Rais Kenyatta azindua kiwanda cha kutengeneza silaha za idara ya usalama Ruiru

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta, Alhamisi amezindua kiwanda kidogo cha kutengeneza silaha zitakazotumika na maafisa wa usalama nchini.

Kiwanda hicho kimezinduliwa eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, Rais Kenyatta akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha hali ya usalama nchini.

“Uzinduzi wa kiwanda hiki unaashiria Kenya itaweza kujisimamia na kujitegemea kutengeneza silaha zitakazosaidia kuimarisha usalama nchini,”akasema kiongozi huyo wa nchi.

Alisema kuzinduliwa kwa kiwanda hicho kunaenda sambamba na mikakati yake katika Ajenda Nne Kuu.

Aidha, Rais Kenyatta alisema mradi huo utasaidia kubuni nafasi za kazi kwa vijana, kupitia wafanyakazi watakaoajiriwa.

“Ni fahari kufungua kiwanda hiki kidogo cha uundaji wa silaha. Hatua hii inaenda sambamba na mikakati iliyoko katika Ajenda Nne Kuu, nafasi za ajira kwa vijana wetu zitapatikana. Isitoshe, ni miongoni mwa malengo tunayopania kuafikia kama taifa kwenye Ruwaza ya 2030,” akasema.

Uzinduzi wa kiwanda hicho unatazamiwa kusaidia kuondoa mawakala wenye tamaa za ubinafsi katika uagizaji wa silaha za idara ya usalama kutoka nje ya nchi, na ambao wametajwa kupunja serikali.

“Safari tuliyoanza leo si rahisi, itahitaji kujitolea, kuwekeza kupitia fedha na nguvukazi, na pia mafunzo kwa watakaosaidia kuifanikisha,” akasema.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Mkuu wa Majeshi Kenya (KDF), Meja Jenerali Robert Kibochi, na vigogo wengine wakuu katika idara ya usalama nchini walihudhuria uzinduzi huo.

“Hii ni hatua kubwa tumepiga mbele na kimaendeleo kama taifa, kusaidia kuimarisha hali ya usalama,” akasema Dkt Matiang’i.

WANDERI KAMAU: Tujinasue sasa kutoka kwa mfumo wa kibepari

Na WANDERI KAMAU

MDAHALO unaoendelea katika ulingo wa siasa nchini kuhusu watu matajiri na wale maskini, ni timio la onyo tulilopewa mapema mara tu baada ya Kenya kujinyakulia uhuru.

Wasomi na wanasiasa walioshabikia mfumo wa ukomunisti au ujamaa, walitoa maonyo kuwa hiyo ndiyo njia iliyofaa zaidi kuiepushia Kenya uwepo wa matabaka hayo mawili—mabwanyenye na walalahoi.

Hata hivyo, viongozi waliokuwa serikalini waliwaona kama maadui na ‘kuwanyamazisha’ mara moja ili “kutoivuruga nchi.” Baadhi ya watu hao ni mwandishi Ngugi wa Thiong’o, wanasiasa Jaramogi Oginga Odinga, Bildad Kaggia, Pio Gama Pinto, JM Kariuki kati ya wengine.

Katika karibu maandishi yake yote, Ngugi amekuwa miongoni mwa waandishi wachache ambao wamejitokeza wazi kuonya na kukashifu mfumo wa kibepari.

Tangu zamani, amekuwa akikita msimamo wake kuhusu mwoano mkubwa uliopo kati ya ujamaa na mfumo wa kimaisha walioishi Waafrika kabla ya uhuru.

Ni mawazo aliyoyarejelea kwenye vitabu kama ‘Weep Not, Child’ (Usilie Mpenzi Wangu), ‘The Trial of Dedan Kimathi ‘(Hukumu ya Shujaa Dedan Kimathi), Matigari ma Njiruungi (Waliobaki Baada ya Vita), ‘Ngaahika Ndeenda’ (Nitaoa Nikipenda) kati ya vingine.

Kwa mfano, katika novela ‘Usilie Mpenzi Wangu’, Ngugi anachora taswira kuhusu vile ubepari ulivyozua pengo na uadui mkubwa kati ya Wazungu na Waafrika.Chini ya mfumo huo, Wazungu walionekana kama ‘miungu’ nao Waafrika kama watumwa.

Ni mfumo ulioonekana kukita mizizi sana kiasi kwamba, Waafrika wenyewe walikuwa wamekubali kuwa wao ni “binadamu wa hadhi ya chini” ikilinganishwa na Wazungu.

Ni katika mazingira hayo ambapo wafanyakazi wa Kiafrika walizoea kuwaita waajiri wao Wazungu kama “lords” (mkubwa wangu) huku nao Wazungu wakiwaita Waafrika “boi” (mtumwa).

Hadi sasa, wazee wachache waliobaki huwa wanarejelea ugumu waliopitia chini ya wazungu, kwani waliwachukulia kuwa duni hata kuliko mbwa wao!Jaramogi aliendeleza mawazo hayo kwenye tawasifu yake ‘Not Yet Freedom’ (Hatujapata Uhuru), Kaggia kwenye kitabu ‘Roots of Freedom: 1921-1963’ (Mizizi ya Ukombozi) huku Kariuki akinakili mawazo yake kwenye tawasifu yake ‘Mau Mau Detainee’ (Mau Mau Kizuizini).

Ujumbe wao mkuu kwenye vitabu hivyo ni kwamba ubepari ungegeuka kuwa chemichemi ya mapigano ya kitabaka, ambayo ni hatari zaidi hata kuliko ghasia za kikabila.

Kinaya ni kuwa, licha yao kuhangaishwa, kudhulumiwa na kunyamazishwa na serikali ya Mzee Jomo Kenyatta, laana hiyo ndiyo inayotuandama sasa.Leo, Kenya ni miongoni mwa nchi zinazoorodheshwa kuwa na pengo kubwa sana kati ya watu matajiri na wale maskini.

Ni kwa hilo ambapo wanasiasa kama Naibu Rais William Ruto wameanza kukita kampeni zao kwenye juhudi za “kuziba” pengo hilo.Ukweli ni kuwa, mkasa huu ni mwiba wa kujidunga.

Tulionywa mapema na wale walioona hatari ya mfumo wa kibepari. Tuliwapuuza na kutupilia mbali mawazo yao. Tuliwaona kama watu duni, wasioelewa chochote.Majuto ni mjukuu. Wakati umefika tuanze kutathmini uzito wa tabiri zao.

akamau@ke.nationmedia.com

Uhuru, Raila wanusurika kufika mahakamani

Na RICHARD MUNGUTI

RAIS Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, sasa hawatahitajika kutoa taarifa katika kesi inayokabili walinzi wawili wa hoteli ya New Stanley, Nairobi.

Wafanyakazi hao wawili wanakumbwa na mashtaka ya kusambaza mitandaoni kinyume cha sheria video ya Rais na Bw Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta Avenue usiku kukagua mradi wa ujenzi wa barabara.

Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani, Bernard Ochoi, alisema Alhamisi ombi la washtakiwa Patrick Randing Ambogo na Janet Magoma kutaka taarifa hizo halina mashiko kisheria.

Walikuwa wamewasilisha ombi hilo kupitia kwa mawakili wao Danstan Omari na Apollo Mboya.

Randing na Janet wanakabiliwa na shtaka la kuchukua rekodi ya video za CCTV zilizoko katika hoteli ya New Stanley ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta usiku wa Juni 2, 2020.

Wawili hao walinaswa wakitembea kwenye kinjia kilichotengenezwa na Mamlaka ya Huduma za Nairobi (NMS).

Mawakili Omari na Mboya walikuwa wameeleza mahakama kuwa ushahidi wa walalamishi ambao ni Rais Kenyatta na Bw Odinga ni muhimu.

Walitaka pia viongozi hao wawili wahojiwe mahakamani.

Upande wa mashtaka ulisema kuwa hautazamii kuwaita Rais Kenyatta na Bw Odinga kuwa mashahidi katika kesi hiyo.

Katika uamuzi wake, Bw Ochoi alisema ni mkurugenzi wa mashtaka ya umma aliye na uhuru wa kuchagua mashahidi wataofika kortini.

Washtakiwa wako nje kwa dhamana ya Sh10,000 pesa tasilimu.

COVID: Uhuru akiri makosa

VALENTINE OBARA na MARY WANGARI

RAIS Uhuru Kenyatta amekubali kuwa mapuuza yake na viongozi wenzake kuhusu janga la corona yamechangia sana nchi kupiga hatua nyuma katika mwezi mmoja uliopita.

Katika hotuba yake kwa taifa Jumatano kuhusu hali ya Covid-19 nchini, Rais alikiri kuwa mikutano ya kisiasa iliyoshamiri katika mwezi uliopita ilichangia ueneaji wa virusi.

atika mwezi huo, viongozi mbalimbali waliandaa mikutano ya hadhara katika pembe tofauti za nchi bila kujali kwamba raia waliokuwa wakiwahutubia walitagusana na wengi hawakuvaa barakoa.

Kando na Rais, mikutano aina hiyo ilisimamiwa na Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, magavana, mawaziri miongoni mwa wengine.

Hii ni licha ya kuwa, serikali ilikuwa imepiga marufuku mikusanyiko ya watu. Hali hiyo ilifanya ionekane kama sheria za kupambana na virusi vya corona hazikuwahusu viongozi wakuu bali walalahoi wanaoadhibiwa vikali kwa makosa kama vile kutovaa barakoa.

Mnamo Jumanne, Dkt Ruto alisimamisha mikutano aliyokuwa amepanga kufanya siku zijazo akisema maambukizi ya corona yameongezeka sana.

“Sisi kama viongozi tumeanguka mtihani kwa sababu tumejifanya ni kama hakuna corona. Kufanya mikutano ya hadhara, kuleta watu bila barakoa na mambo kama hayo yametuumiza,” akasema alipohutubu katika Ikulu ya Nairobi.

Alitoa hotuba hiyo baada ya kukutana na wadau wa Wizara ya Afya na magavana, kuhusu hatua zilizopigwa kufikia sasa na zinazofaa kuchukuliwa kuendelea mbele.

Alijilaumu pamoja na wenzake kwa unafiki, akisema kumekuwa na tabia ya kusema mambo na kutenda vinginevyo.

“Ninawaomba viongozi tuongoze kwa mstari wa mbele. Tusiwe wa kusema na kutenda kivingine. Ni jukumu letu kusema na kutenda yale ambayo tunaambia wananchi wafuate,” akasema.

Katika mwezi wa Oktoba, maambukizi ya virusi vya corona yalipita 15,000 na vifo takriban 300.

Wataalamu wa afya wanaamini hii ilichangiwa na jinsi baadhi ya kanuni za kupambana na ugonjwa wa Covid-19 zilivyolegezwa.

Katika kanuni zilizotangazwa Jumatano, Rais alijizatiti kuepusha hatua ambazo zingeathiri sana uchumi na shughuli nyingine za kijamii.

Baadhi ya wadau wakiwemo magavana, walikuwa wametoa wito kwa Rais Kenyatta kurudisha masharti makali ambayo yalikuwa yametumiwa wakati ugonjwa huo ulipoingia nchini Machi.

“Mikakati asilia iliyowekwa irudishwe ili kupunguza ueneaji wa maambukizi,” Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bw Wycliffe Oparanya akasema.

Badala ya kupiga marufuku mikutano ya kisiasa, Rais alisema mikutano itakubaliwa ikiwa itafanywa ukumbini, chini ya kanuni za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo uvaaji wa barakoa.

Katika sekta ya elimu, serikali imeamua shule za msingi na upili zitafunguliwa Januari mwaka ujao.

Hata hivyo, wanafunzi wa Gredi Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne ambao wako shuleni wataendelea na masomo yao wakijiandaa kufanya mitihani.

Wito ulitolewa kwa wabunge kushauriana na bodi za fedha za hazina za maendeleo katika maeneo yao kuboresha miundomsingi ya shule kwa maandalizi ya kupokea wanafunzi wengi.

“Wawekeze katika kuongeza sehemu za kuosha mikono shuleni, kusambaza barakoa, usafi shuleni na kuepusha mtagusano wa wanafunzi na walimu,” akasema Rais.

Serikali pia iliepuka wito wa baadhi ya wananchi kufunga baa ambazo zinaaminika zimechangia ongezeko la maambukizi. Badala yake, Rais aliagiza ziwe zikifungwa saa tatu usiku, sawa na mikahawa.

Wakati huo huo, alitangaza kubuniwa kwa kikosi kipya cha usalama kitakachojumuisha maafisa wa polisi, maafisa wa utawala wa serikali kama vile makamishna na machifu, na maafisa wa usalama wa kaunti.

Kikosi hicho kitahitajika kuhakikisha wananchi hawakiuki kanuni za kupambana na janga la corona.

Rais alitangaza pia kuwa watumishi wa umma walio na umri wa zaidi ya miaka 58 watahitajika kufanya kazi nyumbani, pamoja na wale wanaougua ambao wanaweza kuwa hatarini kuathirika zaidi wakiambukizwa corona.

Avuna kwa sura kama ya Uhuru

Na PETER MBURU

MWANAMUME ambaye amepata umaarufu ghafla kutokana na kufanana na Rais Uhuru Kenyatta, ameanza kuvuna matunda baada ya kuzawidiwa gari Alhamisi.

Michael Njogo Gitonga ambaye picha zake zimekuwa zikisambaa mitandaoni kwa siku kadhaa kwa kuwa na sura kama ya Rais Kenyatta, alipokea gari hilo na kampuni ya uuzaji magari ya Maridady Motors.

Japo kampuni hiyo haikufafanua aina ya gari ambalo ingemzawidi Bw Gitonga, jana asubuhi ilituma picha katika akaunti zake za mitandao ya kijamii, pamoja na picha za Bw Gitonga akiwa ameketi ndani ya gari na akiwa katika jumba la kuuzia magari.

“Wakenya wenzetu, ni gari gani mnapendekeza Uhunye achukue kutoka duka letu la magari?” kampuni hiyo ikauliza mitandaoni, huku swali likiunganishwa na picha za Bw Gitonga.

Bw Gitonga mwenyewe Alhamisi jioni alithibitishia Taifa Leo kuwa alikuwa katika kampuni hiyo wakiendelea na mazungumzo na wakuu wake, japo hakufafanua zaidi kuhusu walichokuwa wakijadili.

“Nimekuwa hapa Maridady Motors tangu asubuhi na bado tunaendelea na mazungumzo. Labda tutamaliza muda wa saa mbili kutoka sasa,” akasema Alhamisi saa kumi na nusu jioni tulipompigia simu.

Taifa Leo ilijaribu kutafuta wakurugenzi wa kampuni hiyo kufahamu aina ya ushirikiano ambao ilikuwa ikipanga kuwa nao na Bw Gitonga na aina ya gari ambalo ilimzawidi.

Pia tulitaka kuthibitisha ikiwa ni kweli walikuwa wamempa kandarasi ya kuwa balozi wao kulingana na uvumi uliokuwepo mitandaoni Alhamisi.

Kutokea kwa Bw Gitonga mbele ya umma kumechochea gumzo tele miongoni mwa Wakenya wakijiuliza iwapo ana uhusiano wowote na Rais Kenyatta, hasa baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha habari zikiangazia maisha yake.

Awali alikuwa amelalamika kuhusu jinsi hali yake ya kimaisha imeharibiwa na kuibuka kwa ugonjwa wa Covid-19 uliomlazimu kufunga kazi yake ya baa: “Covid-19 imeniathiri sana. Nimekuwa nikiomba Mungu amalize janga hili kwani limenisukuma hadi mwisho.”

Atamani kukutana na Rais

Akihojiwa na vituo tofauti vya habari siku chache zilizopita, Bw Gitonga alikiri kuwa amekuwa na ari ya kutaka kukutana na Rais Kenyatta, kutokana na jinsi watu wengi wamekuwa wakimfananisha naye.

“Mimi hata huwa nashangaa na nashindwa nini kilifanyika kati yangu na Uhuru. Tunafanana sana. Mtaani naitwa Uhuru na kila mtu,” akasema.

Akaeleza: “Swali ambalo ninaweza kumuuliza Rais kwanza ni ikiwa yeye ni kakangu.”

Alisema hali hiyo imekuwa ikimsababishia mseto wa matokeo maishani, mara fulani akiepuka mabaya na wakati mwingine kulazimika kuwapa pesa watu wanaomuomba mara kwa mara kwa kuamini kuwa anafaa kuwa nazo; kwani anafanana na Rais.

“Wakiniona tu wanaanza kuniambia ‘Uhunye sijakula’, ‘Uhunye acha kitu’ na inanibidi niwape kidogo nilicho nacho,” Bw Gitonga akasema alipokuwa akihojiwa wiki iliyopita.

Alisema ana watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike, na kuwa nao pia huitwa “watoto wa Uhuru.”

Japo mamake aliaga dunia, bado anatumai kuwa siku moja babake atajitokeza ili atatue fumbo la ikiwa ana uhusiano wowote na Rais.

“Nikiwa nimeketi hapa leo niliwaza na kujiambia afadhali babangu akiwa alipo angejitokeza tu na kuniambia kuwa ndiye aliyenizaa. Nitamshukuru na kumwambia anibariki,” akasema Bw Gitonga alipokuwa akihojiwa majuzi.

Uhuru aangusha bakora

CHARLES WASONGA na IBRAHIM ORUKO

MISUKOSUKO ya kisiasa ambayo imekuwa ikitokota katika chama tawala cha Jubilee hatimaye ililipuka Jumatatu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kufanya mageuzi makubwa katika uongozi wa chama hicho katika Seneti.

Rais aliwafurusha wandani wa naibu wake William Ruto na mahali pao kuwaweka washirika wake.

Seneta wa Pokot Magharibi, Bw Samuel Poghisio aliteuliwa kiongozi wa Wengi Seneti, nafasi ambayo imekuwa ikishikiliwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen.

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata alipandishwa hadhi na kupewa wadhifa wa kiranja wa wengi ambao umekuwa ukishikiliwa na Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika.

Naibu wake atakuwa Seneta Maalum, Bi Farhiya Ali Haji.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya mabadiliko hayo kutangazwa na Ikulu, Bw Murkomen na Bi Kihika waliandaa mkutano na wanahabari na kutangaza kuwa hawatang’atuka afisini kwa kuwa mkutano uliowabandua kwa nyadhifa hizo, haukupangwa inavyostahili na pia kukosa idadi ya maseneta kuendesha shughuli hiyo.

“Ikulu ya Rais si makao makuu ya chama cha Jubilee na kwa hivyo tutapuuza tangazo la kuondolewa kwetu,” alisema Murkomen, akiongeza kuwa kuondolewa kwao hakuna mashiko na kanuni muhimu za Bunge hazikuzingatiwa.

Wawili hao walipuuza dai la Ikulu kuwa maseneta 20 walihudhuria mkutano huo na badala yake kutoa orodha yao wenyewe inayoonyesha maseneta 22 wanaoegemea kwa Bw Ruto hawakuhudhuria mkutano huo.

Walitangaza kuwa hawataondoka kwa afisi zao na kufichua kuwa wamemwandikia Spika Ken Lusaka wakitaja udhaifu wa kisheria uliopo katika hatua ya Rais na watu wake.

Wakati huo huo, wandani wa Bw Ruto walitishia kupinga hatua hiyo mahakamani.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Bw Caleb Kositany alisema kuondolewa kwa Bw Murkomen na Bi Kihika kutoka nyadhifa hizo ni batili na kinyume cha Katiba ya Jubilee.

“Wale waliotekeleza mabadiliko hayo walishiriki mchakato haramu na usiokubalika na Katiba yetu. Na bila shaka tutaenda mahakamani kubatilisha mageuzi hayo kwa sababu hayakuidhinishwa na Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama chetu,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa simu Jumatatu.

Bw Kositany akaongeza: “Kiongozi wa Chama hafai kuhusishwa katika shughuli kama hizi zinazovunja sheria. Mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi haukuwa halali na hivyo ulifanya mageuzi haramu.”

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto alisema, kuanzia sasa hawatakubali mikutano ya Kundi la Wabunge (PG) wa Jubilee kufanyika katika Ikulu ya Nairobi, ili kuzuia “mienendo hii ya kuwatisha wabunge kupitisha maamuzi ya kidikteta.”

Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Benjamin Washiali alimshtumu Rais kwa kuendesha chama cha Jubilee kama biashara ya mtu binafsi.

Alisema Rais alipuuza utaratibu wa uongozi wa chama pamoja na kamati na baraza la usimamizi wa chama katika kutekeleza mabadiliko kwa chama.

Hata hivyo, kipengee cha 9.1 cha Katiba ya Jubilee kinampa kiongozi wa chama mamlaka ya kuitisha mkutano wa kundi la wabunge wa chama wakati wowote. Na mwaliko wa mkutano wa Jumatatu ulitolewa na Rais Kenyatta mwenyewe.

Bw Murkomen amekuwa akishikilia nafasi hiyo tangu 2017 huku naibu aliyeteuliwa jana seneta wa Isiolo, Bi Fatuma Dullo,amekuwa akishikilia wadhifa huo kwa miaka miwili sasa.

Mkutano huo wa Ikulu ulihudhuriwa na maseneta 20 kati ya jumla ya maseneta 35 wa mrengo wa Jubilee.

Kwenye taarifa iliyotumiwa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Ikulu Kanze Dena Mararo, Rais aliwapongeza viongozi wapya wa Jubilee katika Seneti na akawahikikishia kuwa atawaunga mkono.

“Rais ambaye pia ni kiongozi wa Muungano wa Jubilee anataraji kufanya kazi kwa karibu na uongozi mpya wa seneti katika utoaji huduma kwa Wakenya,” akaongeza.

Shoka liliwaangukia Murkomen na Bi Kihika kwa sababu wamekuwa wakosoaji wakuu wa serikali ndani na nje ya Seneti, hali ambayo inasemekana kumkera Rais Kenyatta.

Kwa mfano, juzi Bw Murkomen alipinga hatua ya kupelekwa kwa wanajeshi wanne kuhudumu katika Kaunti ya Nairobi chini ya mwavuli wa afisi ya Nairobi Metropolitan Services (NMS).

Naye Bi Kihika alipinga kufurushwa kwa zaidi ya familia 5,000 kutoka kitongoji cha Kariobangi Sewerage akiitaja serikali ya Rais Kenyatta kama “dhalimu na isiyojali masilahi ya wanyonge.”

JUBILEE: Tuju athibitisha kikao cha Rais Kenyatta na maseneta Ikuluni Jumatatu

Na CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amethibitisha kuwa maseneta wa chama hicho wamealikwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa mkutano katika Ikulu ya Nairobi, Jumatatu, Mei 11, 2020.

Hatua hiyo inajiri baada ya wabunge na maseneta wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto kuwa katika malumbano ya mara kwa mara na wenzao wanaoegemea mrengo wa Rais Kenyatta.

Kimsingi, uhusiano wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto haujakuwa mzuri na wa karibu katika siku za hivi karibuni kwani wawili hao hawajakuwa wakionekana pamoja kwa kipindi kirefu.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimshinikiza Rais Kenyatta aitishe mkutano wa Kundi la Wabunge (PG) wa Jubilee ili kujadili masuala ambayo yamekuwa yakileta mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala.

Bw Tuju amenukuliwa akisema kuwa suala kuu ambalo litajadiliwa ni kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu ya Kaunti ya Nairobi hadi Serikali Kuu, ambalo limezua utata.

“Hii ndiyo sababu Rais amewaalika maseneta pekee wala sio wajumbe wa Bunge la Kitaifa, kwani maseneta ndio hushughulikia masuala ya ugatuzi,” amesema Bw Tuju.

Hata hivyo, Katibu huyu Mkuu amefafanua kuwa mwaliko wa mkutano huo ulitoka moja kwa moja kwa Rais Kenyatta na “hivyo siwezi kuelezea mengi kuhusu ajenda yake.”

Mkutano huo unatarajiwa kuanza saa mbili na nusu asubuhi.

“Mnavyojua ni kwamba ni Rais mwenyewe aliyewaalika maseneta. Kwa hivyo, siwezi kutoa mwelekeo kuhusu masuala yatakayojadiliwa. Lakini kila ninachofahamu ni kwamba hali katika Kaunti ya Nairobi itajadiliwa kutokana na shida ambazo zimeizonga tangu kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu kwa serikali kuu,” Tuju ameeleza.

Nairobi

Ingawa amehiari kuachilia majukumu manne makuu ya kaunti hiyo yaendeshwa na Serikali Kuu kwa kutia saini muafaka wa kufanikisha hilo Februari 2020 Gavana Mike Sonko alibadili msimamo juzi.

Anadai Serikali Kuu ilivuka mipaka na kutaka kusimamia hata yale majukumu ambayo yalifaa kusalia chini ya usimamizi wa serikali yake.

Kwa hivyo, ametisha kusambaratisha shughuli katika Kaunti hiyo kwa kujiondoa kutoka muafaka huo.

Hii ndiyo maana Aprili, Sonko alidinda kutia saini mswada ambao ulipendekeza Sh15 bilioni zitengewe mamlaka ya Nairobi Metropolitan Services (NMS) iliyobuniwa na Rais Kenyatta kuendesha majukumu hayo kwa niaba ya Serikali Kuu.

Hatua hiyo ilichangia mgongano kati yake na Ikulu na kuchangia kuondolewa kwa walinzi wake na baadhi ya madereva waliokuwa wakimhudumia.

Maseneta wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kipchumba Murkomen pia wamepinga hatua ya Serikali Kuu kuwapeleka wanajeshi kusimamia NMS.

Afisi hiyo inaongozwa na Meja Jenerali Mstaafu Mohammed Badi kama Mkurugenzi Mkuu. Na majuzi Serikali Kuu iliwatuma maafisa wanne zaidi katika makao makuu ya kaunti ya Nairobi, City Hall.

Mkutano wa mwisho wa PG wa Jubilee ulifanyika mnamo 2017 baada ya Rais Kenyatta kushinda uchaguzi na kuanza kipindi chake cha pili na cha mwisho. Ni katika mkutano huo ambapo wenyeviti na manaibu wenyeviti wa kamati za bunge la kitaifa na seneti waliteuliwa.

COVID-19: Rais Kenyatta atia saini mswada wa kupunguza ushuru

Na CHARLES WASONGA

SASA ni rasmi kuwa waajiriwa wanaopokea mshahara usiozidi Sh24,000 kila mwezi hawatatozwa ushuru wowote na wale wengine wanaopokea mishahara ya juu watatozwa ushuru uliopunguzwa zaidi.

Na wafanyabiashara wadogo sasa watalipa ushuru wa asilimia moja kwa faida wanazopata kila mwezi badala ya asimilia tatu ambayo wamekuwa wakilipa tangu Januari 2020.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali za ushuru kuwa sheria.

Sheria hiyo ambayo pia imehalalisha pendekezo la Rais la kupunguza ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa bidhaa za kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14, inalenga kuwakinga Wakenya kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19.

