na Bw Odinga zinaingiliana na miradi minne mikuu inayoshughulikiuwa na Rais Kenyatta.

Kwa mfano, kupunguza kodi ya nyumba inaingiliana na mradi wa Rais Kenyatta wa kutaka kujenga nyumba za bei nafuu.

Mudavadi adai Raila aliwaficha kuhusu muafaka

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, ameibua shaka kuhusu kama Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga alikuwa mwaminifu kwa vinara wenzake wa NASA kabla aungane na serikali.

Kulingana na Bw Mudavadi, uamuzi wa Bw Odinga kushirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta uliashiria kuwa wawili hao walikuwa wakishauriana kwa muda mrefu bila vinara wengine wa NASA kujua.

“Hakuna jinsi angechukua hatua aina hii ghafla. Ni wazi mipango hiyo ilikuwa ikiendelezwa kwa muda mrefu ilhali mimi kibinafsi sikufahamu,” akasema kwenye mahojiano Jumapili usiku katika Runinga ya NTV.

Kwenye mahojiano tofauti, Bw Odinga amewahi kuthibitisha kuwa hatua yake kushirikiana na Rais Kenyatta ilikuwa siri yao wawili ingawa haifahamiki walikuwa wakishauriana kwa muda gani.

Waziri huyo mkuu wa zamani pia amekuwa akikosolewa na wenzake wanaodai alienda kula kiapo kuwa ‘rais wa wananchi’ katika uwanja wa Uhuru Park walipokuwa wakimsubiri kwingine.

Bw Mudavadi alimwonya Bw Odinga na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu ushirikiano wao na serikali akasema hatafuata mkondo huo bali chama chake kitatekeleza majukumu ya upande wa upinzani nchini.

Kulingana na makamu huyo wa rais wa zamani, hakuna ubaya kwa viongozi wa pande tofauti za kisiasa kushirikiana lakini kuna hatari kubwa wakati ushirikiano huo unapotishia kuangamiza upinzani.

“Hatufai kuonekana kwamba sote sasa tunafululiza kujiunga na serikali. Jubilee inakumbwa na matatizo mengi serikalini na hatustahili kuwa washirika wake katika makosa inayofanya,” akasema.

Wiki iliyopita, Bw Musyoka alitangaza kuwa wanachama wa Wiper walikubaliana kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, na wabunge wake wakaagizwa kuunga mkono ajenda za serikali wakiwa bungeni.

Hata hivyo, Bw Mudavadi alisema uamuzi wake haumaanishi amekosana na Bw Odinga kwani wote wana haki ya kuchukua misimamo tofauti kisiasa.

Alisema muafaka ulikuwa muhimu kutuliza taharuki nchini lakini haamini una uwezo wake kuleta mabadiliko ikizingatiwa kuwa Bw Odinga aliwahi kuchukua hatua sawa na hiyo wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 alipoungana na aliyekuwa rais Mwai Kibaki.

“Muafaka wa 2007/2008 ulitokana na wizi wa kura. Wakati huu pia ulitokana na uchaguzi tatanishi. Ni wazi katika ile miaka mitano changamoto iliyokuwepo haikutatuliwa. Sasa mwaka mmoja umekamilika na hatuoni kama kuna juhudi za kusuluhisha mizozo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka,” akaeleza.

Kuhusu uchaguzi ujao wa 2022, Bw Mudavadi alisema si lazima aungwe mkono na Bw Odinga wala kinara mwingine yeyote wa NASA ili ashinde urais bali atajitahidi kushawishi wananchi kuhusu uwezo wake wa kuongoza taifa.

Kumekuwa na fununu kwamba vinara wa muungano huo walikubaliana kumuunga mkono Bw Odinga kwa msingi kuwa atamuunga mkono mmoja wao 2022, ingawa ODM husisitiza kitakuwa na mgombeaji wake wa urais.

TUNARUDI TENA CHAMA KIMOJA? Demokrasia hatarini

Na BENSON MATHEKA

Kenya inarejea taratibu katika utawala wa chama kimoja kufuatia matukio ya hivi majuzi ya wanasiasa kujiunga na Serikali.

Dalili zaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka minne ijayo, kuna hatari ya kurudisha nyuma maendeleo ya demokrasia ya vyama vingi ambayo Wakenya wamekuwa wakifurahia kwa miaka 26 iliyopita.

Tangu Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga asalimiane na Rais Uhuru Kenyatta, wanasiasa wa upinzani wamefuata nyayo na kukubali kuunga serikali ya Jubilee.

Siku mbili kabla ya muafaka wa Rais Kenyatta na Raila, Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye ni mwandani wa Rais, alibashiri kuwa Kenya itakuwa chini ya utawala wa chama kimoja kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Kufikia Desemba 2018, Kenya itakuwa demokrasia ya chama kimoja,” aliandika Bw Kuria kwenye ukurasa wake wa Facebook bila kufafanua.

Hali hiyo inaendelea kujitokeza na kufikia wakati huo, vyama vikubwa vya kisiasa vitakuwa kwa jina tu bila uwezo wa kukosoa serikali kama ilivyo katika nchi za Rwanda na Uganda.

Japo viongozi wa vyama hivyo wanasisitiza wangali katika upinzani na wanachounga ni vita dhidi ya ufisadi na Ajenda Nne Kuu za Maendeleo pekee, dalili ni wazi kuwa wanaelekea serikalini.

Raila mwenyewe amekoma kukosoa serikali na amenukuliwa akisema ni kwa sababu anawasiliana moja kwa moja na Rais Kenyatta. Wabunge wa chama chake cha ODM wamechukua misimamo ndani ya chama cha Jubilee, baadhi wakimuunga Rais Kenyatta na wengine wakimuunga Naibu Rais William Ruto.

Chama cha Wiper ambacho pamoja na ODM, Ford Kenya na Amani National Congress vinaunda muungano wa upinzani wa NASA, pia kimetangaza kushirikiana na serikali na kuna fununu kwamba huenda kiongozi wake Kalonzo Musyoka akapatiwa wadhifa mkubwa serikalini.

Baada ya Wiper kutangaza kuwa kitashirikiana na serikali, kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula alijitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani, hatua ambayo wadadisi wanasema ni kejeli.

“Wetangula amekaribia serikali kama vinara wenzake katika NASA. Tofauti yake na Bw Odinga na Bw Musyoka ni kuwa, anaegemea upande wa Naibu Rais William Ruto katika chama cha Jubilee,” alisema mbunge mmoja kutoka Rift Valley ambaye hakutaka kutajwa jina.

Siku tatu baada ya Wiper kutangaza kuwa kitashirikiana na serikali, Bw Musyoka alimwalika Bw Wetangula katika kilichotajwa kama juhudi za kumshawishi kufuata nyayo za vinara wenzake.

Duru zinasema kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi huenda akapatiwa wadhifa mkubwa serikalini hatua ambayo huenda ikamvuta Wetangula upande wake iwapo juhudi za kuunganisha vyama vyao zitafaulu.

Bw Mudavadi amekubali kuunga vita dhidi ya ufisadi na Ajenda Nne za Maendeleo za Serikali ya Jubilee na iwapo atapatiwa wadhifa serikali hataweza kukosoa serikali.

Kulingana na Profesa David Monda wa City University, New York kurejea kwa utawala wa chama kimoja kwa hali yoyote ni hatari.

“Ni suluhu mbadala na hatari kwa tofauti za kisiasa Kenya,” asema.

OBARA: Twahitaji muujiza wa pili ili mwafaka ufanikiwe

Na VALENTINE OBARA

Baada ya kusubiri kwa miezi mitano, hatimaye mojawapo ya malengo makuu ya muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga imeanza kutekelezwa.

Kamati maalum iliyobuniwa na wawili hao tayari imetoa wito kwa wananchi kuwasilisha maoni yao kuhusu jinsi ya kupambana na ufisadi.

Ingawa hii ni hatua bora katika kuendeleza mbele malengo ya muafaka huo, kuna wasiwasi kwamba kamati hii huenda ikaishia tu kuwa kama zingine nyingi ambazo zimewahi kuwepo katika miaka iliyopita.

Kenya imekuwa maarufu kwa uundaji wa kamati na majopokazi chungu nzima kila mara tunapokumbwa na changamoto mbalimbali lakini kinachosikitisha ni kuwa, ripoti zinazotolea huwa hazitekelezwi.

Hii ni licha ya kuwa kamati hizo hutumia rasilimali za umma kuendeleza shughuli zao ikiwemo kutumia fedha zinazotoka katika kapu linalofadhiliwa na mlipaushuru.

Hakika, masuala mengi ambayo Bw Odinga na Rais Kenyatta walitaja kuwa changamoto wanazolenga kutatua yamewahi kuchunguzwa.

Mfano ni suala kuhusu utendaji wa haki sawa kwa kila mwananchi bila kujali kabila, tabaka wala misimamo ya kisiasa.

Hili ni jambo ambalo lilichunguzwa kwa kina mno na Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) ambayo ilitumia muda na rasilimali tele za umma kuzunguka nchini kote kushauriana na wananchi.

Tume hiyo ilikusanya malalamishi na maoni ya Wakenya hasa kutoka jamii zilizokuwa zimekandamizwa kihaki katika tawala zilizopita.

Utoaji wa ripoti ya tume hiyo ulikumbwa na utata kwa kuwa ilitoa mapendekezo yaliyoshutumu watu mashuhuri nchini kwa kudhulumu haki za raia wa kawaida.

Hatimaye ripoti ilipotolewa, kulikuwa na minong’ono kwamba haikuwa ripoti halisi bali ilifanyiwa ukarabati. Hata hivyo, ripoti hiyo iliyotolewa haijatekelezwa kufikia sasa.

Masuala mengine mengi ambayo yamewahi kuchunguzwa na kamati tofauti ni kuhusu mauaji ya kikatili ya raia na pia ya viongozi mashuhuri, mbali na suala sugu la unyakuzi wa ardhi.

Kwa mtazamo wangu, kamati iliyobuniwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga haingepoteza muda mwingi ila kurejelea ripoti hizo zote na kupendekeza kinachofaa kutekelezwa kutoka kwazo.

Kuna hatari ya kamati hii kutumia muda na rasilimali tele kisha mwishowe ije na mapendekezo yale yale ambayo yamewahi kuwasilishwa kwetu.

Wakifanya hivyo, natumai malaika aliyetenda muujiza wa kuwapatanisha viongozi hao wawili kisiasa atakuwa bado anatembeatembea humu nchini ili atende muujiza mwingine wa kufanya ripoti itakayotolewa itekelezwe kikamilifu.

Bila hilo, tujiandae tu kurudi uchaguzini 2022 tukiwa tungali tumebeba mzigo huu mzito wa matatizo ya ufisadi, ukiukaji wa haki za kibinadamu, dhuluma za kikabila miongoni mwa mengine.

Tuna nafasi bora ya kupata mabadiliko ambayo yatasaidia kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida lakini hilo litawezekana tu kama viongozi wetu watajitolea kuweka kando maslahi yao ya kibinafsi kwa muda.

JAMVI: Hatari ya mwafaka wa Uhuru na Raila kuvunjika

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wanafaa kudumisha mwafaka wao ili nchi isitumbukie kwenye ghasia ukivunjika.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Nairobi anasema kwamba kuvunjika kwa mwafaka huo kunaweza kurejesha ghasia nchini.

“Iwapo mwafaka huo utavunjika, ninabashiri ghasia. Kinyume na wengi  wanavyofikiri, hasira ya wafuasi wa NASA inaweza kuchipuka upya na kwa haraka,” alisema Bw Manyora kwenye maoni yaliyochapishwa katika tovuti ya gazeti moja nchini.

Kulingana na Bw Manyora, wafuasi wengi wa upinzani hawana imani mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Raila. “Kwa hivyo, kiwango cha ghasia na hasira zizoweza kuthibitiwa kinaweza kurudi moja kwa moja,” alisema.

Mchanganuzi huyo anasema ni hatua ya Bw Odinga, kusalimiana na Rais Uhuru iliyofanya nchi kurejea katika utulivu. “ Iwapo Uhuru anaweza kusaliti kusalimiana kwao, kwa sababu ndiye aliye na nguvu za kufanya hivyo, Raila atapungukiwa na nguvu kisiasa,” anasema Bw Manyora.

Hata hivyo, anaeleza kuwa ni rahisi kwa Raila kubuni mikakati mipya na kurejea kwa nguvu katika uga wa siasa. “ Tatizo ni akiamua kuachana na siasa, kutakuwa na shida,” anasema.

“Bila kinara wa kuongoza upinzani, hasa vijana, kinara wa kuelekeza na kutuliza hasira, ghasia  haziepukiki,” anaeleza.

Kwa hivyo, anaeleza, ni lazima tujitolee kwa kila hali kufanikisha mwafaka huu kwa sababu usipokuwepo, ni hatari. Kuna dhoruba za hasira katika nchi hii, dhidi ya utawala wa Jubilee, dhidi ya (Rais) Uhuru Kenyatta.

Tunahitaji kiongozi anayeweza kutuliza hasira hizo, hasira zikikosa kuthibitiwa, nchi hii inaweza kubadilika kuwa kitu tofauti,” anasema.

Anatoa mfano wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo imevurugika kwa sababu ya vita vya ndani kwa ndani vilivyosababishwa na tofauti za kisiasa. Nchi hiyo ni moja ya zile masikini ulimwenguni.

Bw Manyora anakumbusha Wakenya kwamba kusalimiana kwa Rais Kenyatta na Bw Raila kulirejesha amani mara moja nchini.

“Mara tu waliposalimiana, amani ilirejea, biashara zikanawiri na upinzani ukamtambua Uhuru Kenyatta kama rais wa Kenya. Haya yote yanaweza kuwa hatarini mwafaka huo ukivunjika,” alionya.

Anaeleza kwamba kuvunjika kwa mwafaka huo kunaweza kuathiri pande zote mbili. “ Baadhi wanasema sifa na maisha ya kisiasa ya Bw Raila yataharibika kiasi cha kutorekebika.

Wanasema alivunja uhusiano wake na wenzake katika upinzani alipowatenga. Lakini pia Jubilee itakuwa na wakati mgumu kurejesha imani yake kwa wafuasi iwapo mwafaka utafeli,” anaeleza

Sura mpya ya ‘Baba’ baada ya salamu

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga amechukua sura mpya tangu Machi 9, 2018 alipoamkuana na Rais Uhuru Kenyatta. Alibadilika ghafla na sasa si tena kigogo wa upinzani aliyefahamika Afrika na duniani kote kwa ukakamavu wa kisiasa.

Tofauti na awali alipokuwa mkosoaji mkuu wa serikali, Bw Odinga ameacha kulaumu serikali, amepunguza mikutano yake na wanahabari na kueleza kauli zake katika mitandao ya kijamii.

Pia amejitenga na wanasiasa wa upinzani na washirika wake waliokuwa na misimamo mikali kama yeye. Badala yake, ratiba yake imekuwa ya kuwapokoea mabalozi, makundi ya wazee na wakosoaji wake wa zamani kama vile Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Kabla ya kuamkuana na Rais Kenyatta, Bw Odinga alikuwa mstari wa mbele kukashifu Serikali kwa kukopa sana kutoka nchi za kigeni kwa kile alichokuwa akionya kuwa hatua hatari kwa uchumi. Lakini majuzi Serikali ilipokopa mabilioni ya pesa za Eurobond, Bw Odinga hakusema chochote.

Amekuwa msiri hivi kwamba kufikia sasa, hakuna anayefahamu aliyokubaliana na Rais Kenyatta isipokuwa taarifa ya pamoja waliyotoa kwa Wakenya hapo Machi 9 walipotangaza mwafaka.

Jumanne, Bw Odinga aliambia mkutano wa Baraza Kuu la ODM kwamba hivi karibuni yeye na Rais Kenyatta wataandaa misururu ya mikutano kote nchini kuelezea yaliyomo kwenye mkataba wao wa maelewano (MOU).

Kiongozi huyo pia amekuwa kimya kuhusu masuala mengine ambayo hapo awali angekuwa amezungumzia.

Haya ni kama vile juhudi za Serikali kukabiliana na mafuriko ambayo yamekumba maeneo mengi ya nchi ambapo hatua za kusaidia waathiriwa zimeonekana kutotosha.

Hajasema chochote kuhusu ukosefu wa usalama eneo la Kapendo katika mpaka wa Turkana na Baringo ambapo watu watano waliuawa majuzi.

Pia hajazungumzia mauaji ya wanajeshi 8 wa KDF katika eneo la Dhobly nchini Somalia mnamo Jumatatu, licha ya msimamo wake wa awali kuwa wanajeshi hao waondolewe Somalia.

Kabla ya Machi 9, Bw Odinga pia alikuwa mwepesi wa kuitisha vikao vya wanahabari mara kwa mara katika ofisi yake ya Capitol Hill Square ambapo alikuwa akikosoa serikali.

Baada ya kusalimiana na Rais Uhuru Kenyatta vikao vyake na wanahabari vimepungua na mtindo wake siku hizi ni kutuma taarifa moja moja kwa vyombo vya habari kupitia kwa msemaji wake Dennis Onyango.

Jumanne, Raila aliambia wajumbe wa ODM kwamba analenga kuona Kenya mpya katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

 

 

 

Niko tayari kuungana na UhuRaila kuunganisha Wakenya – Kalonzo

Na FRANCIS MUREITHI

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema yuko tayari kujiunga na Rais Uhuru Kenyatta katika juhudi za kuunganisha Wakenya na kuzika siasa za mgawanyiko.

Bw Musyoka alipongeza hatua ya Rais Kenyatta kuanza mikakati ya kuunganisha Wakenya kwa ushirikiano na kinara wa NASA Raila Odinga mnamo Machi 9, mwaka huu.

Bw Musyoka pia alimpongeza rais kwa kuomba msamaha kwa kutoa matamshi ya kugawanya Wakenya wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2017.

Makamu huyo wa rais wa zamani, alisema hayo alipokuwa akihutubia wanahabari katika hoteli moja eneo la Elementaita, Nakuru wakati wa kufunga kongamano la siku mbili la viongozi wa Wiper.

“Ningependa kumpongeza Rais Kenyatta kwa kujitokeza wazi na kuomba Wakenya msamaha. Ni viongozi wachache mno wanaoweza kunyenyekea na kuomba wananchi msamaha. Nimempa hongera kwa hilo. Huu ni wakati wa kusamehe na kuhubiri amani,” akasema Bw Musyoka.

 

Kukutana na Mzee Moi

Bw Musyoka alisema anapanga kukutana na Rais Mstaafu Daniel arap Moi hivi karibuni.

“Ninapanga pia kumtembelea Rais Mstaafu Mwai Kibaki na mama yake rais, Mama Ngina Kenyatta,” akasema Bw Musyoka.

Bw Musyoka alimkejeli Naibu wa Rais William Ruto ambaye juhudi zake za kukutana na Mzee Moi ziligonga mwamba wiki iliyopita.

“Walioshindwa kumwona Rais Mstaafu Moi wajaribu tena,” akasema Bw Musyoka huku akisababisha kicheko.

Alisema mwafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unastahili kuleta maendeleo na wala si kusuluhisha mizozo ya kisiasa tu.

Alisisitiza kuwa muungano wa NASA bado ni thabiti huku akisema kuwa atashinikiza NASA isajiliwe kama chama cha kisiasa. Alisema Bw Odinga hajajiunga na chama cha Jubilee na bado yuko katika Upinzani.

Alisema kabla ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kusalimiana, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kushinikiza viongozi hao wawili wakutane ili kuzungumza.

“Nilikuwa katika mstari wa mbele kuwataka Rais Kenyatta na Bw Odinga wakutane na kusitisha siasa za mgawanyiko. Inaonekana Bw Odinga alisikia wito wangu na akakubali kukutana na Rais Kenyatta japo hakunifahamisha,” akasema Bw Musyoka.

“Chama cha Wiper kiko tayari kuanzisha mchakato wa kuunganisha nchi na kuhubiri amani,” aliongeza.

Bw Musyoka pia alisema anaunga mkono Katiba kufanyiwa mabadiliko.

“Niliitwa tikitimaji kwa sababu nilisema kuwa Katiba ilifaa kuangaliwa kwa makini. Sasa Wakenya wameona umuhimu wa niliyosema.

Chama cha Wiper kinaunga mkono mabadiliko ya Katiba na tunafaa kujadili suala hili kwa makini,” alisema Musyoka.

MUAFAKA: Orodha ya Uhuru na Raila yapingwa vikali

Na WAANDISHI WETU

UAMUZI wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga kuteua jopokazi la watu 14 kuwashauri kuhusu jinsi ya kuleta umoja wa kitaifa, umekosolewa kwa “kukosa uwakilishi unaostahili.

Viongozi mbalimbali jana walisema jopo lililotangazwa Jumapili halina wawakilishi wa vijana, dini tofauti na pande nyingine muhimu za kisiasa.
Kwa hivyo, wanaamini kuwa hilo ni kundi la kutaka kutekeleza maslahi ya wawili hao pekee, wala si ya taifa zima kama ilivyotarajiwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu wa Kenya (CIPK) tawi la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, Sheikh Abubakar Bini, alisema ingawa awali Rais Kenyatta na Bw Odinga walionyesha nia njema kwa kushirikiana, hatua ya kuacha makundi mengine nje kwenye jopokazi hilo haifai.

“Jinsi ilivyo kwa sasa, kikundi hicho hakina sura ya Kenya katika uwakilishi wa kidini kwani Wakristo pekee ndio wanaowakilishwa. Je, hii itaunganisha Wakenya au kuwagawanya?” akasaili kwenye kikao cha wanahabari mjini Eldoret.

Wazee wa jamii za Bonde la Ufa pia walipinga jopo hilo na kusema halitasiaidia taifa. Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bw Gilbert Kabage, walishangaa kwa nini Naibu Rais William Ruto anatengwa katika mashauriano hayo.

“Hatufurahishwi na jinsi Bw Ruto anavyotengwa katika hatua hizi. Sisi tunamfuata Bw Ruto na tumeghadhabishwa na mambo hayo,” akasema akiwa Nakuru.

Wakizungumza bungeni, Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw Cleophas Malala, na Mbunge wa Butere, Bw Tindi Mwale, ambao ni wanachama wa ANC, walisema vijana walitengwa.

“Inavunja moyo kwamba viongozi hao wawili wa heshima hawakuona sababu ya kujumuisha vijana katika kikundi cha kuleta umoja. Ingawa ninaunga mkono walivyojitolea kuleta upatanisho, ninatoa wito kwao wazingatie kujumuisha vijana,” akasema Bw Malala.

Hata hivyo, chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga kilitetea hatua hiyo na kusema wale waliochaguliwa ni mchanganyiko wa wazee wa kijamii, wasomi, viongozi wa dini na wataalamu wenye misimamo thabiti.

“Kikundi hicho ni kizuri. Hakina watu wenye maazimio ya kibinafsi, kwa hivyo hakitasababisha migawanyiko na kitajitolea kuimarisha uwiano kikiungwa mkono,” akasema Mbunge huyo wa Suba Kusini.

Malalamishi pia yalienea kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutoka kwa vijana ambao walishangaa kama kazi yao katika masuala ya uongozi huishia katika kampeni za uchaguzi na upigaji kura.

Miongoni mwa waliochaguliwa ni Seneta wa Busia, Bw Amos Wako, mwenzake wa Garissa, Bw Yusuf Haji na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Samburu, Bi Maison Leshomo.

Wengine ni Dkt Adams Oloo, Bi Agnes Kavindu, Bi Florence Omose, Prof Saeed Mwanguni, Mzee James Matundura, Meja Mstaafu John Seii, Bw Morompi ole Ronkai na Bi Rose Museu. Viongozi wa kidini waliochaguliwa ni Askofu Lawi Imathiu, Peter Njenga na Zacheus Okoth.

Kuria apokelewa vizuri Nyanza baada ya muafaka

NA PETER MBURU

MUAFAKA baina ya mkono kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga umewanusuru viongozi wengi waliochukiwa na wafuasi wa mirengo hasimu, huku baadhi yao wakiishia kuwa mabingwa katika maeneo ya wafuasi wa waliokuwa maadui mbeleni.

Baadhi ya viongozi walionufaika na salamu hiyo muhimu kwa taifa ni mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, ambaye siku chache zilizopita ametembelea maeneo mengi yaliyo ngome za upinzani.

Bw Kuria ambaye mbeleni alikosolewa vikubwa na wadadisi na wafuasi wa Bw Odinga sasa anatembea sehemu za Nyanza na Magharibi kama nyumbani kwake, akila na kuimba na waliomwona kama hasimu mkubwa mbeleni.

Ziara hizo, aidha zimemsaidia kiongozi huyo kueneza ajenda ya haja ya sehemu hizo ambazo kwa miaka mingi zimetofautiana kisiasa na eneo la Mlima Kenya kushirikiana na eneo hilo na kujikomboa kutoka upinzani.

“Tumeanza safari ya ugatuzi wa salamu. Wakati wa siasa umeisha na tunaona nchi yote iko na amani, hata uchumi utaimarika na wawekezaji sasa wanaona umuhimu wa salamu hiyo,” mbunge huyo akaeleza alipokuwa akizungumzia watu Homabay.

Ziara hizo, hata hivyo, zimeonekana kama zinazonuia kukijengea chama cha Jubilee sifa na kukipa hatua, kabla ya uchaguzi wa 2022.

“Mambo ya upinzani hamuwezani nayo, kwani hata kipawa chake hamna, tuungane pamoja ili twende safari hii pamoja kwani nyumba ya Jubilee ni kubwa,” Bw Kuria akasema alipokuwa akihutubia watu Kakamega.

ODM: Ruto anavuruga muafaka wa Uhuru na Raila

VALENTINE OBARA na DAVID MWERE

WABUNGE wa upinzani wamemkashifu Naibu Rais, Bw William Ruto, kwa kupinga pendekezo kuhusu marekebisho ya katiba, wakisema ndiye kikwazo kwa muafaka.

Wabunge sita wa chama cha ODM Jumapili walisema msimamo wa Bw Ruto kupinga uundaji wa nafasi zaidi za uongozi kama vile wadhifa wa waziri mkuu, ni ishara kuwa haungi mkono juhudi za upatanisho zinazoendelezwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Viongozi hao walisisitiza kuwa lazima marekebisho ya katiba yafanywe, Bw Ruto apende asipende.

Wakizungumza katika Kanisa la Church of God lililo katika mtaa wa South B, Kaunti ya Nairobi, wabunge hao walisema matamshi ya Naibu Rais yanaonyesha haungi mkono ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Wakati Wakenya wanapojitahidi kuungana, wengine wanatia bidii kuwatenganisha. Hii haifai. Bw Ruto anafaa ajue tutahamasisha Wakenya ili waunge mkono juhudi zozote za kubadilisha mfumo wa uongozi wakati huo utakapofika,” akasema Mbunge wa Alego Usonga, Bw Samuel Atandi.

Alikuwa ameandamana na Bw Anthony Oluoch (Mathare), Bw George Aladwa (Makadara), Bw Caleb Amisi (Saboti), Bi Florence Mutua (Mbunge Mwakilishi Mwanamke wa Busia) na Mbunge Maalumu, Bw Geoffrey Osotsi.

Marekebisho ya mfumo wa uongozi yanatarajiwa kuwa miongoni mwa mapendekezo yatakayotolewa kufuatia ushirikiano uliotangazwa mnamo Machi 9, kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Wazo la kuunda nafasi ya waziri mkuu limekuwa likishinikizwa zaidi na viongozi wa kidini ambao wanaamini itakuwa njia ya kuleta uwiano wa kitaifa kwa kuwezesha jamii tofauti kushikilia nyadhifa za uongozi.

 

Salamu si makubaliano

Hata hivyo, Bw Ruto Jumapili alisema ‘salamu’ za viongozi ambao walikuwa mahasimu wa kisiasa hazimaanishi kuna makubaliano ya kuunda nafasi mpya au kugawana mamlaka na watu fulani, huku akitaka viongozi wakome kupigia debe marekebisho ya katiba.

“Wakati wa siasa ulipita na uchaguzi mwingine utafanywa 2022, kwa hivyo inafaa tutumie nguvu zetu kuhudumia wananchi ambao walituchagua,” akasema.

Aliongeza kuwa Wakenya ndio wenye mamlaka ya kuchagua viongozi wanaotaka na jukumu hilo halifai kutolewa kwa watu wachache ikizingatiwa kuwa endapo kutakuwa na nafasi ya waziri mkuu, kuna uwezekano mkubwa atakuwa akichaguliwa na wabunge.

“Wakenya ndio wenye jukumu la kuchagua viongozi wanaotaka kwa msingi wa katiba. Hakuna vile watu wachache bungeni wanaweza kupewa jukumu la kuchagua watu kushikilia mamlaka makuu. Hiyo ni kazi ya wananchi,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Turkana ambako aliandamana na Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen na magavana Josphat Nanok (Turkana), Stanley Kiptis (Baringo), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) na Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Daniel Chemno miongoni mwa wengine.

Hili linatokea siku mbili tu baada ya viongozi wa kanisa Katoliki kupendekeza kuwa katiba irekebishwe ili kuunda nafasi zaidi serikalini kwa nia ya kumaliza uhasama wa kisiasa nchini.

 

JAMVI: Muafaka ulivyoyeyusha siasa kali za Raila na NASA

Na BENSON MATHEKA

HUENDA kinara wa NASA, Raila Odinga aliangukia mtego wa kuzima siasa zake kali za kuikosoa serikali kwa kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.

Wadadisi wasema muafaka huo umemdhoofisha Raila kisiasa huku akikosa makali ya kukosoa serikali hata inapokiuka haki za washirika na wafuasi wake wa kisiasa.

Kulingana na wachanganuzi, huku dalili zikionyesha Raila alijikwaa kisiasa, Rais Kenyatta ameibuka mshindi baada ya  kiongozi huyo wa chama cha ODM kumtambua kama rais halali wa Kenya.

Wadadisi wanasema kufuatia muafaka huo, Raila alimtambua Uhuru Kenyatta kama Rais wa Kenya.

“Hilo ndilo lengo kuu la waliopanga mikakati ya muafaka huo na limeafikiwa,” alisema mdadisi wa masuala ya kisiasa, John Ondari.

Anasema jaribio la kurejea Kenya la wakili Miguna Miguna lilikuwa mtihani wa kwanza wa muafaka kati ya Raila na Rais Kenyatta lakini matukio yaliyofuatia tangu Jumatatu yameonyesha hali halisi ya muafaka huo.

“Kwamba Raila hakuweza kumshawishi Rais Kenyatta kuagiza maafisa wa serikali yake kumruhusu Miguna Miguna kuingia nchini ni dhihirisho kwamba muafaka huo ni hafifu,” alisema.

Kabla ya Bw Miguna kurejea nchini, ilisemekana moja ya makubaliano ya Raila na Rais Kenyatta ilikuwa ni kumruhusu wakili huyo kurudi Kenya.

Wakili James Orengo ambaye ni mshauri wa Bw Odinga alinukuliwa akisema, muafaka huo ungemwezesha Miguna kurudi nchi yake ya kuzaliwa bila kizingiti. Hata hivyo, licha ya kuwa na agizo la mahakama la kumruhusu kuingia nchini, Bw Miguna alizuiwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Japo Raila alifika katika uwanja huo ambako Bw Miguna alizuiwa alipowasili Kenya Jumatatu mchana, hakuweza kumsaidia wakili huyo aliyemuapisha.

“Kilichotendeka ni maafisa wa polisi kumnyakua Bw Miguna mbele yake na kumsukuma kwa ndege wakiwa na maagizo ya kumfurusha nchini. Raila hakuweza kutumia ushirika wake mpya na Rais Kenyatta kumuokoa. Iwapo kurejea kwa Miguna kulikuwa moja ya makubaliano yao, basi alichezwa shere,” alisema.

Aliongeza kwamba, hata baada ya haki za wanahabari kukiukwa walipopigwa na maafisa wa usalama wakifuatilia kuzuiliwa kwa Miguna na masaibu aliyopitia, Raila hakutoa taarifa ilivyokuwa kawaida yake kabla ya muafaka wake na Rais Kenyatta.

Wadadisi wanasema Raila amejimaliza hivi kwamba ananyamaza serikali ikiendeleza ukatili aliokuwa akipinga kabla ya kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta ikiwa ni pamoja na kukiuka maagizo ya mahakama.

“Alikuwa msitari wa mbele kutetea uhuru wa mahakama na ni miongoni mwa masuala ambayo alisema alikubaliana na Rais Kenyatta kuhakikisha yamezingatiwa.

Alikuwa msitari wa mbele kutaka mageuzi katika kikosi cha polisi ambao walimpuuza na kumkamata Bw Miguna mbele yake, alikuwa msitari wa mbele kutetea uhuru wa wanahabari ambao walipigwa wakifuatilia masaibu ya Bw Miguna na hajasema lolote,” alieleza.

 

Mateka wa Uhuru

Wachanganuzi wasema muafaka huo umemfanya mateka wa Rais Uhuru kiasi cha kunyamaza hata wakati serikali inawanyanyasa wafuasi wake.

“Ni kama anashindwa atakavyowaambia wafuasi wake baada  ya kugundua alifanya makosa. Baadhi yetu tunasikitika,” asema mbunge mmoja wa ODM ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Mbali na masaibu ya Bw Miguna, amekuwa kimya hata mawakili wa ODM, miongoni mwao wabunge Otiende Amollo na James Orengo walipofurushwa JKIA.

“Muafaka huo umemfanya Raila kuwa mateka wa serikali. Kimya chake kinaonyesha alijifunga katika makubaliano yake na Rais Kenyatta. Serikali inaendelea kupuuza maagizo ya mahakama bila kujali akitazama tu. Tunashangaa ni nini alichopewa kukubali mkataba huo,” aeleza mbunge huyo.

Baada ya kutimuliwa JKIA Jumatano usiku, Bw Orengo alisema inaonyesha muafaka kati ya Raila na Uhuru hauna maana na umuhimu wowote. Raila mwenyewe hakushutumu kitendo hicho.

Baadhi ya wadadisi wanahisi Raila alichezewa shere kukubali kushirikiana na serikali ili kuzima nguvu za upinzani za kushinikiza mageuzi katika uchaguzi, uhuru wa mahakama, na mageuzi katika kikosi cha polisi miongoni mwa masuala mengine.

Wanasema Rais Kenyatta alitaka kuhudumu katika kipindi chake cha pili bila kuhangaishwa na ni Raila pekee anayeweza kumkosesha usingizi.

Siku chache baada ya kutangaza muafaka wao, kamati andalizi ya NASA kuhusu Bunge la Wananchi ilisitisha shughuli zake kutoa nafasi ya maridhiano na waliopanga muafaka huo wakawa wamepiga hatua muhimu.

 

Kutiwa mfukoni

“Jinsi muafaka huo ulivyochezwa ilikuwa mbinu ya kumvuta Raila karibu na kumweka mfukoni. Ulifanywa kwa siri ili kumtenga na vinara wenza wa NASA ambao tayari wamemshtumu na chama chake cha ODM kwa kuwasiliti.

Kwa kumvika nembo ya usaliti, upinzani ulizimwa  na kufuatia matukio ya hivi majuzi katika seneti, ni mlima kurejesha umoja wa NASA,” anaeleza Bw Tom Maosa wakili na mdadisi wa siasa ambaye kwa sasa yuko Sierra Leone.

Baada ya kutangaza muafaka wake na Rais Kenyatta, Raila aliongoza mkutano wa Wabunge wa chama chake cha ODM na wakakubali  kuunga mkono ushirikiano huo licha ya vinara wa vyama tanzu vya NASA Wiper, Ford Kenya na Amani National Congress (ANC) kulalamika jinsi mazungumzo yalivyofanyika kwa siri.

ODM kilimpokonya Moses Wetangula wadhifa wa Kiongozi wa Wachache katika seneti licha ya kuwa kinara mwenza wa NASA, jambo ambalo wadadisi wanasema lilikuwa msumari wa mwisho katika jeneza la NASA.

“Kuvunjika kwa NASA wakati Wetangula na Mudavadi (kiongozi wa ANC) walipotangaza kujipanga upya kisiasa kulikamilisha mchezo ambao waliopanga muafaka huo kumfunga  Raila walilenga,” asema.

Kufikia sasa, muafaka wao haujafafanuliwa kwa kina, japo Raila amekuwa akisisitiza kuwa hajajitenga na NASA licha ya chama chake cha ODM kutenga vyama tanzu.,

Wanasiasa wataka Jubilee iwe macho Raila asije akazima ndoto ya Ruto 2022

GAVANA wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

BAADHI ya wanasiasa wa Jubilee sasa wamesema kuwa hawamwamini kinara wa NASA Raila Odinga kwani huenda akavuruga mpango wa Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022.

Wakiongozwa na Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu ‘Babayao’, mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na Mwakilishi Mwanamke wa Nyeri Rahab Mukami, wanasiasa hao walisema japo wamefurahishwa na hatua ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kukubali kufanya kazi pamoja, kuna haja kwa Jubilee kuwa waangalifu.

“Tumefurahishwa na viongozi hao wawili kukubali kufanya kazi pamoja lakini Bw Odinga haaminiki,” akasema Bw Waititu.

“Naibu wa Rais, Bw Raila akikuambia ufumbe macho muombe usifunge macho kwani anaweza kutoweka na kukimbia na kila kitu,” akasema Bw Waititu. Bw Ichungwa alimtaka Bw Odinga kuwa mwaminifu na asiwe na ‘mguu mmoja nje’.

Bi Mukami alimtaka Bw Odinga kushirikisha vigogo wenzake wa Nasa katika meza ya mazungumzo na Rais Kenyatta ikiwa kweli ana nia ya kuunganisha Wakenya wote.

Lakini Bw Ruto ambaye alikuwepo wakati wa ibada katika kanisa la PCEA mtaani Runda, Nairobi alikwepa na madai ya viongozi hao huku akisema kuwa ushirikiano baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unalenga kuleta amani ambayo ni muhimu kwa maendeleo.

“Ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga si wa manufaa ya kibinafsi bali ni wa kuhakikisha Kenya inapata amani hivyo kupisha maendeleo,” akasema Bw Ruto.

JAMVI: Uhuru afanikiwa kupunguza makali ya vinara wa upinzani kwa utawala wake

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta hatimaye amefaulu kudhoofisha upinzani dhidi ya serikali yake kwa kumshawishi kiongozi wa ODM Raila Odinga kuunga ajenda zake.

Wadadisi wanasema, japo viongozi hao wawili walisema nia yao ni kuunganisha Wakenya,  Rais Kenyatta ndiye mshindi kwa sababu hatakuwa na upinzani wenye nguvu wa kukosoa serikali yake.”

Jubilee ilijaribu kusambaratisha upinzani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana lakini ikashindwa. Kwa kukutana na Bw Odinga na kufikia muafaka, Rais Uhuru amefaulu kulemaza upinzani,” asema Bw Godfrey Aliwa, mdadisi wa masuala ya siasa na wakili jijini Nairobi.

Anaeleza kuwa waliopanga mazungumzo hayo walielewa kuwa upinzani bila Raila ni butu. “Raila ndiye nguzo ya upinzani Kenya na kwa kumleta karibu na serikali ni kusambaratisha upinzani.

Lengo hapa ni kuhakikisha Rais Kenyatta hatakuwa na upinzani wenye nguvu kumsumbua katika kipindi chake cha pili na cha mwisho uongozini,” alisema Bw Aliwa.

Mbali na upinzani kuwa na wabunge wachache, wengi wao ni wa chama cha ODM cha Bw Raila ambao tayari wameanza kuchangamkia muafaka wake na Rais Kenyatta.

Washirika wa Bw Raila katika NASA, Kalonzo Musyoka wa Wiper Democratic Movement, Moses Wetang’ula wa Ford-Kenya na Musalia Mudavadi wa Amani National Congress hawakuhusishwa katika muafaka huo.

Baadhi ya washirika wa kisiasa wa Bw Musyoka, Bw Wetangula na Bw Mudavadi wamenukuliwa wakitaka chama cha ODM kuondoka NASA ili wachukue nafasi ya upinzani rasmi. Hata hivyo, kulingana na Bw Aliwa, hata kama wangeachiwa NASA, hawataweza kukosoa serikali alivyokuwa akifanya Bw Raila.

“Aliyenufaika pakubwa ni Rais Kenyatta kwa sababu atakuwa na mteremko kwa kukosa upinzani thabiti katika kipindi chake cha mwisho mbali na Raila kumtambua kama rais,” alisema.

Chini ya Bw Raila na wanasiasa wake wa ODM, upinzani uliongoza maandamano yaliyong’oa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) chini ya aliyekuwa mwenyekiti Isaack Hassan.

Ni Bw Odinga ambaye alifichua kashfa mbali mbali serikalini ikiwa ni pamoja na ile ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS na Eurobond. “Sidhani kama kuna anayeweza kufuata nyayo za Raila kati ya Musyoka, Wetangula na Mudavadi. Kumbuka ni Raila aliyekuwa akisukuma kubuniwa kwa mabunge ya wananchi yaliyokuwa yakikosesha Jubilee usingizi,” asema Bw Geff Kamwanah, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Anasema masuala ambayo NASA imekuwa ikipigania kama haki katika uchaguzi ni mazito na yanahitaji kiongozi mwenye ujasiri kama Raila.

Bw  Musyoka, Bw Wetang’ula na Bw Mudavadi wanasema wako tayari kusukuma ajenda za NASA bila Bw Odinga lakini hii ni kama mzaha,” asema mwanahabari na mdadisi wa masuala ya siasa Macharia Gaitho kwenye makala yaliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation.”

“Wamekasirika kwa sababu Bw Odinga alizungumza na Bw Kenyatta bila kuwahusisha,” alisema Bw Gaitho.

Bw Kamwanah anasema ishara kwamba Musyoka, Wetangula na Mudavadi hawana ujasiri wa kukabiliana na serikali ni kujitenga kwao na Raila alipokula kiapo kama rais wa wananchi.

“Huo ulikuwa mtihani waliofeli. Raila amejaribiwa mara nyingi kwa moto, ameteswa na kutupwa jela na kuibuka jasiri zaidi. Kwa kuzika tofauti zake na Rais Uhuru ni kama kuua upinzani,” aeleza.

Raila amesisitiza kuwa hajahama NASA akisema muafaka wake na Rais Kenyatta ni wa watu wawili na sio mirengo ya kisiasa. Hata hivyo, matamshi yake na washirika wake wa kisiasa, wakiwemo wabunge wa chama cha ODM, yanatoa ujumbe tofauti. Kulingana na mbunge wa Lugari Ayub Savula, Wiper, ANC na Ford Kenya viko tayari kuunda upinzani rasmi bila ODM.”

ODM ikioana na Jubilee tuko tayari kuunda upinzani rasmi,” alisema. Hata hivyo, wadadisi wanasema wanachotaka wabunge hao wapatao 40 bila ODM ni vyeo vya upande wa upinzani bungeni.

“Kenya imerejea ilipokuwa 1997 upinzani ulipodhoofishwa Raila alipojiunga na serikali ya Kanu. Jukumu la kukosoa serikali lilichukuliwa na vyombo vya habari na mashirika ya kijamii na yasiyo ya Serikali.

Jinsi hali ilivyo wakati huu, uhuru wa wanahabari na mashirika ya kijamii umedidimizwa. Kwa ufupi, hakutakuwa na upinzani Kenya iwapo Raila atamezwa na Jubilee,” asema Bw Kamwanah.

Hisia za wadadisi ni kuwa, muafaka wa Raila na Uhuru ulipangwa ili  kupangua upinzani ukose makali ya kukosoa Serikali.

Ziara ya Rais Uhuru na Raila mjini Kisumu yaahirishwa

Na JUSTUS WANGA

MKUTANO wa pamoja kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa NASA Raila Odinga uliotaribiwa kufanyika wiki hii mjini Kisumu umeahirishwa kutoa nafasi kwa muda wa kushughulikia masuala ibuka yanayotisha kuathiri muafaka kati yao.

Wandani wa Bw Odinga wameanza kushuku kujitolea kwa Jubilee katika mchakato wa mazungumzo baada ya kiongozi wa wengine bunge Aden Duale kupinga kujumuishwa kwa suala ya mageuzi  katika mfumo wa uchaguzi ambalo ni mojawapo yale ambayo Rais na Odinga walikubali kujadili.

Akiongea katika runinga moja ya humu nchini Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini pia alipuuzilia mbali mageuzi katika mfumo wa uongozi nchini.

Wakati huo huo, mpango wa balozi Martin Kimani na Wakili Paul Mwangi kuwahutubia wanahabari Ijumaa ili kuelezea hatua iliyopigwa kuhusu suala hilo iliahirishwa dakika zake mwisho.

Mbw Kimani na Mwangi waliteuliwa na Rais Kenyatta pamoja na Bw Odinga kutayarisha mwongozo ambao utasaidia kufanikisha malengo ya mwafaka huo.
Duru zilisema kuwa “kuna masuala ambayo pande husika hawajakubaliana.” Walipofikiwa kwa njia ya siku wawili hao hawakutaja sababu ya kufutilia mbali kikao na wanahabari.

Taifa Jumapili pia imegundua kuwa Kamati hiyo itapanuliwa kwa kujumuisha angalau wanachama watano kutoka kila upande huku akianza kibarua rasmi.

Shauku ya kambi ya Bw Odinga inatokana na hali kwamba japo ameshawishi uongozi wa chama hicho kuunga mkono ushirikiano huo, kufikia sasa Rais Kenyatta hajaitisha mkutano wa kundi la wabunge wake (PG) au asasi yoyote ya chama hicho kuhimiza wafuasi wake kuunga mkono mwafaka huo. Vile vile, wanasema Rais Kenyatta hajaitisha kikao maalum cha baraza la mawaziri kuwajuza kuhusu yaliyomo ndani ya mkataba kati yake na Bw Odinga.

“Tunataka kuona taarifa kutoka afisi ya Rais ikielezea hatua ambazo zimewekwa kuafikia uwiano na masuala ambayo yalikubaliwa. Sawa na Odinga, tunaamini kwamba Rais ana nia njema. Tunataka kuona wakianza kazi,” mmoja wa wandani wa Bw Odinga alisema.

Chama cha ODM kinashikilia kuwa hatima ya mwafaka huo utategemea kama iwapo Rais alielekeza nchini kufunua ukurasa mpya huku masuala ya serikali yakiendeshwa kwa namna tofauti.

Hata hivyo, hakuna kiongozi kutoka kambi ya Kenyatta ambaye amepinga mwafaka huo isipokuwa Seneta wa Tharaka Nithi Profesa Kithure Kindiki ambaye ameonya Rais kutahadhari anapojadiliana na Bw Odinga kwa sababu, “ni mwanasiasa mjanja”.

Seneta wa Siaya James Orengo, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga aliwaonya Rais Kenyatta na kiongozi huo wa upinzani kuwaonya wafuasi wao dhidi ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kusambaratisha mwafaka huo.

 

Weta na Mudavadi waapa kusambaratisha ndoa ya Uhuru na Raila

Na DERRICK LUVEGA na JUSTUS OCHIENG’

Kwa ufupi:

  • Mudavadi asema Raila ni msaliti na kama jamii ya Waluhya inafaa kuepukana kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee
  • Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”
  • Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila 
  • Ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa

VINARA wa NASA kutoka jamii ya Waluhya sasa wametangaza vita vikali vya kisiasa dhidi ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga na kuwataka wafuasi wao kukataa chama hicho kuelekea uchaguzi wa 2022.

Wakihutubia mikutano ya hadhara katika vituo kadha vya kibiashara kaunti ya Vihiga, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi, walisema Bw Odinga ameikosea heshima jamii ya Waluhya kwa kuisaliti na kuitelekeza.

Walitaja kuondolewa kwa Bw Wetang’ula kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti na wao kutajwa kama waoga kama ishara tosha kuwa ODM imetelekeza jamii ya Waluhya.

“Mliona vile alituhepa na kwenda kuzungumza na Uhuru Kenyatta. Na juzi mliona alivyochochea kuondolewa afisini kwa ndugu yangu Weta kama kiongozi wa wachache katika seneti.

Huyo ni msaliti na sisi kama jamii ya Waluhya tuepukane kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee,” Bw Mudavadi akawaambia wafuasi wake mjini Mbale bila kumtaja Bw Odinga kwa jina.

Aliandamana na wabunge, Alfred Agoi (Sabatia), Ernest Ogesi (Vihiga), aliyekuwa seneta wa Kakamega Dkt Bonny Khalwale, Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka miongoni mwa wengine.

Nao viongozi wa ODM wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, waliwajibu kwa kupuuzilia mbali malalamishi yao.
“Watu wanafaa kuungana kwa masuala yenye umuhimu kwa wananchi kama vita dhidi ya umasikini unaowazonga watu wetu.

Sio masuala potovu kama kuwashambulia wanasiasa wengine,” akasema Bw Sifuna.

Naye Bw Wandayi akasema: “Hakuna aliyeisaliti jamii ya Waluhya. Hakuna mwanasiasa aliye na uwezo kama huo. Hili suala la mabadiliko ya uongozi katika seneti linashughulikiwa na maseneta wenyewe, haifa kutumiwa kumchafulia jina kinara wetu Bw Odinga”.

 

Kusambaratisha ndoa

Na akiongea mjini Chwele awali, Bw Wetang’ula alisema yeye na vinara wengine wa NASA watafanya juu chini kusambaratisha ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM.

Bw Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”.

Migawanyiko imekuwa ikitokota katika muungano wa NASA baada ya Bw Odinga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kwa mazungumzo Machi 9 bila kuwahusisha vinara wenzake.

Akiwahutubia walimu katika kituo cha kibiashara cha Chwele wakati wa kongamano la wajumbe wa chama cha ushirika cha Ngarisha, Bw Wetang’ula alisema uamuzi wa Bw Odinga kukutana na Rais bila kuwafahamisha na kuondolewa kwake kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti ni usaliti “ambao hauwezi kuvumiliwa”.

 

Kulipiza kisasi

“Licha ya sisi kupambana kwa bidii na baadhi ya watu kupoteza maisha yao, mienendo ya mgombea wetu wa urais inashangaza na inaashiria usaliti wa kiwango cha juu,” akasema Bw Wetang’ula huku akiapa kulipiza kisasi.

Alisema ingawa yeye, Mudavadi na Kalonzo wamekuwa wakihimiza kuandaliwe mazungumzo ya kitaifa, utaratibu ufaao haukutumika kuanzisha mchakato huo.

Bw Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila mnamo Januari 30.

Alisema ni Raila mwenyewe aliyewashauri kutohudhuria halfa hiyo katika bustani ya Uhuru, Nairobi, ili waweze kumtetea endapo angekamatwa.

“Ni Raila aliyetushauri kukaa kando, kwa hivyo ni makosa kwa wanachama wa ODM kututaja kama waoga kwa kutohudhuria sherehe hiyo ambayo kwa kweli haikuwa na maana,” Bw Wetang’ula akasema.

 

Fisi

“Kama fisi anataka kuwala wanawe, kwanza huanza kuwashutumu kwamba wananuka harufu inayofanana na ya mbuzi,” akaeleza kwa mafumbo.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alisema yeye na wenzake hawatakubali kutolewa kafara na Raila, akisema wamejipanga kukabiliana naye na Rais Kenyatta bila woga.

“Sasa hafai kujihushisha na masuala ya NASA. Aelekeze nguvu zake katika ushirikiano kati yake na Jubilee na sasa tuko tayari kuendelea na ajenda za upinzani,” Bw Wetang’ula amasema.

Seneta huyo alisema ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa.

“Kondoo amekuwa na wasiwasi kuhusu mbwa mwitu kwa miaka mingi lakini aliishia kuliwa na mchungaji,” Wetang’ula akasema.

 

TAHARIRI: Muafaka usiwe kifo cha upinzani

Na MHARIRI

MALUMBANO ndani ya vyama tanzu vya upinzani unaendelea kupandisha joto la kisiasa ambalo lilikuwa limezimwa na mkutano wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga.

Jumanne, Seneta wa Bungoma Moses Wetangula alivuliwa wadhifa wake wa kiongozi wa wachache bungeni hatua ambayo ilivikera sana vyama vya Wiper, ANC na Ford Kenya.

Chama cha ODM kilimfurusha Bw Wetangula licha ya vinara wa NASA, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Wetangula na Bw Odinga kutoa maagizo ya kukomesha hatua hiyo.

Japo vyama vya kisiasa vina demokrasia ya kuadhibu wanachama waasi, ni vyema mizozo ya ndani ilisuluhishwe kimya na viongozi bila kuchochea uhasama wa kisiasa haswa miongoni mwa jamii.

Mabadiliko yanayoshuhudiwa NASA katika usimamizi wa bunge yalianza baada ya mkutano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Tungetaka kusisitiza umuhimu wa kuwa na chama cha upinzani bungeni ili kukosoa maovu ya serikali.

Bw Odinga alichukua hatua ya busara sana kuweka kando tofauti zake za kisiasa na kukutana na rais, lakini ni vyema Waziri huyo Mkuu wa zamani awape nafasi viongozi wengine wanaotaka kuendelea kuwa kwa upinzani.

Hatua ya ODM kumtimua Seneta Wetang’ula katika wadhifa huo imechukuliwa na wengi kama usaliti wa kisiasa hatua ambayo huenda ikaanzisha siasa za 2022.

Siasa zina ushindani mkubwa na ingekuwa vyema kutoanzisha mjadala wa uchaguzi wa 2022 ili kutoa nafasi kwa serikali kuu na zile za kuanti kuwahudumia Wakenya kabla ya kuingia katika mchakato mwingine wa kisiasa.

Bw Musyoka na wenzake walimuomba Rais Kenyatta awape sikio na tunasisitiza umuhimu wa kufanyika kwa mdahalo wa viongozi wote.
Japo mkutano wa rais na Bw Odinga umewapa wengi matumaini ya kutuliza joto la kisiasa nchini, ni vyema kutopuuza mchango wa vinara wenza katika upinzani.

Madhumuni ya kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga yawe kuunganisha Wakenya wote na wala si kuua upinzani ambao mchango wake ni muhimu sana kuhakikisha mali ya umma imelindwa na kutumika ipasavyo.

Bw Odinga anapaswa kujitokeza wazi kuelezea iwapo chama chake kimemezwa na Jubilee ili kutoa nafasi kwa vyama vingine vyenye uwezo wa kuikosoa serikali.

JAMVI: Wabunge waonekana kutoelewa makubaliano ya Uhuru na Raila yanakoelekea

Na CHARLES WASONGA

HUKU mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga ukiendelea kuibua hisia mseto imebainika kuwa wabunge wa pande zote mbili hawaelewi mwelekeo utakaochukua.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa sasa wanaelezea hofu kwamba huenda hali hii ikalemaza juhudi za kuafikiwa kwa masuala muhimu yaliyoangaziwa katika taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na viongozi hao.

Akiwasilisha hoja ya kuhimiza wabunge kukumbatia maelewano hayo Jumatano, kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi alisema wawili hao walikubaliana kuhusu masuala yenye umuhimu kwa maendeleo ya nchi.

Lakini akaeleza: “Sisi kama wafuasi wao tumekubali kuunga mkono mipango ya kuchochea maendeleo nchini. Kwa hivyo, tunasubiri mapendekezo hayo ili tuyajadili na kuyaelewa kabla ya kuyapitisha.

 

Mambo muhimu

Bw Mbadi, hata hivyo, alioorodhesha masuala amabayo yamekuwa yakiibuliwa na muungano wa upinzani, NASA, tangu 2017 kama vile, haki katika uchaguzi, uhuru wa idara ya mahakama, ukabila, ridhaa kwa wahasiriwa wa fujo za kisiasa, vita dhidi ya ufisadi na kupigwa jeki kwa ugatuzi, kama yatakayoangaziwa katika mazungumzo hayo.

Mwenzake upande wa Jubilee, Aden Duale naye alionekana mwenye ufahamu finyu kuhusu misingi na muundo wa mwafaka huo.

Kiongozi huyo wa wengi akasema: “Wakati huu muafaka huo ungali mchanga. Tungali kushuhudia mengi. Tumeonyeshwa ukurasa mmoja tu.”

Kiranja wa wachache Junet Mohammed ambaye aliandamana na Bw Odinga kwa mkutano na Rais Kenyatta katika jumba la Harambee, Nairobi Machi 9 pia hakutoa mwanga kuhusu yaliyojiri katika mkutano huo.

“Katika bungeni hili mimi niliyepewa nafasi ya kipekee ya kuandamana na kinara wetu katika mkutano huo. Nilisikiza yote na nikaridhika kabisa,” akasema bila kuelezea wenzake yale aliyoyasikia.

Bw Martin Andati sasa anasema kauli za wabunge hao, wandani wa karibu wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, zinaonyesha wazi kuwa wao pia hawaelewi mambo mengi kuhusu muafaka huo.

“Hii ni kwa sababu ya maandalizi ya mkutano huo yalifanywa kwa siri kubwa, hali iliyopelekea vinara wengine wa NASA kulalamika walidai walifaa kuhusishwa,” anasema.

“Japo Wakenya wote wanakubali mkutano kati ya Raila na Uhuru ulipoesha joto la kisiasa nchini kufuata utata uliotokana na pande zote mbili zinafaa kutoa mwongozo utakaotumiwa kuendeleza mazungumzo kuhusu masuala yaliyoorodheshwa kwenye taarifa yao ya pamoja,” Bw Andati anasema.

 

Vioja bungeni

Ukosefu wa mwongozo mahususi kuhusu mwelekeo ambao ushirikiano kati Rais Kenyatta na Bw Odinga utachukua kutimiza malengo yao ndio ulichangia kioja kilichoshuhudiwa bungeni Jumanne alasiri.

Mbunge wa Mavoko Patrick Makau (Wiper) aliamua kuketi kwenye kiti kilichotengwa mahsusi kwa kiongozi wa wachache, Bw Mbadi. Alisema alichukua hatua hiyo baada ya kile alichodai kuwa “hatua ya ODM  kujiunga na Jubilee baada ya Raila kama kiongozi wake kuelewana na Rais Kenyatta.”

“Baada ya ODM kujiunga na Jubilee chama change cha Wiper ambacho ndicho cha tatu kwa ukubwa kimeniteua kuwa kiongozi wa wachache. Hii ndio maana niliketi katika kiti hicho,” aliwaambia wanahabari baada ya Spika Justin Muturi kumfurusha nje kwa kukaidi amri ya kumtaka ampishe Bw Mbadi.

Mwenzake wa Makueni Daniel Maanzo pia aliamua kukalia kiti cha Bw Junet (kiranja wa wachache) kwa sababu hiyo hiyo ya ODM kujiunga na Jubilee. Hata hivyo, aliondoka upesi kabla ya kuadhibiwa na Spika Muturi.

“Kwa sababu Raila, kama kiongozi wa ODM, hakuwahusisha wenzake; Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya) katika mkutano wake na kiongozi wa Jubilee, Rais Kenyatta, tunaamini kuwa amejiunga na Jubilee. Hii ndio maana niliketi katika kiti cha Junet na mwenzao Makau akaketi katika kiti cha Mbadi,” anaeleza Mbunge huyo ambaye ni wakili.

Bw Maanzo anasema Wiper itaunga mkono mazungumzo yatakayoendeshwa chini ya mpangilio “unaoeleweka na kuwekewa mihimili ya kesheria” na kujumuisha wadau wote.

 

‘Hakuna nusu mkate’

Ni  ufasiri aina hii uliomsukuma Bw Duale kufafanua kuwa mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga haumaanishi kwamba kuna mipango ya kubuniwa kwa serikali ya mseto kati ya Jubilee na ODM.

“Hakuna nusu mkate hapa. Na chama cha ODM hakijamezwa na Jubilee kama inavyodaiwa. Sisi kama Jubilee tunataraji ODM kupiga msasa utendakazi wa serikali huku ikishirikiana nasi kusukuma ajenda ya maendeleo kwa manufaa ya Wakenya,” anasema.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini anashauri vyama tanzu katika NASA kukoma kumkaripia Bw Odinga kwa kufuatua uamuzi wake wa kufanyakazi pamoja na Rais Kenyatta.

“Viongozi hawa wawili wameamua kuzika tofauti zao kwa ajili ya kuliunganisha taifa. Wiper, Ford Kenya na ANC ambao ni wenye hisa wadogo katika NASA wanapaswa kuheshimu uamuzi huu wa ODM,” anasema.

Kwa upande wake mchanganuzi wa masuala ya kisaisa Bw Odoyo Owidi anasema kukanganyikiwa huku kwa wanasiasa kunaweza tu kuondolewa ikiwa afisi kuu iliyobuniwa kushirikisha mazungumzo hayo itaanza kufanya kazi na kwa uwazi.

“Wakili Paul Mwangi na Balozi Martin Kimani walioteuliwa kuongoza afisi hiyo, kwa ushirikiano na washauri wengine, wanafaa kuanza kazi. Na watatekeleza majukumu yao kwa uwazi la sivyo hali hii ya wanasiasa kuendelea kurusha cheche za maneno huku na kule bado itaendelea,” anasema, akionya kuwa huenda hali hiyo ikavuruga malengo ya muafaka huu.

“Huu mkutano wa jumba la Harambee ulikuwa ni wa watu wawili. Sisi kama Wiper hauutambui wala kufahamu yaliyojadiliwa,” anasema.

Kauli yake inaungwa mkono na naibu kiongozi wa ANC Bw Ayub Savula ambaye anasema vyama tanzu ndani ya NASA viko tayari kuipa ODM “talaka” kwa kushirikiana na Jubilee.

JAMVI: Tetesi za vinara wa NASA kukutana kisiri na Ruto zilivyoyeyusha misimamo mikali

MKUTANO wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga wiki iliyopita ulianza kuandaliwa hata kabla ya hafla ya kumuapisha Bw Odinga kama “rais wa wananchi” mnamo Januari 30.

Imefichuliwa kuwa wawili hao walianza kuzungumza moja kwa moja  kwa simu na kukutana mara kadhaa kwa siri kuweka mikakati ya kuzika tofauti zao.
Duru zinasema kuwa mazungumzo ya wawili hao kushirikiana yalianza punde tu baada ya uchaguzi wa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26 mwaka jana ambao Bw Odinga alisusia.

Juhudi za kuwapatanisha wawili hao ziliendelezwa na mabalozi, viongozi wa kidini na Umoja wa Mataifa, japo baadhi ya washirika wa kisiasa wa viongozi hao walishikilia misimamo mikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, alikiri kwamba shirika hilo lilimtuma aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obassanjo kuwapatanisha viongozi hao.

Imefichuliwa kuwa muafaka wao ulicheleweshwa kwa kuwa awali, kulikuwa na kutoaminiana.

“Kulikuwa na kutoaminiana hasa baada ya Bw Odinga kujiapisha kama rais wa wananchi. Hata baadhi ya washauri wa rais ambao hawakuwa wakifahamu mazungumzo hayo walitaka akamatwe kwa kujiapisha nao wale wa Bw Odinga hawakutaka mazungumzo.

Baadhi walitaka aunde serikali mbadala. Hii iliweka breki mazungumzo ambayo yangekamilika mapema Januari,” alisema mmoja wa waliohusika  kwenye mazungumzo hayo ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Inasemekana kuwa, wawili hao walikuwa wakizungumza kwa simu na hata kukutana usiku mara kadhaa baada ya marudio ya uchaguzi wa urais kufuatia shinikizo za jamii ya kimataifa.

 

Walivyozika tofauti

Kabla ya mkutano wa Ijumaa wiki iliyopita, walikutana katika nyumba ya afisa mmoja mkuu wa Mahakama ambapo waliamua kutangaza kuzika tofauti zao.

Watu wa familia zao na wazee wa jamii za Waluo na Wakikuyu pia walitekeleza wajibu muhimu kwenye mazungumzo hayo hadi viongozi hao wawili wakaamua kuacha tofauti zao za kisiasa na kushirikiana.

Mchango wa balozi wa Amerika Robert Godec pia ulitajwa kuwa mkubwa kupatanisha mahasimu hao wa kisiasa ambao tofauti zao zilizidi baada ya uchaguzi wa mwaka jana ambapo Raila anadai alipokonywa ushindi.

“Kwamba walitangaza kupatana saa chache kabla ya aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Amerika, Rex Tillerson kuwasili Kenya ilichukuliwa kwamba Amerika na jamii ya kimataifa ilihusika kuandaa muafaka huo,” asema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Geff Kamwanah.

Anasema muafaka huo ulimfaidi Bw Odinga ambaye uhusiano wake na jamii ya kimataifa ulikuwa umedorora tangu alipojiapishwa kuwa rais wa wananchi.

Duru zinaeleza kuwa, ni walipokutana kisiri mara ya mwisho katika nyumba ya afisa mmoja wa mahakama mtaani Karen ambapo waliafikiana kushirikiana na kukubaliana kuweka wazi uamuzi wao.

 

Kuepuka kulemaza mazungumzo 

Waliopanga mikakati ya kuwapatanisha wawili hao walihisi kwamba kuwashirikisha washauri wao wa kisiasa walio na misimamo mikali kungekwamisha mazungumzo.

Waliamua kuacha nje wanasiasa wenye misimamo mikali wakiwemo  vinara wenza wa Bw Odinga na naibu rais William Ruto. Hata hivyo, japo vinara wenza wa NASA Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula wamesema wazi kwamba hawakuhusishwa kwenye mazungumzo hayo, Bw Ruto hajasema wazi hakuyafahamu.

Wanamikakati hao walihisi kwamba,  mvutano kati ya serikali na upinzani ulikuwa hatari kwa uchumi na usalama wa nchi, hasa serikali ilipoanza kuwaandama viongozi wa upinzani.

Raila aliandamana na binti yake Winnie, wakili Paul Mwangi na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed naye Rais Kenyatta aliandamana na balozi Martin Kimani.

 

Siri

Imebainika kuwa mazungumzo ya simu kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta yaliwekwa siri chini ya usimamizi wa mkurungenzi wa ujasusi Philip Kameru ambaye inasemekana alitekeleza wajibu muhimu kupatanisha wawili hao.

Kulingana na duru za kuaminika, ni Bw Kameru aliyemshauri Rais Kenyatta kutomkamata Bw Odinga alipojiapishwa kuwa rais wa wananchi.

Kukubali kwa Bw Odinga kushirikiana na Rais Kenyatta kulichochewa na tetesi kwamba, vinara wenza katika NASA, ambao walisusia hafla ya kumuapishwa, walikuwa wakizungumza na Bw Ruto kuunda muungano wakilenga uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya kuhisi kwamba chama cha ODM cha Bw Odinga kilipanga kujitenga na muungano huo.

Wadadisi wasema hatua ya wawili hao kupatana itabadilisha mwelekeo wa kisiasa nchini katika siku chache zijazo.

“Kwa sasa, huenda ni vinara wenza wa NASA wanaolalamika lakini ukweli ni kwamba,  muafaka wa Raila na Uhuru utayumbisha Jubilee,” alisema Bw Sila Tirop, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

JAMVI: Mkataba wa Raila na Uhuru wazalisha mayatima wa kisiasa

Na WYCLIFFE MUIA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga kutangaza ushirikiano mpya inatishia mustakabali wa wanasiasa wengi walionuia kufaidi na mzozo wa mara kwa mara kati ya viongozi hao wawili.

Wachanganuzi wanakubaliana kuwa, mkutano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulipangua pakubwa mipangalio ya sasa ya kisiasa na italazimu baadhi ya viongozi katika pande zote kujitathmini upya la sivyo, watakufa kisiasa.

Kwa mujibu wa wataalamu wa kisiasa, waathiriwa wa kwanza kabisa wa umoja wa vinara hao ni Naibu Rais William Ruto na vinara wenza wa upinzani Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

Juhudi za Bw Musyoka kutaka rais kumpa sikio zinaonekana kugonga mwamba huku matumaini yake ya kupata uungwaji mkono wa Bw Odinga kuwania urais 2022 yakisalia kitendawili.

Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga tayari kimethibitisha ushirikiano wake na serikali ya Jubilee na kumtaka kiongozi wao (Bw Odinga) asiyumbishwe na walio na azma ya kuwania urais 2022.

Wakili Kamotho Waiganjo anasema, kuna kila sababu ya Bw Musyoka na Bw Mudavadi kuwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu ni bayana macho yote yako 2022 na mkutano wa rais na Bw Odinga unazika Mkataba wao wa kisiasa wa 2017 ambapo chama cha ODM kilikubali kutoteua mgombeaji wa urais 2022 na badala yake, kuunga mmoja wa wagombeaji wa vyama tanzu.

“Iwapo mkutano wa rais na Bw Odinga ni mwanzo wa serikali nyingine ya muungano, bila shaka vigogo kadhaa wa kisiasa wanaathiriwa. Kuna uwezekano wa kuchipuka kwa miungano mingine ya kisiasa inayohusisha wanasiasa ambao hawadhirishwi na umoja wa vinara hao wawili,”anasema Bw Waiganjo.

Bw Waiganjo anahisi kuwa, japo Bw Ruto ana uungwaji mkono wa 2022 wa chama cha Jubilee, anapaswa kufuatilia kwa makini uhusiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Kulingana na mhadhiri wa masuala ya kisiasa Herman Manyora, shida kubwa ya kisiasa inayorudisha taifa hili nyuma, ni usaliti wa kisiasa na rais pamoja na Bw Odinga wanaweza kuleta suluhu.

 

Historia ya usaliti

“Shida kuu hapa ni usaliti wa kihistoria. Shida hii ilianza pale Mzee Jomo Kenyatta alipomruka Jaramogi Odinga, mtindo huu ukaendelea baada ya Mwai Kibaki kusaliti maafikiano yake na Raila.

Kisha Uhuru akaonekana kukandamiza demokrasia ambayo ingemwezesha Raila kutimiza ndoto yake ya kuwa rais. Mkutano wao uliashiria mwisho wa usaliti huo,”anasema Bw Manyora.

Kulingana na Bw Manyora, ili kutatua shida hii, sharti wanasiasa kadhaa watolewe kafara pamoja na ndoto zao za kisiasa.

Bw Manyora anahisi kuwa umoja huu utampa rais mandhari mazuri ya kutekeleza ahadi zake za maendeleo pamoja na kuunda wosia wake wa kisiasa naye Bw Odinga huenda akagawiwa mamlaka.

“Inawezekana kuwa si kweli lakini nahisi kuwa kuna mpango wa kuhakikisha Raila ameonja urais. Huu mjadala unasikia kuhusu mabadiliko ya katiba ni kuhakikisha Bw Ruto hajaachwa nje,”anasema Bw Manyora.

Katika miaka mitano iliyopita, Bw Ruto amekuwa akiunda himaya yake ya kisiasa, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kumrithi Rais Kenyatta mnamo 2022.

 

Mke mwenza’ 

“Lazima Bw Ruto atambue sasa ndoa yao na rais imepata mke mwenza hali ambayo huenda ikabadilisha kabisa mipango ya urithi wa urais,”anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Edward Kisiang’ani.

Prof Kisiang’ani anahisi kuwa, Bw Ruto ni yatima mkubwa wa Jubilee na mustakabali wake wa kisiasa utategemea jinsi atakavyohusiana na Bw Odinga.

Kwa upande wa NASA, MaBw Musyoka, Mudavadi na Seneta Wetangula huenda wakalazimika kusahau ndoto zao za kuwa rais, iwapo  Bw Odinga atasisitiza kuwania urais tena 2022.

“Tayari umesikia baadhi ya viongozi wa Jubilee wenye misimamo mikali kama (Adan) Duale na Seneta (Kipchumba) Murkomen, wakimsifu Bw Odinga na kumtaja kama kiongozi mwenye uzalendo mkubwa. Wanafahamu vyema kuwa yeye ndiye atakayeunda siasa za 2022,” anaongeza Prof Kisiang’ani.

Kando na Duale na Murkomen, Prof Kisiang’ani anahisi kuwa Seneta wa Tharaka Nithi Kindiki Kithure vilevile ni yatima wa umoja huu ikizingatiwa kuwa alikuwa ametangaza wazi kuwa anataka kuwa mgombea mwenza wa urais wa Bw Ruto ifikiapo 2022.

 

Onyo

Tayari Prof Kindiki ameonya kuhusu uhusiano wa Bw Odinga na Jubilee akisema Waziri huyo Mkuu wa zamani ni ‘mtaalamu’ wa kisiasa na huenda akavuruga kabisa mpangilio wa 2022 wa chama hicho.

Iwapo Bw Musyoka na wenzake katika NASA watajumuishwa katika mkataba wa rais na Bw Odinga, viongozi walioazimia kuwania urais 2022 wataathiriwa sana kisiasa.

Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho na mwenzake wa Machakos Dkt Alfred Mutua watalazimika kutathmini upya mipango yao ya kisiasa ya 2022 kwa sababu hawatawania ugavana kwa awamu ya tatu.

Wengine ambao hatima yao haijulikani iwapo Bw Odinga atajiunga na serikali ni Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na mwenyekiti wa chama cha Jubilee Raphael Tuju.

Dkt Matiang’i amekuwa akitoa maagizo yaliyoonekana kuwahangaisha viongozi na wafuasi wa upinzani huku Bw Tuju akitunukiwa nyadhifa zilizolenga kujumuisha jamii ya Luo.

Kando na wanasiasa, wanablogi, mabwenyenye wanaofadhili wanasiasa na vyombo vya habari vitakuwa na wakati mgumu baada ya joto la kisiasa kutulia kufuatia umoja wa rais na Bw Odinga.