Ruto amlima Uhuru

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto alitumia ziara yake katika eneo la Kisii kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta – hatua inayodhihirisha kwamba urafiki baina ya viongozi hao wawili hauwezi kufufuliwa tena licha ya wito wa maaskofu kutaka kuwapatanisha.

Akihutubu wikendi kwenye kikao cha faragha na viongozi wanaomuunga mkono katika Kaunti ya Kisii, Dkt Ruto alisema kwamba serikali ya Rais Kenyatta ilipoteza dira ya maendeleo tangu 2018 alipotangaza kushirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia kwa handisheki.

Alimkosoa Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa akisema kwamba handisheki haikuleta amani nchini. Badala yake, Dkt Ruto alidai, ilivuruga amani ndani ya chama cha Jubilee.

“Kuna wageni (Bw Odinga na viongozi wengine wa uliokuwa muungano wa NASA) waliotutembelea. Walikuja na mapepo kwani walivuruga kila ajenda tuliyokuwa nayo kubadilisha maisha ya Wakenya. Walikuja na mapepo ambayo yalisababisha wakuu wa chama kutimua wanachama wake huku wabunge wakipokonywa nyadhifa Bungeni. Je, hiyo ndiyo amani iliyoletwa na wageni?” akauliza.

Kwenye kikao hicho, Dkt Ruto alisema moja ya mipango iliyovurugika ni ule wa ujenzi wa nyumba 500,000 walizolenga kumaliza kufikia mwaka 2022 ili kuwasaidia Wakenya kupata makazi bora kwa bei nafuu.

Alisema kwamba kufikia sasa, serikali imefaulu kujenga nyumba 3,000 pekee.

Aidha, aliongeza kwamba serikali imefeli kutimiza ahadi yake ya kuboresha sekta nyingine muhimu kama vile afya na kilimo.

“Ikiwa huu ungekuwa mtihani, ni wazi serikali imefeli kabisa. Tatizo kuu ni kwamba tuliacha masuala muhimu na kuegemea shughuli za Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI),” akaeleza.

Alisema kuwa kutokana na mvurugiko uliotokana na handisheki, Chama cha Jubilee (JP) kilisambaratika kabisa na kuanza kuwahangaisha wanachama wake.

Aliongeza kwamba baada ya uchaguzi wa 2017, chama kilikuwa na karibu wabunge 170, lakini sasa kimebaki na wabunge kati ya 20 na 25.

“Tulipoanzisha Jubilee, tulikuwa na lengo la kukifanya kuwa chama cha kitaifa, kinyume na hali ambayo imekuwepo ambapo vyama vingi hubuniwa kwa misingi ya kikabila. Ni kwa ahadi hiyo ambapo Wakenya walituunga mkono kikamilifu na kuwachagua wabunge wengi zaidi ikilinganishwa na vyama vingine. Hata hivyo, chama kiligeuka kuwa jukwaa la vitisho na usaliti. Matunda ya handisheki yalikuwa ni kufukuzwa kwa viongozi chamani na wengine kutolewa katika kamati za Bunge na Seneti,” akasema Ruto.

Alipuuzilia mbali juhudi zinazoendeshwa kuunganisha Jubilee na ODM, akikitaja chama cha Jubilee kama kisicho na ushawishi wowote.

Licha ya mpango wa BBI kuanzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga, Dkt Ruto aliutaja kuwa “ulaghai mkubwa zaidi wa kisiasa kuwahi kushuhudiwa nchini.”

Kauli hiyo ni licha ya Rais Kenyatta kusisitiza kwamba mpango huo ulilenga kuwafaidi Wakenya kwa kuongeza mgao wa fedha unaotumwa katika serikali za kaunti.

“BBI ilikuwa njama ya kuturudisha katika enzi ya Rais mwenye mamlaka kupindukia. Hii ni licha ya Wakenya kupinga hilo kupitia harakati za kushinikiza mageuzi ya kikatiba kwa zaidi ya miaka 30,” akasema.

Hapo Jumapili, Dkt Ruto pia alijitetea vikali dhidi ya lawama za kukataa kushiriki mazungumzo ya kutafuta muafaka kati yake na Rais Kenyatta yaliyoitishwa na maaskofu wa kanisa Katoliki.

Kwenye ujumbe alioweka kwenye mitandao ya kijamii, Dkt Ruto aliambatanisha barua aliyowatumia maaskofu hao, akisema amekuwa tayari kushiriki mazungumzo bila masharti yoyote.

Kauli yake ilionekana kumwelekezea lawama Rais Kenyatta kama ndiye aliye kizingiti kikuu kwa mazungumzo hayo.

Waliosuka majonzi ya Wakenya mwaka 2018

Na CHARLES WASONGA

MNAMO Agosti 21, 2018, Rais Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi walishirikiana kusukuma kupitishwa kwa Mswada wa Fedha ambao umechangia kupanda kwa bei za bidhaa muhimu nchini.

Mswada huo, ambao sasa ni sheria, ulipitishwa kwa ‘baraka’ za watatu hao licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya wabunge.

Kinaya ni kwamba Bw Odinga, Spika Muturi na baadhi ya wabunge ni miongoni mwa viongozi ambao wamelaani kuongezwa kwa bei ya mafuta wiki iliyopita.

Mwishoni mwa wiki jana, Bw Muturi aliwapa changamoto wabunge alipowataka kuleta mswada wa kubatilisha sheria ya kifedha 2018 “badala ya kulalamika”.

Jumanne, Spika wa Bunge la Kitaifa Bw Justin Muturi aliipa Kamati ya Fedha siku 14 ichunguze sababu zilizochangia kupandishwa kwa bei ya mafuta na ipendekeze mabadiliko ya sheria kuipunguza.

Hii ni kufuatia malalamishi aliyopokea kutoka kwa Wakenya – Antony Manyara na John Wangai- ambao walipendekeza kuwa kipengele cha 13 cha Sheria ya Fedha, 2018 kifutiliwe mbali ili kuondoa ushuru wa VAT unaotozwa bidhaa za mafuta.

“Vile vile, ninatoa amri hii kwa mujibu wa malalamishi ambayo yamewasilishwa na Mbunge wa Matungulu Stephen Mule na ombi kutoka kwa Mbw Simba Arati (Dagoretti) na Mbunge Maalum Wilson Sossion kwamba bunge liahirishe shughuli zake za kawaida ili kujadili suala hili lenye umuhimu wa kitaifa,” Bw Muturi akasema Jumanne alasiri bunge liliporejelea vikao baada ya likizo ya mwezi mmoja.

Spika huyo aliitaka kamati hiyo ya Fedha inayoongozwa na Mwakilishi wa Homa Bay, Gladys Wanga kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau wote husika kabla ya kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwa kikao cha bunge lote.

Mjadala kuhusu suala hilo ulichacha bungeni huku wabunge wa mirengo yote wakielekeza lawama kwa Rais Kenyatta kutokana na mienendo yake ya kuingilia utendakazi wa asasi hiyo kwa kurejesha miswada na mapendekezo mbalimbali.

Mnamo 2018, wabunge walipopendekeza kwenye Mswada wa Fedha wa 2018 kuondolewa kwa baadhi ya ushuru kwa msingi kuwa ungelemea raia, Rais Kenyatta alikataa mapendekezo hayo na kuurudisha bungeni.

Kwenye memoranda yake kwa Bunge, Rais Kenyatta alipendekeza kurudishwa kwa ushuru huo ulivyokuwa mwanzoni pamoja na kuanzishwa kwa ushuru wa thamani (VAT) ya petroli.

Awali, Rais na Bw Odinga waliongoza mikutano ya wabunge wa mirengo yao kuwashinikiza waunge mkono kupitishwa kwa mswada huo licha ya kuwa wazi ungewatwika wananchi mzigo mzito.

Rais Kenyatta aliongoza mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee katika Ikulu ya Nairobi huku Bw Odinga akikutana na wabunge wa uliokuwa muungano wa Nasa katika makao makuu ya ODM.

Rais Kenyatta na Bw Odinga, waliongoza mikutano hiyo mnamo Septemba 21, 2018 asubuhi kabla ya suala hilo kujadiliwa na kupigiwa kura bungeni katika kikao cha alasiri.

Mjadala kuhusu suala hilo uliibua joto kali alasiri hiyo kati ya wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga dhidi ya waliokuwa wakipinga hasa kuanzishwa kwa VAT ya mafuta.

Hatimaye kura ya sauti ilipopigwa, Spika wa Muda, Soipan Tuya alitangaza kuwa upande wa “NDIYO” ulishinda na hivyo kupitisha pendekezo la Rais Kenyatta kwenye memoranda hiyo.

Hii ni licha ya kwamba sauti ya upande wa “LA” ilikuwa na wengi zaidi.Fujo zilizuka bungeni kati ya mirengo hiyo miwili na kumlazimisha Spika Muturi kuingilia kati.

Katika uamuzi wake, Bw Muturi alimtetea Bi Tuya, ambaye ni Mbunge Mwakilishi wa Narok, akisema wakati wa kura ni wabunge 173 pekee waliokuwa ukumbini, na hivyo “mapendekezo ya Rais yamepita”.

“Takwimu zilizonaswa kwenye mitambo ya kieletroniki zinaonyesha kuwa wakati wa upigaji kura ni wabunge 173 pekee walikuwepo ukumbini. Kwa hivyo, wabunge wameshindwa kubatilisha mapendekezo ya Rais kwani kikatiba ni wabunge 233 wanaohitajika wakati wa upigaji kura,” akaeleza Bw Muturi.

Akaongeza: “Kwa hivyo, mapendekezo ya Rais yatajumuishwa kwenye Mswada wa Fedha wa 2018 kabla ya kurejeshwa kwake autie sahihi.”

Kulingana na kipengele cha 115 (1) (b) Rais ana mamlaka ya kukataa kutia saini mswada kisha kuurejesha bungeni na memoranda yenye mapendekezo kadhaa anayotaka yajumuishwe na wabunge.

Thuluthi mbili za wabunge (233) huhitajika ili kutupilia mbali mapendekezo hayo ya rais.

Rais Kenyatta aliutia sahihi mswada huo jioni hiyo hiyo, Septemba 21, 2018, na kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, bidhaa za mafuta zikaanza kutozwa VAT ya kiwango cha asilimia nane.

Serikali ililenga kukusanya Sh130 bilioni zaidi kutokana na hatua hiyo.Nayo mafuta taa yalianza kutozwa ada ya ziada ya Sh18 kwa kila lita katika kile ambacho serikali ilisema ni kuzuia mienendo ya wafanyabiashara laghai kuchanganya bidhaa hiyo na dizeli.

Sheria hii pamoja na Sheria ya Ushuru ya 2020 iliyopandisha viwango vyote vya ushuru ili kufidia mfumuko wa bei, ndiyo iliyochangia bei ya mafuta kupandishwa kwa kiwango kikubwa wiki jana.Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, petroli inauzwa kwa Sh134.7 kwa lita jijini Nairobi, dizeli Sh115.5 na mafuta taa ni Sh110.2.

Hatua hii imechangia kuongezeka kwa gharama ya maisha kwa kiwango kikubwa wakati huu ambapo raia wanaathirika na makali ya Covid-19.

Wataalamu wa uchumi wanasema wabunge wamekuwa sehemu ya matatizo ya kiuchumi yanayokumba Kenya kwa sasa.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la International Center for Policy and Conflict, Ndung’u Wainaina, wabunge hawawezi kujinasua kutokana na lawama kuhusu matatizo ya kiuchumi nchini.

“Katiba ya Kenya (2010) iliwapa wabunge mamlaka ya kuamua viwango vya ushuru, kuidhinisha bajeti na matumizi, kuweka sheria za ukopaji madeni ya kitaifa na kusimamia matumizi ya pesa zilizokusanywa kutokana na ushuru,” akasema Bw Wainaina.

Uhuru asimamisha jaji kazi

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amemsimamisha kazi Jaji Muthoni Gathumbi wa Mahakama Kuu kufuatia ushauri wa Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) na kuteua jopo la kuchunguza ufaafu wa jaji huyo kuhudumu.

Rais Kenyatta alisema alichukua hatua hiyo baada ya JSC kumweleza kuwa Jaji Gathumbi hawezi kutekeleza majukumu yake ya jaji ipasavyo.

Kulingana na JSC, Jaji Gathumbi aliyekuwa akihudumu katika kitengo cha kusikiliza kesi za mizozo ya ardhi hana uwezo unaofaa kiakili kutekeleza majukumu yake.

“JSC, baada ya kuchunguza ripoti kadhaa za matibabu, iliridhika sababu za kumuondoa ofisini kutokana na kukosa uwezo wa kutekeleza majukumu ya ofisi zilikuwa zimethibitishwa,” Rais Kenyatta alisema kwenye ilani katika gazeti rasmi la serikali.

Sheria inasema Rais akipata ombi kama hilo kutoka kwa JSC, anafaa kuteua jopo kulichunguza.Jopo hilo litachunguza ombi la kumuondoa Jaji Gathumbi ofisini na kuwasilisha ripoti kwa rais.

Jopo hilo litasimamiwa na Jaji Hellen Amolo na wanachama wake ni Majaji Luka Kimaru, na Linnet Ndolo, Bw Peter Murage, Bi Martha Nyakado, Dkt Frank Njenga na Dkt Margaret Othieno.

Ripoti ya jopo hili itaamua iwapo Rais Kenyatta atakubali ombi la JSC la kumuondoa ofisini Jaji Gathumbi.

Hii ni mara ya kwanza kwa JSC kupendekeza jaji kuondolewa ofisini kwa madai inayochunguza. Rais huwa anakubali ombi la tume jopo analoteua linapochunguza na kuthibitisha madai.

Jopo likikosa kuthibitisha madai jaji husika huwa anaendelea kuhudumu.

Rais Uhuru abadilisha mbinu kuendelea kung’ata Mlimani

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta amebuni mbinu mpya kuimarisha usemi wake katika ukanda wa Mlima Kenya, anapojiandaa kung’atuka uongozini mwaka 2022.

Rais Kenyatta sasa anawatumia mawakala kuwafikia wanasiasa waasi, kinyume na awali, ambapo alikuwa akienda moja kwa moja kwa viongozi kuwalaumu kwa kuikosoa serikali yake.

Duru zinasema hilo ndilo limewafanya baadhi ya viongozi ambao walikuwa wakimkosoa kushusha misimamo yao mikali ya kisiasa na kuonyesha dalili za kuanza kumuunga mkono.

Wiki iliyopita, wanasiasa Mwangi Kiunjuri, mbunge Moses Kuria na kiongozi wa Narck-Kenya, Martha Karua, walitangaza mikakati ya kuwaleta pamoja viongozi wa vyama mbalimbali vya kisiasa katika eneo hilo ili “kubuni sauti ya pamoja” ielekeapo 2022.

Bw Kiunjuri ndiye kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) huku Bw Kuria akiongoza Chama Cha Kazi (CCK).Watatu hao walitangaza juhudi za kuwaunganisha viongozi wa zaidi ya vyama 15 katika Ukumbi wa Jumuiya, mjini Limuru, katika kikao kinachoitwa ‘Limuru III.’

Hata hivyo, imeibuka kuwa viongozi hao wameshusha misimamo yao baada ya Rais Kenyatta kuwatuma mawakala wa kisiasa kwao kuwarai “kutathmini mustakabali wa kisiasa wa Mlima Kenya” kutokana na misimamo yao ya kisiasa.Mbali na hayo, imeibuka mawakala hao waliambiwa “kwenda pole pole”, ili kusikiliza malalamishi yote ya viongozi hao.

“Waliambiwa kusikiliza malalamishi yote ya viongozi waasi ili kubuni utaratibu utakaotumiwa kusikiliza malalamishi yao,” zikaeleza duru.Juhudi hizo ndizo zimetajwa kuwashinikiza baadhi ya viongozi kama Bw Kiunjuri na Bw Kuria kuonekana kubadilisha uungwaji mkono wao dhidi ya Naibu Rais William Ruto.

Duru zimeliambia ‘Jamvi la Siasa’ kuwa lengo kuu la Rais Kenyatta ni kuhakikisha eneo hilo limeungana anapojitayarisha kung’atuka uongozini. Inaelezwa ni baada ya kuhakikisha ngome yake imeungana ndipo atakapoanza kumpigia debe kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwa mrithi wake.

“Lengo la Rais Kenyatta ni kuhakikisha anamuuza Bw Odinga katika mazingira tulivu na ambayo hatapata pingamizi kubwa za kisiasa. Hili ni kinyume na ilivyo sasa ambapo eneo hilo limegawanyika vikali, hasa miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakimpigia debe Dkt Ruto,” akaeleza mbunge mmoja ambaye hakutaka kutajwa.

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa Rais amechukua mwelekeo huo mpya baada ya kubaini kwamba mbinu yake ya awali kuwakashifu viongozi hadharani ilikuwa ikizua migawanyiko baina yao.

Rais Kenyatta alikuwa akiwakosoa wanasiasa wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ hadharani, akiwaonya “atawafikia hata katika mafichoni mwao.”

Rais ametoa kauli hizo mara kadhaa kwa lugha asili ya Gikuyu, ambako amehojiwa na vituo vya redio vinavyotangaza kwa lugha hiyo.Rais pia alitoa maonyo kama hayo katika vikao viwili ambavyo vimefanyika katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, kutathmini mwelekeo wa kisiasa wa ukanda huo.

“Ni wazi kauli za Rais Kenyatta zilizua migawanyiko miongoni mwa viongozi na wafuasi wao. Wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walikuwa wakitumia kauli zake kuonyesha jinsi ‘alivyowasahau’ wenyeji wa Mlima Kenya wakilenga kujijenga kisiasa,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Duru zinasema Rais Kenyatta na washirika wake wamekuwa wakimtumia mbunge Kanini Keega (Kieni) kuwafikia wanasiasa waasi.Inaelezwa hilo ndilo limekuwa likifanya ziara ya kumuuza Bw Odinga Mlima Kenya kuahirishwa kwa mara kadhaa.

Mikakati ya kumpigia debe Bw Odinga katika eneo hilo iliibuka tangu 2019, japo haijawahi kufanyika.Washirika wa karibu wa Rais Kenyatta wamekuwa wakihofia kukabiliwa na pingamizi za kisiasa ambazo zimekuwa zikimwandama Bw Odinga kwa muda mrefu katika eneo hilo.

Mara tu baada ya kuibuka kwa mpango wa kuandaliwa kwa kikao cha Limuru III, Bw Kega aliwashukuru wanasiasa katika ukanda huo, akisema “wameona mwanga.”

“Huu ni mwelekeo wa kuridhisha sana. Ni wazi lazima eneo la Mlima Kenya liwe na sauti moja ielekeapo 2022. Hatuwezi kuruhusu ‘watu kutoka nje’ kutuamulia mwelekeo tutakaofuata. Nawashukuru sana Bw Kuria, Bw Kiunjuri, Bi Karua na viongozi wake wote ambao wameona haja ya Mlima kuzungumza na sauti moja,” akasema Bw Keega.

Wadadisi wanasema mwelekeo huo ndio umemsukuma Bw Odinga kuanza kufanya vikao na mabwanyenye wa kisiaa kutoka Mlima Kenya, wakati Rais Kenyatta anaendelea “kutuliza mazingira ya kisiasa” ili kumpigia debe.

“Wakati juhudi hizo zitafaulu, itakuwa rahisi kumpigia debe Bw Odinga kwani tayari atakuwa amepata uungwaji mkono kutoka kwa mabwanyenye, wanasiasa wenye ushawishi na wenyeji,” asema Bw Oscar Plato, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, washirika wa Dkt Ruto wanashikilia kuwa hakuna juhudi zozote ambazo zimaweza kuwashinikiza wenyeji wa ukanda huo kumuunga mkono Raila kwani “wamechoshwa na utawala wa Rais Kenyatta.”

“Huwezi kuwalazimisha wananchi kuhusu viongozi watakaowaunga mkono. Wao ndio watajifanyia maamuzi huru,” asema mbunge Rigathi Gachagua (Mathira).

Ziara ya Rais eneo la Magharibi yayumba

BENSON AMADALA na SHABAN MAKOKHA

UTATA umezuka kuhusu ziara ambayo Rais Uhuru Kenyatta alitarajiwa kuanza leo katika eneo la Magharibi.

Kulingana na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na Waziri wa Mafuta na Madini, Bw John Munyes, Rais Kenyatta alikuwa amepangiwa kuwasili mjini Kakamega leo Jumapili.

Hata hivyo, kumekuwa na majibizano makali kati ya viongozi wa kisiasa katika eneo hilo kuhusu taratibu za kuwajumuisha viongozi wote kwenye ziara hiyo.

Wabunge kutoka eneo hilo wamekuwa wakitofautiana vikali kuhusu ziara hiyo.

Baadhi yao walitishia kuteka mipango na maandalizi ya ziara hiyo.

Wabunge hao wenye ghadhabu wanawalaumu magavana kwa kuwatenga kwenye mipango inayoendelea kumpokea rais.

“Kwa kuwa hii ni ziara ya serikali ya kitaifa kuhusu maendeleo, tutachukua maandalizi yake kwani usimamizi na uendeshaji wa miradi ya kitaifa ni jukumu letu. Magavana wana serikali zao, hivyo hawawezi kuchukua majukumu yetu,” akasema mbunge wa Lugari, Bw Ayub Savula.

Mkutano maalum wa viongozi uliopangiwa kufanyika Ijumaa kuhusu ziara hiyo haukufanyika, baada ya wabunge kusema hawakuwa wamefahamishwa kuhusu uwepo wake.

Gavana Oparanya alikuwa ameahidi kuandaa kikao cha viongozi kutoka eneo hilo kuwaleta pamoja ili kuondoa tofauti zilizopo baina yao.

Hata hivyo, wabunge wanasisitiza watachukua udhibiti za ziara hiyo kwani inahusu miradi ya kitaifa.

“Tutakutana jijini Nairobi wiki ijayo kujadiliana zaidi kuhusu ziara hiyo. Baadaye, tutawaalika magavana kujiunga nasi kabla ya kukutana na Rais kupanga ziara hiyo kikamilifu,” akasema Bw Savula.

Akaongeza: “Hatujali muda ambao Rais atachukua kabla ya kuzuru Magharibi. Tunaloshikilia ni kuwa lazima mipango inayoendeshwa imshirikishe kila mmoja. Wakati alizuru Nyanza, kiongozi wa ODM, Raila Odinga aliendesha mipango hiyo kwa kuwajumuisha viongozi wote,” alisema.

Akaongeza, “Ndivyo alivyofanya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, wakati Rais alipozuru eneo la Ukambani. Vivyo hivyo, tutawashirikisha viongozi wetu Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kwenye mipango hiyo.”

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamesema hawatahudhuria mkutano huo wa Nairobi, wakieleza kuwa inatosha Rais kukutana na magavana na kupanga ziara hiyo.

Wabunge wanaowaunga mkono Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula walikuwa wametishia kususia ziara ya Rais Kenyatta, wakisisitiza viongozi hao hawakushirikishwa kwenye mipango ya maandalizi ya ziara hiyo.

Hata hivyo, mbunge maalum Godfrey Osotsi alipuuzilia mbali kauli hizo, akisema kuwa ziara ya Rais haipaswi kuingizwa siasa.

“Rais Kenyatta ndiye kiongozi wa nchi. Yuko huru kuzuru mahali popote nchini bila kuomba ruhusa kutoka kwa mtu yeyote. Ninaunga mkono juhudi zozote ambazo zinalenga kulistawisha eneo letu kimaendeleo,” akasema Bw Osotsi.

Alisema wale ambao wanapinga ziara ya Rais Kenyatta pia walisusia mkutano ulioitishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ambaye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa kuhusu Miradi ya Serikali.

Mkutano huo ulifanyika katika Taasisi ya Kukuza Mitaala Kenya (KICD), jijini Nairobi.

Jamii ndogo zataka Rais abuni wizara iwasaidie

Na CECIL ODONGO

VUGUVUGU la Wasomi kutoka jamii ndogo zilizotengwa, limemrai Rais Uhuru Kenyatta kubuni wizara ambayo itayashughulikia haki zao likidai kubaguliwa kuhusu masuala mbalimbali nchini.

Wanachama wa vuguvugu hilo wanatoka katika jamii ndogo 79 kwenye kaunti 29 huku lengo lao kuu ni kuhakikisha matakwa yao yanazingatiwa na serikali kuu pamoja na zile za kaunti.

Viongozi wa kundi hili wakiongozwa na mlezi wake Amos Ole Mpaka, mwenyekiti Charles Nandaini na mwakilishi wa jamii ya Kiarabu katika Kaunti ya Wajir Khadija Mohamed, walisema kuwa wakati umewadia kwa jamii hiyo kupigania haki ili kunufaika kimaendeleo.

Bw Ole Mpaka alisema kutokana na utawala na ubabe wa jamii kubwa kubwa haswa, maslahi ya makabila madogo yamekosa huduma bora za kiafya, miundombinu, maji na pia mara nyingi wao hubaguliwa wakati wa utoaji wa ajira katika taasisi mbalimbali za serikali.

“Tunamwomba Rais abuni wizara au shirika ambalo litatusimamia kukomesha ubaguzi wa tangu jadi dhidi yetu. Hata baada ya ujio wa utawala wa ugatuzi, maazimio ya wawakilishi wetu huwa hayatiliwi manani kutokana na idadi yetu ndogo,” akasema Ole Mpaka katika mkahawa moja wakati wa kuzindua vuguvugu hilo.

Aidha walilaumu viongozi kutoka makabila makubwa kuwahadaa kupitia nafasi za uteuzi kisha kugeuka baadaye na kupuuza maslahi yao.

Hasa walitaja kuwa kutokana na idadi yao ndogo, huwa hawahusishwi hasa katika masuala ya upangaji wa miradi ya maendeleo.

“Ni kweli kwamba hatuwezi kushinda cheo chochote lakini tunapoafikiana na jamii kubwa kuhusu masuala ya uongozi, maelewano hayo yaheshimiwe na yasitumiwe kutudhalilisha,” akaongeza.

Diwani wa wadi ya Terik, Kaunti ya Nandi Osborne Komen alisimulia jinsi ambavyo mswada wake wa kupendekeza ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi ulivyoangushwa na madiwani kutoka jamii kubwa, huku akitoa wito nafasi nyingi za uteuzi zitolewe kwa jamii ndogondogo.

Mawakili wakosoa hatua ya kushtaki rais

Na RICHARD MUNGUTI

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumatano aliiomba mahakama ya rufaa ibatilishe uamuzi wa majaji watano kwamba anaweza kushtakiwa akiwa afisini.

Kupitia kwa mawakili wake, Rais Kenyatta aliyekata rufaa kupinga marufuku ya BBI aliomba uamuzi kwamba anaweza kushtakiwa ufutiliwe mbali.

Majaji saba wa mahakama ya rufaa waliambiwa uamuzi Rais Kenyatta ashtakiwe unaweza kutifua vita, vurumai na umesababisha mtafaruku wa kikatiba.

Mawakili Waweru Gatonye, Mohammed Nyaoga na Kimani Kiragu walisema sheria inamlinda Rais dhidi ya kufunguliwa mashtaka akiwa afisini.

Mabw Gatonye, Nyaoga na Kiragu waliwaambia majaji saba wa mahakama ya rufaa kuwa, majaji hao watano wa mahakama kuu walikosea kisheria walipoamua Rais Kenyatta anaweza shtakiwa.

“Rais Kenyatta hakushiriki kwa njia yoyote ile katika kesi iliyowasilishwa katika mahakama kuu na walalamishi zaidi ya 70 waliopinga mchakato wa mageuzi ya katiba almaarufu BBI,” Bw Gatonye aliambia mahakama ya rufaa jana. Bw Gatonye alisema Majaji Joel Ngugi, George Odunga, Enoch Chacha Mwita , Jairus Ngaah na Teresia Matheka hawakumpa fursa Rais Kenyatta kujibu madai kuwa alichangia kuzinduliwa kwa mchakato wa mageuzi ya katiba.

“Rais Kenyatta alikejeliwa kimakosa na majaji hao watano bila ya kupewa fursa ya kujitetea,” alisema Bw Gatonye.

Bw Nyaoga alisema Rais Kenyatta yuko na haki ya kushiriki katika masuala ya mageuzi ya katiba kama mwananchi na wala sio kama Rais.

“Naomba hii mahakama ikumbuke kuwa mchakato wa mageuzi ya Katiba ni suala la kisiasa linalowahusu wananchi wote,” alisema Bw Nyaoga.

Alisema Rais Kenyatta akiwa kiongozi wa chama kinachotawala cha Jubilee, anaweza kushiriki katika suala lolote la kisiasa.

Majaji hao saba walielezwa kuwa kutatokea mtafaruku wa kikatiba ikiwa Rais atafunguliwa mashtaka kutokana na utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba.

Pia Mabw Nyaoga , Gatonye na Kiragu walisema majaji hao watano wa mahakama hawakufuata mwongozo uliotolewa na Mahakama ya Juu kwamba “ Rais analindwa na katiba kama mwananchi yoyote yule.”

Uhuru atikisa demokrasia

Na WANDERI KAMAU

KENYA imo kwenye hatari ya kuzama kidemokrasia ikiwa Rais Uhuru Kenyatta na washirika wake hawatakoma kuhujumu idara huru za kukuza na kudhibiti utawala wa kisheria.

Wakosoaji wanasema ikiwa Rais Kenyatta atafanikiwa kulemaza Idara ya hakama kama alivyotishia akihutubia taifa siku ya Madaraka Dei mnamo Jumanne, basi atakuwa amefanikiwa kurejesha Kenya katika enzi za udikteta.

Tayari Rais Kenyatta amefanikiwa kudhibiti taasisi zingine muhimu katika kulinda utawala wa kidemokrasia kama vile Bunge, Seneti, Upinzani, vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za umma.

Wadadisi na wataalamu wa masuala ya sheria wamekosoa vikali kauli ya Rais Kenyatta ya kutoa vitisho kwa majaji, wakisema hana haki hata kidogo kuamulia Mahakama utaratibu wake wa kufanya kazi.

“Ni kinaya kwa Rais Kenyatta kuanza kulalamika vile maamuzi ya mahakama yanavyoathiri nchi kiuchumi, ilhali yeye ndiye chanzo kikuu cha hali mbaya ya uchumi nchini.

“Kwa mfano, serikali imekuwa ikifanya kila iwezalo kuwalazimisha Wakenya kukubali BBI licha ya utaratibu mzima kuendeshwa kinyume cha Katiba. Anapaswa kujilaumu mwenyewe,” asema Dkt Barack Muluka, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa.

“Vitisho dhidi ya taasisi huru ni kuturejesha katika enzi ya chama kimoja. Lazima Wakenya wasimame kidete kutetea Katiba na mafanikio yote tuliyopata kutokana na juhudi za wazalendo waliojitolea maisha yao kuipata Katiba mpya,” akasema Kiongozi wa Narc-Kenya, Martha Karua kwenye mahojiano Jumatano.

Kauli yake inawiana na hisia za mwanaharakati Ndung’u Wainaina, anayetaja vitisho vya Rais Kenyatta kama “urejeo wa udikteta.”

“Vitendo vya Rais Kenyatta vinaonyesha yeye ni kiongozi ambaye nia yake ni kuendelea kukwamilia mamlakani,” akasema Bw Wainaina, ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro (ICPC).

Mbunge Rigathi Gachagua wa Mathira, anasema Rais Kenyatta ataacha historia mbaya iwapo hatajitolea kulinda Katiba.

“Ninamfahamu kwa undani Rais Kenyatta kwani nishawahi kuwa msaidizi wake wa kibinafsi. Namshauri kuzingatia Katiba na kuheshimu taasisi huru ikiwa anataka kukumbukwa na vizazi vijavyo,” akasema mbunge huyo.

TAASISI KUHUJUMU SERIKALI

Hata hivyo, watetezi wa Rais Kenyatta wanakosoa vikali taasisi zinazohujumiwa na serikali, wakisema kuna haja ya kudhibiti uhuru wazo.

“Hatuwezi kuwa na taasisi ambazo zinahatarisha uthabiti wa nchi kwa kisingizio cha kuendeleza uhuru wake. Matakwa ya wananchi lazima yazingatiwe na taasisi yoyote ile inapofanya maamuzi,” akasema Mbunge wa Kieni, Kanini Kega.

Mwenzake Ngunjiri Wambugu wa Nyeri Mjini naye aliwataja wakosoaji wa rais kama “wabinafsi.”:

“Wanasiasa na wanaharakati ambao wanamkosoa rais ni watu wanaojali maslahi yao pekee. Lengo lao ni kuvuruga utendakazi wa serikali ili baadaye kupata nafasi ya kumkosoa rais kwa kutotimiza malengo yake,” akasema Bw Wambugu kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Ingawa kulikuwa na matumaini kuwa Idara ya Mahakama ingefungua ukurasa mpya baada ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome majuzi, azma hiyo ilididimia Jumanne baada ya Kiongozi wa Taifa kuikashifu vikali na kuipa vitisho kwa maamuzi ambayo hayamfurahishi ikiwemo kuhusu BBI.

Hatua hiyo inaendeleza mtindo wake wa kudunisha Idara ya Mahakama, ambao amefanikisha kwa kupuuza maamuzi ya majaji na mahakimu.

Jumanne, Rais Kenyatta alifufua uhasama wake na mahakama kwa kurejelea hatua ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali uchaguzi mkuu wa 2017.

Kwenye hotuba yake jijini Kisumu, Rais Kenyatta aliikashifu vikali idara hiyo, akiitaja kuwa “kikwazo katika kuwawezesha Wakenya kuendeleza haki yao ya kufanyia mabadiliko Katiba kupitia BBI.”

Mbali na kurukia mahakama kwa kuzima BBI, Rais Kenyatta amekuwa mkali dhidi ya yeyote anayejaribu kumkosoa, wakiwemo wabunge na maseneta walio na maoni tofauti na yake.

Miongoni mwao ni Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a), aliyekuwa Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, Mbunge Aden Duale (Garissa Mjini) aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) aliyekuwa Kiranja wa Wengi Bungeni.

Katika juhudi za kuzima sauti huru, serikali vile vile haijazisaza vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za umma.

Vita dhidi ya vyombo vya habari vilianza baada ya serikali kubuni Mamlaka ya Kudhibiti Matangazo (GAA).

Ingawa serikali ilidai lengo la kubuni mamlaka hiyo lilikuwa kulainisha utaratibu wa utoaji matangazo ya kibiashara ya taasisi za serikali, mamlaka hiyo imelaumiwa kwa kutumia matangazo kunyamazisha kudhibiti vyombo vya habari.

Vyombo vya habari vimekuwa vikilalamika kuhusu kutolipwa mamilioni ya pesa, hali ambayo inatatiza ustawi wa uanahabari nchini.

Waombaji wasiotenda

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wa kisiasa nchini jana walishutumiwa vikali wakati wa maombi ya kitaifa, kwa kuendelea kuonyesha unafiki mkubwa machoni mwa Wakenya.

“Tuache unafiki. Imani na matumaini peke yake hazitaweza kutusaidia. Tunahitaji vitendo. Kwa hivyo tukitoka hapa, twende tuchukue hatua,” akasema Seneta Amos Wako wa Busia kwenye hafla iliyohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto katika Majengo ya Bunge.

Bw Wako alisema inasikitisha kuwa Wakenya wengi hawawezi kumudu gharama ya matibabu yakiwemo ya Covid 19, licha ya ahadi nyingi za serikali ya Jubilee za kutekeleza mpango wa Afya kwa Wote.

Wakili Peter Waiyaki, ambaye alikuwa mnenaji rasmi kwenye hafla hiyo, alisema Wakenya wanaweza kupata matumaini ya dhati wakipalilia uadilifu katika uongozi, kukumbatia uzalendo, kutekeleza na kuonyesha kwa vitendo kwamba wamejitolea kufanya hivyo.

“Uadilifu ni kutimiza unayoahidi kufanya. Kukosa uadilifu kunawapokonya raia matumaini na kuharibu nchi,” akasema Bw Waiyaki.

Wakili huyo alisema viongozi hawafai kutarajia Wakenya kuwa waadilifu ikiwa wao wanapuuza maadili na utawala wa kisheria.

“Ni jukumu la kila mtu kuwa muadilifu. Ikiwa hauwezi kuzingatia na kudumisha uadilifu, jiuzulu wadhifa wako,” akasisitiza Bw Waiyaki.

Bw Waiyaki alisema kama viongozi wa Kenya wangekuwa wazalendo, hakungekuwa na uporaji wa mali ya umma na kudhulimiwa kwa wananchi.

Jumbe za Bw Wako na Bw Waiyaki ziliwalenga viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakitenda kinyume na matamshi yao.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta aliwataka viongozi kuwajibika zaidi kwa vitendo vyao badala ya kuzungumza mazuri kwenye mkutano kama wa jana na kueneza migawanyiko baadaye.

“Tumesikia yaliyohimizwa hapa na siwezi kuondoa hata moja. Tungekuwa watu wa vitendo, maadili, uwajibikaji na kutenda haki, nchi ingekuwa na matumaini,” akasema.

Rais Kenyatta mwenyewe amekuwa na mazoea ya kukiuka maagizo ya mahakama na kutotimiza ahadi zake kwa umma hasa Ajenda Nne Kuu za afya kwa wote, nyumba za bei nafuu, viwanda na utoshelevu wa chakula.

Hapo jana alilaumu bunge kwa kuchelewesha sheria za kufanikisha ajenda zake hasa kuhusu utekelezaji wa afya kwa wote. Hii ni licha ya ukweli kuwa mpango huo ulikwama katika awamu ya majaribio katika baadhi ya kaunti.

Katika mikutano ya awali ya maombi, wanasiasa hao wakiwemo Rais Kenyatta, Dkt Ruto, Raila Odinga (ODM) na Kalonzo Musyoka (Wiper) wamekuwa wakiahidi makubwa, lakini muda mfupi baadaye huwa wanapuuza ahadi zao.

Hapo jana, viongozi hao wa kisiasa walinukuu maandiko matakatifu na kuomba huku wakitoa jumbe za matumaini kwa Wakenya, ambazo ni kinyume na vitendo vyao.

Walieleza matumaini ya Kenya kushinda janga la corona, ingawa waliodaiwa kupora mabilioni yaliyotengwa kukabili ugonjwa huo hawajachukuliwa hatua hata baada ya Rais Kenyatta kutoa agizo hilo mwaka jana. Baadhi ya waliotajwa katika sakata hiyo ni washirika wa viongozi wakuu serikalini.

Maombi hayo yalifanyika wakati kuna mgawanyiko mkubwa katika serikali na nchi kutokana na tofauti kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto hasa kuhusu siasa za urithi na mchakato wa BBI.

Ingawa viongozi wa kisiasa, kidini na sekta ya kibinafsi waliozungumza walisema kwamba ni muhimu kuungana kukabili changamoto zinazoikumba nchi, tofauti za rais na naibu wake zilikuwa wazi hata katika mkutano huo wa jana.

Dkt Ruto amekuwa akikosekana katika hafla za Rais Kenyatta ukiwemo ufunguzi wa Bandari ya Lamu, ambao alitaja jana kama mojawapo wa mambo mazuri yanayoleta matumaini nchini.

Kufanikisha refarenda sasa ni kama kushuka mchongoma

Na BENSON MATHEKA

Rais Uhuru Kenyatta ana nafasi finyu ya kisheria kutimiza ndoto ya kubadilisha katiba baada ya Mahakama Kuu kuamua alikiuka katiba katika maamuzi yake.

Ingawa anaweza kukata rufaa, itakuwa vigumu kwa kesi kuamuliwa kabla ya muda uliopangwa refarenda ifanyike. Waandalizi wa BBI walipanga kura ya maamuzi ifanyike kabla ya Agosti mwaka huu na utekelezaji wa baadhi ya mabadiliko yaliyopendekezwa ufanyike kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wataalamu wa katiba na wanaharakati wanasema nafasi ya kukomboa mchakato huo ni finyu sana kwa kuwa walalamishi wanaweza kuwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu iwapo korti ya rufaa itasimamisha uamuzi wa majaji wa Mahakama Kuu.

“Kwa maoni yangu haya ya BBI yamekwisha na Rais Kenyatta anafaa kusalimu amri tu na kusubiri amalize kipindi chake uongozini kwa amani,” asema Elias Mutuma. Wakili huyu anasema ikizingatiwa uamuzi huo ulitolewa na majaji watano, huenda ikawa vigumu kwa Mahakama ya Rufaa kuubatilisha.

Ingawa Rais Kenyatta amekuwa akipuuza maamuzi na maagizo ya korti, wanasheria wanasema kukaidi uamuzi kuhusu BBI kunaweza kumuacha na aibu zaidi.

Wanasema akitumia njia ya mkato na mchakato uendelee, kuna hatari ya Wakenya kuukataa katika refarenda kwa sababu mahakama imewafungua macho wakafahamu una nia fiche. “Uamuzi ulikuwa wa kina na nafasi anayoweza kupata ni kusimamishwa kwa uamuzi huo kupitia rufaa.

Hata hivyo, mfumo wa sheria na muda hauko upande wake na hatua atakayochukua itakuwa ya mabavu jambo ambalo litaendeleza sifa zake za kukaidi mahakama na utawala wa sheria,” asema mwanaharakati Oscar Ojiambo.

Baadhi ya maamuzi ambayo rais amepuuza ni kuapisha majaji 41 ambao waliteuliwa na Tume ya Huduma ya Mahakama yapata miaka miwili iliyopita, kumruhusu wakili Miguna Miguna kurudi Kenya, kuvunja bunge kwa kutotimiza hitaji la usawa wa jinsia.

Mahakama pia iliamua kwamba Idara ya Huduma ya Jiji la Nairobi lilibuniwa kinyume cha sheria. Mwezi jana, mahakama iliamua kwamba nyadhifa za mawaziri wasaidizi alizobuni sio za kikatiba lakini akapuuza.

Kulingana na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana uamuzi wa majaji Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Teresiah Matheka na Chacha Mwita ni wa kizalendo na ni vigumu kukata rufaa kuupinga. Majaji hao walikosoa kila kitu kuhusu BBI na kuendelea na mchakato huo itakuwa ni kilele cha ukaidi.

Uamuzi wa mahakama wavuruga urithi wa Uhuru 2022

Na WANDERI KAMAU

UAMUZI wa Mahakama Kuu kufutilia mbali Mpango wa Maridhiano (BBI) umevuruga handisheki na mikakati ya Rais Uhuru Kenyatta kuandaa urithi wake 2022.

Kulingana na wadadisi wa siasa, uamuzi huo uliotolewa Alhamisi, umemwacha Rais Kenyatta kwenye njiapanda, ambapo itabidi atathmini upya mwelekeo wake kisiasa kuanzia sasa.

Tangu Rais alipobuni handisheki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, mnamo 2018, mpango huo umekuwa ukifasiriwa na baadhi ya wakosoaji wake kama njama ya kumtengenezea njia kiongozi huyo kutwaa urais 2022.

Hata hivyo, hali ilibadilika katika siku za hivi karibuni, baada ya Rais Kenyatta kuonekana kuupendelea muungano wa One Kenya Alliance, unaowashirikisha kiongozi wa chama ANC, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Mdadisi wa siasa Javas Bigambo anasema kuna uwezekano mkubwa uamuzi huo “umeashiria mwisho wa handisheki na BBI.”

“Kile kilichowaunganisha Rais Kenyatta na Bw Odinga ni masuala hayo mawili kwa miaka mitatu ambao mchakato umekuwa machoni mwa Wakenya. Kuvurugika kwake kunamaanisha ukaribu wa kisiasa wa wawili hao umeisha, ikiwa hakutakuwa na nafasi yoyote kwa wale wanaoendesha mpango huo kuwasilisha rufaa mahakamani,” asema Bw Bigambo.

Anaeleza hilo pia litatoa nafasi kwa miungano mipya ya kisiasa kubuniwa, hasa miongoni mwa viongozi waliohisi kutengwa na mchakato huo.

“Tutashuhudia wanasiasa wakibuni miungano ya kisiasa kwa misingi ya ‘kulipiza kisasi’ kutengwa kwao katika mpango huo,” anasema.

Wanasema athari nyingine ni kuwa ushawishi wa Rais Kenyatta kama msemaji mkuu kwenye mchakato wa urithi utapungua sana.

“Wanasiasa walikuwa wakipigania kuwa karibu na Rais wakilenga kutangazwa kama warithi wake. Hilo ndilo lilikuwa lengo kuu la kubuniwa kwa One Kenya Aliance. Hali imebadilika. Itabidi aanze mkakati mpya ili kurejesha usemi wake tena,” asema mdadisi wa siasa Mark Bichachi.

Uhuru atupa marafiki

Na BENSON MATHEKA

WALIOKUWA marafiki wa kisiasa wa Rais Uhuru Kenyatta wamesema uhusiano wao na kiongozi wa taifa ulivunjika alipoamua kubadilisha mtindo wake wa uongozi baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Miongoni mwa marafiki hao ni waliokuwa wafuasi sugu wa Rais Kenyatta tangu 2002 alipogombea urais kwa mara ya kwanza, na wengine hata walikuwa wasaidizi wake wa kibinafsi

Wengi wao walikuwa watetezi wake wakuu aliposhtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) pamoja na Naibu Rais William Ruto.

Marafiki hao wa zamani wa rais sasa wanasema walijipata nje ya serikali walipoanza kumkosoa kuhusu mtindo wake mpya wa uongozi baada ya uchaguzi wa 2017, na wengi wao wamelipia gharama kwa kutengwa katika utawala, kufutwa kazi na baadhi kudai kuhangaishwa.

Naibu Rais William Ruto anasema kuwa urafiki wake na rais ulizorota alipoamua kufanya kazi na waliokuwa wapinzani wa Jubilee: “Mtindo wake ulibadilika na ana haki ya kufanya hivyo kwa kuwa ndiye mkubwa. Kwa sababu ya kubadilisha mtindo, nafasi yangu ilichukuliwa na watu wengine.”

Wakati wa kampeni za 2013 na muhula wa kwanza wa serikali ya Jubilee, wawili hao walikuwa marafiki wakubwa, lakini sasa hawaonani uso kwa uso.

Rafiki mwingine wa karibu ambaye aliishia kufutwa kazi ni aliyekuwa waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri, ambaye anasisitiza kuwa masaibu yake yalitokana na yeye kuwa rafiki wa Dkt Ruto: “Kufikia sasa, rais hajaeleza kwa nini alinifuta. Ni haki yake kuajiri na kufuta wakati wowote,” Bw Kiunjuri alisema.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Kenyatta aliwaomba wakazi wa Kaunti ya Laikipia wamruhusu Bw Kiunjuri asigombee ugavana ili amsaidie kama waziri katika serikali ya kitaifa. Lakini muda mfupi baada ya kumteua waziri, rais alianza kumshambulia hadharani na mnamo Januari mwaka jana akamfuta kazi ya uwaziri.

Tangu aliposhtakiwa ICC, Rais Kenyatta alikuwa na uhusiano wa karibu na mwanablogu Dennis Itumbi, na aliposhinda urais 2013 alimteua mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali katika Ikulu. Hata hivyo, mwaka jana yeye na wakurugenzi wengine wa kitengo cha habari za rais walitimuliwa.

Kwa wakati huu, Bw Itumbi amejiunga na Dkt Ruto na amekuwa akikosoa serikali na chama cha Jubilee ambacho alikuwa akitetea vikali.

Bw Itumbi aliambia Taifa Leo kwamba yeye na rais walitofautiana kimawazo lakini anamtambua kama kiongozi wa nchi: “Kuna tofauti za kimawazo na kisiasa kati yetu.”

Aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini, Kabando wa Kabando asema kuwa Rais Kenyatta amesahau safari yake ndefu ya siasa hadi akawa kiongozi wa nchi: “Amekataa kuzingatia maafikiano na viongozi waliounda serikali ya Jubilee, na hiki ndicho chanzo cha kukosana na marafiki wake na kusambaratika kwa umoja wetu. Ninamheshimu sana rais ndiposa mimi humkosoa hadharani na kwa roho safi. Uamuzi ni wake!”

Rafiki mwingine wa rais ambaye amegeuka kuwa mwiba kwake ni Mbunge wa Gatundu Kusini, ambako ndiko nyumbani kwa Rais Kenyatta, Moses Kuria, ambaye uhusiano wao wa kisiasa ulianza tangu utawala wa Kanu. Lakini kuanzia 2018, Bw Kuria amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Kenyatta eneo la Mlima Kenya.

Licha ya Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua kuwa msaidizi wa Rais Kenyatta kuanzia 2001, sasa mwanasiasa huyo kutoka Nyeri ni mmoja wa wakosoaji wakuu wa kiongozi wa taifa.

Bw Gachagua anasema hana uhasama wa kibinafsi na Rais Kenyatta, mbali kilichofanya wakosane ni kutotimiza ahadi yake ya kumuunga mkono Dkt Ruto kuwania urais: “Sina uhasama wa kibinafsi na rais. Tofauti zetu ni za kisiasa kwa kuwa alimruka Dkt Ruto.”

Rais Kenyatta alitofautiana pia na Seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki licha yake kuwa mmoja wa mawakili wake katika kesi za baada ya uchaguzi mkuu wa 2008 katika ICC.

Prof Kindiki, ambaye ni msomi wa masuala ya kisheria na katiba, ni mmoja wa walioandika katiba ya chama cha Jubilee na kuweka mikakati iliyokifanya kushinda uchaguzi mkuu wa 2017.

Katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Kenyatta, Prof Kindiki alikuwa kiongozi wa wengi katika Seneti kabla ya kuteuliwa naibu spika baada ya uchaguzi mkuu wa 2017. Lakini mwaka jana alitofautiana na rais kwa kumuunga mkono Dkt Ruto, ndiposa akapokonywa wadhifa huo.

Wengine waliokuwa marafiki sugu na watetezi wakuu wa Rais Kenyatta lakini sasa wamekosana naye kisiasa ni waliokuwa magavana Mike Sonko (Nairobi), Ferdinand Waititu (Kiambu), maseneta Irungu Kang’ata wa Murang’a, Susan Kihika (Nakuru) na Kipchumba Murkomen (Elgeyo-Marakwet) pamoja na wabunge kadhaa.

Akionekana kujitetea kwa kuhepwa na marafiki zake, Rais Kenyatta alisema mnamo 2018: “Heri tupoteze marafiki. Tutapata wengine na kusonga mbele.”

Serikali yanyonga wanyonge

Na PAUL WAFULA

MAISHA ya Wakenya yatakuwa magumu zaidi hivi karibuni baada ya serikali ya Jubilee kuruhusu Shirika la Fedha Duniani (IMF) kurudi nchini kwa masharti makali ya kusimamia uchumi.

Wataalamu wa uchumi wanasema Wakenya wanafaa kuanza kujiandaa kwa nyongeza zaidi ya ushuru, maelfu ya watumishi wa serikali na mashirika ya umma kufutwa kazi na kupanda kwa bei za bidhaa.

Hatua hii imekuja mwongo mmoja baada ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kufifisha usemi wa IMF kuhusu usimamizi wa uchumi alipopunguza ukopaji wa kiholela kutoka mataifa ya kigeni, pamoja na usimamizi bora wa uchumi.

Masharti makali ya IMF yatakuwa pigo kubwa kwa mamilioni ya Wakenya ambao tayari wamelemewa na bei za juu za bidhaa muhimu kama vile vyakula, mafuta taa, petroli, umeme na nauli kutokana na ushuru wa juu kupindukia.

Mwezi uliopita serikali ilipuzilia mbali kilio cha Wakenya baada ya kuongeza bei ya petroli hadi Sh122 kwa lita moja, msemaji wa serikali, Cyrus Oguna akisema ni muhimu ushuru kuwa wa juu kwa ajili ya kufadhili shughuli za serikali na maendeleo

Umeme nao umekuwa wa gharama ya juu kutokana na kampuni ya Kenya Power kutoza ada za juu ili kulipa kampuni za kuzalisha umeme, ambazo kulingana na mkataba sharti zilipwe hata kama hakuna umeme Kenya Power imenunua kutoka kwao.

Hii imesababisha bei ya umeme kuendelea kuwa ya juu licha ya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa kawi nchini.

Wakenya pia wanaendelea kufinywa, ambapo wiki iliyopita, Benki Kuu (CBK) iliruhusu benki na mashirika ya akiba na mikopo (Sacco) kuanza kutoza ada kwa shughuli za kifedha kwa simu kwa kiasi kinachozidi Sh100.

Mambo yamekuwa magumu zaidi kutokana na hatua za kukabili Covid-19 ambazo zimetangazwa bila mpango wowote wa serikali wa kutoa afueni kwa waliopoteza kazi kama vile wahudumu wa matatu na mabasi, wanaotoa huduma za kitalii, wahudumu wa kampuni za ndege na wamiliki na wafanyikazi wa mikahawa na mabaa.

Mbali na Covid, kumekuwa na hali mbaya ya kibiashara nchini hasa kwa biashara ndogo, ambapo nyingi zimefungwa na zingine kunadiwa mali yao kwa kushindwa kulipia mikopo.

Baada ya IMF wiki iliyopita kukopesha Kenya Sh257 bilioni, sasa shirika hilo litakuwa na usemi mkubwa kuhusu usimamizi wa uchumi kwa matakwa yasiyojali maslahi ya mwananchi wa kawaida.

Mkopo huo umeongeza deni linalodaiwa Kenya kuzidi Sh8 trilioni, na kutumbukiza nchi katika tatizo kubwa zaidi la kulipa deni hilo kubwa.

Kumekuwa na wasiwasi huenda Kenya ikapoteza baadhi ya raslimali zake kuu kwa wakopeshaji hao hasa Bandari ya Mombasa.

Kulingana na masharti ambayo IMF imepatia Kenya, serikali haitakuwa na budi ila kuongeza ushuru ili kutii agizo la shirika hilo kuhusu kupunguza ukopaji katika kufadhili shughuli zake.

Sharti lingine ni kubinafsishwa kwa mashirika ya serikali, hatua ambayo itaambatana na kupunguzwa kwa idadi ya wafanyakazi.

IMF pia inataka Kenya kupunguza bajeti yake ya kila mwaka, jambo ambalo huenda likatatiza miradi ya maendeleo.

Katika utawala wa marehemu Daniel Moi, maelfu ya watumishi wa umma walifutwa kazi katika mpango uliosukumwa na IMF. Utozaji wa ada za hospitali na shule pia ulianza wakati huo.

Mzee Kibaki alifanikiwa kubadilisha hali hiyo kwa kupunguza ukopaji, jambo lililomwezesha kuwa na uhuru wa kusimamia uchumi bila masharti ya wageni.

Lakini mafanikio hayo sasa yamekuwa historia, baada ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto kubadilisha mkondo wa usimamizi uchumi wa Mzee Kibaki na badala yake wakaanza kukopa kila uchao.

Ongezeko la ufisadi na kutumiwa kwa miradi ya umma kwa manufaa ya maafisa binafsi wa serikali na wafanyibiashara pia kumevuruga uchumi wa nchi, huku juhudi zilizoanzishwa 2018 za kupambana na ufisadi zikifeli.

Uhuru ashauriwa kuiga Kibaki

Na TITUS OMINDE

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Eldoret, Dominic Kimengich amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuiga njia ambayo ilitumiwa na rais mstaafu Mwai Kibaki katika kushughulikia ukuaji wa uchumi bila kukopa.

“Wakati wa siku za Mzee Kibaki, mikopo ya kigeni ilikuwa midogo sana. Tulikuwa tunatumia raslimali zetu zilizopo hapa nchini kukuza uchumi wetu. Ni bora twende polepole kwenye masuala ya kukopa na kusimamia uchumi wetu,” alisema Askofu

Akiongea baada ya kulisha familia zaidi ya 300 za barabarani mjini Eldoret wakati wa kuadhimisha Jumatatu ya Pasaka, Askofu Kimengich alisema kuendelea kwa serikali kukopa zaidi kutafanya Kenya kuwa mtumwa wa wakopeshaji.

Askofu Kimengich alieleza kuwa ufisadi na usimamizi mbaya wa rasilimali zilizopo ndio chanzo cha Kenya kukopa kila mara.

Alisema mwenendo wa kukopa zaidi umeiweka nchi katika hali mbaya kwani pesa nyingi zilizokopwa hazina manufaa kwa raia wa kawaida kwa sababu ya ufisadi.

“Utamaduni wa kukopa zaidi umeiweka nchi yetu katika hali ya kutatanisha. Pesa nyingi zilizokopwa hazifaidi nchi kwa sababu ya ufisadi na usimamizi duni wa uchumi,” akasema Askofu Kimengich.

“Natoa wito kwa serikali kuwa na uangalifu sana. Ikiwa tunaendelea kukopa ni nani atakayelipa madeni haya? Hatupaswi kuwaachia watoto wetu mzigo kama huu wa madeni. Serikali inapaswa kwenda polepole kwenye suala la kukopa,” akaongeza.

Hesabu za Uhuru 2022 zamkosesha usingizi

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta ako na kibarua kigumu cha kujipa ushawishi wa kuamua mwelekeo wa urithi wa 2022 huku akisukumwa na mirengo minne ya kisiasa.

Mrengo wa kwanza unahusu wandani wake ambao wameweka ajenda wazi kuwa wangependelea urithi huo umwendee kinara wa ODM Bw Raila Odinga. Nao mtandao wa familia pana ya mwanzilishi wa taifa hayati Mzee Jomo Kenyatta ambaye ni babake rais Uhuru nao ukisemwa kuwa unampendela Seneta wa Baringo Bw Gideon Moi aibuke kuwa rais wa tano baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Wengine ndani ya baraza la mawaziri nao wametangaza wazi kuwa wanampendelea Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i.

Nao wapiga kura wengi wa ngome ya rais ya Mlima Kenya iliyo na nguvu ya ujumla wa kura 8 milioni ambazo kila mrengo wa siasa unachumbia kwa udadisi kuwa ndizo zitaamua mshindi wakisemwa kuwa wanampendelea Naibu wa Rais Dkt William Ruto.

“Hii ni mitandao iliyo na nguvu sana na huenda Rais ajipate katika hali sawa na mchezaji kamari ambaye mkononi ako na kadi za kupoteza,” asema Mchanganuzi wa siasa za eneo hilo Prof Ngugi Njoroge.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mbunge wa Dagorretti Kusini Bw Dennis Waweru “kunao wanaosema kuwa Bw Odinga hawezi akachaguliwa. Huo ni uongo kwa kuwa Bw Odinga ni Mkenya aliye na nafasi sawa ya kuchaguliwa hata na watu wa Mlima Kenya.” Ni wazo ambalo linaungwa mkono na mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi anayesema kuwa “Bw Odinga ako na uwezo wa kumrithi rais Kenyatta.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau aliambia Taifa Jumapili kuwa “kile tu Bw Odinga anahitaji ni wale mabwanyenye na washirikishi wa njama za kumfaa mwaniaji wa Mlima Kenya katika ushindani wa urais wasusie kumhujumu Bw Odinga.”

Anasema kuwa harakati za mabwanyenye hao ndizo zimekuwa pingamizi kuu kwa Bw Odinga kuibuka na ushindi wa kutambulika, akikiri kuwa “kuna mara mbili ambapo Bw Odinga ametushinda (2007 na 2013) lakini ushawishi huo ukatumika kumzima kimabavu kupitia hila na njama.”

Bw Mbau anasema kuwa rais Kenyatta kwa wakati huu anaandaa njama ya uwaniaji wa Bw Odinga akiwa na aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth kama mgombezi mwenza na hatimaye nyadhifa zinazoundwa katika ripoti ya BBI zitumike kuwaleta pamoja wengine walio na ushawishi kutoka jamii za Kalenjin, Abaluhya na Wakamba ndani ya muungano huo ndio uwe na makali ya ushindani.

“Hatimaye, Bw Odinga aungwe mkono na mabwanyenye na mtandao wao wa ushawishi ndio akishinda, asihujumiwe kama ilivyo kawaida,” akasema Bw Mbau.

Njama hiyo ikiandaliwa, nao mtandao katika familia ya Kenyatta unachora jinsi urithi huo utamwendea Bw Moi.

“Familia ya hayati Kenyatta iko na heshima kuu kwa familia ya rais wa pili wa taifa hili Marehemu Daniel Moi. Ni mzee Moi ambaye alichangia pakubwa kumthibiti Bw Uhuru Kenyatta alipokuwa katika njia ya kutojielewa kijamii na kimaisha na akamwongoza hadi akamweka katika mkondo wa kushinda urais. Familia hii inapanga njama kali ya kurejesha mkono kupitia nayo kumuunga mkono mwana wa marehemu Moi na ambaye ni Seneta wa Baringo,” akadokezea Taifa Jumapili mmoja wa wandani katika njama hii.

Kwa upande mwingine, ndani ya baraza la mawaziri kumeibuka mtandao ambao umeamua kuasi msimamo wa rais na familia yake na kichinichini kuzindua mradi wa jinsi mmoja wao katika baraza hilo atatuzwa urithi wa Ikulu 2022.

Mnamo Alhamisi katika Mji wa Kangari ulioko Kaunti ya Murang’a, Waziri wa Uchukuzi Bw James Macharia alitangaza kuwa “sisi ndani ya baraza la mawaziri tumeamua huyu Dkt Matiang’i ndiye chaguo letu na tumefika ile awamu ambayo hatufichi nia yetu.”

Itakumbukwa kuwa wiki jana wandani wa Bw Odinga ambao ni Seneta wa Siasa Bw James Orengo na Mbunge wa Suna Mashariki Bw Junet Mohammed walilia kuwa “ndani ya serikali kuna mtandao ambao unaongozwa na Katibu maalum wa Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho na unapanga njama ya kumsaliti Bw Odinga na kuteka nyara miradi ya BBI na urithi wa 2022.”

Bw Macharia akiandamana na Dkt Matiang’i, Waziri wa Habari na Teknolojia Joe Mucheru na Naibu wa waziri wa Spoti Bw Zack Kinuthia alitangaza kuwa “sisi haja yetu ni kumpa uongozi wa taifa hili mtu ambaye ataelewa kuhusu miradi tele ambayo tumezindua na ndio isikwame rais Kenyatta akistaafu. Mwenye tumetambua ako na uwezo huo ni Dkt Matiang’i.”

Hayo yakizidi, kura za mashirika ya kibinafsi na pia ile fiche ya utathimini wa usalama wa kisiasa katika kitengo cha Ujasusi zinazidi kuonyesha kuwa Dkt Ruto ndiye ako na guu mbele Mlima Kenya katika ushindani wa urais.

“Ni juu ya rais sasa kuelewa kuwa ako na kibarua na akome ule mtindo wake wa kutoa vitisho kuwa atakuwa na usemi na atashangaza kupitia chaguo lake. La busara sasa ni awajibikie kumaliza awamu yake ya uongozi na atuachie sisi hapa nyanjani tukarangane hadi tuamuliwe na raia kupitia kura na kusiwe na wa kujaribu kumhujumu mwingine,” akasema Bw Rigathi Gachagua, mwandani wa Dkt Ruto.

mwangilink@gmail.com

Wanasiasa wa Mlima Kenya walia ‘kunyanyaswa’ na rais

Na JAMES MURIMI

BAADHI ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Kati wamelalamika kuwa Rais Uhuru Kenyatta anazima vyama vidogo vya kisiasa eneo hilo.

Viongozi hao wamemtaka rais kupatia vyama vya kisiasa vinavyoibuka eneo hilo nafasi ya kustawi.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri na Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Laikipia, Cate Waruguru waliungana kumtaka Rais Kenyatta kukuza demokrasia katika eneo hilo.

Wawili hao walionekana kuzika tofauti zao za kisiasa kwa kuitisha kikao cha pamoja na wanahabari, ambapo waliitaka serikali isaidie kukuza vyama vya kisiasa vyenye mizizi ya eneo hilo.

“Kama watu wa eneo la Kati ya Kenya, hatuogopi kutoa malalamishi yetu na kutetea vyama vya kisiasa tulivyo navyo. Tunamuomba Rais Kenyatta aturuhusu tujipange kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao,” alisema Bi Waruguru.

“Maeneo mengine yanafurahia demokrasia, lakini katika Mlima Kenya tumelemazwa. Tunataka demokrasia kuhusu siasa za eneo,” aliongeza.

“Iwapo demokrasia haitahakikishwa na rais, basi eneo la Kati ya Kenya litaendelea kutazama maeneo mengine yakitawala siasa za kitaifa,” alisema Bi Waruguru.

Bw Kiunjuri, ambaye ni kiongozi wa The Service Party, alisema vyama vinavyoibuka katika eneo hilo vinakadamizwa na Jubilee kwa kunyimwa haki ya kufurahia demokrasia.

Raila, Uhuru waamua kupimana nguvu Kisii

WYCLIFFE NYABERI na RUTH MBULA

VIONGOZI wa vyama vya Jubilee na ODM, wameamua kuweka kando umoja wao uliotokana na handisheki ili wapimane nguvu katika uchaguzi mdogo eneobunge la Bonchari, Kaunti ya Kisii.

Vyama hivyo viwili vimekuwa vikiepuka kushindana katika chaguzi nyingi ndogo hatua iliyoonekana kuwa njia ya kudumisha umoja kwa manufaa ya muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Hata hivyo, Jubilee ndicho chama cha hivi punde kumteua mwaniaji wake, baada ya kumpokeza tikiti aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Bw Zebedeo Opore.

Kupitia kwa barua iliyoandikwa na katibu mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju kwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), chama hicho kiliomba mwanasiasa huyo mkongwe aidhinishwe.

Bw Tuju alipuuzilia mbali barua nyingine iliyosambazwa mitandaoni ikidai kuwa Jubilee imeamua isiwe na mgombeaji.

Alisema barua hiyo ilikuwa feki na kusisitiza Bw Opore atapeperusha bendera ya Jubilee katika uchaguzi huo mdogo.

Wakazi wa Bonchari watapiga kura kumchagua mbunge mpya kwenye uchaguzi mdogo wa Mei 18, kufuatia kifo cha Oroo Oyioka aliyeaga dunia mwezi Februari. Marehemu Oroo alifariki katika Hospitali ya Aga Khan mjini Kisumu baada ya kuugua kisukari kwa muda mrefu.

Mwanasiasa huyo mkongwe sasa atamenyana na Bi Teresa Bitutu ambaye ni mjane wa marehemu Oyioka, aliyepewa tiketi ya chama kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, United Democratic Alliance (UDA) na Mhandisi Pavel Oimeke atakayewakilisha chama cha ODM.

Bw Oimeke, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi alipokuwa mkurugenzi mkuu wa bodi ya kudhibititi kawi (EPRA), alijiuzulu wadhfa huo hivi maajuzi ili kujitosa kwenye ulingo wa siasa.

Jumatatu, naibu mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe alidokeza kuhusu kuteuliwa kwa Bw Opore.

Bw Murathe alitupilia mbali madai kuwa hatua ya Jubilee na ODM kusimamisha wagombeaji katika uchaguzi mmoja ni ishara kuwa handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, imeingia doa.

“Uamuzi wa Jubilee na ODM kuwateua wagombeaji watakaoshindana hakutasambaratisha handisheki kwa kuwa kiti hicho kilitwaliwa na chama tofauti uchaguzi wa 2017. Hivyo basi, kiti hicho ni wazi kwa yeyote,” akasema Bw Murathe.

Marehemu Oroo alishinda kiti cha Bonchari kupitia chama cha Peoples Democratic Party (PDP) kinachoongozwa na Bw Omingo Magara.

PDP iliamua kutoteua mwaniaji na badala yake kikatangaza ushirikiano na UDA ili kumuunga mkono mkewe marehemu Oyioka, Bi Bitutu.

Wawaniaji wengine walioonyesha nia ya kumrithi marehemu Oyioka ni Bw Victor Omanwa wa Party of Economic Democracy, kiongozi wa vijana wa KANU Bonchari Douglas Ogari, Onkendi Ondieki miongoni mwa wengine.

Wanaomezea ‘tosha’ ya Uhuru

Na MWANGI MUIRURI

HATUA ya mawaziri kadhaa kujitokeza wazi kutaka mmoja wao awe rais ifikapo mwaka wa 2022, imeongeza idadi ya kambi zinazomtia presha Rais Uhuru Kenyatta kuhusu urithi wake.

Rais Kenyatta amekuwa akivutwa kila upande na mirengo tofauti ambayo kila mmoja una pendekezo tofauti kuhusu anayestahili kumrithi mamlakani baada ya uongozi wake.

Mnamo Alhamisi katika Mji wa Kangari ulioko Kaunti ya Murang’a, Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia alitangaza kuwa mawaziri wameamua kumuunga mkono mmoja wao ili kukamilisha ajenda za maendeleo zilizoanzishwa na Rais Kenyatta.

“Sisi ndani ya baraza la mawaziri tumeamua huyu Dkt Matiang’i ndiye chaguo letu na tumefika ile awamu ambayo hatufichi nia yetu. haja yetu ni kumpa uongozi wa taifa hili mtu ambaye ataelewa kuhusu miradi tele ambayo tumezindua na ndio isikwame Rais Kenyatta akistaafu. Yule ambaye tumetambua ana uwezo huo ni Dkt Matiang’i,” alisema.

Tangazo sawa na hili lilikuwa limetolewa awali na Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya. Kufikia sasa, Dkt Matiang’i hajatangaza wazi ikiwa atawania urais, lakini ziara zake nyingi maeneo ya Kisii husemekana na wadadisi kwamba ni ishara analenga kujitosa katika siasa.

Bw Macharia alikuwa ameandamana na Dkt Matiang’i, Waziri wa Habari na Teknolojia Joe Mucheru na Naibu wa waziri wa Spoti Bw Zack Kinuthia.

Kuna mrengo unaojumuisha wandani wa karibu wa rais ambao huwa hawafichi nia yao kutaka urithi huo umwendee kinara wa ODM, Bw Raila Odinga. Licha ya kuwa Bw Odinga hukataa kutangaza azimio lake kuhusu 2022 wazi na husisitiza hata akiwania hatahitaji ‘tosha’ ya kigogo yeyote wa kisiasa, baadhi ya wandani wake hutaka Rais amuunge mkono 2022 kwa vile alimsaidia kudhibiti serikali yake kupitia handisheki.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, kuna uwezekano mkubwa pia baadhi ya jamaa za Rais Kenyatta wanampigia debe Seneta wa Baringo Bw Gideon Moi kwa wadhifa huo. Hii ni kutokana na kuwa aliyekuwa rais, marehemu Daniel arap Moi, ndiye alimshika Rais Kenyatta mkono hadi akafika mahali alipo.

Mzee Moi naye alikuwa amehudumu kama makamu wa rais katika utawala wa rais wa kwanza wa taifa, marehemu Jomo Kenyatta, ambaye ni babake Uhuru.

Kwa upande mwingine, wanasiasa walioshirikiana kwa karibu na Rais wakati wa chaguzi za 2013 na 2017 Mlima Kenya wanataka atimize ahadi yake ya kumpokeza Naibu wa Rais Dkt William Ruto mwenge wa kuongoza taifa mwaka 2022.

Vigogo wengine ambao hupigiwa upatu kumrithi Rais Kenyatta ni Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Musalia Mudavadi (kushoto) na Kalonzo Musyoka. Picha/ Maktaba

“Hii ni mitandao iliyo na nguvu sana na huenda Rais ajipate katika hali sawa na mchezaji kamari ya pata potea,” asema Mchanganuzi wa siasa za eneo la Mlima Kenya, Prof Ngugi Njoroge.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau aliambia Taifa Jumapili kuwa, endapo Bw Odinga atakuwa kipenzi cha Rais kuwania wadhifa huo, itabidi apate uungwaji mkono wa mabwanyenye wa Mlima Kenya na vile vile awe na mgombea mwenza kutoka eneo hilo.

Kulingana naye, mabwanyenye hao wamewahi kuonyesha ushawishi wao katika chaguzi kuu zilizopita na wakati huu hautarajiwi kuwa tofauti.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth ndiye hutajwa kama anayeweza kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Nyadhifa zinazoundwa katika ripoti ya BBI zitumike kuwaleta pamoja wengine walio na ushawishi kutoka jamii za Kalenjin, Abaluhya na Wakamba ndani ya muungano huo ndio uwe na makali ya ushindani, kwa mujibu wa Bw Mbau.

Kauli hii iliungwa mkono na aliyekuwa mbunge wa Dagorretti Kusini Bw Dennis Waweru aliyepuuzilia mbali wanaoeneza dhana kuwa Bw Odinga hawezi kupata ufuasi Mlima Kenya.

“Kunao wanaosema kuwa Bw Odinga hawezi akachaguliwa. Huo ni uongo kwa kuwa Bw Odinga ni Mkenya aliye na nafasi sawa ya kuchaguliwa hata na watu wa Mlima Kenya,” akasema Bw Waweru, ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta.

Mtandao unaomtaka Rais kumtangaza Seneta Moi kama mrithi wake, hushikilia kuwa jamii ya Kenyatta inafaa ‘kurudisha mkono’ kwa jinsi marehemu Mzee Moi alivyokuwa mwaminifu kwao tangu akiwa makamu wa rais hadi kufariki kwake.

Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi. Picha/ Maktaba

“Familia ya hayati Kenyatta iko na heshima kuu kwa familia ya rais wa pili wa taifa hili Marehemu Daniel Moi. Ni mzee Moi ambaye alimwongoza Uhuru hadi akamweka katika mkondo wa kushinda urais. Familia hii inaweza kurudisha mkono kupitia kwa kumuunga mkono mwana wa marehemu Moi na ambaye ni Seneta wa Baringo,” akadokezea Taifa Jumapili mmoja wa wahusika katika mtandao huo, ambaye aliomba asitajwe jina.

Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua ambaye ni mwandani mkubwa wa Dkt Ruto, alisema Rais hafai kujishughulisha na masuala kuhusu urithi wake.

“La busara sasa ni awajibikie kumaliza awamu yake ya uongozi na atuachie sisi hapa nyanjani tukarangane hadi tuamuliwe na raia kupitia kura na kusiwe na wa kujaribu kumhujumu mwingine,” akasema.

Mnamo Januari, Rais alidokeza hataunga mkono mgombeaji urais kutoka jamii ya Wakalenjin wala Wakikuyu, akisema ni muhimu wadhifa huo uende kwa jamii nyingine.

Rais azima mikutano mikubwa ya kisiasa kwa siku 30

Na MWANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta amepiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa muda wa siku 30 zijazo kama sehemu ya kuangazia upya mikakati ya kupunguza kuenea kwa Covid-19.

Amesema haitajalisha cheo kuanzia kwa Rais hadi kwa kiongozi wa chini kabisa.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta ameongeza muda wa kafyu kwa muda wa siku 60 zijazo.

“Kafyu itaendelea kwa muda wa siku 60 na hivyo maeneo ya burudani na baa zinahitajika kufungwa kuanzia saa tatu za usiku,” amesema kiongozi wa nchi.

Ametaka mazishi yaandaliwe katika kipindi kisichozidi saa 72 za mtu kufariki akihimiza haja ya mikusanyiko katika hafla kama hizo kudhibitiwa vilivyo.

“Uchumi wetu unaweza ukakua tukiendelea kutia bidii katika shughuli za uzalishaji mali. Maisha ni muhimu na hivyo nawahimiza Wakenya tuendelee kuvalia barakoa na kuweka umbali kati ya mtu mmoja hadi mwingine,” amesema Rais Kenyatta.

Taabani kwa kutisha kumuua Rais Kenyatta

Na SIMON CIURI

MWANAMUME mmoja Jumatatu alifikishwa katika mahakama ya Kiambu akidaiwa kutisha kumuua Rais Uhuru Kenyatta ikiwa angepata bunduki.

Mshtakiwa, aliyetambuliwa kama Simon Muchiri, 22, anadaiwa kutoa vitisho hivyo kwenye mtandao wa Facebook mnamo Jumamosi iliyopita.Upande wa mashtaka ulisema kauli hiyo ni hatari kwa Afisi ya Rais na wale wanaohudumu huko.

Mshtakiwa alikamatwa mwezi uliopita baada ya polisi kutumia ujuzi wa kiteknolojia kubaini alikokuwa kupitia namba yake ya simu.

“Umeshtakiwa kuwa mnamo Februari 27 katika eneo lisilojulikana, uliandika kwenye mtandao wa Facebook kuwa ungemuua Rais Uhuru Kenyatta moja kwa moja ikiwa ungekuwa na bunduki,” mahakama ikaambiwa.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu wa Kiambu, Grace Omodho, ambaye alimwachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa taslimu ama mdhamini wa kiasi kama hicho.

Hata hivyo, mawakili wake waliiomba mahakama kumwachilia kwa dhamana isiyo ya juu, kwani yeye bado ni kijana na hilo ndilo kosa lake la kwanza.

Vile vile, walisema kuwa ndiye anayetegemewa na familia yake.“Yeye ni kijana. Hili ndilo kosa lake la kwanza na familia yake inamtegemea kwa mahitaji yao ya kimsingi,” wakaeleza.

Mahakama ilisema kesi hiyo itasikilizwa tena Machi 15. Upande wa mashtaka ulisema utawasilisha ushahidi utakaotumiwa kwenye kesi hiyo. Mnamo Juni 10, 2019 mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) alipigwa risasi na walinzi wa Ikulu ya Nairobi, alipojaribu kupanda ua ili kuingia ndani.

Polisi walisema kuwa mwanafunzi huyo, Brian Kibet, alikuwa amebeba kisu, ambapo alikataa kuwakabidhi walinzi hao alipoagizwa kufanya hivyo.

Mwanafunzi huyo alikuwa akisomea Uhandisi katika chuo hicho.Hata hivyo, ilibainika baadaye kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta (KNH).Alimrai Rais Kenyatta kumsamehe, baada ya kufikishwa kwenye Mahakama ya Milimani, jijini Nairobi.

“Ninaiomba mahakama hii kunisamehe. Sitarudia kosa hilo. Ninamwomba Rais Kentatta na Wakenya kunisamehe,” akasema.

Mnamo 2017, mwanamume mwingine aliuawa baada ya kupigwa risasi na maafisa wa polisi wa kitengo cha GSU karibu na Ikulu.

Kulingana na taarifa za polisi, mshukiwa alikuwa peke yake katika eneo la kuegeshea magari. Wakati wa tukio hilo, Rais Kenyatta alikuwa akihudhuria michezo ya gofu katika Uwanja wa Michezo ya Gofu wa Muthaiga.

Iliaminika mshukiwa aliruka ua na kuingia Ikulu ambapo alianza kuzurura kabla ya kugunduliwa. Mnamo 2013, mwanamume aliyetambuliwa kama Edward Njuguna alikamatwa baada ya kupatikana akizurura karibu na makazi ya kibinafsi ya Rais Kenyatta katika Ikulu jijini Nairobi, mwendo wa saa nane unusu usiku.

Mwanamume huyo alikamatwa na walinzi wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) waliokuwa wakilinda eneo la Nairobi Arboretum.

Eneo hilo liko karibu na makazi rasmi ya Rais.Kulingana na polisi, mshukiwa aliwaambia alitaka kuona mahali anakoishi Rais Kenayatta. Eneo hilo huwa limefungwa nyakati hizo.

Uhuru aomba talaka

Na BENSON MATHEKA

TOFAUTI kati ya Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto zinaendelea kuongezeka kiasi cha rais kumtaka Dkt Ruto ajiuzulu.

Uhusiano wa viongozi hao wawili umekuwa baridi tangu 2018 Rais Kenyatta aliposalimiana na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, lakini ni baada ya kuchapishwa kwa mswada wa kura ya maamuzi ambapo walianika tofauti zao hadharani.

Dkt Ruto amekuwa akipinga marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao ni matunda ya handisheki akisema umelemaza Ajenda Nne Kuu za maendeleo za serikali ya Jubilee.

“Tumeambiwa BBI ndio muhimu kuliko Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee kwa sababu inalenga kubuni nyadhifa za uongozi za watu wachache,” Dkt Ruto amenukuliwa akisema mara kadhaa.

Ijumaa, Rais Kenyatta alimwambia Dkt Ruto na wandani wake kwamba wajiuzulu badala ya kukosoa serikali wakiwa ndani.

Akizungumza akiwa Uthiru, Nairobi alipofungua hospitali mpya iliyojengwa na Idara ya jiji la Nairobi (NMS) na mradi wa maji, Rais Kenyatta alimlaumu Dkt Ruto na wandani wake kwa kuendelea kukosoa serikali ilhali wanataka kuendelea kuwa ndani.

“Tunafaa kushirikiana au kutengana. Iwapo wanahisi kwamba serikali inawafaa, basi wanastahili kushirikiana nasi lakini ikiwa wanataka kujitenga nayo, basi wajiuzulu,” Rais alisema.

Dkt Ruto amekuwa akitumia miradi ya serikali kupigia debe azima yake ya urais huku akikosoa handisheki na mapendekezo la kurekebisha katiba.

Licha ya rais kuagiza wanasiasa kusitisha kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022, Dkt Ruto amemkaidi na kuendelea kujipigia debe akidai BBI inalenga kumzuia kugombea urais.

Kauli ya rais ya kumtaka ajiuzulu, inatarajiwa kuongeza presha kwa Dkt Ruto ambaye amezuiwa kukanyaga ofisi za chama tawala kufuatia tabia yake ya ukaidi.

Kulingana na katiba ya 2010, Rais hana mamlaka ya kumfuta kazi naibu wake ilivyokuwa katika katiba ya zamani ambapo rais alikuwa na mamlaka ya kumtimua makamu wake.

Kipengele cha 150 cha katiba kinasema kwamba naibu rais anaweza kuondolewa ofisini akipata matatizo ya akili au kupitia mswada bungeni kwa misingi ya utovu wa nidhamu, kukiuka katiba au sheria yoyote ile na kutenda uhalifu chini ya sheria za Kenya na za kimataifa.

Ingawa baadhi ya wabunge wamekuwa wakitisha kuwasilisha mswada wa kumuondoa aondolewe ofisini mchakato wa kufanya hivyo ni mrefu ikiwemo kuungwa na wabunge wasiopungua 233.

Ni ulinzi wa katiba na mahitaji ya kisheria kunakomzuia Rais Kenyatta kumtimua Dkt Ruto na kulazimika kumtaka ajiuzulu.

Ijumaa, Rais Kenyatta alimwambia Dkt Ruto kwamba hafai kujisifu kwa miradi ya serikali anayokosoa.

“Huwezi kutusi watu kwa upande mmoja ukisema serikali ni mbaya na kisha ujisifu kwa mafanikio yake. Ondoka serikalini. Heshima sio utumwa,” alisema ishara kwamba ukaidi wa Dkt Ruto na washirika wake umemfika kooni.

Rais alikosoa kampeni ya Dkt Ruto kupitia vuguvugu lake la hasla na kuitaja kama siasa za pesa nane. “Lengo letu ni kuunganisha Wakenya. Hatutaki siasa duni za mgawanyiko kwa kudai wewe ni tabaka hili au lile,” alisema.

Rais Kenyatta ambaye hajaonekana hadharani pamoja na Dkt Ruto ilivyokuwa awali kabla ya handisheki, alisema yeye anaheshimu watu.

“Mimi ninaheshimu watu. Tukiheshimiana katika serikali, tutapata maendeleo na amani kwa wote,” rais alisema.

Dkt Ruto amelaumiwa kwa kumkaidi na kumdharau rais kwa kutounga BBI na kuendeleza kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

MIIBA TELE MBELE YA UHURU

Na MWANGI MUIRURI

JUHUDI za Rais Uhuru Kenyatta kutuliza uhasama dhidi ya mipango anayonuia kutimiza kabla ya kuustaafu hapo 2022, zinazidi kugonga mwamba.

Rais amekuwa akisisitiza kuwa nia yake ni kuhakikisha kuna amani atakapoondoka mamlakani, ametimiza maendeleo yatakayoboresha maisha ya wananchi, na vilevile kufanikisha marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Wiki iliyopita, Rais alijizatiti kushawishi ngome yake ya Mlima Kenya iungane naye katika safari hii nzima kwani eneo hilo limekumbwa na misukosuko tele ya kisiasa tangu alipoweka muafaka na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga mnamo 2018.

Hata hivyo, ziara hiyo iliyojumuisha mikutano na viongozi katika Ikulu ya Sagana, haijafanikisha mengi kwani anazidi kurushiwa makombora na wanasiasa wanaokosoa mienendo yake.

Licha ya rais kusisitiza kuwa ni lazima wanasiasa walio ndani ya chama tawala cha Jubilee wakome siasa za mapema kuhusu 2022, kampeni hizo zingali zinaendelea kuvutia umati mkubwa wa watu.

Vilevile, pingamizi dhidi ya Mpango wa Maridhiano (BBI) zingali zinaendelezwa na wandani wake wa zamani akiwemo Naibu Rais William Ruto.

Cheche za maneno anazorushiwa ndizo zilizomfanya kulalamika majuzi akitaka wanasiasa “waheshimiane”.

“Kufanya kampeni kwetu huzuia namna gani tingatinga za kutekeleza maendeleo mashinani? Tukiwa katika harambee kwa kanisa, huwa tunazima namna gani mawaziri kutoa kandarasi za kimaendeleo ili Wakenya wapate maendeleo?” akauliza mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro.

Lakini watetezi wa Rais wanasema hatababaishwa kamwe na wapinzani wake bali ataendelea kutekeleza wajibu wake. Kulingana na Mbunge Maalumu, Bw Maina Kamanda, ambaye ni mmoja wa wandani wa Rais, kiongozi wa taifa alikuwa akitatizika sana katika awamu yake ya kwanza ya uongozi.

Bw Kamanda alieleza kuwa Rais amefanikiwa kutekeleza mambo mengi ambayo hayangewezekana tangu alipoungana na Bw Odinga.

“Mmesikia mtu akisema Baba (Bw Odinga) alikuja kuharibu Jubilee. Kama si huyu mzee… Uhuru alikuwa na taabu sana. Si mnaona kitambi ya Uhuru imekuwa sawasawa? Hii ni kwa sababu ya Baba,” akasema jana alipokuwa katika Kaunti ya Turkana.

Rais Uhuru Kenyatta. PICHA/ MAKTABA

Bw Kamanda alisema wanaopinga misimamo ya Rais ni bora waondoke kwa upole waachie wengine nafasi ya kushirikiana na serikali kujenga taifa.

Mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri alisema hali itatulizwa tu ikiwa Rais atajitolea kwa Jubilee jinsi ilivyochaguliwa kuanzia 2013, akubali kuwa kuna deni la kisiasa kati ya wafuasi wake na wale wa Dkt Ruto na hatimaye wote katika undugu ndani ya mrengo mmoja wa kisiasa wapange kuhusu kura ya 2022 pamoja “bila ukora wa kusalitiana.”

Tayari, kumeibuka vyama kadhaa ambavyo vinatishia kusambaratisha umoja wa Mlima Kenya ambao umekuwepo kwa miaka mingi kisiasa.

Kinara wa chama cha The Service Party (TSP), Bw Mwangi Kiunjuri, alidai kuwa mienendo ya Rais inafaa kulaumiwa kwa vikwazo anavyokumbana navyo.

“Kile hatutakubali ni anavyotusukuma pembeni na hatimaye awe ndiye pekee ana ruhusa ya kutuharibia majina. Akiniharibia jina hata mimi nitamjibu,” akasisitiza waziri huyo wa zamani wa Kilimo.

Msimamo sawa na huu ulitolewa na Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua ambaye alisema Rais ndiye aliyepoteza mwelekeo kisiasa.

“Tumekuwa naye katika safari yake ya siasa kwa zaidi ya miaka 20 lakini katika siku za hivi karibuni amekuwa wa kupotoshwa, atuchukie na kutuadhibu pasipo sababu kiasi kwamba inatubidi tujitetee,” akasema.

Kulingana na kinara wa Narc Kenya, Bi Martha Karua, itakuwa vyema kama Rais Kenyatta atatulia jinsi mtangulizi wake Mwai Kibaki alivyofanya hadi akastaafu.

Uhuru awasha upya moto mkali ngomeni mwake

Na MWANGI MUIRURI

MATAMSHI ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba atatumia ushawishi wake kuhakikisha mahasimu wake Mlima Kenya hawaingii mamlakani, yamewasha moto upya katika ngome hiyo yake ya kisiasa.

Alipohutubu Jumamosi katika mkutano na wajumbe wa eneo hilo katika Ikulu ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, aliwakashifu wandani wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto pamoja na wanaopinga mpango wa umoja wa kitaifa kupitia Muafaka wa Maridhiano (BBI) na kuwaonya kuhusu hatima yao ya kisiasa ifikapo 2022.

Seneta wa Tharaka Nithi, Prof Kithure Kindiki alimtaja rais kama asiye na shukran yoyote kwa waliojitolea kwa hali na mali kumshikilia hadi akapata urais.

“Mfano ni mimi ambapo baada ya kumfanyia kazi kwa kujitolea, nikawa hata wakili wake katika kesi yake ya ICC baada ya kuorodheshwa kama mshukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, nikatumia taaluma na mali kumshikilia, ahsante yake iliishia kuwa ile ya punda,” akasema.

Prof Kindiki alisema, “Alinitoa kafara kwa genge la kisiasa la washirika wake wapya wa ODM katika Seneti na kwa masaa manne wakaning’atua kama kiongozi wa wengi, nikazomewa na kukumbushwa jinsi ya kumheshimu Uhuru Kenyatta.”

Katika kipindi cha wiki mbili sasa, Rais Kenyatta amewaangazia washirika wa Dkt Ruto kama wezi wa rasilimali za umma, matapeli wa kisiasa waliojawa na tamaa ya uongozi, kabla ya hatimaye kuzindua mpango mahsusi wa kupigia debe BBI Mlima Kenya ambapo leo hii anatamatisha ziara yake ya siku nne.

Rais amelenga kuimarishia udhibiti wa kisiasa katika Kaunti za Tharaka Nithi, Meru, Nyeri, Laikipia, Kirinyaga, Murang’a, Embu, Nyandarua, Nairobi na Nakuru zinazoorodheshwa kama ngome za jamii za Gikuyu, Embu na Meru (Gema.)Akiwa katika kikao na wajumbe 7, 000 katika ikulu ndogo ya Sagana, Jumamosi, rais alikanusha kuwa ashawahi kuwa na mkataba wa urithi wa urais na Dkt Ruto.

Jana, kinara wa Narc Kenya, Bi Martha Karua alimsuta Rais kama aliye na nia ya kuhadaa Wakenya kuwa BBI ina manufaa yoyote kwa taifa hili na pia kwa watu wa Mlima Kenya.

“Sisi si watoto na tuna uwezo wa kujiamulia. Akili tunazo za kujifanyia maamuzi yetu muhimu kuhusu masuala ya uongozi hasa 2022 na BBI. Ningemsihi awajibikie heshima tunayomwonyesha hadi sasa akihudumu awamu yake kama kiongozi na kisha aelekee nyumbani polepole akastarehe kama waliomtangulia,” akasema Bi Karua.

Bi Karua alikashifu BBI akisema kuwa imejaa sumu ya uongo na hadaa, lengo kuu likiwa ni kubomoa taasisi za kiutawala ili kuzigeuza kuwa butu na zisizo na nguvu za kuhudumia Wakenya kwa mujibu wa katiba.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri ambaye pia ni kiongozi wa chama kipya cha The Service Party (TSP) alimshambulia rais kama aliye na mazoea ya kusukuma wengine pembeni huku akiwaharibia majina.

“Kile hatutakubali kama walio ndani ya mirengo mbadala ya kisiasa mbali na ule wa rais, ni atuhujumu kwa kutusukuma pembeni na hatimaye kutuharibia majina. Mfano wangu, alinifuta kazi na hadi leo hajawahi kutoa sababu za kufanya hivyo. Kisha, anaenda kwa mikutano akisema kwamba sikuafikia viwango vya utendakazi ilhali anajua vizuri alinifuta kwa msingi wa msimamo wangu wa kisiasa,” akateta Kiunjuri.

Akaongeza, “Akinishambulia, ajue hata mimi sitakuwa na lingine ila tu kujibu mipigo. Ajue kuwa akiendelea kiniharibia jina sitanyamaza huku nikimpa nafasi ya kunisambazia uoga na hofu ya kisiasa.”

Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua alimtaka Rais aelewe kuwa “hakuna anayehitaji kupendekezwa na wewe ili awanie urais au aushinde na kisha aapishwe kukurithi.”

Bw Gachagua alisema kuwa wajibu huo wa kupendekeza, kuchagua na kuamua aapishwe ni wa raia wapiga kura “hivyo basi ukome kutusambazia vitisho”.

Rais Kenyatta njia panda akikutana na viongozi Mlimani leo Jumamosi

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA wameelekeza macho yote kwa Rais Uhuru Kenyatta kuona ikiwa ataweza kuhimili baadhi ya changamoto za kisiasa na kiuchumi zinazomkabili anapojitayarisha kung’atuka kutoka uongozini mwaka 2022.

Jumamosi hii, Rais Kenyatta anatarajiwa kukutana na viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri kujaribu kuwarai kumsaidia kuipigia debe ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) katika eneo hilo.

Wenyeji wamegawanyika pakubwa kuhusu ripoti hiyo, baadhi wakisema si suala la dharura linalopaswa kuangaziwa na serikali. Wanasisitiza Rais anapaswa kushughulikia masuala yenye uzito kama hali mbaya ya uchumi na kudorora kwa sekta muhimu kama kilimo.

Masuala mengine yanayoonekana kumwandama Rais Kenyatta ni wasiwasi wa ODM kuhusu utekelezaji wa handisheki, kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, madai ya migawanyiko miongoni mwa washirika wake wakuu serikalini na katika kundi la ‘Kieleweke’ ambalo limekuwa likimpigia debe kati ya mengine.

Chini ya mazingira hayo, wadadisi wanasema Rais Kenyatta ana nafasi ndogo sana kufanya maamuzi ambayo yatabadilisha hali ya siasa nchini.

Kulingana na Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa, Rais Kenyatta hana muda wa kutosha hata kidogo.

“Rais hana muda. Kuhusu suala la uchumi, hana muda kubadilisha hali. Uchumi hauwezi kulazimishwa kuimarika sasa kutokana na changamoto zinazotokana na athari za janga la virusi vya corona. Kiwastani, itachukua kati ya miaka mitatu na mitano uchumi kurejea kiwango ulichokuwa kabla ya janga la corona,” akasema Bw Bigambo kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Tangu alipochukua uongozi mnamo 2013, Rais Kenyatta amekuwa akilaumiwa kutokana na ongezeko la deni la kitaifa.

Ingawa serikali yake imekuwa ikijitetea inaelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo, mingi imekuwa ikikumbwa na sakata za ufisadi kama vile ujenzi tata wa mabwawa ya Arror na Kimwarer. Inadaiwa serikali ilipoteza zaidi ya Sh19 bilioni kwenye sakata hiyo. Kenya pia inakisiwa kuwa na deni la nje la zaidi ya Sh7 trilioni.

BBI

Kwenye juhudi zake kutuliza joto Mlima Kenya, wadadisi wanasema bado itakuwa vigumu kuwarai wenyeji kubadilisha msimamo wao kisiasa, hasa ikizingatiwa hawanii urais 2022.

Katika kikao cha Sagana, Rais Kenyatta anatarajiwa kuwarai viongozi kumsaidia kuendeleza ngoma kuhusu BBI, ambayo imezua hisia mseto katika eneo hilo.

Kulingana na Bw Bigambo, njia pekee aliyo nayo Rais ni kuhakikisha eneo limepata mgao mkubwa wa fedha kwenye bajeti ya mwaka 2021/22, kwani ndiyo itakayokuwa ya mwisho kwenye utawala wake.

“Kimsingi, hiyo ndiyo njia ambayo anaweza kuwaridhisha wenyeji. Hata hivyo, hilo bado ni ngumu kutimiza kwani kuna taratibu ambazo lazima zifuatwe katika kuhakikisha kila sekta imepata mgao wake wa fedha kwa mujibu wa kanuni zilizo kwenye sheria,” akasema Bw Bigambo.

Profesa Macharia Munene, ambaye pia ni mdadisi wa siasa, anasema kuwa njia ya pekee ambayo Rais huenda akapunguza uasi unaomkabili ni kukubali hisia zinazotolewa na mirengo yote ya kisiasa badala ya kutoa vitisho.

Rais Kenyatta amekuwa akitoa na maonyo makali, akionekana kuwalenga wanasiasa wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ unaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto kwenye azma yake kuwania urais 2022.

“Rais anapaswa kuanza kuwa mvumilivu. Lengo kuu ni kuhakikisha amedumisha taswira ya taasisi ya urais kama ishara ya umoja wa kitaifa. Vile vile, anapaswa kukoma kuonekana kuwapendelea baadhi ya viongozi hadharani,” asema Prof Munene.

Hapo Jumanne, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa bado yu mamlakani, na hakuna kiongozi yeyote anapaswa kuhisi kama kuna pengo la uongozi nchini.

Kwenye mahojiano na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake na lugha ya Gikuyu, Rais alisema ameanza mikakati kutimiza ahadi alizotoa kwa Wakenya, akieleza imani kuzitimiza kabla ya muhula wake kuisha.

“Mimi niko kazini. Mawaziri yangu pia wako kazini. Tunataka kuhakikisha tumetimiza yale tuliahidi Wakenya. Hiyo ndiyo sababu sionekani sana,” akasema.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanasema muda uliobaki ndio utaamua sifa ambayo Rais ataacha kwa wakati ambao amehudumu kama rais tangu 2013.

“Huu ni wakati ambao Rais Kenyatta anapaswa kuutumia vyema. Ndio utaamua ikiwa atarejesha imani kwa Wakenya au la. Ni wakati anaopaswa kuutumia kuondoa vikwazo vyovyote vinavyomkabili,” asema Tony Wetima, ambaye ni mdadisi wa masuala ya uchumi.

NDIO! HAPA WIZI TU

NA WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta amekiri kuwa uporaji pesa ndani ya serikali yake ni wa kiwango cha kutisha.Akizungumza jana asubuhi kwenye mahojiano na vituo vya redio vya lugha ya Kikuyu, Rais Kenyatta alisema wale wanaodai kuwa BBI itagharimu pesa nyingi ndio waporaji wakubwa na huwa wanaiba takriban Sh2 bilioni kila siku.

“Zile fedha ambazo watu hao huwa wanapora kila siku zinazidi Sh2 bilioni. Watu hao ni bure! Wanataka kutwambia ooh, BBI itatumia Sh2 bilioni, mara Sh1 bilioni! Je, wao huwa wanatumia fedha ngapi kwa mwaka?,” akasema.

Rais alisema hayo alipokuwa akimkashifu naibu wake, William Ruto na washirika wake kuhusu gharama ya kuandaa kura ya maamuzi.

Kauli hiyo inazua maswali kuhusu anachofanya Rais Kenyatta kukomesha wizi huo ikiwa anajua kuna wezi wanaofirisisha nchi ndani ya utawala wake, pamoja na uwezo wa taasisi kama vile Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kukabiliana na uhalifu huo.

Kukiri huko kumetokea wakati serikali inapokabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha, ambapo imeshindwa kutuma fedha kwa serikali za kaunti kutokana na kupungukiwa kifedha.

Wizi huo wa kutisha unaeleza sababu ya baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa kuwa na utajiri wa ajabu, ambao wengi hawawezi kufafanua walivyoupata, huku wananchi wa kawaida wakikosa huduma za kimsingi kama afya bora, ajira, barabara na elimu bora.Rais Kenyatta alitumia mahojiano ya jana kuwasihi wakazi wa jamii yake ya Wakikuyu kuunga mkono BBI, akisema watajuta iwapo haitapita.

Aliirai ngome yake ya Mlima Kenya isifuate wanasiasa wanaopinga ripoti hiyo, akitaja urekebishaji wa Katiba kupitia BBI kuwa njia ya pekee itakayohakikisha eneo hilo limefaidika kimaendeleo.

“Ni muhimu tutwae kilicho chetu sasa kupitia BBI badala ya kupewa ahadi kuhusu mambo ambayo tutatimiziwa katika siku zijazo. BBI ndiyo njia ya pekee itakayohakikisha maslahi yetu yamezingatiwa hata ikiwa mmoja kutoka jamii yetu hatakuwa uongozini,” akaeleza.

“Nitasimama na ukweli kuwa lengo letu ni kupeleka fedha mashinani kuwasaidia wananchi. Lengo kuu la ripoti hii ni kurejesha pesa mashinani kwa wananchi,” akasisitiza.

KUPOTOSHA WAKENYA

Akaendelea: “Wanaozunguka nchini wakiipinga BBI wanapaswa kukoma kuwapotosha Wakenya kwa kuwapa propaganda ambazo hazina msingi wowote. Mabilioni ya fedha ambazo wamepora kupitia miradi ghushi zinazidi zile ambazo zitatumika kwenye kura ya maamuzi.”

Hatua ya Rais Kenyatta kuzungumza kwa Kikuyu kwenye redio za FM ilionekana kama juhudi zake kujaribu kuzima upinzani mkubwa wa BBI katika ukanda huo.

Viongozi wengi na wakazi katika ngome hiyo yake ya kisiasa wanailaumu serikali kwa kulipa kipao mbele suala la BBI, licha ya kudorora kwa sekta muhimu za kiuchumi hasa kilimo, wakisema inaonekana amewasahau.

Hali hiyo pia imewafanya baadhi ya viongozi kuhama mrengo wa Kieleweke ambao umekuwa ukimtetea rais na kujiunga na ule wa Tangatanga, unaompigia debe Dkt Ruto kwenye azma yake kuwania urais mwaka ujao.

Wiki mbili zilizopita, Seneta Maalum Isaac Mwaura alihama Kieleweke na kujiunga na Tangatanga, akisema wenyeji wanataka kusikia serikali ikielezea kuhusu mikakati ambayo itachukua kuboresha hali ya uchumi nchini.

Suala hilo ndilo pia aliangazia pakubwa Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, Irungu Kang’ata, kwenye barua maalum aliyomwandikia Rais kuhusu hali ilivyo kwenye ngome yake.

Hapo jana Rais Kenyatta alikosoa kampeni zinazoendeshwa na Dkt Ruto za “hasla”, akizitaja kama hatari kubwa inayoweza kuizamisha nchi kwenye vita vya matabaka.“Huu ni mwelekeo unaoweza kutuzamisha kwenye janga hatari ambalo huenda ikawa vigumu kujitoa kama nchi,” akaeleza.

Sibabaishwi na matusi yenu, Uhuru awaambia Tangatanga

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu amevunja kimya chake kuhusu tetesi za kundi la Tangatanga linalokosoa matamshi yake ‘mamlaka ya urais yanafaa kuwa mikononi mwa jamii tofauti na zile mbili ambazo zimeongoza tangu Kenya ilipopata uhuru’.

Kundi hilo linalohusishwa na Naibu wa Rais, William Ruto limetaja matamshi hayo kama yanayoendeleza ukabila nchini.

Dkt Ruto pia amenukuliwa hadharani akiyakosoa, pamoja na salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga na Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) inayopendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho.

Akiwasuta wanasiasa wa kundi la Tangatanga, Rais Kenyatta alisema hababaishwi na matamshi mazito wanayomrushia.

Kwenye mahojiano ya pamoja na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Agikuyu, kiongozi wa nchi Jumatatu alisema kwa sasa haja yake kuu ni kuona amefanyia wananchi maendeleo na kuhakikisha ameafikia sera zake.

“Wanadhani wakinitusi nitawatumia askari washikwe? Kama wameona matusi kwa rais ni bora endeleeni, mimi niko hapa kazi hadi nitakapoikamilisha,” akasema.

Akicharura kundi la Tangatanga, Rais Kenyatta alilionya kutojaribu kusimamisha utendakazi wake wala kuzua fujo nchini.

“Hata kabla hawajaongea na kunitukana, huanza kwa kueleza maendeleo yaliyofanywa. Unadhani hiyo kazi hujifanya? Hufanywa na serikali ambayo ninaiongoza,” Rais akasema.

Akieleza kushangazwa kwake na tetesi za wakosoaji wake, Rais alisema hana shida na yeyote, lengo lake likiwa kuafikia ahadi zake kwa Wakenya kabla kukamilisha hatamu yake ya uongozi 2022.

“Lazima nifanye kazi niliyoahidi wananchi na niikamilishe…kauli yangu kuhusu jamii zingine zipokezwe mamlaka hakuna mahali nimesema ni vita ya 2022, haja yangu ni amani, utulivu na maendeleo ya Kenya,” Rais Kenyatta akafafanua, akiridhia salamu za maridhiano kati yake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Handisheki, kwa kile alitaja kama “hatua iliyochangia kuleta amani nchini”.

Rais pia aliendelea kuhimiza Wakenya kukumbatia Ripoti ya Mpango wa Maridhiano, BBI, akisema itasaidia kuangazia tofauti zinazojiri kila miaka ya chaguzi, ikiwa ni pamoja na kuleta maendeleo.

BBI inapendekeza kufanyiwa marekebisho ya Katiba, suala ambalo limeonekana kupingwa na Dkt Ruto na wandani wake.

Naibu wa Rais pia amekuwa akikosoa uhalisia wa Handisheki, akihoji inalenga kuzima ndoto zake kuingia Ikulu 2022.

Uhuru atandika Ruto 3-0

Na BENSON MATHEKA

MPANGO wa Naibu Rais William Ruto (kwenye picha) kushindana na Rais Uhuru Kenyatta kudhibiti jiji kuu la Nairobi umetibuka baada yake kuzidiwa maarifa.

Hii ni baada ya Rais Kenyatta hapo jana kusambaratisha uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Februari 18, kufuatia kutimuliwa kwa Gavana Mike Sonko.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipotangaza tarehe ya uchaguzi mdogo, Rais Kenyatta alitafuta mbinu za kuuepusha kwa kuchukua fursa ya uteuzi wa naibu gavana, Bi Ann Kananu Mwenda, aliofanya Bw Sonko mwaka jana lakini ukakosa kuidhinishwa kutokana na agizo la mahakama.

Mikakati ya Rais Kenyatta ilikuwa ni kuhakikisha Bi Kananu ameidhinishwa na bunge la kaunti kwa wadhifa huo na kuapishwa. Hapo jana, mipango ya mrengo wa Rais Kenyatta ilifikia kilele kwa bunge la kaunti kuidhinisha uteuzi wa Bi Kananu, ambaye muda mfupi baadaye aliapishwa kuwa Naibu Gavana.

Kuapishwa kwake kunamaanisha kuwa mipango ya Dkt Ruto, aliyeunga mkono aliyekuwa mbunge wa Starehe Askofu Margaret Wanjiru imesambaratika.

Hii ni kwa sababu akiwa Naibu Gavana, Bi Mwenda ataapishwa kuwa gavana wakati wowote kuanzia sasa.Nairobi imekuwa bila naibu wa gavana tangu 2018 wakati Polycarp Igathe alipojiuzulu akilalamikia kuhangaishwa na Bw Sonko, na uteuzi wa Bi Kananu kupingwa mahakamani mwaka jana.

Hatua hiyo ilifanya kukosekana mtu wa kujaza nafasi ya Bw Sonko.Uchaguzi huo ungegharimu mabilioni ya pesa na kuzua changamoto za kuzuia kuenea kwa Covid-19, pamoja na kutishia kinyang’anyiro ambacho kingeaibisha Rais Kenyatta iwapo mgombeaji wa Dkt Ruto angeshinda.

Tukio hilo la jana ni pigo kubwa kwa Dkt Ruto ambaye amekuwa akipasha misuli moto akijiandaa kumenyana na Dkt Ruto alikuwa akimuunga mkono Bi Wanjiru kuwania kiti hicho kwa tiketi ya chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA).

Upande wa Rais Kenyatta ulianza mikakati ya kuepusha uchaguzi mara baada ya Bw Sonko kung’atuliwa mwezi uliopita, kwa kuhakikisha kwanza kesi iliyowasilishwa na Peter Agoro akipinga Bi Kananu kupigwa msasa na bunge imeondolewa mahakamani.

Chama cha Thirdway Alliance baadaye kiliwasilisha kesi kupinga shughuli hiyo lakini ikatupiliwa mbali hapo jana asubuhi, na hivyo kupisha Bi Kananu kuhojiwa na kuapishwa.

Mnamo Alhamisi, Mahakama Kuu nayo ilisimamisha uchaguzi wa ugavana Nairobi hadi kesi za kupinga kuondolewa ofisini kwa Bw Sonko zisikilizwe na kuamuliwa, jambo ambalo lina uwezekano mkubwa wa kupitwa na wakati.

SHUGHULI KUHARAKISHWA

Katika moja ya shughuli zilizochukua muda mfupi zaidi katika historia ya mabunge ya kaunti tangu ugatuzi uanze nchini mnamo 2013, kamati ya uteuzi iliyo na washirika wa Rais Kenyatta ilimhoji Bi Mwenda asubuhi, ikawasilisha jina lake katika kikao cha madiwani wote, kikapitisha bila kupingwa na kisha akaapishwa naibu gavana dakika chache baadaye nje ya jumba la mikutano la KICC.

mwaniaji ambaye angeteuliwa na mrengo wa Rais Kenyatta.Sasa Dkt Ruto ameachwa kupambana na vinara wa NASA katika chaguzi ndogo za Machakos (useneta) na ubunge katika Matungu na Kabuchai.

Baada ya kushinda ODM katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Msambweni iliyo Kaunti ya Kwale na udiwani wa Gaturi katika Kaunti ya Murang’a mwaka jana, Dkt Ruto na mrengo wake wa Tangatanga wamekuwa na ujasiri wa kupimana na vigogo wengine wa siasa katika ngome zao.

Mwanamume wa familia ya Rais Kenyatta auawa Gatundu

Na MARY WAMBUI

WAPELELEZI wanachunguza kisa cha mauaji tatanishi ya Joseph Njuguna Mbeca, jamaa wa marehemu Chifu Mkuu Muhoho Gacheca.

Bw Gacheca ni babake mamake Rais Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta. Marehemu aliuawa Jumapili usiku na wakora nyumbani kwake katika kijiji cha Gatwikira eneobunge la Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu.

Mkewe Gatheca, Teresia Wanjiru Njuguna ambaye pia alikuwepo nyumbani alikamatwa kama mshukiwa na hapo jana alifikishwa katika Mahakama Kuu ya Kiambu.

Kulingana na ripoti ya polisi, siku ya tukio, marehemu alikuwa amehudhuria mkutano wa baraza la wazee na akarejea nyumbani akiandamana na wazee watatu mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

BW Gatheca na wazee wenzake walishiriki mlo wa nyama kisha wakanywa pombe ya kitamaduni hadi mwendo wa saa tatu za usiku ambapo wazee hao waliondoka kwenda zao.

Kama kawaida yake aliwasindikiza wageni wake hadi langoni lakini alipokuwa akirejea nyumbani akakamatwa na wanaume watano waliomburuta hadi ndani ya nyumba.

“Walimfungia mkewe katika chumba kimoja na kuanza kucharaza marehemu huku wakimwelekeza katika chumba cha kulala. Walipekuwa nyumba hiyo kisHa wakatoweka,” ikasema ripoti ya polisi.