Wafanyakazi wanaopokea mishahara ya zaidi ya Sh24,000 kila mwezi pia watapata afueni kwani wamepunguziwa ushuru wa mapato kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25.

Waajiri pia wamepunguziwa ushuru wanaolipa serikali kwa kiwango chicho hicho ili kuwapunguzia gharama wakati huu ambapo janga la corona limeathiri shughuli za kiuchumi.

Mswada huo ulipitishwa na wabunge mnamo Jumatano baada ya wao kuujadili hadi saa nne za usiku.

Mswada huo umewasilishwa kwa Rais Kenyatta mnamo Jumamosi katika Ikulu ya Nairobi na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.

Wengine waliokuwepo ni Kiongozi wa wengi Aden Duale, Waziri wa Fedha Ukur Yatani, Wakili wa Serikali Ken Ogeto, Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu Nzioka Waita, Naibu wake, Njee Muturi na Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai.

Simhitaji Uhuru kupenya Mlima Kenya, adai Raila

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga amesema kuwa hahitaji kushikwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta ili kupenya Mlima Kenya, akisema tayari ana uhusiano ulioanza zamani na eneo hilo na kuwa anakubalika kivyake.

Bw Odinga amejitaja kuwa shemeji na rafiki wa Mlima Kenya na kuwa wakazi wa eneo hilo wanampenda kutokana na uhusiano wake na viongozi wa mbeleni eneo hilo, na kuwa uhusiano wake na Mlimani ulianza enzi za babake Oginga Odinga.

Alipoulizwa ikiwa anaogopa kwenda eneo hilo ama anahitaji kwenda na Rais Kenyatta katika runinga ya Ktn News Jumatano, Bw Odinga alisema haogopi chochote.

“Mimi siogopi kwenda Mlima Kenya kwa kuwa fulani amesema (kitu), hayo yote ni maneno ya uzushi. Nakwenda kama rafiki ya Wakikuyu, naenda kama muthoniwa (shemeji), naenda kwa athoni (mashemeji),” Bw Odinga akasema.

Alieleza jinsi babake, Oginga alikataa wadhifa wa Waziri Mkuu ili Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta aachiliwe; jinsi alifungwa pamoja na wanasiasa wa eneo hilo Kenneth Matiba na Charles Rubia miaka ya tisini; na alivyompigania Rais Mstaafu Mwai Kibaki hadi akashinda, akisema mifano hiyo yote ni msingi tosha wa kumpenyeza eneo hilo.

“Wakazi wa eneo hilo wananipenda. Hata Kibaki alipopata ajali wakati wa kampeni, nilitangaza kuwa japo nahodha (Kibaki) amejeruhiwa, sharti mchezo ungeendelea na nikasimamia kampeni. Tulipompeleka Kibaki Othaya, njiani nilikuwa nikiitwa Mutongoria Njamba (kiongozi shujaa) na Wakikuyu,” akasema.

Alitaja pingamizi za viongozi wafuasi wa Naibu Rais William Ruto eneo hilo dhidi yake (Raila) kuwa kelele za chura, na ambazo hazingemzuia kwenda Mlima Kenya.

“Waswahili husema migurumo za chura haizuii ng’ombe kunywa maji, yale unaskia ni ngurumo za chura, ngombe atakunywa maji,” akasema, akijirejelea kuwa ng’ombe na chura kuwa wafuasi wa Dkt Ruto Mlimani.

Kiongozi huyo Jumanne alikutana na viongozi wa eneo hilo, wakihusisha magavana Kiraitu Murungi (Meru), Anne Waiguru (Kirinyaga), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi) na wabunge Kanini Kega (Kieni) na Maina Kamanda, kujadili kuhusu mkutano wa Mpango wa Maridhiano (BBI) uliopangwa kuandaliwa Meru kesho.

Bw Odinga alisema tayari viongozi wa eneo hilo wamemkaribisha, ishara kuwa eneo hilo halina ubaya naye.

“Tuliongea juu ya mambo ya maendeleo eneo hilo, kilimo, elimu, usalama na kadhalika na wakanikaribisha wenyewe kutembea huko,” akasema.

Matamshi yake yamekuja wakati kumekuwa na gumzo kuwa anajaribu kumtumia Rais Kenyatta na BBI ili akubalike Mlimani, na kuwa kuna pingamizi kali dhidi yake.

Lakini alishikilia kuwa maneno hayo si ya kweli, akisema yeye ni shemeji wa Mlimani, na “damu ni nzito kuliko maji.”

Wandani wa Ruto wamrai Rais Uhuru asimteme

BENSON AMADALA na SHABAN MAKOKHA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wamemwomba Rais Uhuru Kenyatta kutomtenga Dkt Ruto anapomaliza muhula wake wa pili kama Rais.

Viongozi hao walisema kuwa Bw Kenyatta anapaswa kurudisha mkono kwa Dkt Ruto kwa kumuunga mkono na kuhakikisha kuwa amemrithi atakapoondoka ofisini mnamo 2022.

Hiyo ndiyo ilikuwa kauli kuu iliyojitokeza kwenye mkutano wa kisiasa uliofanyika Jumamosi katika Uwanja wa Nabongo mjini Mumias.

Wakati huo huo, waliwalaumu vikali kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula kwa kutohudhuria mkutano huo, wakisema wameisaliti jamii ya Abaluhya.

Walisema kwamba walikuwa wakiwatarajia viongozi hao wawili kuhudhuria, lakini wakashangazwa na hatua yao kuwepo katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Bukhungu wiki iliyopita.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale ndiye alianzisha mdahalo huo, akisema kuwa Rais Kenyatta ana deni kwa Dkt Ruto kwa kumuunga mkono kwenye chaguzi kuu za urais za 2013 na 2017.

“Dkt Ruto alimsaidia (Uhuru) kushinda urais mnamo 2013 na 2017. Yatakuwa makosa makubwa kwa Rais Kenyatta kumsahau Dkt Ruto anapomaliza vipindi vyake viwili,” akasema.

Polisi walifutilia mbali mkutano wa viongozi hao Jumamosi iliyopita, kutokana na kile walitaja kuwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, mkutano wa kuipigia debe ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) ulioongozwa na Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega uliendelea bila matatizo yoyote katika Uwanja wa Bukhungu.

Polisi pia walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya watu waliokuwa wamefika katika uwanja huo.

Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali alilazimika kujificha, akidai kuwa uhai wake ulikuwa hatarini.

Kwenye mkutano wa Jumamosi, mbunge wa Malava, Malulu Injendi alisema kuwa Rais Kenyatta hapaswi kusahau matatizo aliyokumbana nayo wakati alifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pamoja na Dkt Ruto nchini Uholanzi kutokana na ghasia za uchaguzi tata wa 2007/2008.

“Uamuzi wao kuhudhuria mkutano wa BBI katika Uwanja wa Bukhungu ulioyesha wazi kwamba hawafai kuwania urais,” akasema Dkt Khalwale.

Yaibuka Ruto ‘alimsindikiza’ Uhuru uchaguzini

Na MWANDISHI WETU

HUENDA Rais Uhuru Kenyatta alisaidiwa na wataalamu wa kampuni iliyosimamia kampeni zake ya Cambridge Analytica, kumwekea mtego Naibu Wake William Ruto alipounganisha chama chake cha URP na TNA kubuni Jubilee Party kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Stakabadhi za siri zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ilimshauri Rais Kenyatta jinsi ya kuendesha kampeni zake kupitia chama kimoja chenye nguvu ili zifanikiwe zaidi.

Katika kile kinachoonyesha kwamba Dkt Ruto alikuwa msindikizaji tu kwenye mipango ya kampeni, mikakati yote ya kampeni ilifanywa na kampuni hiyo na wandani wa Rais Kenyatta.

Waliopigia debe chama hicho kilipobuniwa, akiwemo Rais Kenyatta walidai kingeunganisha Wakenya na kumsaidia Dkt Ruto kumrithi 2022.

Dkt Ruto alishawishika licha ya baadhi ya wandani wake kutochangamkia hatua hiyo na kumshauri asivunje chama chake cha URP.

Kulingana na stakabadhi hizo, ni mshauri wa masuala ya kisiasa wa Rais Kenyatta Nancy Gitau na msaidizi binafsi wa Rais Kenyatta Jomo Gecaga ambao walikuwa wakishirikiana na kampuni ya Cambridge Analytica kuandaa kampeni ikiwemo kuunganishwa kwa vyama vya TNA na URP.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakitaja Bi Gitau miongoni mwa maafisa wa serikali wanaohujumu azma yake na inasemekana alilazimika kujiuzulu kutoka afisi ya rais kufuatia presha kutoka kwa kambi ya naibu rais.

Mawasiliano kati ya kampuni hiyo na wandani wa Kenyatta yanamsawiri Bi Gitau kama aliyesimamia kampeni za Rais Kenyatta akishirikiana na Sabhita Raju wa Cambridge Analytica.

Bi Gitau alisaidiana na Bw Gecaga kupanga mikakati ya kampeni za Jubilee ambayo iliwekwa kwa siri kwa Wakenya wengine na hata wateja wa kampuni hiyo.

Wakati mmoja, afisa wa kampuni hiyo Brittany Kaiser alionya maafisa wenzake dhidi ya kuanika shughuli zao Kenya ili wasikasirishe wanamikakati wa Rais Kenyatta.

“Mnapaswa kukumbuka kuwa hatuwezi kutaja kazi yetu Kenya kwa Wakenya wengine. Ikifikia kundi la Kenyatta kwamba tunawaarifu wengine kuhusu kazi yetu, inaweza kuhatarisha moja ya kandarasi zetu kubwa,” inasema barua ya Kaiser.

Wadadisi wanasema matukio katika chama cha Jubilee baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 ambapo Dkt Ruto anaonekana kutengwa serikalini, yanaonyesha huenda hakufahamu kilichomsubiri.

Wandani wa Rais Kenyatta walianza kuapa kumzuia kuwa Rais wakisema hakuna deni la kisiasa analopaswa kulipwa na wafuasi wa kiongozi wa nchi kwa kumsaidia kushinda uchaguzi mara mbili.

Rais Kenyatta ambaye wakati wa kampeni aliahidI kumuunga mkono Dkt Ruto kwenye uchaguzi wa 2022 amenukuliwa akisema ni Mungu anayejua atakayekuwa Rais wa nchi baada yake huku chama cha Jubilee kikikumbwa na mgawanyiko.

Stakabadhi zilizoanika mawasiliano kati ya wandani wa Rais Kenyatta na chama chake cha TNA, zinaonyesha kwamba mikakati ilitokana na tafiti zilizofanywa na kampuni hiyo na kufadhiliwa na Rais Kenyatta.

Katika nyaraka zake kuhusu uchaguzi mkuu wa Kenya 2013 na 2017, kampuni hiyo inaweka wazi kuwa ilikuwa ikifanyia kazi TNA na Rais Kenyatta ilichangia pakubwa kuunganishwa kwa TNA na URP.

“Kushinda uchaguzi enzi hizi, kunahitaji vyama vya kisiasa vinavyoweza kuendesha kampeni kubwa zilizoshirikishwa vyema kote nchini. Shughuli zinapaswa kupanuliwa hadi viwango vya juu chamani hadi kwa washirikishi wa kujitolea mashinani,” kampuni hiyo ilisema kwenye stakabadhi kwa Rais Kenyatta 2016.

Kampuni hiyo iliporomoka baada ya kufichuliwa kwamba iliendesha kampeni chafu kwenye uchaguzi mkuu Kenya 2013 na 2017 na mataifa mengine ulimwenguni.

Wadadisi wanasema masaibu anayopitia Dkt Ruto huenda yalipangwa wakati wa kuweka mikakati ya kampeni.

Sababu ya Uhuru kumfuata Ruto kanisani

Na VALENTINE OBARA

Wakenya wengine walishangaa kwa nini mchango wake ulitangazwa, ilhali Kanisa Katoliki lilitoa masharti mapya kuhusu harambee kwamba michango inafaa iwe siri ili isitumiwe na viongozi kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

RAIS Uhuru Kenyatta ameanza kufuata nyayo za naibu wake William Ruto katika juhudi za kujenga umaarufu wake uliodidimia eneo la Mlima Kenya.

Katika juhudi hizi, Rais Kenyatta ameanza kumuiga Dkt Ruto kwa kuhudhuria hafla makanisani na kuchangisha pesa.

Hapo Jumapili alihudhuria misa katika Kanisa Katoliki la St Francis of Asisi mjini Ruiru, Kaunti ya Kiambu kisha akashiriki harambee ya ujenzi wa kanisa jipya na akatoa mchango wa Sh3 milioni, na kuahidi kuongeza Sh4 milioni baadaye, kwa mujibu wa kitengo cha habari cha Ikulu (PSCU).

Hii ilikuwa mara ya pili katika muda wa wiki moja kwa Rais kuhudhuria hafla ya kimaendeleo eneo la Kati baada ya kipindi kirefu cha malalamishi ya viongozi na wakazi wa Mlima Kenya kwamba amewapuuza.

Mbinu hiyo ya kushiriki hafla za makanisa imekuwa ikiendelezwa zaidi na Dkt Ruto hasa katika eneo la Kati ambako hafla zake nyingi zimeongeza umaarufu wake kwa wakazi.

Kwa upande mwingine imekuwa nadra sana kwa Rais Kenyatta kushiriki katika harambee kwa muda mrefu sasa, na washirika wake wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto na hata kushutumu michango anayotoa.

Badala ya kushiriki harambee moja kwa moja, wakati mwingine Rais Kenyatta amekuwa akiwaita wasimamizi wa shule na wanafunzi katika Ikulu ya Nairobi ambapo huwa anawakabidhi mabasi ya shule yanayogharimu mamilioni ya pesa.

Hatua yake ya Jumapili kushiriki harambee kanisani ilifanya wengi kujiuliza imekuwaje akafuata mkondo wa Dkt Ruto ambao wandani wake wamekuwa wakishutumu.

“Wale waliokuwa wakimkashifu Naibu Rais kwa kufanya harambee kanisani, mko wapi?” akauliza mtumizi wa mtandao wa Twitter aliyejitambulisha kama @evans_ndaiga.

Naye @BryanSangRutto akasema: “Hatimaye Uhuru amekubali harambee si jambo baya.”

Wakenya wengine walishangaa kwa nini mchango wake ulitangazwa, ilhali Kanisa Katoliki lilitoa masharti mapya kuhusu harambee kwamba michango inafaa iwe siri ili isitumiwe na viongozi kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Katika hotuba yake, Rais Kenyatta alitilia mkazo hitaji la Wakenya kuungana katika vita dhidi ya ufisadi ambao alisema ni kikwazo kikuu kwa maendeleo ya nchi.

“Tafadhali tusiingize siasa katika vita dhidi ya ufisadi. Wakati mtu akipora mali ya umma huwa hafanyi hivyo kwa niaba ya familia yake wala jamii. Kwa hivyo mtu yeyote anayeshtakiwa anafaa kubeba msalaba wake mwenyewe,” akasema.

Aliongeza kuwa kisheria asasi zote zinazohusika katika kupambana na ufisadi hazifai kuingiliwa na yeyote na kwamba, kila anayeshtakiwa anapaswa kuchukuliwa kuwa asiye na hatia hadi wakati mahakama itakapoamua kwamba ana hatia.

“Kama taifa linalotii sheria, inafaa turuhusu asasi zetu zilizotwikwa jukumu la kupambana na ufisadi zifanye kazi zao kwa uhuru na kuhakikisha hakuna ubaguzi kwa washukiwa,” akasema.

Matamshi hayo yalitokea huku Gavana wa Nairobi, Mike Sonko akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Rais alikuwa ameandamana na viongozi wengine wakiwemo Naibu Gavana wa Kiambu James Nyoro, ambaye anashikilia usimamizi wa kaunti hiyo kufuatia uamuzi wa mahakama kwamba Gavana Ferdinand Waititu hastahili kuingia afisini hadi kesi yake ya ufisadi itakapokamilika.

Rais pia alitoa wito kwa wananchi kuwa na umoja kuanzia katika familia zao ili kukuza maadili ya kitaifa.

Ni kubaya lakini msinilaumu – Uhuru

Na GAKUU MATHENGE na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta amekiri kwamba hali si shwari katika utawala wake lakini akajiondolea lawama kuhusu hali hii.

Wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia hali mbaya ya uchumi ambayo imefanya maisha kuwa magumu hasa katika sekta za biashara na kilimo.

Alipozungumza Ijumaa wakati wa mkutano wake na viongozi wa Mlima Kenya katika Ikulu ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, Rais alisema ni kweli kuna mambo mengi ambayo yamemwendea segemnege kinyume na alivyotarajia kiasi cha kutatiza utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

Rais alionekana kuwalaumu mawaziri na wabunge kwa hali hiyo, akisema viongozi husika hawajawahi kumwambia kuhusu changamoto zilizopo.

Ilibainika kuwa katika mkutano huo wa faraghani, baadhi ya viongozi walimwambia Rais kuhusu matatizo yanayokumba wananchi hasa wale wa Mlima Kenya waliompigia kura kwa wingi.

“Ninashukuru viongozi kwa kuleta maswala haya ambayo sote tulichaguliwa kutatua kwa niaba ya wananchi. Hata hivyo, haya mambo yote ambayo yamewasilishwa hapa hayajawahi kufikishwa kwangu. Badala yake, ninachosikia katika runinga, televisheni na mitandao ya kijamii ni matusi na hadithi kuhusu uchaguzi wa 2022. Hawajaniletea sheria wala sera zinazohitajika kubadili hali,” akasema Raia Kenyatta.

Katika sekta ya kibiashara, kumekuwa na malalamishi kwamba utawala wa Jubilee ulibuni sera kali zinazotatiza uwekezaji na ujasiriamali. Wataalamu wa masuala ya kiuchumi husema hii imechangia makampuni mengi na viwanda kufilisika au kulazimika kuhamia mataifa ya nje, huku biashara ndogo ndogo pia zikifungwa kwa wingi.

Kwa upande mwingine, sekta ya kilimo imeathirika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo bei ya juu ya pembejeo na uagizaji bidhaa za kilimo kwa bei ya chini kutoka nchi za nje kama vile Uganda na China.

Wakulima ambao wametatizika zaidi katika miaka ya hivi majuzi ni wa kahawa, majani chai na miwa, huku wafugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa pia wakilia kuhusu hasara wanazopata.

Ubwete

Katika hotuba yake, Rais alionekana kuwalaumu mawaziri Mwangi Kiunjuri (Kilimo na Ufugaji) na Peter Munya (Biashara) bila kuwataja kwa kuzembea katika majukumu yao licha ya kuwa wao pia ni viongozi kutoka Mlima Kenya.

“Tazameni tu muone wale watu ambao nimewapa majukumu ya kutatua mambo haya,” akasema.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria alipozungumza na wanahabari baada ya mkutano huo, alisema hakutakuwa na faida yoyote kama viongozi wataendelea kulaumiana.

Kulingana naye, masuala yaliyojadiliwa Sagana yalikuwa yamewahi kujadiliwa katika mkutano mwingine uliofanywa hapo 2016 lakini hakuna hatua zilichukuliwa.

“Hatutaki kumlaumu Rais kwa lolote lakini pia hatutaki alaumu magavana wala wabunge. Yale tuliyosema hapa 2016 ndiyo yamerudiwa tena leo. Utadhani kuna watu watatoka sayari ya Mirihi (Mars) kutatua shida hizi. Tunataka vitendo,” akasema Bw Kuria.

Hata hivyo, mbunge huyo alitaka pia mawaziri wawajibike kwa kuwa Rais aliwapa kazi akiamini watamsaidia kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi.

Mavazi ya Uhuru, Raila yaibua gumzo

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga waliibua mjadala Jumapili walipowasili wakiwa wamevaa mavazi yanayofanana katika sherehe za Mashujaa zilizofanywa Mombasa.

Bw Odinga, ambaye aliwasili wa kwanza, alikuwa amevaa mavazi meupe kutoka juu hadi chini na kofia.

Rais naye aliwasili wa mwisho akiwa amevaa shati nyeupe iliyofanana na ile ya Bw Odinga pamoja na kofia sawa na yake.

Baadhi ya Wakenya walidai hayo yanaonyesha ushirikiano mpya unaotarajiwa wakati ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) itakapotolewa wiki hii.

Wengine walishangaa kama hali hiyo ilikusudiwa, kwani wakati Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto walipoingia mamlakani walikuwa na tabia ya kuvaa mavazi ya kufanana mara kwa mara kuonyesha ushirikiano wao.

Wakati wa sherehe za Jumapili, usalama katika kivuko cha Likoni uliimarishwa huku Jeshi la Wanamaji likichukua usukani katika kivuko hicho ambacho kipo karibu na bustani ya Mama Ngina ambapo sherehe ziliandaliwa.

Mamia ya wafanyabiashara wanaohudumu eneo hilo pia waliondolewa.

Mamia ya wakazi kutoka maeneo tofauti ya Pwani walikusanyika kuanzia saa kumi na moja alfajiri kwa sherehe.

Ilibidi baadhi ya waliofika kuzuiwa wasiingie huku wengine wakipanda juu ya miti ili kufuatilia yaliyokuwa yakijiri.

Ukarabati

Katika hatua moja ilibidi maafisa wa usalama kutumia nguvu kutuliza umati na watu kadhaa wakaondolewa katika bustani hiyo ili kurudisha hali ya utulivu.

Wengi waliofika katika eneo hilo walisema walitaka kushuhudia ukarabati ambao umefanyiwa bustani ya Mama Ngina kwa gharama ya Sh400 milioni.

Ilikuwa mara ya kwanza Jeshi la Wanamaji kuandaa sherehe hiyo, na kufanya maonyesho yaliyofana baharini.

Maonyesho yao yalijumuisha msafara wa maboti ya kijeshi na meli ambazo ndizo zilitumiwa kufyatua makombora ya heshima.

Kikosi cha jeshi la wanahewa pia kilifanya maonyesho yake angani kwa madoido yaliyojumuisha rubani wa helikopta kuisimama hewani.

 

Imeripotiwa na Mishi Gongo, Ahmed Mohamed na Valentine Obara

Uhuru akosa njia Kibra

Na BENSON MATHEKA

MGAWANYIKO katika chama cha Jubilee kuhusu uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra pamoja na handisheki zimemuacha Rais Uhuru Kenyatta ‘amechanganyikiwa’.

Ingawa Rais Kenyatta alikutana na mgombeaji wa chama hicho kwenye uchaguzi huo Macdonald Mariga katika Ikulu na kumvisha kofia ya Jubilee, matamshi ya wanasiasa walio karibu naye yanaonyesha amechanganyikiwa kuhusu anayefaa kuunga mkono kwenye uchaguzi huo.

Kinyume na sheria ya vyama vya kisiasa, baadhi ya wabunge wa Jubilee wametangaza wazi kuwa hawatamuunga mkono Bw Mariga mkono wakidai wana baraka za Rais Kenyatta kumuunga mgombeaji wa cha ODM, Imran Okoth

Mnamo Jumapili, mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini, Dennis Waweru waliongoza kampeni za Imran.

“Chama chetu cha Jubilee kimemsimamisha mgombeaji lakini roho ya Rais Kenyatta haiko huko. Roho ya Rais Kenyatta iko kwa Imran Okoth,” akasema Bw Kamanda.

Wanachama wa Jubilee wanaompiga debe Bw Mariga wanadai kuwa wanaomuunga mkono wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto walitumia njia za mkato ili kuhakikisha Rais amemuidhinisha kama mgombeaji wa chama tawala kinyume na mapenzi yake.

Kulingana na Waziri Msaidizi Rachel Shebesh, ambaye amejiunga na wanaomuunga mkono Bw Imran, Rais Kenyatta hakuwa na nia ya kumuidhinisha Bw Mariga.

“Mimi nilikuwa Ikulu wakati huo na ninajua presha aliyowekewa Rais ili kupigwa picha akimuidhinisha Bw Mariga,” Bi Shebesh alidai alipokutana na makundi ya wanawake mtaani Kibra kuwataka wampigie kura Bw Imran.

Japo kanda yake akitoa kauli hiyo ilisambazwa mitandaoni na kuibua hisia kali, Ikulu ya Rais Kenyatta haikukanusha madai yake.

Huku hayo yakijiri, Dkt Ruto amekuwa msitari wa mbele kumpigia debe Bw Mariga na kusisitiza kuwa ana baraka za kiongozi wa chama ambaye ni Rais Kenyatta.

“Si mlimuona kiongozi wa chama akimvisha kofia mgombeaji wa chama? Sasa hawa watu wanataka waambiwe nini kingine,” aliuliza Dkt Ruto akiwasuta wanaodai kuwa Bw Mariga ni mradi wa mrengo wa ‘Tangatanga’ katika Jubilee.

Kujitolea

Kulingana na wadadisi, Rais Kenyatta hakutaka Jubilee kusimamisha mgombeaji Kibra ili kuonyesha kujitolea kwake katika handisheki yake na Bw Raila Odinga, lakini baada ya chama kumkabidhi tiketi alijipata katika hali ya kuchanganyikiwa na ikabidi akubali.

Kiti hicho kilibaki wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth aliyekuwa mbunge wa ODM, na kakake Imran.

Alipomuidhinisha Bw Mariga, viongozi wa ODM walitilia shaka kujitolea kwa Rais Kenyatta katika handisheki na baadhi wakamtaka Bw Odinga kuwa mwangalifu.

Hata hivyo mambo yalitulia Bw Kamanda alipokutana na Bw Odinga na kutangaza kuunga mkono Bw Imran “kama mgombeaji wa handisheki.”

Wanaompinga Bw Mariga wanalaumu wanaomuunga mkono kwa kutaka kuvunja handisheki.

Katibu mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju mnamo Jumanne alisema hawana mipango ya kuwaadhibu wanaofanyia kampeni mgombezi wa chama pinzani.

Wabunge wailaumu KRA kwa kushindwa kukusanya Sh158 bilioni

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) Jumatano ililaumiwa kwa kufeli kukusanya ushuru unaofikia kiasi cha Sh158 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2014/2015.

Ufichuzi huo uko katika ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka huo ambayo ilikuwa ikikaguliwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC).

Kamishna Mkuu wa KRA James Mburu ambaye alifika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alisema kufikia sasa mamlaka hiyo imekusanya Sh112 milioni kati ya fedha hizo ambazo zimejilimbikiza kwa miaka minne.

“Hicho ni kiwango kikubwa cha fedha. Ikiwa kufikia Juni 30, mwaka huo KRA ilikuwa haijakusanya Sh158 bilioni inamaanisha kuwa kiasi hicho cha pesa kimeongezeka sasa,” akasema Bw Nassir.

Hata hivyo, Bw Mburu aliwaambia wabunge hao kwamba KRA sasa imeweka mikakati murwa ya kuimarisha kiwango cha ukusanyaji ushuru mwingi.

“Tutahakikisha kuwa kila mtu analipa ushuru kama inavyohitajika kisheria kupitia mikakati ambayo tumeweka,” akasema kamishna huyo mkuu.

Bw Mburu aliwataja wafanyakazi kadha ambao wameshtakiwa kwa kukwepa kulipa mabilioni ya fedha kama ushuru, ishara ya kujitolea kwa KRA kukusanya ushuru zaidi.

Baadhi ya wafanyabiashara ambao hivi majuzi walikamatwa kwa madai ya kukwepa kulipa ushuru ni Bi Tabitha Karanja na Bw Joseph Karanja ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya kutengeneza pombe na mvinyo ya Keroche Breweries Limited.

Naye mfanyabiashara Humprey Kariuki, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza mvinyo ya African Spirits amekanusha mashtaka ya kukwepa ulipaji ushuru unaofikia zaidi ya Sh17 bilioni.

Uhuru ashauri viongozi wa Pwani waungane

Na PSCU Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa viongozi wa eneo la Pwani kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.

Rais alishauri vingozi hao wawe na mawazo pana na mtazamo wa kudumu wa maendeleo akisema wanastahili kuzingatia miradi ambayo itawanufaisha watu wengi zaidi kupitia kuchuma mali na kubuni nafasi za kazi.

Rais ambaye alizungumza katika Ikulu ya Mombasa alipowapokea viongozi waliochaguliwa kutoka eneo hilo, aliwashauri viongozi hao kila mara kuzingatia maslahi ya wananchi badala yale ya kibinafsi.

“Tutafute suluhisho kwa changamoto zetu, hakuna jambo lisilowezekana iwapo tutaungana,” Rais Kenyatta aliwaambia viongozi hao wakiwemo Magavana sita wa kaunti za Pwani: Mombasa, Kilifi, Lamu, Taita Taveta, Kwale, na Tana River.

Rais alisema wakati umewadia kwa viongozi kufikiria jinsi watakavyokumbukwa na kizazi cha sasa na kile kijacho.

“Sharti tukadirie historia yetu kama taifa na pia kama eneo, na tujiulize iwapo watu wetu kama Wakenya wanaweza kuendelea kudumisha siasa za utengano, siasa za chuki, siasa za kuhujumiana na bado tuamini kwamba tutafaulu kuwa taifa lenye mapato ya kiwango cha kadri itimiapo mwaka 2030. Inawezekana kweli?” Rais akauliza.

Kuhusu maendeleo, Rais alibainisha baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali yake katika eneo hilo akiongeza kwamba Serikali itahakikisha utekelezaji wa miradi yote inayoendelea ikiwemo barabara, maji na miundomsingi mingine inakamilishwa.

Uwekezaji

Alisema miradi kama ile ya ujenzi wa barabara kadhaa, Eneo Maalum la Kiuchumi la Dongo Kundu na Bandari ya Lamu inanuiwa kufungua eneo hilo kwa uekezaji zaidi.

Viongozi wote waliozungumza katika mkutano huo wa mashauriano wakiwemo magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kwale), Amason Kingi (Kilifi), Dhadho Godhana (Tana River), Fahim Twaha (Lamu) na Granton Samboja (Taita Taveta) walisema wanaunga mkono ajenda ya maendeleo ya Rais kulingana na ajenda kuu ya nguzo nne za maendeleo.

Msingi wa Mlima Kenya kumkaidi Uhuru watolewa ufafanuzi

Na MWANGI MUIRURI

MATUMAINI ya wanaolenga kutwaa kura za Mlima Kenya kupitia ushawishi wa Rais Uhuru Kenyatta eneo hilo wanaonywa kuwa huenda waangukie pua kufuatia kudorora kwa umaarufu wake miongoni mwa wenyeji.

Sio siri kuwa kuna ukaidi mkuu kwa Rais ambapo umemwingia hadi kwa bongo lake na kwa hasira, amejitokeza hadharani kuteta kuwa atalipiza kisasi kupitia kung’atua mamlakani wanaofadhili ukaidi huo.

Kwa sasa, kuna minong’ono ya wazi kuwa sera zake za kiutawala pamoja na kutotimiza ahadi zake za kampeni za 2017 kwa wenyeji kumechangia pakubwa taswira kuwa aliwahadaa.

Gharama ya maisha kupanda pamoja na mfumkobei, kuonekana wazi kukosa kutoa mwongozo wa kisiasa na pia kukaa kimya wakati sera zinatekelezwa ambazo zinaathiri pakubwa kiuchumi wazawa wa eneo hilo ni miongoni mwa sababu ambazo zinatolewa.

Katika mijadala ya kisiasa mitaani, kuna taswira ya maafikiano kuwa utawala wake ulikuwa makosa makuu yaliyoidhinishwa na wenyeji kupitia kumpigia kura.

Ni taswira ambayo inaelezewa hata na viongozi wa eneo hilo, japo kwa njia isiyo ya kujianika kama wakaidi kwa ‘serikali ya nyumbani’ na ambapo mafumbo yanatandazwa ya kuonyesha kuwa “mtu wetu ametusaliti.”

Katika mitandao ya kijamii, kauli mbiu ya kuwatokeza wenyeji kupigia Rais Kenyatta kura ya “Thuraku Kumira Kumira” ikiwa na maana “Siafu wajitokeze kwa asilimia 100” imeanza kukejeliwa ikitajwa kama kauli ya hadaa inayotesa kwa sasa na iliyoishia kuwa sawa na ujinga wa maamuzi.

Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu anakubali kuwa kuna shida kubwa kwa sasa na imani ya wenyeji kwa ‘serikali yao’ imeishiwa na imani.

“Hii sera ya kubomolea wafanyabiashara vioski vyao bila kuwapa mahala mbadala pa kujitafutia riziki imepunguzia serikali umaarufu. Ni sera ambayo inaonekana kusukumwa kimakusudi na Gavana wa Nairobi, Mike Sonko ili kuzua ukaidi miongoni mwa wenyeji Mlima Kenya,” anasema Waititu.

Kuzima umaarufu

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri anateta kuwa kuna taswira ya Rais Kenyatta kuanza kutekwa nyara na mirengo ya kumharibia umaarufu ili asiwe na uwezo wa kutoa mwongozo mwafaka wa 2022 na iishie Mlima Kenya kutengwa.

Anasema kuwa kuna hatari kubwa sana kwa kuwa Rais Kenyatta haonekani kung’amua hilo na badala yake amebakia kimya huku eneo hilo likiwa limezama katika imani kuwa awamu yake ya pili na ya mwisho ikulu ilikuwa iwape kipaumbele katika kuwaboreshea maisha.

Aliyekuwa mbunge wa Naivasha, John Mututho tayari amejitokeza waziwazi akisema kuwa “kwa sasa hakuna haja ya kujidanganya kuwa Rais ana ule ushawishi wa kuelekeza wenyeji kumuunga mkono yeyote.”

Anasema kuwa Rais amejikwaa pakubwa katika sera yake ya uongozi ya kuongeza ushuru na kupanda kwa deni la kitaifa, hali ambazo zimechangia gharama ya kufanya biashara miongoni mwa wawekezaji wa eneo hilo kukumbwa na kudorora kwa faida.

Aliyekuwa mwenyekiti wa wawaniaji wa Jubilee Mlima Kenya 2017, Samuel Maina ameonya kuwa Rais alifika ikulu na akasahau jinsi wenyeji walijituma Agosti 8, 2017, kumrejesha Ikulu na pia katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

“Yeye mwenyewe (Rais) alizunguka eneo hili akituonya kuwa utawala wake ulikuwa katika hatari ya kung’atuliwa na Raila Odinga. Wenyeji wakajitokeza kwa wingi wao wakiwa na kura mkononi kumpigia na akafanikiwa kujiepushia balaa ya kuondolewa afisini. Tukaamrishwa na Jaji David Maraga na majaji wenzake katika mahakama ya juu zaidi turudie kura hiyo na tukafanya vivyo hivyo na tukahifadhi uongozi wake Ikulu,” anasema Mututho.

Anasema kuwa baada ya kuapishwa kuwa Rais, alikumbatia Odinga ndani ya serikali na akaibua hali ya Wakenya kuumizwa na sera mbovu za uongozi bila ya kuwa na mtetezi kwa kuwa upinzani ni kama vile uliaga dunia na kuzikwa katika kaburi la sahau katika utawala huu wa sasa.

“Leo hii, tukiibiwa kiuchumi na mafisadi, hakuna wa kututetea. Serikali ikikopa kiholela na kupandisha ushuru kwa njia za kikatili, hakuna wa kututetea. Ni kama Rais alimwendea Odinga waridhiane ndio Wakenya waumizwe kisawasawa,” anasema.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu, William Kabogo anesema kuwa utawala wa Rais Kenyatta kwa sasa umeingiwa na hatari kuu ya kukaidiwa.

Anasema kuwa kwa sasa kuna wingu la ukaidi ambalo linajichora Mlima Kenya na ambalo linafaa kushughulikiwa.

Na katika hali hiyo, Rais Kenyatta anaonekana waziwazi eneo hilo kama aliyesaliti matumaini kwa ahadi zake kuwa angetumia awamu yake ya pili mamlakani kuwatuza wenyeji Mlima Kenya mgao wao wa haki wa hisa za serikali yake iking’amuliwa kisiasa kuwa kura za eneo hilo kwa kiwango kikuu zilinusuru meli yake ya uwaniaji kutozamishwa na upinzani.

Uhuru, Raila wakutana kisiri ufuoni

Na CAROLINE WAFULA na VICTOR RABALLA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Ijumaa jioni walifanya mkutano wa kisiri katika kilabu maalum cha Yacht Club mjini Kisumu.

Viongozi hao waliwasili katika klabu hicho kilichoko katika mtaa wa Milimani, ufuoni mwa Ziwa Victoria kwa msafara wa magari 12 pekee ambapo walifanya mazungumzo kwa saa moja huku wakila chakula cha jioni.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walikuwa wametoka kuhudhuria mazishi ya mama ya Gavana wa Kisumu, Anyang Nyong’o katika kijiji cha Ratta, eneobunge la Seme.

Hafla hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi wengi, ilikamilika mwendo wa saa kumi na moja za jioni kabla ya kupanda helikopta tofauti hadi uwanja wa ndege wa Kisumu.

Walipotua, walipanda katika gari moja na kuondoka wakipiga gumzo.

Ajabu ni kwamba, magari kwenye msafara wa wawili hao hayakuwa yale wanayotumia katika shughuli rasmi kwani hayakuwa na ving’ora na vijibendera wala pikipiki za polisi kama ilivyo kawaida kwa msafara wa Rais.

Hali hiyo ilifanya wananchi kutotambua kwamba magari yaliyowabeba Rais Kenyatta na Bw Odinga yalikuwa kwenye msafara.

Kabla ya kuelelea kilabu hicho, wawili hao walifanya ziara ya ghafla katika Chuo cha Mafunzo kuhusu Viumbe vya Majini (Marine Training Institute) kilichoko karibu na bandari ya Kisumu. Walikagua shughuli za ujenzi zinazoendelea hapo huku maafisa wa usalama wakiwazuia wananchi na wanahabari kukaribia eneo hilo.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba, mkutano huo wa faragha katika Yacht Club ulihudhuriwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na mtu mwingine ambaye hakutambuliwa japo alikisiwa kuwa mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua.

Duru zilisema walishiriki mlo wa ugali wa rangi ya kahawia (brown), samaki aina ya tilapia na mboga za kienyeji.

“Vilevile, waliagiza chupa kadha za bia na juisi huku wakipiga gumzo kwa muda wa takriban saa moja hivi,” akasema mhudumu mmoja katika klabu hicho ambaye alitudokezea yaliyojiri katika mkutano huo.

Ni katika klabu hii ambapo viongozi hao wawili, ambao tangu waridhiane kisiasa mnamo Machi 9, mwaka jana, wamekuwa wakijiita “ndugu,” walitembelea mnamo Januari 19 baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Hazina ya Ustawishaji wa Vijana, Bruce Odhiambo katika eneo bunge la Muhoroni.

Wakati huo pia, Rais Kenyatta aliwashangaza walinzi wake na maafisa wa itifaki alipobadili mpango wa kusafiri wakati uliopangwa na kuamua kujivinjari Kisumu akisafiri kwa magari ya kawaida.

Ijumaa, Rais alipowasili katika Yatch Club kwa mara ya pili akiandamana na Bw Odinga na wageni wake wachache, wahudumu walichangamka huku viongozi hao wakielekea moja kwa moja katika chumba maalum karibu na ufuo wa Ziwa Victoria.

“Kama kawaida yake, Rais aliwasalimia wateja na wahudumu kwa kuwapungia mikono kabla ya kuketi katika chumba hicho kilichokuwa na viti vinne,” mhudumu mmoja, ambaye aliomba tulibane jina lake, alituelezea.

Rais Kenyatta alisikika akifurahia upepo wa ziwa.

“Ziwa linafurahisha kwani gugumaji limepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na awali tulipokuwa hapa,” alisikika akisema.

Uwepo wa Dkt Matiang’i katika mkutano huo wa Rais Kenyatta na Bw Odinga unatokana na cheo alichotunukiwa cha Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Kushirikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali Kuu.

Vilevile, Waziri Matiang’i amekuwa haelewani na wanasiasa wandani wa Naibu Rais William Ruto wanayemchukulia kama anayetumiwa kuzima ndoto kiongozi huyo kuingia Ikulu 2022.

Maafisa wengine wachache walioandamana na Rais Kenyatta na Odinga waliketi katika mahala tofauti kwa chakula cha jioni na vinywaji. Mbunge Mwakilishi wa Kisumu ambaye inadaiwa ndiye aliandaa mipango ya mkutano huo pia alionekana katika kilabu hicho.

Lakini mawaziri wengine walioandamana na Rais mazishini, kama vile George Magoha (Elimu), Eugene Wamalwa (Ugatuzi), Sicily Kariuki (Afya) na Raphael Tuju hawakuwepo katika klabu hiyo.

Hata hivyo, shughuli katika klabu hiyo maalum ziliendelea kama kawaida licha ya uwepo wa viongozi hao.

Mwendo wa saa moja na nusu usiku, viongozi hao wawili waliondoka jinsi walivyowasili na kuelekea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu ambapo Rais Kenyatta aliabiri helikopta ya kijeshi kurejea Nairobi.

Rais na ujumbe wake walipoondoka Yacht Club, maafisa wa Ikulu waliwazawadi wahudumu kwa hela chache “ kwa kazi nzuri”.

Safari ya Rais kuelekea uwanja wa ndege ilikuwa ya kasi ya chini. Msafara wake ulipitia barabara za Jomo Kenyatta Highway, Oginga Odinga , Obote na Busia. Wenye magari na waendeshaji boda boda hawakufahamu huo ulikuwa msafara wa Rais kwani walionekana wakiyapita magari hayo kwa kasi.

MAELEZO ZAIDI NA: CHARLES WASONGA

Rais Kenyatta awaonya wafanyabiashara wakiritimba, wenye tamaa wanaochangia mfumkobei

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumamosi amewaonya wafanyabiashara wenye mazoea ya kuongeza bei za bidhaa kiholela hasa za vyakula.

Pia ameagiza Halmashauri ya Bandari nchini (KPA), Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa na Huduma (Kebs) kuacha kuchunguza bidhaa katika bandari zinapoingizwa isipokuwa tu wakati inashukiwa hazijaafiki vigezo vya ubora.

Akionekana kulenga sekta ya kibinafsi, Rais amesema serikali haitakubali kuona wananchi wakiendelea kulemewa na mzigo mzito wa kupanda kwa gharama ya maisha.

Akihutubu katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2019 makala ya 56, kiongozi wa taifa amezitaka sekta za kibinafsi kuwajibika na kujali maslahi ya wananchi.

Wanafunzi kutoka shule nane katika Kaunti ya Narok wakifanya wasilisho kuunda ramani ya Kenya na neno Madaraka Juni 1 2019. Picha/ George Sayagie

Amesema baadhi ya sekta za kibinafsi ‘huficha’ bidhaa kama vyakula na kusababisha upungufu ili waongeze bei.

Mfumukobei wa bidhaa ni suala ambalo husababisha kupanda kwa gharama ya maisha.

“Sekta za kibinafsi, ninawasihi mjali maisha ya wananchi. Hii tabia ya kuficha bidhaa hasa vyakula na kuongeza bei ifikie kikomo,” akasema Rais.

Akaongeza: “Kuanzia sasa na kuendelea tutakuwa tukifuatilia bei ya bidhaa nchini.”

Kauli ya kiongozi huyu wa taifa imejiri wakati ambapo Wakenya wanaendelea kufukua mfukoni zaidi ili kugharamia unga wa mahindi.

Mkuu wa Majeshi, Samson Mwathethe alipokagua uwanja wa Narok mwishoni mwa Mei 2019 tayari kwa siku ya siku ambayo ni Juni 1, 2019. Picha/ Maktaba

Pakiti moja ya kilo mbili inauzwa zaidi ya Sh110.

Licha ya Kenya kuwa mkuzaji mkuu wa mahindi, wasagaji wanasema kuwa kuna upungufu wa nafaka hii. Baadhi ya wakulima eneo la Bonde la Ufa wanalalamikia mahindi yao kuozea kwenye maghala, jambo linalosababishwa na bei duni ya bidhaa hii.

Sherehe mashinani

Naye Naibu Rais Dkt William Ruto amesifu hatua ya sherehe za maadhimisho ya sikukuu ya Madaraka Dei kufanyika katika kaunti mbalimbali nchini.

Kulingana na Dkt Ruto ni kwamba hii ni njia mojawapo kuunganisha taifa hili, ambalo awali lilikuwa limegawanyika kwa msingi wa kikabila na kisiasa.

Amesema hatua hii itasaidia jitihada za serikali ya Jubilee kuleta pamoja Wakenya.

“Kinyume na miaka ya awali ambapo maadhimisho ya Madaraka Dei yamekuwa yakifanyika jijini Nairobi, serikali ya Jubilee imeibuka na mfumo wa kuyaadhimisha katika kaunti tofauti ili kuunganisha Wakenya,” akasema Dkt Ruto katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2019.

Sherehe za mwaka 2019 ni makala ya 56 na zimefanyika katika Kaunti ya Narok kwa maana kwamba viongozi serikalini wameenda huko.

Maadhimisho ya mwaka 2018, yalifanyika katika Kaunti ya Meru.

Kaunti zingine zilizopata fursa ya kuandaa maadhimisho ya kitaifa nchini, Madaraka Dei na Mashujaa Dei tangu serikali ya Jubilee ichukue usukani 2013 ni Nakuru, Kakamega, Nyeri na Machakos.

Sherehe za Madaraka Dei huadhimishwa nchini kila mwaka kama kumbukumbu ya Kenya ilivyopata uhuru wa kujitawala kutoka kwa utawala wa kikoloni.

JAMVI: Sababu za Uhuru kuogopa kuitisha kikao Jubilee

Na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa Rais Uhuru Kenyatta anasita kuitisha mkutano wa kundi la wabunge wa chama cha Jubilee kwa hofu ya kuaibishwa kwa kuelekezewa lawama kuhusu migawanyiko inayotokota ndani ya chama hicho.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa tuliozungumza nao wanasema Rais Kenyatta anawakwepa wabunge wanaegemea mrengo wa naibu wake William Ruto wanataka ufafanuzi kuhusu dhima ya muafaka kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Wabunge hao ambao ni wanachama wa ‘Team Tanga Tanga’ pia wamebainisha wazi kwamba wangemtaka Rais Kenyatta awaeleze waziwazi ikiwa ahadi yake ya kumuunga Ruto kama mrithi wake 2022 ingalipo au la. Rais anafahamau mipango hii na ndio maana amekuwa akitumia majukwaa mengine kuwajibu wabunge hao,” akasema Bw Javas Bigambo.

Wiki jana, Rais Kenyatta alionekana akijibu madai ya wabunge hao kwamba muafaka huo, maarufu kama handisheki, unalenga kumsaidia Bw Odinga kuingia Ikulu 2022 akisema hawajawahi kujadili suala hiyo katika mazungumzo yao na kiongozi huyo wa ODM.

Aidha, alipuuzilia mbali dhana kwamba uhusiano huo unalenga kuivunja Jubilee na kudidimiza ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

“Huyu Raila hajaniambia anataka kuwa Rais 2022; na sijamwambia ninataka kuwa rais 2022. Tumekuwa tu tukijadili masuala yanayowaathiri watu wetu. Ikiwa ni miundo mbinu, tumekuwa tukijadili kile ambacho tunapaswa kufanya kujenga barabara zaidi.

“Tunajadili, tunasaidiana na kukubaliana,” Rais Kenyatta akasema alipohutubu katika mkutano wa kujadili ufadhili wa miradi ya miundo msingi barani Afrika ulioandaliwa katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Mwenyeji wa mkutano huo alikuwa Bw Odinga, ambayo ni balozi wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundo Msingi.

“Ikiwa ni masuala ya afya, huwa ananielekeza kuhusu kile ambacho tunapaswa kufanya. Sisi huketi, kujadiliana na kukubaliana. Yeye pia hunipa mawaidha kuhusu jinsi ya kuimarisha kile ambacho tunafanya. Sasa kuna kosa gani hapo? Rais Kenyatta akauliza.

Alisema mustakabali wa wananchi na taifa la Kenya kwa jumla ndio nguzo muhimu inayohimili muafaka kati yake na Bw Odinga.

Lakini siku moja baada ya Rais kutoa kauli hiyo, Dkt Ruto alioenakana kumjibu alipodai kuwa, “kuna watu mahali fulani ambao wanawachukulia Wakenya kama wajinga.”

Watu ambao, alisema, aidha wanadhani Wakenya hawajui kinachoendelea au wanaamini kuwa Wakenya hawajui nani atakuwa rais wao.

“Kuna watu fulani ambao wanadhani Wakenya ni wajinga. Wakenya wanajua ni nani atakuwa rais wao. Koma kutuletea siasa. Kuna uhaba mkubwa wa wajinga nchini,” Ruto akasema alipohutubia hafla ya Kanisa mjini Nyeri.

Bw Bigambo anasema ni hali kama hii ambapo Rais Kenyatta na naibu wake wameonekana kukinzana waziwazi kuhusu suala hilo la handisheki ambayo imeendelea kuzua tumbojoto ndani ya Jubilee na kufifisha juhudi zozote za kuitishwa kwa mkutano wa kundi la wabunge wake (PG).

“Isitoshe, Rais na naibu wake wametofautiana hadharani kuhusu suala nyeti la vita dhidi ya ufisadi. Rais ameonekana kuunga mkono uchunguzi unaoendeshwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuhusu sakata ya wizi wa Sh21 bilioni za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer lakini Dkt Ruto anampiga vita Bw Kinoti kwa kudai anatumiwa na mahasidi wake kuhujumu ndoto yake ya urais 2022 kwa kulenga wandani wake,” anasema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maseno Tom Mboya anayeshilikia kuwa ni hali kama hiyo ambayo imelemaza juhudi za kuitishwa kwa mkutano wa PG wa Jubilee.

Akiguzia shinikizo hizo za kuitisha mkutano wa PG, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju anasema hamna “mgogoro wowote ndani ya chama chetu wa kuhitaji kujadiliwa katika mkutano kama huo.”

“Kiongozi wa Jubilee Bungeni Aden Duale hajawasilisha ombi kama hilo kwa uongozi wa chama. Kwa hivyo, wale wanaoitisha mkutano huo kupitia mikutano ya hadhara au ya mazishi wanafaa kuelekeza maombi yao kwa Duale. Kufikia sasa hamna ombi kama hili limepokewa ishara kwamba hamna mgogoro au masuala ya kujadiliwa,” anasema Bw Tuju ambaye pia ni Waziri asiye na Wizara ya Kusimamia.

Kwa upande wake Bw Duale, ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini, anasema wajibu wa kuitisha mkutano wa PG sio wa Rais Kenyatta.

“Wale wanataka mkutano huo wanafaa kuwasilisha maombi yao kwa afisi yangu… kisha nitawasiliana na kiongozi wetu Rais Kenyatta na naibu wake Dkt Ruto ili tukubaliane kuhusu ajenda ya mkutano kama huo. Kufikia sasa hamna sijapokea ombi rasmi kutoka kwa mbunge yeyote,” Duale akaambia jarida la Jamvi.

Lakini kulingana na wabunge wandani wa Dkt Ruto, kutoitishwa kwa mkutano huo ndio sababu ya uwepo wa mgawanyiko unaoshuhudiwa katika chama hicho wakati.

Wanasema kuwa endapo mkutano huo hautaishwa hivi karibuni huenda hali hiyo ikadidimisha nafasi ya chama hicho tawala kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2022.

Mbunge wa Bomet ya Kati Ronald Tonui anasema wabunge wa Jubilee wanakinzana kimawazo kuhusu masuala ya kitaifa kwa sababu mkutano wa PG haujaitishwa ili waweze kuchukua msimamo mmoja kuhusu masuala hayo, hususan utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu ya Serikali.

Bw Tonui na wenzake wanasema kuwa Rais Kenyatta hajawahi kukutana na wabunge wa Jubilee kujadili suala hilo ambalo linavumishwa na serikali katika muhula wake wa pili afisini.

“Tulifanya mkutano wa mashauriano kupanga marudio ya uchaguzi wa urais mnamo Septemba baada ya mahakama ya juu kufutilia mbali ushindi wa raia Kenyatta. Mkutano mwingine ambao tulifanya na Rais ni pale alipokuwa akitaka kuwalazimisha wabunge kupitia Mswada wa Kifedha wa 2018 Novemba mwaka jana,” akasema Tonui.

Kulingana na mbunge huyo, inaonekana Rais Kenyatta anakwepa mkutano wa PG kimakusudi.

“Dhana inayojitokeza ni kwamba Rais ameanza kuwasawiri wabunge kama maadui wake badala ya kuwa washirika katika chama cha Jubilee na katika shughuli za kuendesha serikali.

Naye mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri anasema malumbano baina ya wabunge na Rais kwa upande mmoja na Naibu Rais kwa upande mwingine ni ishara ya kukita kwa migawanyiko ndani ya Jubilee.

“Kutoitishwa kwa mkutano wa PG kumeibua minong’ono na uvumi kuhusu mipango ya chama hiki tawala kuhusu urithi wa kiti cha urais na hatuwezi kunyamaza ikiwa mambo hayaendeshwi sawasawa,” akasema Bw Ngunjiri.

Sawa na wenzake, mbunge huyo anachukulia kuwa muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga pia umechochea mikinzano zaidi ya kimawazao na kimasilahi kati ya Rais na Naibu wake.

Waasi watamuweza Uhuru?

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto sasa wanapanga kuwasilisha hoja bungeni ya kuwatimua afisini mawaziri wanaodai wanaendesha njama ya kumhujumu Dkt Ruto.

Katika hatua inayolenga Rais Kenyatta ambaye kikatiba ndiye huwateua mawaziri, wabunge hao wanataka kuchunguza kile wanachodai kuwa sakata ya utoaji zabuni kwa polisi kwa lengo la kupendekeza adhabu kali kwa maafisa katika afisi ya Rais.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na mwenzake wa Kiharu Ndindi Nyoro, wabunge hao sasa wanaonekana kumkabili Rais Uhuru Kenyatta moja kwa moja katika mipango hii.

Hivi ndivyo vitisho vya moja kwa moja kwa serikali ya Rais Kenyatta kutoka kwa wabunge kutoka Mlima Kenya, ng’ome ya Rais Kenyatta.

Wanafanya hivyo kwa kutisha kumng’oa afisini Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na kumhusisha Katibu katika wizara hiyo, Dkt Karanja Kibicho na sakata ya utoaji zabuni ya bima ya polisi.

Rais Kenyatta amewatwika, Dkt Matiang’i na Dkt Kibicho jukumu la kusimamia wizara ya usalama wa ndani wa nchi na ushirikishi wa shughuli za serikali yake.

“Ikiwa mtu anadhani tutaishi kwa woga na kulazimishwa kufuata mkondo fulani wa kisiasa, enzi hizo zimepita,” Bw Ichung’wa alisema.

Ameelekeza ghadhabu zake kwa Dkt Kibicho akisema ndiye amekuwa akimhujumu Dkt Ruto mbali na kuwaagiza polisi kususia mkutano wake juzi katika kaunti ya Nyeri.

“Kibicho ni nani kwa Naibu Rais aliyechuguliwa na mamilioni ya Wakenya kuitisha ratiba ya ziara zake,” Bw Ichung’wa akauliza.

Naye Bw Nyoro anadai maafisa fulani katika afisi ya Rais walipeana zabuni ya utoaji huduma za bima kwa polisi kwa kampuni iliyodai Sh1.7 bilioni na kuacha ile iliyotaja bei ya Sh628 milioni, hatua ambayo ni kinyume cha sheria.

“Sasa tutauliza maswali kuhusu bima ya polisi katika afisini ya Rais. Tutataka kujua ni kwa nini kampuni iliyoitisha pesa nyingi ndio ilipewa zabuni hiyo badala ya ile iliyotaja bei ya chini,” alisema Nyoro ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC).

Wabunge hao wanaonekana kukasirishwa na kuondolewa kwa walinzi wa baadhi ya majuzi, hatua waliofasiri kama adhabu kwao kuunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

Walinzi

Kando na Ichung’wa, wengine waliopokonywa walinzi na wameonakana kukaidi wito wa Rais Kenyatta kusitisha kampeni za mapema ni; Kimani Ngunjiri (Bahati), Mary Njoroge (Maragua), Susan Kihika (Seneta, Nakuru) na Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu.

Wengine ni Sabina Chege (Mwakilishi wa Wanawake Murang’a), Alice Wahome (Kandara), Rigathi Gachagua (Mathira) na Catherine Waruguru (Laikipia).

Hata hivyo, itakuwa kibarua kigumu kwa wabunge hao kufanikisha azma yao ya kumng’oa Dkt Matiang’i kutoka wadhifa wake kupitia hoja bungeni kwa sababu idadi yao ni ndogo na vizingiti kadha vya kikatiba.

Kulingana na kipengee cha 152 cha Katiba, hoja ya kumwondoa afisini Waziri sharti iungwe mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge, ambayo ni sawa na wabunge 177. Wabunge wanaounga Dkt Ruto mkono hawawezi kufikisha idadi hii.

Na kabla ya Spika wa Bunge kuidhinisha hoja kama hiyo, sharti mbunge aliyeidhamini aonyeshe namna waziri amekiuka Katiba, sheria husika au kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake kufaa kuondolewa kazini.

Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi amewahi kutumia hitaji hilo la kikatiba kutupilia mbali hoja kadha za awali za kuwaondoa mamlakani waliokuwa mawaziri, Anne Waiguru (Ugatuzi), Profesa Jacob Kaimenyi (Elimu) na waziri wa Afya Sicily Kariuki mwaka 2018.

Rais Kenyatta pia ana uwezo wa kuwanyamazisha wabunge wandani wa Dkt Ruto kuwa kushinikiza kuondolewa kwa baadhi yao wanaoshikilia nyadhifa kuu bungeni.

Timua wanaotatiza juhudi za kukabili ufisadi, Uhuru aambiwa

Na BARNABAS BII

VIONGOZI kadhaa wa Rift Valley Jumatatu walitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta aadhibu wanachama wa Jubilee wanaotatiza juhudi za kupambana na ufisadi.

Kulingana nao, viongozi aina hiyo wanaweka hatarini sifa itakayoachwa na Rais wakati atakapokamilisha hatamu yake ya uongozi mwaka wa 2022.

Walipuuzilia mbali madai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga viongozi wa eneo moja, wakamtetea Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Bw George Kinoti kwa kukamata washukiwa wa ufisadi.

Viongozi kutoka Chama cha Jubilee, vyama vya upinzani na wa kijamii walikashifu vikali wandani wa Naibu Rais William Ruto kwa madai yao kwamba Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), inatumiwa kuhujumu miradi mikubwa ya Jubilee kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi.

“Inafedhehesha kwa kiongozi ambaye yuko ndani ya serikali kuzungumza kinyume na Rais Kenyatta ambaye amekuwa akisema wazi mara kwa mara kwamba ana imani kwa DCI na asasi nyingine za kitaifa kupambana na ufisadi,” akasema Bw Paul Kibet, ambaye ni mratibu wa Chama cha KANU katika eneo la Rift Valley.

Alitoa wito kwa asasi husika zizidishe juhudi zao katika vita dhidi ya ufisadi na kurudisha mali zilizoibwa huku wakichukua hatua za kisheria dhidi ya washukiwa wa ufisadi bila kujali nafasi zao katika jamii.

Naibu Rais na wandani wake wamekuwa wakidai Bw Kinoti anatumiwa kuhujumu miradi ya Jubilee kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi.

Lakini Mbunge wa Cherang’any, Bw Joshua Kutuny alimuonya Dkt Ruto na wandani wake dhidi ya kutumia jamii nzima kutetea misimamo yao na vile vile kutishia jamii nyingine.

Alionya pia dhidi ya kutusi afisi ya rais katika vita dhidi ya ufisadi.

Katibu Mkuu wa KANU, Bw Nick Salat alisema wanasiasa hawawezi kukubaliwa kumshambulia Rais kwa maneno kwani haifai kuashiria kwamba kiongozi wa taifa anaagiza jinsi uchunguzi ufanywe kwa sakata mbalimbali zilizofichuliwa majuzi.

“Ninataka kuambia hawa wanasiasa wanaojidai kuzungumza kwa niaba ya Wakalenjin waachane na sisi. Vita dhidi ya ufisadi havifai kuchukuliwa vya kibinafsi jinsi wanavyofanya. Inasikitisha wanaingiza jamii nzima katika suala hili. Hili ni jambo ambalo hatutalikubali kamwe,” akasema Bw Salat.

Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter alisema watu waliohusishwa na ufisadi wanafaa wajiandae kubeba misalaba yao wenyewe bila kuingiza jamii nzima kwa biashara zao haramu.

Hii ni baada ya Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang na wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Caleb Kositany (Soy) kumwambia Rais awaeleze sababu halisi kuhusu kwa nini anampiga vita naibu wake.

Viongozi hao waliozungumza wiki iliyopita katika mazishi iliyofanywa eneo la Ziwa, Kaunti ya Uasin Gishu walimlaumu Rais kwa kutumia mwafaka kati yake ya Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuadhibu watumishi wa umma ambao ni wa jamii ya Wakalenjin na kuzuia utekelezaji wa miradi mikubwa katika eneo hilo.

Mnamo Jumapili, viongozi wengine ambao ni pamoja na mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko pia walijitokeza kuwashtumu wenzao wa Rift Valley kudai kuwa wanalengwa katika vita dhidi ya ufisadi.

Bi Mboko hasa alimtaka Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen ajitokeze kuelezea anachofahamu kuhusu kashfa ya mabwawa na sio kutoa madai tu.

Mbunge akemea wanaohoji ziara za rais kwa Mzee Moi

Na JOSEPH WANGUI

MBUNGE wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua, amesuta viongozi wanaohusisha ziara zinazofanywa mara kwa mara na Rais Uhuru Kenyatta kwa Rais Mstaafu Daniel arap Moi na siasa za 2022.

Hatua yake imetokana na jinsi baadhi ya wanasiasa wanavyoshuku kuwa ziara hizo zinahusiana na uchaguzi wa urais wa 2022.

“Moi ni raia mheshimiwa katika nchi hii na ana haki ya kutunzwa na watu wengine wote wadogo wake kiumri ambao wako uongozini. Rais Kenyatta anapomtembelea, hiyo ni tabia njema,” akasema Bw Gachagua.

Alisema Bw Moi anahitaji zaidi kutembelewa, hasa wakati huu ambapo hayuko katika mstari wa mbele kushiriki kwa masuala ya kitaifa.

“Ziara za Rais Kenyatta Kabarak hufuata tamaduni za Kiafrika kutembelea wagonjwa. Ni tabia mbovu kwa Wakenya kushuku kile wanachojadili,” akasema Bw Gachagua.

Aliomba Wakenya wamruhusu rais kufanya kile anachotaka ikiwemo kujumuika na kutembelea yeyote anayetaka.

“Hakuna vile rais atawaambia kila kitu anachofanya. Hafai kuhojiwa kuhusu kwa nini alimsalimia mtu huyo na si yule mwingine. Hiyo ni kukosa adabu,” akasema mbunge huyo, ambaye ni msaidizi wa zamani wa rais.

Alipoulizwa kwa nini Rais Kenyatta hajakuwa akimtembelea Rais Mstaafu Mwai Kibaki jinsi anavyomtembelea Bw Moi, mbunge huyo alisisitiza Wakenya wakome kumchunguza rais.

“Hakuna sheria inayosema unapomtembelea Moi ni lazima pia umtembelee Kibaki. Lazima rais apewe uhuru wa kufanya atakavyo,” akasema.

Bw Gachagua alipuuzilia mbali wakosoaji wa ziara hizo za Kabarak na kusema hizo huwa ni ziara za kibinafsi.

Alisema Wakenya wanaweza kumhoji rais kuhusu masuala rasmi kama vile anavyotumia rasilimali za umma lakini si kuhusu ziara zake kwa Mkenya yeyote au marafiki wake.

Ziara za Rais Kenyatta nyumbani kwa Bw Moi zilizidi kutazamwa kisiasa wakati naibu wake, Bw William Ruto, alipozuiliwa kuingia katika boma hilo hivi majuzi alipotaka kumjulia hali rais huyo mstaafu.

Bw Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi, ambaye ni mwanawe rais mstaafu ni mahasimu wa kisiasa katika eneo la Rift Valley.

Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na jinsi ambavyo rais Kenyatta amekuwa akimtembelea Mzee Moi mara kwa mara.

Wengi wanaamini kuwa huenda hiyo ikawa ishara tosha kwa Bw Ruto kwamba, azma yake ya kutaka urais huenda ikatumbukia nyongo.

Tayari kumeibuka majaribio ya kutaka Bw Ruto na manaibu magavana waliohudumu kwa vipindiviwili wasiwanie nyadhifa za juu.

Kalonzo aonya Uhuru kuhusu wandani wake

Na VALENTINE OBARA

JUHUDI za Rais Uhuru Kenyatta kupambana na ufisadi ziko hatarini kuhujumiwa na wandani wake, Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameonya.

Akizungumza alipokutana na Wakenya wanaoishi Uingereza, Bw Musyoka alisema kwamba anaunga mkono juhudi hizo za rais lakini akamtahadharisha kuhusu wandani wake ambao wamejitolea mhanga kuzivuruga.

“Rais Uhuru Kenyatta ana nia njema katika jitihada zake za kuangamiza ufisadi nchini Kenya lakini kuna watu wenye mamlaka makubwa ambao ni vizingiti na wanaweza kuhatarisha sana lengo lake,” akasema.

Kwa miezi kadhaa sasa, maafisa wa mashirika mbalimbali ya serikali wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kushtakiwa kwa madai ya kuhusika katika ufisadi.

Mashirika hayo yanayojumuisha Kenya Power na shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) yamedaiwa kukumbwa na ufujaji wa mamilioni ya pesa za umma.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa hasa kutoka maeneo ya Rift Valley, wamekuwa wakilalamika wakidai kwamba juhudi hizo zinalenga kuhujumu azimio la Naibu Rais William Ruto kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanywa 2022.

“Natumai rais atasimama kidete na kulenga ruwaza yake ya kuangamiza ufisadi nchini. Kenya iko katika njiapanda na inahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu kukabiliana na ufisadi uliokithiri na kupunguza madeni makubwa ya taifa,” akasema Bw Musyoka.

Akizungumza Jumapili alipokuwa katika Kaunti ya Kilifi, Bw Ruto alitaka wanasiasa wote washirikiane kutatua changamoto zinazokumba wananchi bila kuingiza siasa katika juhudi zinazoendelezwa.

Alitaka viongozi wajiepushe na uchochezi wa kisiasa kwani unaathiri maendeleo ya wananchi, na kuwakumbusha kuwa kipindi cha uchaguzi kilikamilika mwaka uliopita.

“Ninawaomba viongozi wenzangu wote waliochaguliwa, nafasi tuliyonayo si ya kuchochea uhasama bali kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazotukumba. Ni lazima tutafute suluhisho kwa njia yenye heshima,” akasema naibu rais.

Akiwa Uingereza, Bw Musyoka alizindua tawi la Chama cha Wiper katika jiji la Birmingham.

Alirejelea kauli kuwa anaunga mkono muafaka kati ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga kwani unalenga kuleta umoja wa Wakenya na maendeleo nchini.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kwamba chama chake kinaendeleza mikakati ya kutafuta ushirikiano na vyama mbalimbali kwa maandalizi ya uchaguzi wa 2022.

Katika ziara hiyo, aliandamana na Kaimu Mwenyekiti wa Wiper, Bw Patrick Kiilu, Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Makueni, Bi Rose Mumo Museo na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Kennedy Musyoka.

Obama kukutana na Uhuru na Raila

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA rais wa Amerika Barack Obama atafanya kikao na rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwenye ziara yake nchini mnamo Jumatatu. 

Kwa mujibu wa dadake Dkt Auma Obama, kiongozi huyo ambaye babake alikuwa Mkenya na mamake raia wa Amerika amekuwa akifuatilia kwa karibu masuala mbalimbali nchini.

Aliongeza kuwa ziara yake imetimia wakati mwafaka baada ya viongozi hao waliotofautiana vikali kuridhiana kufuatia kipindi cha uchaguzi uliojaa uhasama.

Hata hivyo, Bi Obama alikataa kuzungumzia matayarisho ya ziara hiyo ya siku mbili na maswala yatakayojadiliwa kwenye mikutano inayotarajiwa akitaja sababu za kiusalama na kuahidi wanahabari kwamba taarifa kamili itatolewa na afisi ya Rais kupitia msemaji mkuu wa serikali.

“Siwezi kujua kile atakachozungumza atakapokutana na viongozi wakuu nchini wala sijui ataandamana na kiongozi yupi maarufu ila nafahamu kwamba amekuwa akifuatilia kwa makini matukio nchini na ziara hii kwa bahati nzuri inakuja wakati kuna maridhiano nchini,” akasema Bi Obama huku akikosa kuthibitisha iwapo nduguye ataandamana na muigizaji maarufu duniani Oprah Winfrey

Bi Obama alisema nduguye atafungua rasmi kituo alichoanzisha cha Sauti Kuu ambacho ujenzi wake umekuwa ukiendelea tangu 2009 na kimekuwa kikiwapa usaidizi watoto na familia katika kijiji cha Kogelo na kaunti nzima ya Siaya.

Kituo hicho kikubwa kilichojengwa kupitia ufadhili wa mashirika ya kigeni kimekuwa kikiendesha mafunzo kwa wakazi jinsi ya kujikimu kimaisha na kukuza talanta kwenye fani ya michezo kwa kushirikiana na ligi maarufu kama ligi kuu nchini Uingereaza.

“Sauti Kuu ni kituo kinachowapa mafunzo wanajamii kuhusu jinsi watakavyotumia rasilimali zao kutokomeza umaskini, kuyafadhili masomo ya wanafunzi vyuoni na kuwapa ujuzi wa kiufundi wanajamii ili waimarishe mapato yao,” akasema Bi Auma.

Aidha, kituo hicho kinajihusisha na miradi kama utunzaji wa misitu katika Kaunti ya Siaya, kuendesha vita vikali dhidi ya maambukizi ya Ukimwi na kupigana na utamaduni na mila potovu katika jamii.

Rais Obama anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu na atapitia mji wa Kisumu kabla kuelekea Kaunti ya Siaya kufungua kituo hicho. Ratiba kamili ya ziara yake inatarajiwa kutolewa na serikali.

Bw Obama alitembelea Kenya katika kipindi cha pili cha uongozi wake mnamo 2015 lakini hakuweza kufika Kogelo kutokana na kile kilidaiwa kuwa sababu za kiusalama.

Hata hivyo alitoa ahadi wakati huo kwamba angeitembelea Kenya na Afrika Mashariki baada ya kung’atuka mamlakani na kuwa raia wa kawaida.

MAREKEBISHO YA KATIBA: Raila achokoza Jubilee

KITAVI MUTUA na VALENTINE OBARA

MSIMAMO wa Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa alikubaliana na Rais Uhuru Kenyatta kutakuwa na marekebisho ya Katiba walipoweka muafaka wa maelewano hapo Machi 9, huenda ukaibua upya mgogoro katika chama cha Jubilee.

Wakati Bw Odinga alipotoa pendekezo hilo wiki chache baada ya muafaka wake na Rais Kenyatta, kulizuka mvutano ndani ya Jubilee ambapo mrengo mmoja ukiongozwa na Naibu Rais William Ruto na wandani wake akiwemo Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale ulipinga vikali.

Mjadala huo ulipokuwa ukiendelea Rais Kenyatta alikuwa kimya hadi mwishowe akajitokeza na kusema hakuna muda wala rasilimali za kuandaa kura ya maamuzi ya kufanyia marekebisho Katiba.

“Hakuna nia yoyote ya kurekebisha katiba. Hatuna wakati. Tunataka kufanya kazi muhimu, sio kukimbia hapa na pale kuuliza kama mnataka Katiba mpya au la. Hilo halitatatua matatizo yetu,” akasema rais alipozungumza mwezi Mei katika Ikulu ya Nairobi.

Msimamo huo wa rais unakinzana na ule wa Bw Odinga ambaye amesisitiza walikubaliana suala hilo litakuwa moja ya ajenda kuu za maelewano yao.

Bw Ruto hakuhusishwa kwenye muafaka huo na baadhi ya wandani wake wana wasiwasi kuhusu kile wawili hao walikubaliana kwenye maelewano yao.

Akizungumza katika Kaunti ya Kitui, Bw Odinga alisisitiza ni lazima Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuleta mabadiliko Kenya.

“Tulikubaliana na Rais Kenyatta kwamba tukifanikiwa kurekebisha makosa yaliyo kwenye Katiba tutakuwa tumefanikiwa kuleta mabadiliko Kenya kwa hali ambayo itafanya liwe taifa bora zaidi kwa vizazi vijavyo,” akasema.

Kiongozi huyo alisema Katiba iliyopo, ambayo ilipitishwa mwaka wa 2010, imedhihirisha haiwezi kutatua changamoto nyingi zinazokumba taifa hili.

Miongoni mwa marekebisho anayotaka ni kuhusu mfumo wa uongozi ili kuwe na ngazi tatu za utawala, tofauti na jinsi ilivyo sasa ambapo kuna ngazi mbili ambazo ni Serikali Kuu na za kaunti.

Kulingana naye, muafaka ulipatikana kati yake na rais baada yao kukubaliana kuwa marekebisho ya Katiba yatakuwa kati ya masuala makuu yatakayoangaziwa.

“Tuna Katiba nzuri lakini haitusaidii. Hii ndio sababu nilishirikiana na Rais Kenyatta ili kufanya marekebisho ya kisheria,” akasema.

Mtaalamu wa kisheria ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu wa uundaji wa Katiba iliyopo, Bw Nzamba Kitonga, alisema wakati huu ni mwafaka kwa Katiba kufanyiwa marekebisho.

Kulingana naye, kamati yake ilikuwa imetarajia Katiba itahitaji marekebisho baada ya miaka saba au kumi.

Lakini wandani wa Bw Ruto wamekuwa wakishikilia kuwa marekebisho ya kikatiba ni njama fiche ya Bw Odinga kumharibia nafasi ya kushinda urais 2022.

Jopokazi lililoteuliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga limekuwa likiendeleza shughuli zake kichinichini na kufikia sasa haifahamiki hatua zilizopigwa katika majukumu yao.

Bw Odinga alisema marekebisho ya Katiba ni miongoni mwa yanayoangaziwa na jopokazi hilo, ambalo kulingana naye litaanza kuzuru maeneo tofauti ya nchi hivi karibuni kutafuta maoni ya wananchi.

Alisema baadhi ya maswali ambayo wananchi wataulizwa ni kuhusu jinsi ugatuzi unavyoweza kuimarishwa, mbinu mwafaka za ugavi wa rasilimali za nchi na kama wanataka mfumo uliopo wa uongozi uendelee kutumiwa au ubadilishwe.

Uhuru alitaka kunitupa ndani – Raila

KITAVI MUTUA na WYCLIFFE MUIA

KINARA wa ODM, Raila Odinga Jumanne alifichua kuwa Rais Uhuru Kenyatta alikuwa amepanga kumkamata na kumshtaki kwa uhaini baada ya kujiapisha kama ‘rais wa wananchi’ mnamo Januari 30 mwaka huu.

“Baada ya kuapishwa, niligundua kuwa Uhuru alikuwa anashinikizwa na wandani wake anikamate na akashawishika. Lakini baada ya kubaini athari za hatua hiyo akabadili mpango huo,” alisema Bw Odinga akiwa Kitui.

Kwa upande wake, Bw Odinga alikuwa na shinikizo kali kutoka kwa wandani wake wenye misimamo mikali waliomtaka aingie Ikulu kwa mabavu, awashauri wafuasi wake kuacha kulipa ushuru kwa serikali na pia wachome picha za Rais Kenyatta.

Akisimulia kwa mara ya kwanza matukio yaliyopelekea yeye na Rais Kenyatta kuafikia mwafaka wa maridhiano hapo Machi 9, Bw Odinga alielezea jinsi yeye na Rais Kenyatta walivyojipata katika hali ngumu ya kisiasa hasa kutoka kwa wandani wao wenye misimamo mikali, hali iliyowalazimu kuamua kibinafsi kuchukua hatua za kuepusha Kenya kutumbukia katika ghasia za kikabila na kisiasa.

Akizungumza baada ya kufungua hoteli ya kifahari inayomilikiwa na msomi wa masuala ya sheria Prof Makau Mutua katika Kaunti ya Kitui, Bw Odinga alisema kama hawangeshirikiana Kenya sasa ingekuwa kama Syria ama Yemen.

Alisema wafuasi wake walikuwa wakimshinikiza aingie Ikulu kwa nguvu baada ya kujiapisha kuwa ‘rais wa wananchi’ huku wafuasi wa Rais Kenyatta nao wakimpa presha amkamate na kumfungulia mashtaka ya uhaini, ambayo hukumu yake ni kifo kwa kunyongwa.

“Tayari wafuasi wangu walikuwa wameanza kung’oa picha za Rais Kenyatta kutoka kwenye majengo na biashara zao huku wengine wakitishia kutolipa ushuru.

Wafuasi wetu walikuwa tayari kuanza kutukubalia tuchukue ushuru kutoka kwao,” alisema Bw Odinga katika hafla aliyoandamana na mkewe Aida na kuhudhuriwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana Charity Ngilu wa Kitui na mwenzake wa Makueni, Kivutha Kibwana.

Bw Odinga alifichua kuwa mwanzoni Rais Kenyatta alikuwa amekubali kumkamata na kumfikisha kortini lakini akabadili msimamo baada ya kutathmini athari za hatua hiyo.

“Tulikuwa tumekubaliana tuanze kukusanya ushuru katika ngome zetu lakini baada ya kufikiria zaidi nikaona kuwa kama taifa tungetumbukia shimo sawa na nchi za Yemen na Syria. Rais naye aliacha mpango wa kunikamata na tukaamua kushirikiana,” alisema Bw Odinga.

Alidokeza kabla ya mwafaka, alikuwa kwenye njia-panda kuhusu kuwaridhisha wandani wake, ambao walikuwa wamekasirishwa na ukosefu wa uchaguzi huru na wa haki, ama kufanya kilicho bora kwa taifa zima kwa jumla.

“Iwapo ningetii mwito wa wafuasi wangu waliokuwa na hasira nyingi na kuwaruhusu kuandamana kote nchini, Serikali ya Jubilee ingewakabili kwa dhuluma kali na hili lingepeleka nchi kwenye njia hatari sana,” akasema.

Alisema hivi karibuni Wakenya wataanza kufurahia matunda ya mwafaka mara jopo lililobuniwa kutathmini ajenda tisa za maafikiano litakapoanza shughuli zake.

Aliongeza kuwa baada ya miaka minane ya utawala chini ya Katiba mpya, huu ni wakati mwafaka wa kuichunguza upya na kuziba mianya ambayo itapatikana.

Bw Odinga alimkosoa Naibu Rais William Ruto kwa kudai kuwa alifahamu kuhusu mazungumzo yake na Rais Kenyatta kabla ya kusalimiana nje ya Jumba la Harambee mnamo Machi 9, mwaka huu.

 

Ruto, Kalonzo walikuwa gizani

Bw Odinga alisema walikubaliana na Rais Kenyatta wasimhusishe Bw Ruto katika mazungumzo yao. “Nilimwambia Uhuru kuwa sitaki watu wanaopiga siasa za 2022 wahusishwe katika muafaka wetu. Rais aliahidi kuwa hatahusisha Ruto naye akanitaka pia ni nisimwambie Kalonzo,” alisema Bw Odinga.

Kauli ya Bw Odinga inatofautiana na msimamo wa Bw Ruto kuwa Rais Kenyatta alimshauri kabla ya kufanya muafaka na Waziri huyo Mkuu wa zamani.

Bw Odinga aliwataka wafuasi wake Ukambani kuunga mkono muafaka wake na Rais Kenyatta akisema utawafikisha ‘Canaan’ baada ya kutekelezwa kikamilifu.

Kwa upande wake, Bw Musyoka alimtaka Odinga kutumia muafaka wake na rais kuhakikisha kuwa viongozi wa upinzani wameondolewa mashtaka waliyofunguliwa wakati wa uchaguzi.

“Mheshimiwa Johnstone Muthama angekuwa hapa leo iwapo hangekuwa anakabiliwa na kesi yake wakati wa uchaguzi. Tulitarajia muafaka ungeondolea mbali kesi hizo,” alisema Musyoka.

Bw Odinga alimsifu Prof Mutua na kutaka jamii ya Wakamba kuhakikisha imefaidika kutoka kwa hekima yake ya uongozi.

“Nilipokuwa naja huku nilimfahamisha Rais Kenyatta na akanituma niambie Mutua aache kuwa mkosoaji sugu kwake,”alisema Bw Odinga.