ULIMBWENDE: Jinsi ya kuondoa weusi makwapani

Na MARGARET MAINA

WEUSI makwapani ni mabadiliko ya ngozi yanayotokea na hufanya watu wengi wasiwe na starehe wakivaa nguo za wazi mbele za wenzao.

Hali hii husababishwa na kunyoa mara kwa mara, seli zilizokufa, mtu anapotumia ‘deodorant’ yenye pombe inayobadili rangi, matumizi ya creams za kunyolea (kupakwa makwapani), kikwapa (yaani jasho la kwapani), kuvaa nzuo nyingi au nzito, na mwili kukosa hewa vizuri.

Vipo vitu vya asili unavyoweza kutumia kumaliza kabisa hali hii 

Unaweza ukatoa weusi huo kwa kutumia vitu ambavyo havina kemikali (au visivyo na kemikali zenye athari hasi) kama vile;

 • Limau

Chukua limau au ndimu na ukate vipande vya mduara. Kwa vipande hivi paka sukari au asali juu yavyo na kisha chukua hivyo vipande ujipake makwapani mara mbili kwa siku.

Wakati unapaka unashauriwa uache kwa dakika 10 kabla ya kuoga.

Baadaye osha kwa maji ya fufutende (luke warm).

Limau inatumika kama ‘bleach’ kutoa hiyo rangi na kutoa seli zilizokufa kwenye hiyo ngozi ya kwapani.

 • Hamira (Baking soda)

Inasaidia kutoa seli zilizokufa kwa urahisi.

Changanya baking soda na maji iwe nzito na kisha paka kwapani. Acha kwa dakika 10 halafu osha na jikaushe. Fanya hivyo mara 2-3 kwa wiki.

Unashauriwa kuendelea na shughuli hiyo mpaka utakapoona umeridhika na mabadiliko.

 • Maganda ya machungwa

Chukua maganda ya machungwa na uyakaushe juani. Yakishakauka yaponde, changanya na maji ya waridi (rose water) na ukoroge.

Kwenye mchanganyiko ongeza maziwa na uanze kupaka makwapani kwa dakika 10-20. Baada ya kufanya hivyo, unaweza kuosha makwapa.

 • Viazi

Menya viazi kisha vikate vipande, jipake makwapani yale maji yake yakiingia kwenye ngozi yanatoa rangi nyeusi au unaweza kuponda kikiwa kibichi na kujipaka kwa dakika 10-20 kisha nawa. Unaweza kufanya hivyo mara mbili kwa siku mpaka weusi utakapoisha.

 • Tango (cucumber)

Kata vipande vya tango na ujipake kwapani. Yale maji yake ndiyo dawa. Unaweza pia kuvisaga vipande hivyo viwe nyororo ndipo upake; acha kwa dakika kati ya kumi na ishirini.

 • Sukari

Chukua sukari uchanganye na mafuta ya mizeituni; paka na baada ya muda osha.

 • Mafuta ya nazi

Mafuta haya yana vitamini E na yanasaidia kung’arisha ngozi.

Jipake makwapani na baada ya dakika 10-20 hivi, osha makwapa yako kwa maji moto.

Shughuli hii inaweza kuchukua muda mchache ukaona mabadiliko makubwa au ikachukua muda mrefu mpaka uone mabadiliko; inategemea ngozi ya mtu.

ULIMBWENDE: Tumia mbinu hii ya vitunguu maji kutunza nywele

Na MARGARET MAINA

MTU na hasa mwanamke anayetambua umuhimu wa mwonekano mzuri hutamani kuwa na nywele nzuri za kutosha na zenye afya yake ya asili. Tatizo la kupotea kwa nywele au upara (wengine hupenda hali hii) limekuwepo tangu awali. Kipara kinaweza kuja kwa sababu za kimaumbile za kawaida.

Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha kupotea kwa nywele kama vile:

 • Sababu za kimazingira
 • Kuzeeka
 • Msongo wa mawazo (stress)
 • Kuvuta sigara kupita kiasi
 • Lishe duni
 • Homoni kutokuwa sawa
 • Kurithi vinasaba
 • Maambukizi kwenye ngozi ya kichwa
 • Matumizi yasiyo sahihi ya vipodozi vya nywele
 • Baadhi ya dawa za hospitali
 • Matatizo katika kinga ya mwili
 • Upungufu wa madini chuma, na
 • Magonjwa mengine sugu

Kitunguu maji kina kazi nyingi katika mwili wa binadamu kwani hutibu magonjwa mengi kama kikohozi, vidonda vya tumbo na mifupa, ngozi, koo, figo, na pia kina virutubisho vingi vya vitamini C.

Kitunguu hiki huwa na salfa (sulphur) ambayo husaidia kutengeneza tishu za ‘collagen’ katika mwili ambapo huipa nywele na ngozi nuru ya aina yake.

Hivyo naweza kusema kuwa juisi ya kitunguu maji husaidia kukuza nywele na kwa wale wenye nywele za kukatika, kupaka kitunguu maji mara kwa mara kunaweza kusaidia kupambana na tatizo hilo.

Jinsi ya kuandaa

 • Chukua kitunguu kimoja au viwili kutegemea na na ukubwa wa kitunguu chenyewe
 • Osha vizuri kitunguu au vitunguu na kisha ukimenye au uvimenye
 • Kata kitunguu au vitunguu vipande vidogo vidogo ili iwe rahisi kusaga au kutwanga
 • Saga kwenye blenda au uvitwange kwenye kinu.
 • Visage au vitwange mpaka vilainike kabisa ili uweze kutoa maji kwa urahisi.
 • Vichuje vizuri ili upate majimaji. Hakikisha kwamba huongezi maji kwa hivi vitunguu.

Jinsi ya kupaka

Nywele sio lazima ziwe safi maana unapaswa kuziosha baada ya kupaka maji ya vitunguu.

 • Chukua pamba ambayo utatumia kupaka hayo maji ya vitunguu kwenye nywele zako. Paka zile sehemu ambazo nywele zimekatika. Unaweza pia paka kichwa kizima.
 • Baada ya kupaka unapaswa kuvaa kofia ya plastiki na kitambaa kichwani ili uweze kupata joto.
 • Ukae hivyo kwa muda wa saa 4 – 5
 • Baada ya hapo unaweza kuosha na kukausha nywele zako.

Hitimisho

Ni vyema kufanya shughuli hii ya kupaka vitunguu angalau mara mbili kwa mwezi.

Ikiwa harufu ya kitunguu ni kali, unaweza kuongezea asali kidogo kwenye maji ya vitunguu.

Kwa matokeo mazuri ya kukuza na kutunza nywele zako, tumia vitunguu vidogo kufanya jinsi nilivyoeleza hapo juu.

ULIMBWENDE: Viini vya mipasuko ya visigino na jinsi ya kuzuia na kutibu

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MTU kuwa na miguu au visigino vilivyopasuka ni dalili tosha kuwa katika mwili kuna upungufu wa virutubisho kadhaa, vitamini au madini.

Hata hivyo, wengi wetu tumekuwa na mitazamo kwamba visigino kupasuka ni ishara tosha kwamba mtu ameonyesha kutojali usafi wa miguu yake.

Kwa kawaida, ngozi zetu huwa zina unyevu ambao huiwezesha ngozi ivutike au kutanuka pamoja na kusinyaa bila ya kutokea madhara yoyote kama vile kuchanika.

Pamoja na ngozi kugawanyika katika sehemu tatu; yaani sehemu ya nje ‘Epidermis’, sehemu ya kati ‘Dermis’ na sehemu ya ndani ‘Endodermis’, ni sehemu ya nje, ambayo ipo karibu na unaweza kuigusa au inaweza kuathirika na ukaiona kirahisi; na hii ni kwa sababu inagusana moja kwa moja na mazingira yetu.

Mitembo huanza kutokea katika sehemu hii ya ngozi, Epidermis.

Miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mtu apasuke visigino ni pamoja na:

a) Ngozi kuwa kavu sana

Hii ni sehemu ya nje ya ngozi ambayo inawezekana mtu kwa asili yake akawa na ngozi kavu na hivyo kuifanya ishindwe kustahimili kutanuka au kusinyaa na hivyo kusababisha ipasuke.

Kuiacha miguu katika maji kwa muda mrefu na baadaye kutoipaka mafuta ya kulainisha ngozi husababisha ile asili ya ngozi pamoja na mafuta katika ngozi yapotee na kuiacha ngozi ikiwa kavu sana.

b) Kuwa na uzito mkubwa

Hali hii husababisha presha kubwa iwe katika miguu unapokanyaga chini na endapo ngozi yako haitakuwa na uimara wa kutosha itasababisha visigino vipasuke.

Upungufu wa virutubisho mwilini; hasa madini ya Zinc, vitamini E pamoja na mafuta, na Omega 3. Hii husababisha ngozi kupoteza uimara wake na kuifanya ipasuke.

c) Kuvaa viatu ambavyo nyuma vipo wazi

Hulazimisha mguu au upande wa kisigino katika mguu utanuke zaidi na hivyo kuuweka mguu hatarini kupasuka.

d) Magonjwa

Baadhi ya maradhi kama vile Kisukari na magonjwa ya homoni (thyroid diseases) yana athari hasi kwa afya ya ngozi.

e) Umri mkubwa

Kwa kawaida mtu anapokuwa na umri mkubwa sana, hata utendaji kazi wa mifumo mbalimbali katika mwili wake hupungua kiufanisi; hivyo hata kinga ya mwili pamoja na afya ya ngozi pia hupungua.

Mtu kutozingatia usafi wa miguu yake kwa kiwango kinachostahili pia husababisha mipasuko kwenye visigino.

Moja ya madhara yanayoweza kutokea kwa mtu kupasuka visigino ni kupata maambukizi ya magonjwa.

Hii ni endapo miguu itachanika kiwango cha kufikia dermis, kiasi cha kusababisha damu ianze kutoka na kuchangia maumivu makali.

Mtu anaweza kupata maambukizi ya magonjwa kupitia mipasuko hiyo.

Kuzuia au kutibu tatizo la kupasuka visigino

Unafaa:

 • Kuzingatia ipasavyo usafi wa miguu na mwili kwa ujumla.
 • Kuepuka kutembea katika sehemu zisizo sawa bila kuvaa viatu, hii itaepusha miguu kuchanika.
 • Kwa miguu iliyopasuka tayari, ifanyie usafi miguu yako na kisha tumia mafuta ya mzaituni kupaka sehemu zilizo na mipasuko.
 • Vaa soksi na viatu vya kufunika ili miguu iendelee kuwa na unyevu. Usiku pia fanya hivyo kwa kuhakikisha ukilala miguu imevalishwa soksi baada ya kwamba umeipaka mafuta.
 • Hakikisha unakula vyakula venye madini ya calcium, zinc na iron. (Maziwa, mboga za majani, mafuta ya mimea, nyama, maharage pamoja na samaki)
 • Epuka kusimama kwa muda mrefu pamoja na kutoiweka miguu katika maji kwa kipindi kirefu.
 • Kama unafua jitahidi kuilinda miguu yako isiwe kwenye sabuni kwani aina nyingi za sabuni ya kufulia huvunjavunja mafuta yaliyo katika ngozi na kuiacha ikiwa kavu sana.
 • Jitahidi angalau mara moja kwa wiki kuiweka miguu yako katika maji moto. Hii husaidia kuongeza mzunguko wa damu katika miguu na hivyo kuendelea kuimarisha afya ya ngozi yako.

ULIMBWENDE: Njia rahisi za kutokomeza chunusi usoni

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

CHUNUSI ni ugonjwa wa ngozi unaowaathiri watu wengi katika kipindi fulani cha maisha yao; hasa wanapobaleghe.

Ugonjwa huu husababisha vipele vidogo vya mafuta kwenye ngozi na wakati mwingine hufanya ngozi kuwa na maumivu au kuhisi kuungua.

Vipele hivi hutokea wakati vishimo vya kupitisha jasho katika ngozi vinazibwa kwa mafuta na seli za ngozi zilizokufa au bakteria.

Mara nyingi chunusi hutokea usoni, mgongoni, kifuani na shingoni na huwaathiri watu wenye umri kati ya miaka 11-30.

Huathiri zaidi wasichana kuanzia umri wa miaka 14-17 na wavulana kuanzia umri wa miaka 16-19.

Kawaida ngozi ina vishimo vidogo vidogo vya kutolea jasho, mafuta na seli zilizozeeka kutoka ndani ya mwili.

Katika ngozi pia kuna tezi ya mafuta iitwayo ‘sebacous gland’ inayotoa mafuta yaitwayo sebum.

Uzalishaji wa sebum nyingi na seli za ngozi zilizokufa husababisha kuziba kwa vishimo vidogo vidogo vya ngozi vinavyopitisha jasho katika ngozi na kusababisha chunusi.

Kando na hayo, chunusi pia huchangiwa na sababu nyinginezo kama:

 • Mabadiliko ya homoni
 • Bakteria
 • Matibabu
 • Vinasaba (genetics)

Kuna njia nyingi za matibabu za kupunguza chunusi kama kubadili hali ya maisha, na kujipaka dawa.

Usijaribu kuviminya au kuvisugua kwa nguvu vipele kwa sababu hufanya ngozi kuuma na kutengeneza makovu ya kudumu.

Jiepushe kutumia manukato au vipodozi kwenye ngozi yenye chunusi.

Tumia bidhaa za urembo zisizoziba matundu madogo madogo ya ngozi yako.

Chunusi pia huweza kutibiwa kwa matumizi ya tiba asili kama matumizi ya matunda na viungo kama vitunguu saumu, mdalasini na vingine.

Hii ni njia nzuri ya kupatia ngozi unafuu na tiba mbadala na inayofaa katika ngozi yako. Zifuatazo ni baadhi ya tiba za kiasili za chunusi na salama kwa ngozi yako:

 1. Mdalasini uliosagwa na asali

Tumia mchanganyiko wa asali na mdalasini wa unga kwa kupaka angalau mara moja kwa siku. Asali na mdalasini zinasaidia katika uponyaji kwa sababu zina ‘anti-bacteria’ (zinaua na kuzuia bacteria) Jinsi ya kufanya:

 • Chukua asali kwenye kipimo cha vijiko vitatu vya chai
 • Chukua mdalasini wa unga kwa kipimo nusu kijiko cha chai
 • Changanya pamoja
 • Paka sehemu yenye chunusi na kisha kaa na mchanganyiko huo kwa angalau dakika 10-30 kisha osha kwa maji ya uvuguvugu

Mdalasini unaweza kuwasha kwenye ngozi hivyo unashauriwa ujaribu kupaka kidogo kwenye kiganja cha mkono kwanza ili kupata uhakika kua haitakusumbua.

2. Matango

Unaweza kutumia tango kwa kuondoa chunusi na hata kuondoa mabaka katika ngozi na kuifanya ngozi yako kuonekana yenye afya na yenye kuvutia.

Matango ni mazuri sana kwa kusafishia uso na hasa ukiwa na chunusi. Kata tango na ulimenye kisha paka usoni. Acha likae kwa muda wa dakika 15 hadi 20 hivi, kisha suuza kwa maji baridi.

Unaweza kurudia kwa siku mara mbili mpaka mara tatu hadi utakapopona.

3. Asali

Matumizi ya asali kutibu chunusi huwezesha ngozi, iwe na afya na nyororokwa sababu kwenye asali, kuna virutubisho vingi vyenye kazi ya kuua bakteria na kuzuia uchafu kwa ngozi.

Weka asali kidogo katika sehemu ilioathirika na uache kwa muda mrefu uwezavyo. Unaweza kupaka kwenye uso mzima au hata mwili mzima ukitaka kwa sababu asali inarutubisha ngozi ya mwili na kuifanya iwe na afya na mwonekano mzuri.

Ukisha ridhika na muda wa asali kwenye ngozi yako unaweza kusafisha kwa kutumia maji ya fufutende.

4. Papai

Matumizi ya papai yameonyesha matokeo mazuri sana katika kuondoa chunusi usoni na kusafisha sehemu zingine za mwili.

Pondaponda kiasi kidogo cha papai na upake palipo na chunusi. Acha papai pahala ulipopaka kwa muda mrefu iwezekanavyo.

Ukisha ridhika na muda huo unaweza kujisafisha kwa kutumia maji ya kawaida. Unaweza kurudia mara kadhaa kila siku kama ukitaka.

ULIMBWENDE: Mbinu 8 bora za kulainisha ngozi

Na MAGGY MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

BILA shaka mtu aliye na akili razini huhitaji ngozi laini na nyororo ili kujipa ujasiri wa kukabiliana na changamoto za kila siku pale kazini au nyumbani.

Hata hivyo, mbinu au njia tunazotumia wakati mwingine hutuacha na matokeo tusiyoyatarajia. Ni kwa sababu tumeumbwa sote tofauti na tunadhani kuwa kwa kutumia njia iliyomletea mwenzetu matokeo bora itatusaidia, lakini matokeo huwa kinyume kabisa.

Hizi hapa njia nane za kufuata ambazo zitakusaidia; haijalishi ni aina gani ya ngozi ulio nayo.

 1. Mlo

Vitu unavyokula vina mchango mkubwa katika ngozi na afya yako kwa ujumla. Ili kupata ngozi nzuri iliyo laini, nyororo na inayong’aa inabidi uache vyakula na vinywaji vinavyotengenezwa viwandani, wanga, mafuta na sukari na badala yake kula protini, matunda, mboga na kunywa maji kwa wingi.

Hakikisha unakunywa maji si chini ya glasi nane kwa siku na matunda pamoja na mboga kila unapopata mlo.

Matunda na mboga za matawi husaidia oksijeni kuzunguka vizuri mwilini na kwenye ngozi kuliko mafuta au kipodozi chochote unachoweza kupaka.

Protini husaidia kujenga ulinzi zaidi katika seli za ngozi ambayo ngozi inahitaji kukabiliana na ukavu wa ngozi. Nayo maji husaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini na kusaidia vinyweleo kupumua vizuri, hivyo kuzuia bakteria chini ya ngozi.

 1. Muda wa kupumzika

Watu wengi hawatambui umuhimu wa usingizi katika kutunza ngozi na kuzuia kuzeeka haraka. Usingizi ni muhimu kwa ngozi yako sana, hakikisha unapata muda wa kutosha kulala usiopungua masaa 8. Kifiziolojia, ngozi inafanya kazi kubwa sana wakati wa mchana katika kutunza mwili, kukabiliana na mionzi ya jua, kukabiliana na vijidudu mbalimbali kama bacteria na virusi na kutizamia joto la mwili. Ngozi hujijenga wakati mwili umepumzika ili kuweza kuendelea kuchunga mwili wa mwanadamu ipasavyo.

 1. Acha kujichubua

Kutumbua chunusi na vipele ni tabia tulio nayo sisi wanadamu. Mara nyingi matokeo yake huwa ni kuwa na makovu na wekundu. Kufanya hivi pia huchangia bakteria kusambaa na kuharibu ngozi hata katika maeneo ambayo hayakuwa na matatizo.

Japokuwa ni ngumu kutotumbua chunusi, ni vyema ikiwa italazimu ufanye hivyo, tumia kitambaa safi kutoa chunusi na wala sio vidole au kucha kwa sababu ya uchafu uliopo kwenye kucha na vidole. Yaani hatuwezi kuamini mikono yetu kwa asilimia 100.

Ukiwa na chunusi unashauriwa kumuona mtaalamu wa afya ya ngozi ili akupe tiba ya uhakika.

 1. Usafi kwanza

Osha uso wako. Watu wengi hukimbilia kuosha nyuso zao harakaharaka na sio vizuri kusafisha uso juujuu kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa uchafu kubaki, hasa wanawake ambao wanatakiwa kutambua umuhimu wa nyuso zao. Basi ni bora ukatenga muda wa kutosha katika kuosha na kutunza uso.

Kusafisha uso mara zisizopungua mbili kwa siku ni vizuri kwa utunzaji wa ngozi yako ya uso.

Baada ya kufanya hivyo ni muhimu upake mafuta kiasi. Mafuta ni kwa ajili ya kulainisha na kung’arisha ngozi. Hata ijapokuwa una ngozi ya mafuta mengi, ni vizuri kutafuta mafuta ya ngozi yako (oily skin).

 1. Tunza vizuri macho yako

Watu wengi hupaka kiasi kidogo cha mafuta chini ya macho bila kujua faida tunazoziacha kwa kutokufanya hivyo.Kuna mistari (mikunjo) ambayo inaanzia kwenye jicho na ambayo muda mwingine husogea hadi kwenye maeneo ya karibu na nywele. Paka mafuta ya kutosha chini ya macho. Aidha, fanya ni kama unajimasaji kuanzia kwenye kona karibu na pua mpaka kwenye mfupa wa shavuni (cheekbone) kuzunguka jicho lote.

 1. Barafu

Barafu ni moja kati ya vitu muhimu katika kutunza ngozi. Licha ya upatikanaji rahisi pia ina uwezo wa kutunza ngozi yako bila gharama.

Faida za kutumia barafu katika utunzaji wa ngozi yako ni kwamba; Ukiumia au kujichuna kwenye ngozi waweza kutumia barafu kupunguza wekundu na kupunguza mwasho katika eneo lile.

Sote tunajua unapochubuka au kuumia kuna mwasho ambao tunahisi katika eneo lile la jeraha. Ukitumia barafu itakusaidia. Pia barafu unaweza ukaitumia kupunguza ukubwa wa matundu katika ngozi hasa pale mtu alikuwa amekamua chunusi.

Barafu husaidia kuvuta ngozi ilisiwe imeacha matundu ambayo muda mwingine hayapendezi kuonekana. Ila kumbuka wakati wa kutumia barafu zungusha maeneo tofauti kwasababu huunguza pale inapoachwa sehemu moja. Pia ni vizuri kuweka aloevera katika maji utakayo gandisha kwa ajili ya barafu (hiari yako).

 1. Tumia mafuta yanayofaa ngozi yako

Moja kati ya njia za kutapa ngozi laini na nyororo ni kutumia mafuta ambayo yametengenezwa kwaajili ya kupaka kwenye ngozi na sio ya nywele au ya kupikia.

Kutumia mafuta ya ngozi husaidia kung’arisha ngozi na muonekano mzuri ambao sio wa mafuta. Mafuta ya ngozi hayazibi vinyweleo vya ngozi, hivyo huruhusu ngozi kupumua na kutoa taka mwili kupitia vitundu hivyo na yanasaidia kupunguza uzajishaji wa mafuta katika uso hasa kwa wale wenye ngozi za mafuta.

Kumbuka kupaka mafuta mara mbili kwa siku katika uso safi; yaani baada ya kusafisha uso vizuri ndipo unashauriwa upake mafuta. Ukizingatia hilo utaona mabadiliko katika ngozi yako.

 1. Sunscreen

Kwa wale wenye matatizo ya kuungua wakiwa kwenye jua asubuhi, ni muhimu wawe wakipaka mafuta ya kuzuia mionzi ya jua (sunscreen) inayopenya kwenye ngozi na kuharibu ngozi yako. Na pale unapokuwa nje, hakikisha unajizuia na jua kwanzia mavazi yako; vaa miwani ya kuzuia miale mikali ya jua na kofia pana inayozuia jua kupiga usoni